Simulizi :Barua Kutoka Kwa Marehemu Sehemu Ya Pili (2)
Lakini kila alipojaribu kuvuta kumbukumbu vizuri juu ya ile sauti aliyoongea nayo kwenye simu, anagundua kwamba ni kweli alikuwa anaongea na Jeff. Mpenzi wake wa zamani ambaye kwa sasa ni marehemu. Sasa anazidi kuchanganyikiwa, maana amepiga simu kabisa. Tena ametoa onyo kwamba, hatakiwi kwenda Kondoa na badala yake anatakiwa kugeuza asubuhi inayofuata kurudi Dar es Salaam. “No...haiwezekani...” Davina akawaza huku akifungua begi lake na kutoa suruali nyepesi na blauzi fupi ya kubana, akavaa. Mara moja akapiga simu Mapokezi. Muda si mrefu sana, simu yake ikapokelewa. “Mapokezi hapa, naomba nikusaidie tafadhali!” sauti ya msichana wa Mapokezi ambayo ilijaa uchovu ilisikika. “Room no. 104, ghorofa ya tatu!” “Ndiyo!” “Kuna Klabu gani nzuri ya usiku hapa Dodoma?” Davina akauliza. “Club 84!” “Taxi?” “Zipo. Nimpigie dereva?” “Tena afanye haraka sana, baada ya dakika 10 nitakuwa hapo!” “Ok!” Davina aliogopa kuendelea kulala pale hotelini, aliona ni bora aende disko akapoteze muda hadi asubuhi ili aanze safari ya kwenda Kondoa, bado hakuwa na wazo la kurejea tena Dar es Salaam. Muda mfupi baadaye alikuwa kwenye taxi akipelekwa Klabu, alipofika akamlipa dereva kisha akaingia. Ilikuwa Klabu nzuri kuliko kawaida, hakutegemea kama Dodoma kungekuwa na ukumbi mzuri kama ule. Kilichoendelea ilikuwa ni kunywa sana pombe mpaka akalewa chakari! Uzuri wake, ulikuwa tatizo kubwa kwa wanaume waliomuona akiwa amekaa peke yake tena mwenye mawazo mengi. Wengi walimfuata na kujaribu kutupa ndoano zao, lakini Davina hakuwa na muda huo, hakuwaza wala hakuwa na hamu na wanaume! Alikuwa akiwaza matatizo yake tu! “Siogopi kitu chochote, najua Jeff umeshakufa, ila kuna mtu anajaribu kucheza na akili yangu,” Davina akawaza akiendelea kunywa pombe kwa hasira. Davina aliendelea kunywa hadi saa 10:40 za usiku ambapo wimbo wa mwisho ulipigwa, akaenda kuchukua taxi na kwenda zake hotelini. Hakulala tena, akaendelea kutizama runinga hadi kulipokucha. Saa 12:00 alikuwa kwenye basi, tayari kwa safari ya kwenda Kondoa, nusu saa baadaye. *** Sauti ya kilio cha Davina ndiyo iliwashtua wazazi wake waliokuwa ndani wanapata chakula cha mchana! Ilikuwa ni saa tisa na dakika zake za mchana. Mama yake ndiyo alikuwa wa kwanza kutoka nje na kwenda kumpokea. Alishajua tatizo ni nini, hakuwa na haja ya kumwuliza. Akamwingiza ndani, ambapo alipokutanisha macho na baba yake, akazidi kuangua kilio. “Tulia kwanza mama, mbona unakuwa na hasira hivyo? Umeshakuja nyumbani, sisi ni wazazi wako, tunakupenda na hatutakuwa tayari kuona unapata matatizo!” baba yake Davina akasema akimtizama mwanaye usoni. “Lakini baba, hutaki kuamini kama ni mzimu wa Jeff ndiyo unaonitesa...sasa ona anavyonitesa, jana nikiwa Dodoma, kanipigia simu na amesisitiza nisije Kondoa, sasa amejuaje kama mimi nakuja huku?!” Davina akamwambia baba yake ambaye alionekana kushtushwa na kauli ile. “Amekupigia simu? Una uhakika? Namba zilikuwa zake?” Baba yake akauliza maswali mfululizo. “Ndiyo baba nina uhakika na sauti yake, lakini namba hazikutokea, zilikuwa ni private!” “Nilikuambia ni uongo, yupo mtu anayekuchezea, maana kama angekuwa yeye, kwa nini asingekupigia kwa namba zinazoonekana ili baadaye umpigie kama ukiwa na shida naye?” Mzee Ngamseni akauliza akianza kuonyesha ukali kidogo. Kabla Davina hajajibu kitu, simu yake ikaanza kuita, akaitoa kwenye mkoba na kutizama kwenye kioo cha simu! Ilikuwa private number! Akapokea... Alikuwa ni Jeff. Moyo wa Davina ulizidisha kasi, haikuwa jambo jepesi kuamini kwamba sauti aliyoisikia kwenye simu yake ilikuwa ya Jeff. Lakini kwake yeye, mwanaume ambaye alikuwa naye katika mapenzi kwa miaka mitatu, tena siku za mwisho wa uhai wake alikuwa akilala naye karibu kila siku! Jeff huyu huyu ambaye alikuwa anampigia simu karibu mara ishirini kwa siku, wanayecheka naye pamoja. Wanayekula naye pamoja. Wanayetoka pamoja. Kweli anaweza kusahau sauti yake? Yatakuwa maajabu ya kwanza ya dunia. Sauti haikuwa ngeni hata kidogo! Ilikuwa sauti ya Jeff, tena siyo kwa hisia tu, bali alikuwa na uhakika kabisa kuwa ni yake. Jeff ndiye alikuwa anaongea kwenye simu... “Umesema Jeff?!” Davina akasema kwa woga akiyatoa macho yake. “Ndiyo na sioni sababu ya kujitambulisha kwako kila wakati. Sikiliza Davina...wewe ni mpenzi wangu, nakupenda sana na sipendi kabisa kutumia kauli za ukali au kuamrisha, lakini wewe ndiyo unasababisha. Nitaendelea hivi hadi utakapobadilika... “Kwa nini hutaki kuamini ninachokuambia? Kwa nini unakuwa kichwa ngumu? Nimeshakuambia kwamba mimi nimeuawa na mtu wangu wa karibu ili yeye akupate wewe, ili kuepusha hilo nataka kuja kukuchukua, sasa kwa nini unakuza hili jambo hadi inaonekana kama mimi ni mzimu? Mimi si mzimu...ni Jeff halisi. Jeff, mwanaume wa maisha yako!” sauti ya Jeff ilipenya sawa sawia katika ngoma za masikio ya Davina. Davina hakuzungumza kitu zaidi ya kuanza kulia. Wazazi wake wakawa kama wamepigwa na butwaa, hakuna aliyezungumza chochote zaidi ya kubaki wanamshangaa. “Davina...” Jeff akaita simuni. Davina hakuitika. “Sikiliza kwa kuwa nimeshakuonya mara nyingi na hutaki kusikia, nakuhakikishia, sitakusumbua tena. Hutaona ujumbe wangu wa barua, meseji wala simu. Hutaona yote hayo, lakini nakusisitiza, kamwe usiolewe na mtu yoyote kwa sababu kwa kufanya hivyo utakuwa unajisumbua. Mwanaume ambaye anatakiwa kukuoa wewe ni mimi tu na si vinginevyo. Nitahakikisha hili linatimia. Kwaheri ya kuonana.” “Usikate simu kwanza, sikiliza wewe ni Jeff kweli?” Davina aliuliza baada ya kupata ujasiri wa ghafla. “Ndiyo!” “Kweli?” “Ndiyo!” “Ulikufa lakini?” “Ndiyo!” “Ila bado una nia ya kunioa?” “Ndiyo!” “Kivipi sasa wakati tupo sehemu mbili tofauti?” “Lakini nimeshakuambia kwamba nitakuja kukuchukua na kukuketa huku nilipo?” “Unadhani hilo linawezekana?” “Sana.” “Naomba nikuulize swali la mwisho mpenzi wangu Jeff wa maajabu.” “Uliza.” “Unafahamu kwamba sasa nipo wapi?” “Kondoa.” “Kwa nani?” “Wazee wako.” “Safi kabisa, umepatia....nataka ufanye jambo moja jepesi sana kama ni kweli bado unataka kunioa Jeff!” Ujasiri wa Davina uliwashangaza sana baba na mama yake, hata yeye mwenyewe pia alijishangaa sana. Kuzungumza na mzimu wa Jeff bila woga, moyoni mwake aliona hakuna sababu ya kuwa mwoga tena, wakati kila wakati Jeff alikuwa anapiga simu. Hata hivyo kuuliza kwake maswali mengi kulikuwa na makusudi, alikuwa anataka kuhakikisha kama ni kweli aliyekuwa akizungumza naye alikuwa ni Jeff, marehemu mpenzi wake. Anavyozungumza, anavyojibu maswali, anavyojieleza, anavyojiamini na kila kitu kilikuwa ni Jeff mtupu! Davina alijihakikishia wazi kwamba aliyekuwa anazungumza naye ni Jeff wake! “Sema Davina, unataka nifanye nini?” Jeff akamwuliza. “Baba yupo hapa, naomba uzungumze naye na umweleze nia yako ya kunioa na kunipeleka huko kuzimu ulipo wewe.” “Sawa...mpe mkwe wangu nizungumze naye!” Jeff alisema kwa sauti tulivu sana. Davina akampa baba yake simu. “Haloo haaaalooooo....” baba yake Davina aliita kwenye simu, lakini hakuna aliyeitika. Davina alipochukua ile simu, akagundua kwamba simu ilikatika. “Vipi?” mama yake akauliza. “Imekatika.” Wote wakabaki kimya wakitizamana kwa zamu, lillikuwa jambo la kushangaza sana ambalo walishindwa kabisa kuelewa linavyotokea. Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba Jeff alikuwa marehemu, sasa iweje anapiga simu? Kwa mara ya kwanza mzee Ngamseni alianza kuamini tukio lile! “Mwanangu una uhakika kwamba, sauti ilikuwa yake?” “Ndiyo baba.” “Kweli kabisa?” “Nakuhakikishia baba.” “Basi ni mzimu huu,” mzee huyo alisema kwa sauti ya upole. “Mi’ nilisema tangu mwanzoni hamkuniamini, sasa mmeshuhudia wenyewe!” Davina akasema. “Huu siyo wakati wa kulaumiana mwanangu, kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni mtambiko haraka sana!” “Sawa baba. Nashukuru kwa kukubali kunisaidia.” “Usijali.” Jioni hiyo hiyo, Kikao cha Ukoo kilikaa na kujadili suala hilo. Kwa sababu Davina alikuwa na fedha za kutosha, siku iliyofuata asubuhi na mapema shughuli nzima ya mtambiko ilifanyika. Asubuhi na mapema, Davina alipelekwa mtoni na akina mama, akaogeshwa mwili mzima kwa maji ya kibuyu ambayo yalichanganywa na unga wa nafaka za uwele, mtama na mahindi ya njano! Baada ya zoezi hilo kumalizika, walikwenda kwenye mbuyu mrefu wa maajabu, ambao siku zote hutumika kwa ajili ya ibada za mizimu. Ng’ombe akachinjwa na Davina kupakwa damu mwili mzima kisha akavalishwa ngozi kwenye kidole chake cha mwisho na kiunoni! Wakarudi nyumbani ambapo sherehe ziliendelea huku ngoma za Kirangi zikipamba shughuli nzima. Watu walicheza, kula na kunywa kwa furaha hadi asubuhi! Mzee wa Ukoo akamhakikishia tatizo lake limefika mwisho. “Sasa unaweza kurudi mjini, kuendelea na shughuli zako, hakuna tatizo litakalokupata tena,” baba yake alimwambia Davina wakati wakimsindiza kwenda kupanda baiskeli ambayo ingemfikisha Kondoa Mjini ambapo angepanda basi la kwenda Dodoma na baadaye Dar es Salaam. “Sawa baba nashukuru sana, sasa nina amani.” “Mimi nawaacha, mama yako atakupa maagizo mengine!” “Sawa baba!” Mzee Ngamseni akaondoka zake, mama yake akaendelea kumsindikiza. Walipokaribia kufika kwenye kituo cha baiskeli, mama yake akamwambia: “Kuwa makini mwanangu, lakini kuna masharti mawili makubwa unayotakiwa kuyazingatia.” “Yapo hayo mama?” “Hutakiwi kuvua hiyo pete ya ngozi kidoleni mwako kwa miezi sita. Pili, huruhusiwi kukutana na mwanaume yeyote kimwili katika kipindi cha miezi mitatu. Baada ya muda huo kuisha, unaweza kukutana na mwanaume, lakini bila kuvua ile kamba ya ngozi kiunoni mwako, mpaka miezi mitatu tena baadaye! Baada ya muda huo kupita, utavua na kuvifunga kwenye kitambaa chekundu na kwenda kutupa mtoni! Kumbuka siyo baharini wala ziwani, lazima iwe mtoni...” mama yake akamwambia akiwa amemtulizia macho mwanaye. “Kifupi natakiwa kuvua pete baada ya miezi mitatu na kamba kiunoni baada ya miezi sita, pia sitakiwi kukutana na mwanaume mpaka miezi mitatu ipite. Ukimaanisha kwamba, wakati nakutana na mwanaume huyo lazima niwe na kamba yangu kiunoni siyo mama?” “Ndiyo!” “Unadhani itawezekana?” “Kwa nini isiwezekane? Nini kinashindikina? Tena unatakiwa kufahamu kwamba huu ni mkataba wetu na mizimu ambao unatakiwa kuheshimiwa na kulindwa kwa kila hali, tafadhali sana usitengue sharti hili, kwani kwa kufanya hivyo utasababisha matatizo makubwa sana, siyo kwako tu, bali kwa ukoo mzima,” mama yake alitamka maneno hayo kwa kumaanisha alichokisema. “HAIWEZEKANI MAMA, SITAWEZA...” “Unasemaje?” “SITAWEZA MAMA!” Neno ‘haiwezekani mama’ lilikataa kabisa kuingia kichwani mwa mama yake Davina. Kwa nini isiwezekane? Si ana matatizo? Anasumbuliwa na mzimu wa mpenzi wake ambaye alikufa muda mrefu uliopita? Tiba ndiyo ameshapatiwa na alitakiwa kuhakikisha anafuata masharti aliyopewa ili aweze kupona, sasa kwa nini anasema haiwezekani? Ni Davina huyu huyu ambaye alikuwa anatofautiana na baba yake kuhusu tatizo lake, baba yake akiwa haamini mambo ya mizimu na yeye akiamini kwa asilimia kubwa kwamba mzimu wa Jeff ndiyo ulikuwa unamsumbua. Leo anakataa vipi? Maswali haya yalizunguka kichwani mwa mwanamke huyu aliyekuwa akimtizama mwanaye kwa macho ya mshangao wa wazi kabisa. “Hivi naongea na Davina mwenyewe au na wewe ushakuwa mzimu?” mama yake akauliza kwa hasira. “Swali gani hilo mama? Mimi ni Davina...” Davina akasema kwa woga kidogo. “Haiwezekani Davina mwanangu ninayemjua mimi, aliyekuwa akija akilia akisema kwamba anatakiwa kufanyiwa mtambiko akatae kufuata taratibu za mila, hilo haliwezekani kabisa...” mama Davina akasema. “Mama.” “Mama nini? Mama kitu gani?” “Nisikilize kwanza!” “Kipi cha kukusikiliza, najua ni huo umapepe wako ndiyo unakusumbua, yaani huwezi kuvumilia kwa miezi mitatu baadaye ukaendelea na mambo yako. Yatakushinda mtoto wa kike,” mama Davina akazidi kuwa mbogo. Davina akaa kimya kwa muda, akamtizama mama yake kwa macho ya kuomba msamaha au kuhitaji huruma ya mama yake.
“Sikiliza mama!” “Nini?” “Unajua mama sina maana hiyo unayoifikiria wewe, hebu fikiria ni muda gani tangu Jeff amekufa? Kipindi chote hicho sijawahi kukutana na mwanaume, sina na wala sina matarajio ya kufanya hivyo, sasa kwa nini niwe na wasiwasi na jambo hilo?” “Sasa kumbe nini?” “Na wala sioni tabu kukaa na hiyo kamba kiunoni hata kwa mwaka mzima, bora huo mzimu usinisumbue!” “Sasa kumbe nini?” “Hii pete mama...nilifikiri ni ya muda mfupi, labda siku mbili au wiki...nitakaa vipi na hii pete wazi namna hii?” “Inakuzuia nini?” “Watu mama. Wengine wanaweza kuhisi mimi mchawi, mshirikina au mwanga!” “Acha ujinga mwanangu, mkataa asili si jasiri mama. Hizi ni mila zetu na wewe una matatizo, lazima uvae hiyo pete kwa miezi mitatu mwanangu!” “Lakini siwezi kutengenezea pete nyingine ya kawaida halafu nikaiweka ndani ya kidani?” “Haiwezekani mwanangu, lazima uivae ikiwa halisi, hivyo hivyo bila kubadilisha kitu chochote.” Davina alikaa kimya kwa muda. Hakuutaka mzimu wa Jeff hakika, lakini pia hakupenda kuonekana mchawi wala mwanga. Afanye nini sasa? Kipi bora? Aonekane mshirikina apone au aonekane si mshirikina mzimu wa Jeff uendeee kumsumbua? Alitakiwa kuwa na jibu. “Sawa mama, nitafuata maagizo yote,” Davina alisema akitabasamu. Mama yake akashangaa sana. Kwa bahati nzuri, baiskeli ikapita. Wakamsimamisha kijana aliyekuwa akiendesha. “Wapi dada?” “Kituoni.” “Mia tano tu!” “Usijali nitakupa elfu mbili, unachotakiwa kufanya ni kuniwahisha!” “Ahsante sana dada yangu, utafurahi mwenyewe.” “...mama kwaheri,” Davina akamwambia mama yake, baiskeli ikianza kuondoka taratibu. “Fika salama mama, nakutakia mafanikio mema mwanangu.” “Ahsante mama.” Baiskeli ikaondoka, tayari Davina alikuwa na kitu cha kufanya, hakuogopa tena ile pete, alijua ataifunika na kitambaa muda wote, hapo itakuwa si rahisi watu kugundua kilichokuwa kikiendelea. *** Ni wiki sasa imeshakatika tangu Gerald alipokutana na Nyamangumu Camp wanaoongozwa na Master katika kikao cha siri cha kujadili kuhusu tatizo la Jeff kuwasiliana naye kwa njia ya barua. Kuna kitu kilianza kuzunguka kichwani mwa Gerald akiamini kwamba, yawezekana kabisa kukawa na aina ya ‘changa la macho’ lililokuwa likiendelea chini kwa chini. Kwa bahati nzuri, Jeff hajamwandikia tena barua katika kipindi chote hicho, lakini kichwani ana mawazo mengi sana. Yupo kwenye foleni akitokea ofisini kwake Posta na alikuwa anaelekea maeneo ya Mbezi Beach. Sasa amesimama kwenye mataa ya Morocco ambako kulikuwa na foleni ndefu sana ya magari jioni hiyo. Mara simu yake ya mkononi inaita, haraka akapokea... “Haloo mambo vipi?” Gerald akazungumza kupitia kwenye simu. “Sina haja na salamu yako, nataka kukujulisha kuwa, hutaona barua yangu wala simu yangu tena, nimekuacha huru. Endelea na mambo yako, lakini nakuhakikishia hutamuoa Davina...hutamuoa nakuambia,” sauti ya upande wa pili yenye ukali huku ikiunguruma ilisikika ndani ya ngoma za masikio ya Gerald. “Nani?” “Jeff. Kwaheri rafiki mnafiki.” “Haloo, haloo...” Gerald akaendelea kuita kwenye simu. Haikumchukua muda mrefu sana kugundua kwamba alikuwa anazungumza kwenye simu iliyokatwa. Alipotizama namba ya mpigaji ili ampigie mwenyewe, hakuona. Ilikuwa private number! Jasho likaanza kumchuruzika mwili mzima, alishasahau kwamba yupo barabarani tena kwenye mataa...hilo hakulijua kabisa...honi ndizo zilizomshutua... Akaondoa gari kwa kasi. Mawazo tele kichwani! “Au huyu nyang’au hakufa nini?” Gerald anawaza akiondoa gari kwa kasi. Mwendo aliokuwa akiendesha gari lake ulikuwa wa kasi kuliko kawaida. Hakuchukua muda mrefu sana, alikuwa ameshafika nyumbani. Kichwa kilizidi kumuuma kwa mawazo, akiwaza jinsi ambavyo angemaliza tatizo lile. Kupigiwa simu na Jeff lilikuwa tukio jipya na la ajabu sana, mbaya zaidi halikuwa jambo ambalo anaweza kuomba ushauri kwa mtu yeyote, kwani lilikuwa siri kubwa iliyojificha moyoni mwake. Kitu pekee ambacho angeweza kufanya kwa wakati huo ilikuwa ni kukutana na Davina ili amwulize vizuri kuhusu ishu nzima ilivyokuwa! Mara moja akachukua simu yake na kuanza kutafuta jina la Davina haraka, alipolipata, akaampigia mara moja. Ni yeye peke yake kwa muda huo ndiyo angeweza kuwa msaada zaidi. “Haloo Davina, mambo vipi?” “Poa.” “Shwari?” “Haswaa, vipi mbona kama unahema sana, kuna tatizo?” “Nahema sana?” “Ndiyo!” “Hapana!” “Lakini mimi ndiyo nakusikia na nahisi kabisa kwamba kuna kitu kinakutatiza, ni nini?” “Ondoa hofu Davina, nipo sawa tu, ila nilikuwa nataka kujua kama umesharudi Dar au bado upo Kondoa.” “Kwa nini?” “Nataka kujua.” “Nimesharudi shemeji yangu, tangu jana nipo hapa mjini!” “Kweli?” “Ndiyo!” “Mbona hukunijulisha?” “Kuchanganyikiwa Gerald!” “Umeshasahau kwamba tulitakiwa kuonana baada ya wewe kurudi Kondoa?” “Nakumbuka sana!” “Sasa?” “Tupange tu...” “Enheee, unadhani lini inaweza kuwa siku yetu nzuri kuonana?” “We’ unapenda lini?” “Hata leo!” “Leo haiwezekani Gerald, bado nina uchovu mwingi, nahitaji muda wa kupumzika zaidi.” “Huwezi kujitahidi jamani?” “Hapana, huwezi kuamini lakini kwetu ni mbali sana na shughuli yenyewe iliyofanyika huko si ndogo, nipo hoi Gerald!” “Lakini ingekuwa vizuri zaidi kama tungeonana leo.” Ilikuwa lazima Gerald azungumze na Davina, alitaka sana kujua nini alichoambiwa na Jeff kwenye barua. Kwa muda wote huo alikuwa hajapata nafasi ya kuzungumza naye na kujua ukweli wa tatizo zima, kutokana na barua za Jeff mwenyewe. Tayari Gerald alikuwa kama aliyechanganyikiwa, maneno ya Jeff kwenye simu yalizidi kumfanya ajihisi mkosaji, hilo lisingekuwa tatizo kubwa sana maana lilikuwa lake na moyo wake, lakini lingeweza kuwa tatizo kubwa kama mtu mwingine yeyote angejua! Hakutaka kabisa kuhusishwa na mauaji ya Jeff. Kitu kingine ambacho alikuwa anakiota kila siku ilikuwa ni kuishi na Davina, alitakiwa kutumia mbinu zote amuoe. Kilichomchanganya ni kwamba, ile njia kubwa zaidi na ya mwisho ambayo aliitumia, ndiyo ambayo ilitaka kuharibika. Kutoa uhai wa mtu kwa sababu ya penzi halikuwa jambo dogo! Malipo ambayo yangeweza kutosha kulipia damu ya marehemu Jeff ilikuwa ni penzi la Davina pekee, hapakuwa na kitu kingine tena. Kikapita kimya cha muda mrefu kwenye simu bila mtu yeyote kuzungumza kitu. Baadaye sauti ya Davina ikasikika. “Gerald...” “Yes Davina!” “Naweza kukuuliza swali moja?” “Hata kumi nipo tayari!” “Ok! Lakini mi’ nina moja tu!” “Uliza.” “Mbona una haraka sana ya kuonana na mimi?” “Lakini ulisema Jeff anakusumbua na mimi ni rafiki yake...shemeji yako...ni vyema tuonane leo.” “Ni hilo tu?” “Lingine lipi sasa?” “Ok! Wapi?” “Rose Garden!” “Saa ngapi?” “Saa 3:00 usiku.” “Poa.” “Haya usikose tafadhali.” “Lakini kwa nini unakazania sana Gerald? Unanifanya niogope sasa.” “Nini kinakuogopesha? Nafikiri tukutane tuzungumze.” “Poa, saa 3:00.” “Haya shem,” Davina akajibu kwa upole sana, akionekana kuwa na mawazo tele juu ya kukutana kwao jioni hiyo. Hakujua Gerald alikuwa na nini hasa cha kukazania kiasi kile, maana kama ni matatizo yalikuwa yake, kwa nini yeye anakuwa ndiyo anakazania zaidi? Davina hakuwa na jibu, akabaki na mawazo tele kichwani. Namna ambavyo Davina alikuwa anauliza maswali ilimfanya Gerald aingiwe na wasiwasi tele moyoni mwake. Taa nyekundu ikaanza kuwaka ubongoni mwa Gerald, alishaanza kuhisi kuwa Davina alishagudua kila kitu. Alishajua kwamba yeye ndiye muuaji. Hii ilikuwa siri kubwa sana, siri ambayo hakutaka ijulikane, hasa na Davina. Ni kweli aliua! Ni kweli alitaka kumuoa Davina! Ni kweli Jeff alikuwa anamsumbua kwa kumwandikia barua na siku hiyo alimpigia simu jioni akitokea kazini. Kila kitu kilikuwa cha ukweli, lakini bado alitakiwa kufanya siri kubwa. Kwake yeye kukutana na Davina, kulikuwa mwanzo wa mwanga mpya katika utatuzi wa tatizo hilo. Hata hivyo, mwisho wa yote alipanga kumuoa Davina, hakuwa na kitu kingine zaidi. Hiyo ndiyo siri ya mauaji ya Jeff. Marehemu ambaye haeleweki. Marehemu anayeadika barua! Maajabu! *** Saa 2:30 usiku, Gerald alikuwa ameshafika Rose Garden, alikuwa akimsubiri Davina kwa hamu kubwa! Muda ukazidi kwenda, saa tatu na nusu akaamua kumpigia, akamjulisha kuwa yupo njiani anaelekea hapo. Akavuta subira, lakini hadi saa nne na robo, bado alikuwa hajafika. Akaamua kumpigia tena simu. Hakupatikana! Gerald akachanganyikiwa! Mawazo tele kichwani! Kama kungekuwa na neno lingine ambalo lingeweza kutumika kuonesha kwamba Gerald alikuwa amechanganyikiwa, hapa lingefaa hakika! Alikuwa amechanganyikiwa hadi kufikia kiwango cha mwisho na sasa alitakiwa kupata jina lingine jipya kabisa ambalo lingesherehesha maana ya yeye kuchanganyikiwa. Kuna wakati alianza kuhisi kwamba, labda mtandao ulikuwa unasumbua, hivyo akaamua kupiga kwa mara nyingine...jibu lilikuwa lile lile! Simu haikupatikana! Kichwa kikazidi kumuuma, alama za hatari zikaanza kusoma mbele yake, moja kwa moja alihisi kutokea tatizo kubwa sana mbele yake. Kwa nini amwambie yupo njiani halafu asipatikane? Kuna nini? Gerald aliwaza sana bila kupata jibu yakinifu! Maswali magumu! “Nini kinaendelea hapa? Kwa nini anaonekana kusita kuonana na mimi? Au tayari ameshajua kinachoendelea? Hapa natakiwa kuwa makini sana vinginevyo naweza kuingia kwenye matatizo makubwa ambayo yataniumiza baadaye...natakiwa kuwa na akili za kutosha katika hili. “Yapo mambo ambayo naweza kuyachukulia kwa wepesi lakini si hili...naona kabisa tatizo kubwa lililopo mbele yangu na kwa hakika sitaruhusu matatizo mbele yangu, lazima nifanye jambo fulani hapa,” ubongo wa Gerald ulipata kazi mpya ya kuhifadhi maneno hayo makali. Kuna kitu kilizunguka akilini mwake, kwamba yawezekana kabisa, Davina alivyokuwa kijijini kwako Kondoa, aliambiwa kila kitu na wazee baada ya kufanyiwa mtambiko na yawezekana kabisa kulikuwa na mpango wa kummaliza. Hilo lilichukua nafasi kubwa sana kichwani mwake. “Kipo kitu kipo...lakini mimi ndiyo Gerald bwana, najiamini siku zote. Isitoshe hata mara moja sijawahi kushindwa na hata hili haliwezi kunishinda,” Gerald akawaza akiinuka kwa ajili ya kuondoka. Akapiga hatua za haraka na kwenda kwenye gari lake, akiwa ndiyo kwanza anaingiza funguo kwa ajili ya kufungua mlango, akashtuliwa na mtu aliyemgusa begani. Akashtuka sana na kugeuka kwa shauku akiamini labda alikuwa ni Davina. Akageuka kwa hadhari! Hakuwa Davina! Alikuwa mhudumu! “We’ sister vipi? Hujui wengine tunakuwa na mawazo yetu kichwani...haya sema kwa nini umenigusa?” “Samahani kaka!” “Sema shida yako!” “Ulisahau kulipa,” yule dada akamwambia kwa sauti ya upole akimkabidhi karatasi iliyokuwa na bili yake. Gerald akapokea! “Samahani dada’ngu, nilipitiwa...samahani pia kwa kukufokea, kuna mtu ananichanganya sana akili yangu,” Gerald akasema akitoa pesa kwenye pochi yake na kumkabidhi yule dada. “Ahsante usijali.” Yule dada akaondoka, Gerald akafunga mlango na kuwasha gari, ile anaanza kuondoka tu, akaona gari la Davina likiingia getini. Akazima na kushuka. Akaenda kumpokea.
“Kumbe na wewe ndiyo unafika shem?” Davina akamwambia Gerald akitabasamu. “Siyo nafika, ndio nilikuwa naondoka zangu.” “Samahani kwa kuchelewa, lakini pia nilifanya jambo moja la kijinga sana, sikujua kama naondoka na simu isiyo na chaji, kwahiyo ikazimika ghalfa nikiwa Ilala kwa Salama, najua ulihisi nimekuzimia, lakini siyo...naomba msamaha shem,” Davina alisema akiwa ameganda kwenye mlango wa gari lake. “Umeshasamehewa, usijali Davina.” Pamoja na kwamba, Gerald alikuwa na mawazo mengi sana juu ya Davina, lakini alijishangaa akitumia muda mwingi kuutafakari uzuri wa Davina. Alivutiwa mno na mpangilio wa nguo zake jioni hiyo. “Umependeza sana Davina, hongera...” “Ahsante sana, hata wewe pia.” “Nashukuru.” Wakaingia ndani na kuketi sehemu tulivu sana. “Pole na safari, wazee wazima?” “Wa afya.” “Enhee, hebu niambie vizuri, ishu iko vipi?” “Ah! Shemeji yangu, ni maajabu sana na nakosa pa kuanzia, lakini kama nilivyokuambia awali, marehemu Jeff ananiandikia barua,” Davina alizungumza kwa sauti ya taratibu sana akiwa ameyatuliza macho yake usoni mwa Gerald. Gerald alikuwa kimya akiendelea kumsikiliza kwa makini sana, masikio yake yalikuwa tayari kumeza chochote kutoka kinywani mwa Davina. “Mbaya zaidi, sasa ameanza kunipigia simu, lakini cha ajabu sasa, anatumia private number!” Davina akazidi kusimulia. “Huwa anasemaje zaidi?” “Analalamika kuna mtu amemuua ili anioe!” Gerald akayatoa macho. “Amekutajia?” akauliza akionesha woga wa wazi kabisa. “Vipi mbona umeshtuka hivyo?” “Hapana, hizi ni habari za kutisha shemeji yangu, wewe mwenyewe unajua wazi kwamba Jeff alikufa na tulimzika, unadhani siwezi kushangazwa na habari kama hizi jamani?” “Nashindwa kuelewa kabisa, halafu anajua mambo yangu mengi sana, hata nikiwa nasafiri yeye anajua na hunipigia simu. Ni mambo yanayonichanganya sana,” Davina akasema kwa utulivu sana. Bado moyo wa Gerald haukuwa umetulia, hakutaka kumuamini Davina moja kwa moja, kichwani mwake alikuwa akiamini kuwa, Davina aliambiwa kila kitu na Jeff na alikuwa anamficha tu! Hakutaka kumweleza ukweli wa kinachoendelea, hakumwambia kama naye aliandikiwa barua pamoja na kupigiwa simu na Jeff, hiyo ilikuwa siri yake ya moyoni mwake. Alijitahidi sana kuuficha uoga wake kwa mafanikio makubwa. “Lakini shem, katika hali ya kawaida, umewahi kusikia mtu aliyekufa akafanya mawasiliano na aliye hai?” “Hapana.” “Sasa mbona unakuwa na imani haba? Kwa nini unaamini kuwa ni yeye?” “Hata kama ni wewe lazima ungeshtuka. Hivi unadhani ni rahisi kukubali kwamba marehemu anaweza kuandika barua? Apige na simu? Tena akitoa maneno ya ukali? “Anasema atakuja kunichukua anipeleke kuzimu nikaishi naye huko hilo linawezekana kweli? Fikiria Gerald...hili ni tatizo kubwa?” “Nini kimefanyika kijijini?” “Zaidi ya mtambiko ni nini tena?” “Baada ya huo mtambiko amewasiliana na wewe tena?” “Hapana...naona hali imetulia, wazee wamenihakikishia, ingawa wamenipa masharti ya kufuata.” “Duh! Pole sana Shem, lakini naamini haya mambo yataisha usijali...” Gerald akasema. Hakuthubutu kufungua mdomo wake kueleza kwamba na yeye alikuwa akitumiwa ujumbe pamoja na kupigiwa simu na Jeff, hiyo ilibaki kuwa siri ya moyo wake. Walizungumza mpaka saa sita za usiku, wakaondoka na kwenda majumbani mwao. *** Meza ya Meneja Mkuu wa Posta haikuwa na mafaili mengi asubuhi hiyo, aliyapekuapekua kisha akavuta moja na kulitupa juu. Akaanza kusoma kimya kimya huku akimtupia macho mteja wake aliyekuwa amekaa kimya mbele yake. Alikuwa ni Davina. Alikuwa mtulivu sana, huku macho yake akiwa ameyatuliza usoni mwa Meneja akisubiria kauli yoyote kutoka kwake. “Pole na safari dada Davina!” Meneja alisema akivua miwani yake na kuiweka mezani. “Nimeshapoa...natamani sana kujua kilichotokea! Vipi kuna barua yoyote imeingia?” “Ndiyo!” “Ngapi?” “Moja tu!” “Naweza kuiona?” Meneja hakujibu kitu zaidi ya kusimama na kwenda kufungua droo moja katika shelfu la ukutani kisha akatoa barua na kumkabidhi Davina. Kitu cha kwanza kuanza kusoma ilikuwa ni anwani ya mwandishi. Ilikuwa ni barua kutoka kwa Jeff. Macho ya Davina yakabadilika rangi, yakaanza kuwa mekundu kama nyanya mbivu! Sekunde chache baadaye, mvua ya machozi ikaanza kumwagika machoni mwake. Kazi ilikuwa ndiyo kwanza inaanza! Davina aliyatoa macho yake akiwa haamini kabisa anachosoma katika barua ile, ilikuwa barua yenye maneno mazito kuliko kawada! Kwanza alichanganyikiwa na jinsi barua yenyewe ilivyoingia, maana mwanzoni alikuwa akifikiria labda kuna mtu aliyekuwa akihusika na kupokea zile barua kisha kuziweka kwenye sanduku lake, lakini sasa ni tofauti kabisa! Barua zilikuwa zinapitia ofisini kwa Meneja Mkuu mwenyewe, sasa iweje mtu huyo aingie mpaka ofisini kwa bosi wake? Jambo hilo lilimchanganya sana kichwa chake. Akarudia kuisoma tena ile barua kwa mara ya tatu mfululizo. Alikuwa akisoma maneno yale yale! ‘Hii ni barua yangu ya mwisho kwako, najua upo Kondoa, ukirudi utaikuta! Sijui ni kwa nini unajisumbua kiasi hiki? Unadhani ukikataza barua zako kupitia kwenye sanduku lako nitashindwa kukutumia? Utaratibu ninaotumia ni ule ule wa kawaida, kwahiyo utaikuta barua yako ofisini kwa Meneja Mkuu. Nimeshazungumza na wewe mpaka nimechoka, napenda kukuambia kwamba, sitarudia tena maneno haya, kamwe sitajisumbua tena kukupa angalizo. Endelea na maisha yako, lakini fahamu kwamba nilikupenda sana, nakupenda na bado hujaondoka moyoni mwangu, utaendelea kuwa wangu siku zote. Kila unachokifanya, tambua kwamba nakupenda sana, fahamu yupo ambaye moyo wake unatetemeka kwa ajili yako, yupo anayejua thamani ya pendo lako. Yupo ambaye alia kwa ajili ya penzi lako. Huyo ni mimi, mwanaume ambaye niliukabidhi moyo wangu kwako. Jeff Sebastian.
Kilio cha Davina kilikuwa na sababu mbili, hakulia kwa sababu ya maajabu ya barua yenyewe tu, sasa machozi yake yalisababishwa na ukali wa maneno yaliyokuwemo kwenye barua ile, yalikuwa maneno makali yanayochoma kuliko kawaida. Hata yeye alikiri wazi kwamba alikuwa anampenda sana Jeff, tena kwa moyo wake wote, lakini hakuwa na haja ya kuumia sana kwa sababu tayari alikuwa marehemu! Alishalia mpaka machozi yakakauka, hakuwa na haja ya kujiongezea simanzi ya moyo wake sana, alichotakiwa kufanya kwa wakati huo ni kutulia na kukubaliana na hali halisi ilivyokuwa. Kwamba Jeff mwanaume wa maisha yake, hakuwepo tena duniani! Akayatoa macho yake akimuelekezea Meneja Mkuu. “Vipi dada’ngu?” “Acha tu!” “Kuna nini?” “Niache tafadhali!” “Lakini ni vizuri kama utanijulisha chochote ili nijue jinsi ya kusaidiana na wewe.” “Niachie mimi...acha tu...ahsante sana...” Davina alitamka maneno hayo huku akiinuka kitini. “Sasa barua ziendelee kupitia kwenye sanduku lako la kawaida?” “Vyovyote mtakavyoona!” Davina alijibu kwa hasira huku akibamiza kwa nguvu mlango wa ofisi ya Meneja Mkuu. *** “Nimekuta tena barua ya Jeff!” “Umekuta?” “Ndiyo!” “Inasemaje?” “Kama alivyoniambia kwenye simu, anasema hatanifuatilia tena.” “Mh! Hii hatari sasa!” “Mbaya zaidi, barua zenyewe sasa hivi zinapitia ofisini kwa Meneja Mkuu, yaani nimechanganyikiwa si kidogo, akili yangu haifanyi kazi kabisa, najihisi kama nikitue hivi, maana naona kimezidi uzito!” “Usiseme hivyo shem, haya mambo yataisha tu!” “Yataisha vipi wakati ndiyo kwanza yanaanza?” “Lakini hakuna lenye mwanzo linalokosa mwisho.” “Ila hili langu, naona kama halina mwisho.” “Upo wapi?” “Mjini, natokea Posta.” “Jioni naweza kukutana na wewe?” “Tena?” “Kwani kuna ubaya?” “Hapana, lakini unanitisha, nahisi kama una kitu kipya!” “Sina kitu kipya kwa kweli, lakini nafikiri huu ni wakati wa kuwa karibu zaidi na wewe shemeji yangu!” “Ok! Kama umeona hivyo sawa.” Haya yalikuwa mazungumzo kati ya Davina na Gerald, muda mfupi baada ya Davina kutoka ofisini kwa Meneja Mkuu wa Posta. “Wapi sasa?” “Maeneo ya Sinza!” “Ipi?” “Tukutane Mori, muda ukifika nitakujulisha!” “Sawa, utanijulisha, lakini natakiwa kujua ni muda gani?” “Kuanzia saa tatu....” “Mh! Unaposema kuanzia saa tatu, maana yake ni hadi usiku sana, au nimeelewa vibaya?” “Umeelewa vibaya, siyo usiku sana, ni mazungumzo ya saa moja tu, nataka tupate chakula cha usiku pamoja!” “Sawa shemeji yangu!” “Ok!” *** Tofauti na matarajio yake, saa 3:00 Davina alikuwa ameshafika Sinza, Mori kituoni na alikuwa akimsubiria Gerald, alipoona kimya cha muda mrefu baada ya kusubiri robo saa nzima, akaamua kumpigia. “Uko wapi?” Davina akauliza. “Kwani we’ uko wapi?” “Nimeshafika.” “Oh! Samahani sana, mimi ndiyo nakatisha hapa kwenye mataa ya Bamaga, dakika tatu tu nitakuwa hapo.” “Poa.” Kweli baada ya muda huo, Gerald alikuwa ameshafika Mori, akampigia Davina na kumwambia amfuate kwa nyuma, wakaongozana hadi Kwa-Remmy, Gerald akaegesha kushoto, Davina naye akafanya hivyo, wakaingia ndani ya Mgahawa wa City Garden. Muda mfupi baada ya kukaa kwenye viti, mhudumu akafika na kuwasikiliza. Vyakula vikaletwa, wakaanza kula huku wakizungumza mambo mbalimbali ya kimaisha. Hawakukaa sana, wakaagana. Mazoea ya Gerald wa Davina yakazidi, kila wakati alipenda kumpa ofa, alimtumia meseji mbalimbali zenye tungo nzuri, akimsogeza zaidi karibu yake. Baada ya miezi mitatu wakawa marafiki wakubwa. Sasa walikuwa zaidi ya mtu na shemeji yake, walifanya kila kitu isipokuwa ngono, mpaka wao ulikuwa ni ngono tu! Waliamua kuwa marafiki wa kawaida, huku Gerald akisisitiza kwamba analazimika kufanya hivyo kwa sababu hana mchumba na pia kwa ajili ya kumuondolea upweke moyoni mwake baada ya kuondokewa na rafiki yake mpenzi, Jeff. Davina alilipokea hilo kwa mikono miwili. Kila wikiendi wakawa wanakwenda disko au kwenye maonesho ya bendi mbalimbali, wakati mwingine walikwenda ufukweni na kuogelea pamoja! Mzigo mzito ukazidi kumuelemea Gerald moyoni mwake, wikiendi moja wakiwa ufukweni akaamua kuutua! Hakuona sababu ya kuendelea kuumia wakati mtu wa kumweleza hisia zake alikuwa naye. Akapanga maneno ya kumwambia yakapangika. “Davina, naomba unisikilize, nina mambo ya muhimu sana nataka kuzungumza na wewe leo...” Gerald akamwambia Davina huku akimpapasa tumbo lake, ufukweni mwa Bahari ya Hindi eneo la Coco. “Nakusikiliza Gerald, niambie tu!” “Hivi umeshawahi kuona mtu mzima akilia?” “Ndiyo kwenye msiba!” “Bila msiba, hujamuona mtu mzima akilia?” “Kwa kweli sijaona!” “Utajisikiaje kama utamuona mtu mzima akilia kwa sababu yako?” “Nitajisikia vibaya sana....kwanza sitamani kumliza mtu mzima hata siku moja!” “Lakini yupo ambaye analia kwa ajili yako!” “Nani?” Davina akauliza akiyatoa macho yake. “Mimi Davina...nimekuwa nikilia kwa muda mrefu sana kwa ajili yako, naomba sasa uyafute machozi yangu! Nibembeleze sasa Davina...sikiliza Davina, nakupenda sana, nahitaji uwe mpenzi wangu, mke wangu wa baadaye, mama wa watoto wangu!” Gerald alikuwa akizungumza kwa sauti ya kusihi sana huku macho yake yakidondosha machozi. Davina alikuwa ameyatoa macho yake kwa mshangao, hakuamini kama maneno yale yalikuwa yanatoka kinywani mwa Gerald. Ghafla akajiondoa mikononi mwake na kumsukuma Gerald pembeni... “Noooooooo Gerald, noooooooo....” Davina akapiga kelele huku akikimbia. Gerald akasimama na kumkimbiza! Davina alikuwa kama aliyechanganyikiwa, kwa Gerald ilikuwa ni pigo na hakuwa tayari kumpoteza Davina. Akaanza kumkimbiza kwa kasi ufukweni, watu waliowaona walibaki wanacheka. Hakufika mbali sana, Gerald alikuwa ameshamshika, akamwangusha chini na kumlalia! Akambana kwenye mchanga asifurukute. “Davina kwa nini unafanya hivi?” “Nimefanya nini?” “Huoni ulichofanya? Unadhani watu watatufikiriaje?” “Sikutegemea kama ungeniambia maneno hayo, hivi kumbe ukaribu wetu maana yake ilikuwa ndiyo hiyo?” “Siyo hivyo Davina, lakini unatakiwa kukumbuka kwamba mapenzi ni hisia na si mimi mwenye matakwa ya kukupenda bali hisia kali zilizopo katikati ya moyo wangu. Tafadhali zipokee mpenzi wangu, nakupenda sana Davina.” “Kwahiyo ulifurahia kifo cha Jeff siyo?” “Hapana.” “Sasa kwa nini unanitaka?” “Ndiyo maana nimekuambia mapenzi!” “Sasa unawezaje kutembea na mpenzi wa rafiki yako?” “Nisingeweza kufanya hivyo akiwa hai, lakini amekufa, tena nahisi nitakuwa namuenzi vizuri rafiki yangu Jeff!” “Hayo ni mawazo potofu!” “Si potofu, nakupenda kweli Davina tafadhali naomba uruhusu moyo wangu uingie kwako, usiniache niteseke...” Gerald alizidi kumshawishi Davina ambaye hakuwa na dalili hata moja ya kukubali ombi lake. “Ok! Nipe muda kwanza,” Davina akajibu kwa kifupi baada ya kuona Gerald anazidi kumsumbua. Alifanya hivyo kwa nia ya kujinasua kwake kwa muda ule. Gerald akakubaliana na Davina, akamwachia! Hawakuchukua muda mrefu sana wakaamua kuondoka. Siku hiyo Davina hakutumia gari lake, hivyo Gerald alilazimika kumpeleka kwanza Davina nyumbani kwake kisha naye akarudi nyumbani kwake. Kichwani mwake alikuwa na wazo moja tu, alitakiwa kumpata Davina. ***
Kitanda hakikuwa na raha kwa Gerald, akili yake ilikuwa kwa mrembo Davina, alitakiwa kutumia akili yake yote kuhakikisha anamweka mikononi mwake, kosa ambalo hakutakiwa kulifanya ni kuhakikisha kwamba Davina hafahamu na wala asihisi kama Gerald alikuwa anahusika na kifo cha Jeff kwa namna yoyote ile. Picha nzima ya Davina ilimtokea akiwa pale kitandani. Akahisi moyo wake ukienda kasi kuliko kawaida. Usingizi ukamruka kabisa, kitu pekee ambacho kingeweza kumsaidia akapata usingizi ilikuwa ni kusikia sauti ya Davina. Haraka akachukua simu yake na kubonyeza namba za Davina. Punde, simu ikaanza kuita na kitambo kidogo Davina akapokea... “Vipi mama?” “Shwari, mbona usiku sana?” “Nimeshindwa kulala kabisa!” “Kwa nini?” “Baby, picha yako inanisumbua kichwani mwangu!” “Unaanisha nini kusema hivyo?” “Nakupenda sana mpenzi, tafadhali nipe nafasi katika moyo wako!” “Tena umenikumbusha, mchana nilikuahidi kwamba nitakujibu baada ya kufikiria, haikuwa hivyo!” “Khaaa! Kwahiyo ulikuwa na maana gani?” “Sitaki kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wewe, kama unaona huwezi kuwa rafiki yangu wa kawaida basi!” Davina alisema maneno hayo kwa hasira kisha akazima simu. Gerald akabaki ameduwaa.
MIEZI MITANO BAADAYE Ni muda ambao tayari Davina alishavua ile kamba kiunoni na pete ya ngozi kidoleni mwake. Usumbufu wa Gerald ukiendelea kwa kasi, lakini Davina aliendelea kuwa na msimamo siku zote. Pamoja na msimamo wa Davina, bado Gerald aliendelea kumsumbua. Alipoona hana dalili za kumkubali, akaamua kubadilisha gia! Sasa akamwambia tayari ameshafuta hisia zake mbaya na hakuwa na nia ya kuwa naye tena. Davina alishangaa sana! “Kweli Gerald?” “Kweli kabisa, tena nitakuheshimu kama rafiki yangu!” “Nimefurahi sana kusikia hivyo Gerald, lakini naomba yawe ya kweli!” “Kwa nini nikudanganye? Huo ndiyo ukweli wenyewe!” “Kama ni hivyo sawa!” Uhusiano wao ukazidi kupamba moto, lakini wakati huo walikuwa kama marafiki na siyo wapenzi na wala Gerald hakumsumbua tena. Hiyo ndiyo hali halisi ilivyoonekana kwa nje, lakini ndani ya moyo wa Gerald bado kulikuwa na makovu makali sana ya mapenzi juu yake. Wakawa wanatoka kama ilivyokuwa zamani, kila mwisho wa wiki wakawa wanapunga upepo ufukweni pamoja. Baada ya miezi miwili, tayari Davina alikuwa ameshaamini kwamba Gerald hawezi kumtongoza tena. Wikiendi moja, Gerald aliamua kwenda na Davina Morogoro, wakaponda raha kuanzia Ijumaa jioni hadi Jumapili jioni walipoamua kurudi Dar. Kila kitu walifanya pamoja kama marafiki, lakini hapakuwa na suala la mapenzi, hata chumba kila mtu alikuwa na chake! Wakiwa njiani wanarudi, mbele kidogo ya Chalinze, Gerald alikuwa anakimbiza gari kuliko kawaida, mara nyingi Davina alikuwa anamzuia kukimbiza gari, lakini hakuelewa. Kwa mbali kidogo kulikuwa na gari kubwa la mizigo lililokuwa linakimbia kwa kasi kuliko kawaida. Gerald naye akazidi kukimbiza gari. “Lakini kwa nini leo unaendesha gari kwa fujo hivi?” “Nina maana yangu!” “Maana gani?” “Nataka tufe!” “Tufe? Hivi una kichaa Gerald?” “Bora nife na kichaa changu, kuliko kuendelea kuishi nikiwa mzima huku penzi langu likiwa halithamiwi!” “Una maana gani?” “Wewe si hunipendi? Sasa wote tunakufa, kwa taarifa yako, nalipeleka gari usawa wa lile lori linalokuja, bora tufe pamoja kuliko kuendelea kunitesa!” “Usifanye hivyo Gerald!” “Kwahiyo unanipenda?” “Unasema...” “Jibu haraka, napeleka gari!” Gari lilikuwa katika mwendo mkali sana na Gerald alikuwa akimaanisha kabisa alichokisema, ghafla Gerald akahama njia, akapeleka gari upande wa kulia kwa nia ya kugongana na lile gari, taa za gari lake zikiwa zimewashwa mwanga mkali! “Gerald achaaaaaaaa.....” “Bora tufe...” Gerald alisema huku akikanyaga mafuta sawasawa. Wakati huo lile lori nalo likaanza kuyumba na kupoteza mwelekeo. Davina akazidi kupiga kelele kwa hofu ya kifo kilichokuwa mbele yake! Dereva wa lori akaanza kuyumba akishindwa kuelewa nia ya dereva aliyehamia upande wake akiendesha kwa kasi ile. Taratibu akaanza kupuguza mwendo, lakini Gerald aliendelea kukanyaga mafuta. Alipojaribu kurudi upande wa Gerald akaona gari kubwa likija upande wake! Akili yake ikafanya kazi haraka sana, asingeweza kugongana uso kwa uso na gari kubwa kiasi kile, lakini pia hakuwa tayari kuingiza gari mtaroni, akaona bora avaane na gari ndogo ambalo kwanza asingeumia sana, lakini pia asingekuwa na kosa! Akawa tayari kuvaana! Hatua kama nne tu kabla ya magari kukutana uso kwa uso, Davina akashika usukanu na kukata kushoto akitetemeka, kisha akaliweka gari sawa. Gerald akachukia sana! “Unataka kufanya nini?” “Unanipenda hunipendi?” “Acha ujinga Gerald, bado nauhitaji sana uhai wangu, tafadhali acha kufanya hivyo!” “Achia usukanu!” “Na wewe endesha gari vizuri!” “Sema kwanza kama unanipenda!” “Sikiliza Gerald, kwa sasa tupo kwenye matatizo, yule jamaa anaweza akageuza na kutufuata kwahiyo kimbiza gari, tuepukane na hili tatizo kwanza...” Davina akamwambia Gerald ambaye alitii. Gari likaondolewa kwa kasi ya ajabu, Gerald alipoanglia kupitia vioo vya pembeni, akaona lile lori limeegeshwa pembeni, akahisi kwa vyovyote vile, inawezekana akawa anamfukuza na gari lingine. Akaamua kukanyaga mafuta zaidi. Kasi aliyokuwa nayo ni kama alikuwa ameiba gari, mara kadhaa alikosakosa ajali barabarani, lakini alifanikiwa kufika hadi Kimara salama, hapo akagundua kitu fulani, barabara kubwa ilikuwa hatari sana kwake, hivyo akakata kulia na kuingia kwenye barabara ya vumbi iliyoelekea Bonyokwa! Alikuwa mtalaamu sana wa njia za panya, kwahiyo aliweza kupenyeza hadi akatokea Makoka na baadaye Tabata kisha akapita Buguruni akanyoosha moja kwa moja kama anakwenda Kariakoo, alipofika Boma, karibu na Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye mataa akakata kushoto kuifuata Barabara ya Kawawa. Hapo kidogo roho yake ikawa imetulia, mpaka muda huo hakuna hata mmoja kati yao, aliyemzungumzisha mwenzake, wote walikuwa kimya. Dakika chache baadaye, Gerald alikuwa anaegesha gari nje ya Hoteli ya Mamba, Kinondoni, Studio. “Shuka,” akamuamuru Davina. “Tunaenda wapi?” “Nimesema shuka!” “Mh! Haya, isiwe tabu...” Davina akasema akishuka kwa unyonge. Gerald akamwonyesha ishara kwamba amfuate nyuma, Davina akafanya hivyo. Wakaingia ndani na kuketi kwenye meza moja iliyokuwa kwenye kona. Hakuna aliyeongea! Wakabaki wanaangaliana. Mhudumu akawafikia, kila mmoja akaagiza anachokitaka. Macho ya Gerald yalionesha wazi jinsi alivyokuwa amedhamiria kufa kama angemkosa Davina. Mara moja Davina akagundua jambo fulani, alijua kwa vyovyote vile, kama angekataa kuwa naye, kungetokea tatizo kubwa, hasa kifo! Yeye aue? Hapana...hakuwa tayari kabisa kwa hilo. Davina akawa wa kwanza kuzungumza. “Gerald kwanini ulitaka kuniua?” “Nilitaka kukua au wewe ndiyo unataka kuniua?” “Kukua? Kivipi?” “Hivi unashindwa kujua thamani ya maisha yangu kweli? Huoni umuhimu wa mimi kukupenda siyo? Kwanini unanitesa kiasi hiki, kwanini? Ni kitu gani sina ili niwe nacho unipende?” “Siwezi Gerald, sitaweza!” “Huwezi kunipenda siyo, basi sioni kama kuna haja ya kuendelea kuishi, lazima nife, tena usiku wa leo,” Gerald hakuwa na masihara kabisa katika hilo. Alama ya machozi machoni mwake, ilitosha kabisa kuonesha kilichokuwa moyoni mwake, Davina akatulia kwa muda, akamwangalia Gerald kwa huruma, kisha akamwambia... “Basi mpenzi, huna haja ya kufa...acha nikupe moyo wangu, lakini nahitaji penzi la kweli na siyo la kitapeli.” “Unasema kweli?” Gerald akapiga kelele. “Kweli kabisa, acha nikupe maisha yangu!” “Ahsante mpenzi wangu!” Hadithi zilizofuata baada ya hapo zilikuwa juu ya ndoto ya maisha yao yajayo, kila mmoja akiwa na shauku ya kuwa na familia bora, maisha mazuri na kila kilicho bora. Gerald ndiyo alionekana kuwa na furaha zaidi ya mwenzake, aliwaza ndoa tu! “Tena inabidi tufunge ndoa mapema sana.” “Haraka ya nini mpenzi wangu?” “Sasa kumbe tunasubiri nini?” “Sawa!” Baadaye, Gerald akamrudisha Davina nyumbani kwake, mvua ya mabusu akammiminia, wakaagana kwa ahadi ya kukutana tena kesho yake. “Nakupenda sana Davina, sasa moyo wangu utatulia.” “Karibu moyoni mwangu, uwe mwenyeji wa kudumu sasa.” “Nimefurahi sana, ahsante.” Gerald akaondoka zake. ***
0 Comments