Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MAJAALIWA - 1



Simulizi : Majaaliwa
Sehemu Ya Kwanza (1)

ABDULRAHIM Kasongo alipojaribu kuugusa mlango na kuusukuma, mlango ulifunguka kwa ndani moja kwa moja bila ya kizuizi. Kimya na giza totoro la ndani ya nyumba hiyo lililomkaribisha lilimfanya atilie shaka tendo lake la kufika hapo kama ni sawa sawa. Alijaribu tena kutoa sauti iliyojaa wasiwasi na kutamka: "hodi" kwa mara ya tano.
Hapakuwa na jawabu zaidi ya “swiing, swing” za mlango alioufungua. Alivuta hatua chache na kuingia ndani ya nyumba hiyo sehemu alipodhania kuwa ni
sebuleni. Alisimama tuli na kusiklliza,hisia za masikio yake zilifanya kazi ya ziada kusikiliza kwa matumaini ya kusikia sauti yeyote ambayo ingemfariji, lakini hakusikia kitu chochote, kwani hata ule mlango uliokuwa unayumba nao pia ulikuwa umekwisha tulia. Alijitahidi kufungua zaidi macho yake kwa kuyakodoa lakini bado hakuna alichoweza kukiona. Alijiwa na faharnu huenda ameingia nyumba ambayo hakukusudia, na kama ndivyo, basi jambo aliloitiwa halikuwa la kweli.
Aligeuka taratibu na kuelekea mlangoni alipoingilia, ambapo kidogo palikuwa na mwangaza wa taa zilizokuwa zinawaka barabarani karibu na nyumba hiyo. Alianza kuvuta hatua, ndipo ghafla aliposikia sauti ya mtu, sauti ambayo aliifananisha na sauti aliyowahi kuisikia siku za karibuni. Sauti ambayo ilivunja kimya kile kilichokuwepo kwa kusema: "Oh, hoo! Dokta karibu, samahani sana!"
Mara taa iliwashwa na kando ya sebule hiyo, karibu na mlango unaotokezea kwenye ukumbi mwembarnba uelekeao kwenye vyumba vya flati hiyo, alisimarna mwanaume mwenye sauti hiyo akiwa na tabasamu kubwa usoni mwake.
Aliendelea kusema: ''karibu sana Dokta Imu, nifuate, mgonjwa mwenyewe yuko huku!"
Dokta lmu ambaye ndiye Abdulrahim Kasongo alirudisha pumzi kwa nguvu, aligeka tena na kumfuata yule mwanamme. Vl/aliingia ndani ya chumba kimoja kati ya vyumba vitatu vilivyokuwa katika flati hiyo.
Ndani ya chumba hicho kulikuwa na kitanda kimoja tu kikubwa cha futi sita kwa tano, ambacho juu yake alilala msichana ambaye hali yake ilikuwa mbaya sana. Alikuwa akilalama kwa miguno na kuonekana dhahiri kuwa ana mautnivu makali. Dokta lmu alikwenda karibu na kitanda hicho, akakaa ukingoni mwa kitanda akatua mfuko wake aliokuwa nao chini juu ya sakafu, akaufungua na kutoa vifaa vyake na kuanza kuchunguza.
Wakati Dokta Imu anafanya hivyo, yule mwanamme aliyemkaribisha alisimama kando kimya akimuangalia Dokta anafanya nini.
Dokta lmu baada ya uchunguzi wake alimgeukia yule mwanaume na kusema."Bwanaa ...!" aligwaya kwa vile alitaka kumuita kwa jina lake ambalo hajafahamishwa. Yule mwanamme alitambua hilo naye alimfariji Dokta lmu kwa kutamka: "Dallas, ninaitwa Dallas, nawe niite Dallas tu ".
"Ahsante kwa kukufahamu Bwana Dallas. Ninalotaka kusema ,ni kwamba huyu msichana yuko katika hali mbaya sana, kwa hiyo itabidi aharakishwe hospitali haraka iwezekanavyo! Sijui wewe ni nani wake bwana Dallas?"
Dallas alitoa kicheko kifupi cha dharau na kumjibu: "Mimi ni kaka yake huyu msichana."
" Vema Bwana Dallas. Kwa hiyo tufanye haraka, maana huyu msichana ametokwa na damu nyingi sana...nii...kesi ya "abortion" hii...ametoa mimba!"
Dallas hakuonekana kujali, kuguta wala kuwa na wasiwasi. Alimuangalia Dokta Imu kwa kumtulizia macho, kisha ghafla akatazama pembeni na kusema: "Ndio ninafahamu Dokta Imu kuwa ni suala na tatizo la utoaji mimba...lakini na wewe si ulikuwa unalifahamu hilo?"
"Sikuelewi bwana Dallas!"
Dallas alitoa kicheko kikubwa kama vile mwehu, kisha kasita ghafla.
"Dokta Imu usijaribu kujifanya umjanja kijana. Wewe ndiye uliyempa dawa za kutoa mimba Mwanamtama, wewe ndiye asubuhi ya leo uliyejaribu kumfanyia ulivyoweza kumfanyia kuitoa mimba yake na yako. Wewe si ndiye mvulana wa Mwanamtama? Baada ya kumpa mimba ukajaribu kumruka na kumlazimisha kuitoa kwa kumhofia msichana wako mwingine Zainab?"
Dokta lmu alitamani hali ile iwe ni ndoto mbaya ambayo ingetoweka mara anapogutuka. Lakini haikuwa hivyo hali ile ilikuwa halisi. Jasho jembamba lilimtoka asijue la kufanya. Mwishowe
alijikaza na kusema: "Vyovyote vile unavyofikiri na kusema fikiri na sema, akili na mdomo ni vyako mwenyewe, lakini ninaloomba sasa hivi huyu msichana aharakishwe hospitali ili maisha yake yaweze kuokolewa."
Dokta lmu alisema haya kujaribu kusahau ubinafsi wake na kujali udaktari wake na maisha ya binti yule. Lakini kwa Dallas haikuwa hivyo, aliruka na kusema: “Maisha yake gani unayoyajali wewe bwanaa? Ungekuwa unajali maisha yake ungemtia mimba kisha ukamruka?! Maisha unayoyajali ni ya Zainab na siyo ya Mwanamtama . . . usijidai bure bwana mdogo..."
Dokta lmu alighadhibika, lakini hakujua afanye nini sababu kwanza yumo ndani ya nyumba ambayonni mara yake ya kwanza katika maisha yake kufika. Pili huyu mtu huyu Dallas kwa vyoyote vile si mtu mzuri,ukiachia mbali sura yake nzuri na umbile lake kubwa la kupendeza,pia anaonekana ni mwenye afya na nguvu. Dokta lmu aliamua kufanya awezavyo kufanya. Alisimama kutoka alipokuwa amekaa kwenye ufumbati wa kitanda na kumwambia Dallas. "Basi mimi ninamchukuwa huyu msichana na kumpeleka hospitali, nitampeleka kwa gari yangu iliyo hapo nje. Ninachokuomba tusaidiane kumbeba na kwenda kumuingiza garini."
Dallas aliinamisha kichwa chake na kuangalia chini kama anayefikiria kitu fulani, kisha akasema. "Ahaa, unaonekana unajali sasa kwa hizi dakika za mwisho wa maisha ya Mwanamtama!" Kwa wakati huu yule msichana alikuwa hatoi tena sauti, bali alikuwa anahema kwa taabu pale alipokuwa amelala chali kitandani. Dallas alivuta hatua kuelekea mlango wa chumba kile huku akisema kumwambia Dokta lmu: "Sawa basi hebu nisubiri nitakusaidia sasa hivi."
Dallas alitoka nje ya chumba na kwa mastaajabu yake Dokta lmu, alisikia mlango wa chumba kile alichokuwemo yeye na yule msichana mgonjwa pale kitandani Ukifungwa kwa ufunguo kwa nje. Alirukia kitasa cha mlango na kujaribu kuufungua lakini alikuwa amekwishachelewa,mlango ulikuwa umefungwa tayari.
Aliushika mkono wa kitasa na kuuzungusha kwa kuusuka suka, lakini wapi. Kitasa cha vibano vitatu kilikwisha bana barabara.
Dokta lmu alijihisi moyo unamwenda mbio. Alitulia kidogo akageuka na kuegemea mlango kwa hali ya kukata tamaa huku anamuangalia msichana aliyejulishwa kuwa jina lake ni Mwanamtama pale alipokuwa kitandani. Alizidi kuchanganyikiwa alipoona hali ya msichana yule inabadilika na kuwa mbaya zaidi, kwa kuanza kukoroma kiajabu ajabu.
Alimwendea pale kitandani na kabla hajawahi kufanya chochote, alisikia Mwanamtama anavuta pumzi za mwisho. Mara hiyo hiyo akakata roho.
Dokta lmu alikaa juu ya mfumbati wa kitanda na kujishika tama kwa mikono yake yote miwili. Hakujua afanye nini na wala akili zake hazikuwa na uwezo wa kufikiri kwa wakati huo.
Hakujua alibaki katika hali hiyo ya kujiinamia kwa muda gani, lakini ghafla aligutushwa na sauti ya mlango uliofunguliwa kwa nguvu. Alinyanyua uso wake na kuangalia mlangoni. AlimuonaDallas akiingia nyuma yake akifuatiwa na watu wawili wanaume. Dallas alienda moja kwa moja mpaka karibu na kitanda. Alinyanyua mkono wa maiti ya Mwanamtama akajaribu kuhisi mzunguko wa damu ya msichana yule kwa kubonyeza vidole vyake kwenye mishipa inayounganisha mkono na kiganja kwa muda mfupi,kisha akaurudisha mkono ule polepole huku akimtazama Dokta lmu usoni na kusema: "Kwa hiyo umekwishammaliza sio?!"
Dokta lmu bila kujibu lolote alinyanyua uso wake na kumuangalia Dallas usoni kwa kumkazia macho. Alimtazama kwa sura ya upole, lakini bila kuogopa kiasi kwamba
Dallas alishindwa kukutanisha macho yake na ya Dokta lmu, badala yake aliangalia kando.
Wale watu walimsogelea Dokta lmu na kumwambia kwa pamoja: "Uko chini ya ulinzi Dokta" Mmoja wao aliendelea kusema huku akitoa kitambulisho na kumuonesha Dokta lmu: "Sisi ni askari kutoka ldara ya Upelelezi, mimi kwa jina naitwa Cosmas na huyu mwenzangu ni afande Selemani."
Dokta lmu hakujibu kitu wala kuonesha dalili zozote za kuhamaki.
Afande Selemani alitoa simu yake ya kiganjani na kuanza kupiga nambari fulani, kisha akaiweka simu karibu na sikio lake la kulia na kuanza kujitambulisha kisha akaagizia na kuelekeza eneo la nyumba ile ilipo katika jiji la Dar es Salaam. Ilikuwa ni Upanga. Halafu alirudisha simu yake na kumtazama Dallas na kumwambia: "Ulipotupigia ulituambia kuwa shughuli hii ilifanyika wakati wa asubuhi na kwamba baadhi ya vifaa vilivyotumika na Dokta lmu kuharibu mimba ya binti huyu ulivihifadhi alipoondoka na kabla hajarudi kwa mara ya pili Sio?" Cosmas alimuhoji Dallas kwa kumueleza habari alizofahamishwa.
Dallas alijibu huku akiitikia kwa kichwa “ndio, ndio, nilivihifadhi mara baada ya huyu Dokta lmu kuondoka na kuahidi atarudi tena usiku baada ya kazi zake za kila siku huko hospitali
kwake."
Dokta lmu alimuangalia tena Dallas na kutoa tabasamu la masikitiko. Afande Selemani naye aliendelea kumuhoji Dallas kwa kumuuliza. "Bwana Dallas una uhakika kuwa Dokta lmu aliyejaribu kutoa mimba ya msichana huyu ambaye kwa sasa ni marehemu, ndiye huyu huyu tuliyemkuta chumbani?"
Dallas alicheka kidogo kuonesha kwamba afande Selemani anauliza jibu, kisha akatamka kwa kujiamini kabisa "Hiyo ni dhahiri afande shughuli hiyo ya utoaji
mimba ilifanyika mimi nilikuwepo katika nyumba hii na nina ushahidi zaidi ya hiyo kuwa Dokta muhusika wa jambo hilo ni huyu huyu Dokta lmu."

Dokta lmu aliendelea kumtazama Dallas usoni tu, ambaye yeye Dallas alikuwa anakwepa kabisa kumtazama Dokta lmu usoni. Baada ya muda mfupi gari ilisikika ikifunga breki nje ya nyumba hiyo ambayo ni flati ya chini katika jumba la ghorofa mbili. Cosmas aliondoka chumbani na kutoka nje.
Baada ya muda wa dakika chache, alitokeza tena akiwa ameongozana na jamaa wawili waliokuwa wamebeba machela.¬
Walisaidiana kuifunga vizuri maiti ya Mwanamtama kisha Dallas naye alitoweka na baadaye kurudi na kifurushi kidogo kilichovingirishwa na kitambaa cheupe na kumkabidhi afande Selemani, kisha Cosmas alimwambia Dokta lmu.
"Sasa Dokta tunaweza kwenda kituoni kwanza na baadaye hospitali."
Dokta lmu alijibu kwa sauti ya chini kidogo kwa kumueleza Cosmas: "Sawa afande lakini na mimi nimekuja na gari yangu ambayo ipo hapo nje, sasa sijui itakuwaje."
“Hakuna wasiwasi Dokta, mimi na wewe tunaweza kwenda safari zote hizo kwa gari yako ukiwa unaendesha mwenyewe, naamini huwezi kufanya utundu.”
Dokta lmu alimuangalia Cosmas kwa sura ya kumshukuru kwa hilo na kutamka." Ahsante afande, nashukuru kwa hilo na ninaahidi sitafanya utundu wowote."
Wote walitoka nje ya flati ile na kuingia ndani ya gari zilizokuwepo. Afande Selemani akiwa katika gari waliokuja nayo pamoja na Dallas walitangulia. Walifuatiwa na gari ya Dokta lmu akiwa pamoja na Cosmas na mwisho gari iliyobeba maiti na askari wengine.

*******
Muangaza mdogo wa mionzi ya jua ulioingia katika chumba cha mahabusu alichokuwa amelala Dokta lmu sakafuni juu ya blanketi kupitia kidirisha kilichokuwa juu sana ya chumba hicho, ulimfikia Dokta moja kwa moja kwenye uso wake uliojaa uchovu na huzuni na kumfanya aukunje zaidi.

********
Dokta Abdulrahim Kasongo maarufu kwa jina la lmu na baadaye Dokta lmu, ni kijana mwenye umri wa miaka 30 kamili. Kwa wajihi ni kijana mzuri sana wa sura, mzuri wa umbo na ni mzuri wa tabia zake vile vile hakuna aliyebisha kwa hayo kwa wale wote walioweza kumfahamu na kumjua ,lmu ni kijana aliyepata elimu yake kwa taabu sana na bidii nyingi za mama yake kuanzia shule ya msingi hadi Chuo kikuu ambako alipata shahada yake ya Udaktari.
lmu hamjui baba yake. Kutokana na maelekezo ya mama yake kwamba baba yake alifariki wakati yeye ana umri wa miezi saba. Anachokumbuka yeye lmu maishani mwake ni kuishi na mama yake tu ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama muhudumu wa ofisini.
Muda wao mwingi walikuwa wanaishi katika nyumba ya kupanga eneo la Magomeni Mapipa na hatimaye walijaaliwa kumiliki nyumba yao wenyewe iliyopo Kinondoni Hananasif.
Wakati lmu amekwisha maliza mafunzo yake ya udaktari na yupo hospitali ya Muhimbili anafanya kazi ndipo alipokutana na msichana anaeitwa Zainab Mirambo. Zainabu ni msichana mrembo sana na mchangamfu mno. lmu anaikumbuka siku aliyokutana na Zainabu mwaka mmoja uliopita wakati ndio kwanza ameanza kazi katika hospitali ya Muhimbili. Ilikuwa ni wakati wa jioni ya saa kumi na moja, wakati huo alikuwa bado hajapata gari. Alikuwa kituo cha daladala maeneo ya Masaki akitoka kumtembelea rafiki yake ambaye hakumkuta, kwa hiyo alikuwa akisubiri daladala ili limrudishe kwa Kinondoni. Kituo hicho kilikuwa ni cha katikati, kwa hiyo hapakuwa na mtu yeyote zaidi yake. Mara aliona gari ndogo ikiegeshwa na msichana kwa namna ya kusua-sua, ikampita. Wakati anaiangalia vizuri ile gari, akaiona inayumbayumba na kusimama kando ya barabara mbali kidogo na alipokuwa. Alimuona msichana akiteremka kisha msichana yule alisimama na kujishika kiuno na kuangalia tairi ya gari ya nyuma ambayo kwa wakati huo ilikuwa imepata pancha.
lmu alitulia na kuburudika kwa aliyoyaona kama vile anaangalia fllamu. Mara msichana yule alitumbatumba huku na huko na kumuona lmu. Alianza kurudi na kuja taratibu mpaka alipokuwa amesimama lmu na kusema:
"Habari za saa hizi kaka."
"Ni nzuri tu dada yangu."
" Samahani kaka naomba unisaidie sijui una idea yoyote ya magari?!"
Imu alitabasamu na kuburudika na kubabaika kwa binti mzuri kama yule.
"Kama vipi, sijui?" Alimuuliza.
"Wajua nimepata pancha...nimepata pancha, sasa...waweza kunisaidia? Spea tairi ipo kwenye buti!"
Imu aliona hebu amsanifu kidogo, kwa hiyo akamhoji, "Ina maana sister wewe unajua kuendesha gari tu, lakini hata kubadilisha tairi iliyopata pancha huwezi?"
“Sikiliza kaka, ukweli ni kwamba hata huko kuendesha kwenyewe sijaweza…bado najifunza tu. Tena basi hii gari ni ya kaka yangu, nimefanya kuiiba tu mara moja kwa vile kaka na wazazi wetu wametoka kwa gari ya baba. Sasa kakaangu kama unaweza nisaidie tu mara moja ili niweze kuirudisha kabla kaka hajarudi…ninaishi karibu na hapa. Tafadhali kaka…sijui unaweza?”
Imu alitamani acheke kwa jinsi msichana huyu alivyokuwa amehamanika.
"Mimi ni Mechanical Engineer, kwa hiyo kubadili tairi ya gari ni kazi ya kitoto, twende nikakusaidie." Alimjibu kumtoa wasiwasi.
"Natanguliza shukrani ahsante."
Waliongozana mpaka pale kwenye gari. Kwa makini na ustadi, lmu alifanya kazi ya kuitoa tairi yenye pancha na kuingiza vizuri ambayo ni nzima. Kisha akamuambia yule msichana.
"Unaonaje nikakupeleka hapo nyumbani kwenu? Au utaendesha mwenyewe?”
"Nitashukuru kaka twende, maana ninajiona ninatetemeka, ninaweza kupata ajali nyingine!" lmu aliingia ndani ya gari na kukaa nyuma ya usukani wakati msichana yule amekaa kushoto kiti cha mbele. Kweli nyumbani kwao hapakuwa mbali, waliwasili. lmu akaweka gari alipoambiwa aiweke kisha akatoka na kumkabidhi funguo yule msichana huku akimwambia:
"Siku nyingine usifanye utundu wa namna hii, leo unabahati umekutana na mimi, je ingekuwa ni majambazi? Si wangekupora gari hii? Au kukudhuru? Usibahatishe
vitu kama hivi! Unaonekana u-mrembo mno hustahili kudanganya!"
Msichana yule alitoa tabasamu la dhati, shukurani na kuhusudu. Alimpa jibu ambalo lmu hakulitegemea.
“Ahsante, shukrani nyingi nazitoa kwako. Lakini ufahamu kaka katika maisha upo wakati na sehemu mtu inambidi adanganye!!"
"Kweli?!"
"Kabisa! Ilimradi udanganyifu wenyewe usimdhuru mtu!"
“Na usijidhuru mwenyewe vile vile!"
Wote wawili walicheka kwa pamoja na kisha lmu alimuaga yule msichana. Lakini kabla hajaondoka yule msichana alitamka kwa kuuliza. "Sijui jina lako ni nani kaka?!" "Mimi ninaitwa lmu na kila mtu, nawe niite hivyo!"
"Sawa nimefurahi sana kukufahamu Bwana lmu na mimi ni binti wa Jaji Mirambo... naitwa Zainabu...Zainabu Mirambo.”
Wakaachania hapo.

***

Wiki moja baada ya kazi zake za kila siku za kuwapitia wagonjwa katika hospitali ya Muhimbili, ilitokea akapita katika ofisi za mapokezi. Mara, bila kutegemea akasikia sauti ikimuita kwa shauku kubwa: "lmu...lmuu!"
Dokta lmu aligeuza uso wake na kuangalia wapi na ni ya nani sauti ile iliyokuwa inamuita namna ile. Naam ilikuwa ni sauti ya Zainabu ambaye alikuwa amesimama kando ya benchi alilokuwa amekaa mwanamke mmoja mtu mzima pamoja na bwana mmoja, kijana
aliyekuwa amevalia maridadi sana, suruali nyeusi shati la rangi ya samawati lenye mistari miembamba myeupe na tai iliyokaa vizuri shingoni mwake.
Alionekana na kila dalili ya usomi na nafasi nzuri ya uchumi kimaisha. Dk lmu alitoa tabasamu kubwa alipomuona Zainabu. Alivuta hatua taratibu kumfuata. Zainabu alinyoosha mkono wake mara tu Dk lmu alipomkaribia na kumkabidhi kiganja chake huku akisema: "Oh! Imu sikutegemea kukutana na wewe hapa ...habari za toka siku ile ?"
"Habari ni nzuri tu, Zainabu...sijui wewe?''
"Mimi ni mzima, isipokuwa . .. oh! Hebu kwanza nikutambulishe kwa mama na kaka yangu .. . " Zainabu alimshika bega yule mwanamke aliyekaa juu ya benchi ambapo alisimama karibu yake na kusema: "Huyu hapa ndie mama yangu mzazi, anaitwa bi Tausi, Mrs. Mirambo,maarufu kwa jina la mama Amani, na... (Alinyoosha mkono kumuelekeza yule mwanamme mtanashati aliekaa karibu na mama yake Zainabu juu ya benchi na kuendelea na utambulisho) ... na huyu hapa ni kaka yangu sina kaka mwengine ambaye naweza kumuita mdogo tumezaliwa mimi na huyu tu, sisi tu watoto pekee wa wazazi wetu, yeye anaitwa Amani.” Zainabu alisita kidogo wakati Amani na lmu wanaangaliana na kila mmoja wao akatoa tabasamu kubwa, kisha akaendelea na utambulisho kuwaambia mama na kaka yake: "Mama,kaka,huyu ni bwana lmu, mvulana niliyewaambia habari zake . . .aliyenisaidia siku ile nilipopata pancha ... nilipochukua gari yako kaka !"

Amani alizidi kumtazama lmu huku akiendelea kutabasamu na kuitika kwa kichwa kuashiria kumkubali mno Imu, alinyoosha mkono wake huku anasimama kutoka alipokuwa amekaa juu ya benchi na kukutanisha kiganja chake na cha Imu.
"Nimefurahi kukutana na wewe bwana mdogo, lmu, habari gani za maisha? Amani aliyasema haya huku amekizuilia kiganja cha Dk lmu kwa viganja vyake vyote viwili.
Ki umri Amani na lmu hawakuonekana kupishana sana lakini Amani alikuwa ndie mkubwa kuliko lmu kwa miaka michache. Dk lmu nae aliitikia kwa furaha kwa kusema: "Habari za maisha ni nzuri tu kaka, nami pia nimefurahi kukutana nanyi... familia ya Zainabu." Aligeuza shingo yake na kukitoa kiganja chake toka viganja viwili vya Amani taratibu na kukielekeza kwa mama Amani aliekuwa yeye pekee bado amekaa pale juu ya benchi, na kutoa salamu.
“Shikamoo mama.”
Mama Amani alipokea mkono wa Imu na kuitikia kwa sauti ya chini lakini yenye kuridhia: "Marhaba mwanangu, marhaba baba, tunashukuru kwa ulivyomsaidia Zainabu siku ile, ametueleza yote yeye mwenyewe, wakati mwengine huyu nduguyo ni mtundu sana!"
Wote walicheka kidogo kisha Amani akaendelea kusema: “Huyu Zainabu ndio sasa sasa ameanza kujifundisha kuendesha gari, na anayemfundisha ni mimi, lakini anataka aonekane anaweza yeye mwenyewe…loh! Tumashukuru sana…sijui ingekuwaje bila ya wewe!”
Dokta Imu alicheka huku akimuangalia Zainabu, kisha akasema: “Alinijulisha kuwa gari ni yako kaka na kwamba ameiba kidogo...sasa kumbe halafu alikuja kiri kila kitu kilichotokea!"
Zainabu aliekuwa kimya muda wote huo alitamka kwa kusema: "Si wewe uliyeniambia sistahili kusema uongo lmu? Kwa hiyo kaka aliporudi na mama na baba niliwaeleza kila kitu!"
Kwa muda mchache waliokuwepo hapo lmu na Zainabu pamoja na Amani na mama Amani waliweza kuzoweana kiasi cha haja ki mazungumzo. Mwisho Dk lmu aliwauliza kuwa ni shida gani iliyowaleta pale hospitali. Amani alimweleza kuwa wamemleta mama yao kuja kuchunguzwa afya yake, hususan kifua kwani alikuwa anakohoa-kohoa sana siku hizi za karibuni. Baada ya kusikiliza vizuri tatizo lililowaleta familia ya Zainabu hapo hospitali, Dk lmu aliwajibu: "Vizuri sana nimesikia shida iliyowaleta hapa kaka Amani, sasa ngoja nimuone Dk Mkuu, mhusika na idara hiyo ya vifua, bahati nzuri na mimi pia ni Dk wa maradhi ya kifua, lakini mimi bado Junior, kwa hiyo wacha nimuone Senior wangu, halafu nitakuja kumchukuwa mama. Nisubirini hapa hapa, nyie muorodhesheni mama katika daftari ya mapokezi, halafu nisubirini"
Amani alitoa shukurani zake kwa Dk lmu kwa furaha na uchangamfu mkubwa, Zainabu yeye alibaki kumuangalia lmu tu kwa kumtolea macho bila kusema chochote. Dk lmu aliondoka hapo mapokezi na kutoweka.
Baada ya muda wa robo saa hivi Dk lmu alitokea tena na kumwambia Amani. "Kaka Amani haya nifuateni huku…"
Amani, Zainabu na mama yao waliondoka na kumfuata Dk lmu ambae aliwongoza hadi kwa Dk Mkuu wa ldara ya Tiba ya maradhi ya kifua.
Walipofika kwa daktari muhusika Dk lmu alimtambulisha mama Amani kama ni Shangazi yake kwa hiyo alipewa huduma maalum na baada ya saa tatu na nusu kuanzia hapo utambulisho ulipofanyika, mama Amani alikwishachunguzwa na majibu kupatikana na kukabidhiwa dawa na Dk lmu alikuwa msitari wa mbele kusimamia yote hayo.
Dk lmu alipokuwa anawasindikiza kuelekea sehemu ambapoAmani aliegesha gari lake, ndipo Zainabu alipomuambia Dk lmu kwa kumuuliza, akihakikisha
kuwa mama na kaka yake hawatasikiia "Kwa hiyo wewe sio "engineer" kama
ulivyonijulisha siku tulipokutana kwa mara ya kwanza, kumbe wewe ni daktari… hustahili mvulana mzuri kama wewe kudanganya Dk lmu."
"Upo wakati na sehemu katika maisha ya binadamu inambidi mtu adanganye hasa udanganyifu wenyewe ukiwa ni wa mvulana kumpa moyo msichana ambae amekubali machoni na moyoni mwake kuwa mrembo hasa!" Dk lmu alijibu haya huku anacheka kidogo,kisha akaendelea, "Lakini utani mbali Zainabu mimi nimekwishawahi kujifunza umakinika katika gereji za vichochoroni mara baada ya kumaliza elimu ya msingi kwa miezi kadhaa na nikaingia tena gereji baada ya masomo ya "O"level kabla ya kuendelea na "A"level . Kwa hiyo kwa namna nyingine mimi ingawa kwa taaluma ni daktari lakini tunaweza kusema ni fundi makanika uchwara vilevile." Alimalizia kusema kwa kumtazama Zainabu kwa jicho la kitundu, ambapo Zainabu ilimbidi acheke na kusema "Kwa muda mfupi niliokufahamu, naamini unao uwezo wa kuwa na ujuzi wa aina yeyote ulimwenguni humu Dokta lmu!"
"Ni kweli kabisa kwani mwaka ujao nilikuwa ninafikiria kwenda kuchukuwa mafunzo ya kuendesha ndege...lakini maskini wee ... sina kaka anaemiliki ndege, sasa nitamuibia nani kila nitakaposhikwa na hamu ya kufanya mazoezi ya kuendesha?"
Zainabu alimpiga kofi dogo begani kwake huku akicheka.
“Wee Dk lmu we ...! Unaonekana ni mtundu mno wa matendo na maneno pia!"
Wakati huu Amani aliyekuwa mbele yao alimsaidia mama yake kuingia garini kwa kumfungulia mlango wa nyuma ya gari yake ndogo kisha akageuka na kumuangalia Dk lmu na kusema "Daktari. . . kwanza tunashukuru sana sana kwa yote uliyotufanyia, Mungu atakulipa mema lnshallah,pili ninakuomba uje nyumbani jioni moja ili tupate chakula pamoja na umuone mzee wetu wa kiume vilevile. Sasa tuambie lini utatutembelea?"
Zainabu alidakia na kusema: "Si aje leo jioni?!" Kisha akageuka kumuangalia Dk lmu na kumuuliza: "Au jioni ya leo utakuwa na shughuli?!"
Dk lmu alitabasamu kidogo na kusema "Hapana sina shughuli zozote am•bazo ni muhimu jioni ya leo, isipokuwa tu itabidi nikamjulishe mama yangu kwani amezowea kuwa kila jioni ambayo siko kazini, ni lazima tule chakula cha jioni pamoja."
Zainabu alimtazama Dk lmu na kuonekana wazi kwamba anazidi kumhusudu. Amani alimwambia Dk lmu: "lnaonekana wewe ni mtoto wa mama kama mimi, sawa nenda
ukamjulishe mama kuhusu hili, na muda wa saa kumi na mbili jioni tunakutarajia ufike nyumbani kwetu...si unakufahamu?"
"Ndio kaka, nyumba ninaifahamu na ninaahidi nitafika majira ya saa hizo, lnshallah.”
Jioni ya siku hiyo Dk lmu alikwenda nyumbani kwa kina Zainabu kupata chakula cha jioni, na huo ulik uwa ndio mwanzo wa kuwa na uhusiano wa karibu na Zainabu, kwani miezi iliyofuata ilikuta nyoyo za vijana wawili hawa Zainabu na lmu zikijaa huba kila mmoja kwa mwenzake.
Urafiki wa Dk lmu kwa Zainabu haukutiliwa wasiwasi na jamaa wote wa familia ya msichana huyo kwa sababu tangu mwanzo Dk lmu alionekana kuwa ni kijana mwema na mstaarabu mbele ya familia ya Zainabu. Pamoja na kuwa kaka yake Zai nabu, Amani, alikuwa anampenda sana mdogo wake na mara zote anamlinda na kumzuia asiwe na uhusiano wa karibu na mvulana yeyote, lakini alionekana yu laini mbele ya dokta Imu. Amani alikuwa ni mwana sheria kama baba yake isipokuwa yeye, baada ya kumaliza mafunzo yake ya sheria na kupata shahada ya juu kuhusu taaluma hiyo hakutaka kuajiriwa.
Aliungana na wenzake wawili na kuunda kampuni ya wanasheria wa kujitegemea. Kwa hiyo Amani alikuwa wakili wa kujitegemea. Zainabu naye wakati alipokutana na dokta lmu, alikuwa ndio kwanza amemaliza mafunzo yake kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alikuwa na Shahada yake ya kwanza ya Biashara.
Katika kujuana kwao na urafiki wao, Dk lmu alimchukuwa Zainabu siku moja na kwenda naye nyumbani kwao kwa mama yake. Kabla ya hapo alikwisha mueleza mama yake kwamba yupo msichana ambaye anampenda, na endapo mambo yatakuwa mazuri basi msichana huyo anatarajia kumuoa.

Mama yake lmu ambaye kwa asili alikuwa mpole, mwanamke aliyeonekana na huzuni muda mwingi kuliko anavyoonekana kuwa na furaha, mwanamke aliyekuwa akipenda kushughulika kwa vitendo zaidi kuliko kuzungumza kwa maneno. Mama lmu alimpenda mno motto wake wa pekee ambaye baba yake alifariki wakati yeye lmu bado kutimiza hata mwaka mmoja. Baada ya hapo mama lmu hakutaka kuolewa tena wala hakupenda uhusiano wowote wa kimapenzi na mwanamume.
Alijishughulisha na kazi ndogo ndogo mbalimbali za uchuuzi, kama vile kupika maandazi, chapati pamoja na kuajiriwa kama mhudumu wa ofisi katika Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam. Yote hayo aliyafanya kwa ajili ya kumlea na kumtunza motto wake lmu.
Bahati nzuri aliyoipata mama lmu ni kupata chumba kimoja cha kupanga katika maeneo ya Magomeni mapipa ambapo baba na mama mwenye nyumba walikuwa kama kaka na dada yake.
Aliishi kwa wema na hisani, tangu lmu ni mdogo mpaka akakuwa kufikia umri wa miaka kumi na nne ndipo kwa msaada wa baba na mama huyo mwenye nyumba aliweza kupata kiwanja huko Hananasif Kinondoni, akajenga taratibu na mwishowe kuhamia huko ambako hivi sasa ndiko wanakoishi na mwanawe lmu. Mama lmu alizipokea kwa furaha habari za uhusiano wa Zainabu na mwanawe. Siku zote alikuwa anaug•uza hamu ya kuwa na mtu mwengine wa damu yake zaidi ya mwanawe Imu, na alifahamu hakuna njia isipokuwa lmu kuoa na kumpatia mjukuu. Kwa hiyo pamoja na maswali mengi aliyomuuliza Imu kuhusu Zainabu, siku alipokutana na binti huyo, alimpenda mara moja na kuafiki chaguo la mwanawe. Mama lmu alimuuliza Zainabu kwa sauti ya chini huku amevishika viganja vya msichana huyo pamoja na kumwangalia usoni hapo walipokuwa wamekaa kwenye kochi kubwa, kwa kutamka: "Zainabu?!"
"Bee, mama!"
“lmu ameniambia anakupenda, na angependelea wewe ndio uwe mke mtarajiwa, je na wewe mwanangu unaniambia nini?"
Zainabu aliinamisha uso wake chini kwa haya, akang'ata midomo yake ya chini kwa
kuingiza kinywani mwake, kisha akarudisha pumzi kwa nguvu kama vile anajaribu kuvuta fikra sahihi kabla ya kutoa jibu la swali ambalo hakulitegemea.
Bila kumuangalia usoni mama lmu, Zainabu alitamka kwa sauti ya chini: "Ndiyo mama,
nami pia ninampenda na ninataraji atakuwa mume wangu wa ndoa."
Mama lmu alitoa tabasamu kubwa la furaha kisha akamwambia: "Sipendi nikukatishe tamaa mwanangu, isipokuwa nataka ufahamu kuwa lmu ni mtoto masikini ukilinganisha na wewe, kwa maana hana fedha, hana baba, hana ndugu,hana kaka, hana dada. Kwa hiyo uko tayari kumpa lmu pendo la wote hao aliowakosa? Hasa ukitilia maanani malezi uliolelewa wewe? Malezi ya kupokea pendo kila wakati? Utaweza kutoa pendo kwa lmu la kila aliyemkosa?"
Zainabu hakuchukuwa muda kujibu maswali yale. Alisema kumwambia mama huyo: "Mama palipo na pendo la kweli hakuna kisichowezekana, isipokuwa tu mimi ni binaadamu, sina ukamilifu, ningeomba tu lmu anivumilie na kunirekebisha kila mapungufu yangu yanapotokea. Mimi nampenda mwanao na ninaahidi kuendelea kumpenda kwa lolote litakalotokea!"
Mama lmu alimvuta Zainabu kifuani kwake na kumkumbatia. Baada ya hapo Dk lmu alimsindikiza kwa kumpeleka Zainabu nyumbani kwao. Wakati wapo njiani alijaribu kumliwaza kwa maneno akihofia huenda Zainabu akawa na mawazo ya kuwa mama yake amezidi mno, kutokana na maswali ya uwazi aliyoulizwa.
"Zainabu, usimuelewe vibaya mama yangu. Yeye ni mtu mwema sana, kila jambo linalonihusu mimi, huwa anapenda kulifahamu vizuri na kwa undani, hasa anapojua kuwa jambo lenyewe ni zuri kwangu, lakini amini nikwambiayo, mama siyo mkorofi!"
Zainabu alicheka na kumwambia katikati ya kicheko chake cha taratibu."We lmu wee! Aliekuambia angalau nimedhani kuwa mama yako ni mkorofi ni nani? Hata kama ingekuwa ni mimi nipo katika hali yake, familia yangu katika dunia hii motto mmoja tu wa pekee, ningefanya kama alivyofanya yeye. Usiwe na wasiwasi, ninaelewa na wala sikuchukia, nimezidi kumuhusudu mama yako name pia nampenda."
Dokta lmu alimuangalia Zainabu kwa kumtulizia macho yaliyojaa huba.
“I love you, Zainabu!”
“I love you too, Imu.”
************
Siku moja baada ya dokta lmu kumpeleka na kumtambulisha Zainabu kwa mama yake, wakati yupo kazini anatembelea wagonjwa kwenye wadi zao, alifikia kitanda kimoja ambacho alimkuta mzee mmoja aliyekuwa amelazwa siku hiyo. Alionekana amedhoofu, pamoja na kuwa ni mwenye uchangamfu na kujikaza.
"Habari za saa hizi mzee...shikamoo!" Dokta lmu alimsalimu.
"Marhaba kijana habari nzuri tu dokta." Mzee yule alijibu kwa uchangamfu huku akitabasamu. Dokta lmu alinyanyua kadi iliyokuwepo kitandani pale pamoja na nyaraka nyingine zilizokuwa zimeambatanishwa. Aliangalia, akazisoma huku anaziperuziperuzi, kisha akatamka kumwambia mzee: "Pole sana mzee...!"
Akaangalia tena kwa kukazia macho lile kadi lililokuwa mkononi mwake na kuendelea, “...mzee eeh, Bilali?" alitaja jina la yule mzee kwa mashaka-mashaka, na kwa sauti ya kuulizia. Yule mzee alijikohoza kidogo kisha naye akasema,"Enhe baba, Bilali. Bilali
Majaliwa”
"Mzee Bilali...naona hapa kwenye kadi lako ni kwamba linaonesha unatakiwa uanze kumeza dawa zako leo!"
"Ndiyo dokta,nimeanza leo!"
"Tayari umekwisha meza vidonge?!"
"Enhe baba,tayari mwanangu."
"Sawa mzee Majaliwa, Sasa uhakikishe unakula vizuri."
"Hivyo vizuri nivipate wapi mwanangu?"
Dokta lmu alicheka kidogo na kumwambia: “Sina maana ya vyakula vizuri, nina maana ule sana, hivyo hivyo vyakula unavyopewa hapa."
Mzee Majaliwa alijiinamia kidogo halafu akamtazama dokta lmu na kumuitikia kwa unyonge.
"Sawa baba, sawa dokta. Nitakula, ndio majaaliwa. Haya ndiyo majaaliwa yangu mwanangu!" "Kwani vipi mzee, mbona unasema kwa unyonge na masikitiko? Una tatizo gani mzee Majaliwa?"
Yule mzee alipandisha miguu yake juu iliyokuwa inaning'inia kwenye kitanda kirefu cha hospitali. Alijilaza na kuvuta shuka ya kujifunika, akajifunika. Uchanga mfu aliokuwa nao dakika chache zilizopita ulitoweka na akaonekana mnyonge mno kiasi ya kuwa dokta lmu aliingiwa na huruma ghafla, kwani mzee Majaliwa alijibu wakati anajifuni kashuka kwa kusema.
"Baba, mwanangu, dokta…vyakula vizuri vya vitamin na vya afya nzuri ninavijua. Vyakula vizuri vya starehe na vyenye ladha za aina mbali mbali ninavifahamu, na vyakula vya kukidhi haja vilevile ninavijua. Kwa hiyo nitakula baba...haja ni kupona. Mwenyezi Mungu kama angetaka nile kila ninachokitaka, nisingekuwa hapa baba. Haya yote ni majaaliwa yake Mola. Kwa kuwa mzee Majaliwa alikuwa ni mgonjwa wake wa mwisho kumuhudumia katika wadi ile, na hakuwa na la ziada baada ya hapo, Dokta Imu aliamua kuchukua muda zaidi wa kumfahamu yule mzee.
Hivyo basi, aliketi juu ya kitanda kile cha mgonjwa wake upande wa miguuni kwake na kumuuliza kwa taratibu."Mzee Majaliwa mimi ninaweza kuwa ni kama motto wako, kama siyo mjukuu au siyo?"
Mzee Majaliwa aliyekuwa amejilaza alinyanyua kichwa kisha alipomuona dokta amekaa karibu na miguu yake, alijivuta, akachukua mto akauegemeza kwenye sehemu ya kichwa ya kitanda, halafu yeye mwenyewe akakaa kitako na kuuegemea mto ule huku amenyoosha miguu kumuelekea dokta lmu.
Alitulia dakika chache na kumuangalia dokta lmu kwa makini kama vile anamchunguza vizuri kabla ya kutoa jibu lake.

Alirudisha pumzi kwa nguvu huku akitazama pembeni, halafu alimtazama dokta lmu tena.
"Ndiyo Dokta, unaweza kuwa mjukuu wangu ama mtoto wangu, inategemea... unasemaje Dokta?” bila kumuangalia Mzee Majaliwa aliendelea kusema: "Kwa hiyo tuna tofauti kubwa ki-umri mimi na wewe eh?"
"Sana,tofauti kubwa sana!"
"Lakini pamoja na tofauti yetu ya umri,tunaweza tuwe marafiki au siyo?"
"Ndio, lakini inategemea!"
"lnategemea nini?!"
"lnategemea uwezo wa kila mmoja wetu kumuelewa mwezake!"
"Tutafahamu vipi kama tunaelewana iwapo hatujakuwa marafiki?"
“Tutafahamu kama tunaelewana au la, tukiwa kama mgonjwa na daktari!"
Dokta lmu ilimbidi acheke kidogo kwa kutambua uwezo alionao mzee Majaliwa wa hoja zilizo na kweli. Alimtazama mzee Majaliwa na kusema, "Lakini natumai mpaka sasa umeshanielewa?"
“Kukuelewa nini?"
"Kunielewa kuwa mimi na wewe ninataka tuwe marafiki!"
"Nadhani...nimekuelewa vizuri kabisa…”
“Kwa hiyo tangu leo mimi na wewe tu-marafiki...tafadhali usikatae mzee Majaliwa!"
Mzee Majaliwa alimtazama huku akitikisa kichwa chake na kusema, "Wewe dokta ni mjanja sana. Sawa, nimekubali. Hata hivyo nilikwisha kuwa na hisia tangu nikuone mbele ya macho yangu kuwa mimi na wewe tunaweza kuwa marafiki." Dokta lmu alinyoosha mikono yake yote miwili na kuchukua kiganja cha kulia cha mzee Majaliwa na kukifumbata na viganja vyake viwili. Kisha akarudi akakaa pale pale upande wa miguuni kwa mzee Majaliwa na kumwambia, "Sawa mzee Majaliwa, tuanze mwanzo…na mwanzo ni kujuana. Wacha nikujulishe mimi ni nani nawe utanijulisha wewe ni nani baadae." Dokta lmu alijiweka sawa na kuanza kumueleza mzeeMajaliwa historia ya maisha yake kwa ufupi.
“Mimi ni mtoto pekee wa baba na mama yangu, hata hivyo simjui baba yangu kwa sababu alifariki wakati mimi bado ni mtoto mchanga. Kwa kuwa baba yangu wala mama yangu hawakuwa na ukoo mkubwa, wote wawili kwa sababu walitokea bara, basi baada ya kifo cha baba tulihamia hapa Dar, maeneo ya Magomeni.
Hata hivyo nyumba aliyokuwa amepanga mama yangu hapa jijini huko Magomeni, ilikuwa inamilikiwa na watu wema sana, mtu na mke wake ambao walimfanya mama kama ndugu yao baada ya baba yangu kufariki.Watu hao ambao ni mzee Mussa Shabani na mkewe Bi.Mwema Hussein ndio mjomba na shangazi yangu hapa duniani.
“Nimesoma kwa juhudi ya mama kuanzia vidudu na madrasa mpaka Chuo kikuu kujifunza uganga yaani udaktari. Nimechukuwa utaalamu wa vifua ikiwemo kifua kikuu.
Bado sijakuwa mzoefu sana lakini nina shukuru ninaendelea vizuri. Mama yangu amejaaliwa kupata nyumba mpya huko kinondoni ambayo sasa hivi ndiyo tunayoishi. Mimi bado sijaowa lakini ninaye rafiki yangu mpenzi aitwaye Zainabu, mtoto wa jaji mmoja hapa jijini ambaye ninatarajia kumposa hivi karibuni ili baadaye awe mke wangu. Hii ndiyo historia fupi ya maisha yangu mzee Majaliwa. Nimekuelezea yale ya muhimu yote bila ya kukuficha rafiki yangu na unaweza kuniuliza lolote lile linalohusu katika hayo niliyokueleza ambalo wewe hukulielewa.”
Mzee Majaliwa alitulia tuli pale alipokuwa ameegemea mto, aliinamisha kichwa chake chini kisha akanyanyua uso na kumuangalia dokta lmu akiwa ana huzuni nyingi sana. Alitulia kwa dakika chache akiwa macho ameyakodoa kumuangalia dokta lmu pasipo kusema kitu chochote. Mwishowe alirudisha pumzi na kurudia kuangalia chini huku akisema, "Sijui nikueleze nini rafiki yangu…sijui nianzie wapi kukueleza dokta!"
"Anza mwanzo rafiki yangu Mzee Majaliwa."
“lwapo nitaanza mwanzo, basi leo tutakesha hapa bwana mdogo,kwani mimi ni mzee. Nina mengi yanihusuyo mimi yaliyokwishanifika kuliko wewe...wewe bado u-mdogo sana!”
Dokta lmu alitabasamu na kumuonesha mzee Majaliwa kuwa yupo tayari kumsikiliza kwa muda wowote ule kwa kujiweka vizuri pale kitandani.
"Nieleze kwa kifupi tu mzee, lakini nieleze kila kitu kuhusu wewe, kwa kirefu utanieleza siku nyingine, natumaini tutakuwa pamoja,kwani urafiki wetu ndio kwanza umeanza."
Mzee Majaliwa alikunja uso na kuonekana kama anayetaka kulia.
"Ni kweli. Kwa kirefu nitakueleza siku nyingine. Sasa sikiliza historia yangu kwa kifupi…" Mzee Majaliwa alijikohoza kidogo huku akielekea kando, kisha akamtazama dokta lmu kwa kumtulizia macho, na kuongea kwa sauti ya chini iliyojaa masikitiko, "Nina asili ya Sudan, baba wa baba yangu ni Mnubi, alihamia Uganda na familia yake, babu yangu alipofikia balehe, aliondoka Uganda kibiashara na kuingia mkoa wa Kagera,Tanzania.
Hakurudi tena kwao, aliendelea kuishi huko Bukoba akifanya biashara. Alifanikiwa katika shughuli za kiuchumi kwa hiyo aliamua kubaki huko. Alioa Mtanzania na baba yangu akazaliwa. Baba naye alipofikia umri wa ukubwa, alipata kazi Mwanza na akahamia huko. Alipotaka kuoa alioa mwanamke wa kisukuma ambaye ni mama yangu. Alifanya kazi za kuajiriwa lakini baadaye alianza kazi za biashara na akahamia wilayani
Magu, wakati huo alikuwa ana watoto watano, mmoja mwanaume na wengine wanawake. Huyo mwanaume ndiye mimi ambaye nilikuwa wa pili kuzaliwa.Tulipofikia hapo Magu na kuishi huko, msiba mkubwa ulitokea. Ndugu zangu wa kike walifariki mmoja baada ya mwingine, hatimaye nilibaki mimi tu peke yangu.Wakati huo nilikuwa nina umri wa miaka ishirini hivi.
“Jambo hili lilimtia unyonge sana baba yangu. Hakuwa tena na afya nzuri. Miaka miwili baada ya hapo baba naye alifariki. Tukabaki mimi na mama yangu tu. Baba alikuwa mtu mmoja aliyefuata dini vizuri sana kutokana na utamaduni ulitoka kwa babu yake ambaye alisoma sana dini ya kiislam. Kwa hiyo na mimi nilibidiishwa sana katika kufuata dini yetu sawasawa. Baada ya kufariki baba mimi na mama yangu tuliamua kuhama hapo Magu na kwenda kuishi kijijini Gambosh.
Huko tulilima na kufanikiwa. Mama alinishauri niowe, kwa hiyo nikaposewa motto wa kike mzuri ambaye ni yatima, hana baba hana mama. Alikuwa ni wa kabila la kimanyema kutoka mkoa wa kigoma waliowahi kuishi Magu. Nilimuowa kwa ushauri wa lmamu wetu wa Mskitini.
Tuliishi kwa raha sana na tukajaaliwa kupata watoto, lakini watatu walifariki kila wafikiapo umri wa miaka miwili. Na wote hao waliofariki kwa wakati huo walikuwa wanawake. Sasa chokochoko ilianza pale uzushi ulipozuka kuwa mama yangu ni mchawi.

“Habari hizi zilikuwa zimezungumzwa kichini chini, mpaka mwishowe zikawa zimezungumzwa waziwazi. Masikini mama yangu! Alianza kudhoofu na kukosa furaha. Wakati huo nilikuwa ninamiliki nyumba nzuri na mashamba mazuri. Kwa juhudi za kufuata maagizo yote ya mabwana shamba, mashamba yangu ya mazao ya chakula na mazao ya biashara, yalikuwa yanatoa mazao mengi sana. Jambo hilo pia lilipoanza mama yangu ikasemekana kuwa yeye anakopera mashamba ya wenzake kwa uchawi. Ikasemekana pia kuwa ndiyo yeye anayewauwa watoto wangu wa kike, sababu uchawi wake ameupata kwa kuwatoa kikoa watoto wake wa kike huko anakotoka, kwa hiyo anaendelea kutoa wajukuu. Itikadi za uchawi ziliathiri vibaya raha na amani ya nyumbani kwangu. Licha ya kuwa sisi tulikuwa waumini wazuri wa Mwenyezi Mungu Subhana hu Wataala, pia tulikuwa hatuamini kabisa itikadi za uchawi. Msimamo wetu ulikuwa ni dhidi ya uchawi kabisa, lakini hatukueleweka kijijini hapo.”
Mzee Majaliwa alinyamaza kidogo. Imu hakujua aseme nini…alibaki akimtazama kwa kustaajabia yale aliyokuwa anaelezwa na yule mzee. Mzee Majaliwa aliendelea, “Rafiki yangu dokta hayo yote ni majaaliwa baba. Sasa ngoja nikueleze mkasa ulionipata ambao ulibadili maisha yangu mpaka kunifikisha hapa nilipo…”
Imu alikaa vizuri, wazi kuwa kisa cha yule mzee kilimgusa, na akilini mwake alijaribu kukisia ni nini kitafuata kwenye kisa kile cha yule rafikiye mpya mzee, lakini hakuweza.
“Ilikuwa ni siku ya Jumamosi wakati wa magharibi nilikuwa natoka mskitini ninaelekea nyumbani. Nilipofika karibu na nyumba yangu sikuamini macho yangu. Nyumba ilikuwa inawaka moto, watu wameizunguka lakini hakuna hata mmoja kati yao aliyekuwa anachukua hatua yoyote ya kujaribu kuuzima moto ule. Sauti zilisikika zikisema, ‘Wachawi! Wachawi hao! Wafe tu! Hatuwezi kuishi na familia ya kichawi kijijini petu hapa!’ Nilipatwa na kiwewe...nilikwenda mbio na kuanza kuwachangua watu ili nipate njia ya kwenda karibu na nyumba yangu inayoungua kwa moto mkubwa, nilikuwa kama mwendawazimu. Nilipofika na kusimama kati ya nyumba yangu na watu waliokuwepo, mmoja wao alinitambua, akasema, ‘Kumbe na baba yao yupo! Na yeye ni lazima achomwe moto kama alivyochomwa mama yake, mke wake na watoto wake!’ Mwingine akasema kwa sauti ya juu. ‘Yeye huyu nae atarithi uchawi wa mama yake, asibaki mtu katika familia yake! Na yeye tummalize!’ Basi kabla sijatanabahi, nikavamiwa na watu wasiopungua watano. Kufikia hapo nikatambua kuwa nimekwishapoteza kila kitu changu na kila mtu wangu katika dunia hii iliyojaa uovu, kwa hiyo nilipandwa na ghadhabu…nikapigana kama mbogo aliyejeruhiwa. Kwa muda usiopungua nusu saa nilikuwa ninapigana kwa nguvu zangu zote, sishikiki wala sishindiki. Sikuelewa nini kilichotokea baada ya hapo,lakini nilipofumbua macho nikajikuta niko juu ya kitanda cha hospitali nikiwa nimejaa majeraha ya kichwa…isitoshe, nilikuwa nina pingu mkononi. Pia ilikuwa ni mchana kweupe, kwa maana ilikuwa tayari ni siku iliyofuata kutoka usiku wa tukio lile lililobadili maisha yangu. Nilipoteza mama, mke na watoto wangu wote. Sikujielewa nimefika vipi pale hospitali na kwa nini niwe nimefungwa pingu!
“Siku ilikuwa ni jumapili wakati wa adhuhuri niliporudiwa na fahamu zangu. Hapakuwa na mtu wa kumuuliza wala wa kunieleza. Nilitulia pale kitandani nikiwa nimelala chali mawazo haya na yale yakinipita kichwani mwangu. Baada ya muda wa dakika arobaini na tano au saba kamili walitokea wahudumu wa hospitali na kuniletea chakula. Nilikataa kula kabisa. Walinibembeleza, lakini sikukubali kula. Baadaye ndipo nilipotambua sikuwa peke yangu pale kwenye chumba cha kitanda kimoja
tu cha hospitali. Kumbe nilikuwa na mwenzangu ambaye ni askari. Alikuwa amekaa nje ya chumba kile, kwani baada ya kukataa kula aliingia ndani ya chumba kile na kuanza kusema kwa ukali, "We mtu vipi wewe? Sasa una maana gani kukataa chakula? Umeiteketeza familia yako kwa moto wewe mwenyewe, sasa unamsusia nani kwa kukataa kula?”
Alimgeukia mhudumu wa hospitali na kumuuliza,"Au huyu mtu ni mwendawazimu?"
Mimi ndipo nilipoanza kufahamu, kumbe nimetuhumiwa kwa kosa la kuiteketeza familia yangu kwa moto! Sikujibu wala sikusema neno, lakini niliendelea na mgomo wangu wa kukataa kula.
Siku iliyofuata nilipelekwa mahakamani na tuhuma zikawa ni zile zile, kwamba nimeua watu wa familia yangu kwa kuwafungia ndani ya nyumba yangu na kuwachoma moto mpaka wakafa. Kwa kifupi sikutaka kubishana wala kukataa, kwa sababu sikuona faida ya kuishi. Nilihitaji kufa kwa maana halisi ya kutotaka kuendelea kuishi.Niliijibu mahakama kuwa ndiye mimi niliyewachoma wanangu, mke na mama yangu mpaka wakafa. Kwa sababu ya pili nikuwa watu wote waliokuja mahakamani kama mashahidi, walisema hivyo, kuwa mimi ndiye muuaji wa familia yangu. Tegemeo langu wakati huo lilikuwa ni kunyongwa, lakini kwa mastaajabu, nilijikuta ninapewa adhabu ya kifungo cha maisha, hii ni kwa sababu pia ya ushauri wa madaktari na wazee wa baraza la mahakama ambao kwa namna moja au nyingine, walinipa sifa ya ukichaa kidogo. Hakika haya ni majaaliwa baba mwanangu rafiki yangu Dokta. Kwa hiyo nilifungwa ili nitumikie kifungo cha maisha. Nilipokuwa nipo ndani yaani jela, nilikutana na watu wa aina mbalimbali, kati ya hao baadhi walikuwa wamefungwa lakini hawana hatia na pia walikuwepo wacha Mungu. Nilipewa nasaha na watu hao na nikarudisha matumaini ya kuishi. Waliniambia kuwa nizidi kuomba kwa Mungu, kwani yote hayo ni majaaliwa yake yeye Mola. Niliishi na nikahamishwa katika jela mbalimbali takribani kwa muda wa miaka zaidi ya thelathini. Mwaka 2012 ulipoingia nilikuwa nipo gereza la Ukonga.

Kutokana na hali ya uzee na msongamano wa wafungwa jela, nilianza kuugua kifua. Msamaha wa Rais wa Jamuhuri ya nchi yetu ulipotoka mwaka huo, jina langu lilikuwemo katika kundi la wazee na wagonjwa wa kifua kikuu. Rafiki yangu Dokta lmu, niliachiwa huru pamoja na kuletwa hapa hospitali ya Muhimbili ambapo tumekutana. Kwa hiyo mimi najihesabu sasa hivi kuwa ndiyo nimezaliwa hapa hospitali na mama yangu amefariki.Hii ndiyo historia ya maisha yangu kwa ufupi...ni majaaliwa baba." Mzee Majaaliwa alimaliza kumueleza huku akijipangusa machozi ambayo alijikaza yasimdondoke. Naye Dokta lmu alirudisha pumzi kwa nguvu,kwani alikuwa amechotwa sana na maelezo na historia ya Mzee Majaliwa, kisha akasema kumwambia, “Pole sana rafiki yangu Mzee Majaliwa."
"Ahsante sana Dokta...ni majaaliwa yake Mungu, baba!"
"Sasa rafiki yangu wacha kwanza nikuandikie hapa kwenye kadi lako,wakupatie chakula maalumu (special diet) sababu unahitaji kupata hivyo." Dokta lmu aliteremka kutoka pale kitandani alipokuwa amekaa na kusimama, kisha akachukuwa lile kadi na kuanza kuandika huku akisema, "...pili rafiki yangu mzee Majaliwa…chochote kile unachokuwa una hamu nacho ambacho hakimo katika vyakula ninavyokuandikia tafadhali nijulishe...nitakuletea mimi mwenyewe."
"Ahsante Dokta, ahsante rafiki yangu."
"Hamna shida…mengine zaidi tutajadili siku nyingine.”
Dokta lmu kwa siku ile aliagana na Mzee Majaliwa, akaondoka zake.
***********

Zainabu alikuwa anafika hospitali Muhimbili mara kwa mara kwa madhumuni ya kumleta mama yake. Lakini mara zote hizo huwa anaenda na kaka yake Amani. Na wanapofika hapo hospitali, ni lazima kwanza wamtafute Dokta lmu, kisha ndipo waendelee na ilichowapeleka, ambapo mara nyingi huwa ni kuongeza dawa za mama yao, au mama yao kufanyiwa ukaguzi wa afya na maendeleo ya tiba yake. Siku moja Zainabu alikwenda yeye na mama yake tu, Amani alikuwa na shughuli zilizomfanya asiweze kuambatana nao. Bahati mbaya siku hiyo Dokta Imu naye akawa hayupo hapo hospitali, na yeye alipata dharura ya kazi za kutoka nje ya hapo hospitali.
Zainabu alipofika pamoja na mama yake, ilibidi apokewe na daktari mwingine, kijana mwenye asili ya kiasia (kihindi), mchangamfu na mwenye sura jamali. Dokta kijana huyo aliyewahi kumuona kati ya madaktari vijana anakuja mara kwa mara kumleta mama yake.
Daktari kijana huyo mara alipomuona Zainabu, alimwendea na kumlaki kwa tabasamu, uchangamfu na bashasha, huku akimwambia. "Karibu sister, karibu sana. Samahani, Dokta Imu amepata dharura ya kazi za nje, hivyo usiwe na wasiwasi, sisi tupo tutakuhudumia." Alimgeukia mama yake Zainabu na kumsalimu.
"Shikamoo mama, karibuni. Twendeni huku."
Zainabu na mama yake walichukulia hali hiyo kuwa huenda Dokta lmu baada ya kupata dharura, amemuagiza huyo mwenzake kuwapokea na kuwasaidia. Aliendelea kusema na kujitambulisha yule kijana wakati wanamfuata.
“Mimi ni dokta Faimu...na wewe?" Akawa anamuuliza Zainabu ambaye alikuwa kati yake na mama yake.
"Mimi ninaitwa Zainabu!"
“Sawa Zainabu. Sasa twendeni kule ofisini."
Waliingia ofisi moja ndogo, Dokta Faimu akaenda akakaa nyuma ya meza ya ofisi na kuwakaribisha wakae mbele ya meza hiyo palipokuwa na viti viwili.
Baada ya kukaa na kuwauliza shida yao, Zainabu alimueleza kuwa wamekuja kuchukuwa dawa na kupata maagizo juu ya matumizi yake.
"Hamna wasiwasi, faili lako liko wapi?"
Zainabu alimkabidhi Dokta Faimu faili la mama yake ambalo walikwishalichukuwa mapokezi, Dokta Faimu alilipokea kisha akamwambia, "Sasa Zainabu twende huku mama anaweza kubaki hapahapa...na atusubiritu usimpe tabu ya kuzunguka, twende
kwenye dawa."
Zainabu alinuka na kumfuata. Wakati wanatembea kuelekea kwenye dawa Dokta Faimu alimuuliza, "Samahani sister Zainabu, huyu mama ni nani wako?"
"Huyu ni mama yangu mzazi."
"Ahaa, kwa hiyo wewe ni binamu yake Dokta lmu?"
"Kwani vipi Dokta mbona maswali binafsi yamezidi?"
"Hapana Zainabu, siulizi kwa nia mbaya. Tulifahamishwa kuwa huyu mama ni shangazi yake Dokta lmu!"
Zainabu aliona hakuna haja ya kubishana kwa hilo, hivyo akakubali kwa kusema,"Ndiyo mama yangu ni shangazi yake Dokta lmu."
"Kwa hiyo unakubali kuwa wewe ni binamu wa Dokta lmu?"
"Ndiyo.”
Dokta Faimu alitabasamu na kuendelea kusema huku akitembea taratibu, alitamka kama vile anazungumza peke yake, "Dokta lmu ana binamu mrembo sana!"
Zainabu hakujibu neno lolote lakini alikwishaanza kuhisi harufu ya panya wa kuoza.
Walifika kwenye sehemu ya dawa. Wakachukua dawa zinazohitajika, kisha msafara wa kurudi ofisini ukaanza. Dokta Faimu ndiye alianza kusema.
"Zainabu, sijui una shughuli gani jioni ya leo?"
Zainabu alimuangalia kwa kukunja uso na dalili za kuwa hajamuelewa, lakini hata hivyo akajibu.
"Sina shughuli yoyote jioni ya leo, isipokuwa kazi za nyumbani"
"Sawa, iwapo ninataka nikuone...nina maana tukutane, ninaweza kukuona wapi!"
"Nadhani hivi sasa tumekwisha kukutana na vilevile kuonana."
"Siyo hivyo Zainabu, nina maana kukutana faragha."
Zainabu alishituka kidogo na kusimama badala ya kutembea. Alitulia kisha akatoa sauti ya chini lakini yenye mkazo na kuuliza.
“Faragha?”
“Ndio, tukutane faragha…mbona umeshtuka?”
“Kwa sababu sikuelewi Dokta!”
“Huelewi vipi? Wewe hujui kukutana faragha?”
“Sielewi ni kwa sababu zipi zitakazofanya mimi na wewe tukutane faragha!”
“Sababu ni kutaka tujuane zaidi ya hivi tunavyojuana.”
“Na kama sitaki…nina maana kukujua zaidi ya hivi?”
“Nitasikitika sana…lakini kwa nini ukatae?”
“Na kwa nini nikubali?”
Dokta Faimu aliangua kicheko kisha akasema kwa kujiamini kumwambia Zainabu ambaye kwa wakati huo alikuwa amekasirishwa na ile tabia yake.
“Unataka kuniambia nini? Ina maana wewe ni mmoja wa wale wasichana wanaodai kuwa wao ni bikira?”
“Sijidai kuwa mimi ni bikira, isipokuwa nikuulize na wewe kuwa unataka kunieleza nini? Kwamba mimi si msichana anayethubutu kusema ‘hapana’ kwa mvulana yeyote yule anayenitongoza?” Zainabu aliyasema haya kwa sauti ya uchungu sana, kiasi Dokta Faimu alitahayari kidogo, lakini hakunyamaza.
“Usinielewe vibaya Zainabu. Jambo lolote ni lazima liwe na mwanzo…ninajaribu kukutaka tukutane sababu ninakupenda. Tangu siku nilipokuona kwa mara ya kwanza ulipomleta mama yako hapa hospitali ukiwa na kaka yako nilitia nia ya kukupata ili uwe mpenzi wangu. Sikuwa na maana huwezi kusema ‘hapana’, lakini sioni sababu kwa nini mimi na wewe tusipendane.”
Zainabu kwa wakati huu alikwishachoshwa na Faimu licha ya kuchukizwa naye. Alijibu kwa kujikaza, "Samahani Dokta Faimu mimi tayari ninaye ninayempenda na tayari mtu huyo ni mchumba wangu, kwa hiyo sina nafasi ya kupenda wala kukutana na mtu mwingine faragha, samahani sana!" Baada ya kusema maneno haya, alidhani itakuwa
ndiyo mwisho wa mjadala wao, lakini kumbe kwa Faimu ilikuwa bado.
"Basi kubali tuibane tu, mimi ninaridhika. Kuibana kupo,kwani nina hakika
Huyo usemaye ni mchumba wako upo wakati na mahali anatembea na wasichana wengine pia."
Badala ya kumjibu Zainabu alimuangalia kwa jicho ambalo lilimueleza kijana huyo kila kitu kuhusu chuki na kwamba msichana huyo alimchukia mvulana huyo sana kwa wakati huo, kisha alikwenda haraka haraka akamchukua mama yake na kuondoka sehemu hiyo bila kuaga.

**************

Zainabu alimueleza Dokta lmu kila kitu kilichotokea na kuzungumza kuhusu
mahudhurio yake ya hospitali na hakumficha tabia ya Dokta Faimu, na jinsi alivyomtongoza.
Siku moja Dokta lmu alimchukua Zainabu na kwenda naye kumsalimia Mzee
Majaliwa. Mzee Majaliwa alifurahi sana na wakati huo hali yake ilikuwa inaridhisha.
“Sasa iwapo utaruhusiwa, unafikiri utakwenda wapi mzee?" Imu alimuuliza.
Mzee Majaliwa aliinamisha kichwa kwa muda wa dakika chache kisha akanyanyua uso wake na kumuuliza, “ Kwani wewe rafiki yangu unafikiri nitakwenda kuishi wapi nikitoka
hapa?"
“Mimi sijui na ndiyo maana nikauliza!"
"Kwa umri huu nilio nao na kwa yote yaliyonifika,sioni sababu ni kwa nini nisiwe
karibu na Mola wetu Subhana huu Wataala. Mimi bwana mdogo nikitoka hapa, nitakwenda kuishi msikitini. Bado ninamudu kufanya huduma ndogo ndogo kama vile kufagia na kupiga deki.

Nitakwenda kufanya huduma hizo mskitini. Naamini ipo misikiti mingi inayohitaji huduma hizo. Na riziki yangu itatoka kwake Mwenyeezi Mungu."
Dokta Imu alimuangalia Mzee Majaliwa na kumuuliza, "Je, kama ninakutaka ukaishi na mimi pamoja na mama yangu,nyumbani kwetu…utakubali? Swala la kuwa karibu na Mwenyezi Mungu ni pahala popote, wakati wowote ili mradi tu utekeleze ibada zako…utakuwa karibu na Mungu. Je, utakubali kuja kuishi na mimi?"
Mzee Majaliwa alitikisa kichwa kwa kukataa kabisa swala lile. "Sio suala la kumkufuru Mungu, lakini Dokta mimi nilikuwa na familia yenye watu wanawake na wanaume. Mungu amewachukuwa wote, na akakataa kunichukua mimi, japokuwa nilikuwa ninataka iwe hivyo…sikufa wala sikuuawa. Nimefungwa miaka kadhaa. Lakini pia nimetoka. Basi ni kuwa Mungu anataka niishi maisha ya upweke. Wacha niende nikaishi msikitini. Nitajumuika na wenzangu wakati wa swala tu."
Dokta Imu alipinga mawazo ya Mzee Majaliwa.
"Hapana Mzee Majaliwa, usiseme hivyo. Itakuwani kumchukiza Mungu. Hakukuacha hai na kukurudishia uhuru ili uwe mpweke, la hasha. Si hivi tumekutana mimi na wewe? Ingawa tu-marafiki, lakini tunaweza kuishi kama baba na mtoto wake pia, au siyo?"
Mzee Majaliwa alikukubaliana na hoja ya Dokta Imu, lakini alieleza yake na kutoa ushauri wake kwa kusema, "Ni kweli kabisa Dokta Imu tunaweza tuishi mimi na wewe kama baba na motto wake, lakini nikuambie siri iliyo moyoni mwangu?"
"Enhe, sema. Tafadhali niambie!"
"Nina hisia mbaya ninahisi kila ninachokuwa karibu nacho, nina maana kila mtu nitakaye
kuwa naye karibu na kuhisi kuwa ni familia yangu, basi mtu huyo atapatwa na janga. Samahani sana bwana mdogo…mpaka hivi sasa nitakupenda sana kama rafiki yangu, pia kama mwanangu.Sasa naogopa iwapo tutaishi pamoja...sijui lakini, ninahisi kama na wewe utapatwa na janga la idhara au la umauti, majambo ambayo nisingependa yakufike mwanangu. Naami na wewe pia mpaka sasa unanipenda sana, lakini niache nikaishi msikitini."
"Ninaheshimu hisia zako baba rafiki yangu. Nakuruhusu utekeleze uamuzi wako, lakini ninaamini baadaye unaweza ukabadili mawazo yako. Na wakati huo mimi na Zainabu tutakuwa tumeshaoana Mungu akijaalia, kwa hiyo nitakuomba tena uje tuishi pamoja mimi, mama, pamoja na mke wangu... lnshallah!"
“Aamin." Mzee Majaliwa na Zainabu waliitikia kwa pamoja.

**********

Wakati anarudi kwenye eneo la hospitali kutoka kumsindikiza Zainabu, Dokta Imu alikutana na Faimu, ambaye alitangulia kumsalimu.
"Habari za saa hizi Dokta?"
"Nzuri tu, Habari gani?" Dokta Imu aliitikia kwa sauti ya chini na siyo ya kupendezewa. "Salama tu....naona unatoka kumsindikiza binamu yako Zainabu au siyo?"
"Ndiyo!" 
"Binamu yako amekwisha chumbiwa?”
"Nadhani amekwisha kueleza kuwa tayari ni mchumba wa mtu, sasa unataka nini kutoka kwake?”
Faimu alitaka mengi zaidi kuhusu Zainabu, akamuuliza, "Hivi ngoja ni kuulize...huyo mchumba wake ni nani?"
Dokta Imu hakumjibu.

********
Siku zilizofuatia hazikuwa na matukio yoyote yasiyo ya kawaida. Dokta Imu aliendelea na kazi zake kama kawaida huku uhsuano wake na Zainabu ukiendelea bila vituko vyovyote. Kadiri siku zilivyoenda, ikadhihirika wazi kuwa mchumba wa Zainabu hakuwa mwingine bali ni Dokta Imu.
Ilifika wakati Mzee Majaliwa akawa amepona maradhi yake na akaruhusiwa kutoka pale hospitali. Hii ilikuwa ni furaha kubwa kwake na kwa Dokta Imu, lakini pia ilikuwa ni huzuni kidogo kwani ilimaanisha kuwa hawataweza kuonana kwa ukaribu kama ilivyokuwa wakati mzee Majaliwa alipokuwa pale hospitali.
Kama alivyoazimia, mzee Majaliwa akaishia kuwa mkaazi wa msikitini, akifanya ibada na kuhudumu msikitini kwa kufagia, kupiga deki, kujaza maji kwenye mabirika ya kutawadhia, na mambo kama hayo.
Kwa upande wa uhusiano wa Imu na Zainabu, posa ikapelekwa rasmi, ikapokelewa. Mzee Mussa Hussein, ambaye sasa ndiye alikuwa ni mjomba wa Imu, na mwanaye Jabir, ambaye sasa ndio alikuwa ni kaka wa Dokta Imu, walikuwa mstari wa mbele katika kuwasilisha posa ile kwa akina Zainabu. LakininImu alihakikisha kuwa mzee Makaliwa naye alikuwemo kwenye msafara wa kuwasilisha posa ile, na mzee Majaliwa akahudhuria bila kukosa. Taratibu za ndoa baina yao zikaanza, mahari ikapangwa na ikatolewa, tarehe ya ndoa ikapangwa, na ikasubiriwa.
Ilikuwa miezi, zikabaki wiki na hata zikabakia siku chache tu kabla ya ndoa ile iliyosuburuwa kwa hamu kutimu.
Kila kitu kilikuwa kinaenda sawa na kwa namna iliyotarajiwa.
Siku moja kabla siku ya ndoa yake Dokta Imu alimfuata mzee Majaliwa pale msikitini kwake , na kumpelekea kanzu mpya.
“Hii kanzu utaivaa kesho tukienda kuona mzee wangu…nataka sote tupendeze siku hiyo bwana, au siyo?” Alimwambia kwa bashabsa. Mzee Majaliwa alicheka kwa furaha.
“Oooh safi sana bwana harusi..haina shaka kabisa. Ahante sana!”
“Haina shida mzee wangu, rafiki yangu…mimi nitakufuata saa moja asubuhi hapa msikitini kesho…uwe tayari, Tutasubur sote nyumbani kwetu hadi muda wa kwenda kuoa utakapofika, sawa?”
“In Shaa Allah, mwanangu! Mimi nitakuwa nakusubiri hapa hapa!” Mzee Majaliwa alimwambi, wakaagana.
Siku ile alirejea mapema tu kutokakazini mapema tu na kuamua kutulia nyumbani kusubiri siku iliyofuata akafunge ndoa. Usiku ule akiwa amelala, alishitushwa na simu yake ikiita. Alikurupuka na kuipokea, akaipeleka sikioni kwake bila hata ya kutazama ni namba ya nani iliyompigia.
“Hallow…?”
“Dokta Imu! Nahitaji msaada wako tafadhali…hali ni mbaya huku!”
Imu akashtuka kidogo.
“Ni nani mwenzangu? Naona umenitambua kwa jina….”
Sauti ya upande wa pili ilisema,"Tafadhali Dokta Imu, tena tafadhali sana. Kwanza naomba samahani kwa kukukera usiku huu, lakini nakuomba ufike hapa nyumbani haraka iwezekanavyo! Nina mgonjwa mahututi anayehitaji msaada wa daktari.Tumejaribu kuwasiliana na madaktari wasiopungua watatu, lakini tumeshindwa kupata mawasiliano nao. Kwa kuwa tumekupata wewe, tunaomba msaada wako. Ni suala la kuja kumuona huyu mgonjwa tu kwanza, na kisha unaweza kutupa ushauri wako tumpeleke hospitali au vipi. Tafadhali DoktaImu…tusaidie!"
Dokta Imu kwanza alibaki akiwa ameduwaa, asijue la kufanya, lakini kabla hajatoa jawabu lolote juu ya msaada unaotakiwa kwake, sauti ile iliendelea kusema kwa wahka, "Ni barabara ya Mark Street, nyumba ya pili kutoka nyumba iliyopo kona yaTick Street na hiyo ya Mark Street. Jengo lililoandikwa "Trap Building” Flat ya chini kabisa, mlangoni imeandikwa namba mbili kwa maandishi meupe kwenye kibao cheusi. Ni tumaini letu kuwa utafika...tafadhali, natanguliza shukrani dokta! Ahsante!"
Simu ile ikakatwa kabla hajapata nafasi ya kujibu chochote.
Alipojaribu kubofya simu yake ili aweze kupata kumbukumbu ya namba za simu alikuta ni simu ya huduma ya vibandani.
Alichukua muda kidogo kufikiri halafu, akaamua aende huko alikoitwa. Alivaa nguo zake haraka haraka, akachukuwa mfuko wa vifaa vyake vya udaktari, kisha akatoka chumbani kwake na kwenda kumgongea mama yake na kumfahamisha habari za simu aliyopokea,na uamuzi wake wa kwenda huko alikoitwa. Mama alikuwa mzito kidogo kukubaliana na wito huo, hivyo walianza kubishana.
"Imu… hawa waliokupigia simu unawafahamu ni akina nani?”
"Kusema kweli mama siwafahamu, hawakujitambulisha kwangu…"
"Sasa huoni mwanangu kuwa unafanya jambo la hatari? Kwenda kwa watu usiowafahamu?"
"Mama mimi siwafahamu lakini nina hakika wao wananifahamu na ndiyo maana wakanipigia, isitoshe mimi ni daktari mama, ni wajibu wangu kuitikia wito wa mgonjwa wakati wowote!"
Mama yake hakuonekana kuridhika bali alikubali kwa shingo upande.
“Sawa baba, lakini usiku huu na watu usiowafahmu?"
"Sehemu niliyoagizwa kufika ni upanga katikati ya mji,si kando ya mji wala vichochoroni. Usiwe na wasiwasi mama!"
"Hata huko katikati ya mji pia kuna maovu yanayotendeka, siwezi kuacha kuwa na wasiwasi!"
Mama yake aliutilia shaka sana wito ule lakini Dokta Imu alikwishaamua kwenda.
"Niombee Mungu mama, nitarudi tu mwanao nikiwa na furaha,si unajua ni jinsi gani ninavyoisubiri siku ya kesho? Usihofu, kwa heri ya kuonana mama!"
"Kwa heri ya kuonana mwanagu, ninaomba Mungu ukirudi nyumbani hapa, urudi na furaha kuliko hiyo uliyoondoka nayo...In sha Allah!"
"Amina.”
Dokta Imu alitoa gari lake nje ya hapo na kuelekea Upanga. Alipofika barabara aliyoagizwa, alipunguza mwendo. Aliendesha pole pole huku akigeuza uso huku na huku kwa kukodoa macho kusoma majina ya mitaa kwenye vibao vya Mark naTick.
Baada ya hapo, haikuwa taabu kuiona na kuitambua nyumba ya ghorofa iliyoandikwa “Trap Building” bila taabu. Alipoendesha kusogelea nyumba hiyo, alikiona waziwazi kibao kilichoandikwa namba 2, aliegesha mbele ya Mlango huo uliopo sehemu ya chini ya jingo lile. Aliteremka akiwa na mfuko wake wa kazi, na kuelekea mbele ya mlango wa nyumba, au “flat”, hiyo ya chini.

************
Dokta Imu alitolewa kwenye mawazo na sauti ya askari iliyosema kwa sauti ya juu sana.
"Dokta Imu ndiyo nani kati yenu?" Askari huyo alikuwa akitumbatumba macho kwa kuwaangalia watu watatu waliokuwemo mle mahabusu pamoja naye.
"Ni mimi hapa afande!" Dokta Imu alijinadi.
"Haya nifuate huku, kuna watu wanataka kukuona!”
Dokta Imu alinyanyuka na kumfuata, wakati huo ilikuwa ni saa tatu asubuhi ya Jumapili.

ITAENDELEA

Post a Comment

0 Comments