Header Ads Widget

Responsive Advertisement

SIKUJUA UNGENISALITI MPENZI - 5



Simulizi : Sikujua Ungenisaliti Mpenzi
Sehemu Ya Tano (5)

Dulla akatoka nje haraka, kisha akampigia mbinja Bruno, ambaye alisimama, akiwa hatua chache kabisa kabla ya kulifikia geti la akina Bryson. Akamfinyia mkono akiashiria kwamba anamwita, Bruno akamfuata.
“Vipi?” Bruno akauliza.
“Wewe si una usafiri?”
“Ndiyo!”
“Nakuomba sana, hebu tuondoke kwanza maeneo haya, halafu nizungumze na wewe kuhusu huyo Bryson unayemtafuta!”
“Kwani vipi?”
“Nisikilize mimi!”
Bruno hakubisha zaidi, akaongozana naye hadi kwenye gari, wakaingia na kurudi hadi mjini kabisa. Wakaachana na dereva taxi, wakaingia kwenye baa moja na kuagiza vinywaji.
“Wewe ni ndugu yangu kaka, huyo Bryson unayemtafuta ni tapeli, sasa nimeona ni vyema nikueleze mapema ili kama ni mambo ya pesa uachane naye kabisa!”
“Ni tapeli?”
“Tena mkubwa!”
“Mungu wangu!”
“Kwani vipi, kuna pesa yoyote uliyompa?”
“Ndiyo...”
“Shilingi ngapi?”
“Milioni tano na hapa nilikuwa nampelekea nyingine moja!”
“Za nini sasa?”
“Alinifumania na mkewe!”
“Mungu wangu, hana mke yule, mke mwenyewe ni nani?”
“Ni...”
Bruno akaanza kusimulia kisa kizima, jinsi alivyokutana na Tunu kwa mara ya kwanza na jinsi alivyofumaniwa na Bryson akiwa na wenzake na kusema kwamba ni mkewe!
“Kaka umeibiwa...kwanza kama ni mkewe, kwanini haishi naye? Na hata pale siyo kwake ila huwa anakwenda mara nyingi, huyo Tunu mwenyewe unayemsema ni tapeli sugu, yaani umeibiwa ndugu yangu, lakini bora hiyo moja imebaki!”
“Sasa utanisaidiaje ndugu yangu?”
“Nenda Polisi, chukua askari uende nao pale, unaweza kumkamata maana alikuwa pale!”
“Sawa, nisaidie basi kaka!”
“Twende Chumbageni.”
“Poa.”
Wakatoka na kuachana na kila kitu pale baa, wakaenda zao katika Kituo Kikuu cha Polisi Chumbageni.
***
“Oyaaa wazee dili limebuma!” Bryson alikuwa akiwaambia wenzake.
“Kivipi?”
“Yule boya, atakuja na Polisi muda si mrefu, kuna mjinga-mjinga ameshaunguza picha!”
“Sasa?”
“Sasa nini? Kila mtu si ameshapata mgawo wake, hapa ni kujichenga tu, mimi hapa ni buti hadi Dar, Tanga si mahali salama tena kwangu!”
“Poa, mimi natambaa zangu Korogwe,” mwingine akadakia.
“Mie Moshi.”
Ndani ya nusu saa, kila mmoja alikuwa kwenye basi kwa safari ya kwenda sehemu aliyoona inafaa kujificha.
***
Gari lililojaa maaskari liliingia maeneo ya Sahare kwa kasi sana asubuhi hiyo, wakatafuta kwenye ile nyumba lakini hawakuwepo. Bruno akatoa wazo, kwamba waende Mabawa anapoishi Tunu, huko ndipo kulikuwa na vichekesho!
Tunu alikuwa amehama tangu usiku wa kuamkia siku ile.
“Amehamia wapi?” Mmoja wa askari wale akauliza.
“Alisema anahama mkoa kabisa.”
“Anakwenda wapi?”
“Arusha!”
“Arusha?!” Bruno akauliza bila kutarajia.
Akaketi chini na kuanza kulia kwa uchungu! Si fedha zote kati ya zile alizowapa akina Bryson zilikuwa zake, pale alikuwa na milioni moja na laki mbili tu! Zingine zilikuwa za kampuni. Tayari alishaona amepata hasara kubwa tena bila sababu.
“Usilie nyamaza, kulia hakutakusaidia kitu kama hatutabuni mbinu za kuwatia mikononi mwa dola kwanza!”
Maneno yale hayakuwa tiba yoyote kwa Bruno, tena ndiyo yalizidi kumwongezea simazi moyoni mwake. Hapakuwa na msaada zaidi kutoka kwa maaskari wale, hivyo akaachana nao, yeye na Dulla wakarudi kijiweni. Wakapata taarifa kwamba Bryson amekimbilia Dar.
“Sehemu gani?” Bruno akamwuliza kijana aliyemwambia.
“Usinitaje lakini!”
“Usijali, itakuwa siri.”
“Kwao ni Ilala-Bungoni, ni maarufu sana, kuna duka moja la spea za pikipiki linaitwa G8, kwenye kituo cha daladala, pale ndiyo kijiweni kwake, akishaharibu huku anakimbilia kule, anatulia mpaka soo likipungu anarudi!”
“Ahsante sana mzee, lazima niende Dar leo leo!” Bruno akamwambia Dulla.
“Dar?”
“Ndiyo!”
“Unadhani utampata?”
“Naamini hivyo!”
Jioni ile ile, Bruno alipanda basi la Raha Leo na kwenda Dar es Salaam, hakumuaga mtu yeyote zaidi ya Dulla. Wafanyakazi wenzake aliotoka nao Mwanza hakutaka kuwaeleza juu ya kilichotokea. Alifika Dar usiku wa saa tatu na dakika zake.
Hakuwa mgeni wa jiji, kwahiyo aliamua kuchukua daladala za Kariakoo, akashuka Magomeni – Usalama. Akatembea kwa miguu hadi kwenye mataa na kwenda kwenye kituo cha Magomeni - Kanisani.
Hazikupita dakika tatu, daladala iliyotoka Kawe kuelekea Buguruni ilipita. Bruno akaingia na kutulia kwenye siti. Akashuka kituo cha Bungoni akiwa amechoka sana. Zoezi la kwanza kufanya ni kuangalia lile duka la spea za pikipiki la G8 alilokuwa ameelekezwa.
Hakuchukua muda mrefu sana alifanikiwa kuliona, maana lilikuwa barabari kabisa. Hata hivyo lilikuwa limefungwa!
“Ok! Sasa nimeshajua pa kuanzia, ninachotakiwa kufanya hapa kwanza ni kutafuta mahali pa kulala, halafu mambo mengine yatafuata baadaye,” aliwaza Bruno akiondoka pale Bungoni.
Akachepuka kwenye mitaa miwili mitatu, kisha akaona gesti moja nzuri iliyomvutia. Akaingia na kulipa, akaenda chumbani kwake. Kwanza alioga, kisha akatoka nje kutafuta chakula, baadaye akarudi na kulala. Kitu kimoja kikiutawala ubongo wake; kumpata Bryson!
***
Saa mbili kamili za asubuhi Bruno alikuwa yupo kwenye soko la Mchikichini, Ilala – Boma, kazi kubwa iliyompeleka pale ilikuwa ni kutafuta jaketi na kofia. Aliponunua vitu hivyo, akavaa pale pale. Akaona bado kuna upungufu kidogo, akanunua miwani ya jua na kuvaa.
“Yes, hapa hawezi kunitambua,” akawaza akianza kutembea kwa miguu taratibu kuelekea kwenye mataa ya Boma.
Alitembea taratibu hadi Bungoni, akakaa kwenye Grocery moja iliyokuwa upande wa pili, akaanza kunywa bia zake taratibu huku macho yake yakiwa yanaangalia pale kwenye duka la spea.
Hadi kufikia saa saba mchana, bado hakumuona Bryson akitokea. Hilo likazidi kumuumiza sana kichwa chake. Muda wa kula ukafika, akala lakini bado hakufanikiwa kumuona. Alijua wazi kwamba hakutakiwa kumuulizia, kwani kwa kufanya hivyo asingeweza kumpata!
Saa tisa za alasiri akaamua kurudi zake chumbani kwake. Akaoga na kulala kidogo, saa kumi na mbili akatoka na kwenda moja kwa moja hadi kwenye duka la spea. Akajongea taratibu hadi dirishani.
“Habari yako brother?” Bruno akamsalimia.
“Poa, shwari?”
“Nipo poa.”
“Niambie kaka, unahitaji nini?”
“Samahani nina ndugu yangu namuulizia!”
“Nani?”
“Anaitwa Bryson, ni mjomba wangu!”
“Huna simu yake?”
“Nimepoteza!”
“Kwani wewe unatokea wapi?”
“Morogoro.”
“Hebu eleza ukweli kidogo bwana, ni ndugu yako au una ishu naye?”
“Hapana ni ndugu yangu, kama nilivyokuambia ni Anko wangu!”
“Kwanini umekuja kuulizia hapa?”
“Yeye mwenyewe aliniambia kwamba hapa ndiyo kijiweni kwake.”
Bruno alikuwa makini sana kujibu maswali ya yule mhudumu kwa umakini mkubwa ili aweze kumweleza ukweli. Yule kaka akamwangalia kwa muda akiwa kimya kabisa. Ni kama alikuwa akijifunza vitu fulani kupitia macho yake.
“Sikia...wewe ni mwenyeji sana hapa Dar?”
“Siyo sana, lakini kidogo naijua mitaa.”
“Unajua Club ya Wazee.”
“Hapana, iko wapi?”
“Utavuka barabara hapo, halafu pandisha nayo moja kwa moja, utaona miti mingi ya mijohoro kushoto kwako, hapo ndiyo Club ya Wazee!”
“Enhee!”
“Tangu jana Bryson amekuwa akishinda pale akinywa na marafiki zake.”
“Ok! Kaka nashukuru sana, ngoja niende,” Bruno akasema akiondoka taratibu akifuata maelekezo aliyopewa.


Hakupotea, muda mfupi baadaye alikuwa akiingia kwenye ile baa. Akiwa ndiyo kwanza anataka kuingia ndani, akamuona mtu kama Bryson akiingia kwenye taxi moja iliyokuwa kwenye maegesho, alipojaribu kumuangalia vuzuri, akagundua kwamba hakuwa akimfananisha bali ni kwamba alikuwa Bryon. Haraka akageuza na kurudi. Hatua chache kabla ya kumfikia, Bryson naye akawa amemuona.
“Ondoa gari haraka sana,” Bryson akamwambia dereva taxi.
Bruno akaanza kulikimbiza lile gari akipiga kelele za mwizi. Hakuna aliyemsaidia, maana alionekana kama aliyechanganyikiwa. Lile gari lilipofika barabarani, likanyoosha kuingia kwenye barabara ya vumbi, katikati ya mitaa.
Bruno akaendelea kulikimbilia akiamini kwamba angeweza kufanikiwa kumpata. Akiwa anavuka barabara, gari lililokuwa kwenye mwendo wa kasi, likamgonga na kuanguka chini! Mguu wake mmoja ukasagika kabisa!
Akatokwa na damu nyingi sana.
Akapoteza fahamu!
***
“Nilipozinduka, nilijikuta nikiwa wodini katika Hospitali ya Amana, madaktari walisema ilikuwa siku ya tatu tangu nilipopelekwa pale. Sikuwa na fedha, kadi zangu za benki wala simu, vyote niliibiwa!” Bruno alimwambia Vanessa, akijitahidi kufuta machozi machoni mwake.
“Usilie Bruno, jikaze.”
“Nashindwa kujizuia, moyo wangu una makunyanzi sana!”
“Pole sana, aliyekugonga hakukamatwa?”
“Naambiwa alikimbia, wasamaria ndiyo wakanipeleka hospitalini. Ni kweli nina machungu sana moyoni mwangu, uamuzi niliofikia ni kwamba, lazima Bryson naye apate ulemavu, tena nataka kutoa macho yake kabisa.
“Hata kama si leo wala kesho, siyo keshokutwa wala mtondogoo, lakini lazima na yeye awe na alama kama mimi.”
“Hapana, usifikirie kufanya hivyo, nisamehe mimi badala yake. Tuliza moyo wako tafadhali!”
Vanessa alimuonea huruma sana Bruno, wakatoka na kwenda zao hotelini. Wakazungumza mambo mengi, lakini kubwa ni kwamba Vanessa alipanga kumsaidia Bruno.
***
Walishuka Dar es Salaam kwa furaha, Emma ndiye aliyewapokea Uwanja wa Ndege. Hakuamini kumuona ‘Anko’ Bruno akitembea mwenyewe. Ilikuwa furaha kubwa sana.
“Pole sana!”
“Ahsante sana Anko!”
“Hongera jamani, siamini!”
“Ahsante, usijali!”
Wakaingia kwenye gari na kwenda nyumbani. Kichwani Emma akiwa na mawazo mengi sana. Alishindwa kuelewa namna gani angetakiwa kumshukuru Vanessa kwa msaada wake na kujitolea.
Miezi miwili baadaye, Vanessa akamfungulia Bruno duka la vipodozi Sinza. Akamwambia kwamba lilikuwa duka lake moja kwa moja, kwamba hakutakiwa kulipa kiasi chochote cha fedha.
“Kweli Vanessa?” Bruno akauliza akiwa haamini kabisa alichosikia.
“Ni kweli, hili ni duka lako!”
Bruno alishindwa kujibu, akabaki anamwangalia kwa macho yaliyojaa mahaba mazito, akamsogelea na kumkumbatia, kisha akambusu midomoni mwake.
“Sasa nimeamini kweli unanipenda!”
“Kwani ulikuwa huamini?”
“Naamini lakini leo umezidi kunifanya nikuamini zaidi.”
Vanessa akacheka.
“Naweza kukuuliza kitu?” Bruno akauliza.
“Yes, go on!” (Uliza)
“Hivi haya mapenzi yetu yataishia wapi, ikiwa wewe bado uko na Emma? Nikiwa nyumbani naitwa Anko, nikiwa nje ya nyumbani ndiyo nakuwa mpenzi, itakuwa hivi hadi lini?” Bruno akauliza.
Vanessa akapata kigugumizi!
Kwa dakika tatu nzima, Vanessa alibaki kimya akiwa hana jibu la moja kwa moja! Aliulizwa swali gumu sana ambalo lilihitaji jibu yakinifu. Ni kweli alikuwa na jibu lakini lilikuwa gumu sana kulitamka moja kwa moja.
Anabaki anamwangalia!
“Vanessa, nimekuuliza swali lakini?”
“Ndiyo!”
“Sasa?”
”Hili suala acha nitalishughulikia, wewe endelea na kazi kwanza, sawa baby?”
“Ok! Nimekuelewa!” Bruno akajibu lakini akionekana kuwa na wasiwasi kidogo moyoni mwake.
***
“Uko wapi?” Alikuwa ni Emma akiongea, baada ya kumpigia simu Vanessa.
“Kariakoo!”
“Wapi sasa?”
“Dukani!”
“Ok! Nilitaka kukupa mwaliko mpenzi wangu.”
“Mwaliko? Wa nini?”
“Nataka kutoka na wewe kwa ajili ya chakula cha jioni!”
“Mwenyewe au na Anko?”
“Peke yako. Nahitaji kutumia muda huo pia kuzungumza na wewe mambo muhimu!”
“Sawa mpenzi, nimepokea mwaliko wako!”
“Ahsante sana dear!”
Yalikuwa maajabu makubwa sana kwa Emma, mwanaume yule mkorofi, mwenye maneno mengi, vipigo na lawama kila siku, leo amekuwa wa outing, zawadi, maneno ya mapenzi na kila kitu kizuri kwa ajili ya kuboresha mapenzi. Hakika ni jambo la kheri sana!
Vanessa alishangazwa sana na Emma wa siku hizi, amebadilika na anajua kuheshimu hisia zake. Ilikuwa maajabu sana! Maajabu yaliyomuacha njia panda. Maana alikuwa na wawili; Bruno na Emma.
“Nitajua cha kufanya,” akajisemea mwenyewe akilini mwake.
Lakini alijiandaa kwa ajili ya chakula cha jioni na Emma, mpenzi wake.
***
Kijani kibichi cha Atriums Hotel, kilionekana vizuri sana. Taa za rangi zilizozunguka mandhari ile, zilizidi kuongeza mwonekano wa kuvutia eneo lile. Maji yaliyokuwa yakitiririka kwenda kwenye mabwawa ya kuogelea pia yalizidisha utulivu wa Atriums Hotel.
Emma anashuka kwenye gari, macho yake yakiangalia vizuri Hoteli hiyo nzuri iliyopo Sinza, Afrika Sana, jijini Dar es Salaam. Vanessa naye anashuka, wanakutana na kushikana mikono.
Kushoto kwao kulikuwa na meza, kulia vivyo hivyo! Vanessa anamvutia kulia, lakini Emma anamvutia upande wa kushoto. Wanavutana. Mwisho Emma akaibuka mshindi, maana alikuwa akimvuta kwa kutumia nguvu zaidi.
“Umeshinda,” Vanessa akasema akimfuata Emma kwa nyuma.
Wakaketi kwenye viti vizuri, vikubwa, vilivyotengenezwa kwa mkeka halisi. Muda mfupi tu, baadaye akatokea muhudumu na kuwasikiliza. Wakaweka oda ya chakula na kuletewa vinywaji, wakaendelea kunywa.
“Hivi unafahamu sababu hasa ya kukutoa usiku huu baby?” Emma akamwuliza Vanessa.
Vanessa akashtuka sana!
Swali tata!
Kwake lilikuwa na maana mbili, kwamba yawezekana anamwuliza hivyo, lakini jibu ni kwamba alimtoa ili amwulize kuhusu uhusiano wake na Bruno! Hakujiamini hata kidogo katika hilo.
“Hapana sweetie, sijui!”
“Kwa ajili ya kitu kimoja tu, kuendelea kuboresha penzi letu. Nafahamu kwamba nimekuwa nikikutesa kwa muda mrefu sasa, ni wazi kwamba huenda kichwani mwako unawaza kuachana na mimi, lakini nataka kukuhakikishia kwamba sitakuumiza tena, sitakutesa na sitakufanyia lolote baya kwa mara nyingine tena.
“Ni kweli kwamba sikuwa mwanaume mwema kwako, lakini nataka kukuhakikishia kwamba, nimeamua kubadilika moja kwa moja, sitaki tena kugombana na wewe. Nimeshatambua makosa yangu na najua kwamba natakiwa kukufanya uwe na furaha wakati wote. Nakupenda sana mpenzi wangu,” akasema Emma kwa sauti iliyojaa utulivu.
Vanessa alikaa kimya akimsikiliza, maneno yake yalimwingia sana. Kimsingi Emma hakuwa na haja ya kuzungumza sana, kwani matendo yake yalitosha kabisa kuonesha anamaanisha nini. Emma alibadilika kwa kila kitu, alifaa kabisa kuitwa mume!
Tatizo ni Bruno!
“Nimekuelewa mpenzi wangu, nimefurahi kusikia ukitamka kwa kinywa chako kwamba ulikuwa unanikosea, lakini pia nimefurahishwa na jinsi ulivyoahidi kubadilika. Kuna kitu kimoja ambacho hujakijua...tayari umeshabadilika kwa muda mrefu sasa, naona mabadiliko yako na nataka kusema kwamba yananifurahisha sana mpenzi wangu. Nashukuru kwa kila kitu mpenzi.”
“Ahsante sana!”
Wakaendelea kunywa huku wakisubiri chakula, Emma hakujua kabisa kwamba Bruno hakuwa ‘Anko’ kama alivyotambulishwa, bali alikuwa mpenzi. Kilichokuwa mbele yake kwa wakati huo ilikuwa ni kuongeza mapenzi ya dhati kwa Vanessa ili azidi kumpenda!

MIEZI MITATU BAADAYE
Kichwa chake kilivurugika kabisa, siku zilivyozidi kwenda ndivyo alivyozidi kugundua mambo mapya. Leo amegundua jipya kabisa. Kwamba kumbe hampendi Vanessa! Mapenzi yake na Emma yanamchanganya sana. Wanaelewana, kwahiyo nafasi yake kwa Vanessa inazidi kupungua taratibu.
Kama hiyo haitoshi, hata yeye ndani ya moyo wake, alionekana kuanza kumkumbuka mke wake mpenzi aliyemuacha Mwanza. Akawaza familia yake.
“Natakiwa kufanya kitu,” akawaza Bruno kichwani mwake.
Hakuwa na jambo lingine zaidi ya kufikiria kurudi nyumbani kwake Mwanza, tatizo lilikuwa deni analodaiwa na kampuni aliyokuwa akifanyia kazi.
“Mungu wangu na pesa za watu?” Akawaza Bruno akiwa hana jibu.
“Yeah! Nimeshajua cha kufanya,” akajijibu ghafla.
***
Siku nzima Bruno alikuwa na mawazo, hakuweza kuwahudumia wateja wake vizuri, akili yake yote ilikuwa ni juu ya mkewe Mwanza. Wazo alilolipata usiku wa kuamkia siku hiyo, aliamua alitumie. Akachukua simu yake na kumpigia Vanessa. Akamwomba akutane naye mahali mchana huo.
“Kuna nini?” Vanessa akauliza.
“Ni muhimu sana, naomba tukutane tafadhali.”
“Hapo dukani vipi?”
“Nitafunga.”
“Hapana, napitia hapo sasa hivi.”
“Sawa!”
Nusu saa baadaye Vanessa alikuwa ameshafika dukani, akamkuta Bruno akiwa na mawazo sana. Akaishangaa sana hali hiyo.
“Vipi mwenzetu, mbona hivyo?”
“Mawazo Vanessa.”
“Juu ya nini?”
“Wanangu. Nahitaji kwenda kuwasalimia, lakini nashindwa kabisa. Kuna kitu nahitaji msaada wako.”
“Sema ni nini?”
“Ili niweze kwenda Mwanza, lakini nipeleke na zile fedha za watu, tafadhali naomba unisaidie!”
“Unataka shilingi ngapi Bruno.”
“Nadaiwa milioni nne, lakini naamini hata nikiwapelekea tatu na kuwaahidi iliyobaki watanielewa.”
“Kwahiyo unataka milioni tatu?”
“Ndiyo!”
“Usijali nitakupa milioni kumi, ulipe deni la watu, lakini pia uweze kuwa na balance ya kutatua matatizo madogo madogo huko nyumbani!” Vanessa akasema kwa sauti tulivu sana.
Bruno akachanganyikiwa.
Akachanua tabasamu!
Siku mbili baadaye Vanessa akamwingizia Bruno zile fedha kwenye akaunti yake. Ni kweli, alimwekea milioni kumi! Kilichofuata baada ya hapo ilikuwa ni kutafuta kijana wa kumuacha dukani kwa siku ambazo yeye angekuwa safarini Mwanza, zoezi ambalo lilifanikiwa baada ya muda mfupi sana.
Bila kupoteza wakati, Bruno akaamua kusafiri, siku hiyo alidamka alfajiri, Emma na Vanessa wakamsindikiza hadi katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani cha Ubungo.
“Safari njema Anko!” Emma akamwambia Bruno akimkumbatia.
“Nashukuru sana Emma, nimefurahi sana kuwa na wewe siku zote kwa furaha bila kuwepo kwa migogoro yoyote. Najivunia sana kwa hilo.”
“Hata mimi pia Anko, Mungu akutangulie katika safari yako!”
“Ahsante sana, naamini atakuwa nami!”
“Kwaheri Anko jamani, nitakumisi sana,” akatamka Vanessa kwa sauti ambayo ilijaa mahaba zaidi.
Emma hakugundua sababu ya sauti kutoka vile, aliamini alikuwa na uchungu wa kuachana na mjomba wake kwa muda mrefu.
Hivyo ndivyo alivyojua, lakini ndani yake kulikuwa na ukweli mwingine ambao Emma hakuufahamu.
Saa 11:30 za asubuhi, Bruno alikuwa ameshaketi kwenye siti yake ndani ya basi la Zuberi tayari kwa safari. Saa 12:00 basi liliondoka katika kituo cha Ubungo.
***
Basi la Zuberi liliingia Mwanza saa 3:45 usiku, ikiwa ni baada ya mwendo wa saa kadhaa njiani. Bruno alishuka akiwa amechoka sana. Hakutaka kwenda nyumbani kwake usiku huo, lengo lake likiwa ni kuongea na mabosi zake kwanza ikiwezekana afanye malipo kabisa kabla ya kwenda nyumbani kwake.
Hilo lilisababisha aamue kwenda kulala hotelini, asubuhi alipoamka aliingia bafuni kuoga, akajiandaa na kwenda ofisini kwao. Alipofika Mapokezi, kila mtu alimshangaa, wengi walijua aliamua kutoroka moja kwa moja baada ya kupata matatizo ambayo baadaye waliyasikia kutoka kwa msaidizi wake aliyekuwa akisafiri naye mikoani.
“Za masiku?” Happy, msichana wa Mapokezi alimwuliza.
“Salama!”
“Mbona kama unachechemea kidogo, unaumwa?”
“Ni habari ndefu Happy, kwasasa nahitaji kuonana na Meneja kwanza.”
“Sawa, hana mtu, nenda tu ofisini kwake!”
“Nashukuru.”
Meneja alishangaa sana kukutana na Bruno, lakini cha ajabu, tofauti na matarajio ya Bruno, hakuwa na uso wa hasira, badala yake alionekana kufurahi sana kumuona. Akasimama na kumkumbatia.
“Bruno vipi, umepotelea wapi?” Meneja akasema akiwa amelala begani mwake.
“Matatizo tu bosi, matatizo.”
“Tunajua, hebu keti hapo!”
Bruno akakaa.
Walianza kuzungumza mazungumzo mengine ya kawaida kwa muda mrefu sana, lakini baadaye ukafika muda ambao Bruno alitakiwa kueleza kilichomsibu.
“Nilipata matatizo bosi, naweza kusema ni matatizo ya kujitakia lakini naamini ilikuwa lazima niyapate ili niweze kujifunza. Kweli nimejifunza mengi kupitia matatizo niliyopitia.”
“Ni nini hasa? Na kwanini hukutaka kutushirikisha?”
“Ni aibu bosi, lakini nitakusimulia. Ni hivi...”
Bruno akamsimulia kila kitu kilivyokuwa, kuanzia alivyokutana na Tunu hadi alivyopata ajali na kuumia mguu. Hakutaka kuficha kitu hata juu ya Vanessa, alimweleza jinsi alivyomsaidia hadi kupata mguu wa bandia.
Hata hivyo hakumweleza kama aliingia kwenye uhusiano wa mapenzi na Vanessa, hilo hakulisema. Pia hakumweleza kuhusu kumpatia fedha, alichokisema yeye ni kwamba Vanessa aliamua kumsaidia kwa kila hali kwa kuwa alimwonea huruma baada ya kukutana naye hospitalini alipokwenda kumwangalia mjomba wake.
“Kwahiyo nikaogopa kuja huku bila pesa, nilijua kwa vyovyote vile, mngenikamata na kuniweka ndani, hivyo nimejitahidi kujikusanya, nimekuja na milioni mbili, ambazo nitaomba mzipokee kisha zilizobaki nitalipa polepole,” akasema akidanganya, maana ukweli haukuwa huo.
“Hapana Bruno, Kampuni inatambua mchango wako, tulishafuatilia suala lako kwa karibu, tumegundua kilichotokea. Kama Kampuni, tulishaamua kukusamehe moja kwa moja na mchakato uliokuwa ukiendelea ulikuwa ni kukutafuta kwa ajili ya kukuita kazini uendelee na kazi kama kawaida.
“Hata Mkurugenzi aliagiza hilo lifanyike haraka sana, usijali Bruno, kila kitu kilishaisha, ndiyo maana ofisi iliamua kuendelea kukulipia kodi ya pango baada ya wewe kutoweka na kumwacha mkeo na watoto. Familia yako iko salama na Kampuni inawajibika kwa kila kitu. Ondoa shaka Bruno, nenda nyumbani ukampumzike, kesho asubuhi uje ili tufanye mazungumzo kidogo mbele ya bodi, halafu utaanza kazi,” akasema Meneja.
“Sawa bosi, nimekuelewa vizuri sana. Ahsante sana na Mungu akubariki!”
“Nashukuru sana, siku njema Bruno.”
“Ahsante.”
Bruno akatoka ofisini kwa Meneja na kwenda kusalimiana na wafanyakazi wengine. Maswali yalikuwa mengi, lakini majibu yalikuwa ni kwamba atatoa ufafanuzi wa jumla siku akirudi tena kazini.
Alipofika barabarani, akaingia kwenye taxi iliyokuwa imeegesha kituoni.
“Wapi?”
“Nyakato!”
“Buku tano bro!”
“Hakuna tabu!”
Dereva akaendesha gari kumuwahisha mteja wake sehemu aliyoelekezwa. Baada ya muda gari lilikuwa linaegesha nje ya geti jeusi, nyumba ambayo Bruno alikuwa anaishi humo. Akashuka na kutoa noti moja ya elfu tano na kumkabidhi.
“Ahsante sana kaka!”
“Usijali!”
“Naweza kukupatia namba yangu ya simu, kama utanihitaji siku nyingine?”
“Bila shaka!”
Yule dereva akatoa kadi yake ya mawasiliano na kumpatia Bruno.
“Nashukuru kaka, nikikuhitaji nitakupigia.”
“Ukipiga sema ni yule niliyekuleta Nyakato, ndiyo nitakumbuka kwa urahisi zaidi.”
“Usijali ndugu yangu.”

Bruno akasukuma geti na kuingia ndani, akina mama waliokuwa pale nje, wakifanya shughuli ndogo ndogo, wakashangaa sana kumuona tena akiwa anachechemea! Walikuwa na maswali mengi sana ambayo hayakuwa na majibu ya moja kwa moja. Bruno akawasalimia kwa wakati mmoja kisha akajongea hadi katika mlango wake, wenye vyumba vitatu!
Mlango ulikuwa wazi, hivyo hakutaka kugonga. Alitaka kumfanyia surprise mkewe!
Alipofunua pazia na kuingia ndani, macho yake yakagongana na wanaye wawili, Julius na Irene, lakini cha kushangaza zaidi, mkewe alikuwa amekaa kwenye sofa kubwa, akimnyonyesha mtoto! Mtoto ambaye alionekana bado ni mdogo sana!
Ametoka wapi, wakati alimwacha na watoto wawili? Macho yakamtoka Bruno akiwa haelewi kinachoendelea.
“Monica?!!!” Bruno akamwita mkewe kwa sauti iliyojaa kitetemeshi, akahisi mwili wake kuanza kupungua nguvu, akajikongoja hadi kwenye sofa dogo na kujiangusha hapo!
Ulikuwa mshtuko mkubwa sana, kwa muda wa miezi kumi na moja aliyotoweka nyumbani kwake, halafu kumkuta mkewe akiwa na mtoto ilikuwa maajabu sana. Kitu pekee ambacho kiliingia akilini mwake ni kwamba alikuwa amemsaliti!
Monica, mke wa Bruno akamwangalia mumewe kwa jicho la huruma, aliweza kugundua haraka kilichotokea. Alijua kabisa mumewe alipatwa mshtuko baada ya kumkuta akiwa na mtoto.
“Baba Irene vipi, mbona hivyo?” Monica akamwuliza.
“Umeshindwa kabisa kuwa mwaminifu mke wangu?” Bruno akafoka.
“Uaminifu?”
“Ndiyo!”
“Unamaanisha nini? Mbona maneno yako yananichanganya? Halafu ndiyo kwanza umeingia, sijajua mwenzangu ulikuwa wapi na ulipatwa na matatizo gani? Kwani kuna nini?”
“Huyo mtoto ni wa nani?”
“Mtoto wetu!” Monica akajibu kwa kujiamini.
“Mtoto wako na nani?”
“Na wewe mume wangu!”
“Naona unacheza na akili yangu wewe. Wakati naondoka mara ya mwisho ulikuwa na mimba wewe?” Bruno akaanza kufoka kwa sauti ya juu kidogo.
“Mume wangu, haya mambo si ya kuzungumza kwa sauti kubwa kiasi hicho. Hatupaswi kuwafaidisha watu na mambo yetu. Hebu twende chumbani tukazungumze,” Monica akasema kwa sauti ya chini.
Wakaongazana kwa pamoja hadi chumbani wakiwaacha watoto wao Julius na Irene sebuleni. Bado Bruno alikuwa amekasirika sana na hakutaka kuelewa kitu chochote. Kwa kauli ya taratibu, Monica alifanikiwa kutuliza jazba ya mumewe na kumfanya akubali kumsikiza.
“Sikiliza nikueleza mume wangu, wakati unaondoka mara ya mwisho, sikujua kama nina mimba, lakini baadaye niligundua hilo baada ya kuona tofauti mwilini mwangu. Huyu ni mwanao, tena nimejifungua kwa shida sana mume wangu, nilifanyiwa oparation. Kama una wasiwasi, naweza kuongozana na wewe tukafanye kipimo cha DNA ambacho naamini kitaondoa ubishi wote.
“Pamoja na kuniacha na hali ile, kampuni yenu ndiyo iliyonisaidia kwa kila kitu kwa wakati wote uliokuwa haupo. Hakuna aliyekuwa na maelezo yaliyonyooka baada ya wewe kuondoka. Mara nasikia umetoroka na pesa za mauzo, mara sijui nini...yaani sielewi kabisa, kwani nini hasa kilikupata?” Monica akauliza, macho yake yakiwa yamefunikwa na machozi.
Maelezo yake yalimfanya Bruno atulize jazba na kumsikliliza kwa makini, mke wake hakuwa na tabia ya usaliti tangu alipomchukua nyumbani kwao Maswa miaka saba iliyopita baada ya kupata ujauzito wa kwanza.
Kwa bahati nzuri hakuna aliyemweleza ukweli uliotokea kwa Bruno alipokuwa Tanga, hakuna aliyesema kwamba Bruno alikimbilia Dar es Salaam, baada ya kugundua kwamba alifumaniwa fumanizi feki! Taarifa hizo Monica hakuzijua kabisa, jambo lililomfurahisha sana Bruno.
Kazi aliyokuwa nayo ilikuwa moja tu; kumweleza mkewe alipokuwa na mambo yaliyomkuta hadi kufikia hatua ya kupoteza mguu wake. Alikaa kimya kwa muda akitunga sheria namna ya kumdanganya, lakini uongo ulikuwa unakataa kabisa kukubali.
“Bruno niambie basi mume wangu, nini tatizo?”
“Mke wangu acha tu, kwanza si kweli kwamba nilitoroka na pesa, ukweli ni kwamba nilitapeliwa mke wangu!”
“Ulitapeliwa?”
“Ndiyo!”
“Wapi?”
“Nilikutana na matapeli, wakanidanganya kwamba wao ni waganga na kienyeji na walikuwa na dawa ya kunifanya niwe tajiri. Katika mazungumzo yetu, wakaniambia nipeleke fedha nikazifukie ufukweni mwa baharini, nikirudi ningekuta zimeongezeka, nikafanya hivyo.
“Lakini niliporudi baadaye sikuzikuta, nikachanganyikiwa kabisa. Baadaye nilipowashirikisha watu, wakaniambia kwamba wale ni matapeli na wanapatikana Ilala, Dar es Salaam, nikaamua kufunga safari kuwasaka. Kwa bahati mbaya nikiwa nakimbilia gari baada ya kuwaona, nikapata ajali mbaya ya gari.
“Hapa unavyoniona sina mguu mmoja, huu nilionao ni wa bandia. Niliteseka sana, lakini nashukuru nilipata mtu akanisaidia, nikaishi kwake kwa muda mrefu na yeye ndiye aliyenipeleka India kuwekewa huu mguu wa bandia,” Bruno alidanganya.
Tukio zima lilikuwa la uongo, ingawa maeneo alikuwa akiyataja sawa. Monica alihuzunika sana, akashindwa kabisa kuzuia machozi yake machoni. Aliamini kila kitu na kumuonea huruma mumewe.
“Pole sana mume wangu, maadamu uko mzima ni jambo la kumshukuru Mungu!”
“Ahsante sana.”
“Huyo mtu ni nani?”
“Anaitwa Emma, ni msamaria mwema tu, alikuja kumwangalia ndugu yake pale wodini, basi aliponiona akanionea huruma na kunifuata. Baada ya kumweleza kisa kizima na kwamba mimi sikuwa na ndugu Dar es Salaam, akaamua kunisaidia.
“Ana roho nzuri sana, amenifungulia mpaka duka la vipodozi Dar, ambalo nimemuacha mtu analiendesha kwa kipindi hiki nilipokuja huku nyumbani.”
“Kwahiyo utarudi Dar?”
“Natamani iwe hivyo, lakini nimezungumza na Meneja wangu anasema bado nahitajika kazini, sijui wewe unanishauri nini?”
“Kwani huko dukani lazima uwepo wewe?”
“Sidhani.”
“Unajua kuwa na ajira kwenye kampuni nzuri inayojali wafanyakazi wake kama hii ni vizuri sana. Mimi nakushauri kule muache huyo kijana, ila utakuwa unakwenda kukagua, halafu endelea na kazi Sangara!”
“Kweli mke wangu?”
“Kweli kabisa.”
“Nitaufanyia kazi ushauri wako!”
Tofauti zote zikawa zimeisha ingawa Bruno hakueleza ukweli halisi wa kilichotokea Dar. Tayari Bruno alikuwa ameshamkubali yule mtoto. Hakuwa na jinsi, maana hata sura yake ilikuwa inafanana sana na yeye.
“Anaitwa nani?”
“Kwasasa nimempa jina la Deborah, lakini unaweza kuwa na uchaguzi wa jina utakaloona linafaa zaidi!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Naomba huyu mtoto aitwe Vanessa!”
“Vanessa?”
“Ndiyo!”
“Kwanini umechagua jina hilo?”
“Ipo maana, lakini hutajua leo wala kesho, siku ikifika nitakuambia.”
“Umeniacha njia panda hapo mume wangu.”
“Najua, lakini ni nia yangu pia kukuacha njia panda kwasasa, lakini muda ukifika utajua kwanini nimechagua jina hilo.”
“Sawa bwana.”
Monica akamlaza mtoto kitandani, kisha akasimama na kumwonesha Bruno ishara kwamba asimame. Bruno akasimama. Wakasogeleana na kukumbatiana.
“Nakupenda sana mume wangu!”
“Nakupenda pia mama Vanessa.”
Monica akacheka sana, baada ya Bruno kumwita kwa jina la mama Vanessa.
***
Asubuhi ya siku iliyofuata, Bruno aliamka asubuhi sana na kuwahi kazini kama alivyoagizwa na Meneja wake. Akiwa ndiyo kwanza anaingia katika geti la ofisini kwao, simu yake ikaita, jina alilokutana nalo lilikuwa ni Vanessa.
“Ninalo swali moja tu, kwako Bruno,” Vanessa akasema baada ya Bruno kupokea simu.
“Haaa Vanessa hata salamu?”
“Najua mzima ndiyo maana nimeona nikuulize kama naweza kukuuliza kitu!”
“Enhee hebu niulize.”

“Utajisikiaje nikikuambia tusitishe haya mapenzi yetu ya kudanganyana?” Neno moja moja lilipenyeza kwenye ngoma za masikio ya Bruno akiwa haamini kabisa kama yanatokea kinywani mwa Vanessa.
Bruno hakuwa na jibu.
Alihema kwa kasi bila kujizuia, mihemo ambayo ilisikika vyema kwenye simu ya Vanessa. Kimya cha dakika nzima kilipita, huku kitu pekee kikisikika kikiendelea kuwa mihemo tu!
“Bruno!”
“Nipo nakusikiliza.”
“Ni wewe ndiye unayetakiwa kuzungumza sasa, nimejaribu kukueleza kwa uwazi kabisa juu ya haya mapenzi yetu ya uongo, kwanini tusiachane?” Vanessa akasisitiza.
“Kwanini sasa umeamua uamuzi huo?”
“Hakuna nia mbaya Bruno. Unajua mimi nilipokutana na wewe niliamua kukusaidia kama kaka yangu, lakini nilipokuwa karibu na wewe, nikawaza zaidi ya hapo. Nikatamani sana uwe mpenzi wangu, lakini hilo halikumaanisha kwamba sikuwa na mpenzi.
“Nilikuwa naye na ulimfahamu vyema. Ni Emma, lakini nilitaka kuwa na wewe, baada ya kupoteza amani katika penzi langu, Emma alikuwa mkorofi sana, lakini ndani ya moyo wangu niliendelea kumpenda na kumvumilia.
“Ni kweli nilipanga kuishi na wewe, lakini nitawezaje ikiwa tayari wewe mwenyewe ulishanithibitishia kwamba una mke? Tena na watoto? Kutaka kuishi na wewe ni kukuachanisha na mkeo, jambo ambalo linaweza kuwa hatari katika maisha yangu, maana familia yako ikimwaga machozi, laana itakuwa juu yangu.
“Naamini hata wewe unampenda mkeo, lakini ulilazimika kuwa na mimi baada ya kukusaidia. Bruno nataka kukuhakikishia kwamba Ima amebadilika sana siku hizi, anajua anachokifanya na amekuwa mwanaume mwenye mapenzi ya kweli kwangu.
“Naamini amejifunza kitu na kwasasa sitakiwi kuwa msaliti tena, maana hata yeye natambua kwamba kwamba hanisaliti tena kama zamani. Sikutaka kumsaliti mpenzi wangu na sikujua kabisa kama angenisaliti, lakini tayari yameshatokea, naomba tufungue ukurasa mpya,” akasema Vanessa kwa sauti taratibu sana.
Baada ya hapo alibaki kimya akitaka kumsikiliza Bruno. Bado alikuwa kimya.
“Usiogope Bruno, kila nilichokufanyia, kitabaki kuwa hivyo, duka litaendelea kuwa lako, tutatabaki kama ndugu wa kawaida na tutaendelea kusaidiana,” akasema tena Vanessa.
“Nimekuelewa vizuri sana Vanessa, ahsante kwa yote, hakuna kibaya kilichotokea. Huku nyumbani ni wazima na nina habari nzuri kwako.”
“Nini?”
“Mke wangu nimemkuta ana mtoto mwingine wa kike, kumbe wakati naondoka mara ya mwisho, nilimuacha na ujauzito!”
“Hongera sana.”
“Ahsante sana Vanessa, lakini kitu cha kufurahisha zaidi, nimempa jina lako kama kumbukumbu ya maisha yangu siku zote, binti yangu anaitwa Vanessa!”
“Vanessa?”
“Yes, Vanessa. Yaani wewe!”
“Ahsante sana Bruno kwa kutambua mchango wangu, nadhani ni vizuri nikamuona mwanao na hata mkeo.”
“Karibu Mwanza.”
“Ngoja niangalie ratiba zangu kwanza, halafu nitakujulisha.”
“It’s okay!” (Ni sawa)
***
Bruno aliogopa sana baada ya kukutanisha macho yake na ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni yao. Walikuwa ndani ya chumba cha mkutano, Bodi ya Wakurugenzi ikiwa imetimia.
Punde Meneja Mkuu akasimama na kuanza kuongea: “Kama nilivyozungumza nanyi jana jioni katika kikao cha dharura, Bruno amerudi, tena amekuja mwenyewe baada ya juhudi za kumtafuta kushindikana.
“Alikuja akitambua amekosa, pia alileta sehemu ya fedha anazodaiwa, lakini nilizikataa kama tulivyokubaliana kwenye vikao vyetu vilivyopita, baada ya Bruno kutoweka. Baada ya hayo namkaribisha MD azungumze.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Sangara Distributors, Revogatus Ngeleja, akawatazama watu wote ndani ya chumba kile cha mkutano, akajikohoza kidogo na kuanza kuzungumza...
“Kila kitu kimeshazungumzwa, hakuna kitu kigeni hapa. Makosa yaliyotokea kwa Bruno si ya makusudi, ni ya ujana tu! Hakukusudia kuiba, alifanya kwa ajili ya kujilinda na aibu. Kwa Kampuni ni hasara, lakini tumejaribu kuzingatia muda aliofanya kazi nasi pamoja na uaminifu aliokuwa nao, tukaona bado anahitajika kwenye kampuni.
“Napenda kuchukua fursa hii kukupa pole bwana Bruno. Hayo ndiyo maisha, lakini naamini kwamba utakuwa umejifunza. Kwa muda wote uliokuwa haupo, Kampuni iliisadia familia yako kwa hali na mali, hii ni kuonesha kwamba bado tulikuwa na haja na wewe.
“Umesamehewa hasara uliyosababisha na utatakiwa kuanza kazi haraka sana iwezekanavyo, ukiwa na nafasi yako ile ile. Pole sana na karibu tena Sangara Distributors,” akamaliza Ngeleja.
Bruno hakuamini kabisa maneno aliyoyasikia, machozi ya furaha yakaanza kumiminika machoni mwake, akasimama na kuwatazama watu wote waliokuwa kwenye chumba cha mkutano, akawapungia!
“Nashukuru sana kwa kila kitu, ahsanteni sana. Ahadi yangu kubwa kwenu, ni kwamba nitafanya kazi kwa bidii na nguvu zangu zote!” Alisema Bruno akizidi kumiminika machozi machoni mwake.
Makofi yakapigwa!
***
“Lazima nikuambie ukweli Emma, najua kwamba umenisaliti kwa muda mrefu sana, nimeshasamehe yote maana najua kwasasa huna tabia hiyo tena.
“Lakini ninayo siri iliyonitesa kwa muda mrefu sasa, sihitaji kuendelea kuwa mtumwa kwa kukaa na siri hiyo kwa siku zote hizo. IMA, HATA MIMI NILIKUSALITI!”
“Unasemaje?”
“Ndiyo, nilikusaliti mpenzi wangu, najua utaumia sana moyoni mwako, lakini naomba tuyaache hayo mambo yaende zake, tubaki na maisha yetu!”
“Vanessa...” Ima akasema akiwa ameyatoa macho kwa mshangao.
“Trust me Ima, siwezi kurudia tena, lakini imenipasa niwe mkweli kwako...lazima niwe mkweli zaidi ya hapo, Bruno hakuwa mjomba wangu na wala sina undugu naye wa aina yoyote!”
Ima akatoa macho kwa mshangao zaidi. Hakutegemea kusikia maneno yale kutoka kwa Vanessa.
“Kwahiyo Bruno si mjomba wako?”
“Siyo...ngoja nikusimulie, iko hivi...siku moja nilienda Hospitali ya Amana kumuangalia mjomba wangu Bryson aliyekuwa amelazwa, nikiwa naingia wodini, nikamuona Bruno kitandani, akiwa ameonekana kukata tamaa kabisa, machozi yakiwa yameuchakaza uso wake...” Vanessa akamsimulia kisa kizima kilivyokuwa, jinsi alivyokutana na Bruno, kuamua kumsaidia na hata kusafiri naye hadi India kwenda kuwekewa mguu wa bandia.
Emma alihisi yupo kwenye ndoto mbaya isiyotamanika, akiamini baadaye angeamka usingizi na kuendelea na maisha yake kama kawaida, lakini haikuwa hivyo!
Kila kitu kilikuwa yakini!
Vanessa alimsaliti!
Kama yeye alivyosaliti!
“Vanessa umenisaliti?” Emma akatokwa na maneno hayo akiwa ameukunja uso wake.
“Yeah! Ni kweli mpenzi wangu, lakini inanipasa nikueleze ukweli kuliko kuficha maradhi ndani ya moyo wangu. Nilikusaliti mpenzi wangu, lakini sababu kubwa ni wewe, kwasasa sitarajii kurudia ujinga huo, naamini na wewe pia!” Vanessa akasema kwa sauti ya majonzi na kuonekana kujuta kutoka ndani.
Emma alikuwa na wakati mgumu sana, machozi yakaanza kumtoka machoni mwake, hakutegemea kama angesalitiwa.
“Huna sababu ya kulia Emma mpenzi, yaache ya zamani yabaki kuwa sehemu ya historia yetu.”
Emma hakusema kitu zaidi ya kumsogelea Vanessa na kumkumbatia. Walibaki wameshikana kwa muda wote machozi yakiwatoka. Baadaye wakaachiana na kutazamana, machozi yakiendelea kuchuruzika, wakatabasamu!
“Nakupenda Vanessa!”
“Nakupenda pia Emmanuel!”
“Oooh! Thank you darling...umeniita jina nilipendalo, muda mrefu sana hujaniita jina langu lote!” Emma akasema akizidi kuangua kicheko kilichoungwa mkono na Vanessa ambaye aliendelea kucheka.
***
MWEZI MMOJA BAADAYE
Sebule ilikuwa katika mpangilio wa kuvutia sana, kwenye viti walikuwa wamekaa watu watatu, Vanessa, Emmanuel na Monica mke wa Bruno ambaye yeye alikuwa amesimama. Ilikuwa ni muda mfupi tu baada ya kuwapokea Uwanja wa Ndege wakitokea Dar es Salaam.
Wote walionekana kuwa na furaha sana, Bruno akawatazama tena, kisha akafungua kinywa chake na kuanza kuzungumza...
“Karibuni sana jamani...hapa ndiyo nyumbani kwangu, nyumbani kwa Mr. Bruno...yule pale ndiye mke wangu, anaitwa Monica, lakini napenda zaidi kumuita mama Vanessa, Vanessa ni jina la binti yetu wa mwisho,” akasema Bruno akiwatazama tena kwa zamu.
“Monica,” akasema alipomgeukia mkewe.
“Kutana na rafiki zangu Vanessa na Emma, hawa ni wapenzi, wanaishi Dar es Salaam, ndiyo walionisaidia kwa kipindi chote nilichokuwa na matatizo Dar!” Akasema Bruno akionekana kuwa na ukakasi.
Mara Vanessa akamkatiza...
“Samahani kwa kukukatisha Bruno, nataka tuzungumze ukweli, kwanza Bruno unatakiwa kufahamu kwamba Emma anajua kila kitu kilichokuwa kikiendelea kati yangu na wewe!”
“What?” Bruno akasema akiyatoa macho.
“Usiwe na wasiwasi, yale yalishapita, kikubwa ni kwamba alishasamehe maana ni mimi mwenyewe ndiye niliyemweleza ukweli. Sisi sasa ni ndugu na hutakiwi kuwa na wasiwasi wowote katika moyo wako. Emma ni muelewa na ameelewa kila kitu!”
“Nashukuru kusikia hivyo, nadhani ni vyema sasa kama tutapata maji ya matunda pamoja na kupiga chears kama ishara ya furaha na kufungua ukurasa mpya!”
“Sawa...” Vanessa akasema.
Monica akasimama na kwenda kuchukua juice kwenye friji kisha akamimina kwenye glasi nzuri za kisasa zilizoandaliwa mapema kwa shughuli hiyo. Akaziweka mezani, kila mmoja akachukua yake na kusimama.
“Okey...one, two, three, chears...” (Haya...moja, mbili, tatu...chiazi...) akasema Bruno na wote wakagonganisha glasi zao.
Wakaanza kunywa kwa furaha. Wote walikuwa wanatabasamu, lakini Monica pekee alionekana kuwa na mawazo kidogo, akamwonesha ishara Bruno kwamba anataka kuzungumza naye pembeni. Bruno akamfuata.
“Kuna nini kinaendelea, mbona sielewi?”
“Kivipi?”
“Kwani kulikuwa na kitu gani kati yako na Vanessa, mbona kama kuna siri unanificha?”
“Ni kweli mke wangu, unajua hatuwezi kubadili kilichotokea, kwanza samahani kwa kukudanganya mwanzoni. Msaada mkubwa kwangu alikuwa ni Vanessa, lakini kwa bahati mbaya, alinitaka kimapenzi na kwasababu nilikuwa na shida na nilikuwa naishi kwake, nikajikuta nimetoka naye, lakini nafsi yangu haikuwa tayari kwa hilo kabisa.
“Ni bahati mbaya tu, mpenzi wangu. Ilikuwa ni mara moja tu, kama unavyoona ameamua kukiri kwa mpenzi wake, maana alimdanganya mimi ni mjomba wake, lakini naomba tuyaache haya mambo kama yalivyo, yalishapita hayo,” akasema Bruno akionekana kutulia sana wakati akiongea.
Monica alitulia kwa muda mrefu sana akifikiria, lakini baadaye akamsogelea Bruno na kulala kifuani mwake, maneno mazito yakimtoka kinywani mwake.
“Niahidi hutanisaliti tena Bruno, nakupenda sana. Sitaki kuchangia penzi na mwingine tena.”
“Nakuahidi mpenzi wangu. Unajua nililia sana kutokana na hayo matatizo, najua hata wewe ulilia sana. Bila shaka wote tulidondosha matone ya machozi ya damu, lakini sasa yamekauka mpenzi wangu.”
“Ni kweli mpenzi, lakini unaniahidi kubadilika?” Monica akauliza.
“Nakuahidi.”
“Kweli?”
“Niamini mpenzi wangu!”
Monica akaachia tabasamu pana, kisha akachukua kitambaa na kujifuta machozi machoni mwake. Wakashikana mikono kwenda sebuleni kuungana na akina Vanessa na Emma. Walichojua wao ni kwamba, sasa walikuwa ndugu!
...MWISHO...

Post a Comment

0 Comments