"Dokta Imu ndiyo nani kati yenu?" Askari huyo alikuwa akitumbatumba macho kwa kuwaangalia watu watatu waliokuwemo mle mahabusu pamoja naye. "Ni mimi hapa afande!" Dokta Imu alijinadi. "Haya nifuate huku, kuna watu wanataka kukuona!” Dokta Imu alinyanyuka na kumfuata, wakati huo ilikuwa ni saa tatu asubuhi ya Jumapili. Nje ya mlango wa chumba aliweza kuwaona mzee Mussa, na mwanaye Jabir wamesimama. Kisha nao wakafunguliwa mlango,wakapitishwa ndani na kuelekezwa kukaa sehemu moja iliyokuwa na kochi refu la saruji. Baada ya kusalimiana, mzee Mussa aliyekuwa amejaa hofu na huzuni, alimuuliza kwa wahka, "Haya baba, vipi? Kumetokea nini? Umefanya nini?" Dokta Imu alitoa tabasamu la uchovu na kukata tamaa. "Ah, mjomba! Sina lolote ovu nililofanya, lakini yaliyotokea ni makubwa…hata sijui niyaeleze vipi! Laiti ningee...!" Dokta Imu alishindwa kujizuia, sauti ilikwama, chozi likamdondoka. Jabir alimpigapiga begani na kumliwaza. “Mambo mazuri na mabaya huwafika walimwengu,nyamaza mdogo wangu,tueleze yaliyotokea." Dokta Imu alijipangusa machozi, akashukuru Mungu kwa kusema, "Alhamdulilah." Kisha akawahadithia yote yaliyotokea, kuanzia alipopigiwa simu, alivyomuaga na kubishana na mama yake, jinsi alivyoingia Flat namba 2, namna alivyokutana na Dallas, hali aliyomkuta nayo Mwanamtama, vipi alivyofungiwa na mgonjwa huyo na akafariki, Dallas alivyopiga simu kuwaita afande Selemani na Cosmas, alivyopelekwa kituo cha polisi, alivyokwenda Hospitali na maiti kupimwa na mpaka alivyofikishwa pale mahabusu. Mzee Musa alirudisha pumzi kwa nguvu kisha akamuuliza kwa huzuni na kwa sauti ya chini, "Una uhakika mjomba huyo msichana aitwaye Mwanamtama humfahamu kabisa?" "Sithubutu kudanganya mjomba…yule msichana ndiyo kwanza nimemuona jana wakati akiwa katika dakika za mwisho za uhai wake. Halikadhalika na huyo Dallas anayedai kuniona kabla ya wakati huo, hakika sikuwa ninamjua, naye ndiye aliyekuwa shahidi na shinikizo kubwa la mimi kuwa hapa nilipo hivi sasa." "Usitie wasiwasi sana, hakika ni jambo zito mno lililokutokea. Kutuhumiwa kusababisha kifo sio mchezo, lakini naamini mwisho wa yote utajivua tu katika janga hili!" Jabir alimpa moyo. Dokta Imu alijiinamia kisha akanyanyua uso wake na kusema, " Wakati huo mambo yangu yote niliyopanga yatakuwa tayari yamekwisha haribika!”, kisha kama aliyekumbuka jambo akauliza, “Kweli…vipi mama?" Mzee Mussa na mwanawe Jabir waliangaliana, kisha ndipo mzee Mussa alipomjibu. "Mama yako, jana usiku baada ya kuachana na wewe, alikuwa bado ana wasiwasi juu yako. Na kweli wasiwasi wake ulizidi pale ulipokuwa haukurudi nyumbani. Hakulala kabisa. Usingizi haukumjia, na asubuhi kulipokucha alikuja Magomeni na kutugongea. Alitueleza habari za kutorudi kwako,na wasiwasi wake...sote mimi, mama yako na Shangazi yako, mama yake Jabir na Jabir mwenyewe, tulitoka. Sehemu ya kwanza kwenda ni Muhimbili. Baada ya kuuliza na kutafiti tulipata mtu akatueleza kuwa umepatwa matatizo na huenda ukawa upo polisi. Mama yako kama unavyomjua, hapo hapo alipandwa na presha na kuanguka. Tukampeleka nyumbani...tumemuacha huko akiwa na shangaziyo Bi. Mwema. Mimi na kaka yako hapa ndiyo tukaja huku!" Dokta Imu alitulia kwa muda bila kusema chochote. Hali iliyowatia wasiwasi mzee Mussa na Jabir. Mwishowe Dokta Imu alijikaza na kusema, "Ah, haya yote ni majaaliwa yake mola,mwambieni mama asiwe na wasiwasi.Mimi sina hatia…ninaamini Mwenyezi Mungu, atanisaidia…” Jabir alimuuliza kuhusu mwanasheria Amani, kaka yake Zainabu. "Dokta Imu, huyo shemeji yako na baba mkwe wako mtarajiwa, si ninasikia ni wanasheria?" Dokta Imu aliafiki kwa kichwa huku akitamka, "Ndiyo!" "Sasa waonaje tukawasiliana nao kuhusu hili suala la matatizo yaliyokupata?" "Ah, tena kweli umenikumbusha kaka Jabiri, nitakutajia namba ya simu ya Amani, mtafute na mjulishe kila kitu kuhusu tatizo langu." Mzee Mussa aliongezea kusema kuwa, aambiwe Amani, ikiwezekana aje hapa alipo Dokta Imu ili aje amuelezee mwenyewe, na akaishiliza kwa kusema, "Sasa sisi ngoja tuondoke Imu, ili tukawatulize nyoyo mama yako na shangazi yako. Vile vile tukafanye mpango uletewe chakula." "Hata hiyo hamu ya kula ninayo basi mjomba! Najionea ovyo ovyo tu. Wala sisikii njaa!" "Hapana usifanye hivyo Dokta Imu. Wewe mwenyewe umekwishasema kuwa haya yote yaliyokufika ni majaaliwa yake Mola, sasa mbona unafanya hivyo? Yote mpe Mungu bwana mdogo, chakula kikiletwa, kula!" Jabir alimwambia. *********
Ilikuwa ni saa sita na robo hivi za mchana, wakati Zainabu, Amani na msichana mwingine ambaye Dokta Imu hakumfahamu walipoingia chumba cha kukutana na wageni cha pale mahabusu. Zainabu alionekana dhahiri kuwa alikuwa analia, kwani macho yalikuwa yamemvimba na kugeuka rangi yake na kuwa mekundu. Walisalimiana na Dokta Imu, kisha Amani akamuomba Dokta Imu amuelezee upya yeye mwenyewe habari yote, ingawa alikwishaelezewa na Jabir. Dokta Imu alimueleza kwa kirefu na kwa ufasaha kila kitu jinsi kilivyotokea wakati wale wasichana wawili, wanasikiliza kwa makini. Alipomaliza alisema, "Haya ndiyo yaliyonikuta kaka Amani. Sijui nifanye nini, sijui niseme nini! Maisha yangu yamekwisha kaka…yamekwisha. Naona nitashindwa namna hata ya kujibu na kujitetea, ingawa ukweli ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu huyo msichana anayeitwa Mwanamtama sikuwa ninamfahamu kabisa kabla ya usiku wa jana nilipomkuta yu-mahututi!" Yule msichana aliyekuja na akina Amani aliuliza kwa taratibu. "Ina maana huyo msichana aliyefariki…nina maana huyo anayetuhumiwa Dokta Imu kusababisha kifo chake…anaitwa Mwanamtama?" Ingawa swali hilo liliulizwa kwa wote, lakini lilikuwa lijibiwe na Dokta Imu, naye alijubu kwa kuitikia, "Ndiyo, alikuwa anaitwa Mwanamtama, jina ambalo pia nilifahamishwa hiyo hiyo jana na huyo bwana anayeitwa Dallas!" Msichana yule alitulia na kumuangalia Amani machoni, kisha akasema, "lsije ikawa Mwanamtama huyo ndiye huyo huyo jirani yetu ambaye nimesikia amefariki!" Dokta Imu alimtulizia macho na kumungalia kwa makini, akitamani arudie alilokuwa amesema. Amani alimgeukia Dokta Imu, " Oh, nimefanya kosa Dokta Imu, sijakutambulisha kwa mchumba wangu, sidhani kama mliwahi kukutana!" "Hapana kaka Amani, hatujawahi kukutana. Nimesikia tu habari zake!" Dokta Imu alisema haya na kulazimisha tabasamu ambalo lilitoka kwa majonzi yaliyoonekana wazi machoni mwake, jambo lililomfanya Zainabu azidi kulengwa lengwa na machozi. "Mimi pia nimekusikia ukitajwa sana, lakini hatujawahi kukutana.” Mchumba wa Amani naye alisema kumwambia Dokta Imu. Amani alifanya utambulisho mfupi tu. "Dokta Imu huyu ndiye Fatima, mke wangu mtarajiwa…" kisha akamgeukia Fatima na kumwambia, "Fatima, huyu ndiye Dokta Imu…shemeji yangu mtarajiwa."
Zainabu alibwatua kilio cha kusina sina na ki-kweukweu, na Amani akamgeukia. "Mimi nilikuwambia usije huku! Sasa unaona? Tangu asikie hizi habari zako Dokta...", Akamgeukia Dokta Imu na kuendelea, "…ni yeye na kilio, kilio na yeye! Sasa hata ukilia ndio itasaidia nini ndugu yangu?" Amani alinyamaza kidogo wakati Fatima akimkumbatia Zainabu na kumbembeleza, kisha akaendelea, "Maadamu hili jambo nimekwishalikamilisha, nakuomba Dokta Imu kesi hii unipe mimi nikutetee, nimekwishakumbana na kesi nzito zaidi ya hii, hakika hakuna hoja nzito hapa za kujibu. Sasa enhee, sema Fatima, unasema kuna jirani yako aliyefariki,naye anaitwa Mwanamtama?" Fatima alimuacha Zainabu aliyekuwa amemkumbatia na kusema."Nimesikia kuna msichana amefariki huko kijitonyama jirani na sisi. Naye kama sikosei anaitwa Mwanamtama. Ukweli ni kwamba, sikuzipata sana hizo habari, lakini zipo." Amani alitulia kidogo na kuonekana kama anayewaza kitu, kisha akamuuliza tena mchumba wake. "Samahani Fatima, wewe binafsi unamfahamu huyo msichana anayeitwa Mwanamtama?" “Ndiyo lakini si kwa urafiki wala kwa ukaribu wa aina yoyote, na mfahamu kwa kumuona tu...isipokuwa mdogo wangu Zaituni yeye nina hakika atakuwa anamfahamu zaidi, kwani nilikwishawahi kuwaona katika kundi moja wakienda kwenye 'party' ya sikukuu." Amani alionekana kufurahi na matumaini makubwa, akasema, "Hewaa...hapo ndipo tutakapoanzia. Ninahisi Mwanamtama wa Dokta Imu ndiye huyo huyo, bila shaka yoyote Mwanamtama na Fatima. Si aghalabu Mwanamtama wawili wa mji mmoja kufariki siku moja usiku mmoja. Hata! Aatakuwa ndiye huyo huyo. Kwa hiyo kuanzia sasa hivi Fatima una kazi ya kufanya. Hakikisha unahudhuria maziko ya jirani yako Mwanamtama." Amani alizungumza kwa kujiamini kiasi ya kumpa Dokta Imu nguvu kubwa na matumaini, pia alimfariji kwa kusema, “Kesho tukijaaliwa, watakapokuuliza lolote, waambie kuwa umeweka wakili wa kukutetea ambaye ni mimi. Nami pia nitakuja hiyo kesho." Dokta Imu alifarijika kidogo na kusema kwa kushukuru. "Ahsante sana kaka Amani. Sijui nikushukuru vipi…pia naomba kesho ukija uzungumzie gari langu ambalo nililetwa nalo hapa jana usiku. Naomba ulitoe uwe nalo." Muda wa kusalimu mahabusu kwa wao wakina Amani ulikwisha, naye akazidi kumwambia Dokta Imu huku anaondoka, "Usiwe na shaka Dokta Imu…mambo haya yatakwisha salama. Na hakuna harusi itakayofanyika mpaka tumemaliza jambo hili...hata yangu pia itangoja." Dokta Imu alimuangalia kwa jicho la shukrani huku akisema, "Ahsante, ahsante kaka Amani!" Zainabu alikuwa wa mwisho kuondoka, lakini kabla ya kuondoka, alimwendea Dokta Imu akamwambia, “'Kwa nini hali hii imetutokea sisi, tena wakati usio muafaka? Kwa nini Dokta Imu... kwanini?" "Yatakwisha Zainabu, haya yote ni majaaliwa yake Mola. Ametuchagua sisi kuwa mfano wa kudra na uwezo wake. Sina hatia Zainabu, lakini nipo rumande.Swali na kumuomba Mungu…yatakwisha tu mpenzi wangu...na...tafadhali wacha kulia!" "Kulia ni maisha, ni uhai. Ukizaliwa tu, kwanza unasikilizwa na kutazamwa kama unaweza kulia. Dalili za uhai wa kiumbe chochote ni kulia. Kulia kwa furaha na kulia kwa uchungu. Nisipoweza kulia kwa hili, basi mimi si binadamu mkamilifu. Wacha nilie kwa uchungu, hisia zangu zitapoona kuwa hakuna tena la uchungu, nitalia kwa furaha. Ukamilifu wa binadamu ni kulia." "Sawasawa kabisa Zainabu,lakini basi punguza kulia,matumaini yapo,lia kidogo kisha muombe Mungu, na kweli atakusaidia." **********
Ilipofika saa 4 asubuhi mzee Majaliwa alikuwa tayari amekwisha patwa wasiwasi kwa kutomuona Dokta Imu. Ahadi yao ilikuwa ni saa moja. Kwa kawaida mzee Majaliwa anavyomfahamu Dokta Imu siyo mtu wa kuhalifu miadi, sasa kumetokea nini? Aliwaza . Kwa hiyo alivuta subra kidogo,na ilipofika adhuhuri na baada ya kuswali, aliamua aende akatafute habari za Dokta Imu kwa vile hana alipokuwa anapajua pa kumpata Dokta Imu, isipokuwa hospitali Muhimbili, basi aliamua aende huko huko Muhimbili, kazini kwake, ijapokuwa ni siku ya Jumapili. Alikwenda hadi pale hospitali, na huko alikutana na habari za Dokta Imu kushutumiwa kusababisha kifo kwa kumtoa mimba msichana zimeenea. MzeeMajaliwa alidadisi zaidi na akajulishwa kuwa kwa wakati ule Dokta Imu alikuwa mahabusu. Mzee Majaliwa alichanganyikiwa vibaya sana. Alikwenda moja kwa moja mpaka huko rumande aliposwekwa Dokta Imu. Wakati akina Amani wanataka kuingia ndani ya gari lao dogo lililokuwa sehemu ya kuegeshea magari, mara Zainabu alitupa jicho na kumuona mzee Majaliwa akiwa katika mwendo wa haraka haraka akielekea hapo walipotoka wao. Alitamka kwa sauti ya chini kumwambia kaka yake "Hebu kwanza subiri kidogo kaka Amani…" "Kuna nini?" "Kuna yule mzee anayekuja kwa mwendo wa haraka!" "Enhee,ana nini?" "Nina hakika anakuja kumwangalia Dokta Imu, kwani ni raflki yake, tafadhali nisubirini kidogo nikasalimiane naye. Samahani sana kaka!" "Bila samahani, we’ nenda tu. Tunakusubiri.” Zainabu alimwendea Mzee Majaliwa na kumlaki kwa kumfunulia mikono, kumkumbatia na kuanza kulia. MzeeMajaliwa alianza kumbembeleza, mwishowe alinyamaza. Wakasalimiana na kisha kila mmoja akamruhusu mwenzake aende anakokwenda bila kuzungumza suala la Dokta Imu, kwani kila mmoja wao alitambua nafsini mwake kuwa hapana haja ya kulijadili suala la Dokta Imu kwa wakati ule, hasa kwa vile Mzee Majaliwa alikuwa bado hajaonana na Dokta Imu mwenyewe.
**********
Baasa ya salamu Mzee Majaliwa na Dokta Imu walikodoleana macho bila ya kusema chochote kwa muda usiopungua dakika tatu, mwishowe Mzee Majaliwa alirudisha pumzi kwa nguvu na kumudu kusema: "Haya rafiki yangu Dokta Imu, nieleze…kulikoni?" "Ah, ni majaaliwa tu mzee wangu!" "Naam, kila kitu kinakwenda kwa mpango wake Mola, wewe ukiwaza lako yeye aliye juu ana lake. Nieleze masahibu yaliyokufika." Dokta Imu alijiinamia kama vile hajui amueleze kitu gani mzee Majaliwa, bali baadaye kidogo alinyanyua uso wake, akamuangalia machoni na kuanza kumhadithia, mwanzo mpaka mwisho kuhusu kadhia iliyomlaza ndani na itakavyompeleka mahakamani siku inayofuata. "Dokta Imu rafiki yangu,siyo kama ninajaribu kuwa na itikadi potofu, lakini ni kweli kwamba kila ninayekuwa naye karibu na kumwita ni wangu, basi hufikwa na janga kama siyo mauti...Nadhani nilikwisha kukuambia jambo hili, ingawa hukulipatiliza, lakini je,sasa unaona?" Dokta Imu alimuangalia kama vile hamuelewi, kisha akamuuliza, "Mzee Majaliwa, unataka kuniambia nini? Unataka kusema kuwa haya matatizo yaliyonifika ni kwa sababu ya kuwa wewe u-rafiki yangu wa karibu?" Mzee Majaliwa alijibu haraka haraka bila hata ya kusita. "Kumbe? Ndiyo hivyo hasa, mikosi yangu mimi inaanza au tayari imekwisha kuingia wewe kijana mdogo usiye na hatia masikini mtoto wa watu wewe...urafiki wetu na ukome!" Dokta Imu alitoa tabasamu kubwa huku akitikisa kichwa chake halafu akamwambia Mzee Majaliwa. "Hata nikifa sasa hivi, hata nikiuawa baadaye, bado nitakwenda mbele ya haki nikiamini kuwa, nimeacha rafiki wa dhati na asiye na dosari kwangu, na ambaye hahusiki na kifo changu…rafiki huyo ni wewe!" Alitulia kidogo kumuangalia usoni yule mzee, kisha akaendelea, "Siamini kabisa kwamba kutuhumiwa kwangu au hata ikiwa ni kuuawa kwangu kuna uhusiano na wewe. Maisha yako wewe ya nakwenda kwa jinsi alivyoyapanga Mwenyezi Mungu na maisha yangu vilevile, kila linalonikuta ni kudra yake yeye Mungu, Naa...muumini wa kweli kama ulivyo wewe rafiki yangu anatakiwa aamini hivyo. Ni majaaliwa yake Mola tu baba, hakuna binaadamu mikosi, kila kitu ni majaaliwa tu ya Mungu!” Mzee Majaliwa aliinamisha uso wake akijitahidi kupingana na machozi yasimdondoke. Alibaki katika hali hiyo kwa nukta nyingi, kisha akanyanyua uso wake huku vidole vya kiganja chake cha kuume vikifikicha macho yake yote mawili. Halafu akasita kufikicha macho hayo yaliyokuwa tayari yanaonekana mekundu na yamevimba, akamuangalia Dokta Imu na kumkubalia. "Ni kweli uyasemayo kijana, lakini...hata hivyo...sijui kesi yako itatajwa lini?" aliacha alilokuwa anataka kutamka na baadala yake akamuuliza swali Dokta Imu, ambaye naye alimjibu, "Kesho…wameniambia kuwa kesho Jumatatu jalada la mashitaka yangu litapelekwa mahakamani na huenda kesho hiyo hiyo, kesi yangu ikatajwa." Mzee Majaliwa alitamka kumuombea Mungu Dokta Imu. "Mwenyezi Mungu atakusalim salama Dokta lmu, hata hivyo, mimi sitafika kusikiliza kesi yako wakati itakapofikia kesi hiyo kusikilizwa. Tafadhali usinielewe vibaya kijana na nakuomba uniruhusu nifanye hivyo. lsipokuwa nitahakikisha kuwa, mimi na wewe tunawasiliana." Dokta lmu hakupenda kumdadisi sana Mzee Maja!iwa, hata hivyo alimuuliza, "Ni kwa nini hutaki kuhudhuria mahakani?" "Kwa sababu sipendi mahakama, ingawa mahakama ni pahali pa kudhihirisha haki na batili kuufikisha, lakini kwangu mimi haikufanyika hivyo, kwa hiyo sipendi kuwepo mahakamani!" "Sawa mzee, lakini nakuomba kwa hali yoyote ile, lazima tuwasiliane, na...iwapo nitahukumiwa kifo basi pia usiache kuniombea dua!"
**********
Saa tatu asubuhi siku iliyofuata Dokta Imu alifikishwa mahakamani akiwa pamoja na watuhumiwa wengine. Walipofika ndani ya chumba cha mahakama, watuhumiwa wote waliwekwa pamoja ndani ya chumba hicho. Baada ya kukaa, Dokta lmu alijaribu kutupa macho pande zote kuona jamaa zake. Kweli, kutoka hapo alipokuwa, aliweza kumuona Mzee Mussa, Jabir na mama yake Jabiri, Bi. Mwema, na upande mwingine aliwaona Zainabu, mama yake Zainabu, na Fatima. Wote hao walikuwa wamekaa kimya na nyuso zao zikiwa zimejaa huzuni. Lakini Dokta lmu hakuweza kumuona mama yake, jambo ambalo lilimtia wasi wasi. Halikadhalika upande wa Zainabu alitegemea kumuona Amani, ambaye vilevile hakuwepo, kwa hiyo alikaa hapo alipokuwa, kwa hali ya wasiwasi sana, hasa kwa vile kwa wakati huo, hapakuwa na uwezekani way eye kuwauliza lolote jamaa zake. Ilipofika saa nne, kesi zilianza kutajwa na nyingine kusikilizwa, na haikuwa mpaka ilipotimu saa saba kasoro dakika kumi ndipo jalada la kesi ya Dokta lmu lilipowekwa juu ya meza ya hakimu. Kesi yake ilitajwa na kama walivyotegemea, ilipangiwa siku nyingine ya kusikilizwa na kwa kuwa tuhuma za kesi hiyo zinahusu kifo, basi Dokta lmu alikataliwa kupewa dhamana. Wakati anakwenda kwenye chumba kingine kisichokuwa cha mahakama kusubiri kurudishwa mahabusu, macho yake yalikutana sawa sawa na ya Dallas. Waliangaliana kwa nukta chache, kisha Dallas aliinamisha uso wake, kitu kilichomfanya Dokta lmu atikise kichwa kwa masikitiko na kutabasamu. Mara baada ya kukaa ndani ya chumba hicho Dokta lmu alikuja kuitwa na askari ambaye aliongozana naye mpaka chumba kingine. Huko aliwakuta jamaa zake wote waliokuja mahakamani wakimsubiri baada ya kuruhusiwa kusalimiana naye. Walikuwa ni Mzee Mussa, Bi mwema, Jabiri, Zainabu, Fatima, mama Zainabu na Amani wakati huu naye pia alikuwepo. Dokta Imu alisalimiana na jamaa zake hao wote kisha kwa haraka, akamuuliza Bi. Mwema, "Shangazi, mama yuko wapi?" Bi. Mwema alipiga kimya kwanza, kabla ya kujibu, jambo ambalo lilimpasua moyo Dokta lmu, kisha kwa sauti ya chini Bi. Mwema alianza maelezo. "Ondoa wasiwasi mwanagu na uitazame hii jaala ya Mungu iliyokushukia, mama yako ni mzima ...!" Dokta Imu hakumuacha shangazi yake amalize, alidakia na kuuliza, "Mbona hakuja kuniangalia?" Bi. Mwema alitulia kidogo kutafuta neno la kunena ambalo litamfariji Dokta lmu asihamaki. Mzee Mussa alimsaidia kwa kusema, "Mama yako kama unavyomjua, mara baada ya kupata habari ya hizi tuhuma zilizoelezwa kwako, hali yake kusema kweli haikuwa nzuri, presha ilimpanda. Tangu jana tumemchukua na tunaye huko Magomeni, anaendelea na tiba. Kule Hananasif tumempeleka kaka yako Jabir na mkewe wakakae huko kwa kipindi hiki kwanza. Hata hivyo, sasa hivi hali ya mama yako ni nzuri, isipokuwa yeye mwenyewe pamoja na mimi vilevile hatupendelei kwa sasa yeye aje huku mahakamani, hali ya maswali na majawabu ya kesi za mahakamani, vinaweza kumpandisha tena presha, isipokuwa tutafanya mpango wa kuomba ruhusa ya yeye kuletwa aje muonane huko mahabusu. Na mpango huo, yeye mwenyewe pia ameuafiki. Kwa hiyo, usiwe na wasiwasi mjomba!" Dokta Imu hakuweza kuzuia machozi yasimtoke, alihisi kutambaliwa na kitu chenye joto juu ya mashavu yake, huku akihisi kitu kingine kama jiwe kwenye kongomero lake. Alitoa sauti ya kujikaza na yenye mikwaruzo na kusema, "Ah, imefika hali ya mimi kutokuonana na mama yangu zaidi ya siku mbili pasipo sababu za maana kweli! Mjomba nimemkosea nini Mungu wangu miye...sina hatia mimi... mimi sina hatia!" Machozi yalizidi kumtoka kiasi cha kuwafanya wote waliokuwepo watokwe na machozi. Bi. Mwema, mama yake Zainabu, Fatima na Zainabu mwenyewe akiongazana nao, walikuwa hawatokwi na machozi tu bali walikuwa wanalia. Amani aliiweka sawa hali hiyo kwa kuwaambia. "Haya sasa futeni machozi yenu nyote! Kumbukeni mko mahakamani hapa na mmeruhusiwa kumsalimia tu ndugu yenu na siyo kumlilia hapa.. .!” lngawa na yeye pia chozi lilimtoka kidogo, aliendelea kusema huku akimuelekea Dokta lmu, "Dokta lmu wewe huna hatia, sisi sote tulio hapa tunalifahamu hilo, nami nitahakikisha kuwa Jamhuri ya nchi yetu pia inakubaliana na sisi kuwa wewe huna hatia. Tayari nimekwisha jiandikisha kukutetea wewe, kazi niliyokuwa ninaifanya tangu asubuhi. Nimekwisha onana na waendesha wa mashtaka wa kesi yako, hivyo hii kesi sina wasiwasi nayo. . .naa…” Aligeuka akamtazama mchumba wake Fatima, “.. . Fatima ameshaniletea taarifa za awali ambazo zinapendeza. Mwanamtama, ambaye ni jirani yake aliyefariki, imegundulika kwamba ndiye Mwanamtama huyo huyo ambaye Dokta Imu anatuhumiwa kwa kifo chake, hivyo huo ni mwanzo mzuri…" Wote walimgeukia Fatima, ambaye naye alieleza. "Habari nilizozipata ni kwamba, Mwanamtama jirani yangu aliyefariki, ndiye huyo huyo mmoja ambaye Dokta lmu anatuhumiwa kusababisha kifo chake. Pia marehemu huyo yupo karibu sana na ndugu yangu Zaituni, na nina hakika Zaituni atakuwa anajua habari zake angalau chache." Baada ya kusema hivi, Amani alimwambia Fatima, "Sasa hakikisha unakwenda kwenye msiba wa Mwanamtama kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa matanga. Jifanye kuwa u-mpenzi mno wa marehemu Mwanamtama, na wakati wote ukiwa huko msibani,masikio yako yawe wazi. Zaidi kuwa karibu na shoga zake marehemu, wasichana wa umri wake, ukianzia ndugu yako Zaituni." Amani alikuwa analitawala baraza lile kwa mipango yote, alimgeukia Mzee Mussa na kusema. "Mzee, kabla hatujaondoka hapa, kwa pamoja tutafanya mpango wa mama kumtembelea Dokta lmu, na hilo linawezekana, Dokta Imusiyo mfungwa bwana!" Alipokuwa anamaliza kusema hivyo alimuangalia Dokta lmu aliyekuwa kwa wakati huo yupo kimya anasikiliza tu. Amani alimsogelea, akamshika bega kisha akamwambia. "Gari lako tayari nimelitoa, hivi sasa niambie wapi pa kulipaki tu." Dokta lmu alitamka kwa sauti ya chini na yenye uchovu mwingi. "Maadam halipo tena kituo cha polisi, pengine popote utakapoliweka ni sawa tu kaka Amani, hata ukiwa nalo wewe ni sawa kabisa!" "Basi, wacha nilitumie wiki hii kwa shughuli zangu, pamoja na kwenda kumchukua mama na kumleta huko mahabusu. Kazi hiyo niachie mimi. Sababu gari langu ninataka kulipeleka karakana kwa matengenezo madogo madogo." Fatima aliomba radhi na kuaga kwa sababu ya kutaka kwenda kuhudhuria maziko ya Mwanamtama ambayo yalikuwa yanafanyika siku hiyohiyo wakati wa alasiri, huko kwao kijitonyama. Baada ya Fatima kuondoka, wengine wote nao waliagana na Dokta lmu na kuondoka. Amani na Mzee Mussa walikwenda kwenye ofisi za mahakama, wakaonana na wahusika, na kibali kilitolewa cha mama yake Dokta lmu kwenda kumtembelea mwanaye jioni ya siku hiyo hiyo, lakini iwe ni kabla ya saa kumi na mbili. Na aliyeruhusiwa kuongozana naye ni wakili wake tu, ambaye ni Amani. Amani akaelekezwa nyumbani kwa Mzee Mussa, Magomeni, naye akaahidi kwenda kumchukua mama lmu huko.
*************
llikuwa ndiyo mara ya kwanza kwa Amani kukutana na mama lmu, lakini cha ajabu, mara moja waliweza kuzoeana na kuelawana kama moto unaowaka na petroli. Amani alikuwa pamoja na kujitahidi sana amliwaze mama Imu, lakini pia alijihisi anamjua vizuri mama huyo kabla ya hapo. Kilichompa hisia hizo hakukifahamu, lakini akilini mwake kwa •mbali alihisi amewahi kumuona mama huyo kabla ya hapo. Kwa hiyo wakati wamo ndani ya gari wanaelekea mahabusu kumtembetea Dokta lmu, Amani alijaribu kuifanyisha kazi ya ziada akili yake ili akumbuke ni wapi alipokutana na mwanamke huyo lakini hakufanikiwa, bali uhakika wa kuwa hiyo siyo mara ya kwanza kumuona mama yake Dokta Imu, alikuwa anao. Mwishowe aliona siyo vibaya kumuuliza. "Samahani mama, naomba nikuulize…" "Niulize tu baba, mwanangu!" “ Hivi mimi na wewe, hatujawahi kukutana pahali popote kabla ya leo?" Mama lmu alinyamaza kimya na kuinamisha sura yake chini kuashiria kuwa na yeye anajaribu kufikiria ni mahali gani alipowahi kumuona Amani kabla ya hapo. Mwishowe aliinua sura yake na kumwangalia Amani, akamwambia, " Samahani sana baba, na mimi pia ninahisi ninakufahamu sana, na kabisa siyo mgeni katika maisha yangu, lakini papo hapo ninashindwa kukumbuka ni wapi tulionana kabla ya siku ya leo. Labda, inawezekana katika mihangaiko yangu ya kikazi wakati nilipokuwa bado ninafanya kazi katika ofisi ya Halmshauri ya Jiji, huenda tuliwahi kukutana…" Amanai alitulia kidogo huku akiendesha gari kwa mwendo wa wastani, halafu akasema kwa sauti ya mashaka kidogo. "Labda!!" Amani alitoa vitambulisho na vibali vyake kwenye ofisi husika, kisha askari mmoja aliitwa, akaamriwa kuwachukua Amani na mama Imu kuwapeleka chumba fulani. Walipofika hapo walioneshwa sehemu wakakaa. Muda si mrefu walimuona Dokta lmu anakuja akifuatana na askari, ambaye alimuacha Dokta Imu hapo walipokuwemo wageni wake, yeye akatoweka. Mama na mwana walikumbatiana, machozi yakiwatoka. Kisha mama alimshika mabega mwanaye na kumkalisha kitako kwa taratibu, upendo na uangalifu. Walipokuwa tayari wote wawili wamekaa huku wanaangaliana, Dokta Imu aliaza kumpangusa machozi mama yake, huku akimsalimu. Mama aliitikia kwa sauti ya huzuni na unyonge, halafu ndipo Dokta lmu alipoanza kusema kwa kujuta. "Laiti ningesikiliza maneno yako mama, haya yote yasingenifika, nimetegewa mama ... na mtu nisiyemjua . .. na wala sina kosa ninalolikumbuka kuwa nimemtendea mtu yeyote!" Mama yake alibaki kusinasina tu, huku akitikisa kichwa kwa masikitiko. Amani aliingilia kati na kusema, "Usiwe na wasiwasi wala shaka yoyote mama. Dokta Imu atatoka tu, maadam yeye hahusiki kabisa na suala hili la marehemu Mwanamtama, basi tuna hakika atakuwa huru Inshallah!" "Amina . . . baba!!" Mama aliitika kwa sauti ya chini. Baada ya hapo Dokta lmu alianza kumpa matumaini mama yake. Alijikaza na kumwambia, “Umesikia maneno ya kaka Amani mama? Kwa hiyo usitie shaka,mambo yote yatakuwa mazuri tu, punguza kuwaza sana mama!" "Nitajaribu mwanangu…” "Pia umefanya uamuzi mzuri mama kwa kutokuja mahakamani, tafadhali endelea kufanya hivyo, tutakuwa tunaonana hapa hapa mahabusu mpaka hapo kesi itakapokwisha." Amani, baada ya kuhakikisha kuwa Dokta lmu na mama yake wamekwisha ongea vya kutosha na muda walioruhusiwa kukutana umekaribia kwisha, alimwambia mama ambaye kwa wakati huo alionekana kuwa ana huzuni nyingi kuliko alizokuwa nazo mwenyewe Dokta Imu, "Mama, usiwe na wasiwasi, mambo yote yatakwenda sawa, tumuache Dokta lmu apumzike na wewe nikupeleke ukapumzlke. Shida yoyote ile unayoiyona ungependa uijadili na Dokta lmu kwa wakati wowote ule, nipo mimi. Tafadhali nakuomba usisite kunieleza chochote cha undani wako…waswahili wasema 'ukitaka kucheua nyongo’, ambacho ungetaka kumueleza Dokta lmu, niambie mimi. Usihofu. Sasa mimi ndiye badala ya Dokta lmu au mimi nifanye niwe Dokta lmu mpaka hapo Dokta lmu mwenyewe atakapotoka, umesikia hivyo mama?" "Ndiyo, nimesikia mwanangu…ahsante.” "Naelewa uko karibu sana na Dokta lmu...na mmekuwa pamoja maisha yake yote, umezoea kuzungumza raha na shida zako na mwanao wa kiume Dokta lmu, kwa hiyo naomba tafadhali nafasi hiyo ya Dokta Imu kwa hivi sasa unipe mimi mama. Nione mimi kama mwanao Dokta lmu, na mimi ninaahidi mbele yakemwenyewe kuwa wewe kuanzia sasa utakuwa kama mama yangu mzazi!" Dokta lmu kwa kufikiri yote aliyoyazungumza Amani alimkaribia na kumkumbatia huku akisema, "Ah, kaka Amani, sijui nikushukuru vipi! Sijui pasipo wewe ningelikabili vipi janga hili lililonifika. Ahsante kaka, ahsante sana. Ni Mungu pekee ndiye atakayelipa fadhila na hisani unazonitendea." Amani alimpiga piga bega. "Wa kumshukuru ni Mwenyeza Mungu kwa kutukutanisha sisi bwana lmu. Wewe pia unayo mengi uliyokwisha nifadhili mimi na familia yangu, licha ya kuwa u-mchumba wa mdogo wangu Zainabu pia. lliyobaki tuombeane uzima na umri tu, litamalizika tu hili tatizo, kwani 'bahari kuu ndizo zivukwazo’…yatakwisha tu." Amani aliendelea kumkumbatia Dokta lmu mabega yake kwa mkono wa kushoto, akanyoosha mkono wake wa kulia na kumkumbatia mama mabega yake yote mawili. Kisha ghafla akamuachia Dokta lmu, lakini akawa bado amemkumbatia Mama lmu. "Sasa Dokta lmu, sisi tuache tuende zetu, maana nina miadi na Fatima kwamba atakapotoka mazikoni tu aje nyumbani kunipasha habari za huko. Kwa hiyo ningependa atakapokuja anikute, nipate maelekezo ya awali kuhusu marehemu Mwanamtama."
*********** llikuwa tayari imekwishapita saa moja jioni, lakini Amani hakuona dalili yoyote ya Fatima kufika nyumbani kwao. Alijaribu kumpigia simu yake ya kiganjani, nayo akaikuta imefungwa. Kutokana na hamu kubwa aliyokuwa nayo ya kutaka kujua habari za mazikoni, alijihisi kuchanganyikiwa. Mwishowe aliamua aende yeye huko nyumbani kwa akina Fatima, sababu yeye Amani si mgeni nyumbani huko, kwa vile ni mchumba wa Fatima anayejulikana rasmi, mambo yote ya posa yalikwisha fanyika, na maada yote yalikwishatolewa. Kilichobaki kati yao kilikuwa ni ndoa tu. Kwa hiyo Amani aliaga wazee wake akachukua gari la Dokta lmu na kutoka kuelekea Kijitonyama kwa kina Fatima. Wakati anaegesha gari mbele ya nyumba ya kina Fatima, kabla hata hajauendea mlango wa mbele kubisha hodi kwa mbali kidogo aliweza kumuona mtu kama Fatima anaelekea nyumbani hapo. Alipoangalia vizuri, aligundua ni kweli alikuwa ni yeye Fatima akiwa ameongozana na wasichana wengine. Alitoka nje ya gari, akafunga mlango wa dereva, akasimama na kuegemea mlango huo kwa mgongo huku kafumbata mikono yake mbele ya kifua chake na kungalia upande anaotokea Fatima na wenzake. Wasichana wote walipofika karibu na palipoegeshwa gari, na kumtambua Amani, walisalimia kisha wote wakatoweka isipokuwa Fatima, ambaye alimkaribisha aingie ndani.
Baada ya kusalimiana na wenyeji wa hapo, alibaki na Fatima tu sebuleni, wengine waliendelea na shughuli zao. "Enhe vipi Fatima? Nilikuwa na wasiwasi !" Amani aliuliza. Fatima alitabasamu kidogo. "Kama ulivyoniona, ndiyo kwanza naingia kutoka huko msibani!" “Nilijaribu kukupigia simu, lakini nawe ulikuwa umeifunga. Nikashindwa kuwasiliana nawe!" "Ni kweli nimeifunga na wala sikwenda nayo huko mazikoni. Hizi simu za viganja kwenye shughuli zinazohusisha mkusanyiko wa watu, zinaudhi bwana...zinaleta makuruhu kweli!" "Sawa haya na tuyaache hayo ya simu, nieleze habari za huko msibani. . . za marehemu." Fatima alitulia kidogo kisha akavunja vunja vidole vyake huku akisema. "Kwanza kabisa umefanya vizuri kuja wewe hapa nyumbani, kwani licha ya kuwa tayari umekwishaingia usiku, kwa hiyo nisingeruhusiwa na baba kutoka...lakini pia nisingependa kukueleza habari nilizozipata kuhusu marehemu Mwanamtana, akiwepo Zainabu . ..angalau kwa hatua hizi za mwanzo." Amani alimuangalia mchumba wake kwa mshangao, kisha akamuuliza. "Kwani kuna nini? Kwa nini asiwepo Zainabu?" "Hebu ngoja basi nikueleze." “Enhe, lete habari…" Fatima alianza kusema kwa kusita na kubana bana maneno. "Mwenzangu, kidogo nimetaabika . ..kwa sababu habari zilienea huko msibani na inazungumzwa kwamba Mwanamtama alikuwa ni 'girlfriend' wa Dokta Imu. . . na kuwa ndiye aliyemtia mimba na baadaye kumlazimisha kuitoa mimba hiyo. lsitoshe tendo la kuitoa mimba hiyo inasemekana amelifanya yeye mwenyewe Dokta lmu. Habari zinaendelea kusemwa kuwa marehemu alimpenda mno Dokta lmu na pia hakutaka kuitoa hiyo mimba, lakini yeye Dokta Imu ndiye aliyeshikilia kuwa lazima mimba hiyo itolewe. Sababu zinasemwa ni kuwa, huyo dokta kwa tabia ni mkware sana, na kwa sasa alikuwa tayari anaye msichana mwingine!" Amani alijiinamia kidogo kujaribu kuyaingiza aliyoambiwa na Fatima akilini mwake na kuyapima kabla hajasema wala kuuliza chochote. Fatima aliendelea kumaliza maelezo yake kwa kusema, "Habari nilizozipata ni hizo, ndiyo maana nikaonelea isingekuwa vizuri kuzizungumza mbele ya Zainabu kwanza, au wewe wasemaje Amani?" "Kwa hilo ni sawa, isingekuwa vizuri Zainabu kufahamu habari hizi. . !" Amani aliafiki na kutulia kidogo, kisha akaendelea kusema usemi wa kuzitilia mashaka habari zile kwa kuuliza, "…lakini habari hizi unafikiri Fatima zina ukweli wowote ndani yake? Nina maana zina ushahidi wowote ambao unathibitisha kuwa marehemu Mwanamtama alikuwa ni 'girlfriend' wa Dokta lmu?" "Kusema kweli Amani hiyo ndiyo kesi ya kujibu. Kama siye Dokta lmu, ni nani basi? Mimi binafsi niko upande wa Dokta lmu, kuwa siye yeye aliyekuwa na uhusiano na marehemu Mwanamtama, lakini papo hapo pana suala la urafiki kati ya msichana na mvulana, pana suala la msichana mwenye mimba na Daktari mtoa mimba…kwa hiyo inachanganya! Inawezekana Dokta akawa siye aliyempa mimba marehemu Mwanamtama… je, na kumtoa mimba pia siye yeye? Sababu wanaozungumza wanahusisha vitu viwili tofauti, sasa sijui ukweli ni upi!" Amani alimuangalia mchumba wake machoni na kumwambia, "Ukweli ni kuwa, Dokta lmu hakuwa 'boyfriend’ wa marehemu Mwanamtama wala Dokta Imu hakumtoa mimba Mwanamtama. Hebu nieleze zaidi ulivyosikia kuhusu urafiki wa Dokta lmu na marehemu...unazungumzwa vipi? Yaani ulikuwa wa muda mrefu? Walikuwa wanatembeleana nyumbani kwa kila mmoja wao? Wapo jamaa wowote wa pande zote mbili wanaoufahamu urafiki wao huo? Hebu niambie ulilosikia au kuambiwa kuhusu hayo?" Fatima alikunja uso kidogo na kung'ata midomo yake kwa kuingiza kinywani, kuinamisha kichwa kuashiria kuvuta fikra na kukumbuka, kisha akasema, "Kwa niliyoyasikia na kuelezwa inaonekana marehemu na Dokta lmu, urafiki wao ulikuwa ni wa muda kidogo, si wa juzi na jana. Na suala la kuwa ni nani waliokuwa wanaufahamu uhusiano wao huo kwa hiyo ninaweza kusema watu wazima wa nyumbani kwao inawezekana kuwa hawajui lolote kuhusu uhusiano huo lakini kwa vijana, yaani wadogo zake na rafiki zake, hasa wasichana wenzake nina hakika watakuwa wanajua kuhusu urafiki wa Dokta lmu na marehemu, angalau kwa uchache!" Amani aliitikia kwa kichwa kukubaliana na aliyosema Fatima kisha akasema kwa kuuliza. "Kama sikosei Fatima uliniambia kuwa mdogo wako Zaituni ni mrnoja kati ya shoga zake marehemu waliokuwa karibu naye au siyo?" "Haswa! Nadhani Zaituni ni mmoja kati ya marafiki wa karibu wa marehemu." "Je Zaituni anaweza kuwa anafahamu chochote kuhusu urafiki wa marehemu na Dokta lmu?" "Ndiyo ni kweli. Nafikiri Zaituni anaweza kujua japo kidogo, kuhusu uhusiano wa marehemu na Dokta lmu…" "Waonaje tukamuita sasa hivi tukamuuliza?" "Sawa, ngoja nikamuite." Fatima aliondoka sebleni hapo, na baada ya dakika chache, alitokezea akiwa ameongozana na Zaituni. "Bi Zaituni poleni kwa msiba wa shoga yako Mwanamtama." Amani alimwambia maneno haya Zaituni mara tu baada ya kufika na kukakaa mbele yake. “ Ahsante shemeji Amani." "Samahani sana Zaituni kwa kuchukua muda wako, lakini tulikuwa na ubishani hapo na dada yako Fatima kuhusu huyo aliyekuwa 'boyfriend' wa marehemu Mwanamtama…ati wewe unamfahamu?" Zaituni alicheka cheka kidogo, kisha akamrudishia swali shemeji yake kwa kuuliza, "Yupi mmoja wapo?!" "Ina maana marehemu alikuwa na 'boyfriend' wengi?" “Hapana…ninaowajua mimi ni wawili tu na huyo mmoja walitengana siku nyingi na wala hayupo hapa nchini . . . !" "Tuna ulizia huyo aliyempa mimba, kisha akajaribu kuitoa!" "Ah, haaa...Dokta lmu?" "Enhee huyo huyo…je wewe unamfahamu?" "Mhuu!" "Mbona unaguna Zaituni?" "Kusema kweli shemeji Amani, mimi huyo mtu ninamfahamu zaidi kwa kumsikia na kuelezewa na yeye mwenyewe marehemu, lakini bahati mbaya sijapata kukutana naye au kumuona!" Amani aliinamisha uso chini, akafikiri kuwa hakufikishwa alipokuwa amepataka. Alinyanyua uso na kumuliza, "Je, marehemu aliwahi kukueleza kuhusu huyo ‘boyfriend’ wake?” "lnavyoelekea alikuwa yeye marehemu anampenda sana huyo mvulana ambaye alisema ni daktari, na ni kijana, lakini inavyoelekea huyo daktari hakuwa anampenda marehemu Mwanamtama kama alivyokuwa anampenda yeye. Marehemu alikuwa kila mara analalamika kuhusu yeye huyo rafiki yake daktari!" Amani kidogo alianza kuvutiwa namazungumzo hayo, na kufikiri huenda yakampeleka anapopataka, alimuuliza tena Zaituni. "Samahani Zaituni…katika marafiki zenu wewe na marehemu, unadhani hakuna yeyote ambaye aliwahi kukutana na huyo rafiki yake Mwanamtama ambaye ni daktari?" Zaituni aliweka kidole chake mdomoni na kufikiri kwa kupeleka macho yake juu kisha akasema, "Enhee, nadhani shemeji wapo wengi tu wa rafiki zetu ambao watakuwa wanamfahamu huyo daktari. Kwanza ipo 'party' ambayo mimi sikuhudhuria, lakini marehemu alikwenda na huyo 'boyfriend' wake, na picha nyingi zilipigwa, sasa labda uniachie kazi hiyo ya kuzipata picha za 'party' hiyo. Nina hakika marehemu atakuwa amepiga picha naye, na 'party’ yenyewe siyo ya siku nyingi…ni hizi siku za karibuni, juzi juzi tu!" Amani alirudisha pumzi kwa nguvu za kutua mzigo aliokuwa nao kichwani, aliuliza swali la nyongeza. "Basi kama hiyo 'party' ilifanyika hivi karibuni bila shaka marehemu Mwanamtama tayari alikuwa mjamzito au siyo?" "Enhee, tayari marehemu Mwanamtama alikuwa mjamzito, uvumi wa kuwa Mwanamtama ana mimba ulienea takribani miezi mitatu iliyopita sasa!” "Sawa sawa Zaituni sasa tafadhali jaribu kwa bidii yako yote uzipate hizo picha na mimi nitapenda kuziona!"
Wiki mbili baadaye, siku iliyopangwa kusikilizwa kesi ya dokta lmu ikafika. Kama kawaida, ndugu na jamaa zake wote walihudhuria mahakamani kwa minajili ya kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa mama yake mzazi, na rafiki yake mzee Majaliwa. Amani alikuwapo pale mahakamani, pamoja na kwamba picha za marehemu Mwanamtama ambazo inasemekana alipiga na Dokta lmu zillikuwa bado hazijapatikana kama alivyotegemea. Baada ya kesi zipatazo mbili kusikilizwa, iliyofuata ya tatu ilikuwa ni ya dokta lmu. Dokta aliitwa na kusimamishwa kizimbani, kisha akasomewa mashtaka yanayomkabili. "Sikubali makosa hayo!” Dokta lmu alikana mashtaka. Wakili wa serikali mwendesha mashtaka alirudia tena kumuuliza, "Ina maana hukubali kuwa ulimtia mimba Mwanamtama, kisha ukamshawishi kutoa mimba hiyo, halafu ukamtoa mimba hiyo kwa kutumia vifaa visivyostahiki tena nje ya hospitali na hivyo kusababisha kifo chake?" Imu alirudia tena kukana mashtaka na kuongezea kwa kusema kwa msisitizo: "Kwa mara yangu ya kwanza katika maisha yangu kumuona msichana yule ilikuwa ni usiku wa siku ile niliyoitwa kwa njia ya simu, na nilipofika nikamkuta hali yake siyo nzuri. Niliposisitiza suala la kupelekwa hospitali ndipo bwana mmoja niliyemkuta na aliyenikaribisha na kujitambulisha kwangu kwa jina moja tu la Dallas, aliponifungia mlango wa chumba kwa nje na kuniwacha nikishuhudia kutokwa roho kwa msichana huyo!" Wakili wa serikali muendesha mashtaka, aliyejulikana kwa jina la Zablon Mkuki aliendelea kumuhoji. "Ndugu lmu unaidanganya mahakama kwa kuiambia kuwa ulikuwa humfahamu Mwanamtama?" "Ni kweli kabisa nilikuwa simfahamu Mwanamtama!” Wakili Mkuki aligeuza shingo na kumuangalia hakimu aliyekuwa akiendesha kesi ile ambaye alikuwa ametulia juu ya kiti chake kikubwa nyuma ya meza kubwa juu ya membari akisikiliza kwa makini majibizano yale, kisha akasema, "Mheshimiwa Hakimu, inaonekana mshitakiwa nimuongo, hasemi ukweli. Marehemu Mwanamtama alikuwa hawara yake, vipi leo aseme ati hajawahi kumuona kabla ya hiyo siku ya umauti wake?" Amani alinyoosha mkono, na hakimu alimuashiria kumruhusu kusema, naye alisimama, akainama kidogo kumuelekea hakimu kwa ishara ya kutoa heshima kabla ya kuanza kuongea. "Mheshimiwa Hakimu, mshitakiwa Imu anavyosema kuwa hakupata kumjua, kumfahamu wala kumuona marehemu Mwanamtama kabla ya hiyo siku ya kifo chake hiyo ndiyo hasa…sasa uongo uko wapi? Nani anayethibitisha kuwa ndugu Imu alikuwa ni hawara wa marehemu Mwanamtama?" Kwisha kusema hivyo, Amani aliinamisha kichwa chake tena mbele ya hakimu kisha akarudi kukaa. Hakimu aliendelea kumwambia wakili Zablon Mkuki. "Ndiyo wakili Mkuki…unayo hoja juu ya aliyosema wakili mtetezi Amani?" "Ndio Mheshimiwa…kwanza kabisa ninaomba waitwe kwako mashahidi namba tatu na namba mbili, kabla hajaitwa shahidi namba moja wa kesi hii!" Afande Selemani na afande Cosmus waliitwa mbele ya mahakama, nao mmoja baada ya mwingine waliingia kizimbani na kutoa ushahidi wa jinsi walivyopigiwa simu na Dallas, walivyokwenda nyumbani Upanga na kumkuta lmu ndani ya chumba pamoja na mwili wa Mwanamtama ambaye kwa wakati huo tayari alikuwa amekwisha kata roho. Pia walitoa maelezo ya namna mwili huo ulivyopelekwa hospitali na kupimwa, na ikagundulika kuwa marehemu alifariki kutokana na kutokwa na damu nyingi kupita kiasi baada ya kutolewa mimba kwa taratibu zisizo za kawaida nje ya hospitali, na pia kwa kutumia vifaa visivyo rasmi. Ripoti ya hospitali ilitolewa pamoja na vifaa, ambavyo vilikuwa ni mikasi, spoku za baiskeli, vitambaa vyeupe na 'gloves' ambavyo baada ya Dokta lmu kuviona, alitambua kuwa ni vitu vile vilivyokuwa vimefungwa kwenye kitambaa cheupe ambacho Dallas aliwakabidhi afande Selemani na Cosmus siku ile ya kukamatwa kwake. Ushahidi wa afande Selemani na Cosmus baada ya kutolewa maelekezo yake na kila mmoja wao, wakili mtetezi alisimama na kuwauliza mmoja baada ya mwengine, swali hilo hilo moja tu, lililofanana: "Afande Selemani, ulipofika mbele ya mlango wa chumba alichokuwemo mtuhumiwa lmu na marehemu Mwanamtama, mkiongozwa na Dallas, kabla hamjaingia, kuna kitendo gani unachokumbuka kilifanyika?" Alipokuwa anaulizwa afande Selemani swali hili, alijaribu kufikiri fikiri, kisha akasema: "Hapana sikumbuki kitendo chochote!" "Kwa hiyo unataka kuiambia mahakama kwamba mlipofika mbele ya chumba hicho mlipitiliza tu moja kwa moja na kuingia?" Amani alimuuliza huku akimtazama machoni kwa kumkazia macho. Afande selemani alishituka kidogo na kusema: "Ah, ndio nimekumbuka!" "Umekumbuka nini?" "Dallas aliyekuwa mbele yetu akituongoza, alifungua mlango!" "Alifungua mlango vipi? leleze mahakama afande, wewe ni mzoefu wa shughuli kama hizi!” "Aliufungua mlango kwa ufunguo!" "lna maana kwa kutia ufunguo kwenye kitasa cha mlango, eenh?" "Ndio.” "Kwa hiyo ndugu lmu pamoja na marehemu Mwanamtama walikuwa wamefungiwa, eenh?” "Ndio!" Alijibu afande Selemani kwa kushangaa. "Ahsante afande...sina zaidi." Amani alimshukuru. Afande Cosmus yeye alipoulizwa swali hilo hilo alijibu moja kwa moja kwa kusema: "Tulipofika mbele ya mlango wa chumba, Dallas alitia ufunguo kwenye kitasa cha mlango, nao ulifunguka, ndani ya chumba tulimkuta ndugu lmu na marehemu.” Swali la nyongeza kwa afande Cosmus lilitoka kwa wakili muendesha mashtaka Zablon Mkuki alipouliza: "Ndugu Cosmus, ndani ya chumba hicho mlimkuta nani unasema?" "Tulimkuta ndugu lmu na mwili wa Mwanamtama!” "Ahsante afande Cosmus." Baada ya ushahidi wa afande Selemani na Cosmus kutolewa pamoja na vielelezo kuletwa mbele ya hakimu, ilifika zamu ya shahidi namba moja ambaye alitajwa kuwa ni Dallas. Dallas aliitwa na kuelekezwa aingie kwenye kizimba kilichokuwa upande wa kushoto wa meza ya hakimu. Alipoulizwa kuhusu dini yake akasema kuwa yeye ni Muislam. Kwa hiyo kabla ya kutoa ushahidi wake aliapishwa kwa taratibu za Kiislam. Wa kwanza kumhoji alikuwa ni wakili wa upande wa mashtaka anayemsaidia mwendesha mashtaka, Zablon Mkuki. "Ndungu Dallas, wewe unamfahamu marehemu Mwanamtama?” "Ndio ninamfahamu." "Je unafahamu nini kuhusu Mwanamtama na Dokta lmu?" “Wao walikuwa ni mtu na 'boy friend’ wake!" "Yaani mtu na hawara yake sio?" "Ndio!" "Hebu tafadhali bwana Dallas ieleze mahakama ilikuwaje mpaka kifo cha Mwanamtama kikatokea!" Dallas alijikohoza kohoza kisha akazungusha macho yake kuangalia watu wote waliokuwepo pale mahakamani isipokuwa dokta lmu, ambaye hakumuangalia kamwe, kisha akaanza kueleza: "Marehemu Mwanamtama ni ndugu yangu. Miezi michache iliyopita, nilianza kumuona ana mabadiliko ya kimwili na kitabia vilevile. Alianza kuwa ni mtu mwenye wasiwasi, fikira nyingi na majonzi. Mimi nilihisi ni lazima atakuwa na jambo linalompa wasiwasi. Siku moja wakati wa jioni, nilimkuta amekaa sebleni peke yake amejiinamia. Siku hiyo ndipo nilipomuuliza kwa taratibu na lugha ya kumfariji, naye ndipo aliponieleza undani wake... “Aliniambia kuwa yeye ni mjamzito wa mimba ya zaidi ya miezi miwili na nusu. Nilipomuuliza muhusika wa ujauzito huo ni nani, aliniambia kuwa ni Dokta lmu.Nikamuuliza sasa wana mpango gani? Yaani yeye na huyo dokta lmu…" Alipofika hapo alimuangalia dokta lmu kwa kuiba-iba, na dokta lmu alimtulizia macho huku akitoa tabasabu la kulazimisha na kutikisa kichwa. Dallas aliendelea kueleza: " . . .Jibu alilonipa lilikuwa la kukata tama…Mwanamtama alisema kuwa yeye anampenda sana sana lmu, na mpaka ikafikia hatua hiyo ya kuwa na mimba, ni kwa sababu yeye Dokta lmu alimuahidi kumuoa, lakini sasa amebadilika na anamshauri aitoe hiyo mimba. Mwanamtama aliendelea kunieleza kuwa alipomchunguza rafiki yake huyo, aligundua kuwa kuna msichana anaeitwa Zainab, ambaye ndiye aliyekuwa akilini kwa dokta Imu kwa wakati huo, kwa hiyo Mwanamtama ndipo alipoona ni afadhali mimba aliyokuwa nayo aitoe kwa shinikizo la Dokta lmu. Nilijaribu kumsihi asitoe mimba, lakini alisema atafikiria." Dallas alijipangusa jasho jembamba lililokuwa linamtoka usoni, kisha kwa huzuni kubwa aliendelea kusema: "Siku hiyo ya tukio, mimi nilikuwa nimetoka, sasa wakati ninarudi kama saa nane hivi mchana nilipoingia nyumbani, mara kwa ghafla nilisikia sauti ya malalamiko na maumivu ikitokea chumba alichokuwemo Mwanamtama. Nilitaka nigonge chumba hicho lakini nikasita kidogo, nilihofia huenda marehemu Mwanamtama alikuwa kwenye tendo la mapenzi na Dokta Imu kwa vile alikuwa anataja jina lake humo kwa humo huku akilalama. Mimi nilikwenda chumbani kwangu nikakaa huko kiasi cha nusu saa halafu nilitoka na kuelekea chumbani kwa Mwanamtama. Masikini wee, kwanza mlango niliukuta uko wazi, na dokta lmu sikumkuta alikuwa tayari amekwishaondoka. Mwanamtama kwa hali ya maumivu aliniambia kuwa tayari amekwisha fanyiwa operesheni ya kutolewa mimba, na akaniomba nimpelekee maji ili ameze vidonge vya kupunguza maumivu na vya usingizi alivyopewa na dokta lmu. Vile vile alinikabidhi business card ya huyo huyo Dokta lmu. Nilimpa maji, akameza vidoge vile, kisha akapata usingizi mzito kwa muda mrefu. “AIilala mpaka saa moja jioni, lakini alipoamka hali ilikuwa mbaya, alikuwa ametokwa na damu nyingi sana. Kwa hiyo nilijaribu kuwasiliana na madaktari zaidi ya watatu ambao nilifahamu wapo karibu na ninapoishi, lakini sikufanikiwa kuwapata. Ndipo mwishowe nikaona ni heri nimpigie Dokta lmu mwenyewe. Ndipo nikampigia. Alipofika alimuangalia angalia na kushauri tumpeleke hospitali. Lakini kwa wakati huo Mwanamtama alikuwa yuko hoi kabisa kwa hiyo nikaonelea kwamba ni heri nipige kituo cha polisi ili hata kama tutakwenda hospitali, basi twende pamoja na askari. Hivyo ndivyo ilivyokuwa mheshimiwa!" Dallas alimaliza maelezo yake.
Zablon Mkuki alitabasamu na kuonekana yuko kwenye mawazo ya kumbwaga wakili mpinzani wake kwa wakati huo ambaye ni Amani. Mkuki alimwambia hakimu: "Mheshimiwa hakimu, nadhani mahakama yako tukufu imekwisha sikia shahidi wetu namba moja ndugu Dallas alivyotoa ushahidi wake kwa ufasaha, ukweli na uwazi kabisa. Naamini hakuna kilichobakishwa ambacho kinahitaji kuelezwa kuwa mtuhumiwa anayo hatia. Hakimu aliyekuwa akiandikia kwenye jalada lililokuwa mbele yake pale mezani, akanyanyua uso wake na kutamka kwa kusema: "Ndiyo ... upande wa utetezi, sijui kuna swali lolote ambalo mngependa kumuuliza ndugu Dallas?" Amani alinyanyuka akainama kidogo kumuelekea hakimu huku akisema: "Ndio mheshimiwa hakimu, yapo maswali!" "Vema unaweza kuendelea!" Hakimu alimruhusu. Amani alikwenda mpaka kwenye kizimba alichosimama Dallas, akanyanyua uso wake na kumuangalia Dallas machoni, kisha akamuuliza kwa sauti ya chini kidogo: "Hivi ndugu umesema jina lako nani?!" Dallas hakuonekana kupendezewa na swali hilo, vilevile hakuwa tayari kujibu kwa hiyo alitafuta msaada kwa kumuangalia hakimu kwa jicho la huruma huku akibaki kimya. "Jibu swali uliloulizwa shahidi!” Hakimu alimwambia kwa sauti ya kuamrisha kidogo. Dallas alirudisha uso wake aliokuwa ameukunja na kumuangalia Amani, kwa sauti ya dharau, alijibu: "Jina langu Dallas Meja!" Amani alitoa tabasamu na kumuuliza: "Ndugu Dallas Meja, una uhusiano gani na marehemu Mwanamtama?" "Nimekwisha sema ni ndugu yangu!" "Haitoshi bwana Dallas, kwani kwa watanzania, huwa tunaitana ndugu, kwa hiyo mtu yoyote anaweza akawa ndugu yako kwa maana hiyo ya ki -Tanzania. Nataka uiambie mahakama udugu wenu halisi ni wa vipi?... Baba mmoja, mama mmoja? Mama mmoja baba mbalimbali…Binamu yako, Mpwa wako, Mtoto wa shemeji yako au vipi?" Wakili Zablon aliinuka akatoa heshima kwa kuinama kidogo kisha akasema kwa sauti ya juu, "Kuna pingamizi mheshimiwa hakimu! Wakili mtetezi anajaribu kumuuliza maswali mengi shahidi Dallas yasiyokuwa na maana ili ampotoshe tu katika ushahidi wake mzuri aliotoa!" Hakimu alitoa sauti ya kawaida bali ya kutomkubalia wakili Mkuki kwa kumwambia, "Pingamizi hiyo haikubaliwi wakili wa upande wa mastaka...!” Akamgeukia wakili mtetezi na kumwambia "Unaweza kuendelea kumuuliza maswali shahidi. .. ndugu wakili mtetezi!" Amani alitoa tabasamu kubwa, kisha akamgeukia Dallas tena na kuendelea kumuuliza: ''Enhee, tueleze bwana Dallas uhusiano wako halisi na marehemu Mwanamtama ni upi?" Dallas aliangalia chini kama anaefikiri kisha akamuangalia Amani kwa jicho la kuua na kujibu kwa sauti ya chuki: "Ni binamu yangu!'' "Endelea tafadhali…binamu yako...mtoto wa nani? Baba mkubwa? Baba mdogo? Shangazi, au mjomba?" "Ni...alikuwa ni mtoto wa mjomba wa ng u!" "Mwanamtama enzi za uhai wake alikuwa anaishi wapi?" "Alikuwa anaishi Kijitonyama… " "Na wewe je, unaishi wapi?" "Mimi ninaishi Upanga!" Amani alimuangalia Dallas kwa dakika chache halafu akamuuliza: "Marehemu Mwanamtama alikuwa anaishi na nani. .. yaani huko kijitonyama alikokuwa akiishi?” Dallas alionekana kugwaya kidogo na kuonesha chuki za wazi dhidi ya Amani. "Anaishi na wazazi wake!" "Basi?" "Basi nini sasa?" Dallas alijikuta anamjibu Amani kwa kumuuliza swali na yeye bila kujitambua. Amani alitabasamu na bila kuhamaki akamfafanulia swali lake. "Nina maana marehemu alikuwa anaishi na mama na baba yake tu, basi? Hana kaka, hana dada, hana bibi au shangazi anayeishi ndani ya nyumba ya wazazi wake?" "Ndio, wako dada zake, kaka zake na hata bibi yake mzaa mama yake.” "Ndugu Dallas, je kwa ufahamu wako huo nyumbani kwa mjomba wako yaani baba yake marehemu Mwanamtama, huko Kijitonyama, kuna simu?" Dallas alionyesha dhahiri kuwa amekwisha anza kuchoshwa na viswali vidogo vidogo vya kipuuzi, lakini alihimizwa na hakimu avijibu viswali hivyo. Alimjibu Amani kwa kutoa habari zote kuhusu simu. "Ndio ipo simu ya TTCL ndani ya nyumba hiyo, iliyoandikishwa kwa jina baba yake Mwanamtama ambaye anaitwa Zaidi Halifa Mwangazi. Chombo cha simu ni kimoja tu katika nyumba hiyo, ambacho kipo sebleni…” Dallas alimjibu, na kumalizia kw a kumtajia nambari za simu iliyokuwa nyumbani kwa baba yale Mwanamtama. "Kwa hiyo nyumbani kwa baba yake Mwanamtama,Kijitonyama, kunaishi watu zaidi ya wawili, wake kwa waume wa familia moja. Nyumba hiyo hiyo ina simu ambayo inafanya kazi na bahati nzuri nambari za simu hiyo bwana Dallas unazifahamu…lakini wakati Mwanamtama hajafa na baada ya ' operation' kama ulivyoeleza mwenyewe hukuweza kupiga simu nyumbani huko Kijitonyama na kueleza hali halisi japo kwa mtu mmoja, kwa nini? Na wakati wewe huhusiki na lolote linalohusu utolewaji mimba ya Mwanamtama? Ni kitu gani kilichokufanya uhofie wakati wewe huna hatia yeyote ile katika tukio zima lililotokea?" Dallas alikunja uso na kumkazia macho Amani, kisha akajibu kwa taratibu na sauti ya chini kwa kusema, "Sikumfahamisha jamaa yeyote wa marehemu Mwanamtama, kwa sababu jambo lenyewe la kuwa na mimba lilikuwa halifahamiki kwa mtu yeyote wa familia ya Mwanamtama!” “ lsipokuwa wewe…Dallas?" Amani aliuliza kwa njia ya maelezo huku akimkodolea macho. "Ndio, isipokuwa mimi!” Dalas alijibu kwa sauti ya kushangaa. “Kwanini iwe ni wewe tu Dallas uliyekuwa ukijua ujauzito wa marehemu Mwanamtama katika familia nzima? Familia ambayo wapo dada zake, wapo kaka na bibi yake vilevile ukiachilia mbali baba na mama yake mzazi?" "Ni kwa sababu aliniamini!" "Alikuamini wewe mwanamme kwa suala hili la mimba, ambaye si baba mzazi wala si kaka yake wa kuzaliwa! Na akawacha kumuamini yeyote kati ya ndugu zake wa kike aliozaliwa nao, au mama au bibi yake, ambao ni wanawake?" Zablon Mkuki alisimama baada ya kumsikia Amani anasema hivi, aliinamisha kichwa kumuelekea hakimu kisha akasema: "Samahani mheshimiwa hakimu, inaonekana wakili mtetezi hana hoja ya kumuhoji shahidi Dallas, analojaribu kufanya ni kumbabaisha shahidi na kupoteza muda. Suala la mtu kumuamini mtu, halina ulazima wa kuwa mtu huyo ni mwanamke au mwanaume. Hakuna sheria ya mila, dini wala serikali inayosema kuwa mwanamke ni lazima amuamini mwanamke mwenzake tu, au mwanamke hana ruhusa kumuamini mwanamme!" Hakimu alinyanyua kalamu yake akaandika katika karatasi zake alizokuwa nazo juu ya meza kisha akaitua kalamu hiyo na kumuangalia Amani na kumuuliza: "Wakili mtetezi, unacho cha kuongeza?" "Ndio mheshimiwa hakimu!" "Umemsikia wakili wa upande wa mashtaka alivyosema? Jaribu kuwa muwazi na fanya haraka kwa shahidi, tafadhali. Unaweza kuendelea!" Amani alitoa tabasamu kubwa la shukrani mbele ya hakimu akatoa heshima, kisha akamgeukia tena Dallas, ambaye alionekana wazi surani kwake kwamba alimchukia mno Amani kwa wakati ule. "Bwana Dallas Meja, hivi ni kwa nini ulimfungia dokta lmu alipokuwa na Mwanamtama wakati huo hali yake ikiwa ni mbaya sana, lakini bado hajafa. Ulipokuwa unawapigia simu polisi na kuwasubiri kwa nini uliwafungia kwa nje na ufunguo?" "Nilifanya hivyo nikiamini kuwa kama sikufunga mlango kwa ufunguo, dokta Imu angeweza kwenda zake!" Amani alitikisa kichwa kwa masikitiko, halafu akaendelea kumuuliza, "Bwana Dallas Meja, nakumbuka uliiambia mahakama kuwa Dokta lmu alitaka au alitoa ushauri wa kwamba Mwanamtama kabla hajafa apelekwe hospitali?" "Ndio alitoa ushauri huo!" "Kwanini hukutaka kuufuata?" "Kwa sababu nilijua kuwa dokta lmu atakapofika hospitali, angeweza kutafuta njia ya kulikwepa hili tukio alilofanya la kutoa mimba!" "Lakini je, bwana Dallas…hukufikiri kuwa maisha ya Mwanamtama penginepo yangeweza kuokolewa na umauti?”
Dallas aliinamisha shingo yake chini na kubaki kimya pasipo kutoa jibu. Amani alimpa muda wa sekunde chache na alipomuona kuwa hana jawabu la swali hilo, alimwambia: "Nadhani hilo hukulifikiria bwana Dallas Meja, kwa hiyo ngoja nikuulize swali jingine... uliiambia mahakama kwamba Mwanamtama, kabla ya kifo chake, mara baada ya kufanyiwa utoaji wa mmba, alikupa ulichokiita 'business card' arnbayo ilikuwa ina jina na nambari za simu ya Dokta lmu…" Dalla alionekana kugwaya kidogo na kwa sauti iliyojaa wasiwasi alijibu: “Eeeh! Ndiyo alinipa 'business card' ya Dokta lmu!" "Tafadhali bwana Dallas ninakuomba uioneshe mahakama, hiyo uiitayo 'business card' uliyopewa na marehemu Mwanamtama!" Bwana Dallas alianza kutokwa na jasho na badala ya kutoa alichoambiwa atoe akatoa kihanjifu kutoka mfuko wake wa suruali na kujipangusa jasho lililokuwa likimtoka juu ya paji lake la uso na shingoni. Amani alimuangalia kwa makini na kutambua kuwa suala hilo la 'business card’ nalo limempa shida Dallas. Kabla hajaendelea na kumuuliza maswali mengine, Amani alimuomba hakimu amruhusu yeye Amani amuulize maswali machache mtuhumiwa Dokta lmu, kisha ndipo aendelee tena na Dallas. Hakimu alitoa ruhusa. Amani alisogea upande wa kizimba alichosimama Dokta lmu na kuanza kumuuliza kwa kumwomba, "Tafadhali Dokta Imu ninaomba uioneshe mahakama 'business card' yako, au kama hunayo hapo ulipo, kama yupo jamaa yeyote uliyewahi kumpa, na yuko hapa mahakamani basi mtaje ili mahakama iombwe imuache mtu huyo atoe card hiyo... kama atakuwa nayo!" Dokta lmu alitabasamu kidogo kisha akasema kuiambia mahakama: "Mheshimiwa hakimu ninaithibitishia mahakama yako tukufu kwa kuapa kwa imani ya dini yangu kwamba, pamoja na kuwa ninayo simu ya kiganja na ninayo kazi ya kuajiriwa yenye wadhifa wa udaktari, lakini mpaka leo hii sijawahi kutengeneza au kumiliki 'business card' yeyote ile, licha ya kuambiwa kuwa nilimpa mtu!" Amani alimuangalia lmu kwa uso mchangamfu na wenye kuridhika na jawabu alilotowa, kisha akaendelea kumuuliza swali la msisitizo wa jawabu lake: "Ina maana lmu wewe hujawahi kuwa na 'business card' ya kwako wewe mwenyewe?" "Hapana, bado sijawahi kumiliki 'business card' yangu mimi mwenyewe!" Ndugu Zablon Mkuki aliyekuwa amekaa kimya kwa muda mrefu, alizuka akaomba apewe ruhusa ya kutoa maelezo kidogo, naye aliruhusiwa. "Mheshimiwa hakimu, wakili mtetezi anamuongoza anayemtetea ndugu Imu aseme analolitaka aseme, ambalo ni kukataa kwamba yeye Imu amewahi kumiliki 'business card' zenye jina lake na namba yake ya simu, na ndio maana lmu anakataa, kusudi ionekane kuwa ndugu Dallas amesema uongo, kitu ambacho sio kweli. Ukweli ni kuwa Dallas alimpigia dokta lmu simu, na Dokta lmu alipata na kupokea simu hiyo, isitoshe akatekeleza ujumbe wa simu hiyo ambao ni kuflka nyumbani kwa Dallas, Upanga. Angeweza kuipata vipi namba ya simu ya dokta lmu, kama sio kweli marehemu Mwanamtama alimpa 'business card' Dallas kabla hajafa?" Zablon Mkuki alisema hayo na kukaa. Hakimu alimruhusu Amani aendelee na mahojiano yake. Ndipo Amani aliposema: "Mheshimiwa Hakimu, Dokta lmu hana ‘business card’, na wala hajawahi kutengeneza ‘business card’. Dallas hakupewa 'business card' na marehemu Mwanamtama, na ndio maana akawa hana jibu kuhusu suala hilo. Dallas ndiye muhusika mkuu Mheshimiwa Hakimu…na ndiye aliyesababisha kifo cha Mwanamtama!" Watu wote waliokuwepo mahakamani walinyanyua nyuso zao na kumuangalia Dallas, ambaye yeye mwenyewe hakumtazama mtu yeyote zaidi ya Amani. Alikuwa akimuangalia Amani kwa jicho la kuuwa, naye aliendelea kuieleza mahakama kwa kuzielekeza tuhuma kwa Dallas. "Mheshimiwa Hakimu, kutokana na ushahidi uliotolewa mbele ya mahakama yako tukufu, ndugu Dallas Meja, ambaye ametajwa kuwa ni shahidi namba moja inaelekea ndiye aliyesababisha kifo cha Mwanamtama. Yeye peke yake ndiye aliyefahamu kuwa marehemu alikuwa ana mimba. Ni yeye ndiye ambaye licha ya kuijua namba ya simu ya nyumbani kwa baba yake marehemu, pamoja na kuijua familia nzima ya marehemu, alishindwa kupiga simu kwao wakati Mwanamtama alipokuwa mahututi, kwa sababu yeye Dallas ndiye muhusika wa mimba ile…aliihofia familia ya marehemu. Ameweza kujua kila kitu kuhusu familia hiyo kwa vile yeye ndiye aliyekuwa 'boyfriend’, au hawara, wa marehemu Mwanamtama…na ndio maana Mwanamtama akawa anakwenda Upanga nyumbani kwa Dallas kwa shida zake zote zinazohusu ujauzito huo…kwa vile Dallas ndiye muhusika. “ Mheshimiwa hakimu, ndugu Dallas ndiye aliyejaribu kumtoa mimba Mwanamtama bila mafanikio, na ndipo baadaye akababaika, na bila shaka katika kuhangaika kwake huko akafanikiwa kupata jina la Dokta Imu pamoja na la mchumba wa Dokta lmu, Zainab…na namba yake ya simu. Hapo ndipo alipoona kuwa ndio nafasi ya yeye kujivua kutoka kwenye hatia hiyo na kumvisha Dokta Imu asiye na hatia. “Alimpigia simu Dokta Imu, na Imu alipokubali kwenda Upanga, Dallas akaona kuwa mtego wake umenasa. Dokta lmu alisisitiza suala la kumpeleka Mwanamtama hospltali, lakini Dallas alikataa. Kwa nini? Kwa sababu alikwishajua kwamba maisha ya Mwanamtama yalikuwa katika hatari yakisubiri saa na wakati, na kama angekubali kwenda hospitali, wa kwanza kutuhumiwa angekuwa ni yeye Dallas na wala sio Dokta lmu. Ndipo alipomfungia Dokta lmu chumbani kwa ufunguo, akijua fika kuwa Mwanamtama kwa wakati ule angekata roho, na ndivyo ilivyokuwa. Lngawa suala la hospitali alilikataa, lakini ndugu Dallas hakusita wala kukawia kupiga simu polisi, kwa vile alikuwa ana haraka ya kumtia hatiani Dokta lmu. Mheshimiwa Hakimu, kwa ushahidi zaidi kuwa Dallas ndiye mwenye hatia, ni kule kuleta vifaa vilivyotumika kwa kutolea mimba, na la mwisho na ukweli kabisa, ni kuwa siku ya Jumamosi ya tukio hilo wakati alioutaja Dallas kwamba marehemu Mwanamtama alikuwa anafanyiwa operasheni ya kienyeji ya kutolewa mimba, Dokta lmu kwa wakati huo na tarehe hiyo na siku hiyo, alikuwa yupo sehemu nyingine na mtu mwingine! Kwa hiyo haiwezekani kabisa Dokta lmu huyo mmoja kuwa sehemu mbili kwa wakati mmoja. Ni dhahiri kuwa ndugu Dallas ndiye aliyekuwa akifanya shughuli ya kumtoa mimba Mwanamtama. Mimba ile aliyokuwa amempa yeye mwenyewe. Kwa hiyo Mheshimiwa hakimu, ninaiomba mahakama yako tukufu imtie hatiani ndugu Dallas Meja na kumuachia huru ndugu lmu Kasongo. Ahsante." Amani baada ya kusema haya yote alirudi palipokuwa na kiti chake akaketi. Hakimu aliendelea kuandika na mwisho alinyanyua uso wake na kusema: "Kesi hii lmehairishwa mpaka baada ya wiki mbili kutoka leo.” Pia akaomba pande zote mbili, kama kuna ushahidi wowote zaidi uhusuo kesi ile basi upelekwe siku hiyo iliyopangwa ya kusikiliza kesi tena. Wakati kwa siku ile ulikuwa umekwisha, kesi ya Dokta lmu ilikuwa ya mwisho kusikilizwa kwa siku hiyo. Mahakama bado iliamuru Dokta lmu abaki kuwa rumande, na Dallas hakutiwa ndani ingawa aliambiwa ni lazima awepo siku hiyo nyingine ya kusikilizwa kesi ile kwa vile ushahidi wake bado ulikuwa unahitajika na pia aende na vielelezo zaidi kama vipo.
***** Wakati takriban watu wote wamesambaratika kutoka mahakamani hapo, Amani alikuwa amesimama nje ya mahakama akizungumza na mzee Mussa na Jabir, ghafla alikuja mtu mmoja kwa kasi mpaka pale walipokuwa wamesimama, mtu huyo alikuwa Dallas. Alipofika karibu yao alitoa salamu, kisha akanyoosha mkono wake na kumpa Amani kiganja. Bila ya hofu yeyote Amani alikipokea kiganja hicho kwa kukikutanisha na chake. Dallas ki- umri alikuwa ni mkubwa kuliko Amani kwa zaidi ya miaka kumi na tano, lakini kwa kimo na maumbile na rangi yao ya ngozi vilifanana kidogo. Dallas alitoa tabasamu kubwa na kutamka kumuambia Amani, "Hongera bwana mdogo wakili, unaonekana una kipaji na ni hodari mno wa kutetea unaowatetea lakini nasikitlka kukua•mbia kuwa unayemtetea ndiye mwenye hatia na wala sio mimi uliyetangaza kunitia hatiani . . . hutashinda nduguuu....!” Amani alitoa tabasamu kubwa lililofanana na la Dallas na litokalo kwa mtu anaejiamini, aljitambulisha kwa Dallas bila hofu yoyote, "Amani...Amani Mirambo...wakili Amani Mirambo!" Akatulia kidogo, kisha akaendelea kumwambia, "Bwana Dallas Meja, na mimi ninasikitika kukujulisha kuwa dokta lmu hana hatia, na kama unasema siye wewe uliye na hatia basi nina hakika kwamba unamjua mwenye hatia ni nani, lakini sio Dokta Imu!"
Dallas, kwa mastaajabu ya wote waliokuwepo pale aliangua kicheko kikubwa sana wakati Amani, Mzee Mussa na Jabir wanamtazama. Jabir alikuwa hamuangalii tu bali alimkodolea macho na kumtazama vizuri sana. “Unajua wakili Amani, ninatakiwa, au tuseme inanibidi, nikuchukie sana kwa sababu ya yaliyotokea muda mchache uliopita ndani ya chumba cha mahakama, lakini badala yake ninahisi ninakupenda wakili Amani! Kwa nini tusijaribu kuwa marafiki? Nani anayejua? Penginepo siku moja nitakuhitaji uwe mtetezi wangu katika kesi nyingine sababu katika kesi hii nina hakika utakwama tu." Dallas alisema huku akiendelea kucheka. Amani alimuangalia na kujaribu kumpima akilini mwake, ili aweze kutambua alikuwa anakabiliana na mtu wa aina gani. Kitu kimoja alichojithibitishia ni kuwa Dallas, kwa vyovyote vile atakavyokuwa, ni mtu mjanja sana, ni lazima achukue tahadhari. Lakini hapo hapo alifikiri kuwa ipo haja ya kumtambua zaidi, huenda akapata kitu kitakachomsaidia katika kumtetea Dokta Imu. Kwa hiyo aliamua hapo ajaribu kidogo kuwa mjinga mbele ya Dallas kwa kumkubalia anavyotaka. "Hakuna shaka bwana Dallas, na tujaribu kuwa marafiki…huenda na mimi nikapata hisia za kukupenda, sababu sasa hivi ninakuchukia sana, hasa kwa ajili ya uzushi uliomzushia Dokta lmu." Dallas aliguna kidogo kisha akatabasamu na kusema: "Sawa basi wakili Amani. Niruhusu nikutembelee nyumbani kwenu, tutazungumza mengi tutakapopata nafasi." "Karibu sana nyumbani kwetu, wakati wowote kwani pamoja na kukuchukia lakini sikuogopi! "Nami pia sipendi uniogope Wakili Amani. Ningependa uniheshimu tu kwa vile ni mkubwa kuliko wewe...kwa heri Amani, tutaonana siku nyingine!" Dallas alimjibu na kuondoka kama alivyokuja, kwa mwendo wa haraka haraka na kuwaacha akina Amani wanashangaa. Mara baada ya kuondoka Jabir alimgeukia Amani na kumuambia: "Amani, jihadhari sana na mtu yule, kata kabisa kuwa karibu na jamaa yule tafadhali. Mimi nimemuangalia sana na nimemtambua kuwa nimemuona kabla ya hapa." Amani akawa anavutiwa na maneno ya Jabir yahusuyo Dallas, akatega masikio na kumuuliza: "Unasema umewahi muona Dallas kabla ya kumuona hapa?" "Ndio bwana! Nimekwisha muona jamaa yule lakini alikuwa anajiita kwa jina jingine!" Mzee Mussa pamoja na Amani iliwabidi wamtulizie macho yaliyojaa shauku ya kutaka kujua zaidi. "Ndio...!"Jabiri aliendelea kueleza, "Yule jamaa anayejiita Dallas nimewahi kumuona Arusha tena mahakamani hivi hivi. Siwezi kukosea, ndiye yule…lakini wakati huo,alijiita Abdi na sio Dallas!" Jabiri alimtazama Amani na kumuuliza, "Hapa anajiita Dallas nani?" "Anajiita Dallas Meja!" "Hasa ndie yeye huyo huyo! Sababu hata huko Arusha ilikuwa ni kwenye kesi ihusuyo kashfa moja kubwa iliyozuka na kuzungumzwa na watu wa mji mzima wa Arusha,. Na huyu bwana alikuwa mmoja wa mashahidi hivyo hivyo!" Amani alijiinamia kidogo na kufikiri, k.isha akamuuliza tena Jabir: "Bwana Jabir…unasema kuwa huyu bwana huko Arusha anajulikana kwa jina la Abdi?” Jabiri alicheka kidogo na kutikisa kichwa kwa masikitiko na kujibu, “Kwenye kesi hiyo ilitokea bwana huyu kuambiwa mwongo kwa vile kila mji anakokwenda anajiita kwa jina jingine. Hasa nimekumbuka vizuri sasa, huyu bwana ndiye kabisa, ilisemekana kuwa Arusha anajulikana kama Abdi, Tanga anajulikana Dulla, Mwanza anajulikana kama Abdul na hapa Dar sasa ni Dallas…lakini kitu kimoja, ubini wake ni huo huo wa Meja." Aman, Mzee Mussa na Jabiri walitafakari na kushindwa kupata jibu sahihi kuhusu Dallas, lakini walitambua kitu kimoja…kuwa vyovyote vile itakavyokuwa, Dallas atakuwa ni tapeli, muongo na mtu asiyeeleweka.
******** Wiki moja na siku tano tangu kesi ilipoahirishwa na siku mbili kabla ya kufikia siku hiyo iliyopangwa kesi ya dokta lmu kusikilizwa tena, wakati wa alasiri, Dallas alibisha hodi nyumbani kwa kina Amani, Masaki, baada ya kulipita lango kubwa la chuma lililokuwa wazi, ambalo ni mlango wa uzio mkubwa uliozunguka nyumba hiyo. Mlango huo wa mbele aliokuwa anaugonga Dallas ulifunguliwa kwa ndani na Dallas akajikuta anatizamana uso kwa uso na Zainab. Dakika zaidi ya moja ilipita wakiwa wanaangaliana. Dallas akiwa na tabasamu kubwa usoni mwake wakati Zainab akiwa anatetwa kwa nguvu kwa moyo kumpasuka, pasipo kusema neon lolote. Dallas alikuwa wa kwanza kuondoa hali hiyo,kwa kutamka: "Habari za hapa dada?" Zainab alishindwa hata kujibu. Alibaki kutweta na kumkodolea macho Dallas tu. Dallas alicheka kidogo kisha akasalimu tena: "Habari za hapa dada? Mbona umeingiwa na fadhaa hivyo?" Zainab alijikusuru na kumudu kutoa tabasamu la kujilazimisha, kisha akajibu: "Nzuri tu! Sijaingiwa na fadhaa! Karibu!" Baada ya Zainab kusema hivi alirudi nyuma kidogo kutoka alipokuwa amesimama kwa kutaka kumuonyesha Dallas kuwa hana wasiwasi, lakini ukweli wenyewe ni kwamba alikuwa haamini macho yake, na vile vile fikra mbalimbali zilikuwa zikizunguka ndani ya kichwa chake akiwaza “Amefuata nini huyu mtu hapa nyumbani kwetu? Naye Dallas akaichukua nafasi ya kuambiwa karibu haraka haraka akaingia ndani huku akisema: "Ahsante, asante!" Zainab akawa hana budi isipokuwa kumkaribisha na kumuelekeza sebleni huku akimwambia: “Karibu...ukae!" Dallas alikwenda na kukaa juu ya kochi moja kubwa la kukaa mtu mmoja. Mkabala na kochi hilo juu ya ukuta palikuwa na picha zilizotiwa kwenye 'frame' na kutundikwa vizuri. Moja kati ya picha zilizotundikwa juu ya ukuta huo ilikuwa ni picha ya Amani akiwa mdogo wa miaka miwili amekaa juu ya stuli ananing’iniza miguu. Na nyingine akiwa amesimama katikati ya baba na mama yake ambao wamekaa juu ya viti. Ghafla Dallas alivuta mawazo yake kiasi ya kuwa hakutazama kitu chochote wala upande wowote zaidi ya picha hizo. Alitolewa kwenye mawazo na sauti ya Zainab iliyosema: "Nikusaidie nini Bwana Dallas?” Dallas aligutuka kidogo na kuitikia: "Eeh! Nitakunywa soda; soda yoyote!" Zainab alimtazama kwa woga, sababu aliweza kumtambua tangu mwanzo alipopiga hodi kuwa yule Dallas anaemkandamiza dokta lmu mahakarnani ndie huyu huyu. Na alikuwa ameshangaa moyoni mwake kuona jamaa huyu amekuja nyumbani kwao, na alipomuuliza amsaidie nini, hakuwa na mawazo ya kumkirimu kwa chochote bali ni kumuuliza kuwa Dallas anataka nini hata akafika pale nyumbani kwao. Lakini Dallas naye mawazo yake yalikuwa kwenye picha zilizokuwepo ukutani, kwa hiyo akadhani kuwa ameulizwa atakunywa nini kutokana na kawaida iliyozoweleka anayoulizwa mgeni anapofika nyumbani kwa mtu yoyote, kwa hiyo bila kujijua akatamka kuwa atakunywa soda. Zainabu aliondoka pale sebleni na kumuacha Dallas peke yake. Baada ya dakika tatu alitokeza tena akiwa na chupa ya soda ya Coca Cola kifungulio na bilauri mkononi. Aliviweka vitu hivyo juu ya kimeza kidogo kisha akakinyanyua kimeza hicho na kukitua mbele ya kochi alilokalia Dallas. Akaifungua ile chupa ya soda, akamimina nusu ya soda ndani ya bilauri, kisha akamwambia Dallas ambaye alikuwa bado ametuliza macho yake kwenye zile picha: "Karibu soda!" Dallas alirudisha uso wake kwa Zainabu na kushukuru, "Asante, asante sana!" Zainabu aliondoka mbele ya Dallas na kwenda kukaa kwenye kochi lililokuwa mbali kidogo na kando na alipokuwa amekaa Dallas. Mara tu alipokaa, Dallas alimuuliza: "Samahani dada, hizi picha...huyu motto…nina maana hawa waliomo kwenye picha hizi ni nani?" Zainab alinyanyua uso wake ambao haukuwa na furaha na kuziangalia zile picha, kisha akauliza: “picha zipi?” "Picha hii ya mwanamke na mwanamme na mtoto..." Dallas alifafanua. Zainabu alijibu kwa sauti ya kutokupendezewa na swali aliloulizwa kwa kutambulisha: "Huyo mwanaume ni baba yangu, huyo mwanamke ni mama yangu, na huyo mtoto wa kiume ni kaka yangu Amani!" Dallas aliruka na kumuuliza Zainab kwa kurudia jawabu: "Huyu ni Amani?" "Ndio huyo ni kaka Amani alipokuwa mdogo!" "Na huyu aliyekaa juu ya stuli, si ndiye yeye huyo Amani?" "Eeeh, ndiye yeye." Zainab alijibu pasipokuwa na furaha. Kisha akajikaza na kumuuliza: "Bwana Dallas, sijui una shida gani ambayo imekuleta hapa nyumbani?" Kwa mshangao Zainab alimuona Dallas akinyanyuka kutoka pale alipokuwa amekaa, akasogea kwenye ukuta uliokuwa na picha zile alizoziulizia, na akazidi kuzikodolea macho badala ya kujibu swali aliloulizwa.
0 Comments