Header Ads Widget

Responsive Advertisement

NIHUKUMU MWANANGU




Nihukumu Mwanangu.
Alikuwa anapita mtaani akiwa mchafu na mwenye kila sifa ambayo anaweza akaitwa tondola au masikini. Maisha yake yalijaa masikitiko pamoja na hali duni ambayo kila mtu alikuwa anashangaa kaipata wapi.
Siku zote alikuwa ni mtu wa jalalani kuokota makopo pamoja na mabaki ya chakula yaliyokuwa yanamwagwa katika majalala mbali mbali ya Jijini Dar es Salaam.
Sifa zake zilitapakaa kila mahala katika jiji lile dogo kwa kuliangalia katika ramani ila ni kubwa kupita maelezo ukiamua kulizunguka.
Wengi walipenda kumuita kichaa watoto kwa sababu kila akiwa anaona watoto,hukimbia au kujificha. Si watoto pekee,hata mama wajawazito ilikuwa vivyo hivyo.
Hakuna aliyekuwa anajua sababu ya kijana yule kuwa vile,na wengi walishamzoea hali yake ambayo kila kukicha ilikuwa kama inazidi kumtesa.
Katika pita pita zake za mihangaiko ya hapa na pale,ndipo alipita kwenye mgahawa mmoja ambao ulikuwa una TV, ambayo kwa wakati ule ilikuwa inaonesha habari zilizojiri mjini. Ilikuwa kama hakutegemea,maana baada ya kuomba omba chakula pale mgahawani na kukipata aliamua kugeuka na kutaka kupotea eneo lile,lakini ghafla wakati anaondoka alisikia sauti ya mwanamke kutoka kwenye ile TV akijitambulisha kwa jina la Grace Msafiri.
Hapo aligeuka na kupiga kelele kubwa kumuiita yule mwanamke ni mpenzi wake. Hakuna aliyefuatilia ile kelele zaidi ya watu kucheka na kuendelea na mambo yao.
Baada ya muda kidogo,ilitokea sura luningani ikijitambulisha kwa jina la Raymond Masinga,hapo mzee yule alidondosha kimfuko kilichokuwa na chakula na kupiga kelele ambayo safari hii iliwaweka watu mashakani.
"My Son. You grow up.(Mwanangu. Umekuwa)". Kijana yule ambaye alionekana kama mzee kutokana na maisha yake alipiga kelele hiyo.
Watu waliyokuwepo maeneo yale walitazama mara mbili mbili picha iliyokuwa inaonekana luningani na ya kijana yule kichaa kama wanaifananisha. Na baada ya kupata jibu kuwa kichaa yule anafanana na yule mtu anayeongea kwenye TV walimuita Mzee kijana yule na kuanza kumuuliza maswali mbalimbali hususani ya maisha yake.
ANASIMULIA KIJANA YULE.
"Naitwa Samwel Masinga. Nimesoma chuo kikuu na cha Dar es Salaam na kuchukua degree ya udaktari.
Katika maisha yangu ya ujana,niliwahi kukutana na huyu mama aliyejitambulisha kwa jina la Grace Msafiri. Mama au dada huyo,alikuwa ananipenda sana. Lakini kama mjuavyo wanaume wengi,nikawa sina mapenzi ya kweli.
Dada huyu alinipa kila kitu katika maisha yangu. Wazazi wake walikuwa wana hela za kutosha hivyo hata ada yangu ya chuo alikuwa ananilipia huyu dada.
Maisha yalikuja kubadilika pale alipopata mimba. Alikuja kwangu kwa furaha na kuniambia kuwa ana mimba yangu. Kwa ushenzi nilionao,niliikataa ile mimba katakata,kitu kilichofanya dada huyu kunilaani kwa kila kitu.
Sikujali mdomo wake. Ila maneno ya mwisho kuniambia,ndiyo yanayonitesa hadi sasa.
Aliniambia maisha yangu yote yatakuwa ni taabu na kutanga tanga mtaani kama kichaa,na nitakuja kupona baada ya kumuona mtoto huyu. Kama akifa basi sitapona kichaa hicho. Na kweli,maneno yake yanaishi.
Baada ya kumaliza chuo pale UD. Kwanza nikaajiriwa na hospitali moja binafsi. Sijatimiza hata miezi,vifaa vyao vikapotea. Mimi nikawa mhusika mkuu.
Kesi ikaenda mahakamni hadi leo haijaisha.
Baada ya kutoka tu! Mahakamani,nikarudi kwenye makazi nayoishi. Huko ndipo kichaa kilipoanzia. Moshi ulikuwa umetanda kila mahala pale napoishi. Kuja kutahamaki,ni nyumba yangu ndiyo ilikuwa inamalizikia mbao ya mwisho.
Vyeti vyangu nilivyovipata katika elimu yangu vikateketea. Vitabu,nguo na kila kitu muhimu,vyote vikaenda.Hapo niliondoka taratibu huku nikijipiga kifua kwa uchungu mkubwa,na ndipo kichaa changu kilipoanzia.
Leo nimemuona mwanangu,nimejiona nimerejea katika hali yangu.Nawaombeni mnipeleke kwa mwanangu anihukumu".Alimaliza Mzee Kijana yule kuongea na kuwaacha wasikilizaji wakiwa midomo wazi.
Kulikuwa hakuna swali tena zaidi ya kumchukua bwana Samwel na kumpeleka bafuni,ambapo alioga na kupewa mavazi nadhifu kisha safari ya kwenda anapopataka ikaanza.
Walifika katika nyumba moja kubwa na ya kuvutia,na waliposhuka walilakiwa na walinzi wawili wenye bunduki na kisha maswali kadhaa yakatiririka kuja kwao.
Kwa kila aliyemuona Samwel,hakusita kusema anafanana na Raymond,hivyo hata pale getini haikuwa shughuli sana kuruhusiwa kupita japo maswali yalikuwepo.
Samwel aliingia ndani katika jengo lile akisindikizwa na watu wawili waliyomuokota huko mtaani.
Walikaribishwa vizuri mle ndani na wafanyakazi wa pale, na kisha kupewa dakika kwa ajili ya kumsubiri yule waliyemhitaji.
Zilisikika sauti zas vicheko kati ya mwanamke na mwanaume,lakini vicheko hivyo vilikuja kukatika baada ya kufika pale sebuleni. Mwanamke ambaye ndiye mama wa mtoto alihamaki sana kwa kumuona Samwel,yule aliyeikataa mimba yake.
Huku mwanaume ambaye ndiye mwana,yeye alinamaki baada ya kuona sura yake ikiwa imekaa kochini.
"Nihukumu mwanangu. Naomba unihukumu ili niende salama huko niendako. Naomba unihukumu".Samwel alitoka pale kochini na kwenda moja kwa moja miguuni mwa Raymond na kuanza kutamka maneno hayo.
"Mbona sielewi jamani?Kuna nini hapa. Eti nyie".Raymond alikuwa anaongea kwa mshangao huku akiwauliza wale waliyokuja na Samwel.
"Huyo anasema wewe ni mwanae".Mmoja wa wasindikizaji akajibu.
"Mimi mwanae kivipi".Samwel alizidi kuuliza.
Ndipo mmoja akajitolea kuhadithia maisha ya Samwel tangu ukichaa hadi pale alipowaona kwenye TV.
"Mama,huyu ni baba yangu?".Raymond akageuza swali kwa mama yake.
"Siwezi kusema chochote kama huyu ni baba yako,ila kama ni baba yako angesipofanya yale yote".Mama naye akajibu kimafumbo.
"Kwa hiyo huyu ni nani hasa".Raymond akaendelea kukomelea maswali,wakati huo Samwel alikuwa bado kainamakama anaswali pale miguuni kwa Raymond.
"Muulize mwenyewe anataka nini hapa".Mama mtu akajibu.
"Grace mama watoto wangu,nisamehe. Nimeteseka vya kutosha. Miaka ishirini na tano kama kichaa, si kazi ya kitoto hiyo. Naomba unisamehe Grace".Samwel alitoka miguuni kwa Raymond na kwenda kwa mama mtu.
"Haya sasa. Anakujua hadi jina. Embu mama niambie kwa kunihakikishia kuhusu huyu mtu".Raymond akazidi kumbana mama yake.
Ikambidi mama akae kwenye kochi. Na Raymond akafata lakini Samwel akabaki pale chini akisubiri hukumu.
GRACE ANASIMULIA.
"Baada ya Samwel kunifukuza kwa kubeba mimba ambayo ndiyo ulizaliwa wewe. Niliamua kurudi nyumbani na kuwapa taarifa wazazi wangu. Walichoniambia ni kukusanya kilicho changu na kuondoka pale nyumbani.
Wazazi wangu walinipenda sana,na walinipa chochote nilichotaka. Lakini kitendo cha mimi kubeba mimba,kiliwahudhi sana. Shule ambayo ndiyo nilikuwa kidato cha tatu,ikawa imefika mwisho.
Nilitoka pale nyumbani huku nikiwa sijui naelekea wapi,kwa sababu kwa umri wangu,sikuwa na rafiki anayejitegemea labda nikaishi kwake. Hapo ndipo maisha yangu yakaanza kuwa mabaya.
Miezi tisa ya tumbo langu,nilikuwa nakula mabaki na vitu vya jalalani.Baridi,jua,vumbi,mvua na hali zote za hewa uzijuazo duniani,ziliishia mwilini mwangu kwa miaka saba ya umri wako.
Baada ya wewe kutimiza umri huo,ndipo nikatoka maisha ya mtaani na kwenda kutafuta kazi ambazo zitaendesha maisha yetu. Nikapata kazi mgahawani ya kuosha vyombo,wakati huo nilishasikia wazazi wangu walipata ajali na kufariki wote. Zile mali ambazo mimi ningewepo ningezirithi,zikawa chini ya baba yangu mdogo ambaye naye nilipomfata,alisema hanitambui.
Nilifanya kazi ile ya kuosha vyombo kwa muda mrefu na kwa uaminifu mkubwa kitu kilichofanya nipate ajira ya kupika katika mgahawa ule. Na hapo ndipo wewe mwanangu ulipoanza kusoma.
Mimi nikiwa naendelea na kazi ile,wewe ukaendelea kusoma kwa bidii kubwa sana hadi hivi sasa wewe ni tajiri wa Tanzania hii. Hayo ni maisha tuliyoyapitia. Na huyo ni baba yako aliyekukana".Mama Raymond au Grace akawa amemaliza kusimulia ya nyuma.
"Nihukumuni mtakavyo na ninaomba mnihukumu. Sikujua kama neno linaweza kuishi,leo hii nimeamini. Naomba mnihukumu niende salama. Ni hukumu yenu itakayonitoa kwenye hali hii ya upweke".Aliongea Samwel huku akilia.
"Hamna mwenye mamlaka ya kukuhukumu baba. Sisi ni wewe na wewe ni sisi. Nishakusamehe na nimefurahi kukuona baba yangu. Ni muda sana nilikuwa namtaka mama aniambie upo wapi hata kama ulimtenda. Hatimaye nimekuona.
Mama. Naomba umsamehe baba".Alikuwa ni Raymond akimsihi mama yake huku anamnyanyua Samwel baba yake pale chini alipokuwa amekaa.
"Kabla sijasema chochote,na mimi naomba niombe msamaha kwako mwanangu. Bado roho inanisuta sana kila nikuonapo.
Baada ya kukuleta duniani,nilikuacha pagaleni pale nilipojifungulia kwa nia ya kukuacha ili ufe au mtu yeyote akuokote. Sauti yako ya kilio pamoja na ukali wa joto la Dar es Salaam,nilirudi na kukuchukua tena. Naomba msamaha kwa kutaka kukutupa".Mama wa Raymond naye akakili kosa.
"Usijali mama. Kwa kuwa nipo hai kwa sasa,basi msamaha wako nimeupokea".Alisamehe Raymond.
Mama Raymond alimuangalia Samwel ambaye alikuwa kavalia suruali kubwa kuliko mwili wake na kuchomekea mshati mkubwa kama parachuti,huku mkanda wake ukiwa umekatika katika kama wa miaka themanini iliyopita,akatabasamu na mwisho aliangua kicheko cha nguvu na kwenda kumkumbatia Samwel,ambaye naye alilipokea lile kumbate la Grace kwa furaha.
Wale waliyomleta Samwel mmoja wapo akiwa ni mimi,tulitabasamu na kuwapongeza sana kwa hatua ile. Na mwisho wa siku tuliicha familia ile ikiwa na furaha tele.
..MWISHO.

Post a Comment

0 Comments