Aliongea Jothan huku machozi yakimlenga lenga. Hakika ni uamuzi mgumu aliouchukua kwakua aliamini ilikuwa ni mtihani mkubwa katika mapokezi ya mlengwa. Alipoinua macho yake kumtazama Prisca, tayari mashavu ya prisca yalishalowana kwa machozi huku macho yakiwa mekundu. Kilio cha kwiki kilianza kusikika na kumfanya Jothan kuingiwa na imani baada ya kumtaza mpenzi wake huyo anaye amua kumuacha bila kosa lolote. SONGA NAYO……………..
Machozi na kilio cha kwikwi kiliendelea kwa dakika kadhaa, Prisca alimuangalia Jothan ambaye alikua ana muonea aibu wakati huo. Hakuamini kuwa ndiye yeye aliyetamka maneno yale,. “kwanini mimi?.... kwanini Jothan umeamua kuzichezea hisia zangu kwa miaka yote hiyo niliyokuwa na wewe kumbe ulikuwa huna malengo ya kuwa na mimi. Kwanini Jothan umeamua kunifanyia hivyo?” aliongea Prisca huku analia.
“sorry Prisca. Unafikiri ningefanyaje kwa hali niliyokuwa nayo hivi sasa. Sina jinsi japokuwa bado nakupenda sana. Ningekuwa mtu mwengine hivi sasa ningeendelea kuwachanganya wote wawili. Ila roho huwa inanisuta kufanya hivyo kwakua hata mimi sihitaji kuchezewa hisia zangu. Naomba kubaliana tu na maamuzi yangu japokuwa unaumia.” Aliongea Jothan huku na yeye akijifuta machozi yaliyomdondoka kutokana na hali aliyokuwa nayo Prisca inavyosikitisha.
“thank you for everything.”
Aliongea Prisca na kunyanyuka na kuondoka. Alimuacha Jothan ambaye alijiinamia na kujilaumu kwa alichokifanya. Akili nyingine ilimwambia kama mwanaume wa ukweli na mwenye msimamo basi alifanya maamuzi sahihi na ya busara.
Alirudi nyumbani na kumkuta Shani amejaa tele nyumbani kwake. Alipofika tu, Shani alimfuata na kumkumbatia. Ingawaje Jothan alijichekesha, lakini Shani aligundua kuwa hakuwa sawa.
“una nini mume wangu?. Aliuliza Shani baada ya kumuangalia usoni Jothan.
“kawaida tu mke wangu.. kwani naonyesha nina tatizo?” aliuliza Jothan kuhakikisha alichokisikia kutoka kwa Shani.
“sura yako inaonyesha kama ullikuwa unalia au ulikuwa unahuzunika muda si mrefu.” Aliongea Shani na kumfanya Jothan kumuangalia usoni Shani. “kichwa kilikua kinanigonga sana, hata hivyo sasa hivi niko sawa.” Aliongopa Jothan
“pole mume wangu, kama bado kinaendelea we niambie nikununulie panadol au nikusindikize hospital… usidharau mume wangu.” Aliongea Shani huku akionyesha kwa alikua anajali sana afya ya mwenzi wake.
“usijali, niko sawa tu.”
Aliongea Jothan na kuingia chumbani kwake. Alijilaza na kuwaza yaliyotokea muda mfupi uliopita. Aliamua kupiga moyo konde na kuona yote yalikuwa ni majaribu tu.
Maisha yalikuwa mazuri huku kila mmoja akifurahia uwepo wa mwenzake. Hata Jothan mwenyewe alikiri kuwa uamuzi wake ulikuwa sahihi sana kumchagua Shani katika maisha yake badala ya Prisca ambaye mpaka kipindi hicho alikuwa ameshakatisha mawasiliano naye.
Shani naye alijitahidi kuhakikisha anafanya yale yote apendayo Jothan na kumteka Jothan kisawa sawa.
Ilkuwa akiongelewa mwanamke bora basi Jothan alilipitisha jina la Shani bila kuangalia kuwa alikuwa na nani au alizungukwa na wasichana wazuri.
Alitumia muda mwingi kuwa karibu na Shani. Hata kama alikua anataka kwenda kutanua, basi Shani alikuwa ubavuni kila walipoenda. Siku moja ambayo ilikua ni mwisho wa wiki, Jothan aliamua kulala tu Jumaapili hiyo kutokana na uchovu aliokuwa nao wa jana yake kwakua walienda club yeye na Shani na kurudi asubuhi kabisa.
Nyumbani kwake aligonga hodi mgeni mmoja wa kike na kufunguliwa mlango na Shani ambaye alishaamka na alikuwa anfanya usafi nyumbani kwake. “za saa hizi dada.” Alisalimia yule mgeni ambaye alionyesha wazi kuwa alikua amechoka kutokana na mimba kubwa aliyokuwa nayo.
“salama tu.” Alijibu Shani na kumsikiliza huyo msichana shida yake.
“sijui nimemkuta mwenye nyumba hii?” aliuliza yule dada na kumuangalia Shani aliyekuwa makini akimsikiliza.
“mwenyewe kalala, ila naweza kukusaidia kama hutajali kunieleza shida yako.” Aliongea Shani na kumuangalia yule dada.
“ni vyema kama nita onana nae mwenyewe.” Aliongea yule dada na kumfanya Shani amkaribishe ndani.
Kwakua Shani alikua anaandaa chai, hakuona ubaya kuandaa ya kutosha na kumkaribisha yule mgeni aliyekunywa chai kama anafukuzwa kutokana na njaa aliyokuwa nayo. Shani aligundua njaa aliyokuwa nayo mgeni huyo na kumuongezea vyakula mpaka alipohakikisha ameshiba ndio akaamua kumfuata na kumuuliza maswali machache wakati wanamsubiri bwana mkuwa aamke.
“tunsubiri aamke, si unajua alikesha jana kwa hiyo sio vizuri kumuamsha mtu akiwa katika uchovu kama huo.” Aliongea Shani na wazo hilo likapitishwa na yule mgeni.
Jothan aliamka na kwenda kuoga. Alivaa nguo zake nyepesi na kwenda sebuleni na kumkuta mgeni aliyekuwa anamsubiri. Yule dada alipogeuza shingo kumuangalia Jothan, macho yalimtoka na kujikuta mshangao mkuu umempata.
“wewe, umefuata nini nyumbani kwangu?” aliuliza Jothan kwa hasira.
Yule mgeni hakua na la kujibu zaidi ya kujiinamia. “na wewe unawakaribishwa watu humu ndani wengine ni nyoka kama huyu mwanamke.” Aliongea Jothan na kumuweka Shani kwenye bumbuwazi.
“mbona sielewi, maana mimi aliniambia ni mgeni wako ndio maana nikaona si vibaya kumkaribisha ndani.” Alijitetea Shani.
“mimi simjui huyu, .. kwani wewe msichana unaitwa nani?” aliuliza Jothan na kwenda kukaa kwenye moja ya sofa za pale sebuleni.
“BAHATI.” Alijibu yule mgeni kwa aibu na kuangalia chini.
“WHO A BAHATI BAY THE WAY??”
Aliongea Jothan na kumfanya Bahati kupiga magoti mbele yake na kuanza kulia kwa uchungu.
“sihitaji kupigiwa magoti mama, mpigie magoti mungu wako na umuombe msamaha kwa ulichokitenda kwangu mimi.” Aliongea Jothan na kumuinua Shani pale chini.
“naomba unisamehe, nimehadaika tu na jiji na hivi sasa limeshanifunza Jothan.” Aliongea Bahati huku analia.
“leo hii unamjua Jothan wewe?.. si ulikua hunijui wewe?.. nani kakutajia jina langu?” aliuliza Jothan maswali mfulumizo yaliyomshinda Bahati kujibu na kubaki analia tu.
“nyamaza kulia dada, kwani tatizo ni nini?.. niewekeni wazi jamani.” Aliongea Shani baada ya kukaa kimya muda mrefu. “sikiliza mke wangu, huyu dada ni mpumbavu na hana akili hata kidogo. Alikuwa na matatizo ya macho yaliyomsababishia upofu na hakuwa anaona hapo mwanzo. Mimi kwa imani yangu nikamchukua kutoka kwa mama yake Arusha na kuja naye hapa Dar kwa nia njema ya kumtibu. Sikuhitaji chochote kutoka kwake. Ila malipo aliyokuja kunilipa haki ya mungu kanifanya moyo wangu uwe na sugu na kuwa mgumu kuwasaidia wengine. Yaani alipopata macho ndio akaniona mimi takataka baada ya bosi wangu kumtaka. Siku niliyokutana naye akajifanya sauti yangu kaisahau. Yaani hata nilipojitambulisha bado akijifanya hanijui. Nikasamehe na kuachana naye, bado akaona haitoshi akaamua kunifanyia fitina mpaka nikafukuzwa kazi bila kosa. Sasa huyu utamuita mtu au kiatu tena kisichokuwa na kamba?”
Aliongeea Jothan maneno yaliyomchoma Bahati na kumfanya aanze kulia kwa sauti kubwa zaidi ya aliyokuwa analia.
“msamehe mume wangu, mungu kakujaalia umepata kazi nyingine. Na hujui kakuepusha na nini kukutoa kule. Na huyu adhabu yake ndio hii. Maana amepewa mimba na ametimuliwa. Hana msaada mwingine zaidi yako wewe. Msamehe tu mume wangu.” Aliongea Shani na kumsogelea Jothan aliyekuwa kafura kwa hasira na kuanza kumshika shika. Jothan alivuta pumzi ndefu kisha akamuangalia Bahati.
“ni msaada gani unaotaka kutoka kwangu?” aliuliza Jothan na kumfanya Bahati kufuta machozi.
“naomba unisaidie kunipeleka tu Arusha kwa mama yangu.” Aliongea Bahati huku analia. Kauli hiyo iliwaigia wote wawili.
Ghafla walishangaa kumuona Jothan machozi yanamtoka kwa jinsi alivyokuwa anamuonea imani msichana mzuri walivyomtumia vibaya na kuwa kama kituko.
Hakua Bahati yule kipofu mwenye bashasha usoni kila wakati. Sasa hivi mashavu yalimuingia ndani, nywele zake hazitazamiki mara mbili. Ngozi yake ilijaa makovu ya kupigwa kila sehemu.
Jothan alijikuta ameguswa na kuanza kulia kwa sauti. Alinyanyuka huku analia na kumfuata Bahati na kumuinua kichwa chake na kuitazama sura yake iliyokuwa imelowa machozi na kuvimba kutokana na kulia kwa muda mrefu.
“utakaa hapa mpaka utakapojifungua na kurudisha afya yako… pole sana kwa yaliyo kukuta.”
Hatimaye aliongea maneno hayo yaliyomfanya Bahati kumkumbatia Jothan bila kujali uwepo wa mke wake pale.
Wali muhurumia Bahati na kumpa chumba mule ndani. Siku tatu baadae, Bahati alipatwa na uchungu na kumuwahisha hospitali ya kulipia iliyopo kinondoni.
Uchungu ulidumu kwa siku mbili mfululizo na kwa bahati nzuri Bahati alifanikiwa kujifungua salama mtoto wa kike.
Aliwashukuru sana Shani na Jothan kwa utu wao waliouonyesha juu yake, maana walikuwa nae bega kwa bega na kuhakikisha kuwa anajifungua salama.
Baada ya miezi mitatu kupita, Jothan aliamua kumsafirisha Bahati na kumrudisha kwao Arusha. Alilazimika kwenda naye kwakua Bahati hakua anapajua kutokana na hali yake ya upofu aliyokuwa nayo mwanzo.
Walipofika Arusha mjini, Jothan alikodi taksi iliyowafikisha mpaka nyumbani kwa kina Bahati.
Ilikuwa zaidi ya furaha kwa mama yake Bahati baada ya kumuona mwanaye akiwa anaona . alimfuata na kumkumbatia. “karibuni…. Karibuni nyumbani.” Alikaribisha mama huyo kwa Furaha.
“ahsante, tumeshakaribia.”aliongea Jothan na kuingia ndani.
Kwa furaha ya ajabu, mama huyo alikuwa anatabasamu kila muda kutokana na kumkumbuka mwanaye.
Wakati wanaendelea na stori za kawaida. Ghafla mlango ulianza kugongwa kwa nguvu.
Mama yake Bahati alitoka na kwenda kumsikiliza mtu anayegonga mlango. Alikaa huko kwa dakika kadhaa. Na baadae alirudi huku akiwa hana furaha kama aliyokuwa nayo mwanzo.
“samahani baba, namchukua huyu tukatete kidogo.” Aliongea mama yake Bahati.
“hamna shida mama.” Aliongea Jothan na kumfanya Bahati anyanyuke na kumfuata mama yake..
“mwanangu, aliyekuja kugonga ni mwenye nyumba. Amesema kuwa ametuchoka kutokana na kutomlipa kodi yake kwa muda mrefu. Yaani nimechanganyikiwa hata sijui tutafanyaje.” Aliongea mama yake Bahati baada ya kumuita mwanaye chemba.
“usijali mama, nililijua hili ndio maana nikamuelezea Jothan mapema. Ametuahidi kutusaidia.” Aliongea Bahati na kumfanya mama yake amuangalie.
“kwani, wewe na huyo Jothan mkoje?”
Alijikuta mama yake Bahati anauliza swali lile kutokana na kutoelewa mazingira na makubaliano ya kumponyesha mtoto wake macho na kumrudisha akiwa na mtoto.
“ni story ndefu mama, ila kifupi ni mkombozi wangu na wewe pia. Naweza sema hivyo.” Aliongea Bahati.
“kwa hiyo unataka kusema kuwa hata huyu mtoto si wa kwake.” Aliuliza mama yake Bahati.
“ndio mama.” Aliongea Bahati kimkato huku akitaka kumuonyesha mama yake ni jinsi gani asivyotaka kuaonngelea ile mada kwa muda ule.
Baada ya muda Bahati alirudi sebuleni alipomuacha Jothan na mama yake akaenda kuandaa chakula cha jioni.
“mbona hivyo, kwema?” aliuliza Jothan baada ya Bahati kurejea pale. “sio kwema, kama nillivyokuambia siku ile. Mama kashindwa kulipa kodi hivyo mwenye nyuumba anataka hela yake au tuhame.” Aliongea Bahati na kumuangalia Jothan.
Baada ya chakula cha usiku, Jothan alimkabidhi mama yake Bahati fedha tasilimu shilingi laki saba kwa ajili ya kulipa deni la laki nne analodaiwa na hiyo nyengine kwa ajili ya mkataba mpya. Mama yake Bahati alifurahi kidogo machozi yamtoke na kumuombea sana dua za mafanikio Jothan.
“naomba niwaache, naenda kulala Hotel na mungu akipenda kesho ndio safari yangu ya kurudi Dar-es-salaam” aliongea Jothan baada ya kuangalia saa yake ya mkononi na kumuonyesha kuwa ilishatimu saa tatu kamili.
“sawa mwanangu. Mungu akutangulie katika kila jambo lako.” Aliongea mama yake Bahati na jothan akatoka huku Bahati akimsindikiza.
“nakushukuru kwa yote ulioamua kuyafanya katika maisha yangu. Nakuomba usichoke kuwasaidia wasiojiweza kama nilivyokuwa mimi japokuwa nilikuumiza… kwa mungu kuna fungu lako Jothan.” Aliongea Bahati walipokuwa njiani wakisindikizana.
“usijali, hata mimi naamini mambo yangu yananinyookea kwakua nakigawa kidogo kwa wenzangu wenye shida. Yale yalikuwa maneno tu tena kwa sababu nilikuwa na hasira. Mimi sina kinyongo na wewe. Moyo wangu mweupe na nakuombea pia maisha mazuri na ya furaha na mtoto wako. Naamini hutofanya makosa tena kwakua umeshajifunza.” Aliongea Jothan huku wakiikaribia bara bara.
Baada ya kufika kituoni, waliagana huku Bahati machozi yanamtoka kwakujua kuwa ule ulikuwa mwisho wa kuonana na mwanaume huyo wa ajabu maishani mwake.
Aliondoka huku kila baada ya hatua moja akigeuka nyuma kumtazama Jothan. Kwa mbali kulikuwa na gari linakuja spidi upande aliokuwa Bahati.
Jothan alipotupa macho yake kuitazama ile gari ilikaribia kabisa kumgonga Bahati ambaye wakati huo Bahati hakuiona ile gari kwakua likua bize kumuangalia Jothan.
Aliamua kutupa begi lake na kumkimbilia Bahati, alipofika tu alimsukuma na kwa bahati mbaya ile gari ilikuwa inajaribu kumkwepa Bahati na kumgonga Jothan.
“MAAAMAAAAAA!”
Alipiga kelele Bahati baada ya kumshuhudia Jothan akianguka chini baada ya kugongwa. Damu nyingi zilikuwa zinamtoka puani na mdomoni.
Yule dereva aliyemgonga Jothan, alisimamisha gari na kumuingiza Jothan pamoja na Bahati na safari ya kuelekea hospitali kwa ajili ya kujaribu kuokoa maisha ya Jothan ilianza mara moja..
Walipofika hospitali, walipokelewa haraka na Jothan akakimbizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.
“jamani kwa hali ya mgonjwa wenu, anatakiwa kufanyiwa operation haraka iwezekanavyo ili kuokoa maisha yake.”
Aliongea daktari na wote wakakubaliana kuwa tendo lile lifanyike.
Bahati alikuwa mtu wa kulia tu usiku nzima. Alijua yeye ndio sababu iliyomsababishia Jothan kugongwa na lile gari.. Alilia na kumuomba mungu asimchukue Jothan.
Alirudi nyumbani asubuhi na kumtaarifu mama yake juu ya kilichotokea. Mama yake alisikitika sana na kwenda hospitali ambapo walikaa kwa masaa manne bila kuruhusiwa kumuona mgonjwa.
Walirudi nyumbani na kurudi tena hospitalini jioni ambapo waliruhusiwa kuingia ndani na kumkuta yule mtu aliyemgonga Jothan akwa pale hospitalini. Bahati alimuelekeza mama yake kwa yule mtu aliyeonekana na moyo wa pekee kwa kukubali kuisimamia afya ya Jothan kwa kipindi chote atakacholazwa pale hospitalini.
“kwa maelezo ya dokta, amesema kuwa atarejewa na fahamu kiasi katikati ya wiki hii,.. ila itachukua muda mrefu kurudiwa na kumbukumbu.” Aliongea yule jamaa alyemgonga baada ya kujitambulisha kwa jina la Saimon.
Baada ya taarifa zile, walikubaliana na kuondoka huku zoezi la kumuangalia Jothan likiwa linaendelea kila siku.
Baada ya wiki mbili jothan alifumbua macho. Lakini hakuweza kuongea na hakuwa na kumbukumbu yoyote.
“kwa hiyo dokta tunaruhusiwa kuondoka naye” aliuliza Saimon baada ya daktari kuridhika na maendeleo ya Jothan.
“mnaruhusiwa, ila kwa masharti. Msimsumbue kwa kumlazimisha akumbuke kitu chochote. Maana kumbukumbu zake zitakuja taratibu kutokana na mazingira katika ubongo wake.” Aliongea dakrari katika moja ya kuwapa maangalizo juu ya mgonjwa wao.
“sawa, sasa inaweza kuchukua muda gani hadi kurudiwa na fahamu zake sawa sawa?” aliuliza Bahati.
“inaweza kuchukua miezi sita, nane au mwaka mzima kutokana na ukubwa wa tatizo lenyewe.” Aliongea daktari na kuwafanya wote waliokuwa pale waishiwe nguvu.
Walikubaliana waondoke naye na kwenda kukaa kwa kina Bahati huku Simon akiwaambia kuwa atakuwa pamoja nao katika kila hali.
Kutokana na kuchanganyikiwa siku aliyopata ajali Jothan, Bahati hakuokota kitu chochote alichokuwa amebeba Jothan siku ile. Hivyo hakuwa na mawasiliano angalau amjulishe Shani juu ya ajali iliyompata mpenzi wake.
Siku zilikatika kwa kasi bila Jothan kuonyesha dalili zozote za kukumba yaliyokuwa nyuma. Hata jina lake tu alianza kulizoea baada ya Shani na mama yake kulitamka kila mara.
Kwa upande wa Bahati alijisikia raha kumuuguza Jothan kwakua alikua analipa fadhila kwa yale aliyomtendea. Alihakikisha kuwa kila alichokihitaji mgonjwa wake basi alikua anakipata kwa wakati.
Aliamua kurudia kazi yake ya kuuza maua ili alishe familia inayomkabili.
Baada ya miezi sita kupita, Jothan alianza kuonekana kukumbuka kidogo kidogo. Aliweza hata kuuliza kuwa yupo wapi na ni nini kilichomleta pale. Alitamani kwenda kazini tena kama zamani.
“PRISCA…… PRISCA”
Alisikika Jothan usiku akilitaja jina la mwanamke huyo mara kadhaa. Bahati ambaye alikua amekaa kimya wakati wote, aliamka kutoka kwenye godoro la chini alipolala na mtoto wake na kumsogelea Jothan. Alishangaa kumuona Jothan akitokwa machozi.
“mimi ni Bahati “ alijitambulisha Bahati mbele ya Jothan ambaye alikua macho usiku huo huku akitokwa na machozi.
“yupo wapi Prisca.” Aliuliza Jothan na kumfanya Bahati ashtuke kidogo kwakua hakulifahamu jina hilo..
“Prisca mimi simjui… au ndio Shani ana majina mawili?” aliuliza Bahati na kumfanya Jothan afikirie kwa muda mrefu.
“Shani.. Shani… ndio nani huyo?” aliuliza Jothan huku akionyesha kutokuwa na kumbukumbu nae. “si yule aliyekuwa unaishi nae kabla ya kuja huku ?” aliongea Bahati na kumfanya Jothan avute taswira juu ya mtu huyo aliyekuwa anamzungumzia Bahati.
“huyo simkumbuki, yupoje kwani?” aliuliza Jothan na kumuangalia Bahati ambaye wakati huo alikuwa mbele yake akiongea kwa sauti ya taratibu kwa kuwa usiku ulikuwa tayari ni mkubwa. Hivyo sauti zao zilipea na kusikika kila mahali mule ndani.
“ni mnene kiasi, mweupe na ana shepu Fulani hivi .. anapenda kuvaa ma wigi ya rihanna.” Alijaribu kumkumbusha Jothan kwa kumtajia muonekana halisi wa mtu huyo.
“huyo simukumbuki,….. ninaye mkumbuka mimi ni msichana mzuri niliyeanza naye mapenzi toka tukiwa shuleni. Ni msichana mzuri sana. Na kila siku zilivyozidi kujongea, basi uzuri wake ulikua unaongezeka kila siku iendayo kwa Mungu. Nalikumbuka jina lake huyo dada. Anaitwa Prisca. Ila sijui muonekano wake kwa sasa. Labda ikitokea kuonana nae.”
Aliongea Jothan huku akijaribu kuvuta hisia zake juu ya msichana huyo anaye mkumbuka kwa machache tu.
“daktari alituambia kuwa tusikusumbue kwa kukumbusha ya nyuma. Ila utakumbuka taratibu. Ni vyema ulale Jothan ili uipumzishe akili yako.” Aliongea Bahati na Jothan akakubaliana nae.
Kila siku ambayo Bahati alikua anarudi kutoka katika mihangaiko yake, aliutumia muda huo kupiga stori mbali mbali na Jothan. Wakati mwengine alimtembeza sehemu kadhaa maarufu. Kila akipata fedha nyingi, basi humchukua Jothan na kumpeleka shooping kwa ajili ya kumnunulia nguo.
Baada ya miezi miwili kupita, Jothan alirejewa na fahamu zake kamili. Alikumbuka kila kitu. Hata siku aliyokuwa anataka kurudi Dar na kupata ajali ya gari pia aliikumbuka. Alimkumbuka pia Bahati ambaye wakati huo alikuwa naye bega kwa bega wakishirikiana na Simon ambaye alikua anakuja kumtembela mara kwa mara na kumuachia chochote kitu.
Siku moja Jothan akiwa barazani anapunga upepo, alifuatwa na Bahati aliyekuwa amebeba Juice glasi mbili na kumkabidhi moja. Aliipokea na Bahati akakaa karibu yake.
“lete story” aliongea Jothan baada ya kumuona Bahati kama alikua ana kitu Fulani alichokuwa anataka kumwambia.
“nina mpya basi, zaidi kama hutojali. Nilikuwa nahitaji ushauri kutoka kwako.” Aliongea Bahati na kumtazama Jothan.
“ulikuwa au unahitaji ushauri kutoka kwangu.” Aliongea Jothan kimzaha. “naomba unishauri,.. Simon ameniambia kuwa ananipenda na yupo tayari kufunga ndoa na mimi. Wewe kama wewe unamuonaje Simon. Anafaa kuwa mume wangu?” alifunguka Bahati na kumuangalia Jothan aliyekuwa anamuangalia pia.
“kwa muda mfupi toka nimfahamu huyo mtu, sina shaka naye hata kidogo. Maana alikuwa na uwezo wa kukimbia siku ile aliyonisababishia ajali au hata kunikimbia hospitali. Lakini mpaka sasa ametupa hela nyingi kwa ajili yangu. Huwezi jua Bahati, si ajabu Mungu kamkutanisha na wewe kupitia mgongo wangu. Cha msingi zisikilize hisia zako maana wewe ndio utakuwa naye kipindi hicho mimi nitakapokuwa mbali na wewe. Kama na wewe unampenda na yeye yupo tayari kumlea mtoto wako ni dhahiri shahiri kuwa na yeye anakupenda pia.”
Jothan aliongea maneno yaliyomkuna sawasawa Bahati. Alibaki anatabasamu na kumuangalia Jothan ambaye naye alikua anatabasamu pia.
“nilikuwa nampenda muda mrefu sana, sema nashukuru sana kuwa hata yeye kumbe alikua ananifikiria.” Alingea Bahati.
“hongera. Nilitaka kurudi Dar wiki hii, ila kama ndoa iatapangwa mapema basi nitasubiria mpaka muoane.” Aliongea Jothan na kumfanya Bahati afurahi kupita kiasi.
Siku ya harusi kati ya Bahati na Simon iliwadia na maharusi walionekana kupendeza kupita kiasi. Jothan alilifurahia tukio lile baada ya Bahati kuonekana kubadilika na kuwa mwema na mtu mwenye jitihada kama alivyokuwa zamani.
Baada ya siku mbili, Jothan aliaga na kurudi Dar.
Kwakua hakuwa mgeni wa jiji, alitambua magari ya kinondoni na kuelekea kwake.
Alifika nyumbani kwake na kukuta kufuli nje ya geti lake. Hakuwa na jinsi zaidi ya kukaa pembeni kwenye Café iliyokuwa inatazamana na geti lake ili Shani atakaporudi aweze kukutana naye.
Alikaa mpaka saa mbili usiku, lakini hakukuwa na dalili za mtu yeyote kufika pale. Aliamua kwenda kulala Gesti kutokana na uchovu wa safari aliokuwa nao.
Aliamka asubuhi na kupata chai, baada ya hapo akaelekea nyumbani kwake. Pia alikuta geti likiwa limepigwa kufuli kama ilivyokuwa jana yake. Aliamua kumfuata dalali mmoja aliyekuwa ameweka benchi lake pembeni ya nyumba yake na kumuuliza.
“samahani mzee Sadi, hivi huyu mke wangu ana muda gani toka afunge hili geti?” aliuliza Jothan baada ya kusalimiana na mzee huyo aliyemzoe kwa muda mrefu akiwa pale nje na kufanya shughuli zake za udalali wa nyumba,viwanja na vyumba vya kupangisha.
“hivi hauna habari?” aliongea mzee Sadi na kumshangaa sana Jothan kwakua alikua anajua kila kitu.
“sina habari yoyote mzee wangu. Nimeingia jana tu kutoka Arusha, hivyo sina habari yoyote mie!!.” Aliongea Jothan kwa mshangao mkuu. Alianza kuhisi jambo baya linaweza kuwa lilimkumba Shani kipindi ambacho alikuwa hayupo.
“mbona hii nyumba imeshauzwa miezi miwili iliyopita?... tena matangazo yalibandikwa muda mrefu. Sema wenye nyumba bado hawajahamia. Si unajua watu wenye fedha zao bwana?.” Aliongea yule dalali na kumfanya Jothan apigwe na bumbu wazi.
“OOOOH MY GOD……..WHY ME?????”
Alijikuta nguvu zinamuishia Jothan na kukaa chini. Aliiangalia nyumba yake aliyoijenga kwa gharama kubwa na machozi yalianza kummiminika kama maji. ITAENDELEA
0 Comments