Header Ads Widget

Responsive Advertisement

AHADI YA NDOTONI - 2




Simulizi : Ahadi Ya Ndotoni
Sehemu Ya Pili (2)



“Na ndugu zako wote?”
“Ni mimi peke yangu ndiye niliyebakia.”
“Ina maana wazazi wako hawana ndugu?”

“Heri ningekaa kwenye dimbwi la mamba wenye njaa kuliko hao ndugu wa baba, nina wasiwasi hata kifo cha wazazi wangu huenda wao wakahusika. Baada ya kifo cha wazazi wangu walinichukua lakini mwishoni walinifukuza kama mbwa na matokeo yake ni haya, kuna umuhimu wa kukatisha maisha yangu tabu hizi mpaka lini?”

Jeska alizungumza kwa uchungu mkubwa na kumfanya daktari amuonee huruma, lakini bado aliamini kuna kitu cha kumsaidia kutokana na matatizo yake.
“Jeska nina cha kukusaidia kwa matatizo yako yote?”
“Kivipi?”

“Kwanza kumtafuta aliyekubaka na pili kumjua aliyetaka kukutoa roho kwa kukutoa ujauzito ili sheria ichukue mkondo wake.”
Jeska hakujibu haraka kutafakari aliyosema daktari, kabla ya kumjibu swali lake alimuuliza:

“Samahani dokta.”
“Bila samahani.”
“Eti mama anajua kama nilikuwa natoa mimba?”
“Ndiyo.”
“Alisemaje?”

“Alilalamika kwa uamuzi wako wakati waliisha kueleza usiitoe.”
“Mh!” Jeska aliguna na kuendelea kutafakari swali la daktari kumtaja aliyempa ujauzito.
Aliamini siri yake ni nguzo ya ndoa ya wazazi wa Edna na kuhusu kumtaja aliyemtoa ujauzito vile vile angekuwa amewaharibia wenzake ambao walitumia hospitali ile kutoa ujauzito kama yeye angeitaja na kukamatwa kwa muhusika lazima shoga zake watamuona hana maana hata kumtenga.

Aliamini bado siri yake ni muhimu kwa jambo lile la kutoitaja hospitali aliyotumia kutoa ujauzito. Baada ya ukimya wa muda Jeska alisema:

“Dakta najua unania nzuri na matatizo yangu, lakini mwenye utatuzi wa yaliyo mbele yangu ni yule aliye sababisha yote haya.”
“Hapana Jeska, najua pengine una hofu kuwataja watu hao lakini nakuahidi kukulinda kwa kila kitu ambacho kitajitokeza hata kukuwekea wakili katika matatizo yako ikiwemo ya kudhulumiwa mali uliyoachiwa na wazazi wako.”

“Nashukuru, nipe muda nitakueleza kila kitu.”
“Leo huwezi?”
“Nimekueleza nitakueleza kila kitu naomba unielewe.”
“Vizuri, basi kuna chakula unatakiwa kula.”

“Siwezi niache nilale sijisikii labda asubuhi.”
“Ngoja nikudunge sindano ili upunguze maumivu.”
Daktari alimdunga sindano kisha alimwacha Jeska apumzike kwa vile usiku ulikuwa mkubwa. Baada ya daktari kuondoka hakuchukua muda mrefu naye usingizi ulimpitia.
Daktari alijifanya kushangaa na kuwaita wauguzi kuwaulizia mgonjwa.
“Eti jamani, mgonjwa mmemuona wapi?”
“Mmh, si asubuhi alikuwemo ndani?” Muuguzi mmoja alisema.
“Kwani hamkumkuta?”Mwingine aliuliza.

“Sasa tungemkuta tungemuuliza?” Mama Edna alimjibu kwa hasira.
“Mmh, kwa kweli hatujui.”
“Au amerudi nyumbani mwenyewe.”

Wakati wakishauriana kupotea kwa Jeska, mara aliingia mzee Ezekiel baba yake Edna, wote waligeuka kumtazama.
“Karibu mzee,” daktari alimkaribisha mzee Ezekiel kama hamfahamu.
“Asante.”

“Nikusaidie nini?”
“Hapana huyu ni mume wangu,” mama Edna aliingilia kati.
“Ooh, mzee karibu sana.”
“Asante, vipi naona kuna nyuso sizifahamu, kuna usalama?”
“Usalama upo, ila kuna tatizo moja mgonjwa haonekani kwenye wodi yake.”

“Mmemtafuta nje ya wodi?”
“Bado.”
“Sasa unangoja nini, mtafuteni nje ya wodi mkimkosa ndipo mjadiliane.”

Walikubaliana kumtafuta nje wa wodi kwa kutumwa wauguzi kuranda kila kona ya hospitali kumtafuta mgonjwa lakini hakuna aliyemuona. Mzee Ezekiel alishauri warudi nyumbani huenda amerudi mwewnyewe. Wote walirudi nyumbani kumuangalia Jeska kama kweli amerudi nyumbani, huku siri kubwa ikibaki moyoni kwa mzee Ezekiel.

Walipofika nyumbani hawakumkuta mtu, walikubaliana wasubiri atakuwa amekwenda wapi na kama mpaka siku ya pili hajaonekana walikubaliana wapeleke taarifa polisi. Mzee Ezekiel alimweleza mkewe mambo yote kuhusu Jeska atayashughulikia yeye.

Edna aliamini kabisa chanzo cha Jeska kutoroka ni mama yake, hakuacha kumlaumu mama yake.

“Mama unaona ukali wako ndiyo kila siku unamchanganya da Jeska, sasa unaona kaamua kutoroka?” Edina alimwambia mama yake.
“Sasa atakuwa mtoto wa jicho asiyekanywa akikosea.”
“Lazima mama uangalie yule yupo vipi, hana wazazi lolote utakalo mkalipia atajua humpendi.”

“Ningekuwa simpendi ningemlea muda wote huu.”
“Lakini kataa kubali kutoroka kwa Jeska ni kutokana na kauli zako kali za vitisho.”

“Aah, Mungu ndiye anajua kama nilikuwa simpendi, kipi alichotaka nisimpe nilimfanya kama mwanangu wa kuzaa ndiyo maana hata kumkanya nimemkanya kama ambavyo ningekukanya wewe.”
“Sasa atakuwa amekwenda wapi?”

“Tutajuaje mimi na wewe hatujui.”
“Asiwe ameamua kujiua!”
“Mungu apishe mbali, siamini kama uamuzi kama huo ndiyo suluhu ya maisha yake.”

“Mama Jeska huamini kabisa ni kiumbe kilichoumbwa kwa mikosi toka kifo cha familia yake, tuliweza kumpunguzia maumivu ya msiba ule mzito na kumfanya asahau. Lakini hili la mimba limemuumiza sana, kuna siri nzito moyoni mwake ambayo sijui kwa nini hakutaka kuitoa.”

Wakiwa katikati ya mazungumzo mlinzi wa getini aliingia na barua mkononi.
“Karibu Musa naona una barua.”
“Ndiyo mama.”
“Nani amekupa?”

“Kanipa Jeska.”
“Jeska! Jeska yupi?”
“Si dada Jeska.”
“Huyu Jeska wa kwetu?”
“Ndiyo.”
“Wa humu ndani?”
“Ndiyo mama.”
“Yupo wapi?”

“Alikuja na teksi hadi getini dereva alipiga honi kuashiria ananiita, nilikwenda hadi kwenye gari na kumkuta dada Jeska ambaye alinisabahi kisha alinipa barua hii nikuleteeni kisha gari liliondoka.”
“Alikuambia anakwenda wapi?”
“Hakuniambia”
“Afya yake?”
“Ipo sawa.”

Unaikumbuka namba ya ile teksi?”
“Kwa kweli sikuitilia maanani.”
“Mmh, sawa kaendelee na kazi.”

Waliipokea ile barua na kuifungua kuangalia ndani kuna kitu gani, baada ya kuifungua walikutana na ujumbe ambao ulionesha kweli umeandikwa na Jeska kutokana na kuufahamu vyema mwandiko wake. Barua ilikuwa imeandikwa hivi:
Kwenu wazazi wangu, shikamooni.

Napenda kuandika waraka huu kuwatoeni wasiwasi kwa kutoweka kwangu ghafla, lakini napenda kuwatoa wasiwasi wazazi wangu pamoja na dada yangu kipenzi Edna. Najua kitendo nilichokitenda kitaonekana ni utovu wa nidhamu lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kufanya niliyoyafanya.

Kupewa ujauzito kwa kubakwa kwa kweli kuliniumiza sana kiasi cha kujikuta kiumbe nisiyetakiwa duniani. Lakini ninyi wazazi wangu pamoja na ndugu yangu kipenzi Jeska umeweza kunipa moyo na kufuta dhana mbaya moyoni mwangu ya kukatisha maisha yangu.

Nina mengi ya kuzungumza na ninyi wazazi wangu baba mama na Edna juu ya nini kilinikuta, sikutaka kulitamka hili mapema kwa vile lingeniongezea maumivu moyoni mwangu. Naamini kabisa hakuna hata mmoja angekubali kusubiri kuwaeleza kitu ambacho alikuwa na shauku kukijua.

Nimeamua kuondoka hapo nyumbani ili nipate muda wa kupumzisha maumivu makali ya moyo wangu, baada ya kuupumzisha moyo wangu nitarudi nyumbani, nakuombeni mnipokee japo mimi ni mwana mkosefu pengine kuonekana asiye na shukurani.

Ila siku ilifika kila kitu kitakuwa wazi na mtanielewa zaidi pengine kunionea huruma zaidi kama milivyonionea huruma na kunitunza mpaka leo hii. Sitaki kuwachosha kwa maneno mengi, nilitaka kuwatoa hofu tu msinitafute nipo katika mikono salama na baada ya muda nitarudi nyumbani ni mimi mwanenu Jeska.

Baada ya kuisoma alimpa Edna naye aisome kutokana na kuwa na shauku kutaka kujua kwenye karatasi ile kumeandikwa nini. Edna naye alisoma kimya kimya ile barua kisha alinyanyua macho kumtazama mama yake aliyekuwa akimfuatilia alipokuwa akisoma.

“Mama hii barua umeielewa?”
“Kilichoandikwa si umekisoma?”
“Ndiyo.”
“Basi lazima tuielewe.”

“Sina maana hiyo”
“Una maana gani?”
“Mama kuna fumbo zito ambalo Jeska kalificha, mmh kubakwa...na nani?”

“Tutajuaje naye amefanya siri.”
“Lakini mama ulitakiwa kumuelewa Jeska kuliko kumkaripia.”
“Edna usitake kuniudhi, kwani angenieleza haya aliyoandika kwenye barua nisingemuelewa?”

“Asingeweza kutokana na kauli yako ya ukali, Jeska anaamini toka apatwe na tatizo umemtenga.”
“Nimemtenga kivipi Edna? Mbona unanitia lawama zisizo na msingi.”

“Kweli mama umekuwa mkali kauli zako hata mimi nilijisikia vibaya, ni kweli Jeska alikuwa amefanya kosa hatukutakiwa kutumia vitisho aseme nani aliyempa ujauzito. Lazima angesema tu kama alivyosema alichanganywa na kitendo cha kubakwa, hata ningefanyiwa mimi ningeumia.”

“Sasa atakuwa wapi?”
“Ni vigumu kujua la muhimu tumsubiri baba arudi atatusaidia akiisoma hii barua.”


“Mmh, mwaka huu mbona Jeska ametuchanganya akili,” mama Edna alisema huku akiirudisha barua kwenye bahasha.
Mara simu ya Edna iliita alipoangalia ilikuwa namba ngeni machoni mwake, aliipokea na kusema.
“Haloo”

“Haloo Edna,” sauti ya upande wa pili ilisema.
“Nani mwenzangu?”
“Mimi Jeska.”
“Jeska! Jamani Jeska upo wapi ndugu yangu?”

“Kabla ya yote barua mmeipata?”
“Ndiyo, upo wapi mbona umeondoka nyumbani bado tunakuhitaji?”
“Edna sipo mbali ila baada ya muda nitarudi nyumbani, kama nilivyosema.”
“Lakini ipo wapi?”

“Nimekwambia sipo mbali, akili yangu ikitulia na nikiwa tayari kuyasema mbele yenu nitarudi nyumbani, msalimie mama.”
“Huyu hapa,” Edna alisema huku akimpa simu mama yake.
“Haloo Jeska.”

“Abee mama, shikamoo.”
“Marahaba, upo wapi mama rudi nyumbani...yote yamekwisha ilikuwa ni hasira tu mwanangu.”
“Najua mama, ila usiwe na wasiwasi nitarudi tu mama nakupenda sana.”

“Najua mwanangu chonde chonde mwanangu rudi walimwengu hawatanielewa, hata nduguyo anasema matatizo yote chanzo ni mimi.”
“Hapana mama, nitarudi.”
Jeska alikata simu na kuizima kila walipompigia hakupatikana.

****
Jeska baada ya kurudi kutoka kwa mzee Ezekiel kupeleka barua kutokana na makubaliano yake na mzee Ezekiel kuwa aandike barua ya kuwatoa wasiwasi ili familia yake itulie isimtafute. Baada ya kurudi hotelini kwake alitulia na kumjulisha mzee Ezekiel kwa simu.

“Tayari baba.”
“Vizuri, umempa nani?”
“Mlinzi.”
“Amekuona?”
“Ndiyo.”
“Amesemaje?”
“Alionesha kunishangaa lakini sikumpa muda wa kuuliza swali zaidi ya kuondoka nikimwacha akinitumbulia macho.”

“Jeska umefanya kitu kizuri sana, nakuhakikishia kuyabadili maisha yako kama shukurani ya kuificha siri ambayo ingenichafua.”
“Nitashukuru”

Mzee Ezekiel muda ule aliamua kurudi nyumbani ili akasikie wamepokeaje barua ya Jeska, alipofika nyumbani alikuta hali ya kawaida na yeye alijifanya hajui lolote. Baada ya mapumziko mafupi mkewe alimfuata alipokuwa amekaa kwenye kochi na kumpatia barua ya Jeska. Kabla ya kuipokea alihoji.

“Ya nini?”
“We, soma.”
Aliichukua ile barua na kuisoma kiuongo na ukweli kisha alishusha pumzi ndefu na kumtupia jicho mkewe aliyekuwa akimfuatilia muda wote aliokuwa alipokuwa akiisoma.

“Umeiona?” Mkewe alimuuliza.
“Nimeiona.”
“Una maoni gani?”
“Nani kaileta?”

“Yeye mwenyewe.”
“Alipoileta alisemaje?”
“Sikuonana naye ila alimpa mlinzi.”

“Nafikiri kuna kitu anakiamini, sidhani kuna umuhimu wa kumtafuta kwa vile amesema atarudi tumpe uhuru anaotaka. Nina imani sasa hivi Jeska ana miaka 19 ana maamuzi ambayo yanayokubalika hata kisheria.”
“Lakini bado ni mtoto aliye chini yetu.”
“Ni kweli, lakini mambo mengi amekuwa akituficha sisi walezi wake ambao tulimlea kama mtoto wetu wa kuzaa. Sidhani kama kuna siku ulimpa upendeleo Edna na kumtenga Jeska?”

“Sijawahi na wala sikuwahi kuwaza jambo hilo zaidi ya kufikiria siku moja Jeska ayazungumze mafanikio yake kupitia mikono yetu. Inaonesha jinsi gani Jeska kaumizwa na kubakwa kitendo ambacho kimechubua kovu la kufiwa na wazazi wake.”

“Sasa sisi tutafanya nini ikiwa yeye mwenyewe hataki kusema ukweli ili tumchukulie hatua aliyembaka. Lakini kwa vile amesema ipo siku atarudi na kuyasema yote tumpe muda.”

Baada ya makubaliano mzee Ezekiel aliaga na kuondoka, safari yake ilikuwa kwenda hotelini kwa Jeska akapange mikakati mingine baada ya kufanikiwa mpango wake wa awali wa kumtorosha Jeska. Alipofika hotelini alimkuta Jeska amejilaza akiwa hajui nini hatima ya maisha yake baada ya kukubali kuusaliti moyo wake kwa kuuficha ukweli.

Mzee Ezekiel alikumta amejilaza kitandani akiwa amejifunga taulo lililovuka magoti kidogo. Jicho lake lilitua kwenye maumbile ya mvuto ya Jeska. Alimeza funda la mate na kuingia ndani wakati huo Jeska alikuwa akijiweka vizuri.

“Karibu baba.”
“Asante.”
“Za huko?”
“Mmh nzuri, akili tuliyotumia itakufanya uishi bila wasiwasi.”

“Nitaishi vipi ina maana maisha yangu yote yatakuwa ya hotelini?”
“Hapana, kuna nyumba nimekutafutia nitakupangia nyumba nzima ambayo utaishi huko nitakutafutia mfanyakazi wa ndani. Nitakutoa siku moja moja sehemu za starehe zilizokuwa nje ya mji ili kuhakikisha unafurahia maisha.”

“Kama hivyo nitashukuru.”
“Nia yangu ni kurudisha furaha yako na kuondoa maumivu yote ya kubakwa, ichukulie kama ajali. Si hayo tu nina mpango wa kukujengea nyumba na kukufungulia miradi ili usiwe tegemezi. Leo nipo kesho sipo sitaki upate tabu.”

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa Jeska kuishi mbali na familia iliyomlea huku mzee Ezekiel akiongeza mapenzi kwa Jeska ambaye bila kujielewa alikuwa amenaswa na mtego wa mzee Ezekiel na kumgeuza kuwa mpenzi wake.

Penzi lake na mzee Ezekiel lililipuka kama moto wa volkano, safari zote za ndani na nje ya nchi walikuwa pamoja, Jeska alizidi kupendeza toka umbile la kitoto na kuhamia katika umbile la mtu mzima lisilo tilia mashaka ukaribu wake na mzee Ezekiel watu waliwaona wapo sawa.

Jeska kwa muda mfupi alisahau maumivu yote ya kubakwa na mzee Ezekiel na kujikuta akifurahia penzi la mzee huyo na kutamani awe mke mdogo mwenye haki zote.

Mzee Ezekiel alimhakikishia kumuoa ndoa ya Bomani na kumpatia sehemu ya mirathi ya mali yake. Hatua ile ilimfurahisha sana Jeska na kuamini mwanzo wa maisha mapya ya kuweza kumiliki mali yake kutokana na uwezo mkubwa wa mzee Ezekiel.

Ukaribu wa mzee Ezekiel na Jeska ulianza kuyumbisha nyumba ya mzee Ezekiel kwa mapenzi yote kuhamishia kwa Jeska aliyefahamika kama mke wa pili wa mzee Ezekiel. Kutokana na tabia ya mke wa mzee Ezekiel mama Edna kutotembea mambo mengi ya nje hakuyajua.

Wakati mipango imekaribia na hatua zote muhumu za kufunga ndoa ya Bomani, siku moja baada ya kutoka kwa Jeska majira ya saa tano usiku mzee Ezekiel akiwa katika gari lake alipata ajali ya gari lake kugongwa sehemu ya mlango na kumsababishia maumivu makali sehemu za kifua na mbavu.
“Asante, lakini ndivyo hivyo mwisho wa mwaka siwezi kukaa hapa tena.”

“Unaishi na nani?”
“Nipo peke yangu na mfanyakazi wa ndani, kwa sasa nina pesa kidogo za matumizi zikiisha nitamlipa nini.

Na mwaka ukiisha nitalipa nini na nikifukuzwa nitakwenda wapi kama sio kuadhirika mtoto wa kike,” Jeska alijikuta akitoa siri yake yote bila kujua mtu aliye mbele yake ni wa aina gani kutokana na kupagawa kutokana na kifo cha mzee Ezekiel na maisha atakayoishi.

“Hapa mjini huna ndugu?”
“Wapo lakini ni wabaya wangu.”
“Kivipi?”
“Japo sikujui hunijui lakini msaada wako mkubwa unanifanya niwe muwazi kwako.”

“Ni kweli mimi ni mtu mwema pia naweza kuwa msaada mkubwa katika maisha yako.”
Jeska alijikuta akiitoa siri yake yote toka kifo cha familia yake mpaka alivyochukuliwa na familia ya mzee Ezekiel baba yake shogae kipenzi Edna. Lakini la mzee Ezekiel kumbaka alilificha, lakini kwa ajabu yule mgeni alimwambia.
“Mbona unaficha lingine.”
“Lipi hilo?”
“La kukubaka mzee Ezekiel na kukutorosha hospitali.”
“Mmh, umejuaje?” Jeska alishtuka.
“Namejua tu kwani lilikuwa siri.”
“Mbona unanitisha, hakuna anayejua zaidi yangu na dokta.”

“Sasa hapo siri ipo wapi, tuachane na hilo, mmhu”
“Hapana, inaonekana basi unajua mengi kuhusu mimi.”
“Sijui lolote, hebu endelea kunihadithia ili niweze kukusaidia.”

“Kama hivyo baada ya kubakwa na kufichwa huku lakini mkosi bado ulikuwa ukiniandama na kujikuta niliyemtegemea ndiyo hivyo amefariki.”
“Lakini si mlikuwa na mpango wa kuoana?”
“Eti?” Jeska alizidi kushtuka maneno ya mgeni wake kuonekana kujua mambo mengi ambayo yeye aliamini ni siri.

“Jamani kaka wewe ni nani unayejua mambo yangu mengi?”
“Sijui mengi ila hutaki kuwa mkweli na muwazi kwangu.”
“Kaka yangu mengine nayasahau kutokana na kuchanganyikiwa.”

“Basi nitakuwa nakusaidia, upo tayari nikusaidie?”
“Nipo tayari, japo maneno yako yananitia wasiwasi.”
“Sikiliza Jeska.”

“Ha! Kaka umejuaje jina langu?”
“Jeska hayo si muhimu zaidi la lililo mbele yako.”
“Sasa utanisaidia vipi?”
“Nataka mali zote zilizochukuliwa na wazazi wako zirudi kwako.”

“Kwangu! Wewe ni mwana sheria?”
“Ni mtu wa kawaida ila ninajua jinsi ya kukurudishia mali zako.”

“Utafanya nini?”
“Jeska, wewe shida yako mali zako au kujua zitarudi vipi?”
”Mmh, siamini naona sawa na kunipa matumaini lakini jambo hili siamini kama litawezekana ni muda mrefu sana hata hati zote wanazo wao.”

“Kazi hiyo niachie mimi, sawa.”
Baada ya kusema vile mgeni aliingiza mkono mfukoni na kumpatia noti mpya nne za elfu tano tano na kumueleza.
“Naomba hizi hela usizitumie leo kaziweke chini ya mto mpaka kesho kisha ruksa kuzitumia.”

“Asante,” Jeska alishukuru huku akipokea.
“Nilitaka kusahau na ukiamka asubuhi chukua zote usiache hata moja chini ya mto.”

“Hakuna tatizo.”
“Wacha nikuache niwahi kwenye shughuli zangu nikipata muda nitarudi usiku.”
“Kuja kulala?”

“Utakavyotaka wewe, au nisirudi?”
”Hapana njoo tu.”
“Basi wacha nikukimbie.”

“Ngoja nikaweke pesa zangu ndani,” Jeska alisema huku akinyanyuka kuelekea chumbani kwake.

Jeska alikwenda hadi chumbani na kuziweka pesa zake chini ya mto kisha alitoka sebuleni alipomuacha mgeni. Lakini sebule ilikuwa nyeupe mgeni hakuwepo, alipotoka nje pia hakumkuta pamoja na gari lake.


 Alijiuliza mgeni ametoka vipi kwa muda mfupi bila kuaga wala gari lake kutoa muungurumo wakati wa kuondoka.

Hakutaka kuumiza akili yake zaidi ya kurudi sebuleni na kujitupia kwenye kochi na kujikuta akivuta taswira ya mzee Ezekiel na mipango yao kabambe ya kufunga ndoa na kuyabadili maisha yake kwa kumjengea jumba na kumnunulia gari la kifahari.

Moyo ulimuuma na kujikuta akilia peke yake kwa sauti ya chini huku akipiga mikono kwenye sofa na kusema kwa sauti.

“Haiwezekani kila baya kwa nini liwe kwangu, nimefiwa na wazazi nimedhurumiwa mali nimebakwa na mwisho niliyekuwa namtegemea amekufa kuna faida gani kuendelea kuishi bora nife.

Wazo la haraka lililomujia Jeska ni kujiua, alinyanyuka alipokuwa amekaa na kuelekea chumbani kwake, chini ya kitanda kulikuwa na kamba ya kuanikia nguo ndani wakati wa mvua. Aliichukua na kutoka nje ili aelekee kwenye mti ajiue.

Ajabu ya mwaka aliyokutananayo kidogo apige kelele ya woga baada ya kumuona mgeni akiwa amekaa kwenye sofa akimtazama.

“Ha!” Jeska alishika mkono kifuani kwa mshtuko.
“Mbona umeshtuka?” Mgeni alimuuliza huku ameachia tabasamu pana.
“Ha..a..a..pa..na,” Jeska alijibu kwa kubabaika.
“Hiyo kamba ya nini?”
“Aa..aa. ya kawaida.”
“Unajua kutaka kujiua ni kuingilia kazi ya muumba kwa vile lazima ufe.”

“Umejuaje?”
“La muhimu si kujua nimejuaje zaidi ya kukuonya tena usiingilie kazi ya muumba.

“Lakini wewe nani?” Jeska alimuuliza.
“Jeska hata ukinijua si muhimu zaidi ya kujipanga kwa maisha mapya na si kukimbilia kujiua.

“Ulikuwa wapi mbona nilitoka muda mfupi hukuwepo?”
”Nilikuwa nimeondoka kwa vile nilikuwa na haraka nisingeweza kukusubiri, lakini uso wako ulionesha una dhamira mbaya moyoni mwako kitu kilichonifanya nirudi kabla hujachukua uamuzi mbaya.”
“Nina faida gani ya kuendelea kuteseka kila siku.”
“Nimekueleza nitakusaidia unataka msaada gani zaidi ya huo?”
“Basi nisamehe, nimechanganyikiwa na maisha.”
“Nimekusamehe naomba unisindikize, ila nakuomba usirudie kufanya ujinga wowote, sawa?”
“Sawa.”

Walitoka hadi nje ambapo mgeni aliingia kwenye gari lake Jeska alimfungulia geti na mgeni aliondoka na kumpungia mkono. Jeska alilisindikiza gari lile kwa macho mpaka likapotea huku akijiuliza mtu yule ni nani mbona kama anaonekana wa ajabu ajabu. Lakini aliamini yale ni mawazo yake kutokana na kuchanganyikiwa na maisha.

Jeska alirudi ndani na kwenda moja kwa moja chumbani kwake na kujilaza chali macho alitazama juu ya dali.

Kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi juu ya yule mwanaume msamaria mwema. Alijiuliza ni mtu wa aina gani, bado alipingana na akili yake pengine kuchanganyikiwa ndiko kulikomfanya hata alipotoka hakumuona. Lakini kama hakumuona sebuleni hata gari lake. Bado alibakia njia panda asijue ukweli ni upi.

Kingine kilichomchanganya mtu yule kujua mambo yake mengi, wazo la kuwa mtu yule labda jini hakuwa nalo zaidi ya kuamini mtu yule alikuwa akimjua vizuri kuliko alivyojifahamu yeye mwenyewe. Akiwa amejilaza akitazama juu kwenye dari hakuona faida ya kuendelea kuishi hata kama yule mwanaume angeamua kumsaidia bado asingeweza kuyamudu maisha.

Bado shetani mbaya hakuwa mbali naye ufumbuzi mkubwa katika maisha yake ilikuwa ni kuyakatisha maisha yake. Jeska aliamini hakuna mtu wa kumsaidia tena katika maisha yake. Wazo la kujinyonga bado halikuwa mbali naye alikurupuka na kwenda kuchukua kamba aliyoirudisha chumbani na kutoka nayo tena kwa kujiamini ili akajinyonge.

Alitoka mpaka nje kabla ya kuchukua uamuzi ule mzito alimtuma mfanyakazi wake wa ndani sehemu ambayo aliamini mpaka atakaporudi atamkuta ameisha jinyonga. Hata mlinzi vilevile alimtuma mbali ili tu awe huru kutekeleza mpango wake wa kujinyonga.

Baada ya kukagua eneo lilo na kuliona lipo katika hali ya utulivu, alichukua kamba yake na kuzunguka nyuma ya nyumba kwenye miti na kuifunga kwa kupanda kwenye mti. Alikumbuka alisahau sturi ya kupandia. Alirudi ndani kuchukua kwa haraka kabla hawajarudi wafanyakazi wake.
Alipofika ndani alichukua sturi na kuzunguka nayo nyuma ya nyumba ili atimize dhamira yake ya kujinyonga.
Wakati anatoka ndani alikutana na mfanyakazi wake wa ndani.
“Dada mbona una kisu mkononi?”
“Wewe Sara mbona umewahi kurudi?” Jeska alimuuliza kwa hasira.

ITAENDELEA

Post a Comment

0 Comments