Header Ads Widget

Responsive Advertisement

FUKARA WA FIKRA




1998!!!!!
Lazima na vilevile ni haki yangu kuushangaa mwaka huo. Naam! Mwaka huo ulikuwa na mambo kadha Simulizi fupi: Fukara wa fikra
wa kadha katika kumbukumbu zangu lakini mojawapo kati ya hizo, ilikuwa ni moja ambayo ilizidi uwezo na kunifanya nikuandikie kipande hiki kifupi cha simulizi. Miaka kumi nyuma kabla ya mwaka huo, nilikuwa nikiyaishi maisha yenye amani na furaha tele mno moyoni mwangu. Uso wangu ulitawaliwa na tabasamu kwa kiasi kikubwa kuliko huzuni. Sikuwa na mali lakini kwa kazi ya kulima mtama, ilininufaisha mno. Niliishi na familia yangu iliyokamilika. Nadhani nikisema iliyokamilika hapana shaka naeleweka. Mke wangu Medrina, alinizalia watoto watatu. Wawili wa kike na aliyesalia wa kiume. Nilimpenda naye alinipenda pia. Hakuwabagua wazazi wangu wala ndugu zangu. Alikuwa ni mwanamke asiyekuwa na mapungufu makubwa ndani ya ndoa yetu. Kila siku mama na baba yangu, hawakuchoka kutuhusia kuishi maisha ya namna ile ili kukwepa ugomvi na kuishi pamoja kwa muda mrefu. Busara zao nilizihamishia mpaka kwa wadogo zangu na wanangu pia.
“Wanangu amani ikishapotea kuirudisha ni vigumu. Fahamu zenu zitambue ya kuwa amani haijengwi kupitia elimu ya shuleni, bali ni moyo wa mtu wenye utulivu. Unyang’anyi, ugomvi,tamaa wivu, siasa na udini. Huwa kichocheo kikubwa cha kuporomosha misingi ya amani. Wanangu bila amani hata kuyafuata ya MUNGU itakuwa ni vigumu. Yaogopeni machafuko ya aina yoyote. Ijenge mioyo yenu katika msingi wa uoga.” Nayakumbuka maneno ya baba siku moja baada ya chakula cha usiku. Msomaji, pamoja na mengi ambayo sijayaandika hapa kutoka katika kinywa cha baba yangu, nilijisahau. Moyo wangu ukawashwa moto wa tamaa. Nikajikuta nikiitowesha furaha ya familia yangu. Furaha ikageuka vilio kila kono ya family yangu. Umri wangu wa miaka thelathini na tisa, bado sikuwa na fikra chanya. Nilikuwa na fikra hasi. Au niseme nilikuwa ‘FUKARA WA FIKRA’ nikakifurahia kilio cha familia yangu kama nilivyoifurahia furaha yao hapo kabla. Nikabadilika na kuwa zaidi ya mnyama mkali aliye na njaa kali. Ukawa mwaka wa mabadiliko yangu. Ndugu na majirani wakaomboleza kila mara nami kulia machozi ya kebehi mbele yao. Ama kwa hakika kumbukumbu za mwanadamu hupotea kulingana na mabadiliko ya hali ya kipato chake.
“Vikwazo visikutoe katika lengo, bali iwe chanzo cha wewe kuyafanikisha malengo yako.”
Katika kuyafurahia maisha yangu ya fedha nikasahau kama huwa kuna kifo. Nikaburudika na wanawake wa aina mbalimbali na kujenga marafiki na wapya tena walio na uwezo kama mimi. Nikawasahau wale niliokuwa nao katika ufukara. Nikamiliki mabasi, malori, viwanda vidogovidogo pamoja na migodi ya madini mkoani Shinyanga. Kweli fedha ikakubali lakini ni HARAMU. Upataji wake haukuwa ule aupendezwao Mwenyezi Mungu. Sikuogopa kumwaga damu za ndugu zangu. Haikutosha nikahamia mpaka damu za nje. MIMI NI FUKARA WA FIKRA!!!! Nikupe stori kamili ilikuaje hadi nikageuka muuaji pasipo uoga.
Ni siku moja tu wala siyo mbili iliyoibadilisha roho yangu. Kutoka katika wema na kuingia katika ubaya. Ni katika kuhangaikia soko la mazao yangu, ndipo nilikutana na Bwana mmoja kwa jina Jumunchi huko mpakani mwa Tanzani na Uganda. Sehemu inaitwa Mutukula. Kwa wenyeji wa mkoa wa Kagera watakuwa wakiifahamu. Jumunchi alikuwa na lori lake likiwa limesheheni kahawa. Alionekana ni mtu mwenye uwezo. Akafanikiwa kunishawishi tuchanganye mzigo ili nipate fedha nzuri kutokana na kwamba yeye alikuwa akiuza kwa bei ya juu kutokana na kuwa na mzigo mkubwa. Sikutia shaka nikakubali. Hakuwa muongo. Ni kweli nilifaidika. Urafiki wetu ukaanza kustawi vyema tangu siku hiyo. Miezi miwili tangu tufahamiane, akanipa siri ya mafanikio yake. Ndugu yangu nakuhasa kwa moyo wangu wote nikiwa na akili timamu, wewe unayesoma na pia hakuna ubaya kama utamsimulia na mwingine hili. “Kama unakula na kulala vyema mshukuru MUNGU hata kama maisha yako si ya gharama. Ipo siku utayafaidi hata kama si duniani. Jifunze kuwa mstamimilifu.” Siri yake ilikuwa na mengi mazito mno yaliyonipasua moyo wangu kwa kushtuka. Lakini sijui ilikuaje nikajikuta nami nipo mbele yam zee mmoja mkoani Tanga akiwa na hirizi nyingi sana katika viungo vya mwili wake. Akanipigia ramli. Akanieleza mengi ambayo hata sikuyatarajia. Lakini mwisho nikakubaliana na masharti yake. Nikahadahika kuliko nilivyowahi kuhadaika hapo kabla. Nikatoa kuku mwekundu na damu yake ikapakwa katika chale nilizochanjwa. Nilipotoka hapo, baada ya mwezi mmoja mafanikio yakaanza kunielemea kwa kasi. Nikanyanyuka kiuchumi pasipo kutarajia. Maisha nd’o haya! Yalikuwa wapi siku zote hizo? Nilishangaa na kujiuliza kwa wakati mmoja. Nikafaidi starehe za ulimwengu vile ambavyo hata akili yangu ilistaajabu mno pengine kuliko nilivyowahi kustaajabu. Miezi sita ya mafanikio yangu, moja ikaungua moto na kusababisha hasara kwa wapangaji wangu ila nnachoshukuru hakuna aliyedhurika. Chanzo cha moto ikasemekana ni umeme. Hilo likapita na baada ya siku mbili, basi likapata ajali lakini nalo pia halikusababisha vifo. Nikakumbuka niliambiwa na mganga kama nikiona mambo yangu yanakwenda mrama basi nisisite kumrudia. Nikaifunga safari ya kutoka Arusha hadi Tanga. Nikamkuta mzee huyo. Akaungalia mwendo wangu kupitia ramli ndipo akanishtua moyo wangu.
“Mizimu inataka damu ili iendelee kukunyooshea mambo yako” ndicho alichonambia mganga. Damu! Si kwamba nilichoshangaa ni kutoa dam utu, hapana. Nilitakiwa kutoa damu ya mwanangu wa kwanza. Naweza kuthubutu kusema sijui ilikuaje hadi nikajikuta nimeshafika Arusha bila kutegemea. Ila n’nachokumbuka ni kwamba sikufungua kinywa changu kumuaga mganga. Hiyo ilimaanisha sikukubaliana na kile alichonieleza mganga. Usiku mzima sikulala. Niliota njozi lukuki zisizoeleweka na zenye kutisha mno. Mwili wangu uliloa chapachapa kutoka na jasho lililokuwa likinitiririka. Asubuhi na mapema kabla sijaamka kitandani, nikapigiwa simu kupewa taarifa za mabasi yangu kusimamishwa safari zake kwa muda usiojulikana kutokana na ajali. Mh! Baada ya starehe ikawa karaha. Haikuishia hapo tu, nilikuwa nimeanza kupandisha ghorofa. Nalo wizara ikalisimamisha kwa madai ya kuwa pale ni katika bonde ilihali ni wao walioniruhusu hapo kabla. Nilikaa na kutafakari maandamano yale ya matatizo, nikaona isiwe tabu, moyo wangu ukaridhia kumtoa mwanangu. Nikarudi kwa mganga naye akanipatia kichupa kidogo na kunielekeza sehemu ambayo ilikuwa na kichuguu katika shamba lake. Nikafika na kusimama juu yake kisha nikakifungua kichupa kile kwa maelekezo yam ganga kwamba niumwage unga ule kwenye kiganja changu kisha niupulize huku nikilitaja jina la mwanangu. Hakika nawaambia nyie walimwengu ambao hamjapata kuyapitia haya. Jiwekeni mbali na ushirikina. Una mengi mno ya kusikitisha. Baada ya kuupuliza unga ule nikasikia kishindo kikubwa nyuma yangu. Nikageuka. Hamali!! Alikuwa ni mwanangu. Nikataka kuteremka chini lakini haikuwezekana miguu ilikuwa mizito. Nikabaki kuyashuhudia mateso ya mwanangu ambaye alikuwa amebakisha miezi miwili kuhitimu kidato cha nne. Alikuwa akinitazama kwa huruma huku macho yake yakitoa damu badala ya machozi. Ni kitendo kilichodumu kwa takribani nusu saa ndipo akayeyuka nami miguu ikawa tayari kuniruhusu kutembea. Nikateremka na kutaka kupasogelea pale alipokuwa mwanangu kabla ya kutoweka lakini nilishangaa nia haikutimia. Haikuwezekana mimi kupakanyaga. Nikarudi kwa mganga ambapo alinipongeza kwa ujasiri wangu kuifurahisha mizimu. Akanipatia dawa za kuoga na kuniruhusu kurejea nyumbani kwangu huku kinywa chake kikiniahidi kuyashuhudia mafanikio makubwa zaidi yay ale ya awali. Nikarejea nyumbani. Nikakaribishwa na kilio cha mke wangu akigalagala chini. Alikuwa katika maumivu makubwa mno kuondokewa na mwanaye. Nikajumuika naye kinafki katika kulia. Taratibu za msiba zikaendelea na hatimaye mwanangu tukamzika.
**
Siku na hatimaye miezi ikazidi kusogea. Yale yote aliyoniahidi mganga yakaendelea kujidhihirisha. Nikaruhusiwa kuendelea na ujenzi, mabasi yangu yakaendelea na kazi kama kawaida. Nikazidi kutunisha akaunti zangu za benki. Shida nikazisahau katika maisha yangu. Lakini vilio havikuwa vimekoma. Familia yangu nikaiteketeza kila ilipohitajika damu kwa mizimu. Wakabaki wachache. Nao wakaniweka vikao na bila kunifumbia macho wakanitenga. Sikujali hilo, nikajenga urafiki nje kupitia fedha zangu. Fedha zangu wakazifaidi watu wa nje. Nikabaki na mke wangu baada ya kuwaondoa wanangu. Naye nikamgeuza majani ya miti. Kufuata upepo unapoelekea.
“Mizimu inahitaji damu nyingi sana ila hii si kwa ndugu zako, ni nje kabisa” nilishabadilika roho mno. Kuwa tayari kufanya lolote ili kufanikisha mambo yangu. Hivyo maneno hayo ya mganga, wala hayakunitia hofu moyoni mwangu. Akanipatia maji katika vichupa vinne. Akaniambia nilitakiwa kumwaga maji yale katika pande nne kila moja na chupa yake. Pande nne za dunia ikiwa ni usiku wa manane njia panda. Ndugu zangu msiawaone wanadamu wenzetu mchana katika mwangaza, macho yao yakiashiria huruma na ndimi zao kutamka mema. Wapo wengi mno katika hao usiku ni zaidi ya wanayama wakali wawapo na njaa. Wanaongea machafu nyakati za usiku wa manane. Wanayafanya machafu yasiyoweza kuaminika kirahisi kwa ambao hawajawahi kuyasikia ama wenye mioyo myepesi. Wanayatenda ya kustaajabisha mno. Yenye kuumiza. Yalitayo maumivu katika mioyo ya wengi mpaka kifo.
Usiku wa manane, kama nilivyoambiwa na mganga. Niliamka na kutoka nje. Nikatembea nikiwa uchi kama nilivyozaliwa hadi njia panda. Baridi ilikuwa kali lakini wala haikuniumiza kichwa changu. Nikayamwaga pembe zote kama ilivyotakiwa kisha nikarejea nyumbani. Asubuhi kulipopambazuka, nikaendelea na kazi zangu za hapa na pale lakini ndani ya akili yangu, sikukisahau kile nilichokitenda usiku wa jana yake.
Siku mbili mbele!
Sikutaraji kama kingetokea kikubwa kama kile. Jambo la ajabu ambalo hata nami liliuumiza moyo wangu. Ni wengi niliowatoa machozi. Kama nilivyoyamwaga maji yale katika pembe nne, ndivyo na vilio jinsi vilisikika. Moja ya basi langu lililokuwa likifanya safari zake kutoka Arusha kuelekea mkoani Kagera, lilikuwa limepata ajali mbaya na kusababisha vifo vya abiri wote pamoja na dreva. Haikuishia hapo, mgodi wangu uliokuwa mkoani Kahama, nao ulikuwa umefukia watu zaidi ya ishirini. Basi niseme hakuna ambaye hakutoa chozi kati ajali zile. Lawama zikwa lukuki juu yangu. Kila nilikopita macho mabaya yalinitazama mimi lakini mali zangu zilizidi kuongezeka zaidi na zaidi. Lakini msomaji wangu heri ukose mali upate watu na kauli njema. Miezi sita tangu ajali hizo, nikaanza kuugua magonjwa ambayo hata nilipoenda hospitali hayakuonekana. Nikaenda kwa mnganga wangu naye nikakuta akiumwa ugonjwa huohuo kama wa kwangu. Hakuwa akiongea. Afya yangu ikazidi kuzorota kadri siku zilivyosogea. Nikaonekana kama mti mkavu. Kama ni kuchoka basi mimi ilikuwa ni zidi ya maelezo. Mali zangu zikapukutika kama maua yaliyokauka. Nikawa mtu wa kuota ndoto za ajabu. Kila nilipolala nilijihisi nimo ndani ya KISIWA CHA DAMU. Usingizi haukupatikana kila nilipojihisi ndani ya KISIWA CHA DAMU. Heri kukosa fedha lakini si usingizi. Kifo kikanikaribia mno. Nikachukua kalamu na karatasi na kuandika haya ili wengi wajifunze kupitia mimi. Sikupata faida zaidi ya kuitekteza familia yangu na kuitafuta dhambi kwasababu ya fedha. Ili kuonyesha yeye ni zaidi ya vyote, MUNGU hakuniondoa duniani ili azidi kunipitisha katika nyakati za kujifunza. Sasa mimi ni mzee lakini ombaomba katika mkoa wa Arusha.
Mwisho!!!!
“Ukaribu na starehe pasipo akiba ilihali shida zipo jirani yetu, ni ufukara wa fikra. Hakuna tuzo za kubadilisha wanaume au wanawake. Umri unasogea wala si wa kurudi nyuma. Zipo sababu nyingi za kupenda lakini yupo umpendaye kwa dhati kuliko wote, onyesha kumjali,kumthamini ili ajione yeye ndiye chaguo la moyo wako ili siku moja nafsi yake imkumbushe.”
MWISHO

Post a Comment

0 Comments