Simulizi : Sikujua Ungenisaliti Mpenzi Sehemu Ya Kwanza (1)
HALI ya hewa ilikuwa ya baridi sana asubuhi hiyo, mvua za rasharasha ziliendelea kunyesha na hapakuwa na dalili ya kukatika! Kwa mji wa kibiashara kama Dar es Salaam, mvua hizo zilikuwa kero kubwa sana kwa wakazi wake. Ziliharibu kila kitu, wengi walisikika wakilaumu kwanini ilinyesha mjini badala ya Bagamoyo! Ni mvua ambayo ilikesha usiku kucha ikinyesha hadi asubuhi hiyo bila kukoma. Mavazi makuu sasa yakabadilika, yakawa ni makoti, masweta na majaketi! Mvua ilikuwa kero! Lakini kwa wenye nazo, haikuwa kero kubwa sana, kwani waliamua kupumzika majumbani mwao wakifurahia fedha na mali walizonazo. Lakini kuna ambao walizidishiwa zaidi maumivu na mvua hizo; wagonjwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali. Ndani ya wodi ya majeruhi, katika Hospitali ya Amana, Ilala jijini Dar es Salaam, hali haikuwa shwari kwa kijana huyu! Kwa mwonekano wake, alikuwa anavutia sana. Ana macho makubwa meupe, yenye mboni nyeusi. Mpangilio wa nyusi zake ndiyo unaowachanganya wanawake wengi. Kifua chake cha mazoezi ni kati ya vitu vinavyozidisha mwonekano wake wa kimahaba. Hakuna nguo ambayo anaitia mwilini inamkataa. Kila anachovaa anapendeza sana, huyu ni Bruno. Utanashati wake, mvuto wake wa kimahaba, uchangamfu na kila kitu, vyote vimepotea! Sasa Bruno amekuwa mpya! Amebadilika kwa kila kitu. Hana tabasamu tena! Hana furaha tena! Maisha yake sasa yametawaliwa na huzuni na hofu tupu. Amelala kitandani akionekana kuwa na mawazo na kukata tamaa kabisa. Hana tumaini tena, kila kitu kimeshaharibika. Macho yake yamezingirwa na machozi, anaonekana hana amani wala matumaini ya kuishi muda mrefu baada ya pale. “Mimi ni mzoga tu,” alijikuta akitamka kwa sauti huku mvua ya machozi ikianza kunyesha machoni mwake. Msichana mrembo aliyekuwa akipita jirani yake, aliumizwa sana na machozi yake; akajua lazima alikuwa na jambo zito lililokuwa likimtatiza. Akapiga hatua za taratibu, macho yake yakiwa yanamwangalia sawia Bruno. “Pole!” Akatamka msichana huyo kwa sauti ya chini, lakini kwa haraka kidogo. “Nashukuru sana!” “Pole utapona tu!” “Ahsante sana.” “Naitwa dada Vanessa, sijui wewe!” “Bruno.” “Pole sana Bruno, Mungu atakupa afya njema. Jipe moyo!” “Ahsante sana!” “Umepatwa na nini?” “Ajali, nimepoteza mguu mmoja dada yangu!” “Masikini pole sana.” “Nashukuru.” “Mimi pia nina mgonjwa wangu, mjomba wangu amelazwa hapa. Ndiyo nimetoka kumwangalia!” Akasema Vanessa. “Pole sana, anaendeleaje sasa?” “Ana nafuu kidogo, anaweza kuruhusiwa kesho kama siyo kesho kutwa.” “Pole sana dada yangu!” “Usijali, wewe ndiyo unatakiwa kupewa pole nyingi zaidi kutokana na matatizo uliyoyapata.” “Nashukuru kwa wema wako.” “Usijali...samahani, kuna jambo nataka kukuuliza...sijui utaniruhusu?” “Uliza tu!” “Kuna mtu anayekuja kukuangalia hapa hospitalini?” “Unamaanisha nini?” Bruno akauliza angali macho yake ameyakaza usoni mwa Vanessa. “Namaanisha mtu wa kukuletea huduma muhimu, mathalani chakula na mambo mengine!” Lilikuwa swali baya kwa Bruno, swali lililotibua mambo yaliyojificha ndani ya moyo wake! Vanessa akashindwa kuelewa kwamba swali lile lilikuwa sawa na mwiba wa samaki ndani ya moyo wake! Ghafla, macho ya Bruno yakalowana! Mvua nyingine ya machozi ikaanza kumwagika machoni mwake, yakafunika kope zake...aliumia sana moyoni. Hakupenda kabisa lile swali. Vanessa hakuyapenda machozi ya Bruno, kwa kumtizama tu, akafahamu kwamba, lazima alikuwa na kitu kingine kinachomwumiza zaidi. Bruno akazidi kulia, Vanessa akaketi kitandani kisha akatoa leso yake na kumfuta machozi. “Samahani sana Bruno kama nimekukosea...” Vanessa akamwambia Bruno kwa sauti tulivu sana. “Hapana dada, hakuna kitu!” “Lakini umeanza kulia baada ya kukuliza kama kuna mtu anayekuja kukuangalia...samahani sana kama nimekukosea, siyo dhamira yangu!” Bruno akazidi kulia. “Nyamaza tafadhali, wewe ni mwanaume, hakuna tatizo kubwa kwa mwanaume, jikaze na utulize moyo wako.” “Sawa, nimekuelewa...” Bruno akasema akijitajidi kunyamaza. “Yaani Tunu?!!!” Hatimaye neno hilo likamtoka Bruno kinywani mwake. “Tunu? Ndiyo nani?” “Ni habari ndefu sana dada’ngu, siwezi kuzungumza kitu kwasasa, lakini fahamu hakuna mapenzi ya kweli duniani!” Bruno akamwambia Vanessa ambaye alionekana kushtuka sana. “Hakuna mapenzi ya kweli, kivipi Bruno?” “Fahamu tu, kwamba hakuna mapenzi ya kweli duniani!” Bruno akasema akianza kulia tena. “Kwani hayo mapenzi yana uhusiano wowote na hii hali uliyonayo sasa?” “Tena kwa asilimia mia moja!” “Kivipi?” “Siwezi kuongea chochote sasa hivi, sitaki kujiumiza zaidi ya hapa, nahitaji muda wa kupumzika zaidi, samahani kama nimekuudhi, lakini siku tukionana kwa majaliwa ya Mungu, nitakusimulia kisa kizima!” “Sawa. Sasa unaweza kujibu swali langu?” “Uliuliza nini vile?” “Kama kuna mtu anayekuja kukuangalia na kukupa mahitaji yote ya muhimu?!” “Kifupi hakuna!” Bruno akajibu baada ya kujikaza sana. “Pole sana, kama hutajali, naomba kuanzia sasa nianze kukuangalia, sijui utaniruhusu?” Macho ya Vanessa yalikuwa ya huruma sana wakati akizungumza maneno hayo. Bruno hakujibu! Alibaki akimwangalia Vanessa. “Tafadhali naomba unikubalie, usikatae Bruno nakuomba sana.” Bado hakujibu! Ghafla matone ya machozi yakaanza kumiminika tena machoni mwake. Ikawa machozi ni kitu cha kawaida kwa kijana huyu mtanashati. Kila kitu analia! Kila swali analoulizwa jibu lake ni machozi! Machozi! Machozi! Machozi! Vanessa akaogopa sana, akashindwa kuelewa ni kwanini kila anapomwambia kitu lazima alie! Akilini mwake kukajengeka kwamba lazima alikuwa na matatizo makubwa sana. Ni kweli siku zote alikuwa mtu wa kusaidia watu, moyo wake ulikuwa wa huruma sana, hakupenda kumwona mtu akiwa katika hali ya shida na matatizo halafu amwache, kama anaweza kumsaidia alifanya hivyo. Kwa kijana huyu aliyelala hoi kitandani, akionekana kukosa faraja kabisa, akionekana kukata tamaa ya maisha kabisa. Akionekana kupoteza hamu ya kuishi. Aliyepoteza dira! Ambaye havutii kwa chochote! Hatamaniki kwa lolote! Mlemavu! Moyo wake ulikuwa na zaidi ya huruma, alishawishika kwa kiasi kikubwa sana kumsaidia, alishindwa kuelewa ni kwanini alijikuta akihisi hali hiyo, lakini moyo wake ulishaamua na alikuwa tayari kumsaidia kwa namna yoyote na kwa gharama yoyote. “Tulia Bruno, lazima ujikubali kwanza jinsi ulivyo. Najua una mawazo mengi sana lakini unatakiwa kujitahidi uyaondoe, kwani hayatakusaidia kitu. “Nahisi unavyoumia, naona unavyoteseka. Najua...nafahamu utakuwa na maumivu mengi sana kwa wakati mmoja. Nahisi unavyoungua na moto, lakini hayo yote ni sehemu ya maisha. “Kumbuka matatizo hayakimbiwi Bruno, matatizo yanakabiliwa. Yanatatuliwa. Hayakimbiwi. Kwanza huwezi kuyakimbia. Utakimbia mpaka wapi? Utajificha wapi? Utalia mpaka lini? Nyamaza tafadhali...” sauti ya Vanessa ilikuwa ya kusihi kuliko kawaida. Ilikuwa sawa na msumari wa moto ambao uliingia moyoni mwa Bruno kabla haujapoa vyema. Maumivu juu ya maumivu. Vanessa hakujua kinachomliza Bruno. Hakulia kwa sababu ya maumivu na mateso pekee. Hakulia kwasababu sasa alishakuwa mlemavu. Alilia kwa sababu nyingine zaidi. Sababu kubwa kuliko kawaida, kubwa ingawa kwa mtu mwingine ingeweza kuonekana ndogo! Mapenzi... Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomfanya kila wakati awe analia. Akajuta kuyafahamu mapenzi, akajuta kumfahamu mpenzi wake aliyesababisha awe katika hali ile.
“Sijui ni kwanini nilikutana na Tunu katika maisha yangu? Najuta kukutana na mwanamke yule, kwanza si mwanamke ni shetani, amekuwa maumivu katika maisha yangu. Mwiba na sumu kali ya kuulia mamba! Amepoteza dira yangu, amenipa machungu na mateso. Najuta...najuta kukutana naye...” Bruno anawaza akilini mwake, akiwa ameshasahau kabisa kwamba anazungumza na Vanessa. “Bruno, naomba unijibu basi...” sauti hii tamu ndiyo iliyomnasua mawazoni. “Unasema?” “Mungu wangu! Sijui kwanini unaruhusu maumivu katika moyo wako? Unajua unaweza kujiona huna thamani tena, huna umuhimu tena au hakuna mtu ambaye ataona thamani yako, hayo yanaweza kuwa mawazo yako ya machoni, lakini ndani yako lazima ujitengenezee ushindi, ujijenge wewe mwenyewe kuwa ni mshindi na huna tatizo kubwa. “Thamani hiyo ndogo ambayo unajipa sasa, wapo watu wengi sana ambao wanakuhitaji kwasababu wanakuona una thamani kubwa sana kwao. Acha kijipangia maisha, amini kila kitu kinawezekana, mimi mwenyewe naamini bado hujashindwa. Wewe ni mshindi Bruno. “Tafadhali futa machozi yako na kila fikra mbaya iliyopo kichwani mwako. Tatizo ulilonalo halimaanishi kuwa mwisho wa maisha yako umefika. Bado una nafasi kubwa sana Bruno,” yalikuwa maneno makali sana yaliyotoka kinywani mwa Vanessa kwa sauti laini sana ya kusihi. Bruno akamwangalia Vanessa kwa macho ya huruma, alikuwa mtu pekee aliyempa faraja baada ya kuikosa kwa muda mrefu sana. Alianza kuiona thamani yake ikirejea taratibu, alianza kuona utu wake. “Nashukuru sana Vanessa dada yangu, wewe ni mwanamke wa aina yake, unanifanya nianze kuwa na furaha sasa, ahsante sana,” Bruno akasema. “Usijali Bruno, napenda kuona furaha yako na siyo machozi.” “Ahsante, nashukuru kusikia hivyo.” “Naamini sasa umenikubalia kwa moyo mmoja, usiwe na mashaka na jambo hili tafadhali.” “Usijali, nipo tayari. Sijui nikushukuru vipi, lakini Mungu wangu wa Mbinguni ndiye anajua shukrani iliyopo moyoni mwangu. Ahsante sana Vanessa.” “Nimefurahi kusikia hivyo, mimi naenda kwenye mihangaiko yangu, jioni nitakuja kukuona tena, kuwa huru sasa, sawa?” “Sawa.” “Samahani naweza kuchukua namba zako za simu?” Vanessa akamwuliza. “Sina.” “Ok, baadaye. Ugua pole.” “Ahsante.” Vanessa akaondoka. *** Kama Vanessa alivyoahidi, jioni alikwenda tena hospitalini kumuona Bruno. Alimpelekea chakula kizuri sana, ndizi nyama pamoja na matunda. Akamlisha kwa upendo huku akimtania. Bruno anatabasamu! Anacheka! Muda mfupi kabla hajaondoka, Vanessa anatoa simu kwenye pochi na kumkabidhi Bruno. “Ya nini?” “Yako Bruno, ukiwa na tatizo lolote nifahamishe. Tayari nimeshakuwekea vocha na nimeshaingiza jina langu, so tuwasiliane wakati wowote ukiwa na dharura sawa?” “Ahsante sana Vanessa, lakini kwanini unanifanyia mambo yote haya?” “Sisi wote ni binadamu na tunaishi katika sayari moja Bruno, lazima tupendane. Hilo tu, hakuna kingine!” “Nimefurahi sana kusikia hivyo. Nakushukuru sana.” “Usijali. Mi nakwenda, nitakuja kukuona tena asubuhi.” “Ahsante, usiku mwema.” “Nawe pia...usitegee kunywa dawa Bruno.” “Kwa hilo usijali, nakuahidi.” Wakaagana. *** SAA 3:00 za usiku, Vanessa alikuwa anapiga honi getini kwake, lakini msichana wake wa kazi hakutoka kumfungulia. Kwa dakika tatu nzima aliendelea kufanya hivyo bila mafanikio. Akiwa ndiyo kwanza amefungua mlango akitaka kushuka ili akafungue geti mwenyewe, geti likafunguka. Akaingiza gari huku akifoka. Akaegesha. Wakati anamalizia kushusha mguu wa pili kutoka kwenye gari, akiendelea kufoka, akakutana na kibao cha nguvu shavuni mwake. Kilikuwa kibao kizito alichohisi maumivu makali sana. Hakupata shida kugundua kwamba kilikuwa kibao cha mwanaume. Lilikuwa kofi moja tu, la nguvu lililompotezea mwelekeo. Akiwa anatafakari namna ya kukabiliana na aliyempiga ambaye bado hajamuona, akakutana na kibao kingine! Akaanguka chini! Akagaagaa chini akiwa haelewi kinachoendelea, moyo wake ulishabadilisha mapigo na kwenda kasi kuliko kawaida. Akayatoa amcho yake kumwangalia aliyekuwa akipambana naye. Haikuwa rahisi kuamini! Alikuwa ni Emma! Emmanuel! “Emma?! Ni wewe mpenzi wangu? Kwanini unanipiga?” “Nyamaza!” Emma akasema kwa ukali. “Kwanini unanipiga?” Vanessa akasema akizidisha kilio. Hakuona kosa la kupigwa na mpenzi wake, kila alipojaribu kuvuta picha kama kuna mahali alikuwa amemkosea, hakuona. “Amka uende ndani haraka sana,” Emma akamuamrisha. Vanessa akajizoa-zoa pale chini na kuamka, akaanza kupiga hatua za kivivu, akiwa ameshika shavu lake moja akiugulia maumivu makali. Akaenda moja kwa moja hadi chumbani kwake. Akajitupa kitandani. Muda mfupi baadaye, Emma akaingia akiwa anakazana sana. “Umeanza umalaya siyo?” Emma akauliza kwa sauti iliyojaa ukali. Ni swali lililomshutua sana Vanessa, akabaki kimya kwa muda akitafakari. Alihisi huenda alimfuatilia hospitalini na kumuona akiwa na Bruno. Hata kama alimuona, alikuwa na uhakika gani kwamba Bruno ni mpenzi wake? Hata hivyo Bruno si mpenzi wake. “Sasa kwanini ananiuliza swali hilo?” Akawaza kichwani mwake. “Si naongea na wewe?” Emma akasema, akionesha kujiandaa kumwangushia konde lingine. “Mbona unanifanyia hivi lakini? Majina gani hayo unayoniita? Na kwanini unasema mimi ni malaya?” “Ulikuwa wapi?” Emma akauliza tena. “Mara ya mwisho kuongea na wewe kwenye simu nilikwambia naekea wapi?” “Sitaki kujua mambo ya mara ya mwisho, nakuuliza sasa hivi umetokea wapi?” “Hospitalini kumwona Anko!” “Kumwona Anko siyo?” “Ndiyo!” “Una uhakika?” “Ndiyo!” “Kwanini nakupigia simu hupokei?” “Umenipigia saa ngapi jamani?” “Hebu toa simu yako.” Vanessa akatoa simu yake kwenye pochi, hakuamini alipokutana na missed calls 12 zote za mpenzi wake Emma. “Mungu wangu sikuona calls zako Emma. Lakini ndiyo sababu iliyokufanya unipige kiasi hiki?” “Umeona ni sababu ndogo siyo?” “Sijasema ndogo, lakini action uliyochukua ndiyo kubwa kuliko tukio lenyewe.” “Sasa niambie kwanini hukupokea simu?” “Sikuona Emma, unajua nilipokuwa naingia hospitalini, niliweka simu silence ili nisisumbue wagonjwa, nilipotoka sikukumbuka tena kuirudisha kawaida.” “Nakuambia kwa mara ya mwisho...sitaki kuona napiga simu zaidi ya mara mbili hupokei...nitakuja kukuvunja taya siku moja...” Emma alisema kwa sauti kisha akabamiza mlango na kuondoka. Vanessa akabaki analia peke yake. Vituko vya Emma vilikuwa vimeshamchosha kwa kiasi kikubwa. Kila wakati alikuwa akimpiga, kosa dogo tu, ilikuwa lazima apigwe. Kilichomuuma zaidi ni kwamba, Emma alikuwa akimfanyia vurugu nyumbani kwake, ambapo analipia kodi mwenyewe. Hakufurahia kabisa mapenzi na kijana huyu ambaye ni mkorofi kupindukia, ingawa moyoni mwake alishindwa kuelewa ni kwanini alikuwa akimpenda kwa kiasi hicho. Emma ni mwanaume ambaye alimwingia moyoni na kumchanganya sana moyo wake. “Lakini lazima siku moja nifanye maamuzi, lazima nifanye kitu, siwezi kuwa katika penzi la kitumwa kwa muda wote huu. Mwanaume anafanya vituko vya kila aina. Hana mapenzi ya dhati, mkorofi, ananipiga, kwanini niendelee kumsumbukia mwanaume wa aina hii? Lazima nikubali kujitoa mikononi mwake, lazima...” Vanessa akawaza hayo kichwani mwake kisha akaamka haraka. Akavua nguo zote na kujifunga taulo kifuani, akawa tayari kuingia bafuni, lakini ghafla akasita. Akarudi tena chumbani, akapiga hatua za taratibu kuelekea kwenye dressing table yake.
Akaiachia ile taulo yake, ikaanguka chini. Akayakazia macho yake katika umbo la mtu yule aliyekuwa kwenye kioo. Msichana huyo mrembo ambaye alikuwa na sifa zote. Aliyaacha macho yake kwa muda katika nywele zile zilizotengezwa na mtu ambaye anajua vyema kazi yake. Akarudi kutazama zile nyusi zilizochongwa vyema. Akakaza macho yake katika macho ya kulegea ya mrembo yule, akamtamani. Alikuwa mwanamke mzuri sana. Akayashusha macho yake hadi kwenye matiti yaliyosimama wima ya mrembo huyo. Akashuka chini hadi kwenye kitovu kilichozungukwa na garden love iliyochanua vyema. Hakuchoka, akatazama kiuno chake, akachanganyikiwa. Kiuno kile kilikuwa kimebebwa na hips pana za kutosha ambazo zilizidisha urembo wa mwanamke yule. Akatabasamu! Alikuwa mwanamke mzuri sana kwa kutazama, hakustahili kupigwa wala kunyanyaswa. Alikuwa mwanamke ambaye alitakiwa kutuzwa kwa kila hali, siyo kupigwa! Alitakiwa kubembelezwa kwa kila namna. Mwanamke huyo ni Vanessa! Yeye mwenyewe! “Sitakiwi kunyanyaswa!” Akawaza kisha akachukua taulo lake chini na kuingia bafuni. Akafungua bomba la mvua, akaanza kuoga! *** “Tulia hivyo hivyo!” Tunu akamwambia Bruno ambaye alikuwa amelala kitandani chali, akiwa mtupu kabisa. “Sawa mama, kwani mimi nina neno?!” “Fuata masharti yangu, nataka kukuonesha kwanini naitwa Tunu mtoto wa Kitanga. Mimi nimefundwa kwetu Uziguani...” Tunu akasema kwa sauti laini, huku akiendelea kumpaka Bruno mafuta mwili mzima. Raha aliyokuwa akiisikia ilikuwa siyo ya kitoto, kwani Tunu alikuwa akimpaka kwa staili ya kupapasa au kama ambaye alikuwa anatafuta kitu alichopoteza. Alijihisi kama yupo katika kisiwa kizuri chenye burudani ya aina yake. Macho ya Tunu yalikuwa yanamchanganya sana Bruno aliyekuwa ametulia kitandani, huku miguno ya kimahaba ikisikika. “Nakupenda sana Bruno wangu, nakupenda sana....” “Nakupenda pia Tunu,” Bruno akasema akitabasamu... *** “Nooooooooo....” Bruno akapiga kelele akiwa kitandani hospitalini. Alishtuka kutoka katika ndoto ambayo hakupenda kuikumbuka kabisa. Tunu alikuwa mwanamke mbaya sana kwake. Huyo ndiyo sababu ya yeye kuwa hospitalini muda huu. Kitandani! Akiwa amekatwa mguu wake, kwa maneno mengine alikuwa ameshapata kilema cha maisha! Sababu kubwa ni Tunu. Machozi yakaanza kushuka machoni mwake. *** Ni kama alikuwa anagopa kuharibu marumaru iliyokuwa chini wakati akitembea, alikuwa akitembea kwa mnyato, kama anaogopa kuumia miguu yake. Hata hivyo, si kama alijifanyisha, hiyo ilikuwa tembea yake. Anapiga hatua za taratibu, huku taulo ikiwa kifuani mwake. Anafunga mlango wa bafuni na kuingia chumbani kwake, anajitupa kitandani, anahema kwa kasi kisha anasimama tena. Akabaki akiwa amesimama akiwa hajui ni kwanini alifanya hivyo. “Nilikuwa nataka kufanya nini? Lazima kuna kitu kilinisababisha nisimame, ni nini?” Akawaza Vanessa akiwa hana jibu. “Oh! Yeah, nimekumbuka!” Akasema kwa sauti akisogelea meza yake ya kujipambia. Akaketi kwenye kiti kilichokuwa mbele yake. Akayatupa macho yake kwenye kioo na kumtulizia macho msichana yule mrembo ndani ya kioo. Ilikuwa ni taswira ya sura yake mwenyewe. Akaachia tabasamu la kivivu akiashiria kwamba anaukubali uzuri wa mwanamke yule mrembo aliyepo mbele yake. Anajikubali. “Mimi ni mrembo, sifa unajipa mwenyewe...” akawaza akitabasamu. Siku zote usiku, huwa hana kazi kubwa sana kwenye dressing table yake, akachukua kofia yake yake ya plastiki na kuivaa kichwani. Akajipuliza na manukato mepesi kisha akatoka. Hatua ya kwanza, hatua ya pili hadi sebuleni, akaketi kwenye sofa kubwa akitazama runinga. Pembeni yake alikuwa amekaa msichana wake wa kazi Amina. “Shikamoo dada...” Amina akamsalimia. “Marhaba...” “Pole na kazi!” “Ahsante. Nina maswali kidogo nataka kukuuliza.” “Uliza tu dada.” “Mimi ni nani kwako?” “Bosi wangu!” “Ukiachana na huo ubosi, ni nani kwako?” “Dada.” “Unamaanisha unachokisema Amina?” “Ndiyo dada.” “Hivi, unafahamu ni kwanini upo hapa?” “Ndiyo!” “Enheee...” “Kwa ajili ya kufanya kazi za hapa nyumbani!” “Unazijua vizuri?” “Ndiyo dada!” “Unaweza kunitajia?” “Ndiyo, kusimamia mambo yote yanayohusu usafi, kupika na kazi nyingine ndogo ndogo.” “Ok! Sasa kwanini wakati napiga honi getini hukutoka kunifungulia?” “Shem Emma aliniambia nisitoke!” “Unasemaje wewe? Hivi una akili kweli? Hii ni nyumba ya Emma au yangu? Emma ulimkuta hapa au alikukuta na ni mimi ndiye niliyekutambulisha kwake?” “Alinikuta dada, lakini kutokana na wewe kunitambulisha kwake kama shemeji yangu, sikuona vyema kubishana naye, maana najua ni mchumba wako.” “Sasa Emma amenipiga hapo nje, yote hayo ni kwasababu yako. Sasa natoa agizo, kuanzia leo unatakiwa kunisikiliza mimi kwa kila kitu, fuata kila ninachotaka na siyo Emma, umenielewa?” “Ndiyo dada!” Vanessa akainuka akiwa amefura, akaenda kwenye chumba cha chakula, akaanza kula. Hakuwa na raha ya kukaa sebuleni muda mrefu sana, akaingia zake chumbani kulala. *** Usiku mzima aliishia kujigeuza-geuza kutoka upande mmoja wa kitanda kwenda mwingine, hakupata usingizi kabisa. Bruno alitawaliwa na maumivu makali sana, si maumivu ya jeraha la mguu, yalikuwa maumivu makali ya moyo. Alikuwa akiumizwa na jinsi alivyotendwa na Tunu, mwanamke huyo ndiye chachu ya matatizo yote aliyonayo sasa hivi, ndiyo sababu ya yeye kuwa amelazwa. Kwanini ampende? Kwanini amuone mwema? Hakuwa mwanamke mwenye thamani kabisa, kwake alikuwa sawa na mbwa koko, ambaye hana maana yoyote, zaidi ya kufakamia vyakula jalalani! Kumbukumbu za Tunu zilimsumbua sana. Asubuhi hii ndiyo anaanza kupata usingizi, baada ya kuteseka usiku mzima. *** Honi mfululizo zilikuwa zikipigwa nyuma ya gari la Vanessa kwenye eneo la mataa ya Morocco, kwenye makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Kawawa, hiyo ikiwa ni baadada ya taa ya kijani kuwaka, kuruhusu magari yanayotokea Msasani kuingia barabara inayelekea Posta. Si kwamba, Vanessa hakuona ile taa, aliona vizuri sana, lakini muda wote tangu alipotoka nyumbani, alikuwa hajawa na uamuzi wa moja kwa moja kwamba aanzie ofisini kwake Posta ndipo aende Hospitalini au aende kwanza Hospitalini kisha aende ofisini. Akiwa yupo kwenye foleni na taa kuruhusu, alikuwa hajapata uamuzi wa moja kwa moja. Akasita kwenye foleni. “Niende wapi?” Akawaza kichwani mwake, lakini baadaye akapata jibu. “Acha nianzie kwanza Hospitalini,” akajisemea mwenyewe, akiwa hana habari na zile honi. Aliendelea kusubiri kwa muda mpaka taa ziliporuhusu kunyoosha moja kwa moja kufuata Barabara ya Kawawa. Akaondoa gari kwa kasi. Ndani ya robo saa tu, alikuwa anaegesha gari lake, ndani ya Hospitali ya Amana. Akaenda hadi wodini na kuingia. Alipopita kwenye kitanda cha Bruno, akamuona akiwa amelala. Akasimama kwa muda akimtazama, akazidi kumuonea huruma. Akakata shauri kwamba aanzie kwanza kwa mjomba wake, ndipo arudi kumtazama tena Bruno. Wazo hilo lilipita bila kipingamizi akilini mwake. Akaenda kumuona mjomba wake, kwa bahati nzuri sana, ilikuwa ndiyo siku aliyoruhusiwa. Baada ya taratibu zote kukamilika, akamshika mkono, akimsaidia kutembea kuelekea nje. Kabla hawajaufikia mlango mkubwa, Vanessa akamwomba mjomba wake, amtambulishe kwa rafiki yake wa karibu. “Ni nani?”
“Yule aliyelala pale!” “Sawa.” Walipofika, Vanessa akaanza kumuamsha Bruno aliyekuwa anaogelea katika usingizi mzito. Aliposhtuka, akakutanisha macho yake uso kwa uso na mjomba wake na Vanessa. “What? Bryson?” (Nini? Bryson?) Bruno akapayuka. “Bruno?” Mjomba wake Vanessa naye akamwita Bruno akionekana kushangaa sana. “Bado unaendelea kunifuata? Hujaridhika tu? Unataka kuchukua na roho yangu kabisa?” Bruno akamwuliza, Vanessa akiwa kimya huku akichanganyikiwa kichwani mwake. “....hivi, mnafahamiana?” Vanessa akawauliza. Hakuna aliyejibu. Pamoja na kwamba alikuwa katika hali ya kuugua, lakini Bruno alionekana kupata nguvu za ghafla. Alikuwa amefura sana pale kitandani akimwangalia Bryson kwa hasira isiyo ya kawaida. Vanessa yupo kimya akiwatazama kwa macho ya kuhoji. Anapatwa na maswali mengi sana kichwani. Mjomba wake anafahamiana na Bruno? Lilikuwa swali gumu sana. Hata hivyo halikuwa na ugumu mkubwa au mshangao wa ajabu. Kufahamiana ni jambo la kawaida sana, lakini alishangazwa sana na namna ya kufahamiana kwa watu hawa wawili! Wanatishana! Wanafahamiana kwa shari! Vipi mjomba wake awe mkorofi? Sawa, inawezekana akawa mkorofi, lakini si kwa kijana huyu mwenye macho yanasoma huzuni na simanzi tele machoni mwake. “Wana nini hawa?” Akawaza kichwani akiwa hana amani kabisa. Macho ya Vanessa yakaanza kuwaangalia watu hawa wawili ambao wamekaziana macho. “Hivi mna nini nyie? Anko unamfahamu Bruno?” Mjomba wake hakujibu. “Bruno, kuna nini kati yako na mjomba?” Vanessa akauliza akiwa anawashangaa kwa jinsi tafrani ilivyokuwa kubwa. “Huyu ndiyo mjomba wako?” Bruno akauliza badala ya kujibu. “Yeah! He is my uncle.” (Ndiyo! Ni mjomba wangu.) “Your uncle?” (mjomba’ko?) “Yes!” (Ndiyo!) “Ok! Sikiliza Vanessa, pamoja na misaada ambayo umekuwa ukinisaidia, naomba leo nikukosee heshima, huyu ni mjomba mpumbavu, tena hana maana yoyote kabisa. Huyu ni mpumbavu. Muuaji. Hafai. Kama utaona inafaa, sitisha misaada yako kwangu kuanzia leo,” Bruno akasema kwa hasira sana akionekana kutaka kuamka kitandani! Haikuwezekana! Alikuwa mgonjwa! Mlemavu! Hana ujanja wowote wa kuamka na kufanya kitu chochote. Anamwangalia Vanessa kwa macho yaliyoonesha kwamba yupo tayari kwa lolote na hajali kitu chochote. Baadaye akayarudisha macho yake tena kwa Bryson ambaye alionekana kuwa na hasira zaidi hata ya Bruno, lakini naye alikuwa na tatizo lile lile. Hana nguvu! Angali anaumwa! “Kuna tatizo gani kati yenu?” Hakuna aliyejibu. “Mmedhulumiana?” Kimya! “Mbona nawauliza, halafu mpo kimya? Mna nini lakini mbona mnanichanganya sasa?” Vanessa akasema, lakini hakuna aliyezungumza chochote. “Kwasababu hakuna anayetaka kuzugumza neno, Anko twende nyumbani, haya mambo nitazungumza na Bruno baadaye.” Wote kimya! Vanessa akamshika mkono mjomba wake na kuanza kuondoka hadi nje walipoingia kwenye gari na kuondoka. Njia nzima Vanessa alikuwa na mawazo, lakini katu hakuzungumza kitu na mjomba wake. *** Bruno akayatoa macho yake kwa mshangao, akimwangalia mwanauume huyu anayeonekana kujazia vyema kifuani mwake. Hakuwa na sababu ya kutaka kuuliza mahali popote kama huyu bwana anafanya mazoezi. Yupo peke yake, akiwa amevalia suruali ya jeans ya rangi ya blue na fulana nyeupe ya kukata mikono. Sura yake inatangaza vita! Anaonekana dhahiri kudhamiria kuua mtu! Bruno akiwa bado yupo katika taharuki, anashangaa Tunu anapiga magoti kwa mwanaume huyu akilia na kuomba asamehewe! Woga wake haujifichi, analia na kumwangalia kwa huruma. “Samahani mume wangu, naomba unisamehe, sikufanya kwa makusudi mpenzi, ni bahati mbaya. Naomba msamaha wako baby,” Tunu anazungumza kwa sauti ya kusihi mbele ya mwanaume huyu mwenye miraba minne! “Tunu my wife? Why? Why? Why Tunu? Kwanini umenifanyia hivi?” Mwanaume huyo akazidi kulalamika akionekana kuwa na hasira kuliko kawaida. “Please forgive me my husband, nisamehe mpenzi wangu tafadhali, usinitende hivyo, najua una hasira na unaweza kuniua, lakini nisamehe.” “Nikusamehe?” “Ndiyo?” “Kwa usaliti huu?” “Nisamehe baby!” “Ndani ya nyumba yangu?” “Bryson sweetie nisamehe.” “Kitandani kwangu?” “Najua ndiyo maana naomba msamaha. Najua kiasi kiasi gani una maumivu, nisamehe tafadhali mpenzi wangu.” “No! No! No! I can’t, lazima nifanye kitu kama fundisho.” “Hapana baby!” Bryson hakutaka kusikiliza maneno ya Tunu, akachomoa bastola aliyokuwa ameichimbia kibindoni. Akaielekeza usoni mwa Tunu. “Naanza na wewe, halafu namuua na huyo mshenzi mwenzako, huwezi kunisaliti Tunu, huwezi...” Bryson akasema akionekana kukasirika sana. Muda wote Bruno alikuwa kama amenaswa na shoti ya umeme, lakini alipoona bastola, akachanganyikiwa. Mawazo yake ya mwanzoni kwamba, mambo yangeweza kuisha kwa kuzungumza na kumalizana kiume, yakatoweka kabisa, pale kifo kilikuwa kinanukia wazi wazi! Lakini katika maajabu yote, hili lilikuwa la kwanza, kwasababu kwa kipindi chote cha miezi sita alichokuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Tunu, hakuwahi kumwambia kwamba ana mume. Imekuwaje leo anapiga magoti mbele ya mwanaume huyu akisema ni mumewe? Akamwangalia Tunu kwa mshangao, kisha akayarudisha macho yake kwa Bryson ambaye alionekana dhahiri kudhamiria kuua. Macho yake yalikuwa yanasoma huruma na kuomba msamaha! “Tunu, si ulisema hujaolewa?” Bruno akauliza kwa uchungu sana huku woga ukiwa umemshika. “Nyamaza Bruno, kikubwa hapa ni kuomba msamaha, kama ni kosa limeshatokea.” “Pumbavuuuuuu...mnashauriana ujinga gani hapo? Kwanza inabidi nianze na wewe fala kwanza, kabla ya Tunu. Haya Sali sala zako za mwisho kabla ya kifo chako. Haraka...” Bryson akasema akionekana kutaka kuachia risasi... *** “BRYSON, BRYSON, BRYSON.....Noooooooooo....” Bruno akajikuta akipiga kelele wodini, wazo la kwamba alikuwa wodini, lilishaondoka. Mawazo yake yote yapo kwa Bryson, ambaye kwake ni kama sumu ya nyoka ukiwa porini bila dawa ya kuulia sumu hiyo. Ghafla akamwona mtu ambaye hakutarajia kumuona mbele yake. Alikuwa ni Vanessa. “Umefuata nini?” Bruno akauliza kwa hasira. “Nimefuata nini?” “Ndiyo, umefuata nini hapa? Sitaki msaada wowote kutoka kwako!” “Kweli?” “Ndiyo!” “Hebu niangalie machoni Bruno!” Bruno akamwangalia. “Haya sasa sema hutaki msaada wowote kutoka kwangu!” Bruno hakuweza, kilichofuata ikawa ni machoni mwake. Alionekana kuwa na maumivu makali sana moyoni mwake. Macho yake yalitangaza dhiki, sura yake ikaonesha huzuni na kinywa chake kikizidisha machungu kwa Vanessa aliyekuwa amesimama mbele yake. Kwa kumtizama tu Bruno, Vanessa aliweza kugundua kwamba, tayari Bruno alikuwa mbali sana kihisia, kwamba anaweza kufanya kitu tofauti kama hatapatiwa msaada wa ushauri kwa haraka! Mara moja akaketi kitandani, akajivuta juu ya kitanda na kumuinua kidogo Bruno, kisha akamlaza miguuni mwake. Akayaacha macho yake yaoneshe nia yake ya kumuweka miguuni mwake. Bruno akazidi kushangazwa na wema wa mwanamke huyu mzuri, mwenye sifa zote za kuwa mrembo! Kwa jinsi alivyokuwa amependeza asubuhi hiyo, kwa hakika hakustahili kabisa kukaa katika kitanda kile cha mgonjwa, ambacho si ajabu kulikuwa na unyevunyevu kutokana na Bruno kulala muda mrefu. Lakini amekaa! Amemlaza miguuni mwake akitabasamu! Hana kinyaa!
0 Comments