Header Ads Widget

Responsive Advertisement

SIKUJUA UNGENISALITI MPENZI - 3



Simulizi : Sikujua Ungenisaliti Mpenzi
Sehemu Ya Tatu (3)

“Oh baby...someone is calling you!” (Oh mpenzi, kuna mtu anakupigia) Emma akasema kwa upole, haoneshi wivu kabisa.
Vanessa alipoichukua, akashtuka sana.
Alikuwa ni Bruno.
“Pick up the phone baby!” (Pokea simu mpenzi!)
Vanessa akaganda!
Haikuwa kawaida ya Emma kuchukulia kwa wepesi kama vile, kwake yeye ilikuwa maajabu sana. Yaani Emma anampa simu yake na kumwambia kuna mtu anapiga? Amebadilika kiasi gani?
Muungwana kiasi gani?
Hakika yalikuwa maajabu ya aina yake. Lakini hakutaka kuongea na Bruno, ingawa hawakuwa na mazungumzo mabaya. Alijikuta akiwa hayupo tayari kuzungumza naye tu! Akabaki anaingalia ile simu kwa muda mrefu, mpaka ilipokatika.
“Kwanini hupokei darling?” Emma akamwuliza akionekana kuwa na kauli nzuri sana kwa mpenzi wake.
“Hapana...sijisikii kuongea na mtu saa hizi.”
“Sasa si bora upokee na kumwambia akupigie kesho!”
“Achana naye darling, asikusumbue kichwa.”
“Ni nani?”

“Bwege mmoja hivi, si muhimu sana kumjua.”
“Ok!”
Vanessa akazima simu na kuirudisha mezani. Bado anashindwa kuelewa ni kwanini Emma amebadilika kiasi kile.
“Lakini sweetie, nina maswali kidogo kwako.”
“Uliza.”
“Ni kweli umebadilika?”
“Nadhani matendo yangu yanaweza kuongea zaidi kuliko mimi.”
“Ni kweli dear, lakini nataka kusikia kauli yako.”
“We’ unaonaje?”
“Kweli naona mabadiliko katika mapenzi yetu, lakini siamini kama yatakuwa ya kudumu!”
“Kwanini huamini?”
“Siamini tu!”
“Kwanini mpenzi wangu? Kila kitu kina mwanzo na mwisho wake, unajua wakati mwingine mtu unaweza kufanya makosa kwa muda, lakini ghafla ukagundua makosa yako na kubadilika. Huyo ndiye mimi. Nimegundua na nimeona ni bora nibadilike, ni vibaya baby?”
“Hapana.”
Pamoja na kuhisi kama ndoto, lakini siku hiyo ndiyo aliyofaidi zaidi penzi la Emma. Wakaufurahia vilivyo usiku huo. Kila mmoja akiwa mpya kwa mwenzake.
***
Emma alikuwa wa kwanza kuamka asubuhi, akamwamsha Vanessa na kumbusu mashavuni mwake, ikawa asubuhi nyingine njema tena kwa Vanessa. Anaamshwa?
Anapigwa busu?
Alikuwa na haki ya kushangaa, huyu si Emma wa miezi sita iliyopita. Sasa ni Emma wa kimahaba anayeonekana dhahiri kufahamu umuhimu wa mapenzi. Vanessa akafurahi sana moyoni mwake.
Akaanza kujiona naye ni mwanamke kati ya wanawake bora wanaofurahi jijini Dar es Salaam. Si mwenye simanzi tena, si mwenye kilio tena. Ni mwanamke mwenye amani ya moyo ambaye tabasamu kwake ni wimbo wenye nafasi kubwa zaidi.
“Darling, kweli umebadilika. Ahsante sana kwa kunipenda, nakupenda pia Emma.”
“Usijali mpenzi wangu, natambua uliumia sana, muda wa kuumia umeshapita, furahi pamoja nami mpenzi.”
“Ahsante sana, sasa mbona asubuhi hivi?” Vanessa akauliza akiachia tabasamu mwanana kabisa usoni mwake.
“Mbona umekaa kimya muda wote!”
“Nilishasahau mwenzio, nimenogewa na penzi jipya!”
Wakacheka tena.
“Nawahi kazini mama.”
“Lakini si kawaida yako!”
“Ni kweli, ila kuna jamaa nakutana nao asubuhi hii, nikiwakosa tu, dili linaharibika.”
“Haya baba umeshinda.”
“Sasa?”
“Nini tena zaidi ya kuondoka?”
“Nenda basi bafuni kwanza ujimwagie maji ndiyo uende.”
“Unadhani ni rahisi kutoka bila kuoga?”
“Lakini kama mkeo nina wajibu wa kukumbusha mpenzi wangu!”
“Sawa, ahsante sana mama,” akasema Emma na kumuangushia busu lingine la nguvu.
Emma akaingia bafuni.
***
Macho yake yalitosha kabisa kufikisha ujumbe wa kile kilichopo moyoni mwake, alikuwa akitazama kwa macho ya huruma, huku akionesha wazi kwamba anahisi anadhauriwa.
Bruno alikuwa ameshaanza kuhisi kwamba amekuwa mzigo kwa Vanessa, kitendo cha kutokupokea simu kilitosha kabisa kuthibitisha hisia zake hizo. Kabla hajafungua kinywa chake kusema chochote, Vanessa akamuwahi!
“Sijui nitumie kauli gani Bruno, sijui nizungumzeje Bruno, lakini nataka kukuomba msamaha kwa yote yaliyotokea jana,” Vanessa akasema kwa sauti ya kulalamika.
“Najua unanisaidia Vanessa, lakini kama nakusumbua ni bora uniambie.”
“Hapana Bruno, samahani!”
“Lakini kwanini hukupokea simu yangu?”
“Ndiyo maana nimekuomba msamaha!”
“Kama nilikuwa na tatizo kubwa?”
“Bruno please elewa, naomba unisamehe kwa hilo.”
Kimya cha muda mfupi kikapita. Kila mmoja akitafakari kivyake. Bado Bruno alionekana mwenye mawazo mengi, huku akifikiria maisha yake ya baadaye. Mwonekano wake ulionesha wazi kwamba sasa hana imani tena na Vanessa.
“Lakini nimekuja na wazo,” Vanessa akasema.
“Wazo gani?”
“Naomba uhamie kwangu, nataka kuishi na wewe nyumbani kwangu!”
“Hapana,” Bruno akajibu haraka.
“Kwanini?”
“Sitaki tu!”
“Kila kitu kina sababu!”
“Hujaolewa?”
“Bado, lakini nina mchumba ambaye huwa anakuja nyumbani kwangu!”
“Sasa itakuwaje?”
“Niachie mimi, nitamwambia wewe ni mjomba wangu, kazi ya kuongea naye ni juu yangu,” akasema Vanessa.
“Hapana, roho yangu inakataa kabisa kukubaliana na hilo...kama msaada wako umeishia hapa niambie, nitakachokuomba ni nauli tu ya kunipeleka kwetu basi!” Bruno akasema akionekana kutokubaliana kabisa na mawazo yake.
Vanessa ni kama alikuwa njia panda, maana alipata wazo la kumuhamishia nyumbani kwake ili amtunze na ikiwezekana baadaye awe mpenzi wake, kwani mabadiliko ya Emma hakuyaamini sana.
Bado alihisi penzi lake lipo kwa Bruno.
Akaampa kumsogeza kwake!
Alihitaji sana kuishi naye nyumbani kwake, aliamini kufanya hivyo, kutakuwa kunamsogeza karibu yake zaidi. Hilo ndilo lililounguruma zaidi ubongoni mwake. Akamwangalia Bruno kwa macho ya ushawishi, lakini Bruno alionekana kukosa furaha ghafla.
Alionekana wazi kutofurahishwa na uamuzi wa Vanessa, ndani ya moyo wake alifurahi sana kuona jinsi mwanamke yule mwenye upendo ambaye alijitoa kwa ajili ya maisha yake, lakini hakuwa na wazo kwamba Vanessa alikuwa akiyafanya yote yale kwasababu ya penzi lake la dhati. Hilo hakulijua kabisa.
Anazidi kumwangalia...
Macho yake yanaongea...
Hata uso wake nao unasoma kitu fulani, kitu ambacho kipo ndani kabisa ya moyo wake.
“Sikiliza Vanessa najua una nia ya kunisaidia, hilo nalijua kabisa...”
“Sasa?”
“Ingekuwa rahisi mimi kukubaliana na wazo lako, lakini mazingira hayaruhusu!”
“Mazingira kivipi Bruno?”
“Najua unapenda kunisaidia.”
“Enhee!”
“Pia nafahamu huna nia mbaya na mimi!”
“Ni kweli.”
“Lakini tayari umeshaniambia kwamba unaye mchumba na huwa anakuja nyumbani kwako mara nyingi!”
“Hujakosea kitu Bruno!”
“Sasa unadhani akinikuta atajua kuwa mimi ni rafiki yako na siyo wapenzi akaridhika kirahisi?”
“Kwani tuna nia nyingine mbaya?”
“Najua hatuna.”
“Hata siku moja kuna mmoja wetu aliyezungumza au kuonesha ana nia tofautio na mwenzake?”
“Hapana!”
“Sasa wasiwasi wa nini Bruno?”
“Yule ni mpenzi wako Vanessa, ana haki ya kuwa na mashaka na kuhoji kama kitu hakipo sawa, huoni kwamba nitakuwa navuruga mapenzi yenu?”
“Unavuruga kivipi?”
“Nimeshakuambia kila kitu Vanessa, sioni kama kuna jambo jipya ambalo sijakuambia.”
“Ok! Nimekubaliana na yote kama unavyotaka, lakini unakumbuka nimekuambia nini mwanzoni kabisa? Nitamwambia wewe ni mjomba wangu, hana mamlaka ya kunihoji zaidi, isitoshe hawajui ndugu zangu wote. Maswali mengine niachie mimi.”
Bruno akaonekana kukaa kimya akizidi kutafakari. Akavuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha taratibu, midomo yake ikaanza kutingishika. Ni dhahiri alikuwa anaongea...
“Nimekuelewa vizuri sana, lakini nina jambo lingine nataka kukuuliza.”
“Uliza tu!”
“Vipi kuhusu Bryson?”
“Bryson?”
“Ndiyo Bryson!”
“Unamaanisha nini?

“Vanessa nazungumza kuhusu mjomba wako.”
“Hafahamiani naye.”
“Sijasema anafahamiana naye, lakini si unajua kuwa nina matatizo naye.”
“Sasa kwani hayo matatizo yako na Anko Bry, yanahusiana vipi na mimi?”
“Unaona hayakuhusu?”
“Kivipi sasa?”
“Kama nakuja kuishi kwako, nyumbani kwa mtoto wa dada yake, si huwa anafika pale? Nitamwambia nini wakati nina uadui naye.”
“Halafu huwa unanichanganya sana, hivi una matatizo gani na Anko lakini?”
“Muda ukifika nitakuambia.”
“Kwanini kila siku huwa unasema hivyo na huniambii kitu?”
“Siku ya kukuambia itafika na lazima nitafanya hivyo. Hebu nikuulize kitu kimoja.”
“Niambie.”
“Unamfahamu Tunu?”
“Tunu?”
“Ndiyo Tunu wa Tanga.”
“Hapana simfahamu, lakini nimekuwa nikikusikia sana ukimtaja kila ninapokuuliza kuhusu chanzo cha matatizo yako. Ni nani?” Vanessa akauliza akiwa ameyatuliza macho yake kwa Bruno.
Ikawa kama amemwambia Bruno alie, macho ya Bruno yakaanza kubadilika rangi taratibu na kuwa mekundu, ghafla mvua ya machozi ikaanza kumiminika machoni mwake. Vanessa akazidi kupata utata.
“Kwanini unalia Bruno?” Vanessa akauliza akijisogeza jirani na alipoketi Bruno.
Bruno hakujibu!
Machozi yalijibu!
“Niambie Bruno. Una tatizo gani?”
“Tunu!” Akasema mara moja na kunyamaza.
“Amekufanya nini?”
“Bryson!”
“Mbona maneno yako yamejaa mafumbo sana, nieleze basi niweze kufahamu, kwanini unanifumba kiasi hicho Bruno?”
Akazidi kulia.
Hilo ndilo jibu pekee alilokuwa nalo. Ghafla akaonekana kuyaelekeza macho yake juu ya dari, akayagandisha huko. Akaonekana kuwaza jambo fulani zito, machozi yakizidi kulowanisha mashavu yake. Alikuwa katika lindi la mawazo. Lindi lenye mawazo mazito ya kutesa!
Ya kuumiza moyo!
Akazidi kulia...
***
Ni usiku wa tatu analala kwenye chumba hiki kizuri, chenye vitu vizuri, akiwa na mwanamke mzuri. Mrembo. Anayevutia. Mwenye macho ya kulegea, anayejua mapenzi, aliyeweza kumchanganya mtima wake.
Tunu!
Bruno aliona kama dunia nzima ni mali yake kwa manjonjo aliyokuwa akiyapata kutoka kwa Tunu. Mwanamke huyo alikuwa na kila aina ya ufundi wa kimapenzi. Alikuwa anajua anachokifanya anapokuwa na mwaume faragha. Anajua kiu ya mwanaume inavyokatwa! Tunu anajua kumfanya mwanaume atulie na kusikiliza kila atakachokiagiza faragha kwa raha na kauli zenye kuvutia masikioni.
Tunu alifanikiwa kumnasa mapenzini. Akakumbuka swali alilomuuliza asubuhi ya siku hiyo, hakukumbuka vizuri idadi ya swali hilo kwa Tunu, lakini kwa kukukisia, aliweza kugundua kwamba alimuuliza kwa zaidi ya mara kumi na tano. Swali gumu kwa muulizaji, lakini jepesi sana kwa anayetakiwa kujibu.
“Hivi ni kweli hujaolewa?” Alimwuliza, akimtazama usoni.
“Nikuambie mara ngapi sina mume?”
“Tunu kweli?”
“Sema nifanye nini ili uniamini!”
“Basi nakuamini, lakini napenda sana kujiridhisha, huwa sipendi matatizo yasiyo ya lazima. Enhee, huna hata mchumba?”
“Sina Bruno.”
Hayo ni mazungumzo waliyoongea asubuhi ya siku hiyo, ambayo yalizidi kumpa matumaini kwamba hayupo katika penzi la wizi. Hilo aliliamini kwa asimilia mia moja!
Yupo kitandani mtupu, akiwa anacheza michezo ya kimahaba na Tunu, mara mlango unagongwa! Mgongaji anagonga kwa kasi zaidi.
Anamwangalia Tunu ambaye alikuwa anahema kwa kasi akiwa ameyatoa macho. Akachukua upande wa kanga na kusogea mlangoni.
Akafungua!
“Mume wangu!” Tunu akapiga kelele.

Bruno akabaki anatetemeka akiwa hajui la kufanya. Alikuwa ameingia kwenye matatizo mapya. Alijua vizuri adha ya kufumaniwa.
Mara akaingia mwanaume mwenye miraba minne, akiwa anaonekana dhahiri kupigwa na butwaa na alichokiona.
Alikuwa ni Bryson.
***
“Sikiliza Vanessa, sitaki kwenda kuishi kwako!” Bruno akasema kwa hasira akimwangalia Vanessa usoni bila kupepesa macho.
“Kwanini?” Vanessa akauliza kwa mshangao.
“Nimesema sitaki tu!”
“Sawa hutaki, kuna nini?”
“Mbona huelewi, sitaki!”
Macho ya Bruno yanaonesha kilichomo ndani ya moyo wake, yanasema na kuweka kila kitu bayana. Anaonekana kuwa katika bahari kubwa yenye mateso na simanzi, yupo katikati ya msitu wenye wanyama wakali wasio na huruma!
Yanasema...
Kwamba mzigo alionao ni mkubwa kuliko nguvu zake. amelemewa sana, lakini mbaya zaidi ni kwamba, hayupo tayari kutua mzigo huo na kumpa mwingine amsaidie, na kama anafaya hivyo ni kwa kupunguza kilo moja moja wakati mzigo alionao ni wa kilo elfu moja!
Machozi machoni!
Huzuni moyoni!
“Lakini Bruno, kwanini unakuwa hivyo?” Vanessa akamwuliza tena.
“Nateseka!”
“Na nini?”
“Naumia.”
“Kivipi?”
“Nanyanyasika!”
“Sawa sema basi kwa namna gani?”
“Tutazungumza siku nyingine!”
“Kwanini kila siku huwa unasema hivyo na hujawahi kutimiza hiyo ahadi?”
“Kwasababu hiyo siku haijafika, ikifika nitafanya hivyo!”
“Bruno...” Vanessa akaita kwa sauti ambayo sasa ilisema.
Alishaamua kuonesha kitu tofauti kidogo, sauti yake ilikuwa ya kimahaba yenye kusihi na kuomba kukubaliwa ombi lake. Ni sauti hiyo ndiyo iliyonasua mgando akilini mwa Bruno na kuanza kuhisi kitu kingine zaidi katika msaada wa mrembo yule!
Yeye si mjinga!
Si mshamba!
Ni mwerevu!
Tena aliyeerevuka na kufahamu mambo yanavyokwenda! Kwahiyo hata hapo alijua kuna kitu. Kitu ambacho kinaweza kuwa kizuri na wakati huo huo pia kinaweza kuwa kibaya. Kipo kitu. Alijua kabisa kwamba sasa Vanessa alikuwa anaelekea kwenye mapenzi!
Akakaa vizuri kitandani, akiyatazama macho ya Vanessa yanavyotazama. Naam! Yalikuwa yanatazama kimapenzi, hata midomo yake, ilikaa kimapenzi. Kila kitu kilikuwa kimapenzi-mapenzi. Akaamua kurahisha mambo...
“Najua unachotaka kuniambia...” Bruno akasema kwa kujiamini.
“Ni nini?”
“Ni juu ya kwenda kuishi kwako!”
“Kweli kabisa, hakuna ulichokosea.”
“Ninalo swali moja.”
“Uliza.”
“Unanihakikishia usalama wa maisha yangu?”
“Kabisa.”
“Utahakikisha unamfanya mchumba wako aamini kwamba mimi ni mjomba wako?”
“Ndiyo!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Ok, nimekubali kwenda kuishi na wewe!”
“What?”
“Mbona umeshtuka, kwani ni ajabu sana?”
“Tumetumia muda mrefu sana kujadili jambo hili na wewe umeendelea kukazania kwamba hutaki, lazima nishtuke, ahsante sana kwa kukubaliana na mimi. Nashukuru kwa hilo.”
“Usijali, Tuondoke au?”
“Ndiyo, kwani kuna nini tena?”
Wakacheka pamoja. Kilichofuata ilikuwa ni kukusanya nguo zote na kuweka kwenye begi, kisha Vanessa akapiga simu Mapokezi, waliokuja kumsaidia kumshusha Bruno hadi chini na kumpeleka kwenye gari. Akaketi kushoto kwa dereva.
“Ahsanteni sana...” Vanessa akawashukuru wale dada wa Mapokezi, akiondoa gari taratibu.
“Karibuni tena...” mmoja wao akasema.
Bruno akatoa mkono wake dirishani na kuwapungia. Kwa muda mfupi aliokuwa akiishi pale hotelini, walikuwa wameshazoeana sana.
***
Ilikuwa nyumba nzuri ya kuvutia, yenye maua yaliyopandwa katika mpangilio wa kupendeza. Kila kitu kilikuwa kizuri kwake, kuanzia getini, alikuwa akifurahia uzuri wa rangi. Sasa anaingizwa sebuleni, anakutana na sofa za kisasa zilizonakshiwa na vitambaa vizuri juu yake!
Bruno akawa anashangaa kila kitu, ilikuwa nyumba nzuri ambayo si rahisi kuamini kwamba ilimilikiwa na mwanamke. Lakini ndivyo ilivyokuwa.
“Karibu sana Anko, jisikie huru...” Vanessa akamwambia Bruno mara baada ya kuingia ndani.
“Ahsante sana mpwa wangu, umejitahidi sana...hongera!”
“Kawaida, nashukuru lakini kwa pongezi Anko!”
“Ok!” Akajibu akiendelea kutembeza macho yake kila kona ya nyumba ile nzuri yenye samani za kupendeza ndani!
“Amina...huyu ni mjomba wangu, alipata ajali na kuvunjika mguu, kwa bahati mbaya amekatwa. Tutakuwa naye hapa nyumbani akiendelea kujiuguza!” Vanessa akamwambia msichana wake wa kazi.
“Sawa dada...” akaitikia kwa heshima na kumsalimia Bruno: “Shikamoo Anko!”
“Marhaba!”
“Anko huyu ni Amina, ananisaidia kazi hapa nyumbani!”
“Ok, nimefurahi kumfahamu.”
Kilichofuata ilikuwa ni kupelekwa chumbani na kuoneshwa chumba chake cha kulala. Kilikuwa na kila kitu ndani.


“Hiki kitakuwa chumba chako cha kulala, kuna kila kitu ndani!” Vanessa akamwambia Bruno.
“Ahsante sana Vanessa, nashukuru sana kwa kunijali.”
“Usijali.”
Akamwacha chumbani kwake, akarudi sebuleni. Chakula kilipokuwa tayari akaenda kumwita, wakaungana pamoja sebuleni na kupata chakula. Baada ya hapo ikawa ni kuangalia filamu za kibongo, stori za hapa na pale zikiendelea.
***
Saa 5:30 za usiku Emma alikuwa akipiga honi getini mwa nyumba ya Vanessa, Amina akatoka na kwenda kumfungulia. Akaingiza gari ndani na kushuka akielekea sebuleni.
Macho yake yakakutana na Bruno. Akapigwa na butwaa, moja kwa moja aliamini kwamba mwanaume yule alikuwa na uhusiano na Vanessa.
Hakumsalimia mtu pale sebuleni, akapita moja kwa moja hadi chumbani. Vanessa akasimama na kumfuata nyuma. Alipobamiza mlango wa chumbani, naye akaufungua na kuingia.
“Umeshaanza umalaya wako, umeona kuwa naye huko nje hakutoshi, sasa umemuhamishia nyumbani kabisa, eneheeeee....” Emma akafoka kwa hasira.
“Ndiyo salamu yako?” Vanessa akajibu akionesha kutojali.
Emma hakuongea kitu chochote zaidi ya kuinua mkono na kushusha kibao kizito shavuni mwa Vanessa. Kibao kimoja tu, kilimdondosha Vanessa chini, Emma akavua mkanda kiunoni, akijiandaa kuendelea kutoa kipigo!
Emma alidhamiria kumuumiza Vanessa, alikuwa hachagui mahali pa kupiga, alivua mkanda kiunoni na kuendelea kumchapa kila kona ya mwili wake, pamoja na kilio alichokuwa akitoa Vanessa, lakini Emma hakuonekana kujali!
“Wewe unajifanya malaya, sasa nitakukomesha!”
“Nani malaya Emma, nani malaya?”
“Wewe!”
“Umenifumania?”
“Huyo mwanaume hapo sebuleni ni nani? Unaniletea wanaume hadi nyumbani, leo nitakuua!” Emma alisema na kuendelea kumpiga Vanessa ambaye alizidi kuomba aachwe lakini Emma ni kama aliweka pamba masikioni mwake.
Baadaye Emma akaacha kumpiga na kukaa kitandani, Vanessa naye kwa taabu sana akaketi kitandani akizidi kulia.
“Kwanini unanipiga bila kosa Emma?”
“Unataka kosa gani lingine zaidi ya hili la kuniletea wanaume nyumbani?”
“Una uhakika gani kuwa yule ni mwanaume wangu!”
“Nina uhakika!”
“Kivipi?”
“Unafikiri mimi sijui kinachoendelea?” Emma akasema.
Kidogo Vanessa akashtuka, akiamini huenda Emma alikuwa anajua kila kitu.
“Unajua nini?”
“Najua sana...najua kila kitu!”
“Sasa kwa taarifa yako yule ni Anko wangu!” Vanessa akasema kwa kujitahidi kidogo, maana alikuwa anadanganya!
“Nani?”
“Mjomba!”
“Ni mjomba wako yule?”
“Kwahiyo hujanisikia au hujapenda?”
“Nataka kujua!”
“Tena anaumwa, alikuwa nyumbani na sasa amekuja kwangu kujiuguza, maana huku Hospitali nyingi!”
“Kweli?”
“Nina utani na wewe?”
Emma akanyamaza kimya, akaonekana kuanza kuingiwa na maneno ya Vanessa, tayari ndani ya nafsi yake kulishaingiwa na huruma pamoja na kujilaumu!
Mjomba wake?
Halafu anasema ni bwana’ke?
Aibu kiasi gani?
Uonevu kiasi gani?
“Baby, ni kweli unayosema?” Emma akamwuliza akiwa na sauti ya kimahaba ambayo ilikuwa inahitaji msamaha.
“Nashukuru kwa kunipiga bila kosa...”
“Siyo hivyo, ni mapenzi tu baby!”
“Mapenzi ya kupigana?”
“Sasa nilijua ni mwanaume wako, ndiyo maana nikachukia na kushikwa na hasira!”
“Sasa umegundua nini?”
“Ni mjomba wako!”
“Baada ya kunipiga siyo? Kwani ungeuliza kabla ungepungua wapi?”
“Nisamehe!”
“Umeshaufanya mwili wangu ngoma, kila siku unaudunda unavyotaka, kwanini unanifanyia hivi lakini? Kwanini unaninyanyasa? Ni lini nitakaa kwa amani?”
“Vanessa ndiyo maana nimekuomba samahani mpenzi wangu!”
“Samahani wakati nimeshaumia?”
“Najua baby, lakini bado nahitaji msamaha wako!”
“Kwahiyo kosa langu ni kukupenda siyo?”
“Sina maana hiyo!”
“Emma naona huu uwe mwisho wetu, kama unaweza kunitukana na kusema natembea na mjomba wangu, naona haya mapenzi yetu yafikie tamati, hatuwezi kwenda kwa staili hii. Inaniuma sana, kila siku unanipiga, sina amani na haya mapenzi, naona tufikie mwisho.”
“Hapana sweetie,” Emma akasema, lakini Vanessa akamkatisha haraka.
“Sitaki Emma, naona umeona mwili wangu ngoma, sikutaki tena!” Vanessa alisema akionesha kuwa na hasira kuliko kawaida.
Kazi ya Emma kumbembeleza Vanessa ilikuwa kubwa sana, lakini hapakuwa na dalili za kuelekea kwenye makubaliano. Vanessa aliendelea kushikilia msimamo wake, lakini moyoni alikuwa na lengo lingine kabisa. Alitaka kuachana na Emma ili aanzishe uhusiano mpya na Bruno.
***
“Vipi mbona kama nasikia zogo?” Bruno akamwuliza Amina pale sebuleni.
“Ni kweli mjomba, hujasikia vibaya!”
“Wanagombana au?”
“Ndiyo...lakini ni kawaida yao, baada ya muda mfupi utashangaa wakiwa kimya kabisa!”
“Sababu ni nini?”
“Sijui na sijawahi kufahamu hata mara moja, kwasababu mambo yao ya ndani wanayajua wenyewe!”
“Ok! Nimekuelewa!”
Mara wakiwa wanaendelea kuzungumza, Vanessa akatamalaki sebuleni, nyuma yake akija Emma. Vanessa akaketi kwenye kiti akionekana kuwa na mawazo sana. Akili yake haikuwa sawa, hakupendezwa na tabia ya Emma ambayo ilikuwa ni kumuangushia kipigo kila wakati.
“Emma, huyu ni mjomba wangu, anaitwa Anko Bruno!” Vanessa akasema akionekana kupoteza furaha yake kabisa.
“Nimefurahi kumfahamu!” Emma akasema.
“Hata mimi pia!” Bruno naye akadakia.
“Anko, huyu ndiye mchumba wangu, anaitwa Emma!”
“Ok! Nimefurahi kukutana naye!”
“Na mimi pia.”
Ulikuwa utambulisho usio na furaha, ambao kila mmoja aliweza kugundua hilo, hivyo mazungumzo hayakuwa mengi sana, walikwenda kulala.
***
Usiku Vanessa aliamka kwa siri na kufungua mlango kisha akatoka nje, akiwa varandani, akaanza kupiga hatua za taratibu kuelekea kwenye mlango wa kuingia kwenye chumba cha Bruno.
Ni saa nane usiku!
Akagonga kwa hadhari, Bruno akafungua!
“Vipi usiku huu, kuna nini?” Bruno akauliza akitetemeka kwa hofu.
“Shiiiiiiii....” Vanessa akamnyamazisha.
Vanessa akaingia. Kwa Bruno alitamani kila kitu kiwe ndoto, lakini hilo halikuwezekana, ilibaki kuwa kweli, kwamba Vanessa ameingia chumbani kwake usiku huo, akimuacha mwanaume wake ambaye ni mkorofi! Hiyo ilikuwa ishara mbaya kwa Bruno, ambaye alianza kuona matatizo ya wazi kabisa mbele yake!
Papo hapo, kumbukumbu asizozipenda zikamrudia tena, kumbukumbu za Tunu, mwanamke wa Kitanga ambaye ndiye chanzo cha ulemavu aliokuwa nao.
“Vanessa rudi chumbani kwako!”
“Nyamaza Bruno, please tulia, Emma asije akasikia!”
“Kwanini unafanya hivi lakini?”
“Usijali, nina jambo la muhimu kidogo!”
“Jambo la muhimu?!”
“Ndiyo!”
“Kwanini tusizungumze kesho!”
“Hapana, nimechagua muda huu!” Akajibu Vanessa kwa kujiamini.
Bruno akapata wakati mgumu sana, hapo akagundua kuwa, Vanessa aliamua kumfanyia hivyo baada ya kuwa tayari yupo katika himaya yake, lakini hapo alipata picha ya wazi kwamba Vanessa alikuwa anampenda na ndiyo maana akamfanyia wema wote ule!
Yes, alimpenda!
Hakuwa mwanaume mjinga wa kiwango hicho, mwanaume asiyeweza kujua hisia za mwanamke. Kwanini amsaidie kiasi kile. Kwanini aoneshe uungwana zaidi kwake. Kwanini?
Hakuwa ndugu yake!
Hakuwa rafiki yake!
Nini basi kilimsukuma kumsaidia kwa kiwango kile? Hapo akapata jibu moja tu, mapenzi! Ni kweli yalikuwa mapenzi maana anajijua jinsi alivyo na mshawasha wa kimahaba. Lakini kichwani alikuwa na mawazo sana, yawezekana vipi yeye apendwe leo?
Haikuwa ajabu zamani zile, enzi za utanashati wake! Enzi za kuzungumza kwa sauti ya kuremba, sauti iliyonakshiwa na tungo na semi za kimjini! Haikuwa ajabu! Lakini si leo!
Akiwa mlemavu!
Asiye na kitu!
Apendwe?

Akazidi kuchanganyikiwa. Vanessa alikuwa amemuacha mwanaume mtanashati zaidi yake chumbani, tena mwanaume wake wa kila siku ambaye ana wivu na anamwonesha mapenzi motomoto. Akamfuata yeye. Kwake bado alikuwa anahisi kama yupo ndotoni.
Alitakiwa kujiridhisha kama ni kweli hakuwa ndotoni. Akaketi kitandani, akajikongoja hadi kwenye switch ukutani. Akawasha taa! Macho yake yakakutana na umbo la mwanamke mrembo sana. Alikuwa ni Vanessa.
Vanessa usiku huo alikuwa amevalia gauni la kulalia, gauni jepesi ambalo liliweza kuonesha vizuri sana bikini yake iliyokuwa imeshikiliwa na mikanda midogo! Bruno akachachawa! Hapo akagundua kwamba kumbe Vanessa alikuwa mzuri zaidi ya vile alivyokuwa akifikiria.
Kwamba alikuwa akimwangalia kwa wasiwasi na huyu aliyepo mbele yake, alikuwa Vanessa halisi. Vanessa mrembo. Vanessa mwenye umbo namba nane. Vanessa mwenye rangi ya asili. Vanessa mwenye kiuno chembamba. Vanessa mwenye hipsi za kutosha. Vanessa mwenye miguu ya kuvutia.
Vanessa!
Alikuwa Vanessa original!
Moyo wake ukaenda kwa kasi sana, akaona kabisa jinsi ambavyo angekwenda kufanya kitu ambacho moyo wake haukuwa tayari. Aliona hatari hiyo. Haraka akabadilisha hisia zake, akamng’akia Vanessa...
“Vanessa ni hatari sana kuwa hapa muda huu, akija bwana’ko unadhani itakuwaje?”
“Najua Bruno, lakini miye nimekuja kwa ajili ya jambo moja tu!”
“Jambo gani?”
“Mh! Bwana, mbona unakuwa mkali hivyo? Twende polepole.”
“Nakuwa mkali kwasababu naona unataka kunisababishia matatizo!”
“Acha utoto, wewe ni mtu mzima sasa, unamwogopa nani? Kumbuka hapa ni kwangu, si kwa Emma!”
“Hata kama!”
“Sikiliza Bruno, kubali basi nilichojia!” Sauti ya Vanessa ilikuwa imepoa sana, lakini macho yake nayo yalitoa taswira nyingine mpya.
Vanessa alikuwa anataka penzi!
“Nini, sema basi!”
“Busu!”
“Busu?”
“Ndiyo nimekuja hapa kwa ajili ya kupata busu lako tu, tafadhali sana naomba unibusu, halafu nitaondoka!”
Maneno ya Vanessa yakamchanganya Bruno, ni muda mrefu sana hajambusu mwanamke. Kumbukumbu zake zilimwambia kwamba, mwanamke wa mwisho yeye kumbusu alikuwa ni Tunu, ambaye ndiye alikuwa mwanzo wa yeye kuanza kuwachukia sana wanawake. Leo hii anahisi afanye hivyo. Anaona anapoteza kitu muhimu sana.
“Busu tu!” Akatamka Bruno kwa haraka, lakini kinywa chake kikionekana kushindwa kuhimili vyema kutamka maneno yale.
“Yes, only kiss!”
“Haya sogea!”
“Sogea wewe!”
Wakabishana sana, kila mmoja akimtaka mwenzake asogee, lakini mwishowe, Vanessa akamsogelea, akapeleka shavu lake kwa Bruno, akambusu, baadaye naye akambusu. Wakanata kwa muda wakiangaliana, mara Vanessa akamvamia Bruno. Akaupeleka ulimi wake kinywani mwake.
Bila kutegemea, Bruno akaupokea. Wakaanza kunyonyana ndimi. Ni zoezi hilo ndilo lililosababisha wote kujikuta wameingia kwenye dimbwi la mapenzi. Emma akiwa chumbani kwa Vanessa. Hakujua yaliyokuwa yakifanyika chumbani kwa ‘Anko Bruno!’
***
Anatembea kwa hadhari kubwa sana kwenye korido, anaufikia mlango wa chumba chake. Vanessa akaganda kwa muda akimsikilizia Emma kama alikuwa ameamka! Kama ingekuwa hivyo, asingekuwa na ujanja, maana kama ni choo, kilikuwa chumbani!
Akafungua mlango taratibu sana, kisha akaubana kwa kitasa! Alivyokuwa anamalizia kufunga, akashtushwa na sauti ya Emma akikohoa. Alipogeuza shingo, akakutana na macho maangavu ya Emma!
Hofu tupu!
Emma akazidi kumwangalia Vanessa kwa macho yanayoonesha kwamba alishajua kila kitu. Vanessa akaingiwa na woga wa ghafla. Isingekuwa rahisi kujitetea.
Ametoka wapi?
Swali hilo lingetosha kumbana, maana hata nguo aliyokuwa amevaa ni ya kulalalia. Vanessa alikuwa na wakati mgumu sana wa kujitetea.
“Baby vipi?” Vanessa akajibaraguza.
“Nikuulize wewe!” Emma akajibu.
“Kivipi?”
“Kwani kuna nini?”
Vanessa akaketi kitandani kivivu, kisha baadaye akaamua kulala kabisa. Akamsogelea Emma na kumkumbatia! Kwa muda mfupi sana aliweza kugundua kwamba Emma alikuwa hajafahamu kinachoendelea!
“Ulienda wapi?”
“Toilet sweetie, kwani vipi?”
“Nothing, nilitaka kujua!”
“Poa!”
Emma hakujua kilichoendelea, lakini wasiwasi wa Vanessa ulianza kumtia mashaka kidogo. Alianza kuhisi kwamba kuna kitu kilichokuwa kikiendelea kimya kimya!
Kitu gani?
Hakujua!
Wakalala kila mmoja akiwa na lake kichwani, Vanessa akijipongeza kwa kumzidi akili Emma wakati Emma akiwa na mawazo kidogo kuhusu Vanessa. Mashaka yake yalisababishwa na hali ya ghafla aliyokuwa nayo Vanessa.
Hata kama ungekuwa ni wewe, lazima ungehisi kitu fulani kinaendelea.
“Ana nini?” Akawaza, lakini jibu bado lilikuwa gumu kupatikana.
***
Bruno alibaki na makovu moyoni mwake, hakuwa tayari kulala na Vanessa, lakini kwasababu ya ushawishi akajikuta ameingia kwenye mtego. Vanessa alipoondoka mle chumbani na Bruno kupata muda wa kutafakari zaidi, aliweza kugundua kwamba alifanya kitu cha hatari sana.
Alikuwa mlemavu, halafu anafanya vitu vya hatari kama vile, chumbani kwa mtu, tena mwenye mali akiwa chumbani kwake, lilikuwa kosa kubwa sana.
Kwa mara nyingine tena, Bruno akaingia kwenye kumbukumbu za mateso, kumbukumbu zile zile ambazo hapendi kuzikumbuka kila wakati.
Kumbukumbu za majonzi!
***
Alipoinua macho yake juu, akakutana na sura ngumu ya mwanaume huyu wa miraba minne. Alionekana dhahiri kutaka kufanya kitu kibaya sana. Mwanaume huyu ambaye hana huruma.
Mwanaume wa shoka!
Alikuwa ni Bryson!
Akayarudisha macho yake na kumwangalia mwanamke aliyekuwa naye chumbani. Mwanamke huyu alikuwa akilia sana miguuni mwa Bryson!
Alikuwa ni Tunu, ambaye alikuwa akilia chini ya miguu ya Bryson, akiomba asamehewe!
“Nisamehe mume wangu, ni shetani tu alinipitia!” Tunu akasema akilia.
Alikuwa akilia machozi, tena bila kutania. Bruno anajua vizuri sana adha ya kufumaniwa. Anajua vizuri sana hasira za wafumaniaji. Kwahiyo pale alikuwa amefumaniwa na mwenye mali, ambaye alionekana kuwa na hasira ambayo si ya kutafuta!
Bryson alikuwa amevimba!
“Samahani bro...” Bruno akaanza kujitetea.
“Samahani ya nini? Una nini cha kuniambia we’ mwanaharamu?!”
“Ninacho brother, ni vyema unisikilize kwanza.”
“Kwanza nafanya makosa sana kuzungumza na ninyi bila mashahidi. Ngoja kwanza nikachukue mashahidi ndiyo tuzungumze vizuri, lakini unatakiwa kufahamu, leo nitakufanya kitu kibaya sana ambacho hujawahi kufanyiwa katika maisha yako yote. Hilo nakuhakikishia!”
“Usifanye hivyo bro!”
“Pumbavu, nyamaza wewe. Mi’ naongea na wewe unaongea. Umekuwa nani? Nani wewe?” Bryson akafoka kwa hasira.
Ghafla akasimama na kuufuata mlango, kisha akaubamiza kwa nguvu, kabla ya kuufunga kwa kitasa!
“Lakini Tunu mbona hukuwahi kuniambia kama umeolewa?” Bruno akamwuliza Tunu akizidisha uoga.
“Nyamaza Bruno!”
“Ninyamaze kivipi? Unadhani huyo mumeo atanifanya nini hapa kama siyo kuniua?”
“Tunatakiwa kujadili tatizo, sio kulaumiana saa hizi!”
“Lakini kwanini unanisababishia matatizo ambayo si ya lazima?”
Tunu akakaa kimya.
Wakiwa wapo kwenye mabishano, wakasikia mlango ukifunguliwa, baadaye kidogo, sura za watu wanne zikatamalaki mle ndani. Sura hizi zilikuwa mbaya kuliko kawaida. Siyo ubaya wa sura wala mtazamo, ila zilikuwa sura ambazo zimejiandaa tayari kwa lolote!

Sura za kazi!
Walikuwa ni vijana watatu wakiongozwa na Bryson.
“Ndiyo huyu?” Mmoja wao akauliza.
“Ndiyo!” Bryson akajibu.
“Sasa bro, wanawake wote huko barabarani hukuwaona mpaka ukaona utembee na mke wa mshkaji wetu!”
“Siyo hivyo ndugu zangu, huyu hakuniambia kama ameolewa!”
“Hiyo ni hoja dhaifu sana kueleweka na kama unadhani utaeleweka, nataka kukuambia kwamba umeongea kitu cha kipumbavu kuliko kawaida,” akasema mmoja wa vijana wale.
“Kwanini?” Bruno akauliza akionekana kuwa na mashaka sana.

ITAENDELEA

Post a Comment

0 Comments