Header Ads Widget

Responsive Advertisement

SALAMU ZANGU KWAKO SABRINA

Related image

Ni kipindi kirefu sasa kimepita, sijaiona sura yako Sabrina. Barua nyingi nilizokuandikia, zote umezipuuzia. Nimejaribu kukupigia simu walau nikusalimu na kama hutaki kuisikia sauti yangu basi walau uisikie sauti ya mwanao akilia kwa uchungu kukukosa mama yake, lakini hukutaka kupokea na mara nyingine uliona nakusumbua ukakata simu yangu kwa jeuri.
Kama ni kuumia, Sabrina umeniumiza nimechakaa niko hoi kabisa. Kila nikisoma zile meseji zako mbili za mwisho ulizonitumia kwa njia ya simu yangu,pale nilipokutakia hali, najikunyata nadhoofika moyoni nalia na kutetemeka mwili mzima. Sitakujakuzifuta meseji hizi, wacha ziendelee kuniliza. Huenda umesahau ulivyoniandikia, nanukuu kutoka katika simu yangu ya kiganjani, uliniandikia hivi: “we bwege ukome kabisa kunisumbua, hadhi zetu hizi unazionaje, zinalingana? Mwanaume gani unashinda umekalisha nyumbani kamafurushi? Mi mwanamke mzuri nahitaji matunzo, unauwezo wewe wakunitunza? Eboo! Umeshindwa, waachie wanaoweza kunihudumia. Acha kuniletea uchuro we fisi kongwe”. Niliupokea ujumbe wako huu, nilipomalizia kuusoma, tone la chozi lilidondokea kioo cha simu yangu. Ujumbe wako ulinipa hasira, nikairusha simu yangu chini kwa nguvu labda ingepasuka, lakini wapi, nilipotaka kuikanyaga kwa kisigino changu ili ipasuke kabisa, nikiwa nimeinua mguu juu, kabla sijashusha ikaanza kuimba ule wimbo wa Joseph Chamelion unaoitwa `Mama Neema`, nikajua tu kuwa ujumbe ulikuwa unaingia. Nikashusha mguu wangu kwa upole nikaichukua ili nione ujumbe huo. Kumbe na huu pia ulikuwa umetoka kwako ukiendelea kushindilia matusi. Yaani Sabrina uliona haitoshi, kabla sijakujibu ukaongeza ujumbe mwingine ukinambia, “kila mmoja aishi kivyake, sitaki unifatilie maisha yangu. Kama ni mapenzi mimi na wewe yaliisha kitambo. Mimi nina maisha yangu na wewe uishi maisha ya kwako. Ukiendelea kunisumbua, nitakuja kukufanyia kitu kibaya hutanisahau maisha yako yote.”
Hapo ndipo ulipokomea ujumbe wako wa pili. Kila nikikukumbuka narudia kuusoma, najikuta machozi yanatiririka mashavuni mwangu nakudondoka chini tone moja moja.
Sabrina mpenzi, wacha nikuite tumpenzi japo sasa sistahili tena kukuita hivyo. Katika ujumbe wako umenitishia kunifanyia kitu kibaya endapo nitaendelea kukufatilia, ni kipi hicho kitu kibaya zaidi ya hiki ambacho umenifanyia? Kama ni kuniua, Sabrina njoo unimalizie nijinafuu na suluba ninazopata.
Hivi kweli Sabrina umesahau kabisa tulikotoka? Hukumbuki hata moja kati ya yale tuliyoyapanga kuyafanya maishani mwetu? Uliahidi hutaniacha niteseke, utakuwa nami katika kufurahi na katika suluba za dunia hii, au siwewe ni Sabrina mwingine? Umesahau kabisa upendo wote nilio kuonyesha?.
Kibarua changu kidogo cha udereva wagari la shule, kilitulisha na kutuwezesha kulipa pango la nyumba, tulikula tulivyotaka, tulivaa vizuri, mwanetu mdogo naye akapata matunzo aliyostahili na mambo mengine wala hayakwenda mrama. Nilipoachishwa kibarua hicho japo kwa hila tu za wanadamu wenye wivu, Sabrina ulibadirika ukawa mbogo. Je ulinipendea vishilingi vyangu vilivyotuwezesha kujivinjari? Ni kweli hukuniweka moyoni? Kukupenda kote kumbe nilikuwa najipendekeza tu. Nayakumbuka maneno yako mazuri ya kimahaba ambayo hukuacha kunitamkia. Ninayakumbuka vema kwani maneno hayo hatimaye yamebadirika kuwa matusi ya kunidharau. Sabrina, hivi kweli wewe wakuniita mimi bwege, leo wewe unaniita mimi fisi kongwe. Nilipokuwa muwele ulinipetipeti nakunikanda mgongoni lakini leo unaniona furushi kweli.
Sabrina, mimi ni yuleyule mpenzi wako niliyekupenda na bado nakupenda. Nilipotoka kwenye pilika za maisha ulinipokea kwa furaha na bashasha, tena furaha iliyosindikizwa na kumbatio la mahaba na kuhamasishwa na busu la upendo. Mimi ni yule yule, labda umesahau ulivyokuwa ukijilaza kifuani pangu na kunibembeleza kwa maneno mazuri huku ukiahidi kuwa nami katika hali yoyote ya maisha.
Sina kibarua tena, wala sina pesa za kusaza. Wenye pesa zao wanakutunza, bila shaka sasa unajinoma. Bila shaka, unakula unachotaka, unalala kwa starehe, hutembei kwa miguu tena. Huenda umesahau sasa umasikini wa kwetu wa kula ugali wa sembe, viazi, kande na matembele. Siamini kama Sabrina unachota maji mtoni tena kama ulivyokuwa ukifanya huku kwetu. Naamini kila kitu kwako kipo katika mstari, na maisha yako murua. Hongera sana Sabrina kipenzi changu niliyekupenda kwa dhati.
Mimi peke yangu ningeweza kujizila nikaendelea kuganga na maisha niwezavyo lakini umemsahau na mwanetu Marcelina. Binti yetu angali mdogo pato la ujana wetu, kwa hakika kumlea peke yangu sitaweza. Mwanetu Marcelina ni damu yetu sote lakini umembwaga umeenda. Nimekuwa baba yake na mama yake. Akilia ni kazi yangu kumbembeleza, hakika nimekuwa yaya mzoefu sasa. Nilipokupigia simu na kukusihi urudi tumlee mwanetu ulinitukana matusi ya nguoni. Leo naandika barua hii ili nikusalimu tu. Naomba pokea salamu zangu Sabrina. Utakapo kujua hali yangu, si shwari hata kiduchu. Nimekuwa mtu wa kujiinamia chini na kudondosha machozi kwaajili yako. Sikukukosea lolote kwa hakika, umasikini wangu na maisha duni vimekufanya uone sina maana kwako. Asante Sabrina, asante sana.
Nikikupigia simu hupokei, na wakati mwingine unaikata kwa jeuri. Nikituma ujumbe haujibiwi, basi nakuandikia barua hii ili walau nikusalimu. Natamani salamu hizi zikufikie. Kama na salamu hizi hazitakufikia au hutaisoma barua hii ya salamu basi walau hata asome mtu mwingine yeyote kisha akufikishie salamu walau ujue tu kuwa mimi Baba Marcelina nakusalimu.
Nakukumbuka sana Sabrina, japo umeona sina thamani, umenitupa mimi na mwanangu Marcelina kisa pesa za wenyenazo. Nilikupenda nakukujali sana, lakini sasa penzi letu limetumbukia nyongo. Naomba pokea salamu zangu Sabrina Nakutakia maisha mema, nami naendelea kuganga kwa uwezo wa Jalali. Panapo majaaliwa tutaonana.
____________TAMA TAMA TAMATINI______________

Post a Comment

0 Comments