Header Ads Widget

Responsive Advertisement

LIDAKE TENA CHOZI LANGU - 3

Image result for MY TEARS

Simulizi : Lidake Tena Chozi Langu
Sehemu Ya Tatu (3)

MACHO yangu yalikuja kufunguka tena nikiwa gizani. Sikujua ni wapi nilipokuwa lakini nilikuwa nipo juu ya kitu fulani. Na nilikuwa nayumbayumba huku na kule. Nikatulia bila kufanya papara zozote, akili ikanijia vyema kuwa nilikuwa katika mgongo wa mtu.
Huyu ni nani tena!!! Nilijiuliza huku mapigo yangu ya moyo yakipiga kwa kasi sana.
Nikiwa katika utulivu uleule nilimsikia mtu yule akimuomba Mungu afanikiwe kufika salama aendapo.
Sasa anaenda wapi huyu huku akiwa amenibeba..
“Unanipeleka kuniua?” nikamuuliza nikiuvunja ukimya katika namna ile.
Badala ya kushtuka yule mtu aligeuka akanitua chini kisha akanisihi tupige magoti tumshukuru Mungu kwa dua fupi.
“Nini kinatokea ndugu sielewi hata kidogo?” nilimuuliza.
Akatabasamu kisha akaniambia kuwa ameniiba kutoka mikono ya watu wabaya ambao waliambizana kunichukua kisha kuniua kwa sababu nilikuwa ninaleta mikosi katika ardhi ile. Kabla sijaulizia kuhusu wale wazee akanieleza kuwa wasamaria walionisaidia kwa mara ya kwanza walipewa onyo huku kijiji kikiahidi kuwatenga ikiwa wataendelea kunitunza.
Nilijiinamia na kujiuliza hii mikosi na vizingiti ninavyokumbana navyo ni matakwa yake Mungu ili niendelee kuuona utukufu wake ama ni kitu gani kinaendelea.
Yule bwana akadai kuwa yeye ameamua kunisaidia tu kwa sababu nafsi ilimtuma kufanya hivyo.
“Sasa huku tunaelekea wapi?” nilimuuliza. Akaniambia kuwa hana uhakika na tunapoelekea lakini ikiwa vyema nipate mahali mbali na kijiji kile nikae huko siku kadhaa kabla sijapata msaada wa kunirudisha nyumbani kwetu.
Sasa tukaendelea kutembea ulikuwa ni usiku mnene sana. Tulitembea tukiwa hatuna uelekeo rasmi. Kila tuliposikia kundi la watu ama vishindo yule bwana aliniambia nijifiche na yeye alikuwa akiendelea na safari zake akikutana na watu anawasalimia na wakiachana naye na mimi najitokeza tunaendelea na safari.
Nilimuuliza ikiwa ahofii majambazi maana usiku ule ndo nyakati zao. Alicheka kidogo kisha akasema kule kwao hakuna majambazi kwa sababu haukuwa muda wa mavuno baada ya kilimo.
Tulitembea sana hadi nikahisi kuwa siwezi kutembea zaidi. Akaomba anibebe lakini nikamgomea kwa sababu nilijua jinsi nilivyokuwa mzito na kwa mwendo ambao alikuwa amenibeba kabla sijarejewa na fahamu zangu. Nikamuomba tupumzike kidogo kisha tutaendelea. Akaketi kisha tukajilaza.
Usingizi ukanipitia, sijui nilisinzia kwa muda gani lakini nilikuja kushtuka mvua ikiwa imetanda angani muda wowote ule ingeweza kunyesha.
Nikamtikisa yule bwana naye akaamka. Kitu cha kwanza alishtushwa na lile anga.
Kabla hatujafikia muafaka wowote ule. Mvua ikaanza kushuka.
Ilikuwa ni mvua kubwa sana, ilinyesha huku miale ya radi ikiwaka huku na kule. Hali ikawa mbaya nikamsikia yule mtu akiniuliza katika namna ya mashaka.
“Wale wenzangu walisema wewe ama watu kama wewe ni ishara ya mikosi inaweza kuwa kweli? Mbona… mbona… mbona siielewi hii mvua sasa…..”
Alizungumza kwa sauti ya juu ili niweze kumsikia lakini sikuweza kusikia lolote.
Na hapo kipande cha mkono wangu uliosalia ukaanza kuuma, maji yaliyokuwa yananimwagikia yakalitonesha kovu!!
Wanasema maumivu ya jino sio mchezo lakini haya maumivu niliyokuwa nayapata katika kile kipande cha mkono wangu yalinifanya nilie kama mtoto.
“Mkono wangu unauma sana… nisaidie tafadhali nisaidie…” nilimsihi yule bwana huku nikimuonyesha mkono wangu ambao nisiuite mkono kwa sababu haukuwepo tena. Kilikuwa kipande tu cha mkono hakika nilikuwa naumia sana.
Yule bwana hakunijali tena kama ilivyokuwa awali, mashaka yalikuwa katika macho yake na mashaka yale yakamsababisha akimbie akiniacha katika mvua ile kubwa!!!
Nisingeweza kumkimbiza kwa sababu haikuwa lazima anisaidie, ama hata angeamua kunisaidia angenisaidiaje basi!!
Sina sababu hata moja ya kumlaumu ilimradi hakuonyesha dalili yoyote ya kunidhuru Mungu ambariki popote alipo akiisikiliza simulizi hii.
Maji yakaunda mkondo mkubwa hatimaye yakanizoa na mimi, zamani zile wala nisingeweza kushindwa kukata maji yale. Wakati nipo kidato cha sita nilikuwa bingwa wa kuogelea sana.,
Sasa sikuwa na mkono wangu mmoja nikagundua umuhimu wa kuwa na mikono. Nikawalaani wale walioukata mkono wangu kwa lugha zote nikavilaani na vizazi vyao vyote.
Niliteseka ndugu msikilizaji maji yalinitupa huku na kule, mara ile sehemu iliyokuwa inauma igongane na vitu vikali na kuamsha maumivu mapya.
Kwa kifupi nilikubaliana na wale waliosema kilio cha samaki machozi huenda na maji na asijulikane kama analia ama la!!
Nilikuwa nalia na machozi yalienda na maji. Kuogelea kwa mkono mmoja ilikuwa jambo gumu sana.
Na jaribio lile lilinishinda licha ya kupalangana sana.
Hatimaye mvua ilipungua na uhai bado ilikuwa ni mali yangu!!!
Sikuwa na nguvu kabisa, nilikuwa hoi sana.
Uchovu ule ukanifanya nipitiwe na usingizi palepale.
****
MAISHA YA PEKE YANGU!!
KITENDO cha kunusurika katika kadhia zile ambazo ziliniachia kumbukumbu mbaya kabisa kichwani mwangu sasa sikuweza kumuamini mtu yeyote yule badala yake nilijiamini mimi mwenyewe.
Maji yale yalinitupa huku na kule na pale nilipoibukia palikuwa ni makazi ya watu. Sikuhitaji msaada wa mtu yeyote yule niliamini kuwa ni Mungu tu anayenisababisha niendelee kuwa hai. Hivyo ni yeye ambaye atanionyesha njia.
Nikaamua kuishi maisha ya peke yangu!!
Wapi nitakula? Nini nitavaa? Wapi nitalala? Haya yalikuwa ni maswali ambayo sikuyapa kipaumbele kabisa.
Nilichotaka ni kuishi peke yangu hadi pale nitakapopata namna ya kurejea nyumbani kwa mama yangu kisha niuseme ukweli wote nilioushuhudia na jamii itambue ni kiasi gani watu tulio na ulemavu wa ngozi tunavyoishi kimashaka.
Nikiwa nawaza juu ya nitaishi vipi nikajiuliza pia juu ya miili ya wale wenzangu. Sijui kama ilizikwa upya ama iliendelea kufukiwa mithiri ya mizoga.
Palikucha nikiwa namuogopa kila mtu, bado sikuwa nja uhakika wa moja kwa moja ni mahali gani pale nilikuwa lakini baada ya muda nikatambua kuwa nilikuwa bado nipo kanda ya ziwa!!
Na mji ule niliokuwepo nilikuwa naufahamu vizuri kabisa.
Niliwahi kufika mji ule kwa sababu nilikuwa na marafiki waliokuwa wakiishi kule.
Lakini muda ulikuwa umepita sasa halafu si ni hawahawa marafiki walionipigia simu na kunieleza kuwa kuna kazi ya ualimu.
Marafiki hawahawa waliniunganisha na wauaji ili niuwawe kwa kukatwa viungo vyangu!!
Swali nililojiuliza na kubaki katika sintofahamu lilikuwa je? Ni kweli hawa marafiki walitambua kuwa wale ni watu wabaya?
Nani angenijibu!!! Hakuwepo.
Nikafikiria kucheza pata potea lakini nikajipa tahadhari kuwa natakiwa kuwa makini sana na sitakiwi kumuamini mtu yeyote yule.
Nikaamua kuzifanya harakati hizi kimyakimya!!
Nikafikiria wa kuanza naye wazo jema likawa ni kwa mwanafunzi mwenzangu ambaye nilikuwa nalala naye chumba kimoja enzi zile.
Lakini nilipanga kuwa hadi nihakikishe kuwa sijaweza kupata njia nyingine kabisa mbadala hiyo ndo itakuwa mbinu ya mwisho.
Maisha ya siku ile yakaanza, ama kweli ukiwa na matatizo siku inakuwa fupi sana ama wakati mwingine inakuwa ndefu sana.
Kwangu mimi usiku uliwahi sana kuingia, nilikuwa nimejiweka mbali kabisa na macho ya watu. Nilikuwa siruhusu mtu kunitambua mimi ni nani maana hakuwepo wa kumuamini.
Yaani hadi viongozi wa dini walipita na sikujisumbua kuwakimbilia maana hata wao ni wanadamu tu wangeweza kunisaliti kisha nirejee katika mikono ileile mibaya na huenda safari hii nisingeweza kuchomoka.
Majira ya saa moja hivi kimakadirio na lile giza njaa ilikuwa imenishika na kile kiubaridi cha jioni kikaingia na ukimya nao ukatawala.
Na hapo hofu ikaniingia tena.
Hofu haikuwa juu ya viumbe wakali lakini hofu yangu ilikuwa juu ya wanadamu wenye roho mbaya kabisa.
Masaa yalizidi kwenda miguu ikaanza kuishiwa nguvu na kisha likajirudia lile tatizo la kuumia mkono ule uliokatika.
Mkono ulianza kuuma sana, nikajiona kuwa hii ya sasa imekuwa mbaya zaidi natakiwa kupata msaada wa haraka.
Nilikuwa nafahamu hospitali ilipokuwa hivyo nilijikongoja kutoka katika giza lile nikiwa natokwa machozi kutokana na uchungu. Nikaamua liwalo na liwe.
Nikiwa napiga hatua zile mara nikaisikia sauti nyuma yangu.
“SIMAMA HAPOHAPO!!” ilikuwa sauti ya kiume.
Moyo ukapiga paaa!!!!
JIFUNZE:
USIKATE TAMAA, USIKATISHWE TAMAA na kamwe USIMKATISHE MTU TAMAA.
Haya maisha ayajuaye ni Mungu tu yeye ndiye atupangiaye jinsi gani tuishi!!!
Unapitia mapito mengi, unahisi umelaaniwa la!! Haujalaaniwa.
Simama tena jaribu zaidi na zaidi utafika tu unapohitaji!!!
Ukiona haufiki basi haujapangiwa hilo jaribu jingine!!
**********

Akili ikanituma kuwa kuendelea kwangu kusimama ningeweza kujizulia balaa jingine kutoka kwa hao watu ama mtu aliyekuwa akiniamuru kusimama.
Nikataka kukimbia lakini nikatambua kuwa kukimbia kwangu pia ni kulikuza tatizo.
Upesi nikageuka na kutazama mahali sauti ilipokuwa ikitokea!!
Pasi na shaka mtu yule hakutegemea mimi kugeuka ghafla kiasi kile. Hapohapo akanimulika na tochi yake usoni na mimi palepale nikafanya kitendo ambacho sijui akili ipi iliamuru kifanyike.
Nikaachama mdomo wangu kisha nikaanza kumfuata aisee yule bwana alipiga yowe huku anatimua mbio.
Sijui alikuwa ni mtu wa ulinzi shirikishi ama kijana tu kama vijana wengine wanaopenda kupiga mkwara wenzao na kujifanya wababe.
Sikupoteza muda maumivu ya mkono bado yalikuwa kwa kiasi kikubwa.
Niliondoka pale safari hii nikitembea haraka haraka zaidi hadi nikaingia barabarani.
Nikakata kulia huku maumivu makali yakiendelea kunitafuna.
Hatimaye nikafika hospitali nikiwa sina hata shilingi kumi mfukoni na mbaya zaidi nilikuwa nina njaa na nilikuwa nimechafuka.
Nilifika hadi chumba cha daktari, hakuwepo!!
Nikawasihi sana manesi wanisaidie wakampigia simu daktari.
Daktari akagoma kuwa hawezi kuja tayari yupo na familia yake nyumbani akawaelekeza manesi wanichome sindano fulani kisha siku inayofuata ndiyo nije kwa ajili ya huduma.
Manesi wakafuata maelekezo ya daktari na kunichoma sindano.
Hapo sasa kikazuka kizaazaa kumbe sindano ile inatakiwa mgonjwa awe ameshiba kabisa kabla ya kuchomwa sasa mimi nilikuwa nina njaa kali na sijatia chochote mdomoni tangu asubuhi.
Mwili ukaishiwa nguvu nikakumbwa na kizunguzungu na kuanguka chini. Manesi wakaanza kuhaha huku na kule kutafuta namna ya kuniokoa na lolote baya ambalo lilikuwa linaenda kutokea.
walimpigia simu daktari na baada ya kukata simu upesi wakaniletea chakula na kunisihi nile kwa wingi.
Kwa njaa niliyokuwanayo hawakuwa na haja ya kunisihi!!
Afadhali hata walifanya makosa!!
Nikapata kitanda cha kulala nikapata na chakula cha kutosha pia nikashushia na maji mengi ya kunywa!!!
Asubuhi daktari alifika na kunitembelea!!
Nilipigwa na butwaa kubwa sana, daktari alikuwa ni mwalimu wangu wa baiolojia wakati nikiwa kidato cha nne!!
Yeye hakunitambua upesi lakini mara moja nilimtambua.
“Sir. George!!” nilimuita. Akageuka upesi sana.
Na tulipogonganisha macho alinitambua… aliingiwa na upweke mkubwa sana ghafla!!
“Majaliwa… wameukata mkono wako mwanangu…. Wameukata mkono wako watu wabaya!!!” hakuweza kuendelea kuzungumza alianza kutokwa na machozi akafika pale na kupiga goti.
“Ni kwanini wanathubutu kuwaua, ni kwanini na ni nani aliyeileta imani hii mbaya kabisa ya kishirikina!! Nilikutafuta sana Majaliwa, nilikutafuta hadi ikafikia hatua nikahisi huenda na wewe wamekuua. Najua hii sio ajali hebu niambie ni kitu gani kilikutokea?” aliendelea kuzungumza. Sasa na mimi nilikuwa nimekaa kitako.
Nilitamani kuzungumza lakini kuna kitu kama funda lilikuwa limekaba koo langu.
Ili funda lile litokea sikuwa na budi kulia kwanza!!
Niliyaachia machozi yakatoka na mimi nikiwa nalia sana. Daktari aliniacha nilie bila shaka alijua kuwa ile ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuyapooza machungu yangu!!!
Baada ya kilio kile nilimueleza daktari kwa ufupi kilichonitokea mimi na rafiki zangu na kisha nikamuelezea safari yangu hadi kufika katika mji ule.
Daktari alinitia moyo sana akanieleza kuwa baada ya juma moja ana safari ya kwenda Dar es salaam hivyo tutaondoka wote na kisha ataniacha Dodoma ambapo ndipo nilikuwa naishi na mama yangu. Mama ambaye sikujua hata alikuwa na hali gani.
Lakini kwa juma hilo zima la kusubiri nitaishi nyumbani kwake. Nyumba ambayo anaishi na mkewe pamoja na watoto wao wawili na mfanyakazi wa ndani.
Ndugu msikilizaji niliusikia moyo wangu ukipata nafuu kubwa hakika licha ya kujipa moyo kuwa nitayaweza maisha ya kuishi bila kumwamini mtu lakini hapa nilijikuta nikimuamini tena daktari.
Kwa mara ya kwanza kidonda changu baada ya kukatwa mkono kilisafishwa kwa uangalizi mkubwa sana na jioni ya siku hiyo niliondoka na daktari hadi nyumbani kwake ambapo nilipokelewa vyema na familia kwa ujumla akanitambulisha kwa ufupi kisha akanikabidhi kwa kijana akanionyesha chumba cha kulala.
Nikaanza maisha mapyya!!!
Kesho yake wakati anaenda kazini aliniitan na kunisihi sana.
“Majaliwa hakuna sehemu salama hata moja, hili geti lisikupe ujasiri wa kujiona kuwa upo salama hata kidogo endelea kuishi kwa tahadhari kubwa hadi siku ambayo tutaondoka sawa!!” alimaliza akaondoka.
Maneno yale huenda pia alizungumza na mkewe kwa sababu mama yule hakuwa akinitafutia sababu za kukaa nje hovyo, kila kitu kilikuwa ndani kwa ndani.
Siku nne zikakatika nikiwa ninayo amani ya nafsi kabisa. Siku ya tano nikiwa pale nyumbani nilimuomba mke wa daktari simu ili niweze kuzungumza na mama yangu nyumbani namba yake bado ilikuwa katika kichwa changu.
Ikawa bahati mbaya mama yule hakuwa na salio katika simu yake, na wafanyakazi wote wawili hawakuwepo alikuwa amewaagiza.
Nikamwomba niende mimi ye anielekeze tu duka lilipo. Akapinga vikali akidai kuwa nisubiri tu atatafuta mtu wa kumuagiza.
Sikuona hiyo kama ni sawa nikamsisitiza na hatimaye akaniagiza nikaendsa kununua vocha.
Kitendo cha dakika tano tu nilikuwa nimeenda na kurejea.
Sitaki kuamini hata kidogo eti kuna mtu ambaye alikuwa amekaa kuwinda pale ili anione. Siamini hata kidogo lakini moyo wa mwanadamu ni kichaka!!!
Kweli namba ya mama ilikuwa inapatikana, alifurahi sana kunisikia na wala sikumgusia lolote baya lililonitokea. Akaniuliza kazi inaendeleaje nikamwambia inaendelea vizuri ndo kwanza tunaanza.
Siku ya tano ikapita.
Tukaingia siku ya sita na hatimayer siku ya saba ambayo ndo ilikuwa siku yangu ya mwisho pale. Nilikuwa nimejiandaa nikimsubiri daktari ambaye alinieleza kuwa alikuwa anapita ofisini kumuhudumia mteja mmoja kisha baada ya hapo atanipitia na gari yake binafsi tuondoke.
Majira ya saa nne hivi nilisikia kelele na kisha pakawa kimya nikajiuliza ni kweli nimesikia kelele ama ni masikio yangu. Nikaendelea na shughuli zangu!!
Lakini ni kama nafsi ilinilazimisha kuamini kuwa kuna kelele nilizisikia lakini zikakoma ghafla.
Nikaufungua mlango wa chumba changu na kutoka nje.
Nikafika hadi sebuleni hapakuwa na bughudha yoyote ile.
Mara nikasikia kelele za mwanaume akisisitiza kuwa ameniona.
“Yule pale yulee…”nilisikia akisema.
Ama hakika nilipagawa yaani hadi katika nyumba ile walikuwa wamenifuata.
Nilijaribu kukimbia lakini hapakuwa na sehemu zaidi ya chumbani kwangu.
Nikajifungia huko.
Kimya kikatanda lakini baada ya dakika kadhaa nikasikia watu mbele ya chumba changu.
“Majaliwa fungua mlango wananiua usipofungua!!” ilikuwa sauti ya mama yule mpole kabisa mke wa daktari.
Nikatambua kuwa hata nisipoufungua mlango bado watauvunja na kuingia. Japokuwa nafsi ilijitabiria mabaya lakini ningekuwa mkosefu wa shukrani ikiwa nisingekisikia kilio cha yule mama.
Nikaamua kujitosa, nikaufungua mlango mara wakanivamia na nilichokiona ni kisu kikubwa kikinijia maeneo ya usoni na mara haikuwa usoni tena.
Sikio langu likafyekwa na mimi nikaanguka palepale na kuziacha fahamu zangu!!!


********************************

Sijui nilipoteza fahamu kwa muda gani lakini nilikuja kujitambua na kumuona daktari yule akitapatapa huku na kule, nikajiuliza inakuwa vipi anakosa msaada. Macho yangu yalipoangaza vizuri nilimuona mkewe sakafanu akiwa anavuja damu. Nilitamani kuzungumza lakini koo langu lilikuwa kavu sana.
Nikajaribu kunyanyuka sikuweza mwili haukuwa na nugu kabisa. Nilimuona daktari kama akiniambia vitu fulani lakini sikuweza kumsikia kabisa ni kama alikuwa akiichezesha tu midomo yake.
Nikajiuliza ni kitu gani kinaendelea sasa katika eneo hilo. Na hapo nikajaribu kujishikiza vyema na mkono wangu yaani uwe kama muhimili.
Nilipojaribu kwa mkono wangu ule wa kulia ambao hadi napoteza fahamu ulikuwa eneo lake nilishangaa kuhisi maumivu, na hapo nikaikaza shingo yangu kutazama ni kitu gani kilikuwa kinatokea hadi napatwa na maumivu makali kiasi kile!!
La haula!! Sikuamini kitu ambacho macho yangu yote mawili yalishuhudia.
Mkono wangu wa kuume haukuwepo eneo lake, tofauti na mkono wa kushoto ambao ulikuwa umekatwa nusu na kubakizwa nusu. Huu wa kuume sijui kama ulikatwa yaani huu ulinyofolewa kama mnavyoona nyinyi mliopata nafasi ya kuniona nikiwa nayasimulia haya.
Nilisikia tumbo langu likiunguruma vibaya sana kisha likaanza kukata sana na hapo nikawa natetemeka.
Nikafumba macho na kuiona sura ya mama yangu, nikajijengea picha nilivyokuwa mtoto mdogo, alininyonyesha, aliniogesha na kunilisha chakula. Naam! Kwa wakati ule aliyafurahia haya kwa sababu alikuwa mama na mwana wake ampendaye.
Baada ya hapo akanifundisha kutembea, akanifundisha kula mwenyewe na hatimaye akaniachisha titi akimaanisha kuwa natakiwa kuanza kujitegemea.
Nilipoanza kujitegemea katika kula na kujisafisha nikawa nimempunguzia mama kazi hii.
Miaka inakatika mbele, napoteza mkono wangu mmoja nakaza moyo na kujifariji kuwa nitaweza kufanya shughuli nyingi tu nikiwa na mkono wangu mmoja tena bahati iliyoje mkono waliouacha ulikuwa mkono wa kuume.
Wakati ule ujasiri niliojipa ukiwa haujanikaa vyema katika damu yangu eti mkono wangu wa kulia umechomolewa. Yaani ….. yaani sina mikono yote miwili.
Jiulize hata ungekuwa wewe, jiulize unayenisikiliza. Ni roho ngumu kiasi gani wameumbiwa watu hawa wanaodiriki kutenda madhambi haya.
Nilikata tamaa!! Nilikata tamaa kabisa msikilizaji.
Nikisema lidake tena chozi langu namaanisha kuwa nimechoka, maalbino wenzangu wamechoka, wamekata tamaa wanaishi kwa mashaka. Hebu wewe ambaye kidogo unayo amani kwa sababu tu ya ngozi yako kuwa nyeusi. Ulidake tena chozi langu!!
Tunajiona tusiokuwa na thamani hata kidogo, tunajiona tupotupo tu kama vile nchi hii tulizaliwa kimakosa.
(Anavuta pumzi kidogo na kuishusha)… (kisha anazungumza kinyonge)…
Ilikuwa ngumu sana kuyaanza na kuyazoea maisha bila mikono yote miwili.
Yaani nirudishwe nyumbani kwa mama Majaliwa, aanze kuniogesha na kunibadili nguo, aanze kunilisha, dah!! Moyo wangu uliuma sana kiasi kwamba nikahisi unavuja damu tena damu nyingi sana.
Sikuamka kutoka pale chini nilibaki kumtazama daktari akihangaika sijui kama alikuwa anapiga simu ama vipi.
Ile kumtazama daktari akiwa anaweka simu sikioni kumbukumbu zikarejea upesi kuwa wakati naufungua mlango ili wale watu wabaya wasimjeruhi mke wa daktari kuna mmoja alinyoosha kisu chake kunielekea.
Naam! Nikajikuta nafanya tabasamu hafifu na hapo machozi yakaanza kunibubujika, nilikumbuka kuwa sikio langu lilifyekwa na watu wale wabaya.
Sikuwa na sikio langu moja!!
Nikiwa palepale chini nikamuuliza Mungu ni kwanini basi haichukui roho yangu ili mama yangu asishuhudie mwili wa mwanae ukiwa na uhai ukiwa katika mateso haya.
Lakini Mungu hapangiwi nini afanye na kipi asifanye nilijaribu kuziba pumzi zangu eti niweze kufa lakini nikajikuta naziachia mwenyewe kila mara.
Ni hapo nikatambua kuwa yawezekana Mungu ananiweka ili niendelee kuwa shuhuda, labda aliniacha hai ili wale watu wasiokuwa na imani kuwa Albino huteseka sana kwa sababu tu ya ngozi yao waweze hatimaye kuamini na kisha kuchukua hatua ya mabadiliko.
Labda Mungu aliniacha hai huenda mkiisikia sauti yangu hii mtaingiwa na huruma enyi wenye mawazo mabaya kuhusiana na sisi walemavu wa ngozi. Sijui kwanini nilibaki hai tu!!
Baadaye waliingia watu kadhaa mle ndani wakiwa na nguo nyeupe wakambeba mke wa daktari kisha wakanibeba na mimi.
Niliwatambua baadhi kwani niliwahi kuwaona katika hospitali ambayo daktari yule alikuwa akifanya kazi.
Nilifikishwa hospitali na kuchomwa sindano baada ya hapo nikahisi usingizi mkali sana ambao sikuweza kukabiliana nao nikaingia katika lindi kubwa la giza.
Nilipokuja kurejewa na fahamu haikuwa ndoto ulikuwa ukweli mtu sasa ile mikono yangu miwili niliyozaliwa nayo haikuwepo tena. Waliikata wanadamu!!
Kinachoniuma hadi leo hii ndugu msikilizaji, nisikilize kwa makini tena kinachoniuma hadi leo hii ninapokusimulia haya. Matokeo ya kidato cha sita yalikuwa yametoka na nilikuwa nimechaguliwa kujiunga na chuo kikuu cha Dodoma. Wakati mimi nasoma tulikuwa tunachaguliwa vyuo vya kwenda.
Yaani albino mimi nimechaguliwa kujiunga na chuo kikuu lakini ningesoma vipi wakati sina mikono tena mikono yote miwili na chuo hakina sehemu maalumu kwa ajili ya watu wasiokuwa na mikono.
Basi baada ya kujihakikishia kuwa sikuwa na mikono niliweza kunyanyuka kwa mara ya kwanza.
aaaH! Jamani mateso gani haya, nikatambua kuwa siwezi kutembea vizuri, nikajiuliza kwanini nikaambiwa kuwa dole gumba langu la mguu wa kulia liliongolewa na wale watu na laiti kama asingekuwa mke wa daktari kujitolea kwa hali yoyote ile kunipigania basi huenda kiganja changu chote kingekuwa kimeondolewa.
Kwanini haya yote yanikumbe mimi tu, mikono, kidole cha mguu, sikio langu!! Waliniachia pumzi tu!!
Niliendelea kujifunza kutembea pasi na dole gumba mguuni huku nikiendelea kujizoesha kusikia kwa kutumia sikio moja.
Najiuliza mpaka sasa, hivi asingekuwa yule daktari si ningekufa Majaliwa mimi. Nani angeweza kulipia gharama zote zile ilimradi niweze kupona. Mtu ambaye tumekutana ukubwani tu baada ya kuchana enzi hizo za shuleni.
Baada ya juma moja la kuwa pale hospitalini kila mara wataalamu wa saikolojia wakinitembelea na kunitia moyo. Niliruhusiwa kwenda nyumbani.
Nilipofika nyumbani nikiwa pamoja na yule daktari, alituita kikao cha familia.
Mkewe ambaye alicharangwa usoni bado alikuwa na bandeji hapa na pale na mimi nikiwa na bandeji mikononi, sikioni na mguuni.
Daktari alitueleza kuwa amepata fununu juu ya vijana kadhaa ambao wameonekana wakiwa na viungo vya albino hapo mjini. Daktari akaapa kuwa hawezi kamwe kuwaacha wale watu hivihivi badala yake atalivalia hilo jambo njuga ili ukweli ujulikane na haki pia iweze kupatikana.
Mkewe alijaribu kumsihi kuwa yale mambo amuachie Mungu lakini daktari alikuwa na hasira sana na alikuwa hashauriki.
Ile hali ya daktari ilinishangaza yaani yaliyonikuta mimi yalikuwa yameusurubu moyo wake sana.
Laiti kama wangepatiakana wanadamu kumi kama hawa kila mkoa ama kila wilaya nchini Tanzania wanaoguswa na matatizo yanayotukumba basi amani ingetawala sana na huenda yote hayua yangebakia kuwa stori tu kwa kizazi na kizazi.
Niliendelea kujiuguza majeraha yangu kwa majuma mawili zaidi.
Kikao kingine kikaitishwa!!
Daktari yule mkimya akatupa taarifa ya upelelezi wake wa chinichini kuwa kuna bwana mmoja taajiri ambaye anatarajia kuwania uongozi wilayani hapo alikuwa anahusika na baadhi ya mauaji ambayo yamewahi kutokea wilayani hapo. Anafanya hivyo kutokana na imani za kishirikina kuwa ataimarika kisiasa na kuwabwaga wenzake katika uchaguzi ambao ulitarajiwa kufanyia mwaka mmoja baadaye.
Maelezo ya daktari yalifanya ukimya mkubwa katika nyumba ile.
Nafsi yangu ilipondeka sana yaani mambo ya kiduniani yanamsababisha mwanadamu kuuondoa uhai wa mwanadamu mwenzake!!
Amakweli dunia tambala bovu!!
Usiku ule ukapita, nadhani daktari alifanya kosa kubwa sana ambalo hata mimi sikujua kama ni kosa.
Alisahau kumkanya mkewe kuwqa habari zile asizifikishe popote pale kwa sababu ushahidi bado haujakamilika.
Dah! Wanawakeee!! Wanawake…. Acha waitwe wanawake!!!
JIFUNZE!
DUNIANI hakuna siri ya watu wawili lakini kamwe huwezi kudumu na kila aina ya siri kuna baadhi ya siri unalazimika tu kuwashirikisha watu ama mtu. Kosa ni pale unapomshirikisha mtu asiyekuwa sahihi…
Utamfahamu vipi sasa mtu aliye sahihi….
Swali gumu kabisa jibu unalo wewe!!!
mtu sahihi ni wewe mwenyewe!!


ITAENDELEA................

Post a Comment

0 Comments