Header Ads Widget

Responsive Advertisement

WASHUKURU "MABUNDI"



WASHUKURU "MABUNDI"

Twende sasa moja kwa moja kwenye kile ambacho nimekusudia kukushirikisha wakati huu. Nimefikiria kukusimulia kisa maarufu sana duniani. Ndiyo, ni kisa maarufu na kimesimuliwa kwa miaka nenda rudi. Lakini leo nimeamua nikusimulie kwa namna ya pekee ambayo haijasimuliwa na watu wengi. Siyo kwamba natia swaga! Hasha, nakupa kitu ambacho ulikuwa unakikosa, pengine ulitamani kukisikia. Sasa msimuliaji nipo hapa, weka umakini.
Hiki ni kisa cha kijana mmoja mdadisi sana aliyeamua kufanya utafiti. Utafiti wenyewe ulikuwa ni kuchukua yai la tai na kumuwekea kuku ili aone nini kitatokea! Baada ya majuma matatu alianguliwa tai mzuri sana.
Tai huyo alilelewa na kuku pamoja na vifaranga wa kuku. Alikula na kuchakura kama kuku. Pia aliruka umbali mdogo kama kuku na kufanya kila kitu alichofanya kuku.
Ilikuwa baada ya muda mrefu kupita, ndege mmoja mwenye busara alikuwa akipita akamuona tai akiwa na kundi la kuku akila, kucheza na kufurahia maisha ardhini!
Yule ndege alimfuata tai na kumweleza kuwa; "Wewe ni tai, mfalme wa anga. Hustahili kuishi ardhini kama kuku. Hebu ruka uende zako ukafurahie juu pamoja na tai wenzako"
Yule tai akajitazama, kisha akacheka kwa dharau akisema kuwa yeye ni kuku, kama kuku wengine! Hivyo, haiwezekani awe mfalme wa anga.
Yule ndege aliondoka kwa maskitiko makubwa sana. Alijua uwezo mkubwa alionao tai, ila amechagua kuishi maisha yasiyo stahili. Hakuwa na namna nyingine ya kusaidia. Ilibidi aende zake.
Baada ya siku chache, yule ndege alirudi tena akirudia wimbo ule ule. Kwa bahati mbaya wimbo ulifikia kwenye masikio ya tai yaliyozibwa na nta!
Hatimaye yule ndege alichoka akaamua kwenda zake moja kwa moja.
Siku moja, bundi alikuwa anapita katika harakati zake. Mara akamuona tai akiwa anachakura kama kuku. Bundi akamshangaa sana tai. Hakuishia hapo, aliamua kumfuata na kumweleza nafasi aliyonayo, lakini tai alibaki anazubaa!
Bundi aliamua kumnyakua tai na kuruka naye mbali juu ya mawingu. Akiwa katikati ya anga umbali mrefu sana toka ardhini, aliamua kumuachia yule tai bila msaada.
Mara, tai akaanza kushuka chini kuitafuta ardhi! Wakati huo alianza kutapa tapa huku akipiga kelele kuomba msaada. Wakati akitapa tapa, akagundua kuwa ameweza kuruka. Tangu hapo hakurudi tena ardhini kuishi kama kuku. Aliungana na tai wenzake na kuanza kuishi akiwa mfalme wa anga.
*******
Una kitu cha kujifunza hapa. Ukiachilia mbali jinsi unavyoweza kushindwa kuelewa uwezo mkubwa ulioko ndani yako, hebu tafakari nafasi ya bundi kwenye hatua zako za mafanikio!
Mabundi ni sura mbaya! Bundi ni nuksi, tena bundi hapendwi. Wapo watu maishani mwako, ambao wanakufanyia ubundi. Ukiangalia kwa mtazamo mfinyu, unaweza kudhani kwamba, wapo kwa ajili ya kuuchukua uhai wako ama kukuangamiza!
Lakini ukitafakari kwa kina,utajua kwamba, wapo kwa ajili ya kukusaidia kufika mahali ambapo hukudhani kwamba ungeweza.
Inaweza isiwe rahisi, maana wanaweza kukuweka kikaangoni. Lakini wanakukomaza ili uwe imara. Sasa kwanini usiwapigie makofi? Wapongeze, hata ikiwezekana, washukuru!
Washukuru mabundi maishani mwako, maana hawata kuacha vile ulivyo.
*******

Asante kwa muda wako kusoma makala hii. Naomba unisaidie kushare ili wengine watambue u muhimu wa mabundi maishani mwao

Post a Comment

0 Comments