Ukaribu wa ushemeji unaweza kusababisha haya? Hapana. Alijipatia jibu. “Daktari, Guda amefanya nini?” Naomi alimuuliza Lilian aliyekuwa bado katika mshangao. “Umesema ni mume wako eeeh.” Alijaribu kujirejesha katika hali ya kawaida. “Ndio daktari ni mume wangu, anakaribia mwezi hayupo nyumbani sasa. Amepotea katika mazingira ya kutatanisha” Alikuwa ametaharuki Naomi wakati anazungumza haya.. Hili nalo likawa jipya katika kichwa cha Lilian. Mume ana mwezi mzima haonekani nyumbani, hakuna taarifa. Shemeji mtu anapatwa na maluweluwe juu yake. Maajabu haya. Ina maana shemeji ana mawasiliano na mume aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha. Mwezi mzima. Kazi mpya kabisa.
**** “Naomi…tutazungumza siku na masaa mengine, kwa sasa tumtazame mgonjwa….halafu nina wagonjwa wengine wengine, tutakaa tuzungumze juu ya hili.” Lilian alikatisha mazungumzo yale. Naomi hakuridhika lakini hakuweza kumpinga Lilian ambaye aliweka kigezo cha kuwa na msururu wa wagonjwa. Lilian akaondoka zake akiwa na mzigo mwingine mpya kichwani. Mtihani haswaa.
Lilian hakuwa na msururu wowote wa wagonjwa uliokuwa ukimngoja mahali popote. Aliondoka zake na kujihifadhi katika hoteli ambayo huwa anafikia mara kwa mara akiwa katika jiji hilo. Chumba kilikuwa cha wastani lakini kikaonekana kuwa kidogo sana. Kila kona ilibanwa na mawazo lukuki yaliyokuwa yanamkabili. Lilian alikuwa akimuwazia Naomi. Hakika alikuwa katika wakati mgumu, hali ya mume mpenzi kupotea katika mazingira ya kutatanisha hakika ilikuwa inasikitisha, Daktari huyu alitambua kabisa hali hii kutokana na utaalamu wake wa saikolojia. Lakini angefanya nini?alitamani sana kuketi pamoja na Naomi aweze kuzungumza naye hatua kwa hatua juu ya jambo hilo. Lakini halikuwa jambo dogo, palikuwa na sintofahamu aliyoidhania kutoka kwa ndugu hawa. Hatimaye akafikia maamuzi, safari hii akafikia maamuzi ya kurejea jijini Mbeya, nia kuu ikiwa kuonana na Walter aweze kutambua iwapo ana dalili ya kumpenda ama aliielewa vibaya ‘meseji’ yake.
Siku iliyofuata akapanda basi na kuondoka bila kumuaga Naomi na Suzi.
**** Majira ya saa nne usiku Naomi alikuwa ameketi katika sebule pana, akijaribu kupitia mahesabu ya hapa na pale aliyoletewa na wapambe wa Walter ambao alikuwa amewakabidhi majukumu kadhaa yaliyoachwa na mumewe waweze kuyasimamia. Jukumu mojawapo lilikuwa ni ukumbi mkubwa wa muziki maeneo ya Kinondoni. Naomi alijikita vyema katika mahesabu yale hatua kwa hatua hadi akayamaliza. Alipofikia mahali pa kuweka sahihi, akakutana na jina la Walter. Akalitazama kana kwamba anatazamana na Walter kisha kwa unyonge akaweka sahihi. Akafunika makaratasi yale akaingia chumbani. Kabla ya kulala akaichukua simu yake akabofya namba kadhaa. “Nambie sista unaendeleaje?” Naomi aliuliza. Alikuwa amempigia simu Suzi. “Naendelea vizuri Naomi, asante kwa kunijali. Lakini jambo moja tu linanitatiza ujue.” “Nini tena mpenzi.” “Shem Guda, ujue unavyonambia hajulikani alipo nabaki kushangaa hadi leo. Kivipi sasa hili jambo linaisha, au wewe umeamua kukubali kuwa hayupo na ibaki kuwa hivyo?” Suzi akatoa kauli nzito. Naomi akashusha pumzi kwa nguvu. Kisha akazungumza, “Da Suzi, hebu ngoja nakupigia…” Hakusubiri kusikia Suzi atajibu nini. Huku akiwa ametaharuki alibofya namba kadhaa bila kujali lolote kuhusu muda ama ni nini atakuwa anafanya huyo mpigiwa. Simu ikaita takribani mara nne, ikapokelewa. “Naomi…mbona usiku.” Swali la kwanza kutoka kwa mpokeaji. “Dokta…naomba unisamehe sana kwa usumbufu lakini tafadhali naomba kidogo unisikilize,” Naomi alisita kisha akaenndelea “ Dokta, natamani ungeingia katika moyo wangu huu mdogo usioweza kuhimili machungu haya, natamani sana ujue kuwa ni kwa kiasi gani ninasulubika na jeraha baya. Jeraha la hisia, tazama pete hii kidoleni, inanisuta kila kukicha. Mimi ni mke wa mtu, niliolewa kwa ndoa halali, lakini hadi sasa sijui kama mume wangu ni mzima ama amekufa. Tafadhali Dokta kama kuna lolote una fahamu kuhusia na na Walter tafadhali nambie, kama amekufa basi nianze kuishi kama mjane nikitambua kuwa sina mume, kama ni mzima mume wangu na unafahamu mahali alipo tafadhali nifikishie ujumbe kuwa ninampenda, najuta kwa kumkosea kipindi chote hicho, mwambie mimi ni Naomi mpya, Naomi wa tofauti kabisa….mwambie natubu. Siwezi kuishi bila yeye, mimi ni bure tu pasipo yeye. Mkumbushe pia kiapo alichowahi kutoa kwangu. Dokta nazungumza haya, machozi yakimwagika, chozi hili halinitoki bure, nalia nikijuta. Dokta wewe ni mwanamke mwenzangu nadhani unajua ni uchungu kiasi gani niliojibebea. Nampenda Walter kama unafahamu lolote daktari tafadhali nambie kwa faida ya afya ya Suzi na pia kwa uzima wangu…….” Mazungumzo yakakatika kikasikika kilio cha kwikwi kisha kilio kikubwa.
Lilian alikuwa amekaa kitako, alikuwa anakaribia kusimama bila kujua ni wapi anahitaji kwenda baada ya kusimama. Akakisikia kilio cha uchungu mkubwa. Lakini hakikuwa na maana, kikubwa kilichomfanya ajikute anataka kusimama na kulisikia jina Walter. “Walter ni nani?” hatimaye aliuliza. “Ni mume wangu dokta, Walter na Guda ni mtu mmoja…” alijibu huku analia kama mtoto mdogo. Mara simu ikakatwa. Naomi akajirusha kitandani na kuendelea kulia.
Lilian naye akajikuta amesimama wema akitetemeka. Alifanya ishara ya ombi kwa muumba wake ili kwa namna yoyote ile isijekuwa Walter anayezungumzwa na Naomi akawa Walter huyu anayeisumbua akili yake. Lilian akafikiria kumpigia Walter usiku huo huo, lakini akaona ni kumsumbua akaamua kumtumia ujumbe mfupi. “Nimerejea nipo nyumbani kama upo Mbeya njoo home kesho.” Ujumbe ukamfikia Walter.
Hayakuletwa majibu yoyote hadi Lilian alipoamka asubuhi na kukuta simu zisizopokelewa kutoka kwa Walter. Akampigia. “Mambo Lilian, najiandaa kuja huko, nilikumiss sana.” Walter alizungumza kwa furaha sana. Sauti yake tulivu ikamsulubu Lilian, hisia zikamkaa sawasawa. “Karibu.” Alijibu kwa kifupi Lilian. Alikuwa anathema juu juu
Baada ya kukata simu Lilian alifanya jambo la haraka, jambo ambalo hakuhitaji maamuzi mbadala. Hisia za mapenzi zilikuwa zinamuongoza. Akachukua glasi akamimina juisi ambayo aliinunua safarini, kisha upesi akauendea mkoba wake akarejea na kipakti kidogo cha unga unga akakifungua na kumimina kiasi kidogo katika ile juisi.
Baada ya nusu saa, Lilian alikuwa katika chumba chake ana kwa ana na Walter. Lilian alikuwa amebadilika, Walter aling’amua hilo punde baada ya kumtazama usoni. “Walter, samahani sana kwa kuondoka bila kuaga.” Alizungumza Lilin huku akimkabidhi Walter glasi ya juisi. “Usijali, nawe asante kwa kitabu, kimenifanya niwe nakuona kila siku, we nawe umemfahamu vipi huyo mwandishi?” alijibu Walter kisha akashushia na funda kubwa la juisi. Lilian akatabasamu bila kusema lolote. “Umenuna kweli leo.” Walter alitawala maongezi. “Wala sijanuna jamani…sema uchovu tu wa safari.” “Ehee mgonjwa anaendeleaje lakini.” “Kwa sasa ana unafuu.” Alijibu Lilian kisha akaongezea, “Walter samahani nahitaji kukuuliza kitu…” “Hata mimi nataka kukushirikisha kitu. Aanze nani sasa.” Aliingilia Walter. “Naanza mimi.” Alijichagua Lilian. Walter akamruhusu. “Hivi hilo nd’o jina lako Walter?” “Yeah naitwa Walter nilikwambia siku zile, kwa wazoefu wanaweza kuniita Dj.” Alijibu. “Jingine?” akahoji Lilian. “Mh…lipo jingine wengi hawalijui lakini, naitwa Guda…kwani vipi?” alijibu Walter. Moyo wa Lilian japo ulitegemea hali kama ile lakini ulifyatuka na kupiga kwa nguvu. Aliyekuwa mbele yake ni mume wa Naomi, Naomi ambaye alikuwa amemlilia usiku uliopita akimueleza kuwa anampenda sana Walter na hawezi kuishi bila yeye. Sasa huyu Walter nd’o huyu huyu ambaye yu katika hisia na hajiwezi bila yeye, na safari hii alikuwa amejiahidi kwa kila namna atahakikisha kuwa anampata kimapenzi na kumshikiria milele. “Vipi mbona kimya? Kuna tatizo?” Walter alihoji kwa utafiti. Lilian akaketi kitandani. Akajishika tama lake. “Lilian jamani kuna nini sasa.” Lilian kimya. “Lilian..” “Mhh” akaitika. “Umekuwaje jamani?” “Walter ulikuja Mbeya kufanya nini? Na mbona unaishi hotelini?” “Kuna watu wamekwambia mimi ni jambazi Lilian?” badala ya kujibu swali akajikuta anauliza swali. Lilian akafadhaika kumsikia Walter akiwaza mabaya juu yake. Akanyanyuka akamfikia Walte, akamshika mabega. Akamtazama usoni. Macho yao yakagongana. Ni hapa Lilian alipogundua kuwa hakuwa ana mbinu yoyote ya kujizuia dhidi ya penzi la Walter. Mapigo ya moyo yakawa yanashindana kupiga. Macho yakajikuta yanalegea, akamkumbatia Walter kwa nguvu. Walter naye akajibu mashambulizi. Wakawa kama mwili mmoja. Lilian akaihisi amani aliyokuwa anaipata miaka kadhaa nyuma enzi za marehemu dokta Mbaule ikirejea. Almanusura atumie janja ya mtoto wa kike kumtupia Walter kitandani, lakini akashambuliwa ghafla na wazo tata. Wazo hilo likapambwa na picha ya mgonjwa wa Ukimwi akiwa hoi kitandani. Mgonjwa huyu alikuwa ni Suzi, Suzi dada yake Naomi. Suzi huyu alikuwa na ujumbe mbaya sana, Suzi alikuwa na dalili zote za kuwahi kushiriki penzi na kijana huyu aliyemkumbatia. Mara ujumbe ule ukajiunda katika mfumo wa filamu, Lilian akamuona Suzi akiwa faragha na Walter, hakuweza kuelewa eneo lile ni wapi lakini aliamini palikuwa faragha, akamuona Walter akimshawishi kitu Suzi, Suzi akaanza kulia. Mara akasikia kama maneno yakimtoka Suzi. “Lakini nina Ukimwi mimi…” maneno haya hayakumwingia Walter ambaye mkono wake ulikuwa ukitambaa katika tumbo dogo la Suzi. Kilichofuata pale ni nguo moja baada ya nyingine kudondoka sakafuni kisha……kisha Walter akafanya zinaa na muathirika. Mawazo yale yakakomea pale. Lilian akajichomoa katika mikono ya Walter, akawa anamtazama kwa hofu kana kwamba anatazamana na kiumbe kinachotishia uhai wake. “Lili umekuwaje wewe?” Walter akamuuliza huku akiwa amepigwa butwaa. Majina yake aliyomtajia Lilian yalikuwa na madhara gani hasa. Walter hakupata jibu.
Lilian naye alikuwa katika mtihani, hisia za kimapenzi zilizidi kumtawala. Lakini likafuata swali. Je ashiriki mapenzi na mtu ambaye amefanya mapenzi na muathirika wa UKIMWI? Swali zito sana, swali ambalo laiti kama angeamua kufanya maamuzi, angejikuta aidha akiangukia kuukwaa Ukimwi kwa maksudi mazima kwa kuzisikiliza hisia zake. Lilian akajikuta akikosa la kufanya. Katika kukosa huko maamuzi, Lilian alisahau kuwa kuna kitu alimchanganyia Walter katika juisi. Alifanya hivyo ili Walter aweze kutii kiu yake kwa lazima. Katu binti huyu asingeweza kuzizuia tena hisia zake. Jeraha lilikuwa kubwa sana. Walter akaanza kubadilika, akajikuta katika hisia mbaya zinazotesa. Maungo katikati ya mapaja yake yakaanza kuongezeka kwa kasi. Walter alikuwa amenyweshwa dawa za kuongeza nguvu za kiume. Lilian akiwa anashangaa bado mara Walter alimfikia na kumkumbatia. Lilian akajaribu kujitoa. Bahati mbaya Walter alikuwa ni mtu wa mazoezi. Lilian hakuweza kufurukuta. Lilian akataka kupiga kelele lakini akahofia majirani watamfikiriaje. Akazidi kupambana na Walter. Baada ya sekunde kadhaa, ile nguo yake nyepesi iliyokuwa mwilini ikasalimia sakafu. Mara suruali ya Walter nayo ikajiunga na ile nguo. Hakika Walter alikuwa katika uhitaji. Na laiti kama Lilian angechomoka katika mikono yake, hakika yangekuwa mateso makali. Lilian akafanya jaribio la mwisho, akamng’ata Walter. Super shaft na meno wapi na wapi. Walter hakusikia chochote. Lilian alikuwa akipambana na jinamizi aliloamini lilikuwa na virusi vya UKIMWI.
Lilian alijaribu kumpiga piga vibao Walter katika mgongo wake lakini hiyo yote ilikuwa kazi bure. Hisia alizokuwanazo Walter hazikuzuilika hata kidogo. Walter akawa anazungumza lugha zisizoeleweka, mara amuite Lilian mpenzi wake mara amuite mke wake. Hali ilikuwa tete. Ghafla mikono imara ya Walter ikamnyanyua Lilian, kama kikaratasi akarushwa kitandani. Akaangika kifudifudi, alipojaribu kugeuka kutazama yu wapi Walter. Alikuwa amechelewa. Baada ya dakika kadhaa Lilian alikuwa chali na Walter alikuwa juu yake. Jasho lote lililomtoka Walter lilitiririka katika uso wa Lilian. Zoezi halikuwa dogo, Lilian alizidi kuchoka na bado dawa ilikuwa haijaisha mwilini mwa Walter. Shughuli ikamzidia, akanyoosha mikono kuomba msamaha, lakini Walter hakuelewa. Dawa ilikuwa imechachamaa na misuli ilikuwa imeimarika vyema. Pumzi zikazidi kukata, daktari huyu akakiri kuwa alikuwa katika hatari ya kupoteza uhai wake. Akajaribu kumfinya Walter kwa kucha zake fupi. Hii nayo ikawa sawa na kumtekenya. Mara akakumbuka kuwa Walter hakuwa amevaa kinga yoyote, akaukumbuka ugonjwa wa Ukimwi. Akajikuta anapiga kelele mara moja kisha akatulia tuli. Walter akabaki kujiridhisha peke yake. Lilian alikuwa amepoteza fahamu.
Walter hakuwa na akili zake timamu, aliongozwa na hisia, na hakuwa akifurahia lakini alifanya kwa bidii ili kujipooza maumivu makali katika maungo yake. Ilimchukua masaa matatu kurejea katika hali ya kawaida. Kitanda kilikuwa kina madoadoa mekundu ya damu. Lilian alikuwa ametulia tuli. Walter alikuwa dhaifu sana, hakika alikuwa amechoka. Alichoka kwa sababu alifanya tendo hilo kupita kiasi. Na hakufanya kwa kupenda bali kwa kushurutishwa na dawa zile za kuongeza nguvu za kiume. Maskini Walter akajihisi yu katika ndoto, ndoto ya mchana. Akajaribu kusimama wima huenda yu ndotoni lakini haikuwa hivyo. Alishindwa kusimama, hapo ndipo alipogundua kuwa alikuwa na kiu kikali, lakini mbaya zaidi alikuwa yu uchi wa mnyama. Akakumbwa na pigo la aibu, akahisi Lilian anamuona, akatazama nguo zake. Zilikuwa mbali. Walter akashuka kitandani na kujikongoja, alipojaribu kusimama wima, akakosa muhimili, akaanguka chini. Walter alikuwa amesafiri maili nyingi sana kwa muda mfupi bila yeye kujijua, sasa alikuwa taabani. Walter akaanza kutambaa huku akihema juu juu. Wakati anatambaa akahisi maumivu. Akajitahidi akapeleka mkono wake na kujishika katikati ya mapaja. Alipojitazama alijikuta na damu nyingi. Walter alikuwa amechubuka sana. Mchubuko uliosababishwa na msuguano mkali kwa muda mrefu. Walter akajikaza na kuzifikia nguo zake, akajizoazoa hadi miguu ikaingia katika suruali. Kisha akavaa shati lake hovyo. Akaanza kutembea kwa magoti, akalifikia gudulia lililokuwa na maji. Akachukua kata akazamisha katika ndoo, akaibuka na maji. Akayagida kwa fujo bila kujalisha yalikuwa salama au la. Maji ni tiba sahihi. Walter akausikia mwili wake ukipata afueni kidogo. Baada ya dakika kadhaa akasimama kwa kutetereka. Sasa akapata nafasi ya kumwona vyema Lilian akiwa yu uchi wa mnyama. Akitokwa damu sehemu za siri. Hofu ikamwandama. Sasa picha ikajijenga vyema katika ubongo wa Walter. Akakumbuka jinsi mchezo ulivyoanza. “Nilibakaaaa.” Akatokwa na neno hili? Hapa sasa akakosa subira. Hali ya hatari. Akaondoka kwa kunyata hatua moja baada ya nyingine, akakiacha chumba kile. Aibu ilikuwa imemshika. Iwapo Lilian akiamka watatazamana vipi? Akiwa katika kumfikiria Lilian mara jina jingine likamvamia ghafla, jina lile likaambatana na jicho lake kutua katika kidole chake. Akakutana na pete….Pete ya ndoa!! Akamkumbuka Naomi. Walter kwa mara ya kwanza tangu aingie katika mahusiano na Naomi alikuwa amezini nje ya ndoa. Mapigo ya moyo yakaanza kwenda kasi, ni kana kwamba ile pete ilikuwa imemchungulia na kumsuta kwa kitendo alichokuwa amefanya. Walter akakosa msimamo. Na hapo akajigundua kuwa licha ya kumpenda Naomi alikuwa anamuogopa pia. Kwa hatua za upesi upesi walter akatembea huku akizidi kupata nguvu, hadi akafika hotelini. Akachukua kibegi chake kidogo, akafanya malipo ya siku alizokaa pale. Kisha akaaga na kuondoka. Hakuwa tayari kuonana na Lilian, na alijua fika kwa kitendo cha kubaki katika hoteli ile alikuwa anakaribisha balaa jingine ambalo lingeweza kumuingiza katika mkono wa dola. Kesi ya ubakaji!!..... Walter hakuwa tayari kurejeshwa jijini Dar kwenda kusikiliza kesi ya ubakaji. Kwanza alikuwa hajawahi kuingia walau rumande hata siku moja. Leo hii asimame mahakamani kujibu kesi ya ubakaji?? Hapana!! Walter akatoweka.
****
Giza lilitanda, wale wazoefu wa mji waliwahi kufunga biashara zao na kurejea majumbani mwao. Giza hili lilikuwa na maana yake, halikuwa giza kama giza jingine. Hili lilikuwa limetiwa nakshi na wingu zito. Dalili tosha ya mvua. Badala ya mji kuwa na baridi, lilianza joto kali la aina yake. “Ifula jikutima lilino (Mvua itanyesha leo)” Wanawake wa kinyakyusa walinong’onezana huku wakianua biashara zao mapema. Hali ilikuwa tete.
Majira ya saa nne usiku, lile giza likaanza kutawanywa na radi za hapa na pale. Baada ya muda mvua ikaanza kushuka, joto likapotelea mbali baridi likachukua hatamu. Baridi kali sana.
Nyumba za waliotambua madhara ya mvua hiyo walifunga madirisha ipasavyo, cha kushangaza nyumba ya mtaalamu kabisa yenyewe haikufungwa madirisha. Maajabu sana. Daktari mzima hafungi madirisha…ilistaajabisha sana. Mvua ikaanza kunyesha hatimaye. Mvua kubwa. Madirisha yakajibamiza huku na huko kutokana na upepo. Hakuna aliyejali. Chumba kilikuwa tulivu kabisa. Mara upepo ukageuza uelekeo, sasa mvua ikaanza kuingia ndani, kitanda kikaanza kulowana. Mwanamke tulivu kabisa akaanza kurejewa na fahamu. Majimaji ya mvua kitandani yakakumbana na mwili. Dokta Suzi akajigeuza. Makelele ya madirisha kujibamiza yakairejesha akili yake katika ufahamu. Akafumbua macho akakumbana na giza nene. Akatuliza akili, akataka kukaa sawa akahisi amenatana katika godoro, akajaribu kujitoa akakumbana na maumivu makali. Lilian akapapasa huku na kule akakutana na kitufe cha kuwashia taa kilicho karibu na kitanda. Akabofya. Waaa!! Taa ikawaka. Akatazama, akakumbana na damu. “Walter…” akaanza kuita. Hakupata majibu. Ilikuwa hali ya hatari. Alikuwa anatetemeka, meno yalikuwa yanagongana kutokana na baridi. Aliita tena na tena lakini hakupata majibu. Walter hakuwepo. Akaliachanisha shuka lililomganda kutokana na ile damu nyingi. Akafanikiwa kutoka. Alipojaribu kuifikia sakafu akakumbana na maji yakamvuta mguu akateleza, akatulia mgongo. Miguu yake ikatanuka, jeraha katikati ya mapaja likawa limejitonesha upya. Uchungu mkubwa ukamshika. Akatokwa na yowe la hofu. Hakuwepo wa kumsaidia. Taaluma ya udaktari iliweza kumsaidia, japo wanasema mganga hajigangi, Lilian aliweza kulifikia koba lake akaibuka na dawa kadha wa kadha akameza na nyingine akajipaka katika makovu. Kilio kikamtoka, dawa ilikuwa kali haswa. Usingizi ukamkutia katika kochi la sebuleni. Akalala hapohapo.
**** Walter alikuwa kama kichaa, akili ilikuwa haijatulia kila mara alitembea huku akiangalia nyuma kana kwamba kuna mtu ambaye anamfuata kwa nyuma. Kibaya zaidi alikuwa ni mgeni kabisa katika jiji lile. Sasa alikuwa katika mitaa ya kwa ‘Mama John’ akizagaa bila kujua ni wapi anaelekea, mara akajikuta katika fujo za hapa na pale za mitaa changamfu ya Soweto jijini Mbeya. Bado hakuwa mtulivu. Kiza kilikuwa kimetanda na kila mtu alionekana kuwa na haraka sana. Hata yeye naye akajifanya kuwa na haraka vilevile. “Samahani kaka, stendi kuu ni wapi?” Walter alimuuliza kijana mmoja muuza karanga. Kijana yule akamtazama kwa muda kabla ya kumjibu. “Ukuti fhiki” kijana akajibu kikabila Walter akabaki kuduwaa hakuelewa kijana yule alimaanisha nini. Kijana akatokomea baada ya kumwona Walter akimshangaa. Hatimaye mvua ikaanza kumwagika. Walter akazidi kupagawa, alikuwa mpweke katika mji wa kigeni kabisa lakini katika ardhi ya Tanzania. Walter akajipekua na kugundua kuwa kuna kitu kikubwa sana anachokikosa. Alijikuta na pesa taslimu shilingi elfu ishirini, hizi zilisalia baada ya kulipa bili yake ya hoteli. Akili ikasimama, joto kali katika mvua. Walter hakuwa na kadi yake ya benki. “Nimeisahau nyumbani kwa Lilian” alisema kwa sauti ya juu. Joto likatoweka tena, ikafuata baridi kali, mwili chepechepe kwa kunyeshewa na mvua. Walter akapagawa. Alikuwa amepanga kwenda kituo cha mabasi aweze kuukimbia mji. Lakini sasa anagundua hawezi kutoka bila kuwa na kadi yake ya benki. KIZUNGUMKUTIII.
Walter akazizima kwa baridi, mianga ya radi ikamulika, ikawa kama bahati. Akaona maneno kadhaa. “UTULIVU LODGE” matumaini yakarejea upya, akakatisha katika matope bila kujali lolote akaifikia nyumba hiyo. Mlinzi akamuona akamfungulia geti. “Kuna vyumbaa.” Akapaza sauti kuu, akasikika. Mlinzi akajibu kwa sauti ya juu pia. Alimjibu kuwa hapakuwa na vyumba. Walter akafadhaika. “Angalia hapo mtaa wa pili.” Mlinzi akamshauri Walter. Walter akatoweka, akazidi kulowana. Akaifikia nyumba ya kulala wageni aliyoelekezwa. Hapa alifanikiwa kupata chumba. Akafanya malipo. Shilingi elfu kumi na tano. Akasaliwa na shilingi 5000 mfukoni. Akakivagaa chumba akavua nguo zake zilizolowana. Akajirusha kitandani na kujifunika shuka zito lililokuwa pale kitandani. Baridi kali ikaondoka na mawazo yake ya awali. Lakini yakajiunda mawazo mengine mazito. Mawazo haya yalichanganyikana na kumbukumbu nyingine mbaya. Kumbukumbu za vifo. Vifo vya wazazi wote wawili, babu na kisha dada yake mpenzi. Vifo hivi vikamkumbusha kiapo alichoapa mbele ya Frank na Muganyizi. Aliapa kamwe hatakanyaga ardhi ya Tanzania, aliapa hivyo kwa sababu ardhi hiyo haikuwa inamtendea haki. Kiapo hicho kikalegea baada ya maneno ya busara kutoka kwa Muganyizi, hatimaye Dj Walter akarejea Tanzania katika ardhi iliyomeza uhai wa baba, mama , bibi na dada mpenzi. Ile ardhi aliyoikataa hatimaye ikamkutanisha na Naomi. Msichana wa ndoto zake. Msichana aliyeishi naye na kumpenda tangu utotoni. Ndoa ikafungwa. Ndoa hii ya aina yake ikazua kizaazaa. Cha kumuhamisha Walter kutoka katika jiji la Dar es salaam na kuwa mkimbizi huru katika nchi yake. Akabadili namba za simu na kulikimbia jiji, katika kulikimbia akakutana na Lilian. Lilian akawa msaada mkubwa sana kwake kupitia vitabu vya riwaya, lakini sasa anajaribu kumkimbia Lilian maana anayo kesi ya kujibu. Amebaka!! Walter akamlaani mjomba wake (Muganyizi) kwa kumshawishi kurejea tena nchini Tanzania. Nchi ambayo sasa inampelekesha puta. Laiti kama asingekuwa Muganyizi, hakika nisingekuwa katika hali hii. Alijisemea Walter. Usingizi ukampitia bila kujua.
Asubuhi sana aliamka, nguo zilikuwa zimekauka. Akazitupia mwilini. Akaisikia njaa kali ikivuma tumboni. Akajilaza tena kitandani. Baadaye akatoka bila kukabidhi chumba. Akauendea mgahawa akajishibisha kabla ya kuamua jambo moja. Kuifuata kadi yake ili akutane na Lilia nana kwa ana ama achukue maamuzi mengine. Sasa alikuwa na shilingi elfu tatu tu mfukoni. Walter akaanza kutembea pembezoni mwa barabara akirejea kule alipotokea usiku uliofika, macho yake yalikuwa makini sana akimtazama kila mtu mapema ili atambue kama alikuwa anafuatiliwa ama la. Hatimaye akafika Ilomba. Akapinda kushoto na kuanza kunyata kwa tahadhari kubwa akielekea ilipo nyumba ya Lilian. Mapigo ya moyo yalikuwa juu sana. Kiubaridi kilipuliza, Walter alikuwa hajiamini hata kidogo. Akiwa katikati ya kundi la watu mara kikatokea kitu ambacho hakutaka kitokee, akajaribu kukibadilisha kuwa ndoto lakini haikuwa ndoto. Muda ulikuwa ni saa nne asubuhi na hakuwa kitandani bali barabarani.
****
Chai ya moto iliuchangamsha mwili wa Lilian. Alifanya tabasamu mara ya kwanza baada ya masaa kadhaa kupita. “Mh…jana palikuwa na shughuli aisee.” Alikiri huku akiyatazama mashuka ambayo alikuwa anayaloweka katika maji yenye sabuni ya unga. Baada ya zoezi hilo alirejea ndani, akapita mbele ya kile kioo chake, alikuwa na kanga moja. Akajaribu kutembea na kujitazama akagundua kuwa mwendo wa namna hiyo aliwahi kuutembea siku ambayo alitolewa usichana wake. Lilian akalazimisha tabasamu. Mara simu yake ya mkononi iliita. Akaisogelea na kuitazama, mpigaji alikuwa ni Suzi. Yule muathirika wa gonjwa hatari. Mwili ukamsisimka Lilian, akaipokea kwa hofu. Suzi akamsalimia kwa furaha. Naye akamjibu kwa shangwe ya kujilazimisha. “Eti daktari unafahamu Guda alipo jamani…..nimemkumbuka sana kwa kweli.” Sauti ya manung’uniko kutoka kwa Suzi. “Nitakupigia nahudumia mgonjwa.” Alidanganya Lilian akakata simu. Hapo zikarejea zile hisia za kuambukizwa gonjwa la Ukimwi baada ya kuzini na Walter ambaye kwa hisia zake binafsi aliamini kuwa Walter alikuwa katika mapenzi na Suzi. Lilian akaanza kutetemeka. Picha za wagonjwa wa Ukimwi wakikohoa na kujiharishia vitandani zikapangana kwa fujo, vilio vyao wakiwa katika hatua za mwisho za uhai wao nazo zikamwandama. Vidonda vinavyowatoka, mkanda wa jeshi unavyowashambulia. Lilian akajiona yu katika mkondo huohuo. Kama mtoto mdogo akaanza kulia. Alilia akizilaani hisia zake. Hisia mbovu kabisa za kimapenzi zilizompelekea kumwekea Walter dawa katika juisi na hatimaye wakazini. “Nimekinunua kifo changu mwenyewe….” Alijilaani Lilian huku akigalagala chini. Akarusha miguu huku na kule lakini haikusaidia. Akajigeuza huku na kule mara kanga ikauacha mwili akabaki kama alivyozaliwa. Ile aibu atakayoipata kwa kufa na gonjwa hili ikamtesa kwa dakika hizo. Alitia huruma kumtazama.
Akiwa katika hali hiyo, akamkumbuka Walter. Hakujua yu katika hali gani. Hatia ya kumtenda kijana huyu wa watu kisaikolojia ikamkumba, akakaa kitako. Akajiona hayupo sahihi kubaki kimya. Kilio cha Naomi nacho kikayakabili masikio yake na kuushambulia ubongo wake. Mwanamke analilia penzi la mume wake. Analia kwa kumkosa mwanandoa mwenzake. Lilian akakusudia kufanya mambo mawili. Kwanza amueleze Walter ni jinsi gani mke wake anampenda kwa dhati, na pili ajiue baada ya kumweleza kila kitu Walter kuhusu hisia zake na historia yake. Uamuzi huu ulikuwa sahihi kabisa. Lilian hakutaka kufa kwa mateso makali ya kuteseka kitandani, kuwapa shida ndugu zake wachache kuanza kumlea kama mtoto mdogo huku akiwaharishia na kuwatapikia hovyo. Kisha azikwe akiwa na kilo moja na nusu. Aibu kuu!! Daktari mzima nakufa hivi? Hapana. Nafsi ilikataa. Hisia mbovu za kupata unyanyapaa wa hali ya juu kutoka kwa wauguzi nao ukamsulubu. Hapo ndipo alipoguindua kuwa wale wagonjwa ambao huwakaba madaktari baada ya kupewa majibu kuwa wameathirika huwa wapo sawa kabisa na wanastahili kupagawa. Lilian alikuwa amepagawa haswaa. Mbaya zaidi alikuwa yu peke yake ndani. Akasimama wima akabadili nguo zake akatoka kwa mwendo mkali kuelekea katika hoteli ambayo Walter alikuwa amefikia. Lilian hakuamini kama atamkuta kweli Walter. Na kama ulivyokuwa wasiwasi wake. Hakika hakumkuta. “Aliondoka jana baada ya kukamilisha malipo yake?” muhudumu alimwambia Lilian. Liliy akashusha pumzi kwa nguvu, akamtazama yule muhudumu huku akiwa amekata tamaa. Akaondoka zake bila kuaga. Asingeweza kujiua bila kusema neno na Walter katu. Alihitaji kumweleza kitu kisha afe akiwa na amani.
Lilian alitembea bila kujua iwapo alikuwa anaenda wima ama alikuwa katika kuyumbayumba. Akaufikia mlango na kutoka nje. Akaendelea kutembea kwa myumbo ule ule hadi akaufikia umati mdogo wa watu. Hapa akagongana na kijana mmoja. Akili ikasogeleana kidogo. Akawa anatazama mbele. Ghafla kama ndoto. Jicho likaona…..likaona alichokuwa anakitafuta. Lilian alimuona Walter. Wakajikuta wanatazamana, kila mmoja akaganda bila kusogea hatua ya ziada mbele. Walter mdomo wazi, Lilian macho kodo mkono mdomoni.
Kwa sekunde kadhaa bila kusema neno mara ghafla Walter aligeuza alipotokea na kuanza kutembea kwa kasi. Lilian naye akili ikafunguka, akanyanyua mguu na kuanza kukimbia. Nyuma Lilian mbele Walter. Riadha ya kimya kimya ya viumbe wawili. Lilian akimkimbiza Walter ili amueleze kuwa Naomi anampenda sana kisha ajiue. Walter akikimbia kwa kuhisi anatafutwa kwa kesi ya ubakaji. KIVUMBIII!! !! !! !!
Walter alijaribu kukimbia huku na kule mara akaelekea kushoto mara akate kulia. Alipogeuka nyuma, hatimaye akashusha pumzi kwa nguvu sana. Alikuwa amefanikiwa kumpoteza Lilian. Walter akafanya ishara ya msalaba, kisha akajipangusa kijasho kilichoanza kumtiririka. Walter akaanza kupiga mahesabu upya kabisa ya namna ambayo anaweza kutoka katika jiji hilo salama. Kwani aliamini alikuwa anatafutwa na polisi kwa udi na uvumba. Uamuzi alioufikia ni kutafuta mawasiliano na rafiki zake wa karibu ambao wanaweza kumpatia pesa kwa namna nyingine tofauti na benki. Akajisachi na kuipata kadi ya simu yake ambayo alikuwa akiitumia siku zote kabla ya kubadili wakati anaondoka jijini Dar es salaam. Akajibanza pembeni kidogo katika kibanda cha kuuza bidhaa ndogondogo, akabadili kadi ya simu yake. Akaweka ile ya zamani. Akaanza kutafuta majina kadhaa ya watu wanaoweza kumpa msaada. Akapata majina mawilimatatu, akajaribu kupiga. Simu haikuwa na salio. Alijitazama mfukoni. Akashusha pumzi kwa kasi zaidi huku akifadhaika. Pesa iliyokuwa katika mfuko wa shati lake, shilingi elfu tatu haikuwepo tena. Akaghafirika. Akasonya mara kwa mara bila kujua ni kwa nini ardhi hii ya Tanzania inazidi kuwa chungu kwa upande wake. Walter akiwa bado hajajua nini cha kufanya, mara ghafla alijikuta amezungukwa na wanaume wawili. Miiili yao ilionyesha kuwa aidha wanafanya kazi ngumu ama ni mazoezi yamewafanya kuvimba vifua. “Nini? Kwani nini?” alihoji Walter kwa uoga huku akijaribu kutafuta upenyo akimbie. “Upo chini ya ulinzi mkali.” Mmoja wao alijibu. Walter akataka kukimbia, akakumbana na watu wenye shibe zaidi yake wakamminya. Akatulia. Wawili hawa wakamkwida vyema na kumsihi awe mtulivu. “Lakini mimi sijabaka?” alijitetea Walter bila kuulizwa lolote. Badala ya kujibiwa walimshangaa tu. Walter akaanza kulia akidhani hiyo yaweza kuwa suluhu. Wakati Walter akilia kama mtoto mdogo mbele ya wanaume wawili wababe kabisa. Upande wa pili, Lilian akiwa mwenyeji wa jiji la Mbeya akizijua kona zote kuanzia utotoni. Alifurahia riadha fupi aliyofanya na Walter. Alikuwa anaujua mji ipasavyo, hivyo alipomuona Walter anakata kona fulani yeye alipita upande mwingine huku akimini kuwa iwe isiwe lazima wakutane mbeleni. Hakika ilikuwa hivyo. Wakati Walter anatazama nyuma na kujipa uhakika kuwa amempoteza Lilian, binti huyu mwenye taaluma ya udaktari alikuwa anamtazama huku akifanya tabasamu hafifu. Walter akizidi kujiona yu katika amani. Lilian akafanya maamuzi. Aliamini kuwa Walter ni mwanaume hivyo hawezi kufika na kumdhibiti. Alihitaji wanaume kumsaidia. Mcheza kwao hutunzwa. Lilian akiwa mnyakyusa haswaa. Alizungumza kikabila na wanaume wawili ambao bila shaka walikuwa wapiga debe. Akaelewana nao. Pesa ilizungumza. Wanaume wakaingia kazini. Kisha likafuata zoezi ambalo lilimshtua Walter na sasa kujikuta katika mikono ya watu ambao anaamini kuwa ni askari. Laiti kama Walter angekuwa anafahamu kuwa askari huwa hafugi rasta basi angeweza kuushtukia mchezo huu lakini maskini kijana huyu hakujua lolote juu ya maisha ya askari. Akatetemeshwa akatetemeka haswaa.
Wanaume wale wakamfikisha Walter mbele ya mahakama ya mtu binafsi, hakimu, jaji na wakili, shahidi akawa mtu mmoja. Kwa jina alifahamika kama Lilian. Walter akaanza kutetemeka, alitazamana na sura ambayo alizoea kuiona ikitabasamu huku ikitokwa na maneno changamfu. Sasa sura hii ilikuwa imekasirika sana. Haikuwa na hata chembe ya furaha wala mzaha. Walter akatetemeka zaidi. Hakujua nia ya Lilian ni ipi na hao polisi wamemkamata na wataondoka naye hadi wapi. Wakiwa bado hawajasemezana lolote. Mara simu yaw alter iliita. Walter akawatazama wahuni alioamini kuwa ni askari. Akasubiri neno kutoka kwao iwapo anaruhusiwa kupokea simu ama la. Wazimu ukampanda muhuni mmoja, akamzaba kibao cha mgongoni Walter. “Weee..” akakaripia Lilian. Adhabu ile ilimuumiza, hakutaka Walter afanyiwe kitu chochote kibaya. Hakuwa mkosaji. “Toa hiyo simu Walter.” Hatimaye Lilian alimwambia Walter. Walter akaitoa ile simu, bila hata ya kuombwa ile simu akamkabidhi Lilian. Lilian akaitazama kwa sekunde kadhaa ikakoma kuita. Mara ikaanza kuita tena. Lilian akaitazama, akaunganisha meno yake, kisha akafumba macho midomo ikaanza kugongana. Akaunganisha mikono yake na kuanza kujiminyaminya lakini hakuweza kuzuia hicho alichokuwa anajaribu kukizuia. Mara machozi yakaanza kumtoka. Kilio cha kwikwi kikafuata.
****
Mungu ana maajabu yake na ukimlilia kwa namna ya kumaanisha atakujibu japo muda atakaokujibu kamwe hawezi kukupa taarifa. Mungu huliliwa kwa namna tofauti tofauti, wapo wanaowalilia babu zao, wengine huwalilia wazazi wao ambao wametangulia katika haki. Wapo wanaolilia mizimu, wengine hujikuta katika imani ya kimya kimya. Lakini yote haya humwendea Mungu mmoja, kinachohitajika ni Imani. Imani thabiti huleta majibu bila walakini.
Naomi hakuwahi kujua kama kumlilia bibi yake aliyefariki miaka kadhaa nyuma, ni sawa na kumlilia Mungu. Hii ilikuwa ni imani thabiti ya kuamini katika kitu kisichoonekana. Kilio cha Naomi kilisikika.
Jibu likapatikana baada ya muda fulani. Naomi alikuwa ofisini akijaribu kuweka mambo sawa katika makablasha kadhaa. Katika pitia ya huku na huku akakumbuka kitu. Ni siku nyingi sana alikuwa hajafanya mchezo wake ambao alikuwa amezoea kuufanya kila siku. Mchezo wa kuwasiliana na mume wake. Mchezo ambao ulimfanya kuhisi kuwa yu karibu na mume wake ambaye ametoweka kwa siku nyingi sana. Naomi akafanya tabasamu kisha akachukua simu yake. Akajaribu kupiga. Moyo ukashtuka na kupiga kwa namna ya kukaribia kupasuka. Simu iliita, tofauti na matarajio yake kuwa simu itajibiwa na mwanadada ambaye atamwambia kuwa simu ile haipatikani. Hali haikuwa hivyo. Simu ya Walter ilikuwa inaita. Lakini haikupokelewa. Akapiga mara ya pili ikaita tena. Naomi akaanza kutokwa jasho, mshawasha wa kusikia mtu ambaye atapokea simu ile ukampanda lakini bado simu haikupokelewa. Sasa alikuwa wima. Akihaha.
Wakati Naomi anahaha…simu ile ambayo ilikuwa inaita ilikuwa mikononi mwa mwanadada Lilian. Simu haikupokelewa. Mume aliyepigiwa simu alikuwa hana walau shilingi moja mfukoni na alikuwa mikononi mwa wahuni ambao anaamini kuwa ni maaskari. Simu ikaendelea kuita. Sasa ikatimia mara sita bila majibu. Naomi hakuchoka aliamini kuwa simu ile itapokelewa. Mara akakumbuka huduma ya kutuma ujumbe wa sauti, iwapo Walter hakutaka kupokea simu yake basi kwa namna yoyote angeweza kuisikiliza sauti yake nahuenda angejirudi. Naomi akaamua kupiga simu ili aweze kuacha ujumbe wa maneno ‘voicemail’ “Walter mume wangu pokea simu yangu tafadhali nakuomba….pokea unisikie mkeo…itazame pete yako ya ndoa..nilikuvalisha mimi Walter kumbuka maneno yangu kumbuka maneno yako…TULIAPA.” Ujumbe ukatumwa.
Hali ya sintofahamu ikaonekana kuwashangaza maaskari wale wa bandia, hawakujua nini kinaendelea kwa wawili. “Kulinifiki? (Kuna nini?)” waliuliza kinyakyusa. Walter hakuelewa nini kinaendelea. Lilian akanyanyua uso wake akakutana na Walter akiwa amefadhaika bila kujua nini kinaendelea. Lilian akapiga hatua mbili akamfikia Walter, akaikutanisha mikono yake akamkumbatia kwa nguvu huku akilia. Machozi ya Lilian yakalowanisha shati la Walter. Lilian alikuwa analia kwa mengi. Kuambukizwa Ukimwi kwa kujitakia pia kilio cha Naomi kilimpagawisha akajikuta katika hatia. Almanusura aseme ya moyoni mwake, lakini alipogeuza jicho lake jekundu akakutana na askari bandia. Akaingiza mkono mfukoni akatoka na noti mbili za shilingi elfu kumi akampatia kila mmoja noti yake. Wakaridhika wakatoweka na kuwaacha wawili hawa. “Walter..naomba usinikimbie, niruhusu niseme nawe kidogo tu nikimaliza unaweza kukimbia utakavyo.” Lilian alisema maneno hayo huku akimtazama Walter, macho yake yalikuwa mekundu sana na mashavu yake yaligandia michirizi ya machozi. Walter alibarikiwa jambo moja kubwa, jambo ambalo mara kwa mara lilimpelekea kuumia sana moyo hata kwa matatizo yasiyomuhusu. Walter alibarikiwa upole, huruma na hekima. Hali ikamuathiri alivyokutanisha macho na sura ya Lilian, ile hali ya kuogopa kusimama mahakamani ikatoweka, akajikuta katika huruma kuu. Akajizuia kwa kutazama kando nyingine ili machozi yasiweze kuchukua nafasi. Akafanikiwa kuidhibiti hali ile. “Walter nakuomba tuondoke eneo hili nahitaji kusema nawe kidogo tu.” Lilian alimweleza Walter kwa sauti ya chini iliyobembeleza. Walter akagutuka kidogo, akaijiwa na maneno kadhaa katika kichwa chake. ‘Mwanamke ni sumu..sumu inayoua upesi.’ Maneno haya hayakumburudisha, zaidi yalimtia mashaka. Alijikuta katika mtihani, je ni kweli Lilia nana neno la kumweleza ama ndo danganya toto aweze kumkamata na kumkabidhi katika mkono wa dola? Walter akamtazama Lilian vyema, akaanza kuhisi huenda Lilian anafanya kazi katika jeshi la polisi. Na sasa alikuwa anajiandaa kumkamata. Walter akajiuliza mara mbilimbili iwapo Lilian alikuwa na nia mbaya. Mbona tayari alikuwa amemkamata kwa kuwatumia wale vijana. Mbona hakumfikisha popote? Walter akaamua kumuamini Lilian na hata kama asingemwamini bado alikuwa anamuhitaji aweze kupata kadi yake ya benki. Walter akakubaliana na Lilian, Lilian akasimamisha taksi wakaingia ndani na kujibweteka wote katika siti ya nyuma. Safari ya kuelekea alipoagiza Lilian. Wakaifikia hoteli nzuri ya kifahari ambayo ilikuwa ina bustani. Wakajiweka katika viti viwili. Muhudumu akawasikiliza, kisha akawahudumia. “Walter unamfahamu Naomi?” “Naomi? Naomi gani?” alijibu kwa kuuliza swali huku akiwa amehamaki. “Aliyekuvika hiyo pete kidoleni?” alijibu Lilian kwa upole na unyenhekevu. “Ndio kwani vipi?” aliuliza tena. Lilian akachukua maji aliyoagiza, akapiga funda kadhaa kisha akamtazama Walter. Sekunde kadhaa akimfanyia tathmini. “Walter, sijui hata niseme nini ili niweze kuyaanza mazungumzo haya. Lakini napenda utambue kuwa ni heri kumwaga damu ya mtu, mtu huyo hataonekana tena itabaki kukulaani mizimu yake na kamwe hautajua kama unalaaniwa. Lakini kulimwaga chozi la mtu kwa kuupondaponda moyo wake hii itakutesa sana maana chozi hilo litaendelea kukusulubu taratibu lakini katika namna ya kustaajabisha na mwisho wa siku hautafanikiwa katika maisha yako. Walter nadhani ulikuwa haunifahamu, mimi ni daktari. Daktari maarufu sana mwenye mapungufu yake ya kibinadamu, lakini mapungufu haya yamekuja na mikosi ndani yake. Mimi ni mtu wa mikosi kila mara. Lakini mikosi yangu isiwe tija ya kutafuta ya kumwaga chozi la mtu mwingine, sihitaji mtu alie kwa ajili yangu, naomba niseme jambo moja kubwa labda hukuwahi kulijua. Ninakupenda sana Walter na ninaomba unisamehe kwa sababu sikuwahi kukwambia. Licha ya mimi kukupenda yupo mwanadamu anayekupenda kupita wote….” Alisita kidogo Lilian, akachukua maji yake tena akapiga funda jingine kubwa. Walter alijaribu kunywa maji, akajikuta anafanya kichekesho mbele ya Lilian, kopo la maji yake lilikuwa halijafunguliwa bado lakini aliweka mdomoni akitegemea maji kuingia kinywani. Lilian akatabasamu baada ya Walter kujishtukia. “Walter, Naomi anaweza kuwa mwanamke anayekupenda kupita wote duniani, nina hisia juu yako lakini Naomi ni mke wako wa ndoa. Nisamehe kwa kitendo changu cha usiku ule mbaya kwako. Lakini chukua fursa hii kupokea maneno haya kutoka kwangu. Na kama inawezekana nakuomba urejee jijini Dar, nenda ukazungumze na Naomi. Sihitaji kujua ni kipi alikukosea, lakini tambua kuwa Naomi analia kila leo.Na wakati tupo pale na wale vijana. Alipiga simu.” Lilian alimalizia kauli hiyo kisha akachukua simu. Akaitazama. Akakutana na ujumbe alipoufungua alikutana na ‘voicemail’ kutoka kwa Naomi. Bila kumwomba ruhusa Walter alipiga namba aweze kuisikiliza ‘voicemail’ hiyo. Akaweka simu katika spika za nje. “Walter mume wangu kama ni kweli nimekuwa wa kuchukiza kiasi hicho machoni mwako, naomba nisikuchukize tena, wacha nikamchukize mama yangu mzazi aliyenizaa, huu mzigo usiubebe wewe..ACHA NIFE WALTER…acha nife kwa ujinga wangu.” Sauti ya Naomi ilisikika ikizungumza huku ikilia. Ilikuwa inasikitisha sana. Ujumbe huu wa sauti ukabadili kila kitu, hapakuwa na mazungumzo tena. Walter akapagawa, Lilian naye ujumbe huu ukamvuruga. Ujumbe huu ukawafanya wawili hawa wawe wamoja. Walter alikuwa anatokwa jasho. “Walter mpigie simu….mpigie simu tafadhali. Mwambie asijiue” Lilian alimsisitiza walter huku akisimama wima. Walter kama bwege akachukua ile simu, akajaribu kupiga simu. Mara akakumbuka kuwa hakuwa na salio katika simu. Lile jeraha la kumpoteza mama, baba, bibi na dada..likaibuka upya. Walter akaona dalili za kumzika Naomi. Penzi la dhati alilokuwanalo moyoni likasimama wima. Walter akajisikia yu hatiani na iwapo Naomi angejiua kwa namna yoyote basi alikuwa anahusika. Lile neno la Lilian kuwa ni heri kumwaga damu kuliko kumwaga chozi likaonekana kuwa si sahihi..damu ikawa nzito kuliko chozi. Lilian alimpatia Walter simu yake aweze kuitumia kupiga. Akapiga simu. Maajabu mengine, Walter akaishiwa nguvu. Akajikuta anakaa chini kama mtoto mdogo. Lilian akabaki kushangaa.
****
Naomi alikuwa na subira sana lakini subira hii ilifikia kikomo baada ya kuhisi kuwa Walter alikuwa anamuonea kwa manyanyaso haya yasiyokuwa na kikomo. Naomi aliamini kuwa Walter alikuwa anaitazama simu yake jinsi inavyoita na kuipuuzia bila kuipokea. Naomi akaamua kutuma ujumbe wa sauti. Ujumbe ambao alisema kile ambacho nafsi yake ilimtuma. Baada ya ujumbe ule akajiona hana maana yoyote ya kuendelea kuishi duniani. Ataishi vipi iwapo Walter hataki kuwa naye, ataishi vipi iwapo anachukiwa na Walter? Kuchukiwa na Walter ilikuwa sawasawa na kuchukiwa na dunia nzima. Asingeweza kuishi wakati anamchukiza mume wake. Naomi akafikiria kujumuika na marehemu mama yake, pia marehemu bibi ambaye alimtabiria kuwa siku moja atakuwa mke wa Walter. Baada ya kutuma ujumbe ule alitoweka akafunga ofisi. Akaondoka akiwa na wazo moja tu la kujiua. Aliamua kujiweka mbali na Walter.
Wakati anaiweka simu yake katika mkoba wake, bahati mbaya kitufe cha kuzimia simu kilijibonyeza. Simu ikazima. Huu ni wakati ambao Walter alikuwa anajaribu kumpigia simu bila mafanikio.
Walter akalegea na kukaa chini. Hali ilikuwa mbaya sana. Lilian akachukua ile simu naye akajaribu kupiga, simu ilikuwa haipatikani. Naye hofu ikamwingia. Ujasiri wa kidaktari ulimsaidia kuweza kuishinda hofu hii. Akamkabili Walter na kumpa maneno mawili matatu. Walter akasimama na kumfuata kwa nyuma. Wakarejea tena katika taksi na kutoweka. Lilian alikuwa katika wakati mwingine mgumu sana. Alikuwa na mpango wa kumpa taarifa Walter kisha baada ya hapo aweze kujiua ili asiweze kuaibika kwa kufa kwa gonjwa la Ukimwi. Lakini sasa Walter yu matatani na ujumbe wa sauti kutoka kwa Naomi unawavuruga. Naomi alikuwa anataka kujiua. Lilian aliijiwa na wazo la kusitisha kujiua. Alitaka kujipa muda kwanza. Akashambuliwa na namna fulani ya kupata njia mbadala. Kuishi na Walter wakijiuguza gonjwa la Ukimwi huku akiipata furaha ya namna yake. Mara akajiona mjinga kuwaza hali hiyo. Kwani kwa kuwaza kuwa na Walter ni sawasawa na kubariki uamuzi wa Naomi kujiua ili aweze kubaki huru na kijana huyu. Lilian alikuwa mkimya sana lakini kichwani alikuwa akichemka haswa haswa. Baada ya muda wakaifikia nyumba ya daktari. Upesiupesi Lilian akaingia ndani, akarejea baada ya dakika tatu. Akamuamrisha dereva waondoke. Wakaelekea maeneo ya Uyole. Huko Lilian akafika mahali akaingia katika geti kubwa jeusi. Aliporejea alikuwa ndani ya gari aina ya Landcruiser 4wheel drive. Akamlipa dereva wa taksi. Akamsihi Walter aingie ndani ya gari. “Walter tunaenda jijini Dar es salaam, kama Mungu amepenga tumkute Naomi hai. Tutamkuta. Na ninaamini itakuwa hivyo.” Lilian aliongea kijasiri. “Funga mkanda Walter.” Akamkumbusha. Lilian alikuwa ameamua jambo moja tu. Kuokoa kwanza uhai wa Naomi kisha atapata maamuzi baada ya kufanya jambo hili. Kitendo cha kuombea Naomi aweze kufa ili aweze kumfaidi Walter alikitupilia mbali. Akaweka utu mbele. Landcruiser ikaingizwa gia mwanadada aliyevaa miwani nyekundu akaiingiza barabarani, Walter alikuwa anashangaa hakutegemea mambo hayo yanaweza kutokea kwa pamoja namna hiyo. Ni kama alikuwa ndotoni. Ndoto ya mchana.
Naomi alikuwa na subira sana lakini subira hii ilifikia kikomo baada ya kuhisi kuwa Walter alikuwa anamuonea kwa manyanyaso haya yasiyokuwa na kikomo. Naomi aliamini kuwa Walter alikuwa anaitazama simu yake jinsi inavyoita na kuipuuzia bila kuipokea. Naomi akaamua kutuma ujumbe wa sauti. Ujumbe ambao alisema kile ambacho nafsi yake ilimtuma. Baada ya ujumbe ule akajiona hana maana yoyote ya kuendelea kuishi duniani. Ataishi vipi iwapo Walter hataki kuwa naye, ataishi vipi iwapo anachukiwa na Walter? Kuchukiwa na Walter ilikuwa sawasawa na kuchukiwa na dunia nzima. Asingeweza kuishi wakati anamchukiza mume wake. Naomi akafikiria kujumuika na marehemu mama yake, pia marehemu bibi ambaye alimtabiria kuwa siku moja atakuwa mke wa Walter. Baada ya kutuma ujumbe ule alitoweka akafunga ofisi. Akaondoka akiwa na wazo moja tu la kujiua. Aliamua kujiweka mbali na Walter
****
Lilian akiwa ameuvaa uhusika wa kigaidi kabisa. Sura ikiwa ya kazi kikamilifu aliliingiza gari katika kituo cha mafuta. Akatoa noti kadhaa mafuta yakajazwa. Gari iakondoka kwa mwendo wa kasi. Lilian aliendesha kwa mwendokasi ambao katika enzi za uhai wa mzee Mbaule alikuwa akiupinga kabisa. Sasa yu katika gari alilonunuliwa na mzee Mbaule miaka kadhaa na anaendesha ule mwendo ambao alikuwa anaupinga akiwa binti mdogo. Walter akiwa amefunga vyema mkanda wake alikuwa anatetemeka. Roho mkononi. Alitamani kumwambia Lilian apunguze mwendo lakini akaikumb uka roho ya Naomi. Akaiona ni ya umuhimu zaidi. Ilikuwa bora afe kwanza lakini katika jitihada za kuipigania roho ya Naomi lakini si Naomi afe halafu yeye abaki hai. Aliamini katu hataweza kuwa na furaha ya aina yoyote ile. Uzuri wa barabara ya kutoka Mbeya kuelekea jijini Dar es salaam ni lami mwanzo mpaka mwisho. Lilian akiwa amejikita katika kumung’unya peremende, hakuna jingine alilofanya zaidi ya kuwa makini katika usukani, barabara ilisikika ikilalamika kadri mwendo ulivyokuwa unaongezeka. Gurudumu madhubuti ziliitesa lami ile. Kwa mwendo mkali kabisa wakaipita Makambako. Walter alikuwa mkimya akitafakari mambo aliyokuwa anayapitia. Lilian alikuwa ametenga pesa kwa ajili ya askari wa barabarani iwapo watamzuia njiani usiku huo. Aliamini kuwa hawatakosa jambo la kumzuia.
Walipoufikia mji wa Morogoro. Walter kwa mara ya kwanza akagundua kuwa ni kipindi kirefu kilikuwa kimepita tangu atie chakula mdomoni. Ni kama Lilian aligundua jambo hilo. Akaingiza gari katika hifadhi ya magari katika mgahawa uliokuwa katikati ya mji. Giza lilikuwa nene, alkini palionekana kuwa na huduma katika mgahawa huo. Wakajipatia chakula. Hakuna aliyeonyesha kukifurahia lakini ilikuwa lazima wale. Baada ya pale. Lilian akaingia garini tena. “Walter unaweza kumalizia safari.” “Unamaaniha kuendesha?” “Yah, nimechoka haswaa halafu nina usingizi.” “Lilian, sidhani kama nitaweza naona maluweluwe mbele yangu.” Alijibu Walter. Lilian akapiga moyo konde akarejea mgahawani tena, bahati nzuri akapata kahawa nyeusi. Akagida vikombe kadhaa. Akachangamka. “Hapa poa.” Daktari alimnong’oneza Walter. Kwa mara ya kwanza Walter akatoa tabasamu. Daktari akamkonyeza. Safari ikaendelea tena. Hapakuwa na na magari barabarani. Lilian akateleza kwa kasi kubwa. Ndani ya saa moja na nusu wakaingia jijini Dar es salaam. Kwa mujibu wa saa ya Lilian. Walikuwa wametumia masaa saba tu. Kutoka Tukuyu Mbeya na kulifikia jiji la Dar es salaam. Lilian alikuwa na haki ya kujipongeza. Mwanadada akaliongoza gari hadi katika eneo la hoteli maarufu, jirani na kituo cha mabasi cha Ubungo. Akaegesha. Akaenda mapokezi na kulipia chumba. “Walter hatuwezi kuendelea na shughuli usiku huu.” Walter akaelewa maana ya Lilian. Kwa unyonge akajikongoja chumbani. Chumba kikawa katika hali ya upweke hakuna aliyeanzisha mazungumzo. Ni kama kila mmoja alikuwa katika dunia yake ya kipekee lakini kimwili wakiwa katika kitanda kimoja. “Lilian…” hatimaye Walter aliita. Lilian hakujibu badala yake akageuka na kumtazama Walter ambaye alikuwa amejisitiri katika taulo baada ya kuwa ametoka kuoga. “Hivi Naomi wangu hajajiua kweli.” Walter aliuliza huku sauti yake ikikwama. Lilian akafumba macho, hakutaka kumtazama Walter usoni, mwanaume huyu alikuwa na moyo wa kike. Hakuwa jasiri katika taarifa hizi ambazo alitegemea kuzipokea. Lilian alisimama, akaenda katika kitufe cha kuzima taa, akaizima. “Lala Walter mambo yote yatafahamika asubuhi.” Hatimaye Lilian alitoa kauli. Walter akasikika akitokwa na kilio cha chinichini. Lilian akatambua kuwa kitendo cha kujaribu kumbembeleza Walter kingezuka kilio kingine kikubwa. Lilian aliyechoka kabisa akawa wa kwanza kusinzia. Walter naye akafuata.
Majira ya saa mbili asubuhi Walter alimkurupua Lilian. Hakika kijana huyu alikuwa katika mashaka makubwa sana. “Lilian….kuna jambo moja nadhani haulifahamu.” “Jambo gani?” “Mimi ni maarufu sana hapa mjini. Najua kutoweka kwangu palizua mengi sana. Kama itawezekana tukishuka chini unichukulie miwani nyeusi.” “Usijali.” Lilian alimhakikishia.
Baada ya kujiandaa walitoweka Lilian akafanya kama Walter alivyoomba.
Walter akamuelekeza Lilian, nyumba yake ilipo. Ni hapo waliamua kuanzia shughuli yao. Lilian kadri alivyofikiria kuwa anampigania Naomi ili apate raha na kijana Walter alifadhaika na kujikuta lile jeraha lake likirejea kuwa kidonda kibichi. Lakini atafanya nini wakati tayari ameamua iwe hivyo. Hatimaye wakaifikia nyumba ya Walter. Nyumba ilikuwa imetulia sana. Muda huo mlinzi alikuwa ameondoka tayari. Walter akatangulia mbele Lilian nyuma. Wakaifikia nyumba. Ilikuwa imefungwa. Walter akapapasa mahali ambapo huwa wanaweka funguo akaukuta. Akafungua kile kitasa kwa kukoseakosea kutokana na haraka lakini hatimaye kikafunguka. Ana kwa ana na picha kubwa ukutani. Picha aliyopiga akiwa na Naomi. Walter akapagawa. “Hayupo Naomi wangu.” Walter alimwambia Lilian huku machozi yakimlenga.
Mara jicho la Lilian likaona kitu mezani. Kilikuwa ni kipande cha karatasi. Wakati Walter anakimbia chumbani Lilian akachukua kile kikaratasi. Akakifunua upesi na kukisoma pasi na umakini. “Nakupenda Walter, nisamehe kabla haujafa.” Mwandiko wa kike uliandika maandishi yale. Lilian akakificha, na kisha akafanya tafsiri kuwa Naomi atakuwa amefanya jambo baya tayari. Huenda atakuwa amejiua. Lilian hakutaka Walter akione kikaratasi kile. Ilikuwa ni heri habari za kifo cha Naomi zitangazwe redioni kuliko Walter kukisikia palepale akiwa ndani ya nyumba yake. Kwa udhaifu aliokuwanao Walter, Lilian alimini kuwa lazima apatwe na mshtuko mkubwa ambao kwa namna moja ama nyingine unaweza kupoteza uhai wake. Daktari mzoefu akaficha siri hiyo.
Walter akaparangana huku na kule. Akamwomba Lilian apige simu ofisini kwake. Jibu likawa kuwa Naomi hajafika kazini. Walter akataharuki, akakosa utulivu na kuchachawa kabisa. Lilian akaendelea kumpa moyo kwa lugha mbalimbali.
****
Basi lilionekana kama haliendi wakati lilikuwa katika mwendo mkali kabisa. Wakati abiria wengine wakionekana kuwa na hofu na mwendo wa basi lile, abiria mwingine alikuwa akitamani liende mwendo wa mara kumi zaidi ya pale. Lakini haikuwa hivyo. Hakutulia katika kiti chake, mara asimame mara atazame nje, mara ajikune. Hakuwa akijielewa. Fujo zake zote hizo hazikubadilisha mwendo wa gari lile. Safari hii ya dharula ilikuwa mwendelezo wa mauzauza aliyoyahisi katika kichwa chake baada ya kupewa maelezo kadhaa. Wakati akijifikiria kujiua, alipata wazo la ghafla ambalo alilifanyia kazi na aliamini kuwa pesa yake kama itahitajika itatumika. Naomi alihitaji kufahamu simu ya Walter ilikuwa inapatikana katika mkoa gani. Aliingia katika ofisi kuu za mtandao anaoutumia. Akajieleza kwa ufanisi akaeleweka. “Namba hii inapiga kutoka Mbeya….” Alijibiwa. Akalichukulia jibu lile kuwa ni la kawaida tu. Kabla hajaondoka akakumbwa na pepo la machale. Machale asiyojua yanatoka wapi.
Akamfikiria Dokta Suzi. Huyu daktari aliwahi kumuuliza juu ya mumewe lakini hakusema neno zaidi na kisha akatoweka. “Samahani na hii pia napenda kujua ipo mkoa upi?” Naomi aliuliza kwa staha. Akamkabidhi yule kijana namba ya Dokta Suzi. Baada ya dakika tano akapewa jibu. “Na hii ipo Mbeya mpaka muda huu.” Alijibu yule kijana. Hapa sasa Naomi akachanganyikiwa. Wivu ukachukua hatamu kisha ukampa suluba ya namna yake ambayo ilimyumbisha kimawazo. Ina maana dokta suzi anafahamu mume wangu alipo na hajaniambia? Alijiuliza Naomi huku akichukua mkoba wake aweze kuondoka. Alisahau kabisa kuaga. Akatoka kichwa chini mikono kiunoni. Alipofika nje akaketi katika benchi la fundi viatu. Hakuwa katika ulimwengu wa kawaida kabisa. Naomi alisulubika, akaumuona Daktari Suzi kama msaliti mkubwa, tena mwenye roho mbaya na pia mnafiki. “Kumbe wakati nampigia simu alikuwa Mbeya na mume wangu?” Naomi alijikuta anasema mwenyewe. Kisha akasimama wima akaingia katika gari lake. Akajitahidi kujiweka sawa kimawazo. Mawazo yakatulia, jeraha la hisia likachachamaa. Likaanza kumchokonoa katika namna inayokera. Machozi yakatiririka. Bora yangetiririka mashavuni angeweza kuyafuta, machozi haya yalitiririka katika moyo mpweke. Nani wa kumfuta machozi haya? Wa kumfuta alikuwa katika kifua cha mwanamke mwingine….Hisia zilimtuma hivyo. Naomi akahisi kupagawa.
Nyumba haikuwa inakalika. Alitembea huku na kule, alijikuta akipanga kusafiri kuelekea huko huko Mbeya kupigania penzi lake. Naomi akajiona mjinga sana kuwaza kujiua. Alikuwa mjinga haswaa. Utajiua vipi umwachie mwanamke mwenzako starehe kama hizo? Hii ni aibu ya karne. Naomi akaamua kufanya pigano la mwisho. Aliamini kuwa katika vita hii majibu yatakuwa mawili tu. Ama zake ama za daktari Suzi. Akiamini kuwa anaenda katika vita ambayo aidha atakufa ama ataua. Naomi kwa upendo wa dhati hakutaka Walter alaumiwe kwa lolote, akajipinda na kuandika ujumbe mfupi na kuuacha mezani, ujumve ambao aliamini kwa namna yoyote utamuumiza Walter lakini utamwacha huru kijana huyu. Hasira zikajihifadhi katika nusu ya moyo wake. Akapanda nazo katika basi, baada ya kugundua kuwa hataweza kuendesha gari kuelekea Mbeya. Sasa yu pamoja na hasira ambazo zimebeba kiapo cha ‘ama zangu ama zake’…Naomi anaelekea jijini Mbeya. Cha kuchekesha hajui hata ni wapi katika jiji la Mbeya ataanzia.
Majira ya saa kumi na mbili jioni Naomi alilifikia jiji la Mbeya.
Jambo la kwanza kabisa. Alijiweka katika hali ya kuwa mwenyeji sana. Akaangaza huku na kule na kukutana na banda la chipsi, akaingia na kuagiza. Wakati anakula alikuwa akipepesa macho huku na kule kuangaza ramani za kuweza kumfikisha mahali ambapo kwa usiku huo atauweka mgongo wake. Baada ya kumaliza kula na kuilipia huduma ile. Aliondoka moja kwa moja akiifuata barabara, akatoka nje ya kituo kikuu cha mabasi jijini Mbeya. Alitegemea kukutana na nyumba za kulala wageni karibia kabisa na kituo hicho na hakika ilikuwa hivyo. Alikutana na nyumba ambayo kimtazamo ilimridhisha. Akaingia pale na kama ilivyokuwa bahati katika upande wake alipata chumba, akalipia kisha akaingiana na kujitupa kitandani. Hakutegemea kulala mapema kiasi hicho lakini pasipo kujua alijikuta akilala na viatu bila hata kujimwagia maji. Mbu wakali lakini wachache walipokitembelea chumba hicho na kumsalimia kwa kumng’ata ndipo aliposhtuka. Jicho lake katika saa yake ya mkononi. Ilikuwa saa sita na dakika arobaini usiku. Naomi akasimama wima, akatoa viatu vyake kwa kuvikanyaga kanyaga. Viganja vikiwa machoni vikijipekechapekecha kuondoa mang’amung’amu ya usingizi. Baada ya hapo aliondoa gauni lake la bei ghali alilonunuliwa na mume wake. Mara macho yake yakakutana na mlango wa bafuni ukiwa wazi. Akakumbuka kuwa hakuwa ameoga tangu afike katika jiji hilo. Akajikongoja hadi bafuni. Maji yalikuwa ya baridi sana lakini alijikaza ili kutimiza ule usemi wa maji ukiyavulia nguo sharti uyaoge. Naomi akajimwagia maji kwa uoga sana. Hakika yalikuwa yana ubaridi mkali. Hata alipomaliza kuoga usingizi nao ulikuwa umepaa malikiti. Naomi akakivamia kitanda tena kujaribu kuendelea kuutafuta usingizi. Haikuwezekana baada ya kuingiliwa na pepo la kutojiami. Hali hii ya kutojiamini ilimfanya aamini kuwa hakika alikuwa ameusahau uchangudoa, kwani wakati akishiriki katika biashara hii hakuna chochote kilichomshinda. Hakuogopa lolote na alifanya mambo mazito bila hofu yoyyote, lakini cha ajabu sasa analiogopa jiji la Mbeya. Naomi alinyanyuka kitandani akajiweka kitako. Akakuna kichwa chake, kisha akaichukua simu yake akaiwasha. Jambo la kwanza aliloamua kulifanya ni kumhadaa Dokta Suzi (Lilian), ili aweze kujua mawili matatu kutoka kwake. Naomi aliamini kuwa muda huo Lilian atakmuwa amemkumbatia Walter wakipeana joto katika baridi hilo kali la Mbeya. Naomi akauvaa uigizaji wa kichangudoa akaiandaa sauti ya kumhadaa Lilian. Simu ikaanza kuita, iliita kwa muda mrefu lakini haikupokelewa. Apapiga mara ya pili bado haikupokelewa. Naomi akafumba macho yake na kuiona picha ya Walter akiwa uchi ya mnyama na daktari naye akiwa kama mwenzake wawili hawa walikuwa wanatabasamu. Na walichokuwa wakifanya kwa kushindana kilimfanya Naomi afumbue macho. Hakika ilikuwa ndoto mbaya ambayo hakutakiwa kuiota tena. Naomi akajaribu kupiga tena simu, hali ikawa ileile. Naomi akakata tamaa akakoma kupiga simu, kwani kila alivyokuwa anapiga simu alizidi kuwaza mabaya juu ya Walter. Pia akajikuta katika hasira mbaya sana, hasira juu ya daktari mnafiki. Hasira ya Naomi ikamtuma jambo moja bay asana, ambalo alimini kuwa litamuweka matatani, lakini ilikuwa lazima alifanye ili kuhakikisha kuwa kama anaingia matatani aingie akiwa analipigania penzi lake. Naomi akafumba macho yake, akahesabu vidole vyake mara kwa mara, akajilaza. “Yes..hivyo hivyo….” Alitokwa na maneno hayo huku akitabasamu kidogo. Akaichukua simu yake akaizima. Kwa mara nyingine akajifunika shuka lakini safari hii alijifunika kwa mtindo wa gubigubi. Akasinzia. Alisinzia akiwa na lake kichwani.
****
KAMA wangeweza kuhesabiwa kilomita amabzo wamezurura hakika wawili hawa wangeweza kuwa watu waliotembea mwendo mrefu kupita wote katika siku ile. Walter akiandama na Lilian walipita kila kona kuhakikisha kama kweli Naomi hayupo katika jiji la Dar. Mara wapiti saluni alizozoea kwenda kutengeneza nywele zake, mara wapiti katika hoteli ambazo hupendelea kula chakula chake, wakapitia na kumbi za starehe ambazo Naomi baada ya kucharuka alikuwa anapendelea kwenda huko. Baada ya kukosa jibu huku wakitegemea taarifa zozote katika vyombo vya habari bil,a mafanikio yoyote waliamua kurejea nyumbani. Kila mmoja alikuwa kimya. Upweke wa hali ya juu ulitawala. Walter alichukua simu yake. “Lilian nampigia Frank anipe ushauri.” “Frank ni nani?” “Baba yangu…” alijibu Walter. Lilian akamtazama, Walter akabofya namba kadhaa. Simu ilikuwa haipatikani. Akajaribu tena hali ileile. Akashusha pumzi kwa nguvu zote. Sura ikamshuka dalili za uchovu na kufadhaika. Lilian hakutia neno. Walter akafumba macho na kujikuta katika hisia mbaya na dhaifu sana, tena tatanishi. Tatizo ni kwamba hakuwahi kujua madhara yake, maneno ya watu ya kujisafisha yakamchanaganya. Naye akajiaminisha kuwa pombe yaweza kusaidia kupunguza mawazo. Akasimama upesiupesi akalifikia jokofu. Akatoka na mvinyo asioujua kwa jina, akachukua glasi mbili. Akazifikisha mezani. Akamimina katika glasi zote mbili.li pombe sio Lilian bila kuuliza swali naye akajikaribisha, glasi moja yak wake, nyingine ya Walter. Sasa ni kama walikuwa wanashindana kugida ule mvinyo. Amakweli pombe sio chai, ione na uipishie mbali. Ndani ya saa zima Walter alikuwa anafanana na wale wanamuziki kutoka kongo, Walter alikuwa muimbaji. Mara Lilian akajihisi kuwa kiuono chake hakina mfupa, akaanza kukatika. Dj Walter katika mitambo. Lilian katika jukwaa akilikata sebene barabara. Muziki ukafunguliwa kwa sauti ya juu. Wahusika hawa hawakujali. Mlinzi alibaki na sintofahamu. Lakini ataanzia wapi kumkabili bosi wake na kumwambia apunguze sauti? Ilikuwa ngumu. Mara Walter akaingiwa na tamaa, akajikuta akaimwonea donge Lilian kwa jinsi alivyokuwa anakata mauno katika namna ya upweke wa hali ya juu. Walter akajiunga. Akakinasa kile kiuno cha daktari kilichokuwa kinakaribia kuanguka. Akakikamata vyema. Daktari akazidi kukizungusha. Mara wakasahau kuwa walikuwa wakikata mauno, wakajikuta wamekumbatiana, wote wakiwa na furaha. Walter akiwa amelewa zaidi ya Lilian. Wakasukumana huku na kule, Walter akajikuta akiropoka matusi ya kiingereza. Lilian naye alijitetea kwa kinyakyusa basi ikawa lugha gongana. Hakuna aliyemuelewa mwenzake anachomaanisha. Walter akawa wa kwanza kupaparuka na kumshika Lilian kifuani. Wakazonganazongana na kujikuta katika zulia. Pombe ikawafanya wawili hawa kuwa marafiki. Sasa hakuna ambaye alimwekea mwenzake dawa ya kuongeza nguvu za kiume ama kuleta hamu ya kufanya mapenzi lakini kila mmoja alijikuta katika uhitaji mkubwa. Ni hili huwa linafanya wazinzi wengi wailaumu pombe kila baada ya uzinzi wao. Pombe inafanya tendo hili maarufu livutie maradufu. Nguvu za kucheza zilikuwa zimewaishia mwilini lakini nguvu za kuvuana nguo zilikuwepo. Nani kama ulevi? Wakajikuta bila kulazimishwa wakiibanjua amri ya sita. Tena bila kinga kwa mara nyingine. Kila Walter alivyokazana kumuita Lilian kwa jina la Naomi ndipo naye alivyozidi kumuita majina tofauti tofauti, aidha ya wagonjwa wake aliowahi kukutana nao katika huduma ama hata wanaume waliowahi kumtaka kimapenzi. Dj na Daktari zuliani. Nani wa kuwazuia wakati mkewe Walter hayupo?
Simu ya Lilian ilivyoita, ni masikio pekee yalikuwa na muda wa kusikiliza lakini viungo vingine vilikuwa dhaifu sana. Lakini imara katika uasherati. Simu iliita sana hatimaye ikakoma, ikaita tena. Hakuna aliyejali. Laiti kama Walter asingekumbwa na pepo la kunywa pombe basi usiku huo angeweza kuisikia tena sauti ya mkewe mpenzi Naomi, na huenda ugomvi wao ungeishia hapo na ndoa yao imara kujengeka tena. Lakini bahati haikuwa upande wowote ule. Walter alikuwa amelewa na alikuwa anafanya uzinzi katika nyumba ambayo alikuwa akiishi na mkewe.
****
Taksi ilisimama katika mlango mkuu wa kuingilia katika hospitali ya mkoa wa Mbeya. Baada ya mlango kufunguliwa alitelemka mwanadada wa kisasa ambaye kwa wenyeji wangeweza kugundua kuwa msichana huyu alikuwa mgeni wa jiji lile. Alikuwa ameziba macho yake na miwani ya rangi za bluu bahari ambazo zilirandana haswaa na gauni lake fupi lililoukaa vyema mwili wake. Aliposhuka garini, alitoa miwani yake na kuanza kupiga hatua kuelekea mapokezi. Wakinamama na akina baba walijikuta wakimshangaa bila kujua kama walikuwa katika hali hiyo ya mshangao. Changudoa wa zamani mwenye pete ya ndoa kidoleni alikuwa anatembea mithili ya twiga. Alikuwa ananyata. Naomi mtoto wa Holela hakuwa mrembo sana lakini alijua jinsi ya kuvaa na kuonekana mrembo wa kutisha. Marashi yake yaliacha miguno huko nyuma. Hakujali. Akafika mapokezi. Lengo lake kuu likiwa kuonana na Daktari Suzi (Lilian) katika namna ya kustukiza. Alihitaji kumkoromea juu ya mumewe. Naomi aliamini kuwa daktari yule kamwe hakutegemea ujio ule wa ghafla. Mapokezi alipewa maelekezo zaidi ya kufuata. Akaelekezwa katika mlango wa ushauri nasaha. Naomi aliondoka pale akiwa mwingi wa tabasamu. Kwanza alijipongeza sana kwa kufikiria kuwa Dokta Suzi ni mtu maarufu na katika hospitali kubwa kama ile hawezi kukosekana. Hakika Suzi alikuwa mtu maarufu na alikuwa akifahamika na kila mtu katika hospitali ya mkoa. Sasa anaelekea ofisini kwa mwanadada huyu. “Yaani akileta za kuletwa nafanya fujo hapahapa halafu tuone nani atakayeaibika. Na ka akitaka tufanyiane ubabe Wallah namchomachoma masindano akifa shauri yake…..” Naomi alijiapiza kimya kimya huku aking’ata papi za midomo yake minene. Akaufikia mlango, akaomba ruhusa ya kuingia, akaipata. Akaingia, macho yake yakakabiliana na mtu ambaye hakumuhitaji. Huyu hakuwa dokta Suzi. “Samahani namuulizia dokta Suzi.” “Ulikuwa na ahadi naye.” Aliulizwa badala ya kujibiwa. Swali lile likamkera Naomi lakini hakutaka kuonyesha kuwa amekereka. “Hapana ila ninashida naye sana.” “Samahani ana dharula na hapatikani kwa sasa nadhani mpaka juma lijalo.” Alijibu huku akimtazama Naomi usoni.
Naomi akajisikia hasira ikifurukuta kifuani mwake. Akaondoka bila kuaga. Mtoa huduma hakujali. Akaweka miwani yake vyema machoni. Akaendelea na shughuli zake.
****
Lilian alikuwa wa kwanza kugutuka kutoka katika ulevi. Akajikuta yu uchi wa mnyama, akataka kukimbia akasita. Akajiziba matiti yake, mara akaghairi akajiziba katikati ya mapaja. Akageuka nyuma, Walter akiwa uchi wa mnyama naye alikuwa anakoroma. Lilian akaijiwa na ujasiri kiasi fulani. Picha ya usiku uliopita ikarejea katika kichwa chake. Lilian akafanya tabasamu. “Nimefanya na muathirika mwenzangu..” Kauli hii ikasafiri na macho yake hadi kuifikia simu yake. Simu ilikuwa inawakawaka. “Nani tena alinipigia usiku?” Lilian aliuliza kana kwamba kuna mtu anayemsikiliza na atampa jibu. Akaikwapua simu na kuitazama. Ghafla akaruka mbali kama aliyepigwa shoti. Akatokwa na yowe kubwa la hofu. Yowe ambalo lilimkurupua Walter kutoka katika usingizi mzito. Lilian alikuwa kama aliyeona jinamizi. Jina la Naomi ambaye anaamika kuwa huenda amekufa kutokea katika jina lake hali hii ilizua utata. Lilian akamshirikisha Walter, naye akapagawa na kujisahau kuwa wote wapo uchi bado. Haraka Walter akathubutu kumpigia simu Naomi aweze kusema naye lolote.
***NAOMI katika jiji la Mbeya ameenda kumsaka WALTER ambaye hayupo tena katika jiji lile. ***LILIAN na WALTER…wakiwa uchi..wanakutana na jina la NAOMI katika simu ……..ni kizungumkuti….hakika
0 Comments