Simulizi : Usinililie Mimi Kawasimulie Wanao Sehemu Ya Tatu (3)
Hatimaye nilipatwa na usingizi nikiwa nawaza na kuwazua kulikoni!! Na nitaishi vipi katika hali ile na Hamisa. Je, atanielewa? Nd’o swali nililojiuliza pasi na majibu ya moja kwa moja!! Majira ya saa kumi na moja nilikuwa nimegutuka kutoka usingizini na Hamisa alikuwa kifuani kwangu akiwa amesinzia. Nilimtazama binti yule na kumfananisha binti fulani niliyewahi kumwona katika filamu za kifilipino tofauti yao ilikuwa moja tu!! Yule alikuwa anaigiza na huyu alikuwa katika maisha halisi. Licha ya kugutuka alfajiri nilisinzia tena na niliposhtuka tena Hamisa alikuwa amefanya karibia kila kazi ambayo alistahili kuifanya mle ndani, alifua nguo zangu na nilipoamka alinipa habari njema kabisa. Ratiba ile iliendelea hata siku tatu mbele ambapo Hamisa alikuja na wazo. Alinieleza kuwa anatoka kwa ajili ya kwenda kunitafutia kiti cha kutembelea wagonjwa wasiojiweza katika kutembea, alipotaja kiti kile nikamkumbuka kaka yangu Japhet ambaye alimkaba mama na kukiiba kiti changu cha kutembelea, ni siku kadhaa nilikuwa sijamuona nyumbani. Mama alimuelekeza Hamisa kituo cha magari kilipo, na maelekezo ya ziada akampatia. Hamisa akanibusu shavuni kisha akatoweka huku akizidi kunitia moyo kuwa ipo siku nitakuwa na furaha tena!! “Gerlad.. nife leo nife kesho nisije nikasikia kuwa kwa namna yoyote ile uliachana na huyu binti… anakupenda sana…. Yaani sana… na hakupewndi wewe tu, huyu ana upendo wa kuzaliwa!!” kauli hii ya mama ilinisisimua sana. Nikajipapasa shavuni na kulikumbuka tena busu alilonipatia Hamisa. Nikayasahau yaliyotokea usiku aliponikumbatia, nikajipa tumaini jipya kuwa iwapo ananipenda atakubaliana nami katika kila hali. Akirejea nitamueleza kila kitu juu ya hali niliyonayo!! Nilijiapiza….. kisha nikatamani Hamisa arejee niweze kusema naye. Maneno ya mama yakanifanya nijihisi nimelivua taji la miiba!! Lakini lile busu lilikuwa ni ishara ya kuniaga bila yeye wala mimi kujua. Hamisa hakurejea!! Hadi majira ya saa mbili tukiwa na ndoto kuwa atarejea haikuwa hivyo, mama akanibeba na kuniingiza ndani. Chakula alichokuwa amekiandaa hakuna aliyekuwa tayari kula pasipo na uwepo wa wa Hamisa. Mama alijaribu kunibembeleza ilipofika saa nne usiku kuwa nilale lakini haikuwezekana, niliyafumba macho lakini yakanisaliti na kufumbuka tena. Bila shaka yalihitaji kumuona Hamisa kisha yangejifumba na kisha ningesinzia nikiwa na amani. Muungurumo wa gari majira ya saa tano na nusu kwa mujibu wa saa yangu ulinishtua, nikajaribu kumuita mama yangu lakini hakujibu! Bila shaka alikuwa amelala tayari. “Hodi!!...” sauti nzito ya kiume iliunguruma. Ilirudia hivyo mara kadhaa hadi mama aliposikika akijongea mlangoni na kwenda kufungua mlango. Awali mazungumzo yao sikuweza kuyanasa lakini mwanaume yule aliongea kwa jazba sana na mama alikuwa akirudia kauli ambayo sikuweza kuiskia. “Hakuna Gerlad nyumba hii jamani mimi ni mjane na ninaishi peke yangu!!” hatimaye mama alipaza sauti nikaisikia. Palepale nikajiuliza ni kitu gani kinajiri hadi mama anatoa jibu lile kwa hasira vile tena kwa kusisitiza. Watu wabaya!! Niliwaza huku hofu nayo ikianza kunitwaa. “Nitahesabu hadi nne tu na ikifika tano haujatoa jibu la ukweli nitakachokifanya mama…. Nasema nitakachokifanya utajuta!!” sauti ya kiume ilikaripia. “Nimesema naishi peke yangu..” mama alisema huku dhahiri akiwa amekata tamaa. Na hapo nikaisikia ile sauti nzito ikianza kuhesabu, upesi nikatambua kuwa mambo si mambo. Nikajinyoosha na kuitoa neti iliyokuwa kitandani na kisha nikabiringita upande uliokuwa jirani na ukuta. Nilitarajia kuwa nitadondokea chini na kutulia huko lakini haikuwa hivyo, kitanda kilikuwa karibu sana na ukuta hivypo ilikuwa kazi bure sikuweza kudondoka. “Tano!!!...” nilimsikia akimalizia kwa sauti kauli na kisha likasikika yowee fupi kutoka kwa mama. Nikabaki nimekodoa macho yangu, hadi pale mwanga mkali wa tochi uliponimulika machoni. “Mshenzi nd’o huyu (akanitukania mama yangu na matusi mengine mazito ya nguoni)” Nikabaki kushangaa vilevile nisiweze kumuona mtu aliyekuwa akinimulika na ile tochi. “Japhet we Japhet…ujue mimi ni mdogo wako wa damu Japhet” nilijaribu kubashiri nikiamini aliyevamia kwa mara nyingine tena alikuwa ni Japhet. Lakini haikuwa hivyo!! Ghafla nikanaswa kibao kikali sana katika shavu langu na kutukanwa matusi mengine, kisha wakanikamata walikuwa wawili, wakanibeba mzegamzega, maumivu niliyoyapata katika mgongo wangu natamani wangeyapata wao walau kwa sekunde tano tu na kamwe wasingeweza kunibeba katika mtindo ule. Nililia sana!! Nilimshudia mama yangu akiwa amelala chini akionekana wazi kutokwa na fahamu!! Wakanirusha katika gari walilokuja nalo na kisha kwa mwendo mkali tukatokomea!! Hadi wakati huo hawakunieleza lolote juu ya sababu za wao kunichukua mimi. Mpenzi msomaji sikujua kama nitaipata fursa hii ya kusimulia mkasa huu ili walau ujifunze mawili matatu kutoka katika maisha yangu, niliamini kabisa kuwa ule ulikuwa usiku wa mwisho katika maisha yangu ya mateso. Na kwa namna moja ama nyingine niliombea iwe hivyo. Naam! Nife tu nipumzike, ndivyo nilijisemea. Nilipojaribu kuwahoji maswali kadha wa kadha watu wale, mmoja wao alinigonga kisogoni mara likawa giza nene. Bila shaka nilipoteza fahamu maana nilikuja kufumbua macho na kujikuta sehemu nisiyoifahamu kabisa. “Ameamka bosi!!” sauti ilisema baada ya kuwa nimefumbua macho. Nikasivisikia vishindo vya huyo mtu wa kuitwa bosi vikitokea mbali, na vilizidi kukaribia zaidi. Hatimaye ana kwa ana na bosi wao. Sura haikuwa ngeni hata kidogo machoni mwangu, niliwahi kukutana nayo tena. Mkononi alikuwa ameshikilia mkanda mnene na kiunoni ilichungulia bastola. Uso wake ukitangaza chuki ya waziwazi. Alikuwa ni baba yake mzazi na Hamisa. Inspekta!!! Nilichoka na kukata tamaa kabisa. Lile taji nililohisi nimelivua nikawa nimelivaa tena!! Yule mzee asiyekuwa na huruma aliyeuondoa uhai wa Joshua akanirukia na kunikanyaga kifua. Nilipumua kwa shida kisha nikaanza kutema damu!! Hakika nilikuwa nimepatikana. Hakuniacha aliendelea kunigandamiza pale chini kwa kutumia kile kiatu chake kigumu na kizito, nilianza kukosa pumzi zaidi na kurusha mikono huku na kule. Nakufa!! Neno hilo lilipita na kukaa kichwani mwangu. “Ni….sa…..nisame….he…” nilimwomba kwa shidashida na sijui kama sauti ile aliisikia. Badala yake alizidi kuikunja sura yake kwa hasira. Nilijiuliza ni kwanini sifi wakati nilikuwa nimeteseka sana, lakini jibu nililojipatia katika kichwa changu ni kwamba labda sikufa ili leo hii kizazi chako wewe kijifunze mengi kupitia mimi, na labda sikufa ili niushuhudie muujiza na nishirikiane nawe kuamini kuwa Mungu yupo. Wakati Inspekta Mustapha, baba yake mzazi na Hamisa akiuondoa mguu wake katika kifua changu aliingia mama mbaya kupita wote niliowahi kukutana nao duniani. Mama yake Hamisa! Huyu alinigeuza gunia la mazoezi, alinipiga kila kona ya mwili wangu bila kunipa japo nafasi ya kunisikiliza. Nililegea kila kiungo na kuyazoea maumivu hatimaye. “Hautakufa lakini utajuta!!” alinitamkia wakati akiniacha nikiwa sina hali sakafuni. Nilijiuliza maswali mengi sana juu ya wazazi hawa….. ni kosa gani kubwa nililowafanyia hadi wanitende hivi!! Sikupata jibu kwa siku ile…. Nikaachwa bila msaada wowote….nikaifanya sala yangu ya mwisho kabisa. Niliamini kuwa nitakufa usiku ule!!
JIFUNZE! HAKUNA majaribu yanayodumu milele, adui yako anayekujaribu utafikia wakati wake wa kujaribiwa na huu utakuwa wakati muafaka way eye kulia na kusaga meno huku akitamani wakati urudi nyuma asikutende alivyofanya, lakini wakati kamwe haurudi nyuma. Tenda wema sasa ulipwe wema baadaye!!
KUFA sio jambo jepesi hasahasa ukikusudia lakini usipokusudia huja kama ajali tu na kukuzimisha moja kwa moja. Nilitamani usiku ule wa giza nikifumba macho nisifumbue tena lakini ajabu ni kwamba alfajiri niliyafumbua macho na kujikuta katika chumba kilekile nisichokifahamu, nilinyanyua uso na kutazama kona kadha wa kadha lakini sikupata walau mwangaza juu ya sehemu niliyokuwa. “Gerlad Masembo…. “ sauti kutoka nyuma yangu iliita, nilitamani kugeuka, akili ilikubali lakini mwili ukagoma, mgongo ulikuwa unauma sana na pia lilikuwepo jambo jipya kabisa. mguu wangu wa kulia ulikuwa na maumivu makali sana. Kuyatambua maumivu yale ya mguu nikakumbuka kuwa katika mojawapo ya kuta pale ndani kuna picha niliiona. Picha ya mchezaji wa soka!! Nikaukumbuka mguu ule wa dhahabu ambao uliwapa furaha mashabiki wa soka enzi hizo nikiwa katika ubora wangu. Sasa ulikuwa unauma sana. Huenda mzee Mustapha ama mkewe waliukanyaga!! “Sina kiburi mimi… unanionea kuniambia maneno hayo…” nilijitahidi sauti ikatoka kumjibu mtu aliyekuwa akizungumza nami. “Hivi na afya yako hii ya kufa leo ama kesho kwanini ujiingize katika hatari mbaya kama hii… unamfahamu Hamisa wewe…. Unamfahamu vizuri??” sauti ya kiume ilizidi kuunguruma nikiitambua kuwa ni ya inspekta Mustapha. Sikujibu kitu akaendelea kuzungumza….. “Gerlad jiweke mbali kabisa na huyu binti. Jiweke mbali na Hamisa, maana humjui kabisa hata chimbuko lako, atakugharimu sana kijana. Ninao uwezo wa kukuua hata sekunde hii lakini moyo wangu umenisihi kuwa bado unaweza kubadilika na kujiweka mbali kabisa na Hamisa….. hili litakuwa onyo la pili baada ya lile onyo la kule hospitali…. Usipuuzie nakusihi vinginevyo sitakuwa na huruma nawe tena.” Alimaliza kuzungumza na hapo sauti ya kike ikaendelea kuzungumza. “Hautatoka humu mapema Gerlad, hautatoka mpaka tuhakikishe umebadilika…. Unajua kuna kitu hukifahamu Gerlad…. Hebu wewe mlete huku kwanza…” sauti ile iliamrisha… mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi, niliamini yule mwanamama alihitaji kunipa onyo jingine la vitendo. Mwili ulioanza kupoa kutoka katika maumivu ukasisimka na kujiandaa tena kwa ajili ya kuumia. Wanaume wawili walininyanyua vyema na kunipeleka katika chumba kikubwa wakanifikisha katika kiti. Baada ya dakika kama kumi hivi ndani ya kile chumba akaingia mama Hamisa, alikuwa amevaa nadhifu haswa unadhifu ulioficha ukatili wake. Alinitazama vyema huku akitikisa kichwa kama anayenisikitikia, hakusema neno lolote badala yake alibofya simu yake ya mkononi, kisha akasikiliza kwa muda. “Njoo upesi…” alizungumza na kisha akakata simu. Punde ndani ya kile chumba akaingia mwanaume aliyevalia nguo nyeupe. Mama Hamisa akazungumza kwa lugha isiyokuwa kiingereza wala Kiswahili, sikuambulia kitu lakini yule mwanaume alionekana kumwelewa vyema. Baada ya mazungumzo yao akatoka nje akimwacha yule mwanaume pale ndani. Bila kunisemesha lolote alikisukuma kile kiti hadi katika chumba kingine. “Naitwa dokta Finias….” Alijitambulisha tukiwa tumekifikia chumba kilichofanana na hospitali. Wauguzi wawili wa kike na kiume wakasaidiana na daktari, wakaniweka kitandani, daktari akaanza kwa kunisafisha majeraha yangu kwa umakini wa hali ya juu huku kila mara nilipolalamika kuumia akinipa pole. Baada ya siku nne za huduma ile hatimaye niliwekwa kitako na wazazi wa Hamisa katika jumba lile ambalo hadi leo ninavyosimulia mkasa huu sitambui lilikuwa nchi gani mkoa gani. “Tunakuacha huru na kukurudisha nyumbani kwenu… lakini umejifungulia mlango wa mateso makali. Uwezo wetu wa kukusaidia uliishia siku ile hospitali tulivyokupa onyo nawe ukapuuzia. Sasa hatuna namna…” inspekta alizungumza kwa unyonge na mkewe akatikisa kichwa kuunga mkono alichokuwa anakisema mumewe. Walizungumza mengi lakini akili yangu ilinasa mstari mmoja muhimu sana. “Umejifungulia mlango wa mateso” Mateso gani zaidi sasa!! Mbona nilikuwa nimeteseka na bado nilikuwa katika mateso makali. **** Usiku niliondolewa katika lile jumba katika namna ya ajabu, nilichomwa sindano na yule daktari. Macho yakawa mazito nikajaribu kupambana na ile hali huku nikijua fika kuwa nimedungwa sindano ya usingizi. Lakini hatimaye kiza kikatanda na ule ukawa mwisho wa kujua ni kitu gani kiliendelea. Maumivu ya mguu wangu wa kuume yalinifanya nijaribu kujipaposa, nikajikuta nikigusa kitu kigumu. “Mbona umenichoma sindano sasa!!” niliuliza ilihali nikiwa sijafumbua macho yangu…. Nilitegemea kupata jibu lolote lakini haikuwa hivyo, nikawasikia ndege wa ajabu ajabu wakipiga kelele. Bundi!! Akili yangu ikafanya kazi!! Nikafumbua macho yangu na kujikuta katika giza nene lililopewa nafuu na mwanga wa mwezi uliochomoza. Niliangaza huku na kule nikatambua kuwa nilikuwa peke yangu!! Ndugu msomaji, ama wewe unayenisikiliza. Umewahi kushuhudia muujiza?? Ama unayajua mauzauza? Kama haya huyajui, vipi kuhusu mazingaombwe? Vitu hivi ni kama havina tofauti vile, kwa kuvitazama lakini kwa kusimulia hapa kilichotokea itakuwa juu yako kutambua maajabu haya!! Nakusimulia kwa sababu tu yalinitokea na ninakosa neno la kukuaminisha haya!!! Uoga ukatanda, mguu nao ukizidi kuuma. Gizani peke yangu!!! Nikajivutavuta hatimaye nikaketi, nikapekecha macho yangu ili kupambana na lile giza. Bundi akalia tena…. Nilikuwa porini.. pori nisilolijua!! Nikakumbwa na kitendo kisichotarajiwa!! Nguvu za ajabu zilizochangiwa na uoga!! Nikasimama wima! Nikapiga hatua moja mbele… Kwa mara ya kwanza baada ya mwaka mzima nikapiga hatua peke yangu, sikujua ni wapi nilikuwa naelekea lakini nilizidi kupiga hatua!! Hatimaye nikaanza kupata taswira juu ya wapi nilikuwa!! Nilikuwa katika kipori kidogo jirani na nyumbani kwetu! Nikaitambua na njia ya kuelekea nyumbani, nikaongeza mwendo huku mapigo ya moyo yakiwa juu kwa hofu, nikaikaribia nyumba. Yule bundi akizidi kunipigia kelele, sikujali japo nilikuwa naogopa! “Mamaaaa!!!” niliiita kwa sauti ya juu kabisa baada ya kuiona nyumba yetu. Niliona mishumaa ama ni mwanga wa kibatari!! Nikatambua kuwa mama alikuwa hajalala bado. Nikaita tena kwa sauti ya juu…. Mara mlango ukafunguliwa!! Mama akasimama mlangoni. “Asante Mungu kwa sababu umejionyesha kwangu katika uzee huu!!” mama alisema maneno yale kisha akapiga magoti na kuzitazama mbingu. Nilijisogeza hadi alipokuwa nikamkumbatia kwa nguvu. Na hapo ndipo nilipoona mabadiliko katika eneo mojawapo katika kiwanja cha nyumbani. “Mama… ni nini kile..” nilimuuliza. “Nilimuomba Mungu walau anipe faraja kidogo tu kabla sijafa, nilimuomba hayo siku mbili zilizopita nikiwa namzika kaka yako Japhet. Alilala na hakuamka tena baada ya kuwa ameniomba msamaha, baada ya kufanya jitihada za kukutafuta na wewe akuombe msamaha pasi na mafanikio. Nilimsamehe lakini hakuianza siku mpya tena.. alikufa kitandani kwake, jana tumemzika. Na hilo ndilo kaburi lake…. Ni furaha gani ningehitaji tena zaidi ya kukuona wewe mwanangu!!! Nilipiga goti kwa imani, maneno ya majirani kuwa nimemtoa kafara Japhet na wewe pia nimekutoa kafara hayakunidhuru sana maana niliamini fika kuwa yupo Mungu aijuaye kweli na asiyetushuhudia uongo!! Amekuleta tena kwangu. Ubarikiwe sana Gerlad!!” mama alizungumza kwa sauti ya chini kabisa huku akiwa bado amenikumbatia. Maumivu ya mguu wa kuume yaliendelea kunisumbua, nilijitahidi kujikaza. Nilipoingia kitandani usingizi uligoma kabisa, nililia sana, safari hii mgongo haukuwa tatizo bali mguu wa kuume. “Umejifungulia mlango wa mateso” nikaikumbuka kauli ya yule inspekta!! Nikajaribu kuifananisha na hali niliyokuwanayo kwa wakati ule. Sikuupata usingizi hadi asubuhi, sikuwa na haja ya kumweleza mama hali halisi. Aliiona yeye mwenyewe. “Tupo katika mapambano magumu sana na shetani!!” mama alinieleza huku akinikanda. Maumivu hayakupungua hatimaye mama akatafuta usafiri na kunipeleka hospitali ya wilaya ya Morogoro. Ndani ya gari nilijikaza lakini hali ilizidi kuwa mbaya na kunifanya nitokwe machozi. Mama kwa kutumia senti kadhaa za rambirambi alimlipa daktari akanifanyia utafiti wa kina kiasi. Mwishowe akaja na jibu ambalo linaifanya simulizi hii iendelee kupitia hali isiyokuwa na nafuu walau ya kutabasamu. “Mguu wako umeoza vibaya sana, unatakiwa kuwahishwa jijini Dar es salaam kwa ajili ya kukatwa maana ukichelewa hali hiyo italifikia paja jambo ambalo ni baya sana.” Mama alisema haya akiwa amesimama mbele yangu, machozi yakimlengalenga!! Nilifumba macho kisha nikayafumbua, nikamkuta mama amenifikia tayari na kunikumbatia!! “Nililie mimi mwanangu kisha unisamehe kwa kukuzaa katika ulimwengu huu uliojaa imani potofu kupindukia, usijilaumu kamwe kwa kukutana na Hamisa…. Jilaumu kwa sababu ya wazazi wake!!!” mama alinieleza akiwa bado amenikumbatia. Kumtaja Hamisa kukanifanya nijikute nina maswali mengi ya kuuliza ambayo nilihisi mama anaweza kuyajibu lakini alinizuia kwa kusema kuwa pale si mahali muafaka. JIFUNZE: BAADHI ya wanadamu wanajaribu kujilinganisha na Mungu kwa nguvu zao za kichawi, wanatumia nguvu hizo kubabaisha na kunyanyasa wanadamu wengine…. Wanasahau kuwa Mungu wetu ni Mungu wa wachawi, Mungu wa majambazi, Mungu wa watu wema na Mungu wa watu wabaya… Ole wao siku hasira ya bwana ikawaka juu yao!! WATALIA NA KUSAGA MENO!!
Sikuupata usingizi hadi asubuhi, sikuwa na haja ya kumweleza mama hali halisi. Aliiona yeye mwenyewe. “Tupo katika mapambano magumu sana na shetani!!” mama alinieleza huku akinikanda. Maumivu hayakupungua hatimaye mama akatafuta usafiri na kunipeleka hospitali ya wilaya ya Morogoro. Ndani ya gari nilijikaza lakini hali ilizidi kuwa mbaya na kunifanya nitokwe machozi. Mama kawa kutumia senti kadhaa za rambirambi alimlipa daktari akanifanyia utafiti wa kina kiasi. Mwishowe akaja na jibu ambalo linaifanya simulizi hii iendelee kupitia hali isiyokuwa na nafuu walau ya kutabasamu. “Mguu wako umeoza vibaya sana, unatakiwa kuwahishwa jijini Dar es salaam kwa ajili ya kukatwa maana ukichelewa hali hiyo italifikia paja jambo ambalo ni baya sana.” Mama alisema haya akiwa amesimama mbele yangu, machozi yakimlengalenga!! Nilifumba macho kisha nikayafumbua, nikamkuta mama amenifikia tayari na kunikumbatia!! “Nililie mimi mwanangu kisha unisamehe kwa kukuzaa katika ulimwengu huu uliojaa imani potofu kupindukia, usijilaumu kamwe kwa kukutana na Hamisa…. Jilaumu kwa sababu ya wazazi wake!!!” mama alinieleza akiwa bado amenikumbatia. Kumtaja Hamisa kukanifanya nijikute nina maswali mengi ya kuuliza ambayo nilihisi mama anaweza kuyajibu lakini alinizuia kwa kusema kuwa pale si mahali muafaka.
**** IKAWA safari yangu ya tatu kurejea jijini Dar es salaam. Safari mbili nikiwa natabasamu lakini hii ya tatu nikiwa katika kilio kikubwa moyoni na simanzi isiyosemekana usoni maumivu nayo yakiutafuna mwili wangu. Tulisafiri kwa kutumia basi la abiria wa kawaida, hata kabla safari haijaanza maumivu na fedheha zilianza kujitokeza. Dada mmoja ambaye hadi sasa sura yake haijabanduka kichwani mwangu aliifanya safari yangu kuwa ngumu sana. Awali alijiziba na kitambaa usoni kisha akamnong’oneza mwenzake jambo, wakacheka! Kisha uvumilivu ukamshinda akasema waziwazi kuwa nilikuwa natoa harufu mbaya, mama alinitetea kuwa nilikuwa naumwa na hapo nilikuwa naelekea hospitali. Yule dada mweupe kwa kutumia mkorogo hakuridhishwa na utetezi wa mama akatoa hoja kuwa lile halikuwa basi la wagonjwa. Hasira ilinikaba kooni, machozi yakajiunda na kisha yakatiririka mashavuni. Nilitamani kusema neno lolote kwa yule dada lakini ni kama mama aligundua, akanifuta machozi kisha akaninong’oneza. “Wafuasi wa shetani hawa wametumwa kukukatisha tamaa halafu umkufuru Muumba wako, funika kombe mwanaharamu apite mwanangu!!” Maneno ya mama yalinipa ujasiri na imani tena! Sikusema neno lolote. Baadaye viongozi wa lile basi walimfanyia utaratibu yule dada na kumhamishia sehemu nyingine ya kukaa mbali na mimi. Niliyasikia maneno ya baadhi ya abiria wakikilaani kile kitendo cha yule dada kunitupia maneno makali ya kuniumiza kiasi kile. Mungu amsamehe popote pale alipo!! Safari ilikuwa ngumu sana, hasahasa basi lilipokuwa likipita katika mabonde, mguu ulikuwa unaumia sana… mama hakulala alikuwa macho na kila nilipokumbwa na maumivu alikuwa akinibembeleza na kuzidi kunitia moyo kuwa hayo yalikuwa maumivu ya muda tu na yatakwisha na kusahaulika. Nilijua fika kuwa mama alikuwa katika kunipa moyo tu.. lakini ilikuwa heri kuwa na mmoja wa kukupa moyo kuliko wote kukukatisha tamaa…
***
Tuliingia jijini Dar es saalam majira ya mchana, mama akakodi taksi ambayo ilitufikisha moja kwa moja hospitali ya taifa ya Muhimbili. Jengo lile kubwa likanifanya nifumbe macho na kukumbuka siku ya kwanza kuingia ndani ya jengo lile kwa sababu mgongo unauma lakini baada ya uchunguzi nikagundulika kuwa na kansa iliyonilaza kitandani tangu siku ile na kisha kuniachia mateso ya kudumu. Awali niliingia katika jengo lile nikiwa naweza kutembea japo kwa kuchechemea lakini sasa ni macho tu yalikuwa yale ya zamani lakini kila kona ya mwili wangu ilikuwa imebadilika na kuwa ya aina yake. Maumivu yalitanda kila kona! Tulionyesha barua ya daktari kutoka Morogoro, tukapokelewa na kupewa maelekezo. Tukayafuata!!
TABASAMU LA UCHUNGU!!
KIZA kilitanda kisha mwanga ukafuata kwa kiasi kidogo, nikajigeuza ili niweze kulala vyema zaidi. Lakini sikuweza nikamsikia mtu akinipapasa…. “Mpenzi muda wa mechi umekaribia amka bwana….” Alikuwa ni Hamisa nikamtazama kisha nikaitazama na saa ya ukutani, kweli zilikuwa zimebaki takribani dakika hamsini. Nikajitoa kitandani Hamisa akanipatia taulo nikatambua kuwa ameniandalia maji tayari bafuni. Nikaingia na kujiosha vyema. Nikajiandaa upesiupesi na kuvaa kimichezo. Hamisa akaniongoza katika sala fupi kisha nikaongozana naye kuelekea uwanjani. Niliachana naye nilipoungana na wachezaji wenzangu!! “Utafunga na utakuwa shujaa katika mechi ya leo!” aliniambia kisha akanibusu shavuni! Mchezo ulikuwa wa nguvu sana na kila upande ulikuwa umekamia ili kuupata ushindi. Kipindi cha kwanza wapinzani wetu wakapata bao la kwanza hivyo kuwanyong’onyesha mashabiki wetu. Nilijitahidi kupambana lakini mambo yalizidi kuwa magumu kwetu mwanzoni mwa kipindi cha pili ambapo tulifungwa bao la pili. Mashabiki wetu wakaanza kuzomea baadhi ya wachezaji ambao walikuwa wanacheza kwa kiwango cha chini. Zilibaki dakika kumi na tano mpira kumalizika, mashabiki wetu walianza kutoka uwanjani, nikatiwa nguvu na yale maneno ya Hamisa nilipoupata mpira nikiwa karibu na goli, nikapiga chenga ya kwanza, nikapiga chenga ya pili kisha bila kupoteza wakati nikaubutua ule mpira kwa nguvu zote. Kipa hakuweza kuuona zaidi ya kuona nyavu zikitikisika. Matokeo yakawa mbili kwa moja!! Nilienda kushangilia upande wa mashabiki wetu tu…. Ajabu alikuwa amebaki Hamisa na wengine wawili. Hamisa alikuwa amebeba bango lililokuwa likinisifu mimi kuwa ni shujaa. Wapinzani wetu kuona tumerudisha goli moja wakaanza kucheza kwa kujilinda zaidi kuliko kushambulia. Kosa kubwa kabisa katika soka, nikawasihi wenzangu tushambulie kwa kasi zaidi. Hakika ikawa faida kwetu tena, mpira ukapigwa mabeki wakajichanganya wao kwa wao wakaukosa mpira, nikachomoka kwa kasi ya hatari nikaufikia mpira na kipa akiwa anakaribia kuufikia. Lakini macho yangu yakaona kosa alilofanya kwa kutanua miguu yake, nikaugusa mpira na kumpiga tobo. Kisha nikamzunguka upesi na kuumalizia mpira golini. Hakika lilikuwa goli langu bora kabisa kufunga kwa mguu wangu wa kulia. Wakati goli linaingia refa alikuwa anangoja kupiga filimbi ya mwisho. Nilitamani kuruka jukwaani nikamkumbatie Hamisa lakini sikuweza kumfikia. Mchezo ule ukaamuriwa kuisha kwa mshindi kupatikana kwa njia ya penati. Nikachaguliwa kuwa mpiga penati wa kwanza kabisa. mashabiki wetu walikuwa wamerejea na walikuwa wanashangilia kwa nguvu sana wakati nautenga mpira niweze kupiga penati. Nilirudi nyuma hatua tatu nikamtazama kipa wao, kisha nikaanza kusogea. Ile nataka kuupiga ule mpira mguu ukawa mzito, nikajaribu tena haikuwezekana mguu ukazidi kuwa mzito zaidi. Mashabiki wakaweka mikono yao kichwani na wengine midomo ikiwa wazi. Nini hiki? Nikajiuliza huku nikijitahidi kuunyanyua mguu wangu… haikuwezekana. Nikainama niupapase mguu wangu, na hapo macho yakafunguka nikashuhudia ule mguu na kutambua ni kwanini nilishindwa kuupiga ule mpira. Mguu wangu mguu ulikuwa umekatwa na pale nilipokuwa ni hospitali ya Muhimbili!! Yote yaliyopita kichwani mwangu yalikuwa ndoto tu!! Ndoto ya mwisho kabisa iliyonipa nafasi ya kuuona mguu wangu ukiwa uwanjani ukicheza mpira na kufunga magoli. “Mama mguu wangu nd’o haurudi tena??” nilimuuliza mama aliyekuwa ameketi kando yangu. Swali ambalo nilijua jibu lake kuwa ni NDIYO…. Lakini mama wa ajabu hakunijibu kama nilivyotaraji. “Ipo siku utatembea tena! Na hapo nitakupa jibu lako” Jibu la mama lilinistaajabisha mno, nilifahamu fika kuwa ananitia moyo lakini ilikuwa vyema kuliko kunikatisha tamaa. Tabasamu la uchungu lilichukua nafasi nilipoikumbuka ile ndoto ya mchezo ule ambao nilifunga magoli mawili. Baada ya siku mbili nikaanza rasmi mazoezi ya kutembea kwa kutumia magongo, zoezi lilikuwa gumu haswa nilitokwa jasho haswa. Mama alikuwa kando yangu kunipa moyo kuwa hata kile nilichokuwa napitia ni mtihani katika maisha. Mabega yaliuma sana, makwapa yaliwaka moto haswa na nilikuwa naanguka mara kwa mara, bado mama alikuwepo kuninyanyua “Usipomkufuru Mungu katika hili unalopitia, digrii utakayoitwaa hapa ni mara elfu ya hiyo ambayo ungechukua huko chuoni kwenu!!” mama alinieleza wakati nikiwa nimepumzika. Alipozungumzia juu ya digrii nikaikumbuka hiyo tarehe na mwezi nikakumbuka kuwa wanafunzi niliosoma nao darasa moja, iwapo hawakufeli basi walikuwa wapo mwaka wa pili wa chuo SEMISTA YA KWANZA. Nami nilikuwa mwaka wa pili wa mateso SEMISTA YA KWANZA. Mwaka niliouanza kwa kukatwa mguu wangu wa kulia!!
Siku ya sita ya mazoezi nikiwa nimeanza kuyazoea ndipo nilikutana na kitu ambacho sikukitegemea hata kidogo. Ukawa mwanzo wa tabasamu la muda mfupi na kisha ukafuatia ule muda wa kumtambua mbaya wangu, shetani aliyeniadhibu hivi lakini licha ya haya yote ile pingu ya uchungu na majanga ya mara kwa mara ikaendelea kunifunga. Amakweli kumjua adui yako waweza kulimaliza tatizo ama kuliongeza maradufu hasahasa ikitegemea ulifanya nini baada ya kumgundua adui yako!! Nilikosea sana kwa njia nilizotumia!! Ewe mwenyezi Mungu nisamehe!!
NB: kuna baadhi ya wadau wanatoa maoni kuwa simulizi hii inajenga matabaka na kuonyesha waisilamu wana roho mbaya….. tafadhali tuwe waelewa wa riwaya na simulizi kama hizi… lengo hapa sio dini gani ama dhehebu gani.. hii ni simulizi ambayo inazungumzia jamii yetu moja kwa moja….. Kama ni roho mbaya hata JAPHET kaka wa Gerlad alikuwa na roho mbaya…. Je wakristo nao waweke kiulizo juu ya hili??? TUSIZIRUHUSU AKILI ZAKO KUFIKIRIA PAFUPI KIASI HICHO!!!
KUMBUKA: DINI YAKO NI IMANI YAKO na sio jina lako… Mustapha, Gerlad, Hamisa, yanabakia kuwa majina tu!!!!
0 Comments