Header Ads Widget

Responsive Advertisement

SIMULIZI FUPI : MALAIKA WANGU


Ilikua siku ya jumapili, lakini mvua kubwa sana ilikua inanyesha.
Kijana wangu mdogo wa miaka 11 aliniuliza “Baba leo hatuendi kusambaza vipeperushi?”
Kikawaida huwa tunatembelea nyumba baada ya nyumba kila Jumapili tukitoka kanisani. Mimi ni mchungaji katika kanisa fulani na nilifanya maamuzi kuwa nitatumia muda wangu wa jumapili baada ya ibada kuwaeleza watu juu ya upendo wa Mungu. Niliandaa vipeperushi vyenye kutoa maelezo kwa ufupi.

Kijana wangu alipenda kufanya na mimi kazi hiyo na mara nyingine alinisisitiza juu ya kwenda na muda. Haikuwahi kutokea hata siku moja tumewahi kuahirisha na hata siku nilizoingiwa na uvivu na kutaka kuahirisha zoezi hilo,kijana wangu alikua hodari kunisisitiza huku akinambia jinsi gani watu wengi wanahitaji kujua juu ya upendo wa Mungu

Hali ya hewa na mvua kubwa ya siku hiyo ilinifanya niamue akilini mwangu kuwa hata kama kijana angesisitiza,nitamwambia tusiende… Swali lake lilinifanya nimuangalie kwa kumshangaa na kisha kumuuliza,”Mvua huioni?” “Kwani siku za mvua watu hawahitaji upendo wa Mungu?” Alisema. Jibu lake hilo lilinifanya nikose cha kusema lakini mimi nilikua tayari nimefanya maamuzi ya kutozunguka siku hiyo. Kwa kujua nia yangu ya kutotaka kwenda,aliniomba nimruhusu aende peke yake, na kwa jinsi alivyokuwa amedhamiria, sikuweza kumkatalia

Jumapili iliyofuata tukiwa kanisani alisimama mwanamke mmoja wa umri wa kati ya miaka 35-40. Alionekana ni mtu asiye na shida ya kifedha na haikuwa rahisi kuhisi kuwa ni mwanamke aliyepitia matatizo mengi sana ya maisha hadi kujikatia tamaa.

Alisalimia kanisa sababu alikuwa mgeni kisha alizungumza kwa ufupi ni kwanini amekuja kanisani hapo siku hiyo. “Miaka miwili iliyopita nilifiwa na mume wangu aliyekuwa mmiliki wa kampuni moja kubwa. Sikujua kuwa kampuni aliyoniachia mume wangu ilikuwa inadaiwa mpaka alipofariki. Sitaelezea kirefu lakini ndani ya miaka miwili maisha yetu yamebadilika sana. Watoto wangu tuliowalea kwenye maisha ya kifahari sana wamenipa wakati mgumu kukubali kuwa hali imebadilika kwani akili zao zimekataa mabadiliko. Maswali yao, lawama na mahitaji yamenifanya nijione kama mama nisiyewajibika ipasavyo. Kwa sasa wanasoma shule za bweni wote na nyumbani ninaishi pekeangu na wafanyakazi ambao siku za jumapili huwa nawapa mapumziko(off) wote

Usiku kuamkia jumapili iliyopita niliwaza mambo mengi sana. Pamoja na ugumu wa kiuchumi tunaopitia pia kipindi hiki nimepoteza marafiki na watu wengi wa karibu ambao wamejiweka mbali nami. Nilijiona kama mtu aliyebaki pekeyake dunia nzima. Niliwaza na kulia usiku kucha na kesho yake nilifanya maamuzi ambayo sikuwahi kudhani ningeyafikia. Niliamua kujiua. Niliona hakuna faida tena ya kuishi kwenye dunia ambayo hainihitaji tena. Nikiwa chumbani,juu ya kiti,tayari nimetundika kamba, nilisikia mlango ukigongwa. Nilisema kuwa nitaacha anayegonga agonge mpaka achoke kisha akiondoka nitaendelea,lakini ilinishangazwa kuona kuwa huyo mtu hakuchoka. Alipiga hodi muda mrefu sana kiasi kwamba niliona bora nikamfungulie. Nilishangaa kuona kijana mdogo aliyekuwa amelowa na mvua kubwa ilokuwa inanyesha akinisalimia.

Nilimuuliza shida yake akaomba aongee na mimi kidogo. Kijana huyu ambaye mimi namuita Malaika alinieleza kwa kifupi juu ya rafiki ambaye ananipenda sana. Alisema kuwa nikimkubali rafiki huyo ataondoa upweke wangu. Kijana huyo alinieleza juu ya upendo wa Mungu na kisha kunipa kipeperushi chenye maelezo zaidi na anuani ya kanisa hili. Niliposoma kile kipeperushi, si tu kuwa nilighairi juu ya uamuzi wangu wa kujiua, bali pia niligundua kuna maisha mema mbele yangu Mungu ameyakusudia. Leo hii wiki moja imepita lakini nimejihisi kama Mungu amerejesha furaha yangu iliyopotea miaka miwili iliyopita. Kama yule kijana, malaika aliyeyaokoa maisha yangu yuko hapa, naomba nimjulishe kuwa siku ile Mungu alimtuma kwajili yangu”
*********** MWISHO *********

Post a Comment

0 Comments