Nipende kuwakaribisha tena muda huu wa wakubwa (18+). MAIMUNA KISHIMUNDU ndio jina langu la kikungwi. Nimefurahi sana siku ya leo kupata nafasi hii adimu ya kuzungumza nanyi wapendwa wangu. Mimi wala sina maneno mengi mtoto wa watu, kuna jambo moja muhimu sana kwenye mahusiano watu wanawake wanakosea, "KAULI"
Naanza na wanawake kwasababu wamepewa jukumu kubwa sana duniani juu ya watoto na wababa. Naomba mnisikilize kwa makini sana maana elimu hii ni bure jamani. Kuna mambo matatu tuzingatie sana kwenye kutoa KAULI
1. KAULI KWA MTOTO
Bibie, tambua kuwa ubongo wa mtoto ni kama karatasi nyeupe, unachokitamka kibaya kinajiandika na hakitoki. Ni kazi kubwa sana malezi ya mtoto lakini kumbuka kuwa hatuwezi kupewa sifa nzuri kwa kazi nyepesi. Mdomo wako utumie vizuri kwa mwanao, na chunga asikusikie ukiongea na watu wengine stori za ajabu. Wamekuja wageni unashangaa na mtoto wako yupo sebuleni anasikiliza mnachoongea ni tabia mbaya sana. Wanawake wenzangu tujitahidi kujenga kizazi bora cha baadaye.
2. KAULI KWA MAJIRANI
Umbea, utatupeleka motoni wanawake, mwanamke anayejielewa huwa wa namna hii, haongei kidogo wala haongei sana. Fikiria kwanza kabla hujaongea, breki za mdomo zifanye kazi bibie. Lakini, sijakwambia uwe mpole, utaonewa sana. Jua wapi pa kupandisha sauti yako na wapi pa kushusha, utaishi vyema sana. Kauli mbaya kwa majirani zinaweza kukufanya udharaulike wewe na mumeo pia, hata muda mwingine kuonekana wa tofauti sana.
3. KAULI KWA MUMEO
Wanawake tumeharibika na haya mambo ya usawa, hata siku moja tambua huwezi kushindana na mwanaume. Ukijaribu kushindana naye utajikuta unaharibu mambo mengi na kuwaadhibu wasio na hatia(watoto). Pia tukirejea upande wa pili, mwanaume kama mtoto, anatakiwa abembelezwe na apewe maneno matamu kila muda, usikurupuke kuongea jambo kama huna uhakika nalo, jua muda sahihi wa kuongea na mumeo. Hivi unajua kama kuongea na mtu kunahitaji akili nyingi sana! Na ndio maana tuna watumiaji vibaya wa maneno(matapeli) wa mapenzi na wa mali. Maneno yanajenga pia yanabomoa, inategemeana na matumizi yako. Mtunze mumeo kwa kauli nzuri ili apawaze nyumbani kila muda
MUHIMU: Usihisi ni mwanamke tu ndio mwenye majukumu hayo, kwavile wewe kidume basi ndio itulie tu. Mwanaume pia unatakiwa kuchunga mdomo wako kwa watoto, mkeo na kwa majirani pia. Nimemzungumzia sana mwanamke kwasababu kwa upande wa watoto ndiye anayekaa nao kwa muda mwingi, kwa upande wa majirani, ndiye kiungo kikubwa cha kuleta sifa ndani ya familia na kuboresha mahusiano mema kwa majirani.
Kauli nzuri haziishii maeneo hayo tu, pia hata njiani jamani tujitahidi, Lakini kumbuka kuwa watu wanakera tena sana, kwahiyo shika hili... BORA KIMYA KULIKO KUONGEA VIBAYA.
0 Comments