Simulizi : Upendo Kutoka Sayari Nyingine Sehemu Ya Tano (5)
13 Mpelelezi mtalii.
Sebastiani Akiwa ofisini kwake alitupia macho yake dirishani huko akakutana na sura aliyoifahamu sana ya mtu ambaye alikuwa akiongozana na walinzi pamoja na Meneja wa Psychological Mental Hospital. Hakuyaamini macho yake mpaka alipoyafikicha na kutazama tena kwa utulivu. Safari hii alihakikisha kuwa aliyemwona ndiye hasa. Alikuwa ni Andrew Charles. Moyoni alicheka kwa utundu wa mwandishi huyu wa habari kujifanya mtalii huku akitembezwa na walinzi katika maeneo yale. Ni yeye Seba pekee aliyejua sababu ya ujio wa mwandishi huyu wa habari. Alijua ni kwa namna gani waandishi wa habari wa Tanzania wanavyohaha kutafuta mahali yeye na Judith walipo. Mpaka hapo wengi walishakwama kupata mbinu ya ziada ya namna ya kumpata. Andrew anajulikana vizuri kwa kutokukata tamaa katika harakati zake, maswala magumu kwake ndio hupenda kucheza nayo zaidi. Furaha yake inakamilika ikiwa atapambana na mikikimikiki katika kazi yake na kufaulu kuishinda na kupata kile alichukusudia kupata. Ujasiri na kupenda kucheza na vitendawili vigumu katika maisha ni hali inayopendwa sana na timu ya waandishi wa shirika la UWARIDI. Watu hawa wamehusika mara nyingi kuibua siri nzito zilizofichwa hata kwa viapo. Sebastiani aliwaangalia meneja yule na kundi lake wakiwa wanampeleka Andrew katika maeneo ya kutalii ndani ya Hospitali ile pamoja na chuo kisha akaendelea na shughuli zake. Alishajua kuwa tayari amepatikana katika maficho yake naye hakuwa na budi kujitokeza ili akutane na mpelelezi huyo ili wapange mambo ambayo yatakuwa faida kwa jamii ya Watanzania pindi tu watakapopewa habari kuhusu yeye na Mchumba wake. Aliendelea kufanya kazi ya masomo yake kwa utulivu huku akijipanga namna atakavyokamilisha mipango yake katika nchi ile ili arudi nyumbani Tanzania kwa ajili ya kujenga Taifa lake akiwa na wazo jipya kabisa. *** Mazingira ya maeneo haya yaliacha picha zote zikielea kichwani mwake na kila wakati alikuwa ndani ya eneo moja baada ya jingine alilotembelea mchana huo. Akiwa chumbani kwake jioni hiyo alikuwa akifurahia kiyoyozi huku akipanga matukio na picha alizozichukuwa mchana huo. Kamera yake ilinasa kila alichokihitaji kwa picha za mnato na kamera yake ya video. Alipokuwa katika harakati za kupanga kila picha ndani ya loptop yake alishtuliwa na alamu ya mlangoni. Hakutarajia kupata mgeni kwa wakati huo muhimu kwake. Hakujua ninani aliyekuwa mlangoni wakati alijua utaratibu wa kuja mgeni chumbani kwake ni lazima apigiwe simu kusudi awe tayari kumpokea kabla hajaja. Wazo la kuamka na kuuendea mlango alilipata wakati alam ilipolia kwa mara ya pili, aliuendea mlango kwa hatua za kivivu akiwa amekereka kutokana na kukatishwa katika kazi yake ya kupanga matukio muhimu. Alipoufikia mlango aligusa kitufe kando ya mlango na mlango ukafunguka. Mshangao wake uliochanganyika na furaha ulimfanya agande mahali alipokuwa amesimama akiwa kausahau mdomo wake wazi. Mbele yake alisimama Sebastiani Changawe akiwa na tabasamu la kukata na shoka. “Habari yako mtalii? Alisema Seba na kunyoosha mkono ili wasalimiane. Ohooo Seba! Mambo vipi ndugu yangu? Alisema Andrew wakati wakisalimiana kwa kukumbatiana. Nilitegemea ujio wako japo ulichelewa sana kunipata mahali nilipopotelea katika hili kombolela!” Sebastian alisema maneno hayo huku wakiachiana na kuelekea kwenye viti. “Mpaka hapa Seba jasho la meno limenitoka, japo kati ya wote mimi ndio nimefaulu kwa asilimia zote kukugundua mahali ulipo kwa hiyo katika kombolela hili mimi ndio mshindi!” Alisema Andrew kwa furaha kubwa. Sebastian alijipweteka kwenye Sofa dogo lililoko mkabala na meza kubwa ambayo ilipambwa na loptop pamoja na kamera za Andrew. “Nakupa ushindi asilimia zote japo umechelewa kugundua mahali nilipo kwa zaidi ya mwaka.” Alisema Seba baada ya kuketi sofani. “Nimefurahi sana kukuona Seba japo nilitegemea kukutana na wewe ndani ya siku hizi chache, lakini kwangu imekuwa mshitukizo kwa wewe kuniibukia kabla sijaendelea kusumbuka namna ya kukupata.” Alisema Andrew huku akikaa kitini akiikabili meza yenye vifaa vyake vya kazi, tayari kwa kunasa mazungumzo yote yatakayofanyika mahali pale, sambamba na kuchukuwa picha bila hata Seba kuwa na habari. “Kwakweli sikutaka usumbuke zaidi ya hapo nikaona ni vema nije ili tufanye mazungumzo muhimu usiku huu.” Alisema Sebastian wakati akijiweka sawa kitini, kisha akaendelea. “Habari za nyumbani ninazipata kwa ufinyu kidogo kwa sababu taarifa za habari hazielezi kila kitu. Na mitandao ya kijamii ikiwepo facebook twiter na WatsApp pia hainipi mengi kama ambavyo ningekuwepo mwenyewe huko.” Alisema Seba. “Nafikiri hamu yako ya kutaka kujua habari za nchi yako haizidi ya Watanzania walio wengi kutamani kujua habari zako wewe na Mchumba wako Judith Martin. Kilichonipa msukumo mkubwa wa kufika hapa ni shauku ya watu na maswali yao yasiyojibika.” Alisema Andrew wakati akinyanyuka na kuelekea mahali lilipo Jokofu na kufungua ili achukue vinywaji. “Nikuletee kinywaji gani maana ni vizuri wakati tukiendelea na mazungumzo tuwe tunapata vinywaji.” Aliuliza Andrew. “Niletee Redbull.” Alijibu Seba huku akiminya minya simu yake. Andrew alirudi mahali pake baada ya kuweka kopo la Redbull kwenye meza ya Seba. “Andrew ujio wangu huu una mambo zaidi ya kujuliana hali na kuulizana habari za nyumbani Tanzania. Ninajua kabisa kuwa umekuja Nairobi ili kupata habari za maendeleo yetu hasa mchumba wangu Judith Martin. Ninajua kiu waliyonayo Watanzania ya kujua maendeleo yetu na ninini tunafanya mbali na wao kutokujua kuwa tuko nchi gani. Najua pia habari kuhusu mahali tulipo na maendeleo yetu vitaleta mlipuko wa furaha kwa watu wanaotupenda na chuki kwa baadhi ya watu wasiotutakia mema. Lakini kwangu binafsi nimekuwa na mapendekezo muhimu sana kwa ajili yetu na kwa habari zozote kuhusu sisi. Kwa sasa ninaomba usiweke neno lolote kwenye makaratasi kuhusu habari zangu na Judith. Ni furaha yangu kukujulisha kuwa Judith kwa sasa ni mzima kabisa na yuko kwenye kozi ya kujifunza udaktari na mimi ninaingia kipindi cha mwisho cha mafuzo ya juu ya udaktari kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa akili. Huu ni uchaguzi wetu mpya baada ya kusumbuka kwa muda mrefu nikitafuta tiba kwa ajili ya mpenzi wangu Judith Martin. Sababu ya kutaka habari za kuonekana mahali nilipo na maendeleo ya afya ya Judith nimeona kuwa sio muhimu sana kuliko kile tunachotaka kufanya kwa ajili ya jamii ya watanzania. Pia isingekuwa vizuri kuwapakulia watu habari ambazo bado hazijaiva vizuri. Sitaki katika hili kuongelea ahadi tu bali nahitaji kufanya jambo kwa vitendo hasa.”Alisema Sebastian Kisha akatulia kidogo akaiinua Redbull yake na kuanza kuifungua. “Ninafurahi kusikia kuwa Judith amepona na yuko kwenye kozi ya udaktari. Hizi ni habari njema sana Seba, kuna madhara gani ya kuandika mambo haya kwa sasa ili watu wajue ulipo na yale yaliyofanyika kwenu kama ushuhuda?”Aliuliza Andrew kwa shauku. “Usiwe na haraka muda sio mrefu Utajua kila kitu kwa mtiririko ili uandike mambo kwa ukamilifu sio mambo nusunusu. Kama utatoa habari kwa sasa juu ya kuwepo kwangu Kenya pamoja na kupona kwa Judith, bado kuna maswali ambayo watanzania watabaki nayo.” Alisema Seba kisha akapiga funda moja la kinywaji chake. Baadaye akaendelea. Natagemea kuwa shirika la habari la UWARIDI litatoa mambo kamili juu yetu na mengine mengi tuliyo nayo kwa ajili ya nchi yetu. Na hili ndio lengo kwa faida ya watanzania walio wengi Sawa mtalii?” Alisema na kuingiza utani huku akitabasamu. “Sawa Seba nadhani mpaka hapa najaribu kukuelewa kuwa unataka kuwafanyia mshtukizo Watanzania kwa kile ulichoazimia kukifanya wakati wa mahafali yako. Kwangu mimi niliyekuja na kukutana na wewe uso kwa uso siwezi kujua japo kwa kidokezo kile ambacho unataka kukifanya?” Alisema Andrew kwa hali ya kuvunjika moyo baada ya kuambiwa kuwa asingeruhusiwa kuandika lolote hata baada ya kumwona Seba na mahali alipokuwa amejificha
Kwa mwandishi yeyote hiyo ni nafasi ya dhahabu na angeandika habari zake na kuziweka kwenye vyombo vya habari Ingempatia sifa kubwa yeye na gazeti analoliandikia.“Nitakuambia kwa kidokezo tu rafiki yangu na kwako itakuwa ni sifa kubwa kuandika mambo hayo yakiwa katika viwango vya kuiletea Tanzania sifa. Kwa sasa nitakukutanisha na judithi na kukueleza mpango mzima niliouandaa kwa ajili ya siku hiyo muhimu.” Alisema kisha akapiga funda jingine la Redbull. ** * Mazungumzo yalikuwa matamu sana na mipango ilipangwa kitaalamu na kwa utaratibu mzuri sana. Maswali yote yaliyoko kichwani mwa mwandishi huyu wa habari yaliisha na moja kwa moja aliingia katika mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa kile walichopanga kinatimia bila mwandishi wa habari yoyote kubumburua habari hizi.Ndani ya siku hii alikumbuka kumwandikia Chief na kumtaarifu kuwa mambo yote yako sawa ila tu aweke tahadhari juu ya mashushushu wa UWARIDI kuweza kuandika kitu chochote ikiwa tu wangeweza kunusa na kugundua mahali Seba na mpenzi wake walipo. Jibu la kwamba Chief ameelewa liliibua furaha na siku hiyo ilikuwa ni sherehe kati ya Sebastian na Andrew pamoja na Judith Martin aliyeonekana kuwa mzima kabisa na mwenye sura ya kuvutia. Mara zote Judith alionekana mwenye Tabasamu akiwa mchangamfuna mwenye maneno ya busara sana. Mawazo mengi alikuwa akiyatoa yeye kuhusiana na mipango waliyokusudia kuifanya baada ya kukamilisha masomo yao. Hii ilivutia sana kwa Andrew kuona mtu aliyekuwa kichaa kabisa leo akiwa ni mwenye akili na busara za hali ya juu. Siku ile walikuwa wakiagana na kwamba kila mara watakuwa wanawasiliana kwa mipango kamili mbele yao. Jioni hiyo Andrew alipitia nyumbani kwa Mkurugenzi wa Phsychological mental Hosptal Dr. Matlda na kuagana kuwa kesho asubuhi angerudi nyumbani Tanzania. “Najisikia kuwa mtalii mwenye bahati kubwa kutalii katika maeneo haya yenye historia ya ajabu sana.Hili ni eneo la fahari sana na lenye kusaidia watu na shida zao. Nimejifunza mengi ya kuvutia katika ziara yangu hii na ninakuahidi kuwa nitatangaza uzuri wa mahali hapa na huduma zinazopatikana katika Hospital hii maarufu.” Alisema Andrew wakati akiagana na Dr. Matlda. “Karibu sana andrew unapojisikia tena kututembelea na hata unapoona kuwa kuna haja ya kutuletea wanafunzi wa Chuo chetu wakaribishe. Nadhani kila kitu unacho kuhusu sisi na tegemea kuwa utatoa ushirikiano mzuri juu ya hilo.” Alisema Dr. Matlda kisha wakapeana mikono na kuagana. Gari ilikuwa tayari ikimsubiri Andrew kwa ajili ya kumpeleka uwanja wa ndege kwa safari ya kurudi Tanzania akiwa amesheheni habari za kusisimua, japo alitakiwa kubaki nazo yeye peke yake mpaka siku atakayoruhusiwa kuzirusha hewani.
14 Timu ya kazi katika harakati
Magazeti mengi yaliibuka na habari hii habari ambayo ilianzia kwenye hoja Bungeni. Hoja zenye malumbano mengi kati ya wabunge wa vyama vya upinzani na chama tawala. Swali la mmoja wa wabunge ilikuja kama cheche ndogo ya moto katika msitu wenye miti majani na wanyama wa kila aina. Kubainika kwa upotevu wa mabilion ya shilingi kwenye Acount ya mradi wa Escrow Tegeta ilikuwa ni kama njiti ya kiberiti iliyowashwa karibu tanki la mafuta ya petrol. Hii ni hoja iliyobeba ukweli ambao uliwafanya viongozi mbalimbali wa kisiasa kuguswa. Sio mguso wa kuihurumia jamii ya watanzania bali ni kwamba kila walio wengi walihusika ama kuhusishwa na ufisadi huo.Wimbi hili la Escrow liliifunika ile rasmu ya katiba mpya iliyokuwa ikijadiliwa ili kupata mwafaka katika mivutano iliyokuwepo. Mgawanyiko wa makundi hayo mawili ulitokana na kutofautiana kimaoni. Kutokea kwa kashfa hiyo ya wizi wa zaidi ya Shilingi bilioni 320 za Escrow kulizima kelele za wananchi kuhusu Katiba mpya. Macho na masikio yakageukia kwenye kufuatilia wanaohusishwa na kashfa hii. Pamoja na vyombo vingi vya habari kuandika kuhusu kashfa hiyo, vikiwepo mitandao ya kijamii redio, Televission na magazeti lakini mmoja wa wakurugenzi wa habari aliwazuia waandishi wake kuandika chochote. Kutokuandika habari hizo haikuwa woga wa kutoa habari wala ukarimu wao kwa wezi hao bali ilikuwa ni katika kutafuta undani wa habari hii nyeti. Hii ni kawaida ya shirika hili la uandishi wa habari kuandika habari mwishoni kabisa baada ya vyombo vingine kuandika. Shirika hili lilikuwa bingwa wa kugundua habari mapema zaidi na kuitoa na wengine wanapopata chanzo cha habari hiyo jamii inakuwa imepata picha juu ya jambo hilo. Inapotokea shirika hili la habari halijatoa habari fulani na mashirika mengine yakatangulia kutoa habari hizo waandishi maalumu huzamia habari hizo kwa kina sana ili kupata mambo ambayo yakija kuandikwa watu wapate undani wa mambo hayo sio kwa sura ya nje tu. Huu ndio hasa utendaji wa kazi wa shirika hili kubwa la habari ambalo mara kwa mara limekuwa likiripotiwa kuwa ni shirika linalofanya vizuri hata kwenye vyombo vya habari vya kimataifa. Habari nyingi zilipatikana zikionyesha namna wanasiasa wakuu wa nchi wanavyohaha kutafuta namna ya kujisafisha mbele ya Rais na mbele ya jamii lakini hakukupatikana sabuni nzuri yenye kuondoa madoa hayo mabaya.Wengine wameswekwa mahabusu ili mambo yao yafuatiliwe kwa uhuru zaidi na wengine wamejiuzulu. Mawaziri na hata mwanasheria mkuu wa serikali naye aliamua kung’oka madarakani kwa ajili ya kashfa hii hii.Mambo yamechachamaa kila mtu katika kiti chake ikiwa bungeni ama katika vyeo vya uwaziri na katika idara nyeti wamechafuka sana juu ya mambo haya. Kuzamia kwa waandishi wa habari juu ya mambo haya kuliibua mambo mengi yaliyoainishwa kwa maandishi mwishoni kabisa baada ya wengi kuandika. Wasomi wengi walikuwa wanapenda zaidi magazeti yanayotolewa na shirika hili la habari pamoja na kuangalia vipindi vyake kwenye luninga. Sababu ni kwamba shirika hili halitoi habari bila kuichunguza kwanza. Utafiti wa hali ya juu sana ndio uliokuwa sababu ya kupata wasomaji na wafuatiliaji katika vipindi vyake. Tangu Chiefu apotee katika mazingira ya kutatanisha mwanzoni mwa kashfa hii ya upotevu wa hela nyingi za mradi wa umeme wa Escrow Tegeta wafanyakazi wa shirika hili walijua nini watarajie kutoka kwake. Japo ni wachache sana waliofahamu sababu ya kutoweka kwa bosi wao huyo. Ushupavu wa bosi huyu wa shirika la uandishi umesababisha kila mwandishi wa habari wa shirika hili kuwa tofauti na waandishi wengine kimbinu.Katika sakata hili waandishi wengi wa habari walitawanyika na kupiga mbizi ili kuyapata mambo haya kwa undani na sio habari za kuokoteza juu juu. Kwa upande wa habari kuhusu yule mfanya biashara tajiri na mchumba wake, Andrew amezamia na kugundua mahali watu wale wanaopendana sana walipo. Kila sehemu nyeti yenye vyanzo vya uhakika vya habari vilikuwa vinakamatwa vema ili habari zinazotoka ziwe za uhakika bila kuongeza chumvi. Na hii ndiyo sababu habari kutoka katika shirika hili zinapendwa sana kwa kuwa watu hawapewi habari zisizo na udhibitisho yakinifu. Vijana wanaojiunga na shirika hili wanahakikiwa kwa mambo mengi sana na makamanda wazoefu waliobobea
15
Maandalizi ya Arusi ya Kihistoria Marafiki mbalimbali walikuwa wamekusanyika nyumbani kwa mheshimiwa Mbunge Changawe huko Arusha. Marafiki hawa ambao wengi wao ni wabunge wenzake, baadhi ya mawaziri, pamoja na ndugu na marafiki mbalimbali ambao pia walikuwa ni wafanya biashara wakubwa. Kusudi la kikao hiki ni kupanga kamati ya maandalizi ya arusi ya Sebastian Changawe. Hii ilikuwa ni kamati iliyowahusisha marafiki wa mzee Changawe tu na ililenga kufanikisha arusi hii kwa kiwango cha kipekee sana. Katika ukumbi mkubwa wa kifahari ulioko katika nyumba ya mheshimiwa Changawe kulionekana kujaa watu wengi. Kila mmoja wa watu hawa alikuwa katika nafasi yake na kukaa kwa utulivu mkubwa. Kwenye kona moja kulikuwa na minong’ono iliyosikika. Baadhi ya wajumbe waliokuwepo mahali pale waligeuza shingo zao na kuona kumbe kamati ya vinywaji ilikuwa kazini katika kugawa vinywaji kwa wageni hawa. Mara moja baada ya muda kila meza ilijaa vinywaji vya kila aina na baadaye fundi mitambo alikwenda kukaa nyuma ya meza yenye seti ya Redio la kisasa lililokuwa na sabufa ambayo ilieneza muziki laini katika ukumbi wote ule kupitia spika ndogo ndogo zilizowekwa kila mahali ukumbini hapo. Baada ya kuwekewa vinywaji kila mmoja alianza kuchangamka na mazungumzo ya chini kwa chini yalisikika kila mahali ukumbini hapo. “Hivi ndoa ya huyu kijana Seba inafanyika kati yake na yule msichana waliyecheza naye filam ya uwendawazimu miaka ile au mwingine?” Aliuliza Mr. Edger Mwakibasi mfanyabiashara maarufu mjini Arusha.
“Kwakweli sijajua kuhusu hilo ila ninasikia tetesi kuwa wote walikuwa wako nchi jirani wakichukuwa masomo ya juu ya udaktari. Huenda ndiye au siye ila ukweli wote tutaujua tu baada ya muda si mrefu. Alijibu bwana Kibasila Lusajo ambaye pia ni mfanyabiashara mkubwa Jijini Dar es Salaam na mikoa ya kanda ya ziwa. Wakati muziki ukiendelea na vinywaji vikiendelea kuongezwa kwenye meza za waheshimiwa wageni mara Mc. Alisimama na kuchukuwa kipaza sauti na kuanza kuongea. “Waheshimiwa wageni waalikwa mabibi na mabwana habari zenu?” Alisalimia Mc. Na kuweka pozi. “Nzuriiii!” zilisikika sauti za pamoja zilizofanana na sauti ya piano kwa kuwa na mchanganyiko wa sauti nzito nyembamba na za kati. “Ninayo furaha kuwakaribisha ndani ya ukumbi huu. Mjisikie huru na amani kabisa. Kwa taarifa tu ni kwamba tuko hapa kwa ajili ya wito wa ndugu yetu Mheshimiwa Changawe ambaye muda sio mrefu kuanzia sasa atakuwa ndani ya ukumbi huu ili kutujuza kusudi la wito wake kwetu.” Alisema Mc. Huku akimhimiza Dj. Aweke mziki laini wakati waheshimiwa wakiendelea na vinywaji. Muda haukuwa mrefu mara Upande wa kushoto wa ukumbi ule walitokea vijana wawili mabausa ambao walivalia fulana nyeusi mmoja alienda kwenye kona moja ya ukumbi na mwingine alisimama mahali palipoandaliwa kwa ajili ya mheshimiwa Changawe kukaa. Wakati huo huo mziki ulipunguzwa sauti ukawa unasikika kwa mbali. Sauti ya viatu ilisikika ikitokea kwenye ngazi upande wa kulia na mara wahudumu wote upande wa vinywaji wakiwa kwenye sare maalumu walisimama na baadhi ya watu ndani ya ukumbi ule kwani Mheshimiwa Changawe alikuwa akiingia ndani ya ukumbi huo. Vazi lake la kinigeria lilionekana kumpendeza sana kwani liling’aa kwa weupe na darizi za rangi ya dhahabu na nyeusi kuanzia kofia. Pindo la vazi hilo lilikuwa linaburuzika chini na kumfanya aonekane kama mmoja wa machifu wa nchi ya Nigeria. Akiwa ameongozana na mke wake ambaye hali kadhalika alikuwa amevaa sare na mumewe vazi jeupe lililosindikizwa na kilemba kilichomkaa vema. Mheshimiwa Changawe alienda moja kwa moja mpaka kwenye Sofa kubwa la watu wawili alikaa kwa utaratibu kabisa akifuatiwa na mkewe na baada ya kukaa watu waliokuwa wamesimama walikaa pia kwa utulivu mkubwa. *** Waandishi wa habari wengi waliiganda ofisi ya Seba & EllyChangawe Enterprises kwa ajili ya kuhoji mawili matatu juu ya mambo yaliyotokea miaka mitatu iliyopita juu yake na mchumba wake. Vyombo vya habari vingi vilitarajia kupata mambo muhimu kuhusu mtu huyo aliyepotea siku nyingi. Taarifa za kuonekana kwake katika ofisi hizo zilizagaa kwa njia ya simu na kila mmoja alitamani kumwona na kujua mengi kuhusu yeye na mchumba wake. Shauku zao hazikupatiwa jibu la kutosheleza. Mara zote hawakuruhusiwa kumwona. Wakati mwingine Seba alijitokeza na kuongea nao hatimaye kuomba namba za wakurugenzi wa vyombo hivyo vya habari. Maneno aliyoongea nao yalileta jibu la waandishi wa habari kuondoka na hawakuweza kurudi tena katika ofisi ile. Siku zilizidi kusogea huku kila kitu kikienda vizuri kwa upande wa kampuni. Vyombo vya habari vilinyamaza kimya kwa habari za Seba na Judith huku watu wakiongea mengi bila kujua. Mambo yaliyotokea miaka mitatu iliyopita kwao waliyatafsiri kama walivyotaka. Wengine waliamini kuwa Seba na mchumba wake waliingia mkataba na kampuni za nje za Filamu na yale waliyokuwa wakiyafanya kwa kipindi cha miezi sita ilikuwa ni moja ya tamthilia ambayo inaweza kurushwa wakati ukifika. Wengine waliwaza mengi ambayo tafsiri zao hawakuweza kuzibainisha zaidi ya kuishia kuguna huku wakiyasindikiza kwa kusema “Ya ngoswe mwachie ngoswe mwenyewe.
*** Asubuhi ya siku hii Sebastian alipata simu kutoka kwa mkurugenzi Matlda na kumtaka apande ndege waonane Nairobi kwa mipango zaidi. Simu hiyo ya wito aliipata akiwa bado kitandani kwake hiyo ikiwa ni saa kumi na mbili za asubuhi. Maneno ya mkurugenzi yalijirudia mara kwa mara masikioni kwake. “Inabidi upande ndege uje Nairobi kwa ajili ya mipango zaidi, si unajua kuwa kuna mengi yanayokusubiri mbele yako na mchumba wako?.” Kwa kuwa hakuwa na majukumu yaliyokuwa yamemshika alikubaliana na mkurugenzi wake kwa kumwitikia wito wake. Wakati uleule aliamka na kuingia bafuni na baadaye akapata chai ambayo alikuwa amejihifadhia jana yake kwenye chupa ya chai pamoja na mayai na mikate. Baada ya chai akavaa nguo na kujitayarisha kwa safari hiyo ya dharura huku akiwa amefarijika kwani ajijiona kuwa mpweke sana kukaa mbali na mchumba wake. Baada ya dakika kumi na tano za matayarisho alikuwa yuko ndani ya gari huku Dereva wake akikata mitaa ya jiji la Dar es Salaam akielekea Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Na baada ya saa moja alikuwa yuko angani ndani ya ndege akielekea jijini Nairobi. Mawazo ya hili na lile kuhusu mambo yaliyoko mbele yake yalimfanya asijue ni wakati gani ulitumika hadi kuwasili katika anga la uwanja wa ndege wa kimataifa Jijini Nairobi. Sauti ya mtangazaji iliyowataka abiria kufunga mikanda ndiyo iliyomshtua katika lindi la mawazo aliyonayo. Ndege ilizunguka angani kama mara tatu kabla ya kutua na baadaye kuruhusu abiria kushuka na kuelekea mapokezi. Seba alijivuta kivivu kutoka kwenye siti aliyoikalia na kuelekea mlangoni akiongozana na abiria wenzake. Mapokezi alimwona Mchumba wake Judith ambaye alimkimbilia na kumlaki kwa furaha. Kisha wakaongozana kuelekea kwenye gari. “Habari za hapa Nairobi?” Aliuliza Sebastian kwa shauku baada ya kupokelewa begi lake dogo na mchumba wake huyo. “Sio mbaya ninapambana na mitihani tu kumaliza kabisa masomo yangu ya udaktari. Vipi nyumbani Tanzania hawajambo?” Aliuliza Judith kwa shauku. “Tanzania ni kuzuri tu. Vyombo vya habari vina hamu na sisi hujapata kuona. Magazeti, Redio, Runinga na hata mitandao ya kijamii vinatutamani ile mbaya!” Seba aliongea hayo huku akipanda gari lililokuja na Judith kumchukuwa. Judithi akapanda sehemu ya Dereva na kuiwasha gari tayari kwa kuondoka uwanjani hapo. “Walikusumbua sana kwa ajili ya kupata habari?”Aliuliza Judith wakati akitia gea namba tatu na gari likizidi kuongeza mwendo kuelekea mjini. Sana tu lakini niliwaomba wakurugezi wa vyombo vyote vya habari watulie kidogo tu maana nina mambo mazuri sana baadaye kidogo yatakayofaa kuandikwa na kuleta maana mbele ya jamii. Walionyesha kunielewa na kuwajulisha watu wao wa habari nao mpaka sasa wanasubiri kwa utulivu.” Aliongea Sebastian huku akionekana kushikwa na mshangao. “ Mbona umeduwaa ghafla kuna nini?” Aliuliza Judith wakati akikata kona kuingia katika maeneo ya chuo cha Psychological Mental Hospital. “Ninashangaa kukuona ukiendesha mwenyewe gari katika miji ya watu.” Alisema kwa utani Seba kisha wakacheka pamoja. “Usiwe na wasiwasi, mimi pia ni mmoja wa watu hao.” Alisema Judith huku akifungua mkanda kwani tayari walikuwa wamefika kwenye jengo kuu la Utawala. “Sawa mama hongera kwa kuwa dreva mzuri.” Seba alisema huku akishuka na moja kwa moja wakaelekea kwenye ofisi ya mkurugenzi. *** Kamati ya maandalizi ya arusi ya Seba na Judith chini ya Gideon Rutashobya ambaye ndiye mkurugenzi mwajiri wa shirika la Uingizaji na uuzaji wa magari yenye ubora wa hali ya juu ilikuwa imeanza. Mwenyekiti wa kamati hiyo alikuwa ni Mkurugenzi Rutashobya mwenyewe akifuatiwa na meneja wa Seba &EllyChangawe Interprisess. Makampuni haya mawili yaliunda kamati ya maandalizi ya arusi hiyo ya kihistoria wakishirikisha wafanyakazi wao wote. Kwa nia moja walikusudia kufanikisha arusi hiyo kwa kiwango kikubwa sana. Malengo yao waliyaweka na kuchangisha fedha nyingi sana ambazo walisubiri taarifa juu ya nini cha kufanya na mchango huo. *** Ilikuwa ni jambo la kushangaza kwa Seba baada ya kukabidhiwa tiketi ya ndege kwa safari ya Berlin Ujerumani, kwa ajili ya kufanya manunuzi ya vitu muhimu kwa ajili ya arusi na Send off. “woooow! Umenishangaza sana mkurugenzi. Seba alisema maneno hayo huku akimkumbatia mkurugenzi wake ambaye alikuwa amesimama tayari kwa safari kuelekea uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyata.
“Nashukuru sana kwa kutujali kwa kiwango kikubwa hivi.”Alisema hivyo Seba na wote watatu wakatoka na kuliendea gari lililokuwa mbele ya jengo la makao makuu na kuingia ndani yake wakiwa na mabegi yao na gari likaondolewa kuelekea uwanja wa ndege. Baada ya masaa mawili ndege ya shirika la ndege la Ujerumani ilikuwa hewani ikiwa na abiria wengi wakiwepo Seba, Judith na Matlda. Seba na Judith waliona tunu kubwa kusafiri na mkurugenzi wao kwenda ughaibuni kwa maswala yao. Walijisikia kujaliwa kwa kiwango cha juu sana. Waliongea mengi ya kufurahisha na yenye malengo ya mbele zaidi ya maisha yao. Walipochoka katika kubadilishana mawazo usingizi uliwapitia na kila mmoja alizama katika upeo mwingine wa fikra. Ndani ya ulimwengu unaoona mambo kwa viwango visivyofikika na kukutana na vitu ambavyo haviwezi kushikika. Seba aliyaona mambo yakimpambazukia kwa viwango vizuri sana na vikubwa sana ndani ya ndoto zake wakati wa safari yao. Alijiona akiwa msaada kwa kila mtu nchini kwake hasa kwa wenye matatizo ya akili. Alijiona akiwa msaada kwa watu kutoka katika nchi mbalimbali watakaohitimu mafunzo katika chuo chake ambacho kitakuwa chini ya usimamizi wake. Alijiona mwenye fahari kubwa akiwa na mke wake mpenzi ambaye kila wakati alikuwa naye karibu yake. Hizo ni ndoto zinazokwenda kutimia. *** Mapokezi ya watu hawa watatu yalitia fora kwenye uwanja mdogo wa ndege za binafsi ulioko kwenye mji wa Dormagen St. Michael, katika nchi ya ujerumani. Taarifa za kufika katika jiji hili zilipelekwa masaa ishirini na nne kabla ya kuanza safari kwa Matlda na wageni wake. Watu walijipanga safu mbili kutoka iliposimama ndege yao kuelekea mapokezi ambapo ndio ofisi kuu ya shirika hilo la afya ya akili duniani. Mavazi meupe yaliyokuwa na nembo ya shirika hilo ilikuwa kwenye fulana zao walizovaa.Muziki wa taratibu sana ulisikika ukilia kutoka kwenye spika zilizofungwa kiufundi sana ndani ya kuta za jengo hilo kubwa na la kifahari. Muziki huo wa ala uliwaongoza wasichana warembo wenye miamvuli kwenda kuwapokea Mkurugenzi Matlda pamoja na Sebastian na mchumba wake Judith. “Nifuateni ndio tumefika msishangae.” Alisema Matlda kwa uchangamfu baada ya kuwaona akina Seba wakiwa wameduwaa. “Hatukutegemea mapokezi haya mkurugenzi, kwetu ni mshtukizo kwa kweli.” Alisema Sebastiani huku akimwonyesha Judith mabango yaliyoandikwa maneno haya: Karibuni Ujerumani Mr. Sebastian na Malkia Judith Martin. Woooow! Judith alisema wakati akimfuatia Mkurugenzi kushuka na yeye akifuatiwa na Sebastian. Pale chini ya sakafu kulikuwa na maua ya rangi mbalimbali pamoja na harufu nzuri ya uturi iliyonyunyizwa. Wajakazi warembo wenye mavazi mazuri sana tofauti na watu wengine waliovaa fulana nyeupe zenye nembo. Idadi ya wasichana wale walikuwa sita watatu walibeba miamvuli, ambapo walikwenda kuwafunika mkurugenzi seba na Judith wakati wale watatu wengine wakicheza kufuatisha mziki wa ala huku wakimwaga maua. Hatua zao zilikuwa ni fupi fupi kutokana na wamwagaji wa maua wanavyoenda kwa kufuatisha muziki uliokuwa hewani. Na hii iliwapa nafasi waandishi wa habari kupata picha za wageni wao pamoja na Mkurugenzi wao. Watu waliosimama katika safu walikuwa wakipunga mikono kwa furaha sana huku wakishangilia wakati mkurugenzi na wageni wake wakielekea kwenye chumba cha mapokezi kabla ya kuelekea ofisini kwao. Katika chumba cha mapokezi walikuwepo viongozi wa shirika hilo la afya katika kituo cha hapo nchini ujerumani. Ulikuwa ni mkutano wa watu wapatao mia moja viongozi pamoja na wafanyakazi. “Ninayo furaha kuwatambulisha wageni wangu ambao ni Mr. Sebastian na Malkia wake Judith Martin.” Alisema Mkurugenzi, akachukua glasi ya maji na kunywa kidogo kisha akaendelea. Seba na mchumba wake wamekuwa watu wa muhimu sana kwangu na kwa shirika letu kwa ujumla kutokana na wao kuwa sehemu ya familia. Kwa mambo mengi. Najua kuwa kila mmoja anakumbuka kiu yangu ya kuyafikia mataifa mengi katika Afrika India na bara lote la Asia kwa ujumla. Kwa miaka mingi tangu nichukue jukumu la kusimamia kituo cha afya nchini Kenya nilitamani kupanua wigo zaidi kwa kujenga vituo kwa mataifa jirani nikianzia na Tanzania. Kwa hiyo ninataka kuiweka furaha yangu mbele yenu kuwa Sebastian na Judith ni raia kutoka nchini Tanzania. Nafikiri kuwa kwa kusema hivyo utakuwa umeelewa vizuri furaha yangu ni kubwa kiasi gani.” Alisema mkurugenzi na watu wote kwenye kikao kile wakapiga makofi na kushangilia. “Vema, Labda kwa kidokezo tu ni kwamba tayari tuna mpango na kisiwa kile cha amani ili kuifanya huduma ya Psychological mantal Hospital iweze kuwafikia. Na hawa walioko hapa ndio mawakala wa shirika hilo katika nchi ya Tanzania.” Makofi yalirindima zaidi kuunga mkono kauli hiyo. “Na sasa watu hawa wapo katika matembezi maalumu hapa nchini wakijiandaa na Arusi yao baada ya hapa. Kwa sababu ni wageni wetu nitafurahi kuona kila mmoja wetu kutoa ushirikiano wake kwa ziara yao. Wiki hii tutaingia katika maeneo mbalimbali muhimu na kufanya manunuzi ya vitu muhimu tukirudi hapa tutakuwa tayari kuingia kwenye ndege kwa safari ya kurudi Afrika.” Alisema Mkurugenzi kisha akamalizia kwa kuwataka Seba na Judith kuwasalimia wafanyakazi na viongozi wa idara ya mbalimbali katika kituo kile kikuu. Ilikuwa ni ziara ya siku chache lakini iliyoshiba matukio. Mengi yalifanywa yakiunga mkono shauku yao ya kuwepo katika Taifa hili. Ndege ndogo ya shirika hilo ilitumika kuwapeleka katika maeneo mbali mbali ya kihistoria tangu katika ukumbi wa Berlin Confrence chini ya Mfalme Otto Von Bismark, hadi katikanyumba walizokuwa wakiishi wafalme wa wakati huo akina Kaisari Welhelm II na Aldoph Hitler yule Dikteta. Mambo mengi mengine yalikuwa ya kushangaza na kufurahisha. Muda wa kurudi Afrika ulipofika walirudi kwa ndege binafsi ya shirika hilo. “Tumefurahia sana safari hii, pia tumejifunza mengi ya kushangaza.” Alisema Sebastian akijiweka sawa kwa kufunga mkanda kwa mujibu wa tangazo toka kwenye kipaza sauti. “Kwa kweli safari hii ilikuwa ya faraja kubwa sana kwa upande wangu pia.” Aliongeza Judithi akimtazama Mkurugenzi Matlda aliyeko kiti cha mbele yao. Na mimi pia nimefurahi kuwa nanyi katika safari hii hata marafiki zangu wamewapenda sana. mmekuwa sehemu ya furaha kwao.” Alisema Matlda huku akitabasamu. Ndege ilizidi kupaa hadi ilipochukuwa usawa na kila abiria alifungua mkanda wake. Safari iliendelea kila mmoja akitafakari mambo mbalimbali huku wengine wakipotelea usingizini.
Ushuhuda
“Ilikuwa ni maisha ya ajabu sana yaliyojaa huzuni na matukio ya kusikitisha.” Alisema Mzee Martin mara tu baada ya kupokea kipaza sauti kutoka kwa Seba. “Baada ya kuingia kwenye ukurasa wa giza zito katika ufahamu wa binti yangu nilijitahidi kuficha hali hiyo kwa watu wengi. Miongoni mwa watu niliowaficha kwa bidii zote ni Sebastian. Nilijua mwisho wa uhusiano wa vijana hawa ni tatizo ambalo limempata mmoja wao. Sikuwa na sababu ya kumweleza lolote kuhusu mabadiliko yaliyotokea katika maisha ya mchumba wake. Lakini baada tu ya wiki mbili baada ya tatizo hili kutokea Seba alikuja nyumbani kwangu jioni moja hivi. Nilishindwa kujua alirudi kwa sababu ipi wakati aliniaga kuwa anakwenda masomoni nchini marekani?! Mbaya zaidi alimwona Judith akiwa yuko nje ya nyumba akiwa katika harakati zake huku akiwa hana ufahamu sahihi.
Moyo ulimuuma alipomwona mwenzake na alichofanya ni kumvutia ndani ya nyumba japo ilikuwa si rahisi sana. Baada ya kuingia ndani kijana alilia sana mbele yangu huku akimwuliza mchumba wake “Umekuwaje mchumba wangu? Mbona sikukuacha hivi?” yalikuwa ni maswali ambayo hayakupata jibu lolote zaidi ya kicheko kirefu kutoka kwa mchumba wake. Kwangu nilishindwa la kumwambia kijana huyu zaidi ya kumwambia kuwa binti yangu hakufai tena sasa ni kichaa kwahiyo tafuta mwingine uoe kwakuwa Judith uliyempenda sio wa aina hii huyu ni mwingine asiyejua lolote jema ama baya. “Usiseme hivyo baba! Mimi nimempenda Judith kwa hali zote, nimeuahidi moyo wangu kuwa hata kutokee tatizo gani mimi niko tayari kupambana nalo nikiwa na Judith mpaka liishe bila kujali litaisha lini.” Judithi ni mke wangu mtarajiwa kwa hiyo nipe nafasi nitafute namna niwezavyo kumsaidia katika matatizo haya.” haya yalikuwa ni majibu ya ajabu sana kutoka kwa Seba. Alikuwa bega kwa bega na Judithi katika njia zote za maisha mapya aliyokuwa nayo. Ziara za majalalani na maeneo mengineyo walikuwa wote huku akitafuta pamoja nami namna ya kumsaidia atoke katika tatizo lake. Mengi yameelezwa katika mlolongo wa matukio katika ushuhuda wake mpaka kufikia hapa. Kwa upande wangu sina la kusema zaidi ya kuusifu upendo wa kijana huyu. Sijawahi kuona Upendo kama huu. Huu ni upendo kutoka Sayari nyingine.. Pambano lake dhidi ya hali iliyokuwepo lilipata jibu kwa kupata Hospital nzuri iliyopo Nairobi Kenya. Na sasa wapo hapa wakiwa ni wazima namtukuza Mungu wa mbinguni na kuibariki safari yao ya kuiendea ndoa yao.” Alihitimisha Mzee Martn huku akifuta machozi na kumwachia binti yake Kipaza sauti. *** Kilio cha kwikwi kilisikiika kila mahali, utulivu wa watu waliokuwa wakifuatilia historia hii ya kusisimua uliruhusu kwikwi hizi za kilio cha Judith Martin zisikiike vema kila mahali zikisaidiwa na vipaza sauti vilivyopangwa mbele yake. Waandishi wa habari walifurika ukumbini akiwepo Gadna ambaye alipata mwaliko maalumu kutoka kwa Mchungaji Wilfred Dulanga. Miongoni mwa waandishi hawa walikuwepo Andrew Charles kutoka gazeti la UWARIDI ambaye aliambatana na Sebastian na Judith baada ya kupata taarifa kuwa siku hiyo ilikuwa maalumu kwa kuijua Historia kamili ya maisha yao. Kwa Andrew alijiona mwenye bahati ya kuwa na mambo mengi ya kuandika kuliko waandishi waliokuwepo mahali hapo. Kwa kuwa Tangu aliposafiri kuwasaka Seba na Mchumba wake hajapata kuandika hata nukta moja ya habari juu yao. kwake aliamua kwenda mbali zaidi kwa kuandika kitabu chenye jina la: “Upendo kutoka Sayari nyingine.” Vipaza sauti vilitegwa na vilikuwa vikifanya kazi yake bila chenga na kila neno lilirekodiwa. Kilio cha Judith Martin hakikukata mapema na hii haikuwashawishi waandishi wa habari kuyumbisha kamera zao maana walijua katika kilio hicho kuna nguvu ya habari inayohitajiwa kuwafikia watu. Judith alikuwa amejiinamia huku akilia na akina Seba walisimama wakimsubiri atoe ushuhuda wake. Wahudumu wa kanisa waliduwaa kwa historia iliyotangulia kutolewa na Mzee Martin na Sebastian Changawe viliwafanya maelfu ya watu kusisimka huku wengine wakilia kimya kimya kwa kuguswa na habari za maisha ya vijana hao. “Ndugu zangu, nashindwa kujizuia japo ninatamani kuokoa muda kwa kueleza kwa haraka yaliyoko ndani yangu…”Alisema kwa taabu Judith Martin kisha akainua macho yake na kuwatazama watu waliofurika ndani ya Kanisa nao wakimwangalia kwa utulivu. Mambo yaliyopita kati yangu na Sebastiani ni kama hadithi iliyotungwa na mtunzi mahiri kusudi kuwasisimua watu. Hadithi ambayo imepatiwa wacheza sinema wazuri, ambao wamecheza kiuhalisia kila kipengele ili kugusa mioyo ya watu juu ya maisha ya kufikirika na upendo uliokosa mfano katika sayari hii. Lakini hii sio hadithi wala sinema bali ni mambo halisi yametokea. Maelezo ya baba yangu mzazi kuhusu maisha yangu ni kweli. Upendo wa Sebastian kwangu ni wa ajabu sana na wa thati. Nikiwa kichaa kabisa kutokana na matatizo niliyopata na nikifanya mambo ya ajabu majalalani na mitaani kwake halikuwa kwazo la upendo wake kwangu. Alinipenda sana kiasi cha kujitia wendawazimu na kutembea nami kila kona ya mji tukiripoti kwenye majalala mbalimbali huku tukizomewa na kutupiwa mawe na watoto wakorofi. Hayo nimekuja kuyadhibitisha kwa picha na video fupi fupi baada ya mimi kupona. Umaarufu wake na utajiri aliviona vyote havina maana kuliko mimi. Heshima zake zote kazini na katika kampuni zake aliwapa watu wengine waheshimiwe wao badala yake ila yeye adhauliwe na kila mtu sambamba na mimi.” Alisema Judith huku akishika mkono wa Sebastian na machozi yakimwagika. Kisha akaendelea. “Baadaye sana Seba akishirikiana na baba yangu na shangazi pamoja na baba mdogo walitafuta namna ya mimi kupata Tiba ya kuniondoa katika hali niliyokuwa nayo. Hapo sina maneno ya kuongeza kwa sababu kila kitu ametangulia kukisema katika ushuhuda wake. Nataka nitoe shukrani zangu nyingi kwa Madamu Matilda na uongozi wa Sychological Mantal Hosptal. Kwa namna ya kipekee wamenihudumia mpaka kurudi katika hali yangu ya kawaida. Na Leo hii madamu Matilda mkurugezi wa Psychological Mental hospital yupo hapa katikati yetu tafadhali nikuinue watu wakuone.” Alisema Judith na kunyamaza huku akiangalia upande aliko Mkurugenzi Matilda. Watu walipiga makofi baada ya mwanamke wa kizungu kuamka na kupunga mikono yake kwa watu. Huyu nimemchukulia kama mama yangu maana ndiye aliyenilea nikiwa katika hali mbaya na baada ya kupona kwangu amekuwa mwalimu wangu nilipojiunga na Chuo cha udaktari wa magonjwa ya akili. Mpaka sasa Mimi na Seba tumekuwa madaktari wazuri kutokana na mwongozo wa Mkurugenzi Matilda. Mungu akubariki sana Madamu Matilda ninathamini mchango wako katika maisha yangu. Alisema Judith na Madamu akakaa huku watu wakiendelea kumpigia makofi. Kwa sasa inatosha kusema Ninamshukuru sana Mungu wa Mbinguni kunipatia Sebastian ambaye kwangu ni zaidi ya rafiki na hata baada ya kufunga ndoa bado atakuwa zaidi ya mume. Kwangu atakuwa kurwa na mimi ni doto kwake ndani ya maisha haya.” Alihitimisha Judith Martin. Mchungaji Wilfred Dulanga alipokea kipaza sauti mkononi mwa Judith. Kisha akaongoza zoezi la kuvishana pete kwa wawili hao huku maelfu ya watu wakishuhudia na kupiga vigelegele. “Jamani ushuhuda huu ni wa ajabu sana katika shuhuda nilizowahi kusikia. Hii inaonyesha kuwa bado katika dunia hii wapo watu wenye upendo halisi wa Kimungu. Nami kama Mtumishi wa Mungu nawatakia maisha marefu yenye upendo wa thamani kwenu wote wawili. Leo ni zoezi la kuvishana Pete za uchumba lakini baada ya majuma matatu harusi kubwa itafanyika mkiwa mmefunga ndoa yenu kwa ajili ya maisha ya mume na mke. Nawatakia heri na Mungu awabariki wote. Watu wote wakaitikia Ameeeeeen!! makofi na vigelegele vilifuata na ibada ikaisha.
16 Arusi Ukumbi wa huduma ya EPMT ulifurika maelfu ya watu wenye furaha ya aina yake. Nje ya ukumbi huo kuliwekwa mahema makubwa yaliyochukuwa mamia ya washirika na wageni kutoka nchi mbalimbali. Safu ya mbele wana kwaya walikuwa wamekaa kwa utulivu katika viti vyao. Wapiga vyombo walikuwa katika eneo lao juu ya gorofa ya kwanza wakitazamana na Madhabahu ya kifahari. Upande wa kushoto wa ukumbi huu wazee wa kanisa walikuwa wametulia wakiwa na mavazi yao rasmi ya majoho. Mashemasi walikuwa wako kila mahali wakiwaelekeza watu mahali pa kukaa. Wageni kutoka ujerumani walikuwa ni wengi, wakifuatiwa na wanafunzi na madaktari kutoka katka Shirika la afya la Sychological Mental Hospital. Mkurugenzi wa shirika hilo alikuwa yupo sambamba na timu yake. Wachungaji waliketi katika viti vya mbele karibu na madhabahu wakiwa katika utulivu wa hali ya juu. Mziki wa ala ulikuwa ukitoka kwa taratibu katika spika zilizoko ndani na nje ya ukumbi huo. Kila mahali kulipambwa kwa viwango vikubwa sana. Mara kiongozi wa sherehe alisimama na kutangaza: “Sasa ni wakati wa kusimama kwa heshima kwani bwana arusi anaingia kanisani akiongozana msimamizi wake.” Watu wote walisimama wakiangaza angaza macho kwenye lango kuu la kuingilia katika kanisa hilo. Vigelegele vilisikika mlangoni wakati huo mabinti wa shoo wakiingia kwa mziki maalumu toka kwa DJ huku wakimwaga maua. Nyuma ya wacheza shoo hawa walifuatiwa na bwana Arusi na msimamizi wake. Mwendo wao ulikuwa wa taratibu wakifuatisha mziki uliokuwa hewani. Bwana arusi alikuwa katika vazi la Suti nyeupe na viatu vyeupe shati jeusi na tai nyeupe na msimamizi wake hali kadhalika. Baada ya kuingia ndani ya ukumbi bibi arusi naye aliruhusiwa kuingia akiwa na msimamizi wake na Matron akisimamia kila kitu kiende sawa. Mwendo huo uliwafikisha mbele ya madhabahu na Mchungaji Wilfred Dulanga alikuwa tayari madhabahuni kwa ajili ya kufunga ndoa hiyo. “Sebastian Matias Changawe na Judith Martin Sebwaka sasa ni mume na mke, alichokiunganisha Mungu mwanadamu asikitenganishe.” Hayo ni maneno ya Mchungaji ya mwisho baada ya kufunga ndoa hiyo takatifu. Watu walishangilia kwa makofi na vigelegele. Baada ya mambo yote walielekea kwenye ukumbi wa sherehe. Mamia ya watu wenye kadi maalumu walielekea kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee. Sherehe ilifanyika ikihudhuriwa na viongozi wa Serikali.Wakati wa zawadi ulipofika watu walitoa zawadi za aina mbalimbali kubwa na za kuwashangaza maarusi. “Jamani katika sherehe hii yupo mkurugenzi wa Sychological Mental hospital nimenong’onezwa kuwa ana jambo la kusema kwa ajili ya Maarusi wetu.” Alisema MC Christofer Jafari, mara hiyo Mkurugenzi Matilda alisogea mbelena kushika Mic. “Kwa upande wangu nimejawa na furaha isiyo kifani kwa arusi hii. Bila shaka mtajiuliza imekuwaje mzungu huyu akafurahishwa kipekee na arusi ya akina Seba na Judith?! Lakini ukweli ni kwamba Seba na Judith ni rafiki zangu wakubwa! Mbali na kwamba wamekuwa wanafunzi wangu lakini kwangu ni kama ndugu kabisa. Naomba nichukuwe nafasi hii kutangaza zawadi yangu kwao. Kama mkurugenzi wa shirika la Sychological Mental Hospital (SMH). Nawatangaza Sebastian na Judith kuwa wawakilishi wa Shirika hili hapa nchini. Taratibu za ujenzi zinakamilika baada ya miezi miwili hospitali pamoja na Chuo cha Udaktari vitakuwa tayari kabisa. Shirika hili litaanza kazi ya kuwahudumia wananchi wenye matatizo ya akili kwa viwango vikubwa sana. Yote haya yatafanyika chini ya usimamizi wa Sebastian na Judith. Watu hawa ni Madaktari kamili kwani wamesoma katika chuo changu na mimi nikiwa mwalimu wao nimewahakikisha. Watasimamia madaktari zaidi ya mia moja watakaoanza kazi hiyo baada ya miezi hiyo miwili. Chuo chetu kiko Kibaha katika eneo lenye zaidi ya hekari kumi. Utaratibu huo umefanywa kwa zaidi ya mwaka na ujenzi umekuwa ukifanyika kwa kipindi chote hicho bila Seba na Mwenzie kujua leo ndio nawaambia rasmi.” Alisema mkurugenzi kisha akaenda waliko Seba na Judith ambao walikuwa midomo wazi kwa mshangao, akawakumbatia kisha akarudi kukaa mahali pake huku shangwe na vigelegele vikimsindikiza, wakati Sebastian na Judith wakiwa wameduwaa. Baada ya mambo yote sherehe ilimalizika kwa watu kula na kunywa wakifurahia Arusi hiyo ya kihistoria.
0 Comments