ILIPOISHIA: "Ngoja kwanza tumuhudumie shemeji." Gift alipewa huduma ya kwanza na kurudiwa na fahamu, alipopata fahamu aliangua kilio cha sauti ya juu. "Oooh maskini mama yangu...kwa nini umechukua uamuzi huo, japo kila baya malipo yake ni mabaya…mama hukutakiwa kujihukumu." SASA ENDELEA…
Kauli ile ilimshtua daktari na kulaumu wauguzi kwa kushindwa kumficha Gift na kumweleza ukweli bila kujua ni hatari unaweza kumuua mtu hata mwenye hali ya ujauzito. "Kwani Mr Tell me, wauguzi wakati mnaingia waliwaambia nini?" "Hawakutuambia kitu zaidi ya muuguzi mmoja kumletea barua mke wangu ambayo aliisoma na kukutwa yaliyomkuta." "Sasa hizi habari kazitoa wapi?" "Habari gani daktari?" "Ya hali ya mama yake." "Kwani mama mkwe amefanya nini?" "Hali yake sio nzuri." "Atiii...ina maana ni ule mshtuko tu?" "Hapana." "Sasa ni nini?" "Alifanya jaribio la kujiua." "Kujiua! Kwa sababu gani?" "Kwa kweli mimi sijui lazima mtajua ninyi wahusika." "Kwani kwenye barua kumeandikwa nini?" "Muulize mkeo?" "Eti mpenzi barua imeandikwa nini?" "Ni aibu ni aibu nilidhani nimeepuka kumbe aibu imenifuata ndani, eeeh Mungu mbona umetuumbua hivyo?" Tell me aliichukua ili barua iliyokuwa bado ipo chini na kuanza kuisoma. Aliisoma kijasho kikimtoka mpaka mwisho alishusha pumzi nzito. Alimuangalia daktari Eliud kama mgeni kwake au ndio siku yake ya kwanza kumuona kisha aliamisha macho yake hadi kwenye uso wa Malon ambaye alikuwa aliendelea kulia kwa sauti ya kwikwi. Alimalizia kwa kumwangalia Gift ambaye alikuwa amekaa chini mikono kichwani. Daktari Eliud alikuwa na maswali mazito kichwani mwake kutaka kujua ile barua ina siri gani. Wakati huo Tell me machozi yalikuwa yameweka mfereji kwenye mashavu yake. Kwa sauti ya chini Tell me aliuliza: "Daktari mama mkwe ni mzima au?" "Kwa kweli hali yake ni mbaya sana, lakini kila kitu tunamuachia mwenyezi Mungu...Mpaka sasa unapumulia mashine." "Mmmh shughuli ipo...kuna matumaini ya kupona?" "Siwezi kusema lolote kwa sasa hivi, kwa vile tukio lina saa moja toka litokee hivyo tunajitahidi kadri ya uwezo wetu. Tena Mungu mkubwa kama angetumia kamba sasa hivi tungekuwa tunaongea mengine." "Sasa unatuambiaje daktari?" "Sina la kuwaambia la muhimu rudini nyumbani na kumuombea dua mgonjwa nina imani dua ndio pekee inayohitajika kipindi kama hiki." Tell me alimnyanyua mkewe aliyekuwa amekaa chini. "Gift hebu jikaze kumbuka kuna mdogo wako anahitaji ukaribu wako kipindi hiki mama yupo kwenye wakati mgumu." Gift alinyanyuka na kumkumbatia mdogo wake na kuongozana wote kutoka nje. Walikwenda hadi kwenye gari lao na kurudi nyumbani, walipofika nyumbani Gift alikuwa na maswali mengi kichwani mwake juu ya mdogo wake Malon atamwita vipi Tell me. "Mume wangu haya ni maajabu ya Mungu, sijui hata huyu mdogo wangu atakuita vipi, baba au shemeji na mimi sijui ataniita mama au dada?" "Sikiliza mke wangu, hili jambo halikuwa la makusudi bali bahati mbaya la muhimu naomba hili libakie siri kwetu, Malon japo ni mwanangu ataendelea kuniita shemeji na wewe ataendelea kukuita dada." "Haya kwetu, na kwa mama kama Mungu atamjalia kupona?" "Kama nilivyosema hii ni aibu yetu iliyo ndani hakuna anayejua labda tuitoe nje sisi wenyewe." "Mmh hayaa." Mama Gift alirudiwa na fahamu baada ya siku tatu na kuweza kula hata kuongea. Daktari ambaye na yeye alikuwa hajui lolote alikuwa makini kuhakikisha mama Gift haonani na familia yake mpaka hali yake itakapo tulia. Wiki moja alikuwa hajambo kabisa na kuweza kukaa peke yake lakini tokea afanye tukio lile amekuwa kwenye ulinzi mkali. Baada ya kulizika na hali ya mgonjwa, daktari Eliud aliiruhusu familia yake ionane na mgojwa ambaye wakati wowote angeruhusiwa kutoka hospitali. Gift aliamua kwenda peke yake hospitali kwa mama yake, mama yake alipomuona alijikuta akibubujikwa na machozi huku akisema: "Gift mwanangu nisamehe kauli yako imetimia." "Mama yaliyopita yamepita japo yanauma la muhimu tujipange upya." "Una maana gani?" "Mama haya yaliyotokea niliyaogopa, ndiyo maana nilikimbilia kuolewa kumbe nilipokimbilia sipo, lakini najua hii ni hukumu inayomkuta mwanadamu aliye hai kabla ya kufa." "Ni kweli mwanangu, mbona najuta sioni faida ya kuendelea kuwepo dunia tutatazamanaje?" "Mama ni makosa kujihukumu, kila mwanadamu atahukumiwa kwa makosa yake, la muhimu ungetafuta suruhu na muumba wako kuliko kukimbila kujiua. Hebu ona, Mungu kama hataki ufe hata ikimezwa na papa utatoka ukiwa hai." "Unafikiri nitaiweka wapi sura yangu?" "Mama hili tumeishaliongea na mume wangu na kulipatia ufumbuzi." "Ufumbuzi gani huo?" "Hii itabakia siri ya familia tena ya watu watatu mimi wewe na mkweo." "Tutaitanaje?" "Kwa vile ilikuwa bahati mbaya tutaitana kama tulivyokuwa tukiitana." "Malon atamwitaje mumeo?" " Nimekueleza tutaendelea kuitana hivyohivyo, atendelea kumwita shemeji ikiwezekana siri hii asiijue Malon mpa mwisho wa maisha yake." "Mmh! Itawezekana?" "Ni uamuzi kila kitu mkiamua kinawezekana." "Haya huyo mumeo tutaangalia vipi?" "Mama huo ni wasiwasi wako, tukio hili ni la bahati mbaya hakuna aliyetalajia, ila nakuomba kitu kimoja tena hili nakuomba sio ombi bali ni amri," Gift alisema kwa sauti mkavu. "Kipi tena hicho, mbona unanitisha?" "Nakuomba ili tukio hili lisipate nafasi wala kuila akili yako ni wewe kurudi kwa baba kumuomba msamaha ili mrudiane." "Mwanangu naona kama ngamia kupita kwenye tundu la sindano." "Kwa nini?" "Sidhani kama baba yako atanielewa?" "Mama ni mimi ndiye nitakaye kuwa kiunganisho chenu, niamini muombe msamaha wa kweli hakika baba atakusamehe." "Nitafanya hivyo mwanangu, sina jinsi mkubwa numevukwa na nguo hadharani sina budi kuchutama." Siku ya pili mama Gift alitoka hospitali akiwa mzima wa afya njema, muda wote Gift aliutumia kuwa karibu ya mama yake kuhakikisha achukui uamuzi mbaya ambao hapendi kuuona tena. Baada ya wiki mama Gift aliongozana na mwanaye Gift hadi kwa baba yake Tabata Kisukuru. Walimkuta baba yake akiwa anatengeneza gari lake lililokuwa limeharibika alipowaona aliwakaribisha, lakini moyoni akijiuliza mtalaka wake umekosea njia mpaka kufika pale kwake. Baada ya kutengana hapakuwa na mawasiliano zaidi ya miaka saba. "Karibuni." "Asante." Walijibu kwa pamoja. "Shikamoo baba." "Marahaba mumeo hajambo?" "Hajambo anakusalimia." "Shikamoo baba Gift," mama Gift alimuakia mumewe wa zamani. "Marahaba mama Gift karibu." "Asante." Aliwaacha wageni watangulie ndani na yeye kutoa maelekezo ya mwisho kwa mafundi, kisha na yeye aliwafuata ndani huku ajifuta mikono kwa tambala kutoa gilisi iliyokuwa mikononi baada ya kulizika na usafi wa mikono yake alilitupa lile tambala na kuingia ndani.
Siku ya pili mama Gift alitoka hospitali akiwa mzima wa afya njema, muda wote Gift aliutumia kuwa karibu ya mama yake kuhakikisha achukui uamuzi mbaya ambao hapendi kuuona tena. Baada ya wiki mama Gift aliongozana na mwanaye Gift hadi kwa baba yake Tabata Kisukuru. Walimkuta baba yake akiwa anatengeneza gari lake lililokuwa limeharibika alipowaona aliwakaribisha, lakini moyoni akijiuliza mtalaka wake umekosea njia mpaka kufika pale kwake. Baada ya kutengana hapakuwa na mawasiliano zaidi ya miaka saba. "Karibuni." "Asante." Walijibu kwa pamoja. "Shikamoo baba." "Marahaba mumeo hajambo?" "Hajambo anakusalimia." "Shikamoo baba Gift," mama Gift alimuakia mumewe wa zamani. "Marahaba mama Gift karibu." "Asante." Aliwaacha wageni watangulie ndani na yeye kutoa maelekezo ya mwisho kwa mafundi, kisha na yeye aliwafuata ndani huku ajifuta mikono kwa tambala kutoa gilisi iliyokuwa mikononi baada ya kulizika na usafi wa mikono yake alilitupa lile tambala na kuingia ndani. Aliwakuta wakiwa sebuleni wamekaa kwenye makochi alipofika alikaa mbali nao na kuwa wakitazamana. "Haya wageni karibuni." "Asante." "Baba huu mguu ni wako." "Mwanangu mguu ungekuwa wangu usingekuwa nao?" baba yake kama kawaida alimtania mwanaye. "Baba Gift hujaacha masihara yako,"mama Gift alisema huku kila mmoja akicheka. "Haya mama hebu nipe huo mguu wangu?" "Baba kwanza napenda kukuomba samahani kujibebesha madaraka mazito ambayo hayalingani na uwezo wangu wala umri wangu. Lakini ina imani busara si umri wa mtu bali maneno hutamkayo." "Sawa kabisa mwanangu," baba Gift alikubali. "Baba mimi ni mtoto wa watu wawili yaani wewe baba na mama, bila mmoja wenu mimi nisinge kuwepo sijui nipo sawa?" "Sawa kabisa mwanangu," baba Gift alijibu. "Basi siku zote tangu baba na mama mtengane nimekuwa kiumbe kilichopungukia kitu fulani maishani mwangu ambacho hakionekani kwa macho, kitu ambacho kimenighalimu siku zote. “Kila kukicha nilimuomba Mungu ili aweze kusikiliza dua zangu ili siku moja wazazi wangu mrudiane na muishi kama zamani na kutenganishwa na kifo, kama ndoa yenu ilivyofungwa mbinguni itakayotenganishwa na kifo. “Siku zote shetani hutumia udhaifu uliopo kwenye maisha ya wanadamu kuhakikisha anaharibu kila kitu. Nina imani aliweza kufanikiwa azima yake lakini uwezo wake haushindani na nguvu za Mungu. “Leo hii kwa uwezo wa Mungu naomba wazazi wangu muijenge upya ndoa iliyojengwa na Mungu, Baba." "Naam mwanangu." "Naomba uziheshimu juhudi zangu nilizozifanya usiku na mchana, uyaheshimu mapenzi yangu kwako, unilindie heshima yangu kwako na kuhakikisha baada ya kunipa idhini ya kuolewa naomba unipatie kilicho baki. “Si kingine ni furaha ya milele ili niliapo basi nibembelezwe na wazazi wangu wote wawili nakuomba nipo chini ya miguu yako nakuomba kwa uwezo wa Mungu umsamehe mama kwa yote aliyotenda. Siku zote Mungu humpenda yule awae tayari kusamehe, aliyekosea hata bwana wetu Yesu Kristo alitufundisha tusamehe saba mara sabini. Najua baba dini umeishika sina shaka na hilo, naomba umrudie mama." Gitf aliyazungumza yale huku akilia. Yalikuwa maneno mazito yaliyomtoa machozi kila mmoja aliyekuwepo pale. Lilikuwa pigo mujarabu kwenye moyo wa wa Mzee Bilikila ambalo lilifanya akose la kusema, kwenye ubinadamu mwanaye kamaliza kwenye dini kamaliza hata kwenye malezi. Akiwa ametulia huku machozi yakimtoka mzee Bilikila aliwaza mengi huku akiamini siku zote busara si umri bali maneno ya mtu. Hakuamini maishani mwake kama wanaye tena wa kike ataweka kuongea maneno mazito kama yale. Akiwa bado ameinama machozi yakimtoka mama Gift alitoka kwenye kochi na kutembea kwa magoti kwenda kumuomba msamaha mumewe. "Baba Gift naomba unisamehe mume wangu maneno aliyoongea mtoto ni mazito, najua nimefanya kosa tena kubwa nahitaji msamaha, siku zote ng'ombe akivunjika mguu hurudi zizini," mama Gift aligaagaa chini huku akilia. Mzee Bilikila hakujibu kitu machozi yaliendelea kumtoka kama maji na kamasi nyembamba nazo ziliendelea kumwagika. Gift aliongezeka kumuangukia baba yake. "Baba wewe ndiye nguzo ya familia, siku zote haiyumbi, baba wewe sawa na chini kila kirukacho hutua chini mpokee mama." Mzee Bilikila aliwanyanyua wote na kuwakumbatia kuonyesha amekubali kumsamehe mkewe. Walikubaliana kumaliza tofauti zao na mama Gift alirudi rasmi kwa mumewe huku wakiendelea kuichicha siri ya mtoto Malon. Naye Tell me aliendelea kumpenda mkewe na kumheshimu mama mkwe kama mkwewe. Wakiwa wamekaa siku moja Gift na mama yake wakiongea mama yake alimshukuru mwanaye kwa kazi nzito aliyoifanya kurudisha upendo kwenye familia naye Gift alimweleza mama yake kuwa siku zote mwanadamu unapofanya kosa usikimbilie kujihukumu bali kilio chako mkimbizie mwenyezi Mungu kwani ndiye mwenye uwezo wa kusamehe peke yake. Mwisho tuziheshimu ndoa zetu tuvumiliane wakati wote wa shida na raha wakati wa furaha na majonzi na wakati wa uzima na ugonjwa. Mungu azipe nguvu ndoa zote. Na siku zote kutenda kosa ni kosa ila kurudia kosa ni kudhamilia.
0 Comments