Header Ads Widget

Responsive Advertisement

LIDAKE TENA CHOZI LANGU - 4

Image result for MY TEARS


Simulizi : Lidake Tena Chozi Langu
Sehemu Ya Nne (4)


Ilikuwa ni baada ya siku mbili za kupewa taarifa na daktari kuwa kuna tetesi kuwa bwana mmoja anayetaka kujiingiza katika siasa katika uchaguzi ujao.
Ikiwa ni saa mbili usiku tukiwa tunafurahia kwa pamoja chakula cha usiku ule tukiwa familia nzima, mara tulipata ugeni wa ghafla.
Na mgeni mwenyewe hakuna aliyekuwa anamjua.
Alipokaribishwa hakutaka kuketi badala yake alimuita daktari kiurafiki tu daktari akamfuata wakazungumza waliyozungumza kisha wakaagana juu kwa juu.
Nilichokisikia ni kitu kimoja tu yule bwana alimsisitiza kuwa afike kesho yake walipokubaliana.
Daktari aliingia ndani akiwqa na uso ambao ulionyesha mashaka sana.
Na hakuweza tena kuendelea kula kile chakula alifika na kunywa maji mengi sana. Alikuwa ameshikilia bahasha mkonononi.
“Hebu washa feni!” alimwambia mkewe, mke akawasha na kumuelekezea lile feni.
Licha ya kuelekezewa feni bado aliendelea kujipepea kwa kutumia ile bahasha.
“Mume wangu kwani kuna nini… na huyo alikuwa ni nani sasa” aliuliza mke wa daktari huku naye akiwa ameacha kula na kunilisha mimi pia.
Badala ya kujibu daktari alishusha pumzi kwa nguvu sana.
Akanitazama mimi kisha akamtazama mkewe, akashusha tena pumzi.
“Eti kesho kutwa natakiwa mahakamani kuna bwana mmoja ameniletea samasi eti nimemdhalilisha.” Alijieleza huku akitutazama.
“Unamfahamu huyo mtu ama…” nilimuuliza kwa utulivu.
Akanitazama na kisha akamgeukia mkewe.
“Mama Sikudhani, umezungumza na mtu yeyote kuhusiana na lile jambo?” daktari alimuuliza mkewe kwa makini sana.
“Jambo gani tena mume wangu….” Mkewe aliuliza huku akijiweka sawa kwenye kiti.
“Ama… au achana nalo hebu ngoja kesho tutazungumza….” Alisema na hapo akasimama na kuelekea chumbani kwake. Mkewe hakungoja akamfuata kwa nyuma hukohuko chumbani, sikuwa tena na mtu wa kunilisha chakula. Nilikitamani sana chakula kile lakini nisingeweza kula mwenyewe nilihitaji kulishwa.
Kwa unyonge kabisa na mimi nikasimama na kutoweka. Nikaenda kulala.
Nililala huku nikimuwaza mama yangu, nilijiuliza sana juu ya mapokeo yake katika hali yangu ile ya kuumiza nafsi.
Nikapitiwa na usingizi nikimuwaza mama yangu. Mama Majaliwa!!

Asubuhi daktari aliwahi sana kuamka, akaondoka kuelekea kazini akituaga sote mimi na mke wake kuwa atawahi kurejea.
Hakurejea kama alivyoahidi badala yake mkewe alipokea simu majira ya saa saba simu ambayo ilizua mtafaruku.
Aliniita kwa sauti ya juu huku akihangaika kuifunga vyema kanga yake kiunoni.
Licha ya kwamba nilikuwa karibu yake sana lakini alikuwa akiongea kwa sauti ya juu nikaziona dalili za mwanamke yule kuchanganyikia.
“Mama kuna nini kwani kinatokea.”nikamuuliza lakini hakunijibu badala yake aliendelea kutokwa na maneno mengi.
“Majaliwa natoka, natoka kidogo mume wangu ana matatizo kidogo sijui niseme matatizo makubwa sasa njoo huku nifuate” alinielekeza pa kumfuata nikafanya hivyo hadi chumbani kwake.
“Ingia katika mlango huu, usitoke hata mtu agonge vipi. Wewe utatoka ukitaka mwenyewe, nikifika mimi nitakuita kwa jina la Steve hapo ndo utatoka lakini isiwe vinginevyo sawa. Nakusihi hivi kwa sababu hakuna adui yetu hata mmoja kati ya wale waliotuvamia ambaye amekamatwa tunaamini bado wanatuwinda lakini ukiwa katika sehemu hii hawawezi kamwe kufungua bi9la wewe kutaka. Tunakupenda sana Majaliwa…”alimaliza akanibusu shavuni.
Nikaingia katika kifaa kile ambacho kilifanana na kabati lakini lilikuwa kubwa sana, sikuweza kuelewa ni kwanini kifaa kile kilikuwa pale chumbani.
Mama akaondoka huku mashaka yakijitangaza waziwazi katika uso wake. Lazima kulikuwa kuna tatizo kubwa tu.
Tatizo gani sasa?
Sikuweza kupata jibu hadi mama aliporejea baadaye jioni. Alikuwa analia sana, na aliponiona kile kilio cha kimyakimya kikakatika na kuanza kulia kwa sauti ya juu sana.
Alinifikia na kunikumbatia na hapo akaanza kunieleza kijuu juu kuhusu tukio lililotokea.
Akanieleza kuwa mume wake alikuwa ametiwa kizuizini kwa kosa la kumzalilisha mfanyabiashara mkubwa wilayani pale kwa kupakaza kuwa anahusika na mauaji ya Albino.
Huku akiwa analia bado aliendelea kunieleza kuwa kwa hofu ya Mungu kabisa ni heri asiseme uongo. Akanieleza kuwa ni kweli baada ya kuelezwa jambo lile na daktari juu ya muhusika wa viungo vya albino na yeye alitamani pakuche akamueleze.
Baada ya kumweleza huyo rafiki hajui kama na yeye amezisambaza sana ama kulikuwa na lolote kati ya huyo msambazji
Kesi ile ilienda kwa kasi na wakati huo ikiwa imechukua nafasi kubwa sana hapo wilayani.
Nilikuwa sijui cha kuzungumza. Nikajiuliza maswali makuu ambayo yanaweza aidha chanzo cha kesi ile kwenda kasi kiasi kile.
Hapakuwa na jibu moja nilibaki kuamini kuwa pesa ndo chanzo….
Pesa ilikuwa ikihusika katika kuifanya isokuwa halali ionekane kuwa halali.
Daktari alinyimwa dhamana, daktari hakupewa nafasi ya kuongea na mkewe eti kisa tu upelelezi utaharibika.
Na hatimaye daktari akageuziwa kesi eti yawezekana anahusika katika tukio la kuikata mikono yangu na sikio.
Ilianza kama tetesi na baadaye ikatapakaa wilayani kuwa daktari amenikata mikono yangu.
Nilishangaa kilichokuwa cha ajabu ni kwamba sikutafutwa ili kutoa ushahidi wowote.
Majuma mawili yakapita daktari akiwa mahabusu. Si kwa kesi ya kumdhalilisha mtu bali kesi ya kuhusika katika kukata viungo vya albino na kuvifanyia biashara.
Kitendo cha kuendelea kuishi katika nyumba ya mtu mwema yule huku nikishindwa kumtetea kwa jambo lolote lile katika shutuma hizi za uongo mkubwa kilinifanya nijisikie fedheha sana, hasahasa mbele ya mkewe ambaye hakuchoka kunilisha kila siku.
Yaani mzigo aliotakiwa kuubeba mama yangu yeye aliubeba kwa mikono yake yote miwili.

Sikutaka siku ziendelee kwenda mbele huku kila mara nikiwa nafungiwa katika chumba kile chenye mlango wa chuma ili nisiweze kujeruhiwa na kisha kuuwawa kabisa na wale watu wabaya walioukata mkono wangu pamoja na sikio.
Nilitambua wazi kuwa nikimshirikisha mke wa daktari kuwa nahitaji kwenda kumtetea daktari ili akiepuke kitanzi kinachomkabili waziwazi atakataa katakata.
Nikafikiria kuwa liwalo na liwe, nitatoroka na kisha kupambana ili ukweli umweke huru daktari yule.

Mke wa daktari alikuwa akinitia moyo kila kukicha kuwa kesi inendelea vyema tu, hakuwahi kabisa kuniambia kuwa mumewe amegeuziwa kesi. Habari hizo nilizipata kupitia redio.
Mke wa daktari hakujua kabisa kuwa hatimaye nilikuwa naweza kuwasha simu na kubofya vitufe kadhaa kwa kutumia vidole vya mguu wangu.
Naam!! Nilitambua kuwa hakutaka niumie na kisha kukata tamaa kabisa.
Aliendelea kukonda kila siku na tabasamu likitoweka usoni mwake.

Ni hapo nilipogundua kuwa jukumua langu kuu kabisa ni kulirejesha tena tabasamu lililokuwa limetoweka na kisha kuuleta tena uhuru wa daktari.

Siku aliyopanga kwenda mahakamani kusikiliza kesi ya mumewe nd’o siku hiyo niliyopanga na mimi kuifanya kuwa siku ya tukio. Liwalo na liwe!!

Kweli baada ya siku mbili baada ya kunilisha akaniaga kuwa anaenda mahakamani yawezekana siku hiyo ikatolewa hukumu. Alizungumza nami huku macho yake yakionyesha kabisa dalili ya uoga mkubwa na ni kama alikesha huku analia.
Nikajiuliza… nilikatwa mikono yangu yote bila ganzi, nikakatwa sikio langu na kidole cha mguu bila ganzi.
Nina kitu gani cha kuhofia kupoteza katika maisha haya.
Kama ni pumzi zangu wanazozitafuta basi na wazichukue nilikuwa nimeridhia.
Alipotoka na kunipa angalizo la kila siku kuwa nisitoke wala kumuitikia mtu.
Nilimkubalia kama kawaida na kumuaga.
Alipotoka na mimi nyuma nikatoka.
Nilipolifikia geti nikazitazama mbingu.
Na hapa nikaongea na aliyeniumba ambaye dunia nzima ipo chini yake.
“Baba… wewe ndiye baba yangu pekee, yule baba uliyemteua kuwa baba yangu hapa duniani alinikataa. Sina baba mwingine ila wewe. Sina wa kumuomba kwa lolote lile ila wewe. Wewe ni baba yangu mwaminifu, nakuamini hata kama umeruhusu mikono yangu kukatwa, wewe ni muaminifu kwa sababu haujawahi kunitoza kwa kuvuta pumzi zako. Kama uliweza kunipa pumzi zako bure bila kunibagua, baba naomba unipe hekima na ikiwa umenipa nafasi ya kushuhudia miujiza mingi bila mimi kukuomba miujiza hiyo naomba leo sasa unipe muujiza. Nipatie kwa sababu na uhitaji, lakini kama ikiwa utazinyakua pumzi ambazo ni mali yak oleo… mkumbuke mama yangu mpe maono mwambie Majaliwa mimi mwanaye ninampenda sana. Asante baba”
Sikurudi nyuma nikalifungua geti nikatoweka. Nilikuwa napajua mahakamani vizuri sana.

JIFUNZE
Umewahi kumuomba Mungu? Umewahi kulalamika kuwa Mungu hajibu maombi?
Acha kulalamika tena. Mungu wetu anakupa majibu wakati ambao wewe hutarajii. Na ule muda anaokupa majibu ndo wakati muafaka kabisa ambao ulikuwa unahitajika.
Usichoke kumuomba yeye, kwa sababu yeye hana udini, yeye hana ukabila.
Ilimradi sisi sote ni wanaye anatupa uzito sawa kabisa!!!


*******************

Nilifika mahakamani na kukuta kesi kadha wa kadha zikiendelea. Niliendelea kuwa mtulivu hadi nilipomuona daktari akipandishwa kizmbani.
Masikini wa Mungu alikuwa amevimba uso, alikuwa akitembea huku akichechemea.
Na wakati anapanda pale kizimbani watu walimnyooshea kidole huku wengine nikiwasikia wakisemezana kuwa yule ndiye muuaji wa Albino na lazima ahukumiwe kunyongwa la si nhivyo wanaandamana.
Amakweli wema huwa hawaishi siku nyingi na hii ni kwa sababu moja tu!! Wabaya wengi wanawazunguka hivyo kuwagandamiza sana.
Niliendelea kusubiri hadi pale aliposoimewa mashtaka yake na kuyakana. Alikuwa hawezi kuongea kwa sauti ya juu na alionekana wazi kuwa alikuwa amekata tamaa.
Ile hali yake ya kukata tamaa ikanikumbusha na mimi njilivyokuwa nimekata tamaa akanishika mkono na kunipa tumaini jipya sasa ilikuwqa zamu yangu kumwonyesha kuwa nazilipa fadhila zake hapahapa duniani na liwalo na liwe.
Nikaamua kutofuata utaratibu wa mahakama nikaamua kuipaza sauti yangu ilimradi tu wachache wanisikie wakaitangazie Tanzania na dunia kwa ujumla.
Nikaingia katikati ulinzi haukuwa imara sana kwa sababu mahakama ile ilikuwa haiwezi kutoa hukumu kwa kesi ya jinai kama ile basi walikuwa wanatoa tamko la kuifikisha kesi ile katika mahakama ya makosa ya jinai.
Nikasimama katikati ya mahakama nikiwa sina mikono yote miwili. Nikiwa sina sikio na sikuwa na kidole changu mguuni.
“Naitwa Majaliwa… naomba nisikilizwe!!” niliipaza sauti na mahakama nzima ikatulia badala ya kuchukua hatua za kunitoa pale.
Bila shaka kila mmoja alikuwa amepigwa na bumbuwazi!!
“Huyu mbele yenu anayetuhumiwa kuwa ni muuaji wa albino si kweli badala yake mwenye haki anagandamizwa kama muonavyo…. Huyu si muuaji bali mtetezi wa haki zetu sisi walemavu wa ngozi. Ameniokoa mara mbili bwana huyu, si mtu mbaya na ninatamka mbele yenu kuwa wakati akiwa katika harakati za kumtambua muuaji wa albino na kufanikiwa kumpata ndipo hapo amegeuka kuwa mtu mbaya. Nikataja jina la yule kiongozi ambaye daktari alitueleza kuwa anahusika na unyama huo. Na hapo nikawa kimya nikisubiri muujiza nilioumba kutoka kwa muumba wa nchi na ardhi.
Nilitazamana na daktari walau alionyesha uhai katika macho yake na alionekana kujaribu kutabasamu lakini akaishia katika maumivu. Naam! Ukawa muujiza kweli ulioambatana na kizaazaa…..
Askari wakanifuata pale waweze kuniondoa pale mahakamani, yule kiongozi alikuwa pale mahakamani. Watu wakaanza kumzongazonga na kumuuliza kulikoni.
Nguvu ya umma!! Iache iitwe nguvu ya umma.
Askari walikuwa wachache raia wakamvuta yule bwana njer na sijui kilichofuata ni kitu gani zaidi niliyasikia tu mabomu ya machozi yakifyatuliwa na kikazuka kizungumkuti kila mmoja akijitafutia usalama wake.
Polisi waliokuwa wamenidhibiti wakaniachia na mimi nikawaponyoka kwa kasi na kuelekea popote ambapo ningeweza kuwa salama.
Lakini sikufika mbali nikaanguka chini, nilichokiona ni umati mkubwa ukija upande wangu na kisha kupita kwa kasi wakinikanyaga kana kwamba hapakuwa na mtu pale chini. Nilijaribu kuwasihi kuwa wasainikanyage lakini haikuwezekana.
Nikaanza kukosa hewa palepale chini, nikatambua kuwa iwe isiwe kwa safari ile siwezi kupona tena. Nikayafumba macho yangu na kumtukuza Mungu kwa kila jambo lililotokea na hapo kiza kinene kikatanda.

Fahamu zilirejea tena!! Mungu yu wa ajabu sana!!!
Sawa nilikuwa hai lakini nilipokuwa hapakuwa sehemu sahihi.
Kweli ilikuwa nyumba nzuri haswa na nilikuwa nimevalishwa nguo nyingine kabisa.
Lakini nilipotazama ukutani nikaiona picha fulani ambayo haikuwa ngeni hata kidogo.
Ilikuwa sura mbayo nimewahi kuiona kabisa, nikaitazama vyema sana na hatimaye nikakumbuka kuwa sura ile niliiona pale mahakamani.
Ilikuwa ni sura ya yule bwana mwanasiasa ambaye alikuwa akimtuhumu daktari kuwa anahusika katika harakati haramu kabisa za kuwaua maalbino.
Nikiwa bado pale ndani niliusikia mwili wangu ukiwa katika maumivu makali sana. Nikajitahidi kujiweka sana, nikaweza kuuona mguu wangu ukiwa katika bandeji gumu maarufu kama P.O.P.
Nikatambua kuwa nilikuwa nimevunjika mguu wangu. Bila shaka nilipoanguka pale chini kisha watu wakanipandia juu yangu.
“Naona umeamka mwanaharakati..” nikaisikia sauti ikitokea nyuma yangu.
Nilipojitahidi kugeuka nikakutana na sura ya yule mwanasiasa.
Sikujibu kitu chochote kwa sababu swali lake lilikuwa la kinafiki haswa.
Nikajilaza na kusubiri kitu ambacho ataamua juu yangu. Mwili wangu ulikuwa umeingia ganzi tayari na sikuwa mwenye hofu kama awali nilijiona mimi kama mtu wa kufa tu ambaye sina haki ya kuishi tena.
Yule bwana alizungumza mambo mengi sana alinitukana kila aina ya tusi ambalo kinywa chake kilihimiri kuweza kulitamka. Akanitukania mama aliyenizaa na ukoo wangu kwa ujumla. Akawatukana walemavu wote wa ngozi na kisha akaanza kujisifia kuwa yeye na nguvu alizonazo, nguvu zake dhidi ya viongozi wa serikalini, nguvu zake dhidi ya mahakama na penginepo ambapo alijisikia fahari kupataja.
Katika maongezi yake kuna kitu alisema nikajikuta natabasamu. Alisema eti anamshukuru Mungu kuwa utajiri wake amepambana mwenyewe kuupata na si wa kurithi kutoka kwa wazazi wake.
Nilitabasamu kwa sababu nilitambua kuwa hata watu wakatili wanatambua kuwa Mungu yu hai. Sasa kama wanatambua hili ni kwanini wanathubutu kufanya uasi mkuu kama huu ilihali wakitambua wazi kuwa siku ya kiama tunahukumiwa kutokana na matendo yetu??
“Unanicheka eeh!!” alinichimba mkwara alipoona natabasamu wakati yeye anazungumza.
“Hapana sikucheki mkuu, natabasamu kwa sababu stori ya maisha yako inatia hamasa sana!!” nilimjibu vile kwa lengo la kumtia hasira. Ikiwezekana achukue maamuzi hata ya kunipiga risasi nife kuliko kuendelea kuwa pale kisha aendelee kukata viungo vyangu na nilitambua wazi kuwa sasa wangenikata sehemu zangu za siri!!
Ndugu msikilizaji damu ilinienda kasi sana baada ya kufikiria jambo hili, ule uoga ukarejea upya kabisa na kujikuta nikiwa katika mtetemeko wa ajabu!!
“Ujue kijana ulijifanya mjuaji sana ulipojitokeza mahakamani ukiamini kuwa utaniumbua. Ni vile tu hauuijui serikali yetu vizuri wewe… serikali yetu katika ngazi za chini imejaa ubadhjilifu mkubwa. Pesa ina nguvu kuliko hiyo haki uliyokuja kuitafuta. Dah! Ulinitisha kweli ulipojitoikeza pale nikasema sasa leo nd’o mwisho wangu lakini nilipokumbuka kuwa pesa inazungumza hofu ikapungua. Najua ulipoteza fahamu hata hujui kilichotokea hadi sasa upo hapa…” alisita kidogo kisha akaiendea glasi ya maji na kugida kwa kipimo alichoridhika kisha akaitua glasi.
Alipotaka kuendelea kuzungumza nikamuuliza swali.
“Samahani kaka… kwani umnaamini kuwa Mungu yupo?”
Lile swali likawa zito kwake na lilionekana kumkera kwa sababu nilimuuliza ukweli kabisa.
Nilimuona akipumua kwa kasi bila shaka ishara ya hasira. Nikaona niendelee kumpandisha hasira ili afanye maamuzi kwa kutumia hasira yake.
“….tazama nilikatwa mkono mmoja, ukafuata mkono mwingine, nikakatwa sikio kisha dole gumba langu, sikia nilikanyagwa na watu hadi kupoteza fahamu na kuvunjika mguu pia….. ni kitu gani unajifunza kupitia maisha niliyopitia. Unadhani Mungu unayemshukuru kwa kukupatia maisha bora anapendezwa na haya?? Naomba unijibu tafadhali la si hivyo jicho langu litakushuhudia siku ya kiama ukiteketea na mto usiopungua makali na sitasita kukuuliza tena ikiwa unayo hofu na Mungu!!!” nilitokwa na maneno yake kwa mtiririko usiokoma.
Maneno yale yakamkera sana kwa sababu moja tu, nilikuwa nasema ukweli mtupu.
Akanifuata pale nilipokuwa!! Kabla hajanigusa nikamchokonoa tena.
“Labda uniue lakini kama ni kunipiga nimepigwa sana moyo na mwioli wangu vimekufa ganzi, tazama usivichafue vigaye vyako kwa damu kwa jambo linaloewpukika!!! Mtanzania mtaka madaraka na hatendi haki kwa baadhi ya wananchi wake….. kiti cha uongozi utakachokikalia kitakuhukumu viobaya sana…..” nilimaliza kisha nikamfanyia ishara kluwa anaruhusiwa kufanya jambo ambalo alikuwa anataka kulifanya!!
Upesi akaondoka na kurejea akiwa na panga kali sana, makali yale yalinitonesha moyo upya na kutambua kuwa nilikuwa naenda kufa kile kifo ambacho nilikuwa nakikataa kila siku.
Huyu bwana angenicharanga mapanga na kuniua!!!
Nakufa bila kumuona mama yangu!!

“Unajifanya unajua sana kutoa ushauri sivyo, hebu lishauri panga hili lisikukate sasa….” Alisema huku akijilazimisha kutabasamu. Nilimtazama kisha nikafumba macho yangu!!
Nafsi ilikuwa katika unyonge mkubwa sana.
Alifika na kuanza kunivua ngua zangu.
Dah! Nilichowaza kukatwa sehemu zangu za siri kilikuwa kinaenda kutimia!!
Hofu ikanitetemesha zaidi na kujikuta koo likinikauka.
Alifanikiwa kunivua nguo hovyohovyo na kujikuta nikiwa uchi wa mnyama!!
Yule bwana alikuwa amenuia kabisa kuniumniza…
Sikuwa na mikono ya kujitetea…. Mtanzania mwenzangu anaenda kunipa maumivu ambayo yeye binafsi hatamani kuyapata na hawezi kuyahimili!!!
Nikafumba macho nikijilamisha kupoteza fahamu lakini haikuwezekana nilimsikia kila alichokuwa akisema na kutenda!!!

JIFUNZE!!
KILA JAMBO LENYE MWANZO HALIUKOSI MWISHO WAKE. FANYA SASA BAYA LINALOKUFURAHISHA NAFSI YAKO LAKINI TAMBUA KUWA MWISHO WA UBAYA NI AIBU NA UCHUNGU MKUBWA



**********

Nikiwa nimeyafumba macho yangu huku nikitambua fika kuwa iwe isiwe lazima tu yule bwana ataniua. Nikajiona mzembe kufa kirahisi bila hata kuparangana kana kwamba ni haki ya yule bwana kuniua.
Nikayafumbua macho ghafla na kumkuta akiwa anajiandaa kunifanyia alichotaka kunifanyia. Bila kutarajia nikajikuta nafanya kitendo cha kijasiri bila kuwa na mikono yangu.
Ningetumia silaha gani kama sio meno yangu.
Mpenzi msikilizaji, hii sio simulizi ya kutungwa ukalichukulia lililotokea kama jambo la kawaida.
Ni kweli yalinitokea.
Nikamrukia yule bwana nikiwa nimeyaandaa meno yangu na kutua vyema katika shingo yake. Ikawa bahati nzuri kwangu na mbaya zaidi kwake.
Meno yakainasa shingo ipasavyo.
Nilitumia nguvu zangu zote zilizokuwa zimebakia mwilini kumjeruhi yule bwana, nikayaunganisha meno yangu, kwa sikio langui moja nikakisikia kisu alichokuwa amekuja nacho kikidondoka chini na yowe kubwa likimtoka.
Nikazidi kumtafuna shingo yake huku nikijua kuwa ule ndio ulikuwa mwisho wangu. Sikujali damu iliyokuwa inaruka nilichotazama ni kwamba na yeye anaumia kama tulivyokuwa tunaumia sisi.
Nikiwa nimemng’ang’ania yule bwana hadi sauti ikawa imekatika. Nikasikia mtu akijaribu kunivuta kwa nyuma, wakati huo yule bwana alilegea na kutua chini, nikiwa nimelowa damu vibaya mno na mguu wangu wenye lile hogo gumu kabisa, nikamtandika tege kwa kutumia ule mguu wenye hogo.
Kimyaa!! Hakutikisika!!
Nikageuka nikakutana na mwanamke ambaye alikuwa akijaribu kunizuia nisiendelee kumsulubu yule bwana. Sikujali lolote sasa nilikuwa kama kichaa, nilimvaa yule mwanamke nikaanguka nay echini.
Wakati naanguka nikakutana na picha ukutani yule mwanamke akiwa na yule mwanasiasa.
Kumbe ni mke wake!!!
Hasira maradufu ikanipanda tena, nikaendelea kutumia silaha ya meno. Nikamng’ata mkono wake kwa nguvu zote akatapatapa na kunirusha huku na kule.
Naam! Akafanikiwa kunitoa katika mkono lakini sasa nikatua katika paja lake, bahati iliyoje. Niliingiza meno yangu pale kwa jinsi yalivyopenya nikahisi ni kwa namna gani alikuwa akiumia yule mama.
Na aumie tu kwa sababu nilitaka aumie sikumg’ata ili afurahie.
Alipiga kelele kubwa sana na kisha akapoteza fahamu.
Upesi nikatoka katika chumba kile nikiwa natamani sana kuwa ningekuwa na mkono nilichukue bisu lile na yeyote atakayekuja mbele yangu awe halali yangu.
Lakini sikuwa na mikono tena. Nikaifungua milango kwa kutumia miguu na mikono.
Hatimaye nikalifikia geti na huko nikakutana na mlinzi.
Bila shaka alipagawa kuniona nikiwa nimevuja damu kiasi kile.
Akaanza kunionya kuwa nisimsogele.
Ebwana eeh!b nikaisikia lafudhi yake, alikuwa na lafudhi ya kabila langu.
Aikwambie mtu kuwa kabila halina thamani tafadhali sana jifunze lugha mbalimbali jifunze makabila mbalimbali pia ukiweza. Wakati mwingine ukizungumza na mtu kwa kabila lake ama lugha yake anajikuta anakusikiliza na kukupa nafasi ya kujitetea.
Palepale nikatumia faida ile ya lafudhi ya mlinzi nikamsemesha kikabila.
“Naitwa Majaliwa mwenyeji wa Dodoma, Mgogo halisi kabisa… ikiwa sawa kushiriki katika kuniua mimi ndugu yako basi uniue kwa kutumia hilo gobole lakini kama si sawa kushuhudia mimi ndugu yako nikifa tafadhali nisaidie, nimeteseka imetosha sikuzaliwa unavyoniona nilivyo, wamenikata viungo vyangu, tafadhali usishiriki dhambi hii…’ nilizungumza kiujasiri sana.
Na kweli kabila likaleta uzito akaniuliza ni kipi kimetokea hadi nimelowa damu vile. Nikamweleza kuwa ilikuwa niuwawe. Ni Mungu tu ameniokoa.
Kweli ikawa yale ya damu nzito kuliko maji. Akanisogelea huku akionekana kuwa na hofu akanichukua na kunitoa nje, huko akaniambia kuwa yeye ni mlinzi na huwa hajui ni kitu gani kinaendelea pale.
Lakini kuna watu ambao huwa anawaona wakija eneo lile na kuondoka. Na yale sio makazi ya mtu bali kwa msimu tu.
Aliposema kauli hizi akanifanya nitambue kuwa eneo lile ni la siri sana na ni maalumu kwa maovu kama haya.
Ajabu sasa akanieleza kuwa eneo lile lilikuwqa lipo Dodoma!!
Nilistaajabu mpenzi msikilizaji, yaani kumbe nilikuwa nimepelekwa kufia katika ardhi yangu ya nyumbani.
Yule mlinzi akanieleza kuwa sitakiwi kuwa pale na hata yeye pia hawezi kuwa salama ikiwa watafika watu wengine ambao huja katika nyumba ile na kutambua kuwa kuna kitu anakijua kilichotokea pale ndani.
Wakati anamalizia haya mara ikasikika gari iija kwa kasi.
Akaniamrisha nipotee, na hapoi akaqongoza njia na mimi nikimfuata nyuma.
Msikilizaji, sikio la mwanadamu hutumika katika kubalansi mwendo, kwa jinsi nilivyosoma shuleni ni kwamba mtu asipokuwa na masikio hawezi kuendesha baiskeli wala hawezi kukimbia mwendo mrefu.
Sasa nilikuwa katika kuona kwa macho yangu, nilikuwa naanguka hovyo hovyo yule mlinzi akawa ananinyanyua na kuendelea kukimbia sikujua hata ni wapi tulikuwa tunaenda.
Ila sikuchoka kwa sababu nilijua kuwa Mungu yu pamoja nasi na ni yeye aliyeniokoa hadi kufikia pale nilipokuwa.
Baadaye yule mlinzi mzee ambaye ndiye aliyekuwa anaongoza njia alishikwa na kichomi, akaapa kuwa hawezi kuendelea kukimbia. Nilitamani basi mimi nimbebe lakini ningeanzaje sasa.
Akanisemesha kilugha akanisihi nikimbie tu na nikifika kijiji cha tatu kutoka hapo niulizie kwa mzee anayeitwa Chilongani. Nikishampata nimeweleze kila kilichotokea na kisha yule bwana akajitambulisha kwa jina la Gaspa.
Nikaendelea kukimbia huku nikiamini kuwa utakuwa muujiza tu kufika salama.
Nilikimbia huku nikiendelea kuburuza mguu wangu wenye bandeji gumu.
Ilikuwa ngumu lakini ningefanya nini, walau nilikuwa katika ardhi niliyozaliwa huenda nilikuwa nimeikaribia mikono salama.
Sikuwa hata naelewa ni umbali gani kukimaliza kijiji kimoja hadi kingine lakini nilikimbia tu bila kukoma.
Hatimaye na mimi nilichoka hadi hatua ya mwisho.
Lakini bado niliendelea kutembea mwendo wa taratibu sana.
Na hatimaye nikaamua kucheza pata potea. Nikaiendea nyumba fulani nikaugonga mlango. Niligonga kama mara tatu, hatimaye mlango ulifunguliwa na mwanaume aliyekuwa na panga kali.
Akauliza kikabila, na mimi nikajibu kikabila. Nikataja jina la Chilongani!!
Akaniuliza iwapo mimi ni mwenyeji eneo lile nikamwambia kuwa ni mwenyeji kiasi kiasi fulani.
Akaniuliza jina la ukoo wangu, nikamjibu!!
Nilipojibu jina langu la ukoo, ghafla nikasikia kilio kikubwa sana kutoka ndani.
Kilikuwa ni kilio cha mwanamke…..
Na mara yule mwanaume pale mlangoni akasukumwa na kuangukia mbali na hapo nikajikuta natazamana ana kwa ana na mama Majaliwa!!
Akanikimbilia kwa nguvu sana na kunikumbatia tukaanguka chinbi wote.
Nilibaki tu kuita mama mama… nisijue ni kitu gani naweza kusema.
Yaani usiku mnene kama ule nikiwa nahitaji msaada mkubwa kabisa nakutana na mama yangu mzazi??
Nilistaajabu msikilizaji, nililia sana….
Mama yangu naye alilia sana!!
Wakati haya yakiendelea yule bwana aliyekuwa ameanguka mbali alikuwa sasa amesimama akishangaa kilichokuwa kinaendelea!!
Na tukiwa bado pale chini mama yangu alikoma kulia kisha akaanza kuzungumza.
“Maiko nilikwambia ukabisha, nilikwambia mwanangu anateseka, nilikwambia kuwa moyo wangu hauna amani hata kidogo ukasema niache imani potofu. Mungu alikuwa anasema na mimi, angali wamenitesea mwanangu, angali wamemkata mikono… yaani… yaani kweli wameniumizia mtoto wangu hivi..” mama hakuendelea kuzungumza tena akaanza kulia kwa sauti ya juu sana.
Sikuhitaji kuwaza juu ya nini kinachopita katika moyo wa mama yangu. Nilijua ni misumari mikali sana inaupasua moyo wake!! Mama yangu alikuwa anaumia sana!!!
JIFUNZE!!
Pendo la kweli ni pale ambapo mtu anakupenda bila kujalisha mapungufu yako, anakupenda ukiwa hai na hata ukiupoteza uhai, anakupenda ukiwa unalia ama ukiwa unacheka… unahitaji kuupata mfano wa penzi la kweli??
Pendo la mama ni pendo la kweli!!!


**************************************

Mama aliendelea kulia kwa uchungu mkubwa sana akiwa bado yupo pale chini. Alilalamika sana mama yangu, nililisikia kila neno ambalo alizungumza yule mama ambaye umri nao ulikuwa unamtupa mkono.
Aliilaumu serikali kuwa huenda haitulindi ipasavyo, akailaumu nchi kwa ujumla huenda haituhitaji watu kama sisi na hatimaye akaanza kumlaumu yule mwanaume ambaye alimpachika mimba na baada ya kujifungua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi akakimbilia mbali na kuitelekeza familia akaoa mke mwingine.
Alimlaumu kwa yote mema aliyowahi kumuahidi na kumsababisha apate uhakika kuwa mtoto atakayezaliwa atalelewa vyema lakini mwisho wa siku akaishia kutelekezwa, mama akalia sana akijilaumu na yeye kwa kutowasikiliza wazazi wake waliomsihi kuwa asikurupukie mapenzi.
“Labda nipo katika kuitumikia adhabu sasa, adhabu ya kilio cha wazazi wangu. Lakini mbona sasa imekuwa adhabu nzito kuliko uwezo wangu, mbona imekuwa suluba isiyofanana na yote niliyowahi kufanya. Mwanangu Majaliwa, sijawahi kukuchukia mtoto wangu, sijawahi hata kufikiria kukuchukia nd’o maana hadi umekuwa mtu mzima nikiwa nakulinda. Nilishauriwa mara nyingi sana ulipokuwa mdogo kabisa kuwa nikutelekeze kwa sababu utaniletea mikosi… sikuwahi kukubaliana na hilo jambo hata siku moja. Tazama nipo nawe hapa tena nakuambia tena neno hili na liishi nawe kila utakapokuwa aidha kwa uhai ama uzima. Nakupenda sana mwanangu wa pekee…”
Maneno haya ya mama yalikuwa mfano wa suluba kubwa sana katika nafsi yangu, nililia sana kumsikia mama yangu mzazi akiyasema yale tukiwa katika giza lile.
Wakati tukiwa pale kwa mbali tukawasikia mbwa wakibweka.
Nikamweleza mama kwa ufupi sana juu ya kilichokuwa kikitokea huko nilipotoka, upesi akishirikiana na yule mwanaume ambaye alikuwa ni mdogo wake yaani mjomba wangu.
Wakaniingiza ndani na kuniambia niingia chini ya uvungu na kisha nitulie tuli.
Kweli nilidumu pale kwa takribani dakika kumi kabla ya kusikia mlango ukigongwa, yule mjomba akajikausha kama aliyelala na baadaye akaamka. Akatoka nje na nikawa nayasikia mazungumzo ambayo walikuwa wakizungumza.
Nilijikuta natabasamu kwa ujanja alioutumia mjomba wangu, yule mgeni aliuliza Kiswahili na yeye akamjibu kigogo. Hivyo ikawa hakuna kuelewana!!
“Wewe jifanye haujui Kiswahili, nakuuliza hivi kuna ugeni wowote mmepokea hapa mkwenu usiku huu….” Akauliza kwa ukali sana lakini mjomba aliendelea kujibu kikabila.
Bila shaka yule bwana alichukizwa nikasikia akiongea maneno maneno kisha ni kama aliondoka. Maana mjomba aliingia ndani na kuufunga mlango.

Baada ya dakika takribani mbili mlango uligongwa tena, safari hii sasa hakuwa mtu mmoja bali watatu. Wakajitambulisha kuwa wao ni watu kutoka jeshi la polisi Tanzania, wanahitaji kufanya upekuzi kuna jambazi ametoroka hivyo msako unafanyika kijiji kizima kwa sababu wanaamini kuwa bado yupo hapo kijijini.
Hapo sasa nilianza kutetemeka sana, mjomba alijaribu kuweka ngumu akijifanya aelewi wanachomaanisha na mara wakamsukuma akaangukia pale ndani. Wakaanza kumurika na tochi zao. Nilitulia kama gunia ambapo limehifadhiwa pale ndani.
Wakakifikia chumba alichokuwa amelala mama wakamuamsha nikamsikia akilalamika kikabila pia kuwa anasumbuliwa. Hatimaye akaamka na yeye akaendelea kujifanya hajui Kiswahili.
Bila shaka jambo hili lilisaidia sana watu hawa kupunguza umakini katika kufanya ukaguzi. Hawakufika kabisa uvunguni nilipokuwea, qwakaondoka huku wakijiuliza kuwa nitakuwa nimekimbilia wapi.
Na hapo nikaamini kuwa uwepo wangu hai ulikuwa unaenda kuwaweka watu wengi sana matatani.
Na ilikuwa ni heri kabisa katika mtazamo wao kuwa nife na wao wabaki na uhuru wao. Mtazamo wqa kiuaji kabisa na usiokuwa wa kibinadamu!!
Usiku ule ulipita kimashaka sana na kisha ukakuchwa ule wakati wa kuanza rasmi harakati za kufichua maovu yote.
Harakati ambazo zilijawa na ushuhuda wa damu za wenzangu wengi. Nilivishuhudia vifo vyao kwa macho yangu!!
Usiombe kupambana na adui mwanadamu mwenye roho yap aka ambaye hana huruma kabisa.
Nami nilijikuta katika vita hivi baada ya kuanza harakati hizi na niseme neno moja laiti kama wasingekuwa mama na mjomba kujitolea hata uhai wao nisingekuwa hapa kukusimulie hiki kilichonitokea.

Niliishi pale kijijini nikiwa nimefungiwa ndani muda wote na eneo langu la kulala likiwa ni palepale uvunguni. Yalikuwa maisha yanayostaajabisha lakini ilibidi tu kuwa vile. Sikuwa na mikono hivyo ilimlazimu mjomba wangu kuniogesha usiku na nilipohitaji kwenda haja kopo lilikuwa pale ndani hivyo ni kama tu nilikuwa mfungwa.
Ilifikia wakati nikazungumza na mama yangu na kumuuliza mambo mengi sana kuhusu mimi na familia yangu na pia juu ya watu wenye ulemavu wa ngozi, nilimuuliza mama ambaye ni mwanamke pekee ninayemuamini kupita wote hivyo hata jibu lake ni lazima tu ningeliamini.
Nilimuuliza na kumtaka anieleze ukweli ikiwa sisi albino tulikuwa nayo haki ya kuishi ama la!!
Mama alitabasamu kisha akajisogeza karibu yangu na kunieleza maneno yaliyonitia moyo. Yalikuwa machache lakini yalitosha kuwa tiba kwa jinsi nilivyokuwa nimekata tamaa.
“Majaliwa ulipotoweka hata na nilipopatwa hisia kuwa utakuwa hatarini baada ya vyombo vya habari kutangaza juu ya miili ya albino waliokutwa wamekatwa viungo vyao na kisha kufukiwa. Nilipiga goti na nilimuuliza Mungu swali hilo, nikamwambia kuwa ikiwa mwanangu Majaliwa na maalbino wengine wamekuja duniani bahati mbaya basi naomba iwe kwa heri kabisa kwa sababu wamerejeshwa sehemu waliyostahili lakini ikiwa wapo sawa kabisa na sisi na ule mzigo wa miezi tisa nilioubeba sikuubeba kuzaa kiumbe kisichokupendeza wewe basi nipe nafasi ya kumuona mwanangu tena akiwa hai. Upo nami hapa majaliwa unadhani Mungu wetu huwa anaongopa??” alimaliza kwa kuniuliza swali. Nikatabasamu kisha nikamkumbusha mama ya kuwa nampenda sana.
Naye akanambia kuwa ananipenda zaidi!!
Akasimama na kuniacha pale ndani!!

****

Siku iliyofuata mjomba alishughulikia mpango wa mimi kutoroshwa kimyakimya kutoka pale kijijini.
Nakumbuka siku ile nilimwambia mama kuwa ipo siku haya yanayonitokea mama yangu nitayasimulia siku moja huku nikiwa natabasamu kabisa tena tabasamu kutoka moyoni.
Naam! Leo hii nawasimulia huku natabasamu.
Harakati za kutoroka hazikuwa nyepesi ilibidi mjomba na mama wasaidizane kunipaka masizi usoni ili nionekane kuwa ni mweusi wakanipaka na miguuni.
Nilipowekewa kioo mbele na kujitazama, nililia sana lakini leo hii nikiikumbuka ile hali niliyokuwanayo nacheka tu kwa sababu kiukweli nilikuwa kituko.
Lakini ningefanya nini kwa wakati ule na hali tayari ilikuwa mbaya sana.
Nikaondoka mimi mama na mjomba tukapita njia za hapa na pale na hatimaye tukapata gari ambalo lilikuwa likifanya safari zake kuelekea jijini Dar es salaam.
Hata kabla sijafika jijini nikakabiliana na balaa kubwa barabarani.
Nasema tena kama usingekuwa uimara wa mama yangu na mjomba basi mimi Majaliwa nisingekuwa hapa.
Mungu awajaze nguvu zaidi watu hawa!!
Baada ya kupanda gari na kuchukua siti, mita takribani mia sita mbele tairi ikapata pancha, ikatengenezwa tukaendelea na safari baada ya muda kidogo tena gari likachemsha. Yaani gari lilikuwa linaharibika mara kwa mara. Sijui ila nahisi tangu awali gari lile lilionekana kuwa bovu tu lakini kama kawaida huwa hakosekani mbuzi wa kafara. Abiria wakaanza kulalamika kuwa kuna kitu ndani ya gari ambacho si sawa kabisa.
Wengine wakasema patakuwepo na mtu amebeba maiti, wengine wakasema hili na lile.
Na mwisho ikakubalika kuwa gari likiharibika tena itabidi mbuzi wa kafara atafutwe ilimradi tu safari iweze kuendelea vizuri!!
Ilikuwa baada ya nusu kilomita tu, gari likazima tena.
Sasa ikawa kwamba kila abiria amkague mwenzake na akihisi kama kuna utofauti wowote ule atoe taarifa na baada ya hapo itakaguliwa mizigo yote.
Pembeni yangu alikuwepo mzee mmoja mkimya sana. Akanigeukia!!! AKAANZA kunitazama kwa mashaka huku akijaribu kunikaribia zaidi.

Naam! Majanga hayamwishi Majaliwa yu safarini akiwa amefanikiwa kutoroka kijijini lakini tena anakutana na hili.



************

ITAENDELEA!!!
 

Post a Comment

0 Comments