Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MAWIO NA MACHWEO - 4





Simulizi : Mawio Na Machweo
Sehemu Ya Nne (4)



“Aaah. Kipindi kile ‘Uncle’ na mtoto wake walikuwa wananilinda sana.Walikuwa wakiniona na mwanaume wanakuwa wakali sana kwangu”.Alijibu Miriam.

“Kwa hiyo sasa hivi hawakufatilii tena?”Nikamuuliza tena wakati huo tulikuwa tunasubiria gari zipite ili na sisi tuvuke na kwenda upande mwingine ambao ndipo madarasa yetu yalipokuwepo.

“Sasa hivi wameondoka na hawatarudi tena huku kwa sababu baba kawaonya sana kuhusu mimi. Kama kampuni wamenifungulia basi waiache niiendeshe mwenyewe na siyo kufuatiliwa”.Alinijibu tena Miriam na kunifanya mimi nibaki kimya kwa sababu nilikuwa najua sababu za mjomba wake kuwa Dodoma.

“Halafu ujue mwenzako siwezi kuvuka barabara”.Miriam alikatisha ukimya uliotanda kwa sekunde chache kwa kuniambia suala linalomsibu.

“Njoo nikubebe ili nikuvushe”.Nilimwambia kiutani, lakini yeye alifanya kweli na kuja hadi pale nilipo na kutaka nimbebe kweli.

“Mimi nilikuwa nakutania bwana,wewe unafanya kweli!!”.Niliongea kwa hamaki.

“Utajua mwenyewe, mimi nataka unibebe hapa”.Alisisitiza nia yake.
Niliangalia magari upande wa kushoto na kulia na baada ya kuridhika, nilimnyanyua Miriam kama vile wanavyonyanyuana maharusi na kuanza kuvuka naye barabara kuelekea katika jengo lenye madarasa yetu ambalo lilikuwa linaonekana vyema wakati tunavuka.

Wapita njia na hata waendesha magari walikuwa wakishangaa tendo linaloendelea kati yangu na Miriam. Wengi walitabasamu na wengine kusimama na kushuhudia furaha iliyotawala katika nyuso zetu. Hakika hata ndege angani walitaharuki na kugongona kwa matendo yale tuliyokuwa tunayafanya.
Ukiacha ndege na viumbe wengine waliokuwa katika taharuki hiyo, nadhani hata jua lilichanua tabasamu na kutuangazia mwanga wa Amani katika mahusiano yetu.

“Jay Zeeeeeeeeee”.Ilisikika sauti moja kutoka juu kabisa ya ghorofa lile tunalosomea. Nilipoangalia ni nani aliyeropoka vile, nilikutana na wanafunzi kibao wakituangalia tunachokifanya kule chini.

Nilimshusha Miriam na baada ya kufika upande wa pili, na kisha tukaanza kutembea huku wote tukiwa tuna furaha sana mioyoni mwetu.

Tulifika pale getini na kuingia na kuanza kuuutafuta mlango wa kuingilia katika jengo lile.
“Masai. Masai… We Masai”.Ilisikika sauti nyuma yangu ikiniita na baada ya kugeuka nilimwona Mzee Soji akinioneshea ishara ya kuniita ili niende pale alipo.

Nilimuomba Miriam anisubiri mara moja, na kisha nilienda pale alipo Mzee Soji.
Hakuongea chochote zaidi ya kunipa kikaratasi na kisha kunipa mgongo na kutokomea eneo lile.

“Alikuwa anasemaje yule mzee?”Aliniuliza Miriam baada ya kurudi pale alipo, wakati huo nilishakifutika kile kikaratasi katika mifuko yangu ya jinzi.

“Juzi alinikopa hela kwa ajili ya chakula ndiyo alikuwa ananilipa”.Nikamdanganya Miriam kwa mara ya kwanza,na alikubaliana na uongo wangu.

Safari ya kulipanda ghorofa lile ikaanza na tuliimaliza salama salmini.

Tulipoingia darasani tulishangiliwa kama maharusi wameingia au wahusika wa sherehe fulani walikuwa wameingia. Wengi walitupongeza huku Chris akiwa mstari wa mbele kama kawaida, na wengine walituhasa sana hasa Solomon na Silvia.

Baada ya pongezi na kuhasana, Miriam alinichukua hadi sehemu ya mbele na kunitaka nikae pembeni yake. Nilikubaliana naye lakini nilimuomba niende uwani kabla hatujaanza kipindi.
Alikubali bila kipingamizi kuhusu ombi hilo.

Nilienda uwani na kukitoa kile kikaratasi na kukisoma. Kilikuwa kimeandikwa maneno machache tu! Yakisema,

“MWANZO MZURI, KARIBU KAZINI”.

Nilishindwa kuelewa maana ya maneno yale na yalinishitua, ila nilijikaza na kutoka uwani huku kikaratasi kile nikiwa nimekichana na kukiacha mle mle.
Nilikaa na Miriam na kuendelea kumsubiri Mkufunzi aje amalizie somo lililobaki.
******

MWAKA WA TATU CHUONI.

Mwaka wa tatu uliingia chuoni huku mapenzi yetu yakiendelea kunawiri kila kukicha. Furaha kati yetu ilikuwa inazidi kupamba moto huku kila mmoja akiwa ana hamu ya kutaka kumjua mwenzake kiundani zaidi. Kiukweli mapenzi yalizidi kipimo,na sasa kila mtu aliyetuona alijua kuwa sisi ni wapenzi.

Hatukuwa nyuma katika masomo. Kila somo lililokuja mbele yetu tuliweza kufaulu vizuri sana. Wakufunzi nao hawakuisha kututaja darasani kama mfano wa kufanya mambo yako katika mpangilio,hasa ukiwa mapenzini huku na wakati huo huo unasoma..

Rafiki zetu wote tuliokuwa nao,kila muda walikuwa karibu yetu huku wakituhasa sana kuhusu maisha. Hata Chris aliyezoea utani, kuna muda alikuwa anaongea mambo kama si yeye, kwa kifupi mahusiano yangu na Miriam, yalibadili watu na kufanya wawe na busara midomoni mwao.

Mara nyingi hasa siku za mapumziko, nilikuwa namchukua Miriam na kwenda naye nyumbani kuwasalimia wazazi na ndugu zangu wengine waliyokuwepo. Kila mtu aliyemuona Miriam alimsifu kwa sababu alikuwa anajiheshimu na kuheshimu wengine japo alikuwa ana hela ambazo kiukweli zilimfanya aonekane maridadi kila siku iendayo kwa MUNGU.

Si wapita njia tu! Hata wazazi wangu walipomuona walisema kuwa yule ndiyo chaguo sahihi katika maisha yangu. Nilifurahi sana hasa pale walipokuwa wananipa baraka zao za mwisho japo nilikuwa bado sijatambulika kwa akina Miriam.

Licha ya kunipa baraka zao za mwisho, wazazi na ndugu zangu walikuwa mstari wa mbele katika kunihasa sana kuhusu maisha ya ujana. Baba yangu ndiye alikuwa chachu tosha ya kila neno kuhusu maisha yetu hasa kwa maneno yake mazuri na ya kuvutia kutoka kinywani mwake.

“Wanangu. Nafurahi sana kuwaona mkiwa mnatabasamu na kutembea pamoja kila kukicha. Siyo siri nafurahi sana. Lakini kuna kitu kimoja nataka kuwauuliza”. Ni Baba yangu ndiyo alikuwa anaongea hayo siku moja tulipomtembelea.

“Sawa Mzee. Wewe uliza tu!”Nilimwambia baba yangu huku nikiwa nimekaa katika kochi moja na Miriam.

“Mmeshawahi kujiuliza maisha ni nini?”Mzee alituuliza swali ambalo kamwe sikuwahi kujiuliza maana maana yake.

Tulikaa kimya huku mimi na Miriam tukiinamisha vichwa vyetu chini kama tunatafuta jibu.

“Najua hamjawahi, mnachojua nyie ni kuwa mnaishi katika maisha hayo,ila hamjui maana yake,si ndiyo mama”.Baba aliongea huku mwishoni akitaka uhakika wa maneno yake kwa Miriam.

“Ndiyo baba”.Miriam naye akajibu huku bado aibu ikiitawala uso wake.

“Kama ndivyo, basi mimi sina cha kuwaongezea hadi hapo zaidi ya kuwaambia kila mmoja kwa wakati wake atafute nini maana ya maisha halafu mkikaa pamoja ulizaneni.

Mimi sitaki majibu yenu kwa sababu najua maana yake,ila nachotaka ni nyie muambiane na muwe na maana moja juu ya maisha”.Baba alikuwa akiongea huku sura yake kaiweka katika hali ya msisitizo ambao kila ambaye angemuona kwa mara ya kwanza,angesema huyu mzee si wa kuchezea hata kidogo.

“Kingine nachotaka niwaambie hapa leo hii ni kuhusu watu.
Kila mtu nadhani anawajua watu.Ila watu hao wamegawanyika katika makundi makuu mawili.

Kuna marafiki na maadui,hayo ndiyo makundi ya watu,japo wengine watasema kuna wanaume na wanawake,au wakubwa na watoto,vyovyote watakavyowaweka wao. Lakini mimi nimeweka watu kutokana na mambo wafanyayo.

Najua watu wengi sana wameshawahasa kuhusu binadamu, lakini mimi leo hii nawahasa nyie katika namna tofauti ya hao wengine.

Heshimuni sana marafiki na wapendeni kila wanao wazunguka, wawe marafiki au maadui kwa sababu hamjui kesho ni nani atakayewazika au kuizika familia yako.

Lakini pia nataka kuwaambia kuwa, nyie mna bahati ya kupata haya nayoongea sasa hivi,kwa sababu wapo ambao walitamani hata kusikia sauti yangu lakini walishindwa kutokana na mapenzi ya MUNGU. Na ndiyo maana nawaambia haya huku nikijitahidi kujiweka mbali na kukandamiza tabaka fulani la kimaisha.

Hakuna mtu asiye na maadui katika maisha haya. Unaweza ukawa unatembea mtaani ukiwa na furaha tele lakini kuna nusu ya wanaokuangalia wana matatizo na wewe. Na vilevile, unaweza ukawa na marafiki zaidi ya milioni lakini wote hao wakawa ni marafiki uchwara tu! Yaani namaanisha, kuna rafiki hawapo kiukweli kama unavyodhani.

Wanangu nawaambieni, marafiki ni “Demo Products”. Demo Products maana yake ni bidhaa kama za majaribio tu, ukiipenda baada ya kuitumia ndiyo unaweza kununua “Full Version” kwa ajili ya kufurahia bidhaa hiyo.

Hapa na maana kwamba.Marafiki wanakuja kwa ajili ya majaribio,kama mkilandana ndiyo wanakuwa wa ukweli kwako. Lakini swali nawaachia nyie.Mtamjuaje rafiki aliyekuja na nia nzuri kwako?.

Kaeni mjiulize na mjipe majibu wenyewe. Mimi naishia hapa japo nina mengi sana ya kuwaambia”.Baba alimaliza kuongea maneno hayo ambayo hayakuwa na tofauti sana na yale aliyowahi kuniambia Mzee Soji,yule mzee mlinzi wa yale madarasa tunayosomea.

“Mzee tutafanyia kazi ushauri wako,na ni vyema umetuambia ili tukae na kujiuliza sana kabla ya kufanya maamuzi yaliyo sahihi. Naamini kila ukisemacho, hasa hapo uliposema kuwa,unaweza kutembea mtaani ukiwa una furaha,kumbe nusu ya wanaokuangalia wana matatizo na wewe.

Maneno hayo hayapingiki hata kidogo. Na mimi kila siku nimekuwa makini kuwasoma watu wa namna hiyo kwa sababu wapo kila mahali.Wanajidai wana furahia sana mahusiano yangu na Miriam na kumbe rohoni mwao kumejaa chuki na visasi ambavyo anakutafutia sababu ili uingie akulipizie.

Huyo ndiye binadam, mwingi wa tabasamu usoni mwake,lakini ni mwingi wa chuki moyoni mwake pia. Na kamwe huwezi kumjua mtu wa hivyo kwa sababu kila mara ndiye akupaye ushauri na kukusaidia uwapo na shida”.Niliongea hayo kama kumsapoti baba ambaye wakati naongea haya yote alikuwa anatikisa kichwa kukubaliana na mimi.

“Nashukuru hata wewe mwanangu umeelewa hayo machache,endelea kutafuta yawe mengi zaidi na kuelimisha wengine”.Baba yangu alikubaliana na mimi kwa nisemayo.

Wakati wote tunaongea hayo,Miriam alikuwa bado kainamisha kichwa chini kama mtu anayetafakari jambo moja muhimu sana. Nilitambua nini anafikiria kwa wakati ule,lakini nilimuacha aendelee kubaki na siri yake hadi pale atakapoamua kuniambia,ila kwa kifupi yale maneno niliyoongea,yaligusa zaidi yanayoendelea katika maisha yake.

“Sawa Mzee. Basi ngoja sisi tukuache na kurudi chuoni kwa maana kuna kazi nyingi sana za kufanya hasa kwa wakati huu ambapo tupo mwaka wa mwisho”.Nilimuomba Baba ruhusa ya kuondoka na yeye wala hakuwa na hiyana kuhusu hilo.

Alituruhusu tuondoke na kitendo bila kuchelewa,tulifuata gari tulilokuja nalo ambalo lilikuwa ni mali ya Miriam. Tulipanda na safari ya kurudi chuoni ikachukua nafasi yake.
________________

Masomo ya mwaka wa tatu yaliendelea vizuri na hatimaye ukafikia ule muda wa sisi kumaliza chuo.

Ilikuwa ni furaha kwa wapenzi kama sisi ambao maisha yetu yangebaki kuwa pale pale Dodoma,lakini ilikuwa huzuni kwa wale tuliyowazoea kwa wao kurudi mikoani wanapotokea.

Mahusiano yangu na Miriam yalikuwa yamekomaa sana,yaani tulikuwa tumezoeana kiasi kwamba kila mmoja alikuwa anamuona mwenzake kama mwili wake.

Licha ya hayo yote ya kuzoena kiasi hicho,bado tulikuwa hatujawahi kushiriki tendo la ndoa. Hiyo ni kwa sababu kila mtu alikuwa bado ajajisikia furaha ya kufanya tendo hilo wakati bado tupo chuo.

Tulikuwa tunapanga mengi sana kuhusu maisha yetu,lakini kamwe hatukuwahi kuanza kufikiria mambo ya ngono tukiwa bado tunasoma.

Najua wengi watashangaa kwa nini tulikuwa hivyo,ila kwa kifupi ni kwamba,ngono inarudisha nyuma sana maendeleo ya wanafunzi hasa pale mwanafunzi anapokuwa anaifikiria ile hali ya raha aliyoipata wakati wa tendo lile.

Mara nyingi akili huama sana na kuwa anafikiria ni jinsi gani atakavyoipata hiyo raha tena. Sababu kama hiyo,inasababisha mtu ashuke kimasomo kwani huwaza ngono zaidi ya masomo. Hiyo ni kwa mtazamo wangu tu!.
**************

Nakumbuka siku hiyo ndiyo tulikuwa tunamaliza mtihani wa mwisho.Mtihani ambao ulikuwa unatutoa katika uanachuo, na kutupeleka katika uraia. Siku hiyo baada ya mtihani ule wa mwisho,kundi letu zima lilikutana na kupanga cha kufanya baada ya maisha ya chuo.

Mawazo mengi sana yalipita,lakini wazo lililokubalika na wengi lilikuwa ni kuwa wajasiriamali,yaani tujiajiri wenyewe,hilo ndilo haswa tulilipitisha.

Baadhi ya wana kundi letu waliondoka.Hivyo kundi likabakiwa na Christopher Jengo au Chris, Solomon na Silvia,Miriam na Mimi,pamoja na Saint Justine Kinala ambaye yeye alikuwa anachukua masomo ya masoko.

Hadi hapo tukawa na watu wengi wa kuanzisha biashara ambayo ingetuingizia kipato cha kutosha katika maisha yetu. Baada ya kupanga hayo yote,ndipo tuliamua kuongeza mtu mmoja ambaye angekuwa muhasibu wetu.

Baada ya kushauriana sana,wazo likapita tumtafute Zaganda Mrwanda ambaye ndiye alikuwa mkali wa masomo ya uhasibu pale chuoni katika miaka yetu mitatu tuliyosoma.
Haikuwa kazi nzito,kwani Zaganda alipopata taarifa hizo,alikubaliana na sisi bila kuweka kipingamizi.

Baada ya hapo,tukapanga tukutane tena baada ya siku tatu kwa ajili ya kuchanga hela ambayo itafanikisha sisi kujiajiri.
*********************

Siku hiyo baada ya kumaliza mitihani kila mtu alikuwa na lake katika kichwa chake.Lakini kwangu mimi nilikuwa nawaza kukusanya kilicho changu na kuvirudisha nyumbani.

Nilikuwa napanga nguo zangu katika ile nyumba tuliyokuwa tumepanga.Muda huo ulikuwa ni kama saa mbili za usiku. Chris yeye alikuwa kaenda kwenye sherehe ya kuwaaga wanafunzi,hivyo pale nyumbani nilibaki peke yangu.

Wakati naendelea kupanga nguo zangu,ndipo nilisikia hodi ikigongwa katika chumba changu,nami wala sikupoteza muda wa kwenda kuufungua mlango ule.

Alikuwa ni Miriam akiwa kapendezea sana kwa mavazi aliyokuwa amevaa usiku ule. Sura yake ng’aavu ilionesha wazi kuwa yeye ni mzuri kupindukia.

“Karibu Mamie wangu”.Nilimkaribisha kwa jina ambalo nilikuwa napenda sana kumuita.
“Asante Dadie”.Na yeye akakaribia kwa kuniita jina ambalo alikuwa analipenda kuniita.
“Mbona hujaenda kwenye sherehe?”.Alianza Miriam kuniuliza baada ya kukaa kitandani.
“Ha ha haaa. Sasa nikasherehekee nini?”.Na mimi niliuliza huku naendelea kupanga nguo zangu.
“Si kumaliza chuo!. Wewe unadhani kumaliza chuo ni jambo la kitoto eeh!. Hapo umeshakwepa mishale kibao hadi kumaliza. Kuna mishale ya ‘sup’, ‘disco’ na mitihani migumu kutoka kwa walimu pamoja na wanafunzi.

Yaani kuna muda ukitaka kuchomoa huo mshale ni lazima utoe hongo kwa mwalimu,na kama sisi wasichana ndiyo tunapata tabu sana. Saa nyingine wanachuo wenzako wanakutaka kimapenzi na saa nyingine hata walimu.

Sasa leo ndio namaliza makashi kashi yote haya,kwa nini nisisherehekee?”.Miriam alijaribu kujieleza nia ya kusherehekea kumaliza lakini kwangu ilikuwa kama anampigia mbuzi gitaa,kwani nilikuwa najua kujieleza kuliko alivyodhani.

“Ujue Miriam, wewe unadhani tayari umemaliza kashikashi lakini kumbe ndiyo unaingia rasmi kwenye kashikashi. Yaani hapa tulipotoka ni kianzio tu cha kashikashi,bado kashikashi lenyewe linatungoja huko tuendapo.

Mimi leo nikisherehekea kumaliza,ni sawa sawa nasherehekea kuvuka mto uliojaa mamba wakati unaenda kuingia katika pori lenye kila aina ya wanyama wakali”.Nilizidi kuongea huku kasi yangu kupanga nguo ikiendelea kukua.
“Mh! Hapo una maana gani unaposema unasherehekea kuvuka mto uliojaa mamba wakati unaenda kuingia katika pori lenye kila aina ya wanyama wakali?
Hapo umeniacha dadie”.Niliacha kupanga nguo na kwenda kukaa karibu na Miriam ili nimfafanulie kauli yangu.

“Miriam. Huu ndiyo mwanzo wa maisha yetu.Maisha ambayo kila siku najiuliza nini maana yake,lakini sipati jibu.
Masomo ni kama mto ulijaa mamba,ambapo muda wowote wanaweza kukumeza na kukupoteza bila kwenda mbele.

Namaanisha masomo ndiyo mamba. Ukifeli,basi na maisha yako yataenda usivyotegemea japo wengine wanasema kufeli mtihani siyo kufeli maisha.
Nakubaliana na huo usemi,lakini mara nyingi ni msemo wa wale waliofeli,au wale wanaowapa moyo waliofeli.

Maisha yetu yamejaa maisha ya bora liende na siyo maisha yanayotegemea malengo. Naposema malengo namaanisha wewe unataka kuwa nani mbeleni. Sisi hatuna hilo,tulichonacho ni bora nipate kazi,lakini kwa watu wenye malengo,wanajua wazi kuwa ukifeli mitihani,basi ushafeli na maisha.

Sasa hapa tumeshavuka mto wenye mamba,na tunaingia katika pori lenye kila aina ya wanyama wakali. Pori hilo ndilo linaitwa maisha,siyo maisha ya chuoni tena bali ni maisha ya kidunia.

Maisha yaliyojaa kila aina ya mambo ndani yake. Humo kuna watu na binadamu,wanyama na nyama,maisha na waishio,na kizuri zaidi huko utafundishwa hadi jinsi ya kuwa kama wao.
Yaani kama wao ni wanyama,basi na wewe utakuwa mnyama,ukikataa utakuwa nyama”.Nilimaliza kumfafanulia Miriam na kisha nikanyanyuka pale kitandani na kuendelea kupanga nguo huku nikimuacha Miriam akiwa hajui cha kusema zaidi ya kubaki mdomo wazi.

“Ujue hadi sasa hivi bado nayafikiria haya maneno uliyoniambia. Nahisi kama umenigusa mimi vile”.Miriam aliongea baada ya ukimya uliotanda kidogo baina yetu.
“Umesahau kuwa mimi ni msanii. Tena siyo msanii gegu ila mwenye meno ya kuweza kumng’ata yeyote kihisia na kifikra”.
“Ama kweli wewe ni msanii.Nimekukubali Dadie wangu”.
“Usijali mamie wangu. Ila kwani haya niliyokwambia yana kukugusa kivipi?”.Bado nilikuwa naaongea na Miriam huku napanga nguo zangu.

“Mh! Nashindwa hata kuelezea. Ujue hata siku ile kwenu,uliongea maneno ambayo hadi leo yananifanya nijisikie kama na makosa sana kukuficha”.Miriam alizidi kuingia katika maongezi ambayo nilikuwa natayaka sana kuyahakikisha kama ni kweli au uongo.

“Ndiyo muda wa kuwa muwazi huu mamie wangu. We ongea tu”.Nilimvuta,lakini safari hii niliacha kupanga zile nguo na kwenda kukaa pembeni yake kwa ajili ya kumsihi aniambie kinachomsibu.

“Hawa marafiki si watu wazuri kabisa nakwambia. Najua huwezi kuamini kirahisi ila yakupasa kuniamini kwa sasa”.Aliongea Miriam kwa upole na kwa kusisitiza kauli yake.
“Kwa nini nisikuamini mamie wangu?.Kuwa huru. Hakuna mtu ninayemuamini kwa sasa kama wewe”.Nilimpa moyo ili aendelee kuongea alichokusudia.

“Rafiki yako Chris, Frank. Chris mara ya kwanza aliwahi kunitaka ila nilimkataa. Baada ya kumkataa akawa ananing’ang’aniza sana tena sana. Sasa kuna wale rafiki zangu wawili,huwa wanapeleka taarifa kwa mjomba wangu ili watu kama Chris wapewe onyo.

Baada ya zile taarifa,Chris alitafutwa na kupewa onyo hilo,ila kwa kiburi chake alikaidi lile onyo na kuzidi kunitongoza tu.

Mara ya mwisho,nilikuwa naye pale kwenye ule mgahawa na bado alikuwa ananitaka. Kumbe yale yote yalikuwa yanaonekana.

Ghafla mtoto wa mjomba,yule Yuri.Akanipigia simu na kuniambia huyo Chris watamuua kama nikiendelea kukaa naye pale. Niliposikia hayo nilinyanyuka na kuondoka kabisa eneo lile.

Balaa nilipofika nyumbani sasa. Mipango yote ilikuwa ni kumuua Chris na zaidi niligundua hata baadhi ya wanachuo waliowahi kunitaka kimapenzi,waliuawa kikatiri. Kama una kumbuka wale wanachuo watatu waliokufa kwa kutolewa maumbile yao,sababu kubwa ilikuwa ni mimi”.Miriam alizidi kunihakikishia maneno ya Mzee Soji kuwa yalikuwa ni ya kweli.
Nilikaa kitako kwa ajili ya kuendelea kumsikiliza japokuwa alikuwa ana huzuni sana.

“Baada ya kusikia Chris anataka kuuawa,ikanibidi mimi nifanye kazi ya ziada kunusuru hali hiyo. Nilichofanya ni kumpigia baba simu ili awaonye ndugu zake kwa tabia ambazo wanataka kuzianzisha. Sikumwambia ni tabia zipi,ila niliahidi wakiendelea nitazisema. Hapo ndiyo ikawa pona ya Chris”.Miriam alipofika hapo alikaa kimya jambo lililonifanya nishindwe kuelewa kamaliza au anaendelea. Sababu ya kuwaza hayo, ni kwa kuwa hakumaliza sababu za msingi kabisa za watu kuawa kwa ajili yake.
“Sasa kwa nini walikuwa wanataka kumuua Chris?Ina maana hawataki wewe uwe na mahusiano na mtu?”.Nilimuuliza kimtego ili nipate uhakika kama kweli mtoto wa mjomba wake alikuwa anataka amuoe.
“We acha tu! Frank. Yule Yuri ananilazimisha eti anioe. Kweli kabisa anataka anioe wakati yeye ni kama kaka yangu. Sababu hiyo ndiyo inafanya aue yeyote atakayeonekana ana nia ya kunitaka kimapenzi.Yaani hadi anaondoka hapa Dodoma,anaapa kuwa lazima atanioa”.Nilishusha pumzi ndefu baada ya maneno hayo na nikakosa cha kusema zaidi ya kukaa kimya huku nikifikiria maisha yangu ya mbele zaidi.


“Hata hapo uliposema tunavuka mto wenye mamba na kuingia pori lenye wanyama wakali na wa kila aina.Umenifanya nifikirie mengi sana kuhusu mahusiano yetu. Yaani naona kama naenda kukuingiza matatizoni,lakini nitafanya nini na maji nishayavulia nguo?”.Miriam alionesha wasi wasi wake.
“Usijali hata kidogo. Mimi ni mtoto wa kiume,na nimezaliwa kupigania nachokihitaji. Kamwe sitajaribu kuukufuru uhusiano wetu kwa kusema kwa nini nimekutana na wewe. Wewe ndiye mke wangu,na nitapigana daima kukulinda na kulilinda penzi letu. Ukiruka nami Nitaruka,unakumbuka haya niliyasema lini?”.Nilimpa moyo Miriam japo moyoni mwangu uoga ulinijaa pia.

“Nayakumbuka hayo maneno,na nitafurahi sana kama utakuwa hivyo daima. Nakupenda sana Frank,nakupenda mno Masai”.Aliongea Miriam,safari hii alimaliza kauli yake huku anakilaza kichwa chake kifuani kwangu.
“Nakupenda pia Miriam,na nitakupenda hadi mwisho wa uhai wetu”.Na mimi niliitikia huku nikizilaza nywele zake kwa nyuma.
Kimya kikatanda baina yetu huku kila mmoja akiwa anawaza lake.

“Leo rafiki yako atarudi?”.Hatimaye Miriam akaukata ule ukimya kwa swali hilo.
“Hapa ndiyo kwake,ni lazima arudi,kwani vipi?”.Nikamjibu na kumuuliza.
“Nataka nilale na wewe hadi asubuhi”.Akajibu.
“Ok. Ngoja nimtumie ujumbe kuwa asije”. Nilimwambia Miriam na kisha nikachukua simu yangu na kuanza kuandika ujumbe ambao ulipokelewa na Chris vizuri,na baada ya dakika chache,ulijibiwa kwa kukubali kutorudi.

“Haya mama yangu,waweza kuwa huru sasa kulala”.Nilimwambia na kuendelea na shughuli yangu ya kupanga nguo,ikapata muendelezo zaidi.
Miriam alinyanyuka pale kitandani alipokaa na kuja kunisaidia kukunja nguo zile ambazo tayari zilikuwa zimebakia chache sana.

Tuliendelea kupanga huku tunapiga hadithi tofauti tofauti hadi nguo zile zikaisha.
“Asante sana Miriam. Nilikuwa nafikiria nitazimaliza saa ngapi.

Kweli kidole kimoja hakivunji chawa”.Nilikuwa naongea huku namuangalia Miriam aliyekuwa anatabasamu mwanana usoni pake.
“Na wewe kwa kujidai m’babu na vimisemo vyako hivyo,shauri yako. Nitakuacha kwa sababu unajizeesha”.Alizidi kuupamba uso wake wakati anaongea haya kwa tabasamu lile lile.
“Na mimi nakuacha kwa sababu hupendi maneno ya Wahenga”.Nilimwambia Miriam huku namfata pale alipo na kumsukuma na bega langu kidogo,jambo lililofanya anipige ngumi ya mgongo.
“Ngumi ya mpenzi haiumi”.Nilimjibu huku nikiupeleka uso wangu kama namzomea.
“Mmmmwaaah”.Akanibusu kwenye midomo yangu.
“Busu la mpenzi ni tamu”.Nikazidi kuongea vimaneno vya ajabu ajabu.

Safari hii hakuongea neno zaidi ya kunirukia na kuutafuta ulipo mdomo wangu,kisha akaingiza ulimi wake kinywani mwangu na kuanza kufanya kile kitendo cha kunyonyana.

Na bila kusita,kila mmoja wetu alijikuta akifurahia ile hali ambayo ilitupeleka mbali zaidi na kujikuta tupo kama tulivyozaliwa pale kitandani huku ni lugha moja tu! Ndiyo ikitawala wakati huo,lugha ya mapenzi.
****************

Ni baada ya saa ndiyo kila mmoja wetu alikuwa ameridhika na kukubaliana na matokeo ya kuwa mwenzake ni mkali.Ila sifa kubwa ilikuja kwangu kwa sababu ndiye nilikuwa mvulana wa kwanza kuingia katika mwili wa Miriam.

“Dadie.Naomba uitunze heshima niliyokupa. Nimekuthamini sana hadi nikaamua kukupa mwili wangu,naomba malipo yake yawe ni wewe kuniahidi kuwa hutonisaliti wala kufanya kinyume na mapenzi yetu. Nakupenda Frank,nakupenda sana”.Aliongea Miriam huku akichezea chezea kifua changu.
“Sikudhani kama unaweza kuwa hivi Miriam. Nakuahidi,sitofanya chochote kinyume na utakayo. Wewe ndiye mke wangu,na wewe ndiye mama watoto wangu. Nakupenda mamie wangu”.Nilimjibu Miriam na baada ya hapo kila mmoja wetu akaanza kuusaka usingizi.

Kila mtu alikuwa anayasikia mapigo ya moyo ya mwenzake kwa usiku ule. Kumbate tulilokumbatiana,ni kumbate ambalo sidhani kama watu waliyokuwa hawajafunga ndoa wanaweza kukumbatiana vile.

“Dadie. Kabla hatujalala naomba nikuulize swali”.Miriam alianzisha maongezi baada ya kimya kirefu kidogo.
“Uliza tu mamie wangu”.Nikampa ruhusa.
“Hivi yale maneno ya baba siku ile uliyafanyia kazi?”.
“Yapi hayo mamie”.
“Yale ya kutafuta ni nini maana ya maisha”.
“Mh! Kiukweli hadi leo bado najiuliza lakini sipati jibu sahihi”.
“Kwani wewe jibu lako linasemaje kuhusu maana ya maisha?”.
“Mh! Hapo ngumu kuelezea. Kwani wewe umepata maana yake?”.
“Nilijitahidi kutafuta,ila mwisho wa siku,nilipata jibu moja tu!.Ambalo sijui kama ni kweli au la!”.
“Embu na mimi nishirikishe ili tuchanganye mawazo yetu na kupata jibu moja”.
“Ila usinicheke,maana wewe navyokujua”.Miriam akatoa onyo kabla hajasema jibu lake.
“Siwezi kukucheka katika kitu siriazi kama hiki”.Nikamtoa wasi wasi.
“Maisha ni kama MAWIO NA MACHWEO ,yaani kuchomoza na kuzama kwa jua”.Miriam aliongea kidogo na kisha alinisikiliza mimi nitasemaje.

“Ni kama MAWIO NA MACHWEO au ni MAWIO NA MACHWEO”.Nikamuuliza.
“Vyovyote utavyotafsiri,ila mimi nimefananisha maisha na MAWIO NA MACHWEO”.
“MAWIO NA MACHWEO!!?”.Nilijikuta nanong’ona maneno hayo peke yangu.

“Mbona unanong’ona tu!?”.Miriam aliniuliza kwa upole huku akiendelea kushika shika kifua changu.
“Umeniacha mbali sana kwa maneno yako,nashindwa kuelewa maana yako”.
“Ngoja nikuambie”.Miriam alinyanyuka pale kitandani na kukaa kitako.Kisha akaendelea.

“Maisha ya mwanadam huanza pale alipozaliwa.Baada ya kuzaliwa hufuata furaha kubwa kwa malezi ya wazazi wake na mazingira yanayomzunguka. Kwa kifupi pale unapozaliwa,unakuwa hujui shida wala matatizo.

Lakini maisha huanza kubadilika baada ya yule aliyezaliwa kujitambua. Hapo ndipo maisha yanaanza kumchapa na kumchakaza na mwisho wa hayo yote,ni yeye kupumzika eidha kwa kufa au kupata faraja.

Hapa namaanisha kwamba,pale jua linapochomoza ni sawa na binadam anapozaliwa. Lakini pale maisha yanapoanza kumchapa,muda ule naufananisha na mida ya saa sita hadi saa kumi.
Muda huo ndiyo ambao watu wengi husababisha waichukie asubuhi.

Mtu hachukii asubuhi kwa sababu ni asubuhi,bali huichukia asubuhi kwa sababu ya karaha za saa sita hadi saa kumi. Katika muda huo,utakutana na njaa,kiu,unyanyasaji kutoka kwa watu unaotafuta kupitia wao, pamoja na jua ambalo huwa kama limesogezwa karibu na uso wa dunia.

Faraja ya watu hawa huja baada ya kuona jua linazama.Muda huo wengi huvuta pumzi ndefu na ya furaha kama wamefanikiwa. Na wengine huvuta pumzi ndefu,na baada ya pumzi hiyo, huwa hawezi tena kuvuta pumzi nyingine.

Hayo ndiyo maisha,yana kuzaliwa na kufa kama lilivyo jua,lina mawio na machweo. Lakini kabla hujafa,pale katikati lazima upite katika mapito fulani,sawa na jua. Kabla halijazama lazima lipitie mchana”.Nilikuwa kimya sana hadi Miriam anamaliza maneno haya,na niliendelea kukaa kimya huku nikiyatafakari maneno yale kwa kina zaidi.

“Vipi Dadie,umelala nini.Isije ikawa nilikuwa naongea peke yangu tu hapa”.Miriam alivunja ukimya kwa maneno hayo huku akienda kuwasha taa ili ahakikishe kama nilikuwa macho au nimelala.
“Nitawezaje kulala na maneno makali kama haya?Na sijui umeyatoa wapi”.Nilimtoa wasiwasi baada ya kuiwasha ile taa.

“Ahaa.Mimi nilidhani umelala,ningekuchapa”.
“Haya maneno umeyatoa wapi Miriam?”.
“Ha ha haaa.We hujui kuwa ukikaa karibu na waridi na wewe utanukia?”.
“Ha ha haaa. Na wewe unaanza kujidai mhenga. Jizeeshe tu!”.
“Wewe ndiyo umenifundisha tabia hiyo”.
“Haya bwana,ila maneno yako yamenigusa sana. Na sina cha kukataa hadi hapo.Umenifungua akili sana.Sasa hivi mtu akiniuliza maisha ni nini,namwambia ni MAWIO NA MACHWEO”.

“Ha ha haaa. Na wakikuuliza kivipi,utawajibuje?”.Aliniuliza Miriam.
“Siyo lazima uzaliwe na ufe ndiyo iwe MAWIO NA MACHWEO. Ila hata katika mapenzi,kuna MAWIO NA MACHWEO.

Kuna ule muda ambao mnakuwa na furaha sana,hapo ni sawa na mawio ila kuna muda utakuja kujiuliza kwa nini umeingia penzini.

Kuna muda mapenzi huwa machungu sana tena sana. Muda huo ndiyo kama mchana. Ila baada ya machungu hayo ni lazima usahau na kumpumzika au kwa kupata faraja mpya,hayo ndiyo machweo.

Vilevile katika maisha yetu,kuna kitu kama hicho. Hapa tulipo bado tupo kwenye mawio,sasa tunaelekea kwenda kuanza maisha yetu binafsi,huo ndiyo muda wa mchana.

Huko ndipo kuna karaha za maisha,sijui ni nini machweo yake,ila tumuombe MUNGU atujaalie mazuri”.Nilimwambia Miriam ambaye alikuwa kimya akisikiliza nachoongea.

“Mh! Haya bwana. Ngoja nikazime taa tulale,maana ukianza kuongea hapa haumalizi,japo kila neno kutoka kwako ni elimu”.Miriam alinyanyuka pale kitandani na kwenda kuzima taa.
“Ila wewe mzuri sana mamie wangu”.Nilimwambia baada ya kuona umbo lake wakati anaenda kuzima taa.
“Sitaki uchokozi wako hapa,nitakubatua”.Miriam alipiga mkwara wakati anapanda kitandani.
“Yaishe. Tulale sasa”.
“Usiku mwema Dadie”.
“Usiku mwema Mamie”.
“Ha ha haaa. Hilo jina nalipenda sana Dadie”.
“Usijali. Hilo ndo jina lako daima”.
“Asante Dadie”.
“Asante Mamie”.Tulianza viutani vingine ambavyo mwisho wake ulikuwa ni kubebwa na usingizi.
****************

Kesho yake kila mtu aliamka akiwa na uchovu wake mwilini. Mimi na Miriam tukiwa na uchovu wetu binafsi wa shughuli moja nzito iliyopita usiku wa jana,na wengine kama Chris walikuwa na uchovu wa kukesha wakicheza mziki ukumbini.
Nilionana na Chris lakini sikumwonesha kama najua chochote kuhusu matendo aliyofanya nyuma,hasa ukizingatia alishanidanganya kuwa hakumtaka Miriam. Kwa kifupi niliyafanya yale yapite kwa kuwa Chris alionekana kubadilika na kutokuwa msumbufu tena kwa Miriam.

Lakini endapo ningejua kuwa wivu unapatikana katika moyo wa mtu hasa anapoona wewe umefanikiwa na yeye hajafanikiwa,ningesipompa ruhusa Chris aendelee kuwa rafiki yangu.

“Ee bwana Jay,jana umekosa bonge la uhondo”.Chris alianzisha maongezi ya jana yake baada ya kusalimiana. Wakati huo tulikuwa tupo chuo,mimi nikiwa na Miriam na Chris alikuwepo na Saint pamoja Zaganda ambaye alikuwa tayari rafiki yetu.
“Uhondo gani sasa?”.Nilimuuliza Chris.
“Ohooo. Jana mwenzako hapa kafunika hatari,halafu akaanza kujigamba kuwa hakuna kama yeye pale chuoni.Acha watu wapagawe kwa kelele”.Chris aliongea huku akimwoneshea Zaganda kidole kuwa ndiye aliyasema yale.
“Embu elezea vizuri bwana. Kafunika nini na watu walipagawa na kelele zipi?”.Nilimuuliza Chris,wakati huo Miriam alikuwa amenilalia kwenye bega langu la kulia.
“Nakwambiaje. Jana jamaa alikuwa anavunja hatari,halafu alipomaliza kuvunja akaanza kuchana. Ilikuwa ni noma. Sasa baada ya kumaliza michano,akaanza kujigamba kuwa yeye ndiye bora pale chuoni. Basi makelele yote ya kumsifia yeye yakahamia kwako. Ukumbi mzima ukawa jina la Jay Z”.Chris alizidi kuongea wakati huo Saint na Zaganda walikuwa wanatabasamu bila kuongea chochote.
“Eti ya kweli hayo Ndanda”.Nilimuuliza Zaganda ambaye alikuwa anapenda kujiita Ndanda kutokana na herufi zake tatu za mwisho kutoka katika majina yake,Zaganda Mrwanda.
“Ha ha haaa. Kiukweli siku ile ulinibahatisha tu! Huniwezi Jay,yaani huingii hapa hata kidogo”.Zaganda aliongea huku akiweka tambo zake.
“Ha ha ha haaa. Kweli wewe zimeanza kukutoka. Unasema siku ile nilikubahatisha wakati we mwenyewe ulisema basi?Hapo kaka unanizingua,yaani mmeamua kunizingua kabisa”.Nilimwambia Zaganda.
“Kumbe ndiyo maana jana ulikuwa hutaki kwenda eeh. Ukaanza kunipa visababu na vimaneno vizuri ili tusiende. Kumbe unamuogopa Ndanda!!”.Miriam naye alidakia huku akikitoa kichwa chake begani kwangu.
“Ehee,leo Jay kapatikana. Kumbe alikataa kuja eeh”.Chris naye akachombeza.
“Alikataa katakata. Yaani mimi nilikuwa na hamu ya kuja kuagana na rafiki zangu,lakini huyu akaanza vimisemo vyake”.Nikaanza kutupiwa lawama hata na Miriam. Ilinibidi niwe natabasamu tu!.
“Ona sasa.Kumbe hadi Shem alikuwa anataka aje aone jinsi navyokuadhibu,ukamkataza”.Zaganda naye hakuwa nyuma.
“Sasa kwani tuliagana kuwa kutakuwa na mpambano? Mbona mnaanza kunirusha wazee”.Niliwaambia huku sasa nikianza kama kuumia kutokana na laumu nazotupiwa.
“Hata kama.Mimi mbona nilikuwa nataka kwenda lakini ukaanza kuniambia maneno yako ili tusiende.Ulikuwa una maana gani”.Miriam naye alikuwa kama kasahau maneno tuliyoongea jana usiku na umuhimu wake.
“Kwa hiyo hata yale niliongea na wewe yote yalikuwa ya kipuuzi si ndiyo eeh”.Ilibidi niwe mkali kiasi kwa Miriam. Na baada ya kuona kama nakuwa na hasira alikuwa mpole na kuendelea kuwa msikilizaji.
“Kwanza uliona jinsi nilivyomchakaza Ndanda siku ile au ndiyo umeamua kunipa lawama tu leo”.Nilizidi kumuandama Miriam.
“Niliona ndiyo. Ila sasa hivi atakufunika kwa sababu huna mazoezi na sasa hivi umekuwa kifutu,huwezi kucheza kama siku ile”.Aliongea Miriam huku akiendelea kuivutia ngozi kwa Zaganda.
“Kwa hiyo na wewe upo kwa Ndanda?”.Nikamuuliza Miriam.
“Ukitaka niwe kwako,kubali kupambana naye kesho kutwa”.Aliongea Miriam na kuniacha kinywa wazi.
“Hapo ndipo nilikuwa napasubiri mimi. Kwa kuwa kila mtu anasema yupo juu ya mwenzake basi tuweke mpambano baina yenu ili tuhakikishe nani ni nani,na tuondoe huu utata”.Saint ambaye muda wote alikuwa kimya,alifungua kinywa chake.
“Mimi huyu hata sasa hivi tuite mziki,nitamshinda. Haniwezi hata kidogo. Na kama ulidhani sina mazoezi hilo umebugi mama,mimi na kipaji toka mwilini. Na kufanya yale ni kama baiskeli tu! Ukijua umejua,hata ukae miaka hujaiendesha.siku ukiamua kuiendesha hakudondoshi”.Na mimi nikaanza majigambo.
“Eti hata sasa hivi. Anapenda kuonea huyu. Siku ile kwanza Ndanda alikuwa kishachoka. Kapambana na watu karibu sita,wewe ndiyo ukaenda na kujidai umemfunika. Na leo unataka kufanya hivyo hivyo,mwenzako jana kachoka,halafu unataka mpambano leo. Hilo hamna Dadie”.Miriam alizidi kunitoa nishai.
“Ha ha haaa. Kumbe Shem unajua eeh,huyu alinishinda kwa kuwa nilikuwa nimechoka tu! Sasa nipo gado,kesho kutwa mpambano,unakubali Jay?”.Zaganda akaongea.
“Kwa kuwa una kiburi,nitakuonesha hiyo keshokutwa”.Nikamjibu Zaganda na hapo hapo likatoka shangwe la kufa mtu kutoka kwa Chris na Saint.
Watu wote waliyokuwepo mahala pale walikuja na kutaka kujua nini kinaendelea. Waliposikia kuna mpambano kati yangu na Zaganda,nao walijiunga na kushangilia.
“Vipi nyie?Leo mmewehuka au!!?”.Ilikuwa ni sauti ya Silvia akitushangaa jinsi tulivyokuwa tunapiga kelele.
“Hee,hata Malkia wa Masai na yeye yumo?Makubwa”.Hapo aliongea Solomon mchumba wa Silvia.
“Embu tuambieni kuna nini hadi na mtoto mzuri kama huyu awafate nyie walevi”.Aliongea Silvia huku anavuta kiti na kukaa karibu na mpenzi wake.Wakati huo watu waliokuwa wametuzunguka walishaondoka eneo lile.
“Kuna mpambano keshokutwa kati ya Ndanda na Jay. Wanaenda kushindana kuchana na kucheza”.Aliwajibu Chris.
“Ahaaa. Sasa hilo ndilo la msingi katika kujitengenezea hela kwa ajili ya kuanzisha biashara yetu. Hapo mmefanya jambo la msingi sana tena sana”.Solomon alisema hayo lakini hakuna aliyemuelewa kati yetu ana maana gani.
“Sasa kaka mbona umetuacha soremba na kauli yako?”.Ilibidi Chris aulize na sisi wengine tukakaa kitako kwa ajili ya kumsikiliza Solomon.
“Kanuni mojawapo ya kuwa mjasiriamali ni kuwa mbunifu,si ndiyo eeh”.Wote tukajibu ndiyo.Solomon akaendelea.
“Sasa kama ni hivyo,basi na mimi nimebuni njia ya kujipatia kipato halafu tukichanganya na hizi hela tutakazochanga,tunaweza tukaanzisha biashara kubwa sana.
Mimi nilichofikiria na nimeona kitafaa sana,ni kulifanya hilo shindano liwe na kiingilio ambacho tutatangaza na nia yetu ya kuweka hicho kiingilio. Na kama watu wataafiki mawazo yetu,basi itakuwa rahisi sana kwetu kupata hela ambazo zitasaidia katika uanzishaji wa biashara yetu.Au nyie mnasemaje?”.Solomon alitoa wazo ambalo kati yetu hakuna aliyelifikiria.
“Dah! Sikuwa nimefikiria hilo kaka. Yaani hadi hapo,wewe ni bonge la mjasiriamali kaka. Sasa hapa cha msingi ni kwenda kuongea na uongozi wa chuo halafu tuombe watusaidie kupata ukumbi ambao huo ndiyo tutafanyia kila kitu”.Na mimi niliongezea mawazo.
“Kuhusu ukumbi wala msijali. Mimi nitafanya mpango nichukue ukumbi mmoja wa mjomba ili tufanyie hiyo shughuli”.Miriam naye alikuja na wazo jingine zuri zaidi.
“Hapo sawa. Sasa kilichobaki ni kuwapa taarifa wanachuo ili siku hiyo watokee kwa wingi. Tutafuta watu maalum watakao kaa mlangoni na vilevile mimi kama mimi,nitakuja na baadhi ya rafiki zangu ambao huwa tunacheza na kuimba wote mtaani,hiyo tusiitangaze bali iwe kama sapraizi”.Nilizidi kutoa ushirikiano katika maongezi yale.
“Na kama vipi huu usiwe mpambano bali uwe ni burudani tu! Yeyote mwenye kipaji anaweza akaja na kukionesha,au nyie mnasemaje?”.Zaganda aliongea.
“Ha ha haaaa.Kaniogopa tayari”.Niliongea huku natabasamu baada ya kusikia maneno yale ya Zaganda.
“Ha ha haaa. Mimi nakukubali Jay,wewe ni mkali. Sisi tulikuwa tunakuvuta tu! Ili ukubali kushindana na tuburudike pamoja kwa mara ya mwisho. Hiyo ndiyo ilikuwa nia yetu”.Zaganda alizidi kumwaga ukweli.
“Kwa hiyo si kweli yote mliyoongea?”.Niliuliza.
“Ndiyo maana yake. Hiyo ilikuwa ni kukuvuta tu!”.Zaganda alijibu.
“Sasa na Miriam imekuwaje?”.Niliuliza huku namgeukia Miriam.
“Huyo tulishamset.Ila usijali kaka,mambo yatakuwa sawa keshokutwa”.Zaganda alimaliza huku akiniacha sijui cha kufanya.
“Poa bwana.Ila mlichofanya sijakifurahia”.Nilionesha hisia zangu.
“Samahani Dadie. Halafu na mimi nitakuwa na sapraizi hiyo keshokutwa”.Miriam aliomba msamaha.
Tulizidi kuongea mengi tukiwa pale hadi tukaridhika ambapo mwisho wake kila mtu alikubali kuwa kila kitu kitafanyika keshokutwa yake.Yaani kutoa jina la biashara yetu pamoja na mchango wa hela ambazo zitatusaidia kuanzisha biashara hiyo.
**************

Nakumbuka ilikuwa ni Jumatano ya wiki ambayo ndiyo wiki ya kwanza kuikata tangu tumalize mitihani.
Siku hiyo ndiyo siku ambayo tulipanga tufanye onesho ambalo lilikuwa kwa ajili ya kuwaaga wanafunzi wenzetu pamoja na kuitambulisha biashara tutakayoianzisha.Ni onesho ambalo lilikuwa katika lengo kuu la kujipatia kipato kwa ajili ya kuanzisha biashara hiyo.
Lilikuwa ni onesho kubwa kupata kutokea kwa pale Dodoma. Yaani tokea Dodoma ianze,kulikuwa hakujawahi kuandaliwa onesho kubwa na wanafunzi kama lile. Na hiyo ni kwa sababu wanachuo pamoja na watu wangu wa mtaani kuitikia wito wangu na wa wenzangu pia.
Kazi kubwa tuliyoifanya ni kulitangaza onesho lile kwa vipeperushi mbalimbali ambavyo vilitapakaa kila mahali pale chuoni na hata nyumbani kwetu. Kwa yeyote aliyeona waandaaji wa onesho lile hakusita kupania kuja kuangalia.
Heshima tuliyojijengea pale chuoni na hata nyumbani kwetu,ilikuwa ndiyo chachu kubwa ya kuwavuta watu kuja pale.Misaada tuliyokuwa tunaitoa katika masomo kwa wanachuo wenzetu ndiyo ilikuwa kama shukrani ya wao kuja kwenye onesho lile.

Saa mbili za usiku,onesho lilianza rasmi huku vijana wengi wakipanda jukwaani na kuonesha vipaji vyao ambavyo vilikuwa havipewi fursa ya kuonekana pale chuoni kutokana na sababu mbalimbali za chuo kile.
Kila mmoja alijipanga kivyake ilimradi kila nafsi iliyohudhuria imfahamu na iridhike na anachofanya. Kiukweli onesho lilipambwa na wao kwa sababu walikuwa wengi na kila aliyekamata jukwaa,basi alifanya kweli.Ilikuwa ni burudani tosha. Si kwa hadhira wala kwa hadhara,wote kwa pamoja waliburudika.

Muda ukaenda ,ukaja na kutitia. Hatimaye ule muda wa wahusika wakuu kupanda jukwaani ukawadia. Wakati huo ilishatimia saa tano za usiku.
Mshehereshaji au MC kama tunavyopenda kumuita alikuwa ni mchekeshaji maarufu pale chuoni. Hivyo ikawa ni raha sana kwa wapenda vichekesho pia.
Ilianza kama utani pale sura za mtaani zilipoanza kutokea jukwaani huku wengine wakirap na wengine kuimba. Wengi wa wanachuo walikuwa wanashangaa uwepo wa sura zile ngeni pale jukwaani. Lakini wale waalikwa wangu wa mtaani,wala hawakuona ajabu zaidi ya kushangilia kila msanii aliyekuwa akipanda jukwaani.
Walipanda jukwaani vijana tisa huku kila mmoja akiimba wimbo wake na mtu wa kumi kumaliza kupanda katika lile kundi alikuwa ni mimi. Niliingia kwa wimbo wangu uitwao SAUTI ZA MTAANI ambao ulikuwa unaelezea matatizo mbalimbali yanayowakumba vijana mtaani.
Baada ya kumaliza kuimba wimbo ule,nilimuomba DJ akate kwanza mziki kwa ajili ya kufanya utambulisho wa watu wale.

“Najua mtakuwa mnashangaa na kujiuliza ni nini hiki mkionacho.Lakini kila kitu kimepangwa. Na kama mlivyosoma kwenye vipeperushi vyetu kuwa kutakuwa na sapraizi za kutosha,basi hii ni mojawapo.
Hili ndilo kundi linalonilea nikiwa mtaani. Ni kundi linalofanya mziki wa kila aina. Na siyo mziki tu! Vile vile kundi hili ndilo bingwa wa kucheza hapa Dodoma,naamini hilo japo hatujashindana na yeyote.

Kundi lina wasanii wengi sana,lakini hawa nimewachota baadhi yao. Na hapa wote kwa ujumla tunaitwa Republic Of Black People au Republic of watu weusi,tunatoka Kikuyu. Na huyu hapa anaitwa…..”.Nikaanza kuwatambulisha wanakikundi kile mmoja mmoja hadi likaisha na baadae burudani ikaendelea kwa kila mwanakundi kuimba wimbo wake mwingine.

Burudani ilizidi kikomo pale tulipoanza kuimba nyimbo za kundi huku tunacheza katika mpangilio uliyokaa vizuri na wa kumvutia kila mmoja mle ukumbini. Hapo kila mtu aliwehuka hasa kwa ule mtindo wetu wa kucheza.
Mwisho wa burudani ile ya kundi ilikuwa ni saa saba na nusu za usiku. Na kwa ujumla kila mmoja alifurahia ile burudani,ila shangwe halikuishia hapo.
Liliendelea pale Zaganda alipopanda kwa fujo huku akirap kwa sauti ya hamasisho na inayoeleweka. Alikuwa anafanya hayo huku akionesha manjonjo yake ya kucheza ambayo yaliamsha shangwe zaidi na zaidi.
Zaganda hakuwa na kundi linalomsindikiza,hivyo sisi sote kuanzia Chris,mimi,Solomon,Silvia ,Saint na Miriam,tulienda kumpa kampani Zaganda. Ambapo kwa upande wangu nilianza kucheza na yeye alikuwa kama ananilipa kwa ninachofanya,matokeo yake ukazaliwa ushindani kati yangu na yake,ushindani ambao ulikuja kukatwa na Miriam.

Ilikuwa ni ghafla sana pale tulipokatishwa ule ushindani. Na wote tukiwa katika mshangao,aliingia Miriam huku anaimba wimbo wa Beyonce ule wa Upgrade. Na uzuri DJ alishapewa CD yenye biti ya wimbo huo.
Sikuwahi kujua Miriam anaweza akaimba kwa sauti nzuri kama ile,ambayo kweli bila kificho,unaweza kusema ni Beyonce hata pale alipokuwa jukwaani. Nywele,sura na mavazi,ilitosha kusema ni Beyonce ndiye anayevamia jukwaa kwa muda ule. Hiyo ikawa sapraizi tosha kutoka kwa Miriam na kuja kwa watu tuliyokuwepo pale,hasa mimi.

Miriam akawa anafatilia ile mistari aliyoimba Beyonce kama yeye vile. Hapo shangwe nalo halikusita kuchukua nafasi yake,na kizuri kilichowavutia wengi,ni Miriam alivyokuwa anaimba huku anacheza karibu yangu. Yaani alikuwa anacheza kwa kunikatikia Jay Z wake.
Ilipofika ile sehemu ya kuimba Jay Z,na mimi nikaanza kuimba mistari yangu kwa sababu ya Jay Z nilikuwa sijaiweka kichwani.Zaidi nilikuwa naimba mistari ya kumsifu Miriam.
Furaha kwa watu ikawa maradufu hasa pale DJ alipozidi kuweka biti za nyimbo za Beyonce na Jay Z kama Crazy In Love na Bonnie and Clyde. Na kilichokuja kushangaza zaidi ni pale Silvia naye alipokuja kuimba wimbo wa Beautiful Liar pamoja Miriam,huku yeye Silvia akiwa kama Shakira. Ilikuwa ni raha tupu.
“Hizi ni kama sapraizi kwenu jamani. Ila bado sijamaliza,nina sapraizi nyingine,mimi na Silvia au Shakira kama mlivyoona mambo yake”.Aliongea Miriam baada ya kumaliza ule wimbo wao.

Kimya kikatanda kwa muda na kila mtu akawa anasikiliza sapraizi inayofuata.Bila kutegemea nilianza kusikia biti ya wimbo wa Nameless ule wa Sinzia. Hapo niliganda kama sanamu ile ya Nyerere Square.Wakati huo Miriam alisogea karibu yangu na kuanza kuimba wimbo ule kwa bashasha nyingi na Silvia naye alifanya vivyo hivyo kwa Solomon.
“Nasinzia nikikuwaza”.Miriam alikuwa anaimba hivyo.
“Oooh”. Naye Silvia akawa anajibu huku anampapasa Solomon ambaye kiasi fulani alikuwa anaona aibu.
“Nasinzia nikikuwaza”.
“Ooooh”.
“Miaka rudi,miaka nenda”.
“Oooh”.
“Kila siku za karenda”.
“Oooh”.Wakawa wanaendelea kuimba wakati huo mimi tayari machozi yalikuwa yananilenga lenga. Na jinsi walivyokuwa wanaendelea kuimba,nilijikuta chozi linanidondoka.
Halikuwa ni chozi la furaha kama wengi walivyohisi. Wala halikuwa chozi la kushangaa jinsi Miriam alivyokuwa anaimba kwa kubembeleza. Chozi lile na mengine yaliyoendelea kutiririka,yalikuwa ni ya machungu. Machungu yaliyonikuta miaka mitano iliyopita wakati nipo penzini na Generose.

Wimbo ule ndiyo ulikuwa wimbo wa mwisho kuuimba Generose katika kalia yake ya maisha. Si hivyo tu!,bali wimbo ule ndiyo ilikuwa kauli ya Generose ya mwisho kuitoa mdomoni mwake.
Naam. Hiyo ndiyo sababu ya mimi kubaki nimesimama na kushindwa kuendelea kufurahi na wenzangu bali kutoa machozi yenye uchungu ndani yake. Na hapo ndipo niliamini kuwa penzi la kweli si rahisi kufa,na Miriam alikuwa na kazi kubwa ya kunifanya nimsahau Generose,mwanamke ambaye alinifundisha maana ya mapenzi,mwanamke ambaye alinielekeza jinsi ya kuwaheshimu wanawake,mwanamke aliyenitoa kwenye tabia chafu za kimalaya na kunileta katika tabia iliyompendeza MUNGU na kila mtu katika hii dunia.

Huyo ni Generose,ndiye yule yule kwenye mkasa wangu wa kusikitisha wa My Rose.Mkasa ambao ulimfanya mama yangu alie kama mtoto,akimlilia mwanae ambaye alikuwa kama kichaa kwa yaliyomkuta.
“Dadie mbona unalia?”.Sauti ya Miriam ilinitoa katika fikra zangu za miaka ya nyuma na kunirudisha katika ule ukumbi.
“Hamna Mamie. Ila huo wimbo umenikumbusha mbali sana”.Nikamjibu.
“Wapi tena Dadie hadi ulie?”.Bado akawa ananiuliza huku ananivutia kwenye chumba cha wageni kilichopo kwenye ukumbi ule.
“Kama unakumbuka niliwahi kukwambia kuwa kuna msichana siwezi kumuelezea historia yake”.Nikamwambia na kumsubiri anijibu nione kama anakumbuka.
“Yaap. Nakumbuka. Si yule uliyesema alikufa?”.Akaonesha kuwa anakumbuka.
“Ndiyo huyo huyo. Basi huo wimbo ndiyo ulikuwa wa mwisho kumtoka mdomoni mwake. Alikufa mikononi mwangu huku anaimba wimbo huo”.Nikamjibu na kufuta machozi ambayo yalikuwa yanaendelea kutiririka.
“Aisee, pole sana Dadie wangu. Na samahani sana kwa kukuleta katika hali hiyo”.Aliongea Miriam huku akinifuata na kunikumbatia.
Nilikaa kwa muda nikiwa na Miriam kwa ajili ya kusahau hali ile. Na nilipofanikiwa kuirudisha furaha yangu,ndipo tulitoka kwenye chumba kile na kwenda tena jukwaani,ambapo onesho tuliloliandaa lilikuwa linaendelea.

Ni baada ya watu` kuburudika vya kutosha,ndipo mkubwa wa onesho lile,yaani Solomon alishika kipaza sauti kwa ajili ya kutangaza rasmi biashara tunayoanzisha na malengo yake baada ya miaka kadhaa.
“Kwa niaba ya rafiki zangu,wote tunashukuru sana kwa uitikio wenu wa kuja kwenye onesho hili,ambalo lilikuwa ni kama shukrani kwenu kwa kipindi chote hichi tulichosoma pamoja”.Solomon alianza kwa shukrani na baadae akaendelea.
“Lengo kubwa kwa sasa ni kuwaambia biashara yetu tunayotaka kuanzisha. Mimi na wenzangu tumekaa na kuona kuwa,biashara inayofaa ni kufungua kiwanda kidogo ambacho tutakuwa tunatengeneza juisi pamoja na bidhaa ndogo ndogo nyingine za madukani kama pipi,biskuti,bigijii na vingine vya namna hiyo”.Akakaa kimya kidogo kwa kumeza mate kisha akaendelea.
“Pia katika miaka ijayo,tumepanga kuitanua biashara yetu na kuwa kubwa zaidi. Yaani hii biashara tumepanga itoke hadi nje ya Tanzania,na kadirio la kufanya hivyo,itakuwa ni kama miaka mitano. Hayo ndiyo malengo yetu”.Alimaliza kuongea Solomon na kunipa kipaza sauti mimi kwa ajili ya utambulisho wa jina la kampuni yetu.
“Bado nawashukuru sana kwa uitikio wenu,na zaidi naweza kusema nimefurahi sana. Bila kupoteza muda,nataka kuwaambia jina la kampuni yetu ambayo itahusika na hizi bidhaa ndogo ndogo za madukani”. Niliongea kidogo ,kisha nikatoa kikaratasi ambacho kilikuwa na baadhi ya maadhimio yetu ambayo tayari Solomon aliyataja.
“Kampuni yetu tumeamua kuiita SAINT JESIMA LIMITED COMPANY. Ikiwa ni muunganiko wa majina yetu,yaani Saint ambaye tumeweka jina lake lote. JE ni herufi za jina la Chris la ubini ambalo ni JENGO. SI ni Silvia na Solo na MA ni Masai na Miriam. Hilo ndilo jina la kampuni yetu ambayo kwa sasa tunahangaikia usajili”.Nilimaliza kuongea na shangwe likalipuka huku tukipokea pongezi nyingi.
“Na kwa kuanzia,tumeanza kwa milioni hamsini tulizozipata hapa na nyingine kuchanga sisi wenyewe. Bado tunaendelea kufanya hesabu na kuomba wafadhiri waweze kutusaidia suala hili. Naamini kuwa malengo yatatimia na baada ya miezi sita bidhaa zetu zitakuwa zinasambazwa.
Vile vile tutaajiri wafanyakazi wasiozidi therathini kwa sasa,hiyo ni kwa ajili ya kuendesha kampuni yetu na wataongezeka kadiri kampuni itakavyo kuwa kubwa”.Hapo Saint Kinala ambaye tulimfanya kama Mkurugenzi alikuwa anaongea.
“Kwa upande wangu,mimi sitakuwepo kwenye kampuni.Ila nitakuwa naichangia kwa kila kitu hasa kuitangaza kwa sababu kampuni niliyopo tayari ni kubwa sana.
Hivyo nitashirikiana na hii kampuni yetu mpya katika kila hali”. Naye Miriam ambaye alikuwa kwenye kampuni ya mjomba wake iliyofunguliwa tawi pale Dodoma,aliongea.
“Katika kila mwanakampuni muanzilishi. Yaani sisi saba kasoro Dada Miriam na Dada Silvia ambao wanawakilishwa na Masai na Kaka Solo. Tumepanga kupeana share katika asilimia ishirini(20%) kila mmoja. Hiyo ni kwa sisi watano”.Hapo akaongea Zaganda,muhasibu wetu mkuu.
“Kampuni ikiwa kubwa,tutaongeza bidhaa na kufungua biashara nyingine nyingi zaidi kuliko hii tuliyoanzisha. Hivyo ajira nazo zitakuwepo baada ya miaka mitatu hadi mitano”.Chris alihitimisha mikakati yetu na kisha mambo mengine yakaendelea hadi pale watu waliporidhika.
*************

Maisha yakaanza rasmi mtaani. Miriam akaenda kazini kwake na sisi tukaanza kuhangaika kujenga kiwanda chetu ambacho kwa kiasi fulani kilifanikiwa sana tu!.

Kwa uwezo wetu mdogo wa kifedha,tuliweza kukimaliza baada ya mwaka mmoja ambapo Miriam kila kukicha akiwa msaada mkubwa katika kufanikisha malengo yetu.
Alikuwa anatoa fedha nyingi sana japo mimi nilikuwa sipendi hali ile,lakini sikuwa na cha kufanya kwa sababu ilikuwa ni lazima iwe hivyo.
Hatimaye tukafanikiwa kukifungua kiwanda hicho kidogo na kuanza kutengeneza bidhaa hizo tulizokuwa tumepanga.
Ilikuwa kazi sana kwa watu kukubali bidhaa zetu,lakini kadiri tulivyoendelea,ndivyo kila mtu alikuwa anakubaliana na tufanyacho.
Tofauti yetu sisi na makampuni mengine ilikuwa ni bidhaa zetu kuwa adimu kuliko zao. Juisi kama za ubuyu na mvinyo wa choya iliyobora kabisa,uliifanya kampuni ya Saint JESIMA kuamza kutoka hadi nje ya Dodoma na hatimaye ikafika Dar es Salaam huku msaada mkubwa ukiendelea kuwa Miriam
***************

Baada ya miaka mitatu tangu tuanze ile biashara,moja ya malengo yetu likatimia. Hilo lilikuwa ni kuitanua biashara zaidi. Tuliongeza mafuta ya kupikia pamoja na sabuni ambazo vyote tulivipa jina la kampuni yetu.
Kampuni ikawa kubwa zaidi na zaidi,huku wafanyakazi nao wakiendelea kuongezwa kadiri ya mahitaji yetu

Ni MUNGU pekee ndiye ajuaye mioyo ya binadamu wa hii dunia. Mafanikio yetu yakawa furaha kwetu lakini yalikuwa chuki kwa wengine,chuki ambayo ilijengwa na baadhi ya watu wenye kithirani na sisi. Hapo ndipo mambo yalipoanza kubadilika na kuwa kama ushindani wa kibiashara,lakini ilikuwa si hivyo.

MENDRO FAMILY LIMITED COMPANY,ile kampuni ya Mjomba wa Miriam.Ikaingilia biashara yetu. Na wao wakaanza kutengeneza bidhaa kama zetu. Hapo ndipo kila mmoja alianza kuona chungu ya maisha,hasa pale soko letu lilipoanza kutiwa doa na hiyo kampuni.
Miriam alipoona hivyo,aliachana na kampuni yao na kuja kujiunga kwetu ambapo kama ni bifu,ndio likazidi maradufu.
Ujio wa Miriam kwenye kampuni yetu, ukaongeza ufanisi wa kazi,na kutanuka zaidi kwa biashara yetu kwa sababu tayari Miriam alikuwa ana jina sehemu kubwa ya Tanzania na Afrika Mashariki.
_____________

BAADA YA MIAKA SITA.

Tayari kila mmoja alikuwa na uwezo wa kifedha. Kampuni yetu ikaongezeka umaarufu mara kumi ya ile ya mara ya kwanza. Bidhaa kama mivinyo ya zabibu na mafuta ya kupikia,vilianza kutoka nje ya Africa Mashariki na kwenda nchi za jirani,hiyo ni kwa sababu ya ubora wake.
Baba wa Miriam,tayari alikuwa ni Rais wa Urusi huku Solomon na Silvia wakiwa tayari wana watoto mapacha wote wa kike. Kwetu sisi,bado tuliendelea kuwa wapenzi,huku Chris,Zaganda na Saint wao wakiwa bado hawaeleweki katika mapenzi yao.

Ile kampuni ya zamani ya Miriam,iliendelea kuwa kama mpinzani wetu hapa Tanzania lakini kwa uwezo wa Mungu,tulishawaacha mbali katika uzalishaji wa bidhaa zetu. Kila siku waliwalaghai wafanyakazi wetu na kuwachukua,lakini bado hawakuiweza Saint JESIMA.
******************
Karibu kila siku pato letu kutokana na ile kampuni liliendelea kuongezeka. Kila mmoja kwa wakati wake akaanzisha biashara zake binafsi ambazo ziliendelea kukua kila kukicha.
Kwa upande wangu nilianzisha kituo cha watoto yatima pamoja na sehemu ya mapumziko,ambapo sehemu hiyo ilikuwa ina kila aina ya burudani hasa za watoto. Pia niliweza kuanzisha studio ya muziki ambayo nilimuandikisha kaka yangu kama mmiliki kwa sababu yeye ndiye alikuwa na uwezo wa kutengeneza mapigo ya muziki. Studio ile ikawa kubwa nayo kadiri siku zilivyosegea. Kampuni nayo haiikuwa nyuma katika kuongezea viingiza vipato hapa nchini. Hoteli ya Saint JESIMA pamoja na mashule yaliyotapakaa karibu nusu ya nchi hii,yalitufanya tuwe juu kwa kipato na hata maisha kwa ujumla.

Mafanikio huwa hayaji hivi hivi. Ili ufanikiwe yakupasa kuweka akili yako katika kila lengo unalohitaji kulitimiza. Hapo ndipo utafanikiwa. Tulichukua zaidi ya mika saba kuwa pale tulipo,na miaka hiyo ndiyo ilitufanya hivi sasa tumiliki vitega uchumi mbalimbali hapa nchini.
Hatukuishia hapa tu! Baadhi ya bidhaa zetu kama sabuni,mvinyo na mafuta ya kupikia,vikaanza kutoka na kwenda mabara mengine hasa Asia na Ulaya.Ambapo Ulaya hasa Italia na Hispania tulikuwa tunapeleka sana Mvinyo wetu .
Kwa pale Urusi ambapo Baba wa Miriam alikuwa ndiye Rais,tulifanikiwa kuchukua oda mbalimbali za kutengeneza vinywaji vikali kama Wisky ambazo kwa kule zilikuwa zina soko kubwa kuliko bidhaa nyingine kutoka kwetu. Hapo ndipo kampuni ya Saint JESIMA ilikuja kupata heshima yake hapa nchini.

Kampuni iliendelea kupigana na maendeleo na kila mtu,kila siku alikuwa anaongeza ufanisi wake katika kufanya kazi zake.Hiyo iliifanya kampuni ipande ubora kila kukicha.
***********

Itaendelea

Post a Comment

0 Comments