Kabla sijakuandikia haya nilivuta kumbukumbu ya miaka kadhaa nyuma Maria. Siku ile tulipokutana kisimani kuteka maji, macho yetu yakatazamana na sote kwa pamoja tukajikuta tukiona aibu.
Haikuwa mara ya kwanza kuonana lakini ile ilikuwa siku maalumu, ukaniomba nikutwishe ndoo ya maji, wakati nainyanyua tyukatazamana tena machoni na kujikuta tukitabasamu.
Haikuwa mara ya kwanza kutabasamu, lakini hii siku ilikuwa ya aina yake.
Siku ambayo nafsi zetu zilishindwa kutunza siri na kwa pamoja zikakiri kuwa zilikuwa zinahitajiana. Nilikwambia nakupenda nawe ukajibu unanipenda pia.
Maisha yetu duni hayakutuzuia kufurahi, nyumbani kwetu tukipika magimbi nilijitahidi kuficha pande moja na kukuletea shuleni, na wewe ulinihifadhia mahindi ya kuchemsha na kuniletea katika kile kisima tulichokutana mara ya kwanza. Nakumbuka hekima zako na jicho lililoona mbali, ulisema tusishiriki ngono kwani mwalimu wa sayansi alidai kuwa ni hatari kwa afya na pia husababisha mimba kabla ya wakati.
Nilikusifu na kisha nikateta na moyo wangu nikisema wewe ni msichana wa kipekee sana kwangu. Msichana mwenye ndoto za maisha.
Darasa la saba likamalizika, sikubahatika kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kama ilivyokuwa kwako. Ulilia pamoja nami na almanusura ugome kwenda shule uliyochaguliwa, nikakusihi usome ili siku moja tuiendeshe familia yetu vyema, na hapo rasmi nikajikita katika kilimo.
Maria ukaenda shule huku ukisisitiza kuwa unanipenda sana, shule ilikuwa umbali wa vijiji vitatu kutoka kijiji chetu. Nilipouza mazao nilifunga safari na kukuletea pesa kidogo za matumizi, walimu walinitambua kama kaka yako lakini mimi na wewe tulijua nini kinaendelea. Kila nilipokuja ulinisisitiza kuwa unanipenda sana na mimi ni kinga yako dhidi ya wanafunzi wa kiume wanmaokutongoza kila kukicha.
Nilijisikia fahari, elimu yangu ya darasa la saba lakini nina nafasi kubwa zaidi ya hao wanafunzi wenzako. Nikaongeza bidii katika kilimo na wewe ukaendelea kusoma kwa juhudi. Sifa zako darasani nilizisikia kutoka kwa wanafunzi wenzako, walienda mbali zaidi na kusema kuwa ulipewa zawadi ya mwanafunzi mwenye nidhamu. Hayo yote yalikuwa fahari kwangu, nilikutazama kwa jicho la mke mtarajiwa nawe ukanitazama kama mume.
Mama yangu alitaka nioe baada ya kuwa kilimo kimekaa mkao wa kuniingizia kipato huku ufugaji nao ukishamiri. Nilipingana naye katakata na kumwambia kuwa wakati bado. Mama alilalamika sana akitaka kumshika mikononi mjukuu wake wa kwanza kabla hajafa lakini haikuwezekana kunishawishi kuoa msichana mwingine tofauti na wewe Maria. Sikushtuka ulipochaguliwa kujiunga kidato cha tano maana dalili zilikuwepo za kutia matumaini. Sasa haukuwa umbali wa vijiji vitatu bali mikoa kadhaa ambayo hakika nisingeweza kumudu kuhudhuria mara kwa mara.
Hapo rasmi yakaanza mawasiliano kwa njia ya barua. Nilikuandikia nawe ukaniandikia, kila barua yako haukusita kunikumbusha kuwa unanipenda sana na hakuna mwingine zaidi yangu. Nilizitunza barua zako kama kumbukumbu baada ya ndoa yetu.
Ndoa ambayo tulipanga ifanyike baada ya wewe kumaliza kidato cha sita. Hata mama nilimwambia kuwa nimekaribia kuoa. Akaniuliza namuoa nani sikumjibu upesi!! Nilichomwambia ni ‘avute subira’ Ulipomaliza kidato mambo yakabadilika, ukalalamika kuwa huwezi kuolewa kabla hujawa na shahada ya kwanza, kama kweli nakupenda ningoje miaka mitatu si haba!! Ni kweli nakupenda nikalazimika kungoja.
Huku kijijini nilifanikiwa kujenga nyumba yangu ya tofali za kuchoma, basi wasichana kadhaa walijiweka niweze kuwaoa, lakini kwanini nikusaliti wakati moyo wangu ulinituma kwako pekee.
Maria, ninapoyaandika haya sikulaumu wewe bali nailaumu elimu uliyoipokea katika kichwa chako, nalilaumu na hilo jiji lililokupokea. Sasa ulikuwa na simu hukutaka tena habari za barua, ulitambua kabisa kijijini kwetu mtandao wa simu haukuwa umefika lakini ukanitaka niwasiliane nawe kwa namba yako. Kuupata mtandao nililazimika kunyonga baiskeli yangu vijiji vinne zaidi na hapo ningeweza kusema nawe japo kwa shida. Kuna siku nilinyonga baiskeli yangu, ikapata pancha tairi zote mbili nikalazimika kuisukuma huku natembea, nilichoka sana lakini kila nilipokumbuka kuwa ni safari ya kwenda kuzungumza nawe nilijawa na nguvu mpya na kisha kukaza mwendo.
Nilipokupigia simu ukazungumza kwa sekunde chache tu, nayakumbuka maneno yako hadi leo ninapokuandikia haya, uliniambia upesiupesi “NIPO KWENYE DISKASHENI NICHEKI KESHO” hata hukuniaga ukakata simu.
Maria, hivi ni kwa sababu sikuwa najua maana ya diskasheni ama ni kwa sababu niliishia darasa la saba basi kila kitu ukaniona sijui na sitakiwi kujua?? Yaani hata salamu yangu niliyokupa kwa furaha hukujibu!! Hiyo ilikuwa siku ya kwanza kujikuta nakasirika kwa sababu yako!! Nikaziba pancha na kunyonga kurudi nyumbani, usiku wa kiza kinene. Lakini hata siku iliyofuata nilijikuta sina hasira na ninatamani kuzungumza nawe, na hapa ndipo nikatambua kuna nguvu ya mapenzi inaniendesha nafsini.
Tulizungumza kwa dakika kumi, niliridhika japo sikusikia ukiniomba msamaha kwa kitendo chako cha kunikatia simu, lakini bado sikujali nilichofurahi ni kuwa tumezungumza, nilitaka kukueleza siku hiyo kuwa mama amelalamika tena juu ya mjukuu. Lakini nilisita na kubaki nalo moyoni nikingoja umalize miaka yako mitatu.
Mawasiliano yetu yakaendelea kuwa ya nadra sana na ile hali yako ya kunikumbusha kuwa unanipenda mara kwa mara ikatoweka, ukawa mtu wa kungojea nikwambia nakupenda nawe unajibu kwa sauti ya chini “NA MIMI PIA”…….siku zikasonga mbele bila mimi kuchoka kukwambia kuwa nakupenda, lakini sasa ulijibu “ME TOO” tena kama unayejilazimisha, nilitamani sana kuuliza lakini imani yangu haikuniruhusu kumfikiria mtu vibaya pasipokuwa na uthibitisho. Nikaendelea kungoja!!!
Ujenzi wa barabara ulikuja na Baraka katika familia yangu!! Serikali ikatulipa milioni kadhaa, kwa sababu mimi nilikuwa mtoto wa kiume nilisimamia masilahi yale. Nikaikarabati nyumba yangu na kuwa ya kisasa, wasichana wakazidi kujigonga lakini kila nilipowakaribisha nyumbani kwangu walikutana na picha yako kubwa ukutani. Ulivaa kiheshima sana na ulikuwa unatabasamu!! Hapo wakakata tamaa, na niliwaeleza kuwa wewe ni mama mwenye nyumba ile.
Umbali hunyausha mapenzi!! Nikaamua kukufungia safari kuja huko chuoni kwako Dar es salaam. Nikamuaga mama kuwa kuna biashara naenda kuchukua huko. Akanibariki kwani sikuwahi kumwangusha hata siku moja tangu nikose nafasi ya kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza. Nikaingia jijini, nikajikuta nina utofauti na kila mtu, shati langu kubwa lililochomekewa katika suruali pana ulikuwa utambulisho tosha kuwa nimetoka kijijini. Hayo sikujali, kwa sababu niliamini kuwa najua kusoma na kuandika pia naweza kuzungumza Kiswahili fasaha basi lisingeharibika neno.
Nikajifanya mjinga na kuuliza huku na kule hatimaye nikakipata chuo chenu.
Chuo kikanipokea kwa namna ya kusahangaza, nikataka kufumba macho lakini nikawakuta wenzangu wakiyakodolea macho mapaja yaliyoanikwa nje na asilimia kubwa ya wasichana, wakati nataka kuduwaa kuhusu nywele za bandia katika vichwa vya akina dada mara nikakutana na wengine wakiwa wameyaanika matiti yao nje. Walikuwa wanacheka kama hawayaoni, na waliponipita nikaona jinsi wanavyoshindana kutikisa matako yao.
“Mungu wee!! Maria wangu ameweza vipi kuwavumilia watu hawa….” Nilijiuliza huku nikiendelea na msako wa kumshangaza Maria, nilikuwa nimenunua kanga na vitenge, gauni kubwa refu kwa ajili ya Maria. Nilikumbuka pia kumnunulia nguo za ndani kwa kumkadiria kiuno chake cha enzi hizo.
Niliulizia juu ya Maria na bado sikumpata, niliambiwa kile chuo kina Maria kama mia hivi.
Nikajihifadhi mahali na kumkodolea macho kila anayepita mbele yangu, sasa sikuyaonea aibu matako na matiti yao, mapaja pia sikuyaogopa.
Majira ya saa mbili usiku nikaiona sura ya Maria ikiwa katika mavazi yale ya ajabu, matiti yake yalikuwa makubwa sana, mapaja yalikuwa wazi na matako yake yalizidi kipimo. Nikanyemelea kwa wasiwasi nikamfikia na kuita kwa wasiwasi.
Naam!! Ukageuka Maria, hakika ulikuwa wewe, ajabu hukushtuka badala yake ulishangaa. Rafiki zako wakakuuliza huyu ni nani, na ukasema tumesoma wote shule ya msingi hakuna la ziada.
Kila mmoja alinishangaa Maria! Ni wewe pekee uliyetakiwa kunifanya niwe na amani lakini hukudiriki kunitetea, nilizomewa sana. Na mara akafika mwanaume aliyevaa hereni katika sikio lake akakutwaa, mkaitana majina ya kimapenzi. Mkakokotana mkishikana viuno.
Maria nilistaajabu sana, niliumia sana na kujihisi sina thamani yoyote ile, ni kama ilikuwa ndoto lakini nd’o uhalisia uliokuwepo. Maria haukuwa wewe niliyekuzoea wakati ule, haukuwa wewe niliyekutwisha maji kisimani. Na wala haukuwa wewe niliyekuwa nakutembelea shuleni.
Siku hiyohiyo nilinunua simu na baadaye nikakupigia, uliisikia sauti yangu na kuitambua. Ukaniambia kuwa wewe ni mchumba wa mtu, na hukutaka maongezi zaidi ya hapo. Ukakata simu kisha ukanipigia tena, nilipopokea alikuwa ni mwanaume, akanikanya nisitishe mawasiliano nawe. Na mara akanitukania mama yangu!! Nikakusikia pembeni ukicheka.
Unakumbuka vyema kuwa nilikupigia baada ya siku mbili na hukupokea simu yangu!! Ukanitumie ujumbe kuwa nakusumbua, basi nilikuwa na shida ya kukueleza kuwa yule mama aliyelilia mjukuu tangu zamani hatimaye alikuwa amekufa bila kumuona mjuukuu wake.
Tazama nilivyokuwa mjinga mimi!! Tazama nilivyokuwa hayawani!! Nililazimika kumzika mama yangu huku nikiona haya kuyaaga maiti yake, ni kama alijua siku moja niajuta kuwa na wewe, hakika nimejuta. Yaani miaka yote ya kusubiri mwisho umenisaliti na kuniaibisha mjini??? Nimeamua kukuandikia kwa sababu utasoma na usiposoma wewe atasoma Maria mwingine, muongo, mnafiki na msaliti kama wewe.
Ukiwa unamalizia kuisoma tambua kuwa niliathirika kisaikolojia, nikajikuta namuona kila msichana kama Maria, walipojipendekeza kwangu nilifanya nao mapenzi na kisha kuwatupilia mbali, nikidhani nkuwa nakukomoa huko ulipo kwa kuwakomoa hawa.
Nilifanya kwa fujo huku sura yako ikigoma kufutika katika kichwa changu. Na hadi kufikia hatua hii napenda kukuambia neno moja ambalo linaniumiza sana… Sijawahi kukusamehe, na bila wewe kunitenda vile huenda ningeweza kuishi miaka mingi zaidi, lakini mimi ni wa kufa tu!! Maria kwa maovu yote uliyonifanyia, na kwa kisasi kibovu na cha kipuuzi nilichojaribu kulipa. Nasikitika kuwa kusema neno hili na liishi nawe daima. “MARIA bila wewe nisingeukwaa UKIMWI…..nimeukwaa kwa sababu yako!!! Na ulaaniwe kwa adhabu hii uliyonipa mimi na kizazi changu!!!”
0 Comments