Header Ads Widget

Responsive Advertisement

INATOSHA - 3




Simulizi : Inatosha
Sehemu Ya Tatu (3)

Ilipoishia jana..

uwezo wa kuona nilikuwa nao lakini sikuweza kutambua kitu chochote ikiwa hata na sababu ya mimi kuwa hapa,kifupi sikuwa na fahamu yeyote lakini kilichokuwa kinanishangaza ikifika muda wa kula kuna dada mmoja ndio alikuwa akinilisha chakula na ninapokitema au kutapika naambulia kupigwa vibao na makonzi, nilikuwa si Levina yule aliyekuwa mtukutu kutokana na kupooza kwangu.


Songa nayo sasa…


~ BAADA YA MIEZI 3 ~
Bado nilikuwa sijielewi elewi na kati ya vitu ninavyoweza kuanza kama kukumbuka ni sura ya kijana na mke wake napo nilikuwa siwatambui ni kina nani, pia walikuwa wakiishi na mtoto mdogo aliyeonesha kuwa anatambaa, alikuwa ni mtoto mzuri sana wa kike, kila muda alikuwa miguuni mwangu akinichezea chezea japo sikuwa na hata nguvu yeyote,na ilipofika kipindi cha kuogeshwa au kulishwa alikuwa akilia kwa sauti ya juu sana nakunifanya mchozi uendelee kunidondoka bila kuweza kuufuta.
Mateso kwangu yaliendelea kama kawaida, kunakipindi nilikuwa nalala na njaa bila ya kupata chochote huku nikiambulia kupigwa makofi, na hata sikuwa na kitanda zaidi ya kumalizia usingizi wangu pale pale kwenye kibaiskeli nilichokalia, ilifika kipindi hadi nakaa siku mbili mpaka tatu na kinyesi changu mwenyewe bila kubadilishiwa nguo au hata kusafishwa,kifupi nilikuwa tayari Levina mchafu tena yule mchafu haswa kuanzia juu mpaka chini, nilibabuka sana miguu na magonjwa ya ngozi yalinijaa karibu mwili mzima,nilikuwa mtu wa kung'ong'wa na ma inzi.
Ilifika kipindi nikawa nalazwa nje ya nyumba (uwani) bila kuwa na msimamizi yeyote na kila inapofika jioni ama usiku mateso kwangu huwa ndio kama yanaanza.

~ BAADA YA MWAKA NA NUSU~

Mateso niliyopata kipindi cha mwaka mzima karibia na nusu kilinifanya nipungue sana nikawa kama mtu aliyeathirika na gonjwa hatari tena kama la ukimwi, nguvu za kutembea bado sikuwanazo lakini uwezo wakuwatambua watu nilikuwa ninao, kuongea na kumsikia mtu kwa mbaali niliweza.
Na hata ilipokuwa ikifika jioni kila siku huwa nawaona watu wawili mwanamke na mwanaume wakiingia na gari mpaka ndani ya geti kisha wanashuka nakuingia ndani japo kuwatambua nikawa siwajui ni kina nani kwani ndio hao hao waliokuwa wakinitesa huku wakiongea maneno nisiyoyajua.
*****
CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Yule mtoto alikuwa amekuwa na ikafika kipindi nikawa namshuhudia akinifuata nakukaa pembeni yangu japo hilo swala hawakupenda hata kidogo wazazi, upendo niliokuwa nimeanza kujijengea kwa yule mtoto ilinifanya nianze kuongea,
"Jammy Jammy..., Happy Happy..., Gervas..?"
Nilijikuta naachama mdomo wangu nakuanza kumwita yule mtoto majina mchanganyiko huku nikimwacha akinishangaa mpaka mfanyakazi wa ndani alipokuja kumtoa kinguvu pembeni yangu huku akiniacha kwa kunipiga makofi na mateke,
"...ukome,tena ukome kumfuata fuata huyo chizi..."
Hisia kali nilizokuwanazo zilinifanya niweze kumsikia kwa mbaali japokuwa sikuwa naelewa anamaanisha nini,
"kelly...? Haya baba yako Gervas huyoo amerudi twende nje tukampokee...!"
Bado waliniweka kwenye fumbo tena kubwa kwani sauti nazisikia wanavyoongea japo kwa mbali lakini maana na kumbukumbu sina kabisa hivyo nikabaki nikijiuliza tena kwa sauti ya kimyakimya,
"Kelly...?,Gervas ndio wakina nani tena...?
Nilibaki nikijiuliza bila ya kupata majibu yeyote na hata ya kuelewa kitu chochote.
"...Lakini, jina la Gervas kama nalikumbukaa...? Kwani hapa ni wapi...?"
Nilijikuta nikiendelea kujiuliza maswali mengi bila ya kujua na kwa muda huu nilijaribu kusimama mwenyewe bila ya mtu yeyote kuniona lakini tatizo likawa ni katika kutembea.
Nilianzisha kamtindo tena kipindi ambacho nyumba inakuwa haina mtu niko peke yangu nilikuwa mtu wa kujikokota na kibaiskeli changu huku nikijaribu kufungua vyumba vingine bila ya mafanikio yeyote, nilijaribu chumba kimojawapo mpaka nikahisi kama kuna kitu nimekidondosha then nikafanikiwa nakuingia chumbani, nilijikongoja mpaka kitandani ambapo chumba kilikuwa nikizuri kilicholembwa na picha kubwa ukutani zikionesha mwanamke na mwanaume siku ya ndoa yao,niliangalia bila ya kuwajua ni kinanani,nikaendelea kusachi mule chumbani huku na kule mpaka nikakutana na picha mchanganyiko,
"..My God..! Mamaaaa...."
Nilijikuta natoa sauti kubwa na ya ukali baada ya kuona picha mchanganyiko zikiwaonesha bibi na bwana siku ya harusi yao,
Kumbukumbu zikaanza kunirudia taratibu nakukumbuka,
"..Gervas..! Gervas.., Kelly...! Kelly...!"
Nikawa nayatamka hayo majina huku nikijitahidi kujua atakuwa ni nani kwenye ile picha.
"Namtaka mwanangu..., namtaka mwanangu..., mwanangu... mwanangu...!"
Nikawa kama kichaa si kichaa huku nikitoka nje na kile kibaiskeli cha wagonjwa tena kwa sauti ya juu sana mpaka nilipokutana na yule mdada wa humu ndani,
"...Unakwenda wapi nyang'au wee...? Nani kakwambia utoke nje...?"
Maskini Levina mimi niliambulia kupigwa vibao na mateke kutoka kwa yule Dada wa kazi. Niliumia sana lakini haikuwa na jinsi zaidi ya kuvumilia kupigwa huku machozi na hasira vikinipanda zaidi.
"..kwanini huyu dada ananitesa hivi kila siku, nimemfanyaje lakini...?"
Nilibaki nikiusemea moyo huku kwikwi ikinipanda.

~ BAADA YA MWAKA MMOJA ~
Fahamu yote ikawa imeshanirudia ikiwa ni pamoja nakuwatambua vizuri Gervas na mkewe Jammy, muda wote nilijifanya bubu japokuwa yule dada wa kazi aliwabishia sana wakina Gervas nakuwaambia kuwa mimi naongea, kwa upande wa mavazi bado sikuwa na nguo nzuri,uwezo wakutembea nilikuwa nao lakini sikutaka wajue zaidi yakujifanya bado nang'ang'ania kukalia kile kibaiskeli, yule mtoto niliweza kumtambua nakumjua kuwa ni wakwangu tena anaitwa kelly nasiyo lauryn, alinizoea sana lakini nikawa mtu wa kuangalia ni jinsi gani nitatoroka na yule mtoto wangu.
Kila siku yule mfanyakazi anapotoka tu unakuwa mwanya kwangu wakupekuwa kila kitu cha Gervas,
Sikufanikiwa kupata pesa zaidi ya kuambulia shilingi elfu ishirini tu pamoja na hati za nyumba,gari na pasport zao za kusafiria, nilitoka nje nakumchukuwa mwanangu kisha tukatoka naye nje kabisa nakukodi teksi nakutokomea kusikojulikana.

*******
Maisha ya mimi na mwanangu hayakuwa mazuri ndani ya wiki moja toka nitoroke kwa Gervas, kwani sikuwa na eneo maalumu la kulala zaidi ya kujibanza vichochoroni huku Tandale na kila ilipofika muda wa asubuhi na mapema kazi kubwa ilikuwa ni kwenda na mwanangu mpaka magomeni usalama tena pale kwenye 'ki prefti' na kazi iliyokuwepo nikumvalisha mwanangu nguo chafuchafu nakumwacha akiomba omba kwenye magari yanapokuwa foleni pale, ilifika kipindi hadi tukawa tunapata shilingi elfu kumi na tano mpaka ishirini kwa siku,nakumbuka siku moja nikiwa nimeshamwandaa mwanangu tayari kwa kuingia barabarani mara nikamwona kama anaongea na mtu huku akinyooshea kidole eneo nililopo, nami sikusita kuwaangalia,
"My God..!, nimekwisha, nimekwisha Levina mimi, si Gervas yule...?"
Nilibaki nikitetemeka huku nikimwangalia akiwa ndani ya gari akiongea kitu na mwanangu huku akinitolea macho kwa hasira pale kwenye foleni ya magari,
Hatimaye magari yakaruhusiwa kwenda lakini cha kushangaza gari la Gervas halikwenda,likasababisha msongamano wa magari pale,lilisimama palepale kisha Gervas akashuka akamshika mtoto huku akinifuata na mimi eneo nililopo.
Niliingiwa na moyo wa kishujaa na sikutaka kumuonesha kuwa nina uoga wowote, pale pale nikainuka na kumfuata kwania ya kukutana naye na nilipomkaribia karibu,
"Gervas nipe mwanangu...?"
"Levina hivi unaakili wewe...? Kwanini umetoroka nyumbani..? Na kwanini unamtesa huyu mtoto asiyekuwa hata na lepe la shida...?"
"Embu nipe mtoto uko...?"
Nilimpokonya Gervas mtoto nakumuacha mdomo wazi huku akinishangaa kwani nilikuwa nimechenji nakuwa Levina tofauti tena yule wa kipindi kile.
Nilimchukuwa kinguvu nakutokomea naye kusikojulikana huku nikimwacha Gervas akitiwa hatiani na trafiki wa usalama.
"Levinaaa...! Levinaaa...?"
Niligeuka kwa jicho la dharau huku nikimwachia fyonyo kali,
"nani arudi...? Mpumbavu mkubwa weee..? Twende mwanangu achana naye.."
Kiukweli Gervas alikuwa ameniharibia siku kwani kwa siku hiyo sikupata chochote zaidi ya kurudi uswahilini kwetu Tandale kupumzika.

*********
Tangu Gervas aliponichefua sikuwa tena na hamu yakurudi kuendelea na biashara ya kuomba omba barabarani na mwanangu.
Nilijiepusha mbali kabisa na Gervas pamoja na Jammy,na kwa muda huu mwanangu alikuwa na umri kama miaka 4 hivyo alikuwa anatambua kipi kibaya na kipi kizuri, mradi niliokuwa nimeuanzisha ni kufungua genge dogo la kuuza angalau vijinyanya ili angalau niweze kujipatia riziki mimi na mwanangu Lauryn.
Nakumbuka siku moja nikiwa katika mizunguko yangu ya kwenda soko kubwa kwa ajili ya kujinunulia mahitaji ya jumla ya kuuza,nikakutana uso kwa uso na Jammy ambaye alionesha na yeye yupo katika hali si ya kawaida kwani alikuwa amechoka, bora yangu hata na mie,
"Levina...?"
Aliniita kinafki,nikamwangalia kwa jicho la dharau kisha,
"...unanitakia nini we mwanamke...? Umeshaniharibia maisha yangu inatosha..."
"hapana Levina, pliz nakuomba kwanza acha hasir...."
"niache nini..? embu achana na mie..."
Muonekano wake tu ulinifanya nijisikie kichefuchefu na hata hamu ya kuongea naye sikutaka kabisa.
"haya sema unasemaje...?"
Nikatulia nimsikilize anachotaka anachokisema.
"Levina, mie ndio chanzo cha yote Levina, naomba kwanza nisamehe...?"
"nikusamehe kwa lipi tena Jammy...?"
"Levina, Gervas ameniacha na yote hayo ni kwasababu yako Levina...."
"hivi wewe Jammy..?,unanifanya sina akili enh? Kwa taarifa yako tu, sidanganyiki...?"
"Levina nielewe, tangu tulipofunga ndoa na Gervas nyumba imekuwa haina amani kabisa.., amini Gervas bado anakupenda Levina..."
"ananipenda...? Na wewe je uliyefunga naye ndoa atakupeleka wapi...?"
"mimi hanitaki tena...!"
"kisa...?"
"Levina mie mgumba, na ndicho kitu kilicholeta matatizo mimi na Gervas mpaka unaniona hapa sokoni, naskia Gervas anakusaka kwa hali na mali ili mradi arudiane na wewe mlee mtoto wenu..."
"pole sana Jammy, nimekusamehe kwa yote yaliyokukuta"
Nilijikuta naingiwa na ile roho yangu ya huruma.
"kwahiyo Jammy unaishi wapi sasa hivi...?"
"sina eneo maalumu, kwani nilirudia ile biashara yangu ya zamani yakujiuza mwili na kwasasa naishi mabibo jeshini,ila ikifika jiona naenda kujiuza mwili pale manzese..na wewe unaishi wapi Levina...?"
"Tandale kwa mtogole,kama vipi twende ukapajue,naishi na mwanangu Lauryn tu...!"
"usijali Levina,siku nyingine nitakuja,ila leo nina buzi nalifukuzia pande za mikocheni nikitoka hapa..."
"sawa bwana,ngoja mie ninakunue vitu vya gengeni kwangu kisha nijiondokee..."
Tulimalizana na Jammy pale kwani alinikumbusha mbali sana haswa mema mengi aliyonifanyia kipindi anaishi na marehemu mama yangu japokuwa mabaya machache aliyenitenda.
Ile tunaachana naye tu mara,
"Levina...!, kwa ajili yako wacha nighairi huko ninapoenda,nipo pamoja nawe hadi kwako leo...!"
"twende Jammy nimefurahi sana, bado nakupenda sana rafiki yangu..."
Tuliondoka naye mpaka nyumbani kwangu.

*********
Tulipofika tu nilienda mpaka nyumba ya jirani nilipokuwa nimemuacha mwanangu Lauryn na baada ya hapo tukaelekea kwangu mpaka ndani.
"karibu Jammy jiskie upo nyumbani rafiki yangu wa zamani.."
"ahsante Levina, Levina ujue rafiki ni rafiki tu siku zote, na rafiki lazima awe na mema na mabaya na ndio maana hata anapokosea husamehewa na kuendelea na urafiki..."
Ni kweli kabisa Jammy..."
Niliingia mpaka chumbani kubadilisha nguo,kisha nikachukuwa kanga na kopo la kuogea tayari kwa kwenda chooni kuoga.
"Jammy wacha nikajimwagie maji kidogo si unajua tena kwetu uswahilini chooni ndipo bafuni...?"
Nilimwambia kiutani kisha nikaenda kuoga huku nikimwacha pale sebuleni na mwanangu,ndani ya muda mfupi nilimaliza kuoga na niliporudi ile naingia sebuleni sikuwakuta zaidi yakukutana na karatasi iliyoandikwa na kuachwa mezani.



"LEVINA...,
NAJUA NI VIGUMU KUAMINI LAKINI ITAKUBIDI UAMINI KWANI MTOTO ULIYEKUWA UNAISHI NAYE SI WAKWAKO BALI NI WAKWANGU NA MUME WANGU GERVAS,NA HAITWI LAURYN BALI ANAITWA KELLY.
MIMI SIYO MGUMBA NA HAITATOKEA,
YALE YOTE NILIYOKWAMBIA NIUONGO MTUPU ILI NIMPATE MWANANGU KELLY NA MTOTO WAKO LAURYN YUPO KWENYE KITUO CHA KULELEA YATIMA 'TAIFA LETU ORPHANS CENTRE' PALE KIGOGO,FANYA UKAMCHUKUE .
NI MIMI,
MKE WA GERVAS,
JAMMY A.K.A MAMA KELLY.


*********

Nilishtuka pale chini nilipokuwa nimelala,
"Lauryn...? Lauryn mwanangu...!"
Nilimwita mwanangu na kumfanya anishangae, kwani ni muda mrefu sijawahi kulala mchana nakumbuka nilipomaliza tu kupika chakula tukala na mwanangu kisha nikajilalia zangu,nilipokuja kushtuka kumbe yale yote yaliyonitokea na Jammy mpaka nikamleta huku nyumbani Tandale ninapoishi ilikuwa ni ndoto tena nindoto kama zile zilizokuwa zinanitokea hapo kipindi cha nyuma.
"mh Levina mie kwa kuota ndoto mbaya...?"
Nilijisemea kimoyomoyo huku nikimwangalia mwanangu kwa jicho na mdomo wa tabasamu kuonesha kuwa nampenda sana tu.
"Mama...?"
"unasemaje mwanangu...!"
"lini tutaenda kwa baba...?"
Tangu nimeishi na huyu mwanangu hajawahi kunitamkia neno kama hilo hivyo aliufanya mwili wangu usisimke sana nakunifanya nikitetemeka ni jinsi gani nitamjibu.
"Lau mwanangu...! Baba yako sasa hivi kasafiri, akirudi tu kutoka safari tutaenda sawa mwanangu...?"
"sawa mama...!"
"haya nenda kacheze na wenzako mie naenda gengeni eenh..!"
Alinielewa hivyo nikarudi gengeni kwangu ambapo huwa kuna mtu ananishkia ninapokuwa sipo.

~ BAADA YA MWAKA ~

Bado niliendelea kumdanganya mwanangu asiweze kukutana na Baba yake kwani niliamini kufanya hivyo kutaleta utata mkubwa baina yangu Jammy pamoja na Gervas mwenyewe.
Mtaji wangu ulizidi kukua siku hadi siku kwani ilifika kipindi mpaka nikajiandikisha kwenye vikoba vya kinamama (upatu) na nikawa natumia majina mengi ili nijipatie hela ya kutosha kukidhi mahitaji yangu,kiukweli ndani ya mwezi nilikuwa ninauwezo wakuingiza hadi laki 4 na nusu,ilifika muda nikahama pale nilipokuwa naishi nakupata nyumba kubwa yenye vumba vitatu na hata lile genge niliokuwanalo nikalibinafsisha nakufungua duka kubwa la bidhaa za nafaka tena la jumla na rejareja, kiukweli sijisifii ila nikweli kabisa nilikuwa na mkono wa biashara, mpaka nikafanikiwa kununua nyumba ya kuishi.
Mwanangu nilimwanzisha chekechea tena ile ya kiingereza tupu.
Habari kuhusiana na Gervas wala Jammy zilifutika kabisa akilini mwangu, jina nililotambulika zaidi maeneo haya niliokuwa naishi ni Salma au Mamaa Sammy.

Ndani ya miaka miwili na zaidi tayari nilikuwa namiliki mashine mbili za kusaga nafaka na kisima cha maji ambapo nilikuwa nikiuza maji kwa bei ya jumla na reja reja pale nyumbani kwangu hivyo nikajipatia fedha nyingi tu.

~ BAADA YA MIEZI 6 ~

Niliendelea na miradi yangu kwa muda mrefu mpaka nikafanikiwa kumiliki gari aina ya Toyota 'Noah.
Nilijizoesha mazoea ya kwenda beach na mwanangu Lauryn ambapo nilikuwa nahakikisha mwanangu anaenjoy vyakutosha, siku moja tukiwa tunatoka maeneo ya beach mara nikashangaa macho yangu yanakutana na sura kama naifahamu, niliingia ndani ya gari nakuliwasha tayari kwa kuondoka lakini kabla sijaondoka pale yule mtu alinisimamisha kwa kutumia ishara ya mkono mmoja kwani kiukweli yule mtu alikuwa ni mlemavu wa miguu,
"Jesus...! Kumbe ni Gervas,hapa kafuata nini...? Nakwanini yupo vile..?"
Maskini yule ni Gervas, na hakunitambua vizuri kama anayemsimamisha ni Levina mimi kwani nilikuwa nimevalia miwani mikubwa meusi,nilichokifanya,
"mwanangu Lauryn...? Unamuona yule mtu...?"
"ndio mama..."
"yule ni baba yako na kila ninapomuona huwa namchukia sana tu, alitutelekeza Lauryn..."
Ilinibidi tu nimweke wazi mwanangu Lauryn kwani hili dukuduku ningekaa nalo muda mrefu hivyo nilichokifanya nikutoka spidi huku nikimlenga kwania ya kumgonga, nilitoka spidi ya ajabu huku nikimfuata,
nilipomfikia karibu ile nimeanza kumgonga tu sauti kali ikatoka ndani ya gari yangu,
"Mamaaa...! Mamaaaa...! Mamaaaa usimuue babaaa....!"
Ilikuwa ni sauti ya mwanangu Lauryn kwa sura yake yenye huzuni na machozi yaliokuwa yameanza kumtoka yalinisababishia kupiga breki ya ghafla kisha nikashuka kumwangalia kama kweli nitakuwa nimeshamgonga au la..!, maskini Gervas wa watu alikuwa akitapatapa pale chini huku magongo yake ya chuma yakiwa nyang'anyang'a, umati wa watu ulianza kutanda pale nilichokifanya,
"Lauryn mwanangu.., fungua huu mlango wa nyuma haraka...!"
Aliufungua kisha kilichofuata nikumbeba Gervas hivyo hivyo nakumpakiza ndani ya gari langu na breki ya kwanza nimpaka nyumbani kwangu mikocheni.
Ndani ya dakika kama arobaini nilikuwa tayari nipo nyumbani kwangu, bado hali ya Gervas ilizidi kuwa mbaya kwani alikuwa akitokwa na damu mdomoni na puani mwake, nilichokifanya nikumpigia simu dokta wangu aje hapa nyumbani kwa ajili kumpatia huduma ya kwanza,niliogopa kama ningempeleka hospitali ya serikali ingekuwa kesi nyingne kwani mimi ndiye niliyemgonga hivyo wasingeweza kumtibia mpaka kibali toka polisi (PF3).
Baada ya kama nusu saa bado dokta niliyempigia simu alikuwa hajafika hapa kwangu, Gervas alikuwa kishapoteza fahamu na nilichokifanya,
"Aaah..! liwalo na liwe...!" nikambeba nakumpeleka kwenye gari nakumpakiza tena nakuelekea hospitali binafsi zozote ili apate kutibiwa.

~ DAVIES MODERN DISPENSARY ~

Ndio hospitali niliyofanikiwa kumpeleka kwa usiku huu kwani ilikuwa kama saa moja usiku na nilipomfikisha tu alipokelewa na manesi mbali mbali pale kisha akatundikwa dripu na mashine yakutolea hewa, muda wote mwanangu Lauryn alikuwa akitokwa na machozi lakini mimi nilikuwa kama nimepigwa ganzi kwani sikuogopa kitu sijui kwakuwa nilikuwa nikimchukia Gervas.
Madokta na manesi walihangaika kuhakikisha Gervas anapona, walimtibia majeraha yake yote niliyokuwa nimemgonga.ikiwa ni nakumpiga x- ray sehemu ya mgongoni.
Ilichukuwa kama masaa 4 pale hospitali na kwa muda huu ilikuwa imeshatimia saa 5 za usiku nikiwa bado nipo pembeni mwa kitanda cha Gervas pale hospitali mara nikamsikia Gervas akikohoa kisha akafumbua macho hapohapo yakagongana na macho yangu,nilianza kusisimka mwili wote nikamwinamia nakumpa busu shavuni mwake nakumuöngelesha,
"Gervas, bado nakupenda nanitazidi kukupenda daima..."
Nilijikuta naropoka hayo maneno kwa nguvu nakufanya mwanangu na manesi wanishangae pale,sikuridhika nikambusu tena kwa mara ya pili huku Gervas akiniangalia kwa jicho la tabasamu,
"Mama...? Unampenda kweli baba...?"
Ni sauti ya mwanangu aliyekuwa pembeni yangu na aliniona nikimbusu Gervas shavuni wakati nilishawahi kumtamkia kuwa namchukia Gervas sana.
"Lau..., huyu ni baba yako inanibidi na mimi nimpende ili tuishi naye si ndio mwanangu...?"
"ndio mama..."
Tukatoka nje na mwanangu huku nikimpisha dokta amtibie Gervas,ndani ya muda mfupi dokta alitoka nakuniita.
"Hali yake inaendelea vizuri hivyo ile dripu ni ya pili na ikiisha nafikiri itakuwa ni kesho asubuhi mtaondoka naye,ila mumeo kapata matatizo ya ndani kwa ndani haswa maeneo ya mgongoni, unaona hii x- ray inavyoonesha, hapa karibia na uti wa mgongo ndio palipoumia sana,lakini usijari kuna dawa za kuchua na za kumeza tutakupatia hiyo kesho asubuhi.

~ KESHO YAKE MCHANA ~
Kwa upande wa mwanangu Lau alikuwa kishapitiwa na usingizi lakini mimi nilijikaza mpaka nihakikishe Gervas anapewa ruhusa nakutoka naye pale.
Ile dripu iliisha nikalipia kila kitu ikiwa ni pamoja na madawa kisha nikamchukuwa Gervas na mwanangu nakwenda nao mpaka nyumbani.
"Dad..? Dad.., i love you..!, I love you dad..."
Njia nzima ilikuwa ni sauti ya mwanangu ikimwongelesha Gervas nakunifanya nisisimke njia nzima huku machozi ya furaha yakinitoka.
Haikuchukuwa muda mrefu sana tukawa tumeshafika,hivyo nikafungua kibaiskeli cha wagonjwa nilichokuwa nimepewa kwa muda kisha nikampakia Gervas nakumwendesha mpaka ndani na breki ya kwanza ilikuwa ni sebuleni nikamwacha na mwanangu Lauryn na zoezi lililofuatia nikwenda mpaka jikoni fasta nakumtengenezea uji ili japo apate nguvu sikuwa naishi namfanyakazi wa ndani zaidi ya mimi na mwanangu Lau, na nilikuwa natumia jiko la gesi hivyo haikuchukuwa muda nikawa nimeshamaliza kutengeneza uji wa ulezi hivyo nikawa naupoza kwenye bakuli huku naelekea sebuleni haraka haraka,nilipofika nilimkuta bado yupo na Lau wanapiga stori kabisa hivyo nikaanza kumnywesha uji Gervas,
"Lau mwanangu nikutume,embu nenda jikoni kaniletee tambaa la kufutia hapa chini uji umemwagika kidoogo inzi watajaa hapa"
Niliendelea kumnywesha huku mwanangu akijiendea jikoni nilipomtuma haikuchukuwa muda nikasikia kama kuna kitu kimelipuka huko jikoni halafu kimya kikatanda,
"Lau...? Lau...? wee Lauryn...?"
Kimyaa, sikusikia sauti yoyote nikamwacha Gervas pale nakukimbia hadi jikoni na nilipofika tu nilikutana moshi mzito sana kuashiria kuna kitu kimelipuka. Nilijihisi moyo kushtuka,akili kukosa nguvu na hata mwili wangu kunilegea. Nilikaa kama dakika moja nzima nikiwa katika hali ya bumbwazi. Hapo hapo nikugundua kuwa nilisahau kulizima vizuri lile jiko la gesi na ndio litakuwa limeleta matatizo,hivyo mwanangu Lau nikamkuta kadondoka chini huku anahema juu juu kuashiria kaivuta ile hewa nzito ya moshi sana,
"Gervas...? Gervas mwanetu anakufa huku nisaidie, Yesu wangu..!Yesu wangu...!, msaada jamani...?"
Mara nikashangaa Gervas anatembea tena kwa haraka haraka huku anakaribia eneo nilipo,
bado nilikuwa na marue rue,kizunguzungu si kizunguzungu kwani kila nikimwona Gervas namuona kama amesimama mara kama amekaa kwenye kibaiskeli cha wagonjwa,nafikiri sikumwona vizuri kutokana na huu moshi uliokuwa umetanda hapa jikoni,nilichokifanya
Nilimbeba mwanangu nakutoka naye mpaka nje huku nikimwacha Gervas akinifuata kwa nyuma na nilipofika nje nikagundua kuwa kumbe bado alikuwa kwenye kibaiskeli cha kubebea wagonjwa,
"Levina...? Levina....."
Aliniita Gervas kuonesha anahitaji msaada ili aongozane na mwanangu mpaka hospitali japokuwa hajiwezi hata kutembea, lakini nilichokifanya nilimuingiza Lauryn kwanza kwenye gari kisha nikamfuata Gervas pale nje,
"Gervas hali ya mtoto ni mbaya kama unavyoiona, mie wacha nikimbie kwanza hospitali narudi baadaye nivumilie kwa hilo...."
Sikuwa na jinsi nilimwacha Gervas pale ndani na baada ya hapo nikamfuata mtu anayenisaidia kuuza maji pale nje kwangu,
"we Baraka,ndani kuna mgonjwa yupo kwenye kibaiskeli cha wagonjwa,hakikisha hatoki humu ndani mie wacha nimkimbize huyu Lau hospitalini...."
"vipi kwani kafanyaje...."
"nikirudi nitakwambia wacha niende kwanza huko....."
Niliwasha gari langu nakutoka spidi breki ya kwanza ilikuwa ni hospitali ile ile niliyompeleka Gervas.
Alipokelewa nakuwekewa oxygen ili kidogo apate pumzi kidogo.
Ndani ya nusu saa mwanangu akawa mzima tu wa afya lakini tatizo kubwa alilegea sana hivyo hakuwa na nguvu zozote, alitibiwa pale kisha nikampakiza kwenye gari nakurudi naye mpaka nyumbani.
*********
Gervas alikuwa anashauku kubwa ya kumuona mwanae na tulipoingia tu alimkimbilia nakumwangalia,
"levina umeambiwaje huko hospitali...?"
"nimepewa dawa hizi hapa na ule moshi aliokuwa ameuvuta ndio umemletea kupoteza kwakè fahamu..."
Kwa hiyo kazi yangu kubwa ikawa nikuwahudumia Gervas na mwanangu Lau kwa muda moja, niliishi nao vizuri sana kwani huduma zote za kwenda msalani nilikuwa nikimsaidia mimi mwenyewe na hata kumuogesha na kumvalisha nguo Gervas ilikuwa ni jukumu langu.
Ndani ya mwezi mwanangu Lau akawa amepona na anaendelea na shule kama kawaida, nilikaa na Gervas katika kipindi chote hicho kwanza bila kumgusia chochote kilichomfanya akawa vile lakini siku moja uzalendo ukanishinda ikabidi nimuulize,
"embu niambie ukweli Gervas imekuwaje mpaka ukawa na matatizo haya ya miguu...?"
Aliinama chini kama dakika moja halafu,
"Levina....?
"abe..."
"ni stori ndefu sana Levina ila kwakuwa tuko pamoja itabidi nikwambie...."
"we niambie tu...!"
"Jammy ndio aliyepoteza muelekeo wa maisha yangu yote mpaka sasa..."
"Eenh ilikuwaje tena...?"
"ujue tulipendana naye sana baada ya kufunga ndoa, alinijali kama mume wake namie nilimjali,ilifika kipindi nilikuwa huru zaidi kwake kwa yote lakini alichokuja kunifanyia sitasahau.."
"alikufanyaje kwani...?"
"yani ninavyokwambia Jammy anatembea na bosi wangu na wamefanya kila njia kuhakikisha sina pakwenda,nilirogwa Gervas mimi..., nilirogwa Levina...!"
Maskini ile stori aliyonisimulia Gervas ilinifanya nisisimke na mchozi kuanza kunidondoka.
"Eenhe ikawaje Gervas...?"
"walinichomea moto vyeti vyangu vyote vya kazi na waliniitia wahuni nakunipiga piga na magongo nakunisababishia kuwa mlemavu mpaka sasa,maisha yangu yakawa nikuomba omba mtaani nakulala kwenye vibanda au beach kama ulivyonikuta nazurura kule..."
Gervas akiwa bado anaendelea kunisimulia mara nikasikia hodi inapigwa nje,mwanzoni nilijua labda atakuwa ni mwanangu ametoka shule lakini hodi ilipigwa tofauti na ninavyosikiaga kila siku,
"nakuja kukufungulia..."
Nilipofika tu nje nilishangaa kukutana na kundi la maaskari kama watano wakiwa na silaha kila mmoja huku wakiongozwa na mdada aliyevalia miwani kubwa meusi,alipovua miwani,
"Jammy...? Jammy umefuata nini kwangu...?"
Kabla hajanijibu chochote.
"polisi, mtuhumiwa mwenyewe huyo hapo kwenye hicho kibaiskeli cha wagonjwa mchukuweni twende..."
Maskini walimchukuwa Gervas,alikuwa mbishi wakampiga vibao nakumburuza huku wakitoka naye nje kwenye gari lao walipolipaki,
"Gervas..., Gervas..., Jammy nimekukosea nini jamani...? Gervas kakukosea nini...?"
"embu nyamaza huko...?"
Aliongea jammy kwa ukali huku akiondoka kwa mwendo wa makogo nakuniacha nikipiga makelele kwa kulia huku kwikwi ikinibana.

*************************
::: Unavyodhani kwanini Jammy ana hasira na Gervas..?? Kwanini anamfanyia yote hayo??

::: Inamaana Levina atawaacha waishi pamoja?? Nini hatma ya Levina katika simulizi hii kali na ya kusisimua, kusikitisha na hata kukutoa machozi??

::: Neno moja kwa Levina au Jammy..

ITAENDELEA

Post a Comment

0 Comments