Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MAMA SEMA NA MWANAO BADO NA MAPEMA



HAPO kale ilikuwapo familia moja ya kimasikini iliyojumuisha baba, mama na binti yao. Pamoja na kushindwa kukidhi baadhi ya mahitaji ya msingi, baba wa alijikusuru kwa kadiri ya hali, kuhakikisha binti yake anapata mahitaji ya msingi shuleni. Ndoto ya baba ilikuwa ni kuhakikisha siku moja binti yake anakuwa daktari bingwa duniani. Mahaba yake kwa bintiye hayakuwa na mfanowe.

Yalipotoka matokeo ya kidato cha sita, binti alifaulu kwa alama za juu kuliko mwanafunzi yeyote shuleni kwao. Kwa furaha, bila kujali hali yake ya kiuchumi, baba alimwambia binti yake, "Ninajivunia sana kuwa baba yako. Kwa ufaulu huu, niambie chochote utakacho nikununulie."

Binti akajibu, "Ahsante baba, ninaomba uninunulie zawadi ya kompyuta niliyokuonesha siku ile dukani ili inirahisishie masomo. Inauzwa shilingi laki tatu."

Uso wa baba ulijawa furaha ilhali moyoni akiteketea kwa huzuni. Alijua fika hana uwezo wa kununua kompyuta kwa gharama ile. Lakini aliahidi kumnunulia.

Katika hali ya kushangaza, siku iliyofuata baba alirudi nyumbani akiwa na kompyuta mkononi - alimnunulia binti yake kama alivyoahidi. Mama alimfikia mumewe na kumuuliza, "Mume wangu, ni wapi umepata fedha ya kununulia kompyuta hiyo?"

Baba alijibu, "Leo nilitoa damu yangu na kuiuza, nikaongezea na akiba kidogo niliyokuwa nayo ndipo nikapata kiasi kilichohitajika kununulia kompyuta hiyo. Sikutaka kumkwamisha binti yetu kufikia malengo yake na kutimiza ndoto zetu."

Maisha yakaendelea - na kwa bahati, binti alifanikiwa kuingia chuo. Baba aliendelea kupambana kwa machozi, jasho na damu ili kumlipia gharama zote za masomo. Ilipofika mwaka wa mwisho wa masomo, ilihitajika takribani shilingi milioni mbili ili kukamilisha gharama za masomo. Hofu na simanzi vikatanda ndani ya nyumba kwa kukosekana fedha hizo. Dalili za kukwama masomo ya binti zilianza kujionesha waziwazi.

Lakini kama ilivyokuwa awali, katika hali ya kushangaza, ndani ya mwezi mmoja tu tangu kuhitajika kufanya malipo, baba alifanikiwa kupata pesa na kulipia gharama zote. Mshituko ulimfanya tena mke kumuuliza mumewe, "Umepata wapi fedha zote hizo mume wangu? Usije kuwa umeanza kujiingiza kwenye matendo mabaya ili kujipatia fedha za haraka!"

Baba alijibu, "Hapana mke wangu, siwezi kujiingiza kwenye vitendo vibaya. Baada ya kuona hatuna uwezo wa kupata fedha hizo, niliamua kuuza figo yangu moja - na pesa nilizopata ndizo nimemlipia binti yetu ili tutimize ndoto zetu. Lakini, AlaAla usimweleze haya, atajisikia vibaya sana."

Ilikuwa ni furaha kwa binti na simanzi kwa mama. Masomo yaliendelea bila mkwamo mwingine. Baada ya masiku mengi kukatika, hatimaye ilifika siku ya mahfali ya binti. Familia ilijaa furaha isiyo kifani. Siku hiyo, baba na mama waliandaa maakuli nyumbani, wakimsubiri binti yao kwa mara ya kwanza akiingia nyumbani kama daktari.

Lakini,

Siku hiyo binti alirudishwa nyumbani akiwa maiti. Aliamua kujiua kwa sababu alisalitiwa kimapenzi na mwanamume aliyempenda sana 😭.

Binti ameshindwa kuthamini na kuyatunza maisha yake kwa ajili ya kutimiza ndoto na furaha za wampendao (baba na mama), badala yake ameharibu malengo yake na kujiua kwa ajili ya yule mpuuzi mmoja (mwanamume) asiyejua dhiki walizopitia wazazi wake.

Mama sema na mwanao bado na mapema.

Post a Comment

0 Comments