Header Ads Widget

Responsive Advertisement

LIDAKE TENA CHOZI LANGU - 1

Image result for MY TEARS



Simulizi : Lidake Tena Chozi Langu
Sehemu Ya Kwanza (1)


Mungu akulaze pahala unapostahili Judith!! Najua wazi kuwa laiti kama ungekuwa hai leo hii basi huu ungekuwa wakati wako wa kupoteza uhai kutoka na uchungu ambao ungepitia. Uchungu uleule uliokuwa ukipitia tangu tulipokuwa watoto wadogo, wanmafunzi waliponiita kwa jina baya kabisa la Zeruzeru ulichukizwa na licha ya kwamba ulikuwa msichana ulijaribu uwezavyo kunipigania na mara nyingi ulishinda. Walipokushinda kwa nguvu uliwashinda kwa maneno!!
Laiti kama wangepatikana watetezi mia moja kama wewe Judith huenda pasingekuwa na simulizi hii.
Naam! Ingetoka wapi sasa wakati pasingekuwa na tofauti kati yetu sisi Albino na wenzetu wanaoamini wamebarikiwa na Mungu anawapenda sana kwa kuwapa ngozi hizo!!
Mungu hana upendeleo hata kidogo jama!! Alivyokuumba hivyo usijihesabia kuwa wewe ulipendwa zaidi, kamwe Mungu haumbi kiumbe asichokipenda!!
Looh! Judith ulikufa mapema sana Judy!! Ulikufa wakati ule hata mauaji haya hayajawa kitu cha kawaida!!
Ninapoyasimulia haya naamini roho yako ipo hapa ikitiririkwa machozi na kutapatapa kwa hasira kali!
Nayasimulia haya kwa kuanza na jina lako Judy. Naamini Judy ulikufa wakati ambao haukustahili kufa!!
Eti ulikufa kwa homa kidogo tu mara ikawa homa kali na hata hospitali hukufika!!
Nimeanza nawe Judy katika simulizi hii!!
Mungu aipumzishe nafsi yako pema lakini walau aiamshe sasa na kuipa nafasi ya kuisikiliza simulizi hii mwanzo hadi mwisho!!
Nakupenda Judy!!!
*****
Mnamo mwaka 1996 nikiwa darasa la kwanza ndio kwa mara ya kwanza kabisa nilipiotambua kuwa palikuwa na tofauti kati yangu mimi na watoto wengine pale darasani.
Mama yangu hakuwahi kuniweka wazi kuwa nilikuwa nina tatizo la ugonjwa wa ngozi lakini shule ilinuipa majibu!!
Shule nzima ni mimi pekee nilikuwa albino.
Nilikuwa sina rafiki hadi pale alipohamia shuleni kwetu msichana aliyeitwa Judith!!
Sijasahau kitu hata kimoja katika simulizi yangu, miaka saba niliyokuwanayo inatosha kabisa kukumbuka kila kitu.
Ninakumbuka hadi maonyo ya mama yangu, kuna kipindi aliwahi kuniita na kuzungumza nami!!
Alinieleza kuwa kuna fununu zinatapakazwa na imekuwa mazoea kabisa kuwa eti ni jambo la kawaida kabisa kwa Albino kupotea hasahasa ukifika wakati wao wa kuaga dunia!!
Naikumbuka sauti ya mama ambaye alinieleza kuwa baba yangu alimkimbia baada tu ya kunizaa mimi nikiwa albino!!!
“Mwanangu Majaliwa nilimuomba Mungu sana na Mungu hadanganyi kamwe, Mungu akanijibu kuwa alinipatia mtoto na huyo mtoto ni wewe. Wewe ni mwanadamu kama wanadamu wengine, Majaliwa!! Nilikuwa jasiri sana baba yako alivyonikimbia na wewe jifunze kuwa jasiri pale ambapo watu watakukimbia. Nitakusimamia mwanangu, utasoma hadi utamaliza chuo kikuu sawa mwanangu”
Naam! Sijaisahau sauti ile ya mama, sauti inayozungumza katika masikio yangu hadi leo hii!!!
Yale maneno ya mama yakaanza kutimia, wanafunzi wakaanza kunitenga. Wakajiweka mbali nami kasoro Judith tu!!
Naumia sana msikilizaji, naumia kwa sababu Judith alikufa akiwa bado namuhitaji sana!!
Ila nisilalamike sana isijekuwa nafanya kufuru!!!
Nilifanikiwa kumaliza darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza!!
Nilikutana na changamoto zilezile…. Lakini kwa kutoka kwa wanafunzi hazikuwa na matatizo kwangu kwa sababu mama alikuwa akinitia moyo kuwa wananichukia kwa sababu nilikuwa na uwezo mkubwa sana darasani kuwazidi.
Maneno ya mama yalikuwa yakiniimarisha sana!!
Lakini sikuweza kuwa imara pale mwalimu wangu wa darasa siku ile nimechelewa kufika darasani wanafunzi wakiwa kimya kabisa akanitamkia maneno ambayo kwa mara ya kwanza yalianza kunipa mashaka katika maisha yangu na hapo nikaitazama ngozi yangu mara mbilimbili. Hadi ninaposimulia haya nakiri kuwa sijawahi kumsamehe Yule mwalimu!!!
Yule mwalimu aliniambia kwa dharau kubwa kabisa.
“Jichunge sana kuchelechelewa huku watu tunakutafuta sana wewe tuepukane na haka kamshahara kadogo ka ualimu!!” maneno yake yaliniingia na nikayashika kama yalivyo.
Yalikuwa maneno magumu kuyaelewa na mama alikuwa ameniambia kuwa kila nikiambiwa maneno nisiyoyaelewa nisiste kumweleza. Nikaenda kumweleza mama kauli ile ya mwalimu wangu!!
Mama alihema juu juu, akajaribu kuongea hakuweza, akabaki kutupa mikono huku na kule…. Neno pekee aliloweza kutamka ni ‘yaani….. yaani…’ hakuweza zaidi akaanza kulia. Ni hapo nikatambua kuwa kauli ya Yule mwalimu ilikuwa kauli mbaya.
Mama hakulilazia damu, siku iliyofuata tukaenda wote shuleni hadi kwa mkuu wa shule!!
Akamweleza mashtaka yale!!
Ajabu mkuu wa shule hakuonekana kushtuka!! Akamtazama mama kasha akamuuliza.
“Mwanamke ni hili tu limekuleta?”
Mama akabaki kushangaa. Yule mwalimu akaendelea tena.
“Mama tena bora umekuja mwenyewe, kwa sababu nilikuwa nimepanga kukuita!! Na ninapenda kutoa onyo mbele ya mtoto wako, mama hapa shuleni ni mtoto wako pekee ambaye ana hali hii… sasa nakwambia mama ni ama umtafutie uhamisho lakini ikitokea shule yangu inapata matokeo mabovu basi utanijua mimi ni nani??” alizungumza kwa ghadhabu kasha akatoka nje na kutuachia ofisi.
Nilimtazama mama yangu akiwa na kanga yake iliyochakaa akikosa la kufanya. Akageuka na kunitazama nikayaona machozi yakimtoka mama yangu ambaye alikuwa yu mweusi kabisa si kama mimi.
“Majaliwa mwanangu, Mungu ananiweka hai hadi sasa ili nikulinde, kama baba yako mzazi alikukataa watu baki kama hawa wanashindwa nini kukukataa, shule zipo nyingi mwanangu na hawa wanakuchukui kwa sababu tu una akili kuwazidi. Utasoma mwanangu utasoma!!” alizungumza mama huku nikimsikia kuwa alikuwa analia!!
Chozi la mama likanidondokea katika utosi wa kichwa changu, likanisisimua nami kujikuta ninatokwa na kilio huku nikimkumbatia mama yangu kwa nguvu zaidi!!!
Mwalimu mkuu akafika na kutuamrisha tutoke ofisini kwake!!
Siku iliyofuata sikwenda shuleni bali niliongozana na mama hadi kwa mkuu wa wilaya. Mama akajieleza vyema kuhusu maneno makali ya mkuu wa shule na Yule mwalimu wa darasa.
Mkuu wa wilaya hakuwa muongeaji sana. Akaandika barua na kuifunga katika bahasha na kisha akamwambia mama kuwa siku inayofuata aifikishe barua shuleni.
Barua ile ikawa mwisho wa mwalimu mkuu ya Yule mwalimu mwenzake kunitamkia maneno mabovu!!!
Hadi namaliza kidato cha nne hapakuwa na matatizo sana na hiyo ilikuwa ni mnamo mwaka 2006!!
Ilikuwa heri nikachaguliwa kujiunga kidato cha tano.
Nikachagulia kwenda shule iliyopo kanda ya ziwa!!
Siichukii kanda ya ziwa hata kidogop na ninawapenda sana watu wa kanda ya ziwa hadi ninapousimulia mkasa huu lakini napenda kuwaeleza waziwazi bila kificho kuwa ni hapohapo kanda ya ziwa mikono ya albino wenzangu ilikatwa, sehemu zao za siri zilikatwa tena bila ganzi, naumia sana naumia kwa sababu niliona kwa jicho langu!!!
Niliona miguu ikikatwa, nilipata bahati mbaya zaidi kushuhudia jicho la mwanadamu ambaye hajakata roho likinyofolewa!!
Walionyofoa walikuwa wakitabasamu na bila shaka walijiona watu waliobarikiwa sana kupata bahati ile ya kuvipata viungo vya albino!!!
Zikipitishwa sura zao hapa hao wauaji hata wawe wamezeeka vipi naapa kwa jina la Mungu aliyeniumba….. naapa nitawakumbuka!! Akili yangu haijawahi kuwasahau!!!
Kanda ya ziwa iliimeza damu ya wenzangu wengi tu!!!
Siichukii kanda ya ziwa lakini walaaniwe waliothubutu kututenda vile!!!
Ni huku nilipochaguliwa kujiunga kidato cha tano na cha sita!! Nilikuwa sina wasiwasi lakini mama yangu alikuwa na mashaka tele. Aliniambia kuwa nilikuwa nimekomaa akili basi nijifunze jinsi ya kujilinda!!
Nilikuwa muoga sana kuchinja kuku, mama akanilazimisha niwe nachinja kuku. Nilipomuuliza ni kwanini ananilazimisha alinifokea.
“Yaani wewe wanaweza wakatokea majambazi hapa wakanipiga halafu wewe una kisu ukashindwa kupambana nao”
Hayo yalikuwa ni maneno ya mama yangu mzazi!!!
Maneno ambayo ilifika siku nikaijua maana yake!!
Kumbe mama hakutaka tu kuniambia waziwazi kuwa wapo watu wabaya sana duniani!!
Kule Kanda ya ziwa, nasikitika kuwa sitautaja huo mkoa moja kwa moja. Sihitaji uuchukie mkoa ule bali wachukie wale wauaji!!
Nilisoma pale kidato cha tano nikamaliza salama kabisa, mama alijitahidi kuniandikia barua mara kwa mara na ikafikia hatua akanunua simu yake ya kwanza ya mkononi kwa ajili tu ya kuwasiliana na mimi.
Alinisihi sana niishi kwa tahadhari. Maneno ya mama yalijikita katika kichwa changu vyema.
Kitu kibaya ni kwamba sikuona nini maana ya zile tahadhari sasa ikiwa sijaona baya lolote likikaribia kunitokea.
Amakweli mdharau mwiba mguu huota tende asilani!!
Na ni heri nusu shari kuliko shari kamili.
Nilipomaliza kidato cha sita nikajiona ya kuwa mimi nimekuwa mtu mzima. Ile kujichanganya na watu wasiokuwa na ulemavu kama mimi nikajiona nipo sawa kabisa. Sikujua hata kidogo kuwa baya hujificha likisubiri ukosee maelekezo ndipo liibuke.
Maisha magumu ya mama yangu yakanifanya nijione mpuuzi sana kuendelea kukaa nyumbani nikiyasubiri matokeo ya kidato cha sita. Mama hakuuchukulia uwepo wangu nyumbani kama tatizo badala yake alifurahia kuwa amekuza mtoto.
Maneno ya marafiki yakaanza kuibomoa akili yangu, wakanisifia kuwa nilikuwa najua sana somo la hesabu hivyo nitafute shule niwe nafundisha kwa muda ili nimsaidie mama yangu.
Nilipomwambia mama akanipinga vikali sana akaniambia nikae nyumbani.
“Majaliwa mwanangu wewe ndiye mwanangu wa pekee, tangu baba yako anikimbie unajua wazi kuwa sijawahi kuolewa tena. Kaa mwanangu tutakachopata tutakula pamoja, bado unahitaji uangalizi wangu majaliwa we kaa tu usijali!!” mama alinisihi lakini sikuelewa nikalazimisha hatimaye akakubali.
Sikuwa na ujanja wa kutafuta shule mimi mwenyewe, wale marafiki wakanieleza kuwa yupo mtu ana shule yake anahitaji waalimu. Wakampatia mtu Yule namba ya mama ili waweze kuwasiliana naye niweze kwenda kufundisha shule yake!!
Sitazisahau nyakati hizo kamwe!!!
JIFUNZE: IMANI ni kitu bora katika ulimwengu huu na ulimwengu wa kiroho. Lakini jichunge sana usimwamini mtu sana kutokana na maneno yake, jifunze kwanza mienendo yake kabla haujaamua kuamini maneno yake…
Kosa moja tu katika kuamini linaweza kubadili ukurasa mzima wa maisha yako!!!!

******************

MAMA alipigiwa simu na watu hao asiowaelewa wakajitambulisha kwa majina yao na vyeo vyao walitaja vyeo vigumu vigumu ambavyo mama hakuweza kuvishika ipasavyo!!
Wakadai kuwa sifa zangu wamezisikia kutoka mbali wakaitaja shuleni niliyokuwa nasoma.
Na hatimaye wakamweleza mama kuwa wanahitaji kufanya kazi na mimi!!
Wakati huo wote nilikuwa pembeni nimejilaza katika bega la mama yangu nikizichezea nywele zake mbele palikuwa na mafiga tukiwa tunaota moto.
Mama aliwauliza maswali mawili matatu kubwa aliwauliza juu ya usalama wangu, wakamtoa hofu kabisa kuwa kama itakuwa vyema basi mwakilishi wao anaweza kufika nyumbani. Kisha wakaongezea kuwa hata wao wanaelewa changamoto ambayo inalikabili taifa letu kuhusiana na watu wenye ulemavu wa ngozi!! Yaani albino!!!
MANENO yao yakamlainisha mama akawakaribisha nyumbani!!
Wakaahidi kufika baada ya siku mbili.
Kweli ugeni wa wanaume wawili nadhifu kabisa ukafika nyumbani kwetu baada ya hizo siku mbili.
Walikuwa wachangamfu sana na kwa kiasi kikubwa walikuwa wanaonekana kujali sana, wakanishauri mambo mengi sana huku wakimpongeza mama yangu kwa kunizaa kunilea lakini kubwa zaidi kwa kunilinda hadi umri ule niliokuwanao.
Lugha zao zilikuwa nadhifu kama wao, walipoondoka wakamuachia mama kiasi cha shilingi elfu thelathini!!!
Mama akatabasamu huku akizipokea pesa zile.
Tabasamu lile likamaanisha kuwa alikuwa amekubali.
Ama kwa hakika usilolijua lina tofauti gani sasa na usiku wa kiza kinene!!!
Naam! Tulikuwa gizani!!
Baada ya siku tatu wale watu wakafika na kunichukua, nilipofungasha mzigo wangu mdogo ndipo nilipogundua kuwa nilikuwa nampenda sana mama yangu nilimkumbatia na nikayasikia maneno yake mengine.
“Fanya kazi mwanangu uheshimike, ukishakuwa na pesa watajifanya hawaioni tofauti yako na hatimaye sote tutakuwa sawa. Wewe si shetani, wewe si mchawi wewe si jini Majaliwa, wewe ni mwanadamu. Uliwakomesha shuleni wao waliongea wewe ukatenda, sasa ni wakati wa wewe kufanya kazi kwa bidii watakaa kimya tu!! Laiti ningekuwa na uwezo kifedha nisingekuruhusu uondoke mwanangu, ningebaki kuwa mlinzi wako daima. Ila sasa namuachia Mungu… akulinde uendapo awe nawe daima!!!” alipomaliza kuzungumza yale akaniachia kisha akanisogelea na kunibusu shavuni kisha akanibusu paji langu la uso!!!
Sikujua kabisa kuwa mama alikuwa ananiaga, ninapokusimulia haya natamani siku zingerejea nyuma tena na kamwe nisikubali kuandamana na watu wale huku nikiwa tayari kuwa mbali na mama yangu.
Mwanadamu mwanadamu mwanadamu!!!
_____
Tuliondoka na siku ile nililala hoteli nzuri sana, nilijitazama na kuyaona matunda ya kusoma kwangu yaani elimu ya kidato cha sita tu tayari nimeshaanza kuheshimika!!
Lilikuwa jambo la kupendeza sana.
Nilifurahia hali ile ya kutukuzwa nikayakumbuka na maneno ya mama na kujiapiza kuwa nitafanya kazi kwa bidii sana hadi niheshimike.
Nililala huku nikiwa nina furaha kubwa!!
Asubuhi tuliianza safari kuelekea kanda ya ziwa. Tulikuwa katika gari binafsi lakini safari hii nilikuwa na watu wengine tofauti kabisa.
Wale wawili wa awali walidai kuwa wana mkutano na waalimu wengine hivyo nitangulie na watu wale.
Safari ilianza vyema!!
Nilikuwa mkimya nikiwatazama tu wenyeji wangu wakibadilishana mawazo, tulizidi kuchanja barabara nikiwa natamani tufike upesi. Nilipata nafasi ya kuwaza juu ya mshahara wangu wa kwanza kabisa. Nilipanga mshahara wote nimpatie mama yangu, na pia niliwaza kununua simu yangu ya kwanza ili niwe nazungumza na mama yangu.
Yalikuwa ni masaa kadhaa tu tangu niachane naye na tayari nilikuwa nimeukosa uwepo wake kwa hali ya juu sana.
Baadaye mwendo wa gari ukawa unapungua na hatimaye gari lilipaki pembeni. Wakaanza kujadiliana juu ya ubovu wa gari lile!!
Niliwasikia wakizungumza na kwa mbali nikazisikia dalili za kulala njiani.
Nilitamani isiwe kama nilivyowasikia lakini ilikuwa vile ilikuwa hakuna safari iliyokuwa inaendelea pale tulitakiwa kulala kwa sababu hapakuwa na namna yoyote ya kufanikisha safari ile. Nilitamani kusema neno ambalo lingeweza kubadilisha maamuzi yale lakini sikuwa na neno lolote la kushauri, sikuwa najua jambo lolote lile kuhusiana na magari.
Basi kwa shingo upande nikajipa moyo kuwa kila jambo huja kwa sababu maalumu huenda tungesafiri usiku ule tungeweza kupata ajali ama lolote baya.
Nikiwa nasubiri kupewa utaratibu nikaona si mbaya ikiwa nitaanzisha maongezi walau niijue sehemu ninayoenda niyajue mazingira ya kule ili niwe tayari nikifika nisionekane mgeni sana.
“Aah! Samahani kaka hivi hiyo shule kuna wanafunzi wengi eeh!” nilimuuliza. Hakunijibu upesi badala yake alikuwa kama anayenishangaa.
Nikauliza tena nikidhani hajanisikia vizuri.
Badala ya kunijibu akanitupia swali.
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Majaaliwa kwani hawakuwaambia jina langu, hawakuwaambia kama mimi ni mwalimu naenda kufundisha somo la hesabu?” niliwauliza katika namna ya kuwashangaa.
Badala ya kunijibu niliona wawili wakivutana pembeni na kuanza kuteta sikujua walilokuiwa wakizungumza.
Baada ya dakika kama moja hivi wawili wakarejea na kunikabili.
“Aaah! Umesema unaitwa Mwalimu Majaaliwa, sasa tuna tatizo la gari na inabidi tulale tu njiani hadi kesho tena kuna kifaa tumeagiza kitafika asubuhi hivyo tutaendelea na safari.” Alizungumza bwana yule nami nikatikisa kichwa ishara ya masikitiko.
Baadaye kiza kilivyotanda kabisa tukapangiana namna ya kulala.
Kiuwazi kabisa ilionekana kuwa tusingeweza kulala katika gari lile. Basi ikaletwa hoja ambayo ilinifadhaisha sana, hoja ambayo ndani yake ilionyesha kutengwa!!
“Sasa Majaaliwa kama unavyojiona wewe una matatizo, tumekutafutia hifadhi hapo kijiji cha jirani utalala hapo na asubuhi tutakutana hapa. Haiwezi kuwa salama kabisa kulala katika eneo hili sawa!!” hakusubiri nitoe jibu lolote akamchagua bwana mmoja akanishika mkono tukaondoka huku nafsi ikiwa haijaridhia kabisa.
Hakika tuliifikia nyumba moja nikakaribishwa na kisha kupewa maji nikaoga na baada ya hapo nikapatiwa chumba ambacho nilitakiwa kulala.
Katika chumba kile alikuwa amelala mtoto mdogo kama miaka sita ama nane kimakadirio.
Nilijilaza kitandani, nikajaribu kusinzia lakini usingizi haukukubali kabisa. Nikajaribu kujigeuza bna hapo nikajikuta nimemuamsha yule mtoto.
Pale ndani kulikuwa na mwanga kiasi fulani kwa sababu ile ilikuwa ni nyumba isiyoezekwa vyema basi mbalamwezi ilipenyeza mwanga wake.
Kile kitoto kikaamka na kupekecha macho yake kisha kikaketi!!
“Shkamoo mzungu!!” kikanisalimia… hata kabla sijajibu kikaendelea.
“Halafu wewe jana ulinidanganya ukasema utarudi haujarudi, haya machungwa yangu nataka!!”
Nilimtazama nikahisi itakuwa ni ndotoni tu.
“Haya lala kesho ntakupa!!!” nilimweleza nikidhani atalala. Haikuwa hivyo mtoto alikuwa anajitambua kabisa.
“Halafu mzungu lile swali lako lile nimeliweza sasa..” akazungumza huku akishuka kitandani akaenda na kuchukua mfuko wake. Akatoa daftari, kweli nikakuta kuna swali alikuwa ameandikiwa na alikuwa amejaza jibu.
Hisia bado zilikuwa mbali kufikiria kuwa yule mtoto kuna kitu cha msingi sana nilitakiwa kujua kutoka kwake.
“Yaani nyie mkiondoka hamrudi, halafu waongo nyieee we jana ulinidanganya wewe ni mwanamke huyoooo nimejua!!” mtoto aliongea huku akiwa ananichungulia.
Hapa akili ikasogeleana kuwa siku iliyopita ama hata kama sio siku iliyopita basi siku kadhaa nyuma kuna msichana ama mvulana mlemavu wa ngozi aliwahi kupita na kulala pale.
“Mimi mwanaume bwana…..” nilimwambia.
“Sasa mbona uliniambia wewe mwanamke sijui wewe mwalimu unaenda shuleni huko. Tena … tena ehee ngoja…” kakaruka kale katoto na kufukua nguo zake akatoka na picha.
Naam!! Ilikuwa picha ya msichana mwenye ulemavu wa ngozi!! Kama mimi.
Moyo wangu ukapiga kwa nguvu sana.
Wale jamaa waliniambia kuwa pale shuleni hakuna mwalimu mwenye ulemavu wa ngozi tena wakasema mimi ndio wa kwanza kabisa sasa ile picha ilikuwa na maana gani!!
Sikutaka kuionyesha ile hofu waziwazi kwa mtoto yule nikajilazimisha kutabasamu lakini moyo wangu ulikosa amani kabisa na hakika nisingeweza kulala pale.
Lakini hata kama nisingelala pale ningeenda kulala wapi, walau basi yule angekuwa ni mtu mzima nimuombe ushauri tatizo yule alikuwa ni mtoto mdogo.
“Kwa hiyo huyu dada yupo wapi?” nilimuuliza.
“Alinitoroka nikiwa nimelala huyo.” Kalinijibu huku kakiwa kanalegeza macho yake ishara ya usingizi.
Na baada ya jibu hilo kikasinzia kitoto kile.
Nilisimama na kuanza kutapatapa pale ndani sikujua ni wapi ambapo naweza kukikmbilia machale yalikuwa yamenicheza kulikuwa na sintofahamu.
Nilitambua kuwa iwapo nitaamua kulala basi hii inamaanisha kuwa nikiamka nitakuwa katika wakati mbaya zaidi.
Nikaufungua mlango taratibu kabisa. Nikatazama huku na kule eneo lilikuwa tulivu sana.
Nikapiga hatua mbele na kisha nikazitazama anga nikamwomba muumba wangu.
Nilimwambia neno moja tu.
“Baba ulinipa uhai ukazijaza pumzi katika mwili huu ukaupa na ulemavu, baba wewe hukosei katika kuumba baba uliamua ile roho na pumzi kuziweka katika mwili huu. Mwili wako upo matatani baba wanaitaka roho yangu!!! Nipiganie sasa…”
Wakati namalizia kusema hayo mara nikasikia mbwa wakibweka.
Nikafanya kosa nikajaribu kukimbia!!
Mbwa wawili wakawa wananibwekea huku wakinikimbiza kwa kasi sana.
Nilianza kukimbia na kamwee nisijue ni wapi naelekea na niliwasikia mbwa wakizidi kukikaribia.
Kwa mujibu wa saa yangu ya mkonomni ilikuwa yapata saa nane za usiku. Katika kijiji nisichokijua kabisa!!!
Naam! MAJALIWA amechezwa machale na kuamua kukimbia amegundua kuwa wale si watu wazuri hata kidogo.
Je nini kitatokea na sasa anakimbizwa na mbwa usiku wa manane.
JIFUNZE!!!
KILA mwanadamu kuna ishara huwa anapewa linapokuja jambo ambalo ni hatari kwake. Wazo hili ama ishara hizi huitwa MACHALE!! Jitahidi sana kuheshimu hisia hizo… wakati mwingine zinasaidia sana!!!!

***********************

MBWA walizidi kunikimbiza na wala sikupiga hatua nyingi zaidi NIKAJIKUTA napiga mweleka chini. Mbwa walikuwa wamenifikia, mbwa mmoja aliyekuwa mkubwa zaidi alinikwangua na makucha yake katika paja langui nilipiga kelele kuomba msaada maana kukaa kimya ningeweza kujisababishia balaa zaidi.
Ni heri ningekaa kimya!!
Lakini ningekaa vipi kimya wakati mbwa walikuwa na lengo moja tu la kunidhuru!!
Nilivyopiga kelele wakazi wa ile nyumba niliyokuwa nimepelekwa kulala wakatoka nje upesi.
Lahaula!! Walikuwa ni watu walewale ambao tulikuwa katika safari moja kutokea mjini tulipoachana na wale wageni wawili walionichukua kutoka katika mikono ya mama. Walionilaghai kuwa wao watalala garini na mimi wanaenda kunilaza sehemu salama!!
Hapo sasa nikakiri katika nafasi yangu kuwa hisia zangu zilikuwa sahihi kabisa.
Nikabaki pale chini wakati wale watu wakijongea kunikaribia.
“Mzunguu!!” nilisikia sauti ya kale katoto. Kalikuwa kameamka pia kakiwa uchi.
Aliponiita vile akakoromewa na wale wenyeji wangu ambao awali walisema kuwa watalala garini na mimi nilale katika nyumba ile.
Kumbe sote kwa pamoja tulikuwa tumelala nyumba moja!!
Hawakusema nami jambo lolote badala yake niliwasikia wakihamasishana kuwa wafanye upesi.
Wakafika na kunibeba kisha wakaniingiza ndani, na hapo jamaa mmoja akaanza kuwatukana wenzake akiwaambia kuwa wameharibu dili.
Sikujua ni dili gani walilokuwa wakizungumzia lakini amani sikuwanayo tena.
Mbaya zaidi wale watu hawakuniuliza lolote kuhusu ni wapi nilikuwa naenda usiku ule.
Hali hiyo ilinifanya niumie sana nafsi na kujisikia kama nusu mfu!!!
“Mpake dawa fasta!!” aliamrisha tena yule bwana.
Nikapakwa dawa iliyokuwa inauma sana. Nilijikazaa lakini sikuweza nikapiga kelele. Hilo likawa kosa kubwa sana.
Nikapigwa kibao kikali sana usoni ulikuwa ni usiku hivyo niliziona nyotanyota vizuri.
“Mpumbavu mkubwa wewe…” alinifokea yule bwana wakati huo niliyasikia macho yangu yakichonyota na hatimaye chozi likanitoka!!
Nikayakumbuka maneno ya mama yangu!! Mama yule alikuwa anaona mbali sana!!
Baada ya tiba ile wakazungumza pembeni kisha wakanichukua na na kunivuta kuelekea mahali. Sikujua ni wapi lakini sasa nilikuwa nawasihi wanisamehe tu bila kujua kosa langu ni lipi!!!
Hawakujibu chochote.
Tulipofika eneo la nyuma ya nyumba bwana mmoja alinichota miguu yangu. Halafu kwa jinsi walivyojipanga na kwa namna walivyo na uzoefu katika shughuli hiyo haramu walinidaka hata sikutua chini.
Na hapo nikauona mfuko nikalazimishwa kuingia katika kiroba kile.
Ndugu zangu, ninayokusimulieni haya endeleeni kuyasikia tu na yabaki katika masikio na akili zenu lakini kamwe msiyapitie kama nilivyoyapitia. Ni magumu sana hasahasa kwa mwanadamu ambaye uliumbwa kwa udongo!!
Sikuwahi kudhani kama ipo siku nitatabasamu na kukubaliana na hali niliyonayo lakini natabasamu sasa!!
Wale jamaa walinishika kwa nguvu na ndani ya dakika moja tu nilikuwa ndani ya kiroba cha chumvichumvi. Nilipojaribu kupiga kelele jamaa mmoja alinizamishia soksi kubwa mdomoni. Ilikuwa inanuka sana jamani!! Lakini iliingia katika mdomo wangu!!!
Na hapo sikuweza kuzungumza na nilikuwa napumua kwa shida sana!!
Nilisema kimoyomoyo kuwa ile iwe ndoto ya ajabu sana nizinduke nipige kelele na mama yangu aje kuniuliza nini kimetokea lakini nilifumba na kufumbua hapakuwa na ndoto pale!!!
Ilikuwa hali halisi Majaliwa mimi nilikuwa katika matatizo makubwa sana, nilikuwa mdomoni mwa kifo!!
Licha ya kunijaza soksi ile mdomoni walikifunga kile kiroba!!!
Wakanibeba nikiwa kama kiroba na safari ikaanza. Niliumia sana kwa sababu kuna muda walinigusa macho kuna muda walibinya tumbo. Hakika niliamini kuwa wakinitoa ndani ya kile kiroba nitakuwa mfu tayari.
Lakini haikuwa hivyo walinifikisha hadi katika gari na hapo walinifungua.
Waliponitoa na kunitupa nuje ile soksi nayo ikachoropoka mdomoni.
Nilitapika vibaya mno, nilihema juu juu huku nikitamani kuongea na sauti haikuweza kutoka!!
Kabla sijakaa sawa walinichukua tena na kunirusha katika gari jingine. Hapo sasa nilitua kwa kutumia mdomo, nikaacha kuchuruzika damu!!
Wale viumbe hawakuwa na huruma hata kidogo!!
Walipanda garini na hapo gari likaanza kuondoka, sikujua hata ni wapi tulikuwa tunaelekea. Lakini njia ilikuwa mbaya sana nilijigonga huku na kule gari lilivyokuwa linarukaruka kwenye mabonde,.
Kadri tulivyozidi kwenda hatimaye mwezi ulitoweka na mwanga ukaanza kutokea. Wale jamaa mwanga ulivyoanza kutokea wakafunika turubai. Sasa hapo tukaanza kuteseka na joto.
Ajabu wale wenzangu walikuwa wanaonekana kutosumbuliwa kabisa na hali ile.
Mimi iliniendesha haswa.
“Jamani kwani ni nini nimewakosea?” hatimaye nilifungua kinywa na kuzungumza.
Badala ya kunijibu yule bwana akainama na kunionyesha soksi nyingine.
Nikajua anachomaanisha nikawa kimya.
Lakini katika ukimya ule nilikuwa nikitafakari sana juu ya kujiokoa. Kwa sababu kuwaacha jamaa katika utulivu waliokuwanao ilikuwa si sawa hata kidogo. Na haikuwa njia ya kuniponya bali kunipeleka machinjioni kirahisi.
Hapa tayari nilikuwa nimetambua ilikuwaje hadi watu wakawa wanaishi na imani kuwa eti sisi walemavu wa ngozi tukipoteza uhai huwa tunapotea tu kwa sababu sio wanadamu wa kawaida!!
Kumbe kuna maharamia kama hawa wanatuteka na kutuua.
Gari lilivyozidi kwenda nikafanya maamuzi magumu na nikabaki kusubiri muda tu!!
Hatimaye gari lilipunguza mwendo.
Nikajirusha upesi nikalifunua lile turubai na kutua nje.
Mungu wangu!! Sikujua kama nilikuwa sehemu mbaya kiasi kile. Kushoto na kulia lilikuwa ni shimo kubwa.
Hivyo pale palijengwa daraja. Nilibaki nimeduwaa baada ya kutua chini, ni kweli sikupenda kufa kifo kibaya cha kukatwa na mapanga lakini hapohapo sikuwa tayari kujirusha katika shimo lile.
Nikajaribu kukimbia lakini sikufika mbali wale vijana wepesi wakanifikia na kunikamata hii ni baada ya kupiga kelele na dereva kusimamisha gari.
Nilitambua fika kuwa nitapokea kipigo kikali sana lakini haikuwa vile. Dereva aliwakataza kabisa kunigusa wakanichukua na safari hii wakanifunga kamba miguuni.
Walinikaza ipasavyo wauaji wale!!
Safari iliendelea kwa mwendo kasi mkali na wakati mwingine mwendo wa taratibu ama wastani sikujua ni wapi tunaelekea!
Baada ya safari ndefu tulisimama nikaachwa garini.
Ni wakati huo ambao nilitambua kuwa nilikuwa nimelalia kitu ambacho kilikuwa kikinichoma sana mgongoni, nikapapasa ili niweze kukitoa ndo hapo nikachomoka na kitu kilichonipa mshtuko ambao ulitaka kuondoka na uhai wangu, yaani muda wote huo wa kuumia nilikuwa nimelalia kiungo cha mwili wa mwanadamu.
Ulikuwa mkono na ulikuwa umegandiana na damu kuonyesha kuwa haukuwa na muda mrefu sana tangu ulipokuwa umekatwa.
Ndugu msikilizaji uliyebarikiwa kuwa na mikono yako yote miwili, jitazame sasa itazame mikono yako, itazame kwa sekunde chache tu kisha fumba macho yako ujiulize.
Ni maumivu kiasi gani utayapata pale ambapo mkono huo utakatwa tena kwa mapanga huku ukiwa unajitazama.
Tumbo liliniuma na kibofu kikajaa mkojo nikajikuta najikojolea palepale.
Hasira kali sana ilinikaba katika koo langu lakini ningefanya nini na ile hasira yangu!!!
Nikachungulia nje na kuzitazama mbingu!!
Sikusema neno bali niliamini Mungu wetu halali kamwe na kila muda yupo kazini nilijua ananiona na unyama ule hakututuma duniani tuufanye!!!
Niliamini Mungu atajibu!! Lakini hapo hapo nikaingiwa na uoga mkubwa sana, nikajiuliza mbona wezi wanaiba hawakamatwi mbona watu wanaua na wanaachwa hai!!
Inamaana Mungu ataniacha nami niteketekee katika mikono ya watu wale wabaya!!!
Naam!! Ni kizungumkuti, wakati mgumu kabisa katika maisha ya MAJALIWA!!
Je ni kitu gani kilitokea baada ya hapo……
Usikose sehemu inayofuata!!!
JIFUNZE.
MAISHA ya duniani ni mafupi sana. Ni kweli kuna watu hawaamini kama kuna maisha baada ya kifo!!
Lakini kamwe Mungu wetu hawezi kukuacha wewe muuaji uishi maisha haya mafupi kwa raha zote hizo.
Hasira ya Mungu isipowaka juu ya koleo piga goti na uombe msamaha kwa sababu wakati unakuja hautapata nafasi ya kuomba msamaha!!!

ITAENDELEA.

Post a Comment

0 Comments