“Tukija kwenye swala lako, ni kwamba ameniambia siku nyingi habari zako na jinsi ulivyo hodari, mpole na mzuri wa kila kitu.Pia akaniambia kama yupo mume ambaye angenifaa anioe basi ni wewe…na akaahidi kukuleta na kutukutanisha...” Wakati aliponitajia haja yake kuomba nimsitiri kwa kumuacha atuangalie wakati tumo ndani ya kufanya mapenzi leo, wakati ule mlipokuja, na mimi na yeye tukaingia ndani. Dhana yangu ilikiwa ni kwamba labda na wewe pia amekwisha kukuambia. Hiyo ndio hali halisi ya mimi na mzee Subeti, sina cha kumpa zaidi ya kumsitiri udhaifu wake alio nao kama alivyoomba." Nilimkumbatia Huba baada ya maelezo yake hayo na kumuahidi kuwa tutamsitiri pamoja mzee Subeti, kwa sababu kusema kweli licha ya kuwa na mimi pia mzee huyo alinisaidia sana, lakini pia nilikuwa tayari nimo mapenzini na Huba, niliona wachilia mbali, liwalo na liwe. Kama mzee anafarijika kutuona wajukuu tukicheza huku akituangalia wacha atuangalie. “Tulikaa Tanga kwa zaidi ya wiki mbili, na katika siku hizo, Huba alionesha kila aina ya mapenzi kwa kunienzi, kunijali na kunibembeleza. Aina ya vyakula ambavyo sijawahi kuvila nilivila kwa Huba. Nilikuwa naogeshwa kama motto mchanga na yeye mwenyewe alizidi kujiweka katika hali ya usafi na urembo wa asili wa kuvutia. Niliyafurahia mno maisha katika kipindi hicho, kwa hiyo sikujali kumsaidia mtu aliyenifanya nifurahi hivyo kwa jambo nililoliona mimi na mpenzi wangu Huba kuwa sio kubwa sana. Kwa hiyo tuliendelea, kila baada ya siku moja Mzee Subeti alikuwa anakuja kushuhudia.Tulizowea tukawa tunacheza mbele yake kwa fujo na vikumbo bila kujali kama tunaangaliwa.Sasa siku moja majira ya saa tatu usiku tulikuwa tayari tumeshamaliza shughuli zetu lakini mzee bado yupo hajaondoka. Mara tulisikia mlango wa mbele unagongwa kwa nguvu na vishindo kiasi tulipasukwa na mioyo. Haraka niliendea nguo zangu za ndani na suruali nikavaa na nikamrushia Huba gauni lake la kulalia. Vishindo vilizidi, mzee Subeti akatuambia tutulie tumuache aende yeye akafungue. Alikwenda kufungua na kwa vishindo waliingia wavulana watatu wa haja, wakaanza kumzogoma kwa maneno hapo sebleni…” "Leo tumekufuma. Mzee wewe hasidi ni lazima utaipata!" Mmoja wao alisikika akisema kwa sauti ya juu yakujinaki. Mwingine aliuliza kwa pupa, "Yuko wapi huyo hayawani mwenzio...pumbavu yake, amemroga kaka yetu afe ili apate nafasi ya kutembea na wewe, eenh? Basi leo mtaipata wewe mzee ovyo sana wewe! Mambo mabaya yote unayo wewe!" Mzee Subeti naye alisikika akisema kwa sauti isiyo na hamaki. "Lakini vijana ni kwa nini hamtaki kumuacha Huba awe huru na kuendesha maisha yake mwenyewe? Ni miaka miwili sasa tangu binti huyu afiwe na mume wake, mumemnyang'anya kila kitu pamoja na mtoto wake sasa hata uhuru wake pia mnataka kuuchukua?" Mwingine alisikika akisema kwa sauti ya kilevi levi kidogo, "Wacha wee mzee usijidai mwanafalsafa ukatumwagia busara zako unazozielewa mwenyewe! Leo siku yenu imefika...au sio? Mbweha nyie kasoro mikia!" Bado Mzee Subeti alisikika kuja chini kwa sauti kila wale jamaa walipokuja juu, aliwauliza kwa taratibu, "Kwani nyinyi mnataka nini?" Sauti ya yule wa kwanza ilisikika ikisema kwa kufoka, "Tunataka nini?" Unatuuliza tunataka nini? Sisi bwana tuna usongo naye huyu binti pamoja na wewe hawara yake! Mmeshirikiana kumroga kaka yetu ili muwe pamoja…" “Wakati wote sisi, yaani mimi na Huba tulikuwa bado tupo chumbani, ilipofikia hapo, baada ya kusikia maneno hayo ya mwisho Huba aliniambia, "Wewe baki humu humu ndani,na kwa lolote litakalotokea usiseme kuwa Mzee Subeti ana udhaifu wa kuangalia watu wakifanya mapenzi, tafadhali na kuomba. Wacha wafikirie kuwa mimi ni hawara yake!" Baada ya kusema hivyo alitoka chumbani na kuniacha mimi peke yangu, akaenda kule sebleni. “Nilisikia sauti ya mmoja wao ikisema mara baada ya kumuona Huba, "Enhe, umejitokeza wewe firauni, eenh?" Nilimsikia Huba akapandisha sauti kwa hamaki na kuanza kuwashutumu jamaa hao kwa jinsi wanavyojaribu kumnyanyasa katika maisha yake, aliwatishia kwa kuwaambia ni lazima awapeleke mbele ya sheria iwapo wangeendelea kumfuata fuata. Ghafla nilisikia sauti ya Huba ikilalamika kama vile alishikwa kwa nguvu huku Mzee Subeti naye akilalama na kusema "Hamuwezi kufanya hivyo! Ni udhalilishaji huo!" Mmoja wao aliendelea kusema "Ni lazima tuwafanyizie, ili mkome ujinga wenu!" Hapo hapo sikujizuia tena. Nilitoka chumbani nikiwa nimepandwa na hasira, nilipofika sebleni, nilimkuta mmoja wao amemshika Huba kwa kuibana mikono yake nyuma na wawili wamemtia kabari Mzee Subeti huku wakijaribu kumvua nguo zake, sikujua kusudio lao. Waliponiona waligutuka kidogo, lakini mimi sikuhitaji maelezo zaidi ya yale niliyokwisha yasikia. Kwa hiyo kama cChui aliejeruhiwa, niliwapa jamaa hao kipigo ambacho hawakukitegemea. Pamoja ya kuwa walikuwa watatu, lakini walikuwa wepesi kwangu. Niliwapiga vibaya sana hasa pale nilipowatoa uani na kuhakikisha kuwa hakuna chombo cha Bi. Huba kitakachoharibika. Kila walipoonekana kutaka kunizidi, nilipata msaada kutoka kwa Bi. Huba kwa kuwachapa kwa gongo alilolipata hapo uani. Mmoja wao nilimpiga kichwa kizito na kusababisha kudondosha meno na damu kumtapakaa usoni. “Mwishowe walipoona vita ni nzito walitoka wakakimbia. Tulirudi chumbani, mimi nikaingia bafuni na kuoga, kisha nikamuambia Mzee Subeti, kwa usalama wake ni vyema wakaondoka mji ule. Lakini siku ya pili nililetewa askari waliokuja kunikamata nami, Mzee Subeti na Huba tukafunguliwa mashitaka ya kuwapiga wale jamaa na kuwasababishia maumivu makali. Kwa hiyi hatukuweza tena kuuhama mji ule mpaka kesi ile iishe. “Kesi ilidumu kwa wiki tatu, lakini mwishowe, sote watatu, yaani mimi, Huba na Mzee Subeti tukaachiwa huru kwani ilikuwa wazi kuwa ni wale jamaa ndio waliokuja kufanya fujo nyumbani kwa Huba, nasi mimi na Subeti tukiwa ni wageni wae pale nyumbani, tulijitahidi kumtetea na kujitetea pale jamaa wale walioanza kutupiga. Ile kesi iliisha mheshimiwa hakimu…na ndio hiyo hadithi ya Dulla na Huba, kutoka Tanga, na ni jinsi gani nililipata hilo jina la Dulla ndani ya mkoa huo!” Dallas alimaliza maelezo yake na kumtulizia macho Amani. Amani aliinuka na kuonesha ishara ya kutaka kuongea, lakini Hakimu alimuashiria akae, naye akatii. “Nashauri wakili mtetezi uweke hoja zako mpaka tutakapokutana tena kuendelea na kesi hii, maana leo muda umekwenda sana. Kesi hii itasikilizwa tena baada ya wiki moja…” Hakimu alisema, na kumgeukia Dallas, “…na ningependa sana huo ushahidi wako ufikie tamati siku hiyo tutakapokuja tena kwenye kesi hii ili tuweze kwenda mbele…namaanisha ufupishe masimulizi ili tufikie kwenye hoja!” Dallas aliinama kuonesha heshima kwa mahakama. “Ahsante sana mheshimiwa Hakimu…kwa hapa nilipofikia, kilichobaki ni kuielezea mahakama yako adhimu ni jinsi gani, baada ya mimi kuwa Dulla kule Tanga, nikaja kuwa Dallas hapa Dar…na ikawaje nikakutana na marehemu Mwanamtama!” Dallas alisema kwa upole sana, kisha akabaki akimtazama Amani kutokea pale kizimbani alipokuwa amesimama. Hakimu atangaza tena kuwa kesi ilikuwa imeashirishwa mpaka baada ya wiki moja. ***** Walitoka nje ya mahakama, na wakati Amani anaelekea pale kwa Mzee Majaliwa, alikutana na Dallas akitoka nje ya mahakama ile. “Usiwe na wasiwasi wakili Mani, kesi yako inaelekea kuzuri…nadhani unastahili ushindi kwenye hili ila inabidi usikie upande wangu kwanza…!” Dallas alimwambia, na Amani alimuangalia kwa mshangao mkubwa, kwa sababu ya mabadiliko ya Dallas ya mara moja hiyo kutaka upande unaoutetea Amani ushinde, pili kwa yeye Dallas kumuita Amani kwa jina Mani. "Mani?!!" Amani alitamka mshangao wake kwa hili la pili kwa kuuliza. Dallas alimwangalia kwa sura ya upendo na huruma, na kumjibu: "Ndio...Mani! Jina lako linawezekana kubadilishwa kwa wanavyopenda kukuita wakuitao. Mimi jina langu ni Abdallah lakini nimeitwa Abdul, Abdi, Dulla na sasa Dallas, basi na wewe pia ndungu yangu, inawezekana jina lako likawa ni Amani, lakini ukaitwa Mani, Rahmani au Abdulrahman...kutokana na mazingira ya maisha unayoishi...kwaheri…Mani.” Dallas aliondoka haraka haraka na kumuacha Amani akiwa kinywa wazi. Baada ya Dallas kuondoka Amani alijivuta pole pole kuelekea alipokuwa mzee Majaliwa. Alimkuta yule mzee bado amekaa palepale akiwa anaonekana mwenye mawazo mengi sana. "Samahani mzee, siku yako ya leo tumeipoteza bure, shahidi aliyekuwa bado anaendelea kutoa ushahidi wake, kama ulivyomsikia, alikuwa na hadithi nyingi za kusema, na bado hajamaliza. Na wewe tunakuhitaji uwepo mahakamani kila wakati kesi hii inaposikilizwa mpaka utakapotoa ushahidi wako...sasa sijui itakuwaje?" Alimwambia yule mzee. Mzee Majaliwa akiwa bado yumo kwenye mawazo, alimuuliza Amani kwa sauti ya chini: "Kwani wewe bwana mdogo wasiwasi wako ni nini?" "Wasiwasi wangu mzee ni kuwa tunakupotezea wakati wako!" "Kwa hilo usitie hofu kwani mimi niko tayari kufika hapa wakati wowote ninapohitajika mpaka hapo nitakapotakiwa nitoe ushahidi. Ondoa shaka kijana, nitafanya lolote lile ambalo ni la msaada kwa Dokta lmu. Nitafika tena siku ya kesi na wala hakuna ninachopoteza kwa kufika kwangu hapa!” Baada ya hapo Amani na Mzee Majaliwa waliungana na ndugu na jamaa wengine wakaenda kumsalimia Dokta lmu ambaye kwa umbile alikuwa amepoteza uzito kidogo. Kisha Amani alimrudisha Mzee Majaliwa msikitini kwake anakoishi.
****** Wiki ilikatika kama mchezo,ndani ya wiki hiyo Amani alikwenda kumchukua mama •yake Dokta Imu na kumpeleka mahabusu kukutana na mwanaye. Vile vile alikutana na mzee Musa na Jabir na kumjadili Dallas kwa kirefu sana na kwa pamoja walifikia uamuzi kuwa mtu huyo haeleweki. Hata hivyo Amani alisema wangoje waje wamsikilize hicho kisa chake cha Dallas wa Dar es Salaam, kwani hicho ndicho hasa kitakacho husika na kesi yao. Siku hiyo ilifika na kama kawaida wakati ulipofika wa kusikilizwa kesi ya Dokta lmu, Dallas aliitwa kizimbani na kuendelea na kutoa ushahidi wake. Dallas alisimama na kuonekana kuwa hana wasiwasi kabisa. Alianza kwa kusema, mara baada ya kuruhusiwa kufanya hivyo: "Mheshimiwa Hakimu, kabla sijaanza kuielezea mahakama yako tukufu kisa cha Dallas na marehemu Mwanamtama, nataka nirudi nyuma kidogo kwa Dulla na Huba…Baada ya kesi ya Huba kumalizika na kushinda, urafiki wetu mimi na Bi. Huba ulizidi kushamiri. Kwa hakika mwanamke yule nilimpenda mno,naye alionesha dalili zote na vitendo vyote vya kunipenda, na kubwa zaidi aliniomba tuoane. Nami pia kwa wakati huo nilikuwa niko tayari kumuoa,isipokuwa jambo moja lilinitia mushkeli mkubwa moyoni mwangu,nalo ni lile la kufanywa sinema na mzee Subeti. Sikuliona gumu jambo hilo kwa wakati huo kwa sababu mbili, kwanza nilikuwa nampenda mno Huba, pili nilikuwa sipendi kabisa kumuudhi mzee Subeti aliyekuwa mfadhili wangu wa kila kitu pamoja na kunikutanisha na huyo Huba. Ilikuwa ni rahisi kumkubalia mzee Subeti kila wakati anapojisikia kufanya hivyo yaani kutukutanisha mimi na Huba atukutanishe, kwa vile pia Huba hakuwa mke wangu wa ndoa. Nisingeweza kukubali hilo kama mimi na Huba tungekuwa mume na mke wa ndoa. “Sasa je, tukioana itakuwa vipi? Mzee Subeti atatutaka tuendelee na mpango huo? Shaka yangu ilinifanya nisite kukubali kuoana na Huba. Nilimueleza ukweli wa hisia zangu na kumuomba tuvute subira kwanza wakati ninajiandaa kutafuta kazi sehemu nyingine. Huba alinikubalia. Wakati huo huo rafikiyangu Gevas naye aliachakazi kwa Mzee Subeti na kuhamia DaresSalaam. Nilikaa Arusha na Tanga kwa kwenda na kurudi kwa muda wa miezi kumi baada ya kuondoka Gevas, kisha na mimi niliamua kujiunga na rafiki zangu Gevas na Mabula hapa Dares Salaam. Na sababu mojawapo kubwa iliyonifanya nifanye hivyo ni kutaka niwe mbali na Mzee Subeti na nitafute njia ya kuwa karibu na Huba, mimi na yeye peke yetu.” “Lakini kupata kazi ndani ya jiji la Dar esSalaam haikuwa rahisi licha ya kupata sehemu ya kuishi. Kwa hiyo nilipata chumba Mbagara rangi tatu. Wenzangu Gevas na Mabula wao walikuwa wakiishi Temeke. Niliishi katika jiji hili kwa misaada ya akiba niliyokuwa nimejiwekea nilipokuwa Arusha nikifanya kazi. Akiba ilimalizika, hali ikaanza kuwa mbaya kimaisha. Siku za kwanza nilikuwa nikipata nafasi ninakwenda Tanga kukutana na Huba na kumpa matumaini ya kuwa anisubiri, lakini mwishowe nikawa hata senti za nauli sina. Niliishi kwa misaada toka kwa Gevas na Mabula, hasa Mabula sababu hata huyo Gevas mwenyewe alikuwa na kazi za kubabaisha tu, hakuwa na kazi maalum. “Jina la Dallas nimepewa na mtoto mdogo, mjukuu wa mwenye nyumba ninayoishi, ambaye alikuwa anaanza kusema. Kwa hiyo yeye watu wakiniita Abdallah, yeye huniita Dalla. Hivyo basi akawavuta watu wengi au wote pale nyumbani wakawa wananiita Dalla, ikaenda ikawa ni mtaa mzima na mwishowe mji mzima kwa kila anayenifahamu. Nami sikukinza, nilikubali moja kwa moja kuitwa kwa jina hilo la Dalla, ingawa wengi waliongezea mbwembwe na kujumlisha 's' mbele yake na nikawa ni Dallas, sikujali. “Katika hizi tabu za maisha ya Dar es Salaam zilizonikumba za kutokuwa na kazi maalum, ndipo siku moja Gevas aliponiambia: "Wewe Dallas…" sababu na yeye pia alivutwa na mvuto wa kuniita kwa jina hilo la Dallas. Aliendelea kusema: "Unao uwezo mkubwa na uzoefu pia wa kuzungumza mahakamani rafiki yangu, kutokana na kesi zako ulizokwishakabiliana nazo Mwanza, Arusha na Tanga. Kwa hiyo kuna kibarua ambacho kitalipa vizuri, na sisi tunahitaji pesa sasa hivi ili tuendelee kuishi mji huu, kwa nini usikichukue kibarua hicho?" “Mimi nilimuuliza Gevas kwa sauti ya chini na pole pole: "Ni kibarua gani hicho rafiki yangu Gevas?!" "Cha ushahidi kwa jambo utakalolishuhudia!" "Jambo hilo bila shaka litakuwa ni la kupangwa!" "Basi hapo ndipo ninapokuvulia kofia wewe mshikaji, tayari umekwisha tambua kuwa ni jambo la kupangwa, naamini kibarua hicho utakiweza, wewe una kipaji bwana!" Nilitulia nikamtazama Gevas kwa dakika kadhaa, kisha nikamwambia "Lakini unafahamu rafiki yangu Gevas kwamba kesi zote zilizowahi kunikabili zilikuwa sizitafuti bali zinakuja zenyewe? Sasa huu ushahidi wa kupangwa mimi nitaujua vipi? Na kwa nini iwe hivyo?" Gevas alicheka kidogo kisha akanimwagia falsafa zake kidogo kwa kusema: "Rafiki yangu Dallas maisha yana rangi tofauti ambazo zinaashiria raha, shida, amani, msiba, huzuni, hatari na ufahamu kuwa siku zote sio Jumapili. Sasa hivi sisi tunakabiliwa na shida, hatuna matumizi, hatuna kodi za kulipa wenye nyumba, sasa nafasi hii imekuja unataka tuiwache?" “Mimi nilitabasamu na kumfahamisha kwa maelezo zaidi: "Lakini bwana Gevas mimi pia ninayafahamu hayo, sio mtoto mdogo,na wala sijakataa hicho unachokiita kibarua, lakini ninauliza nipewe ufafanuzi zaidi. Pia nisingependa jambo lolote la kumsingizia mtu, kama ni ushahidi basi uwe wa kweli!" Gevas alinishika bega huku akisema kwa ishara za mkono na vidole vile vilivyokuwa huru: "Sikiliza Dallas, hii ni kesi ya kumtetea mtu. Yupo msichana ameonewa, na hivi sasa hali yake taabani, anaweza hata kukata roho sasa hivi. Kwa hiyo kinachotakiwa ni kumtia mbaroni huyo mhusika haraka iwezekanavyo." Miguno ikazagaa mahakamani, macho yakawatembea mashuhuda, Amani na Dulla wakatazamana bila kuelewa, wote mioyo ikiwapiga kutokea mahala walipokuwa. Wakili Mkuki naye alikunja uso na kumtazama shahidi wake kwa mashaka. Kule kizimbani Dallas alikuwa anaendelea na maelezo yake, “ Wakati huo ilikuwa ni saa kumi alasiri. Niliendelea kumuuliza Gevas: "Sasa nitamtia vipi mtu huyo muhusika mtegoni?" “Hapo ndipo nilipopewa historia yote ya Mwanamtama na Dokta lmu. Nilielezwa kuwa Mwanamtama ni girlfriend wa Dokta lmu, tena wa muda mrefu. Isipokuwa siku za karibuni Dokta lmu amepata msichana mwingine aitwaye Zainabu, na kwa hiyo hana tena wakati wa kukutana na Mwanamtama, ni yeye na Zainabu tu. Baya zaidi nililoelezwa ni kuwa tayari Mwanamtama alikuwa ana mimba ya Dokta lmu. Wakati Mwanamtama alipoonekana kuchachamaa kwa kumtishia Dokta lmu kwamba atakwenda kumshitaki, Dokta huyo alimlaghai Mwanamtama na kumshawishi aitoe mimba hiyo. Mwanamtama alipokubali, Dokta lmu aliamua kuifanya kazi yeye mwenyewe nyumbani kwa jamaa zake ambao hawapo hapa nchini wamesafiri kwenda Ulaya. “Niliambiwa kuwa Dokta huyo ameifanya shughuli hiyo ndivyo sivyo, na kuacha maagizo kuwa iwapo litatokea jambo lolote lisilo la kawaida, anaweza akajulishwa kwa njia ya simu, na namba zake za simu nikapewa. Vilevile, niliambiwa kwamba mimi niwe ni binamu yake Mwanamtama, na nikapewa wasifu wake pamoja na anuani na namba za simu zote za nyumbani kwao. Pia nikaelezwa muda gani Dokta lmu alipofanya shughuli hiyo na muda alipofika pale nyumbani asubuhi ya siku ile.Jambo nililosisitizwa ni la kumtia Dokta lmu mbaroni, sababu Mwanamtama hakuna tama ya kuishi…” Dokta Imu alitikisa kichwa kwa masikitiko wakati akisikia maelezo haya, ambayo Dallas alikuwa akiyaeleza bila ya wasi wasi wowote. “Nilipewa simu ya mkononi, nikapewa na anuani ya ldara ya Upelelezi Polisi. Nilipofika nyumbani mle baada ya kukubali kuifanya hiyo kazi, nilioneshwa vile vifaa alivyotumia Dokta lmu, na chumba allchokuwemo Mwanamtama. Llikuwa saa moja na nusu jioni. Aliyenipeleka alikuwa Gevas pamoja na kijana mmoja. Kilichofuata baada ya hapo, mahakama yako tukufu muheshimiwa imekwisha kisikia kutoka kwa mtuhumiwa, mimi mwenyewe na mashahidi wengine. Ninakiri kitu kimoja mheshimiwa hakimu, ambacho ninaomba mahakama yako tukufu inisamehe, nilibabaika na sikusema kweli pale niliposema kuwa Dokta lmu nilimuona kabla ya saa zile alizokuja usiku, hapana. Mara yangu ya kwanza kumuona ni wakati huo alipoingia usiku ule!” Dallas alipofika hapo alitulia na kumuangalia Amani. Mahakama iliduwaa. Hakimu alimuuliza: "Je, umemaliza kutoa maelezo yako sasa shahidi Dallas?” Ndipo Dallas alipogeuza shingo na kumuangalia Hakimu na kusema: "Mheshimiwa hakimu jingine ambalo ningependa kulisema ninaona halihusu kesi hii, pamoja na kuwa ningependa kulisema hapa hapa mahakamani…kwa hiyo ninaiomba mahakama yako iendelee isipokuwa hapo baadaye, au itakaponibidi niseme wakati wa kuhojiwa nitasema!" Dallas alirudisha uso wake kumuangalia Amani huku akitabasamu.
Amani aliomba aseme kuhusu Dallas na akaruhusiwa. Alianza kwa kusema: "Mheshimiwa hakimu, ni wazi kuwa katika maelezo yake ya mwisho aliyoiambia mahakama kuwa yeye kama Dallas wa Dares Salaam,ndipo kesi hii ilipolalia, na kama ndivyo hivyo basi moja kwa moja yeye huyu Dallas ndiye mhusika mkuu wa kifo cha Mwanamtama. Kwanza ni muongo jambo ambalo amekiri kuwa alidanganya mahakama kuhusu kumfahamu Dokta Imu, vilevile upo uongo mwingi tu alioleta mbele ya mahakama yako tukufu. Amekiri kuwa hamjui Mwanamtama, kubwa zaidi amekiri kuwa yeye ameingia kwenye ushahidi wakati wa mtego wa kumtia mbaroni Dokta lmu ambaye hamjui. “Ni dhahiri kuwa anaicheza shere mahakama pamoja na sheria zake kwa kusema uongo, kuipotezea wakati, na kusema hadithi za kutunga anavyotaka yeye. Mheshimiwa ninaiomba mahakama yako imtie hatiani kwa kosa la kifo cha Mwanamtama na vilevile kwa kuichezea mahakama kwa kutoa riwaya za maisha yake za uongo na kutoa ushahidi wa uongo!" Kabla Hakimu hajajibu wakili upande wa mashtaka bwana Zablon Mkuki alisimama na kuomba kusema, aliporuhusiwa alisema hivi: "Mheshimiwa Hakimu, tupo hapa kwa ajili ya kesi ya Dokta lmu inayomkabili kutokana na kujihusisha kwake kumtoa mimba Mwanamtama isivyopasa, wala isivyo sheria na kusababisha kifo cha msichana huyo. Nasikitika kusema kuwa wakili mtetezi ndugu Amani bado hajaweza kumtetea na kumtoa kutoka tuhuma hizo ambazo ni za kweli, isipokuwa amekazana kumtuhumu Dallas ambaye hahusiki kabisa. Hata kama Dallas katika kutoa ushahidi wake amesema uongo hapa na pale, lakini jambo hilo la kuwa muhusika wa kifo cha marehemu Mwanamtama linabaki palepale kuwa ni Dokta lmu. “Dallas ameeleza kuwa marehemu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Dokta lmu hata kama ameelezwa. Vile vile ameelezwa kuwa Dokta lmu alipata mpenzi mwingine aitwaye Zainabu, jambo ambalo ni kweli. Hapo hapo marehemu Mwanamtama alipata mimba, jambo ambalo ni kweli,marehemu alitolewa mimba kienyeji nje ya hospitali, jambo ambalo ni kweli. Tunataka ushahidi gani tena zaidi ya huo ambao unadhihirlsha wazi kuwa Dokta lmu anayo hatia? Muheshimiwa kutokana na ushahidi uliotolewa na kuthibitishwa na Dallas naiomba mahakama yako tukufu imtie hatiani Dokta lmu. Ahsante muheshimiwa!" Bwana Mkuki baada ya kusema haya alikaa. Amani naye alitoa tabasamu kubwa na kuomba aruhusiwe kuendelea kusema tena. Hakimu alitamka kwa kusema: "Unaweza kuendelea wakili Amani!" Amani alikwenda mbele ya Dallas ambaye naye alikuwa anamuangalia, waliangaliana kwa nukta chache kisha Amani akamuuliza . "Samahani bwana Dallas…naomba urudie kuieleza mahakama ni nani aliyekupa wewe kibarua hiki cha ushahidi na kumtia mbaroni Dokta Imu?" Dallas aliinama na kufikiria kidogo kisha akasema: "Nadhani...!" Kabla hajamaliza Amani alisema kwa sauti ya ukali. "Wacha kudhani, tupo mahakamani hapa na hatupo hapa kudhani! Sema lenye uhakika na ukweli!” “Aliyenipa kibarua hiki, mwenyewe hasa simjui, anayemjua ni rafiki yangu Gevas!" “Unaajiriwa kazi inayohusiana na sheria za serikali ya nchi pamoja na maisha ya mwananchi, unakubali bila hata kumjua anayekuajiri ni nani?" Dallas hakuwa na la kusema, alinyamaza tu. Amani aliendelea kumuuliza. "Naomba utueleze tena ni nani uliyekwenda naye katika nyumba aliyokuwemo marehemu Mwanamtama kabla hajafa? Nyumba iliyopo Upanga ambayo pia uliitumilia kama mtego wa kumtegea Dokta lmu kwa kosa lako wewe?" Dallas alionekana amekasirika kidogo, kwa hiyo alijibu kwa chuki kidogo. "Nimesema nimepelekwa na Gevas pamoja na kijana ambaye sikuweza kumfahamu jina lake. Jingine ni kuwa pamoja na kuwa ni kweli nyumba hiyo imetumika kama mtego wa kumtia mbaroni Dokta Imu, lakini mimi sina kabisa uhusiano na kifo cha Mwanamtama!" "Hata Dokta lmu pia hana uhusiano wowote ule na kifo cha Mwanamtama zaidi ya kushuhudia binti huyo akikata roho, kwa sababu tu wewe ulitaka iwe hivyo...kwa nini? Amani alimjia juu. Dallas alionekana kugwaya kidogo, akababaika na kusema kwa ghadhabu: "Nadhani nlmekwisha eleza kila kitu nilichotakiwa nieleze na zaidi. Sasa sijui ndugu yangu unataka nini tena kwangu?” "Ninachokitaka kwako ndugu Dallas ni kusema ukweli, uliosema wewe ni uongo mwingi tu. Sasa ninataka uiambie mahakama ukweli kuwa ni nani alihusika na kifo cha Mwanamtama? Yaani nani aliyemtoa mimba? Nani aliyempa mimba? Hebu kwa mara ya kwanza tangu ufike na kuhudhuria mahakama hii sema kweli, kweli tupu isiyo na uongo!" Kwa mastaajabu ya mahakama nzima, Dallas aliangua kicheko. Alicheka kwa sauti kubwa, alicheka huku akitikisa kichwa chake kushoto na kulia, kisha akatulia. Akamtazama Amani na kumuuliza kwa sauti ya chini: "Mani nikisema kweli utaniamini?" Amani aliitikia kwa kichwa huku akitabasamu kidogo. Dallas aligeuka akamtazama Hakimu. “ Muda mchache uliopita nilisema kuwa nina historia ya kuieleza mahakama hii lakini ni yangu binafsi. Haihusiani na kesi hii. Lakini nilikwambia endapo nitahojiwa na ikabidi niseme basi nitasema. Nimetakiwa niseme kweli na bwana Mani!" Alisema, kisha akamgeukia Amani, halafu kwa sauti ya taratibu akamwambia: "Ukweli wa kwanza ninaotaka kukueleza ni kuwa mtu anaweza akasema kweli na asiaminike kuwa amesema kweli. Hivi wewe Amani unaweza kuamini kuwa mimi na wewe tu watoto wa tumbo moja, baba mmoja, mama mmoja?” “What?” Amani alimaka, sanjari na miguno mingi iliyoibuka pale mahakamani kutoka kila kona, hata kwa wakili Mkuki pia. “Basi huo ndio ukweli hasa!" Dallas alimthibitishia huku akimtazama kwa macho yenye yakini.
Amani alimtazama Dallas huku akitikisa kichwa kusikitika. Alimgeukia hakimu na kumwambia: "Nasikitika kusema muheshimiwa kuwa mahakama imemruhusu mwendawazimu kuwa ni shahidi. Licha ya kuiambia mahakama yako tukufu porojo za uongo, sasa hivi bwana Dallas anajaribu kueleza habari za uendawazimu. Itakuwaje mimi na yeye tuwe ndugu wa baba mmoja na mama mmoja, wakati mimi nina baba yangu na mama yangu? Na yeye amejieleza tangu mwanzo hadi mwisho maisha yake ya Mwanza alikotokea mpaka akafika Dar es Salaam? Muheshimiwa, hii inadhihirisha ni jinsi gani bwana Dallas alivyo muongo na kwa hiyo ushahidi wake haufai." Dallas alitoa tabasamu kubwa huku naye akitikisa kichwa kisha akasema kumuelekea hakimu, "Mimi si mwendawazimu. Na yote niliyoieleza mahakama yako ni kweli tupu kwa upande wangu...lakini sishangai iwapo mtu yeyote anayenisikiliza ataniona ni mwendawazimu au muongo, sababu hali halisi ndivyo ionekanavyo kuwa mimi ni muongo." Alipofika hapo alitulia kidogo, akainamisha kichwa chake chini kwa sekunde kadhaa na aliponyanyua uso wake tena na kumungalia hakimu, macho yake yalikuwa yamejaa machozi ambayo hakuyapangusa bali aliyawacha yakatiririka juu ya mashavu yake, jambo ambalo liliwafanya watu wote pale mahakamani, akiwemo Amani, wawe makini kusikiliza alilotaka kulisema. "Muheshimiwa hakimu huyu wakili mtetezi bwana Amani, ni ndugu wa damu, baba mmoja, mama mmoja. Naomba nisikilizwe kwa nini nasema hivyo!” Alitulia kidogo akimuangalia Amani, kisha akaendelea kwa sauti ya masikitiko. "Niliieleza mahakama hii kuwa nilipofika Mwanza nikiwa nina umri wa miaka kumi na sita hivi, nilikuwa ninatokea kijijini, ila sikuwaambia ni kijiji gani na wala sikueleza ni jinsi gani wazazi wangu walifariki. Sasa ngoja nihadithie!" Alitulia kidogo akamuangalia Amani kwa kumtulizia macho. Halafu akasema: "Nilitokea Kijiji cha Gambosh wilayani Magu. Siku ambayo sitaisahau, siku ambayo ilibadilisha maisha yangu yakawa juu chini, chini juu, ni siku ambayo nilitoka kijijini pamoja na baba yangu wakati wa asubuhi tukaelekea Magu kwa ajili ya shughuli mbali mbali za baba yangu, lakini nia yangu mimi kubwa ilikuwa ni kufuata picha nilizopiga, mimi nikiwa na mdogo wangu katika studio iliyoko Magu. Baada ya shughuli za baba zilizompeleka huko mjini Magu kumalizika, tulipitia studio na nikachukua picha zangu mbili, nilizopiga nikiwa na mdogo wangu, moja nimembeba, nyingine nimemshika mkono na kuna ya tatu ambayo ni yake yeye peke yake. Picha hizo tulipigwa kijijini na mpiga picha anayetembea tembea vijijini kupiga watu picha, na alikuwa anakuja kila baada ya wiki mbili. Sasa kama umepiga picha na bado hazijapita wiki mbili, lakini umeweza kwenda wewe mwenyewe mjini Magu, basi ukifika kwenye studio yake, anakupa picha zako, na hivyo ndivyo nilivyofanya siku hiyo. Baada ya mishughuliko yetu, mimi na baba yangu tulifunga safari ya kurejea kijijini kwetu Gambosh. Ilikuwa ni wakati wa magharibi tulipowasili kijijini, yeye baba aliniambia kuwa mimi nitangulie nyumbani, yeye anakwenda msikitini. Alinipa mfuko wenye bidhaa chache na fedha kidogo nitangulie navyo nyumbani. Mimi sikwenda moja kwa moja nyumbani, nilipitia nyumbani kwa rafiki yangu ili nimuoneshe picha zangu nilizopiga na mdogo wangu. Nilipofika nyumbani kwa rafiki yangu, nilikaa kwanza nikawa ninamueleza habari za Magu. Ghafla alitokea mama wa rafiki yangu, na aliponiona alianza kubabaika kama vile amepagawa na kuniambia: "Abdallah, Abdalah, kimbia mwanangu, kimbia nawe watakuua!" Mimi na yule rafiki yangu tulibaki tumeduwaa tunamuangalia, mwishowe rafiki yangu akamuuliza mama yake: "Kwani kuna nini mama?" Mama yule alijibu huku anatetemeka na kuonesha shauku zote za kutaka mimi niondoke pale mara moja. "Nyumba yenu imechomwa moto pamoja na bibi yako anayehisiwa kuwa ni mchawi. Kwa hiyo bibi yako, mama yako na ndugu zako wote wameteketea na moto na hivi sasa baba yako wamemkamata, naye wanataka kumchorna moto…kimbia baba mwanangu uokoe maisha yako, watakuchoma na wewe, hawataki mtu wa familia yenu kijijini hapa. Wanasema bibi yako ana macho mekundu na anaua watoto na wajukuu wa wenzake." “Sikutaka kusikiliza zaidi, nilitoka mbio na mfuko wangu, lakini sikukimbia kwenda kwingine bali nilikimbilia nyumbani. Mungu wangu, kabla sijaikaribia nyumba niliona ni namna gani nyumba yetu ilivyokuwa inateketea kwa moto. Kwa kuwa giza lilikwisha ingia nilisogea kwa kujificha ficha na nilipofika karibu zaidi niliweza kumuona baba yangu anavyopigana na mwishowe walimpiga gongo la kichwa akazimia. “Walipomnyanyua na kuonekana wazi kuwa walitaka kumrusha kwenye moto mimi ndio nilipogeuka kuanza kukimbia. Nilikimbia kutoka kijijini hapo, pasipo kujua ninaelekea wapi, lakini nilikimbia kwa kasi, kwa nguvu zangu zote, sijui ni mita ngapi lakini niliweza kufika kijiji kingine pasipo kujijua. Kando ya kijiji hicho palikuwepo na zizi la ng'ombe na kibanda cha mbuzi. Nilijipenyeza kwenye banda la mbuzi kama vile na mimi ni mbuzi nikapumzika humo kwa usiku huo. Nilianza kuwawaza mama yangu, bibi yangu, baba yangu na wadogo zangu. Katika kuzaliwa tumboni mwetu mimi nilikuwa wa kwanza. Nilifuatiwa na wadogo zangu watatu wote wanawake, nao wote walifariki. Baada ya hapo ndipo alipozaliwa mdogo wangu ambaye nilimpita sana ki umri naye ni Abdurahmani." Dallas alipofika hapo alipangusa machozi, kwa kihanjifu alichokitoa mfukoni mwake. Dokta lmu aliyekuwa mkabala na Dallas kwenye kizimba kingine alianza kuvutiwa mno na hadithi hii ya Dallas kiasi cha kukaribia kumuuliza 'halafu ilikuwaje?’, lakini hakuweza, badala yake alimuangalia kwa kumkodolea macho na kumtegea masikio kwa makini. Katika watu wote waliokuwepo hapo mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi ile, watu wawili kila mmoja amekaa upande wake, mzee Majaliwa na mama yake Amani walionekana kuwa tuli na kimya visivyo kawaida, hawakusema, hawakucheka, hawakununa wala hawakuonekana kuwa katika hali yeyote ile, isipokuwa kumtazama Dallas tu. Hakimu alimuhimiza Dallas kwa kumwambia, "Endelea…ilikuwaje baadaye?" Dallas alirudisha pumzi kwa nguvu na sura yake kwa yakini ilionekana kuwa na huzuni. Aliendelea kusema kwa sauti ya taratibu, "Abdulrahmani alikuwa ni kama . . . sijui niseme nini! Alikuwa kama kito cha thamani sana kwangu. Sikuwa tu ni kaka yake, bali nilikuwa mlezi wake, yaya wake na watu wote nyumbani, hata mama sikutaka amhudumie. Abdulrahmani alipofikia umri wa miaka miwili, huduma zote nilikuwa nikimfanyia mimi, kumlisha, kumuogesha kumfulia na hata kulala naye. Alichukua nafasi ya wadogo zangu wote waliofariki. Nilimpenda mno. Sikumuamini mtu mwingine yeyote kuwa na Abdulrahmani, ambaye hapo nyumbani sote tulimwita Mani. Tukio hilo lilipotokea Mani alikuwa ndio anaanza kusema, maneno aliyokuwa akiyajua wakati huo ni Mama, Baba, Bibi, Kaka na Mani, ambae ni yeye mwenyewe. Usiku huo kwenye banda la mbuzi sikupata hata tone la usingizi, kulipoanza kupambazuka tu, nilitoka kwenye banda hilo kabla wenyewe hawajaamka nikaelekea barabarani. “Nilipofika huko nikakaa kwenye kituo cha mabasi yanayokwenda Mwanza. Kunako saa mbili na nusu hivi nilipata gari linaloelekea Mwanza, ambako nilibadilika kutoka Abdallah na kugeuka kuwa Abdul…naa…maisha yangu yote kuanzia hapo Mwanza mpaka nikaenda Arusha nikawa Abdi, mpaka nikafika Tanga nikageuka Dullah na hata nilivyowasili hapa Dar es Salaam na kuwa Dallas nimeshaieleza mahakama hii . . .na ni kweli tupu sio uongo. “Sasa ngoja nirudi kwa Abdulrahmani. Katika muda wote huo wa maisha yangu niliyoishi, niliamini kabisa kwamba mimi sina ndugu wa damu yangu, mpaka siku ya kwanza nilipofika ndani ya mahakama hii. Baada ya kesi hii kuanza ambayo mimi ni shahidi, niliona ukali wa wakili mtetezi bwana Amani, kwa hiyo nilijishauri na kuamua kwenda kumuona bwana Amani nyumbani kwao, ili nimueleze mambo ambayo sikutaka kuyaeleza hapa mahakamani, ambayo baadaye niliyaeleza yote ya Mwanza, Arusha na Tanga. Nilifika kwao kwa madhumuni ya kumpa historia ya maisha yangu tukiwa nje ya mahakama. Nilipofika, lakini bahati mbaya sikumkuta Amani, nilikutana na ndugu yake Zainabu.
“Wakati nipo sebleni, moyo ulinipasuka nilipoona picha zilizotungikwa ukutani. Picha hizo ni za Amani alipokuwa na umri wa miaka miwili na tayari alipokuwa mkubwa. Nilimuuliza Zainabu kuwa yule mtoto ni nani, naye alinijibu kuwa picha zile ni za kaka yake Amani." Dallas alipofika hapo alitulia, akamuangalia Amani, kisha akasema kwa sauti ya chini. “Picha zile ni za Abdulrahmani mdogo wangu, na ushahidi kamili, picha nilizopiga kijijini kwetu miaka karibuni thelathini iliyopita, ambazo ndizo pumbazo langu la moyo kila ninapoziangalia, ninazo hapa, hazina tofauti. Amani...muheshimiwa hakimu ni Abdulrahmani...hasa ndiye yeye!" Dallas alitoa pochi toka kwenye mfuko wake wa suruali wa nyuma, akatoa picha tatu akanyoosha mkono wake juu huku akisema "Hizi hapa picha zetu tulizopiga tulipokuwa wadogo Mani...hebu nawe ziangalie mdogo wangu!" Amani alizipokea zille picha, akaziangalia kwa kuzikazia macho, alizitazama kwa muda mrefu akajihisi kijasho chembamba kinamtoka kwenye paji la uso wake ambao kwa wakati huo ulijaa simanzi. Kisha alivuta hatua chache na kumkabidhi hakimu picha hizo. Baada ya hakimu kuziangalia alimuuliza Dallas: "Ndugu Dallas, pamoja na kuwa umepewa nafasi kubwa ya kueleza historia ya maisha yako, inawezekana kuwa kweli wewe u kaka wa damu wa ndugu Amani, lakini kesi iliyokuleta hapa ni kutoa ushahidi juu ya tuhuma zinazomkabili Dokta lmu zihusuzo kifo cha Mwanamtama. Kwa hiyo basi suala hili la udugu wa wewe na bwana Amani, tunashauri limalizwe nje ya mahakama hii kati ya wewe na Amani. Kwa leo kesi imeahirishwa…itaendelea kusikilizwa tena wiki moja baada ya siku ya leo. Ndugu Dallas unaombwa utakapokuja tena uje na ushahidi ulio kamilifu uhusuo kesi hii ya Dokta lmu, halikadhalika na upande wa mshitakiwa, wakili mtetezi ajitayarishe na ushahidi wake kamili...” Picha zile alirudishiwa Dallas, na watu wakaanza kuchangukana. ***** Kwa mara ya kwanza Amani alionekana kuduwaa na kuchanganyikiwa, wakati watu wanatoka kwenye chumba cha mahakama yeye alibaki amesimama hapo aliposimama na kupotea kwenye mawazo. Sauti nyororo ya kike iliyoandamana na kushikwa bega, ilimtoa kwenye mawazo. Ghafla akageuza uso wake na kumuona aliyemgusa na kumwita, alikuwa mchumba wake Fatima ambaye aliendelea kumwambia: " usiwache mawazo yasiyo na uhakika yakavuruga akili yako Amani, twende zetu, tutajadili jambo hilo tufikapo nyumbani." Amani alianza kuvuta hatua kutoka chumba cha mahakama huku akimwambia Fatima: "Kusema kweli nimechanganyikiwa, unajua kitu kimoja Fatima?" “Hapana, sifahamu !" "Zile picha... zile picha hazina tofauti kabisa na picha zangu za utotoni, ni mimi hasa! Yule Dallas alizipata vipi? Imekuwaje? Au aliwahi kuwa 'houseboy' wetu na akapiga picha na mimi nilipokuwa mdogo?” Amani aliuliza maswali chungu nzima ambayo hakutarajia kupata majibu yake. Aliendelea kutilia shaka uzawa wake kwa kutamka: "Au mimi sio mtoto wa mzee Mirambo? Haiwezekani!"
***** Dokta lmu wakati anatolewa kizimbani kupelekwa kwenye chumba kilicho na mahabusu wengine hapo mahakamani ili wasubiri gari la kuwachukua na kuwarudisha rumande, alimuomba askari amuitie Mzee Majaliwa na aruhusiwe kusalimiana naye kwa dakika chache. Imu alimuona Mzee M ajaliwa na alimtulizia macho wakati Dallas alipokuwa akitoa habari zake za alipokuwa kijijini. Mzee Majaliwa alionekana kupotea kwenye mawazo wakati ule, kwa hiyo Dokta lmu alihitaji sana azungumze naye japo kwa mara moja. Mzee Majaliwa alipofika mbele ya Dokta Imu, waliruhusiwa kusalimiana wakiwa wamesimama kando kidogo na wengine. Dokta Imu hakusubiri kusalimiana, alimuuliza: "Rafiki yangu kutokana na historia halisi ya maisha yako uliyopata kunihadithia siku za nyuma ulipokuwa umelazwa hospitalini, inaonekana huyu Dallas ni motto wako, au vipi… wewe unaonaje?" Mzee Majaliwa alionekana kushikwa na bumbuwazi, lakini Dokta Imu alipozidi kusisitiza kusikia kauli ya mzee Majaliwa juu ya Dallas, hatimae mzee Majaliwa alimlaani shetani kwa kupiga 'Audhubillahi Mina -shaitwaani Rajim', kisha akaanza kuitika kwa kichwa na kufuatia na tamko lake kwa kusema: "Naam yule kijana anayejiita Dallas ni mwanangu kabisa, yule ndiye Abdallah, mwanangu wa kiume wa kwanza, siamini macho yangu, siamini kuwa kumbe bado ipo damu yangu iliyo hai. Na yote yale aliyosema ya mimi na yeye kutoka kijijini Gambosh na kwenda Magu, halafu kurejea wakati wa swala ya magharibi ni kweli kabisa. Pia kuhusu picha alizopiga pamoja na mdogo wake Abdurahman, ni kweli kabisa, na jinsi alivyokuwa akimpenda mdogo wake huyo ni kweli kabisa! Sasa sijui hili suala la Amani kuwa ndiye Abdulrahmani, hili siwezi kulisemea kwa sasa!" Dokta Imu alitoa tabasamu, akamsogelea zaidi mzee Majaliwa na kumkumbatia huku akimwambia: "Mzee jambo jingine nililoligundua ni kuwa sauti zenu, wewe na Dallas zinafanana sana, hata siku ya kwanza nilipokutana na Dallas nilisikia na kuhisi sauti ya mtu ninayemfahamu, sasa nimetambua kumbe ni wewe." Aliacha kumkumbatia na akamuangalia machoni, kisha akamwambia: "Sikiliza rafiki yangu, matokeo yeyote yale yatakayotokea juu ya hii kesi yangu nakuomba usimchukie mwanao Dallas ama Abdallah, kuwa naye na uhakikishe kuwa mko pamoja. Yule ni mwanao mzee, mwanao wa damu yako, mwanao wa kumzaa. Nakuomba nenda ukaonane naye, nawe ujitambulishe kwake, nina imani mtatambuana, nenda mzee wangu ukamuone Dallas!" Wakati Dokta Imu anamaliza kumwambia Mzee Majaliwa maneno haya, Amani aliingia na kwenda moja kwa moja pale walipokuwa. Mzee Majaliwa na Imu waligeuza nyuso zao kwa pamoja kumuangalia , na kwa mara ya kwanza Dokta lmu, aliweza kuuona wajihi wa Amani na kutambua kuwa amefanana mno na Dallas. Alitambua kuwa rangi ya ngozi zao, vimo vyao, na hata maumbile yao yalifanana mno, tofauti ilikuwa ni umri tu. Amani alipofika pale alimwambia Mzee Majaliwa: "Nilikuwa nikikutafuta mzee ili nikurudishe msikitini, kumbe upo huku na rafiki yako!"Aliyasema haya huku akilazimisha tabasamu kwenye uso wake ulioonesha kuchoka wazi wazi. Dokta lmu alimwambia: "Kabla hujampeleka mzee Majaliwa huko kwake, nakuomba kaka Amani, tafadhali mkutanishe na Dallas, kwani Dallas ni mtoto hasa wa kuzaliwa na mzee Majaliwa!" Amani aligutuka na kushangaa. Akamuangalia Dokta Imu, kisha mzee Majaliwa, kisha Dokta lmu tena, na kusema: "Eeenhe!! Mtoto wake wa kumzaa?" "Ndio kakaAmani, Dallas ni mtoto wa mzee Majaliwa waliyepoteana zamani. Hadithi aliyoisema Dallas ya kijijini kwao, ni ya kweli, kwani mzee Majaliwa alikwisha nihadithia kabla ya leo, na ndivyo ilivyokuwa kuhusu kuteketea kwa familia ya mzee Majaliwa kwenye nyumba yake iliyounguzwa..!” Amani alichoka maradufu. Alizidi kuonekana amechanganyikiwa. Alijiinamia, kisha akanyanyua uso wake taratibu na kumuangalia mzee Majaliwa kwa kuibaiba huku akiwaza kichwani mwake: kwa hiyo kama ni kweli mimi ni ndugu yake Dallas, nitakuwa ni mtoto wa Mzee Majaliwa vile vile. Alipowaza hivyo alizidi kuchanganyikiwa. Alinyanyua uso wake akamuangalia Mzee Majaliwa usoni, ambaye naye kwa wakati huo alikuwa anamuangalia. Walibaki katika hali hiyo ya kuangaliana kwa muda wa sekunde kadhaa ikiwa nyuso zao wote wawili zimejaa huzuni. Mwishowe Amani alianza na kusema; "Sawa mzee, tuende tukamuangalie Dallas huko nje ya mahakama iwapo atakuwa bado yupo hajaondoka." Mzee Majaliwa na Amani waliagana na Dokta Imu na kutoka kwenye jengo la mahakama. Wakati Amani na Mzee Majaliwa wanatumba tumba kumtafuta Dallas, Dallas ndio alikuwa anaagana na wakili Zablon Mkuki. Mara baada ya kuachana na Mkuki, Dallas alitupa jicho na kumuona Amani ambaye naye kwa wakati huo alikuwa amemuacha Mzee Majaliwa amesimama sehemu, akawa anamfuata Dallas. Kwa hiyo, na y eye Dallas alianza kumuendea Amani, walipokaribiana Dallas alikunjua mikono yake kuashiria kutaka kumkumbatia Amani, lakini Amani hakuonekana kupendezwa, hakuwa tayari kukumbatiwa na Dallas, hivyo alipuuza mikono ya Dallas na kujitenga nayo huku akisema: "Kama upo tayari kukumbatiana na mtu, basi nifuate, yuko mtu muhimu zaidi wewe kumkumbatia kuliko mimi." Amani alipomaliza kusema hivyo, aligeuka na kuelekea upande aliotokea, naye Dallas alimfuatia huku akitikisa kichwa chake kwa masikitiko. Walipofika alipokuwa amesimama Mzee Majaliwa, Dallas hakuchukua muda kumtambua baba yake, aliita kwa mshangao mkubwa. "Baba!!! Naye mzee akaitikia kwa sauti iliyojaa mikwaruzo. "Mwanangu! Ab ...dallah!" Chozi lilikuwa linamdondoka Mzee Majaliwa. Dallas alikunjua mikono yake tena kumtia katika mikono hiyo mzee kwa kumkumbatia huku akiita mfululizo. "Baba!...Baba!.... Babaa!!" Naye mzee akawa anaitikia kwa kulitaja jina lake kila anapoita. "Abdallah ...Abdallah ... Abdallah mwanangu!” Wakati wote huu Amani alikuwa amesimama kando yao aliwaangalia kwa sura isiyofahamika na kuendelea kuwaza: 'Hivi inaweza kuwa ni kweli huyu jamaa Dallas ni kaka yangu na kwa hiyo huyu mzee Majaliwa akawa ni baba yangu?!! Na Mzee Mirambo naye je?? Kweli inawezekana asiwe baba yangu? Hata! Mimi ni mtoto wa Baba na Mama Mirambo!' Mara ile ile Dallas aliwacha kuendelea kumkumbatia baba yake Mzee Majaliwa, na kusema kumwambia mzee huyo, huku akimuelekeza kidole Amani. "Baba, huyu ni mwanao Abdulrahman huyu! Ni Mani huyu Baba, Oh Mungu wangu! Shukrani ziwe kwako Mola wa viumbe wote! Sikujua kama nitaishi na kukutana na baba yangu na ndugu yangu mpendwa!" Alinyoosha mikono juu wakati akisema maneno haya ya mwisho. Amani hakugutuka wala kushawishika na maneno yale. Alibaki kuwa kimya na kumuangalia Dallas kwa sura ya kutomuamini anayosema kuwa yeye ndugu yake. "Mani ndugu yangu, mimi ni kaka yako, na bahati nzuri Mungu ametukutanisha na baba Yetu kwa wakati mmoja. Niamini Mani, wacha tukumbatiane na kumshukuru Mungu kwa kutuunganisha tena wakati tungali hai" Dallas alimwambia Amani kwa sauti ya kubembeleza. Amani alitoa tabasamu la kulazimisha. "Mimi jina langu Amani bwana, Amani Mirambo, na sio Mani. Ni sawa kabisa kumshukuru Mungu bwana Dallas, kwa kukutanisha na baba yako mliopoteana zamani, kwa hiyo tosheka na ridhika na hilo bwana. Usilazimishe mambo mengine yasiyokuwepo!” Alimjibu, kisha akamgeukia mzee Majaliwa, ambaye macho yake yalikuwa yamewiva kwa kulia, na kumwambia: "Mzee…twendeni niwapeleke popote pale ambapo mngependa kwenda wewe na mwanao Dallas ili muweze kuketi na kuzungumza vizuri!" Mzee Majaliwa alimuangalia Amani na kujihisi damu inamsisimka. Mpaka hapo walipofikia pasipo kuona au kupata ushahidi wowote ule zaidi ya aliosema Dallas, aliamini kabisa kuwa Amani pia ni mwanaye, lakini vile vile hakumlaumu Amani kwa kulikataa jambo hilo la yeye kuwa ni ndugu wa Dallas. Kwa hiyo, kwa sauti ya chini na iliyojaa huzuni, Mzee Majaliwa alimuomba Amani kwa kusema, "Amani baba, mimi ningependa nikapate chakula cha mchana nyumbani kwenu, kwa baba na mama yako, nikiwa pamoja na mwanangu Dallas…” Amani alimuangalia Mzee Majaliwa kwa dakika zisizopungua mbili, kisha akamjibu. "Sawa mzee. Kwa hilo usiwe na wasiwasi, isipokuwa itanibidi niwapeleke Mama, Zainabu na Fatima kwanza halafu ndipo nije niwachukue nyinyi. Sasa sijui mtanisubiri wapi?" Mzee Majaliwa alimwambia Amani kuwa wao watawakuta nje ya msikiti ambao alimuelekeza upo karibu na mahakama,akisema: "Kwani nitakwenda kuswali kabisa katika msikiti huo!" Walipofika na kuingia ndani kwa akina Amani, Mzee Majaliwa na Dallas, walikuta chakula tayari kimekwisha andaliwa. Walikaribishwa na kuelekea chumba cha kulia. Kwa pamoja, Mzee Mirambo, Mama Amani, Zainabu, Amani, Mzee Majaliwa na Dallas,walizunguka meza ya viti sita wakiwa wameketi juu ya viti hivyo na kuanza kula. Hivyo ni baada ya kusalimiana na kutambuana. Kila mmoja alianza kula na kuendelea kula kwa kujidai kwa wakati huo anachokijali zaidi ni kula tu. Lakini ukweli ni kuwa kila mmoja kati ya watu sita hao, alikuwa na mawazo yake yanayomtembea kichwani mwake. Baada ya kula, mzee Majaliwa alitoa shukrani na wote kwa pamoja walitoka chumba cha kulia na kwenda sebleni. Wakati wapo hapo, Mzee Majaliwa alizitulizia jicho zile picha za Amani zilizokuwepo ukutani, kwa kuwa na zile picha alizokuwa nazo Dallas pia alioneshwa walipokuwa wanamsubiri Amani kuja kuwachukua, vile vile alikwishapata kuziona miaka mingi ya nyuma siku zilipotoka studio, alihakikisha kabisa kuwa hakuna tofauti. Ndipo alipoomba radhi na kusema, "Bwana Mirambo, pamoja na mkeo na watoto wenu Amani na Zainabu, tafadhali ninawaomba mniwie radhi munisamehe, lakini munipe wakati wenu pamoja na umakini wenu, munisikilize hadithi ya maisha yangu ili muweze kunitambua mimi ni nani kwa uhakika na ukweli wa lilahi ya Mwenyezi Mungu…" Mzee Mirambo alijibu na kusema, "Kwa niaba ya familia yangu, ambayo ipo hapa mbele yako, tupo radhi na wala haitakuwa tabu kwetu kukusikiliza kila unachotaka kutueleza." "Ahsante bwana Mirambo, na ninaapa mbele ya Mungu kwamba haya nitakayosema ni kweli tupu kuhusu mimi." Mzee Majaliwa alisema, kisha akaanza kuelezea historia yake kama vile alivyo mueleza Dokta Imu. Alieleza asili yake, alieleza shughuli zake alizokuwa akifanya, akaeleza kuhusu familia yake, watoto aliowahi kuzaa wakafariki, mpaka janga la msiba lililompata. Vile vile maisha yake ya jela, mpaka akapata msamaha wa rais. Akaeleza jinsi alivyokutana na Dokta lmu mpaka wakawa marafiki. Akaeleza ni jinsi gani Dokta lmu alivyo, na namna alivyomtambulisha kwa Zainabu. Pia akawaambia yaliyotokea siku lmu alipokuwa anataka waongozane kwenda kuoa kwake yeye bwana Mirambo. Akaeleza kuhusu kutiwa ndani kwa Imu na kesi yake na namna alivyokutana na Amani na kumuomba aende kutoa ushahidi na kilichoendelea mpaka yeye kukutana tena na Dallas ambaye ni motto wake Abdallah. Akaishia kusema baada ya masaa kupita kwa kumuambia mzee Mirambo, “... Hiyo ndio historia yangu. Nami angalau kwa ufupi naomba unielezee yako bwana Mirambo. Nieleze kwa jina la Mwenyezi Mungu, ukweli mtupu na hasa kuhusu uzawa wa watoto wako!" Mzee Mirambo alitulia tuli na kuonekana kupotea ndani ya mawazo, mwishowe alimuangalia mke wake kama vile anayemuomba idhini ya kuzungumza, jambo lililoonekana kuwa ni kweli kwani mama yake Amani alimuangalia mumewe na kumkubalia kwa kichwa kuashiria kuwa anaweza kusema.
, na alimuashiria hivyo huku chozi likimtoka. Mzee Mirambo alimtazama kwa kumtulizia jicho Amani, ambaye alionekana kukosa raha kabisa, kisha akajikohoza kidogo na kuanza kuongea. "Kwa kuwa umenitaka niseme bwana Majaliwa kwa kumtaja Mungu, basi nitasema ambayo ni kweli tupu kuhusu maisha yangu kwa ufupi na uzawa wa watoto wangu!" Alitulia na kuwaangalia Amani na Zainabu. "Mimi, kabila langu ni Mnyamwezi, kwa baba na mama. Tumboni mwetu tulizaliwa wanne, wanawake wawili, ambao ndio waliotangulia, na wanaume wawili wa baba mmoja mama mmoja, mimi nilikuwa wa mwisho kuzaliwa. Nilipata bahati ya kusomeshwa kuliko wenzangu wote ambao waliishia madarasa ya chini tu. Kaka yangu alisoma zaidi elimu ya dini, na dada zangu waliolewa mara baada ya kumaliza elimu ya msingi. Mimi nilisoma hadi kufika chuo kikuu na kuendelea kusoma ng'ambo…lakini kabla sijakwenda ng'ambo, nilianza kazi kama Hakimu wa Wilaya. “Mwaka mmoja baada ya kuanza kazi, niliozwa mke, ambaye ni huyu hapa mke wangu mpaka sasa. Tuliishi kwa muda mrefu kwa furaha na amani, lakini hatukujaaliwa kupata mtoto. Mke wangu alikwenda kila palipohusika kuchunguzwa na wakati mwingine pamoja na mimi, lakini hatukuonekana na dosari yeyote. Kwa hiyo tuliendelea kumuomba Mungu huku miaka inakatika. Siku moja wakati ninatembelea mahakama ndogo za tarafa, wakati huo nilikuwa wilaya ya Magu…” Alipofika hapo Mzee Mirambo alitulia na macho manne makali kushinda ya wote yalikuwa ni mawili ya Dallas na mawili ya Amani yalitulia juu ya uso wake. Alirudisha pumzi na kuendelea. “ Nilikuwa ninarudi Magu kutoka tarafani, ilikuwa ni wakati wa usiku, ndani ya gari la serikali aina ya Landrover, nilikuwawemo mimi na dereva tu. Ghafla katika barabara ndogo tulizokuwa tunapita tulimuona msichana mdogo wa miaka sita au saba hivi, amembeba mtoto wa kiume wa miaka miwili ubavuni mwake. Cha ajabu ni kuwa wote wawili walikuwa wanalia. Llibidi tusimame na kumuuliza yule msichana kulikoni? “Yule msichana kabla hata hajajibu alitukabidhi mtoto na kusema, "Nimeambiwa na bibi yake haraka nitoke naye kwa mlango wa nyuma wa nyumba yao inayounguwa! Mimi nilikwenda pale kwao mara moja tu…mara watu wakaja wakachoma nyumba! Sasa yule bibi hakuwahi kutoka akanitorosha, pale mlangoni napo pakawaka panaungua…sasa…sasa yule bibi akavunja dirisha moja dogo la mbao akanipitisha mimi kisha akanipa huyu mtoto na kuniambia nikimbie nikamtupe barabarani mbali na nisimpeleke kwa mtu yeyote wa kijiji hiki! Halafu lile dirisha nalo likaanza kushika moto. Yule bibi hakuwahi kutoka. Sasa watu wameizingira nyumba huko…mimi ninaogopa ...!" “Kufikia hapo yule msichana mdogo alikimbia na kutuachia mtoto. Nilichojaribu kufanya baada ya hapo ni kwenda kwenye tukio. Nilifika hapo kwenye nyumba iliyokuwa imechomwa na inaungua, na kweli...nilikuta watu waliokuwa na hasira kali wameshampiga baba mwenye nyumba hiyo gongo la kichwa, amezimia na wamembeba na kutaka kumrusha kwenye moto huo. “Ni mimi niliyezuia kitendo hicho kisitendeke na kuamuru iwapo wanakijiji hao wanaona kuwa mtu huyo ni muhalifu, basi wampeleke mahakamani. Wakati huo mtoto nilimuachia dereva ndani ya gari na nilimuamuru amnyamazishe na asithubutu kutoka naye. Kwa kuwa ilikuwa ni usiku hakuna aliyeweza kuona kama ndani ya gari ile kuna mtoto. “Kesi ya bwana yule sikui endesha mimi, lakini niliifuatilia sana. Na nikagundua kuwa ushahidi wote ulikuwa dhidi yake na alihukumiwa kufungwa maisha. “Sasa tukirudi nyuma kuhusu mtoto, katika uchunguzi wangu niligundua kuwa watu wa familia yake wote wamefariki kwa kuteketea na moto. Mtoto yule nilimpeleka kwangu usiku ule ule. Na nilipomueleza mke wangu nimempata vipi yule mtoto, aliniambia kwa wakati wote nitakaokuwa ninafanya upelelezi kuhusu familia ya mtoto yule, basi nimwache hapo hapo nyumbani. “Kwa hiyo baada ya kupata matokeo hayo mke wangu hakuniruhusu kusema lolote kuhusu mtoto huyo. Na tukapeana ahadi kuwa kuanzia hapo mtoto huyo atakuwa ni wetu, kwani tuliamini kuwa Mungu ndiye aliyetujaalia. Tulipojaribu kumuuliza kuhusu familia yake masikini yule motto alikuwa hajui lolote. Tulipomuuliza jina lake alikuwa akisema 'Mani,' nasi tulilichukulia kuwa jina lakeni 'Amani.' Kwa hiyo hatukutaka kumpa jina jingine hata sasa bado mimi na mke wangu tunamwita Amani kwa jina la Mani. “Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Baada ya miaka kumi tangu tumpate Amani, mke wangu alishika mimba, ambayo hapo awali hatukuamini, na ndipo tulipomzaa Zainabu. Hatukupata mtoto mwingine tena baada ya hapo, lakini tuliishi kwa furaha na amani, na hata jina la utani la Zainabu tunamwita 'Furaha' tukiwa na maana tunayo 'Amani na Furaha', kwa kuwa na wototo wetu wawili hawa…” “Kwa hiyo bwana Majaliwa, Amani si mtoto wetu wa kumzaa na uhakika atakuwa ndiye mtoto wako, kwa sababu niliweza kuzitambua sura zako maru tu nilipokuona...Amani ndiye Abdulrahmani…!”
**** Wakati wote Mzee Mirambo alipokuwa anahadithia historia ya maisha yake na uzawa wa watoto wake, Amani alikuwa amekodoa macho kumuangalia. Mwisho wa simulizi hizo zamaisha ya Jaji Mirambo, macho ya Amani yalikuwa yamejaa machozi ambayo hakuweza kuyazuia, bali yalianza kutiririka juu ya mashavu yake. Alikutanisha viganja vyake na kuvifanya visuguane vyenyewe kwa vyenyewe, lakini hakuweza kunyanyua hata kidole kimoja cha viganja hivyo na kukielekeza machoni au shavuni kwake kufuta machozi hayo. Mke wa Jaji Mirambo alisogea karibu na alipokaa Amani, alishika ncha ya kanga aliyokuwa ameiweka mabegani mwake kwa wakati huo na kuanza kumpangusa yale machozi. Kisha akachukua kichwa cha Amani na kukiegemeza kifuani kwake, kama vile Amani alikuwa mtoto mchanga anayembembelezwa. "Nyamaza mwanangu, nyamaza baba, yote aliyosema baba yako ni ya kweli kabisa. Umeyasikia na nakuomba uyaamini…”
“Sasa nisikilize ninavyosema mimi…iwapo niliweza kukubali kuwa wewe u mwanangu niliyepewa na Mungu tangu siku ya kwanza ulipoletwa kwangu, basi utabaki kuwa mwanangu mpaka siku ya mauti. Lwapo hatukuweza . ..mimi na baba yako mzee Mirambo… kubadili nia zetu juu yako wewe kuwa u mtoto wetu hata pale Mungu alipotujalia kupata mtoto mwingine ...ambaye ni ndugu yako Zainabu, basi hatuwezi kubadili nia zetu tena juu yako. Wewe ni mtoto wetu na itabaki kuwa hivyo kwa vyovyote vile itakavyokuwa! Pangusa machozi mwanangu ukutane na baba yako Mzee Majaliwa, na pia ukutane na kaka yako Dallas, ambaye nilitambua tangu pale mahakamani alipokuwa akieleza kuhusu familia yake…alivyokuwa akisema ni kweli. Kutana na watu hawa wawili muhimu kwako. Ama kwa upande wangu, najua bado Mungu ananipenda, kwani kuanzia sasa Mzee Majaliwa atakuwa ni kaka yangu, Dallas atakuwa ni mwanangu, mtoto wa kaka yangu, lakini wewe Amani…wewe utabaki kuwa wangu." Mama Amani alisema kwa kirefu. Wakati huu ulikuwa ni wamachozi, sababu, baada ya maneno hayo kusemwa, Dallas naye alikuwa ametota kwa machozi ya furaha. Alisimama kutoka alipokuwa amekaa, akavuta hatua chache, akapiga magoti mbele ya mama yake Amani, akainama na kumshika miguu, huku akisema, "Ahsante mama, naamini yote uliyosema ni kweli, na baba naye pia atakubaliana nami. Nisingependa kumtoa Mani sehemu yeyote ile iliyo na upendo, amani na furaha juu yake. Ninamshukuru Mungu kuwa mdogo wangu yu hai anaishi maisha ya furaha. Mama naa..." Dallas aligeuza kichwa na kumuangalia Mzee Mirambo, akaendelea kusema ". .. Baba. Amani ni mtoto wenu pasipo na shaka. Ninachokiomba ni kuwa Mani alikubali tu kuwa na mimi ni kaka yake na ninampenda sana ...vilevile Mzee Majaliwa naye ni baba yake. Vinginevyo yeye kwao ni hapa hapa kwa Baba na Mama yake, pamoja na mdogo wake Zainabu!" Amani alijitoa taratibu mikononi mwa mama yake, akasimama, akamshika mabega Dallas kwamikono yake miwili na kumnyanyua kutoka alipokuwa amepiga magoti, kisha wakawa wamesimama wakitazamana, halafu wakakumbatiana. "Nisamehe kaka!" Amani alibwabwaja. "Hapana, Amani...hakuna ulonikosea mdogo wangu. Yote yaliyotokea mahakamani, ulikuwa unafanya kazi yako ambayo ni wajibu wako." Mzee Mirambo alisimama akamwendea mzee mwenziye Majaliwa, ambaye wakati wote huu alikuwa ametulia tuli, akijihisi kama vile yumo ndotoni. Alimshika mkono, nao wakakumbatiana. Kisha Amani alimuacha Dallas akamjia mzee Majaliwa na kumkumbatia. Mtu aliyekuwa anaonekana amewachwa nje kidogo ya mkusanyiko huo, ingawa naye alikuwa yupo pale pale ni Zainabu. Baada ya mazungumzo yote hayo na watu kuendelea kukumbatiana na kutakana radhi, yeye ghafla alianza kumuwaza Dokta Imu, na kuingiwa na wasiwasi na hatima ya kesi yake. Aliwaza kichwani mwake, iwapo mtetezi wa Dokta lmu ambaye ni Amani ametokea kuwa ni ndugu wa shahidi mkandamizaji Dallas. Vile vile shahidi mtetezi wa Dokta lmu aliyekuwa akitegemewa ambaye ni Mzee Majaliwa, ametokea kuwa ni baba mzazi wa Dallas na Amani, je Dokta lmu atakuwa na usalama hapa? Alitolewa kwenye mawazo na sauti ya Mzee Majaliwa ambaye kama vile alimuona ndani ya kichwa chake kuwa anawaza nini, alimuuliza, "Mbona umejiinamia mama, mwanangu Zainabu…unafikiria nini? Unamuwaza Dokta lmu?" Zainabu alinyanyua uso wake na kumuangalia. "lnaonekana maisha ya Dokta lmu yamo mashakani!" Alimjibu huku akimtazama kwa huzuni. Mzee Majaliwa alikumbuka maneno ya mwisho aliyoambiwa na Dokta lmu walipoachana, kuwa asijali lolote lile litakalo tokea kwake ili mradi yeye awe na mwanaye Dallas. Kwa mara ya kwanza toka mkutano ukutanike na kuelezwa mengi, Mzee Majaliwa alijihisi kulia. Ndipo alipomwambia Zainabu, "Mungu atamsaidia, lakini mimi ninaahidi na nafsi yangu, iwapo kuna jambo lolote la kumsaidia Dokta lmu, ambalo limo ndani ya uwezo wangu, basi mimi nitamsaidia!" Zainabu alitamka matamshi ya kukata tamaa kumwambia mzee Majaliwa. "Kwa hali ilivyo hivi sasa, itakuwa ni miujiza kama lmu atashinda" Maneno haya yalisikika na kila mtu. Amani alikwenda pole pole mpaka mbele ya Zainabu akakaa karibu yake juu ya kochi na kumuuliza, "Kwa nini unasema hivyo Zainabu?” Zainabu hakumjibu. Aliinamisha kichwa chini. Amani akamuuliza tena. "Zainabu, kwa nini unasema hivyo?" Chozi lilianza kumdondoka Zainabu. Aling'ata ng'ata midomo yake, lakini hakujibu. Amani alimuuliza kwa njia nyingine ambayo alihisi kuwa ndiyo itakayomfanya Zainabu ajibu, aliuliza kwa sauti ya unyonge, "Ina maana. . .ina maana mimi sio kaka yako tena Zainabu?" Zainabu aliposikia swali hilo, alimuangalia, akamrukia na kumkumbatia huku akisema, “Samahani kaka, wewe ni kaka yangu . ..ndio! Wewe ni kaka yangu!" "Sasa mimi kama ni kaka yako, ninapenda mdogo wangu uwe na furaha, ... kama jina lako lilivyo. Furaha yako wewe ndio yangu mimi. Wewe ndiye mdogo wangu pekee. Kama nimepata kaka ambaye ni Dallas, ananipenda, lakini na mimi ninampenda mdogo wangu vile vile ambaye ni wewe. Nitahakikisha nitaushinda ushahidi wa Dallas mahakamani, kwa ajili ya furaha yako wewe ...mdogo wangu." Amani alimwambia kwa msisitizo. Dallas naye alimwendea Zainabu na kumwambia huku amemshika bega moja. "Zainabu, wewe na Amani ni wadogo zangu, nyote wawili. Na kwa kuwa wewe ndie mdogo zaidi na ni mwanamke wa pekee kati yetu, basi mimi nitakupenda zaidi ya ninavyompenda Mani kama ndugu yangu. Suala la Dokta lmu, siwezi kusema chochote, sababu ni mapema mno. lsipokuwa, mimi ninaahidi kumsaidia Mani kwa njia yeyote ile iwayo, ilimradi tu mwisho wa yote haya... yaani hii kesi, wewe uwe na furaha na amani ... hata kama itakuwa mmoja wetu kati ya mimi na Dokta lmu kuingia hatiani, lakini wewe tutahakikisha unabaki furahani."
*****
Siku ile Mzee Majaliwa alirudishwa Msikitini ambako alisisitiza arejeshwe, na Dallas akapelekwa kwake kwa gari la Amani. Walipoachana tu, huku nyuma Dallas alitoka kwenda kumtafuta Gevas. Walipokutana, kwanza Dallas alimueleza rafiki yake Gevas habari zote za kukutana na baba yake na mdogo wake. "Nashukuru sana rafiki yangu kwa kunikabidhi kesi hii, ingekuwa sio hivyo sijui ni wapi ambapo ningekutana na mdogo wangu Mani ambae yeye hivi sasa ni mwanasheria, mimi mwenyewe si lolote, si chochote, hohe hahe. Tena Mani anaishi Masaki... kwa wakubwa huko. Ingekuwa vig umu watu wawili sisi kukutana. Pia, sijui ningekutana vipi na baba yangu, ambae yeye sasa hivi anaishi ndani ya msikiti. Kwa hiyo, kazi uliyonipa, mimi nimefaidika nayo sana, isipokuwa tatizo ni moja ambalo ni kubwa!" Alipofika hapo Dallas alibadilika na kuonekana amekosa furaha ghafla. Gevas alimuuliza rafiki yake, "Dallas, ni jambo gani hilo?" "Unajua kuwa huyo Zainabu anayetajwa kuwa ni mchumba wake Dokta lmu!!" "Eh, ana nini?" "Basi bwana huyo msichana ni ndugu yake Amani kweli, ambaye nami Amani ni mdogo wangu. Na Amani ndiye wakili mtetezi wa Dokta Imu…" "Habari kubwa hiyo!" "Sasa utafanya nini…yaani ni jambo gani la kufanya ili maisha ya Dokta Imu tuyaokoe kwa ajili ya ndugu yangu Zainabu . . .ndugu wa ndugu yako. .. nawe ni ndugu yako!" Gevas alipiga kimya kwa muda, kabla ya kumwambia, "Unajua…hili suala ni kubwa na sio dogo rafiki yangu? Hili ni suala la kusababisha maisha ya mtu ambaye tayari amekwishafariki, sasa unafikiri linaweza likamalizwa kirahisi rahisi tu?" Dallas aliinama akafikiri, mwishowe akasema kumwambia rafiki yake. "Lakini unajua Gevas, kuwa katika maisha yetu ya kila siku ni kiasi gani sisi wanaume tunawadanganya wanawake? Na wanawake nao huwadanganya wanaume? Mimba zinazotolewa kila siku ulimwenguni ni nyingi mno. Bahati mbaya tu imemkuta Dokta lmu, hakufanikiwa kuitoa mimba ya Mwanamtama ipasavyo. Lakini kila siku ya Mungu, mimba zinatolewa vichochoroni na vitoto kutupwa vyooni, kufukiwa na kutupwa majaani!" Gevas alimuangalia rafiki yake Dallas kwa hali ya mshangao sana na kumkumbusha kwa kusema, "Ni sawa usemayo Dallas, lakini bahati nzuri kwa hao unaowasema kesi zao hazifiki mbele ya sheria. Hazifiki mahakamani. Lakini hii ya Mwanamtama na Dokta Imu, tayari ipo Mahakamani, kwa hiyo ni lazima ihukumiwe vilivyo. Kazi yetu ni kutoa ushahidi dhidi ya Dokta lmu, ambao umekwisha anza kuutoa, kwa hiyo ni lazima ihukumiwe vilivyo. Endelea bwana ...hakuna njia nyingine. Dokta lmu ni muhalifu, anaweza akaja kumtia matatani hata huyo ndugu yenu Zainabu. Ni bora yametokea haya kabla hajamuoa!” Dallas alijihisi kuchanganyikiwa.
0 Comments