Header Ads Widget

Responsive Advertisement

BARUA KUTOKA KWA MAREHEMU - 5



Simulizi :Barua Kutoka Kwa Marehemu
Sehemu Ya Tano (5)


Jioni hii, Baa ya Penny Pub ilikuwa imetulia sana, ilikuwa na watu wachache kuliko kawaida ya siku nyingine. Hili halikuwa jambo la kushangaza sana hasa kutokana na ukweli kwamba ilikuwa Jumatatu.
Kwenye meza ya pembeni kabisa, Roy alikuwa amekaa kwa utulivu sana, mezani kukiwa na chupa kubwa ya pombe kali, mkononi akiwa na sigara yake ambayo aliivuta kwa mapozi huku akitolea moshi puani na masikioni.
Ilikuwa siku yake ya burudani, pamoja na kwamba aliamua kustarehe, lakini suala la atataumia mbinu gani ili aweze kumuua Kijasho, bado liliisumbua sana akili yake.
Mara akapeleka mkono wake mezani, akachukua glasi yake yenye pombe kisha akaipeleka kinywani, akaukunja uso kidogo akisikilizia uchungu wa kinywaji kile. Alipoishusha ile glasi chini, alikuwa akitabasamu!
Tabasamu mwanana!
Tabasamu la ushindi!
“Yes, nimeshapata njia, tayari! Sasa nitamuua Kijasho kirahisi sana...” akasema kwa sauti kidogo akitabasamu.
Akachukua simu yake, kisha akatafuta namba za Kijasho, alipozipata akabonyeza kitufe cha kupiga haraka, halafu akaikimbiza sikioni kwa pupa. Kitambo kidogo, sauti ya Kijasho ikasikika.
“Sema mkubwa, upo?”
“Niende wapi ndugu yangu, vipi Moro shwari?”
“Tunapambana tu, kaka sema dili huku ziii, nyie wa town huko najua ni bata kwa kwenda mbele!”
“Siyo kiivyo kaka!”
“Nipe mchongo!”
“Ni kweli nina mchongo, ndiyo maana nimekupigia usiku huu. Kifupi nina milioni mbili zako hapa, ambazo kama unazitaka hata sasa hivi naweza kukupa.”
“Usitake nifunge hiki kibaa hapa Kihonda, niwaambie watu wanywe pesa nalipa kesho, enheee lete mwanga sumu hiyo!”
“Kuna dili, kesho jioni nakuja, tena na pesa yako kabisa, mchongo mzima hiyo kesho!”
“Poa, ahsante sana kwa kunipa dili.”
“Usijali.”
*****
Siku iliyofuata saa 1:20 za usiku gari ndogo aina ya Mark II Baloon ilikuwa inaegesha eneo la Masika, pembeni kwa keep left cha Masika, mvua za rasharasha zikiendelea kunyesha. Ndani ya gari hilo alikuwemo Roy Maketo ambaye alifika mjini hapo kwa kazi moja tu; mauaji!
Mauaji ya Kijasho.
Tayari giza lilishaanza kuchukua nafasi na mwanga kwenda zake kusubiri siku mpya! Muda mfupi tu baada ya kuegesha eneo hilo ambalo ni jirani kabisa na Kituo cha Taxi, simu ya Roy ikaita, macho yake kwenye kioo, jina la Kijasho likaonekana.
Akapokea haraka; “Nimeshafika kaka, uko wapi?”
“Fungua mlango, nimeshakuona.”
“Ok! Njoo.”
Muda mfupi baadaye mlango ukafunguliwa, Kijasho akaingia na kuketi. Si Kijasho wala Roy aliyeongea neno lolote, Roy akanyoosha mkono wake siti ya nyuma, akatoa bia mbili za kopo, akazifungua zote na kumkabidhi moja Kijasho.
“Karibu kaka.”
“Ahsante,” Kijasho akasema akiipeleka kinywani ile bia.
Roy naye akaanza kunywa yake. Bia ikiwa mkononi mwake, akaliondoa gari lililokuwa silence, akashika barabara inayoelekea kwenye keep left cha kuelekea Barabara ya Boma na ile ya Sabasaba, alipofika keep left akakata kushoto kuifuata barabara inayoelekea Posta, akaendesha gari kwa mwendo wa taratibu mpaka alipofika darajani na kukata kulia akielekea Uwanja wa Jamuhuri. Akaegesha gari jirani kabisa na uwanja.
“Kaka hapa noma, huoni majangu wapo pale?” Kijasho akamwambia Roy akimuonesha kwa kidole Kituo Kikuu cha Polisi.
“Acha uoga kaka, siku zote huwezi kudhamiwa mbaya ukiwa sehemu iliyo chini ya usalama,” Roy akasema akitabasamu.
Muda huo huo akatoa bahasha yenye fedha na kumkabidhi Kijasho. Akaanza kuhesabu akitabasamu.
“Zipo sawa kaka, ni milioni mbili taslimu!”
“Ok!, sasa twende tukafanye kazi.”
“Wapi?”
“Utapajua tukifika.”
Roy akaondoa gari taratibu hadi barabara kubwa, akakata kulia akielekea Kilakala. Baada ya mwendo wa dakika tano tu, Kijasho alikuwa ameshalala kwenye siti. Roy akaegesha gari pembeni kidogo. Akaanza kumtingisha kwa nguvu, lakini hakujigusa!
“Tayari huyu...” Roy akasema akitabasamu.
Ilikuwa kazi ya sumu, bia aliyokunywa Kijasho ilikuwa na sumu, jambo ambalo Kijasho hakulitambua. Roy akawasha gari na kuliondoka kwa kasi. Aliendesha kwa kasi ile ile hadi alipofika eneo la Mvua, akapanda milimani na kutafuta sehemu ya pori dogo. Hakutaka kuiamini sana ile simu. Akakishika kichwa cha Kijasho vizuri, akakizushusha mara moja kwa nguvu. Ukasikika mlio mdogo wa kwichwaaa!
Kikawa kinaning’inia!
Alikuwa marehemu.
Akachukua zile fedha mfukoni mwake na kumtupa porini!
“Nisamehe rafiki yangu Kijasho, sikuwa na njia nyingine ya kukufunga mdomo, lazima ungeniharibia. Pumzika salama rafiki...” Roy akasema akipiga hatua kulifuata gari lake.
Morogoro haikuwa sehemu salama tena kwake. Akaliondoa gari kwa kasi. Alikuwa akirudi Dar es Salaam.
“Kazi imeisha!” Roy alisema akipiga usukani


*****
Roy aliingia Dar usiku sana, akaenda moja kwa moja nyumbani kwake. Asubuhi na mapema, kama kawaida akaenda zake kazini. Akaendelea kama kawaida na majukumu yake. Moyoni mwake akiwa na siri nzito, hakutaka kupoteza hata siku moja nyumbani, ili kuepusha ushahidi au kumuhusisha kwa namna yoyote na mauaji ya Kijasho.
Wakati wa chakula cha mchana, hakujisikia kabisa kwenda kula, alichokifanya ni kuomba ruhusa na kwenda nyumbani kulala, akisema kwamba anajisikia kuumwa, ingawa ukweli ulikuwa ni kwamba, alizidiwa sana na usingizi.
Siku ya pili yake, magazeti mengi yaliandika habari za kuokokotwa kwa maiti iliyoonekana kunyongwa! Roy alisoma karibu magazeti yote, eneo la mauaji lilikuwa lile lile, Mvua! Lakini kilichomfurahisha ni kwamba, hapakuwa na dalili zozote za kumuhusisha na mauaji yale.
“Na wala hawataweza, mimi ni kiboko!” Akawaza akijipiga-piga kifua chake akitabasamu.
Baada ya habari hiyo kuandikwa na magazeti, siku hiyo wakazi wa Mji wa Morogoro na Vitongoji vyake, wakafurika katika Hospitali ya Mkoa huo kutambua mwili wa marehemu.
Hatimaye ukweli ukabainika!
Kwamba aliyekufa ni Kijasho!
Fumbo likaendelea kubaki vile vile, nani aliyemuua? Hakuna aliyejua. Mazishi ya Kijasho yakafanyika, huku marafiki wengi wakihudhuria. Hata Roy alikuwepo. Katika hali ya kustaajabisha zaidi, kati ya marafiki walionekana wana simanzi zaidi ni Roy!
Alilia sana!
Lakini siri alikuwa nayo moyoni!
Kwamba yeye ndiye muuaji!
*****
Jeff alipanga katika gesti ya uchochoroni Mtaa wa Ghana ambapo alilipia shilingi 3000 kila siku. Siku zikazidi kwenda akiwa hana kazi, hapo akapata wazo la kuhamia katika chumba chake, ndipo aliposaka chumba na kufanikiwa kupata pango la chumba kimoja, katika nyumba ya Mzee Maige, iliyopo Nyakato.

Moyo wa Jeff ulikuwa mzito sana, lakini alikuwa tayari kuteseka kwa muda mrefu lakini baadaye amrudishe mpenzi wake Davina mikononi mwake. Akiwa katika chumba hicho kimoja, alichopanga katika nyumba ya mzee Maige, alilipa jumla ya shilingi 15000 ikiwa ni fedha ya miezi mitatu, yaani kwa mwezi alilipa elfu tano!
Ukiwa ndani ya chumba hicho, unaweza kuona matundu madogo yaliyotobolewa na misumari iliyoshikilia bati, hilo lilitosha kabisa kudhibitisha kwamba chumba hicho kilikuwa kinavuja kipindi cha mvua.
Ndani ya chumba chake kulikuwa na kapeti alilotandaza chumba kizima, juu yake akaweka godoro dogo na ndoo ya maji pembeni! Zaidi ya hapo ni begi lake dogo la kuhifadhia nguo.
Kilikuwa chumba kwa ajili ya kulala tu, mchana anakwenda kuhangaika kutafuta riziki Mwaloni (forodhani), jioni anarudi chumbani kwake na kujifungia. Huo ukawa ndiyo utaratibu mpya wa maisha yake.
Siku zote alikuwa na nywele ndefu, kofia haitoki kichwani na alipenda sana kuvaa koti wakati wote. Ilikuwa ndiyo utaratibu wake mpya, hakutaka kabisa kujulikana. Hata jina alikuwa anatumia jipya; Sasa alikuwa anatumia jina la Christopher Mkumbo au Chris, huku akidai yeye ni Mnyiramba wa Singida.
Wakati akiendelea kufanya kazi ndogondogo Mwaloni, pia alikuwa akihangaikia ajira ya taaluma yake katika ofisi mbalimbali, alikuwa na sifa zote, lakini tatizo hakuwa na vyeti. Hakutaka kuonesha vyeti vyake kwasababu hakutaka kabisa kujulikana jina lake halisi!
Kwa bahati nzuri, akafanikiwa kupata kazi katika Kiwanda kimoja cha Samaki jijini Mwanza, akaajiriwa kama Afisa Masoko, nafasi ambayo aliitendea haki! Kwa miezi mitatu tu, alikuwa ameshapandishwa mishahara mara mbili.
Utendaji wake ukawafurahisha sana viongozi wake. Aliendelea kuyafurahia sana maisha, lakini kichwani mwake aliendelea kuteswa na fikra juu ya mpenzi wake Davina, wazazi wake na Gerald ambaye alipanga kifo chake ili aweze kumuoa mpenzi wake.
“Lazima nifanye jambo la kuwatisha kwanza, ili Davina achanganyikiwe, ashindwe kukubali kuolewa na Gerald, hapo nitakuwa nimecheza. Nitafanyaje?” Akawaza Jeff akiwa bado hajapata wazo juu ya nini cha kufanya ili kutimiza azma yake.
“Acha niombe likizo, niende Dar mara moja nikutane na Frank, anaweza kuwa msaada mkubwa sana kwangu,” akawaza.
Kama alivyopanga, aliandika barua ya kuomba likizo kwa Meneja Mkuu wa Kampuni na aliporudishiwa majibu, alikuwa amekubaliwa. Hakuwa na muda wa kupoteza, akapanda basi na kwenda Dar, lakini aliingia kama alivyoondoka! Kofia kubwa ya pama kichwani, ndevu alikuwa ameziachia sana na koti kubwa la kufika miguuni!
Hata angekutana na nani, isingekuwa rahisi kugundua kwamba aliyekuwa mbele yake alikuwa ni Jeff. Aliposhuka kwenye basi, akachukua taxi na kumwambia dereva ampeleke Tandika, akashuka na kufika hadi kwenye nyumba anayoishi mpenzi wake Davina.
Akasimama nje ya geti akiikodolea macho! Vitu viwili vikimsukuma kufanya mambo tofauti, msukumo wa kwanza ulimwambia asiondoke mpaka ahakikishe ameonana na Davina wake, lakini upande mwingine ukimwambia katu asijaribu kukutana na Davina.
Moyo ukamuenda mbio.
Hisia kali zikamvaa.
Hisia za mapenzi!
Akabaki amesimama akiugulia moyoni. Hakutakiwa kuingia ndani, kwani kufanya hivyo angekuwa ameshaharibu kila kitu. Alitakiwa kuwa mvumilivu sana. Avumilie ili baadaye ale mbivu!
Zilizoiva!
Machozi ndiyo ikawa dawa yake ya muda huo, aliamini kwa kulia kungeweza kumpunguzia machungu makali aliyokuwayo moyoni mwake.
“Lakini kwanini nateseka kiasi hiki? Kwanini? Nitaishi maisha haya mpaka lini? Kwanini tatizo hili linakuwa kwangu tu, kwanini?” Jeff akawaza akiwa amesimama karibu kabisa na geti la kuingia chumbani kwa Davina.
Alitamani sana kumuona Davina wake, angalau basi asikie hata sauti yake, aone tabasamu lake. Alitamani sana kukumbatiwa na Davina, ambusu na kumpiga-piga mgongoni, alitamani sana mambo hayo, lakini hayakuwezekana tena. Isingekuwa rahisi kwake kupata nafasi hiyo.
Akaamua kuondoka zake, akiwa ndiyo kwanza anaanza kupiga hatua ya kwanza, akasikia sauti ya mlango wa geti likifunguka, akasita na kusimama. Akageuza kichwa chake nyuma kwa tahadhari, macho yakakutana na mwanamke mrembo sana!
Davina!
Akasimama.
Akamwangalia mwanamke huyo akitembea kwa mwendo wa taratibu ambao, uliweza kabisa kuonesha huzuni aliyokuwa nayo ndani mwake. Davina alionekana dhahiri kuwa na kitu kinachomtatiza, tena kitu kizito cha kumuumiza moyo wake, akatembea kwa madaha akionekana kuelekea dukani.
“Masikini mpenzi wangu, yawezekana hapo anawaza kwamba mimi nimeshakufa, sipo tena duniani...kumbe nipo, tena ninateseka kwa ajili yake...” Jeff akawaza akiendelea kumwangalia Davina aliyekuwa akizidisha kasi ya kutembea polepole. Haikuwa rahisi kuendelea kusikilizia maumivu yale makali ya moyo. Akageuka na kumwacha Davina andelee na mambo yake, akapiga hatua za taratibu hadi kwenye kituo cha taxi.
Akaingia.
“Wapi?” Dereva akauliza.
“Nipeleke Sinza tafadhali.”
“Ipi?”
“Mori.”
“Mori?”
“Ndiyo, Sinza Mori, halafu nisingependa maswali zaidi, twende Mori, kama hupafahamu sema nishuke nichukue gari lingine.”
“Napafahamu bro, hakuna tabu, nilikuwa nataka kujua sehemu unayokwenda ili niweze kufahamu, sikuwa na maana nyingine.”
“Twende.”
Dereva akawasha gari na kuliondoa kwa kasi. Usiku huo hapakuwa na foleni kubwa sana, hivyo dakika tano tu baadaye walikuwa kwenye mataa ya Tazara katika Makutano ya Barabara ya Nyerere na Mandela. Akanyoosha na Barabara ya Mandela moja kwa moja hadi kwenye mataa ya Ubungo, kwenye makutano ya Barabara ya Morogoro na Sam Nujoma, akashika Barabara ya Sam Nujoma, akaenda moja kwa moja hadi kwenye mataa ya Super Star alipokata kulia kuifuata barabara inayoelekea Sinza Makaburini.
Hadi muda huo walikuwa hawajaongea chochote, Jeff akiwa na mawazo yake kichwani na dereva akiwa amefuata msimamo wa mteja wake ambaye alimtahadharisha kwamba hapendi kuzungumza sana. Mwisho wa makaburi ya Sinza, dereva akakata kushoto kuishika Barabara ya Shekilango, akanyoosha moja kwa moja na kupita Sinza ya Kwaremmy kabla ya kushika breki Sinza ya Mori na kumgeukia abiria wake.
“Tunaingia ndani kidogo au utashukia hapa brother?”
“Kata kulia!”
“Tunafika hadi wapi?”
“Johannesburg Hotel.”
“Ok!”
Dereva akaondoa gari na kuifuata barabara kubwa ya vumbi, dakika moja baadaye aliegesha gari nje ya Johannesburg Hotel. Jeff hakuzungumza neno lolote, zaidi ya kufungua pochi yake na kutoa noti mbili; moja ya elfu kumi na nyigine ya elfu tano, akamkabidhi jumla ya shilingi elfu kumi na tano.
“Ahsante sana brother, ahsante.”
“Usijali,” akasema akishuka.
“Sasa naweza kuchukua simu yako, ili ukihitaji usafiri siku nyingine uniite?”
Jeff hakujibu.
Tayari alikuwa anapanda ngazi fupi za hoteli ile ya kisasa na ya kuvutia! Macho yake yakafuata kibao kidogo chenye mshale, kilichoandikwa Reception, akafuata mshale huo mpaka alipopokelewa na tabasamu mwanana na msichana mrembo aliyekuwa Mapokezi.
“Habari yako sister?” Jeff akasalimia kwa sauti ya upole.
“Salama tu kaka’ngu, karibu.”
“Ahsante sana, naweza kupata malazi?”
“Karibu sana, umeshapata.”
“Ok! Nipatie self-contained room please!”
“Umepata kaka, vyumba vyetu vyote ni self-contained, tofauti yake ni kwamba vingine vinatumia Ac na vingine feni, halafu kuna single room na double room, sijui ungependa kipi?”
“Nipe single self-contained room, chenye Ac!”
“Ok! Karibu sana, andikisha hapa...” yule dada wa Mapokezi akamwambia akimkabidhi kitabu cha kuandikisha wageni.
Jeff akaanza kujaza, kama kawaida akadanganya jina lake na taarifa zake zote. Akalipa na kupandishwa ghorofa ya tatu sehemu kilipo chumba chake, akajitupa kitandani.
“Ooh! Thanks God....” akasema akijinyoosha.
Alikuwa amechoka sana, mara moja akaingia bafuni kuoga kisha akabonyeza namba za Restaurant na kuomba apelekewe chakula. Akala na kulala fofofo.
******
Macho yake hayakutaka kabisa kufumbuka asubuhi hiyo, ingawa kila alipojaribu kuyafumbua, aliona mwanga mkali kuashiria kwamba tayari ilishafika asubuhi! Akajinyoosha-nyoosha pale kitandani baadaye akajilazimisha kufumbua macho yake.
Akakutana na nuru. Mwili wake ulikuwa umechoka kuliko kawaida, alichoshwa na vitu vingi; kwanza safari ya Mwanza mpaka Dar, halafu akapitiliza mpaka Tandika usiku ule ule na kwenda kufikiria jinsi ya kukutana na Davina. Ili aweze kuchangamka, akaamua kuingia bafuni na kujimwagia maji baridi! Alipotoka mwili ulikuwa na nguvu kidogo!
Akayatupa macho yake ukutani akashangaa sana kugundua kwamba tayari ilikuwa imeshafika saa 3:30 za asubuhi. Haikumshangaza sana hasa kutokana na uchovu wa safari ndefu. Akapiga simu na kupelekewa kifungua kinywa chumbani mwake, kitu kimoja tu, kikabaki kinasumbua, angewezaje kuonana na Frank?


****
Bado mawazo yake yalikuwa ni jinsi gani atakavyoweza kumpata Frank. Aliyagandisha macho yake juu ya dari akiwa hana amani kabisa. Hakuwa na namba zake, wala za mtu wake wa karibu, lakini pia ilikuwa vigumu kidogo kuulizia.
Akili yake ikafanya kazi kwa kasi ya ajabu sana. Alipoyatuliza macho yake juu ya meza mle chumbani, akaona kitabu kikubwa cha Orodha ya Wateja wa Kampuni ya Simu na Posta. Akaanza kukagua namba za Frank, ikawa kazi kubwa sana kuzipata.
Alipoendelea kuangalia vizuri, akafanikiwa kuona namba za Makao Makuu ya Posta. Akaziandika haraka kwenye simu yake ya mkononi kisha akabonyeza. Upande wa pili ukaita.
“Hallow!”
“Hallow, habari za kazi?”
“Nzuri tu!”
“Makao Makuu ya Posta, naomba nikusaidie tafadhali!”
“Ndipo nilipopiga, tafadhali naomba uniunganishe na Frank Maganga.”
“Frank Maganga?”
“Ndiyo!”
“Nimwambie ni nani?”
“Mwambie Moses!”
“Unapiga simu kutoka wapi”
“Mwanza!” Akadanganya.
“Ok! Subiri kidogo....” sauti ya pili ikamwambia.
Kikapita kimya kifupi, kabla ya sauti ile tena kusikika; “Hallow, yupo kwenye line, ongea.”
“Hello Frank, vipi rafiki yangu?”
“Salama, nani mwenzangu?”
“Moses kutoka Mwanza.”
“Moses? Nadhani nimekusahau kidogo, ni Moses yupi?”
“Hapana rafiki yangu mimi siyo Moses, lakini naomba nikuambie kwanza kitu kimoja!”
“Nini? Ni vyema kwanza uniambie wewe ni nani ili nijue nazungumza na nani?”
“Nitakuambia, lakini kabla sijafanya hivyo nataka kukueleza jambo la msingi kwanza.”
“Ok, niambie.”
“Usiogope rafiki yangu Frank na wala usipige kelele nikikutajia mimi ni nani?”
“Mbona unanitisha? Niambie basi?!”
“Sikiliza Frank, najua unajua nimekufa, sikufa Frank, bado nipo hai na kuna mambo ya msingi sana nataka unisaidie.”
“Lakini mbona unanichanganya? Nieleze kwanza wewe ni nani?”
“Haya, acha nikuambie, kama unavyotaka. Mimi ni rafiki yako Jeff, ambaye watu wengi, ukiwemo wewe, wanaamini nimekufa.”
“Nani Jeff? You must be joking!” (Jeff? Lazima unatania!)
“I’m not jocking, ni mimi Jeff naongea, sikiliza nikuambie...Frank! Frank! Frank...” Jeff aliita kwenye simu, lakini Frank hakuitika.
Hakuchukua muda mrefu sana kugundua kwamba alikuwa akiongea kwenye simu iliyokatwa!
“Shiiiit!” Jeff akasema na kutupa simu yake kitandani.
*****
Frank Maganga alikuwa rafiki wa karibu sana na Jeff, lakini pamoja na ukaribu wao, alikuwa hajawahi kumkutanisha na mpenzi wake Davina, ingawa alishawahi kumsikia. Ni siku ya msiba wake pekee ndiyo Frank aliweza kumfahamu Davina kwa kumwangalia kwa macho!
Hata hivyo hakuwafahamiana na wala hapakuwa na mtu wa kuwatambulisha, maana wa kufanya hivyo alikuwa ni Jeff mwenyewe ambaye tayari alikuwa ndani ya jeneza.
Frank alikuwa mfanyakazi wa Posta kwa miaka mingi sana, ni kijana mtaratibu sana ambaye alisoma na Jeff kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, waliachana wakati wakienda vyuoni kwasababu kila mtu alikuwa anasomea fani tofauti na mwenzake. Baada ya kumaliza masomo ya chuo, wakakutana tena Dar, kila mmoja akiwa na kazi yake!
Kazi kubwa aliyokuwa nayo Frank, ilikuwa ni kukusanya barua zote zilizotumwa kutoka sehemu mbalimbali na kuziingiza kwenye masanduku! Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake.
Asubuhi hii inakuwa chungu kwa Jeff kutokana na kukosa ushauri wa rafiki yake huyu ambaye anaamini anaweza kuwa msada mkubwa sana wa nini afanye. Jeff anapiga zile namba za Mapokezi kwa mara nyingine, simu ikaita na baada ya muda, sauti ya msichana ikapokea.
Akatoa ombi lile lile; kuongea na Frank.
“Lakini ni muda mfupi uliopita nimekuunganisha naye.”
“Ni kweli dada’ngu, lakini hakukuwa na maelewano mazuri, kwa bahati mbaya simu ikakatika.”
“Ok! Subiri kidogo, nakuunganisha moja kwa moja, sawa?”
“Nitashukuru sana,” akajibu Jeff akijitahidi sana kuficha pumzi zake zilizokuwa zikishuka kwa kasi sana.
“Ongea, yupo kwenye line,” akasikia tena sauti ya yule dada.
Kwanza akavuta pumzi ndefu sana kabla ya kuzishusha taratibu akijiandaa kuzungumza kwa ushawishi ili asikatiwe simu!

Moyo wa Jeff ulilipuka kwa woga, akitamani sana asikatiwe simu. Alijua ni kwanini Frank alifanya hivyo. Ilikuwa ni vigumu sana kumuaminisha kwamba alikuwa mzima wakati alishuhudia maziko yake. Ugumu huo hata Jeff mwenyewe aliuona, lakini alilaumu kitendo chake cha kukataa hata kumsikiliza.
Alitamani sana apewe nafasi, hata ya dakika tatu tu ili aweze kueleza ukweli, ni yeye pekee ndiye angeweza kuwa msaada kwake, lakini Frank haamini, haelewi! Akavuta pumzi ndefu sana, kisha akazishusha taratibu sana. Akafungua kinywa chake na kuanza na kuanza kuzungumza kwa sauti ya kusihi sana...
“Hallow, please usinikatie simu, naomba unisikilize.”
“Unajua wewe ni tapeli ambaye unataka kunihadaa kwa kutumia jina la Jeff, halafu usivyokuwa na haya, umeiga mpaka na sauti yake ili uweze kuniibia vizuri, sasa nataka kukuambia umekosea sana, hii ni namba nyingine kaka.”
“Unaweza ukahisi hivyo, lakini ukweli siyo huo, Frank rafiki yangu nikuambie nini ili uamini kuwa ni mimi rafiki yake mpenzi Jeff?”
“Sema wewe!”
“Wewe ndiyo unataka nikuaminishe, sema nini ambacho uliwahi kufanya na Jeff na unaamini kabisa mnajua wewe na yeye, nikuambie ili uamini?”
“Jeff rafiki yangu nilisoma naye kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita, sasa kama kweli ni wewe, niambie tulisoma wapi na wapi?”
“O Level tulisoma Old Moshi Sekondari Moshi, halafu A Level tulisoma Usagara Sekondari Tanga, wakati huo mimi nilikuwa School President!”
Frank akashtuka sana!
“Kidogo naanza kuamini, unajuaje mambo yote haya?”
“Kwasababu ni mimi mwenyewe Jeff naongea, najua una maswali mengi, lakini mimi ndiye mwenye majibu na ndiyo sababu hasa iliyonifanya nikupigie simu.”
“Ni wewe Jeff kweli?”
“Ni mimi brother!”
“Lakini si ulikufa kaka?”
“Hapana, zile ni njama tu kaka, mimi ni mzima wa afya njema. Nina mambo mengi sana ya kuzungumza na wewe, lakini cha msingi unatakiwa kufahamu kwamba, kwasasa jambo hili lazima liwe siri, tukutane. Tuzungumze na kupanga jinsi ya kunisaidia.”
“Nini hasa kilitokea?”
“Mapenzi ndugu yangu.”
“Love? What do you mean by that?” (Mapenzi? Unaamaanisha nini kusema hivyo?)
“It’s a long story brother, nadhani tu-meet, halafu nikupe mkanda mzima ulivyokuwa, ni ngumu sana kuamini, lakini lazima utaamini ninachokuambia.”
“Ulikuwa wapi kwa kipindi chote hicho?”
“Kwasasa naishi Mwanza kaka, nilihangaika sana, lakini kwa bahati nzuri nikabahatika kupata kazi. Nina likizo ya mwezi mmoja, nimefikia Johannesburg Hotel, Sinza, Mori. Tafadhali sana tuonane leo.”
“Sawa, nikitoka tu, kazini nitakuwa hapo.”
“Kabla hujakata simu, naomba unipatie namba zako za mkononi tafadhali.”
“Ok! Unayo kalamu hapo?”
“Ndiyo, nitajie!”
Akatajiwa namba za simu na kuzinakili kwenye note book yake. Mwishowe wakaagana. Jeff akazihifadhi zile namba haraka kwenye simu yake, halafu akajaribu kama zinapatikana, akapokea Frank.
“Ndiyo namba yangu kaka,” Jeff akasema.
“Poa, baadaye basi!”
“Ahsante sana.”
Wakakata simu.
Tayari mbele ya Jeff kulikuwa na mwanga, hata kama ni mdogo, lakini angalau alikuwa na mahali pa kuanzia. Angenda kubwa kichwani mwake ni kuhakikisha Davina haolewi na Gerald na badala yake, yeye ndiye aje kumuoa. Haijalishi hata kama itakuwa baada ya miaka kumi!
Alitaka ndoa!
Yeye na Davina!
******
Saa 2:18 za usiku, Jeff akiwa sehemu ya vinywaji ya hoteli ile, alimuona Frank akiingia. Kwanza alikaa kimya akimwangalia jinsi alivyokuwa akibabaika kumtafuta. Baada ya muda akaona si sahihi kumuhangaisha. Akatoa simu yake na kupiga.
Frank akapokea haraka; “Uko wai kaka, nimeshaingia hapa!”
“Angalia mbele yako, kama unaelekea toilet!”
“Ni wewe mwenye kofia ya pama?”
“Ndiyo!”
Wakakata simu zao.
Frank akapiga hatua za kivivu hadi alipokaa Jeff. Akaonekana kusita kukaa, macho yake yalionesha woga wa wazi kabisa. Jeff akamwonesha ishara akae. Kwa woga Frank akakaa.
“Usiwe na wasiwasi ndugu, ni mimi ndugu yako Jeff, usishangae na unatakiwa utulie sana. Najua unajua nimekufa, lakini nipo sijafa.”
Frank akazidi kuyatoa macho yake kwa mshangao. Muda mfupi mhudumu akafika. Wote wakaagiza glass za mvinyo mweupe. Wakaanza kunywa. Macho ya Frank hayakuficha woga uliomo ndani mwake.
“Najua unashangaa nina ndevu nyingi, sizipendi lakini ndiyo maisha yangu mapya ya kujiepusha na matatizo.”
Jeff akavua kofia yake na kuachwa sura yake halisi ionekane. Alikuwa na tofauti mbili tu, nywele ndefu na ndevu nyingi.
“Ilikuwaje hasa?” Hatimaye Frank akauliza.
“Acha tu ndugu yangu, aliyezikwa si mimi ni mtu mwingine kabisa, sababu kubwa ni Davina.”
“Unamaanisha nini?”
“Mimi sikuwa nafahamu chochote, lakini kumbe bosi wangu Gerald alikuwa amempenda Davina, akafikiria jinsi ya kumpata akakosa, akaona bora afanye njama za kuniua ili aweze kumpa.”
“Enheee...”
“Kwahiyo akaletwa mtu kazini, anaitwa Roy, ambaye ndiyo alitakiwa kunipeleka kwenye mauaji. Kama unakumbuka siku ya kifo changu nilikuwa safarini kwenda Dodoma, sasa nilitakiwa kufa njiani kwa ajali ya kupangwa, lakini kwa bahai nzuri yule jamaa akaingiwa na huruma na kuamua kunisaidia...” Jeff akamwambia Frank.
Hakuna kitu alichomficha, akamweleza jinsi mipango ilivyofanyika mpaka maii nyingine ikapatikana na yeye kwenda Mwanza. Frank akaelewa kila kitu na hapo sasa woga ukaanza kupungua.
“Aisee pole sana ndugu yangu, ndiyo maana hawakutaka marehemu aonekane?”
“Hiyo ilikuwa ni kwasababu ile maiti iliharibiwa usoni, hii ni dili ambayo tunafahamu wau watatu tu, mimi, Roy na jamaa mwingine anaitwa Kijasho yupo Morogoro. Nakuomba sana, jambo hili liwe siri ndugu yangu, usimwambie mtu yeyote.
“Najua ni vigumu kuwa na siri kubwa kama hii lakini vumilia, tukamilishe uchunguzi wetu, halafu siku moja mambo yatakuwa hadharani.”
“Ok! Nimekuelewa, sasa unadhani mimi nitakusaidiaje?”
“Nataka siku moja, jamii ielewe ukweli wa tukio zima, lakini kumbuka sitaki kabisa kumpoteza Davina. Tayari nina wazo kichwani.”
“Nini?”
“Kitu cha kwanza kabisa ambacho tunatakiwa kufanya ni kuwatisha Gerald na Davina, ili wote waogope kuwa pamoja, wakati mipango mingine ikiendelea.”
“Tutatumia njia gani?” Frank akauliza akipeleka glass ya mvinyo kichwani mwake.
“Barua.”
“Barua kivipi?”
“Natakiwa niwe naandika barua na kuzituma Posta, ndani naandika jina langu kila kiu, lakini anuwani zinakuwa na kuzimu, nje pia tunagonga muhuri wa kuzimu, halafu inakuwa na maudhui ya kutisha tu!
“Kazi yako wewe ni kupokea barua zote kupitia sanduku lako, halafu unazisambaza kwenye masanduku yao.”
“Nimeshakupata, lakini lazima jambo hili liwe siri maana unaweza kunipotezea kazi.”
“Usijali kaka, nitakuwa makini katika kila hatua ya kila jambo ndugu yangu, siwezi kukuangusha kaka.”
“Poa, nitafurahi kama ikiwa hivyo.”
“Halafu kitu kingine nahitaji sasa uanze kuwafuatilia kwa karibu, nitakuwezesha kidogo, kuwa karibu kwa kipindi hiki, ujue nyendo zao, halafu utakuwa ukinitumia taarifa zote sawa mkubwa?”
“Nimekuelewa vizuri sana, ondoa shaka.”
“Kumbuka kila kitu tulichozungumza hapa ni siri, halafu nimekuja Dar kwa ajili ya kuzungumza na wewe, kwahiyo sina muda kesho narudi Mwanza. Nahitaji sana msaada wako ndugu yangu.”
“Usijali kaka, pole kwa yote ndugu yangu. Dunia ina mitihani mingi kaka.”
“Kawaida,” Jeff akasema akimpatia kiasi cha laki tatu mkononi mwake.
“Huu ni mwanzo tu kaka, fanya hii kazi vizuri na kwa uaminifu mkubwa utafurahi.”
“Ahsante sana kaka, nami pia nitakufurahisha. Poa basi, acha mimi nikuache.”
“Nakutakia utekelezaji mwema.”
“Tegemea ushindi,” Frank akasema akitabasamu wakati akiinuka.
Akaondoka zake.
Mwanga wa mafanikio ukaanza kuonekana, Jeff akamwangalia Frank akiishilia huku akijihesabu ameshakuwa mshindi. Njia ya mafanikio ilianza kuonekana, mafanikio ya kumnasa tena Davina. Mwanamke wa ndoto yake.
“Safi sana...” akasema kwa sauti akipiga meza kwa nguvu kisha akapandisha ngazi kuelekea chumbani kwake.


Jeff alifurahi sana kuona ombi lake limekubaliwa na Frank, moja kwa moja. Akamwangalia kwa jicho la kuibia na kuachia tabasamu mwanana usoni mwake, kisha akatamka kivivu: “Ahsante sana rafiki yangu, mipango yangu sasa itakuwa sawa.”
“Tupo pamoja Jeff ndugu yangu, wala usiwe na wasiwasi katika hili.”
“Ok, poa! Chukua hizi fedha zikusaidie japo kwa mafuta,” Jeff akasema akimpatia kiasi cha laki tatu mkononi mwake.
“Nashukuru sana rafiki yangu!”
“Huu ni mwanzo tu kaka, fanya hii kazi vizuri na kwa uaminifu mkubwa utafurahi.”
“Ahsante sana, nami pia nitakufurahisha. Poa basi, acha mimi nikuache.”
“Nakutakia utekelezaji mwema.”
“Tegemea ushindi,” Frank akasema akitabasamu wakati akiinuka.
Akaondoka zake.
Mwanga wa mafanikio ukaanza kuonekana, Jeff akamwangalia Frank akiishilia huku akijihesabu ameshakuwa mshindi. Njia ya mafanikio ilianza kuonekana, mafanikio ya kumnasa tena Davina wake. Mwanamke wa ndoto yake.
“Safi sana...” akasema kwa sauti akipiga meza kwa nguvu kisha akapandisha ngazi kuelekea chumbani kwake.
Hakuwa na kazi nyingi sana chumbani, aliishia kuoga kisha kupanga-panga baadhi ya bidhaa zake, tayari kwa safari ya siku inayofuata kisha akashuka chini, alipokula na kuanza kufakamia mvinyo kwa fujo!
*****
Kitu cha kwanza Jeff kufanya alipofika Mwanza, ilikuwa ni kwenda kwa fundi wa kutengeneza mihuri kisha akamwomba amtengenezee muhuri aliouhitaji. Fundi alishangazwa sana na maandishi aliyokuwa akihitaji kuandikiwa katika muhuri huo.
“Kwanini unaandika hivi?”
“Vipi?”
“Kuzimu Mjini!”
“Wewe shida yako nini? Unahitaji kujua sababu ya kuandika maneno hayo au unataka kazi?”
“Kazi, ingawa pia ni vyema kujua matumizi ya muhuri wako.”
“Sasa mimi nasema si kazi yako, amua kutengeneza nikulipe bila kukuambia sababu za kuutengeneza au nimpelekee fundi mwingine.”
“Nitatengeneza kaka.”
“Fanya kazi yako.”
Zoezi hilo lilipokamilika, Jeff alichukua muhuri wake na kwenda nyumbani. Akakaa mezani kwa utulivu na kuanza kuandika barua za Davina na Gerald. Alizisoma mara mbilimbili na kuridhika. Alipomaliza akaziweka kwenye bahasha, kisha akaziingiza tena kwenye bahasha nyingine na kuandika anuwani ya Frank.
Kazi ikawa imeisha!
Huo ukawa mwanzo wa barua za vitisho kwa Gerald na Davina. Utaratibu ukawa ule ule, anaandika kisha anaweka kwenye bahasha aliyogonga muhuri wa kuzimu, kisha akaweka tena ndani ya bahasha nyingine ambazo aliandika anwani ya Frank na kumfikia.
*****
Frank alitimiza kazi yake ipasavyo, hakuwa na mchezo na kazi, kila barua zilipofika alichana bahasha ya juu na kuziweka kwenye masanduku ya Davina na Gerald! Frank aliamua kumsaidia rafiki yake ipasavyo. Hata pale Davina alipofika ofisini kwao na kuzungumza na Meneja, alimpa taarifa zote.
“Amekuja kuonana na Meneja, uamuzi waliouchukua ni kupitisha barua zote ofisini kwake kwa kipindi ambacho uchunguzi unaendelea.”
“Uchunguzi? Unamaanisha nini?”
“Anahisi kuna mtu anamchezea mchezo hapa ofisini kwetu.”
“Duh! Sasa mambo si ndiyo yameshaharibika kaka?”
“Hapana, hayawezi kuharibika, kwasababu hata hiyo kazi ya kupeleka barua ofisini kwa Meneja nimepewa mimi.”
“Kwahiyo?”
“Endelea kutuma barua kaka.”
Frank akaendelea na kazi yake kama kawaida, aliwafuatilia kwa karibu sana, hata pale Davina alipotaka kwenda Kondoa, alijua na kumpa taarifa Jeff.
Jeff akampigia simu Davina usiku ule ule na kumtishia kama kawaida yake, mwisho wa siku akaamua kusitisha vitisho vyote. Wakati huo alikuwa na taarifa zenye uthibitisho wa kutosha kwamba Davina na Gerald walikuwa mbioni kufunga ndoa.
Hilo hakutaka kulipa nafasi kabisa.
“Hawawezi kuoana, labda mimi siyo Jeff, Davina atarudi tena mikononi mwangu,” Jeff alimwambia Frank kwenye simu wakati alipompigia kumpa taarifa za ndoa ya Davina na Gerald iliyokuwa mbioni kufungwa.
“Kivipi?”
“Subiri.”

****
Ni usiku wa sita sasa, katika chumba hiki kizuri, chenye hewa safi, lakini kukikosekana kitu kimoja muhimu kwa Jeff. Usingizi. Ni siku ya sita leo, Jeff hajalala! Mawazo yake yote ni juu ya mpenzi wake Davina ambaye dalili zilionekana wazi kabisa kwamba anampoteza!
Ilikuwa ni siku nane kabla ya ndoa ya Davina na Gerald kufungwa! Ndoa ya mpenzi wake. Ndoa haramu, ambayo kwa hakika asingeweza kuiruhusu. Bado ana mawazo akijaribu kufikiria jinsi atakavyoitengua ndoa hiyo kabla ya kufungwa.
“Nitafanyaje jamani? Mbona akili yangu ipo kama imefikia mwisho? Lakini siamini kabisa kama hapa ndiyo mwisho wangu wa kufikiri? Kweli ndiyo mwisho wangu wa kufikiri? Siamini kabisa. Lazima kuna kitu natakiwa kufanya.
“Kuna mahali sijafika kimawazo. Siamini kama kweli mawazo yangu yanaweza kuwa mwisho wake hapa. Mimi? Mwisho wa kuwaza unaweza kuwa hapa kweli? Kuna kitu nimesahau....ni nini?” Anawaza Jeff bila kupata majibu yakinifu.
Akiwa katikati ya lindi la mawazo, simu yake ikaita, mara moja akaichukua. Akakutana na jina la Frank likizunguka kwenye kioo cha simu yake. Hakupokea haraka. Akatulia kwanza na kuwaza: “Ana nini kipya?”
“Ngoja nipokee....” akasema kwa sauti akibonyeza kitufe cha kupokea na kupeleka simu sikioni.
“Sema kaka...mbona usiku, kuna jipya?” Jeff akauliza kwa sauti ya taratibu sana.
“Siyo jipya sana kaka, ila nataka kukukumbusha kwamba kesho ni Jumapili!”
“Najua, kwani vipi?”
“Ndoa ya Davina na Gerald inatangazwa kwa mara ya mwisho Kanisani.”
“Pia najua.”
“Kujua pekee hakusaidii kitu, umepanga kufanya nini?”
“Nipe muda hadi kesho asubuhi nitakuwa na la kufanya. Nitakupigia kukujulisha, usijali.”
“Usiku mwema.”
“Nawe pia.”
Wakakata simu zao.
Jeff alikuwa na mawazo sana, simu ya Frank ilimchanganya sana. Akaendelea kuusumbua ubongo wake. Mwisho akapata jibu.
“Nimeshajua cha kufanya, acha nilale sasa.”
******
Jumatatu, saa 4:15 za usiku, Jeff alikuwa akishuka kweye basi, katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani, Ubungo jijini Dar es Salaam, akitokea Mwanza. Hiyo ikiwa ni siku mbili baada ya kuzungumza na Jeff kwenye simu. Ilikuwa safari ya ghafla na ya siri kubwa.
Kama kawaida, alikuwa amevalia kofia kubwa kichwani, koti refu na ndevu za bandia. Akachukua taxi iliyompeleka moja kwa moja Johannesburg Hotel iliyopo Sinza ya Mori. Hapo akajifungia chumbani kwa siku tatu, bila kutoka nje ya hoteli hiyo. Safari zake ziliishia Restaurant na chumbani tu!
Alipopigiwa simu na Frank, alimdanganya yupo Mwanza, alipoulizwa kuhusu ndoa ya Davina, aliendelea kusema aachwe bado anafikiria. Yalikuwa majibu ya ajabu, yaliyomchanganya sana Frank. Lakini kichwani Jeff alijua kila kitu. Aliendelea kuishi hotelini pale mpaka siku ya Ijumaa, ambayo siku iliyofuata ilikuwa siku ya kufunga ndoa Davina na Gerald, hapo ndipo Jeff alipotoka na kwenda katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay kutoa taarifa za tukio zima. Jeff alitoa maelezo ya jinsi tukio zima lilivyokuwa mpaka mauaji yake feki na jinsi Gerald alivyo katika hatua za mwisho za kufunga ndoa na mpenzi wake siku iliyofuata.
“Kwahiyo afande ndiyo hivyo, bado nampenda sana mpenzi wangu, najua hafahamu kinachoendelea, lakini pia nataka Gerald na kundi lake wakamatwe, iwe fundisho, hawa watu hatari sana,” Jeff alimwambia askari aliyekuwa akichukua maelezo yake.
“Umeingia lini hapa jijini?”
“Jumatatu.”
“Umefikia wapi?”
“Johannesburg Hotel, Sinza Mori.”
“Taarifa ulizonazo, ndoa ni saa ngapi?”
“Ibada ya ndoa inaanza saa nane kamili za mchana afande.”
“Ok, acha namba zako za simu, sisi tunajipanga vyema, kesho kuanzia saa tano kamili uwe hapa.”
“Sawa afande.”
Jeff akaondoka zake.
*****
“Siamini kama unaweza kukubali Gerald amuoe Davina,” Frank alimwambia Jeff kwenye simu, alipompigia mchana huo.
“Nitakuwa mwanaume mpumbavu kuliko wote.”
“Sasa una mipango gani?”
“Njoo hotelini tuongee.”
“Hotelini wapi?”
“Pale pa siku ile.”
“Johannesburg?”
“Ndiyo.”
“Upo Dar?”
“Ndiyo maana yake.”
“Tangu lini?”
“Njoo tutaongea huku.”
“Poa.”
Nusu saa baadaye Frank alikuwa chumbani kwa Jeff. Alishangaa sana jinsi alivyoingia Dar kwa siri! Jeff akafungua begi lake na kutoa suti yake ya kisasa, nzuri ya kuvutia.
“Ya nini tena?”
“Ya ndoa yangu.”
“Ndoa yako?”
“Ndiyo.”
“Na nani?”
“Davina.”
“Kivipi?”
“Kaa kwanza nikupe michapo kaka...” Jeff akamwambia Frank akitabasamu.
Akamweleza kila kitu jinsi alivyopanga mpango mzima na maaskari. Frank hakuamini macho yake, akampongeza rafiki yake kwa ujasiri wake mkubwa!
“Lakini lazima unyoe hayo mandevu na manywele yako.”
“Ni kweli, lakini sasa nitawezaje kuingia salon?”
“Kazi nyepesi sana, hapo barabarani kuna salon nyingi sana, kitu cha kufanya, tutatoka muda wa saa tano hivi, muda ambao wanakaribia kufunga, kwahiyo hakutakuwa na wateja wengi. Tutatumia muda huo kunyoa na hakuna mtu atayekuona.”
“Kweli kabisa.”
Ndivyo ilivyokuwa, saa tano walitoka na kwenda barabarani, ambapo Jeff alinyolewa bila kuonekana na mtu yeyote hatari kwake. Zoezi hilo lilipokamilika, wakarudi hotelini. Jeff akavaa ile suti yake na viatu, kisha akamgeukia Frank akitabasamu.
“Haya niambie kaka!” Jeff akamwambia Frank akicheka.
“Sina la kuongeza kaka, yaani ni bwana harusi kamili....yaani wagejua kuwa wewe ndiye muoaji, siyo Gerald, waalikwa wasingejisumbua!”
“Watajiju!!!”
Frank akaondoka na kumwacha Jeff mwenyewe chumbani kwake, akili yake ikiwaza mambo yatakavyokuwa Kanisani siku inayofuata. Aliwaza sana juu ya ndoa yake. Alimpenda sana Davina, lakini bado ndani yake kulikuwa na wasiwasi, aliwaza kama Davina bado alikuwa akimpenda!
Hilo hakulijua!


Alitakiwa kusubiri!
Kesho tu!

*****

Saa 5:00 za asubuhi, Jeff alikuwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay kama alivyoagizwa na maaskari. Alikuwa amevalia suti yake ya rangi nyeupe, viatu vya kisasa na alinyoa nywele zake katika mpangilio wa kuvutia kabisa.
Alionekana kama bwana harusi kamili!
Tena halali!
“Kaka naona umepania sana, eeh!” Askari mmoja akamwuliza Jeff kwa mtindo wa kumtania.
“Si unajua tena kaka, isitoshe ni haki yangu.”
“Ok! Endelea kusubiri kidogo, tutakujulisha kinachoendelea, lakini cha msingi unachotakiwa kufahamu, tayari kuna gari zima la maaskari lipo maeneo ya Kanisani linafanya doria, Ibada ikianza, wapo askari kanzu watakaokuwa Kanisani wakitujulisha kila kitu, kwahiyo shaka ondoa.”
“Sawa afande, nitafurahi sana mkinisaidia.”
“Hiki ni chombo cha usalama ndugu yangu, ni wajibu wetu kuhakikisha unakuwa salama katika kila kitu. Ondoa hofu uliyonayo, kila kitu kitakuwa sawa.”
“Nashukuru sana. Sijui nitatoa zawadi gani kwenu nikifanikiwa!”
“Huna haja, serikali imetuweka hapa kwa kazi hii, nayo imekuwa ikitulipa masilahi mazuri na yanayotosha kabisa, kwahiyo huna sababu ya kutoa chochote ndugu yangu!”
“Ahsante sana, nimefarijika mno kusikia hivyo.”
*****
Kanisa lilikuwa limefurika watu wengi sana mchana huo, walikuwa wakishuhudia tukio muhimu sana la ndoa ya Gerald na Davina. Kwa Gerald ilikuwa siku ya kihistoria sana kwake, maana alikuwa anatimiza ndoto yake ya siku nyingi.
Ndoto ya kumuoa Davina wake!
Ndani ya kuta za jengo la Kanisa lile, kulikuwa na makachero wa Polisi zaidi ya watano, wakiangalia kila hatua ya kilichokuwa kikiendelea! Hatimaye muda wa tukio muhimu kabisa, ukafika. Muda wa kufungisha ndoa.
Kama kawaida Mchungaji aliuliza, kama kuna mtu ana pingamizi ili aweze kufunga ndoa ile. Akauliza kwa mara ya kwanza, ya pili na alipofika ya tatu, akasikia sauti kuu kutoka lango kubwa la kuingilia ikitoa pingamizi...
“Noooo....nooo Pastor...nina pingamizi...” ilikuwa sauti ya Jeff, akiingia mbio kuelekea madhabahuni ambapo Gerald na Davina walikuwa wamesimama tayari kwa kufunga.
Macho yaliwatoka kwa mshangao, vipi Jeff atokee Kanisani wakati alikuwa ameshakufa? Jeff alikuwa marehemu! Ukumbi mzima ukapigwa na butwaa!
*****
“Mchungaji hivyo ndivyo ilivyokuwa, huyu Gerald ni mtu mbaya sana, alitaka kuniua mimi ili yeye atimize lengo lake la kumuoa mpenzi wangu, nilifanya yote hayo kwa ajili ya mpenzi wangu.
“Bado nampenda sana Davina wangu na sipo tayari kabisa kumpoteza. Nampenda, nataka kufunga naye ndoa...” Jeff akasema kwa sauti kuu, huku akilia machozi ya uchungu.
Ghafla alipogeuza macho yake upande wa waumini, akakutanisha uso wake na Roy! Mafia ambaye aliamua kumsaidia katika mauaji yake, akamkonyeza na kumuonesha kwa ishara kwamba kulikuwa na hatari na aondoke haraka.
Hakuna aliyegundua tofauti hiyo, taratibu Roy akasimama na kutoka nje ya Kanisa. Ilikuwa kitedo cha haraka na siri kubwa. Hakika Jeff asingefurahi kuona Roy anaingizwa hatiani, hasa kutokana na ukweli kwamba ndiye alimyemsaidia kuwa hai mpaka muda ule.
“Je,Davina unamfahamu Jeff?” Mchungaji akamwuliza Davina kwa sauti ya taratibu sana.
Jeff akayatupa macho yake kwa Davina, akionekana kuhitaji huruma yake, hakutaka kukataliwa, alimpenda sana mwanamke huyo.
“Ndiyo Mchungaji, namfahamu, nampenda bado. Kama itawezekana naomba kufunga naye ndoa.”
Moyo wa Jeff ukalipuka kwa furaha!
“Gerald ni ya kweli hayo yaliyosemwa na Jeff?” Mchungaji akamgeukia Gerald na kumwuliza.
Gerald hakujibu kitu.
Akabaki akilia!
“Tulia hivyo hivyo, upo chini ya ulinzi. Nyoosha mikono yako juu haraka,” ilikuwa ni sauti ya mmoja wa maaskari waliongia Kanisani ghafla wakiwa na bastola mikononi.
Gerald hakuwa na la kufanya, akanyoosha mikono yake yake juu, kabla ya kuamriwa baadaye aishushe na pingu zikafungwa mikononi mwake, akatolewa katika lango kuu la Kanisa, tayari kwa kufikishwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay. Kelele zikatawala Kanisani, kila mtu akiwa haamini kabisa kilichotokea.
Jeff akashindwa kujizuia, akajikuta akimkimbilia Davina na kumkumbatia huku akilia!
Davina akampokea!
Wakakumbatiana!
“Kuna mtu mwenye pingamizi kabla sijafungisha ndoa hii?” Sauti ya Mchungaji ikasikika, ndiyo iliyowanasua Davina na Jeff waliokuwa wamekumbatiana.
Hakuna aliyejitokeza.
Mara moja ndoa ikafungwa na mambo kubadilika, ikawa huzuni kubwa sana kwa upande wa akina Gerald, lakini ilikuwa furaha kwa upande wa akina Davina, kwani walifahamu ni kiasi gani ndugu yao alivyokuwa akimpenda sana Jeff.
Muda mfupi tu baada ya ndoa kufungwa, wazazi wa Jeff pamoja na ndugu wengine, wakaingia Kanisani. Furaha ikageuka kilio. Walikuwa wakilia kwa furaha baada ya kumuona mwanao akiwa hai tena. Walipata taarifa hizo muda mfupi uliopita, baada ya kupigiwa simu na jamaa mmoja aliyekuwa kwenye sherehe ya harusi hiyo.
Bila kujali utaratibu wa Ibada, Jeff alitoka mbio na kuwafuata wazazi wake. Akawakumbatia!
“Nipo hai wazazi wangu!”
“Ilikuwaje?” Baba yake Jeff akauliza.
“Ni habari ndefu sana, nitawasimulia nyumbani.”
“Pole sana baba, pole mwanangu. Mungu apewe sifa,” mama Jeff akasema akimpiga-piga mgongoni.
“Aika-mai...” (Ahsante mama) Jeff akaitikia kwa lugha yao ya Kichagga.
Wakaachiana.
Wakatizamana wakitabasamu.
Mara Davina naye akaja mbio, akajitupa kifuani mwa Jeff, akalala akiwaangalia wazazi wake ambao tayari walikuwa wameshaungana na wazazi wa Jeff. Wakaachia tabasamu!
Muda mfupi baadaye Vyombo mbalimbali vya Habari vilikuwa Kanisani. Wakichukua picha na kutaka kufanya mahojiano na Jeff.
“Kaandikeni nipo hai, maelezo mengine nitatoa nikiwaita kweye press Jumatatu,” ndivyo Jeff alivyowajibu Waandishi wa Habari.
Kama ndoto ya kupendeza, hatimaye Davina na Jeff wamerudi kuwa pamoja tena. Ndoto zao zikiwa zimerejea kwa upya. Kila kitu kikabaki kuwa sehemu ya historia ya maisha yao, sasa walikuwa katika penzi jipya.
Penzi la milele!

...Mwisho...


Post a Comment

0 Comments