“Sikiliza Masai. Pale ni wewe ndiyo unasubiriwa uende kuufungua ukurasa wenu wa mapenzi. Mwanamke kama mwanamke, hasa hawa waliyolelewa katika maadili mazuri au mazingira mazuri, hawawezi kuja kwako na kukutaka uwe wao mpenzi. Ila kuna njia kadhaa ambazo wanazitumia kukufikishia ujumbe huo. Na wewe tayari umeshapata ujumbe, basi ufanyie kazi”.Aliongea Solomon.
“Na vilevile kaka Masai, jipange sana na maneno ambayo unajua hatayasahau katika maisha yake kila akiyafikiria. Hapa namaanisha kuwa, maneno utakayoyaongea, hakikisha akiyafikiria mara mbili, hawezi kukukataa japo tayari tunajua yule ni wako”.Aliongezea Silvia.
“Aisee, asanteni sana. Nitalifanyia kazi suala hilo”.Nikawashukuru.
“Na kumbuka kitu kimoja Masai. Hisia ni mzigo mzito sana, na jinsi ya kuepukana na mzigo huo ili usikutese, ni wewe kwenda kuzielezea hisia zako kwa mhusika. Hata kama atakataa, lakini utakuwa tayari una amani katika moyo wako”.Alisisitiza Solomon wakati huo mimi nilikuwa nanyanyuka ili nirudi darasani.
“Sawa kaka nimekuelewa”.Nilimjibu na kuanza kupiga hatua za kuhama eneo lile.
“Hatimaye Masai kapenda, nimefurahi sana siyo siri”.Alitania Silvia na kuniacha sina neno zaidi ya tabasam la haja lililotoka baada ya ushauri wao mzuri uliyonirudisha katika hali yangu kiasi fulani.
Amani ya moyo wangu ilirudi tena.Yale mawazo ya mapenzi kidogo yakapungua huku sasa wazo kubwa likawa nikupanga maneno ya kumuambia Miriam ni jinsi gani navyojisikia juu yake. Wakati nafanya hayo yote, sikumwambia Chris wala mtu yeyote tofauti na Solomon na Silvia. Niliepuka sana kutaniwa hasa pale Miriam angenikataa.
Nilikaa wiki mbili na nusu bila kuonana na Miriam wala kuongea naye. Wakati tunaelekea kuikata wiki hiyo ya pili ili twende ya tatu, ndipo Miriam alipokuja chuo na kusababisha furaha irudi tena katika moyo wangu. Kila nilipomuangalia, moyo wangu ulikubali kuwa yule ndiye chaguo langu. ******* Nakumbuka ilikuwa ni Ijumaa moja tulivu, huku watu wakiwa katika pirika zao za maisha, wengi wao wakiwa wanaenda kwenye nyumba za ibada kwa ajili ya kuabudu, hasa Waislam. Na wengine wakiwa wanatoka shuleni na makazini kwao kuelekea majumbani mwao. Tofauti na hao wenye harakati zao, kulikuwa kuna wengine wanaangaliana uso kwa uso huku wakisindikizwa na vinywaji walivyoviagiza. Hao walikuwa siyo wengine bali ni mimi na Miriam.
Tulikuwa kwenye ule mgahawa wetu tuliopenda kwenda kupata chakula baada ya masomo yetu. Mgahawa ambao kila mhudumu alipenda kuja kutuhudumia kwa sababu tulikuwa siyo wababaishaji kwenye masuala ya malipo. Siku hiyo ndiyo hasa niliipanga iwe maalum kwa ajili kutoa hisia zangu kwa Miriam,na kwa kuwa Ijumaa kulikuwa hakuna masomo mengi,basi mapema kabisa tukakutana eneo lile.
“Ulikuwa wapi Miriam?”.Nilianzisha maongezi kwa swali.
“Yaani wewe.Na siku mbili tangu nije chuo,hujawahi kuniuliza,halafu leo ndiyo unaniuliza”.Aliongea kitoto huku kama anadeka kiasi fulani.Hapo tena nikaamini maneno ya akina Solomon.
“Hamna Miriam,ujue sikupata nafasi kama hii ya leo”.Nilimjibu kwa kumbembeleza kiasi.
“Hata kama,ulitakiwa hata unipigie simu na kuniuliza”.Akazidi kudeka.
“Hata simu yako ilikuwa haipatikani ujue.Yaani wewe acha. Ungeniona nadhani ungenionea huruma”.Nikaongea huku nanyanyua gilasi yangu juisi na kunywa kidogo .
“Ha ha haa,unanidanganya wewe. Ina maana ulikonda kisa mimi!!?”.
“Nakuambia we acha tu!”.
“Haya bwana.Ehee, Niambie ulikuwa unataka kusema nini hadi ukanileta huku?”.Miriam akahamisha mazungumzo yetu na kuyapeleka katika sababu ya mimi kumuita pale. Nilianza kujiuma uma kidogo huku nikishindwa nianzie wapi na wakati huo mapigo ya moyo wangu yalikuwa yanazidi kupanda na kusababisha kijasho fulani cha uoga kunitokea.Kitu ambacho nilikumbuka ili kisioneshe uoga ule ni kuchukua gilasi ya juisi yangu na kunywa kilichomo mle. Nilipoiweka mezani,tayari nilishaamua kuwa liwalo na liwe.
Nilitoa kitambaa changu kidogo cha kufutia jasho,kisha nikafuta maji maji yaliyo mikononi mwangu yaliyotokana na ile gilasi iliyokuwa na kimiminika cha baridi. Baada ya kuridhika kuwa mikono yangu ni mikavu,niliweka kitambaa changu mahala husika na kisha nikairudisha mikono yangu miwili katika meza.
“Naomba mikono yako Miriam”.Nilimwambia Miriam ambaye muda wote alikuwa kimya akiangalia na kusubiri jipya kutoka kwangu. Alivuta pumzi kidogo kwa ndani na kuitoa kwa nje,na kisha alikata shauri na kuitikia nilichomwambia. Akaikutanisha mikono yake na yangu kisha niliibana vizuri kama sitaki kumuachia kwa wakati ule.Hapo nilifumba macho kidogo kama nasali, na nilipofumbua,nilianza kuongea aliyonijaalia Mola wangu.
“Miriam. Sina cha ziada cha kukuambia katika masikio yako. Najua umesikia mengi kama haya,na umeyaona mengi pia kama haya.Ila kuyaona au kuyasikia kutoka kwangu,na asilimia zaidi ya mia moja, hujawahi. Katika historia yangu ya maisha sikuwahi kufikiria kama nitakuja kupenda tena.Lakini ujio wako katika upeo wangu wa uso….”.Hapo niliinama kidogo na kutikisa kichwa kushoto na kulia kama kujikataza nisiseme maneno yaliyobaki,lakini sikufanya hivyo. Nilinyanyua uso wangu na kumwangalia Miriam ambaye alikuwa bado kagandisha macho yake katika paji la uso wangu kama alivyokuwa mwanzo.Nikaendelea.
“Ujio wako katika upeo wangu wa uso,umenifanya nivunje hiyo historia niliyokuwa nimejiwekea. Bado sijajua sababu ya mimi kusema nakupenda,lakini nachojua moyoni mwangu ni kuwa nakupenda sana tena sana. Siwezi bila wewe,na sijui kama nitaweza endapo utakataa ombi langu la mimi kuwa na wewe. Miriam. Wewe ni mwanamke wa ajabu sana katika hii dunia. Sikuwahi kufikiria kama unaweza kusababisha nisile au kulala kwa ajili yako. Niliapa mbele ya MUNGU kuwa sitokuja kupenda,lakini ndiyo tayari nimependa na nimempenda Miriam. Sipo tayari kukukosa Miriam,UKIRUKA NAMI NITARUKA Miriam. Haya ni maneno nayopenda kumuahidi kila ajaye katika maisha yangu. Nakupenda Miriam”.Nilimaliza kuongea hayo maneno machache ambayo sikujua hata yalitokea wapi.Sikuyaandika wala kuyakariri,ila nilikuta yakinitoka tu! Baada ya maneno hayo nilishuhudia Miriam akiitoa mikono yake kwenye mikono yangu na kisha kunyanyuka na kushika mkoba wake na kuanza kuonda eneo lile.Kabla hajaondoka kabisa pale mezani,niliudaka mkono wake na kuongea maneno machache ya mwisho.
“Miriam. Nakupenda sana.Nitapigania penzi langu kwako mpaka siku roho itakapoacha mwili wangu”.Baada ya maneno hayo,Miriam aliuputa mkono wangu na kisha kuusogelea uso wangu,na kufungua kinywa chake.
“Sikudhani Frank na wewe unaweza kutamka maneno kama hayo,sikudhani kabisa”.Aliongea hayo na kutoa chozi moja ambalo moja kwa moja lilidondokea kwenye suruali niliyovaa.
“Miriam samahani kama nimekuhudhi”.Nilijikuta naomba msamaha mwenyewe baada ya kuona chozi la mrembo kama yule kudondoka.
“Niache kabisa kwa sasa”.Aliongea kwa hasira kidogo na kisha akanza kuondoka eneo lile akiniacha mimi nikiwa roho juu na kujilaumu kwa nilichokifanya. Nilichoshuhudia ni wale wenzake wawili wakimalizikia kupanda kwenye taksi na kutokomea kabisa mahala pale.
Nilishindwa nifanye nini maana hata nilipopiga simu yake,iliita na kukatwa na baadae kuzimwa kabisa. Nyumbani napoishi,nilipaona napo ni mbali sana kurudi kwa wakati ule. Nilichofanya ni kurudi katika yale madarasa yetu yaliyo ghorofani na kwenda lile darasa la juu na kisha nikatoa kiti nje ya ghorofa lile na kuanza kuwaza huku mawazo mengi yakiwa ni Miriam.
Nilikaa pale nje kwa muda mrefu sana bila kuongea na mtu wala kuinuka zaidi ya kubofya simu yangu huku saa nyingine chozi likinidondoka hasa nilipofikiria maneno ya mwisho ya Miriam. Mawazo yakiwa mengi kichwani kwangu huku maumivu ya hisia za mapenzi nayo yakiula moyo wangu,ndipo nilihisi kama mtu ananigusa begani kwangu kwa upole na kistaarabu.
Nilipogeuka nyuma kuangalia ni nani aliyekuwa ananigusa,ndipo nilikutana na uso wa Mzee Said Soji,yule Mzee ambaye ni mlinzi wa madarasa yale tuliyokuwa tunasomea. Alikuwa ni mwingi wa mshangao,na sura yangu ya majonzi niliyoibeba kwa wakati ule,ikamfanya kuwa na mashaka yaliyoonekana dhahiri usoni pake.
“Vipi kijana? Mbona upo hapa peke yako kwa muda mrefu halafu huu mwingi wa mawazo sana. Nini kinachokusumbua kijana”.Alianza Mzee Said Soji kuongea baada ya mimi kugeuka na kumsalimia huku nikiwa na mashaka.
“Hamna kitu mzee. Ni maisha tu ya chuo,ndiyo yananifanya niwe hivi”.Nikamjibu huku nikiwa naangalia chini kwa sababu niliongea uongo.
“Maisha ya Chuo au mapenzi?”. Mzee Said naye akaniuliza huku anazuga kwa kuangalia angalia pembeni na juu huku tabasamu la uchokozi likipamba uso wake. Swali lile likanifanya nishtuke kidogo,ila nikajikaza huku nikiamini kuwa alikuwa anakisia kinachonisibu kwa wakati ule.
“Hamna Mzee,ni masomo tu. Si wajua jinsi degree inavyosumbua”.Nikamjibu tena kwa kudanganya huku nikijibaraguza na tabasamu la kizushi kwenye uso wangu uliyokuwa umenishuka kwa sababu ya mawazo na kulia.
“Masomo kwa jina lingine yanaitwa Miriam,au nimekosea”.Akaongea tena Mzee Said huku akiongeza zaidi manjonjo yake ya kuangalia pembeni na juu kama anatafuta kitu kilichopotea. Hapo alizidi kuniongezea maswali kichwani na kunifanya nishindwe cha kumjibu na kubaki nimekodoa macho kama nimepigwa shoti ya umeme.
“Sikiliza kijana.Nafahamu mengi sana kuhusu urafiki wako na Miriam. Na sikuwa mjinga pale nilipokwambia kaa naye mbali. Kama mimi navyojua kinachokusumbua kwa sasa,na ndivyo kuna watu wanavyojua kila muenendo wa urafiki wako na Miriam”.Mzee Said Soji aliongea kwa umakini mkubwa huku akiweka kituo mahala panapostahili kwa ajili ya kusikia ni neno gani nitakaloongea. Alivyoona nashangaa tu,akaendelea.
“Hutanielewa kwa sasa.Ila yaitajika uelewesho mkubwa sana ili usije kuingia kwenye dimbwi walilowahi kuingia wengine. Ila kabla ya kukuelewesha,naomba kwanza nikuulize”.Mzee Said akatoa ombi ambalo na mimi bila hiyana nilimpa ruhusa ya kulitendea haki ombi lake kwa kuniuliza.
“Hivi umekula wewe?”.Akauliza.
“Ndiyo nimekula mzee.Lakini bado sijafahamu unataka nini na kwa nini unaniambia hayo yote”.Nikamjibu nakutoa dukuduku langu.
“Utafahamu tu. Umekula nini na saa ngapi?”.Aliniuliza tena,swali ambalo lilifanya nikae kimya kwa muda huku nikifikiria nimpe jibu gani ambalo litaondokana na maswali yale.
“Usinidanganye tafadhari. Kuwa muwazi tu,maana ukweli wako,ndiyo utanifanya mimi nikwambie mengi usiyoyajua. Nataka ufahamu kwa kifupi kuwa umekalia matatizo lakini hujui kama umefanya hivyo”.Aliongea Mzee Said kwa msisitizo baada ya kugundua nataka nimdanganye.
“Nilikunywa juisi pamoja na keki”.Nikamjibu huku naangalia chini.
“Sema ulikunywa juisi nusu kikombe na kipande cha keki. Haya ilikuwa saa ngapi?”.Aliongea tena Mzee Soji jambo lililonifanya sasa kuamini kuwa nilikuwa nafatiliwa sana. Ni kweli. Baada ya kutoka na Miriam na kwenda pale mgahawani,niiliagiza kikombe cha juisi na keki ambavyo sikuvimaliza baada ya ule mtafaruku uliyotokea baina yangu na Miriam.
“Ilikuwa ni saa tano na nusu,ndipo nilikuwa nimekula”.Nikamjibu swali lake alilouliza.
“Vizuri sana. Hivyo ndivyo inavyotakiwa kujibu msomi. Sasa tangu saa tano hadi sasa hivi saa kumi na mbili kasoro,hujala kitu zaidi ya huto tudude twenu mnatotupenda. Eti keki, sijui karanga na juisi. Hivi kweli tumboni kwako utakuwaje? Halafu inavyoonekana huna mpango kabisa wa kula hata ukirudi kwako. Kisa nini? Je. Kisa ni huyo binti ambaye hujui hata anatokea wapi”.Mzee Soji alikuwa anaongea maneno ambayo yalikuwa yananichanganya huku mengine yakiwa ni ukweli moja kwa moja.
“Sasa mzee,mimi hapa sikuelewi hata kidogo. Unaposema simjui hata kidogo yule binti na wakati mimi namjua anaitwa Miriam Mendrovic. Baba yake kwa sasa ni waziri wa ulinzi wa Urusi,na ndiye anapewa nafasi kubwa ya kuwania kiti cha Urais mwakani kwenye nchi yake,sasa hapo utasema simjui Miriam hata kidogo,mzee wangu?”.Niliongea kwa utulivu na heshima japo Mzee Soji yeye alikuwa anaongea kwa ukali kiasi fulani.
“Hayo yote najua wajua. Lakini je? Wajua anaishi na nani hapa Tanzania? Unajua kazi zao?”Aliuliza tena Mzee Soji.
“Aliniambia kuwa anaishi na mjomba wake ambaye ana mtoto wa kiume aitwaye Yuri.Pia wana shirika lao lililosambaa karibu kila kanda Tanzania,na mwaka juzi walifungua tawi la kanda ya kati ambapo Miriam ndiye msimamizi mkuu wa shirika la kanda hii”.Nilikuwa namuangalia usoni kwa makini sana wakati najibu swali lake hilo.
“Siyo mbaya kwa hayo machache uyajuayo. Lakini unajua kuwa upo kwenye matatizo makubwa kama ikifahamika kuwa unataka kuanzisha mahusiano ya mapenzi na Miriam?”.Niliutoa mgongo wangu katika egemeo la kiti nilichokalia, kisha nikavuta pumzi ndefu ambayo baadaye iliambatana na ukimya. Nilinyamaza kimya baada ya kinywa cha Mzee Soji kuuliza swali hilo.Na baada ya hapo nilitega sikio ili nisikie atajibu nini nilipomuuliza kivipi aseme yale aliyoyasema.
“Wewe ni wa tofauti sana kuliko vijana wengine niliyowahi kuongea nao. Japo nilikuwa naongea na wewe kwa jazba kiasi, lakini umekuwa mpole na mwenye hekima katika kila tendo na tamshi lako lililokutoka katika kinywa chako. Sasa fanya hivi,tushuke chini kwanza ili tukaongee vizuri”.Mzee Soji alitoa pendekezo ambalo sikulipinga,na kitendo bila kusita,nilinyanyuka pale kitini na safari ya kuanza kulishusha lile ghorofa ikaanza, na mwisho wake ulikuwa kwenye mgahawa mmoja ambao ulikuwa katika mazingira ya pale pale karibu na yale madarasa yetu.
Baada ya kuvuta viti vya mgahawa ule na kukaa.Mzee Soji aliniamuru niagize chakula chochote huku akitaka nifanye hivyo bila kupinga. Niliagiza ugali na samaki kisha nikaanza kula na wakati huo,Mzee Soji naye alikuwa anakula alichokiagiza.
“Kwa nini unataka kuanzisha mahusiano na Miriam?”.Alianzisha maongezi Mzee Soji baada ya kuridhika na ulaji wangu wa chakula nilichoagiza.
“Sijui mzee wangu. Ila najua ni nguvu ya mapenzi ndiyo iliyonisukuma mimi kutaka kuwa na mahusiano na Miriam. Nampenda sana Miriam”.Nikamjibu.
“Wanakuita Masai,si ndiyo eeh”.Niliitika kwa kichwa kuonesha kuwa nimekubali kwa alichokiongea.
“Bwana Masai. Hivi unajua Miriam kuwa anakuletea matatizo ambayo anakuepusha yasikukute lakini wewe unayang’ang’ania yaje?”.Safari hii mzee Soji aliongea maneno hayo kwa sauti ya chini huku akiwa anamsisitizo usoni mwake.
“Mzee bado unaniweka kwenye mabano. Miriam ananiepusha kivipi na ni matatizo gani ambayo unayasemea hapa”.Niliongea huku nimemkazia macho ya hamasa ya kutaka kupata majibu ya maneno niliyoyaongea.
“Umewahi kujiuliza ni kwa nini haongozani na wewe wakati wa kwenda kupata chakula? Si hiyo tu!. Unajua alikuwa wapi kwa wiki mbili hizi ambazo hakuja chuo?”.Maswali mawili mfululizo yalikuja kwangu. Majibu ya maswali hayo niliyatoa kwa kukipeleka kichwa changu kushoto na kulia kuonesha kuwa sikufahamu.
“Ha ha haaa. Masai.. Masai.. Masai.. Najua umechoka maswali na maneno yangu ya mafumbo. Ngoja sasa niende moja kwa moja ili unielewe”.Mzee Soji alitoa ahadi ya kuacha mafumbo na maswali,lakini kabla ya kuendelea kuongea aliyodhamilia,alinyanyua gilasi yake yenye juisi, kisha akameza mapigo kadhaa na kuishusha gilasi ile mezani.
“Miriam analindwa kuliko hata unavyofikiria. Wale mabinti wawili uwaonao,ni walinzi wanaopeleka kila tendo ambalo Miriam anafanyiwa hasa la hawa wavulana wanaomtaka kimapenzi Miriam. Na siyo hao wadada tu!. Kuna watu wanaomfatilia Miriam kwa kila hatua anayopiga. Na ndiyo maana alikuwa anakataa kutembea na wewe ili asionekane na kukutia matatizoni”.Alinyamaza kidogo Mzee Soji huku akinipa wasaha wa mimi kusema au kuuliza chochote kama ninacho.
“Sasa kwa nini wanamfatilia hivyo? Yule si ni mtu mzima na anajitambua kabisa. Mbona wanamfanya kama mtoto?”.Maswali yakamuendea Mzee Soji.
“Ha ha haaaa.Masai upo katika upofu mkubwa sana. Yawezekana hufahamu kuwa hata rafiki yako Chris sasa hivi angekuwa Marehemu”. Mzee Soji alinifanya nizidi kujaa na wingi wa maswali.
“Kwa nini unasema hivyo mzee”.Nikauliza.
“Ni kwa sababu alitaka kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na Miriam”.Akajibu Mzee Soji.
“Mmh”.Ikabidi nigune huku naurudisha mgongo wangu kwenye egemeo la kiti nilichokalia. CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/ “Nilijua ni lazima hutoamini kwa sababu yule ni rafiki yako. Lakini kama ungelijua kuwa rafiki ni mkia wa fisi,usingelitoa huo mguno wako wa ubishi.Ngoja nikuambie kitu kimoja Masai kuhusu urafiki. Katika maisha ya kila mwanadam hapa duniani,ni lazima awe ana rafiki. Lakini hao hao marafiki ni rahisi sana kugeuka kuwa maadui wakubwa katika pigana yako ya maisha. Na rafiki yako mkubwa ni rahisi sana kuwa adui yako namba moja. Na pia,mtu uliyemuona kama adui,akiamua kuwa rafiki yako,huwa ana urafiki wa kweli sana.
Hakuna rafiki hapa duniani zaidi ya wazazi wako na ndugu zako.Hao ndiyo wawezao kuacha shughuli zao na kuja kukusikiliza matatizo yako,na hao ndiyo walioradhi kuachana na rafiki zao muhimu kwa ajili yako wewe. Usidanganyike kuwa una rafiki wa kweli hapa duniani. Huyo unayemuamini,ndiye huyo ambaye kesho anampa mimba mkeo,na ndiye huyo huyo ambaye atakuweka gerezani ili yeye apate anachokihitaji. Na ndiye huyo huyo,atakayekugombanisha na watu wengine ili roho yake ifurahi,na mbaya zaidi kuliko vyote,rafiki anaweza kuutengua moyo wako na kutomuamini mtu yeyote katika maisha yako,yaani hata wazazi.
Usidanganyike na ukaribu wa rafiki yako yeyote yule. Rafiki mwenye wivu wa vitu vidogo kama mapenzi,huyo si rafiki. Kwani mwisho wa siku,atakusariti katika mambo yako makubwa mliyopanga pamoja. Sidhani hata kama rafiki zako wengine wanafahamu kuwa Chris alimtaka Miriam. Na kwa alivyomshenzi,wala hakukwambia kuwa yeye ndiye sababu ya kumfanya Miriam asije chuo kwa wiki mbili”.Hadi Mzee Soji anamaliza kuongea maneno hayo,mimi nilikuwa kinywa wazi huku nikishindwa kuamini kinachomtoka mdomoni mwake.
“Mmmh. Mzee,hapo kazi ninayo leo. Sasa angekufa kwa sababu gani? Na kama angekufa kwa sababu ya kumtaka,basi na mimi si naelekea huko?”.Nilizidi kumchimba Mzee Soji wakati huo ilikuwa inaelekea saa moja na nusu,na muda wa mzee yule kuingia kazini ulikuwa saa mbili,lakini saa kumi na mbili alikuwa anatakiwa awe amewatoa wanafunzi wote katika yale madarasa,kitu ambacho alikifanya kabla hatujaendea eneo lile.
“Sasa ulidhani mimi nipo hapa kwa ajili gani? Nimekuita hapa ili kukuonya kwa ambacho unataka kukianza. Kwanza ngoja nikuulize kitu kingine”.Mzee Soji akatulia kidogo kama anasubiria nimpe ruhusa ya kuuliza anachotaka.
“Uliza tu,mzee”.Nikamruhusu. Kabla hajaongea aliangalia huko na huko,na baada ya kuridhika na anachokiangalia,akafungua mdomo wake kuuliza alichokuwa anataka kuuliza.
“Hivi una taarifa gani za wale wanafunzi wenu watatu waliyopoteaga katika mazingira ya kutatanisha,na pale walipopatikana walikutwa ni maiti. Una taarifa gani kuhusu hilo?”.Mzee Soji alikuwa akiongelea matukio matatu,moja lilitokea wakati tunamaliza mwaka wa kwanza, na mengine mawili yalitokea mwaka wa pili, lakini katika muda tofauti. Matukio hayo yalikuwa ni kupotea kwa wanafunzi hao,ambao wote walikuwa ni wa kiume. Na walipopatikana,walikutwa ni maiti huku sehemu zao za siri zikiwa zimenyofolewa. Wote watatu walikutwa na karatasi zilizokuwa na maandishi ya kuwaonya wavulana wengine kwa tabia zao.
“Wale mi sina taarifa zao,ila nachosikia ni vibaka ndiyo walifanya vile”.Nikamjibu Mzee Soji.
“Ujumbe ulisema kuwa kila mmoja atakufa kama akijidai anajua mapenzi”. Nilimjibu Mzee Soji .
“Unaelewa maana yake?”.
“Sikutaka kufuatilia kwa sababu nilikuwa siyo mtu wa mapenzi”.
“Sasa nini kilichokusibu hadi ukijiingiza katika kumpenda Miriam?”
“Mapenzi hayana haja ya kuulizwa kwa nini mzee. Ni hali inayojitokeza hata bila kujijua. Rafiki yangu Solo anaziita hisia. Hisia huwezi kuzizuia kwani ukijaribu kufanya hivyo,ni sawa kama unajiumiza tu”.Nikamjibu hivyo.
“Ha ha haa,kijana unajidai unajua sana mapenzi,lakini hujui unaelekea wapi. Sasa kwa taarifa yako,wale vijana watatu, wote walikufa kwa sababu walimtaka Miriam awe mpenzi wao”.Aliongea maneno hayo Mzee Soji na kunifanya mwili ushikwe na ganzi ambalo hata sikulielewa ni kwa nini lilikuja wakati nilikuwa sina uhakika na asemayo Mzee Soji.
“Sasa Mzee,yaani kisa walimtongoza ndiyo wakauwawa? Mbona hiyo siyo sababu ya msingi?”.Nlimuuliza tena huku nikiwa makini zaidi ili watu wa pembeni wasiyasikie maongezi yale.
“Kijana kweli wewe ni kipofu,na unahitaji muda mwingi sana wa kumjua Miriam. Ila kwa kuwa muda umeishaenda,ngoja nikwambie haraka haraka”.Aliongea Mzee Soji na kisha alivuta kiti kwa mbele na kuanza taratibu kuongea huku akiwa makini na sauti yake.
“Sikiliza mwanangu. Nakuita mwanangu kwa sababu nataka kukulinda na wewe unilinde mimi. Siri hii nakupa,lakini kamwe usijemwambia mtu,hata Miriam. Mtoto wa mjomba wa Miriam,anaitwa Yuri. Yule ndiye hasa anayehusika na mauaji yote yale. Yuri hapendi kumuona mvulana yeyote anatembea na Miriam kwa sababu yeye ndiye anayetaka kumuoa Miriam. Lakini Miriam,anamchukulia Yuri kama kaka yake,hivyo hawezi kukubali kuolewa naye. Kwa sababu ya Miriam kukataa kuwa naYuri,basi hasira zote zimeamishiwa kwenu. Yeyote atakayekutwa na Miriam,au yeyote atakayemtaka Miriam kimapenzi,basi adhabu yake ni K.I.F.O!!!”.Mzee Soji kwenye neno kifo aliweka msisitizo wa hali ya juu.
“Mh!. Kazi ipo. Sasa wewe Mzee, umejuaje haya yote?”.Nikamuuliza.
“Nina mwanangu ambaye kazi yake ni kutembea na Yuri kama mlinzi,na yeye ndiye anahusika na utekaji nyara wa wanafunzi wote waliokufa. Anaitwa Mustapha,wenyewe wamezoea kumuita Muphty. Yeye ndiye anipaye kila tukio linaloendelea kazini kwake,na mimi hunipa kazi ya kuwashauri nyie kabla hamjaingia kwenye hatari hiyo”.
“Kwa hiyo hata Chris,ulimwambia?”.
“Tena yule ndiyo mbishi balaa,nilimwambia lakini hakunisikiliza zaidi ya kuondoka. Na mimi nikazipeleka taarifa kama zilivyo. Walishapanga kumteka na kumuua kama wale wenzenu. Lakini huyu Miriam alipopata taarifa hizo,ambazo alipewa na wale wasichana wawili, Miriam alitishia kujiua. Na baadaye alirudi Urusi kwa lengo la kumwambia baba yake matendo ya mdogo wake na mtoto wake Yuri. Hiyo ndiyo ikawa pona ya Chris,kwani mjomba wake aliahidi kutomuua Chris baada yakupigwa mkwara huo”.
“Kwa hiyo hata mjomba wake yupo upande wa Yuri?”.
“Tena yule ndiye chanzo cha sheria ya atakayemtaka Miriam,atakufa”.
“Mh! Mbona mambo makubwa sana haya?”.Niliongea huku nikishusha pumzi ndefu kutokana na maneno ya yule Mzee.
“Tena makubwa haswaa. Ngoja nikuulize swali”.Akakaa kimya kidogo kabla hajaniuliza.
“Uliza tu,mzee”.Nilimtoa kwenye ule ukimya kwa kumpa uwanja wa kuuliza.
“Umewahi kupita usiku kwenye yale madarasa yenu mnayosomea sasa hivi?”.
“Hapana. Mimi sijawahi kupita”
“Basi nakwambia haya,na kamwe usijekufungua mdomo wako na kuyasema kwa watu wengine. Nlipokuuliza kama unajua biashara wafanyayo ile familia,ukajibu kuwa unajua na ukanieleza vizuri sana. Lakini lile jengo ikifika usiku,huwa ni jengo la kufanyia biashara haramu za madawa ya kulevya na kuuziana siraha za moto kama bunduki. Narudia tena,iwe siri yako,kwani ukiitoa,amini usiami,utawaacha wazazi wako na wewe utakufa.
Lile Jengo ndilo wanafunzi wale watatu walipouawa,lile jengo ndilo sehemu maalumu ya kuulia vimbele mbele wote wanashitukia biashara zao”.Mzee Soji alinifanya mapigo ya moyo yaende kasi huku nikishindwa kuamini kama swali nitakalouliza litajibiwa ndiyo au hapana.
“Kwa hiyo Miriam na yeye anafahamu hayo? Na yeye anahusika au vipi?”.Nikajikaza nikauliza ili nipate jibu sahihi.
“Ha ha haa.Masai wewe muoga na jasiri sana. Yaani haya yote niliyokueleza lakini bado unamtaja tu Miriam!. Haya bwana,najua ni nguvu za mapenzi hizo. Miriam hafahamu chochote,na wala hausiki na biashara ile. Umeridhika sasa?”.Mzee Soji alinijibu huku anasimama hiyo ikimaanisha kuwa muda wa kukaa pale hana tena. Alilipia chakula nilichoagiza na kisha taratibu akaniomba twende wote hadi eneo lake la kazi.
“Unampenda kiasi gani Miriam”.Mzee Soji alianzisha maongezi baada ya kutoka nje ya mgahawa ule. “Mzee, siwezi kusimulia ni kiasi gani nampenda binti yule,ila nampenda sana tena sana tu”.Nikamjibu. “Upo tayari kuwa naye hata kwa maneno haya niliyokwambia?”. “Dah! Naogopa sana kuwa naye,kiukweli nimefanya kosa kubwa sana kumtaka,ni heri ningegugumia maumivu yangu ya kumpenda”. “Usiseme hivyo kijana. Pigania penzi lako hadi pale utakapokufa,hiyo ndiyo njia pekee ya wewe kuwa huru na kumweka huru Miriam. Hakuna watu wanaokupenda pale chuoni kama Miriam na wale walinzi wake. Wale ndiyo wanaopeleka kila taarifa ambayo wanaipata na kuiona kwa Miriam. Kama akilia,basi wale huenda kusema kuwa leo Miriam kalizwa na mtu fulani.Lakini wewe,hawajawahi kufungua mdomo wao hata mara moja na kusema kuwa unatokaga out na Miriam”.Mzee Soji alianza kunipa moyo.Hakuishia hapo,akaendelea. “Penzi la kulazimisha,siyo penzi hata kidogo.Si ruhusa kumlazimisha mtu akupende wakati hata wazo hilo hajawahi kuwa nalo. Penzi hutengenezwa kwa mfumo wa watu wawili ,wenye jinsia tofauti. Mfumo huo,hakuna ajuaye ni vipi unatengenezwa,lakini kichocheo kikubwa huwa ni hisia. Hisia ndizo kila kitu katika mwili wa binadamu. Kama huna hisia za kufanya jambo fulani,basi usilifanye,kwani ukilifanya utaliaribu au litakuaribu. Hata mapenzi,kama huna hisia nayo,waache wenye nazo wazitendee haki. Una hisia juu ya Miriam,na Miriam ana hisia huu yako. Hapo mnatengeneza penzi.Penzi ambalo hakuna binadam awezaye kulitenganisha kama nyie wenyewe mkijitambua na mkiwa mnamaanisha kwa mfanyayo”.Mzee Soji alisimama kwenye geti la kuingilia kwenye jengo lile na kisha akanipa maneno ya mwisho kabla sijaondoka. “Yuri na baba yake wanaondoka wiki ijayo,nadhani hiyo itakuwa nafasi yenu nyie kuoneshana upendo wenu. Mimi sitopenda sana kukuona kijana mwenye hekima kama wewe,unamkosa Miriam. Cha msingi ni kutoamini marafiki zako unaoona ni wa karibu sana. Hao ndiyo wabaya,na kamwe hawapendi kuona tabasamu lako bali ukijifuta machozi tu!. Hapo watafurahi na kunyanyua gilasi zao juu na kugonga”.Mzee Soji alizidi kunisisitizia maneno ambayo yaliingia kisawa sawa masikioni mwangu. “Haya mzee.Asante sana kwa ushauri wako.Siyo siri,umenifanya leo niondokane na uchovu ambao ungenishika kwa wiki nzima”.Nilimshukuru Mzee Soji huku nikijiandaa kuondoka kwa maana muda ulishakimbia sana. “Kitu kimoja cha mwisho”.Mzee Soji alisimamisha safari yangu na kunifanya nirudi pale alipokuwepo. “Maneno katika maisha yako.Yawe ya kimapenzi au ya kirafiki,ili mradi yawe maneno. Maneno ni kama maji kwenye ugali. Ukiyazidisha sana hutengeneza uji,na ukiyapunguza basi ugali lazima uwe kama jiwe.Chunga sana maneno yakutokayo mdomoni kwani yanaweza kujenga na kubomoa pia. Tafuta maneno mazuri ambayo utayatoa katika muda na wakati muafaka. Kama upo kwenye sherehe,basi ongea maneno ya kisherehe na kama upo darasani,ongea ya kiuanafunzi.Na kama ukikutana na Miriam,ongea kama mwanaume rijali.Usiwe mrahisi wa kuomba msamaha au kutoa machozi,hiyo inakupunguzia maksi sana. Maneno yako yakupasa kuyatoa kwa kujiamini sana. Nimekupenda sana kijana wangu,na ukiwa na shida,wewe nitafute. Nimekupa siri nyingi sana,ila hii ya mwisho naomba uitunze zaidi ya zote. Mimi siyo mlinzi kama uzaniavyo,bali ni mtu niliyosomea mambo ya saikolojia na nilikuwa ni mwanajeshi kwa miaka kumi na tano,kutonana na uamifu wangu wa kutunza siri,ndiyo nikaajiriwa na hawa kwa ajili kulinda eneo hili. Mshahara naopata mimi,hata Waziri anifikii. Ni wewe pekee utakayemuokoa Miriam na taifa kiujumla. Najua huelewi,ila utakuja kufahamu tu!”.Alimaliza Mzee Soji na kuingia ndani,huku akiniacha mimi nikibaki na maswali ambayo niliamua kuyapuuzia na kupotea eneo lile.
Baada ya maongezi yale kuisha,nikapanda daladala hadi Makole napoishi,na nilimkuta Chris akiwa katulia peke yake anaangalia TV. “Niambie Jay. Mbona leo umechelewa sana kamanda”.Alianza kunisalimia Chris baada ya kuingia.Sikutaka kuongelea jambo lolote lililotokea nilipotoka,hivyo nilikaa kimya huku nikitunga uongo wa kusema ambao ungefanana na ukweli. “Aaah,nilikutana na yule Mzee Mlinzi,akaanza kunipa sala ndefu kichizi”.Nilimwambia hivyo Chris ili nione atapokeaje akisikia hivyo. Na kama nilivyotegemea,alishituka kiasi na kuuliza kwa hamasa. “Ehee!. Mzee kasemaje?”. “Aaah,wazee wengine chenga tu! Anaanza ooh,kaa mbali na Miriam,mara achana naye kabisa. Sasa mimi nikamuuliza kwa nini?. Yeye akajibu ni kwa sababu mkubwa kasema. Hapo ndiyo nikaanza kubishana naye hadi sasa hivi”. “Sasa anatakaje? Kwani wewe ushamtongoza Miriam?”.Chris akaniuliza swali ambalo nililitegemea sana kichwani mwangu. “Yule ni rafiki yangu tu!Siwezi kufanya hivyo”.Nikamjibu kwa kumdanganya. “Sasa kama hujamtongoza mbona anakuonya?”.Akauliza tena Chris. Swali hilo likafanya nigundue kuwa,kwa asilimia kubwa ya maneno aliyoongea Mzee Soji,ni ya kweli. Kwa nini Chris afahamu kuwa wanaomtongoza Miriam ndiyo Mzee Soji anawaonya? Swali nikajiuliza kichwani. “Mimi mwenyewe nilishangaa,na hilo ndo lilitufanya hadi tugombane”.Nikazidi kumvuta Chris ili aongee ukweli. “Mimi mwenyewe ujue yule Mzee alinifuata na kuanza maneno kama hayo. Nikamtoa baru kama mwizi”.Akaongea Chris na kunifanya niamini maneno ya Mzee Soji. “Ha ha ha haaa. Hapo ulicheza. Kwani na wewe ulimtokea Miriam?”Nikamuuliza kwa kumtega. “Hiyo haiwezi kutokea hata kidogo, Jay. Yaani siwezi kufanya hivyo. Ila zile wiki mbili zilizopita nilimuomba twende kupata chakula pamoja. Wakati tunakula akapigiwa simu.Alivyoipokea na kuiweka sikioni,hakujibu kitu zaidi ya kunyanyuka pale tulipo na kuondoka haraka na wale wenzake. Nadhani yule Mzee aliona hiyo muvu na ndiyo maana akanifuata na kunionya”.Baada ya maneno hayo nikajihisi nilikuwa namfikiria Chris vibaya. Yawezekana hakumtaka Miriam kama Mzee Soji alivyosema,ila kuna vibaraka walipeleka taarifa kuwa Miriam yupo na mvulana. “Aaah. Watajua wenyewe. Mimi kwangu ni rafiki tu!”.Nikamwambia Chris huku nikijionesha sina nia ya kuwa na Miriam. “Ila Jay,twende mbele na kurudi.Yule mtoto unampenda sana,na yeye anakupenda kichizi. Macho yenu yanaonesha kabisa. Ujue siku ile nilivyokaa naye pale mgahawani,kila wakati alikuwa anataja jina lako. Mara Masai anapendaga juisi ya ukwaju au fanta na keki.Basi akisema hivyo na yeye anaagiza. Akataka hadi anunue keki na hiyo juisi ili nikuletee,sasa ile simu ndiyo ikaharibu kila kitu”.Aliongea Chris na kunifanya nianze kubadilika kihisia na kuhisi labda Mzee Soji aliwahisi tu. “Ha ha haaa. Wewe ujue siyo wa kwanza kusema hayo. Hata wakina Solo walishasema. Sasa mimi kwa kuniangalia,utasema kuwa nampenda Beyonce?”. “Kha! Yaani wewe hata ujifichaje,unaonekana ile mbaya.Kipindi kile wakati haji ulikuwaga huna raha hata kidogo. Ilikuwa bado kidogo tu! Nikuzingue,lakini Kaka Solo alinikataza. Sasa alipokuja sasa, duh! Hapo ndiyo niliamini kuwa mapenzi yanaweza kugandisha risasi”.Chris aliongea huku anatabasamu. Nikajikuta nasahau maneno ya Mzee Soji na kuanza kuongea na Chris bila wasiwasi kama ule wa mwanzo. “Ha ha haaa. Chris na wewe kumbe mtambo eeh. Sasa mapenzi yanaweza kugandisha risasi?’.Nikamuuliza swali kutoka kwenye yale maneno aliyoyaongea. “Kwani wewe hujui? Wewe kama una mpenzi wako,hata umfumanie mara ngapi,kama unampenda kweli huwezi kumfanya kitu. Yaani hata kama una bastola,halafu ukamfuma na njemba nyingine,huwezi kumshuti. Hapo mapenzi hayajagandisha risasi?”.Chris akafafanua nakuniacha mimi natabasamu bila kusema neno. “Kaka cha msingi kesho akija,wewe mwambie ukweli tu! Mwambie ni kiasi gani unampenda”.Chris akanipa ushauri ambao mwenzake nilishaufanyia kazi muda mrefu sana. “Kasema kesho haji kwenye diskasheni,si wajua kesho ni Jumamosi. Labda Jumatatu”.Nilimjibu Chris huku nikiwa makini na maongezi yetu ili nisije kuropoka mengine. “Ila Jay. Mimi nimekisia tu! kuwa unampenda. Sasa nataka kwa mdomo wako hapa hapa,useme kama kweli unampenda Beyonce”.Chris akataka ajue ukweli wa moyo wangu. Kwa kuwa alikuwa ni rafiki yangu wa karibu,wala sikutaka kumficha. “Dah!. Kaka kiukweli nampenda sana Miriam,yaani hata yule mzee nilimwambia hivyo hivyo. Najihisi vibaya mno kukaa mbali na Miriam. Natamani hata sasa hivi awepo karibu yangu,ila ndiyo siwezi”.Nikamjibu Chris. “Sasa hapo kazi umeishaimaliza. Kama kweli unampenda,chukua muda wako na kuanza kutoa dukuduku lako kabla mambo hayajawa mabaya”. “Mambo hayajawa mabaya kivipi tena?”. “Ha ha haa. Hujui mapenzi ni kama upepo? Muda wowote hubadilisha muelekeo. Beyonce anakupenda balaa,sasa usimfanye abadilishe pendo lake kwako na kwenda kwingine”. “Ha ha haaa. Halafu Chris unanichukulia mimi ni mtoto sana katika mapenzi. Mi hayo nayajua sana,sema niliamua kukaa na kutulia kwa muda kutokana na historia yangu ya nyuma. Ila mimi ni moto wa kuotea mbali katika mapenzi”. “Jay huna kitu wewe katika mapenzi,usitake kujikweza hapa”. “Wewe ndiyo huna kitu Chris. Unataka kuleta misemo yako mwenyewe hapa kwa kujidai muhenga,kumbe wewe ni malenga wapya.Eti mapenzi ni kama upepo,muda wowote hubadilisha muelekeo,wapi hiyo umeitoa?”. “Ha ha haaa. Jay unajidai leo unayajua mapenzi eeh. Haya niambie wewe,mapenzi ni nini?”. “Nashukuru kwa kunipa nafasi hiyo ndugu mheshimiwa mwenyekiti”.Nikajidai nipo mkutanoni. Nikameza mate na kuendelea. “Kwanza kabisa nakataa kauli yako ya kuwa mapenzi ni kama upepo,muda wowote yanapoteza muelekeo. Naipinga kauli yako kwa kusema kuwa,pale kwenye pendo la kweli,kamwe hakuna atakayebadilisha uelekeo wa pendo hilo,awe Shetani au binadam wa kawaida. Ni Mungu pekee awezaye kubadilisha pendo la mtu. Hata ukienda kwa mganga,atakupa dawa ambayo itakaa siku chache tu.Ikiisha,na pendo la zamani hurudi pale pale”. “Mh!, maneno yako kama kweli Jay”. “Siyo kama kweli,habari ndiyo hiyo. Wanasema pendo la kweli halifi.Kufa kwake,ni kifo chenu”. “Kwa hiyo Jay,wewe unasema mapenzi ni nini?Embu nijibu hapo,usiruke ruke” “Ha ha haaa. Hapa umekutana dokta kijana wangu,nadhani ulikuwa hujui kuwa na mimi naweza.Sasa ngoja leo nikupe vitu hadi kesho uniambie shikamoo”. “Ha ha haaa. Jay leo umekula nini?Mbona unaongea sana?”. “Shida yangu nikuthibitishie kuwa na mimi ni hatari sana katika mambo hayo”. “Haya kaka niambie”.Chris akaomba nimuelezee nini maana ya mapenzi kwa ninavyoona mimi,kwani kila mtu ana maana yake katika mapenzi. “Sikiliza sasa. Mimi nayafananisha mapenzi katika maana mbili. Maana ya kwanza naweza kusema mapenzi ni kama ngozi ya mwanadamu. Hata ujichubue uwe mweupe kiasi gani,lakini ukipita mahala,hawawezi kukuita mzungu,na wakikuita inakuwa ni kusanifiwa tu. Na mapenzi yapo vivyo hivyo. Hata ujifiche vipi,kamwe huwezi kuyaficha yenyewe,kwani ukifanya hivyo,yatakuumbua tu. Ni kama mimi.Japo nilijificha lakini mwisho wa siku si hivyo umejua”.Nilimaliza kuongelea mapenzi kwa pointi ya kwanza na kumuangalia Chris usoni,ambapo alikuwa anatabasamu tu,wakati naongea.
“Maana ya pili,naweza kusema kuwa,mapenzi ni lugha ambayo hakuna asiyeielewa. Hapa na maana kwamba,hata bila kuongea kwa mdomo,macho yako yataongea tu!. Huwezi kuificha lugha ya mapenzi mwilini mwako. Sijawahi kuongelea mapenzi nikiwa na nyie,lakini nilikuwa nacheka sana pale naposikia mnadanganyana kuhusu mapenzi,eti mapenzi ni kama upepo,acha bwana Chris. Penzi la kweli halifananishwi na upepo kwa kusema kuwa upepo unabadilika muelekeo,basi na penzi nalo lipo vivyo hivyo. Lakini ukisema mapenzi ni kama upepo huku ukimaanisha kuwa upepo unaweza kuleta amani au majanga,hapo nitasema ndiyo. Kwani mapenzi ndivyo yalivyo,huleta majanga na muda mwingine amani. Hakuna apendaye kuona mtu mwingine anaishi kwa furaha kwenye mapenzi yake,atajaribu kuyayumbisha yumbisha ili aweze kuleta majanga kwenye mapenzi yako. Na watu hao hufanikiwa kwa muda mchache na kisha hupotelea mbali kwa aibu kubwa ,na saa nyingine MUNGU huwapa maisha marefu ili waone mafanikio yako katika kitu alichokuwa anakiyumbisha. Hapo nimeongelea kuhusu mapenzi na maisha pia,umenipata dogo”.Nilimaliza kumpa somo Chris huku nikianza kukung’uta kitanda kwa ajili ya kulala. “Mh!Aisee. Siamini kama ni wewe ndiye umeongea hayo. Ila mimi siyo dogo”.Aliongea Chris huku akikasirika kidogo baada ya kumuita dogo. Chris alikuwa hapendi sana kuitwa dogo,na ndiyo maana nilivyomuita hivyo,alikasirika kiasi. “Poa usijali kijana,nilikuita hivyo nikimaanisha kwa haya niliyoongea wewe bado ni mchanga sana kwangu”.Nilijitetea huku sasa hivi nikikanza kupanda kitandani kwa ajili ya kuusaka usingizi. “Poa,bwana.Vipi leo hauli? Mbona unalala tu!”. “;Mimi nimeshiba. Huo nitanywea kesho chai,si ulipika wali eeh”. “Ndiyo. Halafu mchele wenyewe unakaribia kuisha”. “Tutanunua kesho. Ngoja mimi nilale kwanza,nitaamka badaye kupitia Cost Accounting”. “Poa. Ngoja na mimi nimalizie haya maswali mawili,halafu nilale”. “Poa.Usiku mwema”.Niliagana na Chris,kisha safari ya kuusaka usingizi ikaanza. *******************
Ilipita wiki moja bila Miriam kuonekana chuo. Nilikuwa na wasiwasi sana.Nikahisi labda maneno ya Mzee Soji yanataka kunitokea na mimi,au labda Miriam alikuwa anataka kujiua baada ya kusikia kuwa na mimi labda nafuatiliwa ili niuawe na ndugu zake. Mawazo yakawa mengi kichwani mwangu. Mawazo hayo yalikuja kukatika baada ya wiki ya pili kuanza.
Iliokuwa ni Jumatatu moja tulivu na yenye kila bashasha katika sura ya dunia yetu,hasa pale Dodoma. Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,walionekana nadhifu sana kwa sababu ilikuwa ndiyo siku ya kwanza ya wiki,hivyo walikuwa ni wasafi sana. Nakumbuka siku hiyo Miriam naye alikuja chuo,ila hakukaa na mimi kama ilivyozoeleka.Alikaa na wale wenzake anaopenda kutembea nao sana. Sikuwa na wasi wala sikushituka kwa ile hali kwani nilikuwa najua nilimfanyia kosa sana kumtongoza. Baada ya kumaliza vipindi viwili vya mle darasani,nilishuka chini na kwenda kwenye mgahawa wangu niliyokuwa napendelea kwenda,na kisha nikaagiza kama kawaida keki na juisi ya ukwaju. Nilianza kuburudika na kinywaji kile taratibu hadi nikakimaliza. Nilimuita muhudumu na kulipia nilichoagiza na kisha nikanyanyuka kitini na kuanza kuondoka. Baada ya kutoka nje ya mgahawa ule,ndipo uso kwa uso nikakutana na Miriam huku uso wake ukipambwa na tabasamu la haja na la kuvutia pia.
Tabasamu la Miriam lilinifanya na mimi nipate faraja hasa pale mwili na miguu yake ilipokuwa inaelekea mimi napotokea.
Alikuwa kavalia mavazi mekundu kwa juu,huku sketi yake ya rangi ya kahawia iliyoishia magotini, ikimfanya apendeze zaidi. Viatu vyake vya mchechemeo navyo vilibeba rangi nyekundu sawa na banio lililoshika nywele zake zenye kila sifa za kuitwa nywele,na siyo nywele kituko,nywele zenye utapiamlo kama nywele za dada zetu fulani mitaa ya uwanja wa fisi. Za Miriam hazikuwa hivyo.
Mwendo wake wa madaha na maringo yaliyokuwa yanaonekana katika shingo yake,huwezi kusita kusema ni Miss Venezuela au ukishindwa kabisa hata kumfananisha,sema anafanana na Beyonce,hapo nadhani kila mtu ataelewa nazungumzia nini.
“Leo umeamua kuja peke yako,si ndiyo eeh”.Alianza Miriam huku tabasamu lake likizidi kuupamba uso wake wake nadhifu,ambao ulikuwa haujakatwa nyusi wala kupaka maduwasha kama poda. “Mimi nilidhani leo huna muda na mimi. Hata ulipoingia darasani,niliona umeamua kukaa peke yako huku wale rafiki zako wakiwa kwa pembeni. Na mimi nilivyoona hivyo,nikasema sawa,mbona nilishajizoelea hali yangu ya upweke”.Niliongea huku na mimi nikizidi kulitengeneza tabasamu langu ili na yeye alielezee jinsi lilivyo moyoni mwake. “Nilijua tu hicho ndicho kitakuwa kisingizio chako. Lakini ni kweli,nilifanya kosa,samahani sana kwa hilo Masai”.Miriam alikubali kosa na kuomba msamaha ambao kwangu mimi niliona kama hakufaa kufanya vile. “Hamna bwana,mimi ndiye nilipaswa kuomba msamaha. Kwa sababu mimi ndiye nilifanya wewe usije chuo,na mimi ndiye sababu ya wewe leo kukaa mbali na mimi.Nilimpa sababu ambazo nahisi ndizo zilikuwa sahihi kwa mimi kuomba msamaha. “Hamna kitu kama hicho Masai. Mimi ndiye mwenye makosa kwa kile nilichokifanya siku ile,ni lazima niombe msamaha”.Alisisitiza kauli yake Miriam ambapo nilikuwa sina jinsi zaidi ya kumkubalia.
Muda wote wakati tunaongea tulikuwa tumesimama mahali fulani ambapo palikuwa ni njia ya wapita miguu. “Sasa wewe si umejidai umekula peke yako eeh.Tutaona leo kama kweli mtu akila sana anaweza akapasuka. Twende tena ulipotoka,nina maongezi na wewe”.Miriam aliniambia na kunishika mkono huku mimi sijui cha kufanya zaidi ya kufuata anapokwenda kama vile zezeta,si mwajua mapenzi bwana.
Nilirudishwa tena kwenye ule mgahawa na bila hata kujali,Miriam aliniagizia keki nyingine na juisi ya niipendayo, nazungumzia juisi ya ukwaju.
Mimi mtoto wa kiume,hivyo sikuona taabu kula na kunywa ile juisi ambayo Miriam alisisitiza niinywe ili maongezi yanoge.
“Masai,naomba nikuulize swali”.Alianzisha maongezi Miriam baada ya tulivyoagiza kuletwa na kuviweka vinywani kwetu. “Uliza tu! Miriam”.Nilimkabidhi uwanja afanye yake. “Unajua nini kuhusu mapenzi?”.Nilitabasamu kabla ya kujibu swali lake huku kichwani mwangu nikikubaliana kuwa katika dunia ya sasa,katika kila kundi moja lenye jinsia tofauti,asilimia themanini ni lazima habari za mapenzi ziwepo. “Kivipi sasa Miriam. Unataka ujue mapenzi yangu ya kitandania au mapenzi yapi wewe unayasemea?”.Na mimi nikamuuliza kutaka ufafanuzi juu ya swali lake. “Ha ha ha haaa,eti mapenzi ya kitandani. Si hayo bwana,mi nataka uniambie ni kiasi gani unaweza kumpenda mtu”.Alifafanua Miriam japo bado nilikuwa najiuliza ni kitu gani alikuwa nacho kichwani kwake kwa muda ule. “Sijui ni kiasi gani nitampenda,lakini nachojua nitampenda sana tena sana”.Nikamjibu. “Kwani umehawi kupenda?”.Akaniuliza tena. “Ndiyo. Tena sana tu!”. “Mara ngapi umewahi kupenda?”. “Penzi la kweli limenitokea mara tatu”. “Hee,kwani kuna penzi la ukweli na la uongo?” “Ndiyo. Mara nyingi penzi la uongo utokea sababu unataka kusahau jambo fulani hasa la mapenzi yako ya nyuma. Penzi hilo unakuwa unajilazimisha tu kupenda na wala unakuwa hulijali. Ila pendo la kweli linakuwa linaugonga sana moyo wako,yaani usipomuona umpendaye, unahisi kupungukiwa kitu”. “Mh! Kumbe na wewe ni mtaalam eeh. Nilikuwa sijawahi kusikia ukiongea hivyo”. “Kawaida tu!. Nimepitia na ndiyo maana nakujibu kwa uhakika”. “Okey,sawa. Embu niambie hao watatu ulikuwaje mpaka sasa haupo nao”. “Mh! Mama,mbona unataka mambo makubwa hivyo? Leo umeniamulia nini?”.Ikabidi nizuge kwa kumuuliza maswali hayo kwa sababu nulikuwa sipendi sana kusimulia mahusiano yangu ya nyuma. “Mi nataka kujua tu! Ukinijibu na mimi nitakuambia kinachonisibu”.Nilikubali kumwambia kwa sababu aliniahidi kuniambia cha kwake ambacho tayari kwa wakongwe kama mimi nilishajua nini kinachokuja kusemwa.
“Okey poa. Wa kwanza nilikutana naye kidato cha pili. Wa pili niliku…….”.Kabla sijaendelea Miriam alinikatisha maongezi yangu. “Aaah!.Mimi sitaki unielezee hivyo. Nataka uniambie na ilikuwaje hadi hivi sasa haupo naye tena”.Miriam akazidi kuniweka matatani na maneno yale ambayo kwangu sehemu nyingine ilikuwa ni kama unachukua nyundo na kuanza kuuponda moyo wangu kama akitaka nihadithie.
Hivyo baada ya kutaka nimwambie kilichonisibu,nilishindwa kuvumilia na kujikuta nimepoa ghafla huku macho yangu nikiyainamisha chini tofauti na mwanzo ambapo yalikuwa yanamuangalia moja kwa moja usoni pake. “Mbona umepoa ghafla Masai? Au nimekukera na maswali yangu?”Akaniuliza swali baada ya kuona hali yangu ya kupoa. “Hamna Miriam. Sema kuna mambo mengine yanipasa kuyasahau kabisa katika kichwa changu ndiyo niyahadithie”. “Kwa hiyo una mambo ambayo hupaswi kuyasimulia?”. “Ndiyo hivyo Miriam. Yalinitesa sana,yaani nikianza kuyasimulia hapa,nadhani utakuwa unakaribisha machozi katika uso wangu”. “Okey. Sipendi nione machozi ya mtoto wa kiume. Huwa naumia sana kuona mwanaume analia”.Aliniambia Miriam huku akiridhika na niliyomwambia. “Basi niambie ambayo hayakukuuma kama yapo”. “Yote yaliniuma lakini moja ndiyo sitaki hata kulisimulia”. “Niambie hayo mengine na hilo moja tulifanye kiporo,hadi pale yatakapokuisha machungu yako”.
“Okey. Kuna wa kwanza,nilikutana naye kidato cha pili. Huyu ndiye mwanamke wa kwanza kumpenda. Tuliachana baada ya yeye kupata mtu ambaye alimuona kwake ni sahihi. Baada ya hapo nikawa mtu wa wanawake sana,yaani kwa lugha rahisi nilikuwa malaya. Sababu kubwa ya kufanya hivyo,ni kulipa kisasi kwa alichonifanyia yule niliyekutana naye kidato cha pili.
Wa pili ndiye alinituliza na mimi kuwa hivi nilivyo sasa. Huyu sitaki kumzungumzia ila kwa kifupi alinitoka katika maisha yangu.Alifariki wakati penzi langu kwake lilikuwa limegusa kilele cha upendo wangu”.Nilimwambia hivyo na kisha niliinama tena chini kama nasali au nakumbuka mbali sana. Nilishituka baada ya kuhisi mikono yangu miwili niyokuwa nimeiweka mezani kushikwa na mikono mingine ambayo ilikuwa ni laini na yenye joto la kubembeleza. “Pole sana Masai. Sikufahamu hilo,pole sana Masai. Nimalizie na huyo watatu basi”.Alikuwa ni Miriam akinibembeleza huku kanishika mikono yangu. Nilitabasamu kidogo baada ya kusikia anataka nimwambie mtu wa tatu.
“Wa tatu aisee,dah! Sijui nimzungumziaje,lakini huyu kaja katika maisha yangu kwa ajili ya kuufungua ukurasa wangu mpya wa mapenzi na kunisahaulisha yaliyopita. Huyu ninampenda sana tena sana. Na nadhani atakuwa wangu hivi karibuni,namuombea kwa MUNGU anisikilize ni nini nachomwambia”.Nilikuwa naongea haya huku nikiuangalia uso wake ambao nao ulichanua tabasamu baada ya kusikia maneno hayo. “Huyo wa tatu anaitwa nani”.Akaniuliza huku akijinyonga nyonga kwa haya\aibu.
“Anaitwa Miriam Mendrovic. Baba yake ni Rais mtarajiwa wa Urusi”.Nilimjibu na kumsababishia Miriam azibe uso wake kwa viganja vyake vya mikono kwa aibu, na alipovitoa alikuwa ametoa tabasamu la kuridhisha, ambalo kwa kila mwanaume ambaye angeliona angesema tayari kashinda.
“Mbona umeziba uso halafu umeufunua na huku unacheka?”.Nilimuuliza kama kumtega tu. “Nimefurahi kusikia maneno yako,na nimeyapenda sana”.Akajibu. “Kwa hiyo jibu lako la mwisho linasemaje kuhusu ombi langu la kuwa na wewe?”.Aliangalia chini kwa aibu tena na aliponyanyuka alikuwa anajibu sahihi. “Masai. Unajua siku ile uliponiambia maneno yale sikuamini hata kidogo,na ndiyo maana nilikuuliza kama ni wewe ndiye ulisema yale. Yaani nilichokiona cha maana ni kutoa chozi, chozi ambalo kwa yeyote angedhani ni la hasira,lakini lilikuwa ni chozi la furaha.
Nilikuwa nasubiri sana siku kama ile ijitokeze katika maisha yangu. Kila siku nilikuwa napiga magoti na kusali ili MUNGU akulete kwangu na kuniambia kuwa unahitaji kuwa nami. Hatimaye MUNGU akaitikia ombi langu hilo.
Masai, nakuhitaji kuliko kitu chochote katika kichwa changu.Nakupenda sana Masai,nakupenda kiukweli kutoka moyoni mwangu. Nipo radhi kufanya lolote ili wewe uwe wangu daima. Siwezi bila wewe na kamwe sitoweza bila wewe. Umeuteka moyo wangu pamoja na akili yangu pia. Ni MUNGU pekee ndiye ajuaye kiasi gani moyo wangu unakuhitaji,na ni MUNGU pekee awezaye kulikatisha pendo langu kwako Masai.
Frank Masai. Mimi Miriam Mendrovic,nimekubali kuwa na wewe katika kila hali itakayo tukuta,iwe shida au raha,furaha au uzuni,cheko na hata kilio,amani au vita,nitakuwa na wewe daima,nakuahidi hilo Masai. Utakuwa baba wa watoto wangu na ninaomba niwe mama wa watoto wako”.Alimaliza Miriam ambapo alinifanya niwe kinywa wazi kwa kushangaa yale maneno yaliyomtoka kwa wakati ule.
Sikuamini kama Miriam anaweza kuongea maneno yale kwani hakuendana kabisa.Ila nilijipa moyo kwa sababu hata mimi kuna watu walikuwa hawaamini kama naweza kuongea maneno matamu ya kimapenzi,na siku waliponisikia,walibaki kinywa wazi.
“Wewe ndiye mke wangu Miriam. Sitakuwa na haja ya kusema sitaki uwe mama watoto wangu,bali nakuambia kuwa wewe ndiye mama watoto wangu,nakupenda sana Miriam,na sitokusaliti katika maisha yangu,na nitakuwa na wewe katika hali zote ulizozitaja”.Niliongea hayo na kisha nilinyanyuka na kumfata pale alipo na kumshika mkono wake wa kuume ambapo tendo lililofuata hapo ni kumnyanyua pale kitini.
Aliponyanyuka nilimshika kiuno chake kwa mara ya kwanza,na yeye alipitisha mikono yake mabegani kwangu,na kisha baada ya hapo lilifuata tendo la kubusiana ambalo ndilo lilifungua rasmi mapenzi yetu.
Watu waliokuwa pale hawakusita kutushangilia kwa makofi na walioweza kupiga vigelegele walifanya hivyo baada ya kuona tendo lile,na wengine waliamua kutupa hadi hela kama pongezi,huku ule mgahawa ukibeba ghalama zote tulizotumia pale kwa kutuacha twende bila kulipa.
Mimi na Miriam tukawa wapenzi.
Baada ya kukubaliana tuwe wapenzi ndipo tuliamua kuanza kurudi darasani kwenda kumalizia kipindi kilichobaki ambapo sidhani kama kingeingia vizuri kutokana na furaha tuliyonayo. Tofauti na kipindi cha nyuma, siku hiyo Miriam alitaka tutembee pamoja wakati tunarudi darasani.
“Leo kweli umeamua, hadi tunarudi wote hivi”.Nilimtania wakati upo njiani tunarudi huku tumeshikana mikono.
“Nipo huru sasa hivi, siyo kama kipindi kile”.Alinijibu Miriam.
“Kwani kipindi kile haukuwa huru?”Nilimuuliza huku nikiwa najua wazi kinachoendelea katika familia yake.
0 Comments