Mara yangu ya kwanza kuja Dar es Salaam, rafiki yangu Tonny alinizungusha kariakoo. Mwanza pamechangamka lakini mji huu ni hatari. Kuna kila aina ya bidhaa, na nyingi hupatikana kwa bei rahisi kuliko Mwanza, hasa za madukani. Tulipita sehemu moja, kununua nguo za ndani maarufu kama boxer, mtaa wa DDC. Niliona boxer nzuri zilizouzwa kwa bei nafuu, nikachanganyikiwa kidogo lakini Tonny akanipeleka duka ambalo alidai ni mteja hapo. Nilitegemea angemchangamkia muuzaji, ama kuonesha anamfahamu, lakini ilikuwa tofauti. Walisalimiana kama watu wasiojuana kabisa, huku mimi nikiwa nimetoa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango.
Nilishindwa kujizuia kumkodolea yule dada muuzaji, kiasi cha yeye mwenyewe kujistukia, hivyo akanitazama na kutabasamu, na kunipa salamu ambayo kwa mara ya kwanza ni kama sikuisikia japo niliisikia. Mara ya pili akanistua tena kwa kuniita, “Kaka, habari yako?”. “Oh, nzuri, za kwako mrembo?”, nilijibu kwa aibu.
Tonny alimuulizia mwenye duka, nikaelewa kumbe yule mrembo hakuwa mwenye duka au muuzaji wa awali.”Ametoka kidogo, ameenda kuniulizia boxer fulani kwa rafiki yake, hapa zimeisha. Lakini naweza kuwauzia chochote mnachohitaji, hakuna shida, pia kama hamniamini, jirani yake huyo anamlindia”. Alizungumza huku akionesha tabasamu mahiri. Hakujua muonekano wake usingefanya mtu yeyote kutomuamini. Kusikia hayo maelezo, moyo wangu ulisononeka kidogo, kwani maelezo yake yalionesha aidha ameolewa ama yuko kwenye mahusiano imara. Baada ya muda mfupi, alikuja muuzaji, aliyezoeana vizuri na Tonny, akampa yule dada mzigo wake, kisha binti akaondoka.
Tulinunua tulichohitaji kununua, tukaondoka, akilini nikiwa na mawazo utadhani nimepoteza hela. Tonny alianza kunicheka, jinsi nilivyomshangaa yule binti ambaye kwa bahati mbaya hata jina au namba ya simu yake sikufanikiwa kuuliza. Tonny ananijua kuwa mimi si kijana ninayezuzuka na mabinti, na nina misimamo yangu fulani kuhusu mahusiano. Hata kwangu pia ilikuwa ni ajabu kuvutiwa na msichana kiasi kile, kwa mara ya kwanza tuu namuona. Miezi miwili iliyopita tuliachana na aliyekuwa mpenzi, bila sababu ya msingi naweza sema, kwani chanzo cha kukosana kilikuwa kidogo sana, kikapelekea kukorofishana mpaka kuachana. Nadhani ni kama nilimsukuma aliyechuchumaa, kwani kabla ya hapo viliwahi kutokea visa kadhaa kuniashiria kuwa Anitha, mpenzi wangu huyo, hakuwa ananipenda tena. Hata hivyo si lengo langu kuelezea sana uhusiano wangu uliopita.
Nilirudi Mwanza, wiki mbili baadaye. Nikaendelea na biashara zangu za kusambaza bidhaa za kula kwenye maduka na supamaketi mbalimbali pale Mwanza. Huwezi amini, akili yangu ilishindwa kupuuza sura ya mrembo niliyekutana naye kariakoo, kwa muda wa miezi kadhaa. Siku ile nilipomtazama kwa kuduwaa, niliona uzuri wa ajabu kwa binti yule. Rangi yake ni ya kahawia, si nyeusi lakini si mweupe pia. Ngozi laini kama ya mtoto, yani utadhani hajawahi hata kung’atwa na mtu. Alipotabasamu, (nadhani anajijua ana tabasamu la kuvutia sana), meno yake meupe sana yalionekana, na kama pengo dogo upande wa kushoto wa kinywa chake pia nililiona kwa mbali nalo liliongeza mvuto. Zaidi ya hayo, mrembo huyu aliongezewa kionjo cha dimpoz katika uumbaji wake, mashalaah, Mungu fundi jamani! Macho yake meupe, makubwa kiasi, niliwaza akilini mwangu, akiwa ndio yuko mikononi mwangu ananitazama kwa mahaba itakuaje? Sitaki kuongelea umbo lake kwani sikupata fursa kulitazama kwa ufasaha, lakini kwa sekunde chache nilizomtizama akiondoka pale dukani, naweza sema ile ni namba sita ndefu, nadhani unanielewa.
Kwa jinsi alivyoiteka akili yangu, haikuwa ajabu kumuota mara kadhaa. Niliota nimekutana naye tena, na mara hii nikamuomba namba yake. Lakini mara ya pili niliota niko naye eneo zuri, kama wapenzi, huku tukifurahia kila mmoja wetu hiyo fursa. Asubuhi kuamka, Kumbe! Ni mawazo na hisia zangu hunipeleka mahala ambapo hakuna matumaini ya kufika. Kumuwaza yule mrembo mara zote kulinisaidia kumsahau kabisa Anitha, kwani mpaka wakati huo nilikuwa nikijaribu kumbembeleza kwa simu turudiane, huku nikiambulia vichambo na matusi. Basi maisha yaliendelea hivyo, kwa miezi kadhaa, nikamkatia tamaa Anitha kabisa, nikawa mpole, nikifarijiwa na hisia zangu hewa za binti mrembo, ambaye hakuna matumaini hata tone ya kumuona tena.
Miezi kadhaa mbele nilipata wazo la kupanua biashara yangu, huku nikiangalia fursa ya kutoa nguo Dar es Salaam kuuza Mwanza. Niliamua nitalenga nguo za ndani, hivyo nilitembelea baadhi ya wadau wangu wenye maduka ya nguo na kuwaonesha sampo za hizo nguo nilizotaka kuuza. Nilipata muitikio mzuri sana, labda kwa sababu ya uzoefu wangu katika biashara, na uwezo wa kutumia lugha vizuri. Niliamua kuanza biashara kwa kusafiri tena ili kupata mzigo. Nilipomshirikisha Tonny alinishauri kwa mzigo wa mwanzo tutachukua kwa yule rafiki yake huku akijaribu kumuuliza wapi anapopata mzigo, na kupata muongozo. Nilianza biashara, nashukuru dada muuzaji hakuwa na hiana, wala hakuogopa kupoteza wateja au kutengeneza ushindani. Alitupa ushirikiano mkubwa, hatimaye mzigo wa tatu niliufata nchini Uganda. Biashara ilinoga haswaa, huku nikiendelea na ile ya awali, kwani ilikuwa imethibitika kwa muda mrefu na yenye wateja wakudumu. Sasa maisha yangu yalikuwa bize sana kiasi cha kutonipa nafasi ya kuwaza chochote kuhusu mapenzi. Sikumkumbuka tena mpenzi hewa niliyekutana naye kariakoo wala Anitha ambaye ninauhakika naye alishanisahau kabisa.
Mwaka mzima ulipita, na wa pili, nikiwa singo kama wanavyosema vijana wa mjini. Biashara zilichanganya, kuna wakati nilipigwa, yaani niliibiwa kidogo na vijana wangu, lakini si kiasi cha kunitia hasara. Niliongeza mtandao, na marafiki katika biashara, kwani nilianza kuwa mkombozi katika upatikanaji wa nguo za ndani kwa urahisi na kwa bei nafuu pale Mwanza. Baada ya muda nilikutana na binti mwingine, tukaanza mazoea na kuwa kama wapenzi. Nadhani nilichoshwa na upweke na kuamua kuwa kwenye mahusiano, japo sikuwa nimemaanisha sana. Mungu anisamehe, kwani mpaka leo nahisi sikumtendea haki yule mpenzi wangu mwingine baada ya Anitha. Utanielewa baadaye.
Miezi michache tena ikapita, nikiendelea na biashara zangu na uhusiano wangu wa kupotezea muda. Nakumbuka siku moja, nikiwa Dar es Salaam, nikisubiri safari yangu kufata mzigo Uganda, siku moja kabla ya safari. Nikiwa kwa rafiki yangu Tonny, tunakula chakula cha mchana kilichoandaliwa na mkewe mpya (walikuwa na mwaka tangu waoane), Tonny alipigiwa simu na jamaa yake fulani akimualika kwa chakula cha jioni. Ni rafiki yake, walisoma naye miaka sita ya sekondari, waliishi naye chumba kimoja, kwa wakati huo walikuwa wamepotezana kama miaka miwili huku huyo jamaa akiwa jeshini ambako hakutakiwa kuwa na mawasiliano na watu. Alipopokea simu, alipata msisimko na hakutaka kutakaa kabisa ule mualiko. Alianza kutushawishi mimi na mkewe twende naye, lakini mke wake aliyekuwa na mimba changa hakutaka kusumbuka kabisa. Nilitaka kumkatalia pia, ili nijiandae na safari kesho yake, lakini alinishawishi sana, nikashindwa. Tukamuacha mkewe, na binti wa kazi, tukaondoka.
Tulikutana hoteli moja nzuri mjini Dar es Salaam, maeneo ya Posta, inaitwa Ramada. Tulifika, na kuongoza kwenye meza moja yenye watu wawili, mwanaume na mwanamke, walioonekana ni wapenzi. Lahaula! Sikutaka kuamini macho yangu kile nilichoona mbele yangu. macho yangu yaligonga moja kwa moja katika sura ninayoifahamu, ya binti aliyewahi kunivutia kuliko wanawake wote kabla. Msichana niliyemuota na kutamani kuwa naye kuliko mwanamke mwingine yeyote. Ghafla akili yangu ilihama, nikajihisi kuchanganyikiwa, nikatamani tungeipita ile meza, yani wasiwe ndio hao watu ambao tutakaa nao. Lakini nikiwa katika lindi la mawazo, nilijikuta tayari tumekaa kwenye meza hiyo hiyo, na muhudumu ameshafika kutusikiliza. Tonny na rafiki yake walisalimiana kwa furaha, Tonny akanitambulisha, huku nikiwa kama mtu aliyenyeshewa. Tukatambulishwa pia huyo mrembo, aliyeitwa Ninah, ambaye jamaa alisema ni mkewe mtarajiwa. Rohoni nikajisemea,”bora ni mtarajiwa”, huku nikijipa matumaini kwa mbaali kwamba kama bado hawajaoana pengine bahati inaweza kunigeukia.
Marafiki wawili walifurahiana, wakipiga gumzo za hapa na pale, huku kwa namna fulani wakijaribu kutufanya mimi na yule mchumba wa jamaa tusijisikie wapweke. Kiukweli akili haikuwa hapo. Kila wakati nilimtupia Ninah jicho la wizi, huku nikitamani azungumze. Kuna wakati alizungumza kidogo, basi nikamuitikia kwa shamra mpaka nikajistukia. Tuliendeleza zogo kwa muda, lakini nilijihisi nahitaji kwenda kupata pumzi, nikainuka kwenda uani. Yaani muda wote niliokaa pale pezani nilihisi hewa hainitoshi. Nilikuwa na hisia mchanganyiko, furaha ya kumuona mrembo wangu kwa mara ya pili, ambaye sikutegemea, lakini pia sikuwa na namna ya kumuiba mrembo huyo kwa jamaa hivyo niliishia kujisikitikia. Niliinuka na kwenda uani, nikajiangalia kwenye kioo, huku nikijiambia,”Ni sawa tuu Balongo, sio wako. Inatosha kumuona kwa mara nyingine na walau kukaa naye meza moja”.
Nilirudi, na haikuchukua muda tukaondoka. Kesho yake nilisafiri, nikimuwaza Ninah akilini, lakini walau nilifanikiwa kumuona kwa mara nyingine, kujua jina lake na zaidi kujua anafanya wapi kazi. Akilini mwangu hakuondoka kuanzia wakati huo, japo nilijilazimisha kumtoa. Sijawahi kupenda hivi, wala kuhisi kama naweza kumpenda mwanamke ghafla kiasi hiki. Ninah aliingia akilini mwangu, aliingia moyoni mwangu, alichukua nafasi ndani yangu kiasi ambacho sikutegemea. Sauti ya maneno machache aliyoongea usiku ule ilijirudia kichwani mwangu kana kwamba yalinihusu mimi. Sura yake haikuniacha akilini hata dakika moja. Hisia hizo zilinipa raha kiasi, kwani niliiruhusu akili yangu imuwaze, iwaze uzuri wake na kila kizuri kumuhusu. Lakini wakati huo huo zilinipa mawazo, na huzuni pia kwani ni kama nilijaribu kujenga ghorofa hewani. Nilifarijika kwa kumuwaza tuu, hivyo safari nzima nilimuwaza binti huyu aliyeuteka moyo wangu kwa kasi.
Maisha yaliendelea kwa miezi kadhaa, nikaendelea na biashara zangu. Kila nilipowasiliana na Tonny nilimuuliza kuhusu rafiki yake. Sikutaka kumwambia kuwa Ninah ndiye binti aliyenipagawisha siku ile kariakoo kwani Tonny hata hakukumbuka ile sura. Nilijaribu kuulizia habari zake za kuoa, huku nikimdodosa kujua kama anamaanisha kumuoa Ninah, japo sikutaka kudodosa sana kwani Tonny angenistukia. Haikupita muda mrefu, nilitafuta tena safari ya Dar es Salaam, kama kawaida nikaenda kwa Tonny ambaye hata baada ya kuoa hakuwa ananiruhusu nifikie hotelini. Siku moja usiku, mkewe akiwa amelala nasi tuko sebuleni kuzungumza kidogo, niliuliza tena habari za jamaa na kama ana nia kweli ya kuoa. Alistuka kidogo, akaniuliza kwanini nafatilia sana habari za huyo jamaa yake. Sikumwambia, lakini nilikazana kuuliza, akaniambia, “Jamaa si muoaji. Labda kama amebadilika sasa hivi, lakini kipindi chote namfahamu huwa, kila binti anayenitambulisha ni kama atamuoa mwezi ujao, lakini ukikutana naye wakati mwingine unamkuta na msichana mwingine”. Kwangu hiyo ilikuwa habari njema sana, hakujua tuu.
Niliacha kuuliza habari hizo tena kwa muda, lakini nikaamua kufanya jitihada zangu binafsi kumtafuta Ninah. Kipindi hicho nilikaa Dar kama mwezi mzima, kiasi cha Tonny kushangaa imekuaje, lakini sikumwambia nini hasa kimenikalisha. Kwa asili, sipendi kuonesha udhaifu wangu juu ya wanawake, hivyo japo Tonny ni rafiki yangu wa ndani sana, sikutaka kumuonesha kiasi gani Ninah aliiteka akili na moyo wangu, hasa kwa kuwa bado hakukuwa na mwanga wowote wa kumpata.
Nilimfatilia alipofanya kazi, nikafanikiwa kumpata, lakini sikujionesha kwake. Niliamua kutumia mbinu fulani kumvuta karibu kwanza, kabla hajanifahamu. Nilianza kumtumia zawadi, huku nijitambulisha kama secret admirer yaani akupendaye kwa siri. Nilifanya hivyo, kwa ujanja, mara kadhaa. Nikaondoka na kurudi Mwanza, na kuendelea kutuma zawadi kadhaa zenye hamasa ya mapenzi. Sikujua anazichukuliaje, labda sikutaka kujua kwa wakati huo. Kiasi, naogopa kukataliwa, pengine nina moyo muoga wa maumivu, hivyo nilijaribu mbinu ambayo ingenipa nafasi ya kukubalika kiurahisi. Kwenye mizigo au parcel nilizomtumia, niliambatanisha na jumbe fupi, nikimsifia, kumwambia namna nilivyohisi mara ya kwanza namuona, na mambo mengine mengi. Sikumpa anuani wala kumpa fursa ya kunijibu. Nilifanya hivyo kwa miezi mitano mfululizo, ndipo nikapanga kuonana naye.
Nilimtumia mzigo wa mwisho wenye ujumbe wa kumuomba kumuona, na namba yangu ya simu, nikimsihi sana anipigie ili tuonane. Hapa nilikuwa narusha kete zangu nikiwa na matumaini kidogo kuwa angenipigia. Hatima ya mimi na huyu mrembo kuwa pamoja ilikuwa juu yake, kama angepiga simu. Nilipata mawazo sana tangu nilipotuma ile parcel kwani hapo ndipo nilielewa nilishapenda kiasi gani. Kitendo cha kukaa siku kadhaa nikisubiri anipigie huku nikishindwa kufuatilia kama kweli atapiga au la, kilinipa mawazo kiasi cha kunipungua uzito.
Siku zilipia, tofauti na matarajio yangu ukapita karibu mwezi mzima, kiasi cha kunifanya nikate tamaa kabisa. Lakini nakumbuka siku kama ya 27 au 28 hivi tangu nitume ule mzigo, nikasikia simu inaita nikiwa bafuni. Nilitamani kutoka na povu kichwani, kwani kwa wakati huo wote sikuwa najiruhusu kukosa simu hata moja. Nilipotoka haraka sana nilishika simu yangu na kuona namba mpya. Lahaula, moyo ulistuka, nikasema ndio nshamkosa hapa. Nilishika simu kupiga huku moyo ukienda kasi kama treni ya umeme, na sijui kwanini akili yangu yote iliniambia ndiye, kwani kama mfanyabiashara haikuwa kitu cha ajabu sana kupokea simu mpya. Lakini nadhani siku hiyo moyo wangu uliamua kunielekeza kwa Ninah. Nilijaribu kupiga lakini haikupokelewa, hapo nikakata tamaa kabisa. Lakini baada ya kama nusu saa simu iliita tena, namba ile ile, nikiwa nimejilaza kitandani kwangu na kuitizama kana kwamba nimeambiwa nisubirie. Niliipokea nadhani kabla aliyepiga hajajua kama imeanza kuita. Ikasikika saauti ya kike
Kwenye simu: Halo!
Mimi: Halo, habari? (nikajibu huku nikiisikilizia sauti, na kujaribu kuwa na sauti nzuri ya kiume na ya upole)
Kwenye simu: Nzuri, naongea na Maxwel? (mzigo wa mwisho kumtumia uliokuwa na namba ya simu, nilijitambulisha kwa jina hilo moja)
Mimi: Ndio, hujakosea, nani mwenzangu? (hapo sasa nilibakiza hatua moja kuhakikisha kwamba huyu ndiye. Sikungoja tena kusikiliza sauti, ilibidi nimuulize)
Kwenye simu: Naitwa Ninah
Sikusubiri aendelee kuzungumza au kujieleza zaidi. Nilipiga kelele, bila hata mimi mwenyewe kujua imekuaje nimepiga kelele kubwa namna hiyo. Lakini nilijikuta nashangilia kwa sauti, huku nikimshukuru sana kwa kupiga nisijali kwamba amepiga kukubali wito au pengine kunionya nisiendelee kumtumia zawadi. Nilianza kumshukuru sana kwa kunipigia, nikimwambia jinsi gani nimekuwa nikisubiria simu yake. Nilitumia kama dakika mbili nzima kujieleza jinsi gani simu yake imekuwa ya maana kwangu. Baadaye nikajistukia, ikabidi nimwambie,”Hata kama umepiga kunionya au kunigombeza lakini kitendo tuu cha wewe kunipigia simu nafsi yangu imefurahi sana”. Alicheka kwa sauti kidogo, nikavuta pumzi nikiwa na matumaini kwamba kwa cheko lile basi kuna shwari.
“Nimekuwa nikipata parcel zako, nashukuru”, alianza kwa kusema hivyo, nami nikamjibu kwa haraka,”Asante wewe mrembo, kwa kupokea”. “Kwani ulinipa nafasi ya kukataa?” alitania, “Hapana lakini kitendo cha kunishukuru sasahivi kimenipa amani kwamba ulizipokea. Sasa niambie kama naweza kukuona tafadhali. Hata kama huna cha kuniambia, au kwenye simu hii ulitaka kunitukana basi utafanya hivyo huku umenitazama sura”, nilijipendekeza na kujihami huku nikimsihi tuonane. Alicheka kidogo na kuniambia, ni sawa. Nadhani unapata picha ni furaha kiasi gani nilikuwa nayo kupata hiyo fursa. Alitaka kuanza kuuliza maswali kuwa naishi wapi na tutaonana wapi nikamkatiza na kumjibu kwa haraka,”Niambie ratiba yako tuu mrembo, lini na saa ngapi ungetaka tuonane. Wapi pa kuonana tafadhali niachie mimi, nitakuchukua ofisini kwako au popote utakapotaka nikuchukue siku hiyo tutakayo onana”. Aliguna na kukubali kwamba tungeonana siku mbili baadaye.
Siku hiyo tunaongea ilikuwa ni Ijumaa kama saa nne asubuhi, lakini haikuwa siku ya kazi nadhani ndiyo sababu alipiga siku hiyo. Tulipanga kuonana Jumapili jioni, saa 11. Wakati huo nilikuwa kwangu Mwanza, lakini baada tuu ya hiyo simu niliondoka haraka sana nyumbani kwenda kutafuta tiketi ya kwenda Dar es Salaam Jumapili asubuhi. Nilipata ndege ya saa 12 asubuhi, nikaona ingenifaa, sasa ilinilazimu kufanya kazi sana siku hiyo na kesho yake ili kuhakikisha nimemaliza vipolo vya wateja wangu, Jumapili nisisumbuliwe.
Sikutaka nifikie kwa Tonny, siku hii ilikuwa maalumu sana kwangu na nisingetaka mtu yeyote aingilie ratiba yangu kwa siku nzima. Nilijipa ofa ya kulala hoteli nzuri sana mjini, nikachekecha na kuchagua hoteli fulani ya nyota tano iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam, Double Trees by Hilton. Tangu nafika kwenye chumba changu hapo hotelini, akili yangu iliwaza huku nikipanga na kupangua nitatokea vipi jioni hiyo. Nilianza kwanza kutafuta saluni asubuhi hiyo, niweke sawa nywele. Kima cha nywele zangu ni kikubwa kiasi, yaani nina kama afro kichwani, lakini si panki. Nikiwa Dar es Salaam, kuna saluni moja nimezoea kwenda iko maeneo ya mikocheni, hivyo ilibidi niende huko ili nisipunguzwe na asiye mzoefu wa nywele zangu, akaniharibu.
Niliweka nywele sawa, na ndevu zangu chache zikasheviwa, nikawa katika hali ya utanashati kabisa. Nilitoka hapo saluni nikifikiria nitavaa nini bila kupata jibu. Kwa asili mimi ni kijana ninayependa kuvaa na kuonekana kisasa kidogo. Napendelea manukato ya gharama, na kuvaa vizuri, japo sio wale wanaoitwa ma brazameni. Mara nyingi hununua vitu vya gharama katika mavazi, viatu au manukato kwani naamini vinaniongezea kujiamini na pia naweza kuvitumia kwa muda wa kutosha mpaka ninapoamua kuviacha. Huu ni mtazamo wangu, pia ni sababu ambayo siku zote imenifanya nitafute pesa kwa bidii sana, kwani hata ndani kwangu napendelea kununua vitu vya thamani ya juu. Nyumba niliyojenga imenichukua muda kumaliza sababu ya kuhakikisha inakuwa katika kiwango ninachotaka. Kitu pekee ambacho hakichukui gharama kwangu ni usafiri tuu. Labda mbeleni nitataka gari ya thamani ya juu, lakini kipaumbele changu kwa sasa ni gari ambayo haitakuwa gharama kwangu kuitumia, yaani haitaniumiza kichwa ila pia itakayoweza kunipeleka ninapotaka kwa unafuu. Hivyo ninatumia gari aina ya Carina TI, inayotumia mafuta kiasi, ni Toyota hivyo spea zake ni nafuu, na haiko chini kwahiyo naweza kupita nayo hata njia zetu mbovu mbovu.
Baada ya kutafuta kichwani kwangu nini cha kuvaa kwa muda, huku nikihisi kama nguo chache nilizokuja nazo si sahihi sana kwa jioni hiyo maalumu, niliamua kwenda kariakoo kuangalia mtoko unaofaa zaidi kwa jioni hiyo. Sikutaka nionekane nimepania sana, sikutaka kutoka maalumu sana ila pia nilitaka niwe mtanashati na mwenye kuvutia. Siku hizi mambo yamerahisishwa, kila kitu kinapatikana mtandaoni. Mara nyingi mimi hupenda kutumia mtandao kupata ladha ninazotaka, hivyo niliangalia mtandaoni namna gani naweza kutoka kimavazi katika first date wenyewe wanaita, au miadi ya kwanza. Nilipata ladha tofauti, nikachagua namna nitakayotoka vizuri zaidi, nikaenda kutafuta kariakoo. Nilinunua shati moja matata linalovalika na jinzi au kadeti, nikapata na suruari flani ya kadeti rangi ya damu ya mzee iliyokolea.
Muda ulipokaribia, nilioga, na kunyoosha nguo zangu na kuvaa. Nadhani kwa watu wazima wenzangu wengi mnafahamu kimuhemuhe cha siku kama hiyo. Yaani nilihakikisha niko mtanashati kuanzia nguo za ndani, soksi na nguo za juu. Sikutaka ikitokea nikapata fursa ya kumkumbatia Ninah ahisi labda harufu ya jasho au yoyote mbaya. Pia nilitaka sehemu ndogo ya vesti itakayoonekana kifuani imuoneshe jinsi gani nilivyo msafi. Nilihakikisha ninapopita naacha harufu ya manukato yangu ya gharama na mazuri sana, Bruno Banani. Muda ulipokaribia nilimpigia simu kumuuliza nimpitie wapi na saa ngapi atakuwa tayari. Hiyo ilikuwa kama saa tisa, akaniambia saa kumi na nusu nimpitie maeneo ya kijitonyama. Nilijaribu kuwa mzungu kidogo kwa kupitia maua rose pale namanga, nikachagua kibando kidogo kilichofungwa kwa umahiri chenye maua ya kuvutia sana.
Kufanya maisha rahisi kwa wakati wangu na Ninah, nilikodi gari nzuri aina ya saluni kunirahisishia mizunguko, hivyo nikawa naendesha.
Saa kumi na dakika 25 tayari nilifika mahala aliposema nimpitie, nikamjulisha na kumsubiri kama dakika kumi hivi, akatoka. Sielewi nikueleze vipi hisia niliyoipata nikimuona anatokea getini. Niliduwaa, kama dakika nzima, nikimuangalia kwa kumshangaa kana kwamba ndio namuona kwa mara ya kwanza. Siku hiyo alikuwa mzuri zaidi ya mara zote nimewahi kumuona hakyanani. Jinsi alivyovaa, staili ya nywele aliyoweka, vipodozi alivyopaka kwa uchache usoni pake, mpaka viatu alivyovaa vilimfanya apendeze mno. Alisogelea gari huku akitazama ndani kwani sikuwa nimefungua vioo vilivyokuwa tinted. Alipofika karibu kabisa nilifungua kioo, nikamtizama nikitoa tabasamu pana sana, nikafungua mlango haraka haraka kabla hajafikia gari.
Nilinyoosha mkono wangu na kumsalimu, lakini alichukua sekunde kadhaa akinishangaa, nakujaribu kuvuta kumbukumbu vizuri aliniona wapi, kisha akanipa mkono tukasalimiana. Kusema kweli nilitamani kuuvuta ule mkono, nimkumbatie lakini haiba yangu haikuniruhusu kufanya hivyo. Nilimualika upande wa abiria, nikamfungulia mlango na kumtaka aingie, nikampa lile ua mara tuu alipoingia kwenye gari.
Tukiwa ndani ya gari, nilijitahidi kuwa mchangamfu sana kwake. Sikujilazimisha, furaha na msisimko uliokuwa ndani yangu ulinifanya nijisikie mchangamfu sana. Nilimuuliza kama amenikumbuka, akajibu,”Nimekukumbuka sana, japo mwanzo ilibidi nichukue sekunde kadhaa kukumbuka nilikuona wapi. Bado najiuliza ulifahamu vipi kazini kwangu, na ulipata wapi ujasiri wa kunitumia hizo parcel siku zote hizo bila mimi kukufahamu”. “Hutakiwi kujiuliza maswali mengi mrembo, cha msingi niko hapa sasa, unamenifahamu, na nadhani itakuwa mwanzo mzuri wa mimi na wewe kufahamiana”, nilijibu kwa kujiamini. Muonekano wangu umenipa kujiamini kidogo, kwani naamini nina umbo ambalo mabinti wengi huvutiwa kirahisi. Sipendi kuzungumza sana juu ya muonekano wangu, lakini ni kati ya wanaume warefu, wenye miili ya mazoezi kiasi na si mnene. Hata hivyo sikujiaminisha kukubaliwa na malkia huyu kwa urahisi, kwani japo naweza nikawa handsome kama wenzetu wasemavyo, lakini kwa uzuri aliokuwa nao Ninah, nilihisi simstahili.
Niliendesha mazungumzo tukiwa kwenye gari, nikiendesha gari kwa umakini, ili binti asije akanitoa hata kasoro ya kukosa umakini barabarani. Nashukuru naye hakuwa mkimya sana, alinipa ushirikiano, ndani ya muda mfupi tukajikuta tayari tumefika hotelini. Tulielekea mgahawa maalumu wa chakula, ulio ghorofani, tukakaa.
Nilianzisha mazungumzo yetu baada ya kuwa tumeagiza aina fulani ya kahawa, cappuccino, na kuanza kunywa taratibu. “Nashukuru sana umenipa fursa hii kukuona. Siku niliyopokea simu yako nilihisi napata kichaa, kwani nimekuwa nikingojea unipigie kwa muda mrefu na shauku kubwa. Naitwa Maxwel Balongo, na nimezoeleka zaidi kama Balongo. Naishi Mwanza, ni mfanyabiashara (utafahamu zaidi kuhusu biashara zangu taratibu). Ila niwe muwazi tuu kwako, nilikuona mara ya kwanza kariakoo”. Nilianza utambulisho huo, na kuweka pozi kidogo. Hapo niliona ametoa macho ya mshangao akishindwa kuelewa, kisha akajibu,”Kariakoo tena?”, “Ndio, kariakoo. Kama unakumbuka, kuna siku vijana wawili walikukuta duka moja la nguo za ndani, ukiwa kama muuzaji, kumbe umemshikia muuza duka kwa muda aliyekuwa ameenda kukutafutia boxer ulizohitaji kwa muuzaji mwingine.” Wakati naanza kumpa hayo maelezo hakuonekana kukumbuka kiasi cha kufanya nihisi nilichanganya madesa, lakini kwa namna alivyoniingia moyoni, niliamini isingewezekana kukosea. Nilipomaliza alionekana kukumbuka vizuri kabisa, na kuongeza maelezo tena kidogo kuonesha amekumbuka vizuri.
“Mara ya pili nadhani unakumbuka, ni siku ile tulionana Lamada hotel posta, nikiwa na Tonny (sitaki nikukumbushe wewe ulikuwa na nani-nilimtania). Ukweli ni kwamba sijawahi kuvutiwa na msichana kiasi ambacho wewe ulinivutia. Nadhani kwa mrembo kama wewe, hiyo ni sentensi ambayo wanaume wengi wameshaitumia kwako. Ila sijali hilo, ninachojua, moyo wangu ulikupenda tangu siku ya kwanza nakuona pale kariakoo. Labda kukuhakikishia uliingia akilini mwangu kiasi gani, nikukumbushe ulivaaje siku hiyo. Ulivaa shati yenye vifungo nyeupe, na suruali ya jinzi ya bluu. Kama utakumbuka, nilichukua kama dakika nzima nikikushangaa, kiasi cha kutojibu salamu yako mara ya kwanza. Ninah, sijawahi kupenda hivi, mimi ni mwanaume ambaye si rahisi sana kujiweka wazi sana kwa msichana, hasa ambaye sina hakika kama atakuwa wangu, na huwa sipendi kutumia maneno mengi kumueleza msichana ninavyomuhitaji kwani nahisi ataniona muongo. Lakini niamini, hujatoka akilini mwangu tangu siku ya kwanza niliyokuona. Mara ya pili nakuona nilihisi niko ndotoni, japo nilihuzunika kukukuta na mwanaume, lakini nilifurahi sana kukupata tena. Siwezi kukuelezea ni hisia gani nimepitia nikiisubiri hii siku, lakini nakuhitaji, nakupenda, nataka uwe wangu, yaani naomba unipe nafasi kukuhakikishia kuwa nakupenda”.
Nilivuta pumzi ndefu, nikijitahidi kumtazama Ninah machoni bila kupepesa, nione walau muonekano wake wa uso unapokea vipi maneno yangu. Kabla hajanijibu chochote, niliendelea,”Najua una mpenzi, labda Mungu awe amenifanyia muujiza mmeachana, lakini maadamu hujaolewa bado nina matumaini naweza kupata nafasi moyoni mwako. Nakupenda, nakupenda mno Ninah. Sina neno kubwa zaidi kukueleza jinsi ninavyohisi sasa hivi kunywa kahawa na wewe, lakini katika utu uzima wangu huu, sijawahi kuwa na hisia kali za mapenzi kama leo. Naomba unipe nafasi ndogo tuu, ya kuwa rafiki maalumu kwako, kama haitawezekana kuwa mpenzi wako. Uniweke kwenye mzani, uangalie kama nastahili kuwa mpenzi wako au la”. Nilimaliza maelezo yangu ya awali ambayo niliamini nimeufungua moyo wangu ipasavyo kwa mrembo huyu.
Wakati huo niliisahau kabisa kahawa yangu, akili yangu iliwaza kama nilichoongea kimeonekanaje kwa Ninah. Moyo wangu ulienda mbio sana, nikimsubiri azungumze naye. Sikutegemea anikubali hapo hapo, ila pia sikutegemea anikatae. Jibu la kukataliwa nilihisi lingenifanya niishiwe nguvu hata za kuinuka pale mezani. Nilimtizama usoni, nikiwa na hisia kali mno, kiasi kwamba bila mimi mwenyewe kujua nilistuka nikihisi machozi yanataka kutoka. Nilimuomba samahani na kuinuka haraka sana kwenda uani. Nikiwa mbele ya kioo, nilijiambia,”Hii si kweli Balongo, huwezi kutoa chozi mbele yake”.
Niliporudi nilikuwa tayari kumsikiliza aongee. “Nimekusikia, nimekuelewa, lakini sijui nini cha kukwambia. Labda uniache kwanza, tuzungumze tuu vitu vingine”. Alisema, na kunyamaza kuashiria amemaliza. Hapo ndipo aliponipa mtihani haswaa, nikaelewa siku zote nilikuwa nacheza, sikuwahi kupenda. Nikahisi kama kupenda ni aina fulani ya utumwa, au mateso bila chuki wenyewe wanavyosema. Maana sikuwa na namna ya kumlazimisha anipe jibu, wala azungumze chochote kuhusu maelezo yangu, lakini pia sikuwa naweza kuvumilia kutozungumzia mapenzi. Nilikubaliana naye, tukaendelea na mazungumzo, lakini kila wakati mazungumzo yangu yalielekea kulekule. Nilimuuliza habari zake za mahusiano ambazo hakuwa tayari kuniambia, akanieleza kwa kifupi tuu na kubadilisha mada. Tulipoendelea kukaa, niligundua si msichana mkimya kama ambavyo nilihisi mwanzo. Alianzisha stori za kunichekesha na kunishangamsha kwa namna fulani kwani jibu lake lilinifanya nipooze.
Siku hiyo tulijikuta tukitumia masaa mengi kuongea kuliko nilivyotarajia. Kufika muda wa kuondoka, nilishangaa kuangalia saa yangu na kuona muda umeenda sana, kwani nilipokuwa nikiendelea kuzungumza na Ninah nilihisi kama tumeongea kwa muda mfupi tuu. Uwepo wake ulinipa raha ya ajabu, na uchangamfu wake ulinifanya nimfanye nimpende zaidi. Kufika saa tano usiku aliangalia saa na kusisitiza tuondoke. Nilitamani kuendelea kukaa, lakini sikuwa na namna ya kupinga. Ilikuwa fursa ya pekee, kupata chakula cha jioni na msichana aliyeupendeza moyo wangu sana, na kuwa na mazungumzo naye kwa urefu. Nafsi yangu iliridhika kwa kiasi. Sikuwaza tena kuwa nimejieleza bila kupewa jibu lolote. Nilimrudisha nyumbani na kurudi hotelini, lakini nilihakikisha nimemuomba kuonana tena siku nyingine. Hakunipa jibu la uhakika wa siku ya kuonana, lakini nilijipa moyo kuwa huo ulikuwa mwanzo tuu wa kuonana mara kwa mara.
Usiku wa siku hiyo nadhani nililala masaa matatu kama si mawili. Nilimuwaza Ninah, wakati wote. Nilijenga magorofa hewani naweza sema, nilijiona nikiwa naye katika mapenzi mazito, nikajifurahia. Nilitamani kumuomba anijibu kama amenikubali, tuanze mahusiano kwa haraka. Akili yangu haikunipa jibu lingine lolote zaidi ya kukubaliwa. Sikutaka kujipa mawazo tofauti na hayo, kwani yangenikosesha raha. Asubuhi kitu cha kwanza akilini mwangu ilikuwa ni Ninah. Nilitaka kumpigia simu, nikasita kidogo nikikumbuka kuwa atakuwa anajiandaa kwenda kazini. Mara nyingi sipendi kutumia ujumbe wa simu, kwani ni mvivu wa kuandika kidogo, pia huwa najistukia nini cha kumuandikia mtu, hasa katika hali kama hiyo ya mahusiano ambayo bado hayana muelekeo wa kueleweka. Nikashika simu na kuiacha, mara mbili, lakini badae nikaamua nipige kumsalimu tuu, mida ya saa mbili asubuhi. Nilizungumza naye kwa kifupi, kumsalimu tuu, kisha tukaagana. Lakini baada ya muda nilimtumia ujumbe mfupi kumuomba nimfate kazini jioni, nimuone japo kwa dakika tuu. Alichukua kama masaa mawili bila kunijibu kiasi cha kunikatisha tamaa kabisa, lakini badae akajibu kifupi kusema sawa.
Kama kawaida yangu kufika jioni mapema tuu nilijiandaa vizuri, nikafika ofisini kwake dakika kumi kabla ya muda tuliokubaliana. Alitoka ofisini kwake na kunikuta kwenye sehemu ya kupaki magari, nikimsubiri. “Nadhani umekuja siku nzuri leo, gari yangu imepata shida, hivyo utanipeleka nyumbani”, alisema mara tuu alipoingia kwenye gari. Hakujua kwangu hiyo ilikuwa kama bahati. “Nitafurahi kumuendesha malkia”, nilijibu haraka. Tukiwa njiani nilimuomba tupite sehemu kula ice cream japo dakika chache tuu. Kiukweli niliona aibu kumuomba tena muda lakini sikuweza kujizuia. Tulipitia sehemu, tukakaa tena jioni hiyo kama masaa mawili kabla sijamrudisha nyumbani.
Baada ya siku hiyo urafiki wetu ulijengeka kwa haraka. Sikutamani kuondoka Dar es Salaam kwani kila siku nilihisi nahitaji kuwa na muda na Ninah. Kuna siku alizoninyima kumuona lakini nilimbembeleza na kutafuta mbinu za kumuona karibu kila siku. Nakumbuka kuna siku hakuniruhusu kumfata ofisini basi nikaenda na kupaki gari sehemu ambayo nitamuona akiwa anatoka. Nilijisikia vizuri tuu kumuangalia akitembea kuelekea kwenye gari yake. Wiki mbili baadaye nililazimika kurudi Mwanza, hivyo ikabidi nimuombe tena muda wa kutosha kumuaga. Hiyo siku ilikuwa nzuri sana kwangu kuliko ya kwanza, kwani kwa kiasi tulishajenga urafiki zaidi kuliko awali, na maongezi yetu yalionekana kama ya watu waliozoeana. Nilipojaribu kuzungumzia suala la mahusiano, nikimtaka aseme japo kidogo, bado hakunipa ushirikiano na hakutaka kuizungumzia hiyo mada. Sasa hapa sikuelewa kama labda ana mpenzi mwingine ambaye hawezi kumuacha hivyo sina nafasi kabisa, lakini ananihurumia kunikatisha tamaa, au labda ananichunguza kwanza kabla ya kunikubali, au pengine ana mpenzi lakini haoni kesho naye lakini bado hawajaachana, au ni vipi. Ila mbali na yote, ilitosha kunipa nafasi ya urafiki.
Nikiwa Mwanza, niliendelea kuwasiliana na mrembo wangu, na niwe muwazi, nilifika mahala nikasahau kama bado hajanikubalia, mpaka siku nilipopokea simu ya mwanaume wiki kama tatu baadaye. Huyu mwanaume hakujitambulisha jina lake, lakini alisema ni mpenzi wa Ninah Mushi, ambaye hivi karibuni amegundua namfatilia sana. Nilishindwa cha kumjibu yule jamaa, nikabaki kimya kwa sekunde halafu nikakata simu. Bila mimi mwenyewe kujielewa nilihisi machozi yananitoka. Mwanamke, kwa mara ya kwanza, alinitoa machozi ya uchungu, hii ilikuwa kama ndoto. Wakati huo nikiwa kwa mteja wangu mmoja, nimesimama pembeni kuongea na simu hiyo, nilibaki hapo kwanza, nikitafuta pozi la kuwa sawa tena. Nilifanya haraka kumuaga mteja, nikamuachia gari ya mizigo kijana aendelee na kusambaza mizigo kwa wateja huku nikisingizia kichwa kinauma, nikarudi nyumbani kwangu haraka sana.
Chumba changu nimekitengeneza kwa namna ya kunipa mapumziko haswa, yani nikishafika chumbani kwangu hua kiasi fulani msongo wa mawazo unapunguzwa na yale mazingira ya chumba tuu. Rangi za chumba, aina ya kitanda, kiyoyosi, luninga ya kisasa, kapeti ya manyoya na ukubwa na mpangilio wa chumba vinafanya muonekano wake uwe mzuri sana. Na nilifanya hivyo sababu chumbani ndipo mahala natumia muda zaidi, hasa ninapomaliza kazi zangu zinazonifanya kuwa bize na wakati mwingine mchovu sana.
Nilijilaza kitandani kama saa nzima huku nikitafakari na kuumia sana, bila kujua nini cha kufanya. Nilishindwa kujizuia kulia, na kuwaza sana, huku moyo ukiuma kama kidonda. Sikufikiri kingine chochote zaidi ya kupoteza ndoto za kuwa na Ninah, jambo ambalo akili yangu haikuwa imelitegemea. Niliumia mno, ukizingatia mpaka wakati huo sikuwa bado na jibu lolote la Ninah kuhusu ombi langu. Nilitamani kumpigia kumueleza juu ya ile simu niliyopokea, lakini sikuwa na ujasiri huo, kwani hakuwa mpenzi wangu bado. Baada ya muda niliamua nitatafuta kitu cha kunipotezea mawazo, hivyo nikaamua kupika (mimi hupika wakati tuu ninaojisikia kufanya hivyo, na hiyo ni kati ya vitu ninavyopenda kufanya). Nilitafuta mtandaoni na kupika chakula kimoja cha kiitaliano, nikitumia nyama laini ya ng’ombe na ngano.
Kama unakumbuka, kipindi nakutana na Ninah mara ya pili, tukiwa na Tonny, nilikuwa tayari kwenye mahusiano mengine. Baada tuu ya kumuona Ninah, niligundua namdanganya yule binti niliyekuwa naye, moyo uligoma kabisa kumpa nafasi japo kidogo ya kuendelea kumpenda, hivyo nikamfanyia visa na kumuacha. Hapa sasa nilianza kujihisi natembelea laana ya mpenzi niliyemuacha, lakini sikujipa nafasi ya kujilaumu wala kujihukumu tena. Adhabu niliyoipata ya kupigiwa simu na mwanaume mwenzangu ilinitosha, hivyo sikutaka kuongezea adhabu ya kujihukumu. Nilipika, nikala nikiwa naangalia muvi chumbani kwangu, na kujiliwaza kwa mziki laini baada ya hapo kwa masaa kadhaa mpaka nikapitiwa usingizi. Niliamka mida ya saa kumi usiku kwenda uani, nikashindwa kulala tena. Nilikaa kitandani, nahesabu masaa, asubuhi sana nikachukua gari na kuanza biashara zangu bila hata dereza wangu. Siku hiyo nilifanya kazi nyingi kweli, na kama isingekuwa na kushusha mizigo, nilitamani nimpe dereva wangu nafasi ya kupumzika. Nilijitahidi kuwa bize ili nisijipe nafasi ya kumtafuta Ninah, huku akilini nikidhamiria nitafanya hivyo mpaka siku nitakapoamua kuomba nionane naye tena na kufikia muafaka wa kama tunaweza kuingia kwenye mahusiano au la.
Nikiwa katikati ya shughuli zangu, mida ya saa kumi jioni, iliingia simu ya Ninah. Haikuwa kawaida yeye kunipigia, kwani mara zote nilianza mimi kupiga, isipokuwa siku hiyo. Nilipokea, tukasalimiana huku nikizungumza kwa unyonge bila uchangamfu kabisa. Najua alihisi unyonge wangu, lakini labda hakuwa na namna ya kuniuliza. Niliongea naye kifupi tuu, na kulingana na namna nilivyozungumza, naye pia alikosa maneno ya kuongea, hivyo baada ya salamu na kuulizana habari tuliagana, akakata simu. Nilihisi pengine amenipigia kwa sababu nimekuwa kimya siku nzima, japo hakuniuliza kwanini. Moyoni nilifurahi kidogo kuhisi hivyo, japo bado nafsi haikuwa na amani kabisa kwa ile simu niliyopokea jana yake. Nilirudi nyumbani usiku kabisa, nikiwa nimekula tayari, nikaoga na kuwasha muvi kuangalia. Mimi si mtu wa marafiki sana, hivyo muda wangu mwingi mbali na kuutumia katika kazi zangu, huwa nakuwa pekeyangu.
Siku iliyofuata nilishinda hivyo hivyo, sikumtafuta Ninah siku nzima, naye hakupiga hivyo ikapita siku nzima bila kuwasiliana. Niliporudi nyumbani, baada ya kuoga na kupumzika, uzalendo ulinishinda. Nilimtumia ujumbe mfupi wa simu, NAKUPENDA SANA NINAH. Hiyo ilipata mida ya saa nne usiku. Sikutegemea anijibu, lakini kwa jinsi nilivyokuwa nahisi, niliona bora tuu niandike. Sikujali kama pengine mida hiyo angekuwa na yule jamaa aliyenipiga mkwara juzi au la. Dakika kama tano baada ya kutuma ule ujumbe alipiga simu. Upande mmoja niliogopa kuipokea, nikihisi ataanza kunionya nisiendelee kumfanya kama mpenzi wangu, lakini kwa upande mwingine nilitamani kusikia sauti yake.
Nilipopokea simu, sauti ikiwa ya chini na ya upole sana, nilimsalimu na kumwambia kuwa nimefurahi kupokea simu yake. Alinijulia hali kisha akaniuliza kama tunaweza kuonana. Moyo ulistuka sana, nikamuuliza tuu, unahitaji kuniona lini? “Hata kesho”, alijibu kwa ufupi. "Ngoja nitafute kama nitapata ndege ya kesho sasaivi halafu nitakujulisha," nilimuitikia.
Kwa penzi nililokuwa nalo juu ya Ninah, gharama ya ndege za dharura sikuona kuwa ni kitu. Umbali wa Dar es Salaam na Mwanza kwangu ulionekana kama ni wa kutupa jiwe. Niliingia mtandaoni usiku huo na kutafuta ndege, kwa bahati haukuwa msimu wa wateja wengi hivyo nilipata ndege ya kesho yake saa 12 asubuhi, ingawa bei ilikuwa juu. Nilimpigia kijana wangu, kumuomba afike nyumbani saa kumi alfajiri, akanisindikiza uwanja wa ndege, nikampa na maelekezo muhimu ya biashara, nikaondoka. Niliwaza ni nini hasa binti huyu anataka kuniambia, kwa dharura ya namna hiyo. Nilijipa moyo kwamba hawezi kunisumbua, kunitoa Mwanza kama hana jambo la msingi la kuniambia, lakini sikutaka kuweka matumaini kwamba atakuwa ananikubali. Ni siku chache tuu, nilipata simu kunithibitishia kuwa yuko kwenye mahusiano, na haingekuwa rahisi hata kidogo kunipa nafasi mimi pia. Hata hivyo, wito wake ulikuwa muhimu mno kwangu.
Jioni ilifika, nikamfata kazini mapema kidogo, kwani alitaka nimfate saa tisa. Tulipoonana, nilishuka kwenye gari kumpokea, nikamshika mkono, nikajikuta nimemvuta kumkumbatia. Nadhani nilichohitaji ni kumkumbatia, nijifariji kwa uwepo wake karibu yangu. Sielewi ujasiri huo niliupata wapi, lakini nashukuru hakukataa kumbato langu, japo hakuniruhusu kuendelea kwa muda mrefu. Tuliingia kwenye gari, na siku hiyo sote hatukuwa wachangamfu kama awali. Tulizungumza tuu mambo ya msingi, hakukuwa na utani wowote kati yetu. Nilimuuliza kama alikuja na gari, akasema alikuja nalo lakini amemuachia rafiki yake funguo hivyo tunaweza kuondoka pamoja. Akili yangu wakati huo iliwaza, kama Ninah angeniambia huu ndio mwisho wetu, sijui ningefanyaje. Nilihisi kumpenda kuliko nilivyowahi kupenda kabla.
Tulienda hoteli fulani kubwa, iliyo kando mwa bahari, tukakaa sehemu ya wazi jirani na maji. Tukiwa tumeagiza vinywaji, ghafla mvua ilianza kunyesha, hizi mvua za Dar zinazokuja bila taarifa. Tulipokaa hapakuwa na mwanvuli juu, palikuwa wazi tuu, mbali kidogo na majengo ya hoteli. Tuliinuka sote kwa haraka, nikamshika mkono ili tukimbie kujikinga na mvua, lakini badala ya kukimbia, tulijikuta tumesimama pale kwa muda kiasi tukitazamana, huku mvua kubwa ikinyesha. Nilimtazama machoni, nikiashiria nataka anitazame pia, zikapita sekunde kadhaa, nikamwambia,’nakupenda sana Ninah, nakupenda’.
Mvua ikiendelea kunyesha, alinivuta kunionesha tunatakiwa kuondoka eneo hilo, tukaelekea sehemu ambapo mvua haifiki, lakini sote wawili tukiwa tumelowa kiasi. Nilimuhurumia kuwa angesikia baridi, hivyo haingekuwa sawa kukaa na nguo mbichi. Nilimuomba tuondoke hapo hotelini, tukaondoka, nikampitisha kwenye duka moja la nguo, nikamnunulia gauni simpo, nikamuomba twende hoteli niliyofikia. Nilimpa funguo ya chumba changu, akaingia kubadili nguo huku nikimsubiri kwa nje, halafu nami nikaingia kubadili alipotoka, nikavaa kinyumbani zaidi yaani pensi na tisheti na viatu vya wazi. Tulipanda juu kwenye mgahawa, tukaagiza kahawa na kuanza kunywa. Nilitamani Ninah aanze kuzungumza, lakini niliogopa kumuharikisha kwani sikuwa najua nini hasa angetaka kuniambia. Muda si mrefu, alianza kuongea.
“Uliniuliza kuhusu mahusiano yangu, sikutaka kuzungumzia. Lakini mara ya pili tunaonana nilikuwa na mpenzi wangu, hilo unajua. Yule mwanaume nilimpenda sana, na nilitegemea tungeoana. Wakati ule alikuwa ametoka masomoni, ni mwanajeshi, hivyo alipokuwa masomoni kwa muda mawasiliano hayakuwepo kabisa, muda wa kama mwaka mzima, lakini alipokuja tuliendelea na sikuwahi kuwa na mwanaume mwingine kwa kipindi kile chote. Tulikaa huku nikitegemea tuanze taratibu za kuoana kwani uhusiano wetu tayari ulifikisha miaka mitatu wakati huo, lakini yeye alikuwa mzito kidogo. Baada ya kuvutana kiasi, alinivisha pete kwa mshtukizo yaani sapraizi, kabla hata hajatoa barua ya posa. Sikufurahia sana kile kitendo, japo yeye alidai kuwa ni hatua kubwa sana katika kuoana.
Tulikaa kama miezi sita bila kuendelea na hatua yoyote. Sasa wiki kadhaa zilizopita nimepata habari kuwa ana mtoto aliyemzaa na mwanajeshi kipindi yuko masomoni, na mama yake amekuja hapa mjini kumtafuta. Nimefatilia nikajua ukweli, japo mwanzo nilimuuliza akakataa kabisa, lakini baada ya kubaini ukweli amekubali na kuanza kuniomba msamaha. Mbaya zaidi huyo mwanamke nahisi bado wanaendelea na mahusiano. Juzi kati, tukiwa kwenye huu mgogoro, alipiga akidai kuwa sitaki kumsamehe kwakuwa nimepata mwanaume mwingine. Kuna kitu aliwahi kufanya kipindi cha nyuma tukagombana sana, alifuatilia simu yangu mitandaoni, kuangalia nani nawasiliana naye sana. Hakukuta siri yoyote, akajikuta ameniambia, tukagombana sana, nikamuonya kuwa hiyo ni kuonesha kiasi gani haniamini.
Hivi karibuni amerudia tena kufanya hivyo japo aliniahidi hangefanya tena. Mimi ni muaminifu kwake, na anaruhusiwa kuchukua simu yangu kuiangalia, lakini si kwenda nyuma ya pazia. Alivyokuta jumbe zako, ambazo kwenye simu yangu sikuwa nazihifadhi, alihamaki sana na kushindwa kujizuia kuniambia. Wakati huo tulikuwa kama tumeachana kwajili ya hayo mambo niliyogundua, kwani sikuwa tayari kuwa naye akiwa na mwanamke mwingine. Sasa baada ya kuona jumbe zako, juzi, alinipigia simu akigomba sana na kuniambia kuwa amekupigia uachane na mke wake. Anadai wewe ndiye unanipa jeuri ya kumuacha japo bado sijakukubali.”
Maelezo ya Ninah yalinifanya nimuhurumie kwakweli. Jinsi alivyo mrembo na laini niliona hakustahili kuumizwa hata kidogo. Nilijikuta nimeropoka,”Watu wanachezea bahati!”, akatabasamu tuu. Nilitamani ningeipata hiyo nafasi mimi, nikajiahidi nafsini mwangu, kwamwe singeipoteza. Sikuongea sana, nikamuacha aendelee na maelezo yake.
“Unisamehe nimekusumbua kukutoa Mwanza, lakini nilihisi nahitaji kuongea nawewe. Sasa hivi sijui tena nini hasa cha kukwambia, ila kiukweli nilihitaji kukuona Maxwel”. Hapo akili za kuambiwa, nilichanganya na za kwangu, nikaelewa binti ananihitaji. Nilisogelea kiti cha karibu naye, nikahama nilichokuwa nimekaa kilichotazamana naye. Niliweka mkono wangu begani kwake, nikamtazama usoni, naye akaniangalia, nikamwambia,”Najua unachotaka kuniambia, naweza kusoma mawazo yako, hivyo usihangaike kusema. Humuhitaji tena huyo mwanaume, lakini unajihisi mpweke kiasi. Niko hapa Ninah, kukufanya ujisikie salama na usiwe mpweke tena. Nakupenda sana, kuliko unavyodhani.” Nilizungumza nikiwa nimemkumbatia kwa mkono mmoja, nikimaanisha kuifariji nafsi yake.
Nilijua najiweka hatiani kutaka penzi kwa binti ambaye pengine moyo wake bado umebeba mtu mwingine, nilifikiri endapo mpenzi wake wa awali akimbembeleza wakarudiana nitakuwa kwenye hali gani. Lakini kwangu faraja ya Ninah ilikuwa muhimu. Sikutaka awe na huzuni japo pia nilitumia fursa hiyo kujiweka karibu. Labda bahati ingeniangukia, akanipenda mimi moja kwa moja.
Usiku ule ulikuwa wa kipekee sana kwangu, nilimrudisha Ninah saa nne na nusu usiku, alipotaka yeye, kwani angeniruhusu tungekaa mpaka asubuhi. Wakati tunaarudi alikuwa amerejea katika hali ya uchangamfu hivyo nikajipongeza kuwa kazi nimeifanya vizuri.
Tulifika kwake, nikashuka na kuja upande wake. Si kuwa nina tabia za kizungu sana, kumfungulia mwanamke mlango wa gari, au nataka kujionesha hivyo kwa Ninah, ila niliona hiyo ndiyo njia rahisi ya kupata kumbato lake kwa mara nyingine tukiwa tumesimama. Alishuka kwenye gari, nikashika mikono yake miwili, nikamvuta karibu na kumkumbatia kwa nguvu sana. Mara hii hakunizuilia mapema, basi nikakaa pale kama dakika nzima au zaidi. Nadhani unaelewa hisia zilizoendelea ndani yangu wakati huo, yani nilitamani kuendelea kumuweka kifuani kwangu hata kwa saa nzima, lakini hilo lisingewezekana. Tuliagana, akaondoka.
Niliporudi hotelini, baada ya kuoga na kuingia kitandani, nilimpigia simu kumuuliza kama amelala tayari. Sikuwa na cha kumwambia hasa, lakini nafsi yangu ilifurahi kumsikia kwa simu. Usiku kucha nilimuwaza Ninah, nikiwaza tulivyokumbatiana na nilivyojihisi, niliwaza huzuni aliyokuwa nayo na nilivyotumia fursa ile kujiweka karibu, niliwaza alivyotabasamu, niliwaza alivyolitamka jina langu, yani kila kitu mpaka alivyokosa cha kuniambia. Nilijifariji kuwa ameanza kunipenda na ndio sababu amenitoa Mwanza ili nikae naye tuu wakati anapitia ugumu kwenye mahusiano yake. Nilitamani kesho yake ifike haraka nimtafute tena, nimuombe kuonana. Wiki hiyo nzima Ninah alinipa nafasi ya kuonana naye kila siku, tukiwa na wakati mzuri wa pamoja jioni, tukitembelea maeneo tofauti tofauti, lakini hata siku moja hakunitamkia neno lolote kunionesha kwamba naweza kuwa nimeanza kuchukua nafasi moyoni mwake. Niliridhika kuwa rafiki wa karibu, nilifarijika kukaa naye, kula naye, kucheka na kuzungumza na huyu mwanamke niliyempenda sana.
Ilinilazimu kurudi Mwanza baada ya siku nane, hivyo siku ya saba jioni tulikaa kwenye mgahawa mmoja wa kimahaba, maeneo ya masaki, kuwa na muda mzuri wa kuagana. Baada ya maongezi ya muda mrefu, kama kawaida yangu, nikajipendekeza, nikajisogeza karibu kabisa na Ninah na kuanza kumwambia jinsi ninavyojisikia kuwa karibu naye. Mara zote huwa nikimwambia hayo maneno, yeye hutabasamu tuu na kusema asante wakati mwingine, lakini, siku hiyo alinishangaza. Nilipoongea nae huku mkono wangu wa kulia umeshika bega lake, alinigeukia na kunitizama machoni, kisha akaniambia kwa lugha ya kiingereza,”I think I love you Maxwel”, akimaanisha, “Nadhani nakupenda Maxwel”. Kidogo nichanganyikiwe siku hiyo, kwa furaha. Niliinuka, nikamshika mkono, nikamuomba arudie hicho alichosema tukiwa tumesimama. Akarudia tena, “Nadhani nakupenda”.
Nikiwa nimemuangalia usoni, nilianza tena kujieleza,”Sitaki kujua kama hicho unachodhani ni kweli au si kweli. Inatosha kudhani unanipenda, nitakusaidia kujua kuwa unanipenda kweli mpenzi, nashukuru sana kwa kuwa muwazi kwangu.” Hapo nilimkumbatia kwa nguvu sana huku nikimshukuru na kumueleza jinsi ninavyompenda sana. Sikutamani muda uende, sikutamani niondoke kesho yake, sikutamani siku hiyo iishe. Nafsi yenye kiu ilikuwa inapata maji bariidi, wakati wa jua kali. Tulikaa muda mwingi zaidi usiku huo, mpaka saa nane usiku, nikamrudisha kwake nikarudi kupumzika kwa ajili ya safari.
Wiki chache baadaye, nikiwa Mwanza, huku tukiendelea kuwasilianza, Ninah alinitamkia kwenye simu kuwa amefanya maamuzi ya kuwa na mimi na hatageuka. Hii habari ilikuwa njema mno hivyo sikutaka niisikie kwenye simu tuu. Nilipanga safari baada ya siku mbili, kuja kuipokea rasmi habari ya kukubaliwa. Niliposhuka uwanja wa ndege wa mwl. Nyerere, mtu wa kwanza kutaka kumuona alikuwa Ninah, hivyo nilichukua gari inipeleke moja kwa moja ofisini kwake. Lakini nilipita pale namanga na kutengeneza ua zuri kwa haraka na kununua kadi ya ASANTE. Kitendo cha yeye kusema ameamua kuwa namimi ni kama kilinipa funguo na ujasiri wa hali ya juu. Nikiwa na boksi ndogo ya zawadi, na kadi na ua mkononi mwangu, siku hiyo nilifika mpaka mapokezi ya ofisini kwake nikamuulizia. Sikuwa nimemjulisha kuwa ninakuja, nikikusudia iwe sapraizi. Alipigiwa simu, akajulishwa kuna mgeni wake, nikaelekezwa ofisi yake ambayo walikaa yeye na mfanyakazi mwenzie mmoja wa kike. Alifurahi mno kuniona, kwa mshangao mkubwa kwani jana yake tuu nilitoka kujilalamisha kuwa natamani sana kuja ila sitaweza kupata nafasi mpaka baada ya siku nne.
“Una tabia mbaya wewe”, alisema. Mbele ya huyo rafiki yake, tulikumbatiana kwa furaha sana, nikambusu kidogo juu ya midomo yake, nikampa maua na zawadi yake nilivyokuwa nimeweka mezani kwake nilipoingia. Ndani ya kadi niliandika ujumbe mfupi,”Umenipa zawadi kubwa mno kunikubali. Asante sana”. Zawadi niliyofunga, ambayo ndiyo ilinichelewesha kuondoka Mwanza ni cheni ya dhahabu ya hadhi ya juu, yenye jina lake, lakini mbele kuna herufi M, yaani Ninah M, nikimaanisha Ninah Maxwel. Nilimuomba afungue hapo hapo, nikamvisha, huku nikimwambia, ikitokea ukaniacha utaenda kuiyeyusha utengeneze kitu kingine. Nilimuomba rafiki yake msamaha kwa kuwasumbua wakati wa kazi, nikamuaga Ninah na kuondoka huku nikimsisitiza kuonana naye baada ya kazi.
Mapenzi kati yangu na Ninah yameanza, mahaba mazito sana kati yetu. Nampenda kuliko nilivyowahi kupenda kabla, nampenda kuliko nafsi yangu nahisi. Niko tayari kufanya lolote kwa ajili yake. Sifikirii maisha bila yeye. Baada ya kuwa naye, nimegundua vitu vingi sana ndani yake, vinavyonifanya kumpenda zaidi. Yeye ni mchangamfu, mchapakazi na binti mwenye maono na malengo makubwa. Licha ya kuwa mrembo sana wa sura, rangi na umbo, lakini ana moyo wa unyenyekevu na si mwenye kukurupuka katika kufanya maamuzi. Miezi sita imepita sasa tangu tuanze uhusiano, sijawahi kumtoa kasoro naweza sema, au pengine upendo wangu kwake umenipiga upofu. Ndani ya kipindi hiki, nimefahamiana na familia yake kwa karibu, na kumtambulisha kwa familia yangu. Nilichagua siku maalumu kumtambulisha kwa rafiki yangu Tonny, ambaye kwajili ya Ninah, tulimaliza kipindi kirefu bila kuonana (Tonny alifurahi sana nilipompa mchakato mzima kuhusu kisa cha mapenzi yangu kwake). Kasi yetu imekuwa kubwa kidogo, lakini nadhani ni vema kwangu kufanya hivyo kwa binti mrembo kama huyu.
Mimi si mpenzi sana wa kuandika, lakini nimetumia muda wangu kuandika kijitabu hiki kifupi, kama zawadi ya pekee kwa mpenzi wangu siku nitakayomvisha pete. Nitafanya hivyo baada ya mwezi mmoja, au mwezi na nusu kuanzia sasa, natumai nitakuwa nimekamilisha kuchapisha kitabu hiki kwa ajili yake. Nafikiria kuifanya siku yetu maalumu kuwa ya kipekee sana
Nitaandaa gari aina ya Limousine nyeusi, yale magari marefu sana. Gari aina hiyo, kuna ambazo mtu akiwa ndani anakuwa kama yuko sebuleni au chumbani. Nitanunua nguo nzuri sana, tukisaidiana na dada yake kuchagua, viatu pamoja na hereni za thamani, na kitu cha kuvaa mkononi, nitavifunga kama zawadi nzuri . Nitaandaa ndugu zake wa karibu, marafiki zake na ndugu wa upande wangu, bila kumpa yeye taarifa yoyote. Sherehe itaandaliwa kati ya hoteli nzuri hapa mjini, na ndugu wote watakuwa huko mida ya saa 12 jioni. Wakati huo yeye atajua niko Mwanza, lakini nitakuwa Dar es Salaam siku hiyo tayari, na nitamtumia ujumbe akiwa ofisini kumwambia kuna mtu amemletea mzigo, dakika chache kabla ya muda wake wa kutoka, nikiweka namba ya huyo dereva wa hilo gari la Limousine, huku nahakikisha dereva ameshafika hapo ofisini.
Akishuka, atampigia simu na kumpata ambapo dereva huyo atampa maelekezo ya kupanda ndani ya gari na kufungua boksi kubwa ya zawadi itakayokuwa nyuma. Akiifungua atakutana na ujumbe wa kumuomba avae kila kitu akiwa ndani ya gari, kwani dereva hataweza kumuona wala hakutakuwa na mtu yeyote (ni sawa na chumbani). Atampeleka mpaka mahala tulipoandaa sherehe hiyo, namimi ndiye nitafungua mlango wa gari na kupiga magoti mbele yake akishuka ndani ya gari, huku nimeshikilia pete ya thamani kumuomba akubali nimuoe. Nimepanga gari hiyo ipaki karibu kabisa na mahala watakapokuwa wamekaa watu wote, na kabla ya kushuka wote watasimama kumtazama akishuka, na endapo atakubali nimvishe pete hiyo, woote watashangilia.
Tayari nilishaanza kufanya maandalizi na dada yake mmoja ambaye tumekuwa karibu baada ya kufahamiana, wamefatana japo anamzidi Ninah miaka mitatu, yeye ameolewa tayari. Pia nimepanga tukiwa ukumbini, nitamkabidhi hiki kitabu kama zawadi, na ombi maalumu.
“Ninah mpenzi, hadithi hii nimeandika toka ndani kabisa ya moyo wangu, hakuna nililotunga kwani yote niliyoandika ni kweli. Hisia nilizonazo juu yako ni halisi, na sijawahi kuwa nazo kwa mwanamke au msichana yeyote. Nimeamua nikupe kitabu hiki kama zawadi kukuhakikishia jinsi gani Nakupenda, lakini pia kukubali kuvua kiburi changu cha uanaume na kujiweka wazi kabisa mbele yako. Hii inamaanisha umeuteka moyo wangu kwa asilimia 100. Nakupenda kupita namna nilivyoeleza. Nina ombi moja tuu kwako, unipe nafasi nikupende mimi peke yangu siku zote za maisha yako. Wewe ni wa kwangu, mmoja na wa pekee mpenzi.”
Nimalize hadithi hii kwa kuusihi moyo wangu. “Moyo wangu, haujawahi kunielekeza kwa msichana kwa nguvu namna hii, haujawahi kupenda kiasi hiki, haujawahi kuwa mbunifu namna hii katika mapenzi na hujawahi kumpa nafasi mwanamke yeyote kukumiliki kama ulivyofanya kwa Ninah Mushi. Nimekusikiliza, na kufuata ulichokitaka. Nimekupa ushirikiano huku nikifanya juhudi zote. Naamini umenipeleka kwa mtu sahihi, hujafanya makosa kwa kutazama muonekano wake wa kuvutia. Tafadhali MOYO WANGU USINIDANGANYE, kwani jeraha la penzi la dhati halitibiki kirahisi”.
……………MWISHO……
0 Comments