Header Ads Widget

Responsive Advertisement

ASANTE MAMA WA KAMBO



SIMULIZI FUPI - ASANTE MAMA WA KAMBO


SHAMRA shamra zilizidi kurindima kwa fujo katika ukumbi wa Sabasaba wilayani Temeke, hakika maharusi walikuwa wamependeza na utakuwa mchoyo wa kuzaliwa usingewapongeza waliotumia ubunifu wa hali ya juu kuupamba ukumbi ule nao ukapambika.

Kila mmoja alitabasamu bila kujalisha linatoka moyoni ama ni la kuzugia!!

Wanawake walipiga vigelegele na wanaume walipiga mbinja kila muda ambapo msema chochote aliamuru!!

Naam!! Ilikuwa sherehe ya aina yake ya kuwaunganisha Maria na Christian kuwa mwili mmoja!!!

Chris alikuwa mwenye furaha sana alipopewa nafasai ya kusema chochote, alizishukuru pande mbili akianza na ule upande wa ukweni akawashukuru kwa zawadi ya mke mwema…..kisha akageukia upande wa pili na kuwashukuru wazazi wake waliomkuza na kumpa elimu dunia pamoja na ile ya darasani!!!

Hatimaye msema chochote (MC) akamkabidhi kipaza sauti Maria!!


Ukumbi mzima ulitambua kuwa Maria hakuwa akitabasamu kutoka moyoni lakini bado hakuna aliyejua kwanini alikuwa katika hali ile.

Maria akashika kipaza sauti mbele ya umati na kuanza kuzungumza.

“Imekuwa safari ndefu sana hadi kuifikia siku hii ya leo…nikimtoa mwenyezi Mungu katika safari hii ninaye mtu mwingine muhimu katika dunia hii wa kumshukuru!! Ni mtu mmoja tu nasisitiza pasipokuwa na unafiki wowote!!

Namshukuru mama yangu…mama yangu wa Kambo” akasita kidogo ukumbi nao ukawa kimya!! Kimya kikuu…Maria akaendelea.

“Asante sana mama wa kambo kwa MATUSI YOTE uliyonitukana maana ulinifanya niyazoee, awali nilikuwa nakasirika sana ukinitukana, ukimtukana marehemu mama yangu, ukinitukania baba yangu. Naam ukaniimarisha zaidi hata nilipokuwa nafanya kazi za ndani sikuhangaishwa na matusi kutoka kwa watoto wa bosi wangu!! Niliyapuuzia tu!!! Maana kila tusi ulikuwa umenitusi tayari

Asante kwa KUNILAZA NJE asante sana kwa jambo lile, nikalizoea giza, mbu wakaizoea damu yangu!! Ukaniimarisha na hata nilipokosa pa kulala nikiwa mtaani stendi ilikuwa sehemu sahihi kwangu na nililala bila hofu. Mama wa kambo siwezi kusahau kukushukuru kwa kunilisha chakula ambacho watoto wako walilalamika kuwa ni kibaya ama kimeharibika. Ulikuwa sahihi mama maana hata kule majalalani sikuhangaika tena kila kinachoitwa chakula mimi nilikula. Unadhani ungenidekeza ningeweza vipi?

Siku uliyoamua rasmi kunifukuza ukinizushia kuwa nakujazia choo na kukumalizia godoro bila sababu za msingi ni hivyo hivyo niliwahi kufukuzwa na mabwana wengi walaghai. Lakini sauti zao na yako zilifanana hivyo sikuogopa chochote kitu!! Nikabaki kuwa imara huku nikihesabu kuwa haya ni mapito tu!!

Kulala bila kula kwa siku mbili hadi tatu katika nyumba yako lilikuwa jambo la kawaida sana hivyo niliweza kumvumilia Chriss wangu alipokuwa hana pesa. Alinishangaa sana kwa uvumilivu wangu lakini leo atambue kuwa bila wewe nisingeweza kumvumilia.

Ulininyima elimu mama wa kambo!! Vyema sana ukanifanya niishi kwa kutumia nguvu zangu tu na akili ya ziada lakini si vyeti!! Sikuwa mtu wa kuchagua kazi, nilibeba kokoto, nikafanya ubaamedi, nikafua nguo za watu, nikafagia barabara na kazi zote zile ambazo zilihitaji watu kama mimi nisiyekuwa na elimu!! Asante mama wa kambo!!!

Sijaisahau ile siku uliyonimwagia maji ya moto na kuondoka na ngozi yangu usoni, tazama ulinisaidia sana hakika, wanaume hawakunitamani!! Ndio…nani wa kumtamani na kumthamini mwanamke asiyekuwa na mvuto.

Ulifanya la maana sana mama maana maumivu niliyoyapata kuondokewa na wazazi wangu, maumivu niliyoyapata kwa mateso yako, ni heri hayo yalitosha na ukaniepushia maumivu ya kudanganywa na wanaume wakware kisa uzuri wangu kisha wanitelekeze pasi na msaada. Ni heri waliidharau na kuichukia sura yangu hadi nilipokutana na Chriss. Hakujali sura akayajali maumivu yangu na akaamua kunipooza!!!

Hata lile kovu uliloniachia kwa kunichoma na mkaa wa moto pajani, yeye hakujali pia. Unadhani ni wanaume wangapi wanaweza kuwa na ujasiri wa Chriss??

Nasema nawe ewe mama uliyevaa nguo nyeupe pee!! Umeketi katika kiti cha tatu kutoka kushoto, mama usiyekuwa na haya uliyenitukana huku ukisema kamwe kuwa sitaolewa!! Nimezisikia tetesi kuwa wale wanao wawili wa kike uliowabatiza cheo cha umalikia walijazwa mimba na kuzaliwa nyumbani, sijui kama ni kweli kuwa yule mwanao wa kiume alinibaka ukanitusi mimi kuwa namfunza tabia mbaya nasikia na yeye ni teja na kila leo anakuibia vitu nyumbani!!

Natoa shukrani kwako kwa mabaya yote uliyonitendea, natoa shukrani kwako kwa moyo wako mgumu unaodhani kuwa niliyasahau yale yote na leo hii umeketi upande wa ukoo wangu ukisubiri kunipa zawadi ya kunipongeza kwa sababu nimeolewa.

U mnafiki ewe mama, u mkatili katika maana halisi ya kuitwa mkatili.

Nayasema haya ili niwe na amani, nayasema haya bila unafiki wala tabasamu bandia la kuigiza!!!

Nilijua itafika siku ya kusema nd’o maana sikusema katika siku hizi zote.

Ewe mama wa kambo umenipa zawadi nyingi sana tena za kudumu, siihitaji zawadi yako siku hii ya leo. Sihitaji chochote kitu katika maisha yangu kutoka kwako!! Umenipa vingi na vinatosha sana!!!

Asante sana mama wa kambo!! Mama mbaya unayesababisha hata wale mama wa kambo wenye utu waonekane kuwa si lolote na si chochote kitu!!!”

Maria alimaliza kuzungumza huku machozi yakiondoka na nuru yake asiweze kuona mbele tena.

Mama yule ambaye ukumbi mzima ulikuwa ukimtazama alibaki akiwa ameinama kama anayesikiliza kwa makini yale aliyokuwa akielezwa na Maria. Watu walingoja sana anyanyuke waweze kuibaini walau sura yake. Lakini hakunyanyuka, aliyeamua kumgusa bega mara kadhaa kwa kumsukuma ndo aliihitimisha safari yake sakafuni.

Mama yule hakuwa na fahamu zake!!!

Zikafuata hekaheka za kumpepea lakini fahamu hazikurejea.

Maria naye alifanya harakati hizo huku akiipuzia shela aliyokuwa ametinga. Hali ilikuwa tete na ukumbi wa sherehe ukageuka kuwa ukumbi wa hekaheka!!

Wakati mama yule anakimbizwa hospitali, Maria alipata fursa ya kukwapua bahasha ambayo ilikuwa mikononi mwa mama wa kambo kabla hajaanguka!!

Akaifungua na kukutana na kipande cha karatasi.

“Sina zawadi yoyote ya kukupa Maria, japo ni wewe wa kunipa mimi zawadi kubwa ya msamaha. Hakuna nikitegemeacho tena duniani zaidi ya msamaha wako!! Siwezi kujieleza nikaeleweka kwa yote yaliyotokea miaka hiyo lakini waweza kunielewa! Ninauhitaji msamaha wako kabla sijafa Maria. Nililelewa na mama wa kambo nikanyanyaswa na kupewa kila aina ya mateso, sidhani kama ilikuwa sahihi kulipizia kwako nakiri mbele yako kuwa nilikosa na leo hii nitaomba msamaha mbele ya umati. Nisamehe Maria!!”

Alipomaliza kuusoma ujumbe ule alihitaji kumwona yule mama na kumweleza kuwa amemsamehe tayari lakini akakutana na taarifa kuwa MAMA WA KAMBO AMEFARIKI TAYARI!!!

Maria alijikuta katika mkanganyiko wa huzuni na amani!!

“ASANTE MAMA WA KAMBO!!” akajisemea.

FUNZO:

Hata wale watu unaohisi ni wabaya katika maisha yako, jifunze kutoka kwao.

Na utakuwa imara zaidi katika maisha yako iwapo ukijifunza kutoka kwa watu wanaokukatisha tamaa. Kaa kimya, inama kama kondoo, waache wanyanyue midomo yao juu na kukusema. Kama wanakusema kwa chuki zao usijali, na wakisema la ukweli lichukue kama funzo.

WAPENDE ADUI ZAKO LAKINI HAKIKISHA HAWAJUI KAMA UNAWAPENDA AMA UNAWACHUKIA!!! Utafaidi kutoka kwao mkiishi hivi!!

MWISHO!!!

Post a Comment

0 Comments