Header Ads Widget

Responsive Advertisement

TONE LA MWISHO LA UVUMILIVU



SIMULIZI FUPI : TONE LA MWISHO LA UVUMILIVU


Naitwa Lusubilo Mwaipaja, marafiki zangu wengi walizoea kuniita kwa ufupi. Waliniita Lusu! Niliyafurahia maisha sana nikiwa mjini Mbeya na familia yangu kwa takribani miaka ishirini na nne, mama yangu alikuwa akinieleza mara kwa mara kuwa watu wengi wananipenda kwasababu ya upole na ukarimu wangu! “Lusu, angalia upole wako usizidi kipimo inaweza kukugharimu siku moja” Mama aliwahi kunipa onyo ambalo sikujua kabisa alikuwa anamaanisha nini. Hakika! Sikujua anachomaanisha kwa wakati ule kwa sababu kila mtu katika jamii alinipenda na kuniheshimu kwa sababu ya huohuo upole. Kivipi mama ananieleza kuwa ipo siku upole wangu utanigharimu?? Sikutilia maanani.

Giza likachukua nafasi, mchana ukaipokea nafasi hiyo. Ikawa usiku ikawa mchana siku zikazidi
kusonga mbele. Hatimaye ukakuchwa ule usiku ambao uliuleta mchana wa kukutana na Neema. Msichana ambaye na yeye kama ilivyokuwa kwa mama alinisifia kwa upole wangu na ukarimu. Lakini yeye aliendelea kunijaza sifa kila siku hatimaye jicho langu likamtazama katika namna ya pekee. Mke mtarajiwa! Sikujiuliza mara mbilimbili siku ambayo niliamua kumtamkia kuwa nahitaji kuwa naye katika mahusiano ya kimapenzi. Mahusiano ambayo yalidumu kwa muda mfupi kabla sijayapeleka katika uchumba, mama alikuwa wa kwanza kumfahamu Neema kisha baba. Hatimaye nami nikajitambulisha kwao.

Nikapokelewa kwa mikono miwili!! Wazazi wake wakanipenda!! Safari ya mapenzi yetu ikaongezeka kasi na hatimaye tukaoana. Siku ile ya harusi mama yangu alinikumbatia kwa muda mrefu kupita ndugu zangu wote. Alidondokwa na chozi ambalo nilidhani kuwa lilikuwa la furaha lakini la! Nayakumbuka maneno ambayo alinieleza kwa sauti ya kunong’ona.

“Lusu mwanangu, hakuna mwanamke anayekupenda duniani zaidi ya mimi mama yako, kama ingekuwa ndani ya uwezo wangu ungeishi nyumbani daima. Nyumba yenye mapenzi ya dhati kwako, ila nenda mwanangu, nenda umekuwa mtu mzima sasa…..” Nikauacha rasmi mji wa Mbeya, mji ambao ulinipenda sana. Nikaondoka mimi na Neema. Tukahamia Morogoro, ambapo nilikuwa nimepata uhamisho wa kuhamia kule kama mwalimu!

****


Awali Neema alikuwa akinionyesha mapenzi ya dhati sana. Jambo ambalo halikuwa geni, nililitegemea vilivyo. Niliamini kuwa kama kweli mama ananipenda kuliko wanawake wote basi Neema ni wa pili katika orodha ile. Miezi mitatu pekee ya ndoa niliishi kwa amani ya moyo. Mwezi wa nne ukaanza kwa mauzauza. Mauzauza ambayo hadi leo hii akitokea mtu ananiomba ushauri juu ya mwanamke gani wa kuoa. Sitakuwa na la kumjibu, zaidi atakuwa amenipandisha jazba tu! Neema alianza kulalamika kuwa amechoka kukaa nyumbani. Anataka nimtafutie naye kazi ya kufanya ilimradi tu asiwe mtu wa kushindia nyumbani.

Nilishangazwa na ombi hili, wakati awali tulipanga vinginevyo. Nikaamua kuuvunja ukimya. “Neema mke wangu, kwani mimi na wewe  tulipanga nini mwanzo? Si tumekubaliana tupate mtoto kwanza nd’o hayo yatafuata.” Nilimuhoji. Akanitazama kwa jicho kali, kisha akasimama kwa ghadhabu akatoa msonyo mdogo wa kuonyesha kukereka, akaingia chumbani akaubamiza mlango. Looh! Ama kweli upole wangu, upole wangu… lakini mama alinikanya!! Nikasimama na kuelekea chumbani, nikamkuta amejifunika shuka gubigubi huku akitupa miguu huku na kule. Nikajongea kitandani nikaanza kumbembeleza…. Nadhani ule nd’o ulikuwa mwanzo wa Yule binti kuanza kuiendesha akili yangu. Nilimweleza kuwa kama kweli ana nia ya kufanya kazi basi ageuke tuzungumze. Neema akageuka huku akipekecha macho yake, ili kulazimisha machozi. Mapenzi bwana! Ndicho nilichowaza kwa wakati ule… kumbe yale hayakuwa mapenzi nilijidanganya tu!

*************

“Haya unataka kazi gani mke wangu!” Neema akaachia tabasamu pana akanikumbatia na kunibusu, kisha akanieleza kuwa anataka kuwa anaenda dar kununua vitenge na nguo za wanawake kisha atakuwa anakuja navyo Morogoro kuwauzia na kuwakopesha wanawake wa mtaani akianza na waalimu ambao naishi nao pale nyumba za shule. Nikalifikiria wazo lake kisha nikamruhusu huku nikimkumbusha kuwa asisahau kuwa huku Morogoro ameacha mume anayempenda sana. Furaha ya Neeema ikarejea. Akapiga mahesabu yake, nikampatia kiasi cha pesa akajipanga kwa  safari baada ya siku mbili! Nafsi yangu ilikuwa imemruhusu lakini kiukweli ni kwa shingo upande!!

Siku ikafika na mke wangu kipenzi akaondoka akiniachia manung’uniko nafsini!! Akaenda jijini Dar es salaam! Siku moja baada ya Neema kuondoka, mwalimu Jackson ambaye alikuwa ni mwalimu mkuu na yeye akaaga kuwa anaenda baraza la mitihani Dar. Nikamweleza kuwa akipata muda wa kuonana na Neema basi kuna zawadi nahitaji kumpa ampatie. Mwalimu akanieleza kuwa hatapata muda kwa sababu anafika na kuondoka!! Lakini pia siku moja kabla Neema hajaondoka Mwalimu mkuu msaidizi naye aliondoka shuleni na sikujua wapi alielekea. Sikuwa na mashaka yoyote…. Niliamini Neema ni wangu peke yangu!!

AWALI mke wangu alisema kuwa atatumia siku zisizozidi tatu kumaliza kile kilichompeleka Dar. Japokuwa hazikuwa siku nyingi sana lakini kwangu mimi ilikuwa ni kama mwaka mzima, nilikuwa nimemzoea sana Neema wangu. Nilimpenda sana mke wangu! Siku ya tatu ilipofika majira ya jioni nilitegemea kupokea simu kutoka kwake. Na sikudhani ingekuwa simu inayoleta ujumbe mwingine tofauti na kunieleza kuwa yupo nijiandae kumpokea siku inayofuata. Lakini haikuwa kama nilivyodhani… Neema akanieleza kuwa mama yake mdogo wa Dar es salaam anaumwa hivyo ataenda kumsalimia kwa siku mbili kisha ndipo atageuza kurudi Morogoro. Nilitamani kutia neno la kipingamizi lakini ningeonekana mwanadamu wa ajabu sana. Ndugu wa mke wangu anaumwa halafu sitaki aende kumsalimia. Nikakubali japokuwa kishingo upande tena. Baada ya kukata simu nilijilaza kitandani kwa muda kidogo kisha nikaingia bafuni ili nijimwagie maji.



Hii ilikuwa kawaida yangu tangu utotoni, mara nyingi nikiwa najimwagia maji bafuni ni muda huohuo najikuta anakumbuka vitu Fulani ambavyo nilikuwa nimevisahau tayari. Na siku hiyo nikakumbuka kuwa Neema wakati tukiwa Mbeya alinieleza kuwa yeye na mama yake mdogo hawapatani hata kidogo na hakuna ambaye ana mawasiliano na mwenzake. Sikumuuliza sana nini chanzo cha ugomvi wao nikalipokea kama lilivyo. Ya ndugu waachie ndugu!! Sasa kivipi leo hii anasema anaenda kumuuguza adui yake? Dah! Nilitamani kupiga simu nimuulize lakini nikapiga moyo konde nikalipuuzia hilo! Pia Neema alisema akiwa Dar hataki kuwasiliana na mtu yeyote Yule anachukua mzigo na kuondoka. Imekuwaje sasa akawasiliana na mama mdogo? Moyo uliniuma sana ndugu msikilizaji, nikajua moja kwa moja mwanamke niliyemkabidhi moyo wangu wote kwa mara ya kwanza alikuwa ananidanganya…… Kwa nini sasa ananidanganya? Lazima ana sababu zake!! Nikajikunyata kitandani kama kinda la ndege lisokuwa na mama. Usingizi ukanipitia. Nikalala bila kula chochote!!

Nilikuja kushtuka majira ya saa tano na nusu usiku. Nikaitazama simu yangu. Neema alikuwa amenitumia ujumbe tatanishi. Umeme unasumbua sana hapa kwa mamdogo, simu haina chaji na muda wowote ule itazima…. Usiku mwema mume wangu nakupenda na nimekumiss sana” Ujumbe ule ulinifanya nitetemeke, na kwa mara ya kwanza katika maisha yangu ya ndoa nikajikuta napatwa na hasira sana. Neema alikuwa akinidanganya tena!! Anazo simu mbili tena kwa pamoja tunakiri kuwa zinaongoza kwa kutunza chaji, ina maana alikuwa anazichezeaje hadi zikaishiwa chaji kwa pamoja. Usingizi haukunipitia tena hadi kunapambazuka. Nikapiga simu ofisini kuwa sitaenda kazini najisikia vibaya. Nikajibiwa kuwa nijikaze tu niende maana mimi ndiye mwalimu wa taaluma na mwalimu pekee ninayeweza kuisimamia shule kwani mkuu wa shule na makamu wake bado walikuwa hawajarejea.


 Kusikia jibu hilo kuwa mkuu wa shule na makamu wake hawajarejea, nikapata tumaini kiasi Fulani kuwa naweza kujua iwapo Neema ananiongopea ama la! Nikampigia simu mwalimu mkuu na kumsihi anisaidie sana jambo moja. “Tafadhali mkuu nahitaji uwasiliane na mke
wangu, nahitaji tu kujua yu wapi. Najua wewe ni mtu mzima tena mshauri wangu wa karibu utajua ni maneno gani utatumia kumtambua yu wapi na kwa sababu gani, ukirejea Moro tutazungumza kwa kina…” nilimsihi akanikubalia. Baada ya masaa mawili akanipigia na kunieleza kuwa Neema alikuwa kwa mama yake mdogo ambaye ni mgonjwa kwa bahati nzuri ni jirani tu na pale alipokuwa yeye. Maeneo ya Mwenge!!


Majibu ya mkuu wa shule yakanifanya upesi niende kwenye kioo na kujitazama jinsi nilivyokuwa nimenuna, nikajipigapiga makofi na kisha nikatabasamu. Nikaitazama picha ya Neema ukutani siku ile ya ndoa yetu. Nikaamini kuwa sijafanya makosa kumuoa. Na hapo nikajiandaa na kwenda kazini!! Baada ya siku mbili Neema akarejea Morogoro akiwa na mzigo aliosema kuwa anaenda kuuchukua Dar. Siku moja baadaye mkuu wa shule na yeye akarejea! Sikuhitaji kumueleza tena wasiwasi wangu juu ya Neema, nilijiona mjinga sana na nitaonekana nina wivu wa kipuuzi. Sikuzungumza naye, badala yake nilizungumza na mke wangu juu ya hali ya mama mdogo. Akanieleza amemuacha akiwa na nafuu sana tu! Kisha akaelezea juu ya tatizo la umeme linalokabili baadhi ya maeneo Dar es saalam. Na hapo akatokwa na kauli ambayo ilinivuruga upya. Yaani kule Tandika anapokaa mama mdogo sio sehemu ya kuishi kabisa.. umeme unakatika hadi siku tatu…”

Akili ikafyatuka!!


Mkuu wa shule alisema kuwa ameenda kuonana na mke wangu maeneo ya Mwenge ambapo mama yake mdogo ambaye ni mgonjwa alikuwa anaishi. Mke wangu anasema mama yake mdogo anakaa Tandika! Sikuwa mwenyeji sana Dar es salaam lakini sio ugeni wa kutojua umbali kati ya Tandika na Mwenge. Neema mke wangu ananidanganya!!Nilijiwazia kichwani mwangu… Kisha nikajiuliza kama kweli ananidanganya ni kwanini ananidanganya? Niliumia sana, nililia sana ndugu msikilizaji……. Mwanamke wa maisha yangu anachezea hisia zangu!!

******************


USIKU Neema alilala fofofo sana. Safari ya kutoka Dar es salaam kuja Morogoro ilikuwa safari ya masaa matatu tu, sikutegemea safari fupi kama ile ingeweza kumchosha kiasi kile mke wangu. Lakini ule upole ambao mama yangu alinieleza ulikuwa kikwazo nikawa mpole pia katika hili. Lakini sikuweza kulala hadi niliponyanyuka na kupekua mkoba wa mke wangu, mwanamke bingwa wa kutunza tiketi hata kama ni safari fupifupi za mjini. Nilitaka kujua alisafiri na basi gani hadi achoke kiasi kile. Nilipekua kila kona! Hapakuwa na tiketi. Mke wangu kuna kitu alikuwa ananificha! Nililala jirani naye lakini sikumgusa kabisa nilihisi kuna utofauti baina yetu, lile joto lake mwanana la kike sasa nililiona kama moto unaounguza. Nikaelekea upande mwingine na yeye akiwa anakoroma huku akiwa anatazama upande wake.
Asubuhi niliwahi sana kutoka nyumbani tofauti na siku nyingine. Sikutaka kuonana na mke wangu kwa sababu nilikuwa najisikia kukasirika. Amakweli mwone mtu ameng’ara na kila muda analo tabasamu usoni, usitamani kuwa kama yeye hata kidogo. Hujui kama lile ni tabasamu kutoka moyoni ama la kuzugia tu!! Sikuingia darasani kufundisha bali nilikaa ofisini nikitafakari ni kipi nifanye ili kuujua ukweli, ni kipi kilikuwa kinaendelea katika ndoa yangu!
Nilitaka kumpigia mama simu lakini nilihisi ni udhaifu wa hali ya juu, yaani miezi minne tu katika ndoa naanza kuonyesha kuzidiwa? Hapana! Nikapuuzia hilo.Nikatafakari ni nani rafiki wa dhati ambaye naweza kuzungumza naye jambo hili. Hata huyo sikumpata… Nikaitazama pete kidoleni mwangu nikakumbuka jinsi mama alivyolia kwa hisia kali huku akiwa amenikumbatia. Siku ile ambayo nilikuwa nafunga ndoa na Neema. Nikaanza kuipata mana ya chozi lake. Pia nikakumbuka maneno yake juu ya upole wangu! Naam! Nikapata jawabu juu ya namna ya kukabiliana na jambo ambalo lilikuwa mbele yangu.

Natakiwa kuuvua upole wangu mara moja, la sivyo nitakufa huku nikiwa ninatembea barabarani. Na pale nikafunga ofisi yangu, nikatoweka pasipo kuomba ruhusa yoyote. Kwa mara ya kwanza nikarejea nyumbani bila kutoa taarifa yoyote. Nilipoifikia nyumba niliyokuwa naishi, nilimsikia mke wangu akiongea kwenye simu katika namna ya kusisitiza sana. Tatizo alikuwa anaongea kwa kabila yao! Kabila ambayo sikuwa naelewa zaidi ya salamu tu! Ila kwa sababu kile ni kibantu walau neno mojamoja ningeweza kukisia maana yake. Kuna maneno mawili yalijirudiarudia sana. “"Ntumbo nuumile…. Ntumbo nuumile"..” Nilikisia kuwa anazungumzia juu ya maumivu ya tumbo na si vinginevyo. Nikatambua wazi kuwa nikiingia ndani atapagawa sana kwa sababu hajanitegemea kabisa. Nilichofanya nikarudi hatua nyuma kisha nikaondoka zangu!


Nilipofika mbali nikampigia simu, kwa mara ya kwanza simu yake ilikuwa inatumika. Nilipopiga mara ya pili ikapokelewa., “Shikamoo mume wangu… nd’o tabia gani kuondoka bila kuniaga? Jamani Lusu” alizungumza kwa sauti ya kitotototo iliyojaa maringo, kana kwamba alikuwa hajaamka kabisa. “Hujaamka hadi wakati huu mpenzi” nilimuuliza, lakini kitendo cha kumuita mpenzi kikanisulubu sana nafsi. Sijaamka hata, si unajua tena uchovu wa safari..” aliendelea kuniongopea mwanamke niliyeapa naye akaapa kunipenda kwa shida raha. Nilidondosha chozi hadharani! Bahati ilikuwa upande wangu hapakuwa na watu wengi barabarani, nikawahi kujifuta. Nikamweleza kuwa nilikuwa narejea nyumbani kwani sikuwa najiskia vizuri pia…. Kisha nikakata simu!!
Nilifika nyumbani na kuingia ndani, nikamkuta mke wangu amejifunika gubigubi, nilipomuita mara ya kwanza na ya pili hakunijibu, kisha mara ya tatu akajibu kama mtu anayetokea usingizini. Ananidanganya kuwa alikuwa yu hoi kwa usingizi! Nilijiwazia. Nikaelekea sebuleni nikawasha runinga kisha nikazama katika dimbwi la mawazo. Nikiwa katika mawazo yale nikamkumbuka rafiki yangu ambaye ni kabila moja na mke wangu. Nikampigia simu alipopokea nikamuuliza kwa sauti ya chini nini maana ya Ntumbo nuumile. Akanieleza kuwa maana yake ni ‘Tumbo linakata’. Nikapigia mstari zile hisia zangu! Kwa sababu mke wangu alijifanya amelala, nami nikajilaza lakini sikupata usingizi kabisa. Moyo wangu ulikuwa unauma sana, mapenzi yalikuwa yananitesa mimi.


Baada ya kuamka mke wangu alienda kuoga. Alipoingia bafuni na mimi nikatumia fursa ile kuichukua simu yake ya mkononi nikatazama namba alizowasiliana nazo, nikazinukuu namba mbili za mwanzo kisha nikarejea sebuleni. Sikukaa sana nikaondoka. Kwa kutumia huduma ya vibanda vya simu nikawasiliana na zile namba walau niweze kujua ni sauti za akina nani. Simu ile ya kwanza ilinikata maini na kunifanya nibadilike na kuwa kiumbe mwingine kabisa. Simu ya kwanza ilikuwa ni sauti ya mkuu wangu wa kazi, mkuu wa shule ambayo nilikuwa nafundisha. Nikajikaza na kupiga ile namba nyingine. Naam! Ilikuwa sauti ya mwalimu mkuu msaidizi…. Watu ambao nafanya nao kazi sehemu moja, wakuu wangu wa kazi, wakubwa wangu kiumri, washauri wangu! Ati! Wanahusika pia katika kunipondaponda moyo wangu! Ni kitu gani wanawasiliana na mke wangu… ni kitu gani kinaendelea? Nilishikwa na kizunguzungu sana lakini ilikuwa bahati tu sikuanguka! Nilichanganyikiwa!!



**************

NILIONDOKA pale huku nikiwa naonekana kuwa mtu na timamu zake lakini waendesha pikipiki kadhaa nd’o waliweza kugundua kuwa sikuwa hali ya kawaida kabisa. Nilipigiwa honi sikusikia, pikipiki moja ikanikosakosa. Niliyasikia matusi juu yangu! Hapo nikagundua kuwa nilikuwa nimepagawa! Ili kujiepusha na hatari zaidi nikauendea mti na kuketi chini yake. Kichwa kilikuwa kinauma katika kiwango cha juu sana. Nilipumzika kwa dakika kadhaa huku nikiilazimisha akili yangu ikae sawa ilimradi tu niweze kuwa makini barabarani. Nikiwa pale chini ya mti ule wazo la ghafla lilinipitia, wazo la kuwavamia mkuu wa shule na makamu wake na kuwauliza ni kitu gani haswa walikuwa wanafanya na mke wangu mbali na upeo wa macho yangu. Nikayafumba macho yangu na kuzikumbuka zile kauli tata kati ya mkuu wa shule na mke wangu, Ni pale mmoja aliposema kwa mama mdogo ni Tandika huku mwingine akisema ni Mwenge. Nikajikuta naufikiria ukweli ambao sikutaka uwe ukweli. Yawezekana Neema wangu alikuwa yu pamoja na mkuu wa shule wakati nampigia simu na kumsihi aonane naye, na iwapo walikuwa pamoja basi baada ya kukata simu walicheka kwa pamoja kisha wakagonga mikono yao, na huenda walifikia hatua hata ya kunitukana!!


Mawazo haya yaliniumiza, na kisha wazo la mwisho kabisa likanifanya nianze kutokwa damu puani kama ilivyokuwa kawaida yangu nikighafirika kupita kawaida!! Wazo kwamba mke wangu kipenzi ameshindwa kuwa mkweli katika ndoa na sasa yu katika mahusiano ya kimapenzi aidha na mkuu wa shule ama makamu wake!! Mapigo ya moyo yalizidi kasi yake wakati napambana na damu iliyokuwa inavuja kutoka puani. Bahati nzuri nilikuwa na kitambaa, nikafanikiwa kukabiliana nayo. Simu yangu ya mkononi iliita wakati huo damu zikiwa zimekata tayari. Kutazama jina katika simu lilisomeka ‘MKE WANGU KIPENZI’…..

Chozi lilinitoka msikilizaji!! Mara ya kwanza sikupokea lakini ile mara ya pili niliipokea huku nikilazimisha uchangamfu. Neema mke wangu alikuwa na kisu kingine kikali tu cha kunichoma. Naam! Akanieleza eti ya kuwa ule mzigo aliouziwa ni feki hivyo ni muhimu arudi upesi Dar maana aliambiwa kuwa zikipita siku nne hajarudisha mzigo kama una matatizo basi hautapokelewa tena. Tutazungumza nikirejea nyumbani mke wangu” nilimsihi kwa upole kama ilivyokuwa kawaida yangu. Hapana mume wangu, naomba tu nikimbie sasa hivi, sasa hivi saa sita natumia masaa matatu kufika kule halafu kesho asubuhi narejea tafadhali.” Alisisitiza Neema. Akili yangu ilikuwa haipo sawa bado nikajikuta tu namwambia aende! Akashukuru huku nikiyasikia mabusu kedekede ambayo alinitumia kisha akasema ananipenda sana kuliko wanaume wote. La haula! Neema alikuwa shetani anayeua polepole!!



**** Baada ya kutoa ruhusa ile bila kujua ni kwa nini naitoa, wazo la ziada likakikumba kichwa changu. TONE LA MWISHO LA UVUMILIVU!! Ni hiki nilikifikiria, na kisha nikasimama kiujasiri na kusema kuwa liwalo sasa na liwe. Ama zangu ama zao! Nikanyanyua simu yangu na kumpigia mwanamke anayenipenda kuliko wote duniani! Mama Lusu mama yangu mzazi! Ama kwa hakika mtoto kwa mama hakui… ile natoa salamu tu, mama akaniuliza iwapo nilikuwa naumwa. Nikakataa! Akasema yawezekana kweli siumwi lakini nina hasira! Nani kanikasirisha? Lilikuwa swali jingine. Ule upendo wa mama ukanifanya nizidi kujisikia vibaya. Nikatamani kumweleza kila kitu lakini niliona muda hautoshi kabisa kwa sababu kuna jambo la haraka sana nilitakiwa kulifanya. Nikatamani kumweleza kwa kifupi lakini asingeweza kunielewa!! Nikiwa sijajua nini cha kusema ghafla mama akaniambia. “Lusu kama ni mke wako amekuudhi, chunga mkono wako usije ukapiga mtoto wa watu. Jichunge kabisa, na kama hasira zako hauwezi kuzizuia nakuomba upande gari urudi Mbeya! Sikutaka kuendelea kuzungumza na mama, nikamuaga na kukata simu.

 Nilipokata simu ya mama, mara ikaingia simu ya mkuu wangu wa kazi. Akanipa taarifa kuwa niende shuleni kwa sababu amepata dharula anaondoka mara moja! Wakati nazungumza naye mara nikaliona gari lake, jirani na maeneo ya Msamvu likiwa limeegeshwa! Bahati mbaya iliyoje, gari lake lilikuwa na vioo vinavyoonyesha hadi ndani. Bora vingekuwa vyeusi nisiweze kushuhudia nilichokishuhudia!! Neema mke wangu wa ndoa katika gari ya mkuu wa shule!!


Nikajikuta nashindwa kuzungumza, nikaikata simu, nikajaribu kusimama miguu haikuwa na nguvu hata kidogo. Hasira ilikuwa pomoni!! Yaani mke wangu tena huenda anayo pete ya ndoa kidoleni ananifanyie ushenzi kama huu. Miezi minne tu ya ndoa!! Swali likawa moja, kuna nini kinaendelea kati yao! Kama ni wapenzi mbona muda mwingi tu mimi nipo ofisini, kwanini wasikutane hapahapa Morogoro maana maeneo ya kukutania ni mengi tu!! Kwanini wasafiri!! Na bila shaka hii si mara ya kwanza kusafiri pamoja, kitendo kile cha kukuta mke wangu akiwa hana tiketi aliporejea kutoka Dar ilikuwa ni ishara tosha. Na hapohapo nikaukumbuka uchovu mkali aliokuwanao mke wangu usiku ule? Sasa kama alisafiri katika gari nzuri kiasi hiki ilikuwaje akachoka kiasi kile! Loh! Mkuu wa shule kuna kitu alimfanyia mke wangu?? Nikajaribu kusimama tena…. Sasa niliweza kusimama kiujasiri nikiwa imara kabisa……



 Nilichoamua kilihamasishwa na ule usemi maarufu wa zama hizo. Ngoja ngoja huumiza matumbo… na heri nusu shari kuliko shari kamili. Nikaongezea na ule usemi wa kitemi, LIWALO NA LIWE!! Nikaamua kwenda pale lilipokuwa gari la mkuu wa shule, niliuona waziwazi mwili wangu ukitetemeka maeneo ya mikononi na misuli ya shingoni ilinikakamaa. Nikajaribu kumeza mate lakini hayakupita. Sikujua nikifika nitafanya nini lakini nilihisi nitafanya kitu ambacho hakuna mtu ambaye ananifahamu angeweza kufikiria kuwa naweza kukifanya. Macho yangu yalikuwa yameelekea sehemu moja tu! Alipokuwa mkuu wa shule na mke wangu!!

Ama!! Mke anauma jama!! Mke anauma, mke si sawa na hawara, mke si sawa na mpenzi tu mnayeishi kimazoea. Mke ni kitu kingine! Maumivu niliyoyapata, ewe msikiliza uliye katika ndoa wayajua hasahasa ukihisi mwenza wako anakufanyia jambo baya nyuma ya kisogo chako na usijue kinachoendelea!! Ikiwa tu unahisi kusalitiwa unaumia kiasi hicho, je mimi niliyemuona mke wangu akiwa na mkuu wangu wa ngazi!! Nilitamani moyo utoe kifuani kwa muda uwe nje ya mwili wangu niumwagie maji ya baridi huenda ungepoa!! Sasa haukuwepo ule upole tena, nilikuwa nimechanganyikiwa kwa jazba.

Wakati navuka barabara huku macho yangu yakiwa bado sehemu moja tu. Hatimaye macho yangu yakagongana na yale ya mke wangu!! Ile taharuki aliyoipata sina maneno ya kukuelezea uelewe! Na hapo akawa amenizidishia hasira! Nilipopiga hatua mbili mbele, hasira zangu zikaishia pale ndugu msikilizaji. Nilijikuta hewani juu juu kisha nikatumbukia mtaroni, kichwa kilijibamiza kwenye kuta za mtaro. Uso wangu ulikuwa unaelekea juu na niliona jinsi mke wangu alivyokuwa shetani. Alizuiwa na mkuu wa shule asije kutazama nini, nikamuona akirudishwa garini. “Nakulaani Neema, nakulaani wewe na kizazi chako… nakuombea utasa, nakuombea umasikini, nakuombea msongo wa mawazo, uishi kama kivuli uwe mtu wa kukimbia kila siku iendayo kwa Mungu, nakuombea huzuni we mwanamke….”

Nilijikuta nikijikaza kuongea ili Neema anisikie lakini mbavu zilikuwa zinauma sana. Baada ya muda kidogo kiza kikatanda!! Naam! Fahamu zangu zikakomea pale, mambo yaliyoendelea nilikuja kuhadithiwa tu nikiwa hospitali. Siku tatu baada ya kupata fahamu. Majira ya saa nne usiku nd’o muda ambao fahamu zilirejea baada ya siku tatu kupita. Nilijikuta na bandeji gumu kichwani mwangu, mbavuni pia nilikuwa nimefungwa bandeji.



Nilijhisi nipo peke yangu lakini nilipojitikisa kidogo na kuguna kwa maumivu nikasikia mtu akiniita. “Lusubilo mwanangu kipenzi!!” Ilikuwa sauti ambayo kamwe nisingeweza kuisahau, sauti ya mama yangu kipenzi.. mwanamke anayenipenda kupita wote duniani.
 Mama, mama… Neema wa kunifanyia vile mimi? Eeh! Mama Neema kweli? Naomba unisaidie kunivua hii pete mama siitaki tena na sitavaa tena pete” nilimsihi mama. Lakini mama hakuwa na papara katika kunijibu.  Alivuta pumzi kisha akanieleza kwa sauti ya wastani. “Lusu, pembeni yako yupo mwanamke anayekupenda kupita wote maishani. Na hata  pasipo na maisha! Sahau yaliyopita sasa, watakusaliti wote lakini sio mimi mama yako. Na nd’o maana nilikwambia kama una hasira urudi Mbeya” “Mama uvumilivu ulinishinda, tone la mwisho la uvumilivu lilidondoka nisingeweza kuvumilia zaidi ya pale… kwanza yupo wapi?” “Pumzika mwanangu, si wakati wake!!”



BAADA ya kupata nafuu, mguu wangu mmoja ulikuwa umevunjika nilikuwa natembelea magongo, mbavuni nilikuwa na bandeji na kichwani pia!! Kadri nilivyoendelea kupata nafuu nikiwa mjini Mbeya, hatimaye mama akanieleza juu ya ushenzi wa yule mwanamke. Kumbe alikuwa na mahusiano na mkuu wangu wa kazi, na aliyemkuwadia alikuwa ni makamu wake. Katika rukaruka zao mkuu wa shule akamjaza mke wangu mimba. Na wazo la biashara aliloleta mke wangu ni ili apate upenyo wa kwenda Dar kutoa mimba. Jaribio la kwanza kwa kutumia kidonge likashindikana, nd’o akapatwa na maumivu ya tumbo wakaamua kurejea tena Dar kujaribu njia nyingine. Kwa habari nyepesi nyepesi tu ni kwamba ile haikuwa mimba ya kwanza kutoa. Nilitabasamu huku machozi yakinitoka! Nilichomwambia mama ni kitu kimoja tu. Na tuache maisha yaendelee, lakini hata maisha yaendelee vipi katu sitakuja kushiriki mchezo uitwao NDOA.


Si mchezo mzuri hasahasa kwa mchezaji kama mimi ambaye nilipenda kwa moyo wote. Mama hakunipinga!!! Nikajiuguza hatimaye nikapona! Mama alihisi nitaubadili uamuzi wangu siku moja, ila hadi naamua kuyasimulia haya ili nawe ujifunze!! Wadogo zangu wawili wameoa na nilishiriki ipasavyo harusi zao, marafiki zangu wengi tu wameoa na hawa walinitumia kadi za michango! Jamaa zangu wengine wapo katika mipango ya harusi. Hawa waache waoe tu! Ndoa iliyotaka kunitoa roho!! Sitaki kuisikia. Nilipata bahati ya kukutana na Neema jijini Dar es salaam, walau nami nikapata kumshukuru Mungu kwa kukisikia kilio changu. Alikuwa hajaolewa tena, alinisihi tuwe pamoja tena nikamwomba abadilishe mada ili amani iendelee kutawala! Tangu hapo sikumuona tena na ni heri kwa sababu sihitaji kuonana naye mwanamke yule mwenye roho ya kishetani!!

JIFUNZE!
  • Mapenzi yana chungu na tamu, waweza penda usipopendwa, na mapenzi yana raha na karaha!!!

MWISHOOO!!

Post a Comment

0 Comments