Juzi nilihudhuria msiba wa rafiki yangu mmoja na mkewe. Yeye na mkewe walifariki kwa ajali ya gari, wameacha watoto wawili mmoja wa miaka kumi na mwingine wa miaka minne wakike, mkubwa ni wakiume.
Sasa tukiwa kwenye ule msiba, mimi kama rafiki nilikua karibu sana na wale watoto kwani wananifahamu kama Baba mdogo, kusema kweli nilichokishuhuduia kilinifanya nije nimpende mke wangu mara mia zaidi.
Kweli nampenda sana mke wangu lakini kuna wakati namchukuliaga poa nikiwa na mambo yangu najifanya kidume na namuudhi. Kwasiku tatu zote nilikua karibu na ile familia tukimalizia msiba, katika kipindi chote hicho watoto walikua wakimlilia Mama yao.
Yaani wakilala wakiamka ni kuniuliza, wananiita anko, Mama yuko wapi (Mara nyingi wnaaniita anko), wanmauuliza Bibi yao Mama yuko wapi. Sasa kilichonifanya nilie nipale ambapo mtoto mkubwa wa miaka kumi ambaye anaelewa kitu kidogo alikua anampembeleza mdogo wake alikua anamuambia.
“Usilie Mama kaenda sehemu nzuri, kaenda kupumzika kwa Mungu na Malaika…” Mdogo wake ndipo alipouliza Baba nayeye, akasema “Amemsindikiza Mama watakaa huko na mimi ndiyo nitakulinda, usiogope nipo hapa. Unakumbuka siku ile Mama alivyotuambia twende kwa Bibi kukaa wenyewe…”
Alimuuliza… “Mimi si nilikulinda…nitakulinda na sasa…Mama anatuangalia lakini sisi hatumuoni….” Kama hapo umelia basi subiri majibu ya yule mdogo wake. Huku akijaribu kujizuia kulia alimuuliza Kaka yake.
“Sasa kama Baba ameenda na Mama si atampiga tena, mimi sitaki Mama apigwe, kwanini asingeenda peke yake….” Nilianza kuwaza namna ambavyo rafiki yangu yule alikua akimnyanyasa mkewe, namna alivyokua akimpiga na kumsimanga, nilishaongea naye mara nyingi lakini hakujali.
Lakini alikua anawapenda watoto wake na kila siku aliwadekeza ila hawakumkumbuka. Jibu la kijana wake ndiyo lilinifanya niamini kuwa wanadamu si chochote. “Huko hawezi kumpiga, Mama ameenda kwa Mungu, huyo ana nguvu zaidi kuliko Baba. Akimsogelea tu atamchanachana kamakaratasi! Mungu ana upendo hapigi watu wema kama Mama!”
Hapo yule mtoto alikua akiongea kwa uchungu lakini kwa hasira na kwa imani kabisa. Sikuweza kuendelea kuvumilia kuwasikiliza, niliwaacha na kwenda kumuangalia mke wangu, nilimkumbatia na kumuuliza “Mke wangu hivi na mimi nakunyanyasa?”
Aliniangalia kwa mshanagao, aliniulzia kwanini unasema hivyo, nilimuambia hapana niambie tu. Niambie kama kuna kitu nakifanya kinakukwaza ambacho watoto wangu watakiona. Nilimuambia “Nataka wanangu waniulizie nikifa, sitaki wanangu wafurahie kifo changu.”
Mke wangu alinikumbatia huku akitokwa na machozi aliniambia “Hakuna mume wangu, wewe ni mume bora, sema uache tu kuweka soksi kwenye makochi na kuacha sahani kitandani.” Nilijikuta natabasmau kidogo, kwani mke wangu alikua na furaha.
Sasa hivi najifunza nisiache soksi kwenye makochi wala sahani kitandani. Najua alikua anatania ila kama kinamkera nitaacha, maisha hapa duniani ni mafupi, watoto ndiyo kitu tunaacha kwaajili ya kututambulisha, sitaki wnaangu wanaitambue kama Baba mkatili
Furaha katika ndoa haidondoki tu kama mvua, ni kitu ambacho kinatengenezwa. Ingawa mapenzi ni ya watu wawili lakini maumivu yake ni ya ulimwengu na huwaumuiza sana watoto.
****MWISHO***
0 Comments