Mapenzi ni kitu ambacho kimechukua nafasi kubwa sana katika maisha ya watu kote duniani. Mapenzi haya yanaweza kuleta furaha sana endapo mtu atampata mtu sahihi ambaye atakuwa ni muwazi, mwenye mapenzi ya kweli na kuheshimu uhusiano huo. Lakini mapenzi yanaweza kuleta karaha au kukosa amani kabisa kama kutakuwa na migogoro ambayo unakuta inasababishwa na kukosa uaminifu na kuleta ugomvi kati ya wawili wapendanao. Mapenzi haya yanaweza yakasababisha ndugu kugombana, marafiki kukosana na hata kuuana.
***** Eliza na Upendo ni wasichana warembo waliozaliwa katika familia ya kitajiri mkoani Morogoro. Wasichana hawa waliishi katika maisha ya kifahari kutokana na Baba yao Mzee Bondi kuwa na uwezo mkubwa sana kifedha. Mzee Bondi aliwapenda sana mabinti zake na alipenda wasome kwa bidii ili baadaye waje kuwa na maisha bora. Eliza na Upendo walisoma katika hali nzuri sana hadi kufikia elimu ya chuo, ambapo Upendo alikuwa akisoma Chuo Kikuuu cha Dar es Salaam na Eliza Chuo cha Uhasibu Arusha. Kutokana na masomo walitengana na kuonana mara chache kipindi cha likizo. Baadaye Eliza na Upendo walijikuta wakijiingiza katika uhusiano wa kimapenzi wote wawili kwa kijana mmoja mtanashati aliyeitwa James bila kujijua. Uhusiano wa kimapenzi kwa mwanamume mmoja ulileta migogoro katika familia yao.
********* Baada ya kumaliza Kidato cha Sita Upendo alipangiwa kwenda kuendelea na masomo ya Chuo Mkoa wa Dar es Salaam. Baba yake alifurahi sana na kumuahidi kuwa angempa zawadi nono kama angefanya vizuri akiwa Chuo. Kabla ya kujiunga na chuo Upendo alifanyiwa sherehe kubwa ya kumpongeza, ambayo ilihudhuriwa na watu wengi sana ndugu jamaa na marafiki. Wakati huo mdogo wake Eliza alikuwa Kidato cha Sita kwani walipishana mwaka mmoja tu na kwa jinsi walivyokuwa, walionekana kama mapacha. Wakati mwingine ilikuwa ni vigumu kwa watu ambao walikuwa hawajawaona kujua mkubwa ni yupi na mdogo ni yupi. Siku zilipokaribia za kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Upendo alijiandaa barabara kwa ajili ya kuanza masomo ya Chuo. Siku moja kabla ya kuondoka Mama na Baba yake walimwita na kuzungumza nayemazungumzo ili kumwasa na kumpa ushauri. “Upendo tumeishi wote kutoka ukiwa mdogo, hujawahi kuishi mbali nasi kuanzia masomo ya elimu ya shule ya msingi hadi elimu ya Sekondari. Umesomea Morogoro, sasa unakwenda Dar es Salaam kuanza maisha mapya ya kuishi mbali na sisi. Ninakuomba ukasome kwa bidii ili ujiandalie maisha yako ya baadaye.” Mzee Bondi alimaliza kutoa nasaha zake, huku Upendo akisikiliza kwa makini kabisa. “Umsikilize baba yako kwa makini kwa sababu dunia ya sasa imeharibika mwanangu. Magonjwa ni mengi na ukifika huko sio ndio ukasahau kilichokupeleka. Kumbuka kinachokupeleka ni masomo na sio starehe. Nadhani umenielewa.” Alisisitiza Mama yake. “Jamani Mama nitasoma kwa bidii mbona unaongea hivyo.” Upendo alihamaki “Lazima niongee mwanangu vijana wa sasa mnakutana na mambo mengi na vishawishi vingi usipokuwa makini utapoteza kabisa mwelekeo na malengo yako.” Mama upendo aliendelea kutoa nasaha. “Baba na Mama nimewasikia, kamwe sitoenda kutenda yasiyo sahihi, nitasoma na nitawafurahisha siku zote wazazi wangu.” Upendo alijibu kwa unyenyekevu. Baada ya maongezi hayo wote walisimama na kuelekea kulala ili Upendo akaanze kujiandaa na safari. Upendo aliingia chumbani na kuanza kupanga vitu vyake akisaidiana na mdogo wake Eliza. “Ndugu yangu si nilikuwa nimekaa na Mama na Baba sebuleni wananipa wosia namna ya kuishi huko Chuo.” Alisema Upendo. “Eheh! Ilikuaje? Kwa sababu Mama naye akiamua kuongea ni balaa wamesemaje hao wazee?” Alidadisi Eliza. “Mwenzangu, Baba na Mama wameniambia nikienda nisisahau kilichonipeleka nisiendekeze starehe.” Alisema Upendo. “Heh! Hao wazee nao inamaana ukakae tu unasoma hata disko usijichanganye? Aka mwaya sisi bado vijana lazima tujirushe we ngoja mi nimalize Kidato cha Sita nikienda chuo nitajirusha sana kwani hapa nyumbani hawa wazee wanatubania sana.” Alizungumza Eliza. “Usiseme hivyo mdogo wangu mimi naona Baba na Mama wapo sahihi, kwani nikianza kujiingiza kwenye starehe nitajikuta nafeli mitihani halafu malengo yangu ya kuwa mwanasheria yasitimie, we mwenzangu unawaza kujirusha tu.” Alijibu Upendo. “Kujirusha ni wajibu na kusoma nitasoma tu, haya bwana tufanye haraka tuwahi kulala hao wazee watakuamsha mapema kesho.” Alimaliza Eliza. Kesho yake asubuhi na mapema Mama yake Upendo alimwamsha na kumshauri Upendo ajiandae kwani safari ingeanza saa nne asubuhi. Eliza siku hiyo hakwenda shule ili amsindikize dada yake. Walikunywa chai kwapamoja na tayari baba yao alikuwa amejiandaa kwa safari. Waliondoka na usafiri wao binafsi hadi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kumwacha Upendo. Upendo alimwaga mama yake na mdogo wake akiwa na huzuni kutokana na kuanza maisha mapya. Upendo alipangiwa kuishi katika hosteli za mabibo ambazo zipo kandokando ya barabara ya Mandela upande wa kulia kutokea Ubungo kuelekea Buguruni. Akiwa chuoni Upendo alikukutana na watu mbalimbali. Alijitahidi sana kusoma kwa bidii akiwa na uwezo mzuri darasani aliweza kufaulu vizuri mitihani yake. Eliza naye alimaliza Kidato cha Sita na kupangiwa kwenda kusoma Chuo cha Njiro Mkoa wa Arusha wakati huo Upendo alikuwa amebakiza mwaka mmoja ili amalize Chuo. Upendo aliishi vizuri na alipendwa sana na wanafunzi kutokana na juhudi zake katika masomo na tabia yake nzuri aliyokuwa nayo, hivyo alikuwa na marafiki wengi na pia walimu walimpenda sana. Wakati akikaribia kumaliza chuo Upendo alipata rafiki wa kiume aliyeitwa James ambaye alikuwa ni mfanyabiashara. James naye alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku za nyuma lakini aliamua kufanya kazi zake binafsi kutokana na ajira kuwa ngumu. Kadiri siku zilivyozidi kwenda urafiki wa James na Upendo ulikua na kuimarika sana kiasi kwamba watu waliokuwa wakiwaona pamoja walijua ni mke na mume. Siku moja James akiwa amekaa nyumbani kwake maeneo ya Kinondoni aligubikwa na wazo zito kuhusu Upendo. “Mimi na Upendo ni marafiki wakubwa sana na huyu binti ni msichana ambaye anajiheshimu sana tokea nilipomfahamu, nimempenda sana kutoka moyoni mwangu natamani awe mama wa watoto wangu. Kwa vile sijawahi kumtamkia lolote juu ya suala la mapenzi kwa kipindi chote cha kufahamiana kwetu, nahisi nikimdokeza tu pengine anaweza akachukia.” Aliwaza James huku akitamani kumwambia Upendo kuhusu alilonalo moyoni mwake. Zilipita siku kadhaa kila James akionana na Upendo akawa anataka kumwambia lakini alikuwa anasita. Siku moja alipanga kumtoa Upendo ili kwenda naye sehemu tulivu apate fursa nzuri na adimu ya kumwambia Upendo juu ya mapenzi aliyonayo moyoni mwake. Ilikuwa siku ya Ijumaa James aliyopanga kumtoa Upendo jioni yake kwenda katika matembezi. Alipomweleza Upendo juu ya azima yake ya kutoka naye alikubali bila pingamizi. Ilipofika jioni ya saa kumi na mbili hivi James alikwenda Hosteli ya Mabibo na gari yake aina ya Benzi kumchukua Upendo. Alipofika Hosteli block A chumba namba 228 alimkuta Upendo akiwa tayari amejitayarisha kwa ajili ya matembezi ya jioni. Upendo alivalia vazi la kutokea jioni ambalo lilimkaa barabara likionyesha vizuri jinsi Mungu alivyompendelea kimaumbile. Alipendeza sana kiasi kwamba James alijiona ni mwanamume mwenye bahati kama angefanikiwa kumpata kimapenzi. James aliendesha gari kuelekea Sinza eneo liitwalo Madukani katika Mgahawa uitwao “Fast Food and Take Away” ambao ulikuwa na utulivu na hali ya hewa nzuri. Walichagua sehemu nzuri na kwenda kukaa pamoja. James alimpa Upendo uhuru wa kuagiza chochote alichopenda kula na kunywa. Waliletewa vinywaji na kuanza kunywa huku wakisubiri chakula. Muda wote mapigo ya moyo wa James yalikwenda mbio akiwaza namna ya kuanza kumwambia Upendo suala la mapenzi. Baada ya kama dakika ishirini hivi za maongezi ya kawaida James aliamua kumwaga sera zake. “Upendo umependeza sana leo hilo gauni ulilovaa limekupendeza sana.” James alianza kwa kumsifia Upendo. “Asante James mbona hata wewe umependeza.” Wote wakacheka na kugonganisha mikono. James alivuta kiti chake na kusogea karibu na Upendo huku moyo wake ukiwa bado unamdunda macho yakiwa na rangi nyekundu kwa hofu ya kumwambia Upendo kuwa anampenda. James alijikaza na kumshika Upendo mkono. “Upendo kuna kitu kinanisumbua sana moyoni mwangu, kitu hicho kimekuwa kinanitesa kwa muda mrefu sana tangu tufahamiane.” Aliongea James huku midomo ikimtetemeka kidogo. “James! Ni kitu gani hicho jamani?” Aliuliza Upendo kwa sauti ya mahaba na macho yake ya kurembua. “Ni kitu cha kawaida sana lakini…” “Lakini nini?” Alimkatisha Upendo akiwa ananyanyua glasi ya soda na kuinywa huku akimwangalia James usoni. “Nitakwambia kitu hicho jioni hii ya leo ingawa kitu hicho kinaweza kuharibu au kuboresha urafiki wetu.” Aliongea James kwa kujihami ili apate ujasiri wa kusema. “We sema tu James, ni jambo gani hilo ambalo unasita kuniambia wakati kuna mambo mengi sana tumekwishaongea mimi na wewe tangia tufahamiane.” Upendo aliongea kana kwamba anampa uhuru wa kusema linalomsumbua James. “Upendo! Aliita James kwa sauti ya chini sana huku akijitahidi kuyakwepa macho ya Upendo. Abee!” Aliitikia Upendo. “Ahhm! Tangu tufahamiane nimetokea kukupenda zaidi ya urafiki tulionao.” James alitulia kidogo huku safari hii akimwangalia Upendo usoni. Kabla Upendo hajasema kitu James aliendelea kumwaga sera zake huku Upendo akiwa kimya. “Ningependa uwe mpenzi wangu na baadaye Mungu akitujalia uwe mama wa watoto wangu.” Aliongea James akimkazia macho Upendo. Upendo aliyekuwa ametulia akimsikiliza aliutoa mkono wake mikononi mwa James ambaye alikuwa amemshika, huku akiinama na kuminyaminya vidole vyake kwa aibu. “Mh! We James! Ina maana hadi sasa hauna mwanamke kijana mzuri kama wewe acha hizo bwana mbona si kitu cha kawaida.” Alihoji Upendo. Ni kweli Upendo lazima utafikiria hivyo, ila nakwambia ukweli kutoka moyoni mwangu, sina mwanamke yeyote. Ila niliwahi kuwa na mpenzi zamani kidogo tukakorofishana na kwa sasa ameolewa. Nilikuwa nampenda sana ila aliniumiza moyo wangu nikajikuta sitamani kuwa na mwanamke tena maishani mwangu. Lakini tulipoanza urafiki mimi na wewe nimegundua kuwa nahitaji kuyaanza maisha yangu upya. Nimekupenda sana Upendo nipe nafasi katika moyo wako.” Alibembeleza James. “Je, kwa sasa huyo aliyekuwa mpenzi wako anaishi wapi?” Aliuliza Upendo. Alikuwa anaishi hapahapa Dar lakini baada ya kuolewa alihamia Mbeya na mume wake. “Mmmh!! Hapana James kwa sasa, naona tuendelee kuwa marafiki, ila nitakujibu kuhusu ombi lako siku yoyote.” Alimjibu Upendo hukuakitafakari kitu.
“Nikupe muda gani Upendo.” Alihoji James huku akishusha pumzi kwa nguvu. Kisha akaendelea kuongea. “Nashindwa hata kusubiri. Ila sawa nitakupa muda ili uweze kunifikiria, fahamu kuwa nakupenda na ni wewe pekee unaye utesa moyo wangu kwa sasa. Natumaini nitapata jibu zuri. Au siyo?” Aliuliza James huku akitabasamu na kuweka mkono wake wa kulia begani kwa Upendo. “Jamani mbona una haraka hivyo usijali tutaona itakavyokuwa.” Alijibu Upendo huku akitabasamu kama alivyofanya James lakini akiuondoa mkono wa James uliokuwa juu ya bega lake. Baada ya hapo chakula kilikuwa tayari kimeletwa, walikula na kuendelea kunywa vinywaji vyao na kuzungumza mambo mbalimbali. Ilikuwa tayari imetimia saa tatu za usiku. “Heh! Kumbe muda umeenda hivi hebu nirudishe hostel James, nina kazi za chuo sijazimaliza.” Alitamka Upendo. “Acha hizo Upendo yaani saa tatu tu ndo muda umeenda. Mimi ningependa twende na disko lakini kwa vile umesema kuwa una kazi za kufanya, sina namna ngoja tu nikupeleke. Ila tumalizie vinywaji kwanza.” Alishauri James. Baada ya kumalizia vinywaji waliondoka kuelekea hosteli. Wakiwa njiani, James aliendelea kubembeleza na kusisitiza juu ya ombi lake. “Please (nakuomba) usiache kunifikiria nakupenda sana Upendo.” Alisisitiza James. Upendo alinyamaza kimya huku akimwangalia James bila kumjibu chochote. Walipofika hosteli kabla hajashuka katika gari James alimshika mikono yote miwili kisha akamkumbatia na kumbusu shavuni. “Nakupenda sana Upendo. Nakutakia usiku mwema na ndoto njema.” Aliongea James wakati akiendelea kumbusu huku Upendo akijaribu kumzuia. Mapigo ya moyo yalimwenda mbio Upendo, huku akijitoa kifuani kwa James. “James asante kwa yote nakutakia usiku mwema nawe.” Alishukuru Upendo kisha akashuka kwenye gari na kuingia hosteli huku James akiondoka kuelekea Kinondoni. Usiku kucha Upendo aliwaza sana akimwaza James moyoni mwake. “Mmh! Mmh! James ni kijana mtanashati siwezi kumpoteza nampenda pia. Lakini wanaume nao hawatabiriki, leo ananibembeleza sana akidai kuwa ananipenda halafu akinipata ataniacha. Ikitokea hivyo ataniumiza moyo wangu sana. Mmh! lakini sidhani kama James atakuwa hivyo, natamani awe baba wa watoto wangu. Sijui nimpigie simu ni mwambie sasa hivi! Lakini hapana! Aa! Hebu ngoja nimpigie sasa hivi.” Alichukua simu yake na kuanza kumpigia simu James, Wakati simu ikiwa inaita Upendo alikuwa na hofu kubwa. “Haloooo! Alipokea simu James. “Yaani nilitaka kukupigia simu muda huu umeniwahi, niambie mpenzi wangu.” Aliongeza James bila kumpa nafasi upendo ya kuongea. “Aha vipi James uko wapi? Unafanya nini saa hizi? Unajua kuna kitu nataka nikwambie ila basi, nitakwambia kesho, usiku mwema.” Akakata simu Upendo. “Aah! Kakata simu.” Aliwaza James kisha akaamua kupiga yeye. “Halooo! Mbona umekata simu kabla hatujamaliza maongezi? Aliuliza James “Haya niambie ulichotaka kuniambia kwani natamani sana kusikia kutoka kwako la sivyo utanifanya nisilale.” Aliomba James. “Hakuna kitu jamani James nilikuwa nataka kujua kama umefika salama.” Alijibu Upendo. Usiku ule Upendo hakumwambia chochote James akabaki akijilaumu baada ya kukata simu huku akiwaza; “Hivi kweli nimeshindwa kumjibu! Ila kesho tukionana nitamwambia.” Upendo aliendelea kumwaza James hata kusoma kulimshinda usiku ule akaamua kulala. Kesho yake ilikuwa ni siku ya Jumamosi, asubuhi Upendo aliingia darasani kujisomea kama kawaida yake. Ilipofika saa sita na nusu aliamua kurudi hosteli. Akiwa chumbani na rafiki yake Grace aliamua kutoka nje ili apate muda mzuri wa kutafakari kuhusu ombi la James. Alimuaga Grace na kumwambia kuwa atakuwa chini ya mti mkubwa ulio nyuma ya hosteli akijipumzisha. Baadaye James alikuja pale chumbani kwa Upendo bila taarifa, baada ya kugonga mlango na kuruhusiwa kuingia alimkuta Grace akiwa amejilaza kitandani akisoma gazeti. “Habari gani dada!” Alisalimia James. “Nzuri kaka karibu kiti.” Alijibu Grace. “Asante dada. Aaahmm! Nimemkuta Upendo?” Aliuliza James huku akitabasamu. “Ndiyo! Ila yupo nje amekaa chini ya mti mkubwa nyuma ya jengo hili.” Alijibu Grace huku akiamka na kukaa vizuri kitandani. “Haya asante hebu nimfuate.” Aliaga James na kuondoka. Upendo alikuwa amekaa kwenye kiti cha plastiki huku amegeukia uzio unaozunguka hosteli akichezea tawi dogo la mti. Mara James alikuja kimyakimya akitokea kwa nyuma na kumziba Upendo usoni bila ya yeye kumwona akiwa amebeba chakula kwenye mfuko. Upendo alishtuka sana katu asijue ni nani aliyemziba macho. “Nani tena jamani? Mimi huwa sipendi michezo ya hivi.” Alilalamika Upendo. “Usiogope Upendo ni mimi.” James alitoa mikono yake na kumbusu Upendo. “Waoo! James mbona hukunipigia simu kunitaarifu kama unakuja?” Aliuliza Upendo huku akisimama kupokea mfuko aliokuwa ameubeba James. “Nimekuletea chakula cha mchana Upendo.” Alitamka James bila kujibu swali aliloulizwa. “Mmh! Nilijua ni watu wameamua kunichokoza. Asante sana kwa kuniletea chakula, umejuaje James kwani mpaka saa hizi sijala njaa inaniuma kweli. Ehee! umeniletea chakula gani?” Aliuliza Upendo. “Fungua uone.” Alijibu James. “Ooh! Chipsi na kuku napenda sana chakula cha aina hii, vipi njoo basi tule wote.” Aliongea Upendo kwa shauku huku akimalizia kufungua mfuko. Upendo alichukua maji ya chupa aliyokuwa nayo na kumwomba James anawe mikono ili wale wote. “Hapana mimi nimeshakula we kula tu usijali nimekuletea wewe.” Alijibu James huku akipokea chupa ya maji ili kumnawisha Upendo. Akiwa anaendelea kula Upendo alikuwa ana mawazo mengi sana juu ya James. “Upendo napenda sana uwe mke wangu, kwa nini unaamua kuutesa moyo wangu hivi?” Aliuliza James huku akimwangalia Upendo kwa kumtamani. “Kwanini unasema nakutesa James nataka tu kuwa na uhakika kwani naogopa sana kudanganywa.” Alijibu Upendo huku akimwangalia James kwa kurembua macho. “Niamini Upendo, mimi kamwe siwezi kukudanganya nakupenda kutoka moyoni mwangu.” Alijibu James huku akimkazia macho upendo. “Kweli James? Hata mimi nakupenda sana James ila...” Alisita Upendo. “Ila nini.” Aliuliza James huku akiweka mkono wake begani kwa Upendo. “Ngoja nije.” Aliinuka Upendo kuekelea chumbani kwake akimwacha James akishangaa kulikoni. Baada ya dakika kama tano, Upendo alirudi akiwa ameshika bahasha mkononi iliyoandikwa “JAMES” ambayo aliiandika usiku ule, ili wakionana ampe. James alimwangalia Upendo kwa mshangao asijue chochote. “James! Nimefikiria sana kuhusu ombi lako, nikatamani kukujibu usiku kwenye simu, lakini ulimi ulinikwama nikashindwa kuongea. Hivyo majibu ya ombi lako yako humu.” Alimaliza kuongea Upendo huku akimkabidhi James ile bahasha. James alipokea ile bahasha huku mkono ukitetemeka kidogo na kumwangalia Upendo usoni ambaye aliukwepesha uso wake na kuangalia pembeni kwa aibu. Kisha akaamua kuifungua bahasha na kusoma yaliyokuwemo ndani kwa makini huku akiinuka kumwangalia Upendo, ambaye sasa alikuwa amefunika uso wake kwa viganja vyake vya mkono. Haya ndiyo maneno aliyoyakuta James: Mapenzi ni matamu kama asali wawili tukipendana. Mapenzi ni machungu wawili tukisalitiana. Mapenzi ni zawadi daima tukipendana. Mapenzi ni lulu dhati tukipendana. Mapenzi ni kufa na kuzikana. Nakupenda Uwe Baba! Watoto! Wangu! Baada ya kumaliza kusoma ile karatasi James alimwendea Upendo na kumnyanyua kisha akamkumbatia huku naye Upendo akizungusha mikono yake na kumkumbatia James kwa nguvu kiunoni. “Nashukuru sana mpenzi nakuahidi wewe ndio mke wangu.” Aliongea James huku akiendelea kumrushia mabusu motomoto, huku naye Upendo akijibu kwa kumbusu James ikiwa ni ishara ya kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa James na Upendo.
************* Baada ya miezi sita ********************
Baada ya mapenzi kukolea James aliamua kumtambulisha Upendo kwa wazazi wake. Baba na mama wa James walimpenda sana na kuwashauri wafunge ndoa pindi tu Upendo akimaliza Chuo. Upendo alikuwa ndo anaingia mwaka wa mwisho ili ahitimu katika shahada ya Sheria. Kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele James na Upendo waliyafurahia sana mapenzi yao. Ili kuimarisha zaidi uhusiano wao James alimwomba Upendo waende kwa wazazi wake ili kutambulisha rasmi. Basi walipanga safari ya kwenda Morogoro ambako walipokelewa vizuri sana na wazazi wa Upendo. Baadaye wazazi wa Upendo waliwaasa juu ya uhusiano wao kuwa usiathiri masomo ya Upendo. Wazazi wake Upendo walishauri kwamba Upendo amalize Chuo kwanza na atafute kazi ndipo wafikirie suala la kufunga pingu za maisha. Wakati James akiwa Morogoro mdogo wake Upendo alikuwa chuoni. Baada ya kukaa siku kadhaa Morogoro James na Upendo walirudi Dar es Salaam. Kutokana na ushauri wa wazazi wa pande zote mbili maisha ya James na Upendo yalikuwa ni ya furaha siku zote yenye mategemeo mazuri katika kuleta maendeleo ya maisha yao ya baadaye.
Akiwa chuoni Upendo alisoma kwa bidii sana na James aliendelea na biashara zake. Siku moja Upendo alimpigia simu mdogo wake na kumwambia juu ya uhusiano wake na James. “Haloo! Mambo mdogo wangu! Mzima wewe! Habari za Chuo?” Ilikuwa ni sauti ya Upendo katika simu. “Nzuri ndugu yangu mambo magumu sana chuoni, bora wewe mwenzangu unakaribia kumaliza.” Alisema Eliza. “We! Hakuna cha uafadhali wowote na hiyo mitihani inavyokuja migumu nimetingwa ile mbaya. Kumbuka wewe si ulisema ukienda chuo utajirusha sana. vipi imekuaje.” Aliuliza Upendo. “Yaani, we acha tu ‘my sister’ (dada yangu) sina hata huo muda wa kujirusha nikicheza mbona nitafeli mmh nipe umbea maisha vipi.” Alihoji Eliza. “We nawe kwa umbea, Eliza mwenzio nimepata mchumba nikimaliza Chuo naolewa.” Alisema Upendo huku akicheka. “Usiniambie! Hongera mwaya, haya huyo shemeji anafanya kazi gani?” Aliuliza Eliza. “Ni mfanyabiashara na pia huwa anakuja Arusha mara kwa mara, nadhani mtaonana au ukija likizo utamwona. Nyumbani nilishampeleka kumtambulisha kwa wazazi.” Alieleza na kufafanua Upendo.“ “He! Kumbe mmefika mbali hivyo hata kuniambia mwenzio.” Alilalamika na kulaumu Eliza. Eliza huku akiwa na shauku ya kutaka kumfahamu shemeji yake, Upendo akajitetea; “Wala sio hivyo ‘my young sister’ (mdogo wangu) mambo yalikwenda harakaharaka lakini, utamfahamu na wewe ndiye utakuwa mstari wa mbele kwenye harusi yangu.” Aliongea Upendo kwa majivuno. “Haya bwana mimi nakutakia mafanikio mema Mungu awajalie mfikie malengo yenu.” Alisema Eliza basi wakaendelea kuzungumza na baadaye walikata simu na kuendelea na mambo mengine. Kutokana na kazi kuwa nyingi za kusafiri mara kwa mara James alipata safari ya kwenda Arusha kikazi. Wakati huo ilikuwa ni kipindi cha mitihani kwa Upendo basi, waliagana. Siku hiyo walikuwa pamoja ikiwa ni siku moja kabla ya James kuondoka . “Mpenzi wangu, utanikosea sana ukichelewa kurudi si unajua nimekuzoea.” Aliongea Upendo kwa sauti ya mahaba. “Usijali mpenzi ni kazi zinanifanya nisafiri nitawahi kurudi ila na wewe si una mitihani kwa sasa inabidi usome kwa bidii ili ufaulu vizuri sawa mama?” Aliongea James huku akimsogeza Upendo kifuani mwake na kumkumbatia. “Sawa lakini si unajua sipendi kukukosa siyo uende huko ukanisahau kwa kujirusha na vimwana vya Arusha.” Upendo alisisitiza. “Ina maana huniamini mamii nakupenda sana hakuna mwanamke wa kunidanganya wala usijali.” Alijibu James huku akitabasamu. Walizungumza sana siku ile wakiwa nyumbani kwa James na baadaye walikwenda kupumzika. Kesho yake mapema saa mbili asubuhi James aliondoka na huku akisindikizwa na mpenzi wake hadi uwanja wa ndege tayari kwa kuanza safari. Baadaye Upendo alirudi chuoni kuendelea na masomo. Alipofika Arusha James alikwenda moja kwa moja hadi katika hoteli ya Ngurdoto yenye mandhari nzuri sana. Alipata chumba na baada ya kuingia kwenye chumba chake alimpigia simu mpenzi wake kumtaarifu kuwa amefika salama. “Mambo mpenzi wangu! Nimefika salama nipo Hoteli ya Ngurdoto natamani tungekuwa pamoja,” Aliongea James kutoka Arusha. “Hata mimi pia natamani tungekuwa pamoja mpenzi, ila majukumu ndiyo yanatubana. Hapa nilipo najisomea yaani hii mitihani inayokuja inaniumiza kichwa sana.” Aliongea Upendo kwa unyenyekevu. Nakuomba usinisaliti mpenzi, najua kuna wanaume wengi wanakufuatafuata. Ziba masikio yako usisikie neno lolote kutoka kwa mwanamume yeyote. Alitahadharisha James. “Mmh we nawe kwa wivu, nakupenda sana siwezi kufanya hivyo hata siku moja.” Alijibu Upendo. Baada ya mazungumzo kila mmoja aliendelea na mambo yake. Akiwa Arusha James alianza kufanya kazi zilizompeleka akiwa na marafiki zake ambao ni wenyeji wa huko walizunguka sehemu mbalimbali ikiwa ni wiki mbili tangu James aondoke Dar es Salaam. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya Ijumaa muda wa saa mbili usiku ambapo James na marafiki zake walikwenda katika matembezi maeneo ya Sakina. Walipofika huko walikunywa sana pombe huku wakiwa wanafurahi pamoja wakati huo walikuwa Sakina Bar, waliendelea kunywa hadi ilipofika saa tano usiku. “Aisee washikaji kwa nini tusiende disko Triple A.” James aliyekuwa ameshalewa aliwashauri wenzake. “Swadakta! Hilo neno! Washikaji twendeni disko sijaenda siku nyingi sana nadhani itakuwa safi sana.” Mmoja wao aliongea huku akionyesha ishara ya kuondoka. Walikubaliana na kuanza safari ya kwenda ukumbi wa Disko wa Triple A ambao haukuwa mbali sana na mahali walipokuwa. Kabla ya kupanda gari waliokuwa nalo James alichukua simu yake na kumpigia Upendo. “Haloo mamii vipi umelala mamaaa!” Aliongea James. “Safi mpenzi wangu nilale kwa raha gani niliyonayo? Hapa nilipo nipo bize sana na maandalizi ya mitihani. Vipi uko wapi mbona nasikia kelele?” Alijibu na kuuliza Upendo. “Nipo na washikaji tunafurahi mpenzi wangu. Mimi nakutakia usiku mwema.” Alijibu James ambaye hakusema kama alikuwa anaelekea disko. “Vipi James yaani huyo mwanamke amekubana mpaka umwambie unakwenda wapi? Kweli ninyi ndiyo wale hata ukitaka kula utampigia simu na kumwambia unachokula. Aaa! hebu twendeni alishauri Rama mmoja wa rafiki zake wapendwa wa James. “Acha hizo Rama huyu mama watoto wangu na kuhusu disko sijamwambia kwani ingekuwa balaa muda huu”. Alijibu James huku akitabasamu. Walipofika disko walikaa na kuendelea kunywa sana. Huko disko kulikuwa na watu wengi wakiwemo wasichana warembo sana ambao James na marafiki zake walianza kutafuta wasichana wa kucheza nao. James alisimama na kumfuata dada mmoja aliyekuwa amekaa karibu naye na kumuomba wacheze. Yule dada alikubali na kusimama na kuanza kucheza naye. Kama kawaida, katika kucheza kuna mambo mengi, wakiwa wanacheza James alimshika yule dada mkono na kumsogeza pembeni sehemu iliyokuwa haina kelele na kufanya mazungumzo naye. “Mrembo umependeza sana, halafu unajua kucheza sijui unaitwa nani.” Aliuliza James huku akimwangalia kwa makini yule dada usoni. ”Asante kaka mimi naitwa Esta.” Alijibu yule msichana huku akitabasamu na kurembua macho. “Una jina zuri sana Esta kama ulivyo mwenyewe.” Alisema James huku akimtazama Esta ambaye alikuwa akitabasamu. “Mbona wewe hujaniambia jina lako.” Aliuliza yule msichana. “Usijali mrembo mimi naitwa Juliasi.” Alijibu James. Basi wakafahamiana na kuendelea kucheza pamoja baadaye James alimwomba Esta waondoke pamoja naye Esta alikubali na kuondoka huku akiwaacha marafiki zake bila hata ya kuwaaga. Walichukua teksi nje na kuelekea katika hotelini, wakiwa njiani walikuwa wamekumbatiana kila mmoja akimwambia mwenzake maneno ya kimahaba hadi walipofika hotelini na kuingia chumbani. Wakiwa ndani James alikuwa amechoka sana kutokana na pombe alizokunywa. Lakini Esta yeye alikuwa amelewa kidogo hivyo alimsogelea James na kumvua shati taratibu pamoja na suruali yake kisha kumwacha akiwa katika bukta. Baada ya kumaliza kumvua kila kitu alimpandisha kitandani James akawa ametulia kimya kama vile amemwagiwa maji. Naye Esta alivua nguo zake na kuziweka pembeni na kisha akamsogelea James. “Juliusi we ni mwanamume mzuri sana nafurahi kuwa pamoja na wewe haijawahi kunitokea nikamwamini mwanaume kwa haraka kama ilivyo kwako nimekupenda naomba usiniache.” Esta aliizungumza maneno huku akiwa anamshika katika paji la uso naye James taratibu alinyanyuka na kuanza kumbusu Esta bila hata ya kuzungumza lolote huku akimkumbatia na baadaye walilala usingizi wa pono. Ilipofika asubuhi Esta aliamka na kwenda kuoga wakati James alikuwa bado amelala usingizi mzito. Baada ya Esta kutoka bafuni alikaa katika sofa lililokuwa pale chumbani huku akiwa anamsubiri James aamke. “Mmh sijawahi kupenda kiasi hiki huyu mwanamume sijamfahamu vizuri ni siku moja tu lakini nimempenda sana naamini atakuwa ni mwanamume wa maisha yangu.” Aliwaza Esta huku akimwangalia James. Wakati akiwa anaendelea kuwaza mara ghafla James aliamka kutoka usingizini na kukaa pale kitandani huku akionekana kuchoka sana. “Habari za asubuhi Juliasi mpenzi wangu umelala sana”. Esta alimsalimia James. “Jana nilikuwa nimekunywa pombe nyingi sana vipi unaweza ukaondoka tu muda huu usijali mimi nipo sawa tu.” Alijibu James. “Sawa mpenzi mimi nitaondoka kwani hata hivyo nilikuwa na kazi ya muhimu naifuatilia ila naamini usiku tutakuwa pamoja nataka tuzungumze zaidi.” Esta alisema huku akiwa ananyanyuka na kumsogelea James kisha kumbusu na kuchukua mkoba wake kuondoka kwa furaha sana. James alichukua waleti yake na kutoa kiasi cha shilingi laki moja na kumkabidhi Esta. “Nimefanya nini mimi nimemsaliti mpenzi wangu Upendo itabidi niwe makini sana hiki kitu asikifahamu vinginevyo itakuwa balaa.” Aliwaza James baada tu ya Esta kuondoka. Basi James alinyanyuka na kwenda kuoga na baadaye aliendelea na kazi zake kama kawaida. Ilipofika jioni Esta alimpigia simu James na kutaka kuonana naye. James alimtaka Esta aende hotelini usiku ili waendelee na huo mchezo huku James akiwa anafanya kwa siri Upendo asijue. Ilipita kama miezi miwili hivi James akiwa bado yupo Arusha akiwa anaendelea na shughuli zake na bado akiwa na uhusiano wa kimapenzi kwa siri na Esta.
*********
****************** Huko Dar es Salaam Upendo alikuwa mpweke sana kwani alikuwa amemaliza mitihani ila hakwenda Morogoro alibaki Dar es Salaam na alikuwa akiishi katika nyumba ya James Kinondoni. Wakati wote walikuwa wakiwasiliana na mpenzi wake vizuri. James alitakiwa kukaa Arusha kwa muda wa miezi minne ndio shughuli zake zitakuwa zimekamilika, kwa hiyo alikuwa akimtaka Upendo avumilie na waendelee na mikakati ya kufunga ndoa ili punde akirudi tu wafunge ndoa. Upendo aliendelea na mikakati ya harusi huku akishirikiana na wazazi wake pamoja ili kuandaa sherehe ya kumuaga Upendo. Akiwa katika mikakati ya harusi alimpigia simu mdogo wake ili kumjulisha mambo yanavyoendelea. Simu iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa lakini baadaye ilipokelewa. “He! We Eliza mbona umechelewa kupokea simu?” Aliuliza Upendo. “Mh dada samahani nilikuwa bafuni, ehe niambie.” Alijibu Eliza. “Ndugu yangu natamani ungekuja huku unisaidie katika mipango ya harusi yangu vipi mnafunga lini chuo?” Aliuliza Upendo. “Makubwa! Kweli mapenzi yamepamba moto ndio unaolewa na huyo shemeji hata simjui jamani?” Alihamaki Eliza. “Wewe nawe! Utakuja kumwona siku ikifika. Kwanza yupo huko Arusha lakini ametingwa sana sijui kama mtaweza kuonana.” Alisema Upendo. “Hee! Jamani kweli shemeji yangu yupo huku halafu huniambii? Vibaya hivyo dada yangu, sasa kuhusiana na mimi kuja huko kukusaidia hiyo mipango yako ya harusi kwa sasa itakuwa vigumu kwani najiandaa na mitihani itakayoanza mwezi ujao.” Alijibu Eliza. “Jamani Eliza mwenzio natamani ungekuwepo ila hakuna tatizo kwani masomo nayo ni muhimu. Mh mdogo wangu hebu niambie sijapata shemeji mmasai huko?” Aliuliza Upendo huku akicheka. “Mmh! mwenzangu nimepata mchumba nampenda sana, mambo yakiwa sawa nitakufahamisha.” Alijibu Eliza. Basi waliendelea kuzungumza na baadaye kila mmoja aliendelea na mambo yake. James kipindi chote akiwa Arusha alikuwa akimsaliti Upendo na kustarehe na Esta. Baada ya siku kadhaa kupita hatimaye siku za James kurudi Dar es Salaam zilikaribia. Esta alimfuata James hotelini ili kuzungumza naye kuhusiana na hatma ya uhusiano wao watakapokuwa mbali. “Juliasi karibu utaondoka kwenda Dar hivi kweli utanikumbuka? Na jinsi warembo walivyo wengi huko Dar?” Aliuliza Esta huku akimpapasa uso James. “Hapana siwezi kukuacha mpenzi wangu tutawasiliana usijali. Arusha nitakuja hata wewe utakuwa unakuja Dar es Salaam.” Alijibu James huku akimbusu Esta katika shavu la upande wa kushoto. “Sawa hakuna tatizo mimi naomba tuendelee kuwasiliana nakupenda sana mpenzi wangu.” Alijibu Esta huku akiwa amemkumbatia na kumbusu James. ****************** Huko Dar es Salaam Upendo alikuwa anaandaa mapokezi ya kumpokea mchumba wake James ambaye walikuwa hawajaonana yapata miezi minne. Alifanya usafi wa mazingira ya nyumba na kubadilisha baadhi ya vitu ili kuonekane tofauti. Alikuwa na furaha sana siku hiyo ambapo kesho yake James ndiyo alikuwa akirud.i Alinunua maua mazuri ya rangi nyekundu pamoja na mvinyo. Kesho yake James alirudi, Upendo alikwenda kumpokea uwanja wa ndege yapata saa moja jioni. James alishuka kwenye ndege na kuelekea sehemu za mapokezi na kumkuta Upendo aliyempokea kwa furaha sana. “Darling (mpenzi) umependeza sana, umezidi kuwa mweupe, nimefurahi sana kuwa nawe tena” Aliongea James huku akiwa amemkumbatia Upendo. “Yaani James nimefurahi sana umerudi nilikuwa mpweke sana.” Alijibu Upendo huku akimpokea James begi. Walielekea Kinondoni nyumbani kwa James. James alishangaa sana kuona mabadiliko ya nyumba yake na jinsi ambavyo Upendo alikuwa amepamba. “Mpenzi unafaa sana katika mambo ya upambaji nyumba imekuwa tofauti kabisa nimefurahi kweli wewe ni mke mzuri.” Aliongea James kwa furaha huku akikaa kwenye sofa. “Asante mpenzi wangu nenda ukaoge uje tule chakula halafu unipe habari za Arusha.” Upendo alimsihi James. Usiku ule ulikuwa ni usiku wa furaha kwa wote wawili walikula na kunywa na kulala huku wakiwa na mikakati ya kufunga ndoa haraka. Hatimaye maandalizi ya kumuaga Upendo yalikamilika na wakati huo wazazi wa James walikuwa wakiandaa harusi. Mawasilianao ya Esta na James yalipungua sana. Kila Esta akimpigia simu alikuwa akimdanganya kuwa ametingwa sana, kitu ambacho kilikuwa kikimuumiza sana Esta. Hata hivvyo Esta aliendelea kujipa moyo kuwa Juliasi anampenda bila kujua kuwa alikuwa ni tapeli wa mapenzi. Baada ya miezi miwili kupita Esta aliugua homa na kwenda hospitali ambapo alipimwa na kukutwa akiwa na ujauzito wa miezi miwili. Kutokana na hali hiyo Esta alichanganyikiwa sana. “Mungu wangu nina mimba ya Juliasi nitafanyaje mimi na huyu mwanamume sijui ana mpango gani na mimi. Nafikiria kuitoa mimba lakini naogopa sana. Hapana lazima nimfahamishe hali halisi kwa sababu sijui nifanyeje. Kwani nyumbani baba akijua ataniua na ndugu zangu watanifikiriaje, nikifika chuo ni lazima nimpigie simu leo.” Aliwaza Esta huku machozi yakimlengalenga. Esta aliondoka pale hospitali akiwa na mawazo mengi sana. Alipofika chuoni aliingia chumbani kwake na kupiga simu. Simu iliita muda mrefu bila kupokelewa. Aliendelea kupiga kama mara mbili bila mafanikio hadi alipojaribu tena ndipo simu ilipokelewa na James aliyekuwa kazini kwake muda huo. “Haloo vipi Juliasi mbona nakupigia simu yangu hupokei?” Auliza Esta. “We mwanamke mjinga kweli inamaana niache kazi zangu nipokee simu yako? Je, hujui kwamba huu ni muda wa kazi? Je, unasemaje?” Aliuliza James kwa sauti iliyojaa hasira . “Samahani mpenzi kwa usumbufu nimekupigia nikwambie leo nimekwenda hospitali kupima nina mimba yako ya miezi miwili.” Esta alimfahamisha James. “Hee! Nini? Mimba! Ya nani!” Alihamaki James huku akionyesha kama mtu aliyekanganyikiwa. “Kweli Juliasi unaweza kuniuliza kuhusu mimba hali unajua ni yako? Halafu unaniuliza ya nani?” Aliuliza Esta huku amebana pua kumuigiza James. “Sikiliza nikwambie Esta, mimi sina mpango wa kuwa na mtoto sasa hivi, kama wewe ulitaka mtoto ni juu yako ninachoweza kukusaidia ni pesa ya kutoa hiyo mamba.” Alisema James kwa sauti ya kutetema tofauti na siku nyingine. Esta hakuamini maneno anayoambiwa na James” “Sikujua kama utanifanyia hivi Juliasi, unajua ni kiasi gani nakupenda, nashukuru sana ila hii mimba sitaitoa na huyu mtoto ni wako na nitamleta huko huko Dar es Salaam.” Kisha akakata simu na kulia kwa uchungu huku akijilaumu moyoni mwake na kujipa matumaini” “Nilijua Juliasi ni mwanaume mkweli kumbe yuko hivi au kwa sababu ya hii mimba imekuja ghafla, sijui nifanyeje naamini mambo yatakwenda sawa, ngoja nimwache kwanza kwa sasa.” Alijipa moyo Esta. Esta aliendelea kuwaza sana na baadaye akamua kuendelea na shughuli zake za kawaida. James naye alibaki akiwaza moyoni mwake. “Hivi nimefanya nini mimi huyu msichana ana mimba yangu na hataki kuitoa na mimi nafunga ndoa hivi karibuni. Sijui itakuwaje ila ngoja nimwache siwezi kumpoteza Upendo nampenda sana na ndio mke wangu, sitaki mawasiliano na huyu mwanamke tena.” Basi naye aliendelea na mambo yake huku akiwa anajiandaa na harusi yake. Wakati huo Upendo alipanga safari ya kwenda Morogoro kwani ilikuwa imebaki kama mwezi mmoja afanyiwe sherehe ya kuagwa na wazazi wake. Baada ya wiki kadhaa kupita mawasiliano kati ya James na Esta yalikwisha kwani kila Esta alipojaribu kupiga simu James alikuwa hapokei. Na ikitokea amepokea alimtaka asiendelee kumpigia simu tena. Upendo aliondoka na kwenda Morogoro kwa ajili ya kuandaa sherehe. Akiwa Morogoro mdogo wake alikuwa bado yupo chuoni, hivyo wazazi wake walimpigia simu na kumwambia ni lazima awepo kwenye sherehe ya dada yake. Zikiwa zimebaki kama wiki mbili kufanyika sherehe ya kumuaga Upendo, Eliza alirudi Morogoro kwa wazazi wake ili kusherekea pamoja na dada yake. Siku Eliza alipofika, wazazi wake hawakuwepo ila Upendo pekee. Upendo alipomwona mdogo wake alifurahi sana, alimpokea begi wote wakaingia ndani. “Jamani hatujaonana siku nyingi sana my young sister (mdogo wangu) mbona umenenepa hivyo ulikuwa unasoma kweli wewe?” Alisema Upendo. Eliza alimwangalia sana dada yake: “Dada Upendo kuna kitu nataka nikwambie, ila iwe siri yako sitaki mama wala baba wafahamu hili.“ Aliongea Eliza kwa kusihi. Upendo alishtuka na kuwaza moyoni mwake: “Je, atakuwa ana tatizo gani?”Aliwaza Upendo. Hebu niambie tafadhali. “Upendo mwenzio nina mimba hapa nilipo ndio maana unaniona nimenenepa.” Alianza kueleza Eliza. “Acha utani wako wewe una mimba ya nani.” Upendo alihoji kwa mshangao. “Nina mimba ya kijana mmoja anaitwa Juliasi sijui hata nitampatia wapi najua anakaa Dar es Salaam, lakini sijui nitaanzia wapi kumpata.” Alisema Eliza huku akiwa ameinama. “Inamaana wewe umepata mimba ya mtu ambaye hata ha umjui vizuri, kweli mdogo wangu umechezea maisha yako.” Aliongea Upendo kwa kejeli. Eliza machozi yakiwa yanamtoka, “Nisaidie dada yangu mimi sijui nifanyeje hapa nilipo kwani hata mwanamume mwenyewe nikimpigia simu hapokei na ameshakataa hii mimba ameniambia niitoe na mimi siwezi kufanya hivyo”. “Haiwezekani! Hiyo mimba usitoe kumbuka nilikuonya mdogo wangu uwe makini na hawa wanaume. Wengi wao ni matapeli sasaa… ngoja, tutajua cha kufanya kesho lakini usijali sana kwani tayari jambo limetokea, kulia siyo sulihisho.” Aliendelea kumbembeleza na baadaye alimtaka akaoge ajiandae kwani wazazi wao wangerudi muda huo. Wazazi wao walikuwa wamekwenda kuwachukua ndugu wengine, lakini walikuwa wanafahamu kuwa Eliza anakuja siku hiyo. Baada ya dakika kadhaa kupita wakiwa wanaendelea na mazungumzo Baba na Mama yao pamoja na ndugu wengine walifika. Upendo aliwakaribisha wageni, na kuwaelekeza sehemu za kukaa. “Karibuni sana, wengine wakae pale na wengine hapa, waswahili husema ‘sherehe ni watu’, na watu wenyewe ni ninyi, sisi na wengine watakao kuja.” Upendo aliwaelekeza wageni. Baba Upendo (Mzee George) alimtuma Upendo akamwite mdogo wake aje awasalimie wageni. Upendo aliinuka haraka na kuelekea chumbani. “Eliza unaitwa na baba ili ukawasalimie baba, mama na wageni. Nakuomba uvae gauni kubwa ili wasielewe mabadilko uliyonayo, kwani mimba uliyokuwa nayo imeanza kujionyesha.” Alishauri Upendo. Eliza alijiandaa kama alivyoshauriwa na Upendo kisha wote wakaelekea sebuleni. Alipofika aliwasalimia wazazi na shangazi yake na wageni wengnie waliokuwepo ”Jamani ni wewe wajina wangu Esta umekuwa mkubwa hivi”. Shangazi yake alishangaa kuona Eliza amekuwa mkubwa. “Yaani dada, hilo jina la Esta mwenzio halitumii anatumia jina la Eliza, wamekuwa wakubwa sana. Hata sisi hatujawaona siku nyingi. Huyu yupo chuoni Arusha anaingia mwaka wa mwisho.“ Alifafanua Baba Upendo huku akimwangalia shangazi yake Eliza na kucheka. “Kweli siku zinakimbia na hilo jina la Esta ha ulitumii unapenda kuitwa Eliza mama jamani watoto wa siku hizi.” Aliendelea kushangaa na kucheka shangazi yake Eliza. “Hapana shangazi, huwa nalitumia mara moja moja.” Alijibu Esta huku akiinamisha kichwa chini kwa aibu. “Lakini bora usilitumie kwani haya majina ya kurithi wakati mwingine sio mazuri unaweza ukampa mtoto jina la mtu mwenye mikosi na mtoto akajikuta anakuwa na mikosi katika maisha kwa sababu ya majina ya kurithi.” Alisema shangazi yake huku watu wote wakiangua vicheko. “Hakuna wifi hizo ni imani tu za watu.” Alijibu mama Upendo huku akiinuka kuelekea jikoni. “Haya jamani huku jikoni vipi?” Aliuliza mama Upendo. “Tayari mama hakuna tatizo.” Alijibu Upendo. Waliendelea na mazungumzo pale sebuleni na baadaye baada ya kupata chakula cha usiku wote walikwenda kupumzika. Hatimaye siku ya sherehe ilifika, sherehe, iliandaliwa pale nyumbani kwa kina Upendo. Kulikuwa na uwanja mkubwa ambao ulipambwa vizuri sana. Ama kweli ilikuwa ni siku ya furaha kwa Upendo. Kwa upande wa mdogo wake Eliza mambo hayakuwa mazuri kwani muda wote alikuwa akiwaza sana kuhusu Juliasi kwa nini hapokei simu yake. “Eliza hii ni siku ya furaha ya maisha yangu naomba uwe na furaha mdogo wangu. Halafu leo pia ni siku mwafaka kwa wewe kumwona shemeji yako ambaye hujawahi kumwona, nadhani utampenda kwani nampenda sana.” Upendo alimfariji mdogo wake huku akimpigapiga mgongoni na kiganja cha mkono wake wa kulia. “Nitafurahi sana kumfahamu shemeji yangu nadhani alikuwa akinisikia tu.” Kwa tabasamu la upole Eliza alimjibu dada yake.“ “Ndiyo nilikuwa nikimsimulia sana kuhusu wewe mdogo wangu kwamba upo chuoni kwa hivyo leo mtafahamiana au siyo mdogo wangu.” Alisema Upendo. “Asante nitashukuru sana kumwona shemeji, sijui atavaa suti, jinsi na tisheti au atakuwa katika pamba za namna gani.” Aliongea Eliza huku akitabasanu na kumwangalia dada yake Upendo. Mipango iliendelea na hatimaye sherehe ilikaribia kuanza. James na wazazi wake walitokea hotelini na kuelekea nyumbani kwa akina Upendo maeneo ya Kihonda ambapo sherehe ilikuwa ikifanyika. Walipofika walipokelewa kwa vigelegele na shangwe nyingi walipelekwa sehemu ya kukaa na baadaye James alifichwa katika umati wa watu ili Upendo aje kumtafuta. Upendo alitoka ndani huku matarumbeta yakipigwa na shangwe nyingi zikitawala akiwa sambamba na mdogo wake Eliza. Upendo akiwa sambasamba na Eliza alielekea sehemu ile kwenye umati wa watu ambako James alifichwa ili akamfichue. James akiwa katikati ya umati alimwona Upendo akiwa anatoka na pembeni akiwa na Esta alishtuka sana kumwona Esta. “Mungu wangu yule si Esta? Anafanya nini hapa na mbona yupo karibu na Upendo? Kuna nini kinaendelea hapa?” James aliwaza na kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. Kwa muda wa takribani dakika mbili hivi James alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa. Watu waliendelea kushangilia huku James akiwa hajui nini cha kufanya baada ya kumwona Eliza ambaye ndio Esta akiwa anatazama huku na kule kama vile mtu anayetafuta njia ya kutokea. James akiwa anahangaika nini cha kufanya Upendo na Eliza waliendelea kuangalia huku na kule wakimtafuta katika umati wa watu. Ghafla Eliza akamwona Julias na kushtuka, lakini hakujua kama ndio mume mtarajiwa wa dada yake. “Haa! Hivi yule si Juliasi? Amefuata nini hapa? Au ni ndugu wa huyo James? Mmh! Nina bahati kweli sikutarajia kumwona. Sasa hii ni nafasi nzuri ya kuzungumza naye kuhusu hatima ya uhusiano wetu na hii mimba yake.” Eliza alijiuliza maswali mengi huku akishangaa na kufurahi kuonana tena na Juliasi. Zoezi la kumfichua James halikufanikiwa kwani Upendo alishindwa kabisa kumwona James alipokuwa. Hivyo waliamua kurudi na kukaa katika sehemu maalumu iliyotayarishwa kwa ajili ya Upendo. Sherehe ilianza rasmi, watu walijaa sana kushuhudia tukio muhimu la kuagwa kwa Upendo. Mshereheshaji (MC) aliimudu barabara kazi yake kwani alifanikiwa kumchangamsha na kumchekesha kila aliyehudhuria. “Ndugu wageni waalikwa ninayo heshima kubwa sana ya kuwakaribisha katika sherehe hii ya kumuaga binti yetu Upendo.” Alianza kuonyesha mbwembwe zake huku akigeuka kumwangalia Upendo. Kisha akaendelea. “Karibuni sana kuja kwenu ndo kumefanikisha sherehe hii. Kwa kuwa leo ni siku ya furaha basi kila mtu afurahi kwa kadiri ya uwezo wake. Vyakula ni vingi, vinywaji vimejaa, burudani kebekebe. Pia kutakuwa na mashindano ya kucheza twisti kwa akina baba wenye vitambi (vicheko) ambapo washindi watano wa kwanza watapewa zawadi na akina mama: Mshindi wa kwanza atakabidhiwa kanga yenye ujumbe ulioandikwa ‘WALIONDANI WANATAMANI KUTOKA.’ Mshindi wa pili ‘atapewa kanga iliyoandikwa ‘WALIO NJE WANATAMANI KUINGIA.’ Mshindi wa tatu atapata kanga yenye ujumbe ‘WADOGO WANATAMANI UKUBWA.’ Mshindi wa nne atapewa kanga yenye maneno ‘WAKUBWA WANATAMANI KURUDIA UTOTO.’ na Mshindi wa tano ‘NDOA NDOANA’”
Aliongea MC huku akishangiliwa na umati wa watu na wengine wakisimama na kwenda kwa Upendo kumrushia maua ya kila rangi. Ama kweli MC alichangamsha sherehe vilivyo. Upendo aliinama chini huku maua yakiendela kumwagwa alipokaa. Alitafakari sana juu ya manjonjo ya MC kwani hakuelewa maana ya ujumbe ulio katika zile zawadi watakazo kabidhiwa washindi wa twisti. Sherehe iliendelea kupamba moto, muda ulifika wa kupata chakula huku vinywaji vikisambazwa kila kona kwa fujo shughuli zote hizo zikisindikizwa na muziki mwororo ulitumbuiza kwa sauti ya chini na ya kubembeleza. Wakati kamati ya chakula ikijiandaa kuanza kugawa chakula, ghafla MC alisimama mbele. “Studio! Studio! Tafadhali!” MC alichombeza kumwashiria DJ azime muziki ambaye naye alifanya hivyo mara moja. Kisha akaendelea. “Wageni wetu waalikwa mabibi na mabwana. Mimi binafsi sitahesabia kama shughuli hii imefanikiwa endapo Mchumba wa Upendo hatutamtambua. Kwa hiyo nakuomba Upendo ututambulishe mchumba wako kwa utaratibu nitakao kupangia.” Alishangiliwa MC hata kabla hajamaliza kusema huku wengine wa kitamka neno kweli kwa sauti za juu. James aliposikia hivyo, moyo ulimdunda alijua sasa muda wa kuumbuka umefika. Alijikaza kiume na kusubiri kitakachotokea. “Upendo njoo hapa!” Alitamka MC huku akiagiza aletewe glasi yenye mvinyo na ua jekundu lililoandaliwa kwa shughuli hiyo. Watu wote walitulia kimya mama mmoja mwenye mtoto aliyekuwa akilia alitoka naye nje haraka sana ili kutoharibu utulivu. Upendo alipofika, MC akaendelea. “Upendo!” Alitamka MC huku akimwonyesha ua na ile glasi yenye mvinyo. “Utakwenda wewe mwenyewe bila mpambe wako hadi alipo mchumba wako. Ukifika mpe hili ua kama ishara ya upendo wenu wa kweli. Kisha mpe huu mvinyo kama ishara ya kumkaribisha mchumba wako katika maakuli kisha utamshika mkono na kumwongoza hadi katika meza ya chakula, halafu utapakuwa chakula ambacho kitawatosha wote wawili kisha utarudi kwangu ili niwaelekeze cha kufanya.” Alipomaliza tu kuongea shangwe na vicheko viliibuka tena huku wengine wakimsifu MC kwa umahiri alionao katika kumudu na kuipamba sherehe. Upendo alikwenda kumtafuta mchumba wake huku ameshika vile vitu alivyokabidhiwa na MC, alitembea kwa madaha yote asijue wapi amekaa James aliangalia huku na kule lakini wapi hakumuona James. Baada ya kuhangaika sana huku watu wakiwa na shauku ya kumwona James mwisho akamwona amekaa katikati ya wazee aliokuja nao, aliongeza mwendo na kwenda moja kwa moja hadi alipokuwa na kupiga magoti kisha akampa lile ua huku akishangiliwa na kila mtu. Wengine wakitamka SAFI SANA! UMECHAGUA!. Wakati Upendo akijiandaa kumpa James mvinyo kama alivyoelekezwa na MC ghafla Eliza alipiga kelele ambazo zilimshtua kila mtu. “Nooooo! Hapana! Hapana! Juliasi!, Juliasi! Haiwezekani! Nasema haiwezekani!” Yalimtoka maneno Eliza kwa mfululizo huku akirukaruka kuelekea alipo James. Watu walijaribu kumshika lakini Eliza aliwazidi nguvu, alikwenda hadi alipo James huku akitweta kama mtu aliyepandisha mapepo. “Kumbe wewe ni shemeji yangu?” Ilikuwa ni sauti ya Eliza mdogo wake Upendo ambaye aliwafanya watu wamshangae ana matatizo gani. Ndipo kabla hajaendelea kuzungumza alianguka na kuzimia. Wazazi wake walishangaa nini kimetokea na huyo Juliasi ni nani. “Kuna nini jamani mwanangu amekuwaje leo?” Aliuliza mama Upendo huku akionyesha mshtuko mkubwa. Basi ndugu walimchukua na kumpeleka ndani huku akipepewa. Upendo alishindwa kuelewa kwa nini mdogo wake alitamka maneno yale, basi alimshika James mkono. “Mmh! Mdogo wangu atakuwa na matatizo makubwa sijui ana nini hebu twende ndani tukamwone.” Alitamka Upendo huku wakiondoka kuelekea ndani. Wakati huo wote James alikuwa kimya kijasho chembamba kikimtoka kwa kuogopa kilichotokea hivyo alishindwa kuongea chochote zaidi ya kumfuata Upendo. Walipoingia ndani walimkuta Eliza ameshazinduka. Alipomwona tu James alisimama na kumshika kwa nguvu huku akilia kwa sauti ya juu. “Kwa nini unafanya hivi? Unataka kutuangamiza mimi na dada yangu Juliasi? Mimi nilikupenda sana na tayari nina mimba yako. Loh! Kumbe ulikuwa una mwanamke tena dada yangu?” Aliongea Eliza kwa hasira na hisia za ajabu huku Upendo akibaki anashangaa na kuuliza. “Vipi Eliza mdogo wangu umechanganyikiwa? Huyu ni James sio Juliasi!” Upendo alijaribu kumfariji mdogo wake. “Sijachanganyikiwa dada yangu huyu bwana nilikutana naye Arusha akaniambia kuwa anaitwa Juliasi. Naomba mmuulize mwenyewe aseme ukweli.” Alisema Eliza kwa uchungu huku wazazi wake wakiwa hawaelewi kinachoendelea. Je, ni kweli anayosema Eliza?” Upendo aliuliza huku alimwangalia James. James alikaa kimya kwa muda kisha alikaa chini kwenye kochi huku akiwa ameinimisha kichwa chini kwa aibu na fedheha. “Upendo yote aliyosema Esta ni kweli, naomba unisamehe ilikuwa ni bahati mbaya sikujua kama ingekuwa hivi. Nisamehe mpenzi wangu nilimfahamu Eliza kwa jina la Esta, siwezi kukupoteza nisamehe mpenzi.” James aliomba na kukiri mbele ya wazazi wake Upendo na wazazi na ndugu zake. James aliyasema hayo akiwa bado ameinama chini huku machozi yakimlengalenga kwa aibu na hofu ya kumkosa Upendo. “Hivi ninasikia au naota jamani, wewe James leo hii unanifanyia hivi? aibu gani hii jamani? Angalia sasa umempa mimba mdogo wangu na mimi nina mimba yako tayari hivi nifanyeje? James Mimi siwezi kukusamehe.” Upendo aliongea kwa jazba huku amemkaba James shingoni kisha akamwachia na kukimbilia nje. Watu walimfuata ili kumshika lakini aliwazidi mbio na kutokomea gizani. Sherehe ilivunjika, watu wote wakatawanyika kumtafuta Upendo. Upendo alikimbia kwa mbio za ajabu kama mbwa mwenye kichaa, hakujali kabisa kiumbe alichokuwa nacho tumboni. Wakati watu wanaanza kumtafuta Upendo tayari alikuwa ameshafika mtaa wa tatu kutoka nyumbani kwao. Baada ya kufika mtaa wa nne alikuwa tayari ameshafika katika barabara kuu iendayo Msamvu, vile anaanza tu kukatisha barabara kulitokea baiskeli iliyokuwa katika mwendo kasi ilimgonga na kumburuza hadi kwenye mfereji. Upendo alilalamika sana kwa maumivu makali tumboni na mgongoni. Wapitaji walisikia mtu akipiga kelele za nisaidieni kutoka katika mfereji. Walifika na kumuinua na kumkalisha pembeni mwa barabara. Wakati wakiendelea kumhoji kilichotokea wale watu waliokuwa wazazi wake, James, Eliza na watu wengine walifika na kumkuta Upendo akiwa hoi. Baba yake Upendo alimfukuza James na kutaka asionekane tena katika familia ile ilikuwa ni aibu kubwa sana kwani furaha ilileta uchungu. Upendo alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matatibu. Huko hospitali hali ya Upendo ilizidi kuwa mbaya, mimba aliyokuwa nayo iliharibika. Eliza alikuwa karibu naye wakati wote akimwomba msamaha lakini Upendo alimfariji mdogo wake. “Usijali mdogo wangu huna kosa mimi ndio mwenye kosa sikukufahamisha shemeji yako. Lakini vilevile James hakuwa mwaminifu alikuwa akinidanganya.” Upendo alisema maneno hayo kwa uchungu sana huku machozi yakimtiririka mashavuni. Baba na Mama yake Upendo walihuzunika sana wakiwaonea huruma mabinti zao. “Wanangu nawapenda sana haya mambo yameshatokea hakuna namna, yule mwanamume ni muuaji sitaki kumsikia tena, kinachotakiwa ni Upendo apone maisha yataendelea.” Baba Upendo aliongea huku akimtazama mkewe. “Ndio! Wanangu hii ni mitihani ya maisha, ni majaribu ila Mungu atawasidia.” Mama Upendo aliongeza. Kadiri siku zilivyokwenda Upendo aliendelea kuumwa sana. James maisha yalianza kumwendea kombo, alikuwa amechanganyikiwa, siku zote alikuwa ni mtu wa kujilaumu moyoni mwake akisema. “Maisha yangu yamebadilika nimemkosa Upendo. Nimemkosea sana Upendo na Mungu pia sistahili kusamehewa kabisa Mungu nisaidie.” Aliongea James kwa kukata tamaa kabisa huku wazazi wake wakimwonea huruma. Siku moja wazazi wa James waliamua kumshauri James waende hospitali kumwona Upendo ili akamwombe msamaha kwa mara nyingine. Walipofika hospitali waliwakuta wazazi wa Upendo pamoja na watoto wao wote wakiwa wamesimama wamekizunguka kitanda alipolala Upendo. Walipoingia tu kabla hata hawajasalimia baba yake na Upendo alianza kuwafukuza. “Sitaki kuwaona hapa naomba mondoke yaani matatizo yote mnayotupa hadi sasa bado mnakuja? James nasema ondokeni!” Alitamka baba Upendo kwa hasira. “Baba usiwafukuze wakaribishe nataka kuongea na James.” Alitamka Upendo kwa taabu tena kwa sauti ya chini sana huku akinyoosha mkono wa kulia akiashiria kumwita James. “Utaongea naye nini yeye ndiyo chanjo cha wewe kuwa hapa leo nasema watoke sitaki kuwaona hapa.” Alifoka baba Upendo. Upendo aliendelea kusisitiza kuongea na James na aliwaomba wote watoke nje abaki Eliza na James tu. Wote walitii na kutoka nje huku wakipigwa na butwaa kwa nini Upendo amewafukuza. James aliomba msamaha kwa Upendo akiwa amepiga magoti akijutia yote aliyoyafanya. Pia James alimwomba msamaha Eliza kwa kumdanganya kuwa hakuwa na mke wala mchumba. Eliza alimsamehe. “James nitakusamehe lakini kwa masharti ya kwenda kuishi na mdogo wangu Eliza mama mtarajiwa wa mtoto wako. Mimi sistahili tena kuwa mke wako.” Aliongea Upendo huku akimkazia macho James na Eliza. Kabla James wala Eliza hawajapata nafasi ya kujibu chochote, Upendo aliyekuwa hoi kitandani aliinuka na kukaa kwa mara ya kwanza tangia afike hospitali. James na Eliza walishangaa sana. Eliza pamoja na kushangaa alifurahi kuona dada yake amekaa, alikwenda haraka nje kuwaita wazazi wake na ndugu wa James ili waone maendeleo ya ghafla ya afya ya Upendo. Huku akiwa amezungukwa na ndugu wa pande zote mbili Upendo alitabasamu na kugeuka ili kumwangalia kila aliye kuwepo katika chumba kile. Kisha Upendo alimshika mkono mdogo wake Eliza pamoja na mkono wa James. “Kama nilivyotoa masharti yangu nimekusamehe James, lakini kuanzia sasa nenda mkaishi kwa furaha na amani na msahau yote yaliyotokea. Uaminifu iwe nguzo ya upendo katika nyumba yenu. Mkaishi kwa kumtegemea Mungu katika kila jambo.” Baada ya kuongea hivyo Upendo akavuta mikono ya wote wawili kuelekea kifuani kwake kisha akaibusu na kutamka maneno mawili tu “Nawapenda sana.” Alipomaliza tu kuongea hivyo ghafla alipatwa na kwikwi na kukohoa kwa nguvu huku akishindwa kupumua vizuri na kuangukia kitandani huku akitupatupa miguu na mikono kama mtu mwenye kifafa na ghafla akatulia na kufumba macho. Eliza alikwenda haraka kumwita Daktari ambaye alifika na kumpima. “Upendo amekata roho.” Yalikuwa ni maneno ya Daktari kutokana na vipimo vyake.
MWISHO
HUU NI MWISHO WA KITABU CHA PILI KATIKA SIMULIZI YA MALIPO NI HAPAHAPA...... USIKOSE KITABU CHA TATU KINACHHOENDA KWA JINA LA “MAMA MDOGO”
0 Comments