Header Ads Widget

Responsive Advertisement

JERAHA LA HISIA - 1




Simulizi : Jeraha La Hisia
Sehemu Ya Kwanza (1)


"Kwa nini hutaki kusahau tabia yako ya kale,kwanini unanitesa hivi, unanifadhaisha, tazama jamii inavyoniangalia kwa jicho baya la kinafiki na dharau ndani yake, kumbuka kwamba hukuzaliwa ukiwa na tabia mbaya kama hii, ni kitu gani sikupi Naomi wangu eeh!!, ni wakati gani unanihitaji na usinione, huko unapoenda wanakupa nini kikubwa hicho niambie kama ni uhai wangu uchukue basi, niambie Naomi usiogope, jamii inaamini nimepotea njia lakini ni wewe macho yamekuona na moyo ukakupokea kikamilifu bila wasiwasi wowote,sasa kwa nini unitese hivi kwa nini unafurahia mimi kulia kila wakati, unapata raha kiasi gani kulewa na kuja nyumbani usiku, mbona hauheshimu pete yako hapo kidoleni, wewe ni mke wa mtu Naomi tambua hilo jaribu kusahau maisha yako ya zamani mpenzi wangu, nakupenda sana unajua, nafanya kazi kwa bidii kwa sababu yako na watoto wetu tutakaowazaa sina mama sina baba wewe ndiye baba na mama yangu katika hii dunia nipende japo kidogo tu hata kwa kujilazimisha Naomi na taratibu utazoea na utanipenda, na hata siku moja sitajisikia aibu kuwa na wewe" Yalikuwa maneno makali yaliyojaa simanzi kutoka kwa kijana Walter ama Dj kama wengi walivyomzoea, kwenda kwa mke wake wa ndoa Naomi Holela huku machozi yakimtoka kwa wingi sana, ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mkewe (Naomi). Ukumbi ulikuwa kimya, ni sauti hii pekee iliyopasua anga na kuyafikia masikio ya mwanamke ambaye hakushangazwa na maneno yale. Labda kwa sababu haikuwa mara ya kwanza kuyasikia ama la alikuwa hamuelewi mumewe. Hakuna aliyejua.
Naomi alikuwa amefika eneo la tukio katika ukumbi wa New Afrikasana majira ya saa saba usiku tofauti na saa mbili kama alivyotarajiwa, pale ukumbini ambapo mwanzoni walikuwepo wageni waalikwa wapatao sitini sasa alikuwa amebaki Walter na mlinzi wa ukumbi huo,Walter alimpokea Naomi kama mgeni wa heshima sana pale ukumbini kama mtu aliyekuja katika wakati muafaka, Naomi tayari alikuwa amelewa chakari jambo hilo Walter hakulijali alichofurahia ni kumuona Naomi machoni pake tena.
"Nipeleke nyumbani nikalale" ndilo jibu alilotoa Naomi baada ya kuyasikiliza maneno mengi ya Walter, maneno ambayo yalikuwa kama ngonjera zisizokuwa na mvuto mbele yake, wakati huo mlinzi ndio alikuwa amegeuzwa 'camera man' ukumbi ulikuwa umepooza sana.
"Kula basi japo keki kidogo halafu uzime mishumaa malkia wangu. Fanya hivyo kwa ajiri yangu nakuomba" alibembeleza Dj, kwa sauti tulivu sana.
"Na bia ziko wapi, panga hapo bia 28 ninywe nimalize ndio miaka yangu hiyo" alijibu Naomi na kumfadhaisha sana Dj.
“Naomi.” Aliita Walter kisha akaendelea, “hata uninyanyase vipi mimi nakupenda" alijikuta akijibu kwa ghadhabu kiasi flani kijana huyu ambaye pesa haikuwa na thamani kwake bali upendo kwa binti huyu.

Pesa yote ya maandalizi aliyotumia Walter kwa ajili ya Naomi ambaye ni mke wake aliyekuwa anasheherekea kutimiza miaka ishirini na nane (28), ikawa imepotelea hewani na hata dakika moja hakukumbuka kuiwaza wakati amemshika bega Naomi wakitoka ukumbini pale. Alikuwa na amani tele kila awapo na mwanamke huyu ambaye aliichukiza jamii nayo jamii ikamchukia haswaa. Lakini kasoro mwanaume mmoja tu. Walter.
Huyu alimpenda vile alivyo. Hakujali.
"Naomi unajua unapendwa sana na watu mke wangu, yaani walikuwa wamekuja wageni zaidi ya mia moja kwenye sherehe yako na wengine walikuwa wanazidi kumiminika, unapendwa mke wangu hadi nimeona wivu" Walter alimpamba mkewe na sifa za uongo ili mradi tu apate kumfurahisha na kujiona yeye ni mtu fulani katika jamii. Sasa walikuwa wanaliendea gari waweze kuondoka
"Wamekuja hao wote kunishangaa mimi?"Aliuliza Naomi kama mtu ambaye ameguswa.
"Ndio mke wangu! Yaani wote kwa ajili yako, nakwambia nimesikia wivu natamani ningependwa hivyo mimi"
"Waambie hivi waende kushangaa makaburini maiti anapandwa lakini haoti wasinishangae mimi bwana na kama ningewakuta ningewaeleza kwa mdomo wangu, ushamba tu!!" alijibu kwa jeuri na nyodo kitu ambacho Dj hakukitegemea lakini alicheka kuonyesha kuwa hajakwazika hata kidogo, moyoni alihisi ametekenywa na kitu kilichokuwa na ladha mbaya inayokera, harufu kali ya pombe nayo ilimuumiza kwa sababu hakuwa mtumiaji lakini hata hakuziba pua wala kukunja sura alitabasamu muda wote hadi wanafika nyumbani.
Kama mtoto mdogo vile Naomi alivuliwa nguo, viatu, heleni,wigi alilokuwa amevaa, bangili pamoja na kucha za bandia akiwa hoi kitandani.
Kisha Dj akajiweka pembeni yake wakalala.
"Naamini ni huyu uliyenichagulia na ni mimi wa kuishi nae sijapotea njia na kama nimepotea nirekebishe baba" aliomba ombi fupi kisha akaivuta shuka kajifunika na kuanza kuutafuta usingizi.
Hatimaye akalala.
Naomi alikuwa anakoroma!!!

* * * *

Miaka 18 iliyopita ndio ilikuwa mara yao ya kwanza na ya mwisho kuwa pamoja kabla ya kukutana tena ukubwani walipowekeana uchumba na hatimaye ndoa.
Familia zao zilikuwa hazifanani lakini wao walifanana, Naomi alikuwa anatoka familia ya kimaskini sana huku Walter akiwa anatokea kwa matajiri.
Walter alizoea sana kucheza na Naomi hata wazazi wake walitambua hilo, alikuwepo dada yake lakini Naomi ndiye alikuwa mambo yote hasa hasa kutokana na kulandana kiumri. Walter na Naomi walikuwa wakiachana miaka miwili
Alichokula Walter kikabaki alihifadhi kwa ajili ya Naomi, iwe biskuti, sambusa, Piza, na chochote kile alichodhani na Naomi kitampendeza.
Hakuna mtoto wa uswahilini aliyeruhusiwa kupenya geti la akina Walter tofauti na Naomi mtoto wa fundi baiskeli mzee Holela na mama mchoma vitumbua Mama Mashimi. Ilikuwa kama bahati kwa mtoto huyu wa kimaskini kupata nafasi hiyo ya kipekee, nafasi ya kwenda kuwatishia wenzake mtaani juu ya ufahari wa hali ya juu katika nyumba hiyo iliyokuwa maeneo ya Magomeni jijini Dar es salaam.
Wazazi wake Walter Bwana Andrew na Bi. Magreth walikuwa na hofu ya mtoto wao kufundishwa tabia mbaya ndio maana hawakutaka achangamane na watoto wa kimaskini, walijaribu kwa kila hali kuzuia hilo lakini juhudi na upendo aliokuwa nao bibi yake Walter kwa mjukuu wake huyo ulizidi amri za wazazi wake.
"Mwacheni mke wa mjukuu wangu tena msimkasirishe mume wangu kabisa asije akaniacha!!" ndivyo ajuza huyu wa miaka 70 alivyojenga mazoea makubwa ya wawili hawa, michezo yote ya uswahilini asiyoijua Walter alifundishwa na Naomi kivitendo kombolela, ukuti wa mnazi, kidali po, kujipikilisha na hatimaye kibaba na mama, alipata raha sana Walter kwa uwepo wa Naomi. Alijisikia fahari kujifunza matukio yanayotokea nje ya geti. Mambo yanayotokea katika dunia nyingine ambayo ni tofauti yao.

** * *


Ajali mbaya ya gari iliyotokea Tinde karibu kabisa na mji wa Kahama ilihusisha vifo vya watu watatu palepale.
Ilikuwa sio ajali ya kutupia jicho mara mbili, gari dogo lililokuwa linaingia barabarani linakutana uso kwa uso na lori kubwa aina ya Scania likiwa limepotea njia na kuiviringisha chini ya uvungu wake, ilikuwa vigumu kuamini kuwa gari ndogo aina ya starlet ilikuwa mpya mwezi mmoja uliopita.
Haikuhitaji kutumia taaluma uliyojifunza darasani kuweza kupata jibu kwamba wahusika ndani ya gari dogo tayari ni maiti kwa jinsi gari yao ilivyopondwa pondwa, ingekuwa ni filamu wangeweza kupona lakini kwa hali halisi kile ni kifo, mwendesha baiskeli aliyegongwa na lile lori alifahamika haraka kwa sababu alirushwa pembezoni mwa barabara na kutua juu ya jiwe alipopoteza maisha palepale bila kutoa hata neno moja la kutangaza urithi wa hiyo baiskeli iliyopona. Na wale waliokuwa ndani ya gari dogo hawakuwa na lolote la kusema, hawakupata muda wa kuhadithia maumivu waliyoyapata kabla ya kukata roho. Mashahidi pekee walikuwa ni wale wamiliki wa gari kubwa, hao ndio wangeweza kuigiza vilio vya uchungu vilivyotolewa na wahusika chini ya uvungu kabla ya mauti kuwachukua lakini hata wao hawakuwa na la kusema kwani walikuwa katika harakati za kumkwepa Israel asizitwae roho zao.
Simulizi ya safari hiyo ikabadilika, ghafla ikawa ya kuvutia mashabiki wakaongezeka barabarani kuja kuwa mashahidi wa nini kimetokea, hapakuwa na kingilio kutazama tukio hili lililotokea majira ya jioni.

* * *
Maandalizi ya safari yao hayakuwa makubwa sana, waliamini ilikuwa safari fupi ya kwenda leo na kurudi baada ya siku mbili, hawakuaga watu wengi tofauti na familia yao na hawakupata fursa ya kumuaga mtoto wao mdogo (Walter) kwani muda huo alikuwa bize anacheza michezo ya kitoto na rafiki yake.
Walikuwa ni Bw. na Bibi Andrew wazazi wa Walter, katika safari yao ya kwenda mji wa Kahama wilayani Shinyanga ambapo Bw. Andrew alikuwa anaenda kwa dhumuni la kuchukua ruhusa kazini kwake 'Kahama Gold Mines' ruhusa ya wiki mbili ambapo alitarajia kusafiri yeye na familia yake kwenda Moshi alipozaliwa kwa mapumziko mafupi na kuwasabahi wazazi wake.
Safari ya kwenda ilikuwa ndefu na yenye furaha mtu na mume wake walipiga domo mwanzo hadi mwisho wa safari mama Maureen ndiye alikuwa muongeaji mkuu baba Maureen akawa anafuatisha, aidha kwa kucheka, kuguna au kutikisa kichwa, lakini safari yao ya kurudi ilikuwa fupi lakini ndefu sana kwani licha ya gari yao kuishia kwenye tairi za Scania huo haukuwa mwisho wa safari wao walisafiri zaidi hadi mbinguni na kusema kwaheri katika uso wa dunia. Wakawa wamewahi kupanga foleni ya masisha mengine.
Zawadi walizokuwa wamewachukulia watoto wao, zikachanganyikana na damu zao pamoja na vipande vya mabati ya gari halafu wakaungana na petroli iliyokuwa imesalia katika tangi lililokuwa limepasuka.
Bwana na bibi Andrew wakaishia kuwa chakula cha barabara.
Miili yao ilibondeka vibaya lakini gari waliyokuwa wanatumia ndio iliwawezesha wanausalama kutambua wahusika wa ajali hiyo.
Taarifa kama upepo zikasambaa nchini kote kupitia vyombo vya habari na katika jumba la marehemu zilifika haraka sana, mtoto wao mkubwa (Maureen) ndiye alipokea simu ya mezani taarifa aliyopewa iliupasua moyo wake kwa mshtuko mkali ambao bibi yake aliutambua pale alipomwona anaachia mkonga wa simu unaanguka chini
"Umekuwaje we mtoto" bibi yake alimuuliza
"Baba na mama wametutoka" alijibu Maureen huku akiwa amesahau kuwa bibi yake ana presha ya kushuka, wakati anazidi kuishiwa nguvu akidhani bibi yake ndiye atamdaka, palepale bibi kama mtu mwenye mapepo alidondoka kwenye vigae pale sebuleni huku kisogo kikitangulia, Maureen alishuhudia damu ilivyotapakaa pale sebuleni lakini mwili haukuwa na nguvu hata chembe, kiungo pekee kilichofanya kazi ni macho.
Bibi, baba ,na mama ndani ya masaa machache wametoweka duniani.
Ni kwa mwanadamu gani anaweza kukabiliana na huzuni hii!!!
Walter kama kawaida shule wakiwa wamefunga basi mida yote yeye na Naomi, Naomi na yeye.
"Nikalete Juisi tunywe eti mama!" Walter alimwambia Naomi walipokuwa wakicheza kibaba na mama, Naomi kwa ishara ya kutikisa kichwa alikubali, Walter ambaye katika mchezo huo alikuwa baba akaondoka kwenda sebuleni.
Japokuwa alikuwa mtoto mdogo alijua maana ya damu aliyoishuhudia kutoka kwa bibi yake na hali aliyokuwa nayo dada yake (Maureen), filamu kadhaa alizokuwa amewahi kuangalia ziliamsha hisia ya uoga.
"Naomiiiii" alipiga kelele kuu, ndani ya dakika moja Naomi akawa amewasili tayari eneo lile
"Mamaaa" naye akapiga kelele mbiombio mtoto wa Kiswahili akaenda nje ambapo alimweleza mlinzi wa getini kilichotokea, sigara aliyokuwa nayo mdomoni ikaanguka naye bila kujibu kitu akatimua mbio kuingia ndani, alichoambiwa ndio hicho kilichokuwa kinatokea kweli sebuleni, alimkuta Walter anamtikisa dada yake huku akilitaja jina lake kwa sauti ya kukata tamaa.
Kwa bibi mlinzi hakuwa na sababu ya kusubiri daktari ampime ndo aujue ukweli, kwani tayari alikuwa maiti swali lilibakia kwa Maureen aliyekuwa amekodoa macho lakini haongei lolote lile.
Mlinzi alijaribu kupiga simu zote za mabosi wake lakini hazikupatikana katu. Akiwa hana hata senti tano mfukoni baada ya kutoa shilingi mia aliyokuwa nayo kununua sigara, mlinzi alihisi kuchanganyikiwa akili, breki za gari zikiambatana na honi kali zilirejesha matumaini, akatambua kuwa ni bosi wake amekuja.
Mungu wangu sijui namuelezaje!!! Aliwaza mlinzi kabla ya kwenda mlangoni.
“Atakuwa ni nani huyo??” Mlinzi alimuuliza Naomi, lakini hakusubiri jibu kwani aliamini alikuwa amekosea kuuliza.
Tofauti na alivyodhani kuwa huyo alikuwa ni bosi wake. La hakuwa yeye alikuwa mtu mgeni sana machoni pake, aliingia mbiombio bila hata kukaribishwa.
"Shkamoo bamdogo"Alisalimia Walter lakini hakupata jibu bwana yule tayari alikuwa amembeba juu juu Maureen na kumpakiza kwenye gari kisha akataka kuondoka mlinzi akaweka ngumu.
"Huyo ni bamdogo Frank" Walter akamwambia.
Huyo alikuwa ni mdogo wake bwana Andrew, ambaye ubize wake nje ya nchi ulisababisha yeye na kaka yake waonane ofisini na zaidi ya hapo kwa njia ya simu.
Madhara ya Sayansi na teknolojia!!!

* * * *
Mshtuko alioupata Maureen kushuhudia bibi yake akikata roho na taarifa ya vifo vya wazazi wake wote wawili ilimsababishia matatizo makubwa ya akili ambayo daktari aliyaita mtindio wa ubongo. Dalili za kupona zilikuwepo japo kwa taratibu sana. Daktari hakuweza kutoa wakati sahihi bali aliwatia moyo ndugu hawa wa mgonjwa.
Wakiwa hawana ndugu mwingine Tanzania Maureen na Walter walichukuliwa na Frank ambaye ni mdogo wake baba yao, ni huyu ambaye alipewa taarifa mapema kwa njia ya simu kutokea eneo la tukio, namba yake pamoja na ile ya nyumbani zilikuwa baadhi ya namba zilizohifadhiwa katika kijitabu cha kumbukumbu cha bwana Andrew.
Maisha ya Tanzania yalisababisha Walter kuwakumbuka wazazi wake kila siku hali ya dada yake pia ilichangia kumfadhaisha mtoto huyu. Maziko ya watu watatu muhimu katika maisha yake, yaani Bibi, Baba na mama lilikuwa tatizo kubwa sana.
Makaburi ya Kinondoni yakawa yamemeza miili hii mitatu kwa pamoja.
Mama mkwe, mkwelima wake pamoja na mwanae wa kumzaa.
Kila mwenye damu na moyo wa nyama alitikiswa na tukio hili. Kilio cha kitoto japo chenye uchungu mkubwa kutoka kwa Walter kiliwaliza kina mama wengi, huku Maureen na mtindio wa Ubongo aliokuwa ameupata ukiamsha hisia kali.
Frank akawa ameubeba rasmi kwa moyo mmoja mzigo huu!!

*****
Kwa kutumia busara zake Frank aliamua kumtafutia Walter shule nchini Uganda na kumkabidhi kwa rafiki yake aliyeitwa Muganyizi ama kwa kifupi Muga ambaye kazi yake kubwa ilikuwa kuandaa muziki, aliishi peke yake kwenye nyumba yake baada ya mkewe kuuawa kwenye vurugu za uchaguzi nchi jirani ya Kenya.
Hakuwa na kipingamizi cha kukaa na mtoto Walter alichofanya ni kumtafuta binti atakayekuwa anamhudumia Walter kwani yeye mara kwa mara alikuwa anabanwa na shughuli zake ambazo hazikuwa na siku maalum.
Japokuwa alikuwa mtoto safari ya kwenda Uganda kwake ilikuwa mwisho wa kucheza na Naomi wake, hakupata hata fursa ya kumwambia kwaheri rafiki huyu wa dhati na hata angemwambia je angemwambia ni wapi anaenda??
Walter aliumia sana na hakuwa na la kufanya akafuata maelekezo aliyopewa na baba yake huyo.
"Bye da Maureen" Walter alimwaga dada yake ambaye alikuwa hatambui lolote lile pale alipo akili yake haikuwa vizuri tena, alikuwa ni mtu wa kukaa tuu, haongei bali anaunguruma, hacheki bali kupiga kelele hayo ndiyo maisha yake yalivyokuwa na elimu yake ya kidato cha tatu ikaishia hapo katika hali ya kusikitisha. Maureen akawa ameurudia utoto akawa mtu wa kuhudumiwa kwa kila kitu!!
Maureen hakujibu kitu Frank akamshika mkono Walter wakaondoka wakimwacha Maureen na msaidizi wa kazi pale ndani.



* * * *
Basi la Akamba liliwasili jijini Kampala nchini Uganda majira ya saa tano asubuhi siku iliyofuata Muga alikuwepo kituo cha mabasi kuwapokea wageni wake hao wawili. Frank na Walter
"Saluuut!!"
"Saluuut!!" walipeana salamu maswahiba hawa wa siku nying huku Walter akishangazwa na salamu hiyo.
"Do he speaks swahili?(Anazungumza kiswahili?)" Walter alimuuliza Frank ili aweze kumsalimia Muga. Frank akamjibu kwa kumwonyesha dole gumba.
"Shkamoo" alisalimia baada ya kupewa jibu hilo. Muganyizi akaitikia huku akimpapasa kichwani mtoto huyu ambaye alionekana kuwa katika uchangamfu mdogo sana.
Baada ya stori mbili tatu,walichukua taksi iliyowapeleka hadi nyumbani kwa Muga. Hapakuwa mbali sana, nyumba ya Muga ilikuwa maeneo ya karibu kabisa na katikati ya jiji.
"Afadhali nyumba yangu itachangamka kidogo" Muga alimwambia Frank ambaye alikaa hapo siku tatu kisha akarejea Dar-es-salaam Tanzania. Siku hiyo walter aliiona kama siku nyingine tena ya kutengwa na ulimwengu kisha kuhamishiwa sayari nyingine.
Hakuwa na lolote la kufanya alikubaliana na hali. Akampungia mkono Frank. Kama alivyopunga kwa dada yake wakati wakiiacha ardhi ya Tanzania.
Maisha mapya yakaanza.
Ilimgharimu Walter majuma kadhaa kuzoea ile hali ya kuwa nchi ya kigeni lakini alipozoeana na msichana wa kazi alianza kujiona kama yupo na dada yake (Maureen). Pia vifaa vya muziki alivyokuwa anafundishwa kutumia na Muga ambaye alipenda kumwita anko vilimsaidia kupoteza mawazo na kupata furaha tele.
"Utakuwa mwanamuziki siku moja akili yako inakariri upesi, sio kama wengine wagumu sana kuelewa"Anko Muga alimwambia Walter siku alipomkuta anapiga gitaa kwa ufasaha kama mzoefu kabisa. Alikuwa akipiga huku akiimba wimbo wa ‘Tanzania nchi yangu nakupenda’. Wimbo alioukariri vyema baada ya Naomi kuwa anapenda kuuimba.
Walter hakujua nini Muga anamaanisha.
Akatabasamu.
* * * * *
Wakati Walter akipiga gitaa na kuimba nchini Uganda. Katika ardhi ya Tanzania katika jiji la Dar es salaam yule binti ambaye alimfundisha na kumkaririsha na kisha kumfanya aupende wimbo ule alikuwa katika hali tete.
Afya ya Naomi ikaanza kuyumbayumba, vyakula vyenye virutubisho vya kutosha kutoka katika jumba la kifahari la akina Walter, havikuwepo tena.
Enzi za kula mihogo ya kukaangwa, kachumbari na maji ilirejea huku utaratibu wa kulalia ugali na dagaa wa mafungu kila siku ukidumishwa, ni hayo maisha yaliyomsukuma Naomi kulilia kwenda kwa dada yake anayeishi maeneo ya Buguruni Malapa ambapo aliamini kuna unafuu kidogo kwa dada huyo aishiye peke yake katika kijumba cha chumba kimoja na sebule uswahilini kabisa, mama yake hakuwa na kipingamizi, kwanza kuondoka kwake ni sawa sawa na kuvuja kwa pakacha nafuu kwa mchukuzi. Hata matumizi yangepungua pale nyumbani.
Naomi akaondoka rasmi
"Maskini Walter angekuwepo ningeenda pale nibonyeze kengele halafu angenifungulia tucheze wote pale kwenye bustani yao." Naomi alijiongelea huku akitazama jumba lao Walter lilivyopooza.
"Hebu angalia mbele, ukijikwaa umlilie nani?" alishtushwa na sauti kali ya mama yake, walikuwa wanaelekea stendi kupanda gari za kwenda Buguruni.
Walizifikia gari, mama akamlipa kondakta pesa yake. Naomi akachukua siti.
Maisha ya dada yake yalikuwa bora tofauti na shughuli anazozifanya, nyumba yake ya chumba kimoja na sebule ilikuwa imebanana, kabati, jokofu, luninga kubwa, sofa, na vikorokoro vingine vingi vilivyodhihirisha kuwa chumba kimezidiwa ujazo na samani zilizomo. Kazi ya kuuza barafu na mihogo katika shule za msingi jirani na Bungoni haikutosha kwa maendeleo hayo.
Hali hiyo ilimfurahisha sana Naomi ambaye hadi wakati huo hata wazo la kwamba siku moja ataenda shule halikuwepo na wala hakutamani kwenda shule akili yake yote ilikuwa kuangalia mikanda mingi ya video iliyokuwa pale kwa dada yake pamoja na kula barafu zinazopasukia kwenye Jokofu.
Maelewano baina yake na dada yake yalikuwa mazuri mno kwani ni huyo dada aliyemlea tangu akiwa mdogo hivyo kwake huyu alikuwa kama mama. Kila aina ya filamu alikuwa akiangalia wakati dada yake hayupo, bila kujali maadili ndani yake.
Chumba chake cha kulala ilikuwa ni ile sebule kwenye sofa kubwa, kamwili kake kadogo kalitosha kabisa pale bila usumbufu, kila usiku kwa jicho lake au kwa masikio yake aliweza kuona au kusikia mwanaume chumbani kwa dada yake, utoto wake ulikuwa unamtuma kuchungulia kupitia upenyo wa kitasa cha mlangoni, alichofanyiwa dada yake kilikuwa sawa na anachokishuhudia kwenye baadh ya filamu pale nyumbani. Mara kadhaa alishuhudia dada yake ambaye kila usiku alirudi akiwa amelewa, akimkaba mwanaume kwa madai ya kulipwa pesa yake, dada yake alikuwa changudoa tena mzoefu na mlevi pia. Biashara ya kuuza barafu ilikuwa ni kwa mchana tu. Tena kwa sababu asingeweza kupiga uchangudoa mchana kweupe mbele ya watu wanaomtambua.
Naomi akajifunza kuvaa hovyo kama dada yake. Mara akajifunza kujipodoa kama dada yake. Maskini Naomi hakuwepo wa kumkanya.
Ule msemo maarufu jijini Dar kwamba ‘mtoto mtoto wako, mtoto wa mwenzio si wako’ ukachukua nafasi ya kumpa uhuru. Nani angemkanya?? Tabia yake ya kujaribu vitu ikahamia kwenye pombe, masalia ya kwenye chupa ye anakunywa, baadae watoto watukutu waliokulia palepale Buguruni na kushuhudia uchafu wa wasichana kadhaa wa pale buguruni wakaanza kufanya nae alichokiona kwenye luninga, kwa kuwa hakujua madhara yake akafanya tabia hiyo ni kama mchezo mzuri. Dada akiwa anauza barafu yeye anakimbilia kwa akina Juma ambaye mama yake ni mwalimu wa shule ya msingi, wanavuana nguo na kujifunika shuka. Naomi na akili yake ya kuelewa upesi akawa anakalili hadi sauti zinazotolewa katika picha chafu za ngono alizokuwa akitazama. Huu sasa haukuwa utoto, ilibadilika na kuwa mazoea. Nani atamkanya mtoto huyu?? Nani atasimama na kumwadhibu iwapo atarudia tena kosa hilo? Hakuwepo. Hakika hakuwepo.
Taratibu akakua na hiyo tabia mwaka mmoja baada ya mwingine, Juma asipokuwepo alienda kwa Samson, mara kwa Kassim, wote aliwaigizia zile sauti. Mara Fred mwenye umri mkubwa kabisa naye akajikuta anavutiwa na Naomi.
Akajiweka na yeye, mwanzoni kama utani. Anampa shilingi mia, mara mia tano, siku nyingine anamnunulia chakula.
Siku moja akamkaribisha kwake.
Akafanya naye mapenzi. Naomi akaiacha bikra yake akiwa na miaka kumi na moja.
Safari yake isiyopendeza kusimulia ikaanzia hapa. Akaachana na vile vitoto alivyokuwa anajifunika navyo shuka kisha kulia sauti za ajabu bila kufanya lolote. Sasa akajiona mtu mzima.
Umbo lake likamdanganya kwa jinsi lilivyotanuka upesi, sasa akajiona yu mtu mzima baada ya miaka kadhaa.
Kitu kupenda hakukijua maishani Naomi akawa malaya anayemvulia mwanaume yeyote kwa kiasi kidogo cha pesa kwa sababu hakuwa mrembo sana. Hakuzijua kanuni za uchangudoa. Uwe na mpira ama usiwe nao. Twende kazi.
Kwa kila mwenye moyo wa nyama aliulaani umasikini.
Umasikini uliowasukuma watoto wadogo katika biashara hii haramu.
Lakini nani ataupiga kikumbo umasikini ili akina dada wasidumbukie katika domo hili la mamba mwenye njaa??
Hakuwepo.
* * * * *
Gharama za kumtunza Maureen zilikuwa kubwa mno, ilimlazimu Frank kupangisha nyumba iliyoachwa na wazazi wake Walter ili kukimu mahitaji ya Maureen ambaye madaktari walidai tatizo lake litapona taratibu na miaka ilikuwa inakatika bila matumaini kuonekana, kamwe Frank hakuchoka kumpenda Maureen. Ukarimu aliofanyiwa na marehemu bado aliukumbuka.
Wafanyakazi walikuwa wamebadilishwa hadi kufikia kumi ndani ya miaka mitatu wengi wao walichoka kumuhudumia Maureen aliyekuwa hajitambui hata kidogo, udenda ulimmwagika mrembo huyu wa zamani kabla ya kupatwa na matatizo yale ya ghafla na mara nyingine kuleta vurugu hadi kuwaponda na kitu chochote wafanyakazi hao, hali hiyo iliwaogofya wengi na kukimbia kazi kuliko kujeruhiwa, Frank hakukata tamaa kwa moyo mmoja aliendelea kuwatafuta wafanyakazi wengine.
Kila Frank alipomtazama Maureen akiwa katika hali ya kutojielewa alisema kauli moja tu. Kauli iliyompa nguvu ya kusimama na kuendelea tena mbele.
“Mungu wangu, ni wewe pekee unayejua sababu ya kwa nini huyu mtoto yuko hivi na kwa nini huu mzigo nimeubeba mimi. Nionyeshe njia eeh baba.”
* * * *

Miaka ilikuwa imekatika na hali ya hewa ya Uganda ilikuwa imemkubali Walter sasa na tayari alikuwa na marafiki. Alichangamka sana na aliweza kuongea maneno mawili matatu ya kiganda, baada ya kuwa ameanza kwenda shuleni, ni miaka mitatu sasa ilikuwa umepita, uelewa wake darasani ulikuwa wa chini mno, jambo hilo halikumshangaza anko Muga kwani katika maisha yake aliamini, mtu akiyashindwa ya darasani basi yapo ya mtaani anayoyaweza sana. Hivyo alijaribu kwa jitihada zote kumtafutia waalimu wa kumfundisha masomo ya ziada ili walau asiwe mbumbumbu sana, kidogo hilo lilisaidia japo sio sana.
Walter alipendelea kusikiliza na kuchezea vifaa vya muziki alivyozoeshwa tangu anafika hapo Uganda.Ulikuwa ni utaratibu uliowekwa kuwa Kila mwisho wa mwaka Walter alirejea Dar es salaam Tanzania kumsabahi dada yake (Maureen) lakini taratibu alivyonogewa na jiji Walter akapunguza kurudi Tanzania, japo mapenzi kwa dada yake hata kidogo hayakupungua alipozungumza na Frank alimwomba amwekee simu Maureen, kelele alizopiga dada yake huyu asiyeweza kusema vyema wala kukaa akatulia zilikuwa salamu tosha kwake. Japo kila mara zilimtoa machozi. Hakuamini kuwa ipo siku Maureen angeweza kuongea tena kama zamani.
Alipotimiza umri wa miaka 19 tayari jiji la kampala lilikuwa limetambua kipaji chake toka moyoni jina lake la Walter Andrew, likabadilika kuwa Dj Walter.
Kwa kiwango cha juu sana Walter ambaye aliacha shule akiwa na miaka 12 alikuwa mtaalam wa kuchanganya mziki, redio ya taifa ya Kenya ilikuwa inamuhtaji lakini malipo aliyokuwa anayapata katika kumbi kubwa za starehe pale Kampala yalikuwa makubwa na ya kuridhisha sana, hivyo hakuona haja ya kwenda Kenya kuhangaika kuizoea tena hali ya hewa ya kule.
"Baada ya miaka miwili nitakuwa na pesa za kutosha nitampeleka da Maureen kutibiwa nchi za nje, asante Mungu kwa kipaji hiki" Alijiwazia Walter siku moja akiwa anahesabu malipo yake.
Maisha yakaanza kubadilika.
* * * * *
Dada yake Naomi alikuwa amejiridhisha kabisa kwa mkondo ambao mdogo wake alikuwa ameufuata. Lakini hali ya Naomi kuendelea kuishi naye ikaanza kuwa kero, hakutaka kumweleza moja kwa moja lakini akapata pa kuanzia.
"Naomi mdogo wangu, kuna dume langu moja limekupatia kazi ya ndani huko Tabata Aroma, usilaze damu amesema wanalipa vizuri kweli" Dada yake Naomi alikuwa akimwambia mdogo wake ambaye hadi umri wake wa miaka 21 na biashara yake ya ukahaba alikuwa hajapata hata nyumba ya kupanga. Kila alipohamia dada yake naye alimfuata. Tayari walikuwa wamemzika mama yao aliyekufa miaka miwili nyuma kwa saratani ya matiti.
"Ah! dada mi makazi ya ndani tena wapi na wapi sitaki bwanae ingekuwa ofisini hapo sawa!"Alijibu kwa jeuri huku amevuta mdomo wake, maskini Naomi anataka ofisi wakati hajui hata maji kwa kiingereza yanaitwaje, na hata jina lake kuliandika ilikuwa tabu sana.
Wasichana wana mambo.
"Mdogo wangu pale ni pa kuzugia tu, unapata pesa yako unapanga kachumba kako kazi inaendelea tena kwa raha zako, tena ukiwa na kwako midume unaitega kweli inatoa pesa nyingi. Sio kama sa’hivi" alijazwa maneno Naomi, yakamwingia kichwani akakubali kwenda kufanya kazi hiyo.
Siku iliyofuata, Naomi akapelekwa hapo Tabata, ilikuwa nyumba nzuri iliyovutia tangu nje, hapakuwa na kelele kumaanisha kuwa hakuna watoto na kama wapo basi wamelala. Naomi akaikumbuka nyumba ya utotoni kwa akina Walter.
"Karibuni sana, karibu dada....dada nani vile" mwenyeji wao aliyekuwa mchangamfu kabisa aliwalaki wageni wake.
"Naitwa Naomi" alijibu Naomi huku akin'gata vidole vyake, sketi yake ndefu aliyovaa ilimfanya aonekane mshamba sana na ungeweza kuhisi ametoka kijijini wiki moja iliyopita. Hii ni janja inayotumiwa na watoto wa mjini kuwalaghai waajiri wao.
Jitihada za kutafuta wasaidizi wa kazi za ndani yeye mwenyewe zilikuwa zimegonga mwamba Frank aliwaomba rafiki zake wamsaidie na ndani ya siku mbili alikuwa amepata msichana wa kazi tayari.
Sasa yupo naye anampa maelekezo ya awali kabisa
"Mimi naitwa Frank" na mwenyeji aliyewapokea akajitambulisha kwa Naomi. Baada ya kuingia sebuleni, sebule kubwa na ya kisasa walipata juisi ya nanasi na vipande vya keki,halafu maelekezo ndani ya kile chumba yakafuata
"Mbona kama ninamjua vile huyu mkaka, nimemwona wapi?" alijiuliza Naomi huku akimsoma Frank kwa jicho la wizi.
"Au amewahi kuninunua? ndio huenda amewahi kuninunua" alijipa jibu Naomi na kuendelea kupokea maelekezo yote huku akizungushwa kuyaona maeneo ya jumba hilo
"Huyu anaitwa Maureen, ni mdogo wangu amepatwa tatizo kidogo anahtaji kuhudumiwa kwa ukaribu sana, hana matatizo utamzoea taratibu" alitoa maelezo Frank walipofika katika chumba cha Maureen.
Kwa mara ya kwanza Frank anashuhudia Maureen anatoa tabasamu la kweli mbele ya Naomi. Maajabu makubwa. Lakini Frank hakusema neno.
"Huyu n’do yule Maureen wao Walter au? hapana hawezi kuwa huyu, yule alikuwa mnene sana..halafu…haiwezekani wala sio yeye."Alijiuliza na kupata jibu tena. Mambo mengi aliyoyapitia Naomi yalikuwa yameivuruga kumbukumbu yake sana, hakuweza kuwakumbuka Frank na Maureen kiuhakika sana.
Kinyume na Frank alivyotarajia kuwa Naomi atashtushwa na kuishi na Maureen lakini hata hakuuliza swali zaidi ya kumshika shavu Maureen aliyekuwa amekaa kitandani. Akiimba mashairi yasiyoeleweka.
Kazi ikaanza rasmi.
Tofauti kubwa ilikuja ndani ya nyumba yake, alikuwa anasubiri huenda Maureen atamsumbua Naomi lakini haikutokea, tofauti na wafanyakazi wengine, Naomi alikuwa akicheza na Maureen kwa furaha. Na kinyume na miezi miwili ya kufanya kazi pale aliyokuwa amepanga ilipitiliza na kuwa sita hatimaye mwaka hata dada yake alishangazwa sana na uamuzi huo. Afya ya Maureen ilikuwa njema, taratibu akaanza kula mwenyewe na mdomoni mwake kila swali aliloulizwa alijibu Naomi. Ilikuwa furaha kubwa kwa Frank, kwani sasa aliweza kufanya biashara zake na hata kusafiri pia aliweza.
"Naomi dada yangu, ninakuongezea mshahara mara mbili badala ya laki moja itakuwa laki mbili" Frank alimwambia Naomi siku moja wakiwa mezani wanakula. Kwa furaha Naomi alimkumbatia Maureen aliyekuwa pembeni yake.
"Asante sana kaka Frank" alishukuru Naomi.
“Dada Naomiii” Maureen naye aliita kwa tabu tabu. Wote wakamtazama wakatabasamu.
Haya yalikuwa maajabu.
Taarifa za kupata nafuu kwa Maureen zilipokelewa kwa shangwe sana na kaka yake (Walter) aliyekuwa anaishi na kufanya kazi na anko Muga ambaye ni rafiki kipenzi cha baba yake mdogo (Frank) , alikuwa ni Walter aliyetuma pesa kwa ajili ya ongezeko la mshahara wa Naomi baada ya Frank kumsifia sana kwa jinsi alivyobadilisha maisha ya Maureen kuwa ya furaha sana.
Sasa Naomi akawa anapokea mara mbili.
* * * 
Tabia ikikaa kwenye damu kuibadili itakuchukua kipindi kirefu sana. Na iwapo itabadilika haitadumu itarejea tena.
Hali hii ilijitokeza pia kwa Naomi ambaye aliishi uchangudoa tangu utoto wake. Kisha akaanza kazi za ndani…lakini Naomi anabaki kuwa Naomi, na hili lilijidhihirisha usiku mmoja.

Ulikuwa ni usiku wa giza majira ya saa tano usiku akiwa ndani ya kisketi kifupi kinachouacha mwili wake uchi, kiblauzi saizi ya mtoto wa miaka saba kilifanikiwa kufunika sehemu ndogo ya kifua chake, miwani kubwa nyekundu ilifunika macho yake barabara. Alikuwa ni Naomi akitoweka katika jumba la kifahari la Frank, kwa nje alisubiriwa na gari nzuri ya kutembelea aina ya Toyota VX. Ndani ya nyumba alibaki Maureen peke yake aliyekuwa amelala tayari.
Alikuwa ni Jacob rafiki mpenzi wa Frank na mwanaume aliyemtafutia kazi ya ndani Naomi katika jumba lile la Frank. Ni huyo alikuwa amemlaghai Naomi watoke kwenda disco, ni kweli Naomi alikuwa amekosa sana burudani chafu alizozizoea siku zote, hakupata pombe kama alivyozoea na hakufanya ngono mara kwa mara.
Ni katika siku hii ambapo Frank alikuwa amesafiri kuelekea Mwanza ndipo Naomi na Jacob walitumia fursa hyo ya kipekee kwenda kujirusha. Tayari alikuwa ametanguliziwa shilingi elfu hamsini na baada ya huduma angepewa elfu hamsini nyingine, thamani ya Naomi ilikuwa imepanda sana hakuwa Naomi wa Buguruni wa kulipwa shiling mia tano hadi elfu moja kwa huduma, hakuwa Naomi wa kwenda na mtu kisa amemnunulia chakula au pombe, kwa sasa alikuwa mwingine, alikuwa na pesa yake nyingi tu aliyokuwa anavuna kwa kazi ya ndani aliyokuwa anafanya kwa Frank. Ukimtaka sharti uingie gharama.
Punde tu baada ya Maureen kupitiwa na usingizi Naomi alijipodoa hasahasa na kutoweka kwa mikogo kama mlimbwende anavyokatisha katika jukwaa mbele ya mashabiki wengi ambao anaamini wanamtazama maungo yake yanavyonesanesa.
Naomi akajituliza ndani ya gari alilokuja nalo Jacob.
Hakujua kama siku ya kufa nyani miti yote huteleza.
Likatokea tukio ambalo lilibadili kila kitu katika maisha yake.

Tumbo lilioanza kumuuma ghafla Maureen ndilo lilikatisha usingizi wake majira ya saa nane usiku.
"Dada Naomi, dada Naomi, Naomi" alianza kuita Maureen, ni jina hilo pekee aliloweza kutamka ipasavyo. Hakupata majibu yoyote, chumba kilikuwa kina giza nene, mvua kali ilikuwa inanyesha kwa fujo, tumbo lilivyozidi kuuma Maureen aliinuka pale kitandani huku akipapasa aliufikia mlango akafungua, giza lilitawala hadi nje, palikuwa hakuna mwanga hiyo ilidhihirisha kuwa hapakuwa na umeme tumbo lilizidi kuuma, Maureen akawa analia kwa uchungu sana huku ameshika tumbo lake kwa mkono mmoja na mwingine akipapasa kutafuta mlango mwingine wa kutoka nje aweze kutafuta msaada zaidi kama upo.
Mvua kali ya upepo ilimpokea alipoufungua mlango wa sebuleni ili atoke nje. Ndani ya dakika moja tayari alikuwa amelowana sana.
Hofu ikamkumba msichana huyu ambaye ndio kwanza alikuwa ameanza kuipata furaha ya maisha.
Upepo ukazidi kupuliza, sasa mvua ikawa inapiga na kuingia ndani.
Kilikuwa kizaazaa.
Tumbo lilivyozidi kukaba. Maureen akajiachia na kuanguka chini kama mzigo.
Maji yote ya mvua yaliyoingia ndani yakapitia kwake kwanza.
Binti akawa akakoroma huku haja zake akizikidhi palepale.
Hali ilikuwa mbaya.

* * * *

Kwa mwendo wa kuyumbayumba,Naomi alijikongoja kuingia ndani ya nyumba,kwa msaada wa simu yake ya tochi aliweza kukabiliana na giza lililokuwepo mbele yake. Licha ya kuwa na tochi bado Naomi alianguka mara mbili kutokana na utelezi ulioletwa na mvua,harufu aliyoanza kuihisi kwa mbali alihisi ni maharage yamemwagika,lakini uwazi wa mlango wa sebuleni ulimtia shaka.
Kadri alivyozid kusogea ndivyo harufu ilivyoongezeka. Pombe aliyokuwa amekunywa ilimwonyesha kitu alichoamini ni gunia pale mlangoni.
"Mshenzi gani ameweka gunia hapa mlangoni, hawataki nipite au?" kwa sauti ya kilevilevi alijisemea huku akizidi kusogea. Ghafla kitu alichoamini ni gunia kiliruka juu na kikatua kwa kishindo kikubwa. Hakuwa amepata ndimu na nyama choma ili pombe iliyokuwa kichwani ikatike, hakumbuki ni muda gani simu yake ilianguka chini lakini tayari ilikuwa kwenye maji.
Naomi hakuwa na pombe kichwani, akili zilikuwa timamu kabisa,alikuwa anatetemeka sio kwa baridi bali uoga mkubwa sana,alikuwa amekodoa macho macho yake, akili ilimruhusu kwenda mbele lakini miguu ikiwa mizito kama amevaa viatu vya chuma.Jasho likamtoka licha ya mvua iliyokuwa imenyesha.
* * * *


* * * *
Jeuri ya pesa aliyokuwa nayo ilimpelekea Dj Walter kufanya manunuzi ya bei ghali sana kwa fujo, alikuwa na furaha kubwa sana kurejea Tanzania kushehereke sikukuu za mwisho wa mwaka pamoja na familia yake. Lakini furaha yake kubwa ilikuwa maendeleo mazuri kiafya ya dada yake Maureen.
Gari yake mpya aina ya Land Cruiser Prado ilikuwa imechafuka kwa mapochopocho. Malipo mazuri aliyokuwa akilipwa yalimfanya Walter awe mmoja kati ya watu maarufu na wenye fedha nchini Uganda lakini hakulewa sifa aliendelea kuwa karibu na Anko Muga na sasa walikuwa naye ndani ya gari wakisafiri kwenda Tanzania. Walter alikuwa yupo kwenye usukani akipambanisha tairi za gari na ardhi kuelekea Tanzania.
Ilikuwa safari ndefu lakini yenye uhakika kutokana na ubora wa gari. Majira ya saa tano usiku mvua kali iliwapokea jijini Dar-es-salaam, Muga alishauri waende hivyohivyo hadi Tabata Aroma lakini Walter hakuafiki kutokana na uwepo wa bonde kubwa jirani na nyumba ya Frank ambalo hujaa maji na kuzuia magari kupita vyema. Walter alihofia kunasa na kushindwa kuifikisha ‘surprise’ nyumbani kwa Frank.
Royal in Hotel ndipo walipoamua kupumzika hadi asubuhi,Walter alikuwa wa kwanza kuamka kisha Muga. Wakati akiwa maliwatoni ndipo Muga naye alipoamka, wakajiandaa kwa hatua kisha wakaondoka kwa pamoja.
Majira ya saa nne asubuhi tayari kupitia kioo kikubwa cha mbele Walter aliweza kuiona nyumba ya Frank, nyumba ambayo ndani yake alikuwepo dada yake mpenzi aitwaye Maureen, Walter alitamani kupaa na kujikuta ndani ili amkumbatie dada yake lakini hakuwa na namna ilikuwa lazima avute subira.
Umati mkubwa uliokuwa eneo lile ulimshangaza kwa kiasi fulani, alidhani huenda amekosea njia ya kupita ama la akaiwazia ile mvua kuwa huenda iliezua paa la nyumba ya jirani yeyote. Yote haya yalipita kama upepo kwa kasi ya ajabu. Muga yeye alikuwa kimya, akisikiliza muziki kupitia simu yake.
"Mh! wamejuaje ninakuja? au...bamdogo Frank ameoa...au ni birthday ya..." alijiuliza yote hayo Walter lakini Muga hakuwa na jibu lolote. Aliendelea kutikisa kichwa kuashiria anavyoburudika na muziki.
"Harusi gani kelele hivi?" aliendelea kuuliza Dj safari hii akiwa kama anayezungumza mwenyewe, huku akishuka kwenye gari bila kuzimisha injini, nyuma yake alifuata Muga.
Kwa mbali akahisi hofu. Huu umati ulimkumbusha miaka kadhaa nyuma, lilikuwa eneo hili hili analolitazama kwa wakati huu, umati mkubwa ulijaa, majeneza matatu yakapangwa kwa ajili ya kuaga miili ya marehemu baba na mama yake pamoja na bibi yake kipenzi waliozoeana sana.
Walter akafadhaika moyoni, miguu ikawa mizito. Alipoyafumba macho yake alikumbuka kuwa siku ya msiba ule usiofutika akilini mwake kulikuwa na vilio vikuu, lakini leo hapa kuna kelele tupu na watu hawana utulivu.
Kuna nini? Alijiuliza kijana huyu ambaye alikuwa na kila hadhi ya kuitwa mtanashati.
Jibu angelipata kwa kulifikia eneo la tukio.

****

Tumbo lililoanza ghafla kumuuma Maureen lilipelekea msichana huyu anayehitaji uangalizi wa karibu sana, kwa kujikaza na kujivuta vuta hadi akaufikia mlango wa sebuleni, alifanya hivi kwa kuwa alikosa msaada, kama ni kulitaja jina la Naomi alilitaja kwa kurudiarudia lakini bado hali ilikuwa ileile. Akaifikia sebule ambapo alipokelewa na mvua kali ya upepo, maumivu yalivyozidi huku akiwa pale mlango Maureen akiwa na nguo yake laini ya kulalia alimaliza haja zake palepale, lakini bado tumbo liliendelea kuuma, mvua nayo ilikuwa inanyesha bado,taratibu alijaribu kupapasa wapi pa kupita arejee chumbani lakini giza likamsaliti na uwezo mdogo wa kuchanganua mambo baada ya kuwa amepata utindio wa ubongo, akajikuta amepotea njia katika hali ya kusikitisha tena iliyomtia katika mateso makuu. Maureen aliishia kulivagaa kabati la vyombo, vikatelemka baadhi vikamponda kichwani, akatokwa na yowe la hofu, mara akahamia katika luninga, nayo akaanguka nayo huku redio ikimponda vidole, akalia tena kwa uchungu mkubwa. Katika kujikwamua kutoka katika redio iliyobana kidole chake Maureen ambaye yu gizani akajikuta akiangukia mbali kwa maumivu makali akajikunja hadi akasalimiana na sakafu iliyokuwa inazidi kuingiliwa maji kutokana na mvua ya upepo. Hakuweza kuamka tena maji yakawa yanapita juu yake. Akabaki kukoroma.
Maskini Maureen bila kujitambua ni wapi hapo amelala aliendelea kulia lakini sauti yake haikusikiwa na yeyote yule hadi akanyamaza kimya. Alikuwa nusu amepoteza fahamu na nusu akiwa hai.
Hadi pale ulipofika wasaa wa kustaajabisha na kupigilia msumari katika kidonda kibichi.
Ni wakati Naomi na pombe zake kichwani akirejea nyumbani ndipo alimshuhudia Maureen lakini pombe ikamwongoza kuamini ni gunia, Naomi anashtuliwa na kunyanyuliwa ghafla kwa alichoamini kuwa ni gunia. Mwanga wa umeme uliokuwa umerejea dakika ile ndio ulimfungua akili Naomi, Maureen alikuwa amelala juu ya kifaa cha kusambaza umeme kutoka kwenye saketi ukutani, maji yalikuwa yamemuunganisha na umeme na sasa umeme ulikuwa ndani ya mwili wake ambapo ulimrusha ukutani. Kwa macho yake Naomi alimshuhudia Maureen akitulia tuli sakafuni, kwa ushahidi wa macho Naomi alitambua kuwa Maureen alikuwa kwenye tatizo kubwa sana na hiyo ilikuwa hatari kwa kibarua chake.
Hofu ikatanda. Hofu kuu.
* * * *
Hali ilikuwa tete sana asubuhi ile, hakuna aliyekuwa na jibu la tatizo hlo. Naomi alikuwa ameupanga uongo vizuri sana na kila mtu alikubaliana nae.
"Ni nini kimetokea" Walter akiwa na uoga waziwazi aliuliza swali hilo kwa kijana mmoja aliyekuwa anatokea kwenye eneo la tukio.
"Tanesco hao mh! Tanzania yetu hii dah!" alijibu huku akiendelea na safari yake.
"Samahan kaka Tanesco wamefanyaje kwani tafadhali" alihoji Walter. "Nenda kajionee kaka.." alijibu na kutoweka huku akitikisa kichwa kwa masikitiko makubwa. Aliutangaza uchungu waziwazi.
Walter na Mega walilazimika kuendelea kusogea mbele zaidi waweze kujua kuna nini, nguvu zilikuwa zinamwisha miguuni Walter, hakutaka kuruhuruhusu masikio yake kupokea taarifa mbaya itakayoharibu furaha aliyokuwa nayo kurudi Tanzania kusherekea sikukuu. Muga alikuwa katika sintofahamu, alishauzimisha muziki wake sasa alikuwa akivuta hatua moja baada ya nyingine ili wapate kujua ni kipi kimejiri katika nyumba ya nani.
"Dada samahani kuna nini?" Walter alimuuliza mwanadada mmoja aliyekuwa pekupeku. Huku usoni akiwa katika taharuki isiyofichika.
"Mh! sijui hata nielezeje lakini…ni Mungu tu…maskini dada wa watu." alianza kujibu kwa wasiwasi, akafumba macho kisha akatokwa na mguno mkubwa. Ni kama alikuwa haamini kilichotokea. Walter alikuwa katika kihoro cha kutambua kuna nini pale.
Hata kabla yule binti hajaanza kusimulia mkasa ule vizuri, macho ya Walter yalishuhudia mwili wa binadamu ukibebwa juu juu na wanaume watatu kuelekea kwenye gari ya wagonjwa iliyokuwa imefika pale, hakusubiri yule binti amalizie maelezo yake akaamua kutimua mbio kuelekea kwenye mwili ule aliamini kwa namna yoyote ile kuwa jibu la maswali yake anaenda kulipata pale, akiwa amebakiza takribani mita kumi kufika macho yake yanatua tena kwenye kundi la watu wakimgombeza mwanamke mmoja ambaye akili ya Walter ilimwambia kuwa anamfahamu, tatizo ni wapi amewahi kumuona?
"Ni nani yule nani kweli!" alianza kujiuliza akiwa amesahau kama alikuwa anawahi kutizama mwili uliobebwa ni wa nani na ni nini kimetokea. Watu waliokuwa wamemzunguka yule binti wengine walimuelewa na wengine hawakutaka kumwelewa kabisa,wengine walimsukuma wengne walimtetea. Hayo yote Walter hakutaka kuyajua alichotaka kufahamu ni wapi amemwona huyo binti, akiwa hajapata jibu alishtuliwa na ving’ora vya gari la wagonjwa barabarani tayari mwili ulishaingizwa na gari limeondoka.
Kama akili yake haikuathirika siku hiyo basi ni bahati, mbiombio akaanza kutimua mbio kuelekea nje tena akiachana na kundi lile alipokuwa yule dada aliyekuwa amemfananisha.
Walter alitaka kuliwahi lile gari la wagonjwa, hakuwa mtulivu kiakili na alitaka kuyajua mambo upesi upesi, kuna roho ilimsukuma waziwazi kuwa kuna jambo zito. Mbio za sakafuni huishia ukingoni, lakini mbio za utelezini huishia maangukoni.
Walter akiwa na moka yake ya bei ghali sana alikutana na utelezi mkali, akajaribu kuutafuta muhimili akaukosa, miguu ikatangulia kisha kisogo kikakutana na kitu kigumu sana.
Akili ikazimika palepale. Hakusema neno la ziada. Huu ukawa mwisho wa papara zake. Papara za kutaka kujua nini kimejiri.
Hii ikawa kesi nyingine watu wakahamia kwa Walter tena, Muga hadi dakika hiyo ni kama alikuwa amechanganyikiwa tayari kwa yote ambayo macho yake yalishuhudia ndani ya dakika chache. Akabaki kuhaha.
* * * *
Maureen alikuwa amepigwa shoti kali ya umeme kutokana na kulala juu ya 'extension' bila kujua kisha maji ya kaingia na kumuunganisha na kile kifaa, ambapo umeme uliporejea yakamkumba maswahibu haya ya kusikitisha, shoti hiyo inazua walakini na utata kwa Naomi, msichana wa kazi ambaye anaujua ukweli lakini akaupindisha kujiweka salama.
Naomi hakuwa tayari kukiri kuwa alimuacha Naomi na kwenda zake katika viwanja vya starehe. Nafsini mwake alitambua wazi kuwa iwapo Maureen atakufa basi yeye ndiye muuaji kwa asilimia zote. Wazo hili lilimtesa sana na kujikuta akikosa amani.
Maswali anayoulizwa yanamchanganya na anajibu kwa kujichanganya, mwisho wa siku anaanza kuonekana muongo, wanaume wanamnasa makofi na wanawake wanamshikia bango. Hali tete.
Naomi anaiona hukumu mbele yake, hukumu ya kuuawa, anamkumbuka Mungu wake. Anamsihi aingilie kati ili apate nafasi nyingine ya kuishi kwa amani.
Ombi lake linakuja wakati muafaka. Ghafla mwanaume aliyekuwa anahaha huku na kule anateleza na kutulia tuli baada ya kuanguka. Waliokuwa wanamwandama wanakimbilia eneo la tukio.
Naomi anaupata upenyo wa kutoroka. Haipotezi baati hii.
Anatoweka.kimya kimya kuepusha tafrani mbele yake.
* * * * *

* * * * *

"Mbona niko hapa, gari la wagonjwa liko wapi? limembeba nani? da Maureen yuko wapi?" maswali mfululizo yalimtoka Walter baada ya kuzinduka na kujikuta kwenye kitanda hospitali. Nesi aliyekuwa pale hakuwa na jibu lolote lile.
"Naomi Naomi yule ni Naomi, Naomi wangu" Walter akaanzisha mkasa mwingine, nesi akadhani tayari mgonjwa ana matatizo ya akili. Mbiombio kaenda kumwita daktari, lakini kama vile alikuwa ameitwa Walter naye aliruka kutoka pale kitandani akatoka nje ya chumba cha hospitali huku akiwa na bandeji kichwani, kwa jinsi ambavyo hakuwa na hofu na wala hakutetemeka hata kidogo hakuna aliyeweza kumdhania kuwa alikuwa anatoroka hospitali. NESI alikuwa amefanya kosa kubwa sana kumwacha mgonjwa peke yake katika kile kitanda.

"Tabata shilingi ngapi?" Walter alikoroma mbele ya taksi.
"Buku saba mjomba"
"Nipeleke fasta!" alijibu Walter alipotajiwa bei na dereva taksi.
"Dah! nyie wagonjwa hamuaminiki nipe changu kwanza" akasema dereva yule wakati akianza kuiwasha gari yake.
Haraka haraka kwa kujiamini, Walter ambaye alionekana kuwa na haraka sana akazama mifukoni mwake, tofauti na matarajio yake hakukuta wallet yake mfukoni na aliambulia shiingi elfu mbili ya Uganda tu katika mfuko wake wa shati.
"Nilijua tu! yaani watu wengne bwana" alianza kuponda dereva alipogundua Walter hakuwa na kitu mfukoni. Walter hakuwa na hadhi tena mbele ya macho ya madereva wengine.
"Hapana nilikuwa na wallet kaka, sijui...."
"Huna lolote mzazi nenda ukapande daladala tena hizo zinapita!" alijibu dereva huku akimwonyesha Walter magari yanayotokea Muhimbili kwenda Buguruni. Walter kwa mfadhaiko mkubwa alisogea barabarani akapiga gari mkono akapanda japo lilikuwa limejaa.
"Yuko wapi mgonjwa!" daktari aliyefuatwa na nesi alihoji.
"Alikuwa hapa..." kwa uoga na kutetemeka alijibu nesi, kwani Walter hakuwepo tena pale.
"Maskini wa Mungu atakuwa ameenda wapi huyu kijana" alijiuliza daktari huku akijikuna kichwa chake.

****
Foleni ya siku hiyo ilikuwa ndefu sana tofauti na siku nyingine zote, kuanzia maeneo ya Magomeni gari alilopanda Walter lilikuwa halisogei mbele na tayari lilikuwa limezimishwa, abiria walikuwa wamekasirika mno na kila aina ya matusi kwa serikali yalisikika. Walter alikuwa mkimya sana, moyoni aliwaza mengi mazito, hakuwa hata na simu aweze kumpigia Muga wala Frank.
Akiwa ndani ya gari kuna mazungumzo yalimvutia kusikiliza.
"Jamani walikuwa wanamkimbiza hospitali na ajali imewazuia tena, mimi simlaumu dereva hata kidogo alikuwa anawahi" mama mmoja alikuwa akimwambia abiria mmoja katika gari alilokuwa amepanda Walter. Mama huyo aliyekuwa anatembea kwa miguu alionyesha huzuni yake dhahiri. Maneno hayo yalipokelewa kwa hofu na Walter, kwa wakati huo aliamini kila mgonjwa ni dada yake (Maureen) hivyo bila kujali jeraha lake kichwani alishuka na kuanza kujikongoja kuelekea kule alipotoka yule mama.
"Ni huyu ni huyu jamani" Walter alisikia maneno hayo nyuma yake lakini hakugeuka kwani macho yake yalikuwa yanatazama gari ya wagonjwa iliyogongwa vibaya ikiwa imeziba barabara. Huku akizidi kukaza mwendo alishtukia akikamatwa kwa nguvu na kufungwa kamba mikononi na miguuni.
Hakujua ni kwa nini kwani tayari alishasahau kuwa ametoroka hospitali
Ilimchukua dakika chache Walter kugundua tayari alikuwa mikononi mwa wauguzi na wahusika wa hospitali ambayo alikuwa ametoroka
"Jamani mimi ni mzima naenda kumwangalia dada yangu ni mgonjwa na alikuwa kwenye ile gari" aliongea Walter huku analia akiwaonyesha gari ya wagonjwa iliyokuwa imepata ajali mbaya sana. Wale watu hawakutaka kumwelewa waliamini amerukwa akili na hakujua anachokizungumza wakati ule. Kwa usalama wa maisha yake hawakumwachia.
"Jamani naomba mnielewe japo kidogo dada yangu anaitwa Maureen ndio namtafuta na mimi naitwa Walter hata nyie nafahamu ni wahusika wa hospitali sijachanganyikiwa mimi najitambua" alijaribu kwa kila hali Walter kuwashawishi watu hao kumwachia lakini badala yake walizidi kuimarisha ulinzi asiweze kupata nafasi ya kutoroka.
Walter hakuwa na njia mbadala hakuwa na nguvu za kuwazidi watu hawa hivyo alilazimika kwa shingo upande kukubali kupandishwa kwenye gari waliyokuja nayo watu hawa na kusubiri hadi foleni ilivyoanza kwenda akarudishwa hospitali alipochomwa sindano za usingizi na kufungwa mikono yake kikamilifu ili akizinduka asiweze kutoroka tena.
Fahamu zilipomrejea yalikuwa yamepita masaa kadhaa.

* * * * *
Ilikuwa taarifa ngumu sana kuingia na kukubalika katika kichwa cha Frank (baba mdogo wa Walter) pamoja na Anko Muga rafiki yake,taarifa ya gari aliyokuwa amepakizwa Maureen ili akimbizwe katika hospitali ya Muhimbili kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya ilikuwa imepata ajali kwa kugongwa na gari kubwa upande wa ubavunh ambapo mwili wa mgonjwa ulirushwa nje ya gari "hali yake ni mbaya sana na foleni ni kubwa inashhndikana kuwahishwa hospitali,na hata madaktari waliopigiwa simu wafike haraka hawawezi kwa sababu ya foleni kubwa" ilimalizia kwa huzuni kubwa sauti ya mwanadada aliyekuwa anasoma habari ya ghafla ama mpasuko "BREAKING NEWS"katika kituo maarufu cha luninga hapa nchini.
"Walter atanielewaje mimi,huyo pekee ndiye ndugu yake aliyebaki hapa ulimwenguni!" Frank alijiuliza huku amejishika kichwa akitembea bila kujua anapoelekea hasa
"Frank nadhani si muda wa kujilaumu, tusubiri na Mungu atatuonyesha njia ya kweli labda atapona" Anko Muga alimpa matumaini Frank ambaye alionyesha kuchanganyikiwa kabisa kwa taarifa ile ya kushtusha. Nyumba yake ilikuwa shaghalabaghala aliamini umati uliofika pale siku ya tukio lazima walikuwepo vibaka hivyo alitegemea sana wizi pia umefanyika.
"Naomi yuko wapi?" ni swali la pekee aliloamini jibu lake lingemfungua akili yake, hakupata wa kumjibu Naomi hakuwa eneo lile tena,na hakuna aliyejua ameondoka sangapi pale, Frank alizidi kuchanganyikiwa.
Lakini hakuweza kuibadili siku hii. Hakuweza kuubadili ukweli uliopo.
Yaliyopangwa yakatimia.

* * * * *
"Ulale pema peponi Maureen, msalimie bibi mwambie mchumba wangu Naomi sijui alipo, wasalimie baba na mama waambie nawapenda sana, kwaheri dada Maureen"Aliongea hayo Walter wakati anauaga mwili wa Maureen uliokuwa umepondekapondeka vibaya kutokana na majanga aliyoyapata, kwanza umeme halafu ajali mbaya ya gari. Maneno na sauti yake vilimchoma kila mtu aliyeyasikia,Walter alikuwa na jeraha kisogoni, nguo zake zilikuwa chafu sana. Hakuhitaji kubadilisha na hakuwepo wa kuweza kumshawishi lolote.
"Nilitegemea kula nawe sikukuu za mwisho wa mwaka kwa nini hukusubiri lakini! Mbona hukutaka walau nipate dakika mbili za kukuona ukitabasamu. Ewe ardhi mwenye tamaa nimeze na mimi uridhike, hivi baba na mama hawakukutosha? Bibi naye je…haya na dadangu umemchukua….eeh Ardhi nimeze sasa hivi niondoke na Maureen" alishindwa kujizuia Walter akaangua kilio kikali, wakati huo Frank alikuwa hajiwezi ameishiwa nguvu akiwa amekaa chini, ulikuwa msiba ulioteka hisia za wengi sana katika mitaa mbalimbali jijini Dar-es salaam.
Kilio cha mtu mzima kikachukua nafasi.



****
Baada ya ardhi kugoma katakata kukisikia kilio cha Walter na badala yake kuyameza machozi yake bila shukrani hatimaye Walter akajikuta akiilaani ardhi ya Tanzania. Aliilaani kwa kuwa ilikuwa imempa uchungu ambao ulikuwa mgumu sana kufutika.
“Huenda hata Naomi naye ilimmeza ardhi hii isiyokuwa na shukrani.” Walter alisema na nafsi yake wakati akimalizia kuilaani kwa lugha zote ardhi ya Tanzania.
“Frank.” Walter aliita kisa akendelea, “Anko Muga.” Wote wakawa makini kumsikiliza.
“Naapa mbele yenu, ndugu zangu mliosalia. Sitakaa niikanyage ardhi hii tena. Frank, usijisikie vibaya na kuhisi kuwa nakukimbia; hapana umekuwa msaada mkubwa sana kwangu, wewe ni baba mwema sana kwangu. Lakini haikupangwa tu nifurahi pamoja nawe. Labda sikustahili kuzaliwa katika nchi hii, n’do maana inanitenda hivi.” Walter alimaliza kuzungumza alichakuwa amepanga.
Frank na Muga, wakabaki kimya, hakuna aliyejazia neno la ziada. Waliamini kuwa maneno yao hayawezi kumbadili Walter na msimamo wake.

Baada ya siku mbili Walter akiambatana na Muga, wakaiacha ardhi ya Tanzania. Safari hii waliondoka kwa usafiri wa ndege. Lile gari jipya walilolitumia kwa safari ya Mwanzo, Walter akamtunuku Frank kama zawadi kwa moyo wake wa upendo.
Maisha mapya yakaanza tena.

****

BAADA YA MIAKA MIAKA MIWILI.
Maandalizi ya tamasha kubwa la Muziki nchini Tanzania yalikuwa yamepamba moto, tamasha hili kwa mara ya kwanza liliwagusa hadi wafuatiliaji wengine katika nchi za jirani.
Liliwagusa watu wengi kwa sababu moja tu, wasanii mapacha kutoka nchini Nigeria walikuwa wamekubali siku ya kilele cha tamasha lile.
Walter aliipokea taarifa hii kupitia vyombo vya habari.
Akakuna kichwa chake, akachangamka kuisikia habari hii.
Akaikumbuka ndoto yake tangu anaanza kuwika katika shughuli za u-Dj. Ndoto ya kufanya kazi na wasanii wale.
Lakini alipokumbuka kuwa wanaifanya kazi yao katika ardhi aliyoilaani nayo ikamlaani, munkari wake ulishuka sana. Na hamu ikamwisha.

Kitu bora hutengenezwa na watu bora. Waandaaji wa tamasha lile walihitaji kufanya kitu bora sana katika kilele cha tamasha hilo.
Hivyo katika sekta zote za muhimu walihakikisha zinashikiliwa na watu wa maana.
“Hebu mpigie simu namba yake hii hapa.” Mshika dau mmoja alitoa wazo baada ya kuwa wamejadili kwa muda mrefu.
Simu ikapigwa na wote wakaunda kimya kikubwa ikabaki kusikika simu pekee.
“Hallo…” ilijibu sauti upande wa pili.
“Unaongea na timu ya Chizika..bila shaka ni Dj Muga.”
“Bila shaka.” Alijibu kwa utulivu.
Upande wa pili ukazungumza lengo la kupiga simu. Walikuwa wakimuhitaji Dj ambaye alikuwa anafanya kazi akisimamiwa na Muga kama mkurugenzi wake.
“Nitawapatia jibu baadaye.” Alijibu Muga baada ya kuwa amekosa jibu la moja kwa moja.

****

MABISHANO yalikuwa makali sana, Walter hakutaka kujadili suala la yeye kurejea Tanzania. Muga alimsisitiza na kumtajia dau kubwa ambalo limetajwa kwa ajili yake.
Dau halikumshtua Walter. Tayari alikuwa majeruhi, jeraha la hisia za ardhi ya Tanzania kuwa inamuonea zilimgalagaza na kumfanya ajione yu mtumwa utumwani.
“Walter.” Muga alimuita kwa utulivu baada ya damkika kadhaa za kutupiana maneno japo si kwa ubaya.
Walter akatikisa kichwa kuashiria amesikia.
“Baba, mama, bibi, dada….wako wapi?”
“Mbinguni.” Alijibu Walter.
“Umewahi kufika huko ukawaona.”
“Najua wapo mbinguni. Nilifundishwa hivyo tangu utotoni.”
“Ok. Hivi unajua kuwa wanakuona unachofanya duniani.”
“Ndio wananiona, hata hilo nilifundishwa pia.” Alijibu Walter upesi bila kuijua nia ya Muga.
“Vyema kama unatambua kuwa wanakuona. Na watu wote hao uliowaheshimu wakati wapo hai umeshindwa hata kuheshimu makaburi yao, umeshindwa kuheshimu makazi yao ya sasa, umewakimbia. Walter watu hawa wa muhimu kwetu wanakutazama na wanalia juu yako. Kila mara ni mimi na Frank tunaenda kufanya usafi katika makaburi. Wewe umegoma, umegoma kuzisafisha nyumba zao.” Muga akaweka kituo kisha akaendelea, “Mimi sikulaumu wewe hata kidogo, ila naomba uamini kila kitu huja na hupita hata hayo yalitokea na yamepita. Kama unailaani ardhi ya Tanzania. Je watu wa Rwanda waliopoteza ukoo mzima wafanye nini?” alimaliza Muga.
Kimya kikatanda, Walter alikuwa anatetemeka. Akajihisi mkosefu. Maneno ya Muga yalikuwa yamemvuruga kwa kiasi kikubwa.
Na kwa upande mkubwa sana yalikuwa yana ukweli ndani yake.

Muga alipomaliza akaaga ili aweze kuondoka maana alikuwa nyumbani kwa Walter wakati ule.
“Anko….hebu subiri kidogo..” Walter akamzuia.
Muga akabaki amesimama akimsikiliza Walter.
Walter akatazama juu, kisha akashusha kichwa chake chini.
“Kwa heshima yako, Frank na roho nilizozipenda lakini zikaitamanisha ardhi yenye tamaa ikazimeza. Nitarejea Tanzania. Kwa moyo mmoja mweupe kabisa nitarejea katika ardhi niliyoichukia, kama bado ina kinyongo nami kwa kosa nisilolijua basi na inimeze, kama haina kinyongo nami na inihifadhi kwa upendo isiniumize tena siku hizi za karibuni. Ni heri inimeze mimi kuliko kuimeza roho yoyote ninayoifahamu. Nina jeraha kubwa sana ambalo halina dalili ya kupona.
Sihitaji kujitonesha upya.” Walter alimaliza kuzungumza.
Muga akamsogelea na kumpigapiga mgongoni ishara ya kumpooza.
Akazua kilio kingine. Walter hakuweza kustahimili kumbukumbu ngumu za kipindi cha nyuma.
Ikabaki kazi ya Muga kumbembeleza.

****
UKUMBI mkubwa na wa kisasa wa Diamond Jubilee ulikuwa umefurika watu wa haiba mbalimbali.
Burudani ilikuwa haijachangamka bado.
Hadi pale alipotangazwa Dj atakayekuwa katika mtambo.
Nani ambaye hakumfahamu Walter. Ni mara ngapi aliitwa kuja kufanya shughuli Tanzania akawagomea wadau.
Akatangazwa kuwa ana dharau sana.
Sasa leo yupo nchini Tanzania.
Baada ya kutambulishwa kila mtu alipiga kelele za aina yake, wapo waliomzomea kwa sauti za juu, na hawa n’do walikuwa wengi, wachache walipiga miluzi ya kumshangilia.
Walter aliligundua hilo, akakichukua kipaza na kusimama mbele ya mashabiki baada ya Mshereheshaji kumruhusu.
Walter akazungumza maneno ambayo yaliunyamazisha ukumbi huo mkubwa wa Diamond.
Wengine aliwaliza, wengine walipiga moyo konde, na wengine waliopitia magumu zaidi yake walipuuzia.

Shuguli ikaanza rasmi.
Hakika Walter alikuwa habari nyingine. Alipangilia mambo kimataifa.
Majira ya saa sita usiku ndipo alipoanza kuzorota.
Ni baada ya kushuhudia jambo la ajabu linalofanana na ndoto.
Jukwaa lilikuwa limekabwa na wacheza viduku, ilikuwa zamu yao kuburudisha watazamaji.
Walter akaona umbo ambalo aliwahi kuliona tena hapo kabla.
Alitamani sana katika mtindo wao wa kucheza waweze kumgeuzia sura amtazame vyema.
Kama walimsikia, huo mtindo ulikuwepo.
Akawa anamrushia jicho.
Sasa aliweza kumwona vyema zaidi. Alikuwa yeye.
“Naomi….Naomi wangu..” walter alijisemea huku akiduwa na kushindwa kufanya michanganyiko ya hapa na pale inayoburudisha.
Alitegemea kuwa baada ya tamasha lile angeweza kuonana naye lakini haikuwa hivyo.
Watu walikuwa maelfu asingeweza kumwona binti yule.
Ulikuwa muujiza mkubwa sana kuweza kumwona Naomi tena baada ya harakati za muda mrefu kugonga mwamba.
Sasa amemwona tena.
Walter akahisi hiyo ilikuwa nafasi nyingine tena ya yeye kuipata furaha iliyopotea katika ardhi ya Tanzania.
Hakujalisha ni miaka mingapi ilikuwa imepita tangu waonane kwa mara ya mwisho.
Walter aliamini kuwa Naomi alikuwa msichana wa kipekee sana.
Si kwamba hakuwa na msichana mwingine kwa wakati huo la. Alikuwa naye lakini hakuwa na wazo la kumuita mke.
Sasa amemuona Naomi ambaye marehemu bibi yake alimbarikia kwa kumwita mkewe.
“Huenda bibi amenionyesha tena.” Alijisemea Walter baada ya tamasha hilo.


KIMBOKA, ni moja ya baa maarufu sana jijini Dar es salaam. Umaarufu wake si kwa sababu ya huduma bora wanazotoa ama mandhari nzuri ya kuvutia katika baa hiyo.
Umaarufu wake ulisambaa sana kutokana na huduma ya bei rahisi pengine kuliko sehemu yoyote katika jiji hilo. Huduma ambayo inawasaidia makapela azidi kusahau kuhusu ndoa mathalani kuishi na mwanamke ndani.
Biashara ya uuzaji miili kwa bei nyepesi sana.
Baa hii ilikuwa makazi ya mwanadada Naomi kwa kipindi tangu akimbie shutuma za kuhusika katika kifo cha Maureen.
Naomi alikimbilia huku si kwa kuwa naye alikuwa wa bei rahisi sana kwa wakati huo la. Alihofia usalama wake na kubwa zaidi alikuwa amechanganyikiwa.
Dawa ya kutuliza mawazo aliamini kuwa ni kunywa pombe, basi kama kweli ni pombe Kimboka zinapatikana kwa bei ya kawaida bila nyongeza yoyote.
Naomi akawa Naomi wa Kimboka.
Dada yake naye alikuwa kitu kingine ambacho kilizidi kumchanganya akili. Tayari walishasahau kuwa walimzika mama yao miaka kadhaa nyuma, leo yule dada aliyemzika mama haishi kuhudhuria hospitali, leo Amana kesho Temeke, Mwananyamala na wakati mwingine Muhimbili.
Afya ilikuwa imezorota na alikuwa amekata tamaa ya kuendelea kuishi.
Haikuhitaji elimu kubwa sana kutambua kuwa mwanadada alikuwa katika siku za mwisho za uhai wake.
UKIMWI ulikuwa unamtafuna kwa kasi.
Changudoa wa zamani alikuwa ameukwaa.
Huenda yalikuwa malipo sahihi kwake.
Naomi akabaki kuishi katika mashaka, akahisi hata yeye alikuwa ameukwaa, kuna baadhi ya wanaume ambao walipita katika mwili wa dada yake na yeye akawapokea vivyo hivyo bila kutumia kinga akawapatia huduma stahiki, wakampa malipo.
Kama walivyomlipa dada yake na kisha kumwachia dubwana lile ambalo linamlaza kitandani, linakula ngozi yake kwa namna ya mkanda wa jeshi, linamfanya akohoe kwa maumivu makali na safari za chooni zikiwa hazina muda maalum.
Lazima naye awe na mashaka, tena mashaka makubwa.
Kwa kuwa wamemuambukiza dada yangu, ngoja nami niwaambukize.
Alijiapiza Naomi, n’do lengo haswaa la kujiweka katika soko jepesi la walalahoi. Buguruni katika baa ya Kimboka.

Katika ukumbi huu wa baa,Naomi licha ya kujiuza kwa kuvaa hovyo hovyo alikuwa na njia nyingine za kuutangaza mwili wake na pia kujiongezea kipato cha kumnunulia dada yake dawa na mahitaji mengine kwa mgonjwa.
Naomi akaamua kutumia kipaji chake ambacho amekuwa nacho tangu utotoni, kipaji cha kucheza muziki. Kila bendi ya muziki ilivyokuwa ikiwaburudisha walevi usiku kucha, Naomi alikuwa akicheza kwa umahiri mkubwa sana na mwishowe anatunzwa shilingi mbili tatu.
Bendi zikamtambua, hatimaye kikawa kibarua chake, kuwaburudisha walevi pindi wanausaka ulevi wao na mwishowe kuwaburudisha kitandani wakiwa tayari wamelewa.
Hawa waliolewa, Naomi alifanya kuwaibia wakizubaa.
Haya yakawa maisha rasmi ya Naomi hadi lilipotoka tangazo la mashindano ya kucheza kwa ajili ya tamasha kubwa la muziki.
Naomi akahudhuria kwa kujaribu.
Matokeo yake akashinda na hatimaye akaingia katika jukwaa kubwa la ukumbi wa Diamond Jubilee.
Ni huku ambapo jicho la Walter lilimuona bila yeye kujua.

Baada ya tamasha Naomi kama kawaida alikuwa ameopolewa na kibopa mwingine, alionekana ni mtu mwenye pesa zake. Naomi akatambua kuwa amepona kwa siku hiyo.
Akiwa na yule kibopa anasikia sauti inamuita kwa mbali, ilikuwa sauti ya kiume.
Sauti ilizidi kuita.
Naomi akatambua kuwa hao walikuwa wateja wake wa zamani na sasa walikuwa wanakaribia kumharibia.
Naomi akacheza karata sahihi. Akamkokota yule mwanaume wakaingia katika gari.
Milango ikafungwa.
“Sihitaji kuonana na mtu tafadhali, yaani mtu ukishakuwa ‘Superstar’ basi kero aziishi.” Naomi alijisemesha, huku kichwani akijishangaa ameitoa wapi hiyo kauli.
“Poleni sana mpenzi mnahangaika kweli. Kwa hiyo huyo anaweza kuwa nani?”
“Sio huyo ni hao wapo wengi, watakuwa waandishi wa habari hao, nishawaambia sipendi mambo yao, bado wananifatilia.”
Alipomalizia ile kauli, yule aliyekuwa anamuita akalifikia gari. Akaanza kugonga kioo.
Kibopa keshajazwa ujinga, akashusha kioo kidogo, akaanza kutukana kana kwamba amefungiwa kifaa kilichorekodiwa maneno yale.
Baada ya matusi gari ikaondolewa, huku Kibopa akiwa ametaharuki.
Aliamini kuwa yupo na mtu wa kuheshimiwa sana katika jamii.
Laiti kama angejua ni wapi ameshikilia, angeachia upesi mahali hapo.

****

UZURI wa jiji la Dar es salaam, kuna usafiri wa aina mbali mbali, ni wewe tu kuamua unataka kusafiri kwa starehe ili uchelewe ama kwa karaha ili uwahi.
Hata usiku ambao Walter alimaliza kushughulika jukwaani, alijikuta katika maamuzi hayo pia.
Bodaboda. Lilikuwa jibu sahihi kwake.
Hakuhitaji kumpoteza Naomi kabisa.
Aliamini kumpoteza kwa siku hiyo basi ungekuwa mtihani mwingine mgumu.
Walter akaamua kuchukua ‘bodaboda’ na kuanza kulifuatilia lile gari lililombeba Naomi.
Mwisho wa safari yao ukawa katika nyumba nzuri nyeupe ya kulala wageni.
Walter akakaza jicho, hakika aliyemuoana alikuwa ni Naomi wake ambaye bibi yake alimuita ‘mkamwana’ .
Kidogo Walter amvamie, lakini akkumbuka kuwa Naomi alikuwa mpenzi wake wa utoto tu si zaidi ya hapo. Na ni miaka zaidi ya kumi ilikuwa imekatika tangu waonane.
Walter akapiga moyo konde.
“Kaka ulikuwa unamfuatilia huyu demu?.” Dereva wa ile pikipiki akmuuliza Walter aliyekuwa anashangaa bado.
“Ndio kaka, lakini sijui kama nimemfananisha ama vipi.”
“Sio Naomi wa Kimboka yule.”
Walter akageuka na kumtazama yule dereva, akawa anamsikiliza anavyomuelezea Naomi.
“Nipe namba zako, kesho nakuchukua mida ya usiku nakupeleka Kimboka, hapo utaonana naye bila shaka, kama alikuibia simu sahau maana haogopi kupigwa huyo. Itakuwa imekula kwako.” Dereva akampatia namba Walter, naye akampatia za kwake.

Usiku huu ukapita katika hali ya kutia simanzi. Walter akiwa na maswali lukuki.
“Kivipi Naomi ajulikane kiasi hicho, na hapo Kimboka n’do kazini kwake nini?” alijiuliza Walter kabla ya kupitiwa na usingizi. Kisha ukauta usiku mwingine ambao kamwe hatausahau maishani mwake.
Usiku wa kukutana na Naomi wake. Msichana ambaye alikuwa amesalia kama faraja pekee ya nchini Tanzania.
Walter alionana na Naomi majira ya saa nane usiku, alikuwa amechoka sana na macho yake yalikuwa yamelegea, mavazi yalikuwa machafu upande wa mgongoni na hata kisogoni alikuwa na uchafu.
Walter akakumbwa na sintofahamu, amkabili ama aendelee kungoja.
Machangudoa nao kwa fujo walikuwa wakimsumbua Walter, mara wamfunulie mapaja, mara wambusu, mara wamtekenye. Ilimradi tu kumtia vishawishi.
Walter hakushawishiwa, badala yake alimsogelea Naomi.
Akamgusa bega.
Akaporomoshewa tusi zito.
“Naomi.” Akaita.
“Naomi mama yako…..” Alijibu yule dada aliyetawaliwa na hasira.
“Naomi njoo basi …”
“Una shi’ng ngapi wewe bata.”
“Njoo tuongee.” Walter alisihi.
Hatimaye sauti ikapiga ngoma za sikio la Naomi, akaanza kuogopa, aliwahi kuisikia mahali, akageuka upesi. Akakutana na sura ikiwa katika majonzi.
Cha mtu chake tu. Naomi angeweza kusahau kila kitu lakini sio sura ya Walter.
Naomi akasimama ghafla. Akayatumbua macho yake kama ambaye amekamatwa na polisi bila kutegemea.
Ana kwa ana na Walter.
“Walter…” akajikuta anaita bila kutaraji.
“Naomi.” Walter akajibu kwa sauti ya chini. Kisha akamshika mkono Naomi, wakajiweka mbali na kelele za muziki na machangudoa waliolewa.
Naomi akaanza kulia, Walter hakuweza kumbembeleza akabaki kulia pamoja naye. Wakakumbatiana.
Naomi aliendelea kutokwa na machozi kwa fujo.
Ilikuwa lazima atokwe machozi, alikuwa amepitia mengi machafu ya kusikitisha na Walter aliyeonekana mbele yake alikuwa na kila dalili za kuwa na upendo wa zamani. Macho yake yaling’ara kwa huba ya ajabu, midomo yake haikuzungumza lakini alikuwa anatangaza mambo kadhaa katika uso wake.
Ni kama vile alikuwa anasema “nakupenda kupita wasichana wote duniani.”
Hakika alikuwa katika hisia motomoto.
Hisia za kukutana na Naomi.
Lile jeraha lake la hisia sasa lilikuwa limempata wa kulitibu vyema.
Hisia za miaka zaidi ya kumi zimepata pa kuzitua.
Hisia za marehemu bibi.

Naomi bado alikuwa katika mshangao. Mshangao mkuu.
Hakuamini kama aliyepo mbele yake ni Walter.
Walter akamchukua hadi katika gari aliyokuja nayo. Akamfungulia mlango kama malkia ama mtu wa kuheshimiwa sana, kisha naye akaingia, huku nyuma vikabaki vicheko tele kutoka kwa machangudoa na baadhi ya wateja ambao walikuwa wanamfahamu Naomi. Waliamini kijana yule alikuwa amepotea njia kumuopoa changudoa yule.

****

“Walter, sio kwamba sikupendi tena. Hapana mimi sio msafi, mimi sistahili kuwa mkeo wala hadhi ya uchumba sina. Walter wewe tafuta mwanamke mwingine oa. Sistahili hata kuwa nawe katika chumba hiki cha kifahari, nielewe Walter sina hadhi ya kuitwa mke. Mimi ni makapi na mfano mchafu kabisa usiofaa kuigwa na jamii.
Walter kwa pale uliponikuta unadhani nilikuwa nafanya nini? Dunia imenisaliti tangu nikiwa mdogo, nilizaliwa maskini na nisiyekuwa na akili na nitakufa hivihivi, na sina siku nyingi za kuishi mimi natakiwa kufa Walter. Duniani si mahali sahihi kwangu. Sina vigezo vya kuwa hapa, ninatakiwa kwenda katika ulimwengu mwingine tu.
Niwe mkeo? Walter hapana, sitaki kukuaibisha mpenzi, sitaki uaibike mtaani, kila mtu anajua mimi ni chawote walter, nakuwa muwazi kwako kwa sababu ulinipenda tangu utoto wako, najiweka uchi kwa kila kitu ili unifahamu mimi, maskini wa kutupa niliyeangukia katika domo la uchangudoa nalo limenimeza na halitaki kunitapika. Niache Walter, niache na umtafute wa hadhi yako.” Alishindwa kuendelea kuzungumza Naomi, kilio kikachukua nafasi. Baada ya muda mrefu wa kulia kwa kuigiza igiza mbele ya wateja wake sasa alikuwa analia kilio cha ukweli mbele ya Walter.
“Naomi, niliyeko mbele yako ni yuleyule Walter uliyemwongoza utotoni na kunifunza mengi, ni yuleyule Walter ambaye alikuita baada ya kushuhudia bibi yake akiwa sakafuni akivuja damu, na ni yuleyule Walter ambaye alitoweka bila kupenda akaenda mbali nawe. Nimekutana na wasichana tofauti wa hadhi tofauti lakini sifurahii kuwa nao, kuna sauti ya bibi inaniambia, ‘Naomi ndiye mkeo. Muoe.’ Siwezi kuipuuza sauti ya bibi yangu, bibi aliyetupenda mimi na wewe.
Bibi aliyekufa nikimwona. Naomi mimi ni Walter na nitabakia kuwa Walter, kama wewe kutembea na wanaume wengi wanakuita changudoa kwa sababu tu unalipwa, basi hata mimi nimetembea na wasichana wengi tu. Mimi ni Malaya zaidi yako…….sote sisi ni wachafu, usijihukumu kwa sababu tu akina fulani wanajua wewe ni changudoa. Kwa ngu mimi wewe ni Naomi. Nafunga mjadala huu kwa sauti kutoka ndani ya moyo wangu, moyo wenye majeraha kadha wa kadha. Nitakuoa Naomi na kamwe sitamsikiliza mwanadamu yeyote.” Alimaliza Walter kuzungumza maneno yale makali, Naomi akawa analia kwa sauti ya juu kila neno lilikuwa kama msumari kwake.
Aliusikia uchungu haswa.
Walter alikuwa ameibua mambo mengi kwake. Mambo yanayoumiza haswaa.


siku ulikuwa mrefu haswaa,hakuna jambo lililozungumzwa kwa kujirudiarudia, kila jambo lilikuwa jipya na lilimwaga machozi ya wawili hawa.
Naomi alikuwa atika msimamo wake na Wallter naye akiwa katika msimamo wake.
Naomi anataka Walter anakataa.
Pagumu.

Majira ya saa nane usiku almanusura kitokee kitu kibaya.
Naomi alikuwa mzoefu katika kutega wanaume na wao wakategeka, haikujalisha wanamnunua kwa bei gani, cha msingi ni wao kutegeka. Ili wakishamlipa watamani tena kushiriki naye katika uovu huo.
Naomi bila kutarajia akajikuta katika hali ile. Walter akazidi kupagawa kwa kutazamana na macho yaliyolegea, na midomo inayolazimisha usisimke.
Walter akategeka, akamvamia Naomi lakini ilikuwa nafasi ya Naomi kuutetea uhai wa mtu ambaye hakufanana na wateja wake wote waliowahi kumnunua. Huyu alikuwa na hisia za ukweli kutoka katika nafsi yake.
Lakini sasa alikuwa amepagawa kama wateja wengine.
Wanaume bwana? Naomi alijisemea katika nafsi yake.
Changudoa hana hisia za kimapenzi mbele ya mteja wake. Yale yote anayoyafanya huwa ni katika kuigiza tu ili mwanaume aridhike na kumaliza shida zake upesi.
Naomi alikuwa mkongwe na Kimboka ilikuwa imemkomaza zaidi.
Ni lipi asilolijua kwa mwanaume. Aliyafahamu madhaifu mbali mbali yanayowafanya wawe watumwa wa ngono.
Naomi alishangaa siku hii alikuwa ana dalili za kumtamani Walter. Lakini ghafla kati yake na Walter ikajengeka picha ya dada yake akiwa anatapika kitandani, akiwa hoi na dalili za kuitwa na yule malaika anayehisiwa kuwa ni mtoa roho zikimwandama.
Ukimwi.
Sauti kutoka pasipojulikana ikamuhangaisha Naomi. Kama dada yake anahangaika na maradhi hayo basi hata yeye alikuwa katika mkondo huohuo.
Walter hakuwa mtu sahihi wa kumwambukiza tena kwa maksudi.
Naomi akamzuia Walter aliyekuwa anahangaika huku na kule.
Akafanikiwa kuituliza mizuka ya Walter.
Usiku huo wa kipekee ukapita.
Asubuhi tamthilia ikaendelea, Walter anamuhitaji Naomi kwa hali na mali. Naomi anajishtukia.

Walter, baada ya kuona kwamba Naomi alikuwa mgumu kukubaliana naye, akaamua kufanya maamuzi ya mengine.
Akamwomba Naomi amsindikize mahali.
Wakakubaliana na kuufikia ufukwe mmoja maarufu jijini. Walter aliaminishwa tangu utoto wake kuwa ufukweni ni mahali ambapo huilainisha na kuisawazisha akili na kuipa uwezo mkubwa wa kufikiri.
Walter aliweka mada nzito mezani. Ilikuwa juu ya kupima virusi vya Ukimwi.
Naomi aliruka maili mia mbali naye na kukataa katakata. Walter alitumia kila aina ya neno ajualo, ikiwemo ahadi ya kumtunza Naomi aidha awe ameathirika ama la.
“Naomi niliposema nakupenda sikuweka neno la ziada, sikujiwekea sharti lolote la kukupenda wewe, kama ningeweka sharti sidhani kama ningeweza kukupenda kulingana na mahali nilipokukuta. Changudoa? Sidhani kama kuna mwanaume wa kumpenda changudoa. Lakini mimi nimekupenda wewe kama nilivyokupenda awali. Naomi nakuahidi na hata ukitaka kuleta mashahidi kamwe sitakuacha.” Alilalamika Walter. Hatimaye Naomi akaguswa wakafikia muafaka wa kwenda kupima afya.

Maajabu makubwa kwa Naomi, alipopimwa hakuwa na virusi vya Ukimwi. Alipima tena na tena hali ikiwa vilevile.
Mungu yu pamoja nami. Alikiri Naomi baada ya vipimo vyote kutoa majibu kuwa alikuwa salama.
Majibu hayo yalikuwa furaha kwa Naomi lakini kwa Walter alifungua ukurasa mwingine.
Akawaza ndoa.
Sasa waliweza kujadili na Naomi, hatimaye Naomi akatoa kauli.
“Walter, umeyabadili maisha yangu na bado unaonesha kunihitaji. Sipingani na wewe kuhusu ndoa lakini nina jambo moja tu….” Akasita, kisha akaendelea, “kwa heshima yako, sitahitaji kufunga ndoa mbele ya watu wengi, kwangu na kwako ni aibu kubwa. Kila mtu anafahamu Naomi ni kahaba. Sihitaji wewe uitwe mume wa kahaba. Tutafunga ndoa ya kiserikali, sihitaji kupiga goti mbele ya madhabahu na kufanya unafiki mbele ya Mungu. Mimi ni mchafu sana, naomba tuanze na hii ndoa ya kiserikali hiyo ya kanisani itafuata.” Alimaliza Naomi.

Walter alikuwa analingoja jibu la ndio, na sasa ni hilo lilikuwa limetoka, habari ya itafungwa wapi na wapi hayo yalikuwa mengine. Naomi alikuwa amekubali ndoa, hiyo ilitosha sana.

Walter alitamani sana baba yake mdogo angekuwepo katika mkataba huo wa ndoa ambapo alijifunga katika kipengele cha kutooa tena baada ya ndoa hiyo. Tatizo Frank alikuwa nje ya nchi, Oman nd’o alipohamishia shughuli zake kikazi.

Walter akajifunga na kuondoka na Naomi kuelekea jijini Kampala. Sasa wakiwa mume na mke.
Ukurasa mpya kwa wawili hawa.

BAADA YA MIEZI SITA.

Ujenzi wa nyumba ya kisasa ulikuwa umekamilika maeneo ya Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Ilikuwa nyumba ya Walter ambaye alikuwa jijini Kampala akiendesha maisha yake pamoja na mkewe Naomi.
Nyumba ilipokamilika, Walter aliandaa ufunguzi ambao ungehusisha jamaa na marafiki wachache.
Naomi na Walter wakarejea Tanzania.
Kama mtu alipata bahati ya kuonana na Naomi wakati akiwa changudoa, basi alihitaji jicho la tatu kumtambua mwanamama huyu aliyevaa mavazi ya asili ya umagharibi mwa Afrika hasahasa Nigeria.
Alikuwa mama haswaa.
Na alikuwa na kila hadhi ya kuitwa mke wa Walter.
Katika ufunguzi huo, ndugu wa karibu wa Naomi alikuwa ni Editha ambaye ni dada yake, baada ya Naomi kuwa katika mikono salama ya Walter Editha ambaye alikuwa muathirika wa virusi hatari vya Ukimwi alikuwa amepatiwa huduma stahiki na ilimwitaji mwendawazimu pekee kusema kuwa dada yule ni muathirika na anaishi kwa matumaini.
Ama kwa hakika pesa ni kila kitu.
Sherehe ilifana haswaa huku kwa upande wa Walter ndugu wa karibu zaidi akiwa ni Muga, yule mjomba wake wa Uganda.
Frank hakuweza kufika kutokana na kutingwa na shughuli nyingi za kikazi na hata familia yake alikuwa ameianzisha Oman. Frank alimtakia heri kijana wake. Huku akiahidi kumtembelea muda wowote.
“Nikija nikute mtoto.” Frank alimwambia Wallter katika simu.
Walter akabaki anacheka tu.

Majira ya saa nne usiku, sherehe ikiwa imepamba moto, wenye kula walikula na wa kunywa walikunywa huku wengine wakiumizwa na mafanikio ya Walter akiwa kijana mdogo.
Wasanii maarufu walialikwa, nao wakafika na wapenzi wao. Lilikuwa jambo la kufurahisha hakika.
Walter alimnong’oneza Mshehereshaji (Mc) ili aweze kumruhusu kusema chochote. Mshereheshaji akachombeza hapa na pale kisha akawasihi watu wote wakae kimya aweze kuzungumza.
Kimya kikatanda….
Walter akapewa kipaza sauti.
Kila mtu akangoja kumsikiliza kijana yule maarufu.
Akawasalimia na kuwauliza mawili matatu kisha akaendelea.
“Mafanikio pasipo na wa kuyafurahia mafanikio yako ni bure, mafanikio pasipo na jitihada na maamuzi pia hayawezi kukufikia, mafanikio yanahitaji jitihada. Nadhani wengi mnanifahamu na wengine mmenifahamu leo.
Nilitamani sana wageni wangekuwa wengi zaidi ya hapa, nilitamani waongezeke wageni wanne tu..kwangu ingekuwa furaha zaidi yah ii niliyonayo leo.
Ardhi ya Tanzania niliwahi kuichukia, niliilaani kwa mkasa ilionitendea.
Mkasa wa kumeza roho nilizozipenda nazo zikanipenda.
Nikiwa katika hatua yangu ya kurejea Tanzania kuishi tena kama zamani sina budi kushiriki nanyi kama ndugu zangu, uchungu mkubwa nilioupata baada ya wazazi wangu kufariki hakukutosha kabisa kuuponda moyo wangu, na bibi naye hii ardhi ikamtwaa, niliumia sana na nadhani moyo wangu ulikufa ganzi, nikabaki na dada yangu wa pekee ambaye naye alishindwa kuhimili mikikimikiki, akapatwa na mtindio wa ubongo, adhabu ya kutetereka kiakili kumbe haikutosha, ardhi hii ikamtamani hivyo hivyo akiwa na akili pungufu, ikammeza na kuamsha tena uchungu katika moyo wangu. Najitahidi kuwa na moyo wa kusamehe lakini mkono uliohusika na kifo cha Maureen sitakaa niusamehe, ni mkono huo umenitonesha na kuniacha na kidonda cha milele. Mkono uliosababisha nilie na kulaani.
Nililia kama mtoto, nikailaani Tanzania. Lakini sasa narejea nyumbani, hata nikikimbilia Marekani, moyo wangu utanisuta tena kwa Kiswahili ukinambia kuwa mimi ni mtanzania. Ninaumia sana lakini sina budi kuwa imara tena na kuamini kuwa haya yote ni mapito.
Kwa heshima ya mama, baba, bibi yangu na dada yangu mpenzi, Maureen nimeijenga nyumba hii kama heshima kwao. Nimeinyanyua kutoka katika ardhi iliyoamua kuwameza.
Maureen, mamii, dadii, bibi…popote mnapoisikia sauti hii tambueni kuwa mtoto mliyemuacha katika dunia hii ya mateso yu hai na salama lakini ana uchungu. Bibi yule mke uliyenipa tangu utoto nipo naye leo ninapokulilia, nimeliamini neno lako la tangu utoto na sasa nimetimiza ahadi….Naomi….Naomi mke wangu….wifi yako walimuua..walimuua” Walter hakuweza kuendelea kuongea akatokwa na kilio kikubwa sana.
Huku watu wakitegemea kuwa Naomi atambembeleza walishangaa akiwa ameganda tu.
Naomi alikuwa anatetemeka pia, alikuwa ana hofu. Simulizi ya kusikitisha iliyosimuliwa na Walter ilikuwa inamuhusu. Alikuwa chanzo pia cha uchungu anaoupitia Walter.
Kumbe yule Maureen aliyekufa alikuwa ni dada yake Walter.
Naomi akahisi kurukwa na akili.
Alichanganyikiwa haswaa. Alikuwa muuaji aliyekimbia mkono wa dola.
Naomi aliamini kwa asilimia mia, kuwa bila yeye kukimbilia katika starehe hakika Maureen angeendelea kuishi.
Patashika.
Amani ikatoweka.

Walter alitulizwa na Muga hadi akatulia vyema. Shughuli zikaendelea kama kawaida hadi ilipofungwa majira ya saa sita usiku.
Walter alikuwa karibu na mkewe. Wakaachiwa nyumba yao.
Kwa mara ya kwanza wakalala katika nyumba hiyo mpya.

Safari yao ya maisha ikaanza kubadilikia hapa.
Naomi akiwa na kumbukumbu ya maneno mazito kutoka kwa Walter kuwa hatakaa aisamehe mikono iliyohusika katika kifo cha dada yake. Alijikuta akiikosa amani na kuangukia katika dimbwi ambalo alikuwa ameshajitoa kitambo dimbwi la ulevi.
Nia ikiwa kupunguza mawazo. Mawazo magumu kabisa ya kuwa alihusika katika kifo cha wifi yake wa pekee. Hali ilikuwa mbaya sana.
Walter hakujua ni kipi kinaendelea. Lakini Naomi alikuwa amebadilika sana.
Alipojaribu kuhoji kwa kubembeleza alikuwa amefanya kosa kubwa sana. Naomi akagundua kuwa Walter alikuwa amekufa juu yake na hana dalili ya kutoka tena.
Ni hapo mshikemshike ulipoanzia na Walter kujikuta katika utumwa wa aina yake.
Alijaribu kufanya kila jambo ili Naomi akae sawa, haikuwezekana.

Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Naomi alitegemea kumfanyia jambo la kipekee sana. Lakini ajabu na kweli Naomi akamtia aibu, hakutokea ukumbini. Aibu kubwa sana.
Walter akaaminika kuwa alikuwa amelishwa vitu ambavyo vimeiteka akili yake.
Ukweli aliujua yeye tu kuwa alikuwa anampenda sana Naomi na hakuhitaji kuona anapotea tena kama awali.
Naomi alikuwa amechanganyikiwa, angeanza vipi kumweleza Walter kuwa anahusika katika kifo kile? Hakuwa tayari kumpoteza Walter ama kumliza tena.
Hakuwa na maamuzi na siku zilizidi kwenda, damu ya Maureen ikazidi kukitekenya kichwa chake. Ilikuwa ni aidha akiri kuwa anahusika ampoteze Walter ama aendelee kuishi na siri hiyo iliyovuruga kichwa chake.




Ni hapo mshikemshike ulipoanzia na Walter kujikuta katika utumwa wa aina yake.
Alijaribu kufanya kila jambo ili Naomi akae sawa, haikuwezekana.

Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Naomi alitegemea kumfanyia jambo la kipekee sana. Lakini ajabu na kweli Naomi akamtia aibu, hakutokea ukumbini. Aibu kubwa sana.
Walter akaaminika kuwa alikuwa amelishwa vitu ambavyo vimeiteka akili yake.
Ukweli aliujua yeye tu kuwa alikuwa anampenda sana Naomi na hakuhitaji kuona anapotea tena kama awali.
Naomi alikuwa amechanganyikiwa, angeanza vipi kumweleza Walter kuwa anahusika katika kifo kile? Hakuwa tayari kumpoteza Walter ama kumliza tena.
Hakuwa na maamuzi na siku zilizidi kwenda, damu ya Maureen ikazidi kukitekenya kichwa chake. Ilikuwa ni aidha akiri kuwa anahusika ampoteze Walter ama aendelee kuishi na siri hiyo iliyovuruga kichwa chake.

Maisha ya Walter yakabadilika na afya yake ikaporomoka.
Si kwa kuwa hakupata lishe bora lakini la!!
Ni mabadiliko ya Naomi mkewe. Walter hakuwa na mtu wa kumshirikisha, hakuwaamini marafiki wanaomzunguka kwani mara kwa mara waliwahi kumshauri afanye mpango wa kuachana na Naomi.
Walter aliwasikiliza na almanusura aingie mkenge lakini akiwa katika hatua za mwisho za kutimiza hayo akauvaa moyo wa Naomi na kujiuliza atajisikiaje punde atakapoipokea taarifa ya kuachwa.
Walter akakumbuka kuwa Naomi aliwahi kukataa katakata kuoana naye, lakini Walter akawa king’ang’anizi hatimaye ndoa ikafungwa kimya kimya.
Naomi akawa kila kitu kwa Walter.
Sasa amekuwa mzigo wa miiba.
Walter hana wa kumlaumu.
Jambo jingine ambalo lilimfanya Walter asifikirie kabisa kuachana na Naomi, lilikuwa suala la mtoto, hadi wakati huo Naomi hakuwa amebeba mimba.
Walter aliamini kuwa tatizo lipo kwa Naomi, lakini aliogopa kumweleza moja kwa moja kwa kuhofia kumwathiri kisaikolojia. Sasa maamuli ya kuachana naye yangeweza kumweka Naomi katgika hali ya kuhisi alikuwa ameachwa kwa sababu hazai.
Walter akauvaa uanaume halisi akasimamia msimamo.
“Nitaishi naye kwa shida na raha.”
Maisha yakaendelea.
Naomi akitulia siku tano, basi siku ya sita lazima asumbue na kisa kipya ama la akirudia basi ni mikasa yake ya maudhi.
Kunywa pombe na kulewa kisha kwenda kuwafanyia vurugu majirani na marafiki zake wa zamani.
Walter hakumbuki ni mara ngapi alimwekea dhamana Naomi baada ya kufikishwa mahabusu lakini anakumbuka kuwa ni mara mbili aliwalipa mawakili waweze kumtetea mahakamani baada ya kukamatwa na makosa ya kuendesha gari akiwa amelewa.
Huyu nd’o alikuwa mkewe wa ndoa ya kiserikali.

Tofauti na mtu yeyote ambaye angeweza kudhani kuwa Naomi anayafurahia yale ambayo anayafanya, haikuwa hivyo. Akiwa faragha Naomi alikuwa analia sana na kuomboleza kwa mambo mabaya anayomfanyia Walter na jamii kwa ujumla.
Walter alibahatika kukumbana na maajabu haya siku moja baada ya kuwa amemtoa mahabusu alikopelekwa kwa kosa la kumtukana matusi ya nguoni kiongozi wa kiroho aliyekuwa anahubiri barabarani kisha alipopita Naomi akiwa na kinguo kifupi akamsema kama mfano.
Japokuwa alikuwa anamjibu mwanzoni alipoanza kutukana kuwa ‘shetani yu kichwani mwake’ matusi yakamzidia. Naomi hakupata shahada ya kawaida ya chuo kikuu lakini katika matusi hapakuwa na la kumshinda.
Kozi ya kiingereza aliyosoma akiwa katika ndoa ilimwezesha kupanua msamiati wake sasa aliweza kutukana na kiingereza.
Nani kama Naomi, mtumishi akazidiwa akamshtaki Naomi. Naomi akakamatwa.
Walter akapewa taarifa.
Siku hii Walter alijifanya kichwa ngumu, akajaribu kutikisa kiberiti ili aone je Naomi ni wa thamani kwake ama la.
Akazuga kuwa hajali lolote.
Ni siku hii ambapo aliamini kuwa hawezi kuishi bila mlevi huyu.
Akiwa katika ofisi yake ya burudani, alishangaa haelewi chochote anachofanya.
Kila alichogusa alikuwa anakosea.
Akili iliganda na kumuaminisha kuwa hawezi kufanya kazi iwapo moyo anaoupenda u mahabusu.
Walter akachukua pesa za kutosha. Akaiendea gari yake, alipoiwasha akagundua kuwa hawezi kuwa makini barabarani.
Akakodi taksi.
Moja kwa moja katika kituo cha polisi.
Pesa ikakohoa, Naomi akatolewa.
Kwa kutumia teksi ileile Walter akizuga kuwa amekasirika alimpakia Naomi kisha akamlipa dereva ampeleke nyumbani.
Hakuandamana naye.

Akaiacha teksi iondoke ili aweze kurejea kazini.
Aliweza kurejea, lakini je? Kazi angeweza kuzifanya bila kumsikia Naomi.
Hapana ikawa ngumu.
Walter akafurahi kwa kuwa alikuwa amejiajiri, bila hivyo huenda angekuwa amefukuzwa kazi kwa sababu ya Naomi.
Akafunga ofisi na kuondoka zake.
Akafika nyumbani.
Kimya kimya akaenda hadi katika mlango wa chumbani kwa kunyata.
Kilio kilisikika, na kuna maneno yalikuwa yakitamkwa na Naomi.
Naomi alikuwa anamlilia Mungu, alimlilia kwa maisha anayoyaishi, alikuwa anajuta kwa anayomfanyia Walter. Aliapa kuwa anampenda Walter kuliko wanaume wote duniani, lakini anajuta kumpenda.
“Kwanini Mungu haunipi japo chembe ya furaha? Hukunipa nafasi ya kuelimika darasani, umeninyima na nafasi ya kufurahia maisha, basi ungeniacha nife tu, ungeniacha kabisa nisikutane na Walter, kwa nini umempa mzigo huu mtakatifu huyu?? Kwa nini umempa zawadi hii mbaya. Zawadi isiyobebeka. Nitafanyaje sasa mimi, ni wewe ujuaye uchungu ninaoubeba, unajua naumia kiasi gani, unajua kuwa sipendi nilivyo. Mimi si msafi mbele yako lakini iweke huruma yako kwangu walau niupate ufumbuzi wa tatizo hili. Siwezi kuishi nikiwa hivi!!” alilia sana Naomi, Walter akiwa msikilizaji.
Kati ya siku ambazo upendo ulijifunga moja kwa moja na kuwa katika damu ya Walter ni siku hii. Hakuwahi kuamini kama Naomi alikuwa anampenda kwa dhati. Alidhani anajilazimisha, sasa leo hii anamsikia akisema na Mungu wake.
Akamtaja na yeye kuwa ni mwanaume wa kipekee.
Walter akawalaani marafiki waliowahi kumshauri kuwa Naomi hamfai na wala hampendi.
Walter akarejea sebuleni na kuugonga mlango kana kwamba ndio alikuwa amefika.
Naomi akachelewa kama dakika tano kisha akafika kuufungua mlango ambao ulikuwa umeegeshwa tu.
Tayari alikuwa amenawa uso wake. Ilikuwa ngumu kutambua kuwa alikuwa ametoka kumwaga machozi.
Walter akamkumbatia na kumbusu shavuni.
Baada ya kuvua nguo za ofisini, aliingia jikoni, akaandaa pishi la mchemsho wa samaki, ambalo lilipendelewa sana na Naomi.
Kisha akampelekea huko huko chumbani.
Naomi akatabasamu huku akikwepesha kumtazama Walter machoni, kwani kwa kufanya hivyo lazima angepitiwa na kumwaga machozi jambo ambalo Naomi hakutaka litokee.

****
Usiku ulikuwa tulivu sana. Walter alikuwa akicheza karata na Naomi, walikuwa na furaha sana siku hiyo. Baada ya kushindia ufukweni sasa walikuwa nyumbani hakuna aliyekuwa na usingizi.
Majira ya saa tatu usiku mlango ukagongwa ishara ya mtu mlangoni.
Haikuwa kawaida kabisa kwa mji huu kupata wageni usiku.
“Anayemfunga mwenzake nd’o anaenda kufungua mlango..” Walter alimtania Naomi baada ya kuona kuna kila dalili ya kufungwa katika awamu ile.
“We chizi kweli, kwa hiyo anayegonga aendelee kusubiri..kwa taarifa yako sikufungi.” Naomi naye akajibu kiutani.
Walter akasimama na kuliendea geti.
Akauliza nani mgongaji, akajibiwa na sauti nzito ya kibabe.
“Baba Farida.”
Walter akafunua kitundu kidogo na kumchungulia.
Hakika alikuwa yeye baba Farida. Upesi akalifungua geti lote.
Akamrukia kwa furaha kubwa huku akipiga mayowe.
Naomi akasikia akatoka mbiombio na kukuta wanaume wawili wakiwa wanashangaana.
“Baba Farida aaaah…..vibaya ulivyonifanyia yaani eeeh dah si jambo zuri hata kidogo. Utaniua kwa presha mwenzako.” Alilalamika Walter. Yule mwanaume akawa hana jipya zaidi ya kucheka.
Ndevu zake nyingi kidevuni zilianza kuwa nyeupe, uzee ulikuwa unajongea.
Alizivuta vuta ndevu zake kwa mkono mmoja huku mwingine ukiambaa katika kitambi chake.
“Ama kwa hakika duniani hakuna wembamba.” Walter alikiri.
Akalichukua begi na kuliingiza ndani ya nyumba, nyuma yake akafuatia Naomi na baba Farida.
“Hamis….umetisha, kwanza shkamoo.”
“Marhabaa….” Aliitikia.
Sasa walikuwa sebuleni.
“Mamaa…huyu ni mlezi wangu, anaitwa Hamis..muite baba Farida anapenda zaidi……Mzee huyu nd’o mkweo..mama Walter.” Alitambulisha Walter wote wakashukuru kufahamiana.
Yule mzee wa kiislamu akawatakia heri.

Maongezi yaliendelea lakini Hamis alikuwa na mashaka, kuna jambo lilimtatiza na aliungoja upenyo aweze kulilipua na kubaki huru.
Aliyekuwa mbele yake alikuwa kama aliwahi kujitokeza katika maisha yake na kisha kutoweka kama upepo ambao bado unahitajika sana.
Lakini huyu alikuwa amenawiri sana.
“Au ni dada yake?” alijiuliza. Hakupata jibu.
“Walter hajui lolote inamaana?” swali jingine akajiuliza.

Majira ya saa sita usiku, Naomi aliaga kuwa anakwenda kulala.
Mzee huyu ambaye aliwahi kuishi Tanzania, kisha akatoweka na kwenda kufanya biashara za mafuta uarabuni kisha kupata mwenza na kuzaa naye hukohuko. Hatimaye akatakiwa kumuoa, akalazimika kubadili jina na dini na hatimaye akajiita Hamis, wakamwita mtoto wao wa kike Faridah.
Akafumba macho yake na kujenga hoja upya kabla hajaifikisha kwa Walter. Akajirejesha miaka kadhaa nyuma ambapo hakuwa na ndevu nyingi na hakuwa akivaa kibalaghashia, akazikumbuka enzi za kwenda kanisa jumapili pekee, akazisahau enzi hizi za swala tano na kufunga ramadhani, Hamis akauvua usasa akauvaa uzamani ili aweze kupata jibu sahihi.
Hamis akarejea kuwa Frank. Baba yake mdogo na pia baba mlezi wa Walter ambaye aliwazika wazazi na bibi wa Walter kisha akamzika na Maureen dada yake Walter huku akijilaumu kwa kumwamini msichana wa kazi na kumwachia nyumba.
Machungu hayo yalimfanya aikimbie Tanzania kwa gia ya kutafuta maisha zaidi.
Hatimaye amerejea kumsalimia na kumwona mke wa mwanae.
Amerejea akiwa ‘mufti’ haswaa.
Lakini anakutana na sura tatanishi ya mke wa Walter.
Sasa anajiuliza je yule ni Naomi muuaji ama ni dada yake Naomi, ama nd’o mambo ya duniani wawiliwawili?
Aliamua kufumbua macho yake, akakutana na Walter akitabasamu.
Hamis akaamua kuutafuta ukweli.
“Walter amemuoa muuaji??” swali hili lilimuumiza.

**FRANK anayeamini NAOMI alimuua MAUREEN ana kwa ana na WALTER…anahitaji kumuhoji juu ya mkewe….UKWELI dhidi ya HISIA ……kipi kitamzidia WALTER????
Hili ni JERAHA la namna yake, lisiloonekana machoni lakini ni hisia zinazoweza kukuvuruga akili…..
ITAENDELEA

Post a Comment

0 Comments