Simulizi : Usinililie Mimi Kawasimulie Wanao Sehemu Ya Tano (5)
“Huwa sihesabu hadi tatu mimi nashtukiza tu kama hutaki kujibu…” alionya huku akiwa antabasamu na kama yule bwana alidhani ni utani basi ni yeye alikuwa anajitania. Getu akarusha ngumi kali na kulitandika jicho la yule bwana bila huruma na hapo akamziba mdomo. Jicho likapasuka kwa chini na kuanza kuvuja damu “Ametutuma Mariam…” alijibu kwa tabu. Getu hakungoja akamtandika ngumi kali katika mwamba wa pua na kuisambaratisha. Hapo akanitia hofu hadi mimi na kujiuliza Getruda ni nani hasa…. Lazima alikuwa zaidi ya mwanafunzi!! Yule bwana ambaye awali sura yake ilikuwa inatambulika, sasa alikuwa damu tupu. Ilitisha kumtazama. Baada ya kuhoji zaidi wawili wale wakamtambulisha Maria kuwa ni mke wa marehemu Dokta Sadath. Nilibaki kuduwaa, mke wa Sadath mtu mwema kwangu anakuwaje anahusika katika vitendo viovu na vya kutisha namna ile. Ni kitu gani anahitaji kutoka kwangu hasa “Tunaenda muda huu... mmeelewa.” Aliamrisha, kisha akasita, “Gerlad unabaki nao hawa…..” alitokwa na kauli ile, macho yake yakiwa mekundu haswa. Nikaingiwa na wasiwasi, naweza vipi kubaki na watu wa hatari kama wale ikiwa siwezi hata kukabiliana nao pindi watakaponicharukia. Wakati nikiwa bado na hofu akazungusha koti lake na kufanya jambo la kustaajabisha. Akachomoa pingu na kuwafunga wawili wale. Nikabaki mdomo wazi, nilitamani kuuliza maswali mengi sana lakini ‘Getu’s principles’ zilikuwa zinanibana. “Usiwe mtu wa kuulizauliza tu hata kwa maswali ambayo unaweza kukisia jawabu lake”….. Naam kanuni hiyo ilikuwa inanibana! “Wakitikisika pasua pasua bila uoga…namfuata Maria… nilijua tu ipo siku yake Malaya huyu… alijifanya mjanja sana.. yaani miaka yote hii namfuatilia mtu mmoja atanikoima aisee” aliapiza huku akijiweka vyema Nikaikumbuka kauli yake aliyosema kuwa Maria si mtu mzuri siku namweleza kuwa mumewe ameniagiza kwake!! Getruda akatoweka akiniacha na bumbuwazi zito. Kumbe ni afisa fulani wa jeshi la polisi!!!! Nikajichagulia hilo liwe jibu langu, sikuwa na uhakika. Amakweli usilolijua!! Saa zima lilipita wawili wale wakinisihi niwaachie watoweke huku mmoja akinikanya kuwa kuendelea kwangu kuwadhibiti nitakuwa najitia matatani zaidi. Sikuvisikiliza vitisho vyao maana nilijua ni watu wabaya tu wanajaribu kunilaghai. “Gerlad, wewe ni kijana mdogo sana. Tuache sisi tuondoke ama la tufungie kwa nje ubaki na uhai wako dogo, fanya hivyo kisha tuachie hili jambo sisi…” alizidi kunisihi lakini kelele zake zikasababisha nimkanyage teke tumboni akabaki kuugulia. “Gerlad mimi si mpumbavu dogo… hatujapenda hata kidogo kuwa hivi, nakusihi toweka humu… tayari tuna pingu wewe ondoka na ujiepushe na hili… hata mwenzako anajua ni hatari lakini hajui kama ni hatari kubwa kiasi hiki” alinionya. Sikumtilia maanani, nilimuamini Getu pekee. “Usije ukasema hatukukuonya!!!” Mwishowe wakanipa onyo la mwisho. Robo saa baada ya onyo hilo la mwisho mlango wa chumba kile ulivamiwa… mitutu ya bunduki ikanitazama, nikaanza kurejea nyuma. Wale walioninyooshea bunduki zao wakaanza kutawanyika mle chumbani na hatimaye akaingia mtu nisiyemtarajia kabisa. Tumbo likaangaza kuunguruma na kisha nikakata tamaa “Nadhani kifo tu nd’o haki yako bwana mdogo.” Sauti nzito ya Inspekta Mustapha baba yake mzazi na Hamisa ilikoroma na alikuwa amekunja ndita. Kabla ya kuendelea kuzungumza aliinama na kuzifungua pingu zilizowaunganisha wale majangili wawili. Lakini hakuzitupa badala yake akafanya jambo la kunishtukiza, akanichapa usoni na zile pingu!! Nikahisi kizunguzungu na kisha nikaanguka chini. Damu ikaanza kunivuja. “Safari hii nakuua Gerlad!!!” aliapiza, nikajiuliza ni kipi nimekosea huyu mzee lakini sikupata mwanga kabisa. Na hakunipa nafasi ya kuupata mwanga, akanikanyaga kifuani na kiatu chake kisha akawa kama anasigina. Kiza kikatanda sikujua kiliendelea nini tena. Niliposhtuka nilijikuta nikiwa nimefungwa, kichwa chini miguu juu!! Macho yangu yakatazama na damu zilizokuwa zimegandiana sakafuni, nilipojilamba midomo yangu nikatambua kuwa ni mimi niliyevuja zile damu. “Ni nini nimewakosea…” nilijaribu kuzungumza lakini nikaishia kutema damu na koo likiniuma sana. Sauti haikutoka. Kichwa kilikuwa kizito sana na miguu ilikuwa imeshika ganzi. Sijawahi kufa wala siwezi kuzijua dalili za kufa lakini hali niliyokuwanayo pale kilikuwa ni kifo tosha kabisa. Nilikuwa katika kupumua tu lakini kila kiungo katika mwili wangu kilikuwa kimekufa tayari. Baada ya dakika kadhaa tangu nijitambue kuwa nipo katika dakika za kufa nilisikia hatua kadhaa zikiingia mle ndani. “Dogo…” sauti ikaniita.. nikajitahidi kumtazama lakini zaidi ya kutambua kuwa anao mwili mkubwa sikuweza kujua jambo jingine kutoka kwake, sikuweza kuuona uso wake. Akanisogelea na kisha akainama, nikauona uso wake. “Dogo… wewe ni mpumbavu wa mwisho kabisa duniani. Tulikuonya ona sasa…” alinikemea yule bwana nikaitambua sura yake, nd’o kati ya wale wawili waliodhibitiwa na Getruda katika hekaheka zile za kule hotelini. Nilitamani kusema neno lakini sauti ilikwama…. “Na hapa hutoki jamaa anakuua..” alipigilia msumari katika kauli yake. Niliisikia vyema lakini ningefanya nini wakati pale nilipokuwa tu nilijihisi ni mfu tayari. Pumzi pekee nd’o ilinifanya niendelee kuwa hai. “Wewe ni kijana mdogo sana mbona umejiingiza katika mapambano na watu wazito hivi??” aliuliza huku wazi akionekana kusikitishwa sana. Nilitaka kujibu kitu lakini nikaishia kukohoa damu tu. Yule bwana akaifungua miguu yangu…. “Nakushusha unakula fasta fasta.. jamaa alidai ule chakula ukiwa umefungwa hivihivi….so nikishusha fasta unakula nakurudisha sawa?” aliuliza huku akinifungua upesi upesi. Akanisaidia kukaa, na hapo damu ikaanza kusambaa tena katika pande nyingine za mwili, akanifuta mdomo kisha akanipatia chakula. Ulikuwa ni ugali na maharage. Nilijaribu kula lakini haukupita kooni, nikajaribu tena ikashindikana. “Niache nife…niache nife nikamfuate mama yangu huko alipo…” sauti ilinitoka kwa tabu. “Wewe ni mwanaume, usiwaze kuhusu kufa. Waza kuhusu kupambana na kutoka katika mikono hii mibaya, sikia sisi tumeajiriwa tu, tunafanya anavyosema yeye. Sasa mdogo wangu wewe na hali hii ukaenda kutembea na mtoto wake yule…huoni ama hukuiona hatari kwa wakati ule!!” aliniuliza kwa masikitiko makubwa. “Hawa ni washirikina na huyo uliyetembea naye ndo shina lenyewe, yaani kulikata lile kama ulivyotaka wewe ni kukomesha mafanikio ya mzee …..ulikosea sana.” “Hamisa ni mchawi ama una maana gani??” “Ni mtoto anayetegemewa kurithi kila kitu….ni mtoto wa kichawi yule…” alinijibu. Nikabaki kupigwa na butwaa nisijue ni kitu gani kipo katika maisha yangu, kwanini kila baya liwe linaniangukia mimi… “Ulifuatilia kwa ukaribu sakata la jamaa kupandishwa cheo hiki alichonacho sasa…… hivi unadhani angeweza kukipata hivihivi?” Yule bwana alinihoji…… na hapo nikavuta kumbukumbu na kupata mwanga juu ya jina la Inspekta Mustapha, utata katika hatua zake za kupandishwa cheo. Yule bwana akanirudisha katika ule mtindo wa kichwa chini miguu juu tena…. Kwa kumtazama hakuwa akipendezwa na jambo lile alifanya tu kwa sababu anatakiwa kufanya. Juma zima lilikuwa la mateso tu, yule bwana alikuwa anageuza sura yake na kunisulubisha haswa akiwa pamoja na yule inspekta na akirejea peke yake alikuwa akifanya kazi ya ziada kunitibu majeraha na kunipatia chakula. “Gerlad unatakiwa kwa namna yoyote utoke humu ndani, vinginevyo huyu bwana atakuua…. Anachotaka nadhani haukijui naye anatambua fika kuwa haukijui sema hashauriki hata kidogo amekusudia kukuua kwa mateso makali…” “Sina haja ya kutoka acha aniue tu, Mungu atanilipia, kama nilifanya makosa yoyote yale juu yake….” Nilimjibu huku nikiendelea kujihesabia siku zangu za mwisho katika maisha yangu.
Yule bwana aliyekuwa ananihudumia alikuwa amenieleza fika kuwa siku yangu ya kumi ndani ya jumba lile nisilolifahamu ilikuwa siku ambayo inspekta alipanga kuniua na kisha kunitoa kafara kiungo kimoja baada ya kingine. Bila kunificha yule bwana alinieleza kuwa yule bwana hashauriki na iwe isiwe lazima tu ataniua. Niliipokea kauli yake kwa uchungu mkubwa mno. Hatimaye ile siku ikafika!! Nilikuwa nimeinama vilevile kichwa chini miguu juu…… Inspekta akaingia akiongozana na yule bwana pamoja na wengine wawili. Kama kawaida sura yake ilikuwa katika hasira. “Nilikwambia nitakuua…..” ikasikika sauti, nikaitambua palepale kuwa yule alikuwa ni mama yake Hamisa. Nikageuza kichwa na kumtazama, sikuweza kumuona vizuri. “Mshushe!” aliamuru, na yule bwana akanisogelea. “Jitetee kadri uwezavyo ili upoteze muda..sawa” alininong’oneza kwa makini sana bila kusikika halafu ili kuonesha kuwa alikuwa na jazba alianza kutokwa na matusi mazito ya nguoni kuja kwangu. Hakika alizichanga karata ipasavyo!! Kweli yule mama alianza kuniuliza maswali kadhaa yasiyokuwa na msingi wa kusamehe bali kuhalalisha kile walichotaka kunihukumu nacho. Nilijitahidi kumbembeleza yule mama na kumsihi kuwa sitaendeleza mahusiano na Hamisa tena. Lakini hakuonyesha kuridhika na utetezi wangu, badala yake alikuwa akinicheka kifedhuli. Baadaye aliagiza kitu ambacho sikukielewa. Mara akaletewa visu vikali vinne. Mwili wangu ukasisimka haswa nilipotambua kuwa alipanga kunifyeka hadi nife. “Nisamehe mama yangu….” Nilimsihi lakini sauti haikutoka nikawa nimejisemea mimi mwenyewe. “Sikio, Pua, Vidole …..nitakukata mwenyewe na utashuhudia hapa.” “Kisha nakutia katika mafuta na kukuteketeza kabisa….” alimalizia huku akinyoosha kidole kuelekea katika pipa ambalo liliingizwa humo ndani na vijana wake. Nikakata tamaa na kujisemea kwa Mungu wangu kama ilikuwa sahihi haya kunitokea basi na anipe nguvu ya kuyakabili maana kiuhakika mwili wangu nulikuwa dhaifu sana. Hatua moja baada ya nyingine yule mwanamke asiyekuwa na huruma alianza kunisogelea. Nilimtazama kwa macho ya huruma lakini sidhani kama alijua tofauti ya macho yenye huruma na mengine ya kawaida. “Gerlad Masembo!!” akaniita, nikamtazama akatabasamu. “Papasa sikio lako uagane nalo… ipo hivi!! Nitakata moja baada ya jingine, tumia wakati huu kuliaga sikio la kushoto…” alizungumza maneno yale kama kwamba ni ya kawaida kabisa kama simulizi. Akakinyanyua kisu chake akalishika sikio langu. Nikaanza kulia kama mtoto mdogo. Ghafla purukushani zikachukua nafasi!! Mlio ukasikika, akasita kunifyeka badala yake akatazama ni wapi mlio ulipotokea. Hakuchukua sekunde kadhaa akarushwa mita kadhaa kutoka pale alipokuwa huku akipiga mayowe. Inspekta akajipekua upesi kisha akaghafirika, bila shaka ni baada ya kugundua kuwa hakuwa na silaha yoyote. Palepale naye akarushwa mbali huku akitokwa na ukelele wa maumivu!! “Nitaanza na masikio yenu kwanza kabla ya kuwapeleka mbele ya sheria…” ilikuwa sauti ya Getruda. Alikuwa amesimama imara huku akiwa na bunduki mkononi. “Inspekta….njia ya mwongo ni fupi sana. Muuaji mkubwa wewe.” “Shenzi taipu umefuata nini huku..” aliwaka inspekta.. “Nipo kazini, nimekuja kukukamata wewe muuaji….” Alijibu huku macho yake yakiwa makini kumtazama yule inspekta aliyekuwa akiugulia pale chini. Ghafla yule inspekta alijirusha na kuniangukia huku akiikaba shingo yangu. Macho yangu yakamshuhudia Getruda akiwa amepagawishwa na tendo lile la ghafla. “Usipoishusha bunduki yako chini navunja shingo ya huyu kimburu….” Alionya. Getruda akagwaya, hakupiga hatua mbele na wala hakuishusha ile bunduki chini. “Hautathubutu inspekta…” alionya tena. Inspekta akaikaba zaidi shingo yangu. “Kanuni namba nne…..kanuni namba nne itakubana…haitakuokoa na inaweza kukuokoa..’ niliyasikia maneno yale kutoka kwa Getruda nikatambua labda anamtishia Inspekta lakini inspekta naye akaonyesha kutotambua. “Unasema nini wewe na kanuni namba nne ya jeshi lipi??” “Kanuni namba nne G…..kanuni namba nne unajifanya huijui ee!” alizidi kumkomalia. Akili yangu ikanasa kitu na kuifungua kanuni namba nne ya Getruda. “Uhai ni mali yako, ni heri kuupoteza ukiupigania kuliko kuupoteza bila jitihada zozote” Palepale nikafanya uthubutu wa mwisho, nikarusha mguu wangu kwa nguvu nikamkanyaga Inspekta korodani, akapiga kelele na kujirusha kando kidogo. Bunduki ya Getruda ikacheua risasi na kuusambaratisha mkono wa inspekta ambaye aliishia kutoa kelele kubwa sana. Mkewe akataka kusimama lakini risasi ikapenya jirani naye akatulia kimya. Baada ya hapo Getruda akawafunga kamba mtu na mkewe, nikashangaa kwanini hakujihusisha na yule bwana aliyekuwa akinitesa. Lakini punde alinieleza kuwa yule bwana ndiye aliyemuwezesha kuingia mle ndani baada ya kumuingiza kwa njia ya pipa wao wakiamini kuwa ni mafuta. Ndani ya nafsi yangu nikamshukuru yule bwana mtesaji, hakika alichofanya kilikuwa na maana kubwa sana. Na hapo nikatambua ni kwa sababu gani alikuwa akinisihi nimpotezee muda mzee Mustapha ili asiniue mapema. Kumbe alijua!! “Mtakufa na tabia zenu mbaya…mlishindwa kuniua nikawaahidi nitawaua” Getruda aliwaambia bibi na bwana na kisha akafyatua risasi!! Ni huyo mtesaji ambaye alituongoza hadi kutoka nje ya ile ngome, Getruda alinipa muhimili katika bega lake. Hadi tukafika nje tukiwaacha mtu na mkewe wakiwa wameungana pale chini. Getruda aliwakaza haswa na hawakutengana hata baada ya kupigwa risasi. *****
JANGA JIPYA!!!
MAHUSIANO ya ukaribu yakitiliwa sukari na hali ya kujali huzaa mapenzi. Na ilikuwa lazima iwe hivyo, hasahasa wawili mkifanana. Baada ya kifo cha Inspekta na mkewe na sintofahamu ya wapi anapatikana Hamisa. Hatimaye nilijikuta taratibu naingia katika kanuni na hatimaye mkumbo wa maisha ya Koplo Getruda ambaye sasa nilimtambua vyema kuwa alikuwa mfanyakazi wa serikalini kitengo cha usalama. Na kweli alinilinda vyema. Kwa sababu wanafunzi wa mwaka wa pili walikuwa wameanza masomo tayari nilitakiwa kusubiri mwaka mwingine nyumbani ili niweze kuanza upya masomo yangu pale chuoni. Getruda alinipangia chumba, tulikuwa huru mimi kumtembelea nyumbani kwake na yeye kunitembelea nyumbani kwangu. Hatua moja baada ya nyingine hatimaye kujikuta penzini. Baada ya kifo cha inspekta Mustapha hali yangu ilikuwa thabiti tena imara niliweza kuwa Gerlad yule wa zamani, japo sikucheza mpira tena lakini nilikuwa imara mno. Getruda alinitambulisha kwa wazazi wake, mimi sikuwa na pa kumtambulisha popote pale, zaidi ya marafiki wachache sana niliokuwanao karibu. Miezi mitano baada ya mkasa wa ‘katikati ya kifo na uhai’ nikatokewa na jambo jingine la ajabu zaidi. Ulikuwa ugeni wa rafiki mpya nyumbani kwangu, alidai kuwa alikuwa ananifahamu vizuri na aliwahi kuniona. Mimi nilimkatalia waziwazi kuwa sura ile sikuwa naifahamu. Alitabasamu na mwisho akaniuliza iwapo namkumbuka msichana aitwaye Hamisa. Kulisikia jina lile nikasisimka upya. Na hapo nikatambua wazi kuwa yule binti alikuwa ameishika akili yangu vibaya mno. “Namfahamu…ama Hamisa yupi?” “Huyu huyu unayemfahamu wewe mtoto wa inspekta.” “Amefanya nini…” nilimuhoji kwa utulivu. “Ameniagiza kwako….” “Yupo wapi hadi akuagize kwangu, Hamisa alikufa naomba uache kunichanganya….” Badala ya kunijibu alibofya simu yake na kisha ilipopokelewa upande wa pili akasema, “Huyu hapa ongea naye….” Nikaipokea ile simu. “Mwanaume wa maisha yangu….” Ilikuwa sauti ya Hamisa. Msomaji amini kuwa kuna kuchanganyikiwa na kupagawa. Sauti ile ilinipagawisha sana. Nikajikuta sina cha kuongea zaidi ya kuita Hamisa Hamisa. “Nahitaji kuonana na wewe, mwanaume wa maisha yangu!!” alitoa kauli ile kimahaba na kuyashika masikio na akili yangu ipasavyo. Yule bwana nilimuomba namba ya simu ya Hamisa lakini hakuwa tayari hata kidogo badala yake alinieleza kuwa natakiwa kuonana na Hamisa yeye mwenyewe. Nilisahau maonyo yote niliyopewa juu ya hatari aliyonayo Hamisa, nikayakumbuka mapenzi yake tu ya dhati. Nikamtumia ujumbe Getruda kuwa natoka kidogo kwenda kwenye mizunguko yangu hivyo sitakuwepo nyumbani. Kwa mara ya kwanza nikamdanganya Getruda wangu, uongo niliohisi hauna madhara yoyote yale lakini ulikuwa uongo mkubwa mno. Tulipanda taksi ambayo ilitufikisha maeneo ya Magomeni Mikumi, yule mwenyeji akaelekeza zaidi. Teksi ikasimama mbele ya nyumba moja ya hali ya kawaida tu. Tukatelemka na kuingia ndani. Ama! Kweli alikuwa ni Hamisa, yuleyule Hamisa niliyekuwa namfahamu. Yule bwana akatoka nje na kutuachia chumba!!! Hamisa hakuwa amebadilika sana, japo kilikuwa ni kipindi kirefu kimepita lakini alikuwa na urembo wake vilevile. “Ni kitu gani kilikutokea Hamisa wangu!!” nilimuuliza lakini badala ya kunijibu aliendelea kunikumbatia huku akilia tu. Sikutaka aendelee kulia badala yake nilianza kumbembeleza tu hadi akawa sawa tena. Lakini hakutaka kutoa maelezo yoyote yale juu ya nini kilimtokea baada ya kuachana na mimi mjini Morogoro. Au wamemtoa kumbukumbu hawa!! Nilijiuliza huku nikimlaani baba yake na mama yake. “Nilikukumbuka sana G wangu….” Alininong’oneza kimahaba, na hapo nikaikumbuka siku ya mwisho ambayo nililala naye kitanda kimoja huku nikishindwa kufanya naye mapenzi kutokana na hali niliyojikuta nikiwa nayo tayari. Hali ile ikanifanya nimvamie Hamisa kwa nguvu na mwisho tukajikuta tumeingia katika dhambi ya uzinzi. Tena pasipokutumia kinga. Usingizi mzito ukanipitia katika kifua cha Hamisa. Nikajitahidi kuitawala ile hali lakini sikuweza, nikajaribu kumtazama Hamisa usoni, ni hapo nilipoiona sura ya mama yake….. hakuwa Hamisa yule. Nikajaribu kujitoa lakini haikuwezekana, yule mwanamke alikuwa akinicheka kifedhuli. Nikarusha mikono huku na kule lakini ni kama nilikuwa natapatapa tu. Nilishtuka baadaye nikiwa maeneo ya jirani na kituo cha magari ya kwenda Mwenge. Sikujua nimekuwa pale kwa muda gani, lakini ajabu sikuwa nimeibiwa kitu chochote kile. Simu yangu ikaita nikaitoa mfukoni alikuwa ni Getruda aliyekuwa amenipigia. “Ukwapi mbona hupokei simu….” Lilikuwa swali la kwanza lililotawaliwa na wivu mkali ndani yake. “Nipo kituoni nawania magari ya kurejea nyumbani….” “Kituo kipi? Nipo na gari ya ofisini nikupitie…” “Hapa Magomeni hapa… Magomeni Mikumi..” “Mbona kama haujiamini mpenzi kuna nini kinakutokea…” “Hapana ngoja gari hili napanda tutaongea!!!” nikamzuga kisha nikapanda garini baada ya kuhakikisha kuwa nilikuwa na nauli mfukoni.
**** Nilimtambua vyema mchumba wangu Getruda kuwa akinuna amenuna kweli na ni shughuli pevu kumliwaza. Hivyo niliingia pale ndani tayari kukabiliana na ukweli. Hakika alikuwa amenuna haswa!! Niliogopa hata kumsalimia. “Nieleze ulikuwa wapi na unafanya nini…macho yako yamevimba na shati umegeuza…” hivi vyote aliviona sekunde kadhaa baada ya mimi kuingia ndani. “Aaargh! Shati… eeh! Kumbe nimegeuza…umesema na macho yamevimba…” nilijifaragua hovyo. Hadi nikajishtukia. Je, nimweleze juu ya simu niliyopigiwa na mtu akajitambulisha kama Hamisa?? Na kama ni hivyo basi itanilazimu pia kuelezea juu ya uzinzi niliofanya na binti huyo na kisha nikiwa katika dalili za mwisho nikatambua kuwa ni mama yake na Hamisa alikuwa ananichezea. Lakini mama yake Hamisa ni marehemu. “Ulikuwa wapi?” akaniuliza tena. “Magomeni kwa rafiki yangu…” “Rafiki wa Magomeni tangu lini? G unanidanganya? Unanidanganya G?” alilalamika na kauli yake hiyo ikawa ya mwisho akaanza kulia kwa uchungu. Nilijitahidi kumbembeleza lakini sikuwa tayari kuusema ukweli. Nilidhani kuuficha ule ukweli kungekuwa utatuzi wa tatizo. Sikujua kama nilikuwa najipalia mkaa. Baada ya msuguano wa muda mrefu, hatimaye Getruda alipoa nami nikaenda kuoga kisha nikaingia kitandani. Hakuna aliyehitaji kupata chakula. Usiku mnene, hisia kali za mapenzi zikanipanda… Getruda alikuwa amenipa mgongo akimaanisha hataki lolote usiku ule. Lakini zile hisia zilikuwa kali sana, nikajikuta nambembeleza Getruda hadi akakubali. Nikafanya naye tendo la ndoa!! Huu ukawa usiku wetu wa mwisho kabisa kufanya tendo hili. Asubuhi tukaamka salama kabisa!! Lakini Getruda alidai anahisi homa, nikajua ni kutokana na kulia kwa muda mrefu sana. Lakini haikuwa hivyo baada ya kwenda hospitali. Akapewa majibu kuwa alikuwa na kisonono kilichokomaa sana…. “Gerlad, sijawahi kukusaliti hata siku moja.,..yaani hata siku moja. Umeniambukiza magonjwa ya zinaa Gerlad. Nimekukosea nini lakini eeh!! Nilikukosea nini?” alilalamika huku machozi yakimtoka kwa wingi. Nilijitetea na kukataa kata kata kuwa sijawahi kufanya jambo kama hilo na sijawahi kuugua kisononono. Na kweli nilivyojaribu kupima sikuonekana na ugonjwa huo. Siku nne baada ya sote kukubaliana na ile hali Getruda akiwa anafua nguo zangu, nami nikiwa ndani natazama runinga mara aliingia kwa fujo mle ndani. “G.. ni msichana gani aliyekuandikia ujumbe huu. Na ninakumbuka siku ile ulivaa hii nguo…..” “Ujumbe gani tena? Nilihoji huku nikikaa vyema Akanirushia kile kikaratasi. Nikakitazama kwa makini huku nikiusoma ujumbe ule. Hofu ikanitawala. “MLANGO MPYA WA MATESO G KARIBU WEWE NA KOPLO WAKO” Ujumbe ulikuwa umeandikwa kwa kalamu nyekundu. Nikajikuta nimepiga magoti chini na kumweleza Getruda kila kitu juu ya haya yanayotokea na yote yaliyotokea. Kuanzia siku napigiwa simu hadi saa ambayo nilirejea nyumbani nikiwa nimegeuza shati. Kilichomliza Getruda ni kimoja tu na aliendelea kulalamika mara kwa mara kuwa nimemdanganya sana juu ya hilo wakati sote tuliyashuhudia madhara yake. Nilikuwa sina la kujitetea na badala yake nikabaki kumsihi tu anisamehe. Tunaishi vipi baada ya jambo hili!! Hili nd’o swali tulilojiuliza. Lawama zote nilizipokea bila kikomo. Siku nne mbele zaidi janga likahamia kwangu. Miguu ikaanza kuwasha, iliwasha sana japo niliweza kutembea ilikuwa inawasha mno. Nilimshirikisha Getruda juu ya hili. Akatoa ushauri kuwa twende kwa mganga wa kienyeji. Nilijaribu kulipinga hili lakini siku iliyofuata hali ilikuwa mbaya sana. Nikakubaliana na wazo lile. Mganga hakuwa na msaada wowote, hospitali haukuonekana ugonjwa wowote. Hatimaye miguu ikaanza kuvimba kwa fujo. Ilivimba kiasi kwamba sikuweza kutembea tena…… Getruda aliendelea kuuguza kisononono chake kisichopona. Mama mzazi wa Getruda alifanya kila awezalo kutusaidia lakini mwisho wa siku upande wa pili walikuwa washindi. Ukafikia wakati wa kumlea mjukuu anayetokana na majuto. Wakati wa kuzishuhudia mbigu zikiwa chini na ardhi ikiwa juu. Wakati wa kukamilisha historia mbaya kabisa yenye machungu ya maisha yangu. Alianza Getruda, kisonono kikawa tatizo, hali ikazidi kuwa tete. Akapoteza fahamu kisha bila kupata muda wa kusema kwaheri akaaga dunia!! Nilibaki kuwa shuhuda wakati miguu yangu yote miwili ikiondolewa kutokana na kuoza. Nikakumbuka kuwa haya yote yawezekana ni kwasababu moja tu. Sikufuata maneno ya watu wema walionitangulia. Joshua, mama yangu na kubwa zaidi dokta Sadath aliyenifia na kunisihi nimlee mtoto wake jambo ambalo sikulitelekeza hata kidogo baada ya kurejea uraiani. Niliyoyapitia ndani ya miaka miwili ilikukuwa shahada tosha ya adhabu. Hadi Napata fursa ya kuyasimulia haya sina uhakika kama nitakuwa hai tena wakati wewe ukiyasoma haya. Lakini ukipata fursa ya kuyasoma na kuyasikiliza. Tafadhali usinililie mimi kwa haya yaliyonisibu bali kawasimulie wanao wapate funzo katika maisha yao!!!! JIFUNZE!! __________ Mkabidhi Mungu maisha yako….. katika uwepo wake yeye hakuna linaloshindikana!!
0 Comments