Simulizi : Sikujua Ungenisaliti Mpenzi Sehemu Ya Nne (4)
Hakusikia jibu lolote kutoka kwa mmoja wao zaidi ya kibao kikali kilichotua usoni mwake barabara! “Mbona mnanipiga!” “Fanyeni kazi...” Bryson akasema. Muda huo huo, wakaanza kumvua nguo Bruno, wakiwa na nia ya kutaka kumfanyia mchezo mchafu! Walionekana kupania kweli kufanya upuuzi ule. Kwa lazima Bruno akajikuta amevuliwa nguo na alikuwa katika hatua za mwisho kabisa kabla ya kufanyiwa ufirauni! “Wewe si umeona raha kutembea na mke wangu, sasa ngoja hawa jamaa nao wakufanyizie ili uwe na adabu na wake za watu!” Bryson akasema kwa hasira. “Tafadhali, nipo tayari kutoa kiasi chochote cha fedha, msinifayie hivi jamani, nawaombeni sana.” “Sema shilingi ngapi?” Bryson akauliza haraka akionekana ndicho kitu alichokuwa akikisubiria kwa hamu! “Milioni moja!” Bruno akatamka kwa haraka, akitaka kujinasua katika mikono ya wanaume wale hatari. “Unasemaje?” Bryson akauliza kwa dharau. “Nitatoa milioni moja brother.” “Wakubwa, endeleeni na zoezi lenu, naona huyu hajui mimi ni nani! Fanyeni kazi niliyowaitia,” Bryson akaagiza. Wale vijana wakawa tayari kumkabili! It’s not fair! Bruno alikuwa akiingia katika historia mbaya zaidi kutokea katika maisha yake. Hakuwahi kufikiria kuingiliwa kinyume na maumbile, kwake yeye lingekuwa tukio ambalo lingeharibu kabisa taswira ya maisha yake. Akawaangalia watu wale ambao hawakuonekana kuwa na huruma kabisa, ambao walikuwa wanavutana naye ili watimize lengo lao. Tunu alikuwa akilia machozi, wakati akimuona Bruno akijitahidi kutumia nguvu zake zote kuhakikisha hawatimizi lengo lao. Vibao vilikuwa halali ya Bruno usoni mwake. Alilia sana, lakini hakuna aliyekuwa tayari kumsikiliza. “Weee...unajifanya mjanja siyo? Nitakuua, nimekuambia nitakuua sasa hivi, acha kucheza na akili yangu wewe mjinga!” Bryson alifoka akivua mkanda wake kiunoni kwa ajili ya kumkabili zaidi Bruno. “Mnanionea, mtaniua bure jamani!” Akasema Bruno lakini hakuna aliyemsikiliza. Hakuna aliyetaka kupoteza muda wake kumsikiliza, mkanda ukatua mgongoni mwake na kumsababishia maumivu makali zaidi ya awali. “Jamani mimi ni mwanaume mwenzenu, nawaombeni mniambie mnachohitaji ili muache kunitenda hivi,” alisema Bruno. “Unatuambie sisi, kwani hujui uliyetembea na mkewe?” Mmoja wa wale vijana akasema. Bruno akageuza uso wake na kumuangalia Bryson, macho yake yalikuwa yanatoa ujumbe mzito sana kwake. Hakutaka kufanya unyama ule. Ulikuwa unyama mbaya sana... “Brother najua ni kiasi gani unaumia, najua nimefanya makosa, lakini naomba msinitende hivi, nipige faini yoyote nitalipa.” “Milioni kumi unazo?!” Bryson akauliza akiwa hapepesi macho yake. “Sitakuwa nayo kaka!” “Una ngapi?” “Naweza kupata milioni tano, nisaidieni tafadhali.” “Milioni tano, haiwezekani.” “Nisaidieni.” “Mwisho saba, vinginevyo kazi iendelee.” “Sina, ninazo tano.” “Acha ujinga wewe, nitawaruhusu waendelee.” “Hapana kaka, usifanye hivyo.” “Haya sita.” “Lakini sina zote kwa hapa, naweza kuwapa kwa awamu.” “Kivipi?” “Hapa nina milioni tatu, nitawakabidhi hapa hapa, halafu mbili twendeni kwenye ATM, halafu moja nikikusanya madeni kesho, nitamalizia.” “Lakini kwanini ukaamua kutembea na mke wangu? Au ulikuwa unataka kupima watu?” “Ndiyo maana naomba msamaha.” “Sawa, nadhani nikubaliane na wewe kwakuwa umeomba sana, lakini unaweza kunitoroka na hizo tatu zilizobakia. Mimi ninayo kamera, kaeni hapo mkiwa watupu niwapige picha, hizi ndizo zitakazokufanya unilipe, ndiyo ushahidi wangu. Tukishalipana, nitazifuta. Kama upo tayari sema.” “Sawa, nipo tayari,” Bruno akatamka haraka akiwa na shauku ya kuachiwa mikononi mwa wale watu wasio na huruma. Muda ule ule, kamera ikatolewa na Tunu kulazimishwa kuvua nguo zote. Akavua. Bruno hakuwa na haja, maana tayari alikuwa mtupu. Wakapigwa picha nyingi sana, kisha Bruno akatoa fedha mfukoni na kuanza kuhesabu hadi kufikia milioni tatu akamkabidhi Bryson. “Ok! Sasa twende kwenye ATM tukamalizie nyingine ziliobakia.” “Sawa.” Bruno akavaa, wakatoka nje akiwa ameongozana na wale wanaume wanne na Bryson. Wakaingia kwenye gari na kwenda hadi kwenye mashine ya kutolea fedha. “Ila jamani kama mnavyojua, mashine haiwezi kutoa zaidi ya milioni moja kwa siku!” “Kwahiyo? Umeanza uswahili?” “Hapana, ni hali halisi?” “Kwahiyo unasemaje?” “Nitachukua hizo milioni moja na kuwapatia, halafu ikifika saa sita kamili za usiku, turudi tena kuchukua nyingine.” “Sawa.” Wote wakakubaliana. Bruno akaingia kwenye mashine akiwa ameongozana na Bryson, akatoa fedha na kumkabidhi. Wakarudi kwenye gari na kuondoka zao. Safari yao iliishia Nguvumali kwenye moja ya baa maarufu, wakatafuta sehemu tulivu na kukaa pamoja. “Tutakunywa hapa mpaka saa sita turudi kwenye ATM, usije ukajidanganya kwa kupiga kelele. Utakuwa umejiharibia mwenyewe. Nategemea sana utulivu wako kwa kila kitu. “Kuwa huru kuagiza kitu chochote, ule utakavyo na unywe utakavyo. Hatutapenda kuona unafanya vurugu ya aina yoyote, ukijaribu tutakuua. Mimi nina roho mbaya kuliko unavyofikiria,” Bryson akasema kwa kumaanisha, maana ni kweli alikuwa hatanii katika kauli yake. “Sawa.” Mbuzi ikachomwa, kuku zikakaangwa na bia zikashuka mezani. Walikuwa wakipiga stori kama wote walikuwa marafiki. Bruno alipotaka kwenda chooni, alisindikizwa, hakwenda mwenyewe. Ilikuwa hivyo mpaka ilipofika saa 6:12 za usiku, ndipo Bryson alipogutuka. “Oya muda tayari,” akasema akimtazama Bruno usoni. “Twendeni,” mwingine akadakia. Hakuna aliyeona umuhimu wa bia tena, wakaachana na vinywaji na kuingia kwenye gari na kwenda kuchukua zile pesa nyingine kwenye ATM. Hapo Bruno akaachiwa huru, akiamrishwa kupeleka mwenyewe milioni iliyobaki kesho yake. “Ahsante sana kaka, nawashukuru sana,” Bruno akasema kwa woga. Pesa kwake haikuwa kitu tena, kwa muda ule, thamani yake kama yeye ndiyo ilikuwa kitu cha kwanza. “Ole wako usilete hiyo pesa!” “Nitaleta.” “Kumbuka picha zako tunazo.” “Najua kaka.” “Ok! Kesho,” Bryson akasema. Bruno akaondoka muda ule ule, alikuwa akielekea gesti kutafuta mahali pa kulala, kichwani akiwa na mawazo yasiyo na kikomo. *** “Nooooooooo....” Bruno akapiga kelele usiku huo, baada ya kukumbuka tukio lile ambalo si rahisi kufutika katika maisha yake. Akiwa bado anaendelea kuwaza pale kitandani, akijilaumu kwa kufanya mapenzi na Vanessa, mchumba wa mtu, tena mwanaume wake akiwa pale nyumbani usiku ule, alisikia mlango wa chumba chake ukigongwa! Taa za hatari zikawaka ubongoni mwake. Msala! Mshtuko alioupata Bruno, ulikuwa hauelezeki. Kwa vyovyote vile, alijua aliyekuwa anagonga mlango alikuwa ni Emma, mpenzi wake na Vanessa. Emma yule yule ambaye anasifika kwa ukorofi na ukali! Emma ndiye anayegonga mlangoni. “Anko...” sauti ya kiume ikasikika mlangoni. Hapo akajua ni kweli alikuwa Emma anagonga... “Vipi?” Bruno akaongea kivivu huku moyo ukimdunda kwa woga. “Fungua...” Emma akasema kama anayeamrisha. Moyo wa Bruno ukaongeza kasi, akili yake ikajua kwa vyovyote vile kulikuwa na hatari iliyokuwa inakuja mbele yake. Hatari ambayo kwa hakika hakutamani kabisa. Lakini hakuwa na jinsi, tayari alikuwa ndani ya nyumba ya watu, akawa tayari kwa lolote. “Nakuja,” akajibu tena, safari hii akijitahidi kushusha mguu mmoja chini na kuchukua gongo linalomsaidia kutembea na kujivuta mlangoni. Akafungua mlango akitweta na kutetemeka kwa woga. Akakutana na uso wa Emma, ambaye hakuwa na maswali zaidi ya kuonesha ishara kwamba anataka kuingia ndani. Bruno akampisha. Emma akaingia na kuketi kwenye kiti pekee kilichokuwa ndani. Uso wake ulionekana kusema jambo, lakini hakuweza kulitoa moja kwa moja. Akamtulizia macho usoni kama anayejifunza jambo fulani. Bruno akaketi kitandani kimya akionekana kuwa na wasiwasi kidogo.
Emma akavuta pumzi ndefu sana kisha akazishusha taratibu kabisa...kinywa chake kikaonekana kuanza kutingishika na kuonekana dhahiri alitaka kuongea lakini hakuwa na hiyari ya maneno gani ayatoe kinywani mwake. “Pole sana,” akaponyokwa na maneno yale, akionekana kama anawaza kukosea kutoa maneno yale. Bruno hakujua pole ilikuwa ya nini, kwahiyo alibaki kimya akimtazama, lakini baadaye akaamua kuonesha ushirikiano ingawa hakujua pole ilikuwa ya nini, akaamua kuitikia kwa kutingisha kichwa! “Pole sana Anko!” “Samahani...pole ni ya nini?” Kwa mara ya kwanza Bruno alitamka maneno hayo. “Nimesikia kama umepiga kelele?” “Mimi?” “Ndiyo!” “Umesikia vibaya!” “Hapana...nimesikia vizuri sana ukipiga kelele, ukisema nooooo....nikashindwa kuelewa ni kwanini, lakini nilihisi labda maumivu ya mguu yanakusumbua!” Bruno akahema kwa kasi tena, angalau sasa alishajua ni kwanini alikuwa anapewa pole, maana mwanzoni alikuwa njia panda, kwasababu hakujua ni sababu gani hasa iliyomfanya ampe pole. “Ni kweli, nilikuwa kwenye mawazo, kwenye kumbukumbu za hatari, nikajikuta nimepiga kelele!” “Pole sana Anko!” “Nashukuru.” “Ni kumbukumbu za nini?” “Acha tu Anko wangu, siku nikiwa na muda nitakusimulia, kwasasa nenda kapumzike!” “Ok! Usiku mwema.” “Nawe pia.” Emma akatoka na kumuacha Bruno mwenyewe ndani, akaamka haraka na kwenda kufunga mlango, akarudi kitandani akiwa anahema. Haamini kilichotokea. Kwamba Emma hakugundua kwamba muda mfupi uliopita, alilala na mpenzi wake. Kwamba yeye si mjomba wa Vanessa bali ni rafiki tu! Rafiki ambaye tayari mchezo wa hatari umeshaanza! Akajichukia ghafla! Akavuta shuka na kujitahidi kuusaka usingizi. Haikuwa kazi ndogo, lakini hatimaye akafanikiwa kupata usingizi. Akalala fofofo. *** Asubuhi na mapema Emma aliamka na kwenda zake kwenye mihangaiko yake, akamuacha Vanessa kitandani mwenyewe. Ilikuwa asubuhi ya saa kumi na mbili! Mapema kabisa, kabla nuru haijalinyang’anya giza nafasi. Vanessa akachepuka haraka na kwenda mlangoni kwa Bruno, akamgongea. Bruno akashtuka sana, akajua lazima alikuwa ni Emma amemfuata tena. Moyo wake ukapiga kambi kwa mshtuko! “Nimepatikana...” akawaza akifungua mlango. Tofauti na matarajio yake, mlango ulipofunguka, akakutana na uso wa Vanessa ukiwa umeachia tabasamu la nguvu! Hakusubiri kukaribishwa, akaingia mwenyewe na kujitupa kitandani. Alikuwa na upande mmoja wa kanga, kwahiyo aliuvua na kubaki mtupu! Akawa anamwangalia Bruno kwa macho yanayosema. Macho yalikuwa yanazungumza jambo moja tamu; kwamba anahitaji mapenzi. Bruno akaogopa sana. Hakuwa tayari kufanya kitu chochote. “No! No! No!” “Acha ujinga Bruno, njoo bwana!” “Sitaki!” “Please naomba uje, Emma ameshaondoka!” “Lakini sijapendezwa na hii tabia yako!” “Usiwe hivyo bwana!” “Sikia, mimi ni kweli nina shida, lakini huwezi kunifanyia hivi.” “Vipi?” “Utumwa! Unataka kunifanya mimi mtumwa wako wa mapenzi.” “Sijasema hivyo, mimi nina mapenzi ya dhati kwako!” “Hata kama, lakini wewe una mwanaume wako.” “Ni kweli lakini hapa ni kwangu, au hujui?” “Hata kama Vanessa, mimi sitaki!” “Bruno kweli hutaki kuthamini yote niliyokufanyia?” “Lakini si kwa njia hii, huku ni kuninyanyasa.” “Nimekwambia ni mapenzi tu, si manyanyaso.” “Hapana Vanessa.” “Mimi nina nia njema na wewe, nataka kubadilisha maisha yako.” Bruno akakaa kimya kwa muda akimsikiliza... “Najua maisha yako yameshabadilika, nataka kukusaidia kukunyanyua tena. Kwanza kabisa nitahakikisha unapata mguu wa bandia, mzuri ambao utakusaidia kuachana na gongo kabisa!” Zilikuwa habari njema kwa Bruno, akaendelea kuwa kimya akimpa nafasi Vanessa aendelee kuzungumza. “Tena kama huamini, sema wiki ijayo nikupeleke India, ukirudi hapa unatembea mwenyewe na nitahakikisha nakupa mtaji wa kufanya biashara. Nataka uweze kujitegemea tena. Yote haya ni kwasababu nakupenda.” “Kweli Vanessa?” Bruno akaponyokwa na maneno hayo akiwa ameyatuliza macho yake usoni mwa Vanessa. “Sijawahi kukudanganya Bruno!” Vanessa akasema akimsogelea Bruno. Hakuhitaji kupewa ruhusu tena! Hakuhitaji kukubaliwa! Macho ya Bruno yaliongea wazi wazi...yalikuwa yanasema, nimekubali! Kwa mara nyingine tena, wakazama kwenye dimbwi la mahaba mazito. Bruno alikubali kufanya yote hayo kwa ajili ya maisha yake, alitamani sana siku moja atembee tena. Ndoto ambayo ilikuwa inanukia! Vanessa alijisikia mshindi maana alijua wazi kwamba, kwa ahadi aliyoitoa Bruno asingeweza kuchomoka kabisa. Akamsogelea akiwa anahema kwa kasi, Bruno akawa hana hiyari tena na kitu chochote. Vanessa akamkalisha Bruno kitandani, kisha akayatuliza macho yake usoni mwake, akatabasamu. Bruno akawa anaangalia kwa macho yaliyojaa huruma, alikuwa ndani ya penzi la kitumwa, maana ndani ya moyo wake hapakuwa na alama yoyote ya mapenzi kwa Vanessa. Ni kwa vile hakuwa na ujanja wa kufanya jambo lolote, lakini ukweli ni kwamba hakuhisi kumpenda Vanessa. Akamwangalia kwa jicho la kuhoji kitu; Vanessa akagundua kwamba Bruno alikuwa na mashaka na jambo fulani au alikuwa anataka kuuliza kitu lakini akawa anasita. “Sema Bruno, nahisi kama kuna kitu unataka kuniuliza ni kweli?” “Ndiyo!” “Hebu niambie ni nini?” “Nataka kufahamu nia yako hasa kwangu ni nini?” “Mapenzi Bruno!” “Halafu?” “Sijakuelewa.” “Mapenzi ya aina gani?” “Nataka kufunga ndoa na wewe!” “Haiwezekani!” “Kwanini?” “Sababu zipo mbili, kwanza wewe una mchumba wako Emma, na mimi nina mke wangu yupo Mwanza!” “Una mke?” “Ndiyo!” “Umefunga naye ndoa?” “Hapana, ila nimezaa naye watoto wawili!” “Sasa kumbe hujafunga naye ndoa, wasiwasi wako wa nini? Unashindwa vipi kuoana na mimi wakati hata ndoa bado hamjafunga?” “Basi tu!” “Kwanini?” “Na Emma?!” “Kwani nimefunga naye ndoa? Emma yupo chini yangu, hana ujanja wowote kwangu, mimi ndiye ninayemlea kwa kila kitu. Kumbuka hapa ni kwangu, hana uwezo wa kufanya lolote.” “Thubutu! Na ukorofi wake wote ule? Siamini kabisa!” “Hayo ya Emma achana nayo, jambo la msingi ni kuangalia moyo wako! Kwani wewe unaonaje, unanipenda?” Bruno akakaa kimya! “Unanipenda Bruno?” “Nakupenda ndiyo!” “Sasa wasiwasi wa nini?” Bruno akabaki kimya! “Kama ni kweli unanipenda, hayo mengine yaache kama yalivyo, we’ angalia mapenzi, kila kitu kitakuwa juu yangu!” “Vipi kuhusu mguu?!” “Wiki ijayo twende India.” “Sawa, nitashukuru sana.” Vanessa akamsogelea Bruno kisha akamwonesha ishara apande kitandani. Bruno akafanya hivyo, kilichofauta baada ya hapo ilikuwa kazi nzito sana iliyowafanya wote wawe hoi baadaye. WIKI MBILI BAADAYE Mambo hayakuwa mepesi kama Vanessa alivyokuwa akifikiria mwanzoni, alitarajia kusafiri na Bruno baada ya wiki moja, lakini hilo halikuwezekana. Utaratibu wa hospitali aliyokuwa anakwenda ulikuwa wa tofauti kidogo. Kwanza aliwasiliana na Uongozi wa Hospitali ambayo ingemshughulikia Bruno, baadaye akaunganishwa na daktari wake ambaye alisema alikuwa na wateja wengi, hivyo akawataka waende baada ya wiki mbili. Maandalizi yote yalikuwa tayari, Emma alipewa taarifa kwamba ‘mjomba’ wake na Vanessa alikuwa anapelekwa India kwa ajili ya kuwekewa mguu wa bandia, hakupinga! “Nawatakieni safari njema.” “Tunashukuru sana Anko, ubaki salama!” “Ahsante sana, nawaombea kila lililo jema!” “Tunashukuru!” Emma akawasindikiza hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wakaagana kwa mara nyingine tena. Bruno akatembea kwa kutumia gongo lake akimfuata vanessa aliyekuwa ametangulia. Wakaingia kwenye sehemu yenye maandishi yaliyosomeka WANAOONDOKA. Vanessa akageuka nyuma na kumpungia Emma. Wakaingia.
Baada ya saa kadhaa angani, ndege waliyokuwa wakisafiria ilitua kwenye ardhi ya nchi ya India jijini New Delhi. Kila kitu kilikuwa kimeshapangwa! Walipokuwa wakitoka waliona bango kubwa lililoandikwa kwa maandishi makubwa; BRUNO AND VANESSA FROM TANZANIA, YOU ARE WELCOME TO INDIA. Lilikuwa bango lilibebwa na wahudumu wawili wa Hospitali wanayofikia kwa ajili ya matibabu. Vanessa na Bruno wakawafuata watu hao. Nao walivyowaona, Bruno akiwa akiwa anatembea na gongo, waliweza kugundua kilichoendelea. Walijua ndiyo wageni wao. “Hello, I hope you are from IPRO Hospital!” (Habari, naamini mnatoka Hospitali ya IPRO!) Vanessa akauliza alipowafikia. “We are fine! Yes, we are coming from there. Are you Vanessa and Bruno?” (Hatujambo! Ndiyo tunatokea kwenye hospitali hiyo. Ninyi ndiyo Vanessa na Bruno?) Mmoja wao akauliza. “Yeah!” (Ndiyo!) “You are all welcome to New Delhi!” (Karibuni sana New Nelhi) “Thank you!” (Ahsante) Vanessa akaitikia. Baada ya hapo wakandoka na kwenda kuingia kwenye gari lililoandikwa IPRO HOSPITAL tayari kwa safari ya kwenda hospitalini. Kila kitu kwa Bruno kilikuwa kipya, alihisi kama yupo kwenye ndoto ndefu sana ya kupendeza, lakini haikuwa hivyo! Ilikuwa kweli, kwamba yupo India kwa ajili ya kuwekewa mguu wa bandia! Furaha kiasi gani? Kila kitu kilikuwa kipya kabisa kwa Bruno, ambaye alikuwa ametulia kimya kwenye kiti akitazama nje, akijionea mandhari ya mji ule. Hakuamini kama kweli siku chache baadaye alikuwa akienda kutupa gongo na kutembea kwa miguu yake mwenyewe kama zamani. Hilo lilimpa furaha sana, hapo akaona jinsi Vanessa alivyokuwa na mapenzi ya kweli kwake. Si jambo jepesi hakika atokee mtu wa kukusaidia katika kiwango kile. Bruno alikuwa na furaha sana. “Mh! Vanessa,” Bruno akaita. “Bee!” “Ahsante sana!” “Nini tena?” “Ahsante kwa kila kitu Vanessa, sasa ndiyo naamini kwamba nakwenda kutembea tena.” “Unatakiwa kuendelea kuamini hivyo Bruno, nimeshajitoa kwa ajili yako mpenzi, amini kwamba nakupenda ndiyo maana nafanya yote haya kwa ajili yako!” “Nashukuru sana Vanessa, ahsante sana.” “Usijali dear!” Safari ikaendelea hadi walipoingia katika geti la hospitali ile, iliyokuwa na mandhari nzuri ya kuvutia. Nje ya hospitali hiyo kulikuwa na bango kubwa lililoandikwa IPRO HOSPITAL, gari likaingia na kwenda kwenye maegesho, likaegesha. Mlango ukafunguka wenyewe! “Karibuni sana!” Mmoja wa wahudumu wale akasema kwa lugha ya Kiingereza. “Tunashukuru sana.” “Nifuateni.” “Ok!” Wakaanza kumfuata Mhudumu yule aliyekuwa akikatiza kwenye barabara ndogo zilizozungukwa na maua mazuri ya kuvutia. Walipita ofisi nyingi, baadaye wakaingia kwenye mlango mmoja wa kioo. Macho yao yakakutana na daktari mwenye asili Japan, akiwa ameketi kimya kitini. Alipowaona akaachia tabasamu. “Karibuni sana!” Akawakaribisha. “Ahsante sana,” wote wakaitikia. “Dokta, hawa ndiyo wageni wetu kutoka Tanzania,” yule Mhudumu aliyewaleta akasema. “Ok! Nashukuru sana, nilijua ndiyo hawa...habari za Tanzania?” Daktari yule aliyejitambulisha kwa jina la Dk. Lives aliuliza akitabasamu. “Tanzania ni kama unavyotuona, tuna shida dokta,” Vanessa akajibu kwa unyonge. “Hapana usijali, huna sababu ya kuwa mnyonge kiasi hicho dada yangu, mgonjwa wako anakwenda kutupa gongo muda si mrefu sana. Mmeshafika hospitalini sasa, hapa ndiyo sehemu pekee itakayomrejeshea ndugu yako furaha yake!” “Nashukuru kusikia hivyo!” “Ok! Kama tulivyoongea kwenye simu, kila kitu kipo tayari, tumeshakuandalia sehemu ya kufikia, kwahiyo ondoa shaka. Huyu mgonjwa mwache hapa, taratibu nyingine zitaendelea. Kesho kutwa asubuhi asubuhi utakuja kuchukuliwa hotelini, kazi ikiwa imeshakamilika!” Dk. Lives akasema. “Sawa.” “Ok! Sabina, mpeleke hotelini tafadhali, hakikisha mnampatia huduma nzuri.” “Bila shaka dokta!” Sabina akaongozana na Vanessa hadi kwenye gari lile lile walilokuja nalo kutoka uwanja wa ndege. Wakaingia, dakika moja baadaye, dereva alifika na kuwapeleka hotelini. Hoteli haikuwa mbali sana na Hospitali, hivyo mwendo wa robo saa tu baadaye gari lilikuwa linaingia kwenye geti lililoandikwa HOTEL IPRO. Wakashuka na kuongozana pamoja hadi Mapokezi. Vanessa akatambulishwa kama mteja wao aliyefika na mgonjwa wake hospitalini. Akapewa chumba kizuri na huduma zote. *** “Room no. 207 ghorofa ya nane!” Ndivyo Vanessa alivyosema mara baada ya kupokea simu iliyokuwa chumbani kwake, iliyoita kwa muda mrefu. “Ndiyo nimepiga hapo kutoka Mapokezi, naitwa Martinah, habari za asubuhi?” “Salama, naomba nikusaidie!” “Ok! Nilipenda kujua utapenda tukuandalie nini kama kifungua kinywa chako kwa leo?” “Mh! Mbona leo mmenipigia mapema sana? Ni saa moja kasoro za asubuhi sasa, bado nimelala. Sijajua bado.” “Nafahamu, lakini saa 3:00 utakuja kuchukuliwa na wahudumu wa Hospitalini ukamuone mgonjwa wako!” “Ok! Sasa nimekuelewa, kuhusu kifungua kinywa, niandalieni maziwa fresh na mayai ya kukaanga!” “Utapenda kawaha au majani?” “Majani!” “Robo saa ijayo, vitakuwa chumbani mwako.” “Nitashukuru sana.” Kama alivyoahidiwa ndivyo ilivyokuwa, robo saa baadaye Mhudumu alifika chumbani mwake na kumpelekea kifungua kinywa. Tayari alikuwa ameshaoga, hivyo aliingia mezani na kuanza kula. Saa 3:00 za asubuhi alipigiwa simu, gari la Hospitalini lilikuwa limeshafika. Akatoka na kwenda kwenye lifti, akaingia na kushuka hadi chini. Akaingia kwenye gari na kupelekwa Hospitalini. *** “Kila kitu kimeshakamilika, kilichobaki kwasasa ni mazoezi tu. Nitakuruhusu uende naye Hotelini, lakini kila siku asubuhi atafuatwa na kuletwa hapa kwa ajili ya mazoezi yatakayomchukua wiki moja, kabla ya kuwaruhusu mrudi Tanzania!” Dk. Lives alimwambia Vanessa muda mfupi baada ya kuingia ofisini kwake. Mbele yake alikuwa ameketi Bruno akiwa hana gongo tena! Furaha aliyokuwa nayo ikamfanya ashindwe kudhibiti machozi yake. Bruno akaanza kulia. “Usilie Bruno, hongera sana...nyamaza tafadhali!” Vanessa akajitahidi kumtuliza. “Siamini Vanessa, siamini kabisa kama ni kweli nimepona!” “Nimeshakuambia usijali, kila kitu kinawezekana, tulia Bruno!” Bruno akanyamaza, Vanessa akamgeukia dokta na kumwambia: “Ana furaha, haamini kama angeweza kutembea tena.” “Ni kawaida, lazima awe katika hali hiyo, lakini msijali!” “Tunashukuru sana Dokta, nadhani sisi sasa twende.” “Sawa, pole sana Bruno.” “Ahsante dokta.” Bruno na Vanessa wakatoka, Bruno akitembea mwenyewe, ingawa bado alikuwa akichechemea, lakini angalau alikuwa na mguu wake bandia. Ilikuwa siku mpya kwa Bruno. Vanessa akamshika mkono na taratibu wakaongozana hadi kwenye gari aina ya Toyota Hiace iliyoandikwa kwa maandishi makubwa ubavuni, IPRO HOTEL, wakaingia na kuketi vitini. Bado Bruno alionekana kujawa na mawazo sana kichwani mwake. “Usiwaze sana!” Vanessa akasema. “Nashindwa kujizuia!” “Najua, lakini usiruhusu sana!” “Nimekuelewa!” “Kweli?” “Ndiyo!” “Lakini kwanini unakuwa hutaki kukubaliana na kilichotokea?” “Nahisi ni kama maumivu yaliyo ndani ya furaha, unajua si rahisi kuamini kilichotokea, lakini ndiyo hivyo tena sina namna lazima nikubaliane nalo. Ahsante sana Vanessa, nakushukuru sana!” “Usijali mpenzi wangu, lazima ufahamu kwamba nimefanya yote hayo kwasababu ya penzi langu la dhati lililojificha moyoni mwangu, nashukuru kwa utambuzi huo, naomba nikushukuru sana Bruno kwa namna ambavyo wewe unaona thamani hiyo!” “Usijali Vanessa, sasa naamini kuwa unanipenda mpenzi!” “Siku zote hizo, ulikuwa hujui?” “Nilijua, lakini leo imethibitika zaidi!” Gari liliondoka Hospitalini pale kwa mwendo wa taratibu hadi Hotelini ambapo wote walishuka na kuingia kwenye lifti kisha wakaenda zao chumbani kwao. Walizungumza mengi sana, lakini kubwa zaidi ilikuwa ni juu ya mapenzi yao na jinsi ambavyo Bruno aliachana na gongo na kutembea mwenyewe!
*** Ilikuwa siku ya sita ya mazoezi ya Bruno, ikiwa ni siku moja kabla ya kumaliza mazoezi Hospitalini hapo na kuanza safari ya kurejea Tanzania. Tayari Bruno alishaanza kuzoea kutembea na mguu wake bila kuchechemea. Hakuamini kama mguu ule wa bandia angeweza kuuzoea na kutembelea kama wake. Yalikuwa maendeleo makubwa sana kwa Bruno. Bado Vanessa alikuwa akiteswa na vitu vingi sana kichwani mwake, kwanza aliwaza kuhusu mjomba wake Bryson, kwanini alikuwa anasema alikuwa mbaya kwake, pia kitu kingine kilichokuwa kikiutesa zaidi ubongo wake ni Tunu, kwanini alikuwa akimtaja kama mwanamke mbaya katika masha yake? Akapanga lazima azungumze naye ili aweze kumweleza ukweli halisi... Alikuwa na maendeleo mazuri sana katika mazoezi, aliendelea vizuri sana na uwezo wake ulishakuwa mkubwa kabisa wa kutembea mwenyewe. Vanessa hakutaka kukubali kuendelea kuwaza mambo ambayo hayajui kichwani mwake, ilikuwa lazima aulize ili aweze kuujua ukweli. “Kuna kitu kinanichanganya sana Bruno, natakiwa kuzungumza na wewe,” Vanessa akamwambia Bruno ambaye alipigwa na butwaa na kauli hiyo. “Ni nini hicho? Unaweza kuniambia tu!” “Usinifikirie vibaya Bruno, nataka tu, kufahamu ukweli.” “Sawa, nakusikiliza!” “Nataka kujua mambo mawili!” “Ni mambo gani hayo?” “Kwanza ni kuhusu Anko Bryson, halafu nataka pia kujua kuhusu Tunu!” “Hatuwezi kuzungumza siku nyingine?” “Nahisi leo ni siku nzuri zaidi.” “Bryson ni mtu mbaya sana kwangu!” “Sawa, ulishaniambia!” “Hata Tunu pia...” “Najua, lakini sijafahamu sababu bado.” “Lakini nahisi kama hapa si mahali sahihi sana pa kuzungumza.” “Hapana Bruno, nakuomba sana kama ni kweli unanipenda, niambie ili niweze kujua ukweli.” “Lakini ni kumbukumbu za majonzi sana, ambazo huwa sipendi kuzikumbuka kila wakati.” “Najua, lakini naona kama zitazidi kukutesa kila siku kichwani mwako, kwanini usiniambie tu mpenzi wangu?” “Hapana!” “Au hunipendi?” “Nakupenda sana Vanessa, tayari nimeshatoa moyo wangu kwa ajili yako!” “Please naomba uniambie basi.” Bruno alikaa kimya akionekana kuanza kukumbuka kila kitu juu ya watu hao wawili, alionekana kuwa na mambo ya kuumiza sana aliyofanyiwa na Tunu pamoja na Bryson, kimya cha dakika mbili kilipita wakiwa pale bustanini, lakini baadaye akaanza kuzungumza... “Mimi ni Msukuma, kwetu ni Mwanza. Nilikuwa nafanya kazi katika Kampuni ya Sangara Distributors ya jijini Mwanza, kama Afisa Mauzo. Kazi yangu ilikuwa kusafiri na gari lenye samaki wa maji baridi na kupeleka Kanda ya Kaskazini, nikimaanisha, Manyara Arusha, Kilimanjaro na Tanga. “Nilikuwa msimamizi wa kila kitu katika gari. Tulishusha mizigo kila mkoa na mimi ndiye niliyekuwa nabaki na mauzo yote. Nyumbani Mwanza nina mke, ingawa sijafunga naye ndoa, lakini nimezaa naye watoto wawili kama nilivyokuambia awali ambao tunaishi nao katika nyumba ya kampuni. “Bosi wangu alikuwa ananipenda sana na alikuwa akinipa kila kitu. Nilifanya kazi kwa uaminifu mkubwa, nikipata mshahara mzuri na marupurupu ya kutosha, lakini siku moja tu, ndiyo iliyoharibu kila kitu katika maisha yangu. Ni siku ambayo nilikutana na Tunu. Siku hiyo nilikwa nimekaa na marafiki zangu kwenye baa moja huko Tanga, tukiwa tunakunywa na kuendelea na stori za hapa na pale. “Nikamuona Tunu...ni kweli nilihisi kumpenda, lakini hata yeye alionekana kuvutiwa na mimi na kusema kweli yeye ndiye aliyenitongoza. Nikazungumza naye na kumwambia nimekubaliana na ombi lake, lakini nilisisitiza kumuuliza kama hana mume, akasema hana! “Basi nikaenda nyumbani kwake, nikalala naye kwa siku mbili mfululizo, usikuwa wake, akaja mwanaume mmoja ambaye ndiye huyo mjomba wako Bryson, akasema ni mume wake. Nikapigwa, nikaumizwa sana na baadaye nikapigwa picha akiwa na vijana wengine wahuni. Ili mambo yaishe, nikakubaliana nao niwape shilingi milioni sita! “Kwanza nikawapa milioni tatu, baadaye nikaenda kutoa milioni moja kwenye ATM kisha tukasubiri hadi saa sita usiku nikaenda kuchukua milioni nyingine moja na kuwapatia kwa ahadi ya kuwapatia milioni moja asubuhi baada ya kukusanya madeni kwa wateja wangu!” Alisema Bruno akionekana kuwa na huzuni sana. “Enhee ikawaje?” “Kweli asubuhi yake nikakusanya madeni na kupata ile milioni moja, nikawa nawatafuta ili niwapatie ili picha zangu zisisambazwe, nikagundua kitu cha ajabu sana. Sikuamini kabisa!” Akasema Bruno huzuni yake ikizidi kuongezeka. “Uligundua nini?” “MJOMBA WAKO NI TAPELI, TUNU HAKUWA MKEWE ILA WALIAMUA KUNITAPELI YEYE NA TUNU! KILA KITU NILIELEZWA, HAPO UKAWA MWANZO WA KUPATA ULEMAVU!” “Kivipi?” Vanessa akauliza akionekana kuwa na shauku ya kutaka kujua. Bruno hakuweza kuongea kitu tena, zaidi ya machozi machoni mwake kuanza kuchuruzika kama maji ya mfereji! *** Bruno alidamkia sokoni kwa ajili ya kudai madeni ya wateja wake aliowauzia samaki. Hazikuwa fedha zake, lakini alitaka kwanza amalize matatizo katika mkoa wa watu ili awe huru. Tayari aliamini kwamba alikuwa ameshajifunza kutokana na kosa alilolifanya! Hakutamani kabisa, picha zake za utupu zisambazwe! Angeficha wapi uso wake? Angemweleza nini mkewe? Vipi kuhusu wazazi wake na marafiki zake? Alikuwa katika wakati mgumu sana. Haikuwa kazi kubwa kupata milioni moja aliyokuwa anaihitaji! Hadi kufikia saa 4:00 za asubuhi tayari alikuwa na milioni kibindoni! Akakodisha taxi na kwenda zake mitaa ya Sahare, ambapo Bryson alimwelekeza azipeleke hizo fedha. Hakuwa mwenyeji wa mitaa hiyo, kwahiyo alipoona salon moja ya kiume jirani na eneo aliloelekezwa... “Paki hapo kaka!” “Wapi?” “Mbele ya hiyo salon hapo!” “Poa.” Dereva akapunguza mwendo na kuegesha sehemu aliyoelekezwa. Akashuka na kupiga hatua za taratibu kwenda kwenye ile salon, akaingia ndani. “Mambo vipi washkaji?” Bruno akasalimia. “Poa mwana, shwari?” Kinyozi wa pale akaitikia. “Poa.” “Sema, karibu kiti mkubwa!” “Siyo mkaaji, ila kuna mshkaji mmoja namwulizia, alinielekeza mitaa hii!” “Anaitwa nani?” “Bryson!” “Bryson?!!!” Sauti za watu wawili zikasikika na wote wakamkazia macho kwa mshangao! Bryson anajulikana mtaa mzima kwa tabia zake za utapeli, si mwaminifu na mara zote amekuwa akifanya utapeli hata kwa watu wa mtaani kwao kabisa. Kumtaja jina lake, kulikuwa na maana mbili; ama ameshatapeliwa au anamtafuta kwa ajili ya mazungumzo ambayo mwisho wake ungekuwa utapeli. “Mbona mmeshtuka washkaji?” Bruno akawauliza, tayari kichwani mwake alishaanza kuingiwa na mashaka kidogo. “Ni ndugu yako?” Mmoja akamwuliza. “Hapana!” “Unamtafutia nini?” “Nina ishu naye muhimu, kwani vipi washkaji, mbona mnanitisha jamani?” “Siyo tunakutisha, tunataka kujua ili baadaye tusilaumiane.” “Tulaumiane kwa lipi tena? Mimi namuulizia tu ndugu zangu, mambo mengine nitajua mwenyewe!” “Poa, hesabu nyumba tatu kutoka hii, mkono wako wa kushoto, utaona nyumba yenye geti jekundu, ni hapo!” “Ok! Poa wakubwa, ahsanteni sana.” “Hamna noma!” Bruno akatoka kwa mwendo wa taratibu sana, akionekana kuanza kuingiwa na mashaka kidogo na akina Bryson. Huku nyuma aliacha mzozo... “Washkaji, yule jamaa atakuwa anakwenda kulizwa, kwanini tusimsaidie?” Dulla akawaambia wenzake. “Unamjua Bryson au unamsikia?” “Atajuaje?” “Kama wewe mwema sana, nenda kamsaidie bwana!”
0 Comments