Header Ads Widget

Responsive Advertisement

BINTI YANGU JOANITHA



Maisha ni kama maua, asubuhi huchanua na kufurahisha macho na kisha baadaye hunyauka”. Sikuelewa maana ya msemo huu mpaka siku nilipopoteza binti yangu mpenzi. Joanitha alikuwa msichana mrembo sana, na japo ni binti yangu wa kumzaa, bado naweza sema kwa ujasiri kuwa kwa hakika alikuwa mrembo mno. Msichana mwenye macho mazuri, sura na rangi ndo usiseme, shepu, urefu wa wastani na hata sauti. Ni kama aliumbwa kwa masaa mengi zaidi na kwa hakika alivutia sana.
Yeye kuwa binti yangu wa pekee kidogo ilinifanya nimlee kwa deko na kwa upendeleo. Sikutaka akose chochote alichokihitaji. Wakati mwingine tuligombana na baba yake kwa ajili yake. Hali yetu ya uchumi ilitupa fursa kusomesha watoto wetu shule nzuri za kimataifa, na kwakua Joanitha alikuwa kipenzi changu, basi nilihakikisha haswaa anasoma shule nzuri sana.
Akiwa bado shule ya msingi aliniomba nimnunulie simu, nikanunua, alipotaka kutoka na rafiki zake sikumzuia japo nilimwekea uangalizi, alipotaka pesa ya matumizi sikumpa chache, yani nilifanya kila kitu kuhakikisha anakua mwenye furaha sana. Kwa namna alivyoendelea kukua ndipo uzuri wake uliongezeka, nami kwa kuona hivyo nilimfanya kuwa rafiki wa karibu sana. Nilimjulisha kuwa yeye ni binti mrembo sana kwani sikutaka sifa za watu wengine hasa wanaume, zimzuzue.
Sikujua kwa kumpenda sana na kumsifia binti yangu nilikuwa namtengenezea tabia ambayo ingemgharimu maisha. Kwani kadiri alivoendelea kukua, alianza kuwa na kiburi na alitaka kumuonesha kila mtu kwamba yeye ni mrembo na ana kila kitu maishani. Alikuwa na marafiki wachache lakini wanaotoka familia za kitajiri, aliingia kwenye mahusiano ya mapenzi akiwa kwenye umri mdogo, kwani japokuwa hakunambia, mara chache nilizoshika simu yake niligundua yuko kwenye mahusiano ya mapenzi. Akiwa kidato cha pili, mwalimu wake mmoja aliongea na mimi kwa kifupi siku ya wazazi na kujaribu kunambia niangalie kwa karibu tabia za binti yangu, na japokuwa shuleni kuna uhuru mkubwa juu ya namna mtoto anataka kuishi, lakini yeye kama mzazi hangefurahia kuona mtoto wa mtu akiharibikiwa.
Kama mzazi ni kweli nilijaribu kuongea na Joanitha kumuonya juu ya tabia zake hasa za kuwa na mahusiano, lakini nadhani mapenzi yangu kwake yalinifumba nisijue namna sahihi ya kumuonya. Hilo pia yeye alilijua, na kila mara nilipojaribu kuwa mkali kidogo zaidi, alilia na hiyo ikaninyima ujasiri kuendelea kumuonya kwa ukali. Kuna wakati alinidanganya juu ya kuachana na wapenzi, alinidanganya vitu vingi sana na hakuwa muwazi kwangu kama nilivyotegemea. Alivyozidi kukua mtoto wangu alizidi kuwa na marafiki wa aina na uwezo tofauti, lakini siku zote aliambatana na wale wenye hali nzuri sana za kiuchumi
Baada ya kumaliza kidato cha nne alitaka sana kusoma shule moja nzuri ya kimataifa iliyoko mkoani Arusha, na kwakua hiyo shule ilisifika kitaaluma na pia kwa viwango vya kimataifa, sikusita kumpeleka. Shuleni kila mtoto alilala chumba chake, chenye kila kitu ndani mpaka televisheni yenye DSTV. Kwa kuwa ilikua mara yake ya kwanza kukaa mbali na nyumbani, mwanzoni tuliwasiliana sana. Alipiga simu kila siku na kutuma meseji. Alionesha kidogo hali ya upweke lakini haikudumu hata miezi miwili. Alinambia ameshapata marafiki na kuzoea mazingira, hivyo alipunguza kupiga simu sana.
Mara kadhaa nilisafiri kwenda Arusha kila nilipomkumbuka sana, na japo alifurahi sana kuniona, lakini nilianza kumuona usoni kama siye Joanitha yule mwenye furaha na maringo niliyemzoea. Hakuwahi kunieleza chochote kila nilipojaribu kumuuliza. Nilijaribu kuwa karibu na rafiki zake ili kujua kama kuna jambo ananificha lakini wao pia walikua wasiri sana
Siku moja nilipigiwa simu iliyonistua sana. Joanitha akiwa kidato cha sita mwanzoni, mwalimu wake mmoja alinipigia simu na kuniomba niende shuleni kuna tatizo kubwa limetokea. Alisema binti yangu anaumwa na yuko kwenye hali mbaya lakini nitaelezwa zaidi nilifika. Tulifanya kila tuliloweza na mume wangu kupata tiketi ya ndege ya siku iyohiyo na tulifika shuleni kwao
Binti yangu alikuwa ameuawa akiwa nyumba ya kulala wageni yeye pamoja na mwanaume aliyekuwa naye. Joanitha alianzisha mahusiano na mwanaume mmoja tajiri mkubwa sana Arusha aliyekuwa na mke na mtoto mmoja. Miezi kama mitatu baada ya uhusiano huo, mke wa yule tajiri alijua na alimtafuta Joanitha na kumpa onyo kwa simu. Bahati mbaya yule bwana hakuwa amemwambia kuwa ana mke hivyo hili jambo lilimuumiza sana, lakini kwa vile alivyokuwa tayari anampenda, alipombembeleza, alikubali kumsamehe na waliendelea na mahusiano. Yule mwanamke aliendelea kumuonya mara kadhaa kwa simu lakini baadaye Joanitha alikuwa akimdharau na kumjibu kwa jeuri kwani bwana yule tariji alimuhakikishia anampenda kuliko mke wake
Rafiki zake Joanitha pia walimuongezea jeuri kwani mara kadhaa waliongea na mke halali wa bwana tajiri na kumtukana huku wakimpa maneno ya kashfa. Siku moja Joanitha na yule mwanaume walikwenda sehemu waliyokua wamezoea kukutana hapo mara kwa mara. Ilikuwa ni nyumba ya kulala wageni nzuri sana iliyokua karibu na shuleni kwao. Mara nyingi Joanitha akiwa shule, isipokua wikiendi ambapo walikutania hoteli kubwa za Arusha, walikwenda hapo kulala hivyo walikua wamezoeleka hapo.
Inasemekana kijana mmoja muhudumu wa hapo alilipwa pesa nyingi na kukubali kuuza kadi ya kufungulia chumba walichokuwa wamelala na kisha akatoroka. Usiku wa manane aliingia mtu chumbani mule bila hata kuvunja mlango, aliwafunga vinywa na kuwaua kimya kimya na kisha akaondoka.
Haya yote nilikuja kuyajua baada ya kumzika binti yangu. Mmoja wa rafiki zake baada ya msiba alikaa na mimi na kuniomba msamaha kwa kunificha mambo mengi ambayo labda ningejua mapema ningeokoa maisha yaa Joanitha
Sina tena Joanitha mwingine, naumia na najilaumu sana kama mzazi niliyeshindwa kumkuza mwanangu kuwa mwanamke anayefaa katika jamii. Historia aliyoiacha inanisikitisha kwani hakuwa mtu wa kuwa na mwanaume mmoja. Alitembea na walimu wake na wanafunzi wenzie, na ndiyo sababu mwalimu wake wa kidato cha pili alinionya. Binti yangu amekwenda, lakini nisingetamani mzazi mwingine afanye kosa nililofanya. Ni kweli tunawapenda sana watoto wetu,lakini daima tukumbuke kuwa malezi tunayowapa ndiyo maisha yao ya baadaye
MWISHO

Post a Comment

0 Comments