Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MKEO AMEFARIKI




SIMULIZI FUPI : MKEO AMEFARIKI.

“Mkeo amefariki Msiba uko hapa nyumbani?” Denis alipokea ujumbe mfupi kwenye simu yake, kuangalia ulitoka kwa Mama yake mzazi. Nguvu zilimuishia, alikuwa akiongea na mteja ofisini kwake lakini sauti ilikauka.
Bila kujijua alijikuta ananyanyuka na kuanza kutembea. tembea ofisini kwake akiwa hajitambui. Wafanyakazi wake walimuuliza bosi vipi lakini hakuwa na jibu la maana la kuwapa.
Akili yake ilikumbuka maneno ambayo alimwambia mkewe asubuhi wakati anaondoka, mkewe alimwambia sukari imeisha na kwa dharau alimjibu, “Sasa unaniambia mimi ili nini? Kwani ni lazima unywe chai, huko kwenu mlikua mnakunywa chai kila siku?”
Alikumbuka namna usiku wake alivyompiga makofi baada tu ya mboga kuungua alipochelewa kuepua kwani alikua ananyonyesha mtoto wao wa mwisho ambaye yeye mwenyewe ndiyo alimuita amnyonyeshe kwani alikuwa analia sana.
Alikumbuka namna siku mbili kabla mkewe alisema amechoka kupigwa na kunyanyaswa, anakumbuka namna alivyomjibu kwa dharau kuwa kama amechoka aondoke amuachie watoto wake.
“Ameniachia wanangu!” Alijikuta anaropoka na machozi yalianza kumtoka. Alishindwa hata kutembea hivyo alikaa chini kabisa sakafuni. Wafanyakazi wake walikuja na kumnyanyua na baada ya kumuuliza ndipo alipowaambia mkewe amefariki.
Walimchukua mpaka kwenye gari na safari ya kurejea nyumbani ilianza, walifika nyumbani, kila kitu kilikuwa kimya, nyumba ilikua imefungwa na hakukuwa na mtu.
Denis alizidi kuchanganyikiwa zaidi asijue nini cha kufanya ndipo alipokumbuka kuwa Mama yake alimwambia msiba uko nyumbani hivyo alidhani kuwa ni nyumbani kwao.
********************

Safari nyingine ilianza, Dennis alikuwa na mawazo, hayakuwa mawazo tu ya kufiwa bali ya aibu. Pamoja na kumiliki kampuni kubwa akiajiri watu zaidi ya kumi lakini mkewe alimnyanyasa na kumtesa kama kinyago, mbali na kumpiga lakini alikua hamhudumii vizuri.
“Atakuwa amefia kwa Mama wakati ameenda kuomba hela ya matumizi…” Aliwaza kwani mara nyingi alipokuwa akimnyima pesa Mama yake mzazi ndiyo alikuwa akimsaidia na ndiye alizuia mara nyingi mkewe asiondoke.
Alifika mpaka nyumbani kwao, kweli kulikuwa na msiba, maturubai yalishawekwa, watu walishaanza kupika na watu walishaanza kujaa taratibu. Alijitahidi kushuka kwenye gari na kuanza kutembea kuelekea nyumbani.
Watu walikua wakimsalimia na kumpa pole, aliipokea kwa aibu huku akiwaza ni kitu gani kiliwasukuma wazazi wake kufanyia msiba pale na ni nini kilikuwa kimesababisha mauti ya mkewe.
“Ameumwa sana muacheni apumzike..” Ilikuwa ni sauti ya Baba yake mzazi ikimwambia jirani yao mmoja. Hapo ndipo alichanganyikiwa zaidi akiwaza ni kwa namna gani mkewe alikuwa anaumwa bila yeye kujali.
Lakini alikumbuka ni mara nyingi mkewe alimwambia anaumwa lakini alidharau na ni mara nyingi Mama yake alimsema kuhusu kutokumsikiliza mkewe na mara nyingi tu Mama yake aliongozana na mkewe hospitalini.
Yeye kwake yote hayo hakujali, kila mke alipomwambia anaumwa yeye alidai haki yake ya ndoa, alizidi kumpiga na alianza kukumbuka namna ambavyo alimpiga mpaka kulazwa lakini bado hakujali.
Aliwaza, "Labda ndiyo ilikuwa sababu ya kifo chake? Au alikuwa anaumwa kimya kimya halafu hasemi akaja kusema nyumbani?” Alitembea mpaka kufika ndani, alikaa na kusalimiana na ndugu wengine ambao nao walikuwa wanampa pole kwa msiba.
Alizipokea huku akijaribu kujizuia machozi yasitoke. Mara mtoto wake wapili wa miaka minne alikuja. Alikuwa akilia akimtaka Mama yake watu wakimwambia asubiri Mama yake anakuja.
Mtoto alimkimbilia Dennis na kuanza kulia "Baba namtaka Mama, namtaka Mama." Denis alichaganyikiwa kwani hakuwa na jibu la kumpa, hakujua amwambie nini kuhusu Mama yake.
Mara mtoto mwingine mkubwa kidogo wa miaka saba alikuja, alikuwa amembeba mtoto wao mdogo mchanga wa miezi sita. Alimfuata Baba yake na kumuuliza, "Baba, Mama yuko wapi Jack anataka kunyonya."
Hapo ndipo aliishiwa nguvu kabisa, maneno yake ya “Ondoka niachie wanangu" yalizunguka kichwani kwake. Aliwaangalia wanawe na kusema, "Kweli nimeachiwa, umeniweza Juddy mke wangu."
Alijikuta anaanza kulia kama mtoto kitu ambacho kiliwafanya na wanawe wote kulia. Dennis alichanganyikiwa, kila mtu aliyekuwa anakuja nyumbani alienda kumpa pole, nguvu zilimuishia alikata tamaa, na majuto ya hali ya juu, kila tendo baya alilokuwa akimfanyia mkewe lilimjia kichwani.
*********************
“Mama Jose njoo umnyonyeshe mtoto analia toka muda mrefu.” Ilikua ni sauti ya Mama yake. Dennis alishtuka na kunyanyuka kuangalia, Mama Jose ni mkewe na hakujua ni kwa nini Mama yake alikuwa anamwambia aje kumnyonyesha mtoto wakati alishafariki dunia.
Kabla hajasema chochote Mama yake aliingia kisha, “Ohhh Dennis umekuja? Nikajua utakuja baadaye kazi zimekubana, mkeo alisema hupatikani kwenye simu.”
Dennis alizidi kuchanganyikiwa, alibaki na mshangao. Mara mkewe aliingia, hapo ndipo alichanganyikiwa zaidi, alishtuka kama vile ameona mzimu, kidogo amdondoshe mtoto aliyekuwa amempakata.

“Vipi Baba Jose…” Mkewe alimuuliza kwa maana namna alivyokuwa akimuangalia haikuwa kawaida yake. “Uko hai mke wangu?” Alijikuta anauliza. “Ndiyo kwani vipi ulitaka nife?” Mkewe alijibu kwa kebehi kidogo kwani alijua ni dharau ya mumewe.
“Lakini Mama......” Dennis aliongea kwa kushangaa huku akimuangalia Mama yake. Mama yake alitabasamu na kumwambia, "Aliyefariki ni Bibi yako si ndiyo alikuwa anakuita mume wangu?
"Wewe mbona kila siku ukipiga simu unaulizia mke wangu hajambo." Dennis alipumua kwa nguvu huku akikaa chini, mkewe alimchukua mtoto kwenda kumnyonyesha. Denis alimfuata huko huko chumbani, alipiga magoti mbele yake na kusema, “Samahani mke wangu nilikuwa sijajua thamani yako mpaka leo. Yaani leo ndiyo nilichanganyikiwa, nilijua umekufa na tayari nilishaona maisha hayawezekani bila wewe. Ninaahidi nitabadilika nitakuwa mume mwema na kamwe sikunyanyasi tena."
Mama yake ambaye alisimama mlangoni alitingisha kichwa na kucheka huku akisema, “Unavyoringa uachiwe watoto kila siku, unajua uchungu wa kulea wewe au unataka uachiwe ili uje kunitupia wanao hapa nianze kulea wajukuu?!”
Hakusubiri hata jibu aliondoka akimuacha mwanaye akiendelea kuomba msamaha akiwa haamini kuwa mkewe yu hai. Siku ile ndiyo ilikuwa siku ya Mabadiliko kwa Dennis kwani hakuwahi kumpiga wala kumnyanyasa tena mkewe
.
*****MWISHO******

BOFYA HAPA KWA KUPATA TAARIFA ZAKO ZA KITAMBULISHO CHA NIDA

Post a Comment

0 Comments