Header Ads Widget

Responsive Advertisement

USINILILIE MIMI KAWASIMULIE WANAO - 4





Simulizi : Usinililie Mimi Kawasimulie Wanao
Sehemu Ya Nne (4)


“Mama mguu wangu nd’o haurudi tena??” nilimuuliza mama aliyekuwa ameketi kando yangu. Swali ambalo nilijua jibu lake kuwa ni NDIYO…. Lakini mama wa ajabu hakunijibu kama nilivyotaraji. “Ipo siku utatembea tena! Na hapo nitakupa jibu lako” Jibu la mama nilinistaajabisha mno, nilifahamu fika kuwa ananitia moyo lakini ilikuwa vyema kuliko kunikatisha tamaa. Tabasamu la uchungu lilichukua nafasi nilipoikumbuka ile ndoto ya mchezo ule ambao nilifunga magoli mawili. Baada ya siku mbili nikaanza rasmi mazoezi ya kutembea kwa kutumia magongo, zoezi lilikuwa gumu haswa nilitokwa jasho haswa.
Mama alikuwa kando yangu kunipa moyo kuwa hata kile nilichokuwa napitia ni mtihani katika maisha. Mabega yaliuma sana, makwapa yaliwaka moto haswa na nilikuwa naanguka mara kwa mara, bado mama alikuwepo kuninyanyua
“Usipomkufuru Mungu katika hili unalopitia, digrii utakayoitwaa hapa ni mara elfu ya hiyo ambayo ungechukua huko chuoni kwenu!!” mama alinieleza wakati nikiwa nimepumzika. Alipozungumzia juu ya digrii nikaikumbuka hiyo tarehe na mwezi nikakumbuka kuwa wanafunzi niliosoma nao darasa moja, iwapo hawakufeli basi walikuwa wapo mwaka wa pili wa chuo SEMISTA YA KWANZA. Nami nilikuwa mwaka wa pili wa mateso SEMISTA YA KWANZA. Mwaka niliouanza kwa kukatwa mguu wangu wa kulia!!
Siku ya sita ya mazoezi nikiwa nimeanza kuyazoea ndipo nilikutana na kitu ambacho sikukitegemea hata kidogo. Ukawa mwanzo wa tabasamu la muda mfupi na kisha ukafuatia ule muda wa kumtambua mbaya wangu, shetani aliyeniadhibu hivi lakini licha ya haya yote ile pingu ya uchungu na majanga ya mara kwa mara ikaendelea kunifunga. Amakweli kumjua adui yako waweza kulimaliza tatizo ama kuliongeza maradufu hasahasa ikitegemea ulifanya nini baada ya kumgundua adui yako!! Nilikosea sana kwa njia nilizotumia!!
Ewe mwenyezi Mungu nisamehe!!
“G….Gerlad…..” sauti ilisikika kutokea nyuma yangu ikiniita kama mtu asiyekuwa na uhakika na anayemuita. Nikayaweka magongo yangu sawa kisha nikageuza shingo yangu nitazame ni nani alikuwa akiniita. Niliangaza vyema na bado sikumuona mtu ambaye sura yake ilikuwa katika kumbukumbu zangu!!
“Kuna Gerlad mwingine hapa aidha mgonjwa ama muuguzi…” nilijisemea huku nikiamua kuchukua uelekeo uleule ambao nilikuwa nimegeukia baada ya kuwa nimeitwa kimakosa. Nilijikongoja na magongo ambayo nilikuwa nimeyazoea.
Ni yeye!! Niliwasikia watu wakisemezana kwa sautiu ya chini, sikuwatilia maanani sana maana wangeweza kumzungumzia mtu mwingine haikuwa lazima niwe mimi.
“Gerlad……Masembo!!” sauti ile ile ikaniita huku ikimalizia na ubini wangu wakati huu. Hapo nikapata uhakika kuwa ni mimi niliyekuwa naitwa!! Nikaigeuza shingo yangu na kukutana na watu wawili ambao hawakuwa wageni sana machoni kwangu lakini hata sikukumbuka ni wapi tuliwahi kuonana.
“Christian Ronaldo!! Ni wewe.” Alisema bwana yule huku akinitazama kwa makini, kisha macho yake yakashuka na kuutazama mguu wangu. Aliponyanyuka tena alikuwa anajaribu kujizuia asitokwe machozi… alijaribu na hakufanikiwa, akaanza kububujikwa na machozi. Huyu ni nani!! Nilijiuliza huku nikijaribu kumtafakari.
“Wanadamu.. wanadamu waliona unafaidi sana… aaah!! Wanadamu.” Alizungumza haya huku akiendelea kulia, kitambaa chake mkononi akijifuta machozi. Mara akazitazama mbingu kwa muda. Aliposhusha kichwa chake akanitazama na kutabasamu.
“Christiano Ronaldo huwezi kunikumbuka kirahisi kaka…. Huwezi kunikumbuka kwa sababu moja tu… ulikuwa na bado una mashabiki wengi sana. Japo na wanafiki waliambatana nasi katika kundi la mashabiki wa ukweli.” “Hulijui jina langu Gerlad hulijui….” Akanieleza, yaani ni kama alikuwa akiisoma akili yangu. Nilikuwa najaribu kulikumbuka jina lake bila mafanikio yoyote.
“Hata hivyo wakati ule nilikuwa mwembamba sana bwana…. Ni haki yako kunisahau. Lakini katika kipindi chote ambacho sikuwa nafahamu ulipo bado niliishi nawe Gerlad….. niliishi nawe. Na sasa naweza kukukumbusha usemi wangu kuwa mimi ni shabiki wako namba moja!!” alisita akaipandisha shati yake juu kidogo kisha macho yangu yakaona kitu kilichonistaajabisha sana. Ilikuwa ni cheni iliyokuwa na herufi ya jina langu. ‘G’. kumbukumbu zikarejea harakaharaka na kumfahamu yule bwana mbele yangu. Kuna mahali niliwahi kukutana naye na alinionyesha ile cheni na kunieleza kuwa yeye ni shabiki wangu mkubwa na mtoto wake wa kwanza amempa jina langu kama lilivyo, Gerlad Masembo. Nilijisogeza karibu yake na kumkumbatia kwa nguvu huku nikijiweka katika tahadhari yale magongo yasije kuniangusha. Alilia sana baada ya kunikumbatia huku akilalamika kuwa wanadamu si wema hata kidogo. “Ulipoanguka siku ile uwanjani nilihisi kitu tu Gerlad… nilihisi kitu ambacho kimenisumbua kichwa hadi nilipokuja kupata jibu!!..... kwanini nilizuiliwa kukutibu, kwa nini wajichague wenyewe tu katika zoezi lile watu wabaya sana wale…… na baada ya kuhisi nitafuatili kwa ukaribu washenzi wakanichezea mchezo mchafu.
Nikatupwa Bugando Mwanza……” alianza kunisimulia bwana yule ambaye alikuwa ni daktari. Nilikuwa makini kumsikiliza huku nikiamini kuwa analo zito la kunieleza.
“Dunia haina siri sasa…. Siri zote nje. Ningejua hila zao nisingeruhusu uje kutibiwa Muhimbili…. Yaani watu wabaya wamejificha humu na kujivika mavazi meupe kisha wanapewa heshima ya kitabibu bastard kabisa.” akasonya huku akitikisa kichwa kushoto na kulia kisha akaendelea, “Unamfahamu vipi Mustapha..huyu Inspekta Mustapha….” Alinieleza kwa kunong’ona…..
“Nilikuwa ama niseme binti yake ni mpenzi wangu…..”
“Aaaargh Gerlad na umakini wako wote uwanjani hukuwa makini katika kuchagua mwanamke mwingine hadi ukajiingiza kwa huyo binti Gerlad!!” alilalama na sikuelewa ana maana gani. “Nani asiyemjua Mustapha na ushirikina wake huyo.. hata mtoto yule wanadai si wake….. tena wanaweza kuwa sahihi…. Mtoto yule anatumika kutafuna tu watu na kuwatoa kafara kwa niaba ya baba yake mshirikina yule na kama ananisikia anisikie tu nimesema tayari. Inspekta Mustapha ni mshirikina, na hata cheo hicho amekipata kishirikina tu…. Haujiulizi vipi mbona ahamishwi kituo miaka nenda rudi….” Alinitupia mfano wa swali huku akinitazama.
“Nani amehusika katika upasuaji.. upasuaji wa mguu wako ama sio hospitali hii…..”
“Daktari mmoja anaitwa Fonga wa Fonga….”
“Whaaaat!!!” akagutuka yule bwana huku akisimama wima… akajishika kichwa chake kisha akazunguka kushoto na kulia.
“Fanga… daktari Fanga?? This is too much sasa…” alizidi kuzungumza peke yake.
“Kwani ana nini …aah kuna nini kwani.” “Fanga died three years ago….. how come he…he…. No it can’t be… washenzi hawa watakufanya kama walivyomfanya Benson Makeve!!” akajibu kwa hamaniko kubwa na sasa alikuwa ananikazia macho.
“Nani alishuhudia upasuaji huo??”
“Mama..”
“Yupo wapi?” akauliza upesi upesi. Bahati nzuri mama hakuwa mbali sana. Nikamwonyesha. Akaondoka upesi upesi nami nikamfuata nyuma nikiwa na magongo yangu. Hofu ilikuwa imeniandama katika nafsi yangu. Nilijaribu kusukuma yale magongo kwa jitihada zote nilizoweza lakini sikumfikia yule bwana aliyekuwa na ghadhabu haswa, alielekea moja kwa moja alipokuwa mama. Nilifika na kumkuta akimaliza kumsalimia.
“Mama samahani naitwa Sadath ni rafiki wa karibu wa mwanao na ni mshabiki wake mkubwa lakini kubwa zaidi ni daktari. Nina swali moja ambalo linaweza kuzaa mengine naomba nikuulize na ninatanguliza samahani kama litakukwaza…”
“Muulize tu…” niliwahi kumjibia mama aliyekuwa akijiuliza iwapo akubali ama la! “Mama unamfahamu daktari aliyefanya upasuaji huu….” Alisema huku akiutazama mguu wangu. “Ndiyo mwanangu… ni baba mnmoja mkarimu sana anaitwa mzee Fanga…” mama alijibu kwa upole.
“Mkarimu!!!” aling’aka Sadath kisha akajirekebisha na kuushusha munkari wake.
“Bila shaka ni yeye anayesimamia maendeleo ya mwanao…. Je anasemaje na anapatikana ofisi gani….” Aliuliza huku akiangaza macho huku na kule. Mama akamuelekeza!! Akataka kuondoka lakini akasita ghafla.
“Na daktari aliyetoa wazo la mguu kukatwa ni huyu huyu ama….”
“Hapana ni daktari mwingine huko Morogoro.. yeye anaitwa daktari Majura.”
“Daktari nani??” “Daktari Majura…” alijibu tena mama huku akionekana kuanza kumwogopa yule bwana.
“Appearance yake ikoje… I mean muonekano wake upoje…”
“Mweusi mfupi….”
“Ndevu zake zikoje…”
“Zimeunga O..” akamalizia mama nami nikatikisa kichwa kwa sababu ninamkumbuka haswa. “Oooh my God…..oooh my oooh my…” alihamanika haswa.
“Gerlad nawe ulimshuhudia huyo dokta Majura..”
“Ndio kama alivyosema mama…”
“Na hata haukushtuka kuwa unahudumiwa na maiti inayoishi?? Washirikina wale…. Pumbavu zao!! Wameondoka na mguu wa dhahabu!!” alizungumza peke yake huku akionyesha wazi kupagawa. Na hapo akatoka mbiombio kuelekea huko alipoelekezwa na mama kuwa ni ofisi ya Fanga wa Fanga. Kilichofuata baada ya dakika kumi zilikuwa ni vurugu za hali ya juu. Makelele yalisikika kutoka huko ndani, wauguzi wakatimua mbio huku na kule wakiwa katika taharuki. Vilio vya wagonjwa vikasikika, walinzi wakaliacha geti kuu na kutimua mbio kwenda huko kelele zilipokuwa zinatokea.
“Masembooooo!!” niliisikia sauti ya ikiniita, ilikuwa sauti ya Sadath. Nikalichukua gongo langu, mama alinizuia bila jitihada zake kufanikiwa. Nikaongoza njia kuelekea mbele sauti ilipokuwa inatokea. Muuguzi mmoja akiwa ametaharuki alikimbia vibaya huku akiangalia nyuma akanivamia na kuniangusha chini. Nikajikongoja nakuinuka, gongo moja lilikuwa mbali nami. Nikatumia lile moja na nilipoona loinazidi kunisumbua nikalitupa mbali na kuanza kurukaruka kwa kutumia mguu mmoja. Nikazidi kupenya hadi nikalifikia eneo husika.
“Kwa mguu wako wa dhahabu mtunze wajina wako, Gerlad Masembo. Mfikishie taarifa mke wangu mwambie nimepotea katika vita ya kuupigania mguu wa dhahabu, ukiniona tena usiniamini…nimekufa.. usiniamini kwa lolote nakufa mimi… kaitafute amani yako na usiwaamini wanadamu. Maiti wanaoishi…. Inspekta mbaya yule mbaya sana…..” akasita kuzungumza kisha akafanya jambo ambalo linaniweka katika wakati mgumu sana kuliamini japo lilitokea nikiwa naona… hakika maneno ya mama kuwa kuna wanadamu wanautumia uwezo wao kunyanyasa wengine ulikuwa sawa kabisa. Masembo akarusha kitu kilichokuwa na kimetapakaa damu,nikatazama kikienda juu kisha kwa nguvu sana kikanivamia pale mguu ulipokatikia. Nikaanguka chini kwa kishindo, kizunguzungu kikanishika na hapo nikayasikia makelele yakizidi kutoweka mbali na kusogea karibu yangu.
“Amka wewe kuna shoti ya umeme utakufa…” nesi mmoja alinikurupusha kutoka mahali nilipokuwa. Nikajisogeza nyuma na kusimama. Amini usiamini, Gerlad Masembo nilikuwa na miguu yangu yote miwili. Hapakuwa na mguu wenye maumivu tena. Nikajaribu kutembea, nikaweza!!

Kwa mara ya kwanza nikaamini kuwa hakika wachawi wanaishi!!
JIFUNZE!! Ni heri kuamini jambo fulani lipo na siku moja utambue kuwa halipo kuliko kuamini kuwa halipo na mwisho unalikuta… hakika litakutesa sana!!!



MAMA alibaki mdomo wazi huku akirudi nyuma hatua kadhaa. Na kisha akasita kurudi nyuma, akaanza kunifuata.
“Mungu anajibu… yashuhudie haya popote uendapo amini Mungu aliumba kwa kusema nawe sema mema na mema yatakutokea. Nilisema kwa kinywa chake Mungu… siku moja utatembea….. nilisema hata juma moja halijapita…..” mama akapiga magoti chini mikono yake juu mbinguni. Hakika lilikuwa jambo la kushukuru sana. Na hilo lilikuwa shuhudio la mwisho la mama kwa mwanaye.
Pigo kuu kuliko yote!!
Ghafla mabomu ya machozi yalianza kupigwa eneo lile, sikufahamu ni kitu gani kinatokea lakini baadaye nilikuja kuelezwa kuwa polisi walipewa tarifa za uvamizi hospitali na aliyetoa taarifa alijitambulisha kuwa ni raia mwema na jina lake ni Fanga.
Hivyo walivyofika pale walianza kuwatawanya watu!! Ukosefu wa umakini wa jeshi letu… hivi kwa nini hawakwenda hatua moja kwa nyingine tazama mabomu yao yakatoa moshi mkali mama akauvuta, akaikosa hewa ya kupumua.
Ooh!! Mama akapoteza uhai huku akiwa ameshuhudia tu mguu wa mwanaye.. mama akanyamaza kimya na kuniachia upweke wa milele, mama akaondoka na nasaha zake, mama aaah!! Sina la kusema zaidi. Madaktari hawakuweza kuzuia hili!
Ulikufa katika imani yako thabiti kama kuna mengineyo maovu nisiyoyajua basi Mungu akusamehe!!
****
hakuwepo ndugu wa kumzika mama yangu, hakuwepo hata mmoja! Kwa huzuni kuu, serikali ikacvhukua jukumu hilo na mama akazikwa na serikali bila mipangilio maalumu. Ni mimi pekee niliyekuwa namfahamu marehemu. Nikautupa mchanga wa mwisho nikamfukia mama yangu katika nyumba yake ya milele. Nilishindwa kuamini nilivyobaki kulia na kugaagaa peke yangu juu ya lile kaburi, bila ndugu hata mmoja wa kuniambia ‘pole’ bila mpenzi wa kunishika bega na kuniambia ‘jikaze mpenzi wangu’. Mwishowe nikalazimika kuamini kuwa mama alikuwa ameenda na kamwe hatarejea tena. Majira ya saa kumi na mbili jioni, nikajikongongoja na hapo ndipo nikakumbuka kuwa wakati wa kuja nilikuja na gari la serikali na sasa natakiwa kuondoka mimi kama mimi na mfukoni sikuwa na nauli. Hili halikuniumiza kichwa niliijua sababu ya kukosa nauli ni moja tu… kwa sababu nilikuwa na mguu unaoweza kutembea tena.
“Gerlad” mara nikaisikia sauti ikisema nyuma yangu… ilikuwa sauti ya kiume na nilipogeuka sikukuta mtu yeyote lakini sauti nilikuwa naifahamu. Ilikuwa sauti ya Sadath!! Nikayakumbuka maonyo yake kuwa akifa amekufa na nisimsikilize tena. Kisha yale maneno yake ya kunisihi juu ya mtoto wake ambaye alimtunuku jina langu.
****
HEKAHEKA CHUONI!!
Nilitembea kwa miguu kutokea Kinondoni makaburini hadi chuoni, nilikata tamaa mwanzo tu lakini mwishowe nikahisi mama anaishi nami kwani kila hatua niliyopiga niliyasikia maneno yake yaliyojaa busara. Ama kwa hakika mama alikuwa amesema nami maneno mengi sana enzi za uhai wake ni maneno yaliyotosha kabisa kuishi nami kwa miaka mingine mingi sana. Nitalala wapi? Hili lilikuwa swali wakati nikiyavuka mataa ya Magomeni bila kujua ni wapi naelekea zaidi.
Chuoni labda!!
Nilijishauri na kukaza mwendo zaidi kuelekea chuoni. Sura nyingi zilikuwa ngeni na isitoshe kwa ugeni ule wa usiku basi kila mmoja alijali mambo yake aliyoyatambua. Kwa mbali niliiona sura ya mwanadada ambaye niliwahi kusoma naye japo alikuwa anachukua masomo ya sheria mwaka mmoja zaidi yangu. Jina lake kamwe halikutoka katika kichwa changu. Getruda!! Nikamuita katika akili yangu bila kutoa sauti nje kisha hatua kwa hatua nikamsogelea na kumgusa bega.
“Vipi wewe…” akanihoji.
“Habari za siku nyingi dada Getu.” Nilimsalimu kwa sauti ya chini.
“We ni nani? Poa lakini …”
“Sogea karibu yangu na unitambue zaidi.” Nilimsihi.. akapiga hatua moja na kunifikia.
“Ge…Gerlad…. Mungu wangu… ooh!! Gerlad.” Aliduwaa huku maneno yale yakimtoka. Nikatabasamu, lakini upesi akanivuta mkono na kunisogeza kando.
“Gerlad what happened? Eer nini kimetokea Gerlad..” aliniuliza nikadhani anagusia juu ya hali yangu ya kuwa kama nilivyokuwa.
“Mungu anatenda muujiza wake juu yangu!!” nikamjibu huku nikizidi kujisikia fahari kuwa ndani ya ushuhuda huo.
“Gerlad.. muujiza wa kushiriki jaribio la kuiba hospitali. Kudanganya kuwa wewe ni mgonjwa ili ukaribishe majangili hospitali… ni nini hiki unakiita miujiza Gerlad eer!!” alizungumza kwa hisia dada huyu ambaye alitokea kuwa rafiki yangu kutokana na ushabiki wake katika mchezo wa soka enzi hizo nikiwa chuo.
“Nini? Unasemaje Getu eeh mimi ni Gerlad Masembo dada. Ninajisikia fahari kutoa ushuhuda huu kuwa …” nilitaka kuendelea kusimulia lakini yule dada mwanasheria akanivuta sehemu iliyokuwa na giza zaidi.
“Gerlad upo katika akili zako sahihi kweli..”
“Ndiyo Getu tena timamu sana, ningewezaje kukukumbuka wewe katika giza hili?” nilimtupia swali ambalo lilileta utulivu kiasi.
“Umetoka wapi muda huu na unafanya nini hapa?”
“Natoka Kinondoni makaburini kumuhifadhi mama yangu na hapa sijui ni kitu gani nimefuata, nimejikuta tu nakuja hapa. Sina sehemu ya kulala!!” “Oooh!! Unazidi kunichanganya Gerlad, wanadai aliyeuwawa ni jambazi tena jambazi katili la kike. Sikia nina watu wangu wananipenyezea haya mambo chinichini….. kuwa mwangalifu Gerlad nadhani ndani ya siku mbili kila mtu atajua juu ya hili. Wewe unajulikana sana tafadhali kama kuna shirki yoyote umefanya jiweke mbali. Unaikumbuka ile kanuni niliyokufundisha.. KUTOIJUA SHERIA SIO UHALALISHO WA KUIVUNJA SHERIA….. Kanuni hii itakufunga kwa namna yoyote…” “Getu sikuelewi ujue yaani mimi nimekuja hapa nikitarajia kupata nafuu unanieleza jambo nisilolijua….”
“Vyeti vya hospitali vipo wapi….” Akanihoji. Nilikuwa mikono mitupu, nikatamani aniamini hivyohivyo pasi na vitambulisho vyovyote lakini haikuwa. Akatambua kuwa nimetetereka.
“Gerlad kipo wapi cha kuthibitisha kuwa ulilazwa wewe hapo Muhimbili…..” akakazia.
“Kuna vurugu zilitokea na mkoba wa mama utakuwa ulipo…”
“Shhhhh! Mkoba gani wa mama, acha Gerlad acha kumsema mama kwanza…mkoba huo wenye bunduki na risasi. Mkoba rangi ya udhurungi uliochakaa.” Getruda aliutaja mkoba halisi wa mama. Kuhusu habari ya risasi nikaamua kuwa mkali.
“Getruda…. Kaa kimya na unisikilize dada… nisikilize ninachosema!!! Mama yangu ameuwawa baada ya jitihada za madaktari kugongwa mwamba. Amezikwa na serikali baada ya kukosekana uwezo wa mimi kumsafirisha Morogoro kwa maziko. Mama hajalizoea hata kaburi mnamzushia kesi ya mauaji sijui kukutwa na bunduki, yaani vitabu vyake vya dini wamevitoa na kuweka bunduki, si waniue na mimi wanangoja nini, waniue tu… kansa wamenirushia wao, mguu wangu wakaukata kimaajabu mwisho umerejea… wamenipotezea chuo changu, wamempoteza na mpenzi wa moyo wangu. Waniue… waje upesi waniue na mimi.” Nilitaka kuondoka nikiwa na ghadhabu Getu akanidaka mkono.
“Kanuni namba tisa!!” akasema, na akili yangu nayo ikafanya kazi ya kukumbuka. Mwanadamu imara haongozwi na hasira, na hawezi kuitwa imara kama hakuweza kuizuia hasira yake!! Nikanywea kisha nikaamua kukaa chini na kuanza kulia. Getruda hakufanya jitihada zozote za kunipooza wala kunibembeleza. Katika nafsi yangu nikakiri kuwa Getu habadiliki hata kidogo, alikuwa yuleyule na kanuni zake ishirini nzito za maisha alizoziita Getu’s principle. Na hata nilipokuwa nalia nilitambua fika kichwani mwake aliiheshimu kanuni yake. Kadri ubembelezavyo zaidi atalia zaidi. Kaa kimya naye atakuiga tu akigundua kuwa anapiga kelele!!! Nikagundua kuwa nami nilikuwa napiga kelele nikakaa kimya. Getruda akasogea pembeni yangu na kunigusa bega.
“Gerlad kwa mtazamo tu.. najua hujafanya kitu chochote ila ni watu wabaya tu wanaosimama nyuma ya hili jambo. Kanuni ya nchi hii LAMENSIA TANGANYIKANA ni tofauti kabisa na ile ya LAMENSIA ANGLIKANA hivyo cha muhimu na klwa usalama wako unapaswa uangalie namna ya kujiweka mbali.
“Anglikana? Tanganyikana ni nini hicho!!”
“Kanuni ya Lamensia ANGLIKANA…. Hii inatumiwa na nchi nyingi zilizoendelea na zinazojali haki za mwanadamu, ambapo wanasema ni heri wakosefu kumi waishi uraiani kuliko mwenye haki mmoja kuozea jela….. hii ni njema na ina hatari zake pia lakini walau inajali haki za mwanadamu. TANGANYIKANA ambayo inatumika Tanzania na nchi za jirani hii inasema ni heri wenye haki mia moja kuozea jela kuliko mkosefu mmoja kuishi uraiani…. Hii haijali haki za mwanadamu. Kwa hiyo ukikamatwa Gerlad LAMENSIA TANGANYIKANA itakufanya ufie jela. Unapaswa kukimbia tu na kuishi huku ukikihofia hata kivuli chako mwenyewe.” Getruda alizungumza kwa utulivu mkubwa huku maneno yake yakipenya vyema katika kichwa changu.
“Nikisema kukihofia hata kivuli chako mwenyewe namaanisha kuwa usimwamini mtu na ifikie kipindi hata wewe usijiamini likija wazo kichwani mwako usilifuate kama lilivyo. Lala usingizi mzito kisha amka uwaze tena….” Alinisisitiza.
“Sasa mi n’tajificha wapi na wakati sina kosa. Kwanini nisijitokeze hadharani tu kila kitu kifahamike wazi.” Nilihoji kwa kulalamika.
“LAMENSHIA TANGANYIKANA…” Alinijibu huku akitikisa kichwa chake kuashiria masikitiko makubwa!!
“Boom halijatoka hadi wakati huu lakini ninayo pesa kidogo ninaweza kukusaidia ili ujue wapi unaanzia….”
“Kabla hatujafikia kwenye pesa, unamfahamu daktari anaitwa Sadath….” “Huyu mtaalamu wa mifupa Muhimbili…” alimalizia. Nikatikisa kichwa kumuunga mkono jibu lake.
“Namfahamu vizuri kwani vipi…”
“Unaifahamu kidogo familia yake!!”
“Mkewe tunasoma naye Sheria… namfahamu kiasi chake japo si rafiki wa karibu. Ama niseme sio rafiki kabisa” Alinijibu bila kutetereka. “Nahitaji sana kuonana naye…”
“Kwa sababu zipi… samahani kwa kuuliza maana….”
“Mume wake kuna maagizo fulani aliniachia….”
“Mlikutana wapi na lini..”
“Amekufa akiutetea uhai wangu hospitali…..”
“Dokta Sadath amekufa??” Sikumjibu zaidi ya kumwacha aendelee kuduwaa.
“Uwe makini sana sidhani kama ni mtu mzuri sana kwa watu yule..” alinionya Getruda
*****
Gerlad Masembo….. naam alikuwa wajina wangu kweli. Umri wa mwaka mmoja tu niliona macho na miguu ya soka kutoka kwa mtoto yule. Alichukua macho ya baba yake kwa umakini, na ngozi ya mama yake kwa unadhifu. Nilimsimulia kila kitu juu ya mumewe na kutoweka kwake na maneno ambayo aliniachia.
Wakati nazungumza na mkewe kuna jambo nilijiuliza, inakuwaje dokta anisisitize juu ya mwanaye tu na asiseme lolote juu ya mkewe ambaye alikuwa mrembo haswa. Lakini baada ya muda nilianza kupata mwangaza. Mwanamke huyu alikuwa ana maringo na alijichukua sana kuwa yu daraja la juu sana. Hali ile haikunipendeza hata kidogo. Kwa hayo niliyoyaona hayakutosha kabisa kunipa jibu sahihi.
Lakini jibu halikuwa mbali sana nami. Ilikuwa safari ile aliyoniahidi Inspekta Mustapha, safari ya mateso. Siku mbili baada ya kukutana na Getruda na siku moja baada kuonana na mke wa marehemu Sadath nilijihifadhi katika nyumba ya kulala wageni huku nikiwa tayari kabisa kufanya safari siku ambayo ingefuata. Getruda aliambatana nami na kunitia moyo kuwa naweza kunyanyuka tena. Majira ya saa mbili usiku wakati Getrude akijiandaa kuondoka na kuniacha nilale, tulipata ugeni wa ghafla ndani ya kile chumba. Wanaume wawili ambao kwa kuwatazama tu walikuwa kisharishari.
“Gerlad….” Mmoja kati yao aliniita huku akinikaribia. Nilimtazama kama nilikuwa namfahamu lakini haikuwa hivyo.
“Kanuni namba sita….” Getruda alinong’ona. Akili yangu nayo ikarejea katika kanuni za ajabu za mwanadada huyu ambazo nilizikariri kama vile kuna siku nitajibia mtihani. Jihadhari hata kama si adui!! Ni heri nusu shari kuliko shari kamili!!!
Akili ikaisoma kanuni ya sita. Na hapo nikaamua kutenda, nikarusha ngumi kali sana usoni kwa yule bwana na ikampata barabara katika usawa wa jicho lake. Kosa kubwa alilokuwa amefanya ni kuvaa miwani ya giza usiku. Miwani ikapasukia jichoni. Yowe alilotoa japo ni mtoto wa kiume lazima umwonee imani. Na wakati huohuo Getrude akanionyesha kitu ambacho nilikuwa sikifahamu kutoka kwake, kumbe licha ya kuishi kwa kanuni zake bado alikuwa na kitu cha ziada. Alikuwa na mbinu za kujihami!!
Akarusha teke kali na kuupata ubavu wa yule mwanaume mwingine. Akaunguruma kwa hasira lakini haikuwa tiba, Getu akajirusha tena na kumtandika teke katika korodani zake na hapo akalikamata koromeo lake.
“Nyinyi ni akina nani… na nani amewatuma.” Aliuliza binti shupavu huku akiwa amemkazia macho yule bwana aliyekuwa akitweta.
“Huwa sihesabu hadi tatu mimi nashtukiza tu kama hutaki kujibu…” alionya na kama yule bwana alidhani ni utani basi ni yeye alikuwa anajitania. Getu akarusha ngumi kali na kulitandika jicho la yule bwana bila huruma na hapo akamziba mdomo.
“Ametutuma Mariam…” alijibu kwa tabu. Getu hakungoja akamtandika ngumi kali katika mwamba wa pua na kuisambaratisha. Hapo akanitia hofu hadi mimi na kujiuliza Getruda ni nani hasa…. Lazima alikuwa zaidi ya mwanafunzi!!
ITAENDELEA

Post a Comment

0 Comments