Header Ads Widget

Responsive Advertisement

TAREHE 11/03/2014




Nilikurupuka kutoka kitandani, jasho lilikuwa likinitoka kwa sababu ya joto kali, simu yangu iliyokuwa ikilia ndio iliyonifanya kuamka na kuanza kuangalia huku na kule. Simu iliendelea kulia, kwa harakaharaka nikaichukua na kukiangalia kioo, ilikuwa simu kutoka kwa bosi wangu.
Kwanza nikashtuka, haikuwa kawaida bosi kunipigia simu asubuhi namna ile, kabla sijaipokea, nikaanza kufikiria kama nilikuwa na majanga niliyoyafanya jana, sikuwa na majanga yoyote yale, nikaipokea simu.
Nilianza kuongea na bosi, akaniambia kwamba kutokana na matumizi makubwa ya fedha ndani ya kampuni yetu, baadhi ya wafanyakazi walikuwa wakipunguzwa kazini, janga hilo likanikuta na mimi. Sikufichi, nilijisikia vibaya moyoni, sikuamini kabisa kwa kuona inawezekana bado nilikuwa nimelala, nikajing’ata lipsi kuona kama nilikuwa usingizini au la.
“Njoo uchukue barua,” alimalizia bosi.
Kwanza usingizi wote ukaisha, mwili ukachoka na kufa ganzi. Nikainuka na kuelekea bafuni kuoga, nilipotoka huko, nikakaa kitandani na kuanza kufikiria nini cha kufanya. Nilipomaliza kila kitu nikaondoka zangu na kuelekea ofisini. Njiani nilikuwa na mawazo lukuki, kupoteza kazi na maisha haya tunayoishi kilikuwa kitu chenye kuumiza mno.

Nilipofika ofisini, nikaelekea kwa bosi na kunikabidhi barua yangu. Nikaondoka huku kila mfanyakazi ofisini mule akinionea huruma kwa kile kilichotokea. Nilipoingia ndani ya gari langu, nikaanza kulia sana, moyoni niliumia kupita kawaida. Nilipanga kumwambia mpenzi wangu, Aziza, sikujua angelipokea vipi suala hili lakini nikaupiga moyo konde, nikawasha gari na kuondoka mahali hapo. Nilipofika Kinondoni, nikasikia simu yangu ikiita, nikaichukua na kuangalia kioo, alikuwa mpenzi wangu, Aziza.
“Baby, nimegonga benz la watu hapa Mbagala, dereva kaniambia gharama ya vifaa ni milioni tano,” aliniambia mpenzi wangu, nikahisi kuchanganyikiwa.
“Unasemaje?” niliuliza kwa kuhamaki.
“Nisaidie mpenzi,” aliniambia huku akianza kulia, kilio kilichonipa hisia ya maumivu moyoni.
Kama kuchanganyikiwa, siku hiyo nilichanganyikiwa mno, nikapiga gia na kuanza kuelekea huko Mbagala. Kwanza niliona gari likitembea kwa mwendo mdogo, nilitaka kuliendesha kwa mwendo wa kasi zaidi. Foleni za Dar zilinichosha mno.
Baada ya saa moja na nusu, nikafika Mbagala, hiyo ilikuwa saa nne na robo asubuhi. Nikafika katika kituo cha polisi, nikaonyeshewa gari iliyokuwa imegongwa na mpenzi wangu na ni fedha tu ndizo zilizokuwa zikihitajika, nikajikakamua na kulipia.
“Ilikuwaje?” nilimuuliza mpenzi wangu, macho yake yalikuwa mekundu.
“Nililigonga kwa bahati mbaya mpenzi,” aliniambia huku akinikumbatia.
“Usijali, tuondoke.”

Tukaingia ndani ya gari, bado nilikuwa nikiendelea kujiuliza kama ilikuwa muda sahihi wa kumwambia kuhusu kazi yangu au la. Huku nikiwa najifikiria nini cha kufanya, bosi akanipigia simu na kuniambia kwamba ilitakiwa nihamishe kila kitu kutoka katika nyumba ya kampuni kwani kuna mfanyakazi mwingine alikuwa akitaka kuingia.
“Mbona hauna raha?” aliniuliza Aziza mara baada ya kukata simu.
“Tutaongea tukifika nyumbani,” nilimwambia huku nikilengwa na machozi.
Mpaka tunaingia nyumbani, ilikuwa ni saa sita mchana. Nikajitupa kitandani na kutulia, kichwa kilikuwa kimejaza mambo mengi mno, nilihisi muda wowote ule ningekufa.
“Ilikuwaje jana ulipokwenda kupima hospitalini?” aliniuliza Aziza. Hapo nikakumbuka, siku iliyopita nilikwenda hospitalini kwa ajili ya kuchukua vipimo. Nilikuwa nikijisikia uchovu kupita kawaida hali iliyomfanya mpenzi wangu anishauri nielekee hospitalini kuona mwili ulikuwa na tatizo gani.
Ikanibidi nichukue simu na kumpigia dokta Ibra Akilimia kumuuliza kuhusu majibu ya vipimo alivyonipima jana.
“Nilichukua vipimo, nimegundua una kansa ya damu,” aliniambia dokta Akilimia.
“Unasemaje?”
“Pole sana Nyemo. Una kansa ya damu.”
Nikakata simu. Nikaanza kujiuliza kwa nini siku hiyo ilikuwa ni siku ya majanga kwangu. Matatizo yalikuwa yameniandama mno. Wakati naendelea kujiuliza zaidi, nikapigiwa simu na kaka yangu, Gideon na kuniambia kwamba nilitakiwa kuelekea nyumbani, baba na mama walikuwa kwenye ugomvi mkubwa na hivyo walitaka kutengana.
Hiyo ilikuwa taarifa mbaya zaidi, yaani wazazi wangu watengane na wakati wameishi pamoja kwa muda wa zaidi ya miaka thelathini.
“Are u serious Gid?”
“Ndiyo. Njoo home, nimempigia simu Nehemiah na Anna, wapo njiani wanakuja, fanya haraka,” aliniambia Gideon na kukata simu. Nikatulia,
mapigo ya moyo yalikuwa yakinidunda mno, sikuamini kama matatizo yote yaliyokuwa yakitokea Mungu alikuwa ameyapanga au yalipangwa na shetani. Nikaondoka zangu kuelekea Kijitonyama walipokuwa wakiishi wazazi wangu, nilipofika kule, nilikuta wakilalamikiana na kila mmoja alisema kwamba ilikuwa ni bora kutengana.
“Ila ninyi ni wakristo, mambo ya kutengana wapi na wapi?” niliwauliza.
“Haiwezekani, kwa hapa tulipofikia, ni lazima tutengane,” alisema mama, kila nilipouliza sababu, sikupewa majibu.

Tulijitahidi kusuluhisha lakini hatukufanikiwa. Nikaondoka huku ikiwa ni saa kumi kasoro jioni. Nikaelekea home huku nikiendelea kuwa na mawazo lukuki. Nikiwa njiani, nikapigiwa simu, hii ndiyo iliyonichanganya zaidi.
Msichana niliyeachana naye miezi tisa iliyopita, alinipigia simu na kuniambia kwamba amejifungua salama. Huyu alikuwa msichana wangu kabla ya Aziza na alikuwa akiishi Masaki. Nikachanganyikiwa, nikamuuliza kama alikuwa na uhakika kwamba mtoto alikuwa wangu.
“Ni mtoto wako Nyemo, nipo tayari kwa vipimo vya DNA,” aliniambia msichana huyo.
Hapo nikabaki na kizungumkuti, sikufahamu kipi nilitakiwa kukifanya. Mwili ulikuwa mzito, macho yalikuwa yamenitoka,msichana niliyeachana naye alikuwa amejifungua, na mtoto alikuwa wangu. Sina kazi, nina ugonjwa wa kansa ya damu, wazazi wanataka kutengana na majukumu yalianza kunifuata.
Nilipofika nyumbani, saa kumi na mbili nikampigia simu Aziza. Simu ilikuwa ikitumika kwa muda mwingi, kila nilipopiga, ilikuwa ikitumika tu. Saa moja na nusu, ikapatikana. Nilimuuliza kuhusu mtu aliyekuwa akiongea naye, aliniambia kwamba alikuwa ni mwanaume wake mpya.
“Unasemaje?”
“Ni mwanaume wangu mpya. Anaitwa Edson. Naomba tuachane Nyemo. Umekuwa muongo mno, kumbe umefukuzwa kazi hutaki kuniambia,” aliniambia.
“Sikiliza mpenzi. Unaj....” hata kabla sijamaliza kuongea na simu, Aziza akakata simu.

Nilichanganyikiwa zaidi, huku nikijiuliza nifanye nini, simu yangu ikaanza kuita. Nilikiangalia kioo, nikagundua kwamba alikuwa kaka yangu, Nehemiah. Niliipokea simu ile. Taarifa aliyokuwa amenipa ilinishtua, ni kwamba mara baada ya kuondoka nyumbani na mama, gari lilipata ajali na hivyo mama alikuwa ameumia vibaya na kupelekwa hospitalini.
“Unasemaje?”
“Mama ameumia vibaya. Wamesema kutibiwa Tanzania haitakiwi, kaumia vibaya hivyo tumpeleke India, matumaini ya kupona ni madogo mno,” aliniambia Nehemiah.
Nilichanganyikiwa zaidi
.
“Upo wapi?”
“Tupo nyumbani. Njoo. Tunapanga safari iwe vipi, inahitajika milioni thelathini. Tumejipigapiga, tumepata milioni ishirini, tunataka uongezee kumi Nyemo,” aliniambia Nehemiah.
Kiukweli katika siku hii ya tarehe 11/03/2014 sitoweza kuisahau maishani mwangu. Nikawasha gari na kuondoka kuelekea nyumbani.
Nilichanganyikiwa mno. Nilipofika nyumbani, nikapigwa na mshangao
.
Kwanza nyumba ilikuwa kimya na taa zilikuwa zimezimwa. Nilijiuliza iweje Nehemiah aseme wapo nyumbani na taa zizimwe? Je walikuwa wameondoka au. Nilipoangalia vizuri kupitia dirishani, nikaona mwanga, nikawa na uhakika ulikuwa mwanga wa simu.
Nikaufuata mlango. Akili yangu haikuwa sawa, kama mtu alikuwa akitamani akione kiama basi siku hiyo ilikuwa kiama changu. Nilipoufikia mlango, nikashika kitasa, mlango haukuwa umefungwa,nikaufungua na kuingia ndani, giza lilikuwa totoro. Nikawasha taa...mwanga ulipomulika tu......
"SUPRISEEEEEEEEEEEEE......” zilisikika sauti za watu wengi, watu zaidi ya 20 wakiniambia huku keki kubwa iliyoandikwa ‘HAPPY BIRTHDAY NYEMO’ ikiwa mezani.
Kwanza nikashtuka, katika watu hao walikuwepo wazazi wangu, bosi, mpenzi wangu Aziza, my X aliyeniambia kajifungua, dokta Akilimia aliyenipima kansa, yule jamaa aliyedai kugongewa gari lake la benz, mkubwa wa kituo cha polisi cha Mbagala, yaani watu wote waliokuwepo kwenye mzunguko wangu toka asubuhi walikuwepo mahali pale, nilistaajabu mno.
Nikakosa nguvu, nikakaa kochini huku nikishika kichwa.
“Nyemo...hii ni birthday yako....” aliniambia kaka yangu, Nehemiah.
“Imekuwaje?” niliuliza huku nikionekana kutokuelewa chochote kile.
“Tulipanga tukufanyie suprise siku ya leo. Kila kilichotokea kilikuwa kimepangwa,” aliniambia Nehemiah.
“Mpenzi....njoo ujumuike nasi...pole kwa kukushtua,” aliniambia Aziza na kunifuata, akaniinua na kunikumbatia, joto lake likanifanya kujisikia kupata nguvu, nikaanza kutoa tabasamu.
“Asanteni kwa suprise yenu, kweli ilikuwa suprise,” niliwaambia. Nikazima mishumaa ya kwenye keki na sherehe kuanza.
“Damu yako haina matatizo, upo mzima kiafya,” aliniambia dokta Akilimia.
“Kwa hiyo kufukuzwa kazi, kugongwa kwa gari, majibu ya kansa ya damu, kuachwa na mpenzi, kugombana kwa wazazi, kumpa ujauzito msichana niliyeachana naye vyote vilikuwa ni mchezo ili kukamilisha suprise?” niliuliza huku nikikata keki.
“Ndiyo. Vyote vilikuwa suprise mtoto wangu wa mwisho,” aliniambia mama na wote kuanza kucheka kwa furaha.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa siku hii....siku ya kuzaliwa kwangu. Nawashukuru wote walionitakia siku ya kuzaliwa, namshukuru Mungu kuifikia siku hii ya leo. Mbarikiwe sana.

Post a Comment

0 Comments