Header Ads Widget

Responsive Advertisement

USINILILIE MIMI KAWASIMULIE WANAO - 2



Simulizi : Usinililie Mimi Kawasimulie Wanao
Sehemu Ya Pili (2)

Baada ya muda mama alirejea tena akiwa ameongozana na wanawake kadhaa, na mwanaume mmoja ambaye nilimtambua fika kuwa alikuwa ni daktari. Walijongea na kukizunguka kile kitanda nilichokuwa nimelalia, yule daktari akapiga goti na kuinama kisha akaanza kusema na mimi kwa utulivu wa hali ya juu sana.
“Gerlad… Gerlad Masembo, napenda kuzungumza nawe maneno ambayo naamini wewe ni jasiri na utanielewa sana, maana umeteseka sana kitandani. Uamuzi wa uongozi kuamuru kuwa utolewe kitandani na kurejeshwa nyumbani ama kupelekwa nje ya nchi usiuone kama wa manyanyaso ama tumekuchoka la! Uongozi unayo nia njema kabisa, wakati huu ambao walau unaweza kusafiri kwa njia ya basi kwa kujikaza uutumie kurejea nyumbani kuliko hali itakavyozidi kuwa mbaya. Licha ya wewe kuwa mgonjwa unaweza kuwa shahidi juu ya jitihada zetu za dhati tunazofanya na tulizofanya kwa kipindi chote tulichokuwa pamoja. Hakuna nafuu yoyote inayoweza kupatikana kila dawa imetumika Gerlad. Waswahili husema kwamba hata hali ya hewa ya nyumbani wakati mwingine husaidia kuleta unafuu kuliko harufu ya madawa makali hospitalini…… nakusihi usiwe na kinyongo. Mwombe Mungu kwa bidii maana ni yeye aliyebaki katika kuamua hili.” Alimaliza kuzungumza kisha akasimama na kutueleza kwa ujumla kuwa atanisaidia kiti kwa ajili ya kutembelea wakati wa ugonjwa wangu, na pia akatuhakikishia kuwa atagharamia safari yetu ya kwenda Morogoro nyumbani kwetu. Maneno yake na moyo wake wa utu ukanipa faraja kubwa, mipango ya safari ikapangwa kwa ajili ya siku iliyofuatia. Usiku mgumu wa kuwaza na kuwazua juu ya maisha bila uangalizi wa daktari ukapita hatimnaye, alfajiri ya saa kumi na moja nikaamshwa kwa msaa wa mama na nesi wa kiume, nikaingizwa katika gari aina ya Noah nikakalishwa katika kile kiti cha kutembelea kilichokuwa kimewekwa katika sehemu iliyokuwa na uwazi baada ya kiti kuondolewa. Daktari akashiriki nasi katika sala fupi kisha akampa dereva wake maelekezo kidogo.
Tukaondoka!!!!

Gari lilivyoanza kuondoka nikaikumbuka safari yangu ya kuja jijini Dar es salaam kwa sababu za kielimu, nilikata tiketi mwenyewe nikisindikizwa na rafiki zangu. Nilipanda gari mwenyewe nikiwa na nguvu zangu mwilini na tabasamu usoni. Ikiwa imepita miezi kadhaa ni safari tena ya kurejea Morogoro, lakini nikiwa sijiwezi, siwezi kuugeuza mwili wangu bila msaada wa watu, sina tabasamu wala furaha bali maumivu makali mwilini. Kilichonipeleka na kuhamishia maisha yangu jijini Dar hakikutimia. Niliumia sana kuondoka jijini bila kuijua hatma ya Joshua na Hamisa, lakini nilijua kwa wakati ule hakuna ambaye ningemueleza na anielewe na hata wakinielewa utakuwa usumbufu kuwaagiza wakamtafute Joshua na Hamisa!!
Nikabaki na maswali mazito huku nikiamini ipo siku nitapata majibu. Niliungoja wakati na siku moja wakati ulifika!!
Ewe unayepumua na kutabasamu sasa.... mshukuru Mungu kila kukicha!!

****
SIKU za awali ndani ya Morogoro maisha yalionekana kuwa shwari tu, mama alikuwa akifuata maelekezo aliyokuwa amepewa na daktari. Alinibadili nguo na kuninywesha dawa. Nilijisikia vibaya sana kumpa mama mzigo ambao alikuwa ameutua miaka kadhaa iliyopita mzigo wa kuhangaika kuninyonyesha kunibadilisha nguo na kuniogesha enzi nikiwa mtoto mdogo. Sasa maisha yale yalikuwa yamerejea tena, kaka yangu niliwaeleza awali kuwa ni mlevi kupindukia asingeweza kufanya lolote kwa ajili yangu. Mama shujaa akauvaa tena wajibu huu!! Nilifadhaika sana kwa hali hii, marafiki kadhaa walikuja kunisabahi huku wengi wao wakiniuliza kulikoni….. sikupenda sana kusimulia juu ya kilichotokea maana ningeweza kulia na kujiumiza zaidi na daktari alinishauri niwe msahimilivu nisilie mara kwa mara.
Ama hakika wanadamu si wema na hawana huruma hata kama ni ndugu yako wa damu. Siku ambazo mvua zilinyesha zilikuwa za mateso makali sana kwangu, licha tu ya baridi kunisababishia maumivu makali, nyumba nayo ilikuwa inavuja na kunisababishia kulowana jambo ambalo sikutakiwa kabisa kukumbwa nalo. Usiku huo wa kulia na kusaga meno mvua ilinyesha pia. Ilikuwa mvua kubwa sana, mama alinihamisha huku na kule hadi hatimaye akanifunika na blangeti lake, nikamshuhudia akiwa anatetemeka huku akihangaika kuziba baadhi ya matundu katika paa la nyumba yetu.
Nilitamani ujitoke muujiza mama alale na mimi nihangaike kuziba yale matundu lakini ni jicho pekee lilibakia kumtazama. Maji yalimmwagikia na meno yake yakaanza kugongana kinywani. Nilifumba macho nisiweze kumtazama zaidi lakini sikuweza, mama alihangaika hadi mvua ilipopungua. Akaingia chumbani na kuchukua godoro lake akaliweka juu ya godoro la kitanda changu ambalo lilikuwa limelowana, kisha akanibeba na kunihamishia kitandani.
“Mama wewe utalala wapi sasa…” nilimuuliza baada ya kuwa nimegundua alichokifanya kuwa ametoa godoro lake ili niweze kulalia mimi.
“Gerlad mwanangu, nimelala sana, nimelala zaidi ya miaka arobaini na tano, hivyo nisipolala leo haimaanishi kitu…. Ni wajibu wangu kukulinda wewe ambaye unanihitaji kuliko chochote kwa wakati huu.
Ningeweza kulala lakini kwanza ulale wewe ukiwa salama.” Mama alinijibu kisha akaendelea, “Hata baba yako alipokuwa anaenda vitani alinieleza hivyo hivyo, kwamba iwapo hatarejea salama basi jukumu la kuitunza familia nzima ni langu, sijayasahau maagizo yake!! Looh! kweli mume wangu hakurejea kabisa, eeh! Mungu amlaze pema peponi…” huku meno yakigongana mdomoni mama alilazimisha tabasamu la kunipa matumaini. Baadaye akaniaga kuwa anaenda chumbani kwake. Akanibusu katika paji la uso na kutoweka.

Sikuwa nafahamu muda ule ulikuwa saa ngapi lakini nilijua tu kuwa ulikuwa ni usiku mnene sana. Nilishtuka kutoka usingizini kutokana na kelele zilizokuwa zinapigwa. Ilikuwa sauti ya mama yangu, alikuwa akilia kwa uchungu huku akisikika kukabiliana na watu, mtu ama kikundi fulani.
“Mama!!.... mama…” niliita lakini sikujibiwa, nikasikia kishindo kingine kikubwa kisha sikuzisikia kelele za mama tena.
“Nyie ni akina nani, mwacheni mama yangu…mwacheni mama yangu nasema….ntawaua mkimgusa mama yangu..” nilizungumza nikiwa sielewi namaanisha nini. Lakini wale watu ama mtu hawakujibu chochote. Nilitamani sana kuwatazama lakini upande ambao mama alinigeuzia ulikuwa mwingine, sikuweza kuona chochote. Nilitamani kugeuka lakini sikuweza kufanya hivyo. Nilibaki kulalamika na kuwatishia vyovyote nilivyoweza. Baadaye kidogo, nikasikia vishindo nje ya nyumba kisha kimya kikatanda.
“Mama…mama….” Niliita na sikujibiwa. Nisingeweza kuvumilia hadi asubuhi nilianza kupiga kelele kwa nguvu sana nikijaribu kuomba msaada, lakini hakutokea mtu yeyote yule. Kile kishindo kilinipa maswali mengi sana na kubwa zaidi nilihofia juu ya usalama wa mama yangu.
“Ewe Mungu… nasema nawe baba katika kiza hiki kinene…. Fanya muujiza wako sasa. Nibariki katika hiki ninachoamini kuwa kinawezekana.” Nilifanya ombi moja fupi kisha nikairuhusu nafsi yangu kufanya jambo ambalo lingeweza kuyamaliza maisha yangu palepale. Lakini sikuogopa kuhusu hilo, maana kupoteza uhai wangu kwa sababu ya mama yangu ni jambo ambalo kwenye orodha ningeliweka la kwanza. Nikaikaza mikono yangu na miguu yangu, nikaanza kuhesabu moja hadi tatu kisha kwa nguvu kubwa kabisa nikajiviringisha huku nikipiga mayowe makali ya maumivu. Hatua ya kwanza tumbo likaangalia juu, sikutaka kungoja nikajiviringisha tena. Nikatua sakafuni kwa tumbo na mdomo ukajipigiza chini, nikaanza kuvuja damu baada ya mdomo kupasuka. Yote niliyapuuzia, nikaanza kujilazimisha kutambaa kuelekea chumbani kwa mama, nilijivuta kwa shida kuu, huku nikihema kwa kasi. Nikazidi kujivuta nikaufikia mlango nikausukuma, nikaingia nikitambaa vilevile.
“Mama…maaaaamaaa…” niliita huku nikipapasa huku na kule kwenye lile giza. “Mama…ukwapi mama yangu eeh! Ukwapi, nipo hapa mama nahitaji kukusaidia mama, nipo hapa sema nami mama. Sema nami mwanao..” nilizungumza peke yangu hakuna aliyenijibu.
Nilishindwa kutambua nini kinaendelea, hofu nayo ilizidi kunitawala na kunifanya niyasahau kabisa maumivu yote mwilini. Ghafla nikasikia kikohozi kikitokea katika kona fulani ndani ya chumba, upesi nikaanza kutambaa kuelekea katika kona ile huku nikiita ‘mama’…..
“Gerla……Gerlad….” Sauti ya mama ilinijibu kwa tabu.
“Mama….ni kitu gani kimetokea mama…”
“Gerlad, kaka yako ni wa kutaka kuniua mimi….kaka….kaka yako analeta majambazi kweli watuue.”
“Nini mama?…kaka yangu yupi..” nilihoji huku nikiwa natetemeka.
“Japhet….Japhet ametuvamia, akanikaba na kunilazimisha nitoa ufunguo wa baiskeli yako. Nikakataa wakanipiga nahisi nilipoteza fahamu… Japhet anadhani alivyoficha sura yake sikuweza kumtambua, hajui kama ameishi katika tumbo langu kisha katika kifua changu akanyonya.. Japhet wa kunivamia mimi…. Japhet kweli yaani alivyougua utotoni nikahangaika mimi hadi daktari akaudhalilisha utu wangu kwa ajili yake, Japhet… natoa kilio hiki usiku huu, najua ameiiba hiyo baiskeli yako mwanangu, nalia kwa niaba yako Gerlad nalia chozi hili litue juu yake, kama ni kweli Mungu ninayemuamini yu hai na anaishi na amuadhibu nikiwa hai, amdhalilishe na dunia nzima ijue, nasema kwa kilio changu na chako dunia haitakuwa mahali sahihi kwake. Na ninailaani siku niliyomzaa nakilaani na kizazi chake chote Japhet, Mungu anisamehe kama nimemuhukumu bila makosa.” Mama hakuweza kuendelea kuzungumza, bali alianza kulia kwa kwikwi, kisha akaninyayua na kunikumbatia!!
Akili yangu ni kama ilikuwa haifanyi kazi tena!!
Nilia sana!!!

_______ JIFUNZE: MALIPO NI HAPAHAPA…. Usiku wa giza hauyafichi madhambi yako mbele ya Mungu. Utayaficha mbele ya wanadamu tu, lakini itafikia wakati kila kitu kitakuwa wazi na kila mmoja atahukumiwa kadri ya matendo yake!!
*Mama aliyekulea unamkaba na kumpiga* UMELAANIWA WEWE NA KIZAZI CHAKO CHOTE!!! _______



MAMA alipowasha mshumaa ndipo niliumia zaidi, mdomo wake ulikuwa umevimba, nilipogeuza macho upande mwingine nikagundua kuwa mama alikuwa amenipatia mimi lile godoro na kisha yeye alilalia upande wa kanga tu. Mama alininyanyua na kunipeleka kitandani kwangu, akanifunika shuka na kunisihi nilale halafu asubuhi tutazungumza zaidi. Sikuwa na kipingamizi… nikalala na hatimaye usingizi ukanipitia.
Nilishtuka majira ya saa nne asubuhi, pembezoni mwa kitanda changu alikuwepo mama akiwa na kisufuria kidogo. Baada ya kumsalimia alinieleza kuwa yupo pale kwa ajili ya kunipatia tiba. “Tiba gani mama?”
“Jana usiku ulipata michubuko tumboni….” Alinijibu huku akinipapasa shavu langu na kunifinyafinya. Nikalifunua tumbo langu, hakika nilikuwa na michubuko ambayo mimi binafsi nilikuwa sijaitambua lakini mama alikuwa ameling’amua hilo tayari. Alinikanda hapa na pale kwa kutumia maji yale aliyonieleza kuwa amechemshia kwa dawa za asili. Baada ya zoezi hilo mama alinieleza jambo zito.
“Gerlad…. Asubuhi mama Kichawele alikuja kukusalimia lakini ulikuwa umelala bado…..” akakohoa kidogo kisha akaendelea, “ licha ya kuja kukusalimia alikuwa amekuja na wazo. Nikaona kuwa mimi pekee siwezi kumjibu lolote mpaka nikushirikishe na wewe, kama tutakubaliana tumjibu. Ni kuhusu afya yako wewe….” Akanitazama usoni, nami nikajitikisa niweze kusikiliza vyema.
“Mama Kichawele amesema kwamba yawezekana ni wanadamu wamesimama nyuma ya hili. Na kama ni hivyo akatoa ushauri kuwa tujaribu kwa waganga wa jadi labda tunaweza kupata mustakabali juu ya hili. Kuhusu huyo mganga amedai atatupeleka yeye na amewahi kumtumia mara kwa mara. Mwanangu mimi sikutaka kumjibu nikasema kuwa wewe ni mtu mzima, nitakueleza ukikubaliana naye mimi sina neno mwanangu, maana nia yangu ni moja tu wewe upone basi!! Sina nia nyingine na unalijua hilo…” mama alimaliza kunieleza kwa upole kabisa. Nilivuta pumzi na kisha kuzitoa kwa nguvu sana….
Nikatulia kwa muda kidogo nikitafakari. Mwisho nikamueleza mama kuwa sipo tayari kushiriki katika tukio la kumtegemea mwanadamu katika kuniokoa katika janga hili.
“Mama ni Mungu ajuaye… kama ni wanadamu atawaadhibu nikiwa hai. Tumwachie yeye…. Utajuaje labda ningesoma sana ungekuwa mwanzo wa kukusahau mama yangu na Mungu amenipa onyo mapema… utajuaje labda pigo hili ni mahususi kabisa ili niuone upendo wako mama kwa mara nyingine. Mama sitaenda kwa huyo mganga, mwambie mama Kichawele nashukuru sana kwa jitihada zake. Mama hakuwa na kipingamizi chochote, akakubaliana nami kwa imani kabisa.
Kukataa huko kwenda kwa mganga kukazua jambo!!

****
ZILIANZA kama tetesi zisizokuwa na mashiko yoyote, tetesi zikazidi kusambaa na hatimaye zikageuka kuwa fununu. Karibia watu watatu kati ya watano waliokuja kunisalimia, walitilia mashaka juu ya mtu wangu wa karibu kuwa anahusika na ugonjwa wangu kitandani. Nilitabasamu na kuwapuuzia. Hatimaye rafiki mmoja asiyekuwa na haya akanieleza moja kwa moja bila aibu.
“Mama yako anakumaliza kimyakimya….” Nilishtuka sana kusikia maneno yale lakini nd’o kwanza akakolezea.
“Mama yako mzazi anakuchezea wewe….shtuka. na laiti kama ungeenda kwa mganga angemuumbua nd’o maana amekwepa.” Nilitamani ningekuwa na uzima ili kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nipige mtu, lakini sikuwa naweza hata kurusha ngumi ya uhakika.
“Naomba utoke nje Kichawele….. niache nipumzike kwanza.” Nilimsihi kwa utulivu mkubwa. Alijitokea huku akiendelea kunisema juu ya mama yangu. Taratibu tetesi zilivyoonekana kuwa kweli, hakuna mtu aliyekuja kunisalimia pale nyumbani. Na kaka yangu Japhet akaanza kulalamika huko vilabuni kuwa mama yetu ndiye aliyemroga na hawezi kuacha pombe japo anayo nia ya kuacha. Mama alinieleza mkasa huu huku akitabasamu, nikatambua kuwa alikuwa amekasirika sana.
“Nipe uzima dakika kumi tu eeh Mungu nimsulubu huyu Japhet kabla hujampa laana yako..” nilijisemea na mama akanisikia.
“Gerlad, usiombee uzima wako kwa ajili ya kulipiza kisasi, ombea uzima wako ili tu Mungu tunayemuamini awaaibishe wanaosema mimi nimekuroga wewe. Kuinuka kwako kitandani kutawanyamazisha na kuwafanya waishi kwa aibu milele yote….” Mama alitema busara zake. Nikamwomba Mungu msamaha kimyakimya.
Baada ya siku kadhaa, ilikuwa siku ya jumapili mchana tulipata ugeni mkubwa kiasi nyumbani. Baadhi ya wazee nilikuwa nawafahamu na wengine sikuwajua hata sura. Nilikuwa nimeketi na mama nje ya nyumba.
Nikamuuliza mama wale ni akina nani, lakini hakunipa jibu lolote. Badala yake alisimama na kwenda kuwapokea, alisalimiana nao vyema na mara kukazuka kitu kama malumbano kila upande ukilazim,isha jambo ambalo unataka. Walivutana huku na kule, mara mama akataka kukimbia.. lakini hakufika mbali akaanguka, wakamkamata wakamnyayua kwa nguvu. Nikajaribu kupiga kelele lakini sauti ilikuwa imekauka kabisa. Wakaanza kuondoka na mama yangu huku wakimlazimisha. Mama alitupa mikono huku na kule huku akiniita kwa jina na kunisihi nimfuate. Lakini sikuweza kufanya lolote. Machozi yakanitiririka kutazama jinsi mama yangu mpenzi alivyozidi kutokomezwa mbali ya macho yangu. Akili yangu iliyoanza kuchoka ikafanya fikra moja tu ya mwisho kabisa.
Kujiua!!
Nisingeweza kuishi peke yangu bila mama yangu… nisingeweza kuteseka zaidi ya pale, maana hakuwepo mtu wa kunihudumia. Nikazitazama mbingu na nikatamani kufika huko badala ya kuteseka ulimwenguni.
Mama akatoweka kabisa!! nikabaki kulia kama mtoto mdogo. Masaa yakakatika nikiwa nimetulia palepale nje huku njaa kali sana ikinisumbua, mama hadi anachukuliwa na wanaume wale hakuwa amepika chakula chochote, nilifumba macho na kufumbua ili iwe ndoto na nishtuke na kumkuta mama lakini haikuwa hivyo. Majira ya saa kumi na mbili jioni ndipo alipofika mgeni mwingine akiwa anahema juujuu….. Nilikuwa namfahamu ni mmoja kati ya marafiki zangu wa utotoni.
“Gerlad… wanataka kukuua… wanataka kukuua… ondoka hapa.” Alinieleza lakini sikushtuka maana hata mimi nilipanga kujiua siku hiyo ili niondokane na suluba hiyo.
“Akina nani.. na mbona wanachelewa!!”
“Wazee wa kijiji wanadai unaleta mikosi katika kijiji na mavuno yanakuwa mabaya sana hivyo mganga ameshauri uondolewe..”
“Na mama yangu je?”
“Wamemficha mbali nawe ataachiwa huru ukishauwawa.”
“Nawasubiri waniue… “ nilimjibu pasipo na wasiwasi. Lakini kijana yule hakuridhishwa na majibu yale, upesi akainama na kunipa mgongo ili nipande anibebe.
“Dulla… nitakuchosha bure acha waniue waridhike na nafsi zao.”
“Hapana Gerlad, panda upesi kuna mahali nakupeleka amini kuwa ni salama kabisa na hautauwawa… na usiwaze kujiua huo ni udhaifu wa hali ya juu.” Alizidi kunisihi. Lakini kabla sijakwea katika mgongo wake tukausikia muungurumo wa gari… “wamefika!!” nilijisemea huku nikianza kupatwa na hofu juu ya kifo. Dulla alitulia akingoja tukio hilo la mimi kuuwawa litokee, alibaki akiwa ameinama vilevile wakati gari lilipofika pale nyumbani. Gari likasimama, akashuka mwanaume na mwanamke. Walikuwa wamejivika miwani usoni.
Wanataka waniue na nisiwajue sura zao!!
Nilijisemea wakati wakizidi kukimbilia nilipokuwepo….. Mwanamke alikimbia zaidi ya mwanaume. Aliponifikia nilikuwa nimefumba macho nikiomba muujiza wowote utokee.
“Gerlad……” aliita yule mwanamke. Nikayafumbua macho yangu…….. Amini usiamini ndugu msomaji niliweza kusimama kwa mshtuko, niliweza kusimama palepale.. na kisha udhaifu wangu ukarejea tena yule mwanamke akanidaka kifuani kwake, nikamzidia uzito nikaanguka naye.
“Hamisaaaaa!!!!...... hamisaaaa” niliita huku nalia, kilio ambacho sikuelewa kina maana gani….. Hamisa mbele yangu, Hamisa kijijini kwetu…..

Kwa wanafunzi wa chuo nilioanzanao masomo bila shaka walikuwa wameumaliza mwaka wa masomo (SEMISTA YA PILI) Nami nikaumaliza mwaka katika namna ya kipekee… Hamisa kijijini kwetu! Msichana niliyempenda kupita wote!!

JIFUNZE _______ MUUJIZA upo… muujiza hutuonyesha uwezo wa Mungu katika nyakati tusizozitarajia. Wakati unawaza kujiua yeye anakuwazia mema, anaamini bado unayo haki na wajibu wa kutimiza ulimwenguni. Majibu yake huwa ni ya kustaajabisha sana, anajibu wakati ule ambao wewe hutarajii!! Usimwabudu mwanadamu, mpe Mungu sifa zake!! _______

“Nawasubiri waniue… “ nilimjibu pasipo na wasiwasi. Lakini kijana yule hakuridhishwa na majibu yale, upesi akainama na kunipa mgongo ili nipande anibebe. “Dulla… nitakuchosha bure acha waniue waridhike na nafsi zao.” “Hapana Gerlad, panda upesi kuna mahali nakupeleka amini kuwa ni salama kabisa na hautauwawa… na usiwaze kujiua huo ni udhaifu wa hali ya juu.” Alizidi kunisihi. Lakini kabla sijakwea katika mgongo wake tukausikia muungurumo wa gari… “wamefika!!” nilijisemea huku nikianza kupatwa na hofu juu ya kifo. Dulla alitulia akingoja tukio hilo la mimi kuuwawa litokee, alibaki akiwa ameinama vilevile wakati gari lilipofika pale nyumbani. Gari likasimama, akashuka mwanaume na mwanamke. Walikuwa wamejivika miwani usoni. Wanataka waniue na nisiwajue sura zao!! Nilijisemea wakati wakizidi kukimbilia nilipokuwepo….. Mwanamke alikimbia zaidi ya mwanaume. Aliponifikia nilikuwa nimefumba macho nikiomba muujiza wowote utokee. “Gerlad……” aliita yule mwanamke. Nikayafumbua macho yangu…….. Amini usiamini ndugu msomaji niliweza kusimama kwa mshtuko, niliweza kusimama palepale.. na kisha udhaifu wangu ukarejea tena yule mwanamke akanidaka kifuani kwake, nikamzidia uzito nikaanguka naye. “Hamisaaaaa!!!!...... hamisaaaa” niliita huku nalia, kilio ambacho sikuelewa kina maana gani….. Hamisa mbele yangu, Hamisa kijijini kwetu…..
Kwa wanafunzi wa chuo nilioanzanao masomo bila shaka walikuwa wameumaliza mwaka wa masono (SEMISTA YA PILI) Nami nikaumaliza mwaka katika namna ya kipekee… Hamisa kijijini kwetu! Msichana niliyempenda kupita wote!!
***
Muda wa mshangao ukapita ukafuatia ule muda wa kustaajabu na kujiuliza mara mbilimbili, je? Haya mateso yalipakuliwa na kisha kuwekwa katika sahani ya maisha yangu ama… mabalaa yote nilipangiwa mimi ili niwe shuhuda wa kila kitu. Nilijitahidi na kujitoa katika tumbo na kifua cha Hamisa ili nipate fursa ya kumuuliza ilikuwaje akafika pale kijijini kwetu na alikijuaje kijiji kile na maswali mengine mengi sana juu ya nini kilimtokea katika maisha yake tangu alipotoweka na jingine kubwa nilihitaji kujua juu ya Joshua!!
Ajabu ni kwamba Hamisa badala ya kuinuka alikuwa anakoroma tu na kisha akaanza kurusha miguu yake huku na kule. Mungu wangu!!! Nilikuwa nimeanguka naye chini kisha nikaligandamiza tumbo lake kubwa kabisa lenye kiumbe ndani yake, zile kelele alizopiga Hamisa hazikuwa za shangwe bali maumivu makali ya tumbo.
Sasa hakuwa akizungumza tena bali kurusha miguu huku na kule. Sikuwa naweza tena kunyayuka hivyo nikaendelea kubaki kama nilivyokuwa, nilijitahidi kuwapigia kelele wenzangu juu ya hali ile, na wao wakapagawa wasijue ni kipi wanaweza kufanya. Ile furaha ya kumuona Hamisa ikayeyuka baada ya binti yule chaguo sahihi kabisa la moyo wangu alipoanza kutokwa na damu sehemu zake za siri huku akiendelea kurusha miguu huku na kule. Macho yakamgeuka na kuanza kuwa meupe ajabu!! Anakufa!!
Nd’o wazo pekee lililopita kichwani mwangu, hali iliyomkuta Hamisa ni wagonjwa wengi sana waliokufa pale hospitali ya taifa ya Muhimbili niliwashuhudia kisha hawakusema tena. Nilijiburuta chini na kujilazimisha kunyayuka lakini maumivu ya wakati huu yalikuwa makubwa zaidi. Hali ile ikanifanya nitokwe nna machozi, machozi yale yakajawa na taswira ya mama yangu na Hamisa. Wote kwa pamoja nilikuwa naelekea kuwapoteza bila msaada.
“Hamisaaaa…. Hamisaaaa… usife Hamisa… usife kabla hujazungumza nami Hamisa… usife Hamisaaaa….” Nilibaki kuugulia nikiwa pale chini wakati Dulla akipiga mayowe kuita msaada kama utapatikana karibu. Vijana watatu waliokuwa machungani walifika eneo lile, kila mmoja akiwa na wazo la kum,peleka Hamisa hospitali ya wilayani… lakini tunaondoka vipi na hakuna hata mmoja aliyekuwa anajua kuendesha gari. Yule kijana aliyefika pale na Hamisa naye hakujua lolote lile. Alikuwa ni mwanakijiji tu aliyemuelekeza Hamisa mahali nilipokuwa napatikana. Mshikemshike, usafiri upo lakini hakuna ajuaye kuendesha.
Wakati mshikemshike huu ukichukua hatamu… Hamisa alizidi kurusharusha miguu na wakati huuu mikono yake ikipiga huku na kule kwa taabu. Hamisa wangu alikuwa katika maumivu makali haswa!! Huenda kushinda maumivu yangu niliyokuwa napitia. Damu ziliendelea kumtoka na alizidi kugalagala…… Watu walizidi kuongezeka na hatimaye wakafika wanawake wawili!! Amakweli ya wanawake waachie wanawake, mara moja wakatambua kuwa Hamisa alikuwa akiugulia uchungu…
“Kamwite bibi Nyagina upesi” mwanamke mmoja alimuamuru mwanakijiji mwenzetu, akatii amri na kuchomoka mara moja. Wao wakamzunguka Hamisa na kuanza kumdhiti asijijeruhi kwa kujirusha huku na kule. Baada ya nusu saa alifika huyo bibi mtu mzima. Bibi ambaye hatafutika katika historia ya maisha yangu hadi leo ninaposimulia kisa hiki. Japokuwa jitihada zake hazikuzaa matunda mema na ya kuvutia lakini alinionyesha dhahiri wanadamu wanaojali uchungu wa wenzao bado wanaishi chini ya jua. Alifanya kila awezalo, aliomba kila dua wakati akipigania jambo hili lakini ikawa ni kisicho ridhiki hakiliki hata kwa asali. Hamisa akajifungua mtoto wa kiume ambaye hakuwa ametimiza miezi tisa tumboni… lakini bahati mbaya iliyoje yule mtoto alikuwa mfu tayari.
****

TAJI LA MIIBA!!!
TUKIO la Hamisa kujifungulia nyumbani kwetu lilibadili mambo mengi, ule mchakato wa mimi kutolewa kafara ukafifia, mama akarejea nyumbani na Hamisa akaishi nasi. Akanisimulia namna alivyotoroka nyumbani kwao. Simulizi yenye maumivu makali. Maumivu niliyodhani sasa yanakwisha lakini baada ya simulizi likafuata taji la miiba kichwani kwangu!!!

HAMISA ANASIMULIA.

PENDO la kweli halibadilishwi kwa vipindi vya mpito, nililiamini hilo baada ya yule baba niliyemuogopa tangu utotoni hadi usichana wangu alipokuwa kama sanamu tu mbele yangu. Ukorofi wake haukuwa mali kitu kwangu, si yeye wala mkewe aliyeiga tabia zake za ukorofi. Lilipojikita pendo lako katika moyo wangu likaibadili na akili yangu, uoga ukatoweka huku ushujaa ukichukua nafasi.
Mimba iliyojiunda ndani ya nyumba yangu ya uzazi ikanizidishia ari ya kukupenda wewe… apumzike kwa amani kiumbe yule. Nyota zake na heshima anayopewa na wafuasi wake kwangu haikuwa na nafasi tena, nilikuwa radhi anipige awezavyo lakini katu sio kubadili maamuzi yangu!! Baba yangu ni Inspekta wa polisi mkoa wa kipolisi wa Kinondoni jijini Dar es salaam, licha ya cheo kile bado ni mfuasi mzuri sana wa dini ya kiislamu na nd’o maana alipagawa nilipogundulika najihusisha na mwanaume wa kikristo. Lakini tulikubaliana mimi nawe, panapo penzi na udini ujitenge mbali nasi. Nilimwamini mama nikamweleza siri ile kuwa mimi ni mjamzito. Nilichoka G..nilichoka kulibana tumbo langu kila siku ili wasitambue kuwa mimi ni mjamzito sikutaka kumtesa mwanao zaidi ya nilivyokuwa nimemtesa tayari. Nikaamua kuwa muwazio kwa mama yangu. Kumbe nilikosea sana, mama hakuwa upande wangu na alikuwa amerithi tabia za yule inspekta wa polisi. Alininasa vibao kama vinne, nikahisi kizunguzungu kisha nikaanguka, baadaye hakuwa mama pekee bali alikuwa na yule inspekta wa polisi. Siku hiyo ilikuwa ya mwisho kabisa kutoka nje, kule chuoni wakatoa taarifa kuwa ninaumwa hivyo nikasimamisha masomo kwa muda. Walichukua simu yangu na kila kitu ambacho kingeniwezesha kuwasiliana na mtu wan je ya nyumba ile. Nikawa mtu wa kulia tu, na siku moja wakanipa maamuzi mawili magumu, kwamba aidha wakuue wewe halafu mimi nizae mtoto asiye na baba ama la nitoe mimba na wewe ubaki huru…. G ningeanza vipi kutoa mimba yako na ningeanza vipi kuruhusu wewe uuwawe. Tambua kuwa nakupenda hata nisiposema bado unajua. Nikawaeleza kuwa nitatoa mimba lakini sio harakaharaka kama wanavyotaka.. wakati huo nikijipanga ni kipi nifanye. Baada ya mkakati wangu kushindikana kabisa kimaamuzi, nikaamua kufanya maamuzi magumu kupindukia. Maamuzi ya kumkabili mlinzi na kutoroka, hiyo ilikuwa siku ya ijumaa wazazi wote walikuwa msikitini. Umri mkubwa wa mlinzi ulinipa upenyo wa kumsulubisha haswa hadi akaliachia geti, nikatoroka na kuja hospitali huku nikijiapiza kuwa kamwe sitarudi nyuma tena…. Nilipofika pale ukanieleza kuwa Joshua alikuja nyumbani kwetu ndipo nikarudi kumfuatilia maana nilijua tu akifika nyumbani atakabiliana na wakati mgumu sana kufuatia vurugu nilizokuwa nimefanya. Ni kweli sikufanikiwa kumwona lakini baadaye alikutwa amekufa huko Kinondoni makaburini…. Alaaniwe baba na mama yangu kwa damu ya Joshua waliyoimwaga…… Lilikuwa pigo Joshua kuuwawa, nikatambua vyema wazazi wangu ni wanyama wabaya…. Hawastahili kuitwa wanadamu. Nikaanguka na kuinuka tena, kama nimempoteza Joshua sikutakiwa kukupoteza wewe Gerlad. Nisamehe kwa haya yaliyotokea katika kipindi kirefu kiasi cha kupotezana nawe. Wazee wangu walizizuia akaunti zangu zote za benki, nilikuwa nimesimamisha mwaka chuoni hivyo sikuwa na jipya, na mbaya zaidi yakawekwa matangazo kuwa ninatafutwa popote nilipo sababu ikiwa kuwa nimetoroshwa na mwanaume. Nikaishi kama digidigi, nikaukosa uhuru wa nafsi na mwisho nikaamua kuisaka pesa. Na hapo nilipoomba radhi ni kwa sababu tu nilikusaliti mara moja… ilikuwa mara moja tu Gerlad na sitaki kuficha nalileta hili mbele yako, nalileta kwa sababu sitaki kuikosa amani moyoni mwangu… nd’o huyo mwanaume aliyenileta hadi morogoro na ndiye aliyeniruhusu kuondoka na gari lake kukufuata wewe huku. Nilipokuwa hospitali nilimpigia simu akalichukua gari lake na nilimweleza wazi kabisa kuwa mkataba wetu umekwisha….. niliyafanya yale ili niweze kukutana nawe tena tuendelee na maisha yetu upya na ikiwezekana kutafuta mtoto mwingine. Nakupenda Gerlad Masembo!!”
Hamisa alimaliza kusimulia, simulizi iliyoniletea joto, hasira na wakati mwingine baridi na neno la mwisho likaugandamiza vyema msumari katika hali ya amani nafsini. Hamisa akanikumbatia, nikayakumbuka mema yake na sikusita kumsamehe palepale.
Wakati nikitaraji kuwa ninaianza safari mpya kabisa na Hamisa kijijini kwetu, nikiita siku ile siku ya matumaini lakini haikuwa vile…. Ukawa usiku wa kulipoteza tumaini tena.. na safari hii nikavikwa taji la miiba kichwani!!!
Nililala Hamisa akiwa pembeni yangu alinikumbatia na kunipapasa mara kwa mara aliniambia maneno ya kimahaba, mazito na ya kupendeza. Lakini nikaigundua tofauti iliyoibuka katika mwili wangu!!
Sikuwa na hisia zozote, sikuwa nakaribia hata kwenye hisia….. Na hapo nikayakumbuka maneno aliyowahi nkunieleza daktari nilipokuwa muhimbili…. Ya kwamnba dalili zinaonyesha kuwa kadri wadudu wanavyozidi kunishambulia basi wqanaweza kunidhuru maungo yangu ya uzazi na ninaweza kupoteza ile hali ya kuwa mwanaume ninapokuwa na mwanamke. “Ina maana nimekuwa hanithi!!!!!” nilijiuliza huku mapigo ya moyo yakinienda mbio sana!!! Hamisa hakujua nini kinapita kichwani mwangu aliendelea kunipapasa pasi na mafanikio. Taji la miiba kichwani kwangu!!
JIFUNZE!!
UKIPENDACHO KITUNZE!! Usitetereshwe na wanadamu katika kutii matakwa ya moyo wako, maana jeraha la moyo halina tiba mbadala zaidi ya maamuzi yako binafsi!!

ITAENDELEA

Post a Comment

0 Comments