Katika enzi za kale, kwenye Mlima wa Emi kulikuwa na majoka mawili yenye umri wa miaka elfu moja, moja jeupe, moja jeusi. Majoka hayo mawili yalipenda sana mandhari ya watu wanapoishi, basi yalijibadilisha kuwa wasichana wawili warembo, moja lilijipa jina la Bai Suzhen , jingine liliitwa Xiao Qing. Siku moja walifika kwenye sehemu maarufu yenye mandhari nzuri, ziwa la Xihu mjini Hangzhou.
Mandhari ya ziwa la Xihu kweli ilivutia sana, walipofika kwenye daraja moja la ziwa hilo ghafla mvua ilianza kunyesha, wakakimbia mvua na kujificha chini ya mti mmoja mkubwa. Wakati huo alikuja kijana mmoja mwenye mwamvuli aliyeitwa Xuxian, ambaye alikuwa akirudi nyumbani baada ya kusafisha makaburi. Alipoona wasichana chini ya mti aliwasaidia kwa mwamvuli wake na baadaye aliwasaidia kuwapeleka nyumbani kwa mashua. Bai Suzhen alianza kumpenda kijana huyo, alipoagana na kijana huyo alimwambia kesho aje kuchukua mwamvuli wake.
Siku ya pili kijana Xuxian alifika nyumbani kwa Bai Suzhen karibu na ziwa kuchukua mwamvuli wake. Bai Suzhen alimshukuru sana na kumwuliza habari za familia yake, akafahamu kuwa alifiwa na wazazi wake mapema tokea alipokuwa mtoto na sasa anaishi kwa dada yake na kufanya kazi katika duka moja la dawa. Msichana Bai Suzhen aliomwomba aolewe naye. Hakika Xu Xian alikuwa na furaha isiyo kifani. Kwa kuongozwa na Xiao Qing walifanya sherehe ya ndoa. Baada ya ndoa walianzisha duka la dawa. Bai Suzhen alifahamu matibabu, kila siku aliwatibu wagonjwa wengi.
Kulikuwa na sufii mmoja wa dini ya Buddha aliyekuwa anaitwa Fa Hai. Fa Hai alikuwa anajua siri ya Bai Suzhen kuwa alikuwa joka mwenye miaka elfu moja, na hakika angewadhuru watu, hivyo alidhamiria kumwokoa kijana Xu Xian.
Siku moja Fa Hai alikuja nyumbani kwa Xu Xian, alimwambia, mkewe ni zimwi. Xu Xian hakuamini. Basi Fa Hai alimwambia, kama haamini, ajaribu kumshawishi anywe pombe tarehe 5 Mei, siku ya mashindano ya mbio za mashua, na kama akinywa atarudia asili yake.
Tarehe 5 Mei ilifika, kila familia hunywa pombe kusherehekea siku hiyo. Majoka yanaogopa pombe, Bai Suzhen alitaka kwenda mlimani kukwepa, lakini alikuwa na wasiwasi kuwa mumewe Xu Xian atamshuku, alikuwa hana budi ila kubaki nyumbani akijidai anaumwa.
Ingawa Xu Xian hakuamini aliyoambiwa na sufii Fa Hai, lakini kila mmoja katika siku hiyo hunywa pombe, hivyo alimshawishi mkewe anywe pia. Mkewe Bai Suzhen alishindwa kukataa, alikunywa glasi moja, mara akaanza kuona kizunguzungu. Xu Xian alimsaidia hadi kitandani, kisha akaenda jikoni kumtengenezea supu ya kuondoa ulevi. Akaja na bakuli moja la supu kitandani, alipofungua chandarua akaona joka kubwa jeupe limelala kitandani, Xu Xian alikufa kwa mshtuko.
Joka jeupe lilipozinduka likaona mumewe amekufa kwa mshtuko, alihuzunika sana, alimwomba Xiao Qing amtunze mumewe, na yeye akatoka haraka na kwenda kwenye mlima mmoja ulioitwa Xianshan ambako kulikuwa na aina moja ya jani la dawa ambalo lingeweza kumwokoa mumewe.
Wakati huo Bai Suzhen alikuwa amepata mimba ya miezi saba. Alipofika mlima Xianshan watoto waliokuwa wananlinda mlima walipojua kuwa anataka kuiba jani la ajabu walipambana naye. Mungu wa mlima huo alipoona jinsi Bai Suzhen alivyohangaika kumwokoa mumewe alimpa jani la ajabu.
Xu Xian alifufuka, lakini bado alikuwa ameshikwa na hofu. Bai Suzhen alipatia mzungu wa kumdanganya, alitumia kitambaa kirefu cheupe na kukigeuza kuwa joka kuzunguka kwenye boriti la dari na kumwita mumewe aone. Kwa kuona joka hilo, Xu Xian aliondoa mashaka yake juu ya mkewe, na waliendelea kuishi kwa mapenzi.
Sufii Fa Hai hakukufa moyo. Siku moja alimdanganya Xu Xian kwenda kwenye hekalu lake na kumzuia asirudi nyumbani. Baadaye mkewe na Xiao Qing walikuwa kwenye hekalu wakitaka kumrudisha nyumbani, wakagombana na sufii. Wakati walipopurukushana, Bai Suzhen alisikia maumivu ya uja uzito, kwa haraka alirudi nyumbani na Xiao Qing, alipofika kwenye daraja alikumbuka jinsi alipokutana na mumewe na kuanza na mapenzi, alihuzunika sana. Xiao Qing alimlaumu Xu Xian kwa kumsikiliza sufii, alimshawishi Bai Suzhen amwache mumewe.
Kwa kusaidiwa na sufii wengine, Xu Xian alitoroka kutoka hekalu na kwenye daraja alimpata mkewe. Mkewe alimwambia ukweli wa mambo, kwamba kweli alikuwa joka. Wakati huo Xu Xian alikuwa ameelewa kwamba mapenzi ya mkewe ni ya kweli na makubwa, akamwahidi kuwa hatajali akiwa ni kitu gani, lakini ataishi naye mpaka kufa.
Baada ya kurudi nyumbani, muda mchache baadaye Bai Suzhen alizaa mtoto. Katika siku ya kutimiza mwezi mzima kwa mtoto walifurahi sana, lakini wakati huo sufii Fa Hai alikuja tena nyumbani, alimkamata Bai Suzhen na kumtia chini ya mnara wa Leifong kando ya ziwa la Xihu.
Xiao Qing alitorokea mlimani Emei, alijitahidi kuinua uhodari wake wa mapambano, mwishowe alimshinda Fa Hai, na alimwokoa Bai Suzhen.
0 Comments