Header Ads Widget

Responsive Advertisement

SIMULIZI FUPI : Sijakusaliti Wewe Mume Wangu


Sijakusaliti wewe Mume wangu....

Alimfuata mumewe chumbani, muda huo watoto walikua wameshalala. Mumewe alikuwa 'busy' akisoma gazeti. 

Akamtazama mumewe kwa macho yaliyojaa huruma na huzuni, akaanza kuongea. "Mpenzi wangu, kuna kitu nataka nikiri kwako."

"Kitu gani?" Mumewe akamuuliza huku macho bado yakiwa kwenye gazeti alilokuwa akisoma. Mke akaendelea "sijawa muaminifu." Mume akatupa gazeti pembeni na kusimama huku akimkodolea macho mkewe.

Akamsogelea na kumchapa kofi, kwa mara ya kwanza katika ndoa yao ya miaka kumi alimpiga mkewe. "Kwanini wewe mwanamke, ndoa ya miaka kumi watoto watatu, na kila kitu nakupa ndio unifanyie hivi kweli??"

Mume akaendelea kufoka "Umenisaliti? , Umenidharau sana" wewe ndiye kila siku umekua ukinisisitiza nikae mbali na wanawake, najitahidi kuwa muaminifu kwako kumbe mwenzangu kwa upande wako unanisaliti kweli??"

Akiwa anataka amkabiri kwa kofi jingine, wakasikia mtu akipiga hodi mlango wa chumbani kwao, binti yao wa kwanza wa miaka 9 aitwae Maria aliingia ndani. "Baba na mama kuna tatizo?" Maria aliuliza.

"Toka, toka nje" Mumewe alimfukuza binti yake! Binti akaogopa. Mama akamwambia " Maria mwanangu nenda ukalale kesho shule, kila kitu kipo sawa ee mama." Maria akaitikia kwa shingo upande na kutoka nje.

"Ehee niambie ni nani? Ni nani ambae unavunja nae uaminifu? Nipe namba zake za simu. Leo atanitambua" mume akaendelea kufoka na kumnyang'anya mkewe simu. "Nioneshe picha na namba yake ya simu haraka"

Mkewe akaichukua simu yake kutoka kwa mumewe, akaipekua na kumuonesha mumewe "Huyu ndio mwanaume ambae nimevunja nae uaminifu" mumewe akatazama simu na kuiona picha ya Biblia. Akashangaa..akauliza nini maana ya hii?

Mkewe akajibu "Ndio sijawa muaminifu kwa Mungu wangu, nimekua busy nikikupenda wewe tu mpaka nimemsahau Mungu. Yote ni jitihada za kuwa mke bora kwako"

Mke akakaa chini. Akaanza kuongea .....

"Tulipokutana mwanzoni nilikuwa namtumikia sana Mungu wangu. Na nakumbukuka kabisa uliniambia sababu kubwa ya kunkchagua na kunioa mimi ni kwa sababu nilikuwa namtumikia Mungu"

"Nilikupenda kwa sababu na wewe ulikuwa na hofu ya Mungu, tulikuwa tukisali pamoja, tukiombea mahusiano bora na kuwa na familia yenye tija.,"

"Mungu ametujalia na baraka tele, familia ina furaha, mali za kutosha, amekupa kazi nzuri, umemaliza na PhD yako hivi karibuni tu.

Mke akamtazama mumewe kwa macho ya upole yaliyojaa huzuni kubwa. Muda huo mumewe akashusha pumzi na kuketi kochi lilikuwemo mle chumbani.

Mke akaendelea....

"Miezi ya mwanzo baada ya ndoa yetu, tulikuwa tukisali pamoja kama familia, tukienda pamoja kanisani, semina mbalimbali na masomo ya Biblia."

"Ila sasa tumekana yale maandiko yasemayo 'chagueni leo mtakaemtumikia, mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA' ..tumezaa watoto, tunawalea alimradi tu, hawamjui Mungu na wala mlango wa nyumba ya ibada hawaujui."

"Kutokana na mafanikio tumebadili hata marafiki, tumeona marafiki wampendao Mungu kama ni wasumbufu. Tumeanza kuabudu mali, pesa na mafanikio"

"Angalia tulivyo sasa, tunanyumba kubwa ila Mungu hayupo. Umeanza kunipeleka maeneo ambayo ni chukizo kwa Mungu wetu, tumeanza kunywa sana pombe, ulevi wetu umekua aibu tupu kwa watoto wetu" Mume akatizama chini kwa aibu!

"Kwa sababu ya upendo wangu kwako, nikajikuta nafanya yale ambayo unayapenda nikifikiri kuwa mke bora ni kufuata kila jambo unalolifanya. Nikashindwa kabisa kukuombea, nikafeli kukurudisha kwa Mungu. Wote tukapotea!

"Nikapotea kiasi ya kwamba nikawa na majivuno, shallow na self-centered; yote nikifikiri kwamba mimi ni mke bora. Ila huyu sio mimi. Nimebadilika sana kutoka yule mwanamke uliyeniona kwa mara ya kwanza. Wote tumebadilika mno na tumepotea katika kiza kinene.

"Vyote hivi, Nyumba nzuri, magari, chakula kizuri tunachokula, pesa tulizonazo vimetufanya tumsahau aliyetupa. Mimi si kitu bila ya Mungu na nimejikuta na aibu kuu kwa usaliti huu juu ya Mungu wangu. Ndio nimemsaliti Mungu."

"Tumeanza kuwa na migogoro isiyokwisha ndani ya ndoa, yote haya ni kwa sababu MUNGU hayupo kati yetu. Tunaendesha upendo wetu sisi kama sisi na tunakolekea tutafeli kabisa!!

"Nataka nirudi kuwa mwanamke yule uliyenikuta mwanzo. Mwanamke mwenye hofu ya Mungu. Nimeikumbuka mno amani ya Mungu wangu. Nimekumbuka kumuabudu yeye. Nimekumbuka kusali na wewe Mume wangu. Ni ipi faida kwangu kuwa na ndoa nzuri lakini nimpoteze Mungu wangu? Ninarudi kwa Mungu."

Akaendelea.....

"Mwanamke anaenyenyekea na kuomboleza kwa MUNGU ndie atakaekuwa mke bora na mama bora kwa watoto wake. Apatae mke amepata kitu chema na amepata kibali kutoka kwa Mungu, sitaweza kukupa kibali kama sitarudi kwa Mungu wangu. Nataka maisha yangu na Mungu yarudi. Nataka Mungu arudi katika familia yetu!

Mke akamaliza kuongea huku machozi yakimtoka. Mume akainuka kutoka kwenye kochi, huku machozi yakimrenga akamfuata mkewe, akambusu kwenye paji la uso, akamkumbatia, akamfuta machozi na akamwambia;

"Nisamehe mke wangu, nisamehe kwa sababu mimi ni kichwa, na kichwa kikipotea na mwili hufuata kupotea kwa kichwa. Ulichagua kuolewa na mimi kwa sababu uliiona hofu ya Mungu ndani yangu. Hata mwenyewe nimekumbuka sana ule uwepo wa Mungu ndani yangu"

"Ndoa isiwe kizuizi katika njia yetu kumfuata Mungu. Mawazo kwamba unanisaliti yaliuralua moyo wangu vipande vipande. Sasa nashindwa ku-imagine Mungu anajisikiaje sisi tunavyokua sio waaminifu kwake"

"Mungu ametubariki na vyote hivi, ni kweli lazima tumrudie yeye. Namimi nataka kurudi kwa Mungu, nataka zaidi kutoka kwa Mungu wangu kuliko haya mambo ya kupita ya duniani hapa. Nataka mungu wa ujana wangu!"

"Samahani kwa kukuchapa kibao, ni hasira za kudhani unanisaliti kumbe hukua unamaanisha usaliti nilioufikiri mimi!"

Usiku ule walisali na kutubu pamoja. Wakaanza kuwafundisha watoto wao ukuu wa Mungu, familia ikawa na furaha na Mungu akarudi katika familia yao!

M W I S H O .

Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani.
Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato. Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake.
Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo."

Post a Comment

0 Comments