Sikufahamu ni pepo gani lilinivaa siku hiyo kwani sikutaka kukaa na marafiki zangu wala kupiga soga kama ilivyo ada kila nitokapo mihangaikoni, nilichokifanya ni kujifungia chumbani mwangu nikampigia simu mpenzi wangu: Sabrina, kwa lengo kubwa la kumuona.
Ni kana kwamba nilikuwa na kiu mbaazi na haikuwa na mbadala. Nadhani ni kwasababu sikumuona mwanamke huyo kwa takribani siku kadhaa.
“Hallow dear!” Nikasema punde tu niliposikia sauti ya kuashiria nimepokelewa.
Sikujua tabasamu lilitokea wapi, lilinivaa ghafla niliposikia sauti yake.
Kinyume kabisa na nilivyodhani, ilikuwa ngumu kumshawishi akaridhia. Muda ulikuwa umeenda, jua lilikuwa dhoofu kukaribisha giza la usiku. Lakini aidha kwa kuhofia kunikwaza ama kwakuona hitaji kubwa ndani ya sauti yangu, alikubali. Tulipeana miadi ya kukutana mgahawa fulani ambao umbaliwe ulitugharimu kama nusu saa kuwasili.
Sikujali nikatumia vijisenti vyangu kununua juisi na vitafunwa kadhaa. Nilifurahi mno kumtia machoni. Sauti yake ilikuwa kama chakula fulani kilichojaza sehemu iliyokaliwa na upweke na uchovu wangu wa siku nzima. Tulisogeza muda na simulizi mbili tatu zilizosindikizwa na matabasamu mwanana na vicheko vilivyoshiba. Ila kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusogea, haja ikashinda ustaarabu. “Sabrih!” Nilimuita nikimtazama ndani ya macho, akaitikia akinitazama na jicho lililozidi kunisisimua. “Unajua ni muda mrefu mi nawe hatujaonana.” Nilisema hivyo tu nikiacha mengine yamaliziwe na macho yangu.
Alitabasamu akatazama chini kabla hajaurudisha uso wake na kunywa fundo moja la juisi. “Sasa mpenzi mbona hilo haliwezekani?” Alisema akitikisa kichwa. “Kwanini?” Nikawahi kuuliza. “Nipo kwenye period mpenzi!” Akanijibu.
Kana kwamba sijasikia vizuri, ama labda nikitegemea anaweza akabadilisha mawazo, nikarudia kauli yake kwa kuuliza: “Upo kwenye period?” “Ndio!” Nilijihisi uso wangu umekuwa wa baridi ghafula. Mate yalikauka mdomoni. Upesi mawazo yalinitinda namna ya kukabili hamu iliyokuwa imenikaba. Japokuwa nililazimisha tabasamu usoni, liligoma kabisa.
Sabrina aligundua mabadiliko hayo. “Vipi mpenzi?” “Poa tu dear.” Nililijibu na kutanua lips mithili ya mtu anayetabasamu.
Story ziliisha. Muda haukupita sana, tukaachana kila mtu arudi alipotokea.
Ingali ni njiani kujirudisha chumbani mwangu nikiwa sasa na uchovu maradufu, bahati mbaya ama nzuri nikakutana na mwanadada mmoja niliyehitimu naye elimu ya shule ya msingi, kwa jina Rehema ama Rey kama alivyofahamika na wengi. Ni mdada aliyekua kiranja mkuu shuleni kwetu, lakini zaidi jambo kubwa nililokuwa nalikumbuka kumhusu ni kwamba alikuwa ananipenda mno japokuwa utoto wangu ulikuwa ni kikwazo kikubwa kwake.
Alifurahi sana kuniona. Japokuwa ni miaka mingi ilipita tukiwa tumebadilika kimwili, macho yake makubwa yenye umbo la nyoka hayakunisahau kabisa. Alikuwa wa kwanza kuniona akapaza sauti yake kana kwamba ameona simba mwituni.
“Sio mbaya.” Alinipokea na kuongezea: “Vijana wengi tuliomaliza nao shule sasa hivi wapo mitaani, wengine wanavuta unga na mabangi.”
Kwa namna moja ama nyingine nikapata ahueni.
“Sasa tunaweza tukakaa eneo fulani, tukala, kunywa na kupiga vijistori vichache?”
“Mmh sidhani. Nina haraka kidogo, si unajua muda umeenda.”
Ilikuwa ni majira ya saa tatu sasa tena ya katikati.
“Jamani, basi naomba namba yako, nitakutafuta.”
Nilimpatia namba tukaagana, nikaelekea zangu maskani mwangu. Siku ikapita.
Asubuhi na mapema kesho yake Rehema alinipigia simu akinitaka tuonane. Kabla ya kuchukua maamuzi yeyote nilimpigia mpenzi wangu Sabrina kumjulia hali.
“Hatuwezi kuonana kabisa, Kelvin. Period inanipelekesha sana isitoshe ndio kwanza imenianza jana, hivyo wiki hii nzima nitakuwa katika hali hii. Nakuwa na hasira sana so sidhani kama itapendeza tukionana.”
Nilimkubalia Rehema tukutane, akashauri muda wa jioni akitoka kazini na iwe maeneo fulani hivi ya starehe, gharama zote zikiwa juu yake.
Muda ulifiika tukafurahi sana hiyo siku kwa kula, kunywa na zaidi kukumbushana yale ya zamani tukiwa shuleni. Kila mmoja wetu alirudi na tabasamu usoni. Angalau nilipata sababu ya kufurahi siku ile kinyume kabisa na namna nilivyokuwa najisikia baada ya kuongea na Sabrina mapema siku ile. Nilitokea kuamini kwamba sio kila nyota njema huonekana asubuhi, hata za jioni pia zaweza kubadilisha siku dhoofu.
Lakini japokuwa mie na Rehema tulifurahia sana siku hiyo, nilikumbana na kibarua kizito cha kumuondoa mwanamke huyo kwenye mstari wa kunishawishi kimapenzi. Utu uzima dawa, wahenga na washenga walishasema, haikuniwia vigumu kutambua kwamba Rehema alinihitaji kimapenzi. Jinsi alivyokuwa ananitazama, na muda mwingine alivyokuwa ananiongelesha kulinipa ishara ambayo sikuhitaji kujiuliza sana kulithibitisha.
Kazi niliyokuwa nafanya kila alipokuwa anaelekea upande wake wa kushoto ni kubadilisha mada upesi. Sikuwa tayari kabisa kumsaliti mpenzi wangu, Sabrina. Sikutaka kufanya tumbo lake la period liwe kama mbolea ya maovu yangu. Nilimpenda na bado niliona anastahili kuthaminiwa.
Siku zikasonga: wiki na miezi ikakatika, bado Sabrina akawa ananiambia yupo kwenye siku zake, bado tumbo linamsumbua!
Mie si mtaalamu wa mambo ya afya, ila kwa hili nilianza kupata shaka na wasi. Ni tumbo la aina gani hili?
Hali hiyo ya ugaga ilinisukuma nifanye kautafiti kadogo ka’ chini kwa chini juu ya mpenzi wangu huyo. Nilitaka nijue nini haswa ni shida. Nilitaka kujua wapi mambo yameenda kombo. Ila laiti kama ningejua nini ningeligundua, basi nisingelijisumbua kufanya hilo zoezi.
Nilikuja kugundua mpenzi wangu: Sabrih, ni mjamzito. Aibu yake ndio haswa inayomkimbiza asitake kuonana na mimi kwa kufahamu fika kuwa ile mimba si yangu bali ni ya kijana mmoja mtaani aitwae Moses, mtoto wa mwenyekiti wa mtaa. Shukrani ziwaendee marafiki zake Sabrih na baadhi ya vijana mtaani ambao pasipo kuficha walinieleza ukweli huo mchungu.
Nilijihisi mwili umepoteza nguvu. Joints zote zilifeli ziikashindwa kunibeba. Damu ilinichemka kichwa kikanigonga vibaya mno.
Siwezi kueleza ni kwa namna gani niliumia maana hakuna maneno ambayo yanaweza kubeba hisia hizo nzito. Nilimpenda sana Sabrina, na nilimchukulia kama mwanamke wa ndoto ya maisha yangu. Sikujua kama alikuwa ana nguvu kubwa kiasi kile kwenye kuniumiza. Machozi yalinichuruza kila nilipojilaza kitandani mwangu, nikalowesha godoro. Nilishindwa kuzuia ulimi wangu kuonja uchungu kila nilipotizama picha zake nilizozibandika kwenye kuta za chumba changu, ikabidi niziondoe. Japokuwa kufanya hivyo bado haikutosha kusuuza nafsi yangu dhidi ya chuki na maumivu.
Lakini siku hazigandi, zikaendelea kupita.
Sikuwa na jinsi mbali na kufanya jitihada za kumsahau Sabrina. Tendo ambalo sikuwahi kutegemea kama n’takuja kulitenda maishani.
Nilikukosea nini lakini Sabrina?
Wakati huo nikiwa njia panda, ndio Rehema alipopata mwanya wa kuuteka moyo wangu wenye jeraha na kuuweka kwenye himaya yake.
“Naomba sasa unipe nafasi hii ambayo nimenyimwa kwa muda mrefu sasa.”
Maumivu aliyoniachia Sabrina yalinikimbiza haraka kwa Rehema kupata dawa na allijitahidi sana kupuuzisha akili yangu, akafanikiwa. Ukurasa mpya wa maisha ukafunguliwa. Niliishi kwa mwanamke huyo. Nilimsahau kabisa Sabrina aliyenitesa na kuniumiza. Maisha yalienda vizuri sana kati yangu na Rehema, amani na upendo vikipamba siku, majuma na miezi.
Mambo yalikuja kuanza kwenda kombo pale nilipoanza kubadilika na kudhoofu kiafya.
Nilishangazwa sana na hayo mabadiliko yaliyochukua nafasi kwa haraka ndani ya mwili wangu. Hali hiyo ilinipelekea niwahi hospitali kujua hasa nini tatizo. Nilipopima, majibu yakatoka nina Gonorhea, kubwa ya yote virusi vya ukimwi!
Sikumbuki kama kuna siku nilichanganyikiwa kama ile. Sikutaka kuamini yale majibu kabisa, nilimbishia daktari japokuwa kila kitu kwenye karatasi ya majibu kilionyesha ni ya kwangu.
Mungu wangu, sasa nakufa! Nilishika kichwa. Nilikaa kwenye benchi, nje ya chumba cha daktari bado sauti ya daktari ikinirudia masikioni mwangu kunitangatazia yale majibu.
Niliona siku zangu za kuishi duniani zinahesabika. Roho iliniuma. Akili ilianza kutafuta nani aliyenipeleka kwenye tanuru hilo, upesi jibu likaja Rehema. Roho ya unyama ikanivaa. Nilirudi nyumbani, njia nzima nikifikiria ni kipi cha kufanya kumuadhibu mwanamke yule aliyezawadia kifo. Nilimkuta yupo chumbani, bila ya salamu nikaelekea jikoni kuchukua kisu kisha taratibu nikanyookea chumbani kwa lengo la kuua.
Niliupiga teke mlango nikamrushia Rehema macho yenye uchu wa kunyofoa roho huku nikihema kwa nguvu.
Alishituka. "Kev, vipi mbona umeshika kisu?” Sikusema kitu. Nilimsogelea nikimkazia macho. Alipiga kelele, lakini sikujali. Nilipomfikia nilimkamata, nikashindilia kisu kwa nguvu kifuani mwake kisha nikamuacha akiwa anatapatapa kama kuku aliyekatwa kichwa. Baada ya kuridhia kwamba amekata roho, nilipotea lile eneo haraka nikaelekea kwa rafiki yangu Jobu maeneo ya Tandale nilipolala kwa hiyo siku, fikra zangu bado zikiwa zimefungwa na lile tendo la kinyama nililolifanya. Nilifikiria mara mbilimbili juu ya lile tukio kuanzia mwanzo mpaka mwisho nikaona bado nitakua sijaitendea haki roho yangu endapo nikimuacha Sabrina hai, ndio, yeye ndiye aliyenifanya nidumbukie kwenye penzi la yule mshenzi, Rehema, aliyenizawadia virusi vya ukimwi.
Niliapa kumtafuta Sabrina kwa udi na uvumba, bila kumsahau mshenzi wake aliyemlaghai na kumpa mimba. Nilingoja tu usiku uishe kesho nikafanye unyama mwingine kwani usingizi ulikua hauji kabisa zaidi ya kuhesabu pingili za bati.
“Siwezi kufa peke yangu, lazima wote wafe na mimi.” Nilitia nadhiri.
Asubuhi ilipowasili, sikupiga mswaki wala kunywa chai. Niliunyanyua mwili wangu na kubeba kisu cha rafiki yangu Jobu tayari kwa mauaji ya watu wawili walio kichwani mwangu, Sabrina na hawara yake, Moses, wakajiunge na mwenzao aliyetangulia jehanam ambaye tayari alishapamba vichwa vya habari vya magazeti ya udaku.
‘MFANYAKAZI WA WIZARA YA UHAMIAJI AUWAWA KWA KISU!: Mpenzi wake atokomea.’ Gazeti mojawapo lilisomeka hivyo.
Wakati nikiwa kwenye daladala, nilimpigia Sabrina simu. Kwa sauti ambayo asingebashiri dhamira yangu niliongea naye nikamuuliza yupo wapi. Bahati mbaya kwake akanielekeza. Alikuwa ufukweni anafanya mazoezi. Kwa kuniona mjinga akanambia eti yupo na kaka yake. "Yule mkaka wa pale mtaani." "Yupi? – Moses?" "Nd – io! Umejuaje?" Nilisikia mkuki wa moto umenichoma alivyoniuliza hivyo. Hasira zilinipanda mno kichwani. Gubu lilijaza moyo wangu nikawa napumua kwa shida. Nilijihisi nachelewa huko beach. Nilitamani nilisukumize gari ama nishuke nikimbie kwa miguu!
Tena wapo pamoja! Bahati iliyoje? Nilijikuta natabasamu kishetani. Kazi ilikuwa rahisi kuliko nilivyodhani.
Mwishowe gari lilifika nikashuka na kuanza kuelekea ufukweni. Macho yangu yaliangazaangaza kuwatafuta watuhumiwa wangu, kwa mbali nikawaona wakirushianarushiana maji ya bahari na kukimbizana kimahaba. Taratibu nikaanza kuwasogelea.
Roho ilikuwa inauma. Jasho lilinitiririka nisijue limetokea wapi.
Hakika nilihisi kifo kinawastahili. Yani wanayafanya haya mambo mie nikiwa hai? Hata kama huyo Moses kanizidi uwezo hawezi kunichezea kihivyo, nilisema na moyo wangu kisu kikiwa nyuma ya mgongo.
Nilipokaribia sikuwashitua. Nilikaa chini na kuendelea kuwaangalia mpaka pale Sabrina aliponiona na kunifuata akimuacha Moses akichezeachezea maji ya bahari.
Macho yangu yalitua tumboni mwa Sabrina na kushuhudia ujazo wa ujauzito. Nikajikuta nasema:
"Hili ndo tumbo la period unh?" Nikaishia kutabasamu. "Mbona watabasamu mwenyewe?" Aliniuliza aliponifikia.
Nilimkata jicho kali, nikakunja ndita. Haraka nilinyanyuka na kuchomoa kisu changu nikakididimiza kwanguvu kwenye tumbo lake.
Alipiga kelele zake za mwisho. Nilitabasamu nikamuambia:
"Ulidhani nilivyoacha kukutafuta nilikuacha ufanye mambo yako, sio?”
Nilimtupia chini kama mzigo tayari kwa kumkabili Moses mtu wa pili kwenye orodha yangu. Mkono wangu uliobeba kisu ulikuwa unachuruza damu nzito ya Sabrina. Macho yangu yote yalimtizama Moses aliyekuwa anatetemeka kwa hofu. Ni wazi hakuamini alichokiona. Alitoa macho kutizama maiti ya Sabrina iliyokua inalowesha mchanga wa bahari kwa damu huku akirudisha miguu yake nyuma, mdomo akiuachama kwa bumbuwazi.
Bila ya hofu, nilimfuata nikiwa nimefura. Sura yangu ilieleza hasa nilichokua nacho kichwani, ni mauaji tu hakuna kingine! Nilisaga meno nikichanganyia mwendo kuelekea kwa Moses aliyeanza kukimbia kuokoa maisha yake.
Bila kuchoka nilimkimbiza. Aliniitia kelele za majambazi lakini sikujali.
Ila ghafla nikiwa mbioni, nilisikia kitu kizito kimenigonga kichwani kwa nguvu, nikaanguka. Kabla sijafanya lolote, mwili wangu ulianza kushambuliwa kwa kipigo kizito na watu nisiowatambua nikisikia sauti zikitangaza mie ni jambazi.
Sikupewa hata muda wa kusikilizwa wala kujitetea. Makelele yangu niliyoyapiga hayakunisaidia chochote. Nilichuruza damu mno kichwani vilevile baadhi ya sehemu zangu za mwili zilivuja lakini haikuwafanya wapunguze wala kuacha kunishushia kipigo. Ni Polisi ndio waliokuja kuniokoa, japokuwa haikunichukua muda mrefu nikapoteza fahamu. Nilipokuja kuzipata nilijikuta hospitali na pingu mkononi. Bandeji zilijaza kichwa na maumivu makali mwilini ambayo sikuwahi kuyapata toka nizaliwe. Kila sehemu ya mwili ilikuwa inaniuma na kuchonyota vilivyo.
Niligeuza shingo upande wa kushoto nikamuona polisi ameshikilia bunduki akirandaranda. Nilipoirudisha shingo ilipokuwa, nilimuona daktari wa kike anasogea karibu yangu. Alitabasamu kwa mbali, akaniuliza, "Unaendeleaje?" Sikumjibu kitu. Mdomo wangu haukuniruhusu nifanye hivyo. Ina mana hakuliona hilo? Nilimtikisia tu kichwa na kumpandishia nyusi. "Pole sana!" Alinihurumia. Aliondoka sura yake ikionesha kubeba mashaka na maswali. Nilihisi hali yangu niliyomo na yule polisi aliyebeba bunduki vilimtisha. Hata mimi viliniogofya pia. Vilikuwa ni vigeni kabisa machoni mwangu, pingu mkononi na bunduki havikuwa vya kawaida kwenye mboni zangu.
Taratibu nilivuta kumbukumbu zikaja na kunijuza kwanini nilikuwa pale. Nilijikuta moyo wangu haujaridhika kabisa, hata kidogo. Kumuacha Moses hai kuliniumiza zaidi. Tena nilivyojiona katika ile hali ya kuwa chini ya ulinzi ndio roho ilizidi kuvuja damu kwani nilifahamu fika ndoto zangu za kummaliza mwanaume huyo zitakuwa zimeteketea.
Hapana, siwezi kukubali! Nilitikisa kichwa. Lazima nitafute njia. Sijali ni ya aina gani ila lazima nimuue Moses, kwa vyovyote vile! Lazima nimtangulize jehanam ninapoelekea muda si mrefu.
Kuwa kwake hai kilikuwa ni kitu kibaya sana kwangu. Sikutaka kukiona, kukihisi wala kukisikia. Nilimchukulia kama adui yangu mkubwa aliyebaki hivyo kumuua ilikua ni wajibu wangu. Sikutaka kufeli kwenye hilo.
Ila sasa nitafanyeje?
Wakati nikiwa fikirani, nilizisikia sauti za kike zinateta. Kutokana na maumivu niliyozawadiwa mwilini sikuweza kujitengenezea na kuwatizama vema hivyo nikaacha masikio yangu yafanye kazi yake, nilihisi mimi ndio mada iongelewayo.
“Litakuwa jambazi!" Sauti moja ilisema. “Umejuaje Grace?" "Ndo’ hivyo! We huoni alivyokung'utwa? Alafu analindwa na askari, pingu mkononi. Tena nahisi atakuwa na hirizi bila hivyo angeshakufa.”
Nilipandwa na hasira lakini niliona hazina msaada wowote kwangu kwa muda ule, hivyo kupuuzia yale maongezi ikawa ndio suluhisho kubwa nililolichukua, angalau likanipa unafuu.
Giza liliingia, asubuhi pakakucha. Giza likaingia, asubuhi pakakucha. Siku zikajongea kama kawaida, nikaanza kupata angalau unafuu kwa kupungua uvimbe na kupona baadhi ya majeraha. Niliweza kujisogeza sasa toka eneo moja kwenda lingine kitu ambacho sikuweza kukifanya hapo mwanzoni. Lakini bado kwa muda wote huo nilikuwa chini ya ulinzi wa polisi.
Nilijisikia faraja kurudi katika hali yangu ingawa haikuwa hali yangu ile ya mwanzoni kabisa. Nilikuwa na makovu na majerah mengi mwilini yaliyonifanya niwe na mabakabaka mithili ya kenge, lakini nilimshukuru Mungu kwa kuwa hai. Niliona nimepewa tena nafasi ya kutimiza ndoto zangu. Si zingine, bali za kumuua Moses!
Kwa makini na taratibu nilianza kupanga mipango ya kutoroka mule hospitali kabla sijapona vizuri, nikiweka wazo kichwani kwamba muda si mrefu naweza nikapelekwa kifungoni, na sitopata nafasi ya kutimiza ndoto zangu.
Hatimaye nilipata mbadala wa kufanya. Niliona siku nzuri ya kutoroka ni siku inayofuata pale nitakapokuwa nafanyiwa upasuaji wa kuondolewa vyuma miguuni. Kwa hamu kubwa, nikaingojea hiyo siku, ikawadia.
Niliingizwa ndani ya chumba cha upasuaji kilichokuwa na madaktari wawili wa makamo ambao nilijua hawatonipa shida. Askari alibaki nje na bunduki. Vifaa vya upasuaji viliandaliwa na kusogezwa kwa ajili yangu, ila kabla chochote hakijafanyika, nilinyanyuka haraka nikakwapua kisu cha upasuaji na kuwaweka madaktari chini ya ulinzi.
Niliwaamrisha wanyamaze kimya, wakatii. Nilimshikia kisu daktari mmoja mgongoni nikamuamuru afungue mlango na kumuita Afande. Akatii. Afande aliitwa, alipoingia tu, haraka niliuvuta mkono wake uliobeba silaha nikauchoma na kisu, silaha ikadondoka chini ikisindikizwa na kelele kali za maumivu toka kwa Afande, sasa bunduki nikaishika mimi.
Nilichana pazia nikawaamuru wajifunge nayo mikono na miguu, wakatii amri. Nilivyoridhika na hali iliyokuwepo nilijiondoa eneo hilo haraka nikilenga kutafuta geti.
Nilipofika tu getini nikasikia sauti kali ya filimbi.
Niliongeza kasi ya mwendo, walinzi wakanitilia mashaka. Walijaribu kunisimamisha lakini sikusimama hivyo wakaanza kunikimbiza. Nilikimbia kadiri ya uwezo nikiuvuta mguu wangu wa kushoto wenye chuma. Sikuwa radhi kupoteza ile nafasi. Nilijikakamua dhidi ya maumivu alimradi niokoke.
Pap! Haraka nikajichanganya kwenye umati wa watu ulionificha vilivyo na kuwapotea walinzi wale wa hospitali. Nilipokutana na barabara ya lami nikakwea gari likanifikisha nielekeapo na kumkimbia kondakta nisilipe nauli.
Sikuwa na haja ya kuremba, nilifahamu kuwa mimi ni ‘WANTED’ na ile fursa niliyoipata ni kama ngekewa hivyo ni wajibu wangu niitendee haki. Nilipiga moyo konde na kushusha pumzi ndefu, nikaanza kutembea kwa uangalifu huku nikielekezea sura yangu chini, mwilini ukivishwa na nguo zenye maandishi ya hospitali nilizopewa baada ya za kwangu kutotamanika.
Kumbuka muda wote huo nilikuwa na ile bunduki ya polisi. Nilikuwa nimeifichama ndani ya suruali na juu nikiiwekea mkono.
Macho huku na kule, kushoto na kulia mpaka nilipojibanza kwenye ukuta fulani uliokaribu na nyumba ya wakina Moses. Kazi kubwa niliyokuwa nayo ilikuwa ni kujichunga na kuzuga kila watu walipokatiza ili nisifahamaike.
Lakini kuna kitu nikakigundua upesi kwa mda mfupi niliokaa hapo, na kitu hicho kilipa maswali kichwani. Ni kwamba watu wengi walikuwa wanakatiza, haswa wakina mama wakijitanda khanga, wakiteta na huku nyuso zao zikibebelea huzuni. Nilitaka kujua kilichokuwa kinaendelea lakini kwa wakati huohuo nifiche utambulisho wangu hivyo nilimuita mtoto mmoja aliyekuwa anapita, kwa makadirio alikuwa ana miaka kama kumi, nikamuuliza: "Eti, kuna nini huko mbele?" Huku nikinyooshea kidole. Akanijibu upesi: "Kuna msiba!" "Nani kafa?" "Mi simjui jina, mkaka mmoja hivi mtoto wa mwenyekiti!"
Moyo ulitulia ghafla alafu ukaanza kukimbia mbio.
Haiwezekani! Nilijikuta nasema mwenyewe. Nilijua fika Moses ndiye mtoto pekee wa mwenyekiti wa mtaa wetu, sasa amekufa?
Nilitikisa kichwa changu kisha nikamuuliza tena yule mtoto, "Amekufa lini?" "Sijui! … jana mama yangu alimwambia dada kuna msiba, mtoto wa mwenyekiti amejinyonga." Nikazidi kuduwaa. "Alafu wakawa wanasema eti alikuwa na ukimwi!" Alimalizia yule mtoto na kuondoka zake. Hapo ndipo nikaishiwa na nguvu kabisa. Moses alikuwa na virusi vya ukimwi! Ina mana aliyeniambukiza ni nani? Rehema au Sabrina?
Baada ya upembuzi wa haraka nilipata jibu. Kama Moses angekuwa ndiye mwenye virusi vya ukimwi asingekuwa na haja ya kujiua, hivyo basi nae aliambukizwa kama mimi. Ina mana Sabrina ndiye aliyetuambukiza!
Na sio Rehema kama nilivyodhani!
Mungu wangu, nini nimefanya sasa?
Hakika nilikuwa mkosefu mkubwa, kwanza nilimuambukiza mdada wa watu virusi vya ukimwi nilivyopewa na Sabrina na kama hiyo haitoshi nikamuua kabisa!
Chozi liliniteremka.
Nilihisi moyo umekuwa mzito na mchungu. Niliishiwa nguvu kabisa nikaketi chini.
Sabrina mama, ulinizawadia lini kifo hiki?
Sikutoka hapo mpaka pale nilipoonekana na kukamatwa, nikapelekwa kituoni.
Nilipewa hukumu yangu ya maisha tena pasipo kumsumbua hakimu kwa kumueleza kila kitu.
0 Comments