Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Simulizi ya kweli

Jifunze kukabiliana na huzuni kama huna uwezo wa kuigeuza kuwa furaha. Usiyatafsiri machozi ya mtu kama maumivu ndani ya moyo wake. Vilevile usikitafsiri kicheko cha mtu kama furaha ndani ya moyo wake.”
Ni moyo wangu na fikra zangu juu ya mengi niyaonayo na ninayoendelea kuyaona katika ulimwengu huu. Nafsi yangu imekuwa ikitaabika kila niyaonapo kwa macho yangu na hata kwa kusimuliwa. Yanaumiza na kuichumbua nafsi yangu. Kila kukicha na hata pale jua lichweapo, yamekuwa yakizidi kujidhihirisha machoni pangu kwa kasi kubwa mno. Macho yangu yakalia machozi ya kawaida yasiyoonyesha rangi ukiyamwaga juu ya karatasi lakini kadri siku zisogeavyo, si machozi tena ndani ya mboni zangu. Yamekuwa machozi ya damu. Yanachafua popote pale yadondokeapo.
Moyo wangu umekuwa wa kuhangaika kuitafuta furaha lakini imekuwa vigumu furaha hiyo kupatikana. Nikaelemewa maumivu ikanibidi kuwageukia marafiki zangu baada ya kuwakosa ndugu zangu tangu nikiwa na umri wa miaka tisa baada ya ajali mbaya ya meli katika ziwa Victoria. Hakuna asiyeikumbuka ajali hiyo ya Mv Bukoba. Tulikuwa tukielekea katika harusi ya shangazi yangu lakini meno yangu yakapoteza mg’ao kutokana na ajali ile. Nikaokolewa na wavuvi ambao nao baada ya kunifikisha nchi kavu hawakuwa na msaada mwingine tena kwangu. Uso wangu ukayajenga makunyanzi nikiwa na umri mdogo. Tabasamu likanipotea na kubaki nikiliona kwa wengine. Macho yangu yakapoteza nuru pale marafiki niliowadhania, waliponitema mate kutokana na hali yangu. Hakuna aliyehitaji kunitazama hata kwa bahati mbaya. Waliogopa uchakavu wangu wa mwili mpaka mavazi. Hatua zangu zikageuka sumbuko kwa wengine kutokana naharufu niliyokuwa nikiitoa katika mwili wangu. Harufu hiyo ilitokana na kidonda nilichokipata baada ya pikipiki kuniunguza kwa bomba la kutolea moshi. Jamii ilikuwepo wakati nikiungua lakini wakakosa kauli vinywani mwao. Wakawa zaidi ya mabubu ilihali ndimi zao zilikuwa zikiyateta maneno kabla ya mimi kupatwa na hilo. Aliyenisababishia ajali akatokomea na kuniacha katika hali ya maumivu yasiyoelezeka. Nikabaki mwenye katika kisiwa cha baridi pasipo msaada wa joto. Baridi ikaikomaza ngozi yangu na hatimaye ikazoea. Nikalisahau joto na kutamani kuishi katika baridi kila wakati.
Kwasababu maisha ni sawa na hadithi ya kuwa lazima uweke kituo na mikato, baada ya baridi likaja joto. Likaniunguza kadri lilivyoweza. Ngozi yangu maji ya kunde ikabadilika na kuwa nyeusi hapana shaka kama mkaa. Hali hiyo nayo nikaizoea na kuitamani kila wakati. Lakini bado haikuwa mwisho wa huzuni yangu. Ikanyesha mvua. Sikuwa na makazi maalum hivyo nikakosa pa kuziweka mbavu zangu kwa ajili ya usingizi ili kupata mapumziko ya mchana kutwa kuzunguka huku na kule kukamilisha maisha yangu ya hapa ulimwenguni. Nikaizoea mvua na lakini sikuitamani kwasababu hiyo ilinizidishia tabu mno. Umri wangu ulizidi kusonga na hatimaye nilitimiza mika kumi na mbili. Kuongezeka kwa umri wangu haukuwa mwisho wa mateso yangu bali ilikuwa kama ndiyo nayo yanaongezeka. Kutokana na kutamani kuoga na kuvaa kama ilivyokuwa kwa wengine niliokuwa sichoki kuwatumbulia macho, ikanibidi kuomba kazi ya kuosha vyombo kwa mama ntilie. MUNGU ni mwema pamoja na kwamba mateso yangu ya miaka mitatu iliyokuwa imepita ni yeye pia aliyekuwa akiniongoza ili mimi kuendelea kuishi. Nasema hivyo kwasababu nakumbuka siku moja nilifanikiwa kupata chuma chakavu nyingi na baada ya kutafuta mteja nilifanikiwa kumpata. Alikuja na gari ili kubeba. Tukaongozana naye ili niende kupima ni kilo ngapi aweze kunipatia fedha yangu.
Lakini kwa bahati mbaya tukapata ajali mbaya mno ila cha kushangaza niliweza kusalimika bila hata kuchumbuka kidole. Hakika ni zaidi ya kumbukumbu yenye kunistaajabisha fikrani mwangu. Wenzangu watatu pamoja na dreva ambaye ndiye alitakiwa kunilipa, wakanitangulia na kuniacha ulimwenguni nikizidi kupumua na kuivuta hewa safi pasipo malipo yoyote. Hapo ndipo huwa nawaona wapuuzi wale wote wenye viburi kisa wanamiliki. Hapo ndipo nawaona wapuuzi wale wote wenye kuishia kunung’unika kisa wamekosa mali. Niseme maisha ni sawa na daraja barabarani. Yupo aliyepata mali akapoteza macho yake. Iko wapi faida ya macho yake? Hawezi kuviona vitu vizuri na hata vibaya. Atabaki kunusa ilihali kaa ukitambua vipo visivyonusika. Vinahitaji macho. Kwanini unung’unike kwa kukosa leo ilihali bado unavyo viungo vyako ambavyo kesho waweza kuvitumia kutafuta mali ikusababishayo kunung’unika? UVUMILIVU na SUBIRA.
Nilibahitika kupata kazi ya kuosha vyomba. Niliifanya kazi ile moyo mmoja nikiamini itaniwezesha kubadilika kimaisha lakini ilikuwa tofauti na vile nilivyowaza. Miezi mine ya kufanya kazi ile huku nikilala palepale hotelini, sikuwa nikichukua malipo yangu ili siku nikiamua kuchua basi nikafanyie kitu cha maana. Nilijinyama. Nikavaa nguo mbili pekee ndani ya miezi hiyo. Lakini nikapata kumbukumbu mbaya kichwani mwangu baada ya fedha za muajiri wangu kupotea katika mazingira ambayo sikuyaelewa. Ikasemekana mimi ndiye mwizi wa fedha ile. Nikapigwa pasipo kuhurumiwa nikitakiwa kutoa fedha zile. Nikayakubali maumivu yanipate kwakuwa sikuwa na uwezo wa kuyageuza yawe salama kwangu. Walipotosheka nikafukuzwa kama mbwa. Nikadhulumiwa fedha yangu. Machozi yangu hayakusaidia. Huzuni ya macho yangu haikutosha kuwadhihirishia walimwengu ya kuwa naumia na nastahili kuhurumiwa na kusahaulishwa maumivu. Nikarejea mtaani huku nikiwa na chuki na wadamu japo maisha ya mwanadamu yanamtegemea mwanadamu kama ngazi ya kufikia mafanikio kwa kiasi kikubwa. Nikatamani kulipa kisasi kwa mama yule kwa kuninyang’anya jasho langu la miezi minne. Lakini kila nilipokuwa nikilala, ilikuwa ikinijia ndoto ya mama yangu mzazi akinisihi kuepuka visasi.
“Mwanangu kulipa mabaya kwa aliyekutendea mabaya, ni sawa na kukata kamba anayoitegemea mtu aliye katikati ya maji ili imvushe ng’ambo ya pili. Kumbuka huwezi kufanikiwa pasipo kupitia kwa wenye kukutendea mabaya ili kukuongeza ujasiri na ari ya kuongeza juhudi katika kutimiza malengo yako. Hasira zako zijenge juu ya mafanikio na si kwa wanadamu ambao kesho watakuwa msaada kwako jap oleo hii wanakutenda yenye kukuumiza. Kumbuka asiyeiona thamani yak oleo, ataiona kesho na hata asipoiona yeye, yupo atakayeiona na kuithamini.” Hayo yalikuwa maneno ya mama yangu kipenzi. Akiongea kwa kutabasamu nakunifanya nami nilijenge tabasamu ndotoni tangu kifo chake. Taratibu nikaanza kusahau hasira zangu na kuamua kutafuta kazi sehemu nyingine. Nikapata kazi ya kumwagilia maua pamoja na usafi wa nyumba kiujumla katika nyumba ya Bwana mmoja tajiri. Nikajibidihisha katika kazi na kusababisha nipendwe na bosi wangu pamoja na mkewe na familia yake kwa ujumla. Hiyo ilikuwa baada ya kukaa bila kazi kwa mwaka mmoja.
“Mwanangu usisahau ya kuwa wapo uliowahi kuwakosea kwa bahati mbaya na hata kwa maksudi. Siku zote msamaha huleta nuru katika nafsi za watu. Hujenga amani moyoni na tabasamu usoni. Ukikosewa fumba macho na ukumbuke na wewe uliwahi kukosea.” Ilikuwa ni siku moja majira ya usiku nikiwa nimelala nyumbani kwa bosi wangu. Hii ikiwa ni wiki moja tangu niianze kazi mpya. Huyo ndiye alikuwa akinipatia furaha. Kila nilipomuona ndotoni, uso wangu ulikunjuka na kutabasamu. Moyo wangu ulisafishika na makovu yote ya mateso kuniondokea. Hakuwa akinipatia nafasi ya kuongea naye. Kila alipokuwa akimaliza kuniambia kilichomleta, alitoweka na kuniacha nikifurahi mwenyewe. Ikawa nikitamani kuwahi kulala ili niweze kutabasamu kwakuwa katika uhalisia sikuwahi kutabasamu tangu kifo chake.
Ni vyema kwa mwanadamu kujiandaa na maumivu kwasababu huwa hayana hodi. Huwa hayatumi maombi bali hujitokeza ghafla muda wowote. Nilishazoea kazi ile na mwili wangu kuanza kurejea katika hali njema. Miaka ikazidi kusogea mbele na kimo changu kuongezeka. Nikawa kijana katika vijana wenye kutamaniwa na wanawake. Ngozi yangu niliyozaliwa nayo ikarejea. Hapo ndipo matatizo yakarejea upya. Niseme kitu kimoja kwamba wengi wetu tumeumbwa na ufinyu wa fikra. Hatuna fikra katika kupambanua mwisho wa jambo. Ni siku moja nikiwa bustanini namwagilia mbogamboga, mke wa bosi wangu aliniita. Nikafunga maji na kwenda kumsikiliza. Nilipoingia ndani nilikuta ukimya kana kwamba hapakuwepo na mtu. Nikataka kurudi nje lakini kabla sijafanya hivyo nikamsikia akinitaka kuelekea chumbani kwake. Mapigo ya moyo wangu yalinienda kasi kwasababu miaka minne ya mimi kufanya kazi katika nyumba ile, sikuwahi hata kuikanyaga korido ya kuelekea chumbani kwa bosi wangu. Hakika nilisita na kuishiwa nguvu nisiweze kuchanganua kwa haraka ni nini ananiitia huko chumbani. Nikiwa nawaza akatoka chumbani kwake na kunisogelea hadi pale nilipokuwa nimesimama.
“Mwanaume gani unakuwa mjinga kiasi hicho?” aliniuliza lakini sikumjibu. Mke wa bosi wangu alikuwa mzuri na umri wake ulikuwa si tofauti sana na wangu. Nikikadiria huenda alinizidi miaka minne. Hivyo kuelewa na bosi wangu kiasi alichemka maana umri wake ulikuwa sawa na baba yake labda alivutwa na fedha. Sikuwa nimewahi kufanya mapenzi wala sikujua njia za kuanza kumshika mwanamke maana siyo kama paipu niliyoizoea kumwagilia nayo maua na mbogamboga. Yeye ndiye aliyenizindua katika bumbuwazi kwa kunivutia kifuani kwake. Kabla hajanifanyia chochote mlango ukafunguliwa akaingia bosi wangu akionekana kama mtu mwenye haraka. Nilihisi nywele zangu kuondoka zote pasipo kunyolewa kwa mshtuko nilioupata. Sikupewa muda wa kujieleza bali alichokifanya ni kutoka nje na kufunga mlango. Mke wake akaniachia na kurejea chumbani kwake huku naye akionekana kutetemeka mpaka jasho likimchuruzika. Ilikuwa ni zaidi ya sinema kitendo kile kwakuwa sikuwahi kukifikiria kama kingeweza kunitokea tena katika mazingira kama yale.
Nilijikuta nikishuka mwenyewe chini na kuketi huku machozi yakinibubujika. Lilikuwa ni pigo ambalo nilitamani liwe ndoto tena ya mchana lakini haikusaidia. Mlango ukafunguliwa wakaingia wanaume wawili na kunikamata kisha kunifunga kamba na kitambaa cheusi usoni. Walifanya hivyo pasipo purukushani yoyote kwakuwa nilikuwa katika mshangao mkubwa na usioweza kuelezeka kiurahisi. Nikaingizwa katika buti ya gari na safari ya kupelekwa kama mzigo sehemu nisiyoitambua ikaanza. Ulikuwa ni mwendo mrefu ambao nilisikia gari likipita katika barabara mbovu. Baada ya muda gari lilianza kupita katika sehemu ambayo lilisikika likikwaruzwa na miti. Haikupita muda mrefu likasimama. Wakateremka na kunishusha. Kisha wakanifungua kile kitambaa. Tulikuwa katikati ya pori lenye miti minene. Mifupi kwa mirefu huku sauti za ndege na wanyama zikisikika. Mbele yangu alisimama bosi wangu akionekana mwenye hasira kali dhidi yangu. Sitaki kuwa muongo kwamba zile ni njama zake na mke wake. Lakini ni kitu kilichoniumiza nafsi yangu.
“Ulikuja kwangu ukiwa kapuku. Ukiwa hutamaniki hata chembe. Ukiwa huna hata nguo ya kubadili. Ukiwa unanuka mwili na matambara yako chakavu. Nikakupokea na kukufanya uwe mpya. Lakini umekuwa kama nyoka kuteleza juu ya ngozi yangu pasipo kunikwaruza na hatimaye kuning’ata sehemu zangu za siri.” Alipomaliza kuongea hivyo, kilichofuata nilisukumwa tu na kuanza kuteremka kwa kasi kubwa mno. Mwanzo nilipaza sauti za kuomba msaada lakini kadri nilivyokuwa nikizidi kuserereka ndivyo nilivyopoteza kauli na kushindwa kutoa tena sauti. Baadaye sauti ilikoma kabisa. Macho yangu yakaona kiza. Kumbukumbu zangu za maisha yangu zikaanza kujionesha katika fahamu zangu kabla ya kupoteza fahamu.
Ni pale nilipozinduka na kuhisi uso wangu ukilambwa. Sikuweza kufumbua macho yangu kutokana na uoga. Uoga ukanikumba nikabaki kutulia huku moyo wangu ukienda mbio kuliko kawaida. Alikuwa ni nyoka wala hapakuwa na ubishi japo bado sikuwa nimemtizama. Baada ya muda akaniacha. Nikasikia akiondoka na kusababisha majani makavu kutoa sauti. Nikapumua kwa nguvu na kufumbua macho yangu. Chatu!! Hata njaa niliyokuwa nikiihisi ilipotea ghafla kutokana na hofu. Hiyo ilikuwa ni mara ya pili nikinusurika kwa kifo. Pengine alidhani mimi ni mzoga kutokana na hali yangu. Madonda yaliyogandamana na damu iliyokauka. Nzi walikuwa wakirukaruka juu ya mwili wangu baada ya kuvutiwa na harufu niliyokuwa nikiitoa. Ndugu zangu nilikuwa nikinuka. Hata nami harufu ya mwili wangu ilinitesa. Waone wanadamu wakiyafurahia ya ulimwengu. Wakirukaruka huko na huku na kumsahau Mungu. Dharau zisizo na maana. Viburi kwa wenzoao. Na majigambo mengineyo lakini hakika ni jambo dogo tu tunabadilika na kuwa takataka. Wanadamu tunanuka ndiyo maana tukatengenezewa manukato. Hicho ni kikwapa tu.
Sijui ni muda gani nilizimia kutokana na kile nilichofanyiwa. Nikajitahidi kuinuka na kusimama lakini nikashindwa. Paja langu lilikuwa na kipisi cha mti uliochongwa vyema. Labda ilikuwa ni kwa ajili ya wawindaji kutega wanyama. Kilikuwa kimezama katika nyama zangu za paja. Sikuwa na jinsi, nikavua shati langu ambalo lilishachanika hii nadhani ni pale nilipokuwa nikibiringita. Nikajifunga na ili kuzuia maumivu kisha nikashika kile kipisi cha mti na kukichomoa. Nikabahatisha lakini damu zikaanza kunitoka kwa fujo. Sikuweza kuzuia hivyo ikanipelekea kupoteza fahamu. Nilipozinduka mara hii sikuwa tena porini bali nilikuwa juu ya kitanda hospitalini. Nikavuta kumbukumbu ya kile kilichonitokea na mara yangu ya mwisho jinsi nilivyochomoa kipisi cha mti katika paja langu, machozi yakaanza kutiririka mfululizo. Nilikuwa nikiipitia tabu ya muda mrefu pasipo kosa lolote. Nilikuwa ndani ya dimbwi zito la simanzi kutokana nay ale niliyokuwa nikiyapitia. Nilikumbuka mengi ya utotoni kwangu wakati huo familia yetu ikifurahi nyakati zote lakini ikageuka simanzi ya muda mrefu kwa upande wangu. Maisha yangu yalibadilika kwa kiasi kikubwa vile ambavyo sikutarajia.
“Machozi ni chocheo la simanzi. Wala usihuzunike kiasi cha kufikia kumwaga machozi kwasababu ya maumivu ya moyo wako. Maumivu ya mayo wako yawe chanzo cha kuitafuta furaha uikosayo na kutawaliwa na huzuni.” Niweke wazi kwamba sauti ile pamoja na kiganja laini kilichonifuta machozi, kwa pamoja vilinifanya kugeuza shingo na kuitazama sura ya faraja ile. Alikuwa ni nesi. Alinisimulia mengi jinsi walivyoniokota nje ya hospitali yao asubuhi bada ya kutupwa na mtu au watu wasiojulikana nikiwa nimezimia. Ilikuwa ni simulizi ambayo nilitamani kuisikiliza kila wakati lakini alipomaliza kunisimulia haikujirudia tena. Kwa msaada wa nesi Joanitha niliweza kupatiwa huduma nzuri kwa msaada wa Joanitha hadi pale nilipopona na kutakiwa kuondoka pale hospitali ya Kemondo.
“Nitaenda wapi?” nilijiuliza swali kwa sauti ya juu.
“Nyumbani kwangu.” Ilikuwa ni sauti ya Joanitha. Nikamshukuru kwa ukarimu wake. Tukaongozana hadi nyumbani kwake ambapo alikuwa akiishi na mama yake mzazi. Ukaribu wetu ukaongezeka na hatimaye tukaanzisha uhusiano wa kimapenzi. Yeye akanipenda na kuniheshimu. Mama yake naye akanipenda na kunithamini. Akaniita mkwe wake nikafarijika. Nikayasahau maumivu. Baada ya kulia kwa muda mrefu hatimaye nikapata faraja. Tabasamu likarejea na moyo wangu ukaondokewa na makovu. Siku si nyingi Joanitha au niseme aliyerejesha faraja yangu akapata ujauzito. Furaha ikaongezeka zaidi. Akanifungulia duka nami nikaliendesha kwa moyo mmoja na juhudi kubwa. Likaongezeka na kuzalisha jingine.
“Hoehae?” nilijiuliza nikiwa siamini kama kweli mimi ndiye yule niliyekuwa nikinuka mwili. Niliyekuwa nikioga katika maji ya mitaro na hata katika madimbwi. Kila niliyepishana naye kabla ya kununua usafiri wangu binafsi, alitamani tupishane tena. Jinsi nilivyokuwa nikinukia manukato ya gharama.
“Mume wangu huwezi kupata tatu pasipo kuanza na moja. Adui mkubwa wa mwanadamu ni kuvunjika moyo. Matatizo yasikufanye kutetereka. Ukimwagiwa pilipili katika macho isiwe chanzo cha wewe kuwa kipofu kwa kushindwa kuchukua maji safi na kuyatakatisha macho yako kwa kuondoa pilipili. Maisha ni kugeuza pande mbili tofauti ikiwa upande wa kwanza umechafuka na ukashindwa kuusafisha kutokana na vikwazo visivyoweka kuvukika.” Kwanini nisifarijike? Kwanini niendelee kuumiza nafsi yangu kwa yaliyopita?
“Asante mke wangu kwa kunifariji na kunijenga kwa maneno yenye hekima. Hakika wewe ndiye umeletwa kwa ajili ya kuyarudishia macho yangu nuru iliyokuwa ikizidi kufifia kila nilipolitizama jua likichomoza na kuchwea.”
“Usijali mume wangu. Hekima ya mtu huanzia katika matendo yake na hatimaye hukamilika katika maneno yake. Kamwe usikubali kuhadaika na tabasamu la mwanadamu ilihali hutambui wapi ulipo moyo wake. Pengine yapo maumivu uliyoyasababisha mwenyewe kwa kudanganyika na cheko la mwanadamu.” Sikuongea tena zaidi ya kumkumbatia na kujilaza katika kifua chake. Kila nilipokuwa nikiyatizama macho ya Joanitha, nilikuwa nikizidi kufarijika. Unajua kwanini? Kwasababu yeye ndiye aliyeibeba furaha ya maisha yangu.
**
Ilipita miaka miwili tangu nikutane na Joanitha. Ndipo nilimuona mtu aliyenisababishia mateso ndani ya pori ambalo hadi leo hii silitambui. Ni katika taa za barabarani nikiwa nimesimama kusubiri ziniruhusu. Kioo cha gari langu kikagongwa nami nikakishusha baada ya kujua ni ombaomba. Nilishtuka mno nay eye pia alistaajabu kuniona. Alikuwa ni bosi wangu enzi nikifanya kazi nyumbani kwake kabla ya mkewe kunitaka kimapenzi lakini kabla ya kutimiza azma yake akatufuma. Alikuwa akihuzunisha. Alikuwa mchafu kuliko mimi enzi zangu nikiwa hoehae. Ama kwa hakika maisha ni sawa na saa. Mishale kusafiri huku na kule lakini kujikuta ikirudi palepale ilipoanzia safari yake. alikuwa kachakaa vya kutosha. Hakuwa yule mwenye kutembea kwa kutanua mikono na simu za gharama mikononi mwake. Mwenye kuning’iniza cheni za gharama shingoni mwake.
“Nisamehe ni maisha tu” hapo ilikuwa ni baada ya kumtaka apande kwenye gari na kuondoka naye hadi sehemu ambayo niliona inafaa kuzungumza naye na ilikuwaje hadi akawa katika hali ile. Aliweza kunihadithia mengi ambayo sikuwa nikiyatambua hapo awali. Kumbe alikuwa akiishi chini ya mkopo wa benki kwa dhamana ya nyumba yake. Pale aliposhindwa kulipa akafilisiwa na mkewe akamkimbia. Kwa jinsi alivyokuwa ametawaliwa na kiburi, hata hakuwa na marafiki. Ndugu zake walishamtenga. Elimu yake ikachomwa na mkewe kwasababu elimu ni vyeti kama vyeti huna basi huna elimu.
“Naomba nisamehe mno maisha yamenifunza kupitia matendo yangu.” Ili moyo wangu upate kuwa huru niliamua kumsamehe. Sikumficha chochote Joanitha naye akanitaka kumsamehe. Nikamsemehe. Sikuwa na baba wala mama na hata Joanitha hakuwa na baba hivyo huyo akawa baba yetu. Familia ikaongezeka. Furaha ikaongezeka maradufu. Nayo biashara kwa usimamizi wangu pamoja na baba yangu wa kufikia ikazidi kushamiri na kuvuka mipaka ya maendeleo. Nikaisahau huzuni japo huja wakati ambao hatutarajii.
“Naishi kwa amani kwasababu naipenda amani. Siitaki chuki kwasababu itanipotezea amani kwakuwa amani ya mwanadamu huanzia moyoni mwake. Ikitoweka ya moyoni hapana shaka hata ya maisha yake itatoweka vilevile.”
Mwisho!!!

Post a Comment

0 Comments