Header Ads Widget

Responsive Advertisement

DAKTARI UMEUA FAMILIA YANGU



Jackline ni jina ambalo tulikua tumepanga kumuita mtoto wetu, ingawa tulikua bado hatujajua jinsia yake lakini moyoni nilijua atakua mtoto wa kike, hata mke wangu alipong’angania tutafute jina la mtoto wa kiume kwani yeye alitaka sana mtoto wetu wa kwanza awe wa kiume nilikataa kabisakabisa na hata alipopendekeza Kelvin hata sikujali, nilimuambia mtoto wetu ni wakike hivyo sihitaji kabisa majina ya kiume.

Hakuna kitu ambacho nilikipenda kama kuongozana na mke wengu kiliniki, yaani ile hali ya kukutana na wakina Mama wajawazito wakinishangaa namna nilivyokua nikimbebea pochi mke wangu ilinipa raha sana, zaidi nilikua nikimfurahisha mke wangu kwani alijihisi kama Malaika, alideka na alijua kudeka kweli, akiwa anatema mate mara kwa mara nilibeba kikopo chake cha kutemea mate.

Sijui kwanini lakini nilijisikia raha kuwa naye na kwa mtoto wetu wa kwanza nilitaka nisiachwe nyuma wakati mke wangu akimuambia mwenetu kuwa mimba yake ilimsumbua, nilitaka itusumbue wote. Lakini zaidi ya kudeka kwa mke wangu na kunitumatuma kila mara mimba yetu haikusumbua kabisa, mpaka anafika siku ya kujifungua kila kitu kilikua sawa.

Ningeweza kumpeleka kujifungulia zahanati ya kawaida lakini sikutaka, sijui kwanini nilikua na wasiwasi na kutaka kumpeleka Hospitali kubwa. Uchungu ulimshika saa kumi na moja asubuhi, hivyo nilipeleka Hospialini ambapo alipewa kitanda kwa ajili ya kupumzika, alipimwa na kuambiwa kuwa mtoto kaka vizuri na njia ilikua vizuri, nilimshukuru Mungu na kuondoka.

Nilirudi kazini kuomba ruhusa kwani nilitaka kuwepo wakati anajifungua, baada ya kuomba ruhusa nilirudi akisubiria kujifungua. Lakini haikua rahisi kihivyo, mpaka saa mbili za usiku mke wangu alikua bado hajajifungua, alikua anapata uchungu unaisha unarudi unaisha unarudi. Daktari alishapita na kila wakati waliniamba kila kitu kiko sawa na atajifungua salama tu.

Nilikua na wasiwasi sana kwani alikua anaumia, Mama yangu alikua ndani na kila wakati alitoka na kuniambia bado, bado mpaka nikachoka. Kama saa sita usiku hivi Mama alitoka na kuniambia hali ya mke wangu imebaidlika ghafla, alipata uchungu lakini ameshindwa kusukuma mtoto, tuliongea na nesi ili kumtafuta Daktari ili afanyiwe upasuaji.

Daktari alikuja na kuanza kumtukana mke wangu kwamba anajidekeza tu avumilie kila kitu kitakua sawa, kisha aliondoka. Nilitaka kumfauta hata nimtukane au nimtandika makofi lakini nilivumilia nikijua kama nikimtibua nitakua na mharibia mke wangu, nilivumilia na kwenda kuongea naye kistaarabu. Jibu lake lilikua ile ni hali ya kawaida wapo wengi tu wanasubiria kujifungua lakini hawalalamiki kama mke wangu.

Aliondoka na kutuacha, lakini ilipofika saa nane usiku hali ilikua mbaya, niliingia katika chumba alichokua mke wangu, alikua amechoka, hata kulia tena hawezi. Nilimuona nesi nayeye ana wasiwasi, nikimuuliza nini alichanganyikiwa hajui chakufanya, alijaribu kumpigia simu Daktari lakini alikua hapokei, mke wangu alikua katika maumivu makali sana.

Ghafla alianza kupiga kelele, nesi aliniambia nitoke lakini nilishindwa, nilimshika mke wangu mkono na kumuambia kila kitu kitakua sawa, sikua na uhakika na maneno yangu lakini nililazimika nimuambie vile kumpa moyo. Daktari bado alikua hapokei simu yake, nilimuambia nesi kama haiwezekani basi nimpeleke sehemu nyingine, hata yeye alichanganyikiwa, ila aliniamba kwa hali aliyokua nayo aisingefika popote.

Ghafla damu zilinza kumtoka sehemu za siri, sikujua ni nini, nilihisi labda ni chupa la uzazi ndiyo hutoa damu, lakini macho ya Mama yangu yalinifanya nihisi kitu kibaya, bado mke wangu alikua akijaribu kusukuma mtoto. Aliishiwa nguvu aliniangalia na nakumbuka maneno yake ya miwsho ilikua ni “Mume wangu waambie wanipasue wamtoe mtoto, mimi sitapona!” Aliongea kwa kukatatamaa lakini akimaanisha.

Wakati huo Daktari alipokea simu, waliongea na nesi kidogo na ndipo niliona mke wangu akiandaliwa kwaajili ya upasuaji. Kama dakika kumi hivi Daktari alikuja na kuingiakatika chumba cha upasuaji. Walikaa huko kama nusu saa tu na kutoka, nilimfuata kumuuliza mke wangu anaendeleaje lakini hakuonyesha kujali.

Aliniambia muulize nesi kisha akaendelea na safari zake, nilitaka kuendelea kumfuata lakini Mama na watu wengine waliokua pale walinizuia. Nilirudi kusubiri nesi atoke na kama dakika kumi baadaye alitoka mtu mwingine, hakuwa nesi aliyemuandaa mke wangu lakini alionekana kukata tamaa, nilimuuliza kuna nini, alitingisha kichwa kusikitika.

“Mke wangu!” Nilipiga kelele alionekana kama kukubali kitu. “Vipi mtoto..” Mama aliuliza na kabla hajajibu alitokea yule nesi ambaye alipomuona Mama tu machozi yalianza kumtoka bila kulia. Mama alimfuata na hapo ndipo alipomuambia kuwa, mtoto alizaliwa tayari ameshakufa na Mke wangu alifariki kwenye kitanda cha upasuaji.

Nilishindwa kuvumilia, niliingia bila ruhusa kwenye kile chumba, walikua wameshawafunika na hata sikuwa na nguvu ya kutembea nilidondoka na kupoteza fahamu. Masaa mawili baadaye nilizinduka nikiwa nimelazwa kitandani, maumivu ya moyo niliyokua nayo yalikua ni makubwa sana. Mama Hakuondoka pembeni yangu, nikama alijua nitafanya kitu kibaya.

Hasira zangu zilikua kwa yule Daktari kwani nilijua kuwa ndiyo sababu ya kifo cha mke na mwanangu. Niliruhusiwa kutoka na baada ya siku mbili nilimzika mke wangu na Mwanangu kipenzi. Kichwa bado kilikua kinauma na nilitaka kuonana na yule Daktari, sijui kwanini sikujua hata ningemfanya nini lakini nilitaka kumuona, wiki moja baadaye nilienda katika ile Hospitali.

Nilimuona yule Daktari lakini kwake ni kama hakukua na kitu kilichotokea, aliendelea na maisha yake na hata hakunikumbuka. Nilijaribu kumkumbusha lakini kwa dharau alinijibu, hapa mbona wanakufa wengi tu nikitaka kukumbuka kila maiti si nitakua kama naishi Mochwari! Nilipatwa na hasira nilitamani kumvamia na kumpiga lakini nilishindwa.

Kila nilipojaribu kumsogelea sura ya mke wangu akitabasamu ilinijia, ni kama alikua annionya nisifanye chochote, bila kujijua nilikuta naondoka natoka katika ile Hospitali. Ni mwaka mmoja sasa umepita tangu mke wangu kipenzi na mwanangu Jackline (Alikua wakike kama nilivyotabiri) kuniacha lakini naona ni kama jana maumivu niliyonao hayaelezeki.

Pumzika Kwa Amani Mke Wangu, Pumzika Kwa Amani Mama Jackline, Pumzika Kwa Amani Mwanangu Jackline.

Post a Comment

0 Comments