Header Ads Widget

Responsive Advertisement

PANDE MBILI ZA MAISHA



Baba yangu aliniambia 'Mwanaume unayempenda hana cha kukupa zaidi ya matatizo',lakini kwasababu tayari moyo wangu ulishakuwa wazi kwa ajili ya kumpokea Sise, maneno ya baba yalikuwa ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa.
Sise aliitawala akili yangu na kuipumbaza, nikajikuta naamini kwamba hakuna maisha bila ya yeye. Nathibitisha kwamba nilimpendana nasadiki kuwa kumpenda kwangu ndiko kulikonisababishia nyakati za vilio na maombolezo.
Uhusiano wetu ulianza nilipokuwa na miaka 13 tu, kipindi hicho nilikuwa mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Iyunga iliyopo mkoani Kigomawakati yeye alikuwa akisoma darasa la saba katika shule hiyo hiyo.

Nakumbuka Mara ya kwanza aliponitongoza nilimkataa, lakini si kwasababu nilikuwa simpendi, La hasha! Bali nilikuwa nikimuogopa baba yangu, nilihofia angeweza hata kuniua endapo angegundua kuwa najihusisha na masuala ya mapenzi ningali mwanafunzi.
Lakini kwa shinikizo la marafiki zangu nilimkubali, wengi walinishauri nimkubali na labda wangeniona hayawani kwa kushindwa kufanya hivyo kwasababu Sise alikuwa ni mtu muhimu na maarufu pale shuleni.
Alikuwa ni mshambuliaji hodari katika timu ya soka ya shuleni kwetu, kila mechi ambayo alikuwa kikosini ushindi ulikuwa ni lazima, aliweka kimiani mipira yote iliyostahili kuwa magoli na kwasababu hiyo tu wanafunzi wakampachika jina la Sise Magoli; jina ambalo lilifuta kabisa lile la Sise Zekila linalofahamika na Serikali.

Nikamkubali na kuanzisha uhusiano ambao ulifahamika na wanafunzi wengi pale shuleni. Wengine hadi walinibadilisha jina pia, badala ya kuniita Sikujua Majuto waliniita Sikujua Magoli.
Mapenzi yalianza kwa kasi kweli kweli huku wawili sisi tukioneshana maana ya mapenzi kwa vitendo. Sise akawa mwanaume wa kwanza kuniingilia kimwili, yaani ni yeye aliyepata bahati ya kupopoa tunda pekee lililoota mtini mwangu na kamwe lisingerudi tena kwenye kikonyo chake. Alipata fursa hiyo kwasababu ya upendo wangu kwake, nathibitishakwa mara nyingine ‘Nilimpenda sana Sise’
Alinipa ahadi nyingi zenye kutia moyo, alinambia atanioa ili tujenge familia ya kisasa pindi tutakapohitimu masomo na kupata ajira za kuendesha maisha yetu, hiyo ikanipa imani juu yake na kuongeza kiwango cha kumpenda.

Nilidumu katika penzi la Sise Kwa takribani wiki sita bila familia yangu kung’amua lolote hadi pale watu wenye mapenzi mema na mimi walipoamua kumtonya baba yangu.
Baba aliniuliza kuhusu hilo lakini nilikataa katakata naye wala hakuonesha kama ni mwenye kiu ya kutaka kufahamu ukweli. Lakini kumbe alikuwa akilifanyia uchunguzi kimya kimya na kwa mara ya kwanza alinifumania na Sisetukingonoka kichaka cha karibu na kisimani.
Sise alikimbia na kuniachia dhahama zito, baba alinitaka nitangulie nyumbani, nilifanya hivyo huku nikiamini kwamba huenda siku hiyo ningeachwa na ulemavu kwa kipigo kizito ambacho baba angenishushia.
Lakini katika hali isiyo ya kawaida baba yangu hakuniadhibu kabisa, badala yake alinikalisha chini na kunipa maneno makali na yenye kunijenga na kuikomaza akili yangu.

"Mwanaume anayekupenda na kukuheshimu hawezi kukushawishi mfanye uchafu ule.Kwanza angethamini malengo yako, yaani angesubiri umalize shule, kisha angetuma wazee wake kuja kukutolea posa na akakuoa." alinieleza baba yangu. Tena hakuishia hapo tu, alizungumza mengi hadi alitokwa machozi jambo ambalo sikuwahi kuliona kwamzee Majuto hapo awali.
Lakini machozi yake yalikuwa ni sawa na maigizo, yaani yalinigusa wakati nikimtazama tu na mara baada ya kumpa kisogo nilisahau kabisa kwamba baba yangu alilia kwa ajili ya kuona binti yake napotea; niliendeleza operesheni za mapenzi na Sise bila kujali.
Nilifanya mambo ya ajabu sana; nilikuwa nikitoroka na kwenda kulala na Sise nyumbani kwao, pia niliwahi kumleta Sise nyumbani kwetu usiku, nikalala naye na kumtoa alfajiri bila mtu yeyote kufahamu; hakika Sise alinifanya niwe binti mchafu wa maadili tofauti na nilivyolelewa.

**************************

Kipaji cha Sise kilipata mdhamini, ni baba mmoja aliyekuja kijijini kwetu na kubahatika kumuona Sise akifanya maajabu yake uwanjani. Alizungumza naye na kumueleza kwamba atakaporejea Dar es Salaam atakwenda kumfanyia mipango katika moja ya klabu kubwa za soka za hapa nchini.
Sise alinipa taarifa hiyo, lakini wakati ananieleza na mimi nilikuwa na taarifa yangu ya kumpa.Taarifa ambayo ni nzito zaidi ya ile ya kwake.
"Sise nahisi nina mimba." nilimueleza na hiyo ndiyo ilikuwa taarifa yenyewe.
Alisituka kama aliyechomwa na sindano ya kushonea nguo na sura yake ilinionesha wazi kwambaanaogopa.
"Ume...umejuaje?" akaulizakwakusuasua kama jenereta lenye mafuta kiduchu.
"Sijatoka damu kwa miezi miwili sasa." nikamjibu na kuzidi kumnyima amani.

"Tufanyaje sasa?" akaniuliza huku akitweta mithili ya swala aliyeponea chupuchupu kuliwa nasimba.
"Nakusikiliza wewe, lakini mimi naogopa sana, baba ataniua endapo atafahamu tatizo hili."
"Nipe muda wa kufikiri, kesho nitakutafuta nikupe jibu."
Hakufanya uongo katika hilo, kesho ya siku hiyo alinifuata na kunieleza kile alichofikiria.
"....kwahiyo nimefikiria nimeona ni heri tutoe hiyo mim..." alinambia, lakini sikumpa nafasi hata ya kumalizia sentensi yake kwasababu nilishaelewa kwamba anataka kusema 'nitoe mimba'
"Nikatoe!? Sise hivi unanipenda kweli?" nikamuuliza kwasababu kwa jinsi ninavyofahamu mimi suala la utoaji mimba ni nusu ya kufa na kupona.
"Ndiyo nakupenda na ndiyo maana nakwambia tukatoe. Wewe unafikiria tutawezaje kulea mtoto wakati sisi wenyewe bado ni watoto, wewe ndiyo kwanza upo darasa la nne na mimi nimebakisha mwezi mmoja tu nifanye mtihani wa taifa, tutamleaje huyo mtoto mwenzetu." akanambia Sise na kunifanya nijione punguwani kwa kukataa suala la kutoa mimba hiyo.

Alinibembeleza sana kuhusu kufanya unyama huo kwa kiumbe kisicho na hatia na nikajikuta nimekubali. Akanitaka nimpe muda atafute pesa ya kunipeleka Kigoma mjini kwa daktari asiye na maadili ambaye atashughulika na zoezi hilo.
Nilivumilia kwa mwezi mzima na nashukuru Mungu sikuwa na tumbo kubwa kwahiyo sikuweza kugundulika hata na wazazi wangu kwani pia nilijitahidi kuficha dalili zingine zenye kuashiria mimba.
Hata hivyo mwezi ulikwisha bila dalili yoyote ya kufanyika kwa zoezi la utoaji mimba tulilokubaliana, nilimtafuta na kumuuliza kulikoni na alichonijibu ni kwamba hakuwa amepata pesa ya kunipeleka mjini. Lakini alinieleza kwamba kuna mtu amemuelekeza dawa ya kienyejiyenye uwezo wa kutoa mimba haraka na kwa usalama zaidi kwahiyo atafanya mpango wa kunitafutia dawa hiyo na kunipatia.
Wiki moja baadae alinipatia dawa hiyo ambayo nilitakiwa kunywa kila jioni kwa muda wa siku tisa mfululizo.

Nikaanza dozi, nikawa nafanya kazi ya kuvizia watu wakilala nakunywa huku nikiamini punde tatizo langu lingekwishwa.
Lakini mambo yalikwenda tofauti na nilivyotaraji, badala ya kuondoa tatizo nilikuza tatizo; katika siku ya sita ya kunywa dawa ile yenye ladha chungu kama shubiri tumbo lilianza kuniuma kweli kweli kana kwamba utumbo, maini bandama na kila kitu huko tumboni vimefungana sehemu moja. Nilijikuta nimepiga yowe la kuomba msaada bila kujali kwamba kwakufanya hivyo siri yangu ingevuja.
Baba na mama yangu walikuja kunipa msaada na walihoji kulikoni lakini sikuwajibu, badala yake walipata jibu kutoka katika chombo nilichokitumia kunywea ile dawa. Mama alipokiona alikinusa na kugundua kwamba nimekunywa dawa gani na kwa lengo gani.
“Sikujua mwanangu una mimba!?” aliniuliza kwa uchungu mama yangu lakini huo haukuwa muda wa maswali.
Haraka walinichukua na kunipeleka hospitali kwa ajili ya kuikomboa roho yangu, nilipatiwa matibabu na kesho yake niliruhusiwa.

Hadi muda huo tayari hakukuwa na siri tena, wazazi wangu walifahamu na hata waliponihoji sikuona sababu ya kuwaficha, niliwaeleza kuwa kweli nilikuwa mjamzito na mimba yenyewe ilikuwa ni ya Sise Zekila.
Wazazi wangu walikwenda kwa wazazi wake ili kufanya mazungumzo nao lakini waliambulia taarifa ya kwamba Sise hakuwepo mkoani Kigoma.
"Amekwenda Dar es Salaam, amepata timu ya kucheza huko." walitaarifiwa wazazi wangu.
"Kwahiyo hatuwezi kuukubali huo ujauzito ikiwa mtu wa kuthibitisha hatunaye." waliongeza wazazi wa Sise.
Baba na mama yangu walinyoosha mikono juu, walirejea nyumbani na kunielezea kila kilichojiri huko.
Nililia sana huku nikiwaomba msamaha wazazi wangu, niligundua kwamba nimewakosea na kuwavunjia heshima, lakini tayari maji yalishamwagika, ilikuwa ni vigumu kuzoleka. Daima na milele ningeonekana mkosefu kwa kosa lile nililolifanya.
Niliendelea kulea mimba yangu kwa gharama za wazazi wangu pekee huku nikisitishwa kwenda shule kwasababu sheria haikuwa ikiniruhusu, hapo ndipo niliamini kwamba 'Kila mchuma janga hula na wa kwao'.

Miezi tisa ikatimu, muda ambao nilitarajiwa kujifungua lakini mambo hayakuwa hivyo. Mwezi huo ulipita bila dalili zozote za uchungu na kwasababu sikuwa nikihudhuriakliniki sikufahamu tatizo ni nini.
Katikati ya mwezi wa kumi wa ujauzito ndipo niliposhikwa na uchungu. Kwa msaada hafifuwa mkunga wa jadi nilijifungua kwa taabu na maumivu makali sana huku mtoto akigoma kutoka kwa muda kadhaa. Ilibidi mkunga atumie uzoefu wake kunisaidia kumtoa mtoto huyo lakini mwanangu alitoka kwa mtindo usio wa kawaida; hakuliahata kidogo wakati kwa kawaida mtoto anapozaliwa huangua kilio cha kuthibitisha kwamba yu hai.
Lakini kama hiyo haitoshi mimi nilipoteza fahamudakika ya tano baada ya kujifungua na nilizinduka masaa matatu baadae.
“Mwanangu yuko wapi?” lilikuwa swali langu la kwanza mara baada ya kurejewa nafahamu kwani hamu na kiu ya kumuona mwanangu ilinikamata kweli kweli.
“Yupo chumbani kwangu.” Alinijibu mama huku akininyanyua ili niketi na si kulala tena.

“Nipeleke nikamuone.”
“Pumzika kwa muda kidogo nitakupeleka, bado haujapata ahueni.” nilijibiwa na nikawa mpole.
Lakini kumbe sikujua kuwa kuna jambo nafichwa, jambo ambalo wao walidhani kwamba laiti kama ningelifahamu mapema basi bila shaka ningeweza hata kupoteza maisha.
Hata hivyo wasingeweza kuitunza siri hiyo milele daima, nilipoona sipelekwi kumuona mwanangu niliyemzaa nikiwa na miaka 13 tu nilianza kusumbua.
“Nipelekeni kwa mwanangu.” Niliwakazania mara kwa mara na ndipo walipoamua kunipeleka kwenye chumba alichokuwa mwanangu.
Nilipooneshwa mtoto niliyezaa sikuamini, tena moyo uligoma kukubali kabisa; kwa muonekano hakuwa akistahili kuitwa binadamu lakini kwasababu alizaliwa na binadamu basi sifa hiyo ilimfaa.
Mwanangu alikuwa na maumbile tofauti na watoto wanaozaliwa na wanadamu wengine. Alikuwa na kichwa kikubwa kama mpira wa kikapu, macho makubwa yaliyovimba na kutoka nje kama gorori, mdomo wake ulikuwa umeziba, haujachanika kama ilivyokawaida hakuwa na pua wala masikio ingawa mwili wake ulikuwa kama watoto wengine tu na mbaya zaidi alikuwa amefariki.

Nililia kwa uchungu, tena uchungu uliokithiri, na maumivu yalizidi maradufu pale mama aliponieleza kwamba hayo yote ni kwasababu ya ile dawa niliyopewa na Sise. Alinieleza kwamba dawa ile hutoa mimba endapo inatumika kwa kiwango sahihi lakini kama hutumiwa vibaya huwa na madhara makubwa.
Kwasababu hiyo tu nikajikuta namchukia Sise kupita kawaida na nasadiki kwamba ningeweza hata kumuua kama angekuwa karibu yangu kwasababu ni yeye aliyeyabadilisha maisha yangu toka katika vijito vya furaha kuwa bahari ya mateso. Amesababisha nimekatisha masomo kwa kunijaza mimba, ameniacha bila msaada kwa kutokomea mjini, amepelekea nimezaa maajabu lakini kama hiyo haitoshi amekuwa chanzo cha umauti wa mtoto niliyemzaa, pia ni yeye ambaye amesababisha nyumbani kwetu naonekana mshenzi nisiyefaa duniani.

****************************

Kuzaa kwangu hakukuniachia jeraha moja tu kwani punde baada ya kujifungua niligundua kuwa nina tatizo jipya.
Siku hiyo nilikuwa naponda chikichi kwa ajili ya kutengeneza mafuta ya kupikia. Nakumbuka nilikuwa nimeketi chini kwa kukunja miguu na kuikalia kwa nyuma lakini ghafla nilihisi kulowana miguuni, nilisimama haraka na nilipotupa jicho pale nilipokuwa nimeketi kulikuwa na maji ambayo pia niligundua kwamba yametoka mwilini mwangu kwani hata sketi yangu ilikuwa imelowana halikadhalika na nguo yangu ya ndani.
“Nimejikojolea!?” nilijiuliza kwa mshangao kwani niliamini kujikolea mchana kweupe tena nikiwa macho hata sijalala ni jambo ambalo haliwezekani.

Niligusa sketi yangu na kunusa na ndipo nilipothibitisha kwamba kweli ilikuwa ni mikojo.Nilijishangaa sana, ni vipi nilishindwa kugundua kuwa nina mkojo na nikauzuia kama ilivyokawaida badala yake najikojolea bila kujitambua.
Lakini tukiokama hilo lilinitokea jioni ya siku hiyo na halikukoma bali lilikuwa endelevu. Lilijirudia tena na tena na kunipa mtihani mzito wa kuficha siri hiyo ambayo hata mimi sikuwa nafahamu nina tatizo gani.
Kwa kifupi ni kwamba nilipatwa na ugonjwa uitwao Fistula, ugonjwa ambao husababishwa na tundu ambalo hutokea kati ya uke na kibofu cha mkojo au kwenye mfuko wa haja kubwa na kusababisha mwananmke kushindwa kuzuia mkojo au haja kubwa ama vyote kwa pamoja. Hiyo hutokea baada ya kichwa cha mtoto kushindwa kupita na kubana kwenye njia ya uzazi kwa muda mrefu.

Zipo sababu nyingi zinazosababisha Fistula lakini kwa upande wangu nilipata Fistula kwasababu ya kujifungua nikiwa na umri mdogo, njia zangu hazikuwa tayari kwa ajili ya kupata mtoto kwa njia za kawaida.
Lakini kwamuda huo sikuwa nikifahamu kwamba nilipatwa na fistula, badala yake nilidhani kuwa nimerogwa. Si mimi tu, hata wazazi wangu walipogundua tatizo langu walinipeleka kwa mganga ambapo baada ya kupigwa ramli tulielezwa kwamba nimerogwa na familia ya kina Sise.
“Wanataka kumchukua msukule, wamejaribu kumuua mwanzoni wamemkosa na sasa wanatumia njia hii nyingine.”Alitueleza mganga lakini pia alitudadavulia mambo mengine mengi lakini yote yalihitimishwa na kututaka tupeleke mbuzi na pesa kwa ajili ya matibabu.
Tulifanya hivyo kwasababu tulikuwa tukiamini sana ushirikina, mganga akanifanyia dawa lakini bado tatizo langu halikukoma.
Fistula ilininyima raha katika maisha yangu, sikuwa nashoga wala rafiki, watu wote walinitenga kwasababu ya tatizo langu. Nani angependa kukaa na mimi wakati nilikuwa nikitoa harufu kali ya kinyesi. Nani angetamani kuwa karibu na mimi ilihali kijijini kote nilionekana ni mwenye laana. 

Si mimi tu, hata familia yangu ilionekana imelaaniwa hasa ukizingatia kwamba watu wote kijijini walikuwa na taarifa ya kwamba niliwahi kuzaa mtoto wa ajabu.
Sikuthubutu kuongozana na wasichana wenzangu kwenda kisimani kama ilivyokuwa awali, sikuthubutu kukaa nao na kupiga soga za umbea kama ilivyokuwa mwanzo na bila shaka vikao vyote vya sasa vilinihusu mimi na tatizo langu.
Niliishi maisha ya aina hiyo kwa miaka mitatu bila matumaini yoyote ya furaha kurejea maishani mwangu.

*****************************

Siku moja nilikuwa nikirejea nyumbani toka kisimani. Nilikuwa nimebeba ndoo yangu yenye maji kichwani kamakawaida ya wanawake waendao kuchota maji.
Nikiwa njiani nilisikia mlio wa pikipiki kutoka nyuma yangu, nikasogea kwa pembeni kidogo ili kupisha pikipiki hiyo ipite lakini haikunipita, ilisimama pembeni yangu.
Ilikuwa na watu wawili, mwanaume ambaye alikuwa ni dereva na mwanamke ambaye alikuwa ameketi nyuma ya dereva, bila shaka alikuwa ni abiria.

"Dada habari yako." alinisalimu yule mwanamke ambaye kwa kumtazama tu niligundua kuwa ametoka mjini; hakuwa amepauka kama mimi, alikuwa ni mrembo mwenye viwalo vya gharama vyenye kumpendezesha na kumuongezea thamani.
“Safi.” Nilimuitikia.
"Samahani naomba kuuliza."
"Uliza tu." nilimjibu.
"Eti unapahafahamu kwa mzee Motimoti?"
"Ndiyo namfahamu" 
"Ni mbali na hapa?"
"Hapana."
"Oooh... Basi naomba unipeleke kama hutojali."
"Sawa." nikamkubalia bila kujali kwani watu tuliokulia vijijini ni wakarimu sana.
Akateremka kwenye pikipiki na kulipa nauli kwa dereva kisha mimi na mwanamke huyo tukaanza safari ya kwenda kwa mzee Motimoti.

Tukiwa tumebakisha umbali kidogo kufika nyumbani kwa mzee Motimoti nilihisi kulowana maeneo ya mapajani, sikujiuliza mara mbili mbili, niligundua kuwa ni lazima nitakuwa nimejikojolea. Mara nyingi huwa hivyo, mkojo unaponishika hutoka tu bila ya mimi kuwa na mamlaka ya kuuzuia.
Nikasimama ghafla kwa fedhea wakati yule msichana niliyekuwa nimeongozana naye alikuwa ametangulia mbele akizungumza bila kujua kwamba anayezungumza naye amemuacha nyuma.
Alipong'amua hilo akasimama na kunigeukia, akanitazama hazikuisha sekunde tatu akagundua kulowana kwangu.
"Vipi?" akaniuliza.
Sikumjibu.
"Unaumwa?" akaniuliza tena huku akinisogelea lakini bado sikumjibu.

Si kwamba sikuwa naweza kuzungumza, La hasha! Bali aibu na fedhea vilinifumba mdomo kabisa na sikuweza hata kumtazama usoni msichana yule.
"Usijali," akanambia na kunifanya ninyanyue uso kumtazama.
"Ndiyo usijali, najua unaumwa Fistula." akanambia na kuzidi kuniacha njia panda kwani sikuwahi kusikia ugonjwa uitwao fistula tangu kuzaliwa kwangu.
Papo hapo akafungua begi lake na kutoa upande wa kanga, kisha akanipatia na kunitaka nijifunge ili kuziba doa la kulowana lilijitokeza kwenye kanga yangu niliyovaa. Nikatua ndoo yangu na kuvaa kanga aliyonipa huku nikishindwa kabisa kumtafsiri yule binti, nilimuona kama ni malaika mwema aliyetumwa na Mungu kuja kunithibitishia kwamba upendo bado unaishi duniani. 
"Nyumbani wapi?" akaniuliza na nikajibu kwa kuelekeza kwa kidole.
"Si mbali na kwa mzee Motimoti?"
"Ndiyo."

"Twende nikusindikize, wewe beba begi langu mimi nitabeba hii ndoo yako." akanambia huku akinikabidhi begi lake dogo lililonona kwa kujazwa nguo, akajitishwa ndoo yangusafari ya kuelekea nyumbani ikaanza.
Hatukutumia muda mwingi tulifika, nikamkaribisha kwa kuingiza begi lake ndani na kuja kumtua ndoo kabla ya kumvutia kigoda cha kukalia.Kisha nikamuita mama ili nijie kumtambulisha kwa binti huyo nisiyefahamu hata jina lake, akatokea ndani kwake kuja nje na baada ya salamu tu nilifanya utambulisho kumueleza mama yangu juu ya wema wa binti huyo ambaye alijitambulisha kwetu kuwa anaitwa Upendo.
Basi Upendo alitaka nimueleze kuhusu tukio lilitokea pale nami sikuona sababu ya kumficha. Nilimueleza kuhusu mateso nipatayo ya kiafya na kijamii na nakumbuka baada ya kumsimulia mambo yote kiundani zaidi alinieleza kwamba amegundua kuwa nimeathiriwa na fistula na akaahidi kunipeleka Dar es Salaam katika hospitali ya CCBRT kwa ajili ya matibabu na alinithibitishia kwamba nitapona kabisa.

"Fistula imetesa watu wengi na mara nyingi hutokea kwa wanawake masikini walio kijijini na wasio na huduma bora za afya hasa katika nchi zinazoendelea." alitueleza.
Pia alitueleza kwamba yeye ni mtoto wa mdogo wake mzee Motimoti na amekuja kijijini kwetu kumtembelea baba yake mkubwa.
“Nitakaa siku nne tu kwahiyo nikirejea Dar es Salaam tutaondoka sote.” Alinambia.
Ikawa hivyo, siku ya siku ilipofika Upendo alisafiri pamoja na mimi hadi Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu huku wazazi wangu wakiwa wameridhia suala hilo.
Kweli nilifika Dar es Salaam na kuishi nyumbani kwake kwa siku mbili kabla ya siku ya tatu kunipeleka hospitali ambapo nilishughulikiwa tatizo langu na kupona kabisa ingawa pia fistula iliniacha mgumba; hayo ni moja ya matokeo ya kuumwa fistula.
Lakini pia Upendo alijitolea kunisaidia baada ya kumuelezea historia ya maisha yangu kwa ujumla. Alinipeleka shule ya ufundi wa kudarizi na nikajifunza shughuli hiyo ambayo hadi sasa ndiyo inayoniweka mjini.

Namiliki kibanda changu hapa hapa Dar es Salaam na pia ninaishi na wazazi wangu ambao niliwafuata Kigoma waje kufaidi matunda ya binti wao japo si kwa kiasi walichokuwa wakitarajia.
Niliwafuata baada ya kuishi Dar es Salaam kwa zaidi ya mwaka mmoja, na nilipowafuata pia nilipata habari za Sise, niliambiwa kwamba amefariki dunia akiwa Kigoma kutokana na kuathirika na madawa ya kulevya ambayo yalimgeuza kuwa mwendawazimu.
“Hakuwa na cha kucheza mpira wala nini, alikuwa anauza maji ya kutembeza mabarabarani na naona ni huko ambako alijifunza ushenzi huo ulimuondoa duniani.’’ Nilipewa taarifa na redio mbao huku akisindikiza kwa kunisimulia jinsi Sise alivyoteswa na madawa.
Alinambia kwamba wazazi wake walihangaika naye kwa waganga wa kienyeji bila mafanikio lakini walipompeleka hospitali walielezwa tatizo na haraka akaingizwa katika kitengo cha matibabu ya waathirika wa madawa ya kulevya.

Hata hivyo walikuwa wameshachelewa, Sise alikuwa kwenye hali mbaya naalifariki katika siku za mwanzo za matibabu.
Mwisho wa yote namshukuru Mungu niko hai na si tegemezi, nina nguvu na uwezo wa kujitafutia riziki ya halali. Kifo cha Sise wala hakina madhara yoyote katika maisha yangu ingawa sitamsahau kwasababu ni yeye aliyenifanya nizijue pande mbili za maisha; yaani furaha, amani, uhuru, upendo, vicheko na tabasamu kwa kipindi kile tulichokuwa tukipendana na upande wa pili ambao ni huzuni, majonzi, vilio, maombolezo, na kukata tamaa kwa kipindi ambacho alinitelekeza na mimba yake.
Mungu amlaze mahali pema.

*************************

Mwisho!

Post a Comment

0 Comments