Header Ads Widget

Responsive Advertisement

NILIKATAA UCHUNGAJI NIKAWA MKUU WA WACHAWI



TAKRIBANI wiki tatu nilikuwa nafuatilia mkasa wa dada Easter Deo. Hakika mkasa huo ulinigusa sana nami nikashawishika kusimulia yaliyonikuta katika maisha yangu.
Naamini kuwa kuna baadhi ya watu hawakuamini mkasa wa dada Easter kama ni wa kweli ama ulikuwa ni wa kutunga.

Ninachoamini ni hiki, uchungu wa maumivu ya ugonjwa ama majeraha yoyote huwa anayasikia mhusika lakini si mtu mwingine. Kwa jina naitwa Steven Frances Soso, ni mwenyeji wa Morogoro Wilaya ya Ifakara.

Nimezaliwa katika familia ya wacha Mungu. Baba yangu mzee Frances Kasela Soso ni Mchungaji wa Kanisa la Living Word Pentecost lililopo Ifakara.

Nilikuwa na hali ya kuwa naumwa mara kwa mara. Pamoja na kwamba baba yangu ni mchungaji, binafsi sikukubaliana na masuala ya ulokole kwani niliona kama ni shida kwangu.
Baba yangu alikuwa anafanya taratibu za kuniandaa kuwa mchungaji hapo baadaye. Alikuwa karibu na mimi na alikuwa ananielekeza mambo mbalimbali yanayohusiana na uchungaji.

Kitendo hicho nilikiona kama mzigo kwangu nikaamua kuondoka na kwenda kupanga chumba Ifakara mjini.
Nikiwa hapo, nilimpata rafiki yangu ambaye sitapenda kutaja jina lake. Rafiki huyo alikuwa msaada mkubwa kwangu.

Tatizo la kuugua mara kwa mara lilionekana kuwa la kawaida. Nilikuwa naumwa kichwa, hali iliyokuwa inanifanya niwe nalia kila kukicha kutokana na maumivu makali niliyokuwa nayapata.

Kila nikienda kupima madaktari hawakuona kitu chochote.
Hali hiyo ilinitesa kwa muda mrefu. Rafiki yangu alinishawishi kwenda kwa waganga wa jadi kwa ajili ya kupata tiba zaidi.

Nilipofika kwa mganga huyo sehemu inayoitwa Ipangalala, alitukaribisha kwa furaha.
Alipoanza matibabu aliniambia kuwa, sisumbuliwi na kitu chochote bali nina mapepo ya kiganga hivyo nalitakiwa nifuate masharti yote ili niwe salama.

Nilianza kupata matibabu kwa ajili ya kuondoa mapepo hayo.
Niliambiwa nikanunue ubani ili niweke ndani ya chumba nilichofikia kwa mganga huyo. Hali yangu niliona kuwa na mabadiliko makubwa.

Kulikuwa na watu wengi ambao walionekana wakiwa watupu isipokuwa sehenu za siri walikuwa wamejiziba na ngozi nyeusi.

Niliwekwa katikati ya kaburi kisha nikakalishwa kwenye kigoda kilichowambwa na ngozi ya mamba.

Nilifunikwa na ngozi ya mnyama aina ya duma huku idadi kubwa ya watu waliokuwa wamenizunguka wakiimba nyimbo nisizozijua.
Mara alitokea bibi mmoja akiwa na kisu akaja nilipokuwa nimekaa kisha akaniambia niinamishe kichwa chini.
Nilipofanya kama alivyonieleza, alinichanja chale moja kwa kutumia kisu hicho na kunipaka dawa ambayo iliniwasha sana.
Wakati anaweka dawa alikuwa anazungumza maneno kwa msisitizo huku akiishindilia izame sehemu aliyonichanja. Bibi huyo alipomaliza kunipaka dawa akapotea ghafla.
Nilinyanyuliwa kwenye kiti hicho na kukalishwa kwenye ungo na kuambiwa huo ndiyo utakuwa usafiri wangu.
Nikiwa kwenye ungo huo, nilikabidhiwa pembe mbili ndefu nyeusi. Pia nilipewa mkuki kisha nikafungwa kitambaa cheusi katika mkono wa kusho.
Mwanamume mmoja aliyekuwa amevaa ngozi nyekundu alisogea karibu nami na kuniambia kuwa, muda wa kufanyiwa taratibu za kuwa mkuu wa wachawi siku hiyo ulikwisha, hivyo nilitakiwa kurudi nyumbani mpaka kesho yake.
Alipomaliza kusema hivyo, alinyosha mikono yake kuelekea juu na kuniambia niondoke. Ghafla nilishangaa nikiwa ndani nimelala.
Niliona kama ni ndoto. Lakini mwili wangu ulionekana mchovu kweli kiasi kwamba nikawa sielewi kama nilikuwa naota ama la.
Kulipokucha yule mganga aliniambia kwamba, tatizo la kuugua kichwa mara kwa mara sitaliona tena kwa sababu tayari tiba yake ilipatikana.
Nilimwambia anipe niimeze ili niondokane na mateso ambayo niliyoyapata kila kichwa kilipoanza kuuma.
Mchana nikiwa nimelala chumbani kwangu, niliona nakimbizwa na simba dume aliyekuwa na hasira kali.

Nilishtuka nikajikuta nipo kitandani. Mapigo ya moyo yalienda mbio. Katika hali ya kushangaza, yule mganga aliingia chumbani kwangu na kuniambia kuwa, nisiwe na wasiwasi lazima nichanjwe chale tatu kisha nipakwe mafuta ya simba.

Aliniambia kuwa, nilikuwa nimetupiwa majini ambayo yalinitaka niwe mkuu wa wachawi. Tulizungumza mambo mengi sana kisha akaondoka akaniacha nimelala.
Kabla ya kukabidhiwa mikoba ya ukuu wa uchawi, usiku nikiwa nimelala niliota ninaletewa dawa za kichawi kisha napewa maelekezo ya kutibu watu.
Nilianza kufundishwa kazi ya uganga wa kienyeji. Nikawa natibu watu wenye matatizo mbalimbali.

Siku moja usiku niliota niko porini naoneshwa dawa kwa ajili ya shughuli za kichawi. Kumbe haikuwa ndoto bali lilikuwa tukio la kweli.

Nilifanya kazi hiyo ya uganga kwa muda mrefu. Mganga alipoona nimefuzu shughuli ya uganga, kama ya wachawi ilikutana na kunipa maelekezo ya kwende Bahari ya Hindi Dar es Salaam kwa ajili ya kuchukua mchanga na baadhi ya vitu ikiwa ni hatua za mwisho za kusimikwa kuwa mkuu wa wachawi nchini.

Niliambiwa kuwa, nikisha chukua mchanga huo wa bahari nitaelekea Songea kwa ajili ya kukabidhiwa rasmi ukuu wa uchawi.
Siku moja saa nane usiku tulienda makaburini kwa ajili ya kujifunza mambo muhimu ya kichawi.

Tulikuwa tunapaa kwa kutumia ungo na wakati mwingine kirungu. Ungo ambao tulikuwa tunautumia si kama unaotumika kupepetea mchele ama unaofahamika na watu wote, bali upo tofauti kabisa.
Kile kirungu nilikuwa nakichukua na kunuiza maneno flani nakiweka kwenye goti kisha nalikunja ghafla napaa kama mshale.

Makaburini huko nilikabidhiwa dawa yenye mchanganyiko wa miti sita. Na tulikuwa tunatembea uchi na ilikuwa nikitaka kuingia kwenye nyumba ya mtu kwa ajili ya kumchezea kichawi, nilikuwa napitia kwenye pembe ya nyumba kwani ni mwiko mchawi kupita mlangoni.

Siku zote wachawi huwa wanapita kwenye pembe ya nyumba na si mlangoni kama wengi wanavyodhani.
Siku moja ilifanyika sherehe makaburini nikiwa pamoja na vijana watatu ambao nao walikuwa wanapewa mafunzo ya uchawi.

Siku hiyo nilichanjwa chale kwa ajili ya kinga mwilini mwangu. Ilitoka damu nyingi kisha nikabadilishana na ya simba.

Simba huyo alionekana amelala kaburini hapo na damu yangu ilichukuliwa ikawekwa sehemu aliyochanjwa na ikachukuliwa yake ikawekwa kwangu.
Niliambiwa kuwa, lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha nakuwa bingwa wa wachawi kuliko wengine.

Nikiwa katika harakati za kujiandaa kwenda kuchota mchanga baharini, nilipata safari ya kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kutembea.


Nilipofika Dar es Salaam nilifikia kwa ndugu zangu lakini sikukaa sana kutokana na kusumbuliwa na kichwa.

Nililazimika kurudi Ifakara kuendelea na kazi za kichawi. Siku moja usiku nilipewa kirungu kama usafiri kwa ajili ya kwenda kuchota mchanga chini ya bahari.
Nilizama chini ya bahari na kukutana na ulimwengu mwingine. Kulikuwa na watu wa ajabu waliokuwa wanafanya kazi saa 24.

Nilikaribishwa na babu mmoja aliyekuwa amevaa mapembe kichwani huku akiwa na watu walioonekana kuwa ni walinzi. Walikuwa wanamsujudu mara kwa mara.
Babu aliponiona alicheka sana na kuniambia hakika mimi ni mtu mwema kwani nilikubali kukataa uchungaji na kuwa mkuu wa wachawi.

Nilikabidhiwa kiganja cha mtoto nikaambiwa nitakuwa nakitumia katika shughuli zangu za uchawi kisha nikapewa mchanga nikaambiwa niondoke nirudi Ifakara.
Nilipofika nyumbani nilimkabidhi yule mganga na kumuambia kuwa, usiku nitakuwa na safari ya kuelekea kuzimu kwa ajili ya kusimikwa rasmi kuwa mkuu wa wachawi mkoa wa Morogoro.

Ilipofika saa tano usiku, safari ya kuelekea kuzimu ilianza na tulizama chini ya baharini kwa ajili ya kupewa zana za uchawi.
Nilikutana na babu aliyenipa kiganja cha mtoto na alikuwa amezungukwa na watu waliokuwa wanamsujudu huku yeye akitikisa kichwa.

Babu alinyanyuka kwenye kiti chake na kuniambia nikakae. Nilipokaa kwenye, ghafla nilihisi kama usingizi mzito na hiyo ilitokea baada ya babu kunimlika na kioo kilichochoma macho yangu.

Wakati huo alikuwa anazungumza maneno ambayo sikuyaelewa. Baada ya nusu saa usingizi ulitoweka na kuniambia hakika nimefuzu kuwa mkuu wa wachawi.
Babu alionekana mwenye furaha, alinipatia usinga mwekundu ambao hutumiwa na wachawi kwa kazi maalum na kuniambia nitakapofika duniani utanisaidia kwa ajili ya kazi zangu.

Alinisisitiza kuzingatia maagizo yote niliyofundishwa ili siku moja nisije nikawasaliti. Sharti moja wapo ilikuwa nisifike kanisani kwa sababu kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kiapo nilichoapishwa.

Niliambiwa nikifika kanisani niende kwa lengo la kudhoofisha nguvu za utumishi na kuifanya ibada kwenda kinyume na walivyopanga wahusika.
Nilionyeshwa dawa za kuwamaliza nguvu viongozi wa dini na kuwadhoofisha kiimani. Niliambiwa nitakuwa naenda kwenye makanisa na kupuliza dawa hiyo ili waumini wawe na usingizi wakati mhubiri akihubiri.

Nilirudi duniani. Nikiwa nimefuzu na kusimikwa kuwa mkuu wa wachawi, siku ya Jumamosi nilipata safari ya kuja Dar es Salaam kwa ajili ya matembezi.

Kesho yake (Jumapili) nilienda katika Kanisa la Huduma ya Neno la Upatanisho iliyopo Bustani ya Edeni Kitunda Kivule zamani ikijulikana kama Matembele ya Kwanza kwa lengo la kufanya nilichoelezwa kule kuzimu.

Niliingia kwenye huduma hiyo nikamkuta mtumishi wa Mungu Askofu na Nabii, Nicolaus Suguye akihubiri madhabahuni.

. Nilijaribu kurusha dawa zangu ili kumdhohofisha lakini haikuwezekana.



Niliamua kurudi nyumbani ili nikajipange upya. Nilikwenda kwenye makanisa mengine kwanza kujaribu kama dawa nilizopewa zinafanya kazi kweli ama la!
Jumapili moja niliingia kwenye kanisa na mtumishi anayejiita askofu mwenye wafuasi wengi. Niliwakuta waumini wachache wanapanga viti kwa ajili ya ibada.

Nilikaa kwenye kiti cha nyuma kama muumini kisha nikachukua dawa yangu na kuanza kunuiza maneno mazito ili kila atakayeingia ndani ya kanisa hilo awe na usinginzi na umeme ukatike ghafla.

Lengo la kukata umeme ukatike ni kuviharibu vyombo vya muziki wanavyotumia pamoja na kipaza sauti cha askofu.
Ibada ilipoanza, kama kawaida walifanya maombi ambayo hayakuwa na athari zozote kwangu. Askofu alisimama kwa ajili ya mahubiri, asilimia kubwa ya waumini walianza kusinzia.

Macho yao yalikuwa mazito hasa, nilifanikiwa kuwanasa wenye imani haba. Wakati askofu anahubiri nilifanya maarifa ya kukata umeme na kufanikiwa kuviunguza vyombo vya muziki na kipaza sauti alichokuwa anakitumia.

Niliondoka baada ya kuona nimefanikisha adhma yangu. Jumapili iliyofuata nilikwenda tena kwenye Huduma ya Neno la Upatanisho kwa Askofu na Nabii, Nicolaus Suguye.

Nikiwa ndani ya huduma hiyo nilishangaa, Suguye alitambua kama nipo ndani na kusema:
Naona leo wachawi wamekuja kutujaribu, leo watapeleka salamu kuzimu kwamba, huduma hii inaongozwa na mtumishi anayemtumikia Mungu wa kweli.'

Kama kawaida, alianza kuhubiri kwa ujasiri wa ajabu pamoja na kujua mimi nipo ndani. Baada ya mabubiri ilifuata zamu ya maombezi na hapo ndipo nilijuta kwa nini niliingia ndani ya huduma hiyo.

Muda wote wa mahubiri mwili wangu ulikuwa unachomwa chomwa na vitu kama sindano. Wakati wa maombezi nilishangaa kuona nimetoka mbele kana kwamba naenda kuombewa.
Aliposogea kwangu, alinyoosha mkono wake kuelekea kwenye kifua changu. Niliona naungua kwa moto, nikaanguka chini na kupoteza fahamu. Nilipozinduka sikuwa na nguvu za kichawi tena, nikajikuta nasema:

Nisamehe Mtumishi wa Mungu, nilikataa uchungaji nikawa mkuu wa wachawi na hapa nilifika kukudhohofisha kihuduma lakini nimeshindwa.'
Kauli hiyo iliwashtua waumoni wengi baada ya kuwasimulia jinsi nilivyokuwa nafanya kazi ya kuwapulizia dawa ili wapate usinginzi.

Baada ya kuombewa nilirudi nyumbani nilipofikia. Usiku wa manane, yule babu aliyenisimika kuwa mkuu wa wachawi alikuja kwa njia ya kishirikina akiwa amekasirika na kusema:

Kwa nini umeamua kutusaliti? Tulikwambia ukiona kanisa ambalo halina nguvu ya Mungu ingia, ila usiingie kama unaona kuna upinzani mkubwa.'

Akiwa anasema hayo, sikujua alipatwa na kitu gani, kwani nilimsikia akipiga kelele za kuomba asamehewe akiahidi kuwa, hatanisumbua tena. Aliponyamaza alipotea kimiujiza.

Msomaji huu ni mkasa wa kweli alionisimulia Steven Soso ambaye sasa ameokoka baada ya jaribio la kutaka kummaliza nguvu za huduma Askofu na Nabii, Nicolus Suguye.
Watu wengi mmekuwa mkinipigia simu kutaka kujua kama mkasa huu ni wa kweli ama ni wa kutunga. Namba ya simu ya Soso ni 0713 271 850.

''MWISHO''

Post a Comment

0 Comments