Header Ads Widget

Responsive Advertisement

DAU LA MNYONGE



SIMULIZI FUPI : DAU LA MNYONGE
MTUNZI : MWL DAMIAN CHIKAWE

(hiki ni kisa cha kweli)
Jina lake halisi (yaani jina alilopewa na wazazi wake) ni Ayubu Twisana,lakini akiwa kazini kwake anatambulika kama Mwalimu Twisana kwa upande wa waalimu wenzake na kwa wanafunzi wanamtambua kama "Chaunoko". Mwalimu Twisana ni mtoto pekee wa Mzee Twisana,akiwa na umri wa miaka saba kipindi anaaza shule ya msingi waalimu wote walimpenda sana kwa jinsi alivyokawa ana nidhamu akiwa darasani na hata nje ya darasa,kila wakati walitamani kuwa naye karibu ili asijiingize katika makundi ya wanafunzi wahuni,na hii ndio desturi ya waalimu wengi ,huwa wanapenda sana kuona mwanafunzi anakuwa na bidii,furaha ya mwalimu ni kuona pale ambapo wanafunzi wanafaulu vizuri.
Ayubu Twisana 'Mwl Twisana' alikuwa mwanafunzi pekee aliyefaulu katika darasa lake na kuendelea na Elimu ya sekondari,wazazi wake walifurahi sana,waliuza kila kitu walichonacho ikiwemo baiskeli na mbuzi wao ili wapate pesa ya kumpeleka mtoto wao shuleni.
Ayubu alifanikiwa kuanza Sekondari,na muda wote alikuwa anapenda kujifunza kwa bidii sana ili siku moja akawasaidie wazazi wake,hali ya umaskini ya nyumbani kwake ndio iliyomfanya apambane sana katika masomo na katu wala hakuwahi kujihusisha na masuala ya mapenzi ingawa wasichana wengi walikuwa wakijiringisha kwake kutokana na umahili wake darasani. Kijiji kizima kilimpenda sana na hata baadhi ya wazazi wengine walisikika wakiwaambia watoto wao "kwa nini musiwe kama mwenzenu Ayubu?".
Miaka ilisonga na hatimaye Ayubu alimaliza elimu ya sekondari na kubahatika kupata alama za kumfanya aende kidato cha tano na sita.
Pia huko nako alifanikiwa kupata alama za kwenda chuo kikuu,ila hakuweza kwenda huko kwani hakuwa na pesa za kuendelea na chuo kikuu na badala yake alienda chuo cha Ualimu ngazi ya diploma. Baada ya miaka miwili alifanikiwa kumaliza na akarudi kijijini kwao akisubiri apangiwe ajira.Mabinti wengi walitamani kuolewa na Ayubu,ila Ayubu wala hakuwa teyari kwa wakati huo kwani malengo yake yalikuwa bado hayajatimia na mpaka wakati huo Ayubu wala hakuwahi kumjua mwanamke.
Ajira zilipotoka, Ayubu naye alipata na akapangiwa kituo cha kazi.Wazazi wake walifurahi sana na waliamini angalau shida zao zitakoma kwa kiasi fulani.
Ayubu 'mwalimu Twisana' alikuwa mwalimu mchapa kazi sana,alijitahidi kwa kadri ya uwezo wake ili kuhakikisha nidhamu ya wanafunzi inarudi kwani aliikuta shule ikiwa na mazingira mabovu sana na wanafunzi pia hawakuwa na nidhamu.Kutokana na Juhudi zake baada ya muda Mwalimu Twisana alipewa kitengo cha nidhamu na huko ndiko lilikozaliwa jina la Chaunoko na pengine furaha yake ya kuwa mwalimu kuisha kabisa.Alipambana na wanafunzi wahuni wote, wanafunzi wengi walimchukia sana na hata baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao walimchukia pia kwani walidhani anawaonea watoto wao.
Siku moja alipoamka asubuhi alikuta nywele zake zote za kichwani zimenyolewa,pia alikuta ujumbe kwenye karatasi uliosomeka hivi "wewe si wa kwanza wala wa mwisho,walikuwepo wakaondoka na watakuja wataondoka,achana na watoto wetu,hill ni dogo tu,ukiendelea kuna baya zaidi litakupata".Mwalimu Twisana hakujali hilo aliendelea na kazi yake kama kawaida.Wanafunzi wahuni wakishirikiana na wazazi wajinga walifanya kila ubaya kwake lakini walishangaa kumuona mwalimu Twisana haachi kuwaadabisha wanafunzi.
Wazazi walimtega mtego wao wa mwisho ambao huo waliamini hachomoki.Waliamua kumtumia mwanafunzi wa kike ili aonekane kama anashiriki naye mapenzi na hatimaye wamtie nguvuni.Ama kweli waliodhamiria hutenda!
Siku moja majira ya usiku,Mwalimu Twisana alikwenda bafuni kuoga.Bafu lilikuwa nje ya nyumba hivyo alivyoenda kuoga aliacha mlango wa chumbani kwake wazi kwani alipanga chumba kimoja na alikuwa akiishi peke yake. Akiwa bafuni,huo ndo muda waliotumia wanakijiji kutimiza adhma yao,walimchukua msichana na kumvua nguo na kubaki na chupi tu kisha wakamwingiza chumbani kwake na kumwambia ajilaze kitandani kwake.
Mwalimu Twisana akiwa hana hili wala like maskini wa Mungu alipomaliza kuoga alitoka bafuni,ile anataka kuingia tu ndani alishangaa sana kuona mkululo wa watu wakimwambia asimame.Alitii wito,mzee mmoja akasema
"mimi ni Mwenyekiti wa mtaa huu,huyu ni mgambo wetu wa kijiji,na hawa ni wazazi ni wazazi wa binti anayeitwa Mariamu,wanamtafuta tangu jana ila kwa bahati nzuri tumepata taarifa kuwa yupo kwako na we we ndio unamrubuni kimapenzi,sasa tumekuja kupekua chumbani mwako ili tumchukue binti yetu"
Huku akishangaa maelezo hayo marefu yaliyotolewa na mzee,mwalimu Twisana kwa kujiamini aliwaambia waingie ndani waangalie mtu wao,alijiamini kwa sababu aljiua ndani kwake hakuna mtu yeyote aliyemwacha.
Walipoingia ndani,Mwalimu Twisana hakuyaamini macho alihisi ni macho ya mtu mwingine wala si yake,alishangaa kumkuta huyo binti akiwa kitandani kwake na chupi tu.Alihisi chumba kinatikisika ,yule mzee akasema "ndo huyu tumemkuta,unasemaje sasa mwalimu hii ndio kazi yenu inavyowatuma mfanye?"
Mwalimu Twisana akasema "kwanza hata siwaelewi mnachokisema,huyu mtoto sijui ameingiaje humu"
Yule MZEE 'Mwenyekiti' akaamrisha akamatwe mwalimu na apelekwe polisi.
Mwalimu Twisana alifunguliwa kesi ya kushiriki ngono na mwanafunzi,hata walipofika mahakamani siku ya kesi yao mwalimu alijaribu kujitetea kwa kila namna ila hakueleweka kwani hata yule binti alitoa ushahidi kuwa amelala mara nyingi tu kwa mwalimu huyo,si walimpanga bwana!!
Hakimu alitoa hukumu ,mwalimu alihukumiwa kwenda jera miaka 30.Maskini!!binadamu wakikuandama huna chako,labda uwe na Mungu ndani yako!,wazazi wa mwalimu Twisana walisikitika sana na hata kijijini kwake walisikitika sana!
Ama kweli dau la mnyonge haliendi joshi,na likienda joshi basi Mungu tu ameamua! Hakika ng'ombe wa maskini hazai!!.Mwallimu Twisana alitegemewa kuwa mkombozi wa familia yake lakini leo hii anajikuta anaenda jera kwa kosa ambalo hakulifanya,upendo wake kwa wanafunzi uligeuka chuki na majanga dhidi yake,alipigania wanafunzi wafanye vizuri lakini akaonekana ni tatizo kwao. Hakuna alichopata kwenye kazi yake hiyo isipokuwa madeni tu mwisho wa mwezi lakini alifanya yote hayo kwa upendo wake kwa wanafunzi ili nao wafanikiwe lakini mwisho wa siku anakuwa kama mshumaa "unatoa mwanga kwa wengine huku wenyewe ukiteketea"

Mwisho.


BOFYA HAPA KWA KUPATA TAARIFA ZAKO ZA KITAMBULISHO CHA NIDA

Post a Comment

0 Comments